1. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatakaswa na kila kiliomo katika
mbingu na ardhi, tangu watu, na wanyama, na hata vitu visio na roho. Na Yeye
ndiye Mwenye nguvu, anaye yaendesha mambo yote kwa mujibu wa hikima yake.
2. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu, si wa
mwenginewe. Yeye huyasarifu apendavyo yote yaliomo humo, Yeye ndiye Mwenye
kuhuisha na kufisha. Na kwa kila kitu Yeye ndiye Mwenye uweza ulio timia.
3. Yeye alikuwapo kabla ya kila kitu, na atabaki baada ya
kutoweka kila kitu. Yeye ndiye aliye dhaahiri, anaonekana, katika kila kitu.
Kwani kila kitu ni Ishara yake. Na Yeye ndiye wa ndani, ambaye hawezi kueleweka
kwa macho. Na Yeye ni Mwenye kutimia ujuzi wake kwa kila kitu kilicho dhaahiri
na kilicho fichikana.
4. Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi na viliomo kati yao
kwa siku sita, kisha akakalia A'rshi (Kiti chake cha enzi) akiangalia ufalme
wake. Anajua kila kinacho ghibu katika ardhi na kinacho toka humo, na kila
kinacho teremka kutoka mbinguni, na kinacho panda kwendea huko. Na Yeye ni
Mwenye kukujueni, anayajua vyema mambo yenu popote pale mlipo. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kuyaona myatendayo, anayajua vilivyo, wala hakifichiki kitu kwake.
5. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Na
kwake Yeye Mtukufu ndiye mambo ya viumbe vyake yanarejeshwa, na kwake ndiko
kunako kwishia mwisho wao.
6. Yeye huziingiza saa za usiku katika mchana, na huziingiza
saa za mchana katika usiku. Kwa hivyo hupatikana khitilafu katika urefu wao. Na
Yeye ndiye Mjuzi wa yanayo hifadhiwa na vifua, na yanayo dhamiriwa na nyoyo.
7. Msadikini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mtoe katika
Sabilillahi, Njia ya Mwenyezi Mungu, katika mali aliyo kujaalieni Mwenyezi Mungu
nyinyi kuwa ni waangalizi katika matumizi yake. Basi hao wenye kumuamini
Mwenyezi Mungu na Mtume wake miongoni mwenu, na wakatoa katika alivyo wapa
uangalizi juu yake, watapata kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hayo malipo
makubwa.
8. Na kwa nini hamumuamini Mwenyezi Mungu, na hali Mtume
anakutakeni mumuamini Mola wenu Mlezi, na anakuhimizeni kwa hayo. Na Mwenyezi
Mungu kesha chukua agano lenu la Imani kabla yake. Kama kweli mnaitaka Imani
basi hoja zake zimekwisha thibiti.
9. Yeye ndiye anaye mteremshia Mtume wake Aya za Qur'ani zilizo
wazi, ili akutoeni kwenye upotovu mwende kwenye uwongofu. Na hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwingi wa upole kwenu, Mkunjufu wa rehema.
10. Na limekupateni nini hata hamtoi kwa ajili ya Njia ya
Mwenyezi Mungu katika mali yenu, na hali Mwenyezi Mungu ndiye wa kurithi mbingu
na ardhi? Yeye atarithi kila kiliomo humo, wala hatabaki yeyote mwenye chochote
humo. Hawawi sawa kwa cheo na malipo kati yenu, mwenye kutoa kabla ya kutekwa
Makka, na akapigana vita; na Uislamu unahitaji wa kuunga mkono na kuutilia
nguvu. Hao walio toa na wakapigana kabla ya Ushindi wana cheo cha juu zaidi
kuliko walio toa baada ya Ushindi (yaani kutekwa Mkka), na wakapigana. Na
makundi yote mawili hayo Mwenyezi Mungu ameyaahidi kuwapa malipo mema juu ya
kukhitalifiana vyeo vyao. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote myatendayo.
Kwa hivyo atamlipa kila mmoja kwa anavyo stahiki.
11. Ni nani Muumini anaye toa katika Njia ya Mwenyezi Mungu
kwa ikhlasi, ili Mwenyezi Mungu apate kumlipa malipo yake mardufu, na tena juu
ya hayo malipo mardufu apate malipo zaidi ya ukarimu Siku ya Kiyama?
12. Siku utapo waona Waumini wanaume na Waumini wanawake nuru
ya Imani yao na vitendo vyao vizuri inawatangulia mbele yao na kuliani kwao.
Malaika watawaambia: Furaha yenu hii leo ni kupata Bustani ambazo chini ya miti
yake inapita mito. Hamtatoka humo kabisa. Malipo hayo ndiyo kufuzu kukubwa kwenu
kulingana na vitendo vyenu.
13. Siku ambayo wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake watapo
waambia Waumini wanaume na wanawake: Hebu tungojeeni tupate nasi baadhi ya nuru
yenu. Wataambiwa kwa kuhiziwa: Rudini huko tuliko pewa nuru hii mkatake huko.
Basi baina ya Waumini na wanaafiki utasimamishwa ukuta wenye mlango. Ndani ya
ukuta upande wa Bustani itakuwapo rehema na neema. Na nje ya ukuta kunako elekea
Motoni upande huo kutakuwa na nakama na adhabu.
14. Wanaafiki watawaita Waumini: Kwani duniani hatukuwa pamoja
nanyi nasi ni wenzenu? Waumini waseme: Kwani! Mlikuwa kweli pamoja nasi, kama
msemavyo. Lakini nyinyi mmejiangamiza wenyewe kwa unaafiki, na mkawa mnatamani
Waumini yawapate masaibu ya kuwaangamiza, na mkatilia shaka mambo yote ya dini.
Na tamaa mbovu zikakukhadaini ya kwamba nyinyi mko katika neema, mpaka yakaja
mauti, na Shetani akakukhadaini kuwa bado mtapata msamaha kwa Mwenyezi Mungu na
maghfira yake. (Ghururi hiyo wanayo wanaafiki wengi walio dhulumu watu na
wakajidhulumu nafsi zao, wakawa wanadhani watasamehewa udhaalimu wao kwa kusali
kwingi na kuhiji, bila ya kujirekibisha nafsi zao na kurejesha haki za walio
wadhulumu.)
15. Basi leo hakitapokelewa chochote mtacho toa (enyi
wanaafiki) kuwa ni fidia ya kujikombolea nafsi zenu na adhabu, hata ikiwa kwa
thamani gani! Wala hakitapokelewa kitu kutokana na makafiri wenye kutangaza
ukafiri wao kuwa ni fidia kadhaalika. Marejeo yenu nyote ni Motoni, na hayo
ndiyo makaazi yenu yalio bora kwenu mnayo stahiki. Na uovu ulioje wa marejeo
hayo!
16. Je! Haujafika wakati kwa walio amini zikalainika nyoyo zao
kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu na Qur'ani tukufu, wala wasiwe kama walio pewa
Kitabu kabla yao, Mayahudi na Wakristo. Walitenda kwa mujibu wa Kitabu kwa muda,
lakini kwa kupita zama ndefu zikawa ngumu nyoyo zao, na wengi wao wakawa
wametoka katika mipaka ya dini yao.
17. Enyi Waumini! Jueni kwamba Mwenyezi Mungu anaitengeneza
ardhi na kuifanya isilihi kwa mimea kwa kuteremsha mvua baada ya kuyabisika
kwake. Na Sisi tumekuwekeeni wazi Ishara na tumekupigieni mifano ili mpate
kuzingatia katika hayo, na zinyenyekee nyoyo zenu kwa ajili ya kumdhukuru
Mwenyezi Mungu.
18. Hakika wanaume wanao toa sadaka, na wanawake wanao toa
sadaka, na wakatoa katika Sabilillahi, Njia ya Mwenyezi Mungu kwa ridhaa ya
nafsi zao, Mwenyezi Mungu atawazidishia thawabu zao mara mbili, na wao juu ya
kuzidishiwa kwao huko watapata ujira wa takrima Siku ya Kiyama.
19. Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala
wasibague baina yao yeyote, hao ndio Masidiqi (walio timia ukweli wao, kama
Sayyidna Abubakar na Bibi Maryam), na Mashahidi (walio kufa kwa ajili ya
Mwenyezi Mungu) kwa cheo na utukufu wa daraja. Siku ya Kiyama watakuwa na
thawabu na nuru kama thawabu na nuru za Masidiqi na Mashahidi. Na ambao
wamekufuru na wakakadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, hao ndio watu wa Motoni,
na wala hawatoki humo milele.
20. Enyi mlio danganyika na dunia! Jueni kuwa uhai wa dunia ni
mchezo usio leta faida, na pumbao la kumshughulisha mtu na yanayo mfaa, na pambo
lisio mleta utukufu wa maana, na kujitapa baina yenu kwa nasaba zenye kuondoka,
na mafupa yanayo oza, na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wa hayo
ni kama mfano wa mvua inayo wafurahisha wakulima kwa mimea yake; kisha ikisha
pevuka na kuiva, utaiona imegeuka manjano kwa kunyauka kwa ukame. Kisha mara
yanakuwa mabua makavu yanakatika katika. Hakibakii chochote chenye manufaa. Na
Akhera ipo adhabu kali kwa mwenye kuikhiari dunia na akaishika kwa isiyo kuwa
haki yake. Na pia yapo maghfira ya Mwenyezi Mungu kwa mwenye kukhiari Akhera
yake kuliko dunia yake. Na uhai wa dunia si chochote ila starehe ya udanganyifu
isiyo ya kweli kwa mwenye tumaini nayo na asiifanye kuwa ni njia tu ya
kutengenezea Akhera.
21. Nendeni upesi upesi kushindania kupata maghfira kwa Mola
wenu Mlezi, na kwendea Pepo ilio enea kotekote, upana wake kama upana wa mbingu
na ardhi, walio andaliwa wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Malipo
hayo makubwa ni fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye katika waja wake. Na
Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye fadhila iliyo tukuka hata akili haziwezi
kuielezea.
22. Haukuteremka msiba wowote duniani, ikiwa ni ukame, au
upungufu wa mazao, au mengineyo; wala katika nafsi zenu, ikiwa kwa maradhi, au
ufakiri, au mauti au mengineyo, ila huwa yamekwisha andikwa katika Lauhu
Mahfudh, Ubao Ulio hifadhiwa, na yamethibiti katika ujuzi wake Mwenyezi Mungu
kabla ya kutokeza duniani au katika nafsi zenu. Hakika kuthibitishwa misiba na
kujua ni mambo mepesi kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ujuzi wake umeenea kila kitu.
23. Tumekujuvyeni hayo ili msihuzunike kwa mnayo kuwa
hamyapati kwa huzuni ya kupita kiasi hata ikakutieni uchungu, wala msifurahie
kwa furaha ya kujitapa kwa anacho kupeni. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye
jivuna na akajifakhiri juu ya watu kwa alicho nacho.
24. Wale wanao fanya choyo na mali yao wasitoe katika
Sabilillahi, Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanawaamrisha watu wafanye ubakhili ati
kwa kuwa ndio wanawafanyia hisani; na mwenye kuacha kumt'ii Mwenyezi
Mungu, basi Mwenyezi Mungu mwenyewe hamhitajii huyo, naye ni Mwenye kustahiki
kuhimidiwa na kusifiwa.
25. Hakika tumewatuma Mitume wetu tulio wachagua kwa miujiza
ya kukata, na tukateremsha pamoja nao Kitabu chenye kukusanya hukumu na sharia
za Dini, na Mizani ya kuhakikisha insafu katika kuamiliana, ili watu wapate
kuamiliana baina yao kwa uadilifu. Na tumekiumba chuma ambacho kina mateso
makali katika vita, na manufaa kwa watu katika amani. Wanakitumia katika ufundi
ili kiwanufaishe katika maslaha yao na maisha yao. Na ili Mwenyezi Mungu amjue
anaye isaidia Dini yake, na anaye wasaidia Mitume wake kwa ghaibu, bila ya
kuwaona. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenyewe Muweza, hamhitajii mtu kumsaidia.
Chuma ni moja katika maadeni saba walizo kuwa wanazijua watu wa kale.
Nazo ni dhahabu, fedha, zaibaki, shaba, risasi, chuma na "tin". Na chuma ni
maadeni iliyo enea zaidi kuliko zote. Na katika asli yake hupatikana ya
kushikana na madda nyengine, kama kuwa ni Oxide, Sulfide, Carbonate,
Silicate. Na pia hupatikana kidogo chuma safi peke yake katika nyota za
mkia.
Aya hii inaashiria kwamba chuma kina nguvu nyingi na manufaa
kwa watu. Na hapana kinacho onyesha hayo kuliko kuwa chuma na namna zake mbali
mbali zinazo khitalifiana katika kustahamili moto, na kuvutwa, na kuingia kutu,
na kuchakaa, na kukubali kwake kutiwa smaku na mengineyo. Na kwa hivyo ndio
ikawa ndio maadeni inayo faa zaidi kuliko zote kwa kufanyia silaha za vita na
vyombo vyake, na kikawa ndio msingi wa uhunzi wote wa sanaa nzito na khafifu; na
kimekuwa ndio msingi wa maendeleo ya ustaarabu.
Na chuma kina manufaa
mengi katika vitu vyenye uhai. Kwani kinaingia katika kufanyika
Chlorophyll, na hiyo ni madda muhimu ya kimsingi katika kazi ya mimea kutumia
nguvu za jua katika kujenga protoplasm iliyo hai na kwa hivyo khatimaye huingia
katika mwili wa binaadamu na wanyama.
Chuma pia kinaingia katika
ujenzi wa Nuclear proteins (Chromatin), katika khalaya hai (living cells) kama
inavyo kutikana katika sawaili (liquids) za mwili pamoja na vitu vinginevyo.
Nacho chuma ni moja katika vitu vinavyo fanya Haemoglobin, madda muhimu katika
damu nyekundu, na inafanya kazi yake katika kuungua ndani ya mwili katika kuweza
kutumia chakula katika uhai. Chuma kinapatikana pia katika ini, na wengu, na
mafigo, na viungo, na ubongo wa mafupani. Mwili unahitaji chuma kwa kiasi
maalumu kwa mambo kadhaa wa kadhaa, na kikipunguka mwili hupata maradhi namna
mbali mbali, na muhimu katika hayo ni hayo yanayo ambiwa "upungufu wa damu",
anaemia.
26. Na hakika tulimtuma Nuhu na Ibrahimu, na tukajaalia
miongoni mwa vizazi vyao Unabii na Kitabu cha uwongofu. Basi baadhi ya wazao hao
wapo walio fuata njia ya uwongofu, na wengi wao wametokana na Njia Iliyo Nyooka.
27. Kisha tukafuatiliza kwenye nyayo za Nuhu na Ibrahimu na
walio watangulia hao au walio kuwa pamoja nao katika Mitume, Mtume baada ya
Mtume, na tukafuatiliza kwa kumleta Isa mwana wa Mariamu. Na tukamfunulia
Injili, na tukatia katika nyoyo za walio mfuata huruma nyingi, na upole, na
rehema.(1) Lakini kwa ziada katika ibada na kupita hadi katika kushika dini,
wakazua Umonaki, ut'awa wa kujitenga na ulimwengu na kuacha kuoana. Sisi
hatukawaamrisha hayo mwanzo. Lakini wao wameshika hayo kutafuta kumridhi
Mwenyezi Mungu Mtukufu. Lakini hawakuuhifadhi huo Umonaki kama inavyo stahiki
kuhifadhiwa. Basi tukawapa walio muamini Muhammad sehemu yao ya ujira na
thawabu. Na wengi wao wanamkadhibisha Muhammad, na wametoka nje ya ut'iifu na
Njia Iliyo Nyooka.
(1) (Injili aliyo funuliwa Nabii Isa A.S. na Mwenyezi
Mungu siyo hizi zinazo itwa Injili za Mathayo, Marko, Luka na Yohana ziliomo
katika Biblia. Injili hizo zinaambiwa kuwa zimeandikwa na hao walio tajwa, kwa
ufunuo wa Roho Mtakatifu, nafsi ya tatu ya Ungu kama wanavyo amini Wakristo.
Lakini kwa hakika wataalamu wachunguzi wa Biblia wanakubaliana kuwa watungaji
wake khasa hawajuulikani kweli. Yajuulikana kuwa ziliandikwa kwa miaka mingi
baada ya Nabii Isa na baada ya kufa wanafunzi wake wote. Juu ya Injili nne zilio
chaguliwa kutiwa katika Biblia na wakuu wa Kanisa katika karne yane baada ya
Yesu, zilikuwapo, na nyengine zingalipo, nyingi ambazo Kanisa la hivi sasa
halizikubali. Mfano wake ni kama Injili ya Barnaba, ya Tomasi na ya Uzawa
(Nativity), na kadhaa wa kadhaa nyenginezo. Lakini katika Injili zote utakuta
baadhi ya maneno ambayo yaonyesha ukweli wa Injili aliyo pewa Nabii Isa a.s. na
Mwenyezi Mungu. Katika Injili ya Marko 1.14-15 inasimuliwa: "Hata baada ya
Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akihubiri Habari Njema ya Mungu,
akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini
Injili." Injili gani hiyo kama sio ilio potezwa na Wakristo? Hizi tuzisomazo
zote zimeandikwa baada ya kwisha ondoka Yesu. Na hizi ni kama hadithi tu za
maisha ya Nabii Isa, kama ilivyo vitabu vya Maulidi kuwa ni masimulizi ya maisha
ya Nabii Muhammad.
Yamkini pia kuwa Injili ya Nabii Isa si kitabu
kilicho andikwa, bali ni yale mafunzo yake ambayo ni sehemu ya Kitabu cha
Mwenyezi Mungu kama ilivyo Qur'ani, ambayo imehifadhiwa katika Lauhun Mahfudh.
Qur'an iliitwa ni Kitabu kabla ya kuandikwa na watu na kusomwa, kwani uandishi
wake ulikwisha kuwa zamani katika Komputa ya Mwenyezi Mungu ya Lauhun Mahfudh
kwa maandishi ayajuayo Yeye Mwenyewe.)
28. Enyi mlio amini, iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu, na
thibitini juu ya kumuamini kwenu Mtume wake. Mwenyezi Mungu atakupeni mafungu
mawili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na nuru ya kukuongoeni, na
atakusameheni yaliyo kuporonyokeni katika madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mkunjufu wa maghfira, Mwenye rehema nyingi.
29. Mwenyezi Mungu anakupeni yote hayo ili wajue Watu wa Kitabu ambao hawakumuamini Muhammad ya kwamba hawana uweza wowote juu ya neema za Mwenyezi Mungu, wazipate wao au wampe mwenginewe. Na hakika fadhila zote zimo katika mikono ya Mwenyezi Mungu peke yake. Humpa amtakaye katika waja wake. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kubwa.