1,2.Arrah'man, Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema
amemfundisha mwanaadamu Qur'ani na akaifanya iwe nyepesi kwake kuisoma na
kuifahamu.
3,4. Yeye amemuumba mwanaadamu, na akamfunza
kubainisha, kudhihirisha yaliyo ndani ya nafsi yake, kinyume na makhaluku
wenginewe.
5. Na jua na mwezi zinakwenda katika njia zake za mbinguni kwa
mujibu wa hisabu na vipimo visio kwenda pogo.
Aya hii tukufu inataja
mwendo wa jua na mwezi kwa kufuata nidhamu madhubuti tangu Mwenyezi Mungu
Mtukufu alipo umba. Wala haukujuulikana mpango huu madhubuti ila karibuni, kiasi
ya miaka 300 iliyo pita. Hapo ndipo ilipo dhihiri kuwa mwendo wa jua kama unavyo
onekana kuzunguka ardhi, na mwezi kuzunguka ardhi, nyendo hizo zinatimia kwa
vipimo vya falaki kufuata kanuni za mvuto. Na hizo ni hisabu za ndani kabisa, na
khasa kwa mintarafu ya mwezi.
6. Na mimea isiyo na vigogo, na miti inayo simama juu ya vigogo
vyake, yote hiyo inamt'ii na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kila
alitakalo kwao.
7,8. Na mbingu ameziumba kwa kuziweka juu, na akaweka
uadilifu ili mipaka isikiukwe.
9. Na wekeni mizani kwa uadilifu katika kila muamala wenu, wala
msipunguze mizani.
10. Na ardhi ameikunjua na amewatandikia viumbe wanafiike
kwayo.
11. Katika ardhi yapo matunda ya namna nyingi, na imo mitende
ambayo ina mafumba ambayo ndani yake ndio imo thamra ya hizo tende.
12. Na katika ardhi zipo nafaka zenye makapi. Hiyo ni riziki
yenu na wanyama wenu. Na humo pia ipo mimea yenye harufu nzuri nzuri.
13. Neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi ambayo nyinyi,
makundi mawili, watu na majini, mnaikataa?
14,15. Ameumba jinsi ya kiutu kwa udongo mkavu usio
chomwa kama wa vyungu. Na ameumba jinsi ya kijini kutokana na ndimi za moto.
16. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi ambayo
mnaikataa?
17. Mola Mlezi wa matokeo mawili ya jua, na Mola Mlezi wa
machwea jua mawili.
Yaweza kuwa hapa makusudio yake ni matokea mawili ya
jua na mwezi, na machwea mawili ya jua na mwezi. Na hivyo inaashiriwa muujiza wa
usiku na muujiza wa mchana. Tazama pia maoni ya wataalamu juu ya Aya 71, 72, na
73 katika Sura Al Qas'as' inayo anzia kwa kauli yake Mtukufu: "Sema: Mwaonaje
kama Mwenyezi Mungu akiufanya usiku ukukalieni moja kwa moja mpaka siku ya
Kiyama.."
Na yafaa pia kuwa Aya hiyo inaashiria jua peke yake, nalo
ndilo tegemeo la maisha katika sayari hii ya ardhi, na hapo makusudio yake ni
kuchomoza na kuchwa kwake siku za baridi, na kuchomoza na kuchwa kwake siku za
joto. Na hivyo ndivyo walivyo fasiri wengi.
Kuonekana huku ni kwa
sababu ya kuinama msumari-kati wa mzunguko wa ardhi kwa mnasaba wa kulizunguka
jua kwa kiasi ya daraja 523.5. Kwa hivyo nusu ya kaskazini ya dunia, kwa
mfano inainamia upande wa jua wakati wa joto, basi mchana huwa mrefu na usiku
huwa mfupi mpaka ufikiliwe mwisho wake. Hapo jua huchomoza mwisho wa umbali
kaskazini, na huchwa hivyo vile vile. Kisha jua huanza kurejea kusini kidogo
kidogo kila siku mpaka lifike kati ya dunia na mashariki na magharibi ya kweli.
Tena nusu hii ya kaskazini huzidi kuinama na kuliacha jua, na usiku huwa mrefu
na mchana ukawa mfupi, na kuonekana jua linaendelea kusini zaidi mpaka kufikia
ukomo wa kusini, na kisha hurejea tena kaskazini siku baada ya siku mpaka lifike
katikati tena kwenye mashariki na magharibi ya kweli kweli. Sehemu ya kusini ya
dunia inakuwa kinyume cha hivyo. Na haya yanayo onekana huzidi kudhihiri
kila ukenda kaskazini zaidi, na kusini zaidi. Na hapana shaka kuwa mpango huu wa
hikima ni kwa maslaha ya hali za maisha juu ya dunia, kwani kutokana na hayo
ndio inapatikana misimu mbali mbali na kwa hivyo miongo ya ukulima na
kuvuna, na mambo yote yanayo onekana katika maisha ya wanyama na mimea.
18. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
19,20. Mwenyezi Mungu anazipeleka bahari mbili, ya
maji matamu na maji ya chumvi, yanakaribiana bali yanagusana khasa juu yao.
Lakini baina yao kipo kizuizi kwa kudra ya Mwenyezi Mungu, kinacho zuia
yasichanganyikane.
21. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
22. Humo hutoka lulu na marijani mnazo zifanya kuwa ni pambo
la
kulivaa.
Tazama maoni ya wataalamu juu ya Aya 12 katika Sura
Faat'ir. (35:12)
23. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
24. Na yake Yeye majahazi yaliyo undwa kwa mikono yenu, yanayo
kwenda baharini, makubwa yamenyanyuka juu kama vilima.
25. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
26,27. Kila kilioko juu ya ardhi kitaondoka, na
atakabakia Mwenyezi Mungu tu, Mwenye utukufu na kuneemesha.
28. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
29. Wote waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi
wanamwomba haja zao Mwenyezi Mungu. Kila wakati Yeye yumo katika jambo, hutukuza
na huangusha, hutoa na hunyima.
30. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
31. Tutakushughulikieni kwa kukusudia kukuhisabieni, enyi
majini na watu Siku ya Kiyama.
32. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
33. Enyi makundi ya majini na watu! Ikiwa mnaweza kutoka
pembezoni mwa mbingu na ardhi kwa kukimbia, basi haya tokeni! Lakini hamwezi
kutoka ila kwa nguvu na kahari; na hayo hamna uwezo nayo!
Mpaka sasa
imethibitika kuwa inahitaji juhudi kubwa mno na nguvu hata kuweza kutokana na
mvuto wa ardhi kwa kwendea huko nje ya anga na mvuto, na kupatikana baadhi ya
kufuzu kulikagua anga. Ni kwa muda mchache sana kwa kulinganisha na ukubwa
wa ulimwengu, ndio imetumiwa juhudi kubwa ya wataalamu wa sayansi katika
sehemu mbali mbali za uhandisi, na hisabu, na ufundi, na ilimu za jiolojia,
mbali na chungu ya mali yaliyo tumiwa na bado yangali yanatumiwa kwa jambo hilo.
Na hayo yanaonyesha kwa dalili ya kukuta kuwa kuweza kuingilia maridhawa
katika mbingu na ardhi, ambayo yanafika mamilioni ya miaka ya mwangaza, ni
muhali kwa watu na majini.
34. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
35. Mtamiminiwa ndimi za moto na shaba iliyo yayushwa, basi
hamtaweza kujilinda na adhabu hiyo.
Shaba inakubaliwa kuwa ni katika
maadeni za mwanzo kujuulikana na binaadamu tangu zama za zamani, na inasifika
kuwa daraja yake ya kuyayuka iko juu sana, kiasi ya daraja 1083 za Centigrade.
Basi ikimiminwa maadeni hii iliyo yayuka juu ya mwili wa mtu, ndio inafananishwa
na adhabu iliyo kuu, na uchungu mkali.
36. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
37. Siku itapo pasuka mbingu ikawa nyekundu iliyo tibuka kama
mafuta yanayo ungua.
38. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
39. Basi siku itapo pasuka mbingu, siku hiyo haulizwi mtu wala
jini dhambi zake.
40. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
41. Wakosefu miongoni mwa watu na majini watajuulikana kwa
alama za kuwatambulisha. Basi watakamatwa washikwe kwa nywele za utosi na kwa
miguu watumbukizwe katika Jahannamu!
42. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
43,44. Wataambiwa kwa kuwashitua: Hii ndiyo
Jahannamu waliyo kuwa wakiikadhibisha wakosefu miongoni mwenu. Watakuwa
wakizunguka baina ya moto na maji ya ukomo wa kuchemka.
45. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
46. Na mwenye kukhofu uweza wa Mola wake Mlezi atakuwa nazo
Bustani mbili.
47. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
48. Bustani hizo zina matawi ya kufurahisha mazuri.
49. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
50. Katika Bustani hizo mtakuwa na chemchem zinazo pita maji
kama wapendavyo.
51. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
52. Humo mtakuwa namna mbili ya kila matunda.
53. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
54. Wametegemea na kutua juu ya matandiko ambayo bit'ana yao
ni ya at'ilasi, hariri nzito; na matunda ya hizo Bustani mbili yatakuwa karibu
kwa mwenye kuyachuma.
55. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
56. Katika hizo Bustani watakuwamo wake wenye kuhifadhi macho
yao hawawaangalii ila waume zao tu, walio bikra hawajakaribiwa kabla yao na mtu
wala jini.
57. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
58. Wanawake hao kwa uzuri wao na usafi wao wa rangi ni kama
yakuti na marijani.
59. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
60. Malipo ya vitendo vyema hayawezi kuwa ila kwa thawabu
njema.
61. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
62. Na mbali ya Bustani hizo zilizo kwisha tajwa, zipo mbili
nyenginezo.
63. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
64. Za kijani, iliyo koza mno rangi yake hata ikawa inaingia
katika weusi.
65. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
66. Ndani humo zimo chemchem mbili zinazo furika maji yasiyo
katika.
67. Basi neema ipi katika neeema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
68. Humo itakuwamo miti ya matunda mbali mbali, na mitende, na
mikomamanga. (mikudhumani).
Huenda huku kutajwa khasa tende na komamanga
kwa kuwa ni matunda bora kuliko mengineyo kama zilivyo thibiti kwa mujibu wa
wataalamu.
Kwa kuchambuliwa tende kwa ujuzi wa kimyaa imeonakana kuwa
ina sukari 75 katika mia takriban, na aghlabu yake ni sukari ya miwa. Na vile
vile zimo sukari zilio geuka (yaani sukari ya matunda Fructose na sukari ya
zabibu Glucose) Nayo ni nyepesi kuungua katika mwili, na kwa hivyo humpa mtu
nishat'i ya kufanya kazi vizuri viungo na kuupa mwili joto. Na pengine labda
ndiyo hikima ya Mwenyezi Mungu kumuamrisha Mariamu ale tende ili arejeshe nguvu
zake baada ya machungu ya kuzaa. Mbali na hayo, tende inayo sehemu kubwa katika
Calcium (chokaa), na chuma, na fosfori (Phospohorus), ambazo mwili unahitajia.
Na imo pia kiasi maalumu ya Nicotinic acid, ambayo ni vitamini ya kulinda
maradhi ya Pelagra, na vitamini A na B. Na zimo pia Protein na mafuta. Na vitu
hivi vinaifanya tende kuwa ni chakula chenye manufaa ya kukamilika.
Ama komamanga (au kudhumani kwa Kiswahili cha kaskazini) imo katika kokwa
zake au maji yake sehemu kubwa (ukilinganisha na matunda mengineyo) ya Lemonic
acid ambayo inasaidia inapo ungua katika mwili kupunguza athari ya ukali acidity
au "humudha", katika mkojo na damu inayo sabibisha kuepukana na maradhi ya
Naqras, au gout (kuumwa viungo aghlabu kidole gumba cha mguu), na kufanyika mawe
katika mafigo. Juu ya hayo katika maji ya komamanga zimo sukari namna mbali
mbali si haba (11 katika mia) zilizo nyepesi kuungua, na zenye kuleta nishat'i
ya kufanyia kazi. Kadhaalika maganda ya komamanga yana maada ya kukausha ya
kuzuia kuhara Tannin inayo linda matumbo madogo (chango) na yanayo yasibu wakati
wa kuwa na maradhi ya kuhara. Kadhaalika maganda ya komamanga hutumika kuuwa
minyoo, michango
69. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
70. Humo watakuwamo wake wenye tabia njema, wenye nyuso za
kupendeza.
71. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
72. Wazuri wa macho, wenye kutawishwa ndani ya makhema yao.
73. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
74. Hawajakaribiwa na mtu wala jini kabla ya waume wao.
75. Basi neema ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
76. Wameegemea juu ya viti vya enzi vyenye makava ya kijani na
mazulia mazuri mazuri yaliyo fanywa kwa ufundi wa ajabu.
77. Basi neema ipi katika neemza za Mola wenu Mlezi mnayo
ikataa?
78. Limetakasika jina la Mola wako Mlezi Mwenye utukufu na wingi wa neema.