1,2. Ninaapa kwa nyota inapo tua kwa kuchwa, ya
kwamba Muhammad hakuiacha Njia iliyo sawa ya kufuata Haki, na wala hakupata
kuitakidi upotovu.
3. Wala halitoki katika anayo yatamka ya Qur'ani kwa mapendo ya
nafsi yake.
4. Hii Qur'ani anayo itamka si chochote ila ni Wahyi (Ufunuo)
ulio toka kwa Mwenyezi Mungu anamfunulia yeye.
5. Aliye mfundisha ufunuo huu ni mwenye nguvu nyingi.
6,7. Ambaye ametua akili zake na maoni yake,
akasimama sawa sawa katika sura yake; naye yuko upande wa juu katika mbingu upeo
wa macho wa mwenye kuangalia.
8,9. Kisha Jibrili alimkaribia, na akazidi kukaribia,
hata akawa ukaribu wake ni kiasi ya mipinde miwili, bali karibu kuliko hivyo.
10. Jibrili akamfunulia mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
alicho mfunulia, nao ufunuo huo ni jambo lenye shani kubwa na athari ya mbali
kabisa.
11. Moyo wa Muhammad haukukanya yale macho yake yaliyo yaona.
12. Hivyo nyinyi mnamkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu na
mnabishana naye kwa aliyo yaona kwa macho yake?
13,14,15,16,17. Na
bila ya shaka Muhammad alimwona Jibrili kwa sura yake mara nyengine, katika
pahala pasipo juulikana ila na Mwenyezi Mungu tu, ambapo amepaita Sidratul
muntahaa, "Mkunazi wa Mwisho". Na akasimulia kuwa hapo ndio ipo Jannatul Ma-awa,
Bustani inayo kaliwa. Vikafunikwa na kuzibwa, kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu,
visio weza kuelezwa. Jicho la Muhammad halikubabaika kwa aliyo yaona, na wala
hakukiuka mpaka ya aliyo amrishwa kwa kuona kwake huko.
18. Hakika ameona mengi katika Ishara za Mwenyezi Mungu na
maajabu yake makubwa makubwa.
19,20. Je! Mmeyajua hayo, na mkayafikiri ya kina
Lata na Uzza na Manata, huyo mwengine wa tatu, mlio wafanya kuwa ni miungu wa
kuwaabudu?
21. Mkagawa, nyinyi muwe na watoto wa kiume, na mkamfanyia
Mwenyezi Mungu awe na watoto wa kike!
22. Huo basi ni ugawaji wa dhulma, mnamgawia Mwenyezi Mungu
kile mnacho kichukia nyinyi wenyewe!
23. Hayo masanamu yenu si chochote ila ni majina tu yasiyo na
maana yoyote ya kiungu. Mmeyatunga nyinyi na baba zenu kwa kufuata pumbao lenu
la upotovu. Mwenyezi Mungu hakuteremsha nayo hoja yoyote ya kusadikisha huo
uzushi wenu mnao wadaia. Na hawa hawafuati ila ni dhana tu, na kipendacho nyoyo
zao zilio potoka na kuacha maumbile yaliyo sawa. Na hakika yalikwisha wajia
kutoka kwa Mola wao Mlezi yenye uwongofu, laiti wangeli ufuata huo!
24,25. Mwanaadamu hapati kila anacho kitamani, ya
kupata uombezi wa haya masanamu au mengineyo anayo yatamani kwa nafsi yake.
Kwani mambo yote, ya duniani na Akhera, ni ya Mwenyezi Mungu peke yake.
26. Na malaika wengi wa mbinguni, juu ya ubora wa vyeo vyao,
haufai kitu uombezi wao isipo kuwa baada ya kupewa idhini huyo mwombezi na
Mwenyewe Mtukufu, na kumridhia huyo mwenye kuombewa.
27. Hakika hao wasio iamini Akhera ndio bila ya shaka wanao
sema kuwa Malaika ni wanawake. Wanasema: Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu!
28. Na kwa kauli hii hawana ujuzi wowote. Hawafuati kitu ila
dhana zao tu zilio potoka, na dhana haifai kitu mbele ya haki.
29. Basi jitenge nao hao makafiri walio ipuuza Qur'ani na
ikawa hamu yao si chochote ila uhai wa duniani tu, wakiyakataa yenye maslaha
nao.
30. Hayo wanayo yafuata katika itikadi zao, na vitendo vyao
ndio ukomo walio yafikilia katika ilimu. Hakika Mola wako Mlezi anamjua vyema
anaye shikilia upotovu, na anamjua vyema aliye elekea kupokea uwongofu.
31. Na ni vya Mwenyezi Mungu pekee vyote viliomo katika mbingu
na ardhi, kwa kuviumba na kuvidabiri, ili awalipe walio potea wenye kufanya
viovu vitendo vyao, na awalipe walio hidika watu wema kwa malipo yaliyo mema.
32. Wema hao ndio wale wanao jitenga na madhambi yenye adhabu
kubwa kubwa, na yanayo chukiza mno. Lakini Mwenyezi Mungu husamehe dhambi ndogo
ndogo. Hakika Mola wako Mlezi ni Mkuu wa kughufiria, naye anajua vyema hali
zenu. Kwani Yeye ndiye aliye kuumbeni kutokana na ardhi, na mlipo kuwa mimba
matumboni mwa mama zenu katika hali zenu mbali mbali za kukua na kugeuka. Basi
msikae mkijisifu nafsi zenu kuwa mmesafika kwa kujigamba na kujifakhari. Na Yeye
ndiye Mjuzi mkubwa kabisa wa kila mwenye kumcha na akajisafisha nafsi yake kweli
kweli kwa uchamngu wake.
33,34,35. Je! Umezingatia ukamwona anaye
puuza kuifuata Haki, na akatoa kidogo katika mali, na khalafu akakata kabisa
kutoa? Je! Huyo anayo ilimu ya kujua mambo ya ghaibu, basi kwa hivyo ndio
anayajua yanayo mpelekea kuiacha kuifuata Haki, na akafanya ubakhili wa mali?
36,37,38. Kwani huyo hakuambiwa yaliomo
katika Vitabu vya Musa na Ibrahim, aliye fika ukomo wa kutimiza aliyo agana na
Mwenyezi Mungu, ya kwamba hapana mtu ataye mbebea dhambi mwenginewe?
39. Na kwamba mtu hapati ila malipo ya vitendo vyake mwenyewe.
40. Na kwamba vitendo vyake vitakuja tangazwa, na ataviona
Siku ya Kiyama, iwe ni kumtukuza mtenda mema, na kumkebehi mtenda maovu.
41. Kisha kila mtu atalipwa malipo anayo stahiki.
42. Na kwamba kwa hakika ni kwa Mola wako Mlezi, wala si kwa
mwenginewe, ndio miadi ya kurejea.
43. Na Yeye peke yake ni Mwenye uweza wa kuufanya uso uonyeshe
furaha au maudhiko, na pia ni Mwenye kuziumba sababu za starehe na dhiki.
44. Na hakika ni Yeye, ndiye Mwenye kuondoa uhai, na kuuleta.
45,46. Na Yeye ndiye aliye umba vitu kwa jozi,
yaani dume na jike, binaadamu na wanyama, kutokana na manii yanayo miminwa.
Makusudio ya Aya hii tukufu ni kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu
kwamba Yeye ameumba waume na wake katika wanaadamu na wanyama wote kutokana na
tone ya manii ambayo humo humo mna ume na uke. Na juu ya udogo wake na udhaifu
wake ndio chemchem ya uhai. Umuujiza wa Qur'ani unadhihirika katika Aya hii
tukufu ukikumbuka kuwa ulimwengu ulikuwa haujui mpaka hivi karibu kuwa katika
maji ya mwanamume ndio zimo mbegu "sperms" na katika maji ya mwanamke mna
vijiyai "ova", ndio vikikutana vijidudu vya manii ya mwanamume na vijiyai vya
mwanamke vikawa kitu kimoja ndio hiyo huwa mimba. Ukweli huu ulitajwa na
Qur'ani kabla ya kuvumbuliwa na ilimu za Sayansi.
47. Na juu yake Yeye ndio kufufua baada ya kifo.
48. Na Yeye ndiye anaye toa kinacho tosheleza, na akaridhisha
kwa kinacho kinaisha na cha kuweka akiba.
49. Na hakika Yeye ndiye Mola Mlezi wa hii nyota kubwa inayo
itwa Shii'ra (Sirius, Dog Star).
Makusudio hapa ni Nyota hiyo inayo itwa
Ash-shi'ra Alyamaaniya, au wanavyo ita Wazungu Sirius au Dog Star. Nyota hii
inang'ara kwa nguvu zaidi kuliko nyota zote ziliomo katika kikundi cha nyota
kinacho itwa Alkalbu l-akbar, kwa Kizungu Canis Major au Greater Dog. Nyota hiyo
ndiyo inayo zagaa sana mbinguni, na huonekana kusini ya mstari wa kati wa
mbinguni kiasi ya daraja 18. Na kwa jina hilo la Nyota ya Mbwa ikijuulikana hata
miaka elfu tatu ilio pita. Katika mabaki ya michoro ya Mafirauni wa Misri
imeashiriwa pia. Mwenyezi Mungu ameitaja khasa kwa kuwa Waarabu walikuwa
wakiiabudu hapo kale, na pia Wamisri wa zamani, kwani kutokea kwake upande wa
mashariki katikati ya mwezi wa Julai kabla ya kuchomoza jua kulikuwa
kunawafikiana na wakati wa mafuriko ya Misri ya kati, yaani katika tukio muhimu
kabisa katika ulimwengu huo wa kale. Na tukio hili huenda ndilo lilio fanya
kuanzisha kuwekea kiwango urefu wa mwaka katika dunia nzima. Kwani kudhihiri
Nyota ya Shiira kabla ya kuchomoza jua hakutokei ila mara moja tu katika mwaka.
Basi huu ndio mwanzo wa mwaka mpya.
50,51. Na Yeye ndiye aliye wateketeza kina A'di wa
mwanzo, kaumu ya Nabii Hudi. Na akawateketeza Thamudi, kaumu ya Nabii Saleh.
Hakuwabakisha.
52. Na aliwaangamiza kaumu ya Nuhu kabla ya kuwaangamiza A'di
na Thamudi. Hakika hao walikuwa wamekithiri kudhulumu, na wamezidi kwa uasi
kuliko A'di na Thamudi.
53. Na miji ya kaumu Lut'i iliyo pinduliwa juu chini, ni Yeye
Mwenyezi Mungu ndiye aliye ipindua.
54,55. Akaizunguka kwa kuiadhibu kama alivyo
izunguka. Basi katika neema za Mola wako Mlezi una shaka nayo ipi?
56. Hii Qur'ani ni onyo katika jinsi ya yale yale maonyo ya
kale waliyo onywa kwayo watu walio tangulia.
57,58. Kiyama kimekaribia; na wala hapana wa
kuujuulisha wakati kitapo tokea ila mwenyewe Mwenyezi Mungu.
59,60,61. Hivyo nyinyi mnapinga
kila la kweli? Na mnaistaajabia kwa kuikaataa hii Qur'ani? Na mnacheka kwa
kejeli na maskhaara, wala hamlii kama wafanyavyo wenye yakini, nanyi mmo katika
pumbao na kutakabari?
62. Basi msujudieni Mwenyezi Mungu aliye iteremsha Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu wote, na muabuduni Yeye tu peke yake Mwenye kutukuka kwa utukufu wake.