1. Imeanzia
Sura hii kwa baadhi ya harufi kama ilivyo ada ya Qur'ani katika Sura kadhaa wa
kadhaa.
2. Hii Qur'ani
imeteremka kutokana na Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima
katika ayatendayo.
3. Hatukuziumba
mbingu na ardhi na vyote vilio baina yake ila kufuatana na sharia zilizo
thibiti, kwa makusudio yanayo ambatana na hikima, na kwa muda maalumu ambao
baada yake utakwisha. Na wale wanao ukataa ukweli huu wanapuuza yale waliyo
onywa kwayo, ya kuumbwa kupya siku watakapo fufuliwa watu kwa ajili ya malipo.
4. Waambie hao
wanao muomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu: Hebu nambieni hali ya hao mnao waomba
badala ya Mwenyezi Mungu. Nijuvyeni wameumba nini katika ardhi, au wana ushirika
wowote katika mbingu? Nileteeni Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, au mabaki
yoyote kutokana na ilimu za watu wa zamani ambayo mnayategemea kwa madai yenu,
ikiwa mnasema kweli.
5. Na nani
aliye zidi kupotea kuliko anaye muacha Mwenyezi Mungu akaiomba miungu mingine
ambayo haitamjibu kitu mpaka mwisho wa dunia, na ambao hao hata hawana khabari
ya maombi yao.
6. Na watu
wakikusanywa kwa ajili ya hisabu Siku ya Kiyama hawa wanao abudiwa kwa upotovu
watakuwa ndio maadui wa walio kuwa wakiabudu, na watajitenga nao, na
kuwakadhibisha kwa madai yao kwamba wao wanastahiki kuabudiwa. (Katika Injili ya
Mathayo inasimuliwa wazi vipi Nabii Isa a.s. atavyo wakataa Wakristo wanao
muabudu yeye. Tazama Mathayo 7.22-23. Yesu anasema: "Wengi wataniambia siku ile,
Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na
kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi
kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.")
7. Na
washirikina wakisomewa Aya zetu zilizo wazi wao husema, kwa ule ukafiri wao na
inadi yao, bila ya kuzingatia, kuzisema hizo Aya: Huu ni uchawi dhaahiri!
8. Bali
wanasema hawa makafiri: Muhammad ameizua hii na akamsingizia Mwenyezi Mungu!
Sema kuwajibu: Ikiwa mimi nimeizua hii Mwenyezi Mungu atanipatiliza upesi upesi,
wala nyinyi hamwezi kunilinda hata kwa chembe ya adhabu. Yeye peke yake ndiye
Mwenye kujua kabisa hayo mnayo ropokwa katika kuzitia kombo Aya zake. Na Yeye
anatosha kunishuhudia ukweli wangu, na kukushuhudilieni nyinyi kuwa
mnanikadhibisha. Na Yeye pekee, ndiye Mkunjufu wa msamaha kwa mwenye kutubu,
Mkubwa wa rehema, kwa kuwapa muhula wenye kuasi ili wadiriki kurejea.
9. Waambie:
Mimi sikuwa Mtume wa mwanzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hata ndio muukatae ujumbe
wangu. Wala mimi sijui Mwenyezi Mungu atanifanya nini na atakufanyeni nini
nyinyi. Mimi sifuati ninayo sema au kutenda ila anayo nifunulia Mwenyezi Mungu.
Wala mimi si chochote ila ni mwonyaji miongoni mwa waonyaji.
10. Sema: Hebu
nambieni, ikiwa hii Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu na nyinyi mkaikataa, na
hali ameshuhudia shahidi katika Wana wa Israili kuwa imeshuka mfano wa hii
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, akawa yeye kaamini na nyinyi mkatakabari, basi hapo
nyinyi si mtakuwa ni wenye kupotea na wenye kujidhulumu wenyewe kuliko watu
wote? Hakika Mwenyezi Mungu hamsaidii kuongoka mwenye kujidhulumu mwenyewe na
akapanda kiburi kuikataa Haki.
11. Na walio
kufuru walisema kuwakhusu walio amini, kwa kejeli na majivuno juu yao: Ingeli
kuwa aliyo kuja nayo Muhammad ni ya kheri, basi wasingeli tutangulia hawa katika
kuyaamini. Kwani sisi ndio twenye ubwana, na akili bora! Na ilivyo kuwa
hawakuyafuata basi wakaangukia kuyatoa kombo, wakisema: Huu ni uwongo wa zamani
unatokana na hadithi za watu wa kale!
12. Na kabla
ya Qur'ani Mwenyezi Mungu aliteremsha Taurati kuwa ni uwongozi na rehema kwa
wenye kuitenda. Na hii Qur'ani wanayo ikadhibisha inasadikisha Vitabu vilivyo
kwisha tangulia. Mwenyezi Mungu ameiteremsha kwa lugha ya Kiarabu iwe ni onyo
jipya kwa wenye kudhulumu, na bishara kwa wenye kusimama sawa juu ya Njia.
13. Hakika
wanao sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu peke yake, kisha wakatengenea kwa
kufanya vitendo vizuri, watu hao hawana khofu ya kushukiwa la karaha, na wala
hawatahuzunika kwa kuyakosa wayatakayo.
14. Hao wanao
sifika kwa kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, na kusimama sawa, ndio walio khusika
kuingia Peponi wakikaa humo milele. Mwenyezi Mungu amewapa hayo kuwa ni jaza yao
kwa mema waliyo kuwa wakiyatenda.
15. Na
tumemuusia mwanaadamu kwa wazazi wake awafanyie wema mkubwa. Kwani mama yake
amechukua mimba yake kwa mashaka, na akamzaa kwa mashaka. Na muda wa kuchukuliwa
mimba mpaka kuachishwa ziwa ni miezi thalathini. Muda wote huo mama kapitikiwa
na kila namna ya machungu. Mpaka huyo mtu alipo fikilia ukamilifu wa nguvu zake
na akili yake, na akafikia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Nijaalie
niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nijaalie nitende
vitendo vyema utavyo viridhi Wewe, na ujaalie huo wema wapate pia dhuriya zangu.
Hakika mimi nimetubu kwako kwa kila dhambi, na mimi ni miongoni wa Waislamu,
yaani walio zisalimisha nafsi zao kwako. Uchache wa mimba ni miezi sita, kwa
kauli yake Mtukufu: " Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi
thalathini." Na kauli yake Mtukufu: "Na kumwachisha ziwa kwake ni miaka miwili",
na kauli yake Mtukufu: "Na wazazi wa kike huwanyonyesha wana wao miaka miwili
kaamili, kwa mwenye kutaka kutimiza kunyonyesha." Basi ukitoa muda wa kuachisha
ziwa kutokana na muda wa mimba na kunyonyesha inabakia muda wa mimba ni miezi
sita. Na haya yanawafikiana na iliyo thibiti kwa ilimu za sayansi kwamba mtoto
mchanga akizaliwa baada ya mimba ya miezi 6 anaweza kuishi.
16. Hao walio
sifika kwa sifa hizo ndio tutakao wapokelea a'mali zao njema, na tutawasamehe
maovu yao miongoni mwa watu wa Peponi. Itawathibitikia miadi ya kweli walio kuwa
wakiahidiwa duniani.
17. Na
waliwafyonya wazazi wao kwa kuchukia na kuchoka nao, walipo wataka waamini
kufufuliwa, na wakawaambia: Mnaniambia tutatoka makaburini na mataifa mangapi
yamepita kabla yangu na hapana hata mmoja aliye fufuliwa kutoka makaburini? Na
hao wazazi wake wanaomba msaada kwa Mwenyezi Mungu jinsi ya kuona ni makuu
makosa ya mwana wao, wakisema kwa kumshikilia aamini: Utaangamia wewe kama
hukuamini. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kufufua ni kweli. Naye bado
amekakamia kukadhibisha kwa kusema: Hayo mnayo yasema si chochote ila ni hadithi
za uwongo za watu wa kale!
18. Hao
wasemao hayo ndio iliyo wathibitikia kuwashukia adhabu sawa sawa na mataifa
yaliyo kuwa kabla yao miongoni mwa majini na watu, kwa sababu hakika hao
walikuwa ni wenye kukhasiri.
19. Na wote,
Waislamu na makafiri, wana vyeo vyao vinavyo lingana na vitendo vyao walivyo
vitenda, ili uadilifu wa Mwenyezi Mungu upate kuonekana kati yao, na ili awalipe
jaza ya 'amali zao, nao hawatadhulumiwa, kwa sababu wanastahiki hayo wanayo
lipwa.
20. Na siku
watakapo simamishwa walio kufuru kwenye Moto waambiwe: Mmekwisha chukua fungu
lenu la vitu vizuri katika maisha yenu ya duniani, na mkavionea raha. Basi leo
ndio mnalipwa adhabu ya kufedhehesha kwa mliyo kuwa nayo duniani, ya kujivuna
katika nchi bila ya haki, na kutoka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
21. Mtaje Hud,
mwenzao kabila ya A'di, alipo wahadharisha watu wake wanao kaa Ah'qaaf, kwenye
vilima vya mchanga. Na Mitume kadhaa walikuja kabla yake na baada yake kwa
maonyo kama yake ya kusema: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu. Mimi nakukhofieni
isikupateni adhabu yenye vitisho vikuu. Maskani ya kabila hii ilikuwa huko
Ah'qaaf, kwenye vilima vya mchanga. Na wapi hapo Ah'qaaf? Zipo khitilafu. Baadhi
ya wanazuoni wa taarikh (historia) wanasema kuwa hapo ni baina ya Yaman na Oman
mpaka Hadhramaut na Shihr, yaani mashariki ya kusini ya Bara Arabu. Na baadhi ya
wachunguzi wa zama za karibu wanaona ni mashariki ya A'qaba, wakitegemea
maandishi ya Nabat'ia waliyo yakuta katika magofu ya hekalu walilo livumbua
katika mlima wa Arim. Walikuta pembezoni mwa mlima huo mabaki ya siku za
Jahiliya za zamani. Wakasahihisha kuwa hapo ndipo ilipo Arim iliyo tajwa katika
Qur'ani tukufu. Kisha kabila hiyo ikatoka hapo kabla ya Uislamu, na hapana
kilicho baki chao isipo kuwa chemchem ya maji ambayo wafanyi biashara na watu wa
misafara wakishukia hapo katika njia yao kwendea Shamu.
22. Kaumu ya
Hud walisema kwa kumkanya: Hivyo ndio umetujia ili utuachishe kuwaabudu miungu
yetu? Basi tuletee hiyo adhabu ikiwa wewe hakika ni mwenye kusema kweli kwa
ahadi hiyo.
23. Hud
akasema: Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kujua wakati wa kuileta adhabu
yenu. Mimi nafikisha ujumbe tu nilio tumwa. Lakini naona kuwa nyinyi hamjui
chochote katika mambo wanayo tumwa Mitume.
24,25.
Ikawajia adhabu kwa sura ya wingu. Walipo liona limetanda kote juu linaelekea
mabondeni kwao, walisema kwa furaha: Wingu hili linatuletea mvua na kheri.
Wakaambiwa: Bali hilo ni hayo mliyo yahimiza, nayo ni upepo wenye adhabu kali na
chungu, itakayo teketeza kila kitu kwa amri ya Muumbaji wake. Nao ukawaangamiza,
yasionekane mabaki yao isipo kuwa nyumba zao. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila
mwenye kutenda kama makosa yao.
24,25.
Ikawajia adhabu kwa sura ya wingu. Walipo liona limetanda kote juu linaelekea
mabondeni kwao, walisema kwa furaha: Wingu hili linatuletea mvua na kheri.
Wakaambiwa: Bali hilo ni hayo mliyo yahimiza, nayo ni upepo wenye adhabu kali na
chungu, itakayo teketeza kila kitu kwa amri ya Muumbaji wake. Nao ukawaangamiza,
yasionekane mabaki yao isipo kuwa nyumba zao. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila
mwenye kutenda kama makosa yao.
26. Na
tuliwaweka kabila la A'di kwa nafasi na nguvu sio kama tulivyo kuwekeni nyinyi
watu wa Makka. Na tuliwajaalia masikio, na macho, na nyoyo, lau wangeli taka
kunafiika kwayo. Lakini hayakuwafaa hata kitu kidogo masikio yao, wala macho
yao, wala nyoyo zao, kwa sababu walikuwa wakizikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu.
Basi hayo yakapinga baina yao na kunafiika kwa waliyo letewa. Na ile ile adhabu
waliyo kuwa wakiifanyia maskhara ikawazunguka.
27. Enyi watu
wa Makka! Tumeiangamiza miji iliyo jirani zenu. Na Sisi tuliwawekea wazi dalili
namna mbali mbali, ili wapate kurejea waache ukafiri. Hawakurejea.
28. Basi kwani
hao walio wafanya miungu badala ya Mwenyezi Mungu ili iwakaribishe kwa Mwenyezi
Mtukufu imeweza kuwakinga na maangamizo? Hasha! Bali miungu hiyo iliwakimbia, na
hali wao ndio wana haja nayo mno iwanusuru. Na hayo yaliyo wafika, ya kutupwa na
miungu yao, na kuwapotea ndio matokeo ya uwongo wao na uzushi wao.
29. Ewe
Muhammad! Taja tulipo kuletea kikundi cha majini waje sikiliza Qur'ani. Walipo
hudhiria ilipo kuwa ikisomwa, baadhi yao wakawaambia wenzao: Sikilizeni! Ilipo
kwisha timia kusomwa wakarudi kwa haraka kwa wenzao, kuwahadharisha na ukafiri,
wakiwataka waamini.
30. Walisema:
Enyi watu wetu! Hakika sisi tumekisikia Kitabu chenye shani kubwa. Kimeteremshwa
baada ya Musa, na kinasadikisha Vitabu vya Mwenyezi Mungu vilivyo tangulia,
kinaongoza kwenye itikadi ya haki, na sharia ya vitendo iliyo simama sawa.
31. Enyi watu
wetu! Muitikieni mwenye kuitia kwa Mwenyezi Mungu anaye ongoza kwenye Haki na
kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na msadikini Mwenyezi Mungu akusameheni madhambi yenu
yaliyo tangulia, na akulindeni na adhabu kali iliyo chungu.
32. Na asiye
muitikia Mwenyezi Mungu basi hawezi kumshinda Mwenyezi Mungu asimtie mkononi
hata akikimbia vipi katika ardhi. Na wala hana isipo kuwa Mwenyezi Mungu wa
kumnusuru na kumkinga na adhabu yake. Hao wanao puuza wasimwitikie mwenye kuitia
kwa Mwenyezi Mungu wamo katika ubabaishi na dhaahiri wako mbali na Haki.
33.
Wameghafilika wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi,
na wala hakushindwa kuziumba, ni Muweza wa kuwafufua maiti? Bali Yeye ni Muweza
wa hayo, kwani Yeye Mtukufu ana uweza kaamili juu ya kila kitu.
34. Na siku
watakapo simamishwa walio kufuru Motoni wataambiwa kwa kukemewa: Adhabu hii si
jambo la kweli linakubaliana na tuliyo kuonyeni nayo duniani? Na wao watasema:
Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu Mlezi, haya ni haki kweli. Atasema: Onjeni kila
namna ya adhabu kali kwa kushikilia kwenu ukafiri na ukanushi.
35. Ewe
Muhammad! Wastahamilie makafiri kama walivyo stahamili Mitume wengine wenye
nguvu na imara wakati wa shida. Wala usiwahimizie adhabu. Kwani hiyo itawafika
tu, hapana hivi wala hivi, hata ikichukua muda mrefu. Siku watapo kiona kitisho
chake watadhani kuwa hawakukaa kabla yake ila saa moja tu ya mchana. Haya uliyo
watolea waadhi yatosha. Hawataangamizwa kwa adhabu isipo kuwa walio toka kwenye
ut'iifu.
Rudi kwenye
sura
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani