1. H'a Mim.
Hizi ni harufi mbili katika harufi za kutamkwa, zimeanzia Sura hii kama ada ya
Sura nyingi katika Qur'ani ambazo zimeanzia kwa harufi kama hivi ili kuashiria
kuwa washirikina wameshindwa kuleta mfano wake, ijapo kuwa hii Qur'ani imeundwa
kwa harufi hizi hizi wanazo zitumia katika maneno yao.
2. Huu
mteremsho wa Qur'ani umetokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Asiye shindika,
Mwenye hikima katika kupanga kwake na kuendesha kwake.
3. Hakika
katika kuumbwa mbingu na ardhi ni katika ufundi wa namna ya pekee wa Mwenyezi
Mungu, bila ya shaka ni dalili zenye nguvu kabisa katika Ungu wake na Upweke
wake, ambao wanauamini wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu kwa maumbile yao yaliyo
sawa.
4. Na vile
Mwenyezi Mungu kukuumbeni nyinyi, enyi watu, kama mlivyo, mna sura nzuri, na
umbo la peke yenu, na mnavyo khitalifiana baina ya wanaadamu na wanyama na
mkaenezwa ulimwenguni, na manufaa mbali mbali, bila ya shaka ni Ishara zenye
nguvu na ziwazi kwa watu wanao tafuta yakini ya mambo yao kwa kuzingatia na
kufikiri.
5. Na katika
kukhitalifiana usiku na mchana, kwa urefu na ufupi, na mwangaza na giza, na
kupeana zamu kwa nidhamu iliyo thibiti, na katika mvua anayo iteremsha Mwenyezi
Mungu kutoka mbinguni, akaihuisha ardhi kwa mimea baada ya kufa kwake kwa ukame,
na kuziendesha pepo pande mbali mbali nazo zinakhitalifiana kwa ubaridi na joto,
na nguvu na udhaifu, ni alama zilizo wazi za kuonyesha ukamilifu wa uwezo wa
Mwenyezi Mungu kwa watu wenye kufikiri kwa akili zao, wakafikilia yakini yao.
6. Hizo ni Aya
za Mwenyezi Mungu zinazo eleza uumbaji alio ufanya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya
watu. Tunakusomea wewe katika Qur'ani kwa ulimi wa Jibrili, nazo Aya hizo ni za
haki. Ikiwa hao hawaziamini hizi basi maneno gani watayasadiki baada ya maneno
ya Mwenyezi Mungu, nayo ni Qur'ani na Aya zake
7. Atapata
maangamizo makubwa kila anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo mbaya, na mwenye
kukithiri madhambi yake kwa kitendo hicho!
8. Mzushi kama
huyu husikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, nazo zinasema haki tupu. Kisha
yeye huendelea na ukafiri wake kwa kutakabari, akaikataa Imani. Hali yake ni
hali ya asiye pata kuzisikia Aya. Basi ewe Nabii! Mbashirie, kwa kumkejeli, kuwa
atapata adhabu chungu kwa huko kushikilia kwake kitendo kitacho mletea adhabu
hiyo.
9. Na huyu
mwenye inda, akijua kitu kidogo katika Aya za Mwenyezi Mungu huzifanya Aya zote
za Mwenyezi Mungu ni kitu cha kufanyia maskhara na mzaha. Wazushi hao wingi wa
madhambi watapata adhabu ya kuwadhalilisha kwa kiburi chao.
10. Nyuma yao
ipo Jahannamu inawangojea, na walicho kichuma duniani hakitawapunguzia hata
chembe ya adhabu yake. Wala hiyo miungu ya uwongo walio ifanya ndio ya
kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu, haitawakinga na chochote katika adhabu
yake. Na wao watapata mateso makubwa, kwa kitisho chake na ukali wake.
11. Hii
Qur'ani ni ushahidi kaamili wa Haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na hao wanao
zikataa hoja zilio kusanywa na Qur'ani zilizo toka kwa Muumba wao na Mlezi wao
watapata adhabu kali mno miongoni mwa namna za adhabu.
12. Mwenyezi
Mungu peke yake ndiye aliye kufanyieni ikutumikieni bahari ili marikebu zipate
kwenda juu yake kwa idhini yake, na uwezo wake, zikikubebeni nyinyi na bidhaa
zenu, na ili mtafute kutokana na fadhila za Mwenyezi Mungu mali ya baharini kwa
kupata manufaa ya ujuzi, na biashara, na jihadi, na zawadi, na uvuvi, na kutoa
vyombo, na ili mpate kushukuru neema zake kwa kumsafia Dini Mwenyezi Mungu.
13. Na
akakudhalilishieni vyote viliomo mbinguni, nyota zenye kung'ara na sayari, na
vyote viliomo kwenye ardhi, makulima, mifugo, maji, moto, hewa, na jangwa, vyote
hivyo vinatokana na Yeye Mtukufu, ili akuenezeeni manufaa ya uhai. Hakika katika
hizo neema zilizo tajwa zipo Ishara zenye kuonyesha kudra yake kwa watu wenye
kuzingatia Ishara.
14. Ewe Mtume!
Waambie wanao msadiki Mwenyezi Mungu na wanakufuata wewe, wasamehe maudhi yanayo
wafikia kutokana na watu ambao hawataraji kuja siku za Mwenyezi Mungu za
kuwalipa watu kwa kheri na shari kwa mujibu walivyo.
15. Mwenye
kutenda mema atapata ujira wake na thawabu mwenyewe; na mwenye kutenda uovu basi
dhambi za kitendo chake zitamuangukia mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Muumba
wenu kwa ajili ya malipo.
16. Ninaapa
kwa hakika tumewapa Wana wa Israili Taurati, na hukumu iliomo ndani yake, na
Unabii ulio funuliwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na tumewaruzuku kheri namna
mbali mbali, na tumewafadhilisha wao katika neema nyingi juu ya viumbe vyote.
17. Na
tumewapa dalili wazi katika mambo ya Dini yao. Basi haikutokea khitilafu baina
yao ila baada ya kwisha wajia ujuzi wa hakika ya Dini na hukumu zake. Na hayo ni
kwa uadui na uhasidi tu ulio baina yao. Hakika Mola wako Mlezi atapambanua baina
ya hao wanao khitalifiana Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa
wamekhitalifiana.
18. Tena
tukakujaalia wewe, ewe Muhammad, baada ya khitilafu za Watu wa Kitabu (yaani
Mayahudi na Wakristo), kuwa ni Mtume wa kwenda Njia iliyo wazi katika mambo ya
Dini tuliyo kuwekea wewe na walio kuwa kabla yako miongoni mwa Mitume. Basi
ifuate Sharia yako ya Haki, yenye kuthibiti imara kwa hoja na dalili, wala
usifuate matamanio ya watu wasio ijua Njia ya Haki.
19. Hakika hao
waongo wenye tamaa ya kuwa ati wewe utawafuata wao, hawatoweza kukuondolea hata
chembe ya adhabu pindi ukiwafuata. Na hakika wenye kupindukia mipaka ya Mwenyezi
Mungu husaidiana wao kwa wao katika upotovu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye
kuwasaidia wale wanao mcha, basi hao haitawafikia dhulma ya wenye kudhulumu.
20. Hii
Qur'ani ulio teremshiwa wewe ni dalili kwa watu kuwaonyesha Dini ya Haki, na
uwongofu wa kuwaongoza kwenye njia za kheri, na neema kwa watu wenye kuyakinisha
thawabu na adhabu za Mwenyezi Mungu.
21. Bali
wanadhani hao walio chuma yanayo chusha katika ukafiri na maasi kwamba
tutawafanya kama walio muamini Mwenyezi Mungu na wakatenda vitendo vyema, na
hivyo tuwafanye sawa baina ya makundi mawili hayo katika uhai na katika kufa?
Hukumu yao ni mbaya mno, ikiwa wanahisi kuwa wao ni sawa na Waumini.
22. Na
Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa mujibu wa hikima na nidhamu, ili
zidhihiri dalili za Ungu wake na uwezo wake, na apate kulipwa kila mtu kwa alilo
tenda, ikiwa kheri au shari. Na wao hawatapunguziwa chochote katika malipo yao.
23. Ewe Mtume!
Umeangalia, ukamwona huyo mwenye kufanya matamanio yake ndiye mungu wake wa
kumuabudu, akamnyenyekea, na akamt'ii, na akaiacha Njia ya Haki na hali anaijua,
na akaziba masikio yake asisikie waadhi, na moyo wake asiamini Haki, na
akabandika vitanga vya macho asione ya kuzingatiwa? Basi nani wa kumwongoa mtu
huyu baada ya kwisha puuzwa na Mwenyezi Mungu? Je! Mnaacha kutazama ili msipate
kukumbuka?
24. Na
walisema wenye kukanya kufufuliwa: Hapana uhai ila huu uhai wa duniani tu tulio
nao sasa. Tunaishi na tunakufa. Na hapana nyuma ya hayo uhai baada ya kwisha
kufa. Na hapana cha kututeketeza isipo kuwa kupita dahari, yaani zama na wakati.
Wala wao hawasemi hayo kwa ujuzi na kuwa na yakini, bali ni kwa kudhania na
kukisia tu.
25. Na
ukiwasomea Aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi zenye kuonyesha uwezo wake wa
kufufua, huwa hawana hoja ila kusema - kwa kuikimbia haki : Wafufueni baba zetu,
ikiwa nyinyi ni wasema kweli katika kudai kuwa kupo kufufuliwa.
26. Ewe
Muhammad! Waambie: Mwenyezi Mungu amekupeni uhai duniani nanyi hamkuwa chochote,
kisha anakufisheni unapo timia wakati wenu. Kisha atakukusanyeni Siku ya Kiyama,
na hapana shaka ya kukusanywa huko. Lakini wengi wa watu hawaujui uwezo wa
Mwenyezi Mungu wa kufufua, kwa sababu ya mapuuza yao kuzingatia dalili ziliopo.
Na huyo Muweza wa hayo pia ni Muweza wa kuwaleta baba zenu.
27. Na ni wa
Mwenyezi Mungu pekee ufalme wa mbingu na ardhi, kwa kuumba, kumiliki, na
kupanga. Na itapo fika Saa ya Kiyama, siku hiyo watakhasiri wenye kufuata
upotovu.
28. Ewe unaye
semezwa! Utawaona siku itapo fika Saa watu wa kila dini wamekalia magoti kwa
khofu waliyo nayo kungojea kuitikia wito. Kila umma utaitwa kwenye daftari la
vitendo vyao, na wataambiwa: Leo mtalipwa sawa malipo ya mliyo kuwa mkiyatenda
duniani.
29. Na
wataambiwa: Hichi hapa kitabu chetu tulimo sajili vitendo vyenu, nanyi
mmekichukua kwa mikono yenu, kinataja juu yenu yale mliyo yatenda kwa ushahidi
wa kweli. Hakika Sisi tulikuwa tukiwataka Malaika waandike, ili tupate
kukuhasibieni yaliyo tokana nanyi.
30. Basi ama
walio amini na wakatenda vitendo vyema, Mola wao Mlezi atawatia katika Pepo
yake. Malipo hayo ndio kufuzu kulio bainika, kulio wazi.
31. Na ama
walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake wataambiwa kwa kuwahizi: Kwani
hawakukujilieni Mitume wangu? Hamkusomewa Aya zangu, nanyi mkajiona bora hamfai
kuikubali haki, na mkawa kaumu ya makafiri?
32. Enyi mnao
kanya kufufuliwa! Akikwambieni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba agano la Mwenyezi
Mungu la kuwalipa ni haki yenye kuthibiti, na Saa haina shaka itakuja, nyinyi
mkisema: Sisi hatujui chochote khabari ya hiyo Saa ya Kiyama, wala ukweli wake;
na sisi ni dhana ya kudhania tu kuwa hiyo Saa itakuja, wala hatuna yakini kuwa
itatokea.
33. Na
utawadhihirikia hawa makafiri ubaya wa vitendo vyao, na itawateremkia jaza ya
maskhara yao waliyo kuwa wakizifanyia Ishara za Mwenyezi Mungu.
34. Na
wataambiwa hawa washirikina kwa kuwahizi: Leo hii tunakuacheni katika adhabu
kama nyinyi mlivyo acha kujitayarisha kukutana na Mola wenu Mlezi katika siku
hii kwa ut'iifu na vitendo vyema. Na pahala penu pa kukaa ni Motoni, na wala
hamna wa kukunusuruni akakuokoeni na adhabu yake.
35. Adhabu
hiyo imekuteremkieni kwa sababu ya ukafiri wenu, na maskhara yenu kuzifanyia
Ishara za Mwenyezi Mungu, na mlivyo khadaika na maisha ya dunia kwa mapambo
yake. Basi leo hapana yeyote awezaye kuwatoa hawa kwenye Moto, wala hawatakikani
kumtaka radhi Mola wao Mlezi kwa kutafuta udhuru.
36. Basi ni za
Mwenyezi Mungu pekee sifa njema, Muumba mbingu na ardhi, na Muumba wa viumbe
vyote. Kwani hivi kuwa ni Mola Mlezi wa kila kitu unawajibika uhimidiwe kwa
neema zote.
37. Na ni wake
Yeye, Subhanahu, utukufu na utawala katika mbingu na ardhi. Na Yeye ni Mwenye
nguvu, asiye shindika, Mwenye hikima, asiye kosea katika hikima yake. Na
Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani