1. H'a Mim.
Imeanzia Sura hii kwa baadhi ya harufi za kutamkwa kama ilivyo ada ya Qur'ani
katika kufungulia Sura nyingi kwa harufi kama hizi.
2. Mwenyezi
Mungu anaapa kwa Qur'ani yenye kuweka wazi Dini ya Haki, yenye kuwabainishia
watu yaliyo na maslaha ya dunia yao na Akhera yao, ili kujuulisha utukufu wa
cheo chake.
3. Hakika Sisi
tumeanza kuiteremsha Qur'ani katika usiku ulio jaa kheri, wenye baraka nyingi,
kwani ni mwendo wetu kuonya kwa kuwatuma Mitume na kuteremsha Vitabu.
4. Katika usiku
huu wenye baraka hupambanuliwa baina ya mambo yote yenye hikima, na Qur'ani ndio
kilele cha hikima, na ndio pambanuo baina ya kweli na uwongo. Na kwa hivyo ndio
ikateremshwa katika usiku huo.
5. Nakusudia
kwa jambo hili, yaani jambo kuu lenye kutoka kwetu kama ilivyo kwisha pita
hukumu ya mpango wetu. Kwani ni shani yetu kutuma Mitume kwa Vitabu ili
kuwafikishia waja wetu.
6. Kwa ajili ya
rehema ya Mola wako Mlezi kwa waja wake, amewatuma Mitume kwa watu wawafikishie
uwongofu wake, kwani hakika Yeye peke yake, ndiye Mwenye kusikia kila cha
kusikiwa, Mwenye kujua kila cha kujuulikana.
7. Yeye ndiye
Muumba mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini na haki, na
mnaifuata, na mnaamini kuwa hakika ndio Yeye Mwenye kuteremsha Qur'ani kuwa ni
rehema na uwongofu.
8. Hapana Mungu
isipo kuwa Yeye anaye stahiki kuabudiwa, Yeye peke yake, Mwenye kuhuisha na
kufisha. Na Yeye peke yake, ndiye aliye kuumbeni nyinyi na kawaumba baba zenu wa
mwanzo.
9. Lakini
makafiri wana shaka na ukweli huu, wamo wakifuata pumbao lao. Na huo ndio mtindo
wa watu wa pumbao na michezo, sio mwendo wa watu wa ilimu na yakini.
10. Basi ewe
Mtume! Ngojea ukame utapo wateremkia, wakasibiwa na kukonda na udhaifu wa kuona,
ikawa mtu huwa anaona baina ya mbingu na ardhi moshi dhaahiri shaahiri, akawa
anasikia mvumo wake wala hauoni.
11. Moshi huu
utawazunguka wale wanao kadhibisha walio sibiwa na ukame, watasema kwa wingi wa
kitisho: Hii ni adhabu kali na chungu!
12. Kama pia
watavyo sema kwa kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu: Hakika sisi tutaamini
ukituondolea adhabu ya njaa na dhiki.
13. Watu hawa
watawaidhika vipi, hata watimize hiyo Imani wanayo iahidi wakiondolewa adhabu,
na hali Mtume mwenye ujumbe ulio wazi kesha wajia na miujiza yenye kuonyesha
ukweli wake, na hayo ndiyo mawaidha makubwa kabisa?
14. Kisha
wakaacha kumsadiki Mtume aliye tiliwa nguvu na miujiza iliyo wazi, na
wakamwambia: Huo uwongo na uzushi! Mara nyengine wakimsingizia kuwa amefunzwa
hayo na mtu, na mara nyengine kuwa akili yake imekorogeka.
15. Mwenyezi
Mungu anawarudi: Sisi hakika tutakuondoleeni adhabu wakati wa duniani, nao ni
wakati mchache, lakini nyinyi mtarejea tu, bila ya shaka, yale yale mliyo kuwa
mkiyatenda.
16. Ewe Mtume!
Watajie ile siku tutapo washika kwa mshiko mkubwa, wa nguvu. Nasi kwa mshiko huu
ndio tunawatesa.
17. Na bila ya
shaka tulikwisha wafanyia mtihani, kabla ya makafiri wa Makka, kaumu ya Firauni
kwa kuwaitia kwenye Imani, na akawajia Musa, Mtume Mtukufu kwa Mwenyezi Mungu.
Wakamkataa kwa inda tu. Na huo ndio mtindo wa hawa washirikina.
18. Mtume
Mtukufu aliwaambia: Nipeni enyi waja wa Mwenyezi Mungu lilio waajibu juu yenu,
nalo ni kuitikia wito wangu, kwani mimi ni Mtume nimetumwa makhsusi kwenu, na ni
muaminifu katika ujumbe wangu.
19. Wala
msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu kwa kumkadhibisha Mtume wake, kwani mimi
nakuleteeni muujiza ulio wazi wa kubainisha ukweli wa Unabii wangu na Utume
wangu.
20. Na mimi
najilinda na Mwenye kuniumba msiweze kuniuwa kwa kunipiga mawe.
21. Na ikiwa
hamnisadiki basi jitengeni nami, wala msiniudhi.
22. Musa
akamwambia Mola wake Mlezi kwa kumshitakia watu wake alipo kata tamaa nao kuwa
hawaamini: Hakika watu hawa shauri yao imekwisha fika ukomo katika ukafiri; basi
Wewe wafanyie wanalo stahiki.
23. (Naye Musa
akaambiwa:) Toka na Waumini usiku usiku kwa kificho, wasije kukupateni, kwani
Firauni na askari wake watakufuateni pindi wakijua, wakukamateni.
24. Na iache
bahari imetulia kama ilivyo baada ya kwisha pigwa kwa fimbo, wapate kuingia hao
wanao kanya; kwani wao watazama tu, hapana hivi wala hivi.
25. Hao watu
wa Firauni baada ya kuzama kwao waliacha mabustani mengi yenye kunawiri, na
chemchem zinazo tiririka maji yake,
26. Na
makulima ya namna kwa namna, na makaazi mazuri mazuri,
27. Na maisha
ya raha na starehe, waliyo kuwa wakiyaonea utamu.
28. Mfano wa
adhabu hiyo Mwenyezi Mungu humuadhibu mwenye kwenda kinyume na amri yake, na
akatoka katika ut'iifu wake, na humwondolea neema yule mwenye nayo akawapa watu
wenginewe wasio kuwa na makhusiano nao yoyote, la ya ujamaa wala dini.
29. Basi la
mbingu wala ardhi hazikuwahuzunukia ilipo wanyakua adhabu, jinsi ilivyo haribika
hali yao; wala hawakungojewa watubu, wala hawakupewa muhula wapate kudiriki
taksiri yao, kwa jinsi walivyo dharauliwa!
30. Na kwa
hakika Mwenyezi Mungu aliwaokoa Wana wa Israili na adhabu ya kuwadhalilisha.
31. Aliwaokoa
kwa Firauni. Hakika Firauni alikuwa jeuri kwa watu wake, amepita mipaka kwa
shari na uasi.
32. Ninaapa:
Tuliwakhiari Wana wa Israili kwa kuwa tuliwajua kwamba wao wana stahiki
kuteuliwa kuliko watu wengine wote wa zama zao. Kwa hivyo tukawatuma miongoni
mwao Manabii wengi kwa kuwa tulijua hali zao.
33. Na
Mwenyezi Mungu akawaletea katika mkono wa Musa dalili kadhaa wa kadhaa za
kuwatia wao katika mitihani iliyo wazi.
34,35. Hakika
hawa wanao kadhibisha kufufuliwa bila ya shaka wanasema: Hapana kufa ila kwa
haya haya mauti yetu ya kwanza ya duniani, wala sisi hatutafufuliwa tena.
34,35. Hakika
hawa wanao kadhibisha kufufuliwa bila ya shaka wanasema: Hapana kufa ila kwa
haya haya mauti yetu ya kwanza ya duniani, wala sisi hatutafufuliwa tena.
36. Na wao
humwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu na Waumini: Ikiwa nyinyi mnasema kweli katika
madai yenu kwamba Mola wenu Mlezi anahuisha wafu kwa ajili ya hisabu katika
Akhera, basi upesi upesi tufufulieni baba zetu walio kwisha kufa, kwa kumwomba
huyo Mola wenu Mlezi!
37. Je!
Makafiri wa Makka wanawashinda kaumu ya Tubbaa' na walio watangulia kwa nguvu,
na ulinzi, na utawala, na mambo yote ya kidunia? Ewe Muhammad! Hao washirikina
wa kaumu yako hawawashindi hao kwa nguvu, na hao Sisi tuliwateketeza katika
dunia kwa ukafiri wao na madhambi yao. Basi nawawazingatie!
38. Na
Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao bila ya hikima.
39.
Hatukuziumba hizo ila kwa umbo lilio ambatana na hikima, kwa nidhamu iliyo
thibiti yenye kuonyesha ushahidi wa kuwepo Mwenyezi Mungu wa pekee, Mwenye
uwezo. Lakini wengi wa hawa wameghafilika, wamo katika upofu, hawazioni dalili
hizi.
40. Hakika
siku ya hukumu kupambanua baina ya mwenye haki na asiye na haki, ni wakati walio
ahidiwa wote.
41. Siku
ambayo jamaa hawezi kumtetea jamaa yake, wala rafiki kumtetea rafiki yake kwa
lolote, hata kwa uchache wa adhabu. Wala wao hawatanusuriwa nafsi zao mbele ya
Mwenyezi Mungu.
42. Lakini
wale ambao Mwenyezi Mungu amewarehemu, miongoni mwa Waumini, Mwenyezi Mungu
atawasamehe, na atawapa ruhusa ya uombezi waweze kuwaombea wenginewe. Hakika
Yeye ndiye Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kuwarehemu waja wake Waumini.
43,44. Hakika
mti wa Zaqqumu unao juulikana kwa ubaya wa sura yake, na ukarihi kuula kwake, na
harufu yake, ni chakula cha wakosefu wenye madhambi mengi.
43,44. Hakika
mti wa Zaqqumu unao juulikana kwa ubaya wa sura yake, na ukarihi kuula kwake, na
harufu yake, ni chakula cha wakosefu wenye madhambi mengi.
45,46. Utamu
wake kama maadeni iliyo yayushwa kwa moto, inatokota matumboni kama yanavyo
tokota maji yanayo chemshwa.
45,46. Utamu
wake kama maadeni iliyo yayushwa kwa moto, inatokota matumboni kama yanavyo
tokota maji yanayo chemshwa.
47. Enyi
Mazabania wa Jahannamu (Walinzi wa Motoni)! Mkamateni huyu mkosefu, mwenye
dhambi, mumtokomeze kwa nguvu na ukali mpaka katikati ya Jahannamu!
48. Kisha
mmiminieni juu ya kichwa chake maji ya moto makali kuzidi kumuadhibu na kumtesa.
49. Ataambiwa
kwa kejeli na maskhara: Onja hii adhabu kali, kwani ati wewe si ndiye mtukufu
mwenye nguvu katika kaumu yako, ndiye mheshimiwa unavyo jiona mwenyewe!
50. Hapana
shaka hii adhabu mnayo ipata ni kweli yenye kuwa, na ndiyo mliyo kuwa mkiibisha
duniani, na mkiitilia shaka kuwa haiwi.
51. Hakika hao
ambao wamejikinga nafsi zao na maasi kwa kufuata ut'iifu wa Mwenyezi Mungu wapo
pahala patukufu ambapo ndani yake wao wanajipatia amani kwa nafsi zao.
52. Katika
mabustani watapo kuwa ndani yake wanastarehe, na chemchem za maji yanayo pita
chini yao, kwa sababu ya kuwakirimu wao kwa kutukuza hizo neema zao.
53. Wakivaa
humo hariri nyepesi na nzito kuzidi kuongeza mapambo yao, nao wakielekeana
katika majlisi zao, ili kutimiza starehe.
54. Na pamoja
na malipo haya tutawaoza huko Peponi mahurulaini, ambao huwezi kuwachanganyia
jicho kwa hadi ya uzuri wao na ukubwa wa macho yao.
55. Nao huko
Peponi watataka kila tunda wanalo litamani, kwa kujua kuwa hayatawaletea
vimbizi, wala hayatakwisha, wala hayataadimika.
56. Huko
Peponi hawataonja mauti baada ya mauti ya kwanza waliyo kwisha yaonja duniani
ulipo kwisha muda wao wa kuishi, na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya
Motoni.
57.
Kuhifadhiwa kwao na adhabu ni fadhila na hisani ya Muumba wako. Kuhifadhiwa huko
na adhabu na kuingizwa kwao Peponi ndio hadi ya mwisho ya kufuzu kulio kukubwa.
58. Basi
hakika Sisi tumekufanyia wepesi kuisoma Qur'ani na kuifikisha kama ilivyo
teremka kwa lugha yako, na lugha yao, ili wapate kuwaidhika, na waiamini, na
watende kwa mujibu yaliomo ndani yake.
59. Basi wewe
yangojee hayo yatakayo wafika, na wao pia wanangojea yatakayo kufika wewe na huo
wito wako, mambo yakibadilika.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani