1. H'a Mim:-
Imeanza Sura hii kwa baadhi ya harufi za kutamkwa kama ilivyo ada ya Qur'ani
katika kuanzishia Sura nyingi kwa harufi kama hizi.
2. Mwenyezi
Mungu, Subhanahu, anaapa kwa Qur'ani inayo eleza wazi yale iliyo yakusanya
katika mambo ya itikadi na hukumu.
3. Hakika Sisi
tumeijaalia Qur'ani iwe kwa lugha ya Kiarabu, ili mweze kuelewa umuujiza wake,
na mweze kuzingatia maana zake.
4. Na hakika
hii Qur'ani iliyo thibiti katika Lauhun Mahfuudh, Ubao ulio hifadhiwa, ulioko
kwetu, bila ya shaka, ina cheo cha juu, na imepangwa kwa mpango wa hikima,
katika mwisho wa ufasihi. (Vitabu vyote vya mbinguni asili yake anayo Mwenyezi
Mungu, katika Ujuzi wake wa tokea azali, Al- I'lmu al-azaliy au Ubao Ulio
Hifadhiwa Al-lauhu al-mahfuudh au Asili ya Maandiko Ummu-l-kitabi. Kwa sababu ya
kuwa Vitabu vilivyo kuja zamani, ikiwa Taurati, Zaburi, Injili n.k. vilikuwa ni
vya muda fulani, na kwa mataifa fulani, basi haikuwepo dharura vibaki kwa usafi
kila neno lake. Ni makusudio yake tu yabakie, yaliyo kuwa ya msingi. Ama ulipo
fika wakati wa kudumisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa zama zote, na kwa watu
wote, ndio ikaja Qur'ani ambayo imehifadhiwa kila neno lake. Na ndio siri ya
kuletwa kwa lugha ya Kiarabu na ikalindwa kwa lugha ile, ijapo kuwa
itatarajumiwa katika lugha nyengine. Mzozano wowote unao tokea unarejezwa kwenye
asli ile ya Kiarabu ambayo haikubadilika hata chembe, wala haitabadilika mpaka
Siku ya Kiyama. Huo peke yake ni muujiza. Ama vitabu vya Biblia ni kama maji
yaliyo tibuliwa na ng'ombe mpaka kwenye chemchem yake. Chemchem ya Qur'ani
haikutibuliwa. Ijapo kuwa wanyama na watu wanaweza kunywa maji yake huku chini,
kwenye kitovu cha chemchem hakuguswi. Huko ni kwenye Qur'ani hiyo ya Kiarabu,
safi kama ilivyo kwenye Ubao Ulio Hifadhiwa.)
5. Je! Tukupeni
muhula, tuache kukuteremshieni Qur'ani kwa kukutupilieni mbali, kwa sababu ya
kupita kwenu mipaka ya ukafiri juu ya nafsi zenu? Hayawi hayo, kwa kufuata
hukumu ya kulazimikana kwenu na hoja.
6. Nasi
tuliwatuma Manabii wengi kuyaendea mataifa yaliyo tangulia, basi hapana ajabu
kitu kumtuma Mtume kwenu.
7. Wala hawajii
Mtume yeyote kuwakumbusha Haki ila huendelea na kumfanyia maskhara.
8. Basi
tuliwateketeza walio kadhibisha walio tangulia; na hao walikuwa wamewazidi
makafiri wa Makka kwa nguvu na ushupavu. Basi wasidanganyike hawa na ujabari
wao. Na zilikwisha tangulia katika Qur'ani hadithi za ajabu za watu wa kale, za
kuwafanya wenginewe wazingatie. Basi enyi mnao kanusha! Zingatieni!
9. Na ninaapa,
ewe Mtume! Ukiwauliza makafiri nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka
watasema kuyajibu hayo: Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba, ambaye anasifika kwa
hakika ya mambo kuwa ni Mwenye nguvu, na Mwenye Ujuzi ulio enea.
10. Ambaye
amekufanyieni ardhi ni pahala palipo tanda, ili muweze kukaa humo na mjitumilie,
na akakufanyieni ndani yake njia mnazo zipitia katika safari zenu mpate kufikia
mtakako.
11. Na ambaye
aliye kuteremshieni maji kwa kiasi ya haja kutoka mbinguni tukaihuisha nchi kavu
isiyo na mimea. Kuhuisha kama huko ndivyo mtavyo fufuliwa kutoka makaburini
kwenu kwa ajili ya hisabu. Basi yawaje mnakukataa?
12. Na ambaye
aliye kuumbieni namna zote za viumbe, akavifanya vikutumikieni vyombo vya
baharini na ngamia kuwa ni vipando katika safari zenu kutimiza haja zenu.
13. Ili mtulie
juu yao, kisha mkumbuke neema za Muumba wenu na Mlezi wenu kwa kuvifanya hivyo
vikutumikieni mnapo tulia juu yao, na kwa kuadhimisha kule kuvifanya vinyonge
kwa njia ya ajabu, na kutambua uweza mlio wezeshwa kuvidhibiti na kuvitawala,
mseme: Subhana, Ametakasika aliye mfanya huyu (au hichi) kuwa dhalili
kututumikia na sisi wenyewe tusingeli weza kumdhalilisha.
14. Na hakika
sisi ni wenye kurejea kwa Muumba wetu baada ya maisha haya, ili ahisabiwe kila
mmoja kwa iliyo tanguliza mikono yake.
15. Na
makafiri washirikina wamemfanyia Mwenyezi Mungu Subhanahu katika viumbe vyake
mwana wakaamini kuwa ni sehemu ya nafsi yake. Hakika mwanaadamu kwa kitendo
chake hichi hadi amepita ukomo katika ukafiri wake, na upinzani wake uwazi.
16. Ati mnadai
kwamba Yeye amejitwalia katika viumbe vyake watoto wa kike, na nyinyi
akakukhiarieni watoto wanaume? Ama hakika haya ni mambo ya ajabu kweli!
17.
Wamekuzulia Wewe hayo, na ilhali wao akipewa khabari mmoja wao kwamba amepata
mtoto wa kike uso wake husawajika kwa kuudhika, naye kajaa masikitiko na huzuni
kwa kuona anapewa khabari mbaya.
18. Hivyo hawa
wana fanya jeuri ya kumpachikia Mwenyezi Mungu mwana, ambaye kwa maumbile yake
amelelewa katika mapambo, na hata hawezi kujadiliana na kupambana kwa hoja kwa
nuksani yake ya kubaini. Ama hili ni jambo la ajabu!
19. Na ati
wakawaita Malaika, viumbe vya Mwenyezi Mungu, kuwa ni wanawake. Kwani wao
waliwashuhudia walipo umbwa, hata watoe hukumu kwa jambo hilo? Hawakuliona! Sisi
tutausajili uzushi wao huu. Na Siku ya Kiyama watakuja hisabiwa.
20. Na
washirikina husema ati: Lau kuwa Mwingi wa Rehema angeli kuwa anataka tusiiabudu
hii miungu basi tusingeli iabudu. Wanakusudia kudai kuwa ati Mwenyezi Mungu yu
radhi kuabudiwa hiyo miungu. Wanasema hayo bila ya kuwa na ilimu yoyote ya
kuyategemezea wayasemayo. Hawa si chochote ila ni wenye kudhani tu. Hunena
maneno yasio na ushahidi wowote.
21. Kwani
tuliwapa Kitabu kabla ya Qur'ani cha kuunga mkono huu uzushi wao, ndio maana
wakashikamana nao kwa nguvu hivi? Hatukuwateremshia Kitabu namna hiyo. Basi
hawana hoja ya kuinukulu.
22. Lakini
washirikina walipo shindwa na hoja zote walisema: Hakika sisi tumewakuta baba
zetu wakifuata dini hii; na sisi tunaendelea kufuata nyayo zao.
23. Mfano wa
hali ya watu hawa ni mfano wa mataifa yaliyo tangulia. Hatukumtuma Mtume yeyote
kwenye mji kabla yako ila walisema wale wenye kuneemeka katika huo mji, nao ndio
walio takabari kwa hizo neema: Hakika sisi tumewakuta baba zetu wakifuata dini
hii, basi ndio sisi tunakwenda mwendo wao. Basi kufuata kijinga ni upotovu wa
tangu kale.
24. Mwonyaji
akasema: Je! Mnafuata baba zenu hata nikikujieni na yaliyo elekea zaidi
kukupelekeni kwenye uwongofu kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema kuwajibu
Mitume wao wakiwakadhibisha kwa Dini: Sisi tunayakataa yote mliyo tumwa
kutuambia!
25. Basi
tukawatesa walio wakadhibisha Mitume wao kwa mateso makali katika dunia. Basi
hebu angalia, ewe mwenye kuzingatia, vipi ulikuwa mwisho wa wenye
kukukadhibisheni kuwa ni mfano wa ajabu, na mawaidha makubwa!
26. Na ewe
Muhammad! Waambie hao wanao kanusha hadithi ya Ibrahim pale alipo mwambia baba
yake: Hakika mimi nimejitenga mbali na ibada ya kuiabudu hii miungu yenu ya
uwongo.
27. Lakini
mimi namuabudu Mwenyezi Mungu aliye niumba; kwani ni Yeye ndiye atakaye niongoza
kwendea Njia ya Haki.
28. Kwa
kuwatangazia hivyo, likawa hilo Neno la Tawhidi, ni neno lenye kubakia katika
dhuriya zake, ili wapate kulirejelea, waliamini.
29.
Washirikina hawakutimiza matumaini ya Ibrahim, wala Mimi sikuwapatiliza papo kwa
papo, bali nimewastarehesha hawa ulio nao, ewe Muhammad, na niliwastarehesha
baba zao kabla yao kwa namna mbali mbali za neema, mpaka ilipo teremka Qur'ani
kuwaitia Haki, na akawajia Mtume mwenye kubaini wazi akiwaita.
30. Na ilipo
teremka Qur'ani kuwaongoza kwenye Tawhid wakaongeza juu ya ushirikina wao kuita
Qur'ani : "uchawi" na "kiini macho", kwa kejeli. Na wakashikilia ukafiri wao.
31. Na
washirikina, kwa kumdharau Muhammad na kuona haiwezi kuwa yeye ateremshiwe
Qur'ani, walisema: Kwa nini basi hii Qur'ani, ambayo yeye anadai kuwa ni Wahyi
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, asiteremshiwe mtu mkubwa mtukufu katika watu wa Makka
au T'aif?
32. Funguo za
Utume hazimo katika mikono ya washirikina, hata wao wawakabidhi watu wenye vyeo.
Sisi tumewapangia maisha yao kwa kuwa wao wenyewe hawajiwezi. Na
tumewafadhilisha baadhi juu ya wengine katika riziki na vyeo, na kwa hivyo
baadhi yao huwafanya wengineo wawasaidie na wawatumikie katika kutimiza haja
zao, ili wategemeane katika kutafuta maisha na kupanga uhai. Na Unabii na yaliyo
khusiana nayo katika neema za Akhera na dunia, ni bora kuliko vyeo vyote vya
duniani.
33. Na lau
kuwa si karaha ya kuwa watu wote wawe makafiri wakiona makafiri wamo katika
nafasi ya riziki, basi tungeli wafanyia wanao mkufuru Mwenyezi Mungu kuwa nyumba
zao ziwe na dari za fedha, na pia ngazi za nyumba zao, kwa kuwa hayo hayana
thamani kitu mbele yetu.
34,35. Na
tungeli wafanyia milango ya nyumba zao na vitanda kuwa ni vya fedha wakineemeka
navyo na wakiegemea juu yake. Na tungeli wafanyia mapambo ya kila kitu. Na
starehe zote hizo tulizo kusifia si chochote ila ni starehe za kupita njia, ni
za uhai huu tu wa duniani. Na malipo ya Akhera mbele ya Muumba wako na Mlezi
wako yameandaliwa kwa wanao jilinda na ushirikina, na wakayaepuka maasi ya
kuangamiza.
34,35. Na
tungeli wafanyia milango ya nyumba zao na vitanda kuwa ni vya fedha wakineemeka
navyo na wakiegemea juu yake. Na tungeli wafanyia mapambo ya kila kitu. Na
starehe zote hizo tulizo kusifia si chochote ila ni starehe za kupita njia, ni
za uhai huu tu wa duniani. Na malipo ya Akhera mbele ya Muumba wako na Mlezi
wako yameandaliwa kwa wanao jilinda na ushirikina, na wakayaepuka maasi ya
kuangamiza.
36. Na mwenye
kujitia upofu na Qur'ani aliyo iteremsha Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kuwa ni
kumbusho kwa walimwengu wote, tunamsalitisha na Shetani, anakuwa naye daima,
akimpoteza na akimzuzua.
37. Na hakika
Mashetani wanao jitia upofu na Qur'ani huwazuia na Njia anayo itia Rahmani. Na
hao wanao tumiliwa wanadhani kwa kuwafuata rafiki zao kwamba wao wamo katika
uwongofu.
38. Hata yule
aliye jipa upofu na Qur'ani atapo fika kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, na
akaona matokeo ya kule kujitia kwake upofu, atamwambia rafiki yake kwa majuto:
Laiti wewe nami tungeli kuwa mbali mbali duniani umbali wa mashariki na
magharibi! Ama wewe ulikuwa sahibu muovu mno kwangu, mpaka umekuja nitumbukize
katika shimo la Motoni!
39. Na hapo
wataambiwa kwa kuwahizi: Leo hamtapunguziwa adhabu, kwani mmejidhulumu wenyewe
kwa ukafiri wenu, kwa sababu mlishirikiana na mashetani wenu. Kwani kila mmoja
anateseka kwa adhabu ya kumtosha mwenyewe.
40. Je!
Unaweza kumwongoa aliye pita mipaka katika upotovu? Je! Unaweza kumfanya asikie
aliye kiziwi hasikii la kweli, kipofu hazingatii, na ambaye katika ujuzi wa
Mwenyezi Mungu atakufa katika upotovu? Huwezi hayo! Kwa sababu hao wamekwisha
thibiti katika ukafiri wao, basi hawanafiiki kwa wanayo yasikia, wala wanayo
yaona.
41. Basi
tukikushika tukakufisha kabla hatuja kuonyesha adhabu yao, na kifua chako
kikatua kwa hayo, na pia vifua vya Waumini, alaa kulli hali, Sisi bila ya shaka
tutawaadhibu duniani na Akhera.
42. Au unataka
tukuonyeshe adhabu tuliyo waahidi kabla ya kufa kwako, tutakuonyesha, kwani Sisi
tunawaweza hao kwa uweza wetu na nguvu zetu.
43. Ikiwa moja
ya mawili haya lazima liwe bila ya shaka, basi shikamana na Qur'ani tuliyo
kufunulia, na simama imara katika kuitekeleza, kwani hakika wewe uko katika Njia
ya Haki Iliyo Nyooka.
44. Na hakika
hii Qur'ani ni utukufu mkubwa juu yako, ewe Muhammad, na wa Umma wako, kwa kuwa
umeteremshiwa kwa lugha ya Kiarabu, na mtakuja kuhojiwa Siku ya Kiyama juu ya
haki yake, na shukrani za neema zake.
45. Na hebu
angalia katika sharia za Mitume wetu tulio watuma kabla yako. Ati umekuja humo
wito wa kuwaita watu wende kuabudu vitu visio kuwa Mwenyezi Mungu? Haukuja! Basi
hao wanao abudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu mmoja hadi wamepita mipaka katika
upotovu wao!
46. Na bila ya
shaka Sisi tulimtuma Musa tukampa miujiza yenye kuthibitisha ukweli wake, ende
kwa Firauni na watu wake. Akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Muumba wa walimwengu
wote na Mlezi wao nimetumwa kwenu. Wakamtaka aonyeshe miujiza.
47. Alipo
wajia kwa miujiza ya kuthibitisha Utume wake mara wakampokea kwa kumcheka, na
kumfanyia tashtiti, na kumcheza shere, bila ya kuzingatia maneno yake.
48. Na kila
muujiza katika miujiza iliyo wajia mfululizo, kwa uwazi wa hoja zake juu ya
ukweli wa Mtume, na kuwa kila mmoja peke yake unatimiza makusudio hayo kwa
ukamilifu wa kila njia, na ukamilifu wa nafsi yake, hata ukiuangalia waweza
kusema: Muujiza huu ni mkubwa kuliko ule mwengine. Na walipo shikilia kuendelea
na uasi tuliwapatiliza kwa balaa za namna kwa namna, ili warejee, waache upotovu
wao.
49. Wakasema,
kumlilia Musa balaa zilipo waenea: Ewe mchawi - ndio Mwanachuoni kikwao -
Tuombee kwa Mola wako Mlezi, kwa kutawasali na ahadi yake aliyo kupa, atuondolee
adhabu hii! Hakika sisi tukifarijiwa bila ya shaka tutaongoka.
50. Mwenyezi
Mungu alipo waondolea masaibu yale kwa kuitikia dua za Musa, wakamshitukia kwa
kuvunja ile ahadi yao ya kuamini.
51. Firauni
akawatangazia watu wake kutangaza nguvu zake na madaraka yake: Kwani huu ufalme
wa Misri si wangu mimi peke yangu, wala hapana mwenginewe, na hii mito ambayo
mnaiona inapita chini ya jumba langu? Hamyaoni haya? Basi hamzingatii mnayo
yaona ya nguvu zangu na udhaifu wa Musa? Na Firauni alitaka kwa wito wake kuutia
imara ut'iifu wao.
52. Firauni
akasema akizidisha ujabari: Bali mimi ni bora kuliko dhaifu huyu mnnyonge, asiye
weza hata kubainisha wazi huo wito wake kwa ulimi wa fasaha.
53. Akazidi
kusema kuchochea kumkadhibisha Musa: Lau ingeli kuwa Mola wake Mlezi angeli
mvika vikuku vya dhahabu kwa kumpa funguo za utawala, au akamsaidia kwa Malaika
wa kumuunga mkono, ingeli kuwa yeye ni mkweli katika madai yake ya Utume?
54. Firauni
akawa anawachochea watu wake, na akawaathiri kwa udanganyifu huu, nao wakamt'ii
katika upotovu wake. Kwani hao walikuwa watu walio kwisha toka kwenye Dini ya
Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka.
55. Basi
walipo tughadhibisha hadi ya kutughadhibisha, kwa kupita kwao mipaka ya ufisadi,
tuliwaangamiza kwa kuwazamisha wote.
56. Tukamfanya
Firauni na kaumu yake kuwa ni viongozi wa makafiri wa baada yao katika kustahiki
mfano wa adhabu yao, na kuwa ni masimulizi ya namna ya ajabu ya watu wote
kuyazingatia.
57. Na alipo
pigiwa mfano Isa bin Maryam katika kuwa kwake kama Adam kwa kuwa Mwenyezi Mungu
alimuumba kwa udongo, kisha akamwambia: Kuwa, na akawa, s.l. Basi yeye ni mtumwa
aliye umbwa, aliye neemeshwa kwa kupewa Unabii, s.l. Haifai kumuabudu badala ya
Mwenyezi Mungu. Na watu wako wanapuuza hizo sifa zinazo pigiwa mfano, na wala
hawafahamu.
58. Makafiri
wamesema: Je! Miungu yetu na Isa, nani bora? Ikiwa yeye yuko Motoni basi sisi na
miungu yetu tutakuwa pamoja naye. Hawakupigii mfano huu wewe ila kutafuta ubishi
tu, na kushindana kwa maneno, si kwa ajili ya kuitafuta kweli ilivyo. Bali hawa
ni watu ambao ni shadidi wa khasama, wamebobea kwa hayo.
59. Isa si
chochote ila ni mja tuliye mneemesha kwa kumpa Unabii, na tumemfanya awe ni
zingatio la ajabu kama ni mithali, kwa kumuumba bila ya baba, kwa Wana wa
Israili, wapate ushahidi wa ukamilifu wa uweza wetu.
60. Na lau
tungeli taka, tungeli wageuza baadhi yenu, enyi watu, mkawa ni Malaika
mkifuatana katika ardhi, kama wanavyo kufuateni watoto wenu, mjue kwamba Malaika
wananyenyekea kufuata kudra ya Mwenyezi Mungu. Basi vipi wao wastahiki Ungu?
61. Na hakika
Isa kwa kuzuka kwake bila ya baba, na kuponyesha kwake vipofu na wakoma ni
dalili ya kukaribia Saa ya Kiyama. Basi usiwe na shaka nayo. Na fuateni uwongofu
wangu na Mtume wangu. Hii ninayo kuitieni ndiyo Njia Iliyo Nyooka yenye
kufikilia Uwokovu.
62. Wala
asikuzuilieni Shetani kuifuata Njia Iliyo Nyooka. Hakika huyo ni adui aliye
dhaahiri uadui wake.
63. Na alipo
tumwa Isa kwa Wana wa Israili naye ana miujiza iliyo wazi, na Ishara zenye
kubainisha, aliwaambia: Nimekujieni na sharia yenye hikima nzuri, inayo kuiteni
muifuate Tawhidi (Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja). Na nimekujieni nikubainishieni
baadhi ya mambo mnayo khitalifiana kwayo katika mambo ya Dini ili mpatane kwenye
Haki. Basi iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi katika hayo ninayo
kuitieni.
64. Hakika
Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye Muumba wangu, na ni Muumba wenu, basi muabuduni
Yeye pasi mwenginewe. Na ihafidhini sharia yake. Hii ninayo kuitieni muifuate ni
Njia Iliyo Nyooka itakayo kufikisheni kwenye uwokovu.
65. Makundi
mbali mbali yakakhitalifiana baina ya Wakristo baada ya Isa, kwa kufarikiana juu
yake. Maangamizo yatawafika hao walio dhulumu kwa waliyo yasema juu ya Isa ya
ukafiri, watapata adhabu kali na chungu Siku ya Kiyama.
66. Makafiri
hawangojei kitu baada ya kuipuuza Imani ila kuwafikia Saa kwa ghafla, nao
wameghafilika nayo.
67. Marafiki
walio kusanyika duniani kwa upotovu, watakuwa maadui wao kwa wao siku itakapo
wafikia Saa kwa ghafla, na yatakatika mapenzi yote, ila mapenzi ya wenye
kuogopa, nao wangali duniani, kuiogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu, na
wakashikamana huko duniani katika kumt'ii Yeye.
68. Mwenyezi
Mungu atawaambia wachamngu kwa kuwafanyia hishima: Enyi waja wangu! Leo msikhofu
adhabu yoyote, wala msihuzunike. Mmekwisha salimika na adhabu. Na Mwenyezi Mungu
amekudhaminieni thawabu.
69. Walio
ziamini Ishara za Mwenyezi Mungu na wakamt'ii Yeye, na wakawa wanamnyenyekea.
70. Siku ya
Kiyama wataambiwa kwa kufanyiwa hishima: Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu,
nanyi mmo katika furaha iliyo kubwa, ambayo itadhihiri kwenye nyuso zenu.
71. Na baada
ya kuingia Peponi watakuwa wakizungukiwa kwa sahani za dhahabu, na bilauri
kadhaalika, na humo watapata vyakula namna mbali mbali, na vinywaji vya kila
namna. Na humo Peponi watapata kila kitamaniacho moyo, na kituzacho macho. Na
kukamilisha furaha wataambiwa: Nyinyi mtakaa milele katika neema hizi.
72. Na
kutimiza neema, wataambiwa: Hii ndiyo Pepo mliyo ipata kwa sababu ya vitendo
vyema mlivyo vitanguliza mlipo kuwa duniani.
73. Humo
mtapata matunda ya namna nyingi, na kwa wingi, mtastarehe kuyala.
74. Hakika
walio tenda makosa kwa ukafiri watakuwamo katika adhabu ya Jahannamu daima
dawamu.
75.
Hawapunguziwi adhabu wakosefu hawa, wala haisitishwi, na wao watakata tamaa ya
kuokoka.
76. Wala Sisi
hatukuwadhulumu wakosefu hawa kwa adhabu hii, lakini wao wenyewe ndio walio
jidhulumu nafsi zao kwa kukhiari upotofu kuliko uwongofu.
77. Na
wakosefu, watapo kwisha kata tamaa ya kupunguziwa adhabu kali, watamwita Malik,
huyo ni askari wa Motoni wakimwambia: Mwombe Mola wako Mlezi atufishe tupumzike
na adhabu ya Jahannamu. Na Malik awambie: Nyinyi mtakaa humu humu katika adhabu
milele!
78. Mwenyezi
Mungu Mtukufu atawaambia kwa kuwarudi: Nyinyi alikujilieni Mtume wetu, enyi watu
wa Makka, kukuleteeni Dini ya Haki. Wakaamini wachache, na wengi wenu mkakataa.
Nao hawaipendi Haki.
79. Kwani ndio
waliweza washirikina wa Makka kutimiza hivyo vituko vyao kumkadhibisha Mtume na
kupanga njama za kumuuwa? Bali Sisi kwa hakika tuliweza jambo katika kuwalipizia
wao na kukupa ushindi wewe juu yao.
80. Ati
wanadhani hawa washirikina kwamba Sisi hatuyasikii maneno yao wenyewe wanapo
panga njama, na wanapo semezana kwa siri katika kukanusha haki? Kwani!
Twawasikia. Na Malaika wanao dhibiti kauli zao wanayaandika hayo.
81. Waambie
hao washirikina: Ikithibitika kwa ushahidi kuwa kweli Mwenyezi Mungu Mwingi wa
Rehema ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu mwana huyo. Lakini
hayo hayakuthibiti kwa hoja yoyote kwamba Rahmani ana mwana, kwa kuwa hayo ni
kumfanya Mwenye nguvu awe hajiwezi, Mwenye kujitosha awe mhitaji. Na Yeye,
Subhanahu, ametakasika na kila la upungufu kwa ukamilifu wake.
82.
Ametakasika kwa mtakasiko wa Mwenye kuziumba mbingu na ardhi na A'rshi Tukufu,
kwa yote wanayo msifia washirikina, ambayo hayaelekeani na Ungu wake.
83. Basi
waachilie wazame katika upotovu wao, na wacheze katika dunia yao, wayaache mambo
yenye maana, wala wasiyashughulikie, mpaka iwajie Siku ya Kiyama waliyo ahidiwa,
ipate kila nafsi kulipwa kwa iliyo yachuma.
84. Na Yeye
ndiye anaye abudiwa mbinguni kwa haki, na anaabudiwa katika ardhi kwa haki. Na
Yeye, peke yake, ndiye Mwenye hikima za mwisho katika vitendo vyake na mipango
yake, Mwenye kujua kila kitu kilicho kuwa na kitakacho kuwa.
85. Na
ametukuka na ametaadhamu Yeye ambaye, peke yake, Mwenye ukamilifu wa kutekeleza
katika mbingu na ardhi na baina yao katika viumbe vya angani vinavyo onekana na
vyenginevyo, na mipango yote iko kwake, na Yeye tu ndiye Mwenye kujua wakati wa
Kiyama, na kwake Yeye peke yake, mtarejeshwa mwishoe kwa ajili ya hisabu.
86. Na hio
miungu yao wanayo iabudu badala ya Mwenyezi Mungu haimiliki uweza wa kuwaombea
hao wanao waabudu. Lakini wenye kushuhudia kwa Tawhidi, yaani hao wanao amini ya
kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mola wao Mlezi kwa haki, hao wanaweza kuombewa
miongoni mwa Waumini atakao Mwenyezi Mungu kuwaombea.
87. Na ewe
Mtume! Ukiwauliza hawa washirikina nani aliye waumba, bila ya shaka watasema:
Kawaumba Mwenyezi Mungu. Basi inakuwaje wakaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu
Mtukufu wakenda kuwaabudu wenginewe, nao wanakiri kuwa Yeye ndiye Muumba wao?
Ama hakika jambo hili ni la ajabu!
88. Naapa kwa
kauli ya Muhammad s.a.w. anapo omba na kuita: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa
wenye inda ni watu wasio tarajiwa kuamini.
89. Basi
waachilie mbali, ewe Mtume, kwa wingi wa inda yao, na waambie: Langu mimi
nikukuacheni kwa salama yenu kutoka kwangu, na salama yangu kutoka kwenu. Nanyi
mtakuja jua kuwa mwisho wa inda yao ni khasara iliyo wazi.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani