1,2. H'a Mim,
A'yn Sin Qaf: Sura imeanzia kwa harufi hizi za kutamkwa kama ilivyo ada katika
Sura nyingi katika Qur'ani.
1,2. H'a Mim,
A'yn Sin Qaf: Sura imeanzia kwa harufi hizi za kutamkwa kama ilivyo ada katika
Sura nyingi katika Qur'ani.
3. Mfano wa
yaliyomo katika Sura hii anakufunulia wewe na Mitume walio kuwa kabla yako,
Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kwa nguvu zake, ambaye amepanga kila kitu kwa
pahala pake, kwa mujibu wa hikima katika vitendo vyake na mipango yake.
4. Ni vya
Mwenyezi Mungu, peke yake, vyote viliomo katika mbingu na ardhi, kwa kuviumba,
kuvimilika, na kuviendesha. Naye ni peke yake aliye tukuka kwa nafsi, na ukawa
mkuu ufalme wake.
5. Mbingu, juu
ya ukubwa wake na kushikamana kwake, zimekaribia kupasuka kutoka huko juu kwa
kumwogopa Mwenyezi Mungu, na kuathirika kwa taadhima yake na utukufu wake. Na
Malaika wanamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisilo elekea naye, na humsifu kwa
analo stahiki. Na humwomba Mwenyezi Mungu awasamehe watu wa duniani. Na Yeye
Subhanahu ananabihisha kwamba hakika ni Mwenyezi Mungu tu, peke yake, ndiye
Mwenye maghfira ya wote, na rehema iliyo kunjufu.
6. Na hao walio
wafanya wengineo badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ndio wa kuwanusuru, Mwenyezi
Mungu anaangalia hayo wayatendayo. Wala wewe hukupewa kazi hiyo ya kuwaangalia
wao.
7. Na mfano wa
ufunuo huo ulio wazi, tumekufunulia wewe hii Qur'ani kwa lugha ya Kiarabu isiyo
na ubabaishi, ili upate kuwaonya watu wa Makka na walio pembezoni mwake katika
Waarabu, na uwaonye watu adhabu ya siku watakao kusanywa khalaiki wote kwa ajili
ya hisabu. Hapana shaka yoyote kuja siku hiyo. Watu siku hiyo watakuwa mafungu
mawili - fungu moja litakuwa Peponi. ma kundi jengine litakuwa Motoni.
8. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu angeli penda kuwakusanya watu wote katika dunia wakafuata njia
moja angeli wakusanya hivyo. Lakini Yeye humtia katika rehema yake amtakaye, kwa
kuwa anajua kuwa hao wamekhiari uwongofu kuliko upotofu. Na wenye kujidhulumu
nafsi zao kwa ukafiri hawana mlinzi badala ya Mwenyezi Mungu wa kudhamini
kuwalinda, wala msaidizi wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
9. Hawa wenye
kudhulumu hawakumfanya Mwenyezi Mungu kuwa ni mlinzi wao, bali wamewafanya
wengineo kuwa ndio walinzi wao. Na wala haiwafalii wao hayo. Kwani Mwenyezi
Mungu, peke yake, ndiye Mwenye kustahiki kuwa Mlinzi kama wao wanataka mlinzi.
Yeye ndiye anaye fufua walio kufa kwa ajili ya hisabu. Na Yeye ndiye Mwenye
madaraka juu ya kila kitu kwa uweza wake.
10. Na mliyo
khitalifiana kwayo katika mambo yaliyo khusu Imani na ukafiri, hukumu yake ya
kukata iko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye amekwisha ibainisha. Yeye huyo ndiye
Hakimu wa kuhukumu mliyo khitalifiana, Mwenyezi Mungu, Mwenye kumiliki mambo
yangu yote. Mimi namtegemea Yeye kwa mambo yangu. Na kwake Yeye peke yake ndio
narejea ili kutafuta uwongozi.
11. Yeye ndiye
aliye ziumba mbingu na ardhi, na akakuumbieni katika jinsi yenu wanaume na
wanawake, na akaumba katika mifugo yenu kadhaalika madume na majike, na kwa
mpango huu ndio wazidi kuwa wengi. Hapana kitu chochote kama mfano wake Mwenyezi
Mungu, basi hana kitu cha kuwa wa pili yake. Na Yeye ndiye Mwenye kujua, kwa
ujuzi wa kukamilika, kuvijua vyote vinavyo sikilizana na kuonekana bila ya
taathira ya hisiya.
12. Yeye
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi, kwa kuzihifadhi na
kuzitumia. Humkunjulia riziki amtakaye, na humdhikisha amtakaye. Hakika Yeye,
Mtukufu, ujuzi wake umezunguka kila kitu.
13.
Amekufanyieni sharia itikadi kama alivyo agana na Nuhu, na tulizo kufunulia wewe
kwa Wahyi, na tulivyo agana na Ibrahim, na Musa, na Isa, ya kwamba mzitie imara
nguzo za Dini, kwa kuyafuata yaliyo letwa na Dini, wala msikhitalifiane katika
jambo hilo. Ni uzito kwa washirikina hayo unayo waitia ya kusimamisha nguzo za
Dini. Mwenyezi Mungu humteuwa kwa ajili ya Ujumbe wake amtakaye, na humwezesha
na kumsaidia katika Imani na kusimama katika Dini mwenye kuacha inda na
kumwelekea Yeye.
14. Wala
hawakukhitalifiana katika Dini wafuasi wa Mitume walio tangulia ila baada ya
kuwafikia ujuzi wa kweli, na hayo ni kwa kutokana na uadui na uhasidi ulio baina
yao. Na lau kuwa si ahadi iliyo kwisha tangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya
kuakhirisha adhabu mpaka Siku ya Kiyama, basi bila ya shaka walingeli teketezwa.
Na kwa hakika wale walio rithishwa Kitabu kutokana na walio kabla yao, na
wakawahi zama zako, wana shaka na Kitabu chao, tena shaka ya kuwatatanisha. Ndio
maana hawaitikii wito wako. (Lau kuwa Mayahudi wameamini kweli yaliyomo katika
Taurati, wangeli muamini Nabii Isa na Nabii Muhammad. Na lau kuwa Wakristo
wameamini kweli yaliomo katika Taurati na Injili basi hapana la kuwazuia
wasimuamini Nabii Muhammad, na kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, wala hana Utatu.
Lakini hawana imani ya yakini, na kwa hivyo wameunda mawazo yaliyo nje ya
Taurati na nje ya Injili.)
15. Basi kwa
ajili ya umoja wa Dini, na kuondoa mtafaruku ndani yake, waite waishike Dini, na
shikilia Wito huo kama alivyo kuamrisha Mwenyezi Mungu, wala usitafute kuyaridhi
matamanio ya washirikina. Na sema: Mimi naamini Vitabu vyote alivyo wateremshia
Mwenyezi Mungu Mitume wake, na Mwenyezi Mungu ameniamrisha nisimamishe uadilifu
baina yenu. Na waambie: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wetu, na ndiye Muumba wenu.
Vitendo vyetu ni vyetu sisi, si vyenu. Na vitendo vyenu ni vyenu nyinyi, si
vyetu. Hapana la kubishana baina yetu na nyinyi, kwani haki iwazi. Mwenyezi
Mungu atatukusanya kwa kutuhukumu kwa uadilifu. Na kwake Yeye peke yake ndio
marejeo ya kurejea.
16. Na hao
wanao bisha katika mambo yaliyo khusu Dini ya Mwenyezi Mungu, baada ya watu
kwisha uitikia Wito ulio wazi, ubishani wa watu hawa wenye shaka shaka ni
baat'ili mbele ya Mola wao Mlezi. Na juu yao ipo ghadhabu kali kwa ukafiri wao.
Na adhabu chungu inawangojea.
17. Mwenyezi
Mungu ndiye aliye teremsha Kitabu cha Muhammad na viliyo kuwa kabla yake katika
Vitabu vya Mitume, vyenye kukusanya Haki na uadilifu. Na nini cha kukujuvya,
pengine wakati wa Saa ya Kiyama ipo karibu na wewe hujui.
18. Wanahimiza
ije Saa ya Kiyama upesi upesi, kwa maskhara, hao wasio iamini. Na wenye kuiamini
wamo katika khofu isitokee. Hao hawaihimizi. Na wanajua kuwa hiyo ni kweli iliyo
thibiti, wala haina shaka. Naye Subhanahu anazindua kwamba hao wanao bisha kuja
kwake bila ya shaka wamo katika upotovu ulio mbali na Haki.
19. Mwenyezi
Mungu, ni mkuu wa kuwafanyia wema waja wake wote. Huwaruzuku awatakao kama
anavyo taka. Naye ni Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye nguvu asiye shindika.
20. Mwenye
kutaka kulipwa kwa a'mali yake thawabu za Akhera atalipwa mara mbili ujira wake.
Na mwenye kutaka kwa a'mali yake starehe ya dunia tu, basi tutampa fungu lake
hilo, na huko Akhera hatakuwa na fungu lolote la thawabu.
21. Kwani wao
wanao miungu walio watungia dini nyengine asiyo iamrisha Mwenyezi Mungu?
Hayakuwa hayo! Na lau halikwisha tangulia agano la kuakhirisha hukumu mpaka Siku
ya Kiyama, basi bila ya shaka pangeli hukumiwa baina ya makafiri na Waumini hapa
hapa duniani. Na hakika walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri watapata adhabu
yenye machungu makali.
22. Ewe unaye
semezwa! Utawaona Siku ya Kiyama hao walio jidhulumu nafsi zao kwa ushirikina
wamo katika khofu kuogopa malipo ya ushirikina wao, nayo yatawateremkia tu
hapana hivi wala hivi. Na utawaona wenye kuamini na wakatenda mema wamestarehe
katika mwahali mzuri kabisa katika Pepo. Humo watapata neema wazitamaniazo kwa
Mola wao Mlezi. Hayo ndiyo malipo makubwa, na ndio fadhila kubwa ya kutarajiwa.
23. Hiyo
fadhila kubwa ndiyo ambayo Mwenyezi Mungu amewabashiria waja wake Waumini,
wat'iifu. Ewe Mtume! Sema: Mimi sitaki kwenu ujira kwa kufikisha huu Ujumbe,
isipo kuwa mumpende Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika kujikurubisha kwenu
kwake Yeye Subhanahu, kwa vitendo vyema. Na mwenye kutenda ut'iifu Mwenyezi
Mungu atampa ujira mara mbili. Hakika Mwenyezi Mungu ni mkunjufu wa maghfira kwa
wenye madhambi, ni Mwenye shukrani kwa waja wake wenye vitendo vyema.
24. Je!
makafiri wanasema Muhammad anamzulia uwongo Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu
akipenda atakufungia moyo wako usubiri maudhi yao, na tuhuma yao kuwa unamzulia
Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ataondoa na ataushinda ukafiri na ataupa nguvu
Uislamu na ataudhihirisha kwa wa'hyi alio mteremshia Mtume wake s.a.w., kwani -
Yeye- Mwenyezi Mungu anajua yote yaliomo ndani ya nyoyo zenu nyote.
25. Ni
Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kupokea toba kwa watu wanao mt'ii hata kwa
makosa yaliyo zaidi kuliko yale wanayo ombea toba. Na Yeye ndiye anaye samehe
madhambi yote isipo kuwa shirki, kwa kufadhili na kurehemu; na anayajua
myatendayo ikiwa ya kheri au shari.
26. Na
huwaitikia Waumini kwa wanayo yaomba, na huwazidishia juu ya hayo wanayo yaomba.
Na makafiri watapata adhabu yenye kufikia ukomo wa ukali na uchungu.
27. Na lau
kuwa Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia waja wake wote, kama watakavyo, basi bila
ya shaka wangeli panda kiburi katika ardhi wakafanya dhulma. Lakini Mwenyezi
Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humdhikisha amtakaye, kwa mujibu wa hikima
yake. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua vyema mambo yote ya waja wake, ya siri na
dhaahiri. Basi Yeye humkadiria kila mmoja kwa linalo msilihi kwa mujibu wa
hikima yake.
28. Na
Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye anaye iteremsha mvua inayo waokoa na ukame
baada ya kwisha kata tamaa na kuzidi kiangazi, kuwa ni rehema kwa waja wake. Na
Yeye hueneza baraka za mvua katika mimea, na miti ya matunda, na wanyama, na
nyanda, na milima. Na Yeye, peke yake, ndiye Mwenye madaraka ya kuyapanga mambo
yote ya waja wake, na ndiye wa kuhimidiwa kwa neema zake, na vitendo vyake
vyote.
29. Na katika
dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu kuumba atakacho ni huku kuumba mbingu na ardhi
kwa nidhamu iliyo pangwa; na kuumbwa vilivyo tenganishwa humo na kuenezwa
wanayama wanao onekana na wengineo. Na Mwenyezi Mungu aliye hakikisha uweza wake
kwa kuumba hivyo vilio tajwa ni Muweza wa kuwakusanya wote katika wakati autakao
kuwafufulia kwa ajili ya malipo.
30. Na msiba
wowote unao kusibuni mnao uchukia ni kwa sababu ya maasi yenu. Na anayo yasamehe
Mwenyezi Mungu duniani au akayachukulia ahadi humo, basi Mwenyezi Mungu ni
Karimu; hatokuwa tena wa kuadhibu kwa hayo Akhera. Na Kwa hivi ametakasika na
dhulma, na amesifika kwa rehema kunjufu.
31. Wala
nyinyi hamwezi kumshinda Mwenyezi Mungu na kumzuilia asilete masaibu duniani
kuwa ni adhabu kwa ajili ya maasi yenu, na hata mkikimbia vipi. Na wala hamna
asiye kuwa Mwenyezi Mungu wa kukurehemuni pindi ikikuteremkieni balaa, wala
hamna wa kukunusuruni nayo.
32. Na katika
dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, ni majahazi yaendayo katika bahari kama
vilima virefu kwa ukubwa wake.
33. Mwenyezi
Mungu akipenda huutuliza upepo kukawa shuwari; basi majahazi yaliyo thibiti juu
ya bahari hutulia hayendi huko yendako. Hakika huko kwenda kwao na kusimama kwao
kwa amri ya Mwenyezi Mungu ni dalili wazi juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu.
Wanayazingatia hayo Waumini wenye kusubiri wakati wa dhiki, na wenye kushukuru
wakati wa furaha.
34. Au
akayateketeza hayo majahazi kwa sababu ya madhambi ya walio panda, kwa
kuwapelekea upepo wa kimbunga. Na Mwenyezi Mungu akipenda anasamehe mengi; kwa
kuwa hawaadhibu kwa kuzuia upepo na kuleta shuwari, au kwa kuleta kimbunga cha
kuwazamisha.
35. Mwenyezi
Mungu, Subhanahu, hufanya hayo ili Waumini wapate kuzingatia, na wajue wale
wanao zirudi Ishara zake kwa upotovu kwamba wao wamo katika mkono wake, wala
hawana pa kuikimbia adhabu yake.
36.
Msidanganyike na starehe za dunia. Kwani enyi watu! Yote mliyo pewa, mali, wana,
na vyenginevyo, ni starehe zenu za maisha ya duniani. Na aliyo yaandaa Mwenyezi
Mungu katika neema za Peponi ni bora na zinadumu zaidi kwa wenye kuamini, na
kumtegemea Muumba wao na Mlezi wao wa pekee;
37. Na wanao
jitenga mbali na kupanda madhambi makubwa makubwa aliyo yakataza Mwenyezi Mungu,
na madhambi yote yaliyo zidi ubaya, na pindi wakichochewa kwa kufanyiwa mabaya
katika mambo ya dunia yao, wao wenyewe wakawa mbele kuanza kusamehe ili kuleta
masikilizano;
38. Na wanao
uitikia wito wa Muumba wao na Mlezi wao, na wakamuamini, na wakazihifadhi Sala
zao, na ukawa mwendo wao ni kushauriana katika mambo yao ili upatikane uadilifu
katika jamii zao, bila ya mtu mmojapo au kikundi cha wachache kutaka kuwatumilia
mabavu wenginewe, na wakawa wanatoa kwa njia za kheri kutokana na neema alizo
mneemesha Mwenyezi Mungu;
39. Na wale
ambao anapo wavamia mwenye kudhulumu wao wanajitetea nafsi zao kuupinga ule
uvamizi wake.
40. Na malipo
ya mwovu, ni kumtendea uovu kama wake, kwa kufuata uadilifu. Lakini mwenye
kusamehe uovu alio tendewa, naye anaweza kulipiza, na akaleta masikilizano baina
yake na yule khasimu yake, kwa kujenga mapenzi, basi thawabu zake ziko kwa
Mwenyezi Mungu. Hapana anaye zijua kadiri yake isipo kuwa Yeye. Hakika Mwenyezi
Mungu hawarehemu wavamizi wanao fanya uadui katika haki za watu, kwa kuzikiuka
sharia za Mwenyezi Mungu.
41. Hakika
wanao wapa adhabu wavamizi kama wanavyo fanya uadui wao, hao hawaingiliwi wala
hawalaumiwi.
42. Bali
lawama na kushikwa haki ni juu ya wanao fanya uadui, wakadhulumu watu, na
wakafanya kiburi katika nchi, na wakafisidi humo bila ya haki. Hao watapata
adhabu yenye uchungu mkali.
43. Ninaapa:
Bila ya shaka, mwenye kuvumilia kudhulumiwa, akamwachilia aliye mdhulumu, wala
asiitetee nafsi yake, pindi ikiwa huko kusamehe kwenyewe hakuupalilii ufisadi
ukapata nguvu katika nchi, hakika hayo ni katika mambo ambayo yanatakikana
mwenye akili ajilazimishe kuyatenda.
44. Na mwenye
kuipotea Njia ya Uwongofu kwa kuwa hana ujuzi mwema, basi hana wa kumnusuru
isipo kuwa Mwenyezi Mungu, ndiye wa kumwongoa na wa kumkinga na adhabu. Na, ewe
unaye semezwa! Utaona Siku ya Kiyama wale wenye kudhulumu watakapo iona adhabu
ya Akhera wanamuuliza Mola wao Mlezi, watumie mbinu gani wapate kurejea duniani,
ili wapate kutenda mema, siyo waliyo kuwa wakiyatenda kwanza?
45. Na
kadhaalika, utawaona walio dhulumu, wakipelekwa Motoni, wamenywea kwa sababu ya
unyonge ulio tokana na hivyo vitisho walivyo vikuta, wakitupia jicho kwa kificho
kwenye huo Moto kwa kuukhofu vituko vyake. Na hapo Waumini watasema: Hakika
walio khasiri kweli ni hao walio dhulumu nafsi zao kwa ukafiri wao, na
wakawakhasiri wake zao na watoto wao na jamaa zao kwa mfarakano walio usabibisha
baina yao. Na Mwenyezi Mungu ananabihisha kwamba wenye kudhulumu watakuwa katika
adhabu ya milele.
46. Na wala
hawatakuwa wa kuwanusuru kutokana na ile miungu ya uwongo walio kuwa wakiiabudu
badala ya Mwenyezi Mungu, na walio kuwa wakiit'ii katika kumuasi Mwenyezi Mungu,
waje kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kupotea Njia ya Haki kwa
kuto kuwa na ujuzi, basi hatokuwa na njia ya kumwokoa na mwisho muovu.
47. Enyi watu!
Kimbilieni kuitikia aliyo kuitieni Mtume wa Mwenyezi Mungu aliye kuumbeni na
akakuleeni, nayo ni Imani na Ut'iifu, kabla uhai haujamaliza fursa ya kutenda
vitendo, na ikafika Siku ya Hisabu ambayo Mwenyezi Mungu hairudishi nyuma tena
baada ya kwisha ihukumia. Siku hiyo hamtakuwa na pa kukimbilia pa kukuhamini na
adhabu, wala hapana cha kuzuia kitakacho kufikieni.
48. Wakipuuza
washirikina kukuitikia wewe, ewe Mtume, basi usihuzunike. Kwani wewe si
mwangalizi wao kwa hayo wanayo yatenda. Wewe umelazimishwa kufikisha Ujumbe tu,
na hayo umeyabainisha wazi. Na tabia ya watu tukiwapa wasaa hupanda kiburi. Na
ukiwasibu msiba kwa sababu ya maasi yao, mara wanasahau neema, wanahuzunika kwa
kuteremkiwa na balaa, na wanaingia katika kufuru.
49. Ni wa
Mwenyezi Mungu peke yake Ufalme wa mbingu na ardhi, kwa kuumba, kuudabiri, na
kuusarifu. Yeye anaumba atakacho. Humtunukia amtakaye wana wa kike, na
akamtunukia amtakaye wana wanaume bila ya wanawake.
50. Na Yeye
Subhanahu humfadhili amtakaye kwa kumchanganyia wanaume na wanawake, na
akamfanya amtakaye bila ya mtoto yeyote. Hakika Mwenyezi Mungu anajua vyema kila
kitu. Ni Muweza wa kutenda kila akitakacho.
51. Wala
haimfalii mtu kusemezwa na Mwenyezi Mungu ila iwe kwa Wahyi (Ufunuo) kwa
kumtilia ilhamu katika moyo wake, au usingizini, au kwa kusikia maneno ya Kiungu
bila ya kumwona Asemaye, au kwa kutumwa Malaika akaonekana sura yake, na
akasikilizana sauti, akamfunulia Nabii kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama
atakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtenda nguvu, basi haziwiliki Mwenye kupita
ukomo hikima yake katika kuendesha mambo yake na kupanga kwake.
52. Na kama
tulivyo wafunulia Mitume kabla yako, basi tumekufunulia nawe, ewe Mtume, hii
Qur'ani ili ihuishe nyoyo kwa amri yetu. Kabla ya kuletewa wewe hii ulikuwa
hujui nini Qur'ani, wala hujui Sharia za Imani. Lakini tumeifanya Qur'ani kuwa
ni Nuru Kubwa ya kuwaongoza wenye kukhiari Uwongofu. Na wewe bila ya shaka
utakuwa ukiwaitia watu kwa hii Qur'ani kwenye Njia Iliyo Nyooka.
53. Njia ya
Dini ya Mwenyezi Mungu ambaye ndiyo vyake Yeye tu peke yake, vyote viliomo
mbinguni na katika ardhi, kwa kuumba, na kupanga, na kuendesha. Naye
ananabihisha, Subhanahu, kwamba kwake Yeye peke yake ndio yanarejea mambo yote.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani