1. (H'a Mim) Hizi harufi mbili
katika harufi za alifbete zilio fungulia Sura hii kama ilivyo ada ya Qur'ani
katika Sura nyingi, ili kuzindua watu watanabahi, na pia kuonyesha dalili ya
muujiza wa Qur'ani.
2. Kitabu hichi ni
mteremsho wa namna ya peke yake, kutokana na Mneemeshaji wa neema kubwa na neema
ndogo.
3. Kitabu hichi ni namna
ya peke yake kwa uzuri wake kwa matamshi na ibara yake ya utungaji, na kwa maana
inavyo pambanua baina Haki na baat'ili, na bishara na onyo, na kuzitengeneza
nafsi, na kupiga mifano, na kubainisha hukumu. Nacho kinasomwa kwa ulimi wa
Kiarabu, chepesi kukifahamu kwa watu wanao jua.
4. Chenye kuwapa khabari
njema Waumini wenye kutenda kuwa watapata neema iliyo andaliwa kwa ajili yao, na
kuwakhofisha wanao kanusha kuwa watapata adhabu chungu iliyo andaliwa kwa ajili
yao. Lakini wengi walikitupilia mbali, wala wasinafiike nacho, kama kwamba
hawakusikia.
5. Na makafiri wakamwambia
Mtume s.a.w.: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko vizito kwa hayo unayo tuitia
yaliyo khusu Tawhidi (Upweke) wa Mwenyezi Mungu. Na masikioni mwetu mna uziwi,
basi hayasikii hayo unayo tulingania. Na baina yetu na wewe lipo pazia nene
linalo tuzuia kukubali hayo uliyo tuletea. Basi fanya utakalo, na sisi tunafanya
tutakalo.
6,7. Ewe Mtume! Waambie:
Hakika mimi si chochote ila ni mtu mfano wenu nyinyi, napata Wahyi (Ufunuo)
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwamba wa kuabudiwa kwa haki na nyinyi ni Mungu Mmoja
tu. Basi fuateni Njia Iliyo Nyooka ya kwendea kwake! Na mtake kwake msamaha kwa
madhambi yenu. Na washirikina wasio toa Zaka kuwapa wanao stahiki watapata
adhabu kali. Na wao tu, si wenginewe, ndio wanao kataa kuwa upo uhai wa Akhera.
6,7. Ewe Mtume! Waambie:
Hakika mimi si chochote ila ni mtu mfano wenu nyinyi, napata Wahyi (Ufunuo)
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwamba wa kuabudiwa kwa haki na nyinyi ni Mungu Mmoja
tu. Basi fuateni Njia Iliyo Nyooka ya kwendea kwake! Na mtake kwake msamaha kwa
madhambi yenu. Na washirikina wasio toa Zaka kuwapa wanao stahiki watapata
adhabu kali. Na wao tu, si wenginewe, ndio wanao kataa kuwa upo uhai wa Akhera.
8. Hakika Waumini wanao
tenda mema watapata malipo mazuri yasiyo katika.
9. Ewe Mtume! Waambie hawa
washirikina: Ama nyinyi mnastaajabisha! Mnamkataa Mwenyezi Mungu aliye iumba
ardhi kwa siku mbili, na huku juu ya hayo, mnamfanyia washirika wa kushirikiana
naye huyo Muumba ardhi, Mmiliki wa walimwengu wote na Mlezi wao? Zimetajwa Siku
moja au Siku nyingi katika Sura nyengine. Katika Surat Al-Hajj, Aya 47 Mwenyezi
Mungu Mtukufu amesema: "Na kwa hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama
miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi." Na katika Surat Assajdah, Aya 5 amesema
Mtukufu: "Anapitisha mambo yote yaliyo baina ya mbingu na ardhi, kisha yanapanda
kwake kwa siku moja tu ambayo kipimo chake ni miaka elfu mnayo hisabu." Na
katika Surat Al-Ma'arij Mtukufu amesema: "Malaika na Roho hupanda kwake katika
siku iliyo kadiri yake ni miaka elfu khamsini." Maoni ya kitaalamu: Vipimo vya
wakati wanavyo vitumia watu vimefungamana na dunia na inavyo zunguka juu ya
msumari-kati wake na kulizunguka jua. Mtu akitoka kwenye ardhi (dunia) akenda
kwenye sayari nyengine za mbinguni vipimo hivyo vya nyakati vinabadilika kwa
kuzidi au kwa kupungua. Na hizi Aya tukufu zinaonyesha ishara ya ukweli huu wa
ki-ilimu, na ya kwamba zama au nyakati ni jambo la mlinganisho tu. Na bila ya
shaka ipo miaka ya ki-ilimu ya Falaki ya kulinganisha yenye kumkinika
kuifarikisha baina yao. Mwaka wa ki-jua wa duniani huhisabiwa kwa kupimwa wakati
ambao dunia inachukua kulizunguka jua kwa ukamilifu mnamo siku 365, na ilhali
sayari zilio karibu na jua kama U't'aarid (Mercury) humaliza safari yake ya
kulizunguka jua mnamo siku 88, na upande mwengine sayari ya Blutu (Pluto) ambayo
ndiyo sayari iliyo mbali mno na jua, na ndiyo inazunguka taratibu mno inachukua
kuzunguka kwake mnamo miaka 250 kwa mujibu wa miaka yetu sisi.
10. Naye Mwenyezi Mungu
amesimamisha juu ya ardhi milima iliyo simama imara ili isiyumbe nanyi; na
akakithirisha humo kheri nyingi, na akakadiria humo riziki kwa watu wake, kwa
mujibu wa hikima yake, mnamo siku nne. Na nyinyi, juu ya haya, mnakwenda
kumwekea washirika? Na Yeye amekadiria kila kitu bila ya upungufu wala kuzidi.
Kufafanua huku katika uumbaji wa ardhi na vilio juu yake ni maelezo kwa hao
wanao uliza.
11. Kisha amekhusisha
uweza wake na kuumba mbingu, nazo zilikuwa kama moshi, basi zikawapo. Na kuumba
kwake mbingu na ardhi kwa mujibu wa mapendo yake ni jambo jepesi kwake, ni kama
kukiambia kitu: Njoo ukipenda usipenda, nacho kikat'ii.
12. Na akatimiza kuumba
mbingu saba mnamo siku mbili nyengine. Na akaweka katika kila mbingu alicho
kiandalia na ilivyo pelekea hikima yake. Na akaipamba mbingu ya karibu na dunia
kwa nyota zinazo ng'ara kama taa, kwa ajili ya uwongofu wasisikilize mashetani
khabari za walio juu. Kuumba huko vilivyo ni mpango wa Mwenyezi Mungu asiye
shindika, Mwenye kuzunguka kila kitu.
13. Basi washirikina
wakipuuza Imani baada ya kuwekewa wazi dalili zake, wewe, Mtume, waambie:
Nimekuonyeni msije kupatilizwa kwa adhabu kali kama iliyo wateketeza kina A'di
na Thamudi.
14. Walijiwa A'di na
Thamudi na hiyo adhabu walipo watokelea Mitume pande zote. Hawakuacha njia ya
kuwaongoza ila waliipitia, na wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu. Wao
wakasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli taka kumtuma Mtume basi angeli tuteremshia
Malaika. Basi sisi hakika tunakataa hayo ya Tawhidi na mengineyo mliyo kuja nayo
nyinyi.
15. Ama kina A'di
walipandwa na kiburi katika nchi bila ya haki ya kuwa na kiburi hicho. Na
walisema kwa kughurika na nafsi zao: Nani huyo anaye tushinda sisi kwa nguvu?
Ama ajabu watu hawa! Wanasema hayo na wao hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu aliye
waumba ana nguvu zaidi kuwashinda wao? Na wao walikuwa wakizikanya Ishara zetu!
16. Tukawapelekea upepo
wenye sauti kali katika siku korofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwafanya wawe
madhalili wanyonge katika maisha ya duniani. Na ninaapa kuwa bila ya shaka
adhabu ya Akhera itakuwa ya hizaya zaidi, wala wao siku hiyo hawatapata wa
kuwasaidia.
17. Na ama kina Thamudi
tuliwabainishia njia ya kheri na njia ya shari. Lakini wao walikhiari upotovu
kuliko uwongofu, ikawatwaa radi iliyo waunguza kwa madhila na unyonge, kwa
sababu ya madhambi waliyo yachuma.
18. Na tukawaokoa
kutokana na adhabu hii wale walio amini, na wakawa wanamcha Mwenyezi Mungu na
wanaiogopa adhabu yake.
19. Ewe Nabii! Siku
watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kupelekwa Motoni, wakawa wa mwanzo
wao wanakutana na wa mwisho wao, ili ipate hoja ilazimike juu ya wote,
20. Mpaka watakapo
ufikilia Moto na wakaulizwa juu ya madhambi waliyo yatenda duniani, na wao
wakakataa, yakawashuhudilia masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa waliyo
yatenda wao,
21. Na hao maadui wa
Mwenyezi Mungu wakaziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Na ngozi
zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu aliye tamkisha kila kitu. Na Yeye ndiye
aliye kuumbeni hapo mwanzo kabla hamjawa chochote. Na kwake Yeye, peke yake,
ndio mtarejea baada ya kufufuliwa, akuhisabieni mliyo kwisha yatanguliza katika
vitendo.
22. Wala nyinyi hamkuwa
mkiweza kuficha vitendo vyenu viovu hata viungo vyenu visivione na ikawa macho
yenu, na masikio yenu na ngozi zenu, vyote hivyo vikakushuhudilieni. Lakini
nyinyi mlikuwa mkidhani kuwa Mwenyezi Mungu hajui mengi katika vitendo vyenu,
kwa sababu mkivifanya kwa uficho.
23. Lakini dhana mbovu
mliyo kuwa mkimdhania Mola wenu Mlezi imekuhilikini, na kwa hivyo mmekuwa Siku
ya Kiyama katika wenye kukhasiri vibaya mno.
24. Basi hata wakijizuia
machungu yao, Moto ndio mwisho wao, na makaazi yao ya daima. Na wakitaka
kumridhi Mwenyezi Mungu sasa hawakubaliwi hayo matakwa yao.
25. Nasi tumewaandalia
duniani marafiki waharibifu, na wao wakawazainishia mbele yao mambo ya Akhera,
basi wakawaghuri kwamba ati hakuna kufufuliwa wala kuhisabiwa, na wakawapambia
pia mambo ya duniani ili wastarehe nayo. Na neno la adhabu lilio wapata mataifa
yaliyo kwisha pita miongoni mwa majini na watu walio kuwa kama wao,
likawathibitikia na wao kwa sababu ya kukhiari kwao upotovu badala ya uwongofu.
Hakika watu hao wote walikuwa katika walio khasiri khasara iliyo timia.
26. Makafiri wakaambizana
wenyewe kwa wenyewe: Msiisikilize hii Qur'ani, na inapo somwa nyie leteni porojo
lisio kuwa na maana, ili pasiwepo mtu wa kuisikia wala kunafiika kwayo, asaa kwa
hivyo mkamshinda Muhammad.
27. Tunaapa: Bila ya
shaka tutawaonjesha walio kufuru adhabu kali kwa vitendo vyao, na khasa kwa hivi
kuipiga vita Qur'ani. Na bila ya shaka tutawalipa malipo maovu kabisa kwa
vitendo vyao.
28. Hizo adhabu zilizo
tajwa ni malipo wanayo stahiki maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto walio andaliwa
katika makaazi ya kuishi milele, kuwa ni malipo kwa kule kuzikataa mfululizo
Ishara za Mwenyezi Mungu na hoja zake.
29. Na makafiri watasema,
nao wamo Motoni: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe hayo makundi ya majini na watu walio
tupoteza ili tuwaweke chini ya nyayo zetu, wawe katika watu wa chini kabisa.
30. Hakika walio sema:
Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, kwa kuukubali Upweke wake, kisha wakasimama
sawa sawa juu ya sharia zake, Malaika watawateremkia mara kwa mara wakiwaambia:
Msikhofu kukuteremkieni shari, wala msihuzunike kuwa mtakosa kheri, na furahini
kuwa mtapata Pepo mliyo ahidiwa kwa ndimi za Manabii na Mitume.
31,32. Na Malaika
watawaambia: Sisi ni wasaidizi wenu katika maisha ya duniani kwa kukuungeni
mkono, na Akhera kwa kukuombeeni shafaa na kukutukuzeni. Na huko Akhera mtapata
kila cha ladha na kizuri kinacho pendwa na nafsi zenu, na mtapata kila mnacho
kitamani kuwa ni takrima, na maamkio yanayo toka kwa Mola Mlezi Mkunjufu wa
maghfira na rehema.
31,32. Na Malaika
watawaambia: Sisi ni wasaidizi wenu katika maisha ya duniani kwa kukuungeni
mkono, na Akhera kwa kukuombeeni shafaa na kukutukuzeni. Na huko Akhera mtapata
kila cha ladha na kizuri kinacho pendwa na nafsi zenu, na mtapata kila mnacho
kitamani kuwa ni takrima, na maamkio yanayo toka kwa Mola Mlezi Mkunjufu wa
maghfira na rehema.
33. Hapana mwenye kauli
nzuri zaidi kuliko mwenye kulingania Tawhid ya Mwenyezi Mungu na ut'iifu wake,
na pamoja na hayo, akatenda vitendo vyema, na akasema kwa kuungama itikadi yake:
Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu, yaani wenye kunyenyekea amri za Mwenyezi
Mungu.
34. Haziwezi kuwa sawa
tabia njema na tabia mbovu. Pinga uovu ukikujia kutokana na adui kwa tabia iliyo
bora kuliko yake. Hapo matokeo yake ni huyo ambaye uliye kuwa na uadui naye
atakuja kuwa kama mwenzio wa kukunusuru mwenye moyo safi.
35. Na hawaruzukiwi tabia
hii, ya kulipa wema kwa uovu, ila wale wenye khulka ya kusubiri, na hawaruzukiwi
hayo ila wenye fungu kubwa la tabia ya wema na ukamilifu wa nafsi.
36. Na akitokea Shetani
akakutia wasiwasi kukuachisha hayo uliyo amrishwa, ewe unaye semezwa, basi
jilinde naye kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu kusikia kwake na kujua
kwake kumezunguka kila kitu. Na Yeye atakulinda naye.
37. Na katika dalili za
uweza wake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni huu usiku na mchana, na jua na mwezi.
Msilisujudie jua wala mwezi, kwani hivyo ni katika Ishara zake tu. Bali
msujudieni Yeye Mwenyezi Mungu peke yake, aliye umba jua, na mwezi, na usiku, na
mchana, ikiwa nyinyi kweli mnamuabudu Yeye peke yake.
38. Ikiwa washirikina
watajiona wakubwa hawafai kufuata amri yako, basi wewe usiudhike. Kwani hao
walio kwa Mola wako Mlezi kwenye utakatifu wake, nao ni Malaika, wanamtakasa
Yeye na kila upungufu katika kila wakati, usiku na mchana, wakimsafia ibada Yeye
tu, wala hawachoki kumsabihi.
39. Na katika dalili za
uweza wake, Mtukufu, ni kwamba unaona, wewe unaye weza kuona, ardhi kavu.
Tukiiteremshia maji inatikisika kwa mimea, na inaumuka na kuja juu. Hakika huyo
aliye ihuisha ardhi iliyo kwisha kufa ndiye aliye elekea kuhuisha wafu katika
hayawani. Yeye ni mtimilivu wa uweza juu ya kila kitu. Aya hii inabainisha
kwamba mawadi za mbolea ambazo ni chumvi chumvi zisio na uhai, pindi zipatapo
maji ya mvua, huyayuka, na kwa hivyo husahilika kufikilia kwenye mbegu za mimea
na mizizi yake. Hapo hugeuka kuingia katika khalaya (Cells) na mifumo na viungo
vilio hai. Na kwa hivyo vinaonekana kuwa ni hai. Na ukubwa wake hukua na kuzidi
kwa kuingiana na kukuzwa na mimea.
40. Hakika hao wanao
iacha Njia iliyo sawa kwa mintarafu ya Ishara zetu na wakaitupilia mbali kwa
kuikadhibisha, mambo yao hayatupotei Sisi wala hayo wanayo yakusudia. Nasi
tutawalipa kama wanavyo stahiki. Kwani anaye tupwa katika Moto ni bora au yule
anaye kuja naye hali katulia Siku ya Kiyama kwa kuokoka kwake na kila ovu?
Kabisa hao hawalingani. Waambie kwa kuwaahidi: Fanyeni mtakavyo. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuzunguka kila kitu kwa jicho lake, naye atamlipa kila mmoja kwa
a'mali yake.
41,42. Hakika wanao
ikataa Qur'ani Tukufu inapo wajia bila ya kuzingatia, watapata adhabu ambayo
hapana mtu anaye weza kuikadiria. Wao wameipinga Qur'ani nacho hakika ni Kitabu
kisicho kuwa na mfano, kinamshinda kila mwenye kukipinga, hakiingiliwi na
upotofu usio kuwa na asli kwake kwa upande wowote ule, kimeteremka kwa
kukufuatana kutokana na Mungu aliye takasika na upuuzi, Msifiwa kwa wingi wa
sifa kwa neema alizo zitoa.
41,42. Hakika wanao
ikataa Qur'ani Tukufu inapo wajia bila ya kuzingatia, watapata adhabu ambayo
hapana mtu anaye weza kuikadiria. Wao wameipinga Qur'ani nacho hakika ni Kitabu
kisicho kuwa na mfano, kinamshinda kila mwenye kukipinga, hakiingiliwi na
upotofu usio kuwa na asli kwake kwa upande wowote ule, kimeteremka kwa
kukufuatana kutokana na Mungu aliye takasika na upuuzi, Msifiwa kwa wingi wa
sifa kwa neema alizo zitoa.
43. Ewe Muhammad!
Huambiwi wewe na maadui wako ila kama walivyo ambiwa Mitume wa kabla yako na
maadui wao, nayo ni matusi na kuambiwa mwongo. Hakika Muumba wako na Mlezi wako
ana msamaha mwingi, na ni Mwenye kuadhibu kwa machungu makubwa. Basi Yeye
humghufiria mwenye kutubu kwake, na humtesa mwenye kushikilia na inda yake.
44. Na lau tungeli ifanya
Qur'ani kwa lugha ya kigeni, kama walivyo pendekeza baadhi ya hao wanao kera,
basi bila ya shaka wangeli sema: Lau zingeli bainishwa Aya zake kwa ulimi tunao
ufahamu! Kitabu hichi cha lugha ya kigeni, na huyu mkhubiri wake ni Mwaarabu!
Yawaje haya? Ewe Mtume! Waambie: Hii Qur'ani ni hivyo hivyo kama walivyo
teremshiwa Waumini, si wengineo, kuwa ni Uwongofu na Poza kwa Waumini; kiwaokoe
na ubabaishi, na kiwaponyeshe na shaka shaka. Na wasio amini wamekuwa kama
katika masikio yao pana kizuizi, uziwi, nayo hii Qur'ani kwao wao ni upofu,
hawaoni chochote ndani yake ila fitna tu. Hao makafiri ni kama wanao itwa
waiamini kwa umbali kabisa. Hawausikii wito huo.
45. Ninaapa: Kwa hakika
tulimpa Musa Taurati, na watu wake wakakhitalifiana kwayo. Na lau ingeli kuwa
hukumu ya Mola wako Mlezi haikuakhirishwa, ewe Muhammad, mpaka muda maalumu
kwake, basi hapana shaka pange amuliwa hukumu baina yako na hao kwa kuwang'olea
mbali wanao kanusha. Na hakika makafiri katika kaumu yako wamo katika shaka na
Qur'ani, na hiyo inawatia dhiki na wasiwasi.
46. Mwenye kutenda
vitendo vyema ujira wake ataupata mwenyewe, na mwenye kutenda uovu madhambi yake
yatakuwa juu yake. Na Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja wake, hata
amtese mtu kwa dhambi za mwengine.
47. Kwa Mwenyezi Mungu
peke yake ndio unarejea ujuzi wa kusimama Saa ya Kiyama. Matunda hayatoki kwenye
vifuniko vyake, wala mwanamke hachukui mimba wala hazai ila awe Yeye anajua. Na
kumbuka siku ambayo Mwenyezi Mungu atawaita washirikina, kwa kuwakebehi,
awaambie: Wako wapi hao washirika wangu mlio kuwa mkiwaomba badala yangu?
Watasema kwa kutaadhari: Ewe Mwenyezi Mungu! Tunakujuvya kuwa sisi hatuna wa
kushuhudia kuwa wewe una mshirika yeyote.
48. Na hao miungu ya
ushirikina walio kuwa wakiwaabudu watawapotea, na waliyakinika kuwa hawana pa
kukimbilia.
49. Mwanaadamu hachoki
kumwomba Mola wake Mlezi kwa kheri za kidunia. Ikimpata shari basi huwa mwingi
wa kuikatia tamaa kheri, na kuvunjika moyo hadi, ya kwamba Mwenyezi Mungu
hamwitikii dua yake.
50. Tunaapa:
Tukimwonjesha mtu neema, kwa fadhila yetu, baada ya dhara kubwa iliyo msibu bila
ya shaka husema: Hii neema niliyo ipata ni haki yangu mimi. Wala sidhani kuwa
Kiyama kitakuja. Na ninaapa ikitokea nikarejeshwa kwa Mola wangu Mlezi basi na
huko kwake bila ya shaka nitapata malipo mema. Lakini Sisi tunaapa: Hapana shaka
tutawalipa walio kufuru, Siku ya Kiyama, kwa vitendo vyao! Na hapana shaka
tutawaonjesha adhabu kali iliyo rindikwa juu kwa juu!
51. Na tukimneemesha mtu
huacha kutushukuru, na akajitenga mbali na Dini yetu. Na tukimwonjesha shari
basi huwa mwingi wa kuomba madua.
52. Ewe Muhammad!
Waambie: Hebu nambieni; ikiwa hii Qur'ani imetoka kwa Mwenyezi Mungu nanyi mkawa
mnaikataa, basi nani aliye kuwa mbali mno na Ukweli kuliko huyo aliye kinyume na
Haki?
53. Karibuni hivi
tutawaonyesha hao wanao zikataa Ishara zetu zenye kuonyesha ukweli wako katika
pande za mbinguni na ardhi, na katika nafsi zao wenyewe, mpaka yawadhihirikie ya
kwamba uliyo waletea ni Haki tupu si vinginevyo. Je! Wanakataa kuwa Sisi
tunawaletea Ishara hizo? Je! Haitoshi kuwa Mola wako Mlezi ni Mwenye kukizunguka
kila kitu?
54. Ama hakika hawa
makafiri wamo katika shaka kubwa kukutana na Mola wao Mlezi, kwa sababu ya kuwa
hawaamini kufufuliwa. Ama hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukizunguka kila kitu
kwa ujuzi wake na uweza wake.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani