2,3. Hii Qur'ani imeteremshwa kutokana na Mwenyezi
Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye kushinda, Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa ujuzi
wake, naye ni Mwenye kupokea toba ya wenye kutubia, na Mkali wa kuadhibu, Mwenye
neema nyingi; hapana wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye peke yake. Ni kwake
Yeye peke yake ndio marejeo na mafikio.
4. Hawazibishi Ishara za Mwenyezi Mungu zenye kuonyesha dalili
zake ila walio makafiri. Basi yasikukhadae huko kutanga tanga kwao katika nchi
ukadhani kuwa Mwenyezi Mungu kawasahilishia mambo yao juu ya ukafiri wao.
5. Kabla ya hawa walikufuru kaumu ya Nuhu, na makundi mengine
yaliyo jumuika kuwapinga Mitume baada ya kaumu yake Nuhu. Na hao wakawa na pupa
ya kumletea shari Mtume wao wamtie nguvuni, na wakawa wanajadiliana katika
upotovu usio kuwa na ukweli wowote, ili kwa upinzani wao wapate kuipindua haki
iliyo kwisha thibiti. Basi Mimi nikawashika, nikawatia katika adhabu ya
kuwang'olea mbali. Hebu angalia ilikuwaje adhabu yangu juu yao!
6. Na kila lilipo thibiti neno la adhabu juu ya mataifa yaliyo
wakadhibisha Manabii wao, basi kadhaalika lilithibiti neno la Mola wako Mlezi
juu ya hao wanao kukanusha wewe, ewe Muhammad, kwani hao ni watu wa Motoni, kwa
kuwa wamekhiari ukafiri kuliko Imani.
7. Malaika wanao beba A'rshi, na wenye kuizunguka, wanamtakasa
Mwenye kumiliki mambo yao na Mlezi wao, wanamtakasa kutokana na kila upungufu,
kwa mtakaso ulio lingana na sifa zake. Na wanamuamini, na wanamwomba maghfira
awaghufirie Waumini, huku wakisema: Ewe Mola wetu Mlezi! Rehema yako imeenea
kila kitu, na Ujuzi wako umezunguka kila kitu, basi yasamehe makosa ya walio
rejea kwako, na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu ya Motoni.
8. Na Malaika hawa husema: Ewe Mola wetu Mlezi! Waingize
Waumini katika Mabustani ya Milele ulio waahidi kwa ndimi za Mitume wako, na pia
waingize pamoja nao walio wema katika wazazi wao, na wake zao, na dhuriya zao.
Hakika wewe peke yako ndiye Mwenye kushinda, wala hushindiki; Mwenye hikima
usiye kosa.
9. Na husema katika dua zao: Waepushe Waumini malipo ya
madhambi yao, na unaye muepusha Wewe na malipo ya madhambi yake Siku ya Malipo
basi hakika ndio umemrehemu kwa fadhila yako. Kuepushwa na malipo ya madhambi
ndio ushindi ulio fikilia ukomo mkubwa mno.
10. Hakika walio kufuru watanadiwa waambiwe: Bila ya shaka
chuki ya Mwenyezi Mungu na bughdha yake kwenu ni kubwa kuliko chuki zenu wenyewe
zilizo kupelekeeni mkapata adhabu pale mlipo itiwa kwenda kwenye Imani mara kwa
mara nanyi mkakimbilia kwenye ukafiri.
11. Makafiri watasema: Mola wetu Mlezi! Umetufishe vifo
viwili, kifo kimoja katika uhai wetu wa duniani, na kifo kingine katika uhai
wetu wa Barzakh, (1) yaani kaburini. Na ukatuhuisha mara mbili, mara moja ndiyo
ya uhai wetu wa duniani, na mara ya pili ni wakati wa kufufuliwa kutoka
makaburini. Basi, hebu, ipo njia ya kutoka kwetu kwenye adhabu?
(1) Na
huenda yakaonyesha uhai wa Barzakh, ambao ni uhai makhsusi hatuujui hakika yake,
aliyo yataja Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kauli yake juu ya watu wa Firauni:
"Moto wanadhihirishiwa asubuhi na jioni; na siku itapo fika Saa ya Kiyama
patanenwa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa." Na kauli yake
Mtukufu: "Wala usiwadhanie wale walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa
ni maiti. Bali ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi."
12. Hiyo ni adhabu mliyo nayo. Kwani mwendo wenu duniani ni
kuwa akitajwa Mwenyezi Mungu peke yake nyinyi mnakufuru, na pindi akishirikishwa
na mwenginewe ndio mnaamini. Na ikiwa huu ndio mwendo wenu basi mnastahiki kweli
malipo ya ushirikina wenu. Basi hukumu ni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Mkuu ambaye
humlipa aliye kufuru kwa anavyo stahiki.
13. Mwenyezi Mungu ambaye anakuonyesheni dalili za uweza wake,
basi anakuteremshieni kwa maslaha yenu maji kutoka mbinguni ambayo ni sababu ya
riziki zenu. Na hapana anaye waidhika kwa haya ila mwenye kurejea akazifikiria
Ishara za Mwenyezi Mungu.
14. Basi muabuduni Mwenyezi Mungu mkimsafia Yeye ibada, na
hata walau wakiichukia makafiri ibada yenu na ikhlasi yenu.
15,16. Mwenyezi Mungu, Mwenye vyeo vya juu, Mwenye
A'rshi, huteremsha Wahyi kwa hukumu yake na amri yake juu ya anaye mteuwa katika
waja wake, ili awaonye watu adhabu ya kwenda kinyume na Mitume Siku ya kukutana
viumbe vyote, Siku ya Hisabu watapo tokeza watu wazi, hapana lifichikanalo kwa
Mwenyezi Mungu, watakuwa wakijisikilizanisha wao kwa wao wito unao tisha: Ufalme
wa nani leo? Na jawabu ya kukata: Wa Mwenyezi Mungu, Mmoja, Mwenye kutengeka kwa
hikima, Aliye pita mipaka kwa nguvu zake!
17. Leo tunailipa kila nafsi kwa iliyo tenda. Hapana dhulma
leo kwa kupunguziwa ujira au kuzidishiwa mateso. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwepesi kuhisabu kwake, basi hachelewi na wakati wake.
18. Ewe Muhammad! Waonye, Siku ya Kiyama ipo karibu. Siku
zitakapo kuwa nyoyo zipo kooni kwa wingi wa khofu, zimejaa majonzi, haziwezi
hata kuyaelezea. Walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri hawatakuwa na jamaa wala
mwombezi wa kuwat'ii katika amri yao.
19. Na Yeye Subhanahu analijua jicho linalo khuni, na siri
zilizo fichikana vifuani.
20. Na Mwenyezi Mungu anahukumu kwa uadilifu, na hao miungu ya
uwongo wanayo iomba badala ya Mwenyezi Mungu haihukumu chochote, kwa kuwa
haiwezi kitu. Hakika Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kuvizunguka vyote
vinavyo sikia na vinavyo ona.
21. Kwani hao washirikina wamekaa kitako tu wala hawatembei
katika ardhi wakaiona vipi ilikuwa hali ya mataifa yaliyo kuwa kabla yao?
Walikuwa wana nguvu kuliko wao na walijenga zaidi kuliko hawa, nao Mwenyezi
Mungu aliwang'olea mbali kwa madhambi yao, wala hawakuwa na mlinzi wa kuwalinda
na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
22. Na adhabu hiyo iliwateremkia kwa sababu ilikuwa Watume wao
wakiwajia na dalili zilizo wazi, nao wakazikataa, basi Mwenyezi Mungu akafanya
haraka kuwapelekea adhabu ya kuwang'oa. Hakika Yeye ana nguvu kubwa mno, na
amefikilia ukomo katika kuadhibu.
23,24. Ninaapa kuwa tulimtuma Musa na miujiza yetu
na ushahidi wenye uthibitisho ulio wazi kumpelekea Firauni na Hamana na Qaruni,
wakasema: Huyu ni mchawi kwa hiyo anayo dai kuwa ni miujiza, na amepita mipaka
kwa uwongo katika madai yake kuwa yeye ni Mtume aliye toka kwa Mola wake Mlezi!
25. Musa alipo waletea Haki kutoka kwetu, Firauni na wafuasi
wake walio kuwa pamoja naye walisema: Wauweni watoto wa kiume wa hao walio amini
pamoja naye, na waachilieni wahai binti zao! Na vitimbi vya makafiri haiwi ila
kuondoka, na kuangamia, na kupotea.
26. Na Firauni akasema: Nachilieni nimuuwe Musa, naye naamwite
huyo Mola wake Mlezi amwokoe kwangu! Hakika mimi nakhofia asije huyu
akaigeuza dini yenu, enyi watu wangu, au akaeneza fitna katika nchi.
27. Na Musa akamwambia Firauni na watu wake: Hakika mimi
nimejilinda na Mwenye kumiliki mambo yangu ambaye ndiye aliye nilea, na ndiye
Mwenye kumiliki mambo yenu pia, na Mwenye kukuleeni nyinyi kwa neema zake na
hisani zake, nimejilinda na kila anaye jivuna na kutakabari, asiye iamini Siku
ya Hisabu.
28. Akasema mtu mmoja Muumini anaye ficha Imani yake katika
watu wa Firauni, akiwasemeza watu wake: Mnataka kumuuwa mtu kwa sababu anasema:
Mungu wangu ninaye muabudu ni Mwenyezi Mungu, naye amekuleteeni dalili
zilizo wazi zinazo tokana na Mwenye kumiliki mambo yenu na Mlezi wenu? Na akiwa
yeye mwongo, basi uwongo wake ni juu yake yeye peke yake, balaa ya uwongo wake
itamwangukia mwenyewe. Na akiwa ni mkweli baadhi ya adhabu anazo tutahadharisha
nazo zitakuteremkieni nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu hamwafikishi njia ya uwokovu
mwenye kupita mipaka, aliye mwongo mno.
29. Enyi watu wangu! Leo nyinyi mnao ufalme, na ni watu wa juu
katika nchi ya Misri, wala hapana mwenginewe. Lakini ni nani atakaye kukingeni
na adhabu ya Mwenyezi Mungu pindi ikitujia? Firauni akasema: Sikwambiini rai ila
ambayo mimi mwenyewe ninayo itakidi. Na sikuongozeni kwa rai hii ila njia ya
uwongofu.
30,31. Akasema yule mtu aliye amini katika watu wa
Firauni: Enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni isikufikieni siku kama ile
siku walipo jikusanya watu makundi mbali mbali kuwapinga Mitume wao, mfano
wa ada ya kaumu Nuhu, na ya A'di, na ya Thamudi, na mataifa mengine yaliyo kuja
baada yao. Wala Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja wake.
32,33. Na enyi watu wangu! Mimi nakukhofieni siku
viumbe watapo pigiana makelele, siku mtapo kimbia kurudi nyuma, hapana wa
kukukingeni na Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuachiliwa na Mwenyezi Mungu kupotea -
kwa kuwa anamjua kuwa amekhiari upotovu kuliko uwongofu - basi hatokuwa na
mwongozi wa kumwongoa.
34. Ninaapa! Bila ya shaka alikwisha kujieni Yusuf na Ishara
zilizo wazi. Nanyi hamkuacha kuwa na shaka na hayo aliyo kuja nayo kwenu, mpaka
alipo kwisha kufa mkasema: Mwenyezi Mungu hatoleta tena Mtume mwengine baada ya
Yusuf. Mfano wa upotovu kama huu mbaya Mwenyezi Mungu humwacha kupotea yule
aliye pindukia mipaka, mwingi wa mashaka na wasiwasi.
35. Wanao bishana juu ya Ishara za Mwenyezi Mungu bila
ushahidi wowote ulio wajia, humkirihisha mno na kumchukiza Mwenyezi Mungu na
Waumini kwa yale majadiliano waliyo yatilia muhuri. Mfano wa muhuri huu Mwenyezi
Mungu anaupiga juu ya kila moyo ulio takabari juu ya viumbe wenzake, na ukataka
kuwatawala.
36,37. Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee
jengo refu nifikilie njia za mbinguni nipate kumwona huyo Mungu wa Musa. Na mimi
nina hakika huyu ni mwongo kwa anavyo jidai kuwa yeye ati ni Mtume. Mfano wa
pumbao la uwongo kama hivi Firauni alipambiwa uovu wa vitendo vyake, hata
akaviona mwenyewe kuwa ni vizuri, na akazuilika na njia ya haki kwa kukhiari
mwenyewe njia ya upotovu. Na havikuwa vitimbi vya Firauni ila katika upotovu tu.
38. Na akasema yule aliye amini katika watu wa Firauni: Enyi
watu wangu! Nifuateni mimi, nitakuongozeni njia njema!
39. Enyi watu wangu! Haya maisha ya duniani si chochote ila ni
kama starehe ya muda ya mwenye kupanda kipando, inakwisha upesi. Na makaazi ya
Akhera, hayo tu peke yake, ndiyo makaazi ya kudumu.
40. Mwenye kutenda uovu duniani hatolipwa kwa uovu huo huko
Akhera ila kwa mfano wake. Na mwenye kutenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke,
naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi watakapo ruzukiwa bila ya kipimo cha
kuhisabiwa na wenye kuhisabu.
41,42. Na enyi watu wangu! Kwani mimi nina nini?
Mimi nakuiteni mfuate njia za kuokoka, na nyinyi mnaniita niingie Motoni!
Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu kwa kumshirikisha Yeye na vitu nisivyo vijua,
na hali mimi nakuitieni mwende kwa Mwenye Nguvu asiye shindwa, Mwingi wa
kusamehe madhambi!
43. Bila ya shaka yoyote huyo mungu mnaye niitia nimuabudu
hana wito wowote unao stahiki kuitikiwa la duniani wala Akhera. Na hakika
marejeo yetu sote ni kwa Mwenyezi Mungu, na wenye kupita mipaka ndio watu wa
Motoni, wala si Waumini walio kaa sawa.
44. Basi watakuja jua ukweli wa niliyo kuambieni, na mimi
namtegemezea mambo yangu Mwenyezi Mungu. Hakika jicho la Mwenyezi Mungu
limewaenea waja wake wote, na Yeye ni Mwenye kuwalipa kwa vitendo vyao.
45,46. Mwenyezi Mungu akamlinda yule Muumini katika
watu wa Firauni mateso ya vitimbi vyao, na ikawazunguka watu wa Firauni adhabu
mbaya, nayo ni Moto wanao uingia asubuhi na jioni. Haya ni ya duniani na wapo
katika ulimwengu wa Barzakh, kaburini. Na Siku ya Kiyama, atasema Mwenyezi
Mungu: Waingizeni watu wa Firauni kwenye adhabu iliyo kali kabisa!
47. Ewe Muhammad! Watajie pale wanapo zozana watu wa Motoni
humo, wakawa walio kuwa wanyonge, nao ni wafuasi, wakiwaambia wanao takabari,
nao ni maraisi: "Sisi tulikuwa duniani ni wafuasi wenu, basi je, hamtuchukulii
baadhi ya adhabu ya moto?"
48. Na walio takabari waseme: "Hakika sote sisi tumo humu,
sisi na nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu amehukumu kwa haki baina ya waja. Basi
kila mmoja wetu amepata adhabu aliyo hukumiwa juu yake."
49. Watasema walio Motoni, wanyonge na wakuu, kuwaambia
walinzi wa Jahannamu wakiwaomba msaada: Muombeni Mungu wenu atupunguzie japo
siku moja tupumzike na adhabu.
50. Walinzi wa Jahannamu watawaambia kwa kuwahizi: Kwani
hamkunabihika kwa yaliyo kuwa mkiteremshiwa, na hali walikuwa wakikujieni Mitume
na ushahidi ulio wazi? Na watasema watu wa Motoni: Kwani? Walitujia Mitume na
sisi tukawakadhibisha. Walinzi wakasema: Ikiwa mambo ni hivyo, basi waombeni
nyinyi! Lakini madua ya makafiri hayana ila kupotea bure.
51. Hakika Sisi bila ya shaka tunawanusuru Mitume wetu na
Waumini katika maisha ya duniani kwa kulipiza juu ya maadui wao, na kusimamisha
hoja juu yao; na Siku ya Kiyama watasimama Mashahidi washuhudie kwamba Mitume
wamefikisha Ujumbe wao, na washuhudie kwamba makafiri waliukadhibisha.
52. Siku ambayo madhaalimu hautawafaa udhuru wao kwa yale
waliyo yakosa kuyatenda duniani. Nao watapata laana, yaani watafukuzwa kwenye
rehema, na watapata makaazi maovu kabisa.
53,54. Naapa kwamba tulimpa Musa cha kuongoa
kwendea Haki, na tukawarithisha Wana wa Israili Taurati yenye kuongoa na yenye
kuwakumbusha wenye akili zilio nzima.
55. Ikiwa umejua tuliyo kusimulia, basi subiri, ewe Muhammad,
kwa maudhi yanayo kupata. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kukunusuru wewe na
kuwanusuru Waumini ni kweli isiyo geuka. Na taka maghfira kutoka kwa Mola wako
Mlezi kwa hayo ambayo kwa mnasaba wako wewe huhisabiwa kuwa ni dhambi. Na
mtakase Mola wako Mlezi na kila upungufu kwa mtakaso unao ambatana na kumsifu
jioni na asubuhi.
56. Hakika hao wanao jadili katika dalili za Mwenyezi Mungu
bila ya hoja iliyo tokana naye Yeye Mtukufu, hamna vifuani mwao ila kutaka
uluwa, ubora, wasiifuate Haki, wala huko kutaka kwao uluwa, ubora,
hakuwafikishii walitakalo. Basi wewe iombe Hifadhi kutokana na Mwenyezi Mungu;
kwani Yeye hakika ni Mwenye kuenea kila kitu kusikia kwake na kuona kwake.
57. Ninaapa: Bila ya shaka kuziumba mbingu na ardhi ni jambo
kubwa zaidi kuliko kuwaumba watu. Lakini wengi wa watu wameitupa ilimu, wakawa
hawaamini kufufuliwa juu ya kukubali kwao kwamba Yeye ndiye Muumba mbingu na
ardhi.
58. Na hawawi sawa, kipofu asiyo iona Haki, na mwenye kuijua.
Wala hawawi sawa wema wenye kuamini na wakatenda mema, na muovu wa itikadi na
vitendo. Ni kwa uchache, uchache mno, ndio mnakumbuka, enyi watu!
59. Hakika Kiyama kitakuja tu, hapana shaka yoyote. Na lakini
wengi wa watu hawasadiki.
60. Na anasema Muumba wenu na Mwenye kumiliki mambo yenu yote:
Niombeni nami nitakupeni! Hakika wale wanao takabari hata wakakataa kuniomba
wataingia Jahannamu nao ni madhalili wanyonge.
61. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kujaalieni usiku
mpate kutua ndani yake mpumzike na kazi, na mchana wenye mwangaza mpate kufanya
kazi ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye fadhila kuu juu
ya watu. Lakini watu wengi hawamshukuru juu ya neema zake.
62. Huyo Mwenye kukuneemesheni kwa neema hizi tukufu ndiye
Mwenyezi Mungu, Mwenye kumiliki mambo yenu, Muumba wa kila kitu, hapana wa
kuabudiwa kwa haki ila Yeye. Basi mtaelekea wapi kwa ibada mkimwacha Yeye?
63. Mfano wa kukengeuka huku kuiacha Haki kuendea upotovu,
walikengeuka walio kuwa kabla yenu. Wakazikanya Ishara za Mwenyezi Mungu na
wakazikataa.
64. Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye kufanyieni ardhi
iwe ni pahala panapo silihi maisha yenu, na mbingu zikawa ni jengo lilio
shikamana. Na akakadiria kukuumbeni nyinyi, akazitengeneza sura zenu, na
akakujaalieni na umbo zuri lilio nyooka. Na akakuruzukuni katika vitu vya halali
mnavyo viona vitamu. Mneemesha huyo kwa neema hizi ndiye Mwenyezi Mungu
Mola wenu Mlezi. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mwenye kuumiliki ulimwengu wote,
na Mwenye kuulea.
65. Yeye pekee Mwenye uhai wa daima dawamu, hapana wa
kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Basi muelekeeni Yeye kwa kumuomba, mkimsafia ibada
Yeye. Sifa njema zote ni haki iliyo thibiti kwa Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa
viumbe vyote.
66. Ewe Mtume! Sema: Hakika mimi nimekatazwa kuiabudu miungu
mnayo iabudu nyinyi badala ya Mwenyezi Mungu, zilipo nijia hoja kutoka kwa Mola
wangu Mlezi, na nikaamrishwa nimfuate Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu
wote katika mambo yangu yote.
67. Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye aliye kuumbeni, enyi
wanaadamu, kutokana na udongo, kisha akaugeuza udongo ukawa tone la manii, kisha
akalifanya tone la manii kuwa pande la damu iliyo gandana, kisha akakutoeni
kwenye matumbo ya mama zenu kuwa ni watoto wachanga. Kisha akaukuza umri wenu
mpaka mkakamilika nguvu zenu na akili, tena ukawa mrefu umri wenu mpaka mkawa
wazee. Na wako kati yenu wanao kufa kabla ya kufikia ujana au uzee. Na Mwenyezi
Mungu akakuumbeni kwa namna hii ili mfikilie wakati maalumu kwake Yeye, nao ni
wakati wa kufufuliwa; na kwa ajili mpate kupima na kufahamu hikima na mazingatio
katika mageuzi haya.
"Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa
tone la manii, kisha kwa pande la damu..n.k."
Maoni juu ya "Tone la
manii", "pande la damu" na "pande la nyama" yamo katika Aya 7,8 na 9 Sura
Assajda; Aya 12, 13 na 14 Sura Al-Muuminuna; Aya 67 Sura Ghaafir; 5 Sura
Al-Hajj. Neno Nut'fa katika lugha hutumika kwa maana ya manii ya mwanamume.
Tukirejea kwenye Aya Tukufu (75.37) "Je! Hakuwa tone la manii lilio
shushiwa?" inadhihiri kuwa makusudi kwa "tone la manii" ni sehemu makhsusi ya
manii. Na ilimu ya sayansi imevumbua kuwa makusudi ya sehemu hiyo ni kile
kijidudu kinacho shushiwa, ambacho kinacho chukuliwa na maji yanayo shushwa, na
kidudu hicho "Sperm" ambacho kikiingia kwenye kijiyai (Buwaydha Kiarabu au
Ovum kwa Kizungu), cha mwanamke ndio huumbika mtoto.
Al-A'laqah
katika maana zake kilugha ni damu iliyo ganda, au inayo tiririka iliyo nyekundu
mno. Na ki-sayansi maana yake ni Khalaya, au Cells za Embryo (Mtoto ndani ya
tumbo la mama) lilio gandamana (ta-a'llaqa) na ukuta wa tumbo la uzazi baada ya
kwisha ingiana kidudu cha ume na yai la uke, na ikapatikana Khalaya moja ambayo
ikagawika ikawa Khalaya kadhaa wa kadhaa zinazo endea kwenye ukuta wa tumbo la
uzazi, kwenda kujibandika na huzua hapo kumwagika damu.
Al-mudhghah huyo ni mtoto katika mageuzi yake baada ya kutoka kuwa
Al-a'laqah, yaani baada ya kwisha shikamana na ukuta wa tumbo la uzazi na
kuviringana bila ya sura maalumu, na huzungukwa na vifuniko, na hubaki katika
hali hiyo wiki chache hivi mpaka yafanyike mafupa. Na Mudhghah ambayo
imefasiriwa kama pande la nyama ina khalaya zenye umbo maalumu, na hizo ndizo
zinakuwa mtoto, na khalaya zisio kuwa na umbo maalumu, na hizi huzunguka
sehemu ile iliyo timia umbo lake, na kazi yake ni kulinda na kutoa chakula.
Mafupa: Ilimu ya mimba Gynaecology imethibitisha karibuni kuwa mafupa
yanadhihiri katika t'abaka ya katikati katika Khalaya za Mudhghah baada ya
kutoka kiwango cha kugawanyika Khalaya za viungo.
68. Mwenyezi Mungu ndiye anaye huisha na kufisha. Akitaka
jambo lolote kulidhihirisha katika kuwepo basi huliambia: Kuwa! Na huwa bila ya
taakhira.
69. Je! Huwaangalii hao wanao zozana katika Ishara za Mwenyezi
Mungu zilio wazi, vipi walivyo geuzwa nadhari yao katika hizo, na wanaendelea
kushikilia ule ule upotovu wao walio nao?
70,71,72,73,74.
Walio ikadhibisha Qur'ani na Ujumbe tulio watumia Mitume wetu, Ufunuo wote,
watakuja jua matokeo ya kukanusha kwao zitapo kuwa pingu na minyororo zipo
shingoni mwao, wakibururwa kwazo katika maji yaliyo fikia ukomo wa moto, tena
baadae watupwe Motoni waokwe kwenye joto lake. Kisha waambiwe kwa kuwakejeli na
kuwahizi: Wako wapi hao miungu yenu mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi
Mungu? Watasema makafiri: Wametupotea. Bali kwa hakika sisi hatukuwa hapo zamani
duniani tukiabudu chochote. Katika mfano wa upotovu mbaya kama huu ndio
Mwenyezi Mungu anawawacha makafiri waipotee Njia ya Haki kwa kujua kwake
kwamba hao wamekhiari upotovu kuliko uwongofu.
75,76. Makafiri wataambiwa: Adhabu hiyo ni kwa
sababu ya mlivyo kuwa katika dunia mkifurahi katika nchi kwa jambo lisilo
stahiki kufurahikiwa, na kwa sababu ya kufurahikia kwenu kwa maudhi yaliyo kuwa
yakiwasibu Manabii wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Basi ingieni kwenye
milango ya Jahannamu, ambako mmekadiriwa mkae daima dawamu. Pahala paovu kabisa
pa kukaa wenye kujivuna ni Jahannamu.
77. Subiri, ewe Muhammad! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu kwako
ya kwamba atawaadhibu maadui wako, ni kweli isiyo na shaka yoyote. Na adhabu
itawafikia tu, ama wakati wa uhai wako au wakati watapo rejea wao kwetu!
Wakiacha baadhi ya adhabu tunayo wahadharisha nayo katika uhai wako, basi. Na
ikiwa tutakufisha, basi watarejea kwetu. Nasi tutawahisabia waliyo kuwa
wakiyatenda.
78. Ninaapa: Bila ya shaka tuliwatuma Mitume wengi kabla yako
wewe. Wengine tumekuzungumzia khabari zao, na wengine hatukukuzungumzia khabari
zao. Wala haikuwa Mtume yeyote kuleta muujiza ila kwa apendavyo Mwenyezi Mungu
na kutaka kwake. Hawezi kuleta kwa nafsi yake tu, wala kwa watakavyo watu wake.
Na inapo kuja amri ya Mwenyezi Mungu ya kuleta adhabu duniani au Akhera
wanahukumiwa kwa uadilifu. Na wakati huo wapotovu huwa ndio wenye kukhasiri.
79. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kudhalilishieni ngamia, mpate
kuwapanda wengine, na wengine muwale.
80. Na mnapata kwao manufaa mengi, mbali ya kuwapanda na
kuwala; na ili mpate kufikilia haja zenu mnazo zishughulikia nafsi zenu, kama
kuburura mizigo na kuibeba, na kadhaalika. Na juu ya ngamia, ambaye ni katika
nyama hoa, na juu ya marikebu, mnajipakia nyinyi wenyewe na mizigo yenu.
81. Mwenyezi Mungu anakuonyesheni dalili zake, basi hebu
nambieni dalili gani katika hizo mnazo zikataa? Na hizo dalili zenyewe ziwazi,
hawezi kuzikataa yeyote mwenye akili hata kidogo.
82. Je! Kwani hao watu wamekaa tu, hawazunguki ulimwenguni
wakaona ulikuwaje mwisho wa wale walio kuwa kabla yao, walivyo hilikishwa na
wakaangamizwa? Hao walio kabla yao walikuwa wengi kwa kuwahisabu kuliko wao, na
walikuwa na nguvu na waliathiri kwa majenzi na maendeleo kushinda wao. Hapana
kilicho wakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu katika hayo waliyo yachuma, si
mali wala nguvu, wala utawala.
83. Basi Mitume wao walipo wajia mataifa haya kwa sharia na
miujiza iliyo kuwa wazi, hayo mataifa yalifurahi na kujitapa kwa kuwa wao ati
wana ilimu za dunia, na wakawafanyia maskhara Mitume. Ikawateremkia adhabu
waliyo wakhubiria Mitume, na hali wao wakiwakejeli.
84. Mataifa haya yalipo ona adhabu imekuwa kali walisema:
Tumemsadiki Mwenyezi Mungu pekee, na tumewakataa miungu ambao kwa sababu yao
tulikuwa washirikina.
85. Imani yao haikuwafaa kitu wakati walipo kwisha ona ukali
wa adhabu yetu. Mwenyezi Mungu alikwenda mwendo ule ule aliyo kuwa akienda nao
waja wake, nao ni kutokukubali Imani wakati wa kuteremka adhabu. Na makafiri
ndio walio khasiri wakati wa kuteremka adhabu.