1. Qur'ani
imeteremka kutokana na Mwenyezi Mungu, ambaye hana wa kumshinda kwa atakayo;
Mwenye hikima katika vitendo vyake na utungaji wa sharia zake.
2.Hakika Sisi
tumekuteremshia wewe, Muhammad, Qur'ani hii yenye kuamrisha Haki. Basi muabudu
Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia ibada Yeye tu peke yake.
3.Jueni na
mtambue kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye Dini isiyo kuwa na ila. Na
washirikina walio wafanya wenginewe kuwa ni wasaidizi wa kuwanusuru, wanasema:
Sisi hatuwaabudu hawa kwa kuwa ni waumbaji, bali tunawaabudu wapate
kutukaribisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa mkaribisho wa kutuombea sisi kwake Yeye.
Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina ya hawa washirikina na Waumini wenye
kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja katika yale wanayo khitalifiana katika matatizo
ya shirki na Tawhidi. Hakika Mwenyezi Mungu hamjaalii afikie Haki mtu ambaye
mtindo wake ni uwongo na kukanya.
4.Lau kuwa
Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana, kama wasemavyo Wakristo kwa Masihi, na
washirikina kwa Malaika, basi angeli jichagulia amtakaye katika viumbe vyake, la
sio kama mtakavyo nyinyi. Mwenyezi Mungu ametakasika na upungufu wa kuhitajia
mwana. Yeye ni Mwenyezi Mungu asiye kuwa na mfano kama Yeye. Mtenda kama
apendavyo, ukomo wa kutenda.
5.Ameumba mbingu na ardhi kwa kushikamana na Haki na kuwa sawa kwa
kufuatana na sharia zilizo thibiti. Usiku unaufunika mchana, na mchana
unaufunika usiku kwa mfululizo. Na amedhalilisha jua na mwezi kwa mujibu
atakavyo na kwa mujibu wa maslaha ya waja wake. Kila kimojapo katika hivyo
vinakwenda katika njia yake mpaka ufike wakati aliyo uwekea Yeye, nao ni Siku ya
Kiyama. Jueni basi kuwa Yeye tu, si mwenginewe, ndiye Mwenye kushinda kila kitu.
Basi hapana kitu chochote kilicho tokana na atakavyo Yeye, ambaye amefikilia
ukomo wa kuwasamehe wenye kutenda madhambi katika waja wake.
Aya hii
tukufu inaonyesha kuwa ardhi ina sura ya mviringo kama mpira, na inazunguka
wenyewe kwa wenyewe juu ya msumari-kati wake. Kwani kule kutumiwa neno Yukawwiru
katika Kiarabu na ikafasiriwa Hufunika, maana yake ni kufunika kitu kwa kitu kwa
namna ya kufuatana, kukariri, mara kwa mara. Na lau kuwa ardhi haina sura ya
mpira, kwa mfano kuwa batabata tu, usiku ungeli enea kote kwa ghafla, au mchana
ungeli angaza dunia nzima kwa mara moja.
6.Enyi watu! Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na nafsi moja, naye
ni Adam, baba wa watu wote. Na amemuumba kutokana na nafsi hiyo mkewe, Hawa. Na
amekuteremshieni kwa ajili ya maslaha yenu namna nane za nyama hoa, wanyama wa
mifugo, madume na majike. Nao ni ngamia, na ng'ombe, na kondoo, na mbuzi. Naye
anakuumbeni matumboni mwa mama zenu kwa kukua na kugeuka geuka, katika viza
vitatu, navyo ni kiza cha tumbo, na tumbo la uzazi, na zalio. Huyo aliye
kuneemesheni kwa neema hizi ndiye Mwenyezi Mungu, Mlezi wenu, Mwenye kumiliki
mambo yenu yote. Ni Yeye tu, si mwenginewe, ndiye Mwenye utawala wa pekee.
Hapana wa kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Basi yawaje hata wanaacha kumuabudu Yeye
wakenda kuwaabudu wenginewe?
Huzuka yai katika mwahala pa kufanyika mayai
kwa mwanamke, hata likisha kuwa tayari hutumbukia katika mojapo ya paipu za
Filopia likapita humo mpaka kufikia kwenye tumbo la uzazi Rahimi (Womb).
Halifiki huko ila kupita siku kidogo, na huenda kijidudu cha manii (Sperm) ya
mwanamume kikaliingia hilo yai, na hapo huanza viwango vya kugeuka na kukua kwa
mwanzo. Na katika tumbo la uzazi hubaki mtoto muda wa mimba, na hujifanyia
vifuniko viwili, na sehemu ya funiko moja hufanyika zalio, placenta. Na funiko
jingine ndio humfunika yule mtoto khasa.
Yapo maoni mbali mbali juu ya hivyo
"viza vitatu" kama ilivyo tajwa katika Aya hii tukufu. Katika hayo ni
(1)
Tumbo, na tumbo la uzazi, na zalio, yaani mfuko unao mfunika mtoto.
(2)
Tumbo la uzazi, na ile mifuniko miwili.
(3) Tumbo na mgongo na tumbo la
uzazi.
(4) Panapo toka mayai (Mabiidh, au Ovaries), na paipu ya kupitia
mayai, Fillopian tube, na tumbo la uzazi (Rahimi au Womb).
Na dhaahiri ni
kuwa hii ya mwisho ndiyo rai yenye nguvu zaidi, kwa sababu ni mahala patatu
mbali mbali. Ama zile rai nyengine zinaonyesha kwa hakika kiza kimoja katika
pahala pamoja palipo zungukwa na t'abaka kadhaa. Na Muumbaji Mtukufu ameashiria
katika Kitabu chake ukweli huu wa kisayansi katika zama walipo kuwa watu
hawajavumbua hayo mayai ya mwanamke na mwendo wake katika mwili ulio kuwa
hauwezi kuonekana kwa macho.
7.Enyi watu! Mkizikataa neema za Mwenyezi Mungu, basi Yeye hakika si
mhitaji wa imani yenu na shukrani zenu. Lakini Yeye hapendi waja wake wakufuru,
kwa sababu hayo yanawadhuru wenyewe. Na mkimshukuru kwa ajili ya neema zake,
Yeye huwa radhi nanyi kwa shukra hiyo. Wala mtu mwenye madhambi hayabebi
madhambi ya mwenginewe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi, na hapo
atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda duniani. Hakika Yeye anayajua mnayo yaficha
katika nyoyo zenu ziliomo vifuani.
Haya yaliomo katika Qur'ani Tukufu
yanaweka wazi msingi wa kutoa adhabu, kama ilivyo vile vile katika Surat Yusuf
katika kauli yake Mtukufu: "Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali sisi kumshika
yeyote ila tuliye yakuta mali yetu kwake; hivyo basi tutakuwa madhaalimu." Na
haya katika Qur'ani ni kusimamisha msingi ulio kwisha tajwa, nao ni msingi ambao
haukuthibiti katika kanuni (sharia) za kutungwa na binaadamu ila katika zama za
karibuni. (Haya ni kinyume cha ilivyo katika imani aliyo itumbukiza Paulo katika
Ukristo, kwamba wanaadamu wamerithi dhambi ya Adam, wanayo ita "Dhambi ya
asili", na kwamba Nabii Isa, Yesu, kafa msalabani kwa kubeba dhambi za
wanaadamu. Biblia yenyewe inapinga haya. Tazama: Jeremiah 31:29-30; Ezekieli 18
Kwa nadhariya ya Paulo Mungu amedhulumu mara mbili:
1. Kutubandika wanaadamu
wote dhambi za Adam,
2. Kumbebesha "mwanawe" Yesu dhambi za walimwengu
wote!)
8.Na mtu
akifikiwa na shida yoyote katika shida za dunia humwomba Mola wake Mlezi, na
hurejea kwake, baada ya kuwa akimpuuza. Kisha Mola wake Mlezi akimpa neema kubwa
husahau zile taabu alizo kuwa akimwombea Mola wake Mlezi amwondolee na amfarijie
kabla hajamneemesha kwa neema hizo. Na humfanyia Mwenyezi Mungu miungu washirika
walio sawa na Yeye kwa kuwaabudu. Huyo mtu hufanya haya ili ajipoteze yeye na
wenginewe waiache Njia ya Mwenyezi Mungu. Ewe Muhammad! Mwambie huyo mwenye sifa
hizi kwa kumwonya: Starehe na huko kuzikanya kwako neema za Mwenyezi Mungu zilio
juu yako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe ni katika watu wa Motoni.
9.Je! Mwenye
kumnyenyekea Mwenyezi Mungu nyakati za usiku anao upitisha na hali yeye yumo
kusujudu na kusimama, akiiogopa Akhera, naye anataraji rehema ya Mola wake
Mlezi, ni kama anaye mwomba Mola wake Mlezi wakati wa shida na akamsahau wakati
wa neema? Ewe Muhammad! Waambie: Ati wanakuwa sawa wenye kujua haki za Mwenyezi
Mungu wakamuabudu Yeye tu peke yake, na wale wasio jua wakapuuza kuziangalia
Ishara? Hakika wenye akili nzuri ndio wanao waidhika.
10.Ewe Nabii!
Sema kwa kufikisha Ujumbe unao toka kwa Mola wako Mlezi: Enyi waja wangu mlio
niamini! Jikingeni na ghadhabu za Mola wenu Mlezi. Mwenye kutenda mema atalipwa
mema, duniani kwa kusaidiwa, na Akhera kwa Pepo. Wala msikae katika unyonge,
kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu ina wasaa. Na subirini kwa kufarikiana na nchi
zenu na wapenzi wenu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wenye kusubiri ujira
wao mara zisio ingia katika hisabu za wanao hisabu.
11.Sema: Mimi
nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ibada yangu isiwe na shirki
ndani yake wala riya ya kujionyesha kwa watu.
12.Na
nimeamrishwa amri iliyo tokana naye Mtukufu, amri ya nguvu, ya kwamba niwe wa
mwanzo wa kufuata amri zake.
13.Sema: Mimi
naogopa adhabu ya Siku Kubwa yenye vitisho ikiwa nitamuasi Mola wangu Mlezi.
14.Ewe
Muhammad! Waambie: Ninamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na ibada yangu haina
shirki wala riya. Na nyinyi ikiwa mnaijua Njia yangu nanyi hamnit'ii, basi
abuduni mpendacho badala yake Yeye. Waambie: Hakika wenye kupata khasara ni wale
walio jitupa kwa upotovu wao wenyewe, na wakawatupa ahali zao kwa kuwapoteza wao
Siku ya Kiyama. Ama hakika kupotoka huko ndio khasara iliyo timia na iliyo
dhaahiri.
15.Ewe
Muhammad! Waambie: Ninamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na ibada yangu haina
shirki wala riya. Na nyinyi ikiwa mnaijua Njia yangu nanyi hamnit'ii, basi
abuduni mpendacho badala yake Yeye. Waambie: Hakika wenye kupata khasara ni wale
walio jitupa kwa upotovu wao wenyewe, na wakawatupa ahali zao kwa kuwapoteza wao
Siku ya Kiyama. Ama hakika kupotoka huko ndio khasara iliyo timia na iliyo
dhaahiri.
16.Hawa walio
khasirika watakuwa na mat'abaka ya Moto yalio rindikwa juu yao, na chini yao
hali kadhaalika. Kwa namna ya adhabu hiyo ndio Mwenyezi Mungu anawahadharisha
waja wake. Enyi waja wangu! Basi yaogopeni mateso yangu.
17.Na wale
wanao jitenga na masanamu na mashet'ani wasiyakurubie, na wakarejea kwa Mwenyezi
Mungu katika mambo yao yote, wanayo bishara tukufu katika mwahala mote. Basi Ewe
Muhammad! Wape bishara nzuri waja wangu wanao sikiliza kauli na wakaifuata iliyo
bora na yenye kuwaongoa kwendea katika Haki. Hao tu, si wenginewe, ndio Mwenyezi
Mungu atao wafikisha kwenye Uwongofu. Na hao tu, si wenginewe, ndio wenye akili
zilizo nawirika.
19.Na wale
wanao jitenga na masanamu na mashet'ani wasiyakurubie, na wakarejea kwa Mwenyezi
Mungu katika mambo yao yote, wanayo bishara tukufu katika mwahala mote. Basi Ewe
Muhammad! Wape bishara nzuri waja wangu wanao sikiliza kauli na wakaifuata iliyo
bora na yenye kuwaongoa kwendea katika Haki. Hao tu, si wenginewe, ndio Mwenyezi
Mungu atao wafikisha kwenye Uwongofu. Na hao tu, si wenginewe, ndio wenye akili
zilizo nawirika.
20.Je! Unaweza
kuniingilia katika Ufalme wangu? Iliyo kwisha pita juu yake hukumu ya
kumuadhibu, je, wewe unaweza kuizuia? Unayo nguvu hiyo wewe? Je! Unaweza
kuwaokoa na Moto baada ya kwisha wathibitikia?
21.Lakini wenye
kumkhofu Mola wao Mlezi watapata vyeo vya juu Peponi na majumba yake ya fakhari,
yenye kupitiwa chini yake na mito. Hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi
Mungu haendi kinyume na ahadi yake.
22.Ewe usemezwaye! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji
kutoka mbinguni, akayapitisha kwenye mito na chemchem za katika ardhi, kisha kwa
maji hayo akaotesha mimea ya namna mbali mbali. Kisha baada ya kustawi kwake
hiyo mimea, ikayabisika ukaiona imekuwa rangi ya manjano baada ya kustawi kwake.
Kisha akaifanya imevurugika na kukatika vipande vipande. Hakika kutoka kwenye
hali moja na kuingia hali nyengine ni mazingatio kwa wenye akili zilizo
nawirika.
Huku kuzunguka maji katika maumbile kutoka mbinguni na kufika
kwenye ardhi na huko yakenda chini na kutimbuka katika chemchem, hakukuwa
kunajuulikana kabla ya katikati za karne ya nane tangu kuzaliwa Nabii Isa a.s.
Fikra iliyo zagaa kabla ya hapo ni kuwa maji ya chemchem na mito yanatimbuka
kutoka chini ya ardhi kutoka kwenye mashimo na visima katika vina vya
bahari.
23.Kwani watu
wote ni sawa? Mwenye kufunguliwa kifua chake na Mwenyezi Mungu kwa Uislamu kwa
kupokea mafunzo yake, na akawa na utambuzi unao tokana na Mola wake Mlezi, huyo
basi ni kama yule anaye kataa kuangalia Ishara zake? Basi hao ambao nyoyo zao
zimekuwa ngumu hata hawamkumbuki Mwenyezi Mungu watapata adhabu kali! Hao wenye
nyoyo ngumu wameitupa Haki iliyo wazi.
23.Mwenyezi
Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, nayo ni Kitabu ambacho zimeshabihiana
maana zake na matamko yake kwa kufikilia ukomo wa kuwashinda watu kuleta mfano
wake, na hukumu zake. Mawaidha na hukumu zinakaririwa, kama kunavyo kaririwa
kusomwa kwake. Kinapo somwa Kitabu hicho na kikasikiwa maonyo yake, ngozi za
wenye kumkhofu Mola wao Mlezi hukunjika, na kisha hulainika ngozi zao na nyoyo
zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hicho Kitabu kilicho kusanya sifa hizi ni
Nuru ya Mwenyezi Mungu ambayo kwayo humwongoa amtakaye, ikamwezesha kufikilia
kumuamini Yeye. Na anaye achwa na Mwenyezi Mungu apotee kwa kumjua kuwa tangu
hapo ataiacha Haki, basi hapati mwongozi wa kumwokoa na upotofu wake.
24.Kwani watu
wote ni sawa? Mwenye kuikinga adhabu ovu, kali, kwa uso wake Siku ya Kiyama
baada ya kuwa mikono yake imetiwa pingu, ni kama anaye kuja kwa amani Siku ya
Kiyama? Na wenye kudhulumu wataambiwa: Onjeni laana ya vitendo vyenu!
25.Walikanusha
walio kuja kabla ya washirikina hawa, ikawajia adhabu kutoka upande wasio
utaraji.
26.Mwenyezi
Mungu akawaonjesha unyonge katika maisha ya duniani. Ninaapa: Hakika adhabu ya
Akhera ni kubwa zaidi kuliko ya duniani, lau kwamba walikuwa ni watu wa kujua na
kuangalia!
27.Na bila ya
shaka tulikwisha wabainishia watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano wa
kuwakumbusha Haki, kwa kutaraji kuwa watakumbuka na watawaidhika.
28.Tumeiteremsha Qur'ani ya Kiarabu kwa ulimi wao, haina upungufu, kwa
kutaraji kuwa watamcha na watamwogopa Mola wao Mlezi.
29.Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mshirikina kama mtumwa aliye
milikiwa na watu kadhaa wenye kushirikiana, na wenye kumgombania. Na mfano wa
mwenye kuamini Mwenyezi Mungu Mmoja kama mtu ambaye amemilikiwa na mtu mmoja tu.
Je hao wanakuwa sawa? Alhamdulillahi kwa kusimama hoja mbele ya watu.
Lakini watu wengi hawaijui Haki.
30.Hakika wewe,
Muhammad, na wao wote mtakufa. Kisha baada ya kufa kwenu mtafufuliwa mbele ya
Mwenyezi Mungu mkishitakiana nyinyi kwa nyinyi.
31.Hakika wewe,
Muhammad, na wao wote mtakufa. Kisha baada ya kufa kwenu mtafufuliwa mbele ya
Mwenyezi Mungu mkishitakiana nyinyi kwa nyinyi.
32.Basi hapana
aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye msingizia Mwenyezi Mungu lisio
kuwa lake, na akaikanusha Haki bila ya kufikiri wala kuzingatia pale inapo mjia
kwa ndimi za Mitume. Kwani katika Jahannamu sio makaazi ya makafiri walio
ghurika hata wakamfanyia jeuri Mwenyezi Mungu?
33.Na wale
walio ileta Haki na wakaisadiki ilipo wajia, hao ndio wachamngu kweli, wala si
wengineo.
34.Wachamngu
hao watapata kutoka kwa Mola wao Mlezi kila wakipendacho. Fadhila hiyo ni malipo
ya kila mwenye kufanya vizuri katika itikadi yake na vitendo vyake.
35.Mwenyezi
Mungu amewakirimu wachamngu kwa alivyo wakirimu, ili awafutie vile vitendo vyao
viovu kabisa, na awalipe ujira wao kwa bora ya vitendo vyao walivyo vitenda
duniani.
36.Mwenyezi
Mungu, peke yake, ni Mwenye kuwatosheleza waja wake kwa kila lilio wakhusu. Na
ati hao makafiri wa Kikureshi wanakutisha, ewe Muhammad, kwa miungu yao wanayo
iomba badala ya Mwenyezi Mungu. Na hayo ni katika upotovu wao. Na mwenye
kupotozwa na Mwenyezi Mungu, kwa kumjua kuwa huyo amekhiari upotovu kuliko
uwongofu, basi hatakuwa na mwongozi wa kumwongoza.
37.Na mwenye
kuongozwa na Mwenyezi Mungu kuendea Haki, na akamwezesha kuifikia, kwa kujua
kwake kuwa huyo amekhiari uwongofu kuliko upotovu, basi hatokuwapo wa kumpotoa
akaiacha Njia ya Uwongofu. Kwani Mwenyezi Mungu si ndio Yeye ambaye hashindiki
kwa kila upande, ambaye ni Mwenye kulipiza kwa ukali? Na kwa hivyo huwalinda
vipenzi vyake na maadui wake?
38.Na ninaapa,
lau ungeli wauliza, wewe Muhammad, hawa washirikina: Nani aliye ziumba mbingu na
ardhi? Bila ya shaka wangeli sema: Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba. Ewe
Muhammad, waambie: Mmezingatia mkawaona hao miungu mnao washirikisha na Mwenyezi
Mungu, wanaweza kuniondolea madhara ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kunidhuru? Au
wanaweza kunizuilia rehema yake akitaka inifikie? Ewe Muhammad! Waambie: Anaye
nitosheleza kwa kila kitu ni Yeyey peke yake, si mwenginewe, ndiye Yeye wanaye
mtegemea wote wanao tegemea na kumwachilia kila kitu.
39.Waambie, kwa
kuwapa ahadi: Enyi watu! Ishikilieni hiyo hiyo njia yenu ya ukafiri na
kukadhibisha, na mimi hakika ninashikilia aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi.
Mtakuja ona nani katika sisi atakaye fikiwa na adhabu ya kumdhalilisha, na
atakaye teremkiwa na adhabu ya daima isiyo mwondokea?
40.Waambie, kwa
kuwapa ahadi: Enyi watu! Ishikilieni hiyo hiyo njia yenu ya ukafiri na
kukadhibisha, na mimi hakika ninashikilia aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi.
Mtakuja ona nani katika sisi atakaye fikiwa na adhabu ya kumdhalilisha, na
atakaye teremkiwa na adhabu ya daima isiyo mwondokea?
41.Ewe Nabii!
Hakika Sisi tumekuteremshia Qur'ani Tukufu hii kwa watu wote, nayo imekusanya
Haki iliyo thibiti. Basi mwenye kuongoka kwa sababu yake basi manufaa hayo ni
kwa nafsi yake, na mwenye kuipotea njia yake basi balaa ya upotofu wake
itamrejea mwenyewe. Wala wewe, Muhammad, si mwenye kuwakilishwa uwongofu wao.
Jukumu lako ni kufikisha ujumbe, nao umeufikisha.
42.Mwenyezi
Mungu huzitakabadhi roho zinapo kufa. Na huzipokea roho zisio kufa zinapo lala.
Basi huzizuia zilizo kwisha hukumiwa kufa, zisirudi kwenye miili yao, na
huzirudisha nyenginezo ambazo hazijafikilia bado ajali yao, wakati wa kuamka,
mpaka itakapo fika ajali yao ilio wekewa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo
Ishara wazi kwa watu wanao zingatia.
43.Bali
washirikina wakawafanya wengineo badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ni waombezi wao
wa kuwakurubisha kwake. Waambie, ewe Muhammad: Mnafanya haya ijapo kuwa hawa
mnao wafanya "waombezi" hawanacho wanacho kimiliki, wala hawana wanacho
kifahamu?
44.Ewe
Muhammad! Waambie: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake! Hapana anaye
upata ila aridhie Yeye. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake Yeye tu. Na kisha
mtarejeshwa kwake, akuhisabieni vitendo vyenu.
45.Na pindi
akitajwa Mwenyezi Mungu peke yake, bila ya kutajwa miungu yao, nyoyo za wasio
yaamini maisha ya Akhera hukunjana na kukasirika. Na wakitajwa miungu yao wanayo
iabudu badala ya Mwenyezi Mungu wao huwa wepesi kufurahi na kustarehe.
46.Ewe
Muhammad! Sema, nawe umemwelekea Mola wako: Ewe Mwenyezi Mungu! Ewe Muumba
mbingu na ardhi bila ya mithali! Ewe Mjuzi wa siri na dhaahiri! Wewe peke yako,
ndiye wa kuhukumu baina ya waja wako katika hayo wanayo khitalifiana katika
mambo ya dunia na Akhera. Basi hukumu baina yangu na hawa washirikina!
47.Na lau kuwa
hao walio jidhulumu nafsi zao kwa ushirikina wanamiliki vyote viliomo duniani na
mara mbili kama hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kuwa ni fidia ya kujigombolea
nafsi zao na adhabu waliyo andaliwa Siku ya Kiyama. Nao watakuja iona adhabu
itokayo kwa Mwenyezi Mungu ambayo haikupata kuwapitikia katika mawazo yao.
48.Na katika
Siku hii ya leo utawadhihirikia uovu wa vitendo vyao, na itawazunguka adhabu ya
yale waliyo kuwa wakiyafanyia maskhaara duniani.
49.Na mtu
yakimpata madhara hutuomba kwa unyenyekevu; kisha tukimpa neema kwa kumfadhili,
mtu huyo huyo husema: Sikupewa neema hizi mimi ila kwa ujuzi wangu nilio nao wa
kujua kuchuma. Naye mtu huyu kasahau kuwa mambo si hivyo kama asemavyo, bali
neema hizo alizo mneemesha Mwenyezi Mungu ni kama majaribio tu, ni mtihani, ili
amdhihirishe nani mwenye kut'ii na nani mwenye kua'si. Lakini wengi wa watu
hawatambui kama hayo ni majaribio na fitna.
50.Maneno kama
haya waliyasema walio kuwa kabla ya washirikina hawa, na hayakuwalinda na adhabu
hayo mali na starehe waliyo yachuma.
51.Yakawasibu
makafiri walio tangulia malipo ya madhambi ya vitendo vyao, na madhaalimu
miongoni mwa hawa wanao semezwa hivi sasa yatawapata vile vile malipo ya
madhambi ya vitendo vyao. Wala hawa hawataiepuka adhabu.
52.Je! Hawa
wanasema wayasemayo, wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki
amtakaye katika waja wake, na humpa kwa kadiri atakacho kwa mujibu wa hikima
yake? Hakika katika haya bila ya shaka ni mazingatio kwa watu wanao amini.
53.Ewe
Muhammad! Sema kwa kufikisha kutokana na Mola wako Mlezi: Enyi waja wangu walio
jizidishia juu ya nafsi zao maasi, msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu huyafuta madhambi yote. Hakika Yeye, peke yake, ndiye Mkuu
katika kusamehe kwake na kurehemu kwake.
54.Enyi mlio
jidhulumu nafsi zenu, rejeeni kwa Mwenye kuyamiliki mambo yenu yote, na Mlezi
wenu. Na mfuateni Yeye kabla haijakujieni adhabu, tena hapo hapatakuwepo wa
kukunusuruni na Mwenyezi Mungu na kukulindeni na adhabu yake.
55.Na fuateni
yaliyo bora kabisa katika mliyo teremshiwa kutokana na Mola wenu Mlezi, nayo ni
Qur'ani Tukufu, kabla ya kukujieni adhabu kwa ghafla, na bila ya kujitayarisha,
na hali nyinyi hamjui kuja kwake.
56.Rejeeni kwa
Mola wenu Mlezi, na Msilimu kwake, na mfuate mafunzo yake, ili nafsi yenye
dhambi isisema itapo iona adhabu: Ee msiba wangu kwa niliyo yawacha upande wa
Mwenyezi Mungu na katika haki zake, na kwamba mimi nilikuwa duniani miongoni mwa
walio kuwa wakiifanyia maskhara Dini yake.
57.Au iseme ile
nafsi yenye dhambi, kutafuta udhuru: Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli niwezesha
kufuata uwongofu bila ya shaka ningeli kuwa duniani katika wale walio jilinda na
adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa Imani na vitendo vyema.
58.Au iseme
nafsi ile yenye dhambi itapo ona adhabu: Laiti ningeli rejeshwa duniani, nikawa
katika wanao tengeneza imani yao na vitendo vyao!
59.Utayapata
wapi, ewe mwenye majuto! Mafunzo yangu yalikujia katika ndimi za Mitume, nawe
ukayakanusha, na ukajiona bora, ukakataa kuyafuata, na ukawa katika dunia yako
miongoni mwa wenye kushikilia ukafiri.
60.Na Siku ya
Kiyama utawaona walio mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, wakamkhusisha yasiyo kuwa
yake, nyuso zao zimesawjika kwa huzuni na majonzi. Hakika Jahannamu ndio makaazi
ya wenye kiburi wakaikataa Haki.
61.Na Mwenyezi
Mungu atawaokoa alio wajaalia ulinzi isiwapate adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa
vile alivyo kwisha wajua kuwa wamefuzu, kwa walivyo ukhiari uwongofu kuliko
upotofu. Na siku hii basi uovu hautawagusa, wala hawatahuzunika kwa kuzikosa
neema walizo kuwa wakizitaraji.
62.Mwenyezi
Mungu Muumba kila kitu - naye peke yake - ndiye Mlinzi wa kila kitu. Anaendesha
mambo yake kwa mujibu wa hikima yake.
63.Maendesho ya mambo ya katika mbingu na ardhi yako kwa Mwenyezi
Mungu. Hayaendeshi hayo isipo kuwa Yeye. Na makafiri kwa hoja za Mwenyezi Mungu
na ushahidi wake ndio wao, peke yao, ndio wenye kukhasiri, mwisho wa
kukhasiri!
(Injili ya Mathayo 16:16-20 imedai kuwa Yesu kampa funguo
za mbingu na ardhi Petro, na hivyo ndiyo Papa wa Roma amerithi funguo hizo na
kuanzisha Kanisa la Kikatoliki, na uwezo wa kufutia watu dhambi na kuwaangamiza
Motoni. Marcello Craveri, mtaalamu wa Biblia wa Kitaliana ameandika katika
kitabu chake Maisha ya Yesu (sahifa 227-28 Panther Edn.) kuwa Mathayo 16:16-20
imeongezwa na ametoa hoja 7 kwa wazo hilo. Licha ya kuwa Yesu hakumpa Petro hizo
funguo za mbingu na ardhi, yeye mwenyewe Yesu hakuwa nazo.)
64.Ewe
Muhammad! Sema: Je! Baada ya kuweka wazi Ishara zote kuwepo Mwenyezi Mungu Mmoja
wa kuabudiwa, mnaniamrisha nimuabudu mwenginewe, enyi wajinga, majaahili?
65.Na ninaapa:
Bila ya shaka, umepewa Wahyi, wewe, Muhammad na Mitume walio kuwa kabla yako,
kwamba bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote kile basi hapana
shaka Mwenyezi Mungu atazibat'ilisha a'mali zako, na utakuwa katika watu walio
khasirika ukomo wa kukhasiri.
66.Ewe Mtume!
Usiwakubalie kwa hayo wanayo kutaka, bali muabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na
uwe katika wanao mshukuru Yeye kwa neema zake.
67.Washirikina
hawakumtukuza Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki utukufu wake, wala hawakumjua
kama anavyo stahiki kujuulikana, kwa kuwa wamemshirikisha pamoja naye wenginewe,
na wakamtaka Mtume naye aingie katika ushirikina, na hali ardhi yote ni milki
yake Siku ya Kiyama, na mbingu zitakuwa zimekunjwa, kama zinavyo kunjwa nguo,
katika mkono wake wa kulia. Mwenyezi Mungu ametakasika na kila upungufu, na
ametukuka vikubwa mno na vyote hivyo wanavyo mshirikisha naye.
68.Na litapulizwa barugumu kwa yakini (1), na watakufa walioko
mbinguni na katika ardhi ila anaye mtaka Mwenyezi Mungu kumuakhirisha mpaka
wakati mwengine. Kisha litapulizwa mara nyengine, na hapo wote watainuka kutoka
makaburini mwao, wakingojea watafanywa nini?
(1) Hilo barugumu (S'ur)
kilugha, ni tarumbeta, mbiu, siwa, parapanda. Barugumu inalo tusimulia Qur'ani
ni katika mambo ya ulimwengu usio onekana, hatujui lilivyo na hakika yake.
69.Na ardhi
itang'ara siku hiyo kwa nuru ya Muumba wake na Mmiliki wake. Na kitatayarishwa
Kitabu kilicho sajiliwa ndani yake vitendo vyao, na watahudhurishwa Manabii na
mashahidi wapate kuwashuhudia viumbe vyote, na wapambanuliwe baina ya viumbe kwa
uadilifu, na wala hawatadhulumiwa kwa kupunguziwa thawabu wala kuzidishiwa
adhabu.
70.Na kila
nafsi itapewa malipo ya a'mali yake, na Mwenyezi Mungu ni mbora wa kujua vitendo
vyao.
71.Na makafiri
watahimizwa kwenda kwa nguvu kuendea Jahannamu kwa makundi makundi. Na hata
watapo fika milango yake itafunguliwa, na walinzi wake watawaambia kwa
kuwakebehi: Kwani hawakuja kwenu Wajumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu wa jinsi
yenu, wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi, na wakakuhadharisheni na mkutano
wenu huu? Makafiri watasema kwa kukiri: Kwani! Walitujia Mitume. Lakini neno la
adhabu limekwisha wajibikia juu ya makafiri, kwa kuwa wao wamekhiari ukafiri
kuliko Imani.
72.Wataambiwa:
Iingieni milango ya Jahannamu mliyo jaaliwa mkae humo milele. Jahannamu ni
pahala paovu mno pa kukaa wenye kutakabari na wakakataa kuikubali Haki.
73.Na wachamngu
watahimizwa kwenda Peponi kwa hishima makundi makundi, mpaka wakifika kwenye
milango yake, wataambiwa na walinzi wake: Amani kubwa juu yenu! Mmet'ahirika
duniani na uchafu wa maasi, na mmet'ahirika Akhera katika nafsi zenu kwa neema
mlizo zipata. Basi ingieni Peponi mliko jaaliwa kukaa milele. Kwani nyinyi mna
neema zisio pita akilini.
74.Na wachamngu
watasema: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu peke yake, ambaye ametutimizia
aliyo tuahidi kwa ndimi za Mitume wake, na akatumilikisha ardhi ya Peponi
tunashukia tutakapo humo. Ama hakika bora ya ujira wa wenye kutenda mema ni
Pepo.
75.Na utaona,
ewe mwenye kuona, Malaika wakiizunguka A'rshi, wakimtakasa Mwenyezi Mungu na
kila upungufu, kwa utakaso unao fuatana na kumhimidi Muumba wao na Mlezi wao, na
akapambanua baina ya viumbe vyote kwa uadilifu, na ulimwengu wote ukatamka kwa
kusema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani