1. S'ad: Ni
harufi iliyo anzia Sura hii kama zilivyo anzia baadhi ya Sura nyengine kwa
mpango wa Qur'ani katika kuanzia kwa harufi moja moja. Naapa kwa Qur'ani yenye
utukufu na shani kubwa kuwa hakika hii ni Kweli isiyo na shaka yoyote.
2. Lakini walio
kufuru wamo katika majivuno, hawataki kufuata Haki, na wanawafanyia inda watu wa
Haki.
3. Mataifa
mengi tuliyateketeza kabla yao, wakapiga kelele kutaka msaada ilipo wafikia
adhabu. Lakini huo haukuwa wakati wa kuiepuka adhabu.
4. Na
walistaajabu watu hawa kuwa amewajia Mtume binaadamu kama wao, na wakasema hao
wanao upinga Ujumbe wake: Huyu ni mdanganyifu, mwongo.
5. Ati
amewafanya miungu yote kuwa ni Mungu mmoja tu! Ama hakika jambo hili ni la
ajabu, mwisho wa kustaajabisha.
6. Wakubwa wao
wakakimbilia kuusiana wao kwa wao wakiambiana: Endeleeni na njia yenu hiyo hiyo,
na shikilieni kuiabudu miungu yenu. Kwani hakika tumepangiwa jambo kubwa hili.
7. Hatujapata
kusikia haya mambo ya Tawhidi, kumfanya Mungu mmoja tu, katika dini ya baba zetu
tulio wawahi kuwaona. Haya si chochote ila ni uwongo tu ulio zuliwa.
8. Basi katika
sote sisi, amechaguliwa Muhammad tu peke yake kupewa hishima ya kuteremshiwa
Qur'ani?
9. Bali sisi
tunawauliza hawa wanao kuhusudu: Kwani wao wanazo khazina za rehema ya Mola wako
Mlezi Mwenye nguvu, Mwingi wa kutoa, hata wao wawe ndio wa kuteua nani wa kumpa
Unabii kwa mujibu wa mapenzi ya nafsi zao?
10. Tena
tunawauliza: Kwani wao wanao ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo baina yao?
Ikiwa hivyo basi nawazipande ngazi mpaka wafikie pahala ambapo watakuwa wakitoa
hukumu kama watakavyo, kama wanaweza!
11. Hao ni
askari wanyonge walio shindwa, hapana hivi wala hivi, kama walivyo shindwa mfano
kama wao walio jikusanya kuwapinga Manabii.
12,13. Kabla
ya hawa, walikadhibisha kaumu ya Nuhu, kina A'adi na Firauni aliye kuwa na
majengo makubwa yaliyo simama imara kama milima, na kina Thamudi na Kaumu Lut'i
na Kaumu ya Shuaibu, na watu wa Machakani, kwenye miti mingi iliyo shikamana.
Hao ndio walio jumuika kuwapinga Mitume wao kama walivyo jumuika watu wako.
12,13. Kabla
ya hawa, walikadhibisha kaumu ya Nuhu, kina A'adi na Firauni aliye kuwa na
majengo makubwa yaliyo simama imara kama milima, na kina Thamudi na Kaumu Lut'i
na Kaumu ya Shuaibu, na watu wa Machakani, kwenye miti mingi iliyo shikamana.
Hao ndio walio jumuika kuwapinga Mitume wao kama walivyo jumuika watu wako.
14. Hapana
mmoja katika hao wote ila alimkadhibisha Mtume wake, na kwa hivyo ikawashukia
adhabu yangu.
15. Na hao
walio jiunga kuwapinga Mitume hawangojei ila ukelele mmoja usio hitajia
kukaririwa.
16. Na
makafiri husema kwa kejeli: Mola wetu Mlezi! Tuhimizie sehemu yetu ya adhabu
kabla ya Siku ya Malipo.
17. Ewe
Muhammad! Yastahamilie hayo wanayo yasema juu yako washirikina. Na mkumbuke mja
wetu, Daudi, mwenye nguvu katika Dini na dunia. Hakika yeye alikuwa mwingi wa
kurejea kwa Mwenyezi Mungu katika hali zote.
18. Hakika
Sisi tuliidhalilisha milima pamoja naye, yeye akichuma manufaa kutoka humo, na
hiyo milima ikimtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kila upungufu, wakati wa mwisho
wa mchana na mwanzo wake.
19. Na pia
tukamdhalilishia ndege walio kusanywa kutokana na kila namna na kila pahali.
Vyote hivyo, milima na ndege, vikimwitikia Daudi kama atakavyo, akivisarifu kama
apendavyo kwa maslaha ya umma.
20. Tukautia
nguvu ufalme wake, na tukampa Unabii na kupambanua baina ya Haki na baat'ili.
21. Ewe
Muhammad! Ati imekujia khabari ya makhasimu wagombanao, walio mjia Daudi kwa
kupindukia kuta za mihrabuni palipo kuwa pahala pake pa ibada? Hawakupita
mlangoni.
22. Walipo
muingilia Daudi, naye akawaogopa, akababaika. Wakasema: Usikhofu kitu. Sisi ni
wenye kuzozana, tumedhulumiana. Basi tuhukumu kwa uadilifu wala usiupindukie huo
uadilifu. Na tuongoze kwenye njia iliyo sawa sawa.
23. Mmoja wa
hao wagombanao alisema: Hakika huyu ndugu yangu anao kondoo wa kike tisiini na
tisa, na mimi ninaye kondoo mmoja tu. Akasema: Nache niwe nakuchungia kama
ninavyo wachunga wangu. Na akanishinda katika usemi.
24. Daudi
akasema kabla hajasikia maneno ya yule mwenye ugomvi mwengine: Hakika huyo
amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako amchanganye na wale wake. Na hakika wengi
wenye kushirikiana hudhulumiana wao kwa wao, isipo kuwa wale ambao Imani yao
imetulia katika nyoyo zao, na wakawa wanatenda mema. Na watu kama hao ni
wachache, shida kupatikana. Na Daudi akajua kuwa jambo hili si chochote ila ni
mtihani tuliyo mfanyia Sisi. Basi akaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, na
akainama kurukuu kwa Mwenyezi Mungu, na akarejea kwa Mwenyezi Mungu kwa
unyenyekevu.
25. Na Sisi
tukamsamehe kule kufanya haraka ya kutoa hukumu. Na hali yeye ana hadhi na
marejeo mazuri kwetu.
26. Na
Mwenyezi Mungu alimfunulia kwa kumwambia: Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya
wewe uwe Khalifa, yaani Naibu, wetu katika ardhi. Basi wahukumu watu kwa sharia
niliyo kupa, wala usiendeshe hukumu kufuata matamanio yao, yakakupotosha njia ya
Mwenyezi Mungu. Hakika wendao pogo na njia ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata
matamanio yao wao watapata adhabu kali kwa kughafilika kwao na Siku ya Malipo.
27. Wala Sisi
hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa mchezo. Hayo ndiyo wanayo
yadhania makafiri. Na kwa hivyo wakapitisha hukumu kwa mujibu wa pumbao zao.
Basi hao walio kufuru watapata adhabu kali ya Moto.
28.
Inaelekeana vipi na hikima yetu na uadilifu wetu tuwafanye sawa baina ya Waumini
wenye kutenda mema, na wale wanao fanya uharibifu katika ardhi? Au yaelekea vipi
tuwaweke sawa baina ya wenye kuikhofu adhabu yetu na wakaiogopa ikabu yetu na
wale walio waasi wakenda kinyume na hukumu zetu?
29. Ewe
Muhammad! Hichi tulicho kuteremshia ni Kitabu chenye manufaa mengi, ili wenye
akili nzuri na nyoyo za kufahamu wapate kuzielewa Aya zake, na wawaidhike kwazo.
30. Na Daudi
tulimtunukia mwana, aitwaye Suleiman, mwenye kustahiki sifa nzuri, ambaye anafaa
kuitwa, "Mja mwema kweli". Kwa sababu yeye alikuwa mwingi mno wa kurejea kwa
Mwenyezi Mungu katika kila hali.
31. Na hebu
taja katika khabari za Suleiman kuwa alipelekewa alasiri farasi wa asli ambao
hutulia wanapo simama, na huenda mbio wanapo kwenda.
32. Suleiman
akasema: Hakika mimi nimenyweshwa mapenzi ya farasi, kwa sababu hawa ni katika
matayarisho ya mambo ya kheri, nayo ni Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu.
Mapenzi haya yametokana na kumkumbuka Mola wangu Mlezi. Na hakusita kushughulika
kuwaangalia mpaka wakapotea machoni mwake.
33. Akaamrisha
warudishwe tena kwake apate kujua hali yao. Akaingia kuwapapasa miundi ya miguu
yao na shingo zao kwa upole na mapenzi juu yao.
34. Na hakika
Sisi tulimfanyia mtihani Suleiman ili asighurike na heba ya ufalme. Tukaweka juu
ya kiti chake kiwiliwili kisicho weza kuendesha mambo. Akautambua mtihani,
akarejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akatubu.
35. Suleiman
alimwomba Mola wake Mlezi kwa kurejea kwake: Mola wangu Mlezi! Nighufirie yaliyo
toka kwangu kwa ghafla, na unitunukie ufalme usio elekea yeyote kuupata baada
yangu. Hakika Wewe ndiye Mwingi wa kutunukia, na ndiye Mwingi wa kutoa.
36.
Tukamdhalilishia upepo, ukenda kama anavyo taka maridhawa, kokote aliko kusudia
na kutaka.
37. Na
tukamdhalilishia kila mjenzi na mpiga mbizi katika bahari kuu miongoni mwa
mashetani maasi.
38. Na wengine
katika hao mashetani wamefungwa wao kwa wao kwa minyororo, kuwazuia na wenginewe
wasifanye ufisadi wao.
39. Na
akamfunulia kwa wahyi : Haya tuliyo kuneemesha kwayo ni kipawa kilicho toka
kwetu. Yaani ni Sisi tulio kupa. Basi mpe umtakaye, na mnyime umtakaye. Hapana
hisabu juu yako kwa kutoa au kunyima.
40. Hakika
Suleiman kwetu Sisi ana ukaribisho mkubwa, na marejeo mazuri.
41. Ewe
Muhammad! Mkumbuke mja wetu Ayubu alipo mwomba Mola wake Mlezi kwa kusema:
Hakika Shetani amenipatisha taabu na machungu.
42.
Tukamuitikia na tukamwambia: Ipige ardhi kwa mguu wako, yatatimbuka maji baridi,
utakoga na utakunywa hayo, na kwa hivyo yatakuondokea machofu na adhabu.
43.
Tukamkusanyia watu wake walio kuwa wametapanyika mbali naye siku zile za mateso
yake. Na tukamzidishia wenginewe kama wale. Na tulifanya hayo kuwa ni rehema
kutokana nasi, na ili yawe ni mawaidha kwa wenye akili, wapate kujua kuwa
matokeo ya subira ni faraji.
44. Ayubu
alikuwa kaapa kuwa atampiga mmoja wapo katika ahali zake fimbo kadhaa wa kadhaa.
Mwenyezi Mungu alimhalalishia aondoe kiapo chake kwa kuchukua kifungu cha fimbo
idadi ile ile alio apia kuwa atampigia. Basi kwa kile kifungu cha fimbo ampige
aliye apa kuwa atampiga, na hapo yamini yake itakuwa imetimia kwa uchache wa
machungu. Mwenyezi Mungu ndiye aliye mneemesha kwa neema hizi, kwa sababu
Mwenyezi Mungu alimwona kuwa ni mtu aliye vumilia masaibu yake. Kwa hivyo
amestahiki sifa. Mbora wa kusifiwa kwa ibada ni yeye, kwa sababu yeye ni mwingi
mno wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu katika kila jambo.
45. Na
mkumbuke mja wetu Ibrahim, na Is-haqa, na Yaa'qubu, wenye nguvu katika Dini na
dunia, na wenye busara ya mwangaza.
46. Hakika
Sisi tumewakhusisha wao kwa sifa, nayo ni kuwa wanaikumbuka Nyumba ya Akhera,
wao wanaikumbuka nao wanakumbukwa kwayo.
47. Na hakika
wao kwetu Sisi ni wenye kukhitariwa walio bora.
48. Na
mkumbuke Ismail, na Alyasaa, na Dhalkifli - na wote hao ni miongoni mwa walio
bora.
49. Haya
tuliyo kusimulia ni khabari za baadhi ya Mitume ili kukukumbusha wewe na
kuwakumbusha watu wako. Na hakika wachamngu walio jikinga na kumuasi Mwenyezi
Mungu Mtukufu watapata marejeo mazuri na natija njema.
50.
Wameandaliwa bustani za milele zilizo funguliwa milango yao hapana wa kuwazuia
wasiingie humo.
51. Watakuwa
wamekaa humo wakiegemea juu ya makochi na vitanda kama wafanyavyo wenye taanusi,
wakistarehe kwa kutaka matunda ya kila namna na vinywaji.
52. Na huko
Peponi watakuwa na wake ambao macho yao hayawatazami ila waume zao tu,
hawawaangalii wengineo, nao ni wa miaka sawa na waume zao. Kwa hivyo
wameelekeana kuwafikiana.
53. Raha hii
ndiyo mliyo ahidiwa kuipata Siku ya Kiyama.
54. Hakika
haya bila ya shaka ni tunayo yatoa Sisi, na wala hayana ukomo.
55. Neema hizi
ni malipo ya wachamngu. Na hakika majabari wenye kuwaasi Manabii wao bila ya
shaka watakuwa na marejeo na mwisho muovu.
56. Na mwisho
huo ni Jahannamu watakayo iingia, na moto wake uwatese. Na malalio maovu mno
hayo!
57. Haya maji
ya moto, mwisho wa umoto, na usaha wa watu wa Jahannamu wataamrishwa wayaonje.
58. Na adhabu
nyengine mfano wa hizi, za namna kwa namna zilizo changanyika.
59. Na
majabari, wale marais wa washirikina, wataambiwa: Hawa chungu ya watu wanao
ingia Motoni pamoja nanyi kwa kusukumana na kwa shida, ni wafwasi wenu. Wale
marais watasema: Hawana mapokezi mema hao! Hakika hao wanaingia Motoni wapate
kuteseka kwa mvukuto wake.
60. Na wafwasi
hao watasema: Bali nyinyi ndio mnastahiki zaidi hayo maapizo mnayo tuapizia
sisi, kwani nyinyi ndio mlio tuletea adhabu hii kwa vile mlivyo tudanganya na
mkatuitia ukafirini, nasi tukakufuru kwa sababu yenu. Basi nyumba ovu kabisa ya
kukaa ni Jahannamu!
61. Wafwasi
watasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Aliye kuwa ni sababu ya adhabu hii, mzidishie
adhabu mara mbili katika Moto.
62. Na watu wa
Motoni watasema: Mbona hatuwaoni wale watu ambao tulikuwa duniani tukiwahisabu
kuwa ndio katika waovu, na wa duni, wasio kuwa na jema lolote? Na watu hao ni
wale mafakiri wa Kiislamu.
63. Imekuwaje
kuwa sisi tukiwakejeli na wala hawakuingia Motoni pamoja nasi? Au wamekwisha
ingia na macho yetu yakazibwa tusiwaone tu?
64, Hakika
hayo tuliyo yataja ya hadithi ya watu wa Motoni ni kweli ambayo haina budi
kutokea, nayo ni ya kugombana kwa watu wa Motoni wao kwa wao.
65. Ewe
Muhammad! Waambie washirikina: Hakika mimi ni mwenye kukuonyeni na adhabu ya
Mwenyezi Mungu, na hapana wa kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu Mmoja ambaye
hana mshirika wake, Mtenda nguvu, Mwenye kumshinda kila mwenye madaraka.
66. Mola Mlezi
wa mbingu na ardhi na viliomo baina yao, Mwenye nguvu asiye shindika, Mwenye
kusamehe, akazifuta dhambi za mwenye kumuamini.
67,78. Ewe
Muhammad! Waambie: Haya ninayo kuambieni ni khabari kubwa, ambazo nyinyi
mnazipuuza. Msizikanye!
67,78. Ewe
Muhammad! Waambie: Haya ninayo kuambieni ni khabari kubwa, ambazo nyinyi
mnazipuuza. Msizikanye!
69. Mimi
sikuwa nikijua khabari za watukufu walio juu walipo kuwa wakizozana juu ya
shauri ya Adam, kwa sababu mimi sikupitia njia za kupata ilimu zilizo zowewa na
watu za kusoma vitabu au kupokea masomo kwa wataalamu. Njia yangu mimi ya kujua
ni kwa kufunuliwa kwa Wahyi.
70. Na mimi
sikufunuliwa kwa Wahyi ila kwamba hakika mimi ni Mtume wa kukufikishieni Ujumbe
wa Mola wangu Mlezi kwa njia iliyo wazi kabisa.
71. Watajie
pale alipo sema Mola wako Mlezi kuwaambia Malaika: Mimi nataka umba mtu, naye ni
Adam a.s., kutokana na udongo.
72. Nikisha
timiza kumuumba na nikampulizia siri ya uhai, nayo ni roho, muangukieni kwa
kusujudu sijida ya kumtukuza na kumuamkia.
73,74. Malaika
wote wakafanya kama walivyo amrishwa, wakamuangukia wakisujudu, isipo kuwa
Iblisi. Yeye hakusujudu, na akajiona bora na akapanda kiburi, na akawa miongoni
mwa makafiri.
73,74. Malaika
wote wakafanya kama walivyo amrishwa, wakamuangukia wakisujudu, isipo kuwa
Iblisi. Yeye hakusujudu, na akajiona bora na akapanda kiburi, na akawa miongoni
mwa makafiri.
75. Mwenyezi
Mungu Mtukufu akasema: Ewe Iblisi! Nini kilicho kuzuilia kumsujudia niliye
muumba Mimi mwenyewe bila ya kuingiliwa na yeyote kati yake! Umejiona mkubwa
hali nawe si mkubwa, au hakika wewe nafsi yako ni katika walio shinda ukubwa?
76. Iblisi
akasema: Mimi ni bora kuliko Adam; kwani Wewe umeniumba kwa moto, na yeye
umemuumba kwa udongo. Basi vipi mimi nimsujudie yeye?
77. Mwenyezi
Mungu Mtukufu, kwa kumlipa Iblisi kwa kiburi chake cha kukataa amri ya Mola wake
Mlezi, alimwambia: Basi toka kwenye kundi la watukufu walio juu, kwani wewe
umekwisha fukuzwa kutokana na rehema yangu!
78. Na hakika
wewe umetengwa mbali na kila kheri mpaka Siku ya Malipo. Hapo utalipwa kwa
sababu ya kunikufuru Mimi na kunifanyia kiburi.
79. Iblisi
akasema: Mola Mlezi! Nipe muhula, wala usinifishe mpaka Siku ya kufufuliwa
viumbe.
80,81. Akasema
Mwenyezi Mungu Mtukufu: Basi wewe utaakhirishwa, utapewa muhula, mpaka siku ya
wakati tunao ujua Sisi, nao ni kumalizika dunia.
80,81. Akasema
Mwenyezi Mungu Mtukufu: Basi wewe utaakhirishwa, utapewa muhula, mpaka siku ya
wakati tunao ujua Sisi, nao ni kumalizika dunia.
82,83. Iblisi
akasema: Basi naapa kwa Ukubwa wako na Utukufu wako, kwa yakini nitawapoteza
watu wote, isipo kuwa waja wako ulio wateuwa kwa ajili ya kukut'ii Wewe. Hao
sina madaraka nao.
82,83. Iblisi
akasema: Basi naapa kwa Ukubwa wako na Utukufu wako, kwa yakini nitawapoteza
watu wote, isipo kuwa waja wako ulio wateuwa kwa ajili ya kukut'ii Wewe. Hao
sina madaraka nao.
84,85. Akasema
Mwenyezi Mungu Mtukufu: Haki ndiyo yamini yangu na kiapo changu; na wala sisemi
ila Haki. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa jinsi yako ya kishetani na
watakao kufuata katika vizazi vya Adam wote. Hapana khitilafu kwangu baina ya
wafuasi na wanao fuatwa.
84,85. Akasema
Mwenyezi Mungu Mtukufu: Haki ndiyo yamini yangu na kiapo changu; na wala sisemi
ila Haki. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa jinsi yako ya kishetani na
watakao kufuata katika vizazi vya Adam wote. Hapana khitilafu kwangu baina ya
wafuasi na wanao fuatwa.
86. Ewe
Muhammad! Waambie umma wako: Mimi sikuombeni ujira kwa ajili ya haya niliyo
amrishwa nikufikishieni yaliyomo katika Qur'ani na Wahyi. Wala mimi si katika
hao wanao jipamba na yasiyo kuwa yao, hata nijidai Unabii.
87. Haikuwa
Qur'ani ila ni ukumbusho na mawaidha kwa walimwengu wote.
88. Na hapana
shaka nyinyi, mnao ikadhibisha Qur'ani, mtakuja jua karibuni hivi ukweli uliomo
ndani yake wa ahadi, na maonyo, na khabari za mambo yatakayo kuja, na Ishara za
ulimwengu.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani