1. Naapa kwa
mataifa katika viumbe vyangu, walio jipanga wenyewe kwa safu zilio sawa katika
msimamo wa ibada na ut'iifu.
2. Na kwa wanao
zuia wanao pindukia mipaka kwa mzuio mkali, nidhamu ibakie, na ulimwengu
uhifadhiwe.
3. Na kwa wenye
kusoma Aya, na wanamdhukuru Mwenyezi Mungu kwa dhikri ya Tasbihi, Kumtakasa, na
Kumhimidi, kumsifu.
4. Hakika Mungu
wenu anaye faa kuabudiwa bila ya shaka ni Mmoja tu. Hana mshirika wake, kwa
dhati, wala kitendo, wala sifa.
5. Yeye - peke
yake - ndiye Muumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao, na ndiye Mwenye
kupanga mambo, na ndiye Mwenye kutawala mashariki za kila chenye mashariki.
Mwenyezi Mungu ndiye Muumba mbingu saba na viliomo baina yao, navyo ni hivyo
vyombo vya mbinguni na nyota zake. Naye ndiye Mwenye kusimamisha, Mwenye kulinda
vile vile juu ya mwahali zinapo chomozea jua na nyota zote. Na Yeye ndiye anaye
vionyesha hivyo kila siku katika pahala huko upeo wa macho, kila siku pahala
mbali na vilipo dhihiri siku iliyo tangulia. Na hayo ni kwa mwendo wa mpango wa
jua maalumu kwa inavyo zunguka dunia juu ya msumari-kati wake kutoka magharibi
kwendea mashariki kila siku na wakati huo huo inavyo lizunguka jua katika njia
yake katika falaki. Na jua na nyota huonekana na wakaazi wa ardhi kila siku kama
zinachomoza mwahala mbali mbali. Na kila ardhi ikigeuza mahala pake katika
safari yake katika mbingu linaonekana jua linachomoza pahala pengine.
Ukiliangalia jua kwa utulivu kuanzia mwishoni wa mwezi wa Machi, yaani linapo
kuwa jua lipo kati ya mstari wa Ikweta mwanzo wa musimu wa Rabii, yaani Spring,
kwa nusu ya kaskazini ya dunia, utaliona linachomoza pahala katika mashariki juu
ya upeo wa macho. Kwa mwenye kupeleleza kila siku ikipita ataona kuchomoza kwake
kunajongelea kaskazini. Na mwishoni mwa mwezi wa Juni utaona linachomozea mwisho
wa kukaribia kaskazini. Kisha baada ya hapo utaliona jua linarejea linafuata
kugeuka kule kule mpaka mwisho wa Septemba (wakati wa kuwa sawa wakati wa
Khariif yaani Autumn) utaliona jua linachomoza pale pale lilipo chomoza mwanzo
wa Machi. Kisha litaendelea kuelekea kusini kuchomoza kwake mpaka mwisho wa
Desemba linakuwa linachomoza karibu kabisa na kusini. Baada ya hapo huanza tena
kurejea kuelekea kaskazini mpaka limalize safari yake ya kufika kati sawa katika
Rabii ya pili. Na safari hii yote inachukua siku 365 na robo siku. Na inaonekana
kuwa nyota nazo zinachomoza mwahala mbali mbali katika upeo wa macho inapo kuwa
dunia imo katika safari yake ya mbinguni, na khasa nyota za buruji (au vituo) 12
vinavyo pitiwa na jua katika mwendo wake wa mwaka.
6. Sisi
tumeipamba hii mbingu ya karibu na watu wa duniani kwa mapambo, nayo ni hizo
nyota zinazong'ara, zenye ukubwa mbali mbali, na mwahala pao mbali mbali kwenye
anga la ulimwengu kama ionekanavyo kwa macho.
7. Na
tukaihifadhi hiyo mbingu na kila shetani jabari aliye a'si.
8. Hao majabari
wa kishetani hawawezi kusikiliza yanayo pita katika ulimwengu wa Malaika. Na wao
hupopolewa kwa kila kinacho faa cha kuwazuia.
9. Hufukuzwa
hao kwa nguvu wasifikilie kuweza kusikiliza khabari za mbinguni. Na Akhera
watapata adhabu kali ya kudumu.
10. Isipo kuwa
anaye lipata neno moja hivi katika khabari za mbinguni kwa kuibia. Na huyo naye
tunamwandama kwa mwenge wa moto unao murika anga kwa mwangaza wake,
ukamuunguzilia mbali.
11. Ewe Nabii!
Hebu waulize hao wanao kanya kufufuliwa wanao ona hayawi hayo: Je! Kwani
kuwaumba wao hawa ni kugumu zaidi au kuziumba mbingu, na ardhi, na nyota, na
vyenginevyo, tulivyo viumba Sisi?
12. Hakika
Sisi tumewaumba wao kutokana na udongo unao gandana. Basi kwa nini wanaona ajabu
kurejezwa tena wao?
13. Na wanapo
kabiliwa kwa dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu kufufua, hata hawazishughulikii
wakanufaika kwa hizo dalili.
14. Na wanapo
ona ushahidi wa kuonyesha uweza wa Mwenyezi Mungu huitana wapate kupita mipaka
katika kumkejeli.
15. Na
makafiri husema juu ya Ishara zinazo onyesha uweza wa Mwenyezi Mungu: Haya
tunayo yaona si chochote ila ni uchawi tu.
16. Hivyo sisi
tukisha kufa tukawa udongo na mafupa tutatolewa tena makaburini kwetu tuwe
wahai?
17. Sisi tuwe
wahai, na pia watafufuliwa baba zetu wa zamani walio kufa kabla yetu, na
wakapotea, na wakateketea?
18. Ewe Nabii!
Waambie: Ndio mtafufuliwa nyote, nanyi ni madhalili na wanyonge.
19. Kwani
hakika kufufuliwa ni Ukelele mmoja tu, mara wote watakuwa wahai wakiyaona waliyo
ahidiwa.
20. Na
washirikina watasema: Ee msiba wetu huu! Hii ndiyo Siku ya Hisabu na Malipo kwa
a'mali zilio tendwa!
21.
Watajibiwa: Hii ndiyo Siku ya Hukumu na kufarikisha vitendo, mliyo kuwa
mkiikadhibisha.
22,23. Enyi
Malaika wangu! Wakusanyeni walio jidhulumu nafsi zao kwa kufuru, pamoja na wake
zao wa kikafiri, na miungu yao waliyo kuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu,
yakiwa masanamu au watu, na waonyesheni njia ya kwendea Motoni waingie humo.
22,23. Enyi
Malaika wangu! Wakusanyeni walio jidhulumu nafsi zao kwa kufuru, pamoja na wake
zao wa kikafiri, na miungu yao waliyo kuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu,
yakiwa masanamu au watu, na waonyesheni njia ya kwendea Motoni waingie humo.
24. Na
wazuieni hapo hapo; kwani wao hakika watahojiwa juu ya imani zao na vitendo
vyao.
25. Enyi
washirikina! Mna nini? Mbona hamsaidiani kama mlivyo kuwa mkisaidiana nyinyi kwa
nyinyi duniani?
26. Leo hii
hawasaidiani, bali leo wanaongozwa tu, wamekwisha salimu amri.
27. Watakuwa
wakikabiliana kulaumiana na kusutana, na wakiulizana khabari za mwisho wao
muovu.
28. Wanyonge
watawaambia walio jipa ukubwa: Nyinyi mlikuwa mkitujia upande tulio udhania ni
wa kheri na mafanikio, ili mtugeuze njia tuache Haki twende kwenye upotovu.
29. Watasema
walio jipa ukubwa: Sisi hatukukugeuzeni njia, lakini nyinyi wenyewe mliikataa
Imani, na mkaipuuza kwa khiari yenu.
30. Na sisi
hatukuwa na madaraka juu yenu hata tuweze kukunyang'anyeni uweza wenu wa
kukhiari. Bali nyinyi wenyewe mlikuwa watu mlio iacha Haki.
31. Basi neno
la Mola wetu Mlezi limethibiti juu yetu. Hakika hapana shaka sisi tutaionja
adhabu ya Siku ya Kiyama.
32.
Tukakuiteni kwenye maasi na upotovu na nyinyi mkaitikia wito wetu. Kazi yetu ni
kufanya hila ya kuwaita watu wafuate upotovu tulio nao. Basi hatuna lawama.
33. Kwani
hakika wafuasi na wenye kufuatwa wote watashiriki pamoja katika adhabu ya Siku
ya Kiyama.
34. Hakika
mfano wa adhabu hiyo Sisi tunawapa wale walio fanya makosa katika Haki ya
Mwenyezi Mungu kwa ushirikina na kutenda maasi.
35. Hakika
watu hao walikuwa wakiambiwa: La ilaha illa 'Llah, Hapana mungu ila Mwenyezi
Mungu tu, wakakataa kukiri kwa kiburi na majivuno.
36. Na husema:
Sisi tuache kuabudu miungu yetu kwa kufuata kauli ya mtunga mashairi aliye zugwa
asiye kuwa na akili?
37. Bali Mtume
wao amewaletea Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, ambayo ndiyo wito wa
Mitume wote, naye akasadikisha kwa hivyo wito wa hao Mitume.
38. Enyi
washirikina! Hakika nyinyi hapana shaka mtaionja adhabu kali ya Akhera.
39. Na
hamtapata malipo Akhera ila malipo ya vitendo vyenu vya duniani.
40. Ila waja
wangu walio safika; hao hawataionja adhabu kwa sababu wao ni watu wa Imani na
ut'iifu.
41. Hawa watu
wa ikhlasi watapata Akhera riziki maalumu kwa Mwenyezi Mungu.
42. Matunda ya
namna mbali mbali. Nao watastareheshwa na kutukuzwa,
43. Katika
Bustani zenye neema.
44. Wakikaa
humo juu ya viti wakikabiliana.
45.
Watawazungukia watoto na chombo chenye kinywaji kilicho toka kwenye chemchem
zisio katika.
46. Kinywaji
chenyewe ni cheupe kinapo changanywa, na kitamu kwa wenye kukinywa.
47.
Hakiwaumizi kichwa na kuwaletea ghururi, wala kwa kukinywa hicho haiwapotei
akili yao kidogo kidogo, yaani hakileweshi.
48. Na watu
hawa wat'iifu walioko Peponi watakuwa nao mahuruleini walio safi, wema, macho
yao hayawatazami ila waume zao tu, basi hawayatafuti matamanio maovu, jicho la
mwema haliangalii ila mema.
49. Hao
wanawake wenye macho ya staha ni kama mayai ya mbuni, yaliyo hifadhiwa na mbawa
zake. Basi hayaguswi na mikono, wala hayapati vumbi.
50. Hao watu
wema watakuwa wakiingia kuulizana hali, na walikuwaje duniani?
51. Hapo mmoja
wao atasema: Mimi nalikuwa na rafiki katika washirikina, akijadiliana nami
katika mambo ya Dini na yaliyo kuja katika Qur'ani.
52. Akisema:
Ati wewe ni katika hao wanao sadiki kuwa kupo kufufuliwa na kuhisabiwa na
kulipwa baada ya kufa?
53. Ati baada
ya kwisha teketea, tukawa udongo na mafupa, tutakuja kuwa hai mara nyengine,
tuhisabiwe na tulipwe kwa vitendo tulivyo kwisha vitenda?
54. Muumini
awaambie wenzie alio kaa nao: Enyi watu wa Peponi, mnawaona watu wa Motoni
nipate kumwona rafiki yangu?
55. Jicho lake
lipige duru kuelekea Motoni, na huko amwone sahibu yake wa zamani yuko katikati
akiadhibika kwa Moto.
56. Akimwona
aseme: Wallahi! Ulikaribia kule duniani kunihilikisha lau ningeli kufuata katika
ukafiri wako na maasiya yako!
57. Na lau
kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi kwa hidaya yake na kuniwezesha kwake
nikamuamini Mwenyezi Mungu na kufufuka, basi ningeli kuwa mfano wako wewe katika
walio hudhurishwa katika hiyo adhabu.
58,59. Je!
Sisi tutakaa milele tukineemeka katika Pepo, wala hatufi kabisa isipo kuwa kule
kufa kwetu mara ya kwanza duniani, na wala hatuadhibiwi baada ya kwisha ingia
Peponi?
58,59. Je!
Sisi tutakaa milele tukineemeka katika Pepo, wala hatufi kabisa isipo kuwa kule
kufa kwetu mara ya kwanza duniani, na wala hatuadhibiwi baada ya kwisha ingia
Peponi?
60. Hakika
haya aliyo tupa Mwenyezi Mungu katika ukarimu wa Peponi bila ya shaka ndiyo
kufuzu kukubwa, na kuvuka kukuu na hiyo adhabu tuliyo kuwa tunatahadhari nayo
tangu duniani.
61. Ili wapate
ukarimu wa Akhera kama walio bahatika kuupata Waumini, basi nawafanye kazi
duniani hao wafanyao kazi, ili wapate kama walio pata wao.
62. Je! Hiyo
riziki maalumu iliyo andaliwa kwa sababu ya watu wa Peponi ni bora, au mti wa
Zaqqum ulio andaliwa kwa ajili ya watu wa Motoni?
63. Hakika
Sisi tumeujaalia mti huu uwe ni mtihani na adhabu ya Akhera kwa ajili ya
washirikina.
64. Hakika huo
ni mti ulioko katikati ya Jahannamu, umekulia huko Motoni, na umeumbwa kutokana
na huko huko.
65. Matunda
yake mabaya kuyatazama, yana sura ya kukirihisha, macho hayapendi kuyatazama,
kama vichwa vya mashetani ambavyo kwa hakika watu hawajaviona, lakini mtu
humpitikia tu katika dhana jinsi ya ubaya wake.
66. Na wao
watakuwa wanakula matunda ya mti huo, na wajaze matumbo yao kwayo. Kwani
hawanacho kinginecho cha kukila.
67. Kisha
washirikina hao juu ya kula mti wa Zaqqum watapewa maji yaliyo changanywa,
yamoto, ya kuwababua nyuso zao, na kukatakata matumbo yao.
68. Tena
mwisho wao ni Motoni. Wao watakuwa katika adhabu ya milele. Wataletwa kutoka
Motoni waje kula mti wa Zaqqum kisha wanyweshe kinywaji hicho, na tena
warejeshwe mahala pao katika Jahannamu.
69,70. Wao
waliwakuta baba zao wamepotoka, na wao wakafanya haraka kufuata zile zile nyayo
za baba zao. Wakawa mbioni kwendea njia yao, wakifuata tu wala hawachungui, kama
walio timuliwa na wakihimizwa wende mbio mbio kuwafuata hao baba zao bila ya
kupima wala kuzingatia.
69,70. Wao
waliwakuta baba zao wamepotoka, na wao wakafanya haraka kufuata zile zile nyayo
za baba zao. Wakawa mbioni kwendea njia yao, wakifuata tu wala hawachungui, kama
walio timuliwa na wakihimizwa wende mbio mbio kuwafuata hao baba zao bila ya
kupima wala kuzingatia.
71. Na hakika
walipotea njia ya sawa na njia ya Imani wengi katika mataifa yaliyo kwisha
tangulia kabla ya hawa washirikina wa Makka.
72. Na bila ya
shaka Sisi tuliyatumia Mitume hayo mataifa yaliyo tangulia ili wawaonye na
wawahadharishe na adhabu ya Mwenyezi Mungu, nao wakawakadhibisha.
73. Basi
angalia, ewe uliye jaaliwa kuangalia, ulikuwaje mwisho wa walio onywa na Mitume?
Bila ya shaka waliteketezwa, wakawa ni mazingatio kwa watu.
74. Lakini
walikuwapo Waumini ambao aliwakhitari Mwenyezi Mungu wamuabudu Yeye, ili wapate
fadhila za ukarimu wake. Basi hao walizipata thawabu zake, na wakaepukana na
adhabu yake.
75. Na hakika
Nuhu alitwita alipo kwisha kata tamaa na watu wake, basi na Sisi tukawa ni
wabora wa kuitikia wito wake, tulipo muitikia ombi lake, na tukawaangamiza watu
wake kwa tofani.
76. Na
tukamwokoa Nuhu na walio amini pamoja naye, wasizame na kuteketea kwa tofani.
77.
Tukawajaalia vizazi vya Nuhu ndio walio bakia katika ardhi baada ya kuteketea
watu wake.
78. Na
tukamwachilia Nuhu kutajwa kwa wema na watu walio kuja baada yake wakimdhukuru
mpaka Siku ya Kiyama.
79. Maamkio ya
Salama na Amani kumuamkia Nuhu kutokana na Malaika, na watu, na majini.
80. Hakika
Sisi huwalipa walio tenda mema mfano wa haya. Basi aliingia katika Jihadi
kulinyanyua Neno letu, na akavumilia maudhi kwa ajili yetu.
81. Hakika
yeye ni miongoni mwa waja wetu walio tuamini, na wakatimiza ahadi yetu, na
wakaufikisha Ujumbe wetu.
82. Kisha
tukawazamisha wenginewe katika makafiri wa kaumu yake.
83. Na hakika
bila ya shaka Ibrahim alikuwa akifuata ile ile njia yake na mwenendo wake katika
kuitia Tawhidi, Imani
84. Alipo
mkabili Mola wake Mlezi kwa moyo ulio kuwa nadhifu hauna ushirikina, umemsafia
ibada Yeye tu.
85. Alipo
chukia kuwa baba yake na watu wake wanaabudu masanamu, akawaambia: Ni nini haya
masanamu mnayo yaabudu?
86. Si mnazua
uwongo tu ulio wazi kwa haya myatendayo, kwa kuwa mnamuabudu asiye kuwa Mwenyezi
Mungu? Na si mnataka kuzua uzushi huu bila ya udhuru wowote ila kupenda kwenu
tu?
87. Mnamdhania
nini huyo ambaye ndiye Mwenye haki ya kuabudiwa kwa kuwa Yeye ndiye Muumba
walimwengu wote, mtapo kutana naye na hali nyinyi mmemfanyia washirika wenginewe
katika ibada?
88. Basi
akazitupia jicho nyota kuzitazama ili apate kuona dalili ya Muumba ulimwengu.
Akaziona zinageuka, zinabadilika
89.
Akajikhofia nafsi yake asiwe ana upotovu na maradhi ya itikadi.
90. Watu wake
wakamwachilia mbali, na wakapuuza maneno yake.
91. Akayaendea
kwa haraka yale masanamu kwa kificho, na akayapa chakula ambacho wale
washirikina walikiweka mbele yao ili nao wapate baraka yao kwa mujibu wa madai
yao. Akasema kwa maskhara na kejeli: Mbona hamli?
92. Mna nini
hata mmeshindwa kusema lolote, hata ndio au sio?
93.
Akayaingilia yale masanamu kuyapiga kwa mkono wa kulia, kwa kuwa ndio wenye
nguvu, akayabomoa.
94. Walipo
baini kwamba kuvunjwa miungu yao ni kwa kitendo cha Ibrahim, basi walimkimbilia
ili wamtese kwa alivyo watendea miungu yao.
95. Ibrahim
akawaambia kwa kuwahizi: Hivyo nyinyi mnaabudu mawe mliyo yachonga nyinyi
wenyewe kwa mikono yenu? Akili zenu zimekwenda wapi?
96. Na
Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, na akayaumba hata hayo masanamu mnayo
yaunda kwa mikono yenu. Basi Yeye peke yake ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa.
97. Hoja ilipo
wapata wale wanao abudu masanamu, wakaona hawana ila waingie kutumia nguvu;
wakaazimia kumchoma moto. Basi waliambizana: Mjengeeni jengo, na mlijaze moto,
na mtupeni katikati yake!
98. Kwa haya
walikusudia kumteketeza, lakini Mwenyezi Mungu alimwokoa na ule moto baada ya
wao kwisha mtumbukiza humo. Hadhi yake ikawa juu kwa utukufu ule, na Mwenyezi
Mungu akawafanya wao ndio watu wa chini.
99. Ibrahim
alipo kata tamaa nao, kuwa hawaamini tena, alisema: Mimi ninahama kwendea pahala
alipo niamrisha Mola wangu Mlezi nende. Mola wangu Mlezi atanihidi aniongoze
mpaka nifike pahala pa utulivu, penye amani, na nchi nzuri.
100. Ewe Mola
wangu Mlezi! Nipe dhuriya walio wema wa vitendo, wasimamie hii kazi ya wito
kuwaitia watu kwako Wewe, baada yangu.
101. Malaika
wakampa bishara ya kwamba atapata mwana atakaye pambwa kwa akili na upole.
102.
Akazaliwa huyo mwana, na alipo kuwa kijana wa kwenda naye baba yake katika
kutafuta haja za maisha, Ibrahim alipewa mtihani kwa ndoto aliyo iota. Ibrahim
akasema: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini ufunuo kutokana na
Mwenyezi Mungu ananitaka nikuchinje! Basi wewe tazama unaonaje? Yule mwana mwema
alisema: Ewe baba yangu! Tekeleza amri ya Mola wako Mlezi. Utaniona mimi katika
wanao subiri, Inshallah!
103. Yule
baba na mwanawe walipo iridhia hukumu ya Mwenyezi Mungu, na akamweka juu ya
fungu la mchanga na akamlaza juu yake, kipaji chake kikawa juu ya ardhi, akawa
tayari kumchinja.
104,105. Na
Mwenyezi Mungu akajua umadhubuti wa Ibrahim na mwanawe katika majaribio,
Mwenyezi Mungu alimwita Ibrahim kwa wito wa kirafiki: Ewe Ibrahim! Hakika
umeuitikia kwa utulivu huo ufunuo wa ndoto, na wala hukusitasita katika kufuata
amri. Basi haya yanakutosha. Sisi tunakupunguzia haya majaribio yetu kuwa ni
malipo kwa wema wako, kama tunavyo walipa walio wema kwa wema wao.
104,105. Na
Mwenyezi Mungu akajua umadhubuti wa Ibrahim na mwanawe katika majaribio,
Mwenyezi Mungu alimwita Ibrahim kwa wito wa kirafiki: Ewe Ibrahim! Hakika
umeuitikia kwa utulivu huo ufunuo wa ndoto, na wala hukusitasita katika kufuata
amri. Basi haya yanakutosha. Sisi tunakupunguzia haya majaribio yetu kuwa ni
malipo kwa wema wako, kama tunavyo walipa walio wema kwa wema wao.
106. Hakika
majaribio haya tuliyo mjaribia Ibrahim na mwanawe bila ya shaka ni majaribio
yaliyo dhihirisha undani wa Imani yao na yakini yao kwa Mola Mlezi wa
walimwengu.
107. Na
tukamkomboa kwa mhanga wenye cheo kikubwa, kwa kuwa hayo ni kwa amri ya Mwenyezi
Mungu.
108. Na
tukaacha atajike kwa sifa nzuri katika ndimi za walio kuja baada yake.
109. Maamkio
ya amani na salama kwa Ibrahim!
110. Mfano wa
malipo kama haya ya kuwakinga na balaa ndivyo tunavyo walipa walio wema katika
kufuata amri za Mwenyezi Mungu.
111. Hakika
Ibrahim ni katika waja wetu wanao ifuata Haki.
112. Na kwa
amri yetu, Malaika walimbashiria kuwa ataruzukiwa mwana, Is-haqa juu ya kukata
tamaa na kuwa mkewe ni tasa. Na kwamba yeye hakika atakuwa Nabii miongoni mwa
walio wema.
113. Nasi
tukamtunukia yeye na mwanawe baraka na kheri duniani na Akhera. Na miongoni mwa
vizazi vyao watatokea watakao jifanyia wema nafsi zao kwa Imani na ut'iifu, na
watakao jidhulumu kwa upotovu wa ukafiri na maasi.
114. Na bila
ya shaka tuliwaneemesha Musa na Haruni kwa kuwapa Unabii na neema kubwa kubwa.
115. Na
tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa iliyo kuwa iwashukie kutokana
na Firauni na kaumu yake.
116. Na Sisi
tukawanusuru na adui zao, wakawa wao ndio wenye kushinda.
117. Na
tukampa Musa na Haruni Kitabu kilicho wazi chenye kubainisha hukumu za Dini,
nacho ni Taurati.
118. Na
tukawaongoza waifuate Njia iliyo sawa.
119. Na
tukabakisha sifa njema za kutajika wote wawili hao kwa watu wengineo walio kuja
baada yao.
120. Maamkio
ya Amani na Salama kwa Musa na Haruni.
121. Hakika
mfano wa malipo tuliyo mjazi Musa na Haruni ndivyo tunavyo wajazi wote walio
wema.
122. Hakika
wawili hao ni katika waja wetu wenye kuifuata Haki.
123. Na
hakika Ilyas ni katika hao tulio watuma kwenda waongoa watu wao.
124. Ilyas
alipo waambia watu wake, nao walikuwa wakiyaabudu masanamu yao: Je! Mnaendelea
juu ya makosa yenu, na wala hamumkhofu Mwenyezi Mungu mkajikinga na adhabu yake?
125.
Mnaliabudu sanamu linalo itwa Baa'li, na mkaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu aliye
uumba ulimwengu na akaufanya mzuri uumbaji wake?
126. Mwenyezi
Mungu amekuumbeni na amekuhifadhini nyinyi na baba zenu wa zamani. Yeye basi
ndiye Mwenye haki ya kuabudiwa.
127. Lakini
walimkadhibisha, basi jaza yao ni kuhudhurishwa kwenye Moto Siku ya Kiyama.
128. Isipo
kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safisha Imani yao. Hao basi ndio wenye kufuzu.
129. Na
tukamjaalia awe anatajwa kwa wema na ndimi za walio kuja baada yake.
130. Salamu
juu ya Ilyasi, au juu yake yeye na watu wake, kwa kuwa kawashinda.
131. Hakika
mfano wa malipo tuliyo mlipa Ilyas tunamlipa kila aliye mwema kwa sababu ya wema
wake.
132. Hakika
Ilyas ni katika waja wetu walio amini.
133. Na
hakika Lut'i ni katika Mitume tulio watuma ili afikishe Ujumbe wetu kwa watu.
134. Kwa
hakika Sisi tumemwokoa yeye na ahali zake wote kutokana na adhabu iliyo wasibu
watu wake.
135. Ila
mkewe mkongwe. Yeye bila ya shaka aliteketea pamoja na walio teketea.
136. Kisha
tukawaangamiza wote isipo kuwa Lut'i na walio muamini.
137,138. Na
hakika nyinyi, watu wa Makka, mnayapitia majumba ya hao kaumu Lut'i katika
safari zenu za kwendea Sham asubuhi au usiku. Je! Mmepotelewa na akili zenu hata
hamwezi kuzingatia yaliyo wapitia hao kuwa ni malipo ya ukanushaji wao?
137,138. Na
hakika nyinyi, watu wa Makka, mnayapitia majumba ya hao kaumu Lut'i katika
safari zenu za kwendea Sham asubuhi au usiku. Je! Mmepotelewa na akili zenu hata
hamwezi kuzingatia yaliyo wapitia hao kuwa ni malipo ya ukanushaji wao?
139. Na
hakika Yunus ni miongoni mwa tulio watuma wawafikishie Ujumbe wetu watu.
140,141.
Alipo wahama watu wake bila ya amri ya Mola wake Mlezi, akaliendea jahazi ambalo
lilio kwisha sheheni pomoni, akalipanda. Jahazi likapatikana na mambo
ikawajibikia lazima mmoja katika abiria atoswe kupunguza shehena yake. Kura
ikamuangukia Yunus, akashindwa kwa kura. Akatoswa baharini kwa mujibu wa ada yao
zama zile.
140,141.
Alipo wahama watu wake bila ya amri ya Mola wake Mlezi, akaliendea jahazi ambalo
lilio kwisha sheheni pomoni, akalipanda. Jahazi likapatikana na mambo
ikawajibikia lazima mmoja katika abiria atoswe kupunguza shehena yake. Kura
ikamuangukia Yunus, akashindwa kwa kura. Akatoswa baharini kwa mujibu wa ada yao
zama zile.
142. Samaki
akammeza, naye hakika alistahiki lawama kwa kuikimbia kazi yake ya Daa'wa, Wito,
kuwaitia watu wafuate Haki, na kuacha kuwasubiria wale walio kwenda kinyume
naye..
143,144. Na
lau kuwa Yunus hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, wanao dumu
kumdhukuru, angeli kufa ndani ya samaki, wala asingeli toka humo mpaka siku ya
kufufuliwa.
143,144. Na
lau kuwa Yunus hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, wanao dumu
kumdhukuru, angeli kufa ndani ya samaki, wala asingeli toka humo mpaka siku ya
kufufuliwa.
145.
Tukamtupa pahali patupu kwenye nchi pasipo kuwa na miti wala majumba, naye ni
mgonjwa kwa yaliyo mpata. Yaliyo mtokea Sayyidna Yunus a.s. ni muujiza. Lakini
nayo si muhali kutokea mtu kumezwa na samaki, na akabakia yuhai ndani yake kwa
muda fulani. Mawili yaweza kuwa - Kwanza, ni kuwa huyo samaki ni namna asiye
kuwa na meno katika kabila ya nyangumi wakubwa kabisa, kama nyangumi wanao
onekana sana katika Bahari ya Kati (Mediterranean). Urefu wake huweza kufika
Mita 20. Alibaki Yunus katika mpandikizi wa kinywa chake huyo nyangumi mpaka
alipo mtema kwenye ufukwe mtupu, kwani koo ya nyangumi ni nyembamba hawezi
kupita mtu. Pili, yaweza kuwa huyo samaki ni namna ya wenye meno pia, kama
nyangumi wa ambari, na ambaye pia urefu wake hufika mita 20. Hawa mara kadhaa wa
kadhaa huonekana katika Bahari ya Kati. Nyangumi hao yawezekana kwa kawaida
kuwameza wanyama wakubwa wanao pita urefu wa mita tatu.
146.
Tukauotesha mmea wa kutambaa, usio simama juu ya kigogo, ukamfunika na kumkinga
na madhara ya hali ya hewa.
147. Hata
alipo pata nafuu kutokana na yaliyo msibu, tukamtuma awaendee watu wengi.
Wanasema walio waona kuwa wanapata laki moja au zaidi.
148.
Wakauwitikia wito wake, nasi tukawakunjulia neema zetu kwa muda maalumu.
149. Ewe
Nabii! Waulize watu wako: Ati Mwenyezi Mungu aliye kuumba ana watoto wa kike
kinyume na wao; na wao ndio wana watoto wanaume kinyuma na Yeye?
150. Ati
tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao hao makafiri waliona kwa macho yao
kuumba kwao, na ndio wakasimulia walio yaona?
151,152. Ewe
mwenye kusikia! Yazingatie maneno yao. Hakika wao kwa uwongo wao wanasema:
Mwenyezi Mungu amezaa! Na hali Yeye ametakasika na upungufu kama huo wa kuwa
mzazi au kuzaliwa. Na hakika bila ya shaka hao ni waongo kwa usemi huo, kwa
ushahidi wa dalili nyingi za Upweke wake.
151,152. Ewe
mwenye kusikia! Yazingatie maneno yao. Hakika wao kwa uwongo wao wanasema:
Mwenyezi Mungu amezaa! Na hali Yeye ametakasika na upungufu kama huo wa kuwa
mzazi au kuzaliwa. Na hakika bila ya shaka hao ni waongo kwa usemi huo, kwa
ushahidi wa dalili nyingi za Upweke wake.
153. Ati Yeye
amejichagulia mwenyewe mabinti ambao kwa madai yenu ndio mnawachukia kuliko
watoto wa kiume ambao mnawapenda, na hali Yeye ndiye Mwenye kuwaumba wote,
watoto wa kike na wa kiume?
154. Ni nini
lilio kusibuni hata mkakata hukumu bila ya ushahidi? Vipi mnahukumu hivyo na
hali ni upotovu ulio wazi?
155. Je!
Mmesahau dalili za uweza wake na kutakasika kwake, ndio msikumbuke mpaka
mkaingia katika upotovu?
156. Hebu
nyinyi mnazo nguvu za ushahidi wa kubainisha wa kuthibitisha hayo mnayo yadai?
157. Basi
leteni hoja zenu, ikiwa mnazo hoja za katika Kitabu cha mbinguni, kama nyinyi ni
wakweli katika hayo myasemayo na mnayo yahukumia.
158.
Wakashikilia katika itikadi zao, na wakazua baina ya Mwenyezi Mungu na majini,
ambao hawawaoni, kuwa ati yapo makhusiano ya nasaba. Na bila ya shaka hao majini
walikwisha jua kuwa makafiri watahudhurishwa mbele ya Mwenyezi Mungu ili wapate
malipo yao yasiyo kimbilika.
159. Mwenyezi
Mungu Mtukufu ametakasika na hizo sifa za kuemewa na za upungufu wanazo mzulia
kuwa anazo.
160. Lakini
waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa wakasafishwa hawana makosa ya huo uzushi
wa makafiri.
161,162,163.
Enyi makafiri! Hakika nyinyi, na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu -
Nyinyi kwa kuwaabudu kwenu badala yake Yeye, hamtampoteza yeyote kwa upotovu
wenu. Isipo kuwa yule ambaye tangu hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anamjua ni katika
watu wa Motoni, na huko ataingia.
161,162,163.
Enyi makafiri! Hakika nyinyi, na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu -
Nyinyi kwa kuwaabudu kwenu badala yake Yeye, hamtampoteza yeyote kwa upotovu
wenu. Isipo kuwa yule ambaye tangu hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anamjua ni katika
watu wa Motoni, na huko ataingia.
161,162,163.
Enyi makafiri! Hakika nyinyi, na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu -
Nyinyi kwa kuwaabudu kwenu badala yake Yeye, hamtampoteza yeyote kwa upotovu
wenu. Isipo kuwa yule ambaye tangu hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anamjua ni katika
watu wa Motoni, na huko ataingia.
164. Na
Malaika kuwania kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu, wakasema: Hapana yeyote
katika sisi ila ana cheo chake maalumu katika ujuzi, na ibada, na wala hakikiuki
hicho.
165. Na sisi
tumejipanga safu wenyewe katika misimamo ya kutumika daima.
166. Na
hakika sisi bila ya shaka yoyote ndio wenye kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila
lisilo kuwa na maelekeo naye katika kila hali.
167,168,169.
Na walikuwapo makafiri wa Makka kabla ya kuteuliwa Mtume s.a.w. ambao wakisema:
Lau kuwa sisi tungeli kuwa na Kitabu kama Vitabu vya watu wa zamani, yaani kama
Taurati na Injili, nasi bila ya shaka tungeli kuwa waja wa Mwenyezi Mungu wenye
kumsafia ibada Yeye.
167,168,169.
Na walikuwapo makafiri wa Makka kabla ya kuteuliwa Mtume s.a.w. ambao wakisema:
Lau kuwa sisi tungeli kuwa na Kitabu kama Vitabu vya watu wa zamani, yaani kama
Taurati na Injili, nasi bila ya shaka tungeli kuwa waja wa Mwenyezi Mungu wenye
kumsafia ibada Yeye.
167,168,169.
Na walikuwapo makafiri wa Makka kabla ya kuteuliwa Mtume s.a.w. ambao wakisema:
Lau kuwa sisi tungeli kuwa na Kitabu kama Vitabu vya watu wa zamani, yaani kama
Taurati na Injili, nasi bila ya shaka tungeli kuwa waja wa Mwenyezi Mungu wenye
kumsafia ibada Yeye.
170. Na
Kitabu kikawajia, nao wakakikataa. Basi watakuja jua nini matokeo ya kukataa
kwao.
171,172.
Ninaapa! Hukumu yetu kwa Mitume tulio watuma imekwisha tolewa mbele, ya kwamba
ushindi na matokeo mema ni yao wao dhidi ya makafiri.
171,172.
Ninaapa! Hukumu yetu kwa Mitume tulio watuma imekwisha tolewa mbele, ya kwamba
ushindi na matokeo mema ni yao wao dhidi ya makafiri.
173. Na
kwamba wafuasi wetu na wasaidizi wetu ndio peke yao watakao washinda walio
kengeuka.
174. Basi
waachilie mbali, nawe ngoja mpaka wakati ujao. Kwani Sisi tutakupa wewe matokeo
mema, na manusura, na ushindi.
175. Nawe
watazame, na uangalie vyema adhabu gani na mateso yatakayo wapata kwa kwenda
kinyume nawe na kukukadhibisha. Basi watakuja ona kwa macho yao zitakavyo
shindwa safu zao, na wataona nusura ya Mwenyezi Mungu inavyo wafikia Waumini.
176. Je!
Wamepoteza akili zao nini, hata wakawa wanaihimiza adhabu yetu?
177. Basi
adhabu hiyo itakapo teremka kwenye uwanja wao mpana, itakuwa asubuhi ovu kweli
hiyo kwa hao walio onywa na adhabu.
178. Na
waachilie mbali mpaka mambo yatakapo waishia.
179. Na
yaangalie yatakayo wafika wao na yatakayo kufika wewe. Wao watakuja yaona hayo
wanayo yahimiza.
180. Mwenyezi
Mungu, aliye kuumba wewe na aliye ziumba nguvu na ushindi, ametakasika na huo
uzushi wanao muambatisha naye.
181. Na
salamu zishuke juu ya Mitume wapenzi walio safika.
182. Na sifa
njema ni za Mwenyezi Mungu peke yake, Muumba wa viumbe vyote, na Mwenye
kuwaangalia makhaluku wote.
Rudi kwenye
sura
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani