2. Ninaapa kwa
Qur'ani yenye kukusanya hikima na ilimu yenye manufaa.
3. Hakika wewe,
Muhammad, ni katika wale ambao Mwenyezi Mungu amewatuma kwa watu wawapelekee
Uwongofu na Dini ya Haki.
4. Juu ya Njia
Iliyo Sawa, nayo ndiyo Dini ya Kiislamu.
5. Ni mteremsho
wa Mwenye nguvu Mwenye kushinda kila kitu, ambaye hapana mtu awezae kumzuia
chochote akitakacho. Mwenye kuwarehemu waja wake, kwa kuwatumia watu wa
kuwaongoza njia ya kuokoka.
6. Ili uwaonye
watu ambao baba zao wa karibu hawakupata kuonywa, na kwa hivyo wamesahau yanayo
wajibikia kwa Mwenyezi Mungu, na kwa nafsi zao, na kwa watu.
7. Sisi
tulikwisha jua kuwa wengi wao hawatakhiari Imani. Basi yale tuliyo kuwa
tunayajua yamewafikiana na yaliyo kwao. Basi haitakuwapo Imani kutoka kwao.
8. Sisi
tumewafanya hao wanao kakamia juu ya ukafiri ni kama walio tiwa minyororo
shingoni mwao, ikawafika videvuni mwao. Na mikono yao ikawa imefungwa kwenye
vichwa vyao, vikawa vimenyanyuka juu na macho yao yameinama. Basi hawawezi
kuvizungusha vichwa vyao wapate kuona.
9. Na
tumewafanya wale walio zuwiwa wasione Ishara na dalili ni kama walio fungwa
baina ya kuta mbili, na macho yao yakagubikwa, wasione yaliyo mbele yao wala
yaliyo nyuma yao.
10. Na ni sawa
kwao ukiwahadharisha au ukito wahadharisha, hawaamini hao.
11. Hakika
wanao nafiika kwa kuhadharisha kwako ni wale wanao ifuata Qur'ani na wakamkhofu
Arrahman, ijapo kuwa hawamwoni. Basi watu hawa wape bishara njema kuwa Mwenyezi
Mungu atawasamehe madhambi yao, na atawalipa malipo mema kwa vitendo vyao.
12. Hakika
Sisi tunawahuisha maiti, na tunayaandika yote waliyo yatenda na wakayakadimisha
duniani, na walio yabakisha humo kuwa ni athari, mabaki, yao baada ya kufa kwao.
Na kila kitu kimo katika Kitabu kilicho wazi.
13. Ewe Nabii!
Watajie watu wako kisa cha mji mmoja.(1) Kwani hicho ni kama kisa chao.
Waliwaendea Wajumbe walio tumwa ili wawahidi. (1) Baadhi wa wafasiri wanasema
mji huo ni Antiokia.
14. Tuliwatuma
wajumbe wawili, wakawakadhibisha. Tukawaongeza nguvu kwa kumpeleka mwengine wa
tatu. Basi hawa watatu wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu!
15. Wale watu
wa mji wakasema kuwajibu: Nyinyi si chochote ila ni wanaadamu kama sisi. Na
Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema hakuteremsha wahyi wowote kwa mwanaadamu. Nyinyi
ni watu mnao sema yasiyo kuwapo.
16. Wale
Wajumbe wakasema: Mola wetu Mlezi aliye tutuma anajua kuwa hakika sisi bila ya
shaka tumetumwa kwenu.
17. Na sisi
hatuna waajibu wowote ila kufikilisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu ufike kwa uwazi.
18. Wana mji
wale wakasema: Sisi tunaona kuwa nyinyi mnatuletea ukorofi. Na tunaapa, lau kuwa
hamsiti na huo wito wenu hapana shaka tutakupopoeni kwa mawe, na hapana shaka
mtapata kwetu adhabu kali yenye kutia uchungu.
19. Wale
Wajumbe wakasema: Ukorofi mnao nyinyi wenyewe, kwa hizo kufuru zenu. Badala ya
kuwaidhika kwa mambo yenye kheri kwenu wenyewe, mnatutuhumu sisi kuwa ni
wakorofi, na mnatutishia kutupa adhabu chungu? Lakini nyinyi ni watu mlio
pindukia mipaka ya Haki na Uadilifu.
20. Akaja mtu
kutoka huko mwisho wa mji akiwakimbilia wale wanamji, akawaambia: Wafuateni hawa
walio tumwa kwenu na Mwenyezi Mungu.
21. Wafuateni
watu wasio taka kwenu ujira wowote kwa kukunasihini na kukuongozeni, na hali wao
wenyewe wameongoka, na nyinyi mtapata manufaa kwa kufuata njia ya kheri na
mafanikio!
22. Na kitu
gani cha kunizuia hata nisimuabudu yule aliye niumba, na ambaye kwake Yeye, si
kwa mwenginewe, ndio mtarejea?
23. Je!
Niishike kwa kuiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, miungu mingine isiyo nifaa kitu
kuniombea kwao, pindi Mwenyezi Mungu akinitakia madhara? Wala hawataniokoa nayo
yakinishukia hayo madhara.
24. Basi
hakika mimi nikiiabudu miungu mingine badala yake Yeye, nitakuwa katika upotovu
ulio dhaahiri.
25. Hakika
mimi ninamsadiki Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni, na ndiye Mwenye kutawala mambo
yenu. Basi nisikilezeni na mnit'ii.
26,27. Kuwa ni
malipo ya Imani yake na wito wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ataambiwa: Ingia
Peponi! Naye, hali yuko katika kivuli cha neema na hishima, atasema: Laiti kuwa
watu wangu wangeli jua alivyo nighufiria Mola wangu Mlezi na kunipa hishima, nao
wakaamini kama nilivyo amini mimi.
26,27. Kuwa ni
malipo ya Imani yake na wito wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ataambiwa: Ingia
Peponi! Naye, hali yuko katika kivuli cha neema na hishima, atasema: Laiti kuwa
watu wangu wangeli jua alivyo nighufiria Mola wangu Mlezi na kunipa hishima, nao
wakaamini kama nilivyo amini mimi.
28. Na Sisi
hatukawaangamiza kwa kuwapelekea maaskari kutoka mbinguni. Wala huo sio mtindo
wetu kupeleka majeshi tunapo yahiliki mataifa.
29.
Kuteketezwa kwao hakukuwa ila ni kwa ukelele mmoja tu tulio wapelekea. Na mara
wao wakawa ni maiti, kama moto ulio zimwa.
30. Ee khasara
yao, inayo faa kusikitikiwa! Hatuwapelekei waja wangu Mtume ila wao huwa
wakimfanyia maskhara.
31. Kwani wao
hawayazingatii mataifa mengi yaliyo tangulia tuliyo yahiliki? Hakika hao
hawarejei tena kwenye maisha yao ya duniani.
32. Hapana
katika mataifa yaliyo tangulia na yajayo ila wote watakusanywa mbele yetu, nao
wamelazimishwa kuhudhuria mbele yetu.
33. Na dalili
kwao ya uweza wetu wa kufufua ni kuangalia vipi ardhi yenye ukame tunavyo
ihuisha kwa maji, na kutoa ndani yake nafaka wanazo zila.
34,35. Na humo
tukafanya vitalu na mabustani ya mitende na mizabibu, na tukapasua humo chemchem
ya kumwagia maji kwenye miti yake, na ikatoa matunda, na wao wakala katika hayo.
Na hayo si kazi ya mikono yao. Basi kwa nini hawatoi haki ya Mwenyezi Mungu
iliyo juu yao kwa kumuamini na kumshukuru?
34,35. Na humo
tukafanya vitalu na mabustani ya mitende na mizabibu, na tukapasua humo chemchem
ya kumwagia maji kwenye miti yake, na ikatoa matunda, na wao wakala katika hayo.
Na hayo si kazi ya mikono yao. Basi kwa nini hawatoi haki ya Mwenyezi Mungu
iliyo juu yao kwa kumuamini na kumshukuru?
36. Wa
kutakasika ni Mwenyezi Mungu aliye umba kila kitu kwa mpango wa ume na uke,
katika mimea na katika nafsi zao watu, na katika vitu ambavyo watu hawavijui.
Hii harufi Min , yaani "Katika" katika Aya hii ni ya kubainisha. Maana yake
Mwenyezi Mungu Mtukufu ameumba madume na majike katika viumbe vyake vyote, sawa
sawa katika mimea, na wanyama, na wanaadamu na vyenginevyo ambavyo watu
hawavijui na hawavioni.
37. Na Ishara
pia ya kuwepo Mwenyezi Mungu na uweza wake, ni huu usiku ambao tunautoa ndani
yake mchana, kama kuivua nguo inayo sitiri. Mara utaona watu wamo gizani lilio
wazunguka kila upande.
38. Na jua
linakwenda katika njia yake maalumu. Mwenyezi Mungu amekwisha kadiria kwa zama
na mahala. Huo ndio mpango wake Mwenye kushinda kwa uweza wake, Mwenye
kuvizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.
39. Na mwezi
kwa mpango wetu tumeujaalia una vituo vyake. Mwanzo wa mwezi unakuwa mdogo na
mwembamba. Kisha kila usiku unazidi kukua mpaka unatimia kuwa mbaamwezi. Tena
unaingia kupungua vile vile, mpaka ukawa kama karara la mtende linapo kuwa
kongwe limepindana na limekuwa manjano.
40. Haipelekei
jua likaacha sharia zake likakutana na mwezi, na likaingia katika njia zake.
Wala usiku hauwi kuushinda mchana ukauzuia usije, bali vyote viwili hivyo
hupeana zamu. Na vyote, jua na mwezi, na vyenginevyo vyote vinaogelea katika
njia zao za mbinguni, wala haviachi njia. Hakika Aya hizi tukufu zinabainisha
ukweli wa ki-ilimu ambao wataalamu walikuwa hawaujui ila mwanzo wa karne ya kumi
na nne ya kuzaliwa Nabii Isa. Na jua ni moja katika nyota za mbinguni, nalo kama
nyota zilizo baki lina mwendo wake wenyewe. Lakini linakhitalifiana na nyota
nyengine kwa kuwa lipo karibu na dunia, na kwa kuwa lina kundi la sayari na
miezi ya mikia na sayari ndogo ndogo zinazo lifuata daima, na zinat'ii mvuto
wake. Kwa hivyo zinakuwa hizo zinazunguka kwa kufuatana kwa utungo kama sura ya
yai. Na mkusanyo wote huu unakwenda angani pamoja na jua kwa mvuto wake. Kwa
ufupi jua, na ardhi, na mwezi na sayari zote na vyombo vyote hivyo vinakwenda
angani kwa mbio maalumu, na kuelekea jiha maalumu. Na yaonekana kuwa jua na
mkusanyo wote huo wake, na nyota zilizo karibu nalo zipo katika mkusanyo ulio
tanda katika mbingu inayo itwa kwa Kiarabu Sadiimu almajarrah, au kwa Kiingereza
Nebula course. Na imebainika kwa masomo ya kisasa sehemu zote za hiyo Nebula
zinaizunguka kati yake kwa mbio ya kunasibiana na kinyume cha umbali wake kutoka
hapo kati. Pia imeonakana kuwa jua na ardhi na sayari zake na nyota zilio karibu
nayo, vyote hivyo vinakwenda mbio, na upande maalumu. Mbio zake zinafika
kilomita 700 kila nukta moja. Na kunatimia kuzunguka kwake kukizunguka hicho
kituo cha kati kwa kiasi ya miaka milioni 200 ya muangaza. Na kiini cha maneno
ni kuwa Aya tukufu iliyo taja kuwa jua linakwenda kwa kiwango chake, hawakujua
wataalamu uzuri wake wa ndani mpaka katika mwanzo wa karne hii. Wala hayamkini
jua kuupata mwezi, kwani kila kimojapo kinakwenda katika njia zake mbali mbali,
basi ni muhali kukutana, kama ilivyo kuwa ni muhali kupitana usiku na mchana.
Hayo ingeli takikana ardhi izunguke juu ya msumari-kati wake kutoka mashariki
kwendea magharibi, kinyume na ilivyo hivi sasa kutoka magharibi kwendea
mashariki. Na mwezi katika kuizunguka kwake ardhi, na ardhi kulizunguka jua,
huenda pamoja na mkusanyo wa nyota unao itwa Manaazil Alqamar au Lunar system.
Na katika robo ya mwanzo na ya mwisho wa mwezi huonekana sura yake kama karara
kongwe au kole lilio kauka, linapo kuwa kongwe na kunyauka.
41. Na Ishara
nyengine kwao ni kuwa Sisi tuliwapakia wanaadamu katika jahazi ilio jaa bidhaa
zao na riziki zao.
42. Na
tukawaumbia mfano wa hiyo marikebu na vyenginevyo wanavyo vipanda kadhaalika.
43. Na
tukitaka kuwazamisha, tunawazamisha. Na wala hawapati wa kuwaopoa, wala hawapati
wa kuwaokoa wasiangamie.
44. Lakini
Sisi hatuwazamishi, kwa sababu ya rehema inayo tokana nasi, na ili
tuwastareheshe kwa muda ulio kwisha kadiriwa.
45. Na wanapo
ambiwa: Yaogopeni mfano wa yaliyo wapata mataifa yaliyo kwisha pita kwa
kukadhibisha kwao, na iogopeni adhabu ya Akhera ambayo itakupateni kwa
kushikilia kwenu ukafiri, kwa kutaraji kuwa asaa Mola wenu Mlezi akakurehemuni
mkimcha Yeye, wao hupuuza.
46. Na
haiwajii hoja katika hoja za Mola wao Mlezi, yenye kuonyesha Upweke wa Mwenyezi
Mungu na uweza wake, ila wao huipa nyongo, hawaijali.
47. Na
wakiambiwa: Wapeni mafakiri kutokana na hicho alicho kuruzukuni Mwenyezi Mungu,
makafiri huwaambia Waumini: Je! Tuwalishe watu ambao Mwenyezi Mungu Mwenyewe
angeli taka angeli walisha? Hivyo inakuwa tunamfanyia inda Mwenyezi Mungu kwenda
kinyume na mapenzi yake! Nyinyi mnao taka tutoe, si chochote ila mmo katika
upofu ulio wazi, hamuioni Haki.
48. Na
huwaambia Waumini kwa kuwafanyia kejeli: Lini yatatokea hayo mlio tuahidi, kama
nyinyi mnasema kweli katika mnayo ahidi?
49. Hawangojei
ila sauti moja tu, iwamalize kwa ghafla, nao wakizozana katika mambo ya kidunia,
wameghafilika na Akhera.
50. Kwa upesi
wa hayo yatakayo wateremkia, hawatowahi kuusia chochote, wala kurejea kwa ahali
zao.
51. Na
barugumu litapulizwa kwa mpulizo wa kufufua watu. Mara watu watatoka makaburini
mwao wakikimbilia kwenda kukutana na Mwenyezi Mungu. Na hilo barugumu, na
kupulizwa kwake, ni katika anayo yajua Mwenyezi Mungu Yeye peke yake.
52. Watasema
watakao fufuliwa kutoka makaburini: Balaa gani lilio tushukia! Nani aliye
tuamsha tukauwacha usingizi wetu? Jawabu ya suala lao itawajia: Hii ndiyo siku
ya kufufuliwa aliyo waahidia Arrahaman, Mwingi wa Rehema, waja wake, na Mitume
wakaisemea kweli kwa waliyo yasimulia.
53. Wito wao
wa kuwatoa hautakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watakusanywa mbele yetu
wahudhurishwe ili tuwahisabie.
54. Basi
katika hii siku ya leo haipungukiwi nafsi na chochote katika ujira wake kwa kazi
iliyo tenda. Na wala hamtopata isipo kuwa jaza ya mliyo kuwa mkiyatenda, ikiwa
ni kheri au shari.
55. Hakika
watu wa Peponi hii leo watakuwa wameshughulika kwa neema walizo nazo,
wakistaajabia na kufurahia.
56. Wao na
wake zao wamo katika vivuli vilivyo enea, wameegemea juu ya viti vilivyo pambwa.
56. Wao na
wake zao wamo katika vivuli vilivyo enea, wameegemea juu ya viti vilivyo pambwa.
58.
Wataambiwa: "Salama", kuwa ni kauli iliyo toka kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.
59. Na
wataambiwa wakosefu siku hii ya leo: Jitengeni mbali na Waumini.
60. Enyi
wanaadamu! Sikukuusieni kuwa msimfuate Shetani kwa ut'iifu kama kwamba ni mungu
wa kuabudiwa. Hakika yeye ni adui yenu, aliye dhihirisha uadui wake.
61. Na nyinyi
mniabudu Mimi peke yangu, kwani kuniabudu Mimi tu ndiyo Njia kuu katika
kusimamisha Dini sawa.
62. Na Shetani
amewapotoa viumbe wengi kati yenu. Nyinyi mmeghafilika na hayo. Basi hamkuwa
mkifikiri mlipo mt'ii yeye?
63.
Wataambiwa: Hii ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa mlipo kuwa duniani. Ndiyo
jaza ya ukafiri wenu.
64. Ingieni!
Na hilikini kwa joto lake hii leo kwa ukafiri wenu!
65. Leo
vitazibwa vinywa vyao, basi havito tamka kitu. Mikono yao ndiyo itakayo sema
nasi, na miguu yao itatamka kwa kutoa ushahidi juu yao kwa waliyo kuwa
wakiyafanya.
66. Na tungeli
taka kuwatia upofu duniani tungeli watia upofu, wakawa wanaipapasa njia ya
kupita wasiweze kuiona. Wataionaje nasi tumewapofoa!
67. Na lau
tungeli taka kuzigeuza sura zao tungeli zigeuza zikawa mbaya, juu ya kuwa wana
nguvu na vyeo. Hata wasinge weza kwenda mbele wala kurudi nyuma, kwa kuwa inge
kuwa tumevunja nguvu zao.
68. Na tunaye
mfanyia umri wake ukawa mrefu, tunamrudisha, kutoka nguvu akawa dhaifu. Basi je
hawayazingatii haya wakayatia akilini ya uweza wetu kuyafanya haya, na wao
wakajua kuwa dunia ni nyumba ya kupita ina mwisho wake, na kuwa Akhera ndiyo
nyumba ya kubaki na kudumu? Na tunaye mfanyia umri wake uwe mrefu tunamrejesha
awe kinyume na alivyo kuwa. Yaani baada ya kuwa na nguvu anakuwa dhaifu. Hayo ni
kwa kuwa maisha ya mwanaadamu yanapitia vipindi vitatu, kukua, kutimia kukua; na
ukongwe unaanza kwa kunywea kwa mafigo, ini, Ghudda Ddarqiya au Thyroid gland,
na Pancreas, yaani Dongoronya. Na haya huleta athari katika kudhoofika mwili
wote. Mishipa ya damu nayo huanza kukacha na kunywea, na kwa hivyo hupunguka
damu inayo kwenda katika viungo vyote vya mwili, basi ndio huzidi udhaifu juu ya
udhaifu. Na katika sababu za kukonga ni kuzidi nguvu za kubomoka kuliko
kujengeka katika mwili, yaani Metabolism. Na hayo ni kwa kuwa Khalaya au Cells,
za mwili zote zimo katika hali ya kugeuka, na pia Khalaya za damu, isipo kuwa
Khalaya za ubongo wa kichwani na wa katika mifupa. Hizo hazigeuki muda wote wa
uhai. Ikiwa kiasi ya kuundika upya ni sawa ya kiasi cha kuharibika, basi hapana
madhara yanayo tokea. Lakini ikiwa kuharibika ni kukubwa kuliko kujengeka katika
kiungo chochote basi hapo hudhihiri madhara kwenye kiungo hicho. Na kwa hivyo
kila umri ukiwa mkubwa kiasi cha kujengeka kinapungua na kinazidi kiasi cha
kubomoka kwa Khalaya, na kunadhihiri kunywea, na kupungua nguvu kote. Na
hukhitalifiana kiasi cha kujengeka kwa mnasaba wa kubomoka kwa kukhitalifiana
namna ya mfumo (Nasiij, Texture). Katika hayo yanayo dhihiri kama ngozi iliyo
funika mwili, na zilio funika paipu za kusaga chakula, na paipu za Ghudad,
Glands, zinachakaa kwa upesi zaidi kila miaka ya binaadamu ikipita. Na hii ni
sababu ya kuonekana upesi alama za kuzeeka.
69. Na Sisi
hatukumfunza Mtume kutunga mashairi. Wala haifai hivyo, kwa kuzingatia pahala
pake na cheo chake awe mtungaji mashairi! Hii Qur'ani iliyo teremka juu yake si
chochote ila ni mawaidha, na Kitabu cha mbinguni kilio wazi. Hakikhusiani kabisa
na mashairi.
70. Hii
Qur'ani ni kumtia khofu mwenye moyo ulio hai ulio nawirika kwa akili. Na ipite
hukumu ya adhabu kuwashukia wanao ipinga Qur'ani, wenye kukataa uwongofu wake.
71. Je!
Makafiri wameingiwa na upofu hata hawaoni kwamba Sisi tumewaumbia kutokana na
iliyo fanya kudra yetu nyama hoa, wanyama wa mifugo, (1) na wao wamekuwa
wanawamiliki, wanawatumilia kama wapendavyo? (1) Ngamia, kondoo, mbuzi na
ng'ombe.
72. Na hao
wanyama tumewafanya wawatumikie. Wengine basi wanawapanda, na wengine wanawala.
73. Na
wanapata kwa hao vitu vya kuwapa manufaa, kama sufi, na manyoya, na nywele, na
ngozi, na mafupa, na vinywaji kutokana na maziwa yao. Je! Wanasahau neema hizi
hata wamekuwa hawamshukuru aliye waneemesha?
74. Na
washirikina wamefanya miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu wakiwaabudu kwa
kutaraji kuwa ati watawasaidia.
75. Hiyo
miungu ya uwongo haiwezi kuwasaidia kwa lolote Mwenyezi Mungu akiwatakia
madhara. Kwani miungu hiyo haiwezi kunafiisha wala kudhuru. Bali wao kwa hiyo
miungu isiyo weza kitu, ni kama askari walio tayarishwa kwa ajili ya
kuwakhudumia na wa kuwalinda na madhara.
76. Basi
yasikuhuzunishe maneno yao kumkhusu Mwenyezi Mungu kwa kumkufuru, na kukukhusu
wewe kwa kukwambia mwongo. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaficha na wanayo
yatangaza. Nasi tutawalipa kwa hayo.
77. Je!
Binaadamu anakataa kuwepo Mwenyezi Mungu na uweza wake, na haoni yeye kwamba
Sisi, baada ya kuwa hata hayupo, tulimuumba kutokana na tone la manii dhalili?
Na sasa amekuwa mkali wa kutukhasimu kwa uwazi kabisa?
78. Tena huyu
mpingaji aliye dhaahiri ametupigia mfano ambao kwao anakanya uweza wetu kufufua
mafupa baada ya kuoza na kusagika. Na amesahau kuwa Sisi tulimuumba yeye, naye
hata hakuwepo aslani. Akasema kwa kukanya na kuona haliwezi kuwa hilo: Ni nani
huyo atakaye yafufua mafupa nayo yamekwisha mung'unyika?
79. Ewe
Muhammad! Sema: Atayafufua yule yule aliye yaumba hapo mara ya kwanza. Kwani
aliye anza anao uweza wa kufanya tena. Naye ni Mkubwa wa kujua kila alicho
kiumba. Basi haemewi Yeye na kukusanya vipande vipande baada ya kutawanyika.
80. Aliye
kuumbieni moto kutoka mti mbichi, baada ya kwisha kauka. Nguvu za jua zinaingia
ndani ya mimea kwa wasita wa mwangaza. Khalaya zenye madda ya kijani katika
mimea Chlorophyl ndizo zinafyonza Carbon dioxide kutokana na hewa, na hii
huchanganyika na maji yanayo fonzwa na mimea, na kufanyika Carbohydrates kwa
kuathiriwa na nguvu zinazo tokana na mwangaza wa jua. Tena hufanyika mbao, kuni,
ambazo sehemu kubwa ni muundo wa kimyaa wa Carbon na Hydrogen na Oxygen. Na
kutokana na kuni hizi hufanyika makaa haya ya miti tuyatumiayo. Ukiyachoma makaa
hutoka nguvu zilizo kuwamo ndani yake kwa ajili ya kupikia, na kwa kazi nyingi
nyenginezo. Na makaa ya mawe si chochote ila ni hiyo hiyo mimea na miti iliyo
kuwa na kufanyika kama ilivyo elezwa, na kisha ikazikika kwa njia fulani na
kugeuka baada ya kupita mamilioni ya miaka kuwa makaa ya mawe, kwa kuathirika na
hali za geology kama joto au mdidimizo au menginewe. Na yapasa kuzingatia kuwa
kutajwa katika Aya hii "mti wa kijani" si bure, bali ni ishara ya hiyo
Chlorophyll ya kijani ambayo ni lazima kwa ajili ya kuimeza Carbon dioxide
katika mimea.
81. Kwani hao
wamepotelewa na akili zao hata hawajui kwamba aliye ziumba mbingu na ardhi, juu
ya ukubwa wao, ni Muweza vile vile kurejesha kuwaumba wanaadamu ambao ni wadogo
na hali yao ni dhaifu? Kwani? Yeye ni Muweza sana, na Yeye ni Mwingi wa kuumba,
ambaye ujuzi wake umeenea kila kitu.
82. Hakika
shani yake katika kuumba anapo taka kiwe kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Kikawa, na
hutokea hapo hapo!
83. Basi
Mtukufu ametakasika na kila kisicho laiki na dhati yake, yule ambaye katika
kudra yake upo Ufalme wa kila kitu, kwa kuumba, na kupanga, na kuendesha - Kwake
Yeye peke yake mtarejeshwa, akuhisabuni kwa a'mali zenu.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani