1. Anaye stahiki sifa njema ni Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye ndiye aliye zifanya mbingu na ardhi zikawa bila ya kuwapo ruwaza ya kuigia mfano wake. Naye ndiye aliye wajaalia Malaika kuwa ni wajumbe kuwatuma kwa viumbe vyake. Wao hao wana mbawa za idadi mbali mbali, mbili-mbili, tatu-tatu, na nne-nne. Yeye huzidisha katika kuumba kwake kama atakavyo kuzidisha. Hashindwi na kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ana uweza mkubwa juu ya kila kitu.
 

2. Mwenyezi Mungu akipeleka rehema kwa watu, rehema yoyote ile iwayo, ikiwa ni mvua, au neema, au amani, au hikima - hapana mtu yeyote awezaye kuwazuilia na kuwanyima. Na chochote katika hivyo akikizuilia Yeye basi hapana mmoja awezaye kukifungulia isipo kuwa Yeye Mwenyewe. Na Yeye ndiye Mwenye kushinda ambaye hashindwi. Mwenye hikima asiye kosea.
 

3. Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu, kwa kuzishukuru na kutimiza haki yake. Na mkiri hayo yaliyo tokea ndani ya nafsi zenu, ya kwamba hapana muumba isipo kuwa Mwenyezi Mungu ambaye anakuruzukuni kutoka mbinguni kwa zinavyo viteremsha, na kutoka kwenye ardhi kwa vinavyo toka humo, ambavyo vinakuleteeni uhai wenu. Hapana mungu isipo kuwa Yeye anaye waruzuku waja wake. Basi yawaje mnavyo geuzwa mkaacha Tawhidi ya Muumba wenu na Mwenye kukuruzukuni mkaendea kumshirikisha katika ibada yake?
 

4. Na hao makafiri wa kaumu yako wakikukadhabisha kwa uwongofu ulio waletea, basi wewe wastahamilie. Kwani Mitume wa kabla yako walikwisha kadhibishwa vile vile, na wakavumilia kwa walivyo kadhibishwa mpaka wakashinda. Na mambo yote yatarejea kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
 

5. Enyi watu! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu, juu ya mambo ya kufufuliwa, na malipo, na ushindi, ni haki ya kweli. Basi msiache dunia ikakukhadaini na Akhera. Wala Shetani akakukhadaini mkaacha kuwafuata Mitume, na akakupeni tamaa kuwa mtasamehewa na hali huku mnaendelea na maasi.
 

6. Hakika Shetani ni adui yenu wa kale, msikhadaike kwa ahadi zake. Nanyi mchukulieni kuwa ni adui yenu. Kwani hakika yeye anawaita wafwasi wake wapate kuwa watu wa Moto uwakao kwa nguvu, na wala hawaitii kwa jenginelo.
 

7. Wanao mkufuru Mwenyezi Mungu na Mitume wake watapata adhabu kali. Na wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wakatenda mema watapewa kutokana na Mwenyezi Mungu kusamehewa madhambi yao, na ujira mkubwa kwa vitendo vyao.
 

8. Wamekuwa hawatambui? Je! Yule ambaye Shetani kampambia vitendo vyake viovu na mwenyewe akaona ni vizuri, ni kama aliye hidika kwa uwongofu wa Mwenyezi Mungu na akaliona jema kuwa ni jema, na uovu akauona kuwa ni uovu? Kwani hakika Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye katika wanao khiari njia ya upotovu, wakaiona ndiyo njia ya kuifuata. Na humhidi amtakaye miongoni mwa walio ikhiari njia ya hidaya kuwa ndiyo njia ya kuifuata. Basi usiihiliki nafsi yako kwa kuwasikitikia wapotovu na kuwaonea huruma. Hakika Mwenyezi Mungu anajua uovu wautendao, naye atawalipa kwa hayo.
 

9. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anaye zituma pepo ziyatimue mawingu yaliyo rindika kwa mvuke wa maji. Tena tukayasukuma hayo mawingu mpaka kwenye nchi yenye ukame, tukaihuisha ardhi yake baada ya kuwa ilikuwa     imekufa. Kama tunavyo itoa mimea katika ardhi, basi hali kadhaalika tutawatoa maiti makaburini Siku ya Kiyama.
Rejea maoni ya ki-ilimu juu ya Aya 57 katika Surat Al Aa'raaf.
 

10. Mwenye kutaka utukufu na nguvu na akazitafute kwa kumt'ii Mwenyezi Mungu. Kwani Yeye ndiye Mwenye nguvu zote. Kumwendea Yeye ndio linapanda neno jema. Na Mwenyezi Mungu huinyanyua a'mali njema na akaipokea. Na wale wanao wapangia Waumini vitimbi vya kuwadhuru watapata adhabu iliyo kali. Na hizo njama zao zitafisidika, hazito leta hayo waliyo yakusudia, wala hazileti natija yoyote.
 

11. Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na udongo. Kwani ndivyo hivyo alivyo muumba baba yenu Adam. Kisha akakuumbeni kutokana na tone ya manii, nayo ni maji yanayo miminwa katika tumbo la uzazi, nayo pia ni katika chakula kinacho toka kwenye udongo. Kisha akakufanyeni waume na wake. Wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai ila kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Wala hauongezwi umri wa mtu yeyote, wala haupunguzwi ila husajiliwa katika Kitabu. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni sahali, mepesi.
 

12. Na haziwi sawa bahari mbili katika ujuzi wetu na makadirio yetu, ijapo kuwa zinashirikiana katika baadhi ya manufaa yao. Haya maji matamu yanakata kiu kwa uzuri wake, na utamu wake, na wepesi wake kuyanywa. Na haya mengine ni maji ya chumvi, uchumvi wake mkali. Na kutokana na namna zote mbili mnakula nyama mpya (fresh, haikuchacha) nayo ni samaki mnao wavua. Na mnatoa kutoka maji ya chumvi mapambo mnayo yavaa, kama lulu na marijani. Na wewe, mwenye kutazama, unaona vipi vyombo vya baharini vinavyo kwenda, vikipasua maji kwa mwendo wake, ili mkatafute baadhi ya fadhila za Mwenyezi Mungu kwa kufanya biashara, na ili asaa mpate kumshukuru Mola wenu Mlezi kwa neema hizi.
Na katika Ishara za Mwenyezi Mungu ambazo anawaitia watu wazizingatie na ambazo amewaneemesha fadhila zake ni mwendo wa marikebu na kukata kwake maji baharini kwa mujibu wa kawaida zake alizo ziwekea katika tabia za maumbile, nazo ni hizo sharia za vitu kuelea, (The law of boayancy). Ni maarufu kuwa baadhi ya mapambo yanapatikana kutoka maji ya chumvi, na baadhi ya watu labda wanaona haiwi maji matamu kutoa mapambo vile vile. Lakini ilimu na mambo yalivyo yamethibitisha kinyume cha hivyo. Ama lulu kama zinavyo patikana katika maji ya chumvi, basi vile vile zinapatikana kwenye namna fulani nyengine za chaza wa mitoni. Hupatikana lulu katika maji matamu katika Uingereza, Scotland, Wales. Czechoslovakia na Japan.. n.k. mbali na lulu za baharini maarufu. Na pia vinaingia katika vinavyo patikana katika maji matamu maadini thamini ngumu kama almasi, zinazo patikana katika udongo unao tupwa na mito. Hupatikana pia Yaakuti, katika mito ya Mojok karibu na Andalas katika Burma ya juu. Ama katika Siam (Thailand) na Sri Lanka hupatikana Yaakuti katika mito. Na katika mawe ambayo yashabihiana na ya ghali na hutumiwa kwa pambo ni Topaz.  Na hupatikana pia kwenye mito mwahali mwingi katika Brazil na Urusi (Ural na Siberia) Fluro-sylicate of aluminium. Aghlabu hiyo huwa ya manjano au rangi ya kahawia. Circom ni jiwe thamini linavutia. Sifa zake zinakaribia za Almasi. Namna zake nyingi hupatikana kwenye mito. (Kadhaalika dhahabu, ambayo inaitwa Alluvial gold yaani dhahabu ya mtoni, hupatikana nchi nyingi, mojawapo ni Zaire.)
 

13. Yeye huuingiza usiku katika mchana, na mchana katika usiku. Matokeo yake ni kuwa saa zao hurefuka na hufupika kwa mujibu wa mipango ya hikima miaka nenda miaka rudi. Na Yeye amelifanya jua na mwezi kutumika kwa manufaa yenu. Kila kimojapo kinakwenda kwa muda maalumu utao ishia kwake. Huyo mwenye shani kuu ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye kuyapanga mambo yenu. Ufalme ni wake Yeye peke yake. Na hao wengineo mnao waomba kuwa ni miungu mnao waabudu hawawezi kumiliki hata ugozi mwembamba ule wa kokwa ya tende. Basi inakuwaje wastahili kuabudiwa?
Aya hii tukufu inaonyesha kuwa jua lina muda utakao kwisha baadae. Na huenda kuwa huo ndio utao kuwa Mwisho kwa mujibu wasemavyo wataalamu wa ilimu ya Falaki (Astronomy) kwamba jua linaunguza kuni zake za Dharra (Nuclear fuel) nayo ni Hydrogen  inayo geuka kuwa Helium. Huenda kuwa ukisha muda wa jua ndio Msiba Mkuu wa Ulimwengu wote.
 

14. Mkiwaomba hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawasikii maombi yenu. Na hata ingeli kuwa wanasikia wasingeli kujibuni kitu chochote kwa hayo myatakayo. Na Siku ya Kiyama watakuja kukataa huo ushirikina wenu kuwashirikisha na Mwenyezi Mungu. Wala hapana wa kukupeni khabari za hali za Akhera kuliko huyo Mwenye kuzijua vyema kwa ujuzi wa ndani kabisa.
 

15. Enyi watu! Nyinyi ndio mnao mhitajia Mwenyezi Mungu kwa kila kitu. Na Yeye Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kujitosha, hawahitajii viumbe vyake. Na Yeye ndiye Mwenye kustahiki kusifiwa kwa kila hali
 

16. Mwenyezi Mungu akitaka kukuteketezeni, basi atakuteketezeni kwa utimilivu wa uweza wake. Na alete uumbaji mpya utao ridhiana na hikima yake.
 

17. Wala kukuhilikini nyinyi na kuwaleta wenginewe si muhali kwa Mwenyezi Mungu.
 

18. Wala nafsi yenye dhambi haitobeba dhambi za mwenginewe. Na mtu aliye kuwa taabani kwa mzigo wake wa madhambi, akimwomba mwenginewe amchukulie, huyo mwengine hatomchukulia hata kidogo, hata angeli kuwa ni jamaa yake. Haya ni kwa kuwa kila mtu kashughulika na yake. Na ewe Nabii! Usihuzunike kwa inadi ya watu wako. Kwani hakika maonyo yako yanawafaa wale ambao wanamkhofu Mola wao Mlezi peke yao katika siri, na wakashika Sala kwa mujibu inavyo faa. Na mwenye kujisafisha na uchafu wa madhambi, basi anajisafisha kwa faida ya nafsi yake. Na marejeo yote mwishoni ni kwa Mwenyezi Mungu, na Yeye atamtendea kila mtu kwa anavyo stahiki.
Rejea maoni ya ki-ilimu juu ya Aya 7 Surat Azzumar: Na mbebaji habebi mzigo wa mwengine.
 

19,20,21. Hawawezi kulingana wakawa sawa:- asiye hidika kuifuata Haki kwa ujinga wake na mwenye kufuata Njia ya uwongofu kwa ujuzi wake; wala uwongo na kweli; wala kivuli na upepo umoto
 

22. Wala hawawezi kuwa sawa walio hai kwa kukubali Imani, na maiti ambao hawahisi kitu na nyoyo zao zimefungika na kuweza kusikia yaliyo kweli. Hakika Mwenyezi Mungu humhidi amtakaye asikie hoja kwa sikio la kukubali. Wala wewe, ewe Nabii, si mwenye kuwasikilizisha walio kufa kwa inadi yao na ukafiri wao, kama ilivyo kuwa huwasikilizishi walio makaburini.
 

23. Wewe huna jukumu ila la kufikisha Ujumbe na kuonya tu.
 

24. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma wewe uwafikishie watu wote hii Dini ya Haki, ukiwabashiria Pepo wenye kuamini, na ukiwaonya kwa adhabu ya Moto wanao ikataa hii Dini. Na hapana kaumu yoyote katika kaumu zilizo pita ila walijiwa na mtu kutokana na Mwenyezi Mungu wa kuwahadharisha na adhabu yake.
 

25. Na ikiwa kaumu yako wanakukadhibisha wewe basi walio kuwa kabla yao waliwakadhibisha Mitume wao vile vile. Na wao waliwaletea miujiza iliyo wazi, na Maandiko ya Mola Mlezi na Kitabu chenye nuru  kwa ajili ya kuwaongoza Njia ya kuokoka duniani na Akhera.
 

26. Kisha nikawashika walio kufuru kwa mshiko mkali. Basi hebu angalia kulikuwaje kuchukia kwangu kwa vitendo vyao, na ghadhabu yangu juu yao!
 

27. Ewe mwenye akili! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu anayateremsha maji kutoka mbinguni, na kwa maji hayo anatoa mazao yanayo khitalifiana rangi zake? Mengine ni mekundu na manjano, na matamu na machungu, mazuri na mabaya. Na katika milima, ipo milima yenye  njia na mistari myeupe na myekundu, yenye kukhitalifiana pia kwa kukoza na kufifia.
Ya kustaajabisha kitaalamu katika Aya hii tukufu sio tu kwa kukhitalifiana rangi mbali mbali katika milima, ambazo zinatokana na hizo sehemu za maadini zilizo fanya majabali, kama vile chuma huonyesha rangi yake nyekundu, na manganese na makaa ya mawe huonekana kwa rangi nyeusi, au shaba ambayo hudhihirisha rangi ya kijani n.k. Lakini ya kustaajabisha khasa ni kuunganisha baina ya kutoa matunda ya namna mbali mbali na hali miti yake inanyweshwa maji yale yale,  na kuumbwa milima myekundu, na myeupe, na myeusi, na yote yana asli moja kwa kuundwa kwake. Wataalamu wa ilimu za t'abaka za ardhi, Jiolojia, wanaita Magma. Na hii Magma moja inapo chomoza pahala mbali mbali katika ardhi, na penye vina mbali mbali (kwenda chini) katika ardhi kutoka juu basi hupatikana khitilafu katika muundo wake na hukusanyika kwa kurindika kuwa ni milima yenye maadini ya rangi mbali mbali. Na huu basi mwendo wa Mwenyezi Mungu ni mmoja. Kwani hakika asli ni moja, na matawi ndiyo yanakhitalifiana kwa kuonekana. Na katika haya yanapatikana manufaa na faida kwa binaadamu.
 

28. Na miongoni mwa watu na wanyama, na mifugo, yaani ngamia, ng'ombe, kondoo na mbuzi, kadhaalika zipo khitilafu katika sura, ukubwa na rangi. Na hawazingatii huu muumbo wa ajabu na wakamwogopa aliye umba ila wanazuoni ambao wanatambua siri ya uumbaji wake. Hakika Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda anaogopwa na Waumini, naye ni Mwingi wa kuwafutia madhambi yao wanao rejea kwake.
Baada ya kueleza kukhitalifiana matunda, na milima, na watu, na wanyama, na mifugo, inaashiriwa kuwa juu ya khitilafu hizi zinazo onekana baina ya hali hizi zote, upo umoja wa asli. Kwani hayo matunda yanatokana na maji yale yale. Na milima inatokana na Magma moja. Kadhaalika khitilafu za rangi, na watu, na wanyama, na mifugo, hazidhihiri katika tone za manii ambavyo vyote hivyo vimetoka mwanzo wake. Na lau hizo tone zingeli chunguzwa kwa darubini ya Maikroskopu kisingeli onekana kitu cha kuonyesha hizo khitilafu zitazo kuwa. Kwani hizo ni siri zilioko ndani yake katika zinazo itwa Genes (Jiinz). Na labda haya pia yanaonyesha kuwa sifa za kurithi ziliomo katika asli ya mimea, na wanyama, na binaadamu, zinalindwa katika maumbile yake, na hazigeuki kwa tabia ya pahala au chakula.
 

29. Hakika wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kwa kukizingatia na kukitenda, na wakashika Sala kwa mujibu itakikanavyo na wakatoa kwa siri na kwa kuonekana baadhi ya alicho waruzuku Mwenyezi Mungu, wanataraji kwa hayo kufanya na Mwenyezi Mungu biashara isiyo anguka faida yake.
 

30. Ili Mwenyezi Mungu awalipe ujira wao, na awazidishie juu yake kutokana na fadhila yake kwa anavyo waongezea mema yao na kuwafutia maovu yao. Yeye ni Msamehevu, Mwingi wa kufutia makosa ya kujikwaa, Mwenye kushukuru, Mwingi wa kushukuru kwa ut'iifu wa waja.
 

31. Na tuliyo kuletea Wahyi wewe katika hii Qur'ani ni Haki tupu isiyo kuwa na shaka yoyote. Tumeiteremsha kuthibitisha Vitabu vilivyo teremshwa kwa Mitume walio kuwa kabla yako, kwa kuwa vyote ni asli moja. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa kujua na kuona kwa waja wake.
 

32. Tena tumekifanya Kitabu hichi ni mirathi ya kurithiwa na waja wetu tulio wateuwa. Basi kati yao yupo aliye jidhulumu nafsi yake kwa kuzidi maovu yake kuliko mema yake; na yupo wa kiasi, hakupita mpaka katika maovu yake na wala hakukithirisha mema yake; na miongoni mwao yupo aliye washinda wenginewe kwa kufanya mambo ya kheri, kwa kusahilishiwa na Mwenyezi Mungu. Huko kushinda katika mambo ya kheri ndio kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
 

33. Malipo yao Akhera ni Mabustani ya daima watayo yaingia. Humo watajipamba kwa vikuku vya dhahabu na lulu. Na nguo zao za Peponi ni hariri.
 

34. Na watasema wakisha ingia: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu aliye tuondolea ya kutuhuzunisha. Hakika Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa maghfira, Mwingi wa shukra.
 

35. Aliye tuweka kwenye Nyumba ya neema ya milele kwa fadhila zake hatupi taabu humo, wala hatuletei machofu.
 

36. Na walio kufuru malipo yao waliyo ahidiwa ni Moto wa Jahannamu watakao uingia. Mwenyezi Mungu hatawahukumia mauti wakafa, wala hawatapunguziwa chembe ya adhabu wakapumzika. Ni kama hivyo tunavyo mlipa kila mwenye kuendelea katika ukafiri na akaushikilia.
 

37. Na humo watapiga makelele kuomba msaada wakisema: Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni, tupate kutenda mema siyo yale tuliyo kuwa tukiyatenda duniani.  Atawaambia: Hatukukupeni fursa ya kufanya a'mali, tukaufanya mrefu umri wenu kwa muda unao mkinika mtu ndani yake kuzingatia kwa mwenye kuzingatia? Na akukujieni Mtume akakuhadharisheni na adhabu hii. Basi onjeni katika Jahannamu malipo ya udhalimu wenu. Kwani mwenye kudhulumu hapati wa kumnusuru wala kumsaidia.
 

38. Hakika Mwenyezi Mungu anajua vyema kila kilicho fichikana katika mbingu na ardhi. Hapana chenye kufichikana kwake. Na lau ange kukubalieni akakurudisheni duniani mngeli rejea yale yale aliyo kukatazeni. Hakika Yeye Mtukufu anavijua vyema vishawishi na vivutio viliomo ndani ya vifua.
 

39. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kufanyeni baadhi yenu wawafuatie wengine katika kuiamirisha dunia na kuifanya itoe matunda yake. Na Yeye ni Mwenye kustahiki kushukuriwa si kukufuriwa. Basi mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu dhambi za kufuru yake zitakuwa juu yake mwenyewe. Na makafiri hawatopata ziada yoyote kwa Mola wao Mlezi isipo kuwa chuki na kukasirika. Wala makafiri hawatazidi ila kupata khasara tu.
 

40. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Hebu nambieni, mmeiona hali ya hawa miungu wenu wa kishirikina mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Hebu nambieni, sehemu gani katika ardhi waliyo iumba wao? Hebu wanao ushirika wowote na Mwenyezi Mungu katika kuziumba mbingu? Sisi hatukuwapa kitabu cha ushirikina wakawa wao wanatoa hoja kutoka humo. Lakini wenye kudhulumu hawaahidiani wenyewe kwa wenyewe kwa uombezi wa miungu yao ya kumshirikisha na Mwenyezi Mungu ila kwa uwongo na kupambia pambia kuso mdanganya mtu ila aliye kuwa akili yake ni dhaifu.
 

41. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye zuia mpango wa mbingu na ardhi usivurugike, na ndiye anaye zihifadhi mbingu na ardhi zisiondoke. Na lau akizijaalia kuondoka hapana wa kuweza kuzihifadhi hizo isipo kuwa Mwenyezi Mungu Mwenyewe. Hakika Yeye ni Mpole, hafanyi papara kuwaadhibu wakhalifu. Yeye ni Msamehevu wa madhambi ya wenye kurejea kwake wakatubu.
Aya hii tukufu inathibitisha kwamba Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la peke yake ndiye Muumba mbingu na ardhi. Yeye ndiye Mwenye kuzishika zisiondoke. Kwani hivi vitu viliomo mbinguni vya karibu na mbali vinavyo onekana katika qubba la mbingu vimeshikamana kwa mujibu wa mpango maalumu wa namna ya pekee alio uumba Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Kutukuka. Na Yeye ndiye aliye viwekea mvutano usio katika kwa kupita zama na vizazi, na ndiye anaye vihifadhi visikosee mizani yao. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala ndiye Mwenye uweza huu, wala hapana mwenginewe.
 

42. Na makafiri waliapa kwa jina la Mwenyezi Mungu mwisho wa juhudi yao kutilia nguvu kiapo chao, ya kwamba bila ya shaka akiwajia Mtume kuwaonya basi wao hapana shaka watakuwa miongoni mwa mataifa walio ongoka zaidi kuliko hao wenginewe walio wakadhibisha Mitume wao. Lakini alipo wajia Mtume kutokana na wao wenyewe, akiwaonya, hakuwazidishia kwa kuwaonya kwake na kuwanasihi, isipo kuwa kuikimbia Haki.
 

43. Wameikimbia Haki kwa kupandwa na kiburi katika nchi, na kuona ari kumnyenyeka Mtume na Dini aliyo kuja nayo. Wakapanga njama za vitimbi viovu. Na ni Shetani ndiye aliye waongoza hata wakaiacha Dini na wakaingia kumpiga vita Mtume. Na wala madhara ya vitimbivi viovu hayampati mtu ila yule yule aliye vipanga.  Basi watu hao wanangojea nini isipo kuwa sunna ya Mwenyezi Mungu  iliyo wasibu wale walio watangulia? Basi hutoipata njia ya Mwenyezi Mungu anavyo yafanyia mataifa  ibadilike, kama wanavyo tumai hawa wapangaji vitimbi yawe kinyume na walio watangulia. Na kabisa hutopata mwendo wa Mwenyezi Mungu ubadilishe njia ulio elekea.
 

44. Je! hao hukaa na wakakanya tu ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa washirikina, bila ya wao kusafiri katika ulimwengu wakaangalia kwa macho yao athari za maangamizo yaliyo wateremkia walio kuwa kabla yao kwa sababu ya kuwakadhibisha kwao Mitume? Na kabla ya wao yalikuwako mataifa yaliyo kuwa na nguvu kushinda wao. Nguvu zao hazikuweza kuzuia adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwani Yeye hashindwi na chochote kilioko mbinguni wala katika ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye ilimu kubwa kabisa, Mwenye uweza mkubwa kabisa.
 

45. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli kuwa anawaadhibu watu duniani, basi hapana shaka adhabu yake ingeli enea. Na asingeli muacha juu ya mgongo wa ardhi hata mnyama mmoja, kwa kuwa wote wametenda madhambi. Lakini anaakhirisha kuwaadhibu mpaka siku maalumu, nayo ni Siku ya Kiyama. Basi ukifika muda wao walio wekewa atawalipa kwa uangalizi kaamili. Kwani Yeye  ni Mwenye kuviona vitendo vya waja wake; hafichikiwi na kitu chochote katika hivyo. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua kushinda wote.