1. Sifa zote
nzuri ni haki ya Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Mwenye kuumba, na Mwenye kumiliki,
na Mwenye kupanga vyote vilioko mbinguni, na vilioko katika ardhi. Na Yeye peke
yake ndiye Mwenye sifa Akhera, kwa kutamalaki kwake kuliko enea. Naye ndiye
Mwenye hikima asiye kosa, Mwenye khabari zote, hapana asicho kijua siri yake.
2. Anajua kila
kinacho ingia katika sehemu za ardhi, kama maji, na khazina, na vilio zikwa, na
sehemu za maiti; na kila kinacho toka, kama wanyama, na mimea, na maadeni, na
maji ya visima, na chemchem. Na anajua vinavyo teremka kutoka mbinguni, kama
Malaika, na Vitabu wanavyo vipokea Manabii, na mvua, na radi; na anajua vinavyo
panda ndani yake na kwendea huko, kama Malaika, na a'mali za ibada, na roho. Na
Yeye ni Mwingi wa rehema, Mkubwa wa kusamehe.
3. Na wenye
kukufuru wakasema: Haitujii Saa iliyo ahidiwa kuwa ni ya kufufuliwa na
kukusanywa watu. Waambie ewe Mtume! Hapana shaka itakujieni, nami naapa kwa Mola
wangu Mlezi, Mwenye kujua ya siri, ambaye hapana chenye kughibu na ujuzi wake
hata ingawa kiasi ya chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi. Wala kilicho
kidogo kuliko chembe, wala kikubwa kuliko hivyo hakikosi kuandikwa katika Kitabu
kilicho timia, chenye kubainisha kila kitu. Dharra , tuliyo ifasiri "Chembe", na
kisayansi ni Atom kwa hakika katika lugha ya Kiarabu ni kitu kidogo sana, kama
sisimizi mdogo, au chembe ya vumbi. Na uzito wa Dharra maana yake ni uzani wake.
Na Aya inaonyesha kuwa kipo kilicho kuwa ni kidogo kuliko Dharra. Na yafaa
kutaja hapa kuwa sayansi za sasa zimethibitisha kuwa Dharra, yaani Atom,
imegawika katika sehemu ndogo zaidi nazo ni Nucleus na Electrons. Na haya haya
hayakuthibitika ila katika karne ya ishirini ya kuzaliwa Nabii Isa.
4. Ili Mwenyezi
Mungu awathibitishe walio amini na wakatenda mema kwa ajili ya nafsi zao na kwa
ajili ya watu wengine. Hao Waumini watendaji watapata kwa Mwenyezi Mungu msamaha
wa kuwafutia madhambi yao, na riziki kunjufu isiyo na masimbulizi ndani yake.
5. Na hao walio
zishughulisha nafsi zao kuipiga vita Qur'ani kutaka kuishinda amri ya Mwenyezi
Mungu katika kumsaidia Mtume wake, hao watapata adhabu katika adhabu za mwisho
wa ubaya na uchungu.
6. Na walio
neemeshwa na Mwenyezi Mungu kwa kupewa ujuzi kuwa Qur'ani ulio teremshiwa kutoka
kwa Mola wako Mlezi, yenye ndani yake mambo ya itikadi na uwongofu, ni Haki
isiyo kuwa na shaka yoyote, wanajua kuwa hiyo ndiyo yenye kuwaongoa watu kwendea
Njia ya Mwenyezi Mungu, Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kustahiki kila sifa
njema.
7. Na makafiri
waliambiana wenyewe kwa wenyewe, kwa kufanyia kejeli kufufuliwa: Je!
Tukuonyesheni mtu ataye kuambieni kwamba mtapo kwisha kufa, na viwiliwili vyenu
vikagawika mapande mapande kuwa ati mtafufuliwa tena kwa umbo jipya?
8. Mtu huyu
amemzulia uwongo Mwenyezi Mungu kwa kumnasibishia kuwa atawafufua wafu, au mtu
huyu ana wazimu ndio anasema asiyo yajua? Siyo hayo wayasemayo. Bali ukweli wa
mambo ni kuwa hao wasio iamini Akhera wataingia katika adhabu na upotovu wa
kupotelea mbali na Haki.
9. Je!
Wamepofuka, hata hawaaoni yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao ya mbinguni na
katika ardhi wakaujua uweza wetu wa kutenda tuyatakayo? Tukitaka ardhi iwameze,
tutawazamisha. Au tungeli taka viwaangukie vipande vya mbingu tuwasage sage
tungeli wateremshia. Hakika katika tuliyo yataja zipo dalili kwa kila mja mwenye
kurejea kwa Mola wake Mlezi katika kila jambo lake.
10. Wallahi!
Kwa hakika tulimpa Daudi fadhila kutoka kwetu kwa kumpa hikima na Kitabu. Na
tulisema: Enyi milima! Karirini pamoja naye Tasbihi kumtakasa Mwenyezi Mungu,
pale anapo sabihi yeye. Na Sisi tuliwafanya ndege pia wamtumikie, nao wawe
wakikariri kumtakasa Mwenyezi Mungu. Na tukakifanya chuma kiwe laini kwake aunde
kwa sura atakayo. Daudi, a.s. ni mmoja wa Manabii wa Wana wa Israili, na mmoja
wa wafalme wao. Aliishi katika zama za baina ya mwaka 1010 na 970 K.K. (yaani
kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s.)
11.
Tulimfunulia kumwambia aunde nguo za chuma pana za kujilinda katika vita na
maadui. Naye azifume kwa hikima na ustadi katika kuviunga viungo vyake. Na
tukamwambia yeye na watu wake: Tendeni yatakayo kuleteeni kheri na maslaha.
Hakika Mimi nayaona vyema yote myatendayo, hapana kinacho niporonyoka nisikione.
12. Na
Suleiman tukamfanyia upepo umtumikie. Mwendo wake wakati wa asubuhi mmoja ni
sawa na safari ya dasturi inayo chukua mwezi mzima. Na mwendo wake wakati wa
jioni moja ni kama safari ya kuchukua mwezi. Na tukamyayushia maadeni ya shaba
ikawa inatiririka kwa wingi moja kwa moja. Na tukawafanya majini wawe
wakimtumikia mbele yake kwa amri ya Mola wake Mlezi. Na yeyote katika majini
aliye wacha kut'ii amri ya Suleiman basi tulimwonjesha adhabu ya Moto unao waka
kwa nguvu.
13. Hao majini
wakifanya atakacho Suleiman, kama misikiti kwa ajili ya ibada, na masanamu, na
madeste au mabakuli makubwa kama mahodhi ya maji, na vyombo vya kupikia, yaani
masufuria, makubwa yaliyo kaa pale pale penye mafya yake hayaondoki kwa kuwa ni
makubwa mno. Na tukawaambia watu wa Daudi: Tendeni kazi ya kumshukuru Mwenyezi
Mungu vilivyo. Na ni wachache miongoni mwa waja wangu ambao wanakumbuka neema
zangu wakawa wananishukuru kwa wingi.
14. Tulipo
mhukumia Suleiman mauti, hapana aliye waonyesha majini kuwa kesha kufa ila
kinyama cha ardhi kilicho ila fimbo yake aliyo kuwa akiiegemea. Alipo anguka
majini wakajua kuwa lau kuwa wangeli jua ya ghaibu wasingeli endelea na ile
adhabu ya mashaka ya kuwadhalilisha.
15. Ninaapa:
Hakika katika watu wa Sabaa katika makaazi yao ya Yaman palikuwa na Ishara ya
uweza wetu. Zilikuwako bustani mbili zilizo zunguka nchi yao, kulia na kushoto.
Wakaambiwa: Kuleni katika riziki ya Mola wenu Mlezi, na mshukuru neema zake kwa
kuzitumilia inavyo faa. Huu mji wenu ni mji mzuri, una vivuli na matunda. Na
Mola wenu Mlezi ni Mwingi wa maghfira kwa anaye mshukuru.
16. Lakini wao
waliacha kushukuru neema, na wakawa maisha yao ya kiburi. Tukawafungulia
mafuriko ya nguvu yaliyo tokea baada ya kupasuka kuta za mahodhi, yakateketeza
mabustani yao. Tukawabadilishia badala ya bustani zao mbili zile zenye matunda
mazuri, zikawa nyengine mbili zenye matunda machungu, na miti isiyo kuwa na
matunda, na mikunazi kidogo isiyo toa hamu. Hili liitwalo "Hodhi" la maji ya
mvua kubwa au "Hodhi la Ma`arib" ni kubwa kuliko mahodhi yote ya Yaman. Hodhi
hili linaweza kubadilisha ardhi kavu ya kiasi ya maili 300 ya mraba ikawa yenye
rutba na mashamba. Na dalili ya hayo ni hizo bustani mbili zilizo tajwa.
Wanazuoni wa taarikh (historia) wanakhitalifiana katika ujenzi wa hilo hodhi
kuu. Vile vile zipo kauli mbali mbali kukhusu kubomoka kwake.
17. Hayo ndiyo
malipo tuliyo walipa kwa kufuru zao kuzikufuru neema na kuto zishukuru. Na kwani
Sisi tunamuadhibu kwa adhabu hii kali yeyote yule ila aliye kuwa mwingi wa
kumkufuru Mwenyezi Mungu na fadhila zake?
18. Na
tulifanya baina ya maskani yao ya Yaman na baina ya miji mingine iliyo barikiwa
miji mingineyo pia iliyo karibiana inaonana. Na tukafanya makhusiano baina yao
ni kiasi maalumu cha mwendo usio kuwa wa taabu. Na tukawaambia: Nendeni humo
usiku na mchana nanyi mko katika amani.
19. Kwa
kutakabari kwa neema, na raha, na amani, walisema: Tuwekee mbali masafa ya
safari zetu, tusisadifu kukuta miji iliyo amirishwa ya katikati mpaka tufike
huko twendako! Mwenyezi Mungu akazifanya ziwe mbali hizo safari zao. Na wakawa
wao wamejidhulumu nafsi zao kwa uasi wao. Tukawafanya hao ni masimulizi ya watu,
na tukawatenganisha mtengano mkubwa. Hakika katika yaliyo wapata hao yapo
mawaidha kwa kila mwenye kusubiri kwa balaa, mwenye kushukuru kwa apewacho.
20. Na bila ya
shaka Iblisi amehakikisha dhana yake juu yao. Nao wakamfuata yeye isipo kuwa
wachache miongoni mwa Waumini.
21. Na wala
Iblisi hakuwa na nguvu za kuwafanya wamt'ii na kumnyenyekea; lakini Mwenyezi
Mungu kawafanyia mtihani apate kuwadhihirisha wepi wanao isadiki Akhera, na wepi
wana shaka nayo. Ewe Nabii! Mola wako Mlezi ni Mwenye kuchungua kila kitu,
Mwenye kusimamia kila kitu.
22. Ewe Nabii!
Waambie washirikina: Waombeni hao mnao dai kwa uwongo kwamba ni miungu badala ya
Mwenyezi Mungu, wakuleteeni manufaa au wakuondoleeni madhara. Hawakujibuni kitu.
Kwani hao hawamiliki hata kiasi ya chembe ya kitu katika mbingu wala katika
ardhi. Wala wao hawana ushirika wowote na Mwenyezi Mungu katika kuumba au
kumiliki. Wala hapana yeyote katika hao miungu ya uwongo anaye msaidia Mwenyezi
Mungu katika kupanga mambo ya viumbe vyake.
23. Wala
maombezi kwa Mwenyezi Mungu hayawafai ila wenye kustahili makamo ya kuombewa.
Mpaka itapo ondoka khofu katika nyoyo zao kwa kutolewa ruhusa ya kuombewa, hapo
watakuwa wakiambiana kwa furaha: Mola wenu Mlezi kakwambieni nini? Na wengine
watajibu kwamba alilo sema ni kauli ya haki, kwa kutoa ruhusa kuombewa aliye
mridhi. Na Yeye peke yake, ndiye Mwenye Utukufu na Ukubwa. Na Yeye ndiye anaye
ruhusu na kumkatalia amtakaye.
24. Ewe Nabii!
Waambie washirikina: Nani anaye kuleteeni riziki kutoka mbinguni na kwenye
ardhi? Watapo kuwa hawajibu kwa inda tu, waambie: Mwenyezi Mungu peke yake ndiye
anaye kuruzukuni kutoka kote kuwili. Je! Ni sisi Waumini au nyinyi washirikina
ndio walio katika moja ya hali mbili, ya uwongofu au upotofu ulio wazi?
25. Ewe Nabii!
Waambie: Nyinyi hamuulizwi khabari ya madhambi tuliyo yafanya sisi; wala sisi
hatuulizwi khabari ya vitendo vyenu.
26. Waambie:
Mola wetu Mlezi atatukusanya Siku ya Kiyama, kisha atatuhukumu kwa haki. Na Yeye
Subhanahu ndiye Hakimu wa kila shauri, Mwenye kujua kwa hakika yetu sisi na yenu
nyinyi.
27. Waambie:
Nionyesheni hao mlio waunganisha na Mwenyezi Mungu kwa kustahiki kuabudiwa, mnao
dai kuwa ni miungu wa shirika na Yeye. Yeye hana mshirika, bali Yeye ndiye
Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye hikima katika kupanga kwake na
kuendesha kwake.
28. Na Sisi
hatukukutuma ewe Muhammad, ila kwa watu wote. Uwe ni mwenye kuwabashiria Waumini
kuwa watapata kheri, na mwenye kuwaonya makafiri kuwa watapata shari. Lakini
aghlabu ya watu hawaujui ukweli wako, wala kuwa Utume wako ni wa kwa watu wote.
(Haya ni kwa sababu hapana Mtume aliye kuja kwa watu wote ila huyu Nabii
Muhammad s.a.w. Nabii Musa alikuja kwa Wana wa Israili kuwatoa Misri. Nabii Isa,
Yesu Kristo, pia kaja kwa Wana wa Israili tu, kama isemavyo Qur'ani 3.49, na
Injili ya Mathayo 10.5-6 Yesu alipo sema: "Afadhali shikeni njia kuwaendea
kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli." Na 15.24 alipo sema: "Sikutumwa ila kwa
kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli." Na Injili ya Yohana 17.9)
29. Na
makafiri wanasema kwa kuifanya haiwi hiyo Siku iliyo ahidiwa kwa ajili ya
malipo: Lini itakuwa ahadi hii tuingie Motoni, na nyinyi muingie Peponi, kama
nyinyi ni wakweli kwa hiyo ahadi yenu?
30. Ewe Nabii!
Waambie: Miadi yenu ni Siku kubwa mno; ikifika hamto chelewa hata kwa saa moja,
wala hamto tangulia.
31. Na walio
kufuru wanasema: Hatuisadiki Qur'ani hii wala hivyo Vitabu vilivyo tangulia
kabla yake kwa hayo vinavyo amrisha na kulingania. Na lau ungeli ona - ewe
mwenye kuweza kuona - wakati wanapo simamishwa madhaalimu mbele ya Muumba wao,
Mwenye kumiliki amri yao, ungeliona maajabu katika msimamo wao, pale wanapo
jibizana maneno wao kwa wao. Walio wanyonge wakiwaambia walio tukuka juu yao:
Ingeli kuwa si nyinyi, kwa kutusaliti na kutamalaki, hapana shaka tungeli kuwa
Waumini.
32. Walio
takabari na wakajiona ni wakubwa, watawaambia wanyonge, kwa kuyapinga maneno
yao: Kwani sisi tulikuzuieni msiongoke ulipo kufikieni uwongofu? Tumekuzuieni
sisi au nyinyi wenyewe ndio mmekhiari upotofu kuliko uwongofu.
33. Na
wanyonge nao watawaambia walio takabari: Bali vitimbi vyenu na uchochezi wenu
kutuchochea usiku na mchana ndio umetutumbukiza katika hilaki, pale mlipo kuwa
mkitutaka tumkufuru Mwenyezi Mungu, na tumfanyie miungu mingine ya
kumshirikisha. Na pande zote mbili zikaficha majuto yao walipo iona adhabu
inawashukia. Wakajua kuwa hapana faida ya kuonyesha majuto. Na tukayaweka
makongwa, (nira), juu ya shingo za wasio amini. Je! Watu hawa wanastahiki
chochote ila malipo kwa yale waliyo kuwa wakiyatenda?
34. Na sisi
hatukumtuma Mtume yeyote kwenda kwenye mji kuwaita watu wake wafuate Haki ila
wale wanao jidekeza kwa starehe zao katika ule mji husema: Hakika sisi
tunayakanusha hayo mliyo kuja nayo.
35. Na husema
kwa kujipa: Sisi tuna mali mengi zaidi na watoto. Wala hatutaadhibiwa Akhera.
36. Ewe Nabii!
Waambie: Hakika aliye niumba humkunjulia riziki amtakaye, katika wanao muasi na
wanao mt'ii. Na humdhikisha amtakaye. Wala hiyo si dalili ya kuwa Yeye yuradhi
na mtu au anamchukia. Lakini watu wengi hawajui haya.
37. Wala mali
yenu wala watoto wenu sio jambo la kukurubisheni kwetu mkawa karibu. Lakini
ambaye Imani yake imethibiti, na akawa anatenda mema, basi watu kama hao ndio
watapata thawabu mara mbili kwa waliyo yatenda. Na Peponi watakuwa ni watu wa
juu na wenye amani.
38. Na hao
ambao wana fanya juhudi kuzipinga Ishara zetu, wakifanya kila hila kuzivunja na
kuwazuia Manabii wetu wasifikishe Ujumbe wake, hao, basi watakuwa katika adhabu,
wamehudhurishwa na wala hawataepuka.
39. Ewe Nabii!
Sema: Hakika Mola wangu Mlezi anamkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na
humdhikisha amtakaye. Na chochote mtacho kitoa Yeye atakilipa. Na Yeye Aliye
takasika ni Mbora wa wenye kuruzuku.
40. Na taja,
ewe Nabii, siku Mwenyezi Mungu atapo wakusanya wote, na kisha Subhanahu awaambie
Malaika mbele ya wale walio kuwa wakiwaabudu: Je! Hawa walikuabuduni nyinyi
khasa badala yangu mimi?
41. Malaika
watasema: Sisi tunakutakasa kabisa na kuwa Wewe una mshirika wowote. Wewe ndiye
tulio shikamana nawe kwa mapenzi na ut'iifu, sio wao. Hao wameghurika katika
madai yao kuwa wanatuabudu sisi. Bali walikuwa wanafuata nyayo za mashetani
walio wapambia ushirikina. Wengi wao wakiwasadiki hao.
42. Basi Siku
ya Mkusanyo hapana atakaye weza kumletea mwenzie manufaa wala kumkinga na
madhara. Na tutawaambia walio jidhulumu nafsi zao: Ionjeni adhabu ya Moto ambayo
mlio kuwa duniani mkiikanusha.
43. Na
makafiri walipo somewa Aya zetu zilio wazi dalili zake kuonyesha Haki, makafiri
walisema: Huyu si chochote ila ni mtu anaye taka kukuzuilieni msiwaabudu walio
kuwa wakiwaabudu baba zenu. Na pia walisema: Hii Qur'ani si chochote ila ni
uwongo ulio tungwa tu. Na walio ikataa Qur'ani ilipo wajia walisema: Hii si
chochote ila ni uchawi ulio wazi.
44. Na
Mwenyezi Mungu hakuwateremshia Waarabu Vitabu vya mbinguni wavisome; wala
hutukupata kuwapelekea Mwonyaji kabla yako wa kuwahadharisha na matokeo ya
ukafiri wao.
45. Na kaumu
zilizo tangulia ziliwakadhibisha Manabii wao. Na hawa washirikina wa kaumu yako
hawajafikia hata sehemu moja katika kumi za nguvu na umadhubuti tulio wapa hao
walio tangulia. Wakawakanusha Mitume wangu. Basi ilikuwaje ghadhabu yangu juu
yao jinsi nilivyo wakasirikia!
46. Waambie:
Mimi nakuamrisheni jambo moja tu - Msimame kwa ikhlasi ya kumtakasia Mwenyezi
Mungu muache kufuata mitindo yenu ya zamani - katika kuchungua kwa kumsafia niya
Mwenyezi Mungu, mkigawika wawili-wawili, au mmoja-mmoja, muangalie kwa uadilifu
na insafu. Kisha mfikiri khabari ya huyu mwenzenu, Muhammad, ambaye mmeishi naye
na mnajua kuwa akili yake ni timamu. Huyu hana wazimu kwa kuliingia jambo hili.
Yeye huyu si chochote ila ni Mwonyaji kwenu, anakuhadharisheni msije mkapata
adhabu kali inayo kukabilini mbele yenu.
47. Waambie
makafiri: Ujira wowote nilio kutakeni juu ya kufikisha Ujumbe ni kwa maslaha
yenu. (Yaani nyinyi mwongoke na mpate malipo kwa Mwenyezi Mungu.) Sina ujira
ninao utaraji mimi ila kwa Mwenyezi Mungu. Naye ni Mwenye kuangalia na kuchungua
kila kitu.
48. Waambie:
Hakika Mola wangu Mlezi huitupa Haki juu ya baat'ili (uwongo) ikauondoa. Na Yeye
ndiye Mwenye kuijua vyema ghaibu; hapana siri inayo fichikana kwake.
49. Waambie:
Uislamu umedhihiri, wala uwongo hauwezi kuwa ndio njia ya kuipinga Haki. Na hizo
mbinu za zamani hazirejei tena.
50. Waambie:
Nikiiacha Haki basi madhara ya hayo yataniangukia mwenyewe. Na nikiongoka basi
nimeongozwa na Mola wangu Mlezi. Yeye ni Mwenye kusikia kauli yangu na kauli
yenu. Yupo karibu nami, na karibu yenu.
51. Na lau
kuwa utaona, ewe mwenye kuona, pale watapo fazaika makafiri kweli itapo dhihiri,
basi hawatakuwa na pa kukimbilia. Na watachukuliwa wapelekwe kwenye Moto kutoka
pahala karibu.
52. Na
watasema, watapo iona adhabu: Tunaiamini Haki! Na vipi wao waipate Imani kwa
wepesi huo kutoka pahala mbali na dunia ambayo wakati wake umekwisha pita?
53. Na ilhali
wao walikwisha ikataa Haki kabla ya Siku hii, na wakavurumiza kwa dhana ya
uwongo kutoka mahala palipo mbali na ukweli.
54. Patawekewa
kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani ya Imani ya kuwafaa, kama walivyo
fanyiwa wenzao wa kabla yao walipo amini baada ya kwisha wakati wake. Kwa sababu
wote hao wote walikuwa katika kuifanyia Haki shaka inayo pelekea kutuhumiwa.
Rudi kwenye
sura
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani