1. Ewe Nabii
endelea hivyo hivyo, kama ulivyo, kumcha Mwenyezi Mungu, wala usiyakubali mawazo
ya makafiri na wanaafiki. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu
vyote kwa kuvijua, ni Mwenye hikima katika kauli yake na vitendo vyake.
2. Na fuata
wahyi unao teremka juu yako kutokana na Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu
anaye kufunulia kwa wahyi anazo khabari hata za mambo madogo madogo unayo
yatenda wewe, na wanayo yatenda makafiri na wanaafiki.
3. Na wewe
mwachilie mambo yako yote Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kabisa kuwa
ni mtegemewa wa kila jambo.
4. Mwenyezi
Mungu hakumjaalia mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake; wala
hakumfanya mke wa yeyote katika nyinyi kuwa ni mama yake, pale anapo sema ati:
Wewe kwangu mimi kama mgongo wa mama yangu! Wala hakuwafanya watoto mnao wapanga
kuwa ni wenenu, kuwa hakika ni wana wenu kwa nasaba. Hayo ya kuwafanya watoto wa
kupanga kuwa ni wenenu, ni kauli inayo toka kwenye vinywa vyenu, wala hayana
ukweli. Hapana hukumu yoyote inayo tokana na hayo. Na Mwenyezi Mungu anasema
jambo lilio thibiti la hakika. Na anakuongozeni mlifikie. Na Yeye peke yake
Subhanahu ndiye anaye ongoa watu kwenye Njia iliyo sawa.
5.
Wanasibishieni hawa watoto kwa baba zao khasa. Hayo ndiyo ya uadilifu zaidi
mbele ya Mwenyezi Mungu. Ikiwa hamwajui baba zao walio nasibiana nao khasa, basi
hao ni ndugu zenu katika Dini na rafiki zenu wa kuwanusuru. Wala nyinyi hamna
dhambi ikiwa mmewanasibisha na watu wasio kuwa baba zao kwa kukosea. Lakini
inakuwa dhambi kwa mlio kusudia kwa nyoyo zenu baada ya kwisha jua yaliyo. Na
Mwenyezi Mungu anakusameheni kwa kukosea kwenu, na anaikubali toba yenu kwa
makosa mliyo kusudia.
6. Nabii
Muhammad ni mwenye kustahiki zaidi urafiki kwa Waumini, na ana huruma zaidi kwa
Waumini kuliko nafsi zao. Basi yawapasa wao wampende na wamt'ii. Na wake zake ni
Mama zao kwa kuwatukuza na kuwahishimu, na kuwa ni haramu juu yao kuwaoa baada
yake. Na jamaa walio khusiana ni karibu zaidi kuliko Waumini wenginewe na
Wahajiri, walio hama Makka, kwa kurithiana wao kwa wao kama ilivyo wajibika
katika Qur'ani. Lakini inafaa kumfanyia wema mlio fanya urafiki naye katika Dini
asiye kuwa jamaa yenu, kwa kuwapa wema na mapenzi au hata kumuandikia mali
katika wasia. Hayo ya kurithiana jamaa walio khusiana yamethibiti katika Kitabu
cha Qur'ani wala hayawezi kubadilishwa.
7. Na kumbusha
pale tulipo fanya agano na Manabii wote walio tangulia kuwa watafikisha ujumbe
na wito kulingania Dini iliyo sawa, na wewe, na Nuhu, na Ibrahim, na Musa, na
Isa bin Maryamu; na tukachukua kwao agano lenye shani kubwa.
8. Ili Mwenyezi
Mungu awaulize Manabii Siku ya Kiyama juu ya waliyo waambia kaumu zao. Na Yeye
amewaandalia wenye kuwakataa Mitume adhabu yenye kutia uchungu.
9. Enyi mlio
amini zikumbukeni neema na fadhila za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu, pale yalipo
kujieni makundi katika Siku ya Handaki. Tukawapelekea upepo mkali wa kimbunga
ubaridi, na Malaika ambao nyinyi hamwaoni. Kikawaingia kiwewe katika nyoyo zao.
Na Mwenyezi Mungu alikuwa Mwenye kuviona vitendo vyenu, na ukweli wa niya zenu.
Basi akaingia kukulindeni.
10. Walipo
kujieni kutoka upande wa juu ya bonde, na kutoka chini, na macho yakakodoka, na
nyoyo zikapanda mpaka kwenye koo, kwa kufazaika na kubabaika. Na nyinyi katika
wakati ule wa shida kubwa kila namna ya dhana zilikujieni juu ya ahadi ya
Mwenyezi Mungu. Si makusudio ya maneno haya kuwa maadui walikuja kutoka kila
upande. Tukiangalia ufafanuzi wa tukio hili inadhihirika kuwa makusudio ni kuwa
walio kuja kutoka upande wa juu ya Waislamu, ni kabila ya Ghat'fan na walio
wafuata katika wakaazi wa Najdi, kwani wao walikuja pande za juu ya Bara Arabu
upande wa mashariki. Na inatudhihirikia kuwa walio kuja upande wa chini ya
Waumini ni Makureshi, kwa sababu wao walikuja kutoka upande wa chini ya Bara
Arabu upande wa magharibi.
11. Katika
wakati ule Waumini walifanyiwa mtihani juu ya kusubiri kwao juu ya Imani.
Wakatikisika kwa khofu kwa mtikiso mkubwa.
12. Na kumbuka
shaka iliyo waingia wanaafiki na wagonjwa wa nyoyo walipo sema: Ahadi aliyo tupa
Mwenyezi Mungu na Mtume ni ahadi ya uwongo, imekusudiwa kutudanganya tu.
13. Na kumbuka
walipo sema kikundi cha wanaafiki na ambao wanao rega rega: Enyi watu wa
(Yathrib, yaani) Madina! Hapana maana kubakia hapa nyinyi katika vita hivi vya
kushindwa. Rudini mwende makwenu. Na kundi jingine kati yao walimtaka ruhusa
Mtume warejee Madina, na wakasema: Hakika nyumba zetu hazina ulinzi. Hatuna budi
kurejea tukazilinde. Wala nyumba zao hazikuwa khatarini kabisa kama walivyo
sema. Hawakutaka ila kukimbia vita tu, kwa udhuru wa uwongo.
14. Lau kuwa
makundi ya majeshi ya maadui wangeli waingilia Madina kwa kila upande, na
wakawataka watangaze kuwa wameuwacha Uislamu na wawapige vita Waislamu bila ya
shaka wangeli wakubalia yale waliyo takiwa, na wala wasingeli sita ila muda
mfupi tu.
15. Na hakika
hawa wenye kukimbia kutoka midani ya vita walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu
kabla yake kuwa watasimama imara katika vita pamoja na Mtume, na wala
hawatakimbia. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa kwa yule mwenye
kuitoa, na yampasa aitimize.
16. Waambie:
Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa ndio mnayakimbia mauti au kuuwawa, maadamu ajali
yenu imekwisha fika. Na ikiwa haijafika, basi hamtobaki mkistarehe katika dunia
ila kwa muda wa umri wenu, nao ni mchache.
17. Waambie
hawa wanao babaika: Nani atakaye kulindeni na Mwenyezi Mungu akitaka kukuleteeni
shari, au atakaye kuzuieni msipate kheri, akitaka Yeye kukurehemuni? Wala
hawatapata badala ya Mwenyezi Mungu yeyote wa kuwalinda au kuwaokoa.
18. Hakika
Mwenyezi Mungu anawajua wanao zuilia miongoni mwenu, na wanao waambia ndugu zao:
Unganeni nasi! Wala hawaingii katika vita vinapo shitadi ila kidogo tu.
19. Wana pupa
juu yenu kwa kuonekana dhaahiri inapo kuwa hapana khofu. Na ikija khofu ya adui
au ya Mtume s.a.w. utawaona wanakuangalia na macho yao yanawazunguka
hawajitambui, kama hali ya mwenye kuzimia wakati wa sumbuko la kukaribia mauti.
Na khofu ikiondoka wanapita mpaka kukutukaneni na kukushutumuni kwa ndimi za
kukata. Hao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao hawakuamini kwa nyoyo zao, ijapo
kuwa wametangaza kuwa ni Waislamu. Basi Mwenyezi Mungu amezibat'ilisha a'mali
zao kwa ukafiri wao walio dhamiria. Na kubat'ilisha huko ni jambo jepesi kwa
Mwenyezi Mungu. Aya hii tukufu inaashiria ukweli wa kisayansi ambao ulikuwa
haukujuulikana namna yake wakati wa kuteremka Qur'ani Tukufu. Ukweli huo ni kuwa
jicho wakati wa kukurubia mauti au wakati wa khofu huzunguka. Na katika sababu
za hayo ni kuwa kwa shida ya khofu utambuzi hutoweka, ikawa mtu hajitambui.
Vituo vya navo zisio tambua katika ubongo hupoteza mizani yake, basi huwa huyo
mwenye khofu kama mfano wa mwenye kuzimia kwa kukaribia kufa, jicho lake
huzunguka na mboni ya jicho hupanuka, na hubaki katika hali ya kukodoa macho
mpaka kufa.
20. Wanadhani
hawa wanaafiki kwamba majeshi ya makafiri yaliyo ungana bado yapo mahali pao
wanaizinga Madina. Na hayo makundi ya maadui yakirejea tena, watatamani hao woga
laiti wangeli kuwa wanaishi pamoja na mabedui huko majangwani wakidondoa khabari
zenu. Na lau wakibaki kwenye kambi zao, na wasikimbie, na majeshi mawili
yakapambana, basi hata hivyo wasinge pigana pamoja nanyi ila kidogo tu, kama
kujionyesha na watajwe kuwa nao walikuwamo.
21. Hakika
nyinyi mna kiigizo kizuri kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa mwenye kutaraji
rehema ya Mwenyezi Mungu, na neema za Siku ya Mwisho, na akamkumbuka na kumtaja
Mwenyezi Mungu kwa wingi katika khofu na kutumai, na katika shida, na katika
neema.
22. Na Waumini
walipo yaona makundi ya washirikina walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi
Mungu na Mtume wake zamani. Kwani walituahidi tutapata shida, na kisha tutapata
ushindi. Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Taabu hizi basi,
hazikuwazidishia ila nguvu za kumuamini Mwenyezi Mungu, na uzuri wa kuinyenyekea
kwao hukumu yake.
23. Miongoni
mwa hawa Waumini wapo watu walio muahidi Mwenyezi Mungu kuwa watasimama imara na
Mtume katika vita. Nao wakatimiza ahadi yao. Miongoni mwao wapo walio pata
utukufu wa kufa mashahidi, na wengine wamebakia wahai wakingojea nao kupata
utukufu huo. Wala hawakuigeuza ahadi ya Mwenyezi Mungu waliyo jikatia juu ya
nafsi yao, wala hawakugeuza chochote katika hayo.
24. Ili
Mwenyezi Mungu apate kuwalipa Waumini walio wakweli kwa sababu ya ukweli wao
katika Imani yao na kutimiza kwao ahadi waliyo itoa. Na awaadhibu wanaafiki -
pindi akitaka - au amwezeshe aliye elekea, kufikia toba. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kusamehe kwa kukubali toba, Mwenye kurehemu kwa kusamehe maasi.
25. Mwenyezi
Mungu akawarudisha nyuma makafiri walio jiunga makundi kumpiga Mtume na nyoyo
zao zimejaa chuki. Hawakupata kheri yoyote kwa ushindi wala ngawira. Na Mwenyezi
Mungu amewatosheleza Waumini wasipate mashaka, kwa kuwapatiliza wale makafiri
kwa upepo na Malaika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza wa kutimiliza alitakalo,
ni Mwenye nguvu hapana wa kumshinda.
26. Na
Mwenyezi Mungu aliwateremsha walio wasaidia makundi ya maadui katika Watu wa
Kitabu, nao ni Mayahudi wa Bani Quraidha, kutokana na ngome zao walipo kuwa
wakijilinda ndani yake. Na akaingiza katika nyoyo zao kitisho. Wengine mkawa
mnawawauwa, nao ni wanaume, na wengine mnawachukua mateka, nao ni wanawake na
watoto.
27. Na
akakurithisheni ardhi zao, na nyumba zao, na mali zao, na ardhi ambazo nyayo
zenu hazijapata kuzikanyaga kabla yake. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Muweza wa
kutimiza kila alitakalo.
28. Ewe Nabii!
Waambie wake zako kwa kuwanasihi: Ikiwa mnataka maisha ya duniani na starehe
zake, basi jongeeni nitakupeni cha kupunguza upweke wa talaka, itakuwa ni tunza
yenu. Na nitakupeni talaka isiyo na uovu ndani yake.
29. Na ikiwa
mnakhiari mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na neema za nyumba ya Akhera,
na mnaridhi maisha magumu mlio nayo hivi sasa, basi hakika Mwenyezi Mungu
amewaandalia mfano wenu nyinyi miongoni mwa wanawake walio wema kwa vitendo
vyao, ujira ambao haukadiriki.
30. Enyi wake
wa Nabii! Miongoni mwenu mwenye kufanya makosa yaliyo dhaahiri ubaya wake, basi
juu ya adhabu yake zinaongezwa adhabu mbili, ili iwe adhabu tatu kwa
kulinganisha na mwenziwe. Na kuongeza huko kwa Mwenyezi Mungu ni kwepesi.
31. Na katika
nyinyi mwenye kudumu juu ya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
akatenda mema, Mwenyezi Mungu atampa ujira mara mbili. Na tumemuandalia kwa
Akhera riziki ya kipimo kizuri.
32. Enyi wake
wa Mtume! Nyinyi si kama wanawake wengine kwa fadhila na utukufu. Kama mnataka
uchamngu, basi msizungumze kwa maneno ya kuregeza sauti, hata ambaye ana
uharibifu katika moyo wake akaingia tamaa. Kusema kwenu kuwe kama kawaida sio
kujitia.
33. Na kaeni
nyumbani kwenu, wala msitoke ila kwa haja. Wala msidhihirishe uzuri wenu na
mapambo yenu kwa wanaume pale mnapo toka, kama walivyo kuwa wakifanya watu wa
ujahili wa zamani. Na timizeni Sala kwa ukamilifu, na toeni Zaka, na fuateni
amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka, kwa yote
anayo kuamrisheni na kukukatazeni, mpate utukufu na hishima, ili muondokewe na
madhambi na maasia, enyi Ahli Baiti Nnabii, Watu wa Nyumba ya Nabii, na
akusafisheni kwa usafi usio kuwa na shaka.
34. Na
hifadhini yanayo somwa katika nyumba zenu ya Qur'ani aliyo iteremsha Mwenyezi
Mungu, na hikima zilio sawa za Mtume wa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kuyajua mambo yalio zama ndani kabisa na ya hakika yake. Basi tahadharini
na kwenda kinyume naye na kumuasi Mtume wake.
35. Hakika
wenye kut'ii miongoni mwa wanaume na wanawake, na wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu
na Mtume wanaume na wanawake, na wenye kusimama kwa ut'iifu wanaume na wanawake,
na walio wa kweli katika kauli zao na vitendo vyao katika wanaume na wanawake,
na wenye kusubiri katika kubeba mashaka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wanaume na
wanawake, na wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu wanaume na wanawake, na wenye
kuzihifadhi tupu zao kwa yasiyo kuwa halali wanaume na wanawake, na wenye
kumdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi katika nyoyo zao na ndimi zao wanaume na
wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia kuwasamehe madhambi yao, na kuwalipa
malipo makubwa kwa vitendo vyao.
36. Haimjuzii
Muumini, mwanamume au mwanamke, kuwa na khiari katika jambo lolote baada ya
Mwenyezi Mungu na Mtume wake wakisha lihukumia. Na mwenye kwenda kinyume na
alivyo hukumu Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi amejitenga mbali na njia iliyo
sawa kwa umbali ulio dhaahiri.
37. Na kumbuka
pale ulipo mwambia Zaid bin Haritha, ambaye Mwenyezi Mungu amemneemesha kwa
kumwongoa kwenye Uislamu, na wewe ukamneemesha kwa kumlea na kumkomboa utumwani:
Shikamana na mkeo, Zainab binti Jahsh, na umche Mwenyezi Mungu, na vumilia kukaa
naye. Na wewe ulikuwa unaficha nafsini mwako ambayo Mwenyezi Mungu atakuja
yadhihirisha, yaani kuwa yeye atampa t'alaka na wewe utakuja muwoa. Nawe
ukakhofu watu wasije kukulaumu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye stahiki umkhofu,
ijapo kuwa hayo ni mashaka juu yako. Basi Zaid alipo kwisha haja naye, na akampa
t'alaka kujiondolea dhiki ya kuishi naye, tukakuoza wewe, ili iwe ni chanzo cha
kuvunja ada iliyo mbovu. Baada ya hayo hapana ubaya tena kwa Waislamu kuwaoa
walio kuwa wake za walio kuwa wamewapanga utoto, baada ya kwisha wat'aliki. Na
amri ya Mwenyezi Mungu aitakayo ni lazima iwe bila ya pingamizi.
38. Nabii hana
makosa kutenda kitendo alicho muamrisha Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ameweka
mwendo huo kwa Manabii walio tangulia, kuwa wasipige marfuku alicho wahalalishia
na akawakunjulia. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni kupitisha alicho pitisha, na
hukumu iliyo thibiti.
39. Manabii
hao ndio walio wafikishia watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu kama tulivyo
wateremshia. Nao wanamkhofu Yeye, wala hawamkhofu yeyote asiye kuwa Yeye. Na
Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Yeye ndiye Muangalizi Mwenye kuhisabu.
40. Muhammad
si baba wa yeyote katika wanaume wenu hata iwe ni haramu kwake kumwoa mt'alaka
wake. Lakini yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ni Mwenye kukhitimisha Manabii
wote. Juu yake ni kufikilisha ujumbe kama alivyo muamrisha Mola wake Mlezi, bila
ya kumchelea yeyote. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa
ujuzi wake.
41,42. Enyi
ambao mmeamini! Msifuni Mwenyezi Mungu kwa namna mbali mbali za sifa, na mfanye
hayo kwa wingi. Na mtakaseni na kila kisicho kuwa laiki naye mwanzo wa mchana na
mwisho wake.
41,42. Enyi
ambao mmeamini! Msifuni Mwenyezi Mungu kwa namna mbali mbali za sifa, na mfanye
hayo kwa wingi. Na mtakaseni na kila kisicho kuwa laiki naye mwanzo wa mchana na
mwisho wake.
43. Na Yeye
ndiye aliye kuahidini kukupeni rehema yake na upole wake. Na Malaika wake
wanakuombeeni maghfira na uwongofu, ili Mwenyezi Mungu akutoeni kwenye giza la
ukafiri na upotovu, mwendee kwenye nuru na ut'iifu. Na Mwenyezi Mungu hakika ni
Mkuu wa kuwarehemu Waumini.
44. Maamkio
yao siku watakapo kutana naye ni: Amani na Salama kwao. Na amewatengezea kwa
vitendo vyao ujira wa ukarimu utakao waonyesha fadhila zake.
45. Ewe Nabii!
Hakika Sisi tumekutuma kwa watu wote uwapelekee ujumbe wa Uislamu. Ushuhudie
Haki, na uwabashirie Waumini kwamba watapata kheri na thawabu, na uwaonye
makafiri kuwa watapata mwisho muovu.
46. Na
umetumwa uwe ni mwenye kuwaita viumbe vyote vimwendee Mwenyezi Mungu kwa amri
yake. Na uwe ni taa ya uwongofu kuwaongoa kwa nuru yake waliopo katika kiza cha
shaka.
47. Na
wabashirie Waumini kwamba watapata kheri kubwa ya kuzidi katika dunia na Akhera.
48. Na wala
usiwafuate makafiri na wanaafiki, wala usijishughulishe na maudhi yao. Na mfanye
Mwenyezi Mungu ndiye Wakili wako wa kumtegemea kukulinda na madhara yao na shari
zao. Na Mwenyezi Mungu anakutosha kabisa kuwa ndiye Mtegemewa wa kukukifia na
kukukinaisha.
49. Enyi mlio
amini! Mkifunga ndoa na wanawake Waumini, kisha mkawat'aliki kabla ya
hamjawaingilia, basi haiwalazimu eda wao mkawa mnaihisabu. Basi wapeni kitu
katika mali kwa kuwapoza. Na mwatoe majumbani kwenu bila ya kuwaletea madhara
yoyote.
50. Ewe Nabii!
Hakika Sisi tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari. Na tumekuhalishia
wajakazi ulio wamiliki mkono wako wa kulia, katika alio kuneemeshea Mwenyezi
Mungu. Na tumekuhalalishia kuwaoa mabinti ami zako, na mabinti wa shangazi zako,
na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada, yaani ndugu wa kike, wa mama
yako, walio hama nawe. Na tumekuhalalishia mwanamke Muumini akijitolea nafsi
yake bila ya mahari, nawe ikawa unataka kumwoa na umempenda. Kujitolea huku ni
kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Kwao haifai hivyo. Tunajua hukumu tulizo
wafaridhia Waumini kwa wake zao na wajakazi wao, na tuliyo kuruhusu wewe, si
wao, ili isiwe dhiki juu yako kwa tuliyo kuhukumia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe madhambi ya waja wake, Mwenye kuwarehemu kwa ukunjufu.
51. Unaweza
kumuakhirisha umtakaye katika kugawa zamu, na ukamjongeza umtakaye. Na kumtaka
uliye muakhirisha zamu yake hapana lawama juu yako. Hivyo kuachiliwa utakavyo
wewe yakaribia zaidi kupelekea furaha yao na baada ya kuwahuzunikia, na wao wote
wawe radhi kwa ulio wapa. Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo ndani ya nyoyo
zenu, ya kuudhika au kuridhika kwa aliyo kufanyieni sharia. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kuyajua yaliomo vifuani, Mpole hafanyi papara kuadhibu.
52.
Hawakuhalalikii wanawake wengine baada ya hawa, wala kuwapa t'alaka kwa ajili ya
kuwabadilisha kwa wengine uwatakao, hata wakikupendeza kwa uzuri wao. Lakini
Mwenyezi Mungu amekuhalalishia wajakazi ulio wamiliki kwa mkono wako. Na
Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu, na anakihifadhi.
53. Enyi mlio
amini! Msiingie nyumba za Nabii ila kwa idhini yake kwa ajili ya kwenda kula
chakula, bila ya kwenda kungoja wakati mpaka kitapo kuwa tayari. Lakini Mtume
akikuiteni, basi ingieni. Na mkisha kula ondokeni. Wala msikae baada yake
mkijizoeza mazungumzo nyinyi kwa nyinyi. Kwani hakika kuingia bila ya idhini
yake, na kukaa muda mrefu baada ya kwisha kula, kunamuudhi Nabii, naye
anakustahini hawezi kukutakeni mtoke. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu hana la
kumzuia asiitangaze haki kama wanavyo zuilikana viumbe. Na mtakapo wauliza wake
za Nabii s.a.w. haja yoyote, basi waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ni usafi
bora kwa nyoyo zenu na nyoyo zao zisiingiwe na uchochezi wa Shetani. Na
haikufaliini nyinyi kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake
baada yake milele, kwa sababu ya hishima yake na yao. Hakika jambo hilo ni
dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu. Yanarejea maelezo ya ki-ilimu juu ya Aya mbili
58, na 59 za Surat An-nur, katika yaliyo khusu adabu za kuzuru.
54.
Mkidhihirisha walau kidogo katika mambo yanayo muudhi, au mkikificha katika
vifua vyenu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
55. Hapana
dhambi kwa wakeze Nabii wakitojificha kwa baba zao, au watoto wao, au ndugu zao,
au watoto wa ndugu zao wa kiume, au watoto wa ndugu zao wa kike, au wanawake
Waumini wenginewe, au watumwa walio wamiliki, kwa sababu ya shida ya kuwahitajia
kwa matumishi. Nanyi wanawake, mcheni Mwenyezi Mungu katika mambo aliyo
kuamrisheni, wala msipindukie mipaka yake. Kwani Yeye hakika anajua kila kitu,
hapana kilicho fichikana kwake.
56. Hakika
Mwenyezi Mungu anamrehemu Nabii wake na yu radhi naye. Na Malaika wanamwombea
yeye. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu.
57. Hakika
wanao muudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kuwapinga na kuchochea watu
wawakatae, Mwenyezi Mungu amewafukuza kwenye rehema yake duniani na Akhera; na
amewaandalia adhabu itayo wavunja kiburi chao.
58. Na wanao
waudhi Waumini wanaume na wanawake kwa maneno au vitendo, bila ya wao kufanya
makosa yoyote, hao basi wamebeba migongoni mwao mzigo wa ule uwongo wao, na
inakuwa wametenda dhambi iliyo dhaahiri ubaya wake.
59. Ewe Nabii!
Waambie wake zako, na binti zako, na wake wa Waumini, wateremshe nguo zao juu ya
miili yao. Na wakivaa namna hii ni afadhali na wanaelekea zaidi kujuulikana na
kwa hivyo wasipate kuudhiwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye
kumrehemu mwenye kuacha madhambi yake.
60. Ninaapa!
Ikiwa hawataacha hao wanaafiki, na wenye maradhi katika nyoyo zao, na wanao
eneza khabari za uwongo katika Madina, hapana shaka nitakusalitisha juu yao,
kisha hawatabakia kuwa karibu yako ila kwa muda mchache tu.
61. Hao
wanastahiki laana na kufukuzwa. Kila watapo patikana wakamatwe na wauliwe moja
kwa moja.
62. Mwendo wa
Mwenyezi Mungu Mtukufu tangu zamani, kwa walio kuwa wakiwafanyia unaafiki
Manabii na Mitume, na wakiasi, ni kuwa huuwawa kila wanapo kutikana. Wala mwendo
wa Mwenyezi Mungu haugeuki.
63. Watu
wanakuuliza lini itasimama Saa ya Kiyama. Waambie hao: Hakika ujuzi wa wakati
wake uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na nini kitakujuvya? Pengine wakati wa
kusimama Saa ya kiyama upo karibu.
64. Hakika
Mwenyezi Mungu amewafukuza makafiri kwenye rehema yake, na amewatengenezea Moto
mkali mno.
65. Hawatatoka
humo kabisa. Hawatampata wa kuchukua dhamana ya kuwahami, wala wa kuwatetea.
66. Siku
zitakapo geuka nyuso zao Motoni kutoka hali hii kwendea hali hiyo, wakisema kwa
majuto: Laiti kuwa sisi tulimt'ii Mwenyezi Mungu na tungeli mt'ii Mtume!
67. Na
watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwafuata maraisi wetu, na wakubwa wetu
katika kukukataa Wewe na Mtume wako. Na wao ndio wakatutenganisha mbali na Njia
Iliyo Nyooka.
68. Mola wetu
Mlezi! Wajaalie adhabu yao iwe mardufu, na uwafukuze kwenye rehema yako kabisa
kwa kadri ya madhambi yao na makosa yao.
69. Enyi mlio
amini! Msimuudhi Nabii kwa namna yoyote ya udhia, kama wale walio muudhi Musa
katika kaumu yake. Na Mwenyezi Mungu akamtoa makosani na akamsafisha na hayo
waliyo mzulia. Na Musa mbele ya Mwenyezi Mungu alikuwa ni bwana mwenye hadhi.
70. Enyi mlio
amini! Iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu mkimuasi, na semeni maneno yalio simama
sawa yasio kwenda upogo.
71. Apate
kukuwezesheni kutenda mema, na azifute dhambi zenu. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi
Mungu na Mtume wake, basi huyo amepata kufuzu kukubwa kwa kuepuka adhabu, na
kupata thawabu.
72. Sisi kwa
hakika tulizitaka mbingu na ardhi na milima zichukue dhamana, nazo zikakataa
kuichukua, na wakaiogopa. Lakini mwanaadamu aliichukua. Hakika yeye amekuwa ni
mkubwa wa kujidhulumu nafsi yake kwa kutojua jukumu la kuchukua huko.
73. Ili
Mwenyezi Mungu awaadhibu wanaafiki wanaume, na wanaafiki wanawake, na
washirikina wanaume, na washirikina wanawake; na Mwenyezi Mungu apate kukubali
toba za Waumini wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
maghfira, Mwingi wa rehema.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani