1. Alif Lam
Mim, ni harufi zilizo undiwa Qur'ani, kama yalivyo undiwa maneno yenu. Ikiwa
mmeshindwa kuleta mfano wake hii, basi ni ushahidi kuwa hii inatokana na
Mwenyezi Mungu, wala hakuisema mwanaadamu.
2. Huu ni
uteremsho wa Qur'ani umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Na Yeye ndiye mwenye kupanga mambo yao. Hapana shaka yoyote kuwa hii imeteremka
kutoka kwake.
3. Ati
wanasema: Kaizua Muhammad, naye akamsingizia Mwenyezi Mungu! Haiwafalii wao
kusema hayo. Kwani hii ni Haki, Kweli, iliyo teremka kutokana na Mola wako
Mlezi, ili upate kuwakhofisha kwayo watu ambao hawajapata kujiwa na Mtume kabla
yako, utaraji kwa onyo hili wapate kuongoka na waifuate Haki.
4. Mwenyezi
Mungu aliye umba mbingu na ardhi na vilio baina yao kwa siku sita, kisha
akatawala juu ya Kiti cha Enzi, A'rshi, kwa utawala ulio laiki naye. Nyinyi
hamna badala yake Yeye yeyote msaidizi wa kukunusuruni, wala mwombezi wa
kukuombeeni. Basi je, mtaendelea kushikilia kuwa katika ukafiri na inda, wala
msiwaidhike kwa mawaidha ya Mwenyezi Mungu?
5. Yeye
huyaendesha mambo ya uumbaji katika mbingu na ardhi, kisha amri yake hupanda
kwenda kwake kwa siku ambayo kadiri yake ni kama miaka elfu kwa mujibu wa miaka
ya duniani mnayo ihisabu nyinyi.
6. Huyo ndiye
aliye sifika kwa kuumba na kutawala na kupanga, Mwenye kuyajua ya ghaibu ya
viumbe vyote na wanayo yaona, ambaye amri yake ni yenye kushinda, Mkunjufu wa
rehema,
7. Aliye umba
kila kitu kwa ustadi, kwa mujibu wa inavyo hitajia hikima yake, na akaanza
kumuumba mtu wa mwanzo kwa udongo,
8. Kisha
akawafanya dhuriya zake wa namna mbali mbali kutokana na maji machache, dhaifu,
yasiyo tamanika kwa kawaida. Katika Aya hii tukufu "utokane na kizazi cha maji
dhaifu". Neno la Kiarabu lilio tumiwa ni "Mahiin". Neno hili likitumiwa kwa mtu
lina maana ya "dhaif", mnyonge, na pia lina maana ya "chache". Basi kauli ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Min maain mahiin" maana yake ni "kutokana na maji
machache dhaifu" , ndiyo ya kudharauliwa. Mfano wa hayo ni kauli ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu: "Au mimi si bora kuliko huyu aliye (mahiin) mnyonge wala hawezi
kusema waziwazi?" (Azzukhruf: 43.52). Na neno "Mahana al-ibila" maana yake
"Kamkama maziwa ngamia". Kwa hivyo basi hapana ubaya kulifasiri neno hili Mahiin
katika Aya hii kwa maana ya maji yanayo toka kwa kuchupa, au kumiminika, (kama
yanavyo toka maziwa kwenye chuchu) au machache.
9. Kisha
akamsimamisha na kumkuza, na akamtia ndani yake siri yake aliyo mkhusisha nayo,
na akakupeni masikio, na macho, na akili, mpate kusikia na kuona na kufahamu.
Nanyi hamshukuru ila kwa uchache.
10. Na wanao
kanya kufufuliwa wakasema: Ati sisi tukisha kuwa mchanga, ulio changanyika na
mchanga wa ardhi, usibagulike, ndio kweli tutarejea kwa umbo jipya? Hao hakika
si kama wanakanya kufufuliwa tu, bali wanakadhibisha yote yatayo kuwako Akhera.
11. Sema:
Atakufisheni Malaika wa mauti, aliyewakilishwa kuzikamata roho zenu utapo kwisha
muda wenu. Kisha kwa Mwenyezi Mungu peke yake ndio mtarejea.
12. Lau kuwa
umejaaliwa kuwaona wakosefu kwenye msimamo wa hisabu ungeli ona ajabu. Pale wale
wakosefu wenye kujivuna watavyo inamisha vichwa vyao kwa hizaya inayo tokana na
Mola wao Mlezi, nao watasema kwa unyonge: Ewe Mola wetu Mlezi! Tumekwisha yaona
tuliyo kuwa na upofu nayo, na tumekwisha yasikia tuliyo kuwa na uziwi nayo, basi
turejeshe duniani tupate tenda mema ambayo tuliyo kuwa hatuyatendi. Hakika sasa
hivi sisi tumeyakinika na walio kuja nayo Mitume wako.
13. Na lau
kuwa tunataka tungeli mpa kila mtu uwongofu wake, lakini kauli yangu ilikwisha
tangulia, nayo ni: Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa majini na
watu. Kwa kuwa tulijua kuwa wengi wao watakhiari upotovu.
14. Basi
ionjeni adhabu kwa vile mlivyo ghafilika na kukutana nami hii leo. Hakika Sisi
tunakuacheni katika adhabu kama watu walio sahauliwa. Na onjeni adhabu ya milele
isiyo katika, kwa sababu ya ukafiri wenu na uasi wenu.
15. Hakika
wanazisadiki Ishara zetu wale ambao wanapo waidhiwa kwazo huanguka chini kwa
kumsujudia Mwenyezi Mungu, na wakamtakasa Mola wao Mlezi na kila upungufu, na
wakamsifu kwa kila ukamilifu. Na wala wao hawatakabari wakakataa kuzifuata
Ishara hizi.
16. Mbavu zao
zinabambatuka na vitanda vyao, yaani wanaacha usingizi wao, kwa kumwomba Mola
wao Mlezi kwa kuikhofu ghadhabu yake, na kutumai rehema yake; na ambao kutokana
na mali tuliyo wapa wanatoa kwa ajili ya mambo ya kheri.
17. Na hapana
mtu yeyote anaye jua kiasi cha Mwenyezi Mungu alicho muandalia na akawafichia
katika neema kubwa kubwa, na ambazo ni za kupoza macho yao, kuwa ni malipo kwa
waliyo kuwa wanayachuma ya ut'iifu na vitendo.
18. Kwani watu
watakuwa sawa katika malipo yao, na hali wamekhitalifiana katika vitendo vyao?
Je! Aliye kuwa mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu ni kama mwenye kumkataa na
akamuasi? Hasha! Hawawi sawa!
19. Ama walio
amini na wakatenda mema watapata Bustani za Utulivu ziwe ndio maskani zao, kuwa
ni ukarimu watao kirimiwa kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
20. Ama wale
walio toka nje ya ut'iifu wa Mwenyezi Mungu kwa kufuru zao, makaazi yao aliyo
watayarishia ni Motoni. Kila wakijaribu kutoka watarudishwa huko huko. Na
wataambiwa: Onjeni adhabu ya Moto ambayo mlipo kuwa duniani mkishikilia
kuikadhibisha.
21. Na
tunaapa: Hapana shaka tutawaonjesha duniani adhabu duni kabla hawajaifikia hiyo
adhabu kubwa kabisa, nayo ni kudumu milele katika Moto. Huenda pengine watakao
adhibiwa kwa hiyo adhabu duni watatubia, waache ukafiri wao.
22. Na hapana
mtu yeyote aliye zidi udhaalimu kuidhulumu Haki na kuidhulumu nafsi yake, kuliko
mtu anaye kumbushwa kwa Ishara za Mwenyezi Mungu na hoja zilizo wazi, kisha
akaacha kuziamini juu ya kuwa ni wazi dhaahiri. Hakika Sisi tutajilipizia juu ya
kila mkosefu!
23. Na Sisi
tulikwisha mpa Musa Taurati. Basi usiwe na shaka na kupokea kwa Musa Kitabu
hicho. Na tumekijaalia Kitabu alicho teremshiwa Musa kiwe ni uwongofu kwa Wana
wa Israili.
24. Na
kutokana na Wana wa Israili tumejaalia wawepo Maimamu, waongozi, wa Dini,
wasimame kuwaongoa watu, kwa kuitikia amri yetu kwa vile walivyo vumilia
kuyatenda yaliomo katika Taurati, na wakawa wanazisadiki Ishara zetu ukomo wa
kusadiki.
25. Hakika
Mola wako Mlezi ndiye peke yake atakaye hukumu baina ya Manabii na kaumu zao
Siku ya Kiyama katika mambo wanayo khitalifiana.
26. Je! Kwani
Mwenyezi Mungu aliwaacha walio wakadhibisha Mitume wao, na hakuwabainishia
kwamba Yeye aliwahilikisha wengi katika kaumu zilizo watangulia, na wao wanapita
kwenye majumba yao, na wanatembea kwenye maskani zao? Hakika katika hayo pana
mawaidha ya kuwaonyesha Haki. Wao wameingiwa na uziwi, hawasikii mawaidha haya.
27. Wameingia
upofu, na wala hawaoni ya kwamba hakika Sisi tunapeleka mvua na mito kwenye
ardhi za ukame ambazo hazimei mimea, na tukaziotesha mazao yake, wakala wanyama
wao, na wao wenyewe wakala nafaka zake na matunda yake? Wamepofuka, na kwa hivyo
hawazioni dalili za Mwenyezi Mungu za kuwafufua wafu.
28. Na
washirikina wanakwambia wewe na Waumini: Wakati gani Mwenyezi Mungu
atakufungulieni mpate ushindi? Twambieni wakati wake ikiwa nyinyi ni wasema
kweli.
29. Waambie:
Siku ya hukumu na kufafanua ikikufikilieni, walio kufuru haitowafaa kitu imani
yao, wala hawatapewa muhula hata chembe ya hiyo adhabu wanayo istahiki.
30. Na ikiwa
kufanya maskhara kama hivi ndio mtindo wao, basi wapuuzilie mbali. Na wewe
ngojea ukweli aliyo kuahidi Mola wako Mlezi juu yao, kwani wao wanakungojea
ushindwe.
Rudi kwenye
sura
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani