1. Harufi hizi zimeanzia
baadhi ya Sura kuashiria kuwa Qur'ani ni muujiza ulio tungwa na harufi kama
harufi wanazo zitumia Waarabu katika maneno yao. Na juu ya hayo wao wameshindwa
kuleta mfano wake. Na pia ni kwa ajili ya kuzindua watu wasikilize na watege
sikio. Na washirikina walikuwa wamewafikiana kuwa wawe wanaropokwa maneno ya
upuuzi tu ikisomwa Qur'ani wala wasiisikilize.
2. Hizi Aya tukufu ni Aya
za Qur'ani iliyo kusanya hikima na ukweli.
3. Hizi Aya ni Uwongofu
ulio kamilika, na Rehema iliyo kusanya kwa wenye kutenda mema.
4. Hao ndio wanao timiza
Sala kwa njia ya ukamilifu kabisa, na wanawapa Zaka wanao istahiki; na wao
wanayaamini maisha ya Akhera kwa imani yenye nguvu kabisa.
5. Hao Waumini wanao tenda
vyema vitendo vyao, wametua kwenye Uwongofu ulio wajia kutokana na Mola wao
Mlezi. Na hao tu - si wengineo - ndio wenye kufuzu kikweli.
6. Na miongoni mwa watu
wapo ambao hununua maneno ya uwongo wawasimulie watu wapate kuwatenga na Uislamu
na Qur'ani kwa kutojua dhambi zilio juu yao, na wanaifanyia maskhara Dini ya
Mwenyezi Mungu na Ufunuo wake. Watendayo hayo watapata adhabu ya kuwatia unyonge
na kuwadhalilisha.
7. Na mpotovu kama huyu
akisomewa Aya za Mwenyezi Mungu huzipuuza kwa kiburi. Hali yake kwa haya ni hali
ya ambaye hasikii, kama kwamba ana uziwi katika masikio yake. Basi mwonye kuwa
hakika Mwenyezi Mungu amemuandalia adhabu yenye machungu makali.
8. Hakika walio amini na
wakatenda vitendo vyema watapata Bustani zenye neema.
9. Watabaki humo daima
dawamu; Mwenyezi Mungu amewaahidi ahadi isiyo vunjika. Na Mwenyezi Mungu ndiye
Mshindi wa kila kitu, Mwenye hikima katika maneno yake na vitendo vyake.
10. Mwenyezi Mungu
ameziumba mbingu zisio na nguzo za nyinyi kuziona. Na juu ya ardhi ameweka
milima iliyo simama imara, ili ardhi isikutingisheni. Na humo katika ardhi
ametawanya kila namna ya wanyama wanao tambaa na kwenda. Na tumeteremsha maji
kutoka mbinguni, na tukaotesha mimea ya kila namna nzuri yenye manufaa katika
ardhi. Rejea uangalie maelezo ya kisayansi juu ya Aya 2, Sura ya Ar-Raa'd.
11. Hivi viumbe vya
Mwenyezi Mungu vipo mbele yenu, basi hebu nionyesheni walicho umba hao mnao
wafanya ni miungu badala yake Yeye hata wawe ni washirika wake! Bali madhaalimu
- kwa ushirikina wao - wamo katika upotovu ulio wazi.
12. Na hakika tulimpa
Luqman hikima, na ilimu, na kauli ya kusibu. Tulimwambia: Mshukuru Mwenyezi
Mungu kwa neema aliyo kupa. Na mwenye kushukuru basi hakika huyo anaitafutia
kheri nafsi yake. Na mwenye kuzikufuru neema, akazikataa, na asishukuru kwa
ajili yake, basi kwa hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuihitaji shukra yake, na
Yeye Mwenyezi Mungu ni Mwenye kustahiki sifa zote njema, na ingawa pasiwepo hata
mmoja wa kumsifu.
13. Taja pale Luqman
alipo mwambia mwanawe: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu na yeyote.
Hakika kumshirikisha Mwenyezi Mungu ni dhulma kubwa, kuwaweka sawa Mwenye
kustahiki na asiye stahiki. Waarabu walikuwa wanawajua watu wawili kwa jina
hili. Mmoja wapo ni Luqman bin A'adi. Nao walikuwa wakimtukuza cheo kwa werevu
wake, uraisi, ujuzi, ufasihi na ujanja. Na walikithiri sana kumtaja na kumpigia
mithali, kama inavyo onekana katika vitabu vya Kiarabu vingi. Ama mwengine ni
huyo anaye itwa Luqman Alhakim, (Mwenye hikima), aliye kuwa mashuhuri kwa hikima
yake na mifano yake, na ambaye Sura hii ya Qur'ani imeitwa kwa jina lake. Na
hikima zake zilikuwa zimeenea kwa Waarabu. Ibn Hisham amesimulia kwamba Suwaid
bin Ass'amit alifika Makka. Naye alikuwa mtu mtukufu kwa watu wake. Mtume s.a.w.
akamtaka asilimu. Suwaid akasema: Huenda labda uliyo nayo wewe ndiyo kama niliyo
nayo mimi. Mtume s.a.w. akasema: Nini ulicho nacho? Akasema: Majalla ya Luqman.
Mtume s.a.w. akasema: Nisomee. Akamsomea. Tena akasema: Hakika haya maneno
mazuri. Na niliyo nayo mimi ni bora zaidi, nayo ni Qur'ani aliyo niteremshia
Mwenyezi Mungu, nayo ni Uwongofu na Nuru. Mtume s.a.w. akamsomea Qur'ani na
akamtaka asilimu. Na pia Imam Malik ametaja kwa wingi hikima za Luqman katika
kitabu chake, Al Muwatt'a. Na baadhi ya vitabu vya Tafsiri ya Qur'ani na Adab
(maandishi ya ufasihi wa lugha) vimetaja namna mbali mbali katika hikima hizo.
Kisha baadae ikakusanywa mithali kwa visa katika kitabu chenye jina la Mithali
za Luqman. Lakini kwa sababu ya udhaifu wa mpango wake, na wingi wa makosa ya
nahau na sarfu, na kuwa kutopokewa kitabu cha jina hili katika vitabu vya
Waarabu wa kale, yatilia nguvu kuwa hichi kimezuliwa tu katika zama za mwisho.
Na maoni yanayo gongana juu ya uhakika wa Luqman Al-hakim: ni kuwa yeye ni Mnubi
katika watu wa Abla au Uhabeshi, au mtu mweusi wa Sudan ya Misri, au ni
Muibrani. Na wengi walio mtaja wanakubaliana kuwa hakuwa Nabii. Wachache tu ndio
wanasema kuwa alikuwa Nabii. Na tunalo weza kutambua katika yaliyo tajwa ni kuwa
hakuwa Mwaarabu, kwa sababu wote wamewafikiana kwa hayo. Na kwamba alikuwa ni
mtu mwenye hikima, na hakuwa Nabii, na kwamba ameingiza miongoni mwa Waarabu
hikima mpya zikawa zinatajwa mara nyingi kama ilivyo onekana baadae katika
vitabu.
14. Na tumemuamrisha mtu
awafanyie wema wazazi wake, na mama yake ampe fungu kubwa zaidi. Kwani yeye
alimbeba katika mimba kwa udhaifu unao zidi kila siku kidogo kidogo. Na tena
kamnyonyesha muda wa miaka miwili ndipo alipo muachisha ziwa. Na tumemuusia:
Mshukuru Mwenyezi Mungu na wazazi wako. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo kwa
ajili ya hisabu na malipo.
15. Na ikiwa wazazi wako
wakikushikilia kwa juhudi umshirikishe Mwenyezi Mungu na vitu usivyo vijua kuwa
vinastahiki kuabudiwa, basi usiwakubalie. Lakini endelea na kusuhubiana nao
duniani kwa wema na ihsani. Na fuata njia ya wanao rejea kwangu kwa Tawhidi,
Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, na Ikhlasi, usafi wa niya na vitendo. Kisha nyote
mtarejea kwangu, na nitakupeni khabari ya mliyo kuwa mkiyatenda, ya kheri na
shari, ili nipate kukulipeni kwayo.
16. Ewe mwanangu! Hakika
wema au ubaya kwa mtu, hata ukiwa, mathalan, kwa udogo wake kama chembe ya
khardali, iliyoko pahali palipo fichikana kabisa, kama ndani ya jabali, au ndani
ya mbingu, au chini ya ardhi, Mwenyezi Mungu ataufichua na autolee hisabu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, hakifichikani kitu hata kidogo
kwake, ni Mwenye khabari ya kujua hakika ya kila kitu.
17. Ewe mwanangu!
Zihifadhi Sala, na amrisha kila wema, na kataza kila baya, na stahamili kwa
shida zinazo kusibu. Hakika anayo usia Mwenyezi Mungu ni katika mambo ambayo
yanahitajia kufanyiwa hima na kuyashikilia.
18. Wala usiwageuzie watu
uso wako kwa takaburi, wala usitembee katika nchi kwa kujiona na majivuno.
Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kuringa na kujiona.
19. Na nenda mwendo wa
wastani, si mbio mbio mno wala taratibu mno. Na teremsha sauti yako. Kwani
hapana sauti mbaya kama sauti ya punda. Inaanzia kwa mngurumo unao ghasi, na
inaishia kwa ukenje unao kera.
20. Mmeona kwamba
Mwenyezi Mungu amekudhalilishieni viliomo mbinguni kama jua, na mwezi, na nyota
na vyenginevyo; na viliomo katika ardhi, kama mito, na matunda, na wanyama. Naye
amekutimizieni neema zake zilio dhaahiri na zilio sitirika, msizo ziona. Na
miongoni mwa watu, wapo wanao jadiliana juu ya dhati ya Mwenyezi Mungu na sifa
zake bila ya dalili wala uwongozi ulio pokewa kutokana na Nabii au Wahyi
(ufunuo) wenye kumurika kwa mwangaza njia ya Haki.
21. Na pindi wakiambiwa:
Fuateni Haki na Uwongofu alio uteremsha Mwenyezi Mungu, wao husema: Bali sisi
tunafuata tuliyo wakuta nao baba zetu. Je! Wanawafuata hao, ijapo kuwa Shetani
ndio anawaitia wende kwenye upotovu utakao waingizia Motoni?
22. Na mwenye kumuelekea
Mwenyezi Mungu kwa moyo wake na uso wake, na akamwakilisha Yeye mambo yake yote,
naye akawa ni mwenye kutenda vitendo vyema, basi amefungamana na sababu za nguvu
kabisa za kumfikisha kwenye radhi ya Mwenyezi Mungu. Na kwake Yeye, Subhanahu,
ndio marejeo ya mambo yote.
23. Na asiye mtakasia
Mwenyezi Mungu dhati yake na nafsi yake, basi usikuhuzunishe upinzani wake na
mapuuza yake. Kwetu Sisi peke yetu ndio marejeo yao Siku ya Kiyama. Hapo
tutawaonyesha vitendo vyao. Kwani Sisi tumezunguka kwa kuvijua viliomo ndani ya
nafsi zao, seuze vitendo vyao vya dhaahiri.
24. Tunawastarehesha kwa
muda mchache katika dunia yao, kisha tutawalazimisha kwenda kwenye adhabu kali
isiyo stahimilika.
25. Ewe Nabii! Nakuapia
ya kuwa ukiwauliza: Nani aliye umba mbingu na ardhi? Hapana shaka watasema: Ni
Mwenyezi Mungu. Sema: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, aliye ziweka dalili
za Upweke wake hata zikaubomoa ushirikina wao wa kumshirikisha na wenginewe
katika ibada. Na lakini wengi wao hawajui ya kuwa kwa kukiri kwao huku, basi
wamesimamisha hoja ya kuwapinga wenyewe kwa ubovu wa itikadi yao.
26. Viliomo katika mbingu
na ardhi ni vya Mwenyezi Mungu, kwa kuviumba, na kuvikadiria, na kuvipanga. Basi
vipi wao wanaacha kumuabudu Yeye? Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika si mhitaji wa
viumbe vyake wala ibada yao. Yeye ni Msifiwa kwa dhati yake. Ni mwenye kustahiki
kusifiwa na waja wake.
27. Na lau kuwa miti yote
ya duniani ikageuka kalamu, na maji yote ya baharini kwa wingi wake yakageuka
wino, kuandikia maneno ya Mwenyezi Mungu, basi zingeli kwisha kalamu na wino
ukamalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mwenyezi Mungu. Kwani hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye nguvu, hashindwi na chochote, Mwenye hikima hakimfutu kitu
katika ujuzi wake na hikima yake. Basi hayeshi maneno yake na hikima yake.
28. Kukuumbeni nyinyi
hapo mwanzo na kukufufueni baada ya kufa, mbele ya uweza wa Mwenyezi Mungu si
chochote ila ni kama kumuumba na kumfufua mtu mmoja tu. Hakika Mwenyezi Mungu
anaisikia kauli ya washirikina wanapo sema ati: Hakuna kufufuliwa. Naye ni
Mwenye kuviona vitendo vyao, naye atawalipa kwavyo.
29. Je! Huangalii, ewe
mwenye jukumu, kwa maangalio ya mwenye kuzingatia, ya kwamba hakika Mwenyezi
Mungu huupunguza wakati wa usiku kwa kadri ya anavyo uongeza mchana? Na
anaupunguza mchana kwa kadri ya anavyo uzidisha usiku? Naye amedhalilisha jua na
mwezi kwa ajili ya maslaha yenu, na amefanya hayo yafuate mpango wa peke yao.
Basi kila moja katika hayo huenda katika njia maalumu ya mbinguni wala haigeuki.
Na mwendo huo unaendelea mpaka Siku ya Kiyama. Na hakika Yeye, Subhanahu, anazo
khabari za yote myatendayo, na ni Mwenye kukulipeni kwayo.
30. Hayo yaliyo tajwa ni
katika ajabu za uundaji wa Mwenyezi Mungu na uweza wake, kwa sababu muundaji
wake ni Mungu aliye thibiti Ungu wake, Mwenye kustahiki peke yake kuabudiwa, na
kwamba miungu yote mnayo iabudu badala yake ni miungu ya uwongo. Na hakika
Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye Mtukufu wa shani, Mkubwa wa utawala.
31. Ewe mtu! Huzitazami
marikebu, vyombo vinavyo kwenda baharini kwa rehema ya Mwenyezi Mungu,
vikichukua ndani yake bidhaa za kukupeni manufaa, ili Mwenyezi Mungu
akuonyesheni baadhi ya maajabu ya uundaji wake, na dalili za uweza wake? Hakika
katika hayo zimo Ishara kwa kila mwenye kuvumilia mitihani yake, mwenye
kuzishukuru kwa neema zake.
32. Hawa makafiri wanao
mkataa Mwenyezi Mungu wakipanda marikebu, na bahari ikawachafukia, na mawimbi
yakaja juu mpaka wakaona yatawafunika, na wakawa yakini watazama bila ya muhali,
humkimbilia Mwenyezi Mungu, wakimwomba kwa ikhlasi na unyenyekevu, awaokoe. Basi
akisha waokoa wakafika nchi kavu wapo kati yao wachache wanao kumbuka ahadi yao,
na wakenda mwendo wa sawa. Na wapo kati yao, nao ndio wengi, walio sahau fadhila
za Mola wao Mlezi, na wakaendelea na kumkataa. Na wala hakatai fadhila za Mola
wake Mlezi na hisani yake ila kila mtu aliye mwingi wa ukhaini, aliye pita mpaka
kumkanya Mola wake Mlezi.
33. Enyi watu! Fanyeni
aliyo kuamrisheni Mola wenu Mlezi, na wacheni aliyo kukatazeni. Na tahadharini
na adhabu yake ya Siku ya Kiyama, Siku ambayo kwamba mzazi hatamfaa mwanawe kwa
lolote, wala mwana hatamfaa mzazi wake kwa lolote. Hakika Siku hii ndiyo aliyo
iahidi Mwenyezi Mungu. Na ahadi yake ni ya kweli, hayendi kinyume. Basi
yasikupumbazeni mapambo ya dunia na uzuri wake, mkaacha kujitayarisha kwa ajili
ya Siku hiyo. Wala msikhadaike na uchochezi wa Shetani, ukakuachisheni
kumuelekea Mwenyezi Mungu na kumt'ii.
34. Hakika ujuzi wa Saa
ya Kiyama uko kwa Mwenyezi Mungu umethibiti. Basi hapana anaye ijua isipo kuwa
Yeye tu. Na Yeye huteremsha mvua kwa wakati wake alio uweka. Na anavijua viliomo
ndani ya matumbo ya uzazi, kama wanaume, au wanawake, hivyo viliomo vimetimia au
havikutimia mimba. Wala hapana mtu ajuaye, mwema na muovu, atapata nini kesho,
kama kheri au shari. Wala hapana mtu ajuaye pahala gani duniani itamfika ajali
yake ya kufa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye timia ujuzi wake na kuwa na
khabari ya kila kitu. Wala hapana yeyote awezae kujua siri yake.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani