1. Sura hii imeanzia kwa Aya hii ili
kufahamisha kwamba Qur'ani imetungwa kwa hizi hizi harufi wanazo zitamka
Waarabu kwa wepesi na kwa uwazi. Lakini wanao kanya wameshindwa kuleta mfano
wake. Nazo vile vile zinawazindua watu wasikilize na wanyamaze, na ziwapelekee
kuusadiki Utume wa Muhammad s.a.w.
Rudi kwenye
Sura
2,3. Waajemi waliwashinda Warumi katika
nchi ya karibu na Arabuni, nayo ni mipakani mwa Shamu. Nao Warumi baada ya
kushindwa kwao watakuja washinda Waajemi...
Rudi kwenye
Sura
4,5... kabla ya kupita miaka tisa. Na
washirikina walifurahi kwa kushinda Waajemi, na wakawaambia Waislamu:
Tutakushindeni kama Uajemi ilivyo ushinda Urumi ambayo ni katika Watu wa Kitabu.
Lakini Mwenyezi Mungu alitimiza ahadi yake, Warumi wakawashinda Waajemi kwa muda
ule ule alio utaja. Ikawa ile ni Ishara ya ukweli wa Muhammad s.a.w. katika wito
wake, na ukweli wa aliyo yaleta. Ni ya Mwenyezi Mungu amri na hukumu kabla ya
kila kitu na baada ya kila kitu. Na siku ya Warumi kuwashinda Waajemi watafurahi
Waumini kwa ajili ya ushindi wa Mwenyezi Mungu anao mpa amtakaye. Na Yeye ndiye
Mwenye kuwashinda maadui zake, Mwenye kuwarehemu vipenzi vyake.
Maoni ya wataalamu juu ya Aya 1-4:
Katika Aya hizi tukufu ipo
ishara ya vituko viwili. Cha kwanza kilikwisha tokea khasa. Na cha
pili kilikuwa bado hakijatokea, na hayo ni kutoa khabari ya ghaibu. (Na imetajwa
kuwa yatatokea mnamo miaka michache, ambayo maana yake ni mitatu mpaka
tisa.)
Na maelezo ya tukio la mwanzo ni kuwa Waajemi na Warumi
walipambana kwa vita katika nchi ya Shamu katika enzi za Khasro Abrawiz, au
Khasro wa Pili, Mfalme wa Uajemi, maarufu kwa Waarabu kwa jina la Kisra,
na Heraklius Mdogo, Mfalme wa Wafalme wa Kirumi, ambaye kwa Waarabu ni maarufu
kwa jina la Heraklu. Katika mwaka 614 Uajemi iliiteka Antiokia, mji mkubwa
kabisa katika jimbo la Mashariki katika Ufalme wa Rumi, na baadae ikatekwa
Dimishqi (Damask), na ukazingwa mji wa Baitul Muqaddas (Yerusalemu) mpaka
ukasalimu amri. Wakauunguza, wakawaingilia wakaazi wake kuwachinja. Moto huo
uliteketeza Kanisa la Kiyama. Wavamizi hao waliuchukua Msalaba wakaupeleka
kwenye jiji lao. Nyoyo za Wakristo zilihuzunika sana kwa msiba huu wa kutisha.
Ilivyo kuwa kushindwa huku kuliwaletea furaha washirikina wa Makka na wakawa
wanawafanyia tashtiti Waislamu kwa kuwa Warumi ni Watu wa Kitabu kama watu wa
Muhammad s.a.w., na Waajemi kama washirikina si Watu wa Kitabu, basi Mwenyezi
Mungu Mtukufu aliye tukuka alimteremshia Muhammad Aya hizi zilizo wazi ili
ambashirie kuwa Watu wa Kitabu watakuja shinda, nao Waumini watafurahi. Na
kushindwa kwa washirikina na uovu wa khatima yao kuliwekewa kiwango cha miaka
michache.
Na ufafanuzi wa tukio la pili ni kuwa Heraklu, Kaisari wa
Rumi, ambaye jeshi lake lilishindwa, hakukata tamaa kuwa atashinda. Akawa
anajiandaa kwa ajili ya mpambano utakao futa ari ya kushindwa. Mpaka mwaka wa
622 wa kuzaliwa Nabii Isa a.s. , yaani mwaka wa kwanza wa Hijra Waajemi
wakalazimika kuingia vita katika nchi ya Arminia. Huko Warumi wakashinda. Na
ikawa hapo ndio chanzo cha ushindi mara nyingi wa Rumi kuishinda Uajemi. Ndio
hivi Watu wa Kitabu wakawashinda washirikina, na ukweli wa bishara ya Qur'ani
ukathibiti.
Na tena kituko cha tatu kinafahamika kwa maana kutokana
na Aya hizi tukufu, nacho kikaleta furaha kwa Waislamu. Nacho ni kushinda kwao
kuwashinda washirikina Makureshi katika Vita vya Badri vilivyo tokea siku ya
Ijumaa, 17 Ramadhani mwaka wa pili wa Hijra, yaani mwaka 623 wa kuzaliwa Nabii
Isa a.s.
6. Mwenyezi Mungu ameagana na Waumini kwa agano
la kweli. Na Mwenyezi Mungu havunji agano lake. Lakini makafiri, wanao kataa, si
ada yao kujua mambo hakika yalivyo.
7. Wanajua mambo na njia za kuamirisha na
kustarehe na mapambo yake, na hali wao wamepita mpaka katika ujinga na
kughafilika kujitengenezea Akhera yao.
8. Yamefutwa macho yao na nyoyo zao, na hivyo
hawajifikirii mambo yaliyo khusiana na roho zao wakaujua mwisho wao. Mwenyezi
Mungu hakuziumba mbingu na ardhi na nyota na vinginevyo viliomo baina yao ila
kwa kweli kweli, si mchezo, na kwa wakati ulio wekewa kiwango chake maalumu
kitakacho kwisha. Na hakika wengi wa watu wanakataa kuwa watakuja kukutana na
Mwenyezi Mungu, na kwamba itakuwapo Saa ya Kiyama.
9. Wao wameshikilia kukaa katika nchi zao tu,
wala hawendi kote kote duniani wapate kushuhudia ulikuwaje mwisho wa walio
kufuru wa kabla yao. Hao walikuwa na nguvu zaidi kuliko hawa makafiri wa sasa,
na wakaugeuza uso wa ardhi wapate kutoa humo viliomo ndani yake, kama maji, na
maadeni, na makulima. Na wakaiamirisha ardhi zaidi kuliko walivyo amirisha hawa.
Na Mitume wa Mwenyezi Mungu wakawajia na miujiza iliyo wazi, na wao wakaikataa.
Mwenyezi Mungu akawatia mkononi, kwani Yeye hawalipi bila ya makosa, wala
hawashiki kabla ya kuwakumbusha na kuwapa muhula. Lakini watu hawakuwa
wanadhulumu ila nafsi zao tu.
10. Tena mwisho wa hao watu walio tenda hadi ya
uovu ni kuzikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazidharau khasa.
11. Mwenyezi Mungu, aliye takasika na kutukuka,
huanzisha uumbaji wa binaadamu tangu mwanzo. Kisha hurejea tena kuwaumba baada
ya kwisha kufa kwao. Tena hao wote wanarejea kwake Yeye peke yake kwa ajili ya
hisabu na malipo.
12. Na kikifika Kiyama makafiri watakata tamaa
ya kuweza kujitetea nafsi zao.
13. Na wala hawapatikani waombezi kutokana na
hao walio waabudu badala ya Mwenyezi Mungu na kwa sababu yao wakawa ni makafiri
duniani.
14. Na itapo simama Saa, yaani Siku ya Kiyama,
kila kikundi kitaendea kwenye ajali yake ya milele.
15. Ama walio amini, na wakaambatisha Imani yao
na vitendo vyema, basi hao watakuwa katika Bustani yenye miti na mauwa,
watafurahi na wataneemeka.
16. Ama wale walio kufuru, na wakazikataa Ishara
zetu na mkutano wa kufufuliwa na kuhisabiwa, basi hao watakuwa wanaishi katika
adhabu, wala hawatoki humo.
17. Basi mtakaseni Mwenyezi Mungu na kila
ambacho hakimuelekei kwa utukufu wake na ukamilifu wake. Na muabuduni Yeye mnapo
ingia jioni na mnapo ingia asubuhi.
18. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye
kustahiki kuhimidiwa na kusifiwa na kushukuriwa na walioko katika mbingu na
katika ardhi. Basi mhimidini na mumuabudu wakati wa alasiri na mnapo ingia
adhuhuri.
19. Yeye hutoa kiumbe kihai kutokana na kitu
kisicho kuwa na uhai. Na hukitoa kitu kisicho kuwa na uhai kutokana na kitu
chenye uhai. Na huihuisha ardhi kwa mimea baada ya kuwa ni kavu tupu. Na mfano
wa anavyo fanya hivi basi ndivyo hivyo Mwenyezi Mungu atakutoeni makaburini
mwenu.
20. Na katika dalili za kuonyesha ukamilifu wa
uweza wake ni kuwa ameumba asili yenu kutokana na udongo usio kuwa na uhai.
Kisha nyinyi mmekuwa watu mlio tawanyika katika ardhi kwa ajili ya kutafuta
kitacho kuleteeni kubaki kwenu.
21. Na katika dalili za rehema yake ni kuwa
kakuumbieni, enyi wanaume, wake wa jinsi yenu mkae nao kwa uzuri na kituo. Na
amekujaalieni baina yenu na wao mapenzi na kuoneana huruma. Hakika katika haya
bila ya shaka zipo dalili kwa watu wanao ufikiria uumbaji wa Mwenyezi Mungu
Mtukufu.
22. Na katika dalili za kuonyesha uweza wake na
hikima yake ni uumbaji wa mbingu na ardhi kwa mpango huu wa namna peke yake
wenye kupendeza, na kukhitalifiana ndimi zenu katika lugha mbali mbali na lafdhi
mbali mbali, na kutafautiana rangi zenu katika weusi na weupe na nyenginezo.
Hakika katika haya bila ya shaka zipo dalili zinazo wanufaisha watu wenye ujuzi
na kufahamu.
23. Na katika Ishara zake zenye kuonyesha
ukamilifu wa uweza wake ni kuwa amekupeni sababu za mapumziko kwa kulala kwenu.
na akakusahilishieni kutafuta riziki usiku na mchana kutokana na fadhila zake
kunjufu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo dalili kwa watu wanao nafiika kwa
wanayo yasikia.
24. Na katika Ishara zake ni kuwa anakuonyesheni
umeme katika mawingu, muone khofu kwa radi na tamaa ya kupata mvua ya kuteremka
kutoka mbinguni ili ardhi ihuike baada ya kuyabisika. Hakika katika hayo bila ya
shaka zipo dalili kwa watu wanao zingatia mambo wakayafahamu kama ifaavyo.
25. Na katika dalili za ukamilifu wa uweza wake,
na hikima yake, na ukunjufu wa rehema yake, ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama
kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kama muonavyo, kwa mujibu wa hukumu za ufundi na
ustadi wa kupanga. Kisha akikuiteni kwa ajili ya kukufufueni mtatoka makaburini
mbio mbio kuitikia wito wake.
26. Na ni vyake Mwenyezi Mungu Subhanahu vyote
viliomo katika mbingu na ardhi, kwa kuviumba, na kuvimiliki, na kunyenyekea.
Vyote ni vyenye kumt'ii Mwenyezi Mungu.
27. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu aliye umba
viumbe vyote bila ya ruwaza, kisha atavirudisha tena baada ya mauti. Na
kurudisha kwake ni jambo jepesi zaidi kuliko kuvizua mwanzo, kwa mujibu wa
nadhari ya vipimo vyenu na itikadi yenu, kwamba kukirudisha kitu ni sahala
kuliko kukizua. Na Mwenyezi Mungu ana sifa ya kutangulia ya shani ya namna ya
pekee katika uweza ulio kamilika, na hikima iliyo timia, katika mbingu na ardhi.
Na Yeye ni Mwenye kushinda katika ufalme wake, Mwenye hikima katika vitendo
vyake na kukadiria kwake.
28. Mwenyezi Mungu amekupigieni mfano unao
tokana na nafsi zenu - na Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwenye kutukuka amempigia mfano
huo huyo aliye wafanya viumbe ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Mfano wenyewe ni:
Kwani nyinyi mnawafanya watumwa wenu washirika katika mali na vyenginevyo
tulivyo kupeni? Basi, je! Nyinyi na wao ni sawasawa katika hayo, mnawaogopa hao
watumwa wenu, na hamfanyi kitu kwa mnavyo miliki bila ya ruhusa yao, kama
wanavyo ogopana waungwana wao kwa wao? Ikiwa nyinyi hamyatii akilini haya wala
hamyafanyi, basi imekuwaje hata mnavifanya baadhi ya alivyo vimiliki Mwenyezi
Mungu kuwa ni washirika wake? Kwa ufafanuzi kama huu tunawabainishia Aya watu
ambao wanazingatia mifano inayo pigwa.
29. Bali walio kufuru wanafuata pumbao zao bila
ya kujua matokeo ya kufuru zao. Basi hapana yeyote aliye achiliwa na Mwenyezi
Mungu kupotoka, atakaye ongoka. Wala hapana ataye waombea, na akawalinda na
adhabu.
30. Basi elekeza uso wako, na uelekee kwenye
Dini mbali na upotovu wao. Na shikamana na maumbile ya Mwenyezi Mungu aliyo
waumbia watu. Nayo ni kuwa wao ni wenye kuikubali Tawhidi, Imani ya Mwenyezi
Mungu Mmoja, wala si wenye kuikataa. Na haitakikani kuigeuza khulka hii. Huko
ndio kuumbwa juu ya Tawhidi, nayo ndiyo Dini Iliyo Nyooka sawasawa. Lakini
washirikina hawaujui ukweli huo.
31. Kuweni wenye kurejea kwake kwa kutubu! Na
tendeni aliyo kuamrisheni, na acheni aliyo kukatazeni. Na hifadhini Sala, wala
msiwe katika wenye kumuabudu mwenginewe pamoja na Mwenyezi Mungu.
32. Katika walio igawanya dini yao, wakawa
makundi mbali mbali, kila kikundi kinawania upande wake, na kila fungu miongoni
mwao linafurahia kwa waliyo nayo, wanajidhania kuwa wao tu ndio wako katika
haki.
33. Na watu yakiwapata madhara, ya ugonjwa au
shida yoyote, humkimbilia Mwenyezi Mungu, na wakamwomba nao wamerejea kwake,
wakitaka waondolewe hiyo shida. Kisha akiwaonjesha kuondokewa na hiyo shida, na
akawapa sehemu ya fadhila yake, baadhi yao hukimbilia mbio kwendea kumshirikisha
Mola wao Mlezi.
34. Upate kuwa mwisho wa mambo yao kuzikanya
neema za Mwenyezi Mungu alizo wapa. Basi enyi makafiri mnao kataa! Stareheni
kama mpendavyo. Mtakuja ujua mwisho wenu.
35. Kwani tuliwaacha katika upotovu wao, wala
hatukuwazindua na ndoto zao, bali tukawateremshia hoja ya kushuhudia kwa yale
walio kuwa wakiyashirikisha na Mwenyezi Mungu?
36. Na tukiwaonjesha watu neema huifurahia kwa
furaha ya kuwatia kiburi. Na ikiwapata shida kwa madhambi waliyo yachuma wenyewe
huwa wepesi wa kukata tamaa na Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema.
37. Je! Wameingiwa na ujinga hata hawajui nini
kinacho fikisha kwenye Imani? Wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia
riziki amtakaye, na humdhikisha amtakaye, kwa mujibu inavyo wafikiana na hikima
yake? Hakika katika hayo zipo dalili wazi kwa watu wanao iamini Haki.
38. Na ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye
anaye kunjua riziki na akaidhikisha, basi mpe aliye jamaa haki yake kwa ajili ya
hisani na kuunga udugu. Na mhitaji na aliye katikiwa safari yake wape pia haki
zao kutokana na Zaka na Sadaka. Hayo ndiyo ya kheri kwa wenye kutaka radhi ya
Mwenyezi Mungu, na wanataka thawabu zake. Na hao ndio wenye kufuzu kuipata neema
ya milele.
39. Na mnacho toa, enyi wala riba, katika mali
ili yakuzidieni kutokana na mali yao, basi kwa Mwenyezi Mungu hakizidi wala
hakiingii baraka. Na mnacho toa sadaka kwa kutafuta wajihi wa Mwenyezi Mungu,
bila ya riya, kujionyesha tu, wala tamaa ya kulipwa - basi hao ndio watakao pewa
malipo mema marudufu.
40. Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Aliye takasika,
ndiye aliye kuumbeni. Kisha akakupeni cha kukupeni maisha. Kisha ndiye anaye
kufisheni; na kisha atakufufueni kutoka makaburini kwenu. Je! Yupo yeyote katika
hao miungu wa kishirikina mnao dai, na mkawaabudu badala ya Mwenyezi Mungu,
mwenye kutenda hayo, ya kuumba, na kuruzuku, na kufisha, na kufufua, au kitendo
chochote? Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mshirikisha
naye.
41. Kumetokea moto, na ukame, na kila maafa, na
kuharibika biashara, na mafuriko, kwa sababu ya uovu na madhambi, ili Mwenyezi
Mungu awaadhibu watu duniani kwa baadhi ya vitendo vyao, huenda labda wakatubia
maasi yao.
42. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Nendeni
pande mbali mbali za dunia, muangalie vipi waliishia walio kutangulieni? Mtaona
kuwa Mwenyezi Mungu aliwaangamiza na akayaharibu majumba yao, kwa sababu wengi
walikuwa washirikina kama nyinyi.
43. Na uelekeze sawa sawa uso wako kwenye Dini
iliyo kamilika kunyooka kwake, kabla haijafika Siku ambayo hapana mtu
atakaye weza kuirejesha kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watagawanyika, na
hali zao zitakhitalifiana.
44. Mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu, basi
itampata mwenyewe laana ya ukafiri wake. Na wenye kuamini na wakatenda mema basi
ni kwa ajili ya nafsi zao tu, wanajitengenezea njia nzuri iliyo nyooka.
45. Kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu huwalipa
walio amini na wakatenda mema kwa yale waliyo yatanguliza. Na tena huwazidishia
malipo yao kwa kuwafadhili. Kwani Yeye anawapenda hao na anawachukia walio
kufuru na wakazikanya neema zake.
46. Na katika dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu
na rehema yake ni kuwa Yeye huzipeleka pepo za kubashiria mvua kwa sababu ya
kumwagia mashambani na kunyweshea wanyama na watu. Na ili akupeni katika
kukumimieni hisani zake manufaa yanayo tokana na mvua, na ili zipate kwenda
marikebu za majini kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kudra yake, na ili mtafute
riziki kwa fadhila yake kwa biashara na kutumia viliomo nchi kavu na baharini,
na ili mpate kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ut'iifu wenu na kumuabudu Yeye tu.
47. Na kabla yako hakika tulikwisha watuma
Mitume kwa kaumu zao. Na kila Mtume alikuja na hoja zilizo wazi, zenye kuonyesha
ukweli wake. Kaumu yake ikamkadhibisha. Nasi, basi, tukawaangamiza wale walio
fanya madhambi na wakaasi. Na Mwenyezi Mungu amejilazimisha nafsi yake
kuwanusuru waja wake Waumini.
48. Mwenyezi Mungu, Subhanahu Wataa'la, Aliye
takasika na akatukuka, ndiye anaye zituma pepo ambazo kwa nguvu zake
zikayasukuma mawingu. Na Mwenyezi Mungu akayatandaza mbinguni kama atakavyo hapa
na kule, kwa uchache au wingi. Na akayafanya mapande mapande. Basi nawe ndio
unaona mvua inatoka kwenye mawingu. Na Mwenyezi Mungu anapo iteremsha mvua kwa
waja wake awatakao, hao huwa wepesi kukunjuka roho na kufurahi.
Rejea
kwenye maelezo ya Aya ya 43 ya Sura An-Nur.
49. Nao hakika kabla ya kunyweshewa na mvua hiyo
walikuwa wamekwisha kata tamaa na wamedawaa.
50. Basi iangalie mvua, muangalio wa kufikiri na
kuzingatia, vipi Mwenyezi Mungu anavyo ihuisha ardhi baada ya kuwa imetulia kama
maiti. Hakika aliye ihuisha ardhi baada ya kufa kwake bila ya shaka ni Muweza wa
kuwahuisha watu. Na Yeye ni mtimilivu wa uweza, hashindwi na kitu.
51. Nami ninaapa! Lau kuwa tukiwapelekea upepo
wa kudhuru mimea, nao wakauona umekuwa manjano kwa sababu yake, hapana shaka
wataendelea hata baada ya kuwa manjano, wakizikanya neema, na wakimkataa
Mwenyezi Mungu.
52. Basi wewe usihuzunike kwa inadi yao na kuto
kukuitikia. Kwani wewe huwezi kuwafanya maiti wausikie wito wako; wala kuwafanya
viziwi wakusikie unapo wanadia, wakizidi uziwi wao kwa wanavyo kukimbia kwa
mapuuza.
53. Na watu hawa ni kama vipofu, kwa vile nyoyo
zao zimefungika hawafuati uwongofu. Na wewe huwezi kuwaongoa vipofu, na
ukawazuia wasifanye ukafiri wao. Ama hakika wewe unaweza kuwafanya wakusikie
msikio wa kufahamu na kukubali wale ambao nyoyo zao zimejitayarisha kupokea
Imani. Basi hao wanaifuata Haki inapo dhihiri.
54. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana
na tone la manii, mkawa dhaifu, hamna nguvu. Kisha akakujaalieni baada ya
unyonge huo mkawa na nguvu. Akakukuzeni hata mkawa watu wazima. Kisha
akakufanyeni baada ya nguvu hizi mkawa na udhaifu wa uzee na ukongwe. Yeye
huumba atakavyo. Na Yeye ndiye Mjuzi wa kupanga uumbaji wake, Muweza wa kuleta
atakacho.
55. Na Siku itapo fika Saa ya Kiyama makafiri
wataapa kwamba hawakukaa duniani au makaburini mwao isipo kuwa kwa muda wa saa
moja tu. Na mfano wa mwendo kama huo ndivyo Mashetani walikuwa wakiwaendesha
duniani, kuwaachisha Haki na kuwapeleka kwenye upotovu.
56. Na walio pewa ujuzi na Mwenyezi Mungu, nao
ni Manabii, na Malaika, na Waumini, watasema: Bila ya shaka nyinyi mlikwisha kaa
katika hukumu ya Mwenyezi Mungu na amri yake mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii
ndiyo Siku ya kufufuliwa mlio ikanya. Na lakini nyinyi duniani mlikuwa hamjui
kama hii ni Haki, kwa ujinga wenu na mapuuza yenu.
57. Basi Siku hiyo watafufuliwa watu.
Hakutowafaa kitu makafiri kutoa udhuru wao kwa kukanya kwao na kuwakadhibisha
kwao Mitume wao. Wala hatawataka mtu yeyote wafanye jambo la kumridhi Mwenyezi
Mungu. Kwa kuwa wao wamekwisha dharaulika mbele yake, na wamefukuzwa kutokana na
rehema yake.
58. Na kwa ajili ya uwongofu wa watu,
tumebainisha katika Qur'ani hii kila mfano wa kuwaongoza kwenye Njia ya
Uwongofu. Na wewe ukiwaletea kila muujiza bila ya shaka makafiri, kwa kupita
hadi inda yao na ugumu wa nyoyo zao, watasema: Wewe na hao wanao
kufuata si chochote ila ni waongo tu katika huo wito wenu.
59. Na muhuri kama huu umepigwa juu ya nyoyo za
hao wasio ijua Tawhidi miongoni mwa majaahili.
60. Ewe Nabii, yavumilie
maudhi yao. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu kukupa ushindi juu ya maadui wako, na
kushinda kwa Uislamu juu ya dini zote, ni kweli isiyo geuka kabisa. Wala wasio
muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wasikuletee dhiki na ukaiacha subira.