1. T'aa Siin,
(T' na S) harufi mbili za kutamkwa, ni harufi za alifbete, ndizo zimeanzia Sura
hii, ili kunabihisha siri ya muujiza wa Qur'ani pamoja na kuashiria kuwa
imeundwa kwa jinsi ya harufi hizi hizi mnazo zitumia katika kusema, na pia
kuzindua akili ziisikilize hii Qur'ani inapo somwa. Hizi Aya zilizo teremka kwa
kusomwa, na ni Kitabu chenye kubainisha mambo yaliyo kuja ndani yake.
2. Na hii
Qur'ani ni Uwongofu wa kuwaahidi Waumini waifuate njia ya kheri, na kufuzu
duniani na Akhera, na inawabashiria kuwa watapata malipo mazuri.
3. Waumini hao
ndio wanao ishika Sala kwa unyenyekevu na kutimiliza nguzo, na wanatoa Zaka kwa
nyakati zake, nao wana yakini ya maisha ya baadaye Akhera, na yatayo kuwa huko
ya adhabu na thawabu.
4. Hakika wale
ambao hawaiamini Akhera, Sisi tumewapambia vitendo vyao kwa kuwaumbia matamanio
ndani yake. Kwa hivyo wao wanababaika humo katika upotovu wao.
5. Hao ndio
watapata adhabu mbaya kabisa, na Akhera ndio watakuwa khasarani kushinda wote.
6. Ewe Nabii!
Wewe unapokea Qur'ani hii unayo teremshiwa kutokana na Yeye ambaye hapana anaye
mkaribia kwa hikima yake, naye anajua kila kitu.
7. Kumbuka pale
Musa alipo mwambia mkewe na walio pamoja naye na yeye ndio anarejea Misri: Mimi
nimeona moto. Nitakwenda kuleteeni khabari ya njia, au nitapata kijinga cha
moto, kitacho kufaeni kwa kuota moto kwa hii baridi.
8. Alipo fika
huko paliitwa: Wamebarikiwa waliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake,
yaani karibu yake. Nao ni Malaika na Musa. Na Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa
walimwengu wote ametakasika na kila kisicho kuwa laiki naye.
9. Ewe Musa!
Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mwenye kustahiki kuabudiwa pekee, Mwenye kushinda
kila kitu, Mwenye kuweka kila kitu pahala pake.
10. Na katika
njia ya kufikisha wito wako, tupa fimbo yako na utaiona inatikisika kama kijoka
jepesi kinakwenda mbio. Yeye akarudi nyuma, wala hakurejea baada ya kurudi
nyuma. Mwenyezi Mungu Mtukufu akamtuza kwa kauli yake: Usiogope. Mbele yangu
hawaogopi. Mitume ninapo sema nao. Kisa cha Musa kimetajwa zaidi ya mara moja
katika Qur'ani. Pengine hutolewa yasiyo tajwa penginepo. Na kila sehemu ina
mnasaba wake. Katika sehemu hii makusudio ni kuondoa yale mastaajabu ya kuwa
Nabii Muhammad s.a.w. kapata Ufunuoa (Wahyi) vile vile.
11. Lakini
mwenye kutenda asicho ruhusiwa, na kisha akaleta wema baada ya kuteleza kwake,
basi Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mkubwa wa kurehemu.
12. Na utie
mkono wako katika mfuko wa nguo zako, utatoka mweupe wala si kwa balanga. Hayo
ni katika Ishara tisa (1) za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika hao
walikuwa watu walio tokana na amri ya Mwenyezi Mungu, ni makafiri. (1) Hizo
Ishara tisa ni:- Kupasuka bahari, T'ufani (Kimbunga), Nzige, Chawa, Vyura, Damu,
Ukame, Fimbo, Kutoka mkono mweupe bila ya maradhi.
13. Ilipo kuja
miujiza hii kwa uwazi na dhaahiri wakasema: Huu ni uchawi wazi!
14.
Wakaikadhibisha miujiza wakikataa kuwa inaonyesha dalili ya Utume. Na hakika
yakini ilikwisha waingia katika nyoyo zao, lakini hawakusalimu amri kwa kuwa
walikwisha tangaza kufuata upotovu na kushika uasi. Basi ewe Nabii! Hebu angalia
vipi yalikuwa matokeo ya walio shikilia ufisadi, wakaikanya miujiza nayo iko
wazi.
15. Hizo ndizo
jeuri za Firauni kwa sababu ya ufalme wake. Hebu sasa angalia utawala muadilifu,
utawala wa hukumu, utawala wa unabii wa Daudi na mwanawe, Sulaiman, Mwenyezi
Mungu awape amani. Sisi tuliwapa ilimu nyingi za sharia na mazoezi ya kuhukumu.
Wakasimamisha uadilifu, na wakamhimidi Mwenyezi Mungu aliye wapa fadhila
kushinda wengi katika waja wake wenye kusadiki, na kuifuata Haki.
16. Ufalme na
hukumu ukatoka kwa Daudi ukenda kwa mwanawe, Sulaiman; naye akasema: Enyi watu!
Sisi tumefunzwa lugha ya ndege, na tumepewa mengi tunayo yahitajia katika
utawala wetu. Hakika neema hizi ni fadhila iliyo wazi aliyo tukhusisha sisi
Mwenyezi Mungu, "Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa
usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri."
Sulaiman a.s. ni mwana wa Daudi, naye ni Nabii na Mfalme kama yeye. Aliishi
mnamo mwaka 974 mpaka 937 K.K. (yaani Kabla ya Kuzaliwa Nabii Isa). Mwenyezi
Mungu alimjaalia kumjuvya kufahamu maneno ya ndege. Uchunguzi wa kisasa
umeonyesha kwamba kila namna ya ndege wana njia zao za kufahamiana wao kwa wao.
Katika njia hizo ni kwa kugusa, na sauti, na ishara.
17. Na Sulaiman
alikusanya majeshi yake ya majini, watu, na ndege, kwenye uwanja mmoja. Na wao
wakawa jeshi moja lenye nidhamu kwa vile kudhibitiwa wa mwanzo mpaka mwisho.
18. Hata walipo
fika kwenye bonde la wadudu chungu, mdudu chungu mmoja akasema: Enyi wadudu
chungu! Ingieni vishimoni mwenu, asije Sulaiman na askari wake wakakuuweni na
wao wala hawahisi kuwa nyinyi mpo. "Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu
chungu, alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu,
asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua." Inafahamikana wazi
katika Aya hii kuwa wadudu chungu wanaishi kwa makundi, yaani wana umoja, na
moja katika sifa zao ni kuwa macho na kutahadhari. Na inajuulikana tangu zamani
kuwa wadudu chungu wana sifa kadhaa wa kadhaa makhsusi ambazo zinaonyesha kuwa
wana umoja wenye nidhamu madhubuti katika hukumu, na wana kiasi kikubwa cha
akili, na werevu, na nguvu za kukumbuka, na kupenda kazi na kukakamia, na juhudi
isiyo jua kunyong'onyea wala kukata tamaa. Kama wanavyo juulikana kuwa wana
wingi wa hila za kuendesha kazi zao. Na dalili ya hayo ni kuwa jamaa wa wadudu
chungu ni peke yao baada ya binaadamu ndio wanao zika maiti wao. Na makundi
mbali mbali yao yanashughulikia kukutana pahala pamoja kwa nyakati maalumu. Kwa
ajili ya hayo zimewekwa siku makhsusi za kusimamisha soko wanapo kusanyika
makundi yote kwa kubadilishana bidhaa na kujuana. Na makundi haya yanapo kutana
hutokea mazungumzo kwa hima kubwa, na huulizana masuala yaliyo khusiana na mambo
yao. Katika yanayo onekana yaliyo fungamana na mikusanyiko hiyo ni kuzuka
mashauri yaliyo khusu umma wao, kama kutengeneza barabara ndefu, kwa subira na
kukakamia kunako staajabisha. Wala makundi haya hayatosheki na kufanya kazi
mchana tu, bali huendeleza kazi zao katika masiku ya mbaamwezi; ama masiku ya
kiza hubaki mwahala mwao. Na jamaa wa makundi haya wana njia za pekee za
kukusanya na kubeba na kuhifadhi vifaa vyao vya kula. Akishindwa mdudu kuchukua
chakula alicho kikusanya kwa mdomo wake hukisukuma kwa miguu yake ya nyuma, na
akakinyanyua kwa mikono yake. Na katika mtindo wao ni kuzing'ong'ona mbegu, na
kuzipasua baadhi ya nafaka kabla ya kuzirindika ili zisije kuchipua. Na mbegu
kubwa kubwa huzigawa vipande vipande ili iwe wepesi kuziingiza katika ghala zao.
Na pindi zikiroana kwa mvua huzitoa zipate upepo na jua zikauke.
19. Sulaiman
akatabasamu akicheka kwa ile kauli ya mdudu chungu yenye kushughulikia maslaha
yao, na akahisi neema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyo juu yake. Akasema: Ewe
Uliye niumba! Nijaalie niwe na shukrani kwako kwa neema ulizo nineemesha mimi na
wazazi wangu, na niwezeshe nitende vitendo vyema unavyo viridhia, na unitie
kwenye rehema yako iliyo timia.
20. Akalikagua
jeshi lake la ndege asimwone Hud-hud. Akastaajabu, akasema: Mbona simwoni
Hud-hud! Yupo hapa na mimi simwoni, au ameghibu hayupo miongoni mwetu?
21. Wallahi!
Nitampatisha adhabu kali ya kumshikisha adabu, au nitamchinja ikiwa kosa lake ni
kubwa! Ila aniletee hoja madhubuti ya kumtoa makosani kwa kuto kuwepo mbele
yangu.
22. Na Hud-hud
alikuwa kakaa si pahala mbali kwa muda usio kuwa mrefu. Kisha akamjia Sulaiman,
akamwambia: Nimejua jambo ulilo kuwa wewe hujalijua, na nimekujia kutoka nchi ya
Sabai na khabari muhimu sana, nayo ni ya kweli kwa yakini. "Basi hakukaa mbali,
na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya
Sabai, na nakuletea khabari za yakini. Hakika mimi nimemkuta mwanamke
anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.Nimemkuta
yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na Shetani
amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo hawakuongoka." Hizi
ndizo Aya khasa zilizo khusu Ufalme wa Sabai. Na hii Sabai ni moja katika falme
za kusini ya Arabuni, inayo itwa Yaman, na ambayo zamani ilikuwa ni maarufu kwa
jina la "Arabia Iliyo Neemeka". Na jina hili la mwisho linaonyesha maendeleo
yake na utajiri wake. Kwani kwa hakika ilikuwa nchi hiyo ina ustaarabu wa juu
tangu miaka elfu mbili kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s. Ikitegemea makulima, kwa
sababu ya rutuba ya ardhi yake, na uzuri wa hali yake ya hewa. Na pia ikitegemea
biashara kwa kuwa ipo kati baina ya Bara Hindi, na Uhabeshi, na Somalia, na
Sham, na Iraq. Na kwa hakika mahodhi yaliyo jengwa kuwekea maji na kuyatumia, na
maarufu yao yote ni Hodhi Maa'rib (Tazama Aya 16 Surat Sabai) na miji iliyo
jengewa ngome, na makasri, na mahekalu, yanashuhudia mpaka hii leo maendeleo ya
kijamii ya utajiri ulio kuwako katika nchi hii. Na hakika nakshi walizo
zinakishi watawala wao, na baina ya nakshi hizo zipo kanuni za kuendesha mambo
ya ujenzi na mengineyo, yanaonyesha kwa kila dalili ukomo wa ustaarabu ulio
nawiri walio ufikilia. Na huu ufalme wa Sabai ambao ulifikilia kilele cha
kustawi kwake katika siku za Sulaiman a.s. kiasi ya karne kumi kabla ya kuzaliwa
Nabii Isa a.s. ulikuwa ni ufalme kama wa kabla yake, yaani watoto wakiwarithi
baba zao. Na kwa hivyo alikuwa akihukumu wakati wa Sulaiman a.s. Malkia.
Wataalamu wa taarikhi wamekhitalifiana juu ya jina la Malkia huyo. Waarabu
wakimwita Balqiis; akisaidiwa na wazee wahishimiwa kama ni Baraza la Mashauri
lake. (Tazama Aya 28-33 katika Surat An-naml.) Wala haikuthibitisha taarikh
(historia) kuwa Ufalme wa Sabai ulikuwa dola ya kuteka nchi, bali ulikuwa ufalme
wa biashara, na misafara. Katika mabaki yake hatuoni kutajwa vita au kuteka nchi
isipo kuwa kwa uchache. Na haya ni kuwa umuhimu wa majeshi yake ulikuwa ni
kuhifadhi ngome zake na kuzihami, na kulinda misafara yake kwa aghlabu. Na
wananchi wa Sabai walikuwa ni mapagani, makafiri, wakiliabudu jua, kama ilivyo
kuja katika Aya tukufu nambari 24 katika Sura hii. Pia wakiabudu mwezi. Na hao
ndio miungu yao muhimu kabisa. Na walikuwa wakiwatolea sadaka na wakifukiza
ubani katika mahekalu yao.
23. Hakika mimi
nimewaona watu wa Sabai wanatawaliwa na mwanamke, na amepewa kila kheri za
kidunia, naye ana kiti cha enzi kikubwa kinacho onyesha dalili ya utukufu wa
ufalme na nguvu za madaraka yake.
24. Nimemwona
yeye na watu wake wanaabudu jua, wala hawamuabudu Mwenyezi Mungu. Na Shetani
amewazainishia vitendo vyao na wenyewe wakaviona ni vizuri na hali ni viovu. Kwa
hivyo amewapoteza Njia ya Haki, basi hawakuongoka.
25.
Hawamsujudii Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye ndiye anayafichua yaliyo fichika
katika mbingu na ardhi, na anajua mnayo fanya kwa siri na kwa dhaahiri.
26. Mwenyezi
Mungu, ambaye hapana wa kuabudiwa kwa Haki isipo kuwa Yeye, ndiye Mwenye
madaraka makuu yasio na ukomo juu ya kila kiumbe.
27. Sulaiman
akasema kumwambia Hud-hud: Tutaichungua khabari yako hii tujue kwamba umesema
kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.
28. Nenda na
barua yangu hii umfikishie yeye na kaumu yake. Kisha jitenge nao ujifiche pahali
karibu, uangalie wanarejesheana maneno gani.
29. Barua
ikamfikia yule Malkia, naye basi akawakusanya wahishimiwa wa kaumu yake, na
halmashauri wake. Naye akasema: Enyi wahishimiwa! Mimi hakika imenifikilia barua
yenye shani kuu.
30. Kisha
akawasomea hiyo barua, nayo imeanzia kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu
na neema zote, ambaye daima anawamiminia waja wake rehema zake.
31. Msifanye
kiburi juu yangu, na nijieni nanyi mmet'ii na wanyenyekevu.
32. Akaiambia
baraza ya washauri wake: Nibainishieni lifaalo katika haya mambo muhimu nilio
wekewa mbele yangu. Kwani mimi sikati shauri juu ya jambo lolote mpaka muwe
nyinyi mmehudhuria.
33. Wakamwambia
nao wametua: Sisi ni watu wenye nguvu za mwili, na tuna moyo na mashujaa.
Hatuogopi vita. Basi angalia wewe jambo unalo taka kutuamrisha nasi ni wenye
kut'ii.
34. Akasema kwa
taratibu na kupendelea salama: Hakika watawala wakiingia katika miji mikubwa
pamoja na majeshi yao huifisidi, wakaondoa matengenezo yake, wakateketeza
makulima na roho, na wakawafanya walio watukufu katika watu wa hiyo miji kuwa
ndio madhalili, na huo ndio mtindo wao daima.
35. Na mimi kwa
kupendelea salama na uzima nitampelekea zawadi Sulaiman na kaumu yake, na
nitatazama wajumbe watarejea na nini - wataikubali zawadi au watairudisha?
36. Wajumbe
walifika kwa Sayyidina Sulaiman na zawadi zao. Huku anazijua neema za Mwenyezi
Mungu Mtukufu zilio juu yake, Akawaambia naye ndio anamsemeza huyo Malkia na
watu wake katika mkabala na wajumbe: Hivyo ndio mnanipa mimi mali? Aliyo nipa
Mwenyezi Mungu ya Unabii, na ufalme, na neema, ni makubwa zaidi kuliko aliyo
kupeni nyinyi. Bali nyinyi kwa hizi zawadi zenu na wingi wa mali yenu mnafurahi,
sio kama mimi. Kwa sababu nyinyi hamjui ila yaliyo shikamana na dunia hii tu.
37. Akasema,
akimsemeza yule msemaji kwa jina lao: Ewe mjumbe! Rejea kwao. Wallahi!
tutawatokea kwa majeshi wasio yaweza kupambana nayo na kuyakabili. Na tutawatoa
kwenye nchi ya Sabai nao wamepoteza utukufu wao, wamefanywa watumwa.
38. Sulaiman
akawaelekea binaadamu na majini aliyo dhalilishiwa na Mwenyezi Mungu kumtumikia,
akawashitua kwa jambo geni. Akasema: Ni nani katika nyinyi anaweza kuniletea
kiti chake cha enzi kikubwa kabla hawajanijia nao wamekwisha nyenyekea wanat'ii.
39. Mmoja
pandikizi la kijini lilisema: Mimi nitakuletea, na wewe umekaa katika baraza
yako hii, kabla hujaondoka. Na mimi hakika naweza hayo, na muaminifu katika
maneno yangu na vitendo vyangu.
40. Akasema
aliye pewa nguvu za kiroho, na ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea hicho kiti cha
enzi kabla jicho lako halijapepesa. Na akatimiza aliyo yasema. Sulaiman alipo
kiona kiti kile kimetua mbele yake bila ya mtingisiko, alisema: Haya ni katika
fadhila za Mwenyezi Mungu aliye niumba na akanipa kheri zake ili anifanyie
mtihani, nitashukuru kwa neema hizi au sitoi haki yake? Na mwenye kumshukuru
Mwenyezi Mungu basi huyo hakika amejiondolea nafsi yake mzigo wa waajibu. Na
mwenye kuacha kushukuru kwa neema basi hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi, si
mwenye kuhitajia shukrani. Naye ni Karimu wa kuneemesha.
41. Sulaiman
akawaambia watu wake: Kigeuzeni geuzeni hichi kiti cha enzi kwa baadhi ya
mabadiliko ya nje, tupate kuona atakijua kwa kukiendea au hato kijua na kwa
hivyo hato kiendea.
42. Alipo fika
jicho lake lilipiga kwenye kiti chake cha enzi. Akaambiwa: Je! Kiti chako cha
enzi ni mfano wa hiki? Akasema kwa vile kilivyo kamilika kufanana: Kama kwamba
ndicho hichi. Na Sulaiman na walio pamoja naye wakasema: Sisi tulisha pewa ujuzi
kumjua Mwenyezi Mungu na uwezo wake na ukweli wa yaliyo kuja kutoka kwake kama
anavyo jua mwanamke huyu. Na sisi tangu hapo ni watu tulio mfuata Mwenyezi Mungu
na tunamsafia Yeye ibada.
43. Na zile
ibada za jua na mfano wake zilimzuia yule Malkia kumuabudu Mwenyezi Mungu. Kwani
yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.
44. Baada ya
hao akaambiwa: Ingia katika jumba la Sulaiman. Na uwanja wake wa ndani ulikuwa
umesakafiwa kwa kiyoo, na chini yake maji, na samaki wakiogelea humo. Kupandisha
nguo miundi yake ya miguu ikaonekana, kwa kuwa alidhania ni maji. Sulaiman
akamwambia hicho ni kiyoo, basi yakamuathiri yale madhaahiri ya kilimwengu, na
akaona kuwa ufalme wake yeye haufai chochote mbele ya ufalme wa Nabii Sulaiman.
Akasema: Mola Mlezi! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu kwa kughurika na
ufalme wangu na ukafiri wangu. Na sasa ninanyenyekea pamoja na Sulaiman
kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye kuumba walimwengu wote na kuwalea na
kuwasimamia.
45. Na
tuliwapelekea Thamud ndugu yao Saleh kuwafunza wamuamini Mwenyezi Mungu pekee.
Wao wakakimbilia kugombana na kukhitalifiana. Wakawa makundi mawili. Moja lenye
kuamini, na moja la kikafiri.
46. Saleh
akasema nao kuwanasihi: Enyi watu! Mbona mnaihimiza adhabu mlio ahidiwa kabla ya
kutubu? Kwa nini hamwombi msamaha kwa Mola wenu Mlezi, mkamuamini Yeye kwa
kutaraji akurehemuni?
47. Wakasema:
Sisi tunakuona wewe na hao walio nawe ni wakorofi, ndio tukapatilizwa na ukame.
Yeye akasema: Sababu za kheri na shari zinazo kuteremkieni bila ya shaka yoyote
zinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Bali nyinyi ni watu mnao pewa mitihani ya neema na
nakama, ili mpate kuamini.
48. Na waongozi
wa shari kati yao walikuwa ni tisa, kazi yao ni kufisidi katika nchi kwa maoni
yao na madai yao. Wala haukuwa mtindo wao kutenda jema lolote.
49. Wale
washirikina wakaambizana wenyewe kwa wenyewe: Apishaneni kwa jina la Mwenyezi
Mungu, kwamba kwa yakini tutamshambulia yeye na ahali zake, na tutawauwa. Kisha
tutamwambia jamaa yao wa damu kwamba sisi hatukayaona mauwaji yake wala ya ahali
zake. Na hakika sisi ni wasema kweli kwa haya tuliyo yataja.
50. Walipanga
kumuuwa Saleh na ahali zake, na Mwenyezi Mungu nyuma yao kapanga kumwokoa Nabii
wake na ahali zake, na kuwateketeza wao, na hali wao hata hawatambui.
51. Ewe Nabii!
Hebu tazama vipi yalikuwa matokeo ya mipango yao na mipango yetu. Sisi
tuliwaangamiza wote hao wao na kaumu yao.
52. Na hebu
yatazame mabaki yao. Utakuta nyumba zao zimeanguka, zimevurugika, kwa sababu ya
udhalimu wao na kufru zao, na kumtakia shari Nabii wao. Hakika kwa walio fanyiwa
kina Thamud ipo Ishara kwa watu wanao ujua uwezo wetu na wakawaidhika.
53. Na Sisi
tukakiokoa kikundi kilicho muamini Saleh kutokana na hilaki hii, na wakawa wanao
gopa kuziacha amri zake.
54. Ewe Nabii!
Mtaje Lut'i na khabari zake pamoja na kaumu ya watendao uchafu, pale alipo
waambia: Je! Mnafanya dhambi hizi ambazo zimepita hadi ya uchafu na kinyume na
maumbile, na hali nyinyi mnaona na mnaangalia uovu wa haya mliyo yashikilia?
55. Hivyo
inaelekea katika nadhari ya akili zenu na maumbile kuwaingilia wanaume kwa
matamanio yenu, na mkwawacha wanawake? Ama kweli nyinyi mmesibiwa na upumbavu na
ujinga wa kufudikiza, hata imekuwa hamwezi tena kuteuwa baina ya kiovu na chema.
56. Haikuwa
jawabu ya watu wake alipo wakataza ila ni kusema: Mtoleeni mbali Lut'i na
wafwasi wake katika mji huu. Kwani wao wanajitakasa hawataki kushirikiana nasi
katika haya tuyatendayo.
57. Basi Sisi
tukamwokoa yeye na ahali zake na ile adhabu walio pelekewa wale watu, isipo kuwa
mkewe. Mwenyezi Mungu alimkadiria awe na walio baki nyuma ili apate kuangamia
kwa adhabu pamoja na makafiri.
58. Na Sisi
tukawanyeshea mvua hao mafisadi, mvua ya adhabu na nakama. Ilikuwa mvua ya
kuwahiliki walio onywa kuwa watapata adhabu chungu, na wala wasisikie.
59. Ewe Mtume!
Sema: Hakika mimi namhimidi Mwenyezi Mungu na namsifu Yeye peke yake. Na
namwomba Mwenyezi Mungu salama na maamkio kwa waja wake alio wateuwa kwa kuwapa
Ujumbe wake. Na ewe Mtume! Waambie washirikina: Je! Kumuamini Mwenyezi Mungu
Mmoja, Aliye Mpweke, ni bora kwa mwenye kuamini, au kuabudu masanamu mnayo
mshirikisha naye, nayo hayawezi kukudhuruni wala kukufaeni?
60. Bali, ewe
Mtume, waulize: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake, na
akakuteremshieni kutoka mbinguni mvua yenye manufaa, na kwa hiyo akakuotesheeni
bustani nzuri zenye kupendeza. Msingeli weza nyinyi kuiotesha miti yake ya namna
mbali mbali, na rangi mbali mbali, na matunda mbali mbali! Mipango hii iliyo
umana sawa katika uumbaji inathibitisha kuwa hapana mungu pamoja na Mwenyezi
Mungu. Lakini makafiri ni watu walio potoka wakaiacha Haki na Imani, na
wameelekea kwenye upotovu na ushirikina.
61. Bali
waulize, ewe Mtume: Nani aliye itengeneza ardhi hata ikafaa kukaliwa na watu
wakatulia humo, na akaumba mito kati yake, na juu yake akaumba milima kuizuilia
isiyumbe yumbe, na akayatenganisha maji matamu na maji ya chumvi hata
yasichanganyike? Hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mwenye kuumba
peke yake. Lakini wengi wa watu hawanafiiki na ujuzi wa Haki kama ilivyo.
Wamekuwa kama kwamba hawajui kitu.
62. Bali
waulize, ewe Mtume: Nani anaye muitikia aliye shikwa na shida katika maombi
yake, pale anapo shikwa na shida, akamtegemea Mwenyezi Mungu kwa unyonge na
unyenyekevu, naye akamwondolea huyo mtu karaha iliyo msibu, na akakufanyeni
warithi wa walio kutangulieni katika nchi? Hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu
wa kukupeni neema zote hizi. Lakini nyinyi makafiri, ni kuchache kabisa
kuwaidhika kwenu.
63. Bali
waulize, ewe Mtume: Nani anaye waongoza katika nyendo za katika giza la usiku
katika safari za nchi kavu na baharini? Na nani anaye zipeleka pepo zinazo
bashiria mvua, nayo ni rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu? Je! Yupo mungu pamoja
na Mwenyezi Mungu anaye fanya hayo? Mwenyezi Mungu Subhanahu ametakasika kuwa na
mshirika.
64. Bali
waulize, ewe Mtume: Nani anaye anzisha uumbaji tangu mwanzo, na kisha baada ya
kupotea kwake akaurejesha kama ulivyo kuwa? Na nani anaye kuteremshieni riziki
kutoka mbinguni, na akaitoa kwenye ardhi? Hakuna mungu pamoja na Mwenyezi Mungu
atendaye hayo. Sema, ewe Mtume, kuwatahayarisha na kuwakanya: Kama nyinyi mnaye
mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu basi tupeni hoja ya hayo, ikiwa mnadai kuwa
nyinyi ni wasema kweli. Na wala hayataweza kuwa hayo kwenu.
65. Sema, ewe
Mtume: Hakika mwenye kutenda yote haya peke yake ndiye Yeye Subhanahu aliye
tengeka peke yake kwa kuyajua mambo ya ghaibu yalioko mbinguni na duniani. Na
Yeye huyo ndiye Mwenyezi Mungu wa pekee. Wala watu hawajui wakati gani
watafufuliwa kutoka makaburini kwao kwa ajili ya kuhisabiwa na kulipwa.
66. Ujuzi wao
wa Akhera umefuatana na ujinga, na huo ukawapelekea kuitilia shaka. Nao wamekuwa
vipofu hawaitambui Haki katika jambo lolote, kwa sababu upotovu umefisidi fahamu
zao.
67. Wakasema
makafiri kwa kukanya kufufuliwa: Hivyo sisi tukisha kuwa mchanga, na ikisha oza
miili yetu na ya baba zetu walio tutangulia, ndio tutarejeshwa tutolewe upya
tuwe wahai?
68. Muhammad
ametuahidi kuwa tutafufuliwa, kama Mitume walio tangulia walivyo waahidi baba
zetu. Ingeli kuwa hayo ni kweli, basi yangeli kwisha kuwa. Haya si chochote ila
ni uwongo tu wa watu wa kale.
69. Ewe Mtume!
Waambie: Tembeeni duniani, na mtazame mabaki ya yaliyo wapata walio kadhibisha,
nayo ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Huenda labda mkayazingatia haya, na mkaikhofu
adhabu ya Akhera.
70. Ewe Mtume!
Usiwahuzunukie makafiri wasio kufuata. Kwani kwa hakika waajibu wako ni
kufikisha Ujumbe tu. Wala usiwe na dhiki kifuani mwako kwa sababu ya hila zao na
vitimbi vyao. Kwani hakika Mwenyezi Mungu atakupa ushindi juu yao.
71. Na makafiri
wanafanya ukomo wa juhudi yao kukanusha, na wanaihimiza adhabu kwa kusema: Lini,
basi, itakuwa hiyo adhabu ambayo mnatutishia kuwa itakuja, ikiwa nyinyi mnasema
kweli kuwa adhabu itawashukia wanao kanusha?
72. Ewe Mtume!
Sema: Huenda ikakukuteni, na imekukaribieni baadhi ya adhabu mnayo ihimiza.
73. Na hakika
Mwenyezi Mungu Mola wako Mlezi, ewe Mtume, ni Mwenye neema na hisani kwa watu
wote. Na katika rehema zake ni kuakhirisha hiyo adhabu kwa hao wanao kadhibisha.
Lakini watu wengi hawaelewi fadhila za Mwenyezi Mungu wala hawamshukuru.
74. Ewe Mtume!
Hakika Mwenyezi Mungu, Mola wako Mlezi, hapana shaka anajua kila wanalo lificha
na wanalo litangaza, ikiwa maneno au vitendo viovu. Naye atakuja walipa kwayo.
75. Na hapana
kilicho fichikana cha ghaibu, na kiwe kidogo vipi au duni, mbinguni au katika
ardhi ila Mwenyezi Mungu anakijua, na amekidhibiti katika Kitabu cha Haki
kilioko kwake.
76. Hakika
Kitabu hiki alicho teremshiwa Muhammad kinawawekea wazi Wana wa Israili ukweli
wa yaliyo kuja katika Taurati, katika mambo ya itikadi na hukumu na hadithi. Na
kinawarudisha kwenye kweli katika mambo waliyo khitalifiana kwayo.
77. Hakika
Kitabu hichi ni Uwongofu wa kuokoa watu wasipotee, na ni Rehema ya kuwakinga na
adhabu wote wenye kukiamini.
78. Ewe Mtume!
Hakika Mola wako Mlezi atawapambanua watu wote Siku ya Kiyama kwa uadilifu wake.
Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, basi hapana wa kuipinga hukumu yake. Yeye
ni Mjuzi wa kila kitu, basi mbele yake kweli haiwezi kuchanganyika na uwongo.
79. Basi, ewe
Mtume, mtegemezee mambo yako Mwenyezi Mungu, na shikilia wito wako kwa kuamini
kuwa utashinda tu, kwa sababu wewe uko juu ya Haki iliyo wazi, na mapuuza ya
makafiri kukupuuza wewe hakutakudhuru kitu.
80. Ewe Mtume!
Hakika wewe huwezi kuwaongoa hao, kwani hao ni kama maiti kwa kuto tambua kitu,
na kama viziwi kwa kutosikia. Basi hao hawako tayari kuusikia wito wako kwa vile
walivyo shikilia kukupuuza.
81. Na wala
huwezi kuwaongoa kwenye Haki wale ambao wamepofuka kuona kwao na kutambua kwao.
Na huwezi kumfanya asikie ila mwenye kukubali kuziamini Ishara zetu. Hao ndio
wenye kut'ii na wenye kuitikia.
82. Na itapo
karibia kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu kuileta Saa ya Kiyama na kuwateremshia
makafiri adhabu, Mwenyezi Mungu atawatolea watu mnyama kwenye ardhi atakaye
waambia miongoni mwa atakayo sema: Hakika makafiri walikuwa hawaiamini miujiza
yetu yote, na pia Siku ya Mwisho. Na hayo waliyo kuwa wakiyakanusha sasa
yamekwisha kuwa. Na hichi basi kitisho cha hiyo Saa na yanayo fuatia! Hii ndio
tafsiri ya Aya hii kwa dhaahiri ya matamko yake. Na zipo tafsiri mbili nyengine
ambazo za hii Aya zinazo weza kuwa: Kwanza ni kuwa makusudio ya "Dabbah" ni
yeyote aendaye "yadibbu", katika watu au wengineo. Na hapa inachukuliwa kuwa ni
watu, watao kuja kabla ya Kiyama. Na maana yake ni kuwa ikiwateremkia kauli juu
yao na adhabu ikathibiti watakuja makundi ya Waumini wakiwaendea, wakienea kote
kote, wakizitikisa nguzo za ukafiri. Tafsiri ya pili neno hilo "Dabbah"
makusudio yake ni watu waovu, ambao kwa ujinga ni kama wanyama, kama alivyo sema
Al As'fahan katika Muqarrarat yake. Na maana yake ni kuwa ikikaribia Siku ya
Kiyama, uovu na ufisadi utazidi, na Kiyama wanacho kikanusha makafiri ndio
kitakuja. Na hiyo kauli itakuwa, nayo si kauli ya kutamkwa kwa mdomo, lakini kwa
kuwa hali yenyewe itakuwa hivyo ni kama iliyo semwa, kama maoni yaliyo kwisha
tangulia.
83. Na ewe
Mtume! Kumbuka siku tutapo wakusanya kutoka kila kundi la wenye kukadhibisha
Ishara zetu, nao ni hao waongozi wanao fuatwa. Basi hao watachungwa wawe mbele
ya kaumu zao kuendea hisabu na malipo.
84. Na pale
watakapo simama mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu, atasema Subhanahu
kuwaambia kwa kuwadhili na kuwabinya: Nyinyi mlizikadhibisha Ishara zangu zote,
na mkazikataa bila ya kuzingatia wala kufahamu. Na khasa mlikuwa mkitenda nini
nanyi hamkuumbwa kwa upuuzi?
85. Na adhabu
itawateremkia kwa sababu ya kujidhulumu nafsi zao kwa ukafiri. Basi watakuwa
hawawezi kujilinda wala kutaka udhuru.
86. Bila ya
shaka wameshuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameufanya usiku ili wapate kupumzika, na
akaufanya mchana una mwangaza, wapate kushughulikia kutafuta maisha yao. Hakika
katika hayo zipo dalili wazi za Ungu wa Mwenyezi Mungu, na Upweke wake, kwa watu
wanao zingatia wakaamini.
87. Na taja,
ewe Mtume, Siku atapo puliza Israfil baragumu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na
watapo ingiwa kiwewe walioko katika mbingu na katika ardhi kwa kitisho cha
mpulizo huo, isipo kuwa huyo ambaye Mwenyezi Mungu atamtuliza na akamhifadhi na
kitisho. Na viumbe vyote watakuja kwa Mola wao Mlezi nao ni madhalili.
88. Na unaiona,
ewe Mtume, milima na unadhani haitaharaki imetulia tu, lakini kwa hakika
inakwenda mbio kama mawingu. Na haya ni katika uundaji wa Mwenyezi Mungu aliye
umba kila kitu na akakizua. Hakika Yeye, Subhanahu, ni Mwenye kutimia ujuzi wake
kwa yote wayatendayo watu, ya ut'iifu na maasi. Naye atawalipa kwayo. "Na
unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu. Huo
ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila kitu. Hakika Yeye
anazo khabari za yote myatendayo." Aya hii inathibitisha kuwa vitu vyote vinavyo
fuata mvutano wa ardhi, kama milima, bahari, na funiko la anga n.k.
vinashirikiana na dunia katika mzunguko wake wa kila siku juu ya msumari-kati
wake, na mzunguko wake wa kila mwaka kulizunguka jua. Lakini mzunguko huu
hauonekani. Ni kama kwenda kwa mawingu angani. Wanao tazama wanayaona, lakini
hawasikii sauti yao, wala hawayagusi. Inaonyesha Aya hii tukufu kwamba Mwenyezi
Mungu Mtukufu aliye tukuka, ameumba ulimwengu na mipango yake ya kuiendeshea.
Naye ni Muweza wa kuifanya hii dunia imetulia tu haizunguki juu ya msumari-kati
wake, au akaifanya kuzunguka juu ya msumari-kati wake sawa sawa na kuzunguka
kwake kulizunguka jua. Na kwa hivyo ingeli kuwa nusu ya dunia imo kizani totoro
kwa muda wa miezi sita, na kwa muda wa miezi sita ikawa nusu ya pili imo katika
mwangaza moja kwa moja wa mchana. Na haya yangeli pelekea kuharibika mizani ya
joto katika dunia yote. Na kwa hivyo uhai ulioko ungeli toweka duniani. Na
Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa Taa'la, ndiye aliye panga mpango huu uliopo kwa
rehema yake na huruma zake kwa waja wake. Na juu ya kuwa Aristakhoris, mtaalamu
wa ilimu ya falaki wa Iskandaria (Alexandria) katika Misri, aliandika (310-230
K.K.) juu ya kuzunguka dunia wenyewe kwa wenyewe, maandishi haya ya kisayansi ya
kale yalikuwa hayajawafikia Waarabu wakati wa Mtume Muhammad s.a.w. au kabla
yake. Bali wa mwanzo wa kuashiria mambo haya katika wao alikuwa Albiruni katika
mwaka 1000 B.K. (Baada ya Kuzaliwa Nabii Isa), baada ya kuingia kufasiriwa
vitabu vya ilimu za zamani kwa lugha ya Kiarabu ulio kuweko katika enzi za Banul
Abbas. Basi kutokea haya kwa ulimi wa Mtume Muhammad s.a.w. ambaye aliye kuwa
hajapata ilimu hiyo, ni dalili kuwa haya yalifunuliwa kwake na Mwenyezi Mungu.
89. Kila mwenye
kuleta wema katika dunia, nayo ni Imani na usafi wa ut'iifu, atapata huko Akhera
thawabu kubwa kabisa kwa ajili ya aliyo yatanguliza. Na wenye mema haya
watasalimika na khofu na kufazaika Siku ya Kiyama.
90. Na kila
mwenye kuleta uovu katika dunia - nao ni shirki na maasia - na akafa na hayo,
basi malipo ya kundi hili ni kuwa Mwenyezi Mungu atawasukumiza juu ya nyuso zao
katika Moto, na wataambiwa hapo kwa kuwatahayarisha: Hakika hii leo hamlipwi ila
kwa sababu ya shirki yenu na maasi yenu.
91. Ewe Mtume!
Waambie watu: Sikuamrishwa nimuabudu yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu, Mola
Mlezi wa mji wa Makka aliye utukuza, na akaufanya mtakatifu wenye amani, usio
faa kumwagwa damu ndani yake, wala kuwindwa wanyama wake, wala kukatwa miti
yake. Na vitu vyote viliomo ulimwenguni ni vya Mwenyezi Mungu kuvimiliki na
kuvitawala, na mimi nimeamrishwa niwe katika wanao mnyenyekea Mwenyezi Mungu.
92. Na
nimeamrishwa nidumishe kuisoma Qur'ani, kwa ibada, na kuzingatia, na kuwaitia
watu wafuate yaliomo humo. Basi mwenye kuongoka, akaiamini, na akakufuata wewe,
basi kheri ya hayo na malipo yake ni kwa nafsi yake. Na mwenye kupotea asiifuate
Haki, na asikufuate wewe, mwambie: Hakika mimi ni Mtume, naonya, na nafikisha
Ujumbe tu.
93. Na sema,
ewe Mtume: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu kwa neema ya
Unabii na Uwongofu. Mwenyezi Mungu atakuonyesheni hapa duniani athari za uwezo
wake, na Akhera atakuonyesheni ukweli wa aliyo kwambieni, na mtayajua vilivyo.
Wala Mwenyezi Mungu hashindwi kukuhisabieni wala haghafiliki na vitendo vyenu.
Copyright ? 22 August 27997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani