1.
Mambo ya Mwenyezi Mungu yametukuka, na kheri yake imezidi. Yeye ndiye aliye
iteremsha Furqani, yaani Qur'ani, ya kufarikisha baina ya kweli na uwongo juu ya
mja wake, Muhammad s.a.w., ili awe mwonyaji na mwenye kuifikisha hiyo Qur'ani
kwa walimwengu wote.
2. Yeye Subhanahu ndiye
peke yake aliye miliki mbingu na ardhi, aliye takasika na haja ya kuwa na mwana,
wala hakuwa na mshirika wowote katika ufalme wake. Na Yeye kaumba kila kitu na
akakipima kwa kipimo baraabara kwa sharia zake ili kiweze kutimiza waajibu wake
kwa nidhamu. "Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana,
wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa
kipimo." Ilimu ya sayansi ya sasa imethibitisha kuwa vitu vyote vinakwenda kwa
mujibu wa hukumu za uumbaji wake, na maendeleo yake namna mbali mbali kwa
kufuata mpango madhubuti ambao hapana mwenye uwezo juu yake ila Muumbaji mwenye
uwezo Mwenye kuanzisha kila kitu. Kwani katika kuwa kwake imebainika kuwa vitu
vyote viumbe vyote na vinga khitalifiana umbo lake na sura yake kwa hakika
vinatokana na madda chache za asli za kuhisabika, na hisabu ya madda hizo
(elements) zinakaribia mia, nazo ni 96 zinazo juulikana mpaka sasa. Nazo zina
khitalifiana kwa sifa zao za maumbile (physically ) na za Al Kimyaa
(Chemically), na pia katika uzito wake wa chembe (Atomic Weight). Zinaanza kwa
madda asli (element) Nambari 1. Nayo ni Hydrogen yenye Atomic weight 1, na
kuishia na element ya nambari 96, Borium, ambayo atomic weight yake bado
haijuulikani. Na element ya mwisho katika sayansi ni Uranium na atomic weight
yake ni 238.57. Na hizi elements hujengeka na kufanyika Compounds kwa mujibu wa
kanuni madhubuti zisio weza kuepukwa. Hali kadhaalika mimea na wanyama. Kila
mmoja wao amegawika katika koo na makundi na namna (orders, families, species
and sub-species) zinazo geuka sifa zake kwa madaraja ya viumbe vilivyo hai mpaka
kuishia viumbe vyenye Khalaya au Cell moja (unicellular) kama microbes mpaka
viumbe vyenye cells nyingi (multi- cellular) mpaka kufikia binaadamu, naye ndiye
aliye kamilika kuliko wote. Na kila namna ya hizi sifa maalumu zinarithika
katika kundi kizazi baada ya kizazi. Na yote haya yanakwenda kufuata kanuni na
mipango iliyo thibiti madhubuti inayo onyesha kwa uwazi utukufu wa Mwenye kuumba
na uwezo wake. Ametakasika, Subhanahu na ametukuka na hao wanao mshirikisha
naye.
3. Na juu ya yote hayo
makafiri wakaacha kumuabudu Yeye, wakenda kuchukua miungu mingine kuiabudu
badala ya Mwenyezi Mungu, katika masanamu, na nyota, na watu. Na hao hawanalo
waliwezalo kuliumba, bali wao ni viumbe vya Mwenyezi Mungu. Wala hawawezi
kujikinga nafsi zao na madhara, wala kujiletea kheri. Wala hawawezi kumfisha
yeyote wala kumhuisha, wala kuwafufua maiti kutoka makaburini kwao. Na kila
asiye miliki lolote katika hayo basi hastahiki kuabudiwa. Na mjinga wa kutupwa
anaye waabudu. Mwenye kustahiki kuabudiwa ni yule Mwenye kumiliki haya yote.
4. Makafiri wakaitia ila
Qur'ani, wakasema kuwa hiyo ati ni uwongo kauzua Muhammad mwenyewe, na
akamsingizia Mwenyezi Mungu. Na wakamsaidia baadhi ya jamaa wengine katika
Ahli-l-Kitab. Basi hawa makafiri wamefanya dhulma kwa kauli yao hiyo katika
hukumu na kuishambulia Haki, wakaleta uzushi usio kuwa na ushahidi wowote. Kwani
hao wanao waashiria katika Ahli-l- Kitab lugha yao hata si Kiarabu. Na Qur'an ni
kwa lugha ya Kiarabu fasihi.
5. Wakaisema Qur'ani pia
kuwa ati ni uwongo walio andika watu wa kale katika vitabu vyao, kisha akawataka
wao wamuandikie na wamsomee asubuhi na jioni mpaka ahifadhi na apate kusema naye
hayo hayo.
6. Ewe Nabii! Waambie:
Hakika Qur'ani ameiteremsha Mwenyezi Mungu ambaye anazijua siri zilizo fichikana
katika mbingu na ardhi. Na ameziweka katika Qur'ani ya muujiza kuwa ni dalili ya
kwamba hiyo ni Ufunuo wake Subhanahu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa
maghfira na rehema, anawasamehe wenye kuasi pindi wakitubu, wala hafanyi haraka
kuwaadhibu.
7. Wakamkejeli Muhammad,
wakasema: Kitu gani kinacho mtengua huyu anaye dai kuwa ni Mtume, hata anakula
chakula kama tulavyo sisi, na anazururuka masokoni kutafuta maisha kama watu
wengine? Angeli kuwa ni Mtume Mwenyezi Mungu angeli mtosheleza kwa hayo, na yeye
angeli mwomba Mola wake Mlezi amteremshie Malaika kutoka mbinguni amsaidie
katika uwonyaji na kufikisha Ujumbe, na amsadikishe katika wito wake, tupate
sisi kumuamini.
8. Na hebu lau angeli
mtaka amtosheleze chakula cha kutosha asihitajie kuzunguka masokoni, akamtupia
khazina kutoka mbinguni ya kutumia, au akamjaalia na bustani ya kumlisha matunda
yake? Na wakubwa wa makafiri walio jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri, wenye
kuwapotoa watu wasimuamini Muhammad, na wenye kufanya hila za kuwaingiza shaka
Waumini, walisema: Nyinyi hamumfuati ila huyu mtu aliye zugwa akili yake, basi
anabwabwatika bila ya kuwa na hakika.
9. Hebu angalia, ewe
Nabii! Vipi wanavyo kupigia mifano hawa! Mara wanakupigia mfano wa mwenye
kurogwa, mara nyengine kuwa ati ni mwendawazimu, mara ya tatu kuwa ni mwongo, na
mara yane kuwa unaipokea Qur'ani kutokana na wasio kuwa Waarabu. Hao kwa hayo
hakika wameipotea njia ya haki, na kuhojiana kulio sawa. Basi hawaitambui njia
ya kufikilia yote hayo.
10. Mwenyezi Mungu
ametukuka, na izidi kheri yake! Yeye ndiye ambaye pindi akitaka atakujaalia
duniani bora kuliko hayo wanayo pendekeza wao. Kwa Akhera Yeye amekwisha
kujaalia kama alivyo kuahidi, nayo ni mabustani mengi yapitayo mito pembezoni
mwake, na baina ya miti yake, na majumba ya fakhari madhubuti.
11. Na kwa hakika hawa
wamepinga kila Ishara. Kwani wao wamekanusha kufufuliwa, na Siku ya Kiyama. Nao
kwa hivyo wanayatia ila matakwa haya ili kuwageuza watu washughulikie upotofu
wao. Na Sisi tumekwisha waandalia wanao ikanusha Siku ya Kiyama Moto wenye
kuwaka vikali mno.
12. Wakiuona Moto, na huo
Moto ukawaona, wataisikia sauti yenye hasira, yenye hamu kuwateketeza. Na katika
hayo ni mfano wa mingurumo inayo toka kifuani mwa aliye kasirika kuwa ni alama
ya ukali alio nao.
13. Na watapo tupwa
katika pahali pembamba kwa kulingana na unene wao, nao wamefungwa pingu mikono
yao kwenye shingo zao, watapiga kelele kuhimiza wateketezwe upesi upesi ili
wapate kupumzika na kitisho cha adhabu.
14. Wataambiwa kwa
kuwahizi na kuwakejeli: Msitake kuangamia mara moja tu, bali takeni muangamie
mara nyingi. Hamtopata kusalimika na hayo mliyo nayo. Na hakika namna ya adhabu
zao ni nyingi.
15. Ewe Nabii! Waambie
makafiri: Je! Marejeo haya waliyo ahidiwa makafiri ni bora au Pepo yenye kudumu
neema zake, na ambayo wameahidiwa Waumini, wachamngu, kuwa itakuwa yao kama ndio
malipo na marejeo ya kwendea baada ya kufufuliwa na kuhisabiwa?
16. Humo watapata
wakitakacho, wataneemeshwa kwa neema za daima, zisio katika. Na neema hizi ni
ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao. Walimwomba Mola wao Mlezi itimie, naye akawaitikia
kwa walilo liomba; kwani ahadi yake hayendi kinyume.
17. Na taja, kwa ajili ya
mawaidha, Siku ambayo Mwenyezi Mungu atawakusanya washirikina kwa ajili ya
hisabu katika Siku ya Kiyama, pamoja na hao ambao walikuwa wakiwaabudu duniani
badala ya Mwenyezi Mungu, kama Yesu (Isa), Ezra (Uzair) na Malaika. Mwenyezi
Mungu atawauliza hao waabudiwa: Je! Ni nyinyi ndio mlio wapoteza waja wangu,
mkawaamrisha wakuabuduni, au wao wenyewe ndio walio potea Njia kwa khiari yao,
wakakuabuduni?
18. Jawabu yao itakuwa:
Umetakasika, na Umetukuka! Haikutafalia sisi kabisa tumtake mlinzi badala yako
atunusuru na aangalie mambo yetu. Basi itakuwaje juu ya haya tumtake yeyote
atuabudu sisi badala yako Wewe? Lakini sababu ya ukafiri wao hawa ni kuwa
uliwastarehesha kwa muda mrefu duniani, wao na baba zao. Hayo yakawapandisha
kichwa, wakasahau kukushukuru, na kukuelekea Wewe tu kwa ibada. Basi wakawa kwa
jeuri hiyo na ukafiri huo wanastahiki kuangamizwa.
19. Wataambiwa wenye
kuabudu, washirikina: Wamekukadhibisheni hao mlio kuwa mkiwaabudu, ambao mkidai
kuwa wamekupotezeni. Basi nyinyi leo mnarejea kwenye adhabu. Hamna hila ya
kuepukana nayo; wala hamyapati manusura ya kukutoeni. Na wajue waja wote kwamba
mwenye kudhulumu kwa ukafiri na uasi kama walivyo fanya hao basi Sisi
tutawaadhibu adhabu kali.
20. Na ikiwa washirikina
wanakutia ila ewe Nabii, kwa kula kwako chakula, na kwenda kwako masokoni kwa
ajili ya kazi na kuchuma maisha, basi huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa
Mitume wake walio kuja kabla yako. Hatukumtuma yeyote kati yao ila alikuwa akila
chakula, na anakwenda kwenda masokoni. Na enyi watu! Tumewafanya baadhi yenu
wawe ni mitihani kwa wenginewe. Na mafisadi wanafanya hila kuziba Njia ya
Uwongofu na Haki kwa namna mbali mbali. Basi, enyi Waumini, mtavumilia juu ya
Haki yenu, na mtaishikilia Dini yenu, mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake kwa
ushindi? Subirini! Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote, na
atamlipa kila mtu kwa kitendo chake.
21. Na wakasema wanao
kataa kufufuliwa na wala hawatumai kuwa yapo malipo kwa vitendo vyao: Kwa nini
hatuteremshiwi Malaika wa kukuunga mkono, au Mwenyezi Mungu akajionyesha kwetu
na akatwambia kwamba kweli Yeye kakutuma? Kiburi kimewajaa katika nafsi zao, na
wamepita mpaka katika udhalimu na ujabari!
22. Siku ya Kiyama
watawaona Malaika kama walivyo tamani, na hayo yatakuwa ni sababu ya kitisho
kwao wala si jambo la kuwafurahisha. Watatafuta kujilinda nao, kama walivyo kuwa
wakitafuta kujilinda na vinavyo watisha duniani.
23. Na Siku ya Kiyama
tutawaletea waliyo yatenda katika mambo ya kuonyesha wema kwa dhaahiri na hisani
katika dunia, na Sisi tutayafanya yaondokee patupu, na tutawaharimisha thawabu
zake, kwa kuwa yamekosa Imani ambayo ni dharura ipatikane ili vitendo vitiwe
maanani.
24. Watu wa Peponi Siku
ya Kiyama ndio watao kuwa na utulivu bora, na mashukio mazuri, na makaazi ya
starehe, kwa sababu hii ni Pepo walio andaliwa Waumini, si Moto walio andaliwa
makafiri.
25. Ewe Nabii! Itaje Siku
itapo pasuka mbingu na ikafunguka, na yakadhihiri kati yake mawingu, na Malaika
wakashuka khasa kwa yakini.
26. Katika siku hii mali
ya watu wenye mali yataharibika, madai yao wanao jidai yatakatika, na Ufalme
wote utabaki ni wa Arrahmani , Mwingi wa Rehema, peke yake. Na itakuwa siku ya
shida ngumu mno kwa makafiri.
27. Siku ya Kiyama mwenye
kujidhulumu nafsi yake atajiuma mikono yake kwa hasira na majuto kwa ukafiri
wake na kumwendea kinyume Mtume, na kwa kutamani atasema: Laiti lau ningeli
mfuata Mtume, nikaifuata njia ya kwendea Peponi, na nikaiepuka njia ya kwendea
Motoni!
28. Na atasema kwa kujuta
kuwafuata walio mpoteza: Laiti ningeli kuwa sikumsadiki fulani, ambaye
nimemwachia aniongoze.
29. Rafiki huyu
amenibaidisha na Ukumbusho, Dhikr, kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kuikumbuka
Qur'ani baada ya kwisha kuwa ni nyepesi kwangu. Ndio hivi Shetani anavyo mkhini
binaadamu, na kumtokomeza kwenye hilaki yake.
30. Na Mtume alisema
akimshitakia Mwenyezi Mungu kwa taabu anazo zipata kwa watu wake: Hakika hawa
wameiacha Qur'ani na wameihama, na wameshikilia katika kuipuuza, na kuifanyia
inda na uadui.
31. Kama tulivyo wajaalia
watu wako, ewe Muhammad, wanavyo kufanyia uadui na kukukadhibisha, basi
kadhaalika tulimjaalia kila Nabii ana maadui miongoni mwa wakosefu, wanao
mfanyia uadui na wanaupinga wito wake. Na Mwenyezi Mungu atakunusuru, na
atakuongoa mpaka uwashinde. Na Yeye anakutosha kwa uwongofu na kukunusuru.
32. Na makafiri kutaka
kuikebehi Qur'ani walisema: Kwa nini haikuteremshwa kwa mara moja? Na Sisi
hakika tumeiteremsha kwa mapande mapande ili moyo wako uthibiti kwayo kwa raha
yako na ili uihifadhi. Na tumeisoma, yaani tumeigawa kwa Aya, au tumeisoma kwa
ulimi wa Jibril, kidogo kidogo kwa utulivu na upole.
33. Na wala hawakujii na
upinzani dhaifu, ila nasi tunakuletea Haki ya kubainisha, na bora ya maelezo.
34. Na walio ukataa
Ujumbe wako watabururwa kupelekwa Motoni kifudifudi na madhalili. Hao ndio watu
wa chini kabisa kwa cheo, na ndio walio zama mno katika upotovu.
35. Na Mtume s.a.w.
anapozwa kwa yaliyo wapata Mitume wa kabla yake. Hakika Sisi tulimteremshia Musa
Taurati, na tukamkalifisha afikishe Ujumbe wetu, na tukamuunga mkono kwa ndugu
yake Harun, awe waziri wake na msaidizi katika kazi yake.
36. Tukasema: Nenda wewe
na nduguyo kwa Firauni na watu wake. Tukamuunga mkono kwa miujiza inayo onyesha
ukweli wake. Hawakumuamini, wakamkadhibisha. Mwisho wao ukawa tukawateketeza na
tukawafutilia mbali!
37. Hali kadhaalika kabla
ya Musa tuliwafanyia kaumu ya Nuhu walipo mkadhibisha, na aliye mkanusha Mtume
mmoja basi amewakanusha Mitume wote. Nao tukawazamisha katika tufani, na
tukawafanya wawe ni zingatio kwa watu. Na tukawajaalia hao na kila mshirikina
kupata adhabu chungu Akhera.
38. Na kadhaalika
tuliwahiliki A'di na Thamudi na watu wa Rass (1) walipo wakanusha Mitume wao. Na
tuliziangamiza kaumu nyingi baina ya kaumu ya Nuhu na baina ya A'di, yakawapata
malipo ya wenye kudhulumu. (1) Rass, kama ilivyo elezwa katika Mufradaat ya
Raaghib Al-As'fahani, ni bonde, na akatolea ushahidi ubeti wa shairi: (Nao ni
bonde la Rass, kama mkono kwa mdomo.) Hao watu wa Rass, kama ilivyo kuja katika
Aya tukufu, ni watu walio kuwa wakiabudu masanamu. Mwenyezi Mungu aliwatumia
Shuaib. Basi hao ndio walio pelekewa Mtume Shuaib a.s. Na Mwenyezi Mungu Aliye
takasika amewaeleza hao kaumu ya Shuaib kuwa ni Watu wa Vichakani (Al-Aykat),
napo ni pahali penye miti mingi panasifika kwa neema, na mara nyengine wanaitwa
Watu wa Rass, nalo ni bonde lenye kheri kubwa, kuonesha neema alizo waneemesha
Mwenyezi Mungu. Nao wakazikufuru neema za Mwenyezi Mungu, wakaabudu masanamu.
39. Na Sisi tumezionya
kaumu zote hizi. Tukawakumbusha mawaidha, na mifano ya kweli yenye manufaa.
Lakini hawakuwaidhika. Tukawashika wote kwa kuwaadhibu, tukawahiliki, na
tukayabomoa majumba yao mpaka kifusi.
40. Na hawa Makureshi
katika safari zao za kwenda Sham wanapita kwenye mji wa kaumu Lut'i, tulio
unyeshea mvua ya shari na ovu kabisa, nayo ni mawe ya Motoni. Je! Hawauoni mji
huo wakawaidhika kwa yaliyo wafika watu wake? Hakika wao wanauona huo, lakini si
kwa macho ya kuwaidhika na kuzingatia. Kwani hawaamini ahadi (za Mwenyezi Mungu)
wala kufufuliwa. Wala hawataraji kuwa ipo siku watakuja fufuliwa kwa ajili ya
hisabu.
41. Na wakikuona watu
hawa hawakuchukulii ila kukufanyia kejeli na maskhara. Na huambiana wao kwa wao:
Ndiye huyu aliye mtuma kwetu Mwenyezi Mungu awe ni Mtume, na sisi tumfuate
twende nyuma yake?
42. Mtu huyu hakika
kajaaliwa kuwa na ufasihi mzuri, na hoja za kuvutia kwa wanao msikia. Na hapana
shaka ameweza kuchota katika imani zetu hata alikaribia kututoa kwa miungu yetu
tumfuate mungu wake. Lakini sisi tumesimama imara juu miungu yetu na dini yetu.
(Mwenyezi Mungu anasema:) Tutakuja wabainishia ukweli wa mambo watapo kuja iona
adhabu Siku ya Kiyama, na watajua nani huyo aliye thibiti katika upotovu na
makosa.
43. Ewe Mtume! Umeona
upotovu wa mwenye kufuata matamanio yake na pumbao lake hata akawa anaabudu mawe
ambayo hayadhuru wala hayanafiishi? Na wewe umetumwa uwe mwonyaji na mbashiri,
wala hukuwakilishwa kwa imani yao na uwongofu wao.
44. Na hivyo unadhani
kuwa wengi wao wanasikia kwa sikio la kufahamu au wanaongoka kwa akili zao?
Wamesha tupilia mbali kama walivyo amrishwa na ndoto zao. Wamekuwa kama wanyama
wa kufuga, hawanalo linalo washughulisha ila kula, na kunywa, na kustarehe na
maisha ya dunia. Wala hawana fikra yoyote baada ya hayo. Bali hali yao ni ovu
zaidi kuliko ya wanyama, kwani wanyama huwafuata bwana zao katika yenye kheri
nao, na wanayaepuka ya kuwadhuru. Lakini watu hawa wanajitokomeza wenyewe kwenye
mambo ya kuwahiliki.
45. Tumesimamisha dalili
za Tawhidi, Upweke wa Mwenyezi Mungu, za kuwaongoa wenye akili. Hebu kiangalie
kivuli. Mwenyezi Mungu amekitandaza na akakifanya kimetulia mwanzo wa mchana.
Kisha tukalipeleka jua likaondoa pahala pake kwa mwako wake. Likawa jua ni kama
ndio linaongoza kivuli. Bila ya jua, kivuli kisingeli juulikana. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu ange penda angeli kifanya kivuli kitulie vile vile
kimewang'ang'ania watu, na yakawaharibikia maslaha yao na mambo yao. " Je! Huoni
jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya
kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake." Aya hii
inadhihirisha hima ya Muumba na uwezo wake. Kwani kutandaza kivuli kunaonyesha
mzunguko wa dunia na kuinama kwa msumari-kati (axis) wake. Na lau kuwa ardhi,
yaani dunia, ingeli tulia tu, haitaharaki kulizunguka jua, na pia ikawa
haizunguki wenyewe kwa wenyewe juu ya msumari-kati wake, basi kivuli kingeli
tulia, na mwako wa jua ungeli piga juu ya nusu ya dunia, na nusu ya pili ikabaki
ni usiku, moja kwa moja. Hayo yangeli leta khitilafu kubwa za baridi na joto, na
ingeli pelekea kutoweka uhai kabisa katika dunia. Na kadhaalika ingeli kuwa hii
ni hali ya dunia basi kivuli kingeli tulia. Na haya pia yange tokea ikiwa muda
wa kuzunguka ardhi juu ya msumari-kati wake ndio muda ule ule muda wa kuzunguka
kwake kulizunguka jua, yaani siku moja ikawa sawa na mwaka mzima. Lakini hapana
awezaye kufanya hayo isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Haya licha ya kuwa kivuli nafsi
yake ni neema miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu
aliviumba vitu vyote vyapenyeza mwangaza (transparent) kisingeli kuwapo kivuli,
na vitu visingeli pata fursa ya kuwepo ambavyo vinahitajia vivuli.
46. Na kukiondoa kwetu
kivuli ni kwa utaratibu, kwa kipimo. Hakukuwa kwa mara moja. Na katika hayo yapo
manufaa kwa watu.
47. Na katika Ishara za
Tawhidi ni kuwa tumeufanya usiku ni sitara kwa kiza chake, ndani yake wanaingia
viumbe ukawazunguka kama inavyo wazunguka nguo kwa mwenye kuivaa. Na
tukawatengenezea malazi, ikawa ni mapumziko kupumzika na machofu, na kwa
mwangaza wa jua wanazinduliwa watu watafute maisha yao na riziki zao.
48. Na Yeye ndiye aliye
zifanya pepo zimtumikie, zikasukuma mawingu, nayo yakawabashiria watu itakuja
mvua, ambayo ni rehema itokayo kwake kuwaendea wao. Na hakika Sisi tunateremsha
kutoka mbinguni maji safi yanayo safisha kuondoa najisi na uchafu. "Na
tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi." Katika Aya hii tukufu Mwenyezi Mungu
anawasimbulia watu kwa kuwateremshia maji yaliyo safi kutoka mbinguni. Na Aya
hii inafahamisha kuwa maji ya mvua katika asli ya kuumbwa kwake ni maji safi
kabisa. Na juu ya kuwa baada yake yanabeba takataka nyingi katika anga, lakini
bado yamo katika daraja ya usafi.
49. Tunaiteremsha mvua
kwa sababu makulima yapate kumea na kukua, na ardhi ipate kufufuka baada ya kufa
kwake, na wanyweshwe watu na wanyama walio umbwa.
50. Na hii Qur'ani
tumeibainisha na tumeisarifu, tumeifanya, ili watu wamkumbuke Mola wao Mlezi, na
wawaidhike, na watende kwa mujibu wake. Lakini wengi wa watu wanakataa isipo
kuwa ukafiri na inda tu.
51. Na lau kuwa tumetaka
basi tungeli mpeleka mwonyaji kwenye kila mji. Basi jitahidi na wito wako; na
wacha maneno ya makafiri; na tupilia mbali wanayo yaleta.
52. Na endelea na
kulingania kwako kwa Haki, na kufikisha Ujumbe wa Mola wako Mlezi. Na wao
wakiupinga wito wako, na wakawavamia Waumini basi wapige vita, na kwa hayo
pigana Jihadi kubwa.
53. Na Mwenyezi Mungu
ndiye aliye ziendesha bahari mbili, bahari ya maji matamu na bahari ya maji ya
chumvi. Na akafanya njia ya kila moja inakaribiana na nyengine. Na juu ya hivyo
maji yao hayachanganyikani. Hiyo ni neema na rehema kwa watu. "Naye ndiye aliye
zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina
yao kinga na kizuizi kizuiacho." Yamkini Aya hii inaashiria neema ya Mwenyezi
Mungu kwa waja wake kwa kuto changanyika maji ya chumvi yanayo penya kutoka
baharini kwenye miamba ya karibu na mwambao, na maji matamu yanayo penya kutoka
bara, yasichanganyike kwa ukamilifu na hali nayo yanakutana. Matamu yanakuwa
yako juu ya maji chumvi kama kwamba baina yao pana kinga kinacho zuia haya
yasiingiane na haya, na kizuizi kizuiacho, yaani kizuizi chembamba tusicho weza
kukiona. Na haya si tu, bali ipo kanuni madhubuti inayo hukumu makhusiano haya,
na inayo yahukumu kwa maslaha ya wanaadamu wanao kaa katika maeneo hayo, na
maisha yao yanategemea kuwepo hayo maji matamu. Kwani imethibiti kuwa t'abaka ya
maji matamu yalioko juu huzidi unene wake kwa mujibu wa kuzidi usawa (level) wa
bahari kwa mpango maalumu. Hata inakuwa yawezekana kuhisabu kina cha mwisho cha
maji matamu ambayo yamkinika kuyapata. Kwani hiyo ni sawa sawa na kadri ya
khitilafu baina ya usawa (level) wa ardhi na usawa wa bahari mara arubaini.
54. Na Mwenyezi Mungu
ndiye aliye umba kutokana na manii hawa watu, na akawajaalia wanaume na wanawake
walio khusiana kwa nasaba ya kuzaana na kwa ushemeji wa kuoana. Na Mwenyezi
Mungu ni Muweza kwa atakayo, kwani kwa hiyo hiyo manii ameumba namna mbili mbali
mbali.
55. Na baada ya Ishara
hizi zenye kuonyesha kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anaye stahiki
kuabudiwa, na kwamba hapana mungu isipo kuwa Yeye, wanatoka kikundi cha watu
kuabudu masanamu yasiyo wafaa wala kuwadhuru. Na hawa kwa kujua kwao haya
wanamsaidia Shetani, na yeye anawapoteza. Basi hao inakuwa wanasaidiana katika
kuipinga Haki ambayo Mwenyezi Mungu anawaitia.
56. Na ewe Nabii! Huna
jukumu ila kufikisha hayo ulio tumwa basi, na kuwabashiria Pepo Waumini, na
kuwakhofisha makafiri kwa haya watayo yakuta. Baada ya hayo huna jengine unalo
takiwa.
57. Na waambie: Hakika
mimi sitafuti kwa huku kukuiteni muufuate Uislamu ujira wowote wala malipo. Ila
nilitakalo ni mwongoke na muifuate Njia ya Haki mrejee kwa Mola wenu Mlezi.
58. Na katika mambo yako
mtegemee Mwenyezi Mungu Aliye Hai, ambaye hayumkini kufa. Na mtakase na mtukuze
kwa kuzisifu neema zake. Na waachilie mbali walio toka kwenye Njia. Kwani
Mwenyezi Mungu anawajua vyema, na atawalipa kwa dhambi zao.
59. Na Mwenyezi Mungu
ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao kwa siku sita. Naye
ametawala juu ya A'rshi, Kiti cha Enzi, cha Ufalme wote, na madaraka yake
yameenea kila kitu. Na Yeye ndiye Mwingi wa Rehema, Arrahman. Na ukitaka lolote
katika sifa zake muulize ajuae atakujibu. Naye ni Mwenyezi Mungu Mwenye hikima.
"Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha
akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Ulize khabari zake kwa
wamjuaye." Hizo Siku Sita ni usemi wa Mwenyezi Mungu, Mtukufu Aliye tukuka,
kueleza wakati. Na Yeye Mtukufu ndiye Mwenye kujua zaidi kipimo cha hiyo Siku.
Na kwa upande wa kiilimu za sayansi kazi ya kuumba ulimwengu unahitaji kupita
vipindi na viwango mbali mbali. Na "Mbingu na ardhi na viliomo ndani yake" ni
ishara ya vyombo vyote vya mbinguni, nyota, majua, sayari, miezi, mavumbi, gesi
za namna mbali mbali, na nishat'i, Energy , na vyote hivyo vinavyo fanya ndio
ulimwengu wa duniani na angani. Na kwa kuupanga ulimwengu wote, yaani uumbaji
wote, kwa tafsili ya ukamilifu inayo kusanya kila kitu, ndio inaweka wazi,
Utawala wa Mwenyezi Mungu, Subhanahu juu ya ulimwengu kwa jumla na kwa tafsili.
"Uliza khabari zake kwa ajuaye". Katika kifungu hichi cha Aya hii tukufu pana
uwongozi wa kisayansi kutokana na Mwenyezi Mungu kuonyesha dharura ya uchunguzi
na utafiti wa mambo yanayo onekana ya uumbaji na mipango yake tuyaangalie ya
ndani, ili tujue siri za uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuanzisha huu ulimwengu.
60. Na wakiambiwa hawa
makafiri: Mnyenyekeeni Arrahmani, Mwingi wa Rehema, na mumuabdu, wao husema:
Nani huyo Arrahmani? Sisi hatumjui, hata tumsujudie. Basi tukufuate amri yako
tu? Na wanazidi kuwa mbali na kutengeka na Imani.
61. Ametukuka Arrahman,
Mwingi wa Rehema, na zimezidi fadhila zake. Ameziumba sayari mbinguni na
akazijaalia na vituo vyake vya kupitia, na katika hizo akaumba jua kuwa ni taa
yenye mwangaza, na mwezi wenye nuru. "Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni,
na akajaalia humo taa na mwezi unao ng'ara." Aya hii tukufu inaashiria maana za
ki-ilimu za sayansi zenye kukusanywa katika mpango wa ulimwengu alio uumba
Mwenyezi Mungu, Aliye takasika, Aliye tukuka, na zikazidi fadhila zake. Na sisi
tunashuhudia nyota za mbinguni kwa sura ya makundi ambayo takriban hayageuki
sura na yangapitiliwa na karne, na Buruuj nayo ndio hayo makundi ya nyota, ni
yale yale yanayo pitiwa mbele yake na jua katika mzunguko wake unavyo dhihiri
kuizunguka ardhi. Hizo Buruuj ni kama vituo vya jua katika mzunguko wake katika
mwaka. Na kila tatu katika hizo huwa ni musimu katika misimu ya mwaka. Nazo kwa
kuzitaja moja moja kuanzia msimu wa Rabii' (Spring) unao kuja baina ya siku za
baridi na joto, ni kama ifuatavyo kwa majina ya Kiarabu na Kizungu: Alh'aml
(Aries, or Ram), Ath-thawr (Taurus), Aljawzaa' (Gemini), Assarat'aan (Cancer),
Al Asad (Leo), Assunbulah (Spica), Al Miizaan (Libra), Al-A'qrab (Scorpion), Al
Jadyu (Capricorn), Addalwu (Aquarius), Alh'uut (Pisces). Na jua ni moja katika
nyota zenye nguvu za kati na kati. Nalo kama nyota zilizo baki lina mwangaza
wake mwenyewe wa dhati kwa vituko vya kichembechembe (atomic reaction) vinavyo
tokea ndani yake. Basi miale ya jua inayo toka kwenye nguvu hizo huangukia juu
ya sayari, na ardhi, na miezi, na vyombo vilio baki vya mbinguni ambavyo havina
mwanga wa nafsi yao. Kwa hivyo navyo hutoa nuru. Basi jua ndio Taa inayo waka
kwa nafsi yake. Ama mwezi unarudisha nuru ya mwanga wa jua kutokana na uso wake,
kama kiyoo. Hakika kwa kusifiwa Jua kuwa ni Taa, na ukasifiwa mwezi kuwa unatoa
nuru, ni ishara ya kuwa Jua ndio chanzo cha nguvu, nishati, (T'aaqah, Energy) za
joto.
62. Mwingi wa Rehema
ndiye aliye ufanya usiku na mchana kufuatana, mmoja nyuma ya mwenzie. Na
tumeyapanga haya ili mwenye kutaka akumbuke mpango huu, na ajue hikima ya
Mwenyezi Mungu na uweza wake; au apate kushukuru kwa neema hii njema.
63. Na waja wa Mwenyezi
Mungu ni wale wanao nyenyekea duniani. Wakitembea katika ardhi wanatembea kwa
utulivu na staha. Hali kadhaalika katika mambo yao yote. Na masafihi katika
washirikina wakiwasubu wanawaachilia mbali na shani yao, na wanawaambia: Hatuna
shani nanyi. Letu sisi ni Assalamu Alaikum!
64. Na wale ambao
wanakesha katika ibada na Sala, wakimdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi.
65. Na wale ambao khofu
yao inashinda matarajio - nao ndio mwendo wa wachamngu. Basi wanaikhofu adhabu
ya Akhera, na hawaachi kumwomba Mwenyezi Mungu awaepusha na adhabu ya Jahannamu.
Kwani adhabu yake ikimteremkia mkosefu inamganda, wala haimwachi.
66. Na hakika Jahannamu
ni kituo kiovu mno kwa mwenye kutua, na makao maovu kwa mwenye kukaa ndani yake.
67. Na katika alama za
waja wa Mwenyezi Mungu ni kuwa wana kiasi katika kutumia kwao mali, kwa ajili ya
nafsi zao na jamaa zao. Wao hawafanyi ubadhirifu, wala hawabanii matumizi bila
ya kiasi. Bali kutoa kwao ni kati kati baina ya hayo.
68. Na katika sifa zao
hao waja wa Mwenyezi Mungu ni kuwa wameisafia niya Tawhid, na wakatupilia mbali
kila athari ya ushirikina katika kumuabudu Mola wao Mlezi. Na wakajizuia kuuwa
nafsi aliyo kataza Mwenyezi Mungu kuuliwa, ila ikiwa imefanya uadui basi huuliwa
kwa haki. Nao hujitenga mbali na uzinzi, na katika mambo ya starehe hawatendi
ila lilio halali tu, ili waepukane na adhabu ya mambo yanayo angamiza. Kwani
anaye tenda katika mambo hayo atakuta shari na adhabu.
69. Na Siku ya Kiyama
atapata adhabu mardufu kuliko hiyo, na atadumu Motoni kwa udhalili na unyonge.
70. Lakini mwenye kutubu
na madhambi haya na akawa mkweli katika Imani yake, na akafuatiliza hayo kwa
ut'iifu na vitendo vyema, hao atawasamehe kwa rehema yake, na atawajaalia bora
ya thawabu badala ya maovu yaliyo kwisha tangulia. Na hakika shani ya Mwenyezi
Mungu ni kurehemu na kusamehe.
71. Na hivyo ndio mambo
yetu yendavyo, yaani kuwa mwenye kutubu madhambi, na akaonyesha matokeo yake
katika kukubali ut'iifu na kuepuka maasi, basi huyo Mwenyezi Mungu huikubalia
toba yake. Na kwa hivyo hurejea kwa Mola wake Mlezi baada ya kumwacha kwake.
72. Na katika khulka za
waja wa Mwingi wa Rehema ni kuwa wanajiepusha na kutoa ushahidi wa uwongo, na
wakisadifu kukutana na mtu asiye kuwa na kauli au kitendo chema hawashirikiani
naye katika hayo, na huacha kufuatana naye.
73. Na katika sifa zao ni
kuwa mwenye kuwaidhi akiwapa mawaidha, na akawasomea Aya za Mwenyezi Mungu,
humwelekea kumsikiliza, na nyoyo zao zikawaidhika, na macho yao hufunuka. Wala
hawawi kama wale ambao wanatapatapa wanapo yasikia, wanapuuza, masikio yao
hayapenyi kitu, wala macho yao hayafumbuki.
74. Na wao humwomba Mola
wao Mlezi awajaalie wake zao na watoto wao wawe wa kuwapoza moyo kwa vitendo vya
kheri, na awajaalie wawe ni waongozi katika kheri ili watu wema wawafuate.
75. Hawa wenye kusifiwa
kwa sifa hizi tulizo zitaja ndio waja wa Mwenyezi Mungu wa kweli. Na malipo yao
ni makao ya Peponi ya juu, kuwa ni jazaa ya kusubiri kwao juu ya ut'iifu. Na
huko Peponi watakuta maamkio, na kusalimiwa.
76. Na neema zao za
Peponi ni za daima, hazikatiki. Pepo ndio kituo na makao mema kabisa.
77. Ewe Mtume! Waambie
watu: Mwenyezi Mungu hakutakini nyinyi ila mumuabudu Yeye, na mumwombe Yeye
katika mambo yenu, wala msimwombe yeyote mwenginewe. Na kwa hayo ndio
kakuumbeni. Lakini makafiri katika nyinyi wameyakanusha waliyo kuja nayo Mitume.
Basi adhabu yao itawaganda hao, wala hapana wa kuwaokoa nayo.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani