1. Umewakaribia washirikina wakati wao wa kuhisabiwa Siku ya Kiyama, nao hali wameghafilika na kitisho chake, wanapuuza kuiamini.
 

2. Haiwajii Qur'ani kutokana na Mola wao Mlezi pale inapoteremka kuwakumbusha ya kuwanufaisha, ila wao huisikiliza na hali wao wameshughulika na mengine yasiyo na faida nao, wakicheza kama wachezavyo watoto wadogo.
 

3. Nyoyo zao zimo katika pumbao, hazizingatii, wameshikilia kuficha njama zao za kumpinga Nabii na Qur'ani, wakiambizana wenyewe kwa wenyewe: Huyu Muhammad si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Na Mtume hawi ila Malaika. Basi, je! Mnamsadiki Muhammad na mnahudhuria baraza za uchawi na hali nyinyi mnaona kuwa hakika huo ni uchawi?
 

4. Mtume, kwa kuwa Mwenyezi Mungu kamjuulisha waliyo kuwa wakiyasema kwa siri, aliwaambia: Mola wangu Mlezi anayajua yote yanayo semwa katika mbingu na katika ardhi, na Yeye ndiye anaye sikia kila linalo sikiwa; na anajua kila linalo tokea..
 

5. Bali wao wakasema: Hizi ni mchanganyiko wa ndoto alizo ziota (Muhammad); bali kazua tu na akamsingizia Mwenyezi Mungu kwa uwongo. Kisha wakaacha hayo na wakasema: Bali huyu ni mtunga mashairi anaziteka nafsi za wenye kumsikiliza. Kama kweli, basi na atuletee muujiza khasa wa kuonyesha ukweli wake, kama walivyo tumwa Manabii wa zamani wakitiwa nguvu kwa miujiza mbali mbali.
 

6. Hizo kaumu tulizo ziangamiza baada ya kukadhibisha hiyo miujiza hazikuamini. Basi, je! Watakuja amini hawa yatapo wajia hayo wayatakayo?
 

7. Ewe Nabii! Kabla yako wewe hatukuwatumia watu ila watu wa kibinaadamu vile vile, ambao tuliwafunulia Dini waifikishe kwa watu. Basi, enyi mnao kataa! Waulizeni wanazuoni wajuao ilimu za Vitabu vilivyo teremka, ikiwa nyinyi hamyajui hayo.
 

8. Wala Sisi hatukuwajaalia Mitume kuwa na miili inayo khitalifiana na miili ya wanaadamu wengine, wakawa wanaishi bila ya chakula, na wakabaki siku zote, na wala hawakuwa wanaishi daima milele.
 

9. Kisha tukawatimizia na tukawahakikishia ahadi, na tukawaokoa wao na pamoja nao tukawaokoa tulio taka kuwaokoa miongoni mwa Waumini. Na makafiri walio vuka mipaka tuliwaangamiza kwa kukadhibisha kwao na kuukataa Ujumbe wa Manabii wao.
 

10. Sisi hakika tumekuteremshieni Kitabu. Ndani yake yamo mawaidha ya kuwakumbusheni ikiwa mtakisoma na mtayatenda yaliyomo ndani yake. Basi huwaje mkakipuuza na mkakikataa? Je, inda na upumbavu umefika hadi ya kukufikisheni hali hii mlio nayo, mkawa hamuelewi lipi lenye manufaa nanyi mkalikimbilia?
 

11. Na wengi katika watu wa miji tuliyo iteketeza kwa sababu ya ukafiri wao na kuwakadhibisha Manabii, na baada yao tukasimamisha kaumu nyengine zenye hali bora na mwisho mwema kuliko hao.
 

12. Na tulipo taka kuwateketeza, na wakahisi ukali wa adhabu yetu na uwezo wetu wa kuwateremshia hayo yatakayo wapata, wakafanya haraka kukimbia, kama wanyama hayawani, ati kutafuta kuokoka!
 

13. Enyi wapinzani! Msikimbie! Hapana kitu chochote kitacho kulindeni na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Rudini kwenye zile zile neema na majumba mliyo kuwa nayo, huenda watumishi wenu na wenzenu watakutakeni msaada na rai kama ilivyo kuwa ada yenu. Wapi! Hamtoweza!
 

14. Kwa kuwa hao makafiri wamekwisha sikia wanavyo kejeliwa na wanavyo itwa kwenda teketezwa na wana yakini nako, basi watasema: Hakika kweli sisi tulikuwa ni wenye kudhulumu tulipo yaacha yanayo tunafiisha, na tusiziamini Ishara za Mola wetu Mlezi.
 

15. Maneno hayo hawaachi kuyakariri na kuyapigia makelele mpaka kwa adhabu yetu tukawafanya kama mimea iliyo fyekwa, na moto ulio zimika, hawana tena uhai.
 

16. Wala hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa mpango huu wa hikima, na muundo huu wa namna peke yake, kwa mchezo. Bali tumefanya yote haya kwa hikima ya juu ambayo wanaifahamu wenye kuzingatia.
 

17. Lau kuwa tunataka kufanya mchezo na pumbao isingeli mkinika kuchukua ila yaliyo katika ufalme wetu, kwani hapana ufalme ila wetu - ingeli kuwa Sisi ni wa kufanya hayo. Wala nasi si wenye kufanya hayo, kwa kuwa si laiki ya haki yetu.
 

18. Lakini jambo linalo tuelekea Sisi kulifanya ni kuipambanisha kweli juu ya uwongo ipate kuuondoa. Na nyinyi makafiri mtahiliki kwa sababu ya kumzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
 

19. Na ni vya Mwenyezi Mungu peke yake vyote viliomo mbinguni na katika ardhi, kwa kuviumba na kuvimiliki. Basi ni haki Yeye peke yake kuabudiwa. Na Malaika walio karibishwa kwake hawana kiburi cha kuwazuia kumuabudu na kumnyenyekea, wala hawaoni machofu na kunyong'onyea kwa ibada ya mchana na usiku.
 

20. Wanamtakasa aliye tukuka shani yake na kila lisio muelekea. Kumtakasa huku hakusiti, bali huo ni mtakaso wa daima, hawana shughuli nyengine ya kuwashughulisha.
 

21. Washirikina hawafanyi wafanyavyo walio karibishwa katika kumsafishia ibada Mwenyezi Mungu, bali wao wamewaabudu wenginewe, na wakafanya miungu duniani isiyo stahiki kuabudiwa. Na huwaje kwenda kuabudu kitu kisicho kuwa Mwenyezi Mungu, ambacho hakiwezi kufufua?
 

22. Lau kuwa mbinguni na duniani kuna miungu isipo kuwa Mwenyezi Mungu wanao endesha mambo yao, basi ingeli haribika nidhamu iliyo simamishiwa hizo mbingu na ardhi kwa kuumbwa, na ikafikilia mwisho wa mpango na hikima. Basi na atakasike Mwenyezi Mungu, Mwenye Ufalme wote, na yote wanayo msingizia washirikina.
 

23. Yeye Subhanahu hahojiwi kwa anayo yatenda, kwani ni Yeye pekee mwenye utukufu na madaraka, Mwenye hikima na ujuzi. Hakosei katika kutenda chochote. Ni wao ndio watahisabiwa na kuhojiwa kwa wanayo yatenda, kwa kuwa wao hukosea kwa udhaifu wao na ujinga wao na kughilibiwa na matamanio.
 

24. Hawaujui waajibu wa Mwenyezi Mungu uliyo juu yao, ndio maana wakawa na miungu mingine isiyo kuwa Yeye wakaiabudu bila ya kuwa na ushahidi wowote wa kuingia akilini, wala uthibitisho wa kweli. Ewe Nabii! Waambie: Leteni uthibitisho wenu kama kweli Mwenyezi Mungu ana mshirika katika utawala hata akafaa kushirikishwa katika kuabudiwa. Hii Qur'ani iliyo kuja kuukumbusha umati wangu kwa linalo wajibikia, na hivi Vitabu vya Manabii wengine vilivyo kuja kukumbusha kaumu za kabla yangu, vyote hivyo vimesimama juu ya Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui yaliyo kuja ndani ya Vitabu hivyo, kwa sababu hawajishughulishi kuyazingatia yaliomo humo. Basi wao wamekuwa wenye kuipuuza Imani ya Mwenyezi Mungu.
 

25. Ewe Nabii! Sisi hatukumtuma Mtume yeyote kabla yako ila tulimpa wahyi (ufunuo) awafikishie watu wake kuwa hastahiki kuabudiwa isipo kuwa Mimi. Basi nisafieni ibada, iwe kwangu tu.
 

26. Na baadhi ya makafiri wa Kiarabu walisema: Arrahman, Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, ana mwana, kwa yale madai yao kuwa Malaika ni binti za Mwenyezi Mungu. Ametakasika na kuwa na mwana! Kwani hao Malaika ni waja wake walio tukuzwa tu kwa kuwakaribisha, na kwa wanavyo muabudu Yeye.
 

27. Hawamtangulii Mwenyezi Mungu kwa kauli yao wainenayo kabla ya Yeye kuwapa ruhusa. Na wao hawatendi lolote ila kwa amri yake tu, wala hawapindukii mipaka ya amri anayo waamrisha.
 

28. Mwenyezi Mungu anazijua hali zao zote na vitendo vyao vyote, walivyo vitanguliza na walivyo viakhirisha. Wala hawamwombei mtu kwake ila kwa aliye ridhia Mwenyezi Mungu. Na wao jinsi ya wingi wa khofu yao kumwogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kumtukuza Yeye, daima wana hadhari naye..
 

29. Na miongoni mwa Malaika atakaye sema: Mimi ni mungu wa kuabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu, huyo tutamlipa kwa kumtia Jahannamu. Mfano wa malipo hayo tunamlipa kila mwenye kupindukia mipaka ya haki, na wakajidhulumu nafsi zao kwa kudai Ungu na kuingia katika ushirikina.
 

30. Wenye kukufuru wamepofuka, na hawaoni kuwa mbingu na ardhi hapo mwanzo zilikuwa zimeshikamana. Kwa uwezo wetu tukazibambandua mbali mbali. Na tukajaalia kutokana na maji, ambayo hayo si kitu hai, kila chenye uhai kutokana na hayo hayo. Basi je! Baada ya yote haya wangali kupuuza tu, na hawaamini kuwa bila ya shaka yoyote hapana mungu isipo kuwa Sisi? "Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini?" Aya hii ina maana ya kisayansi yenye kutilia nguvu nadhariya ya ilimu za kisasa katika kuumbwa sayari na ardhi. Nayo ni kuwa mbingu na ardhi asili yao zilikuwa zimeshikamana. Na ukweli wa sayansi zinazo kubaliwa ni kuwa hakika ziliambatana, na sayansi mbali mbali zinathibitisha hayo. Na zipo nadhariya nyengine kadhaa wa kadhaa ambazo kwazo zaweza kuelezea dhaahiri ya mambo haya. Lakini bado kuthibiti nadhariya mojapo kwa njia ya mkato kwa wanazuoni kwa kuwafikiana wote. Kwa kuonyesha mfano tutaja nadhariya mbili: Nadhariya ya Kwanza: Imekhusu kuumbwa kwa mfumo wa jua (Solar System). Kwa mfano imethibiti kuwa mawingu au umande ulio zunguka jua ulianza kuenea kwenye anga lilio baridi, na chembechembe za gasi zinazo fanya hayo mawingu au moshi zikakusanyika kwenye chembechembe za vumbi linalo kwenda kwa kasi kubwa. Kisha chembechembe hizo zikawa zinagongana na zinarindika, na huku ndani yake zikawamo gasi nzito, na kukazidi kurindika na kujumuika kwa kupita mamilioni na mamilioni ya makarne mpaka zikafanyika sayari na mwezi na ardhi kwa umbali unao stahiki. Na yajuulikana kuwa huko kukusanyika na kurindika huzidisha mbinyo (Pressure), na huo huzidisha joto. Na gamba la ardhi lilipo ingia kupoa, na wakati zilipo ripuka volkano ardhi ikapata mvuke wa maji na gasi ya Carbon dioxide ilio tokana na miripuko ya volkano...na katika iliyo saidia kupatikana Oxygen katika hewa baada ya hapo ni nishati na nguvu za miyale ya jua kwa njia ya mwanga juu ya mimea na majani ya mwanzo. Ama Nadhariya ya Pili: Imekhusiana na uumbaji wa ulimwengu kwa jumla, ambao kwa mukhtasari unaelezwa na kauli yake Mtukufu: "Zilikuwa zimeambatana", yaani zimeshikamana na kuwa kitu kimoja. Na hayo ndiyo yaliyo fikilia mwishoni ilimu za sayansi katika uumbaji wa ulimwengu. Nayo ni kwamba kabla ya kufikilia sura yake hii ya sasa ulikuwa kama donge lilio kusanyika lenye kutisha, la mkusanyiko wa chembechembe zenye kuambatana chini ya mbinyo pressure, hata akili haiwezi kuifikiria. Na hizi sayari zote na nyota zilioko mbinguni hivi leo tunazo ziita mfumo wa jua solar system zilikuwa ni mkusanyiko wa donge moja lisilo zidi 1/2 diameter yake maili milioni tatu. Na neno lake Mwenyezi Mungu: "Tukazibambandua" linafahamisha ule mripuko mkubwa wa mwanzo wa ki-nuclear ukazalisha uumbaji wa anga na sayari za namna mbali mbali tunazo ziita kwa pamoja "Mfumo wa Jua" au Solar System. "Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai": Aya hii imethibitisha uhakika wa kisayansi ulio thibitishwa na ncha mbali mbali za ilimu. Imethibitisha Cytology, sayansi ya "cells", (khalaya), kwamba maji ni muhimu kabisa katika ujengaji wa "cells" zote za vitu vilivyo hai, ikiwa mimea au wanyama. Na ilimu ya "Kimyaa", Chemistry kwamba maji ni lazima yapatikane katika vitendo na mageuko yoyote katika viumbe vilivyo hai. Basi hayo maji ama yawe ni kiungo, kitu cha kusaidia, au cha kuwamo ndani ya kitendo, au ni matokeo yake. Na imethibitisha ilimu ya viungo physiology kwamba maji ni dharura kwa viungo kufanya kazi yao. Bila ya hayo maji hautodhihiri uhai katika viungo.
 

31. Na katika dalili za uweza wetu ni kuwa tumeifanya milima imesimama imara kwenye ardhi ili isiyumbeyumbe nao watu, na tumefanya humo njia pana, za kupitia kwa wasaa, ili waweze kuongoza njia humo kwa makusudio yao. Maoni ya wataalamu juu ya Aya ya 31: "Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka." Ilivyo kuwa ndani ya ardhi kila kitu kimeyayuka, na lau kuwa milima imewekwa tu katika baadhi ya sehemu za huu mpira wa dunia kama majabali yaliyo nyanyuka juu tu, uzito wao ungeli sabibisha gamba la dunia liyumbe, au lipindane na kupasuka. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu kwa utukufu wa shani yake ameifanya milima isimame imara kwa kuwa na mizizi iliyo zama kwenye gamba la ardhi mpaka chini kwenye kina kirefu kulingana na urefu wake kwendea juu. Kwa hivyo imekuwa hiyo milima kama vigingi, kama alivyo jaalia eneo la minyanyuka hii na mizizi ni duni kuliko maeneo ya gamba lilio zunguka. Yote haya ni kwa ajili ya kueneza sawa uzito wa juu ya gamba kwa pande zote ili pasiwepo kuyumbayumba na kupasuka. Kwani hakika kuenezwa kwa uzito juu ya uso wa dunia yakaribia kuwa hakuleti athari kubwa ya kutajika. Na ilimu za kisasa zimethibitisha kuwa kuenezwa kwa nchi kavu na maji juu ya ardhi, na kuwepo mfululizo wa milima juu yake ni katika yanayo hakikisha hali ilivyo ardhi, na imethibitika kuwa chini ya milima mizito kuna vitu vyepesi kubungunyika, na chini ya maji ya bahari kuu vipo vitu vizito. Kwa kuenezwa uzani wa namna hiyo mbali mbali katika dunia, na mgawanyo huu wa milima, makusudio yake ni kusawizisha uzani wa mpira huu wa ardhi. Na ilivyo nyanyuka milima zikatokea nyanda na mabonde na njia baina ya milima na mwambao na bahari na minyanyuko, na zikawa njia.
 

32. Na tumeifanya mbingu kama dari iliyo nyanyuliwa, na tukailinda isianguke, au visianguke viliomo humo. Na juu ya hayo, wao hawazioni wala hawaziingatii Ishara zetu zenye kuonyesha uweza wetu na hikima yetu na rehema yetu. Maoni ya wataalamu juu ya Aya 32: "Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa lakini wanazipuuza Ishara zake. ": Aya hii tukufu imethibitisha kuwa mbingu na vyote viliomo ndani yake vimehifadhiwa visiwe na ila yoyote, na vimehifadhiwa visidondoke juu ya ardhi. Na mbingu ni kila kilicho juu yetu, kuanzia kifuniko hichi cha hewa inayo walinda walioko juu ya ardhi na khatari nyingi za angani ambazo zinazuia maisha, mfano wa vimondo vya nyota za mkia, na miyale. Na juu ya ardhi pana kifuniko cha hewa kinacho linda ardhi kwa nguvu za mvutano, na haifai kukosekana hivyo bila ya maangamizo kabisa. Na juu ya kifuniko cha hewa ndio kuna hizo sayari za mbinguni, na zipo kwa umbali mbali mbali kufuatana na nyendo zao tangu mwanzo. "Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa" yaani hizo sayari na vyote vilio mbinguni vyaonekana kwa nadhari yetu kama kwamba ni dari, na tunaona vilio juu ya vichwa vyetu kama ni vidogo kuliko vilioko upeo wa macho. Na hayo ni kiini macho tu, kama tunapo liona jua kubwa wakati wa kuchomoza na kuchwa kuliko adhuhuri. Na hili qubba la mbingu lina sifa zake, zinazo khitalifiana kila ukizidi mnyanyuko wa ardhi, kama hizo sayari za mbinguni kwa mujibu wa jicho linavyo ona katika qubba la mbingu.
 

33. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba usiku na mchana, na jua na mwezi. Vyote hivyo vinakwenda katika njia zake kama alivyo zijaalia Mwenyezi Mungu, na zinamtakasa bila ya kupotea. Maoni ya wataalamu juu ya Aya 33: "Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote katika anga vinaogelea." Kila sayari ya mbinguni ina mzunguko wake makhsusi inayo ogelea kuufuata. Na zote hizo hazisiti, na zinakwenda kwa mwendo wao maalumu katika anga. Na sisi tunaona hayo kwa hakika kwa kutazama mwendo wa jua na mwezi. Kama kadhaalika mzunguko wa ardhi wake wenyewe ndio unao leta usiku na mchana kwa zamu, kama kwamba unaogelea.
 

34. Ewe Nabii! Hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako wewe aishi milele, hata ikawa hao makafiri wakawa wanakutamania ufe wewe. Vipi wanakutamania mauti wewe na hali na wao vile vile watakufa kama wewe? Ukifa wewe, je, ndio wao watabakia kushinda wanaadamu wote?
 

35. Kila nafsi haina budi kuonja mauti. Na Sisi tunakufanyieni hapa duniani kama wenye kukupeni mtihani, kwa kukupeni yenye manufaa yenu na yenye madhara pia, ili abagulike mwenye kushukuru kwa kupewa kheri na kuvumilia balaa, na yule asiye na fadhila kwa neema aipatayo na anapapatika akipata misiba. Nanyi mtarejeshwa kwetu, na hapo tutakuhisabieni vitendo vyenu.
 

36. Na wakikuona, ewe Nabii, wale walio mkataa Mwenyezi Mungu na ulio kuja nayo wewe, hawakufanyii wewe ila maskhara na kejeli. Huambiana wao kwa wao: Ndiye huyu anaye watia aibu miungu yenu? Na hali wao hawasadiki kumdhukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliye waeneza rehema yake!
 

37. Na ikiwa wao wanataka waletewe adhabu kwa upesi, basi ndio tabia ya binaadamu kutaka kila jambo kwa haraka. Basi enyi wenye haraka! Nitakuonesheni neema yangu duniani, na adhabu yangu Akhera. Msijishughulishe kuhimiza kitu ambacho hakina budi kuwa. Maoni ya wataalamu juu ya Aya 37: "Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi msinihimize." Makusudio ya kauli ya "Ishara" ni ishara za maumbile zenye kuonyesha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na uweza wake. Na ujuzi wa ilimu za sayansi utavumbua kwa mujibu wa itavyo nyanyuka akili ya binaadamu. Na hayo ni kwa mujibu wa miadi ilio wekwa kwa wakati wake. Kila ukifika wakati maalumu Mwenyezi Mungu hudhihirisha Ishara yake, au huwasahilishia wanaadamu njia za kuzifikilia Ishara hizo.
 

 

39. Lau kuwa hao walio mkufuru Mwenyezi Mungu wangeli ijua hali yao wakati watapo kuwa hawawezi kuuondoa Moto kwenye nyuso zao na migongo yao, na wala hawampati wa kuwasaidia kuuondoa, wasingeli sema wayasemayo.
 

40. Kiyama hakiwajii kwa kukitarajia kutokea kwake, bali kitawazukia kwa ghafla tu kiwababaishe, wasiweze kukirudisha, wala wao hawatapewa muhula wa kutubia na kutafuta udhuru kwa waliyo kwisha yatenda..
 

41. Na Mitume wa kabla yako yaliwapata vile vile ya kufanyiwa kejeli na makafiri katika kaumu zao. Ikawateremkia hao walio wakataa Mitume na kuwafanyia maskhara adhabu hiyo hiyo ambayo wao waliifanyia maskhara na kejeli.
 

42. Ewe Nabii! Waambie: Ni nani anaye kuhifadhini na nakama zake wakati wa usiku na mchana, na akakurehemuni na kukuneemesheni? Hapana awezae hayo. Lakini wao wanaipuuza Qur'ani ambayo ndiyo inawakumbusha ya kuwafaa na kuwalinda na adhabu.
 

43. Kwani wao wanao miungu wa kuwalinda na adhabu itokayo kwetu? Hasha! Hiyo miungu yao haiwezi kujilinda wenyewe, licha kumlinda mwenginewe. Wala hapana yeyote awezae kumlinda yeyote kati yao karibu yake au pamoja naye pindi tukitaka kumuadhibu na kumteketeza.
 

44. Sisi hatufanyi haraka kuwaadhibu hawa kwa ukafiri wao, lakini tunawapururia na kuwastarehesha katika uhai wa dunia, kama tulivyo wastarehesha baba zao kabla yao, mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je! Wanajitia upofu hawaoni yanao wazunguka wakaona kuwa Sisi tunaiendea nchi na tukaipunguza ncha zake kwa ushindi wa Waumini? Ni wao ndio wenye kushinda au Waumini ambao Mwenyezi Mungu amewaahidi kuwasaidia na kuwaunga mkono? Maoni ya wataalamu juu ya Aya 44: "Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza mipaka yake? Basi je! Hao ni wenye kushinda?": Aya hii ni katika Aya za miujiza ya kisayansi katika Qur'ani Tukufu. Hii inaonyesha kuwa dunia si mduwara kaamili. Na wataalamu wa sayansi hawakutamakani kupima masafa ya dunia baraabara mpaka kiasi ya miaka 250 tu takriban, walipo ingia kikundi cha mabingwa walio khusika na ilimu ya kupima marefu baina ya daraja mbili za urefu longitudes. Na hayo kwa pahala mbali mbali duniani. Katika kupima huku ikadhihiri kuwa nusu ya kati ya dunia kwenye equator inazidi kuliko nusu ya poles kwa takriban kilomita 21.5. Yaani dunia imepungua katika ncha zake, yaani katika poles. Na inajuulikana maalumu kuwa sura ya dunia na masafa yake ndio msingi katika kuchorwa kwa ramani.
 

45. Ewe Nabii! Sema: Sikuhadharisheni kwa maneno yanayo tokana nami. Lakini nakuhadharisheni kwa Wahyi (Ufunuo) unao tokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu ulio nijia mimi. Na huo ni wa Haki na kweli. Lakini hao kwa sababu ya kupuuza kwao kurefu kuipuuza Sauti ya Haki, Mwenyezi Mungu ameyaziba masikio yao mpaka wakawa kama viziwi. Na kiziwi hasikii Wito anapo hadharishwa na adhabu!
 

46. Na kuwa na yakini kuwa nao wakisibiwa hata na chembe ya adhabu ndogo wanayo ifanyia maskhara, hupiga kelele kwa khofu wakisema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa tunajidhulumu nafsi zetu, na tukiwadhulumu wenginewe, tulipo yakataa tuliyo ambiwa.
 

47. Na Sisi tunaweka mizani ya kupimiwa kwa uadilifu Siku ya Kiyama. Basi hadhulumiwi mtu kwa kupunguziwa wema wake au kuongezewa maovu yake. Hata ikiwa ni kiasi ya uzani wa chembe ndogo hii tutaileta na tutaihisabu. Na yatosha kuwa ni Sisi ndio wa kuhisabu. Basi hapana atakaye dhulumiwa kitu. Maoni ya wataalamu juu ya Aya ya 47: "Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu.": Aya hii tukufu inaonyesha kuwa chembe ya khardali ni hadi ya udogo katika mizani. Imethibitika kwa majaribio ya sayansi kuwa Kilogram ya chembe za khardali ni chembe 913,000. Kwa hivyo chembe moja ya khardali ni takriban sehemu moja katika elfu ya gram, yaani ni takriban sawa na Miligram moja. Na huu ni uzito mdogo kabisa unao juulikana katika mbegu za mimea mpaka sasa. Kwa hivyo hutumiwa katika kupimiwa vitu vidogo vidogo kabisa.
 

48. Na Musa na Haaruni tuliwapa Taurati ya kupambanua baina ya kweli na uwongo, na halali na haramu. Na juu ya hivyo hiyo ni nuru ya kuwaongoa watu wafuate njia ya kheri na uwongozi mwema, na ni kumbusho la kuwafaa wachamngu...
 

49. Ambao wanamkhofu Muumba wao Mwenye kumiliki mambo yao yote, juu ya kuwa wako mbali na watu, na wala hawamwoni mtu. Nao wamo katika khofu ya daima kuikhofu Siku ya Kiyama.
 

50. Na hii Qur'ani ni kumbusho, lenye kheri nyingi. Tumekuteremshieni kama tulivyo mteremshia Musa. Basi yawaje nyinyi muikatae, na hali nyinyi ndio mnao stahiki zaidi kuiamini kuliko watu wote!
 

51. Na hakika Sisi tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu na fikra ya kutafuta Haki kwa usafi wa niya kabla ya Musa na Haaruni. Na Sisi ni Wenye kujua vyema hali yake na fadhila zake zilizo mfanya astahiki kuchukua Utume.
 

52. Ewe Nabii! Kumbuka pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na watu wake kuwaonya juu ya masanamu waliyo kuwa wakishughulikia kuyaabudu: Ni nini haya masanamu ambayo nyinyi mmeshika kuyaabudu?
 

53. Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyatukuza na wameshika kuyaabudu. Nasi tukawafuata.
 

54. Yeye akasema: Nyinyi na baba zenu kabla yenu, ni wazi kuwa nyote mko mbali na Haki.
 

55. Wakasema: Je! Umetujia kwa haya uyasemayo na hakika ya kweli unayo iamini, au kwa maneno haya wewe ni katika wanao fanya pumbao na mchezo tu bila ya kuwa na maana yoyote?
 

56. Akasema: Hapana maskhara katika niyasemayo. Bali Mola wenu Mlezi anaye stahiki peke yake kutukuzwa na kuogopwa na kuabudiwa ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akazileta bila ya kuwapo mfano wake wa kuigiza. Basi ni haki yake Yeye tu peke yake kuabudiwa. Na mimi kwa haya niyasemayo ni katika wenye hakika ambao hunena wanayo yashuhudia na wanayajua.
 

57. Na akasema moyoni mwake: Naapa kwa Mwenyezi Mungu, nitayafanyia vitimbi haya masanamu yenu niyavunje pale mtapo ondoka, ili mpate kuona upotovu wenu.
 

 

59. Baada ya kwisha ona yaliyo wapata miungu yao wakasema: Nani aliye itendea haya miungu yetu? Hakika mtu huyu hapana shaka ni katika walio jidhulumu wenyewe kwa adhabu itayo mpata..
 

60. Wakasema baadhi yao: Tumemsikia kijana mmoja akiitaja kwa kuisubu; naye anaitwa Ibrahim.
 

61. Wakasema wakubwa wao: Nendeni mkamlete, ahukumiwe mbele ya macho ya watu, na washuhudie aliyo yatenda!
 

62. Baada ya kwisha mhudhurisha, wakasema: Ni wewe ulio itenda haya miungu yetu, ewe Ibrahim?
 

63. Kuwanabihisha upotovu wao, alisema kwa kuwakejeli: Hili kubwa lao ndilo lililo tenda hayo! Iulizeni hiyo miungu aliyo yatenda huyu, kama kweli inaweza kujibu suala yenu!
 

64. Wakazirejea nafsi zao wakiifikiria ile ibada yao kuabudu vitu visivyo mnufaisha yeyote wala haviwezi kujitetea wenyewe. Wakayaona makosa yao. Baadhi yao wakasema: Ibrahim si katika walio dhulumu, bali nyinyi ndio madhaalimu kwa kuabudu vitu visio stahiki kuabudiwa.
 

65. Kisha wakarejea tena, wakaacha uwongofu, wakarudia upotovu. Wakamwambia Ibrahim: Hakika wewe umekwisha jua kuwa haya masanamu tunayo yaabudu hayasemi kitu. Basi vipi unatutaka tuyaulize?
 

66. Ibrahim akasema: Ikiwa hali yao haya masanamu ni hii, hayawezi kitu, na nyinyi ndio makhusiano yenu nao ni hivi, basi nyinyi mmekuwa mnaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu, na badala yake mnaabudu vitu visivyo kupeni faida hata chembe mkiviabudu, wala havikudhuruni kwa lolote mkiviachilia mbali?
 

67. Aibu yenu! Nyinyi na miungu yenu mmelaanika! Mnaacha fikra zenu zipotee, na mnapuuza kuzingatia? Bila ya shaka haya masanamu hayafai kuabudiwa!
 

68. Wakaambiana wenyewe kwa wenyewe: Mchomeni moto mpate kuinusuru miungu yenu kwa mateso haya, ikiwa nyinyi mnataka kufanya kitu cha kuiunusuru miungu yenu.
 

69. Sisi tukaufanya moto ule uwe baridi na salama, hauna madhara yoyote, kwa Ibrahim.
 

70. Wao walitaka kumuangamiza, lakini Sisi tukamwokoa, na tukawafanya wao ndio watu walio khasiri mno.
 

71. Na tukamwokoa yeye na Luut'i na njama zilizo pangwa, wakaelekea kwenye nchi tuliyo ijaalia kheri nyingi kwa watu wote, na tukawapeleka huko Manabii wengi.
 

72. Na tukampa Ibrahim mtoto Is-haq, na kutokana na Is-haq tukampa Yaaqubu, zaidi kuliko aliyo taka. Na wote wawili, Is-haq na Yaaqubu tuliwajaalia kuwa ni watu wema.
 

73. Na tukawafanya ni Manabii wakiwaendea watu, wakiwaongoa kwenye kheri kwa mujibu wa tulivyo waamrisha. Na tukawaonyesha vitendo vyema, na kudumisha Sala kama inavyo faa, na kutoa Zaka. Na wakawa wanatunyenyekea na kutusafia ibada Sisi tu.
 

74. Luut'i tukampa kauli ya kukata na madhubuti katika hukumu na ilimu yenye manufaa. Na tukamwokoa kutokana na mji ambao watu wake wanafanya kitendo cha namna ya peke yake katika uovu. Hakika hao walikuwa watu walio shikilia kufanya maovu, walio toka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu na tabia iliyo zowewa.
 

75. Tukampeleka njia ya watu wa rehema yetu. Hakika huyo alikuwa miongoni mwa watu wema alio wakusanya Mwenyezi Mungu katika rehema yake na akawakunjulia msaada wake.
 

 

77. Tukamlinda kwa nusura yetu na vitimbi vya kaumu yake walio zikanusha Ishara zetu zenye kuthibitisha Utume wake. Hakika hao walikuwa watu wa shari. Basi tukawagharikisha wote!
 

78. Ewe Nabii! Wataje Daud na Suleiman walipo toa hukumu katika kesi ya konde, ilio ingiliwa na mbuzi wa watu mbali usiku na wakala mazao yake. Na Sisi tulikuwa tunaijua hukumu iliyo khusiana na kesi hiyo. Kisa cha hiyo hukumu: Mbuzi waliingia usiku mmoja katika konde ya mtu, wasibakishe kitu. Daud akahukumu kuwa wale mbuzi wawe wa mwenye konde kulipia khasara yake. Suleiman akatoa hukumu nyengine, akasema: Mbuzi wale wabakie mkononi mwa mwenye konde mpaka itapo mea tena mazao yake, na avumilie kwa yaliyo mpata. Na baada yake warejesheane.
 

79. Basi tulimfahamisha Suleiman hiyo fatwa. Na wote wawili tuliwapa hikima na ilimu ya maisha na mambo yake. Na tulimfanyia Daud pamoja na milima it'ii na imtakase Mwenyezi Mungu kama alivyo kuwa anamtakasa yeye Daud na kila lisio kuwa linamwelekea Mwenyezi Mungu. Na kadhaalika tuliwafanya ndege hivyo hivyo wamsabihi Mwenyezi Mungu pamoja naye. Na tulifanya hayo kwa uweza wetu usio shindika.
 

80. Tukamfundisha Daud kufuma nguo za chuma, ili zikulindeni katika vita vyenu. Basi mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa neema hii aliyo kuneemesheni.
 

81. Na tulimsahilishia Suleiman upepo unao vuma kwa nguvu umtumikie, nao huo ulikuwa unakwenda kwa kufuata amri yake mpaka kwenye nchi tuliyo izidishia kheri yake. Nasi ni wenye kuyajua yote hayo. Halitupotei kubwa wala dogo.
 

82. Na tukawafanya mashetani wamtumikie kwa kuzamia chini baharini kumletea lulu na marijani; na wakifanya kazi nyenginezo, kama kujenga ngome na majumba ya kifalme. Na Sisi tulikuwa tukiwaangalia katika kazi zao hizo, basi hapana hata mmoja wao aliye pata shida, wala hawakuvunja amri ya Suleiman.
 

83. Ewe Nabii! Mtaje Ayyubu, pale alipo mwita Mola wake Mlezi, na maradhi yalikwisha mdhoofisha, na akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika nimesibiwa na madhara na yananiuma! Na Wewe ni Mbora wa wanao rehemu..
 

84. Tukamwitikia kwa aliyo yaomba, tukamwondolea madhara, na tukampa watoto kwa kadri ya waliyo kwisha kufa. Na tukamwongezea mfano wa wale, kuwa ni rehema iliyo tokana na fadhila yetu, na pia ni kuwa ni kumbusho kwa wenginewe wanao tuabudu ili wapate nao kusubiri kama alivyo subiri yeye, na watumai kupata rehema ya Mwenyezi Mungu kama alivyo tumai yeye.
 

85. Ewe Nabii! Watajie watu wako khabari za Ismail, na Idris, na Dhulkifli. Wote hao ni miongoni wanao subiri wakahimili taklifa na shida.
 

86. Na tukawajaalia miongoni mwa watu wa kupata rehema yetu. Hakika hao ni katika waja wetu wema.
 

87. Ewe Nabii! Taja kisa cha Yunus, aliye mezwa na samaki..Pale alipoona dhiki kwa vile watu wake walipo puuza wito wake, naye akawahama akenda mbali nao na huku amewakasirikia. Akadhani ya kuwa Mwenyezi Mungu amemruhusu kuwahama, na kwamba haitopita hukumu juu yake. Samaki akammeza, na akaishi katika kiza cha bahari. Akamwita Mola wake Mlezi kwa kumnyenyekea, na kuungama aliyo kuwa nayo, akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hapana wa kuabudiwa kwa haki ila Wewe. Ninakutakasa na kila lisio kuelekea Wewe. Ninaungama kuwa hakika mimi nilikuwa miongoni mwa walio dhulumu nafsi zao kwa kutenda yasio kupendeza.
 

88. Tukamwitikia kwa aliyo kuwa akiyaomba, na tukamvua na dhiki aliyo kuwa nayo. Na mfano wa hivi ndivyo tunavyo waokoa Waumini wanao ungama makosa yao, na wakatuomba kwa usafi wa moyo.
 

89. Na kitaje kisa cha Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi baada ya kwisha ona uweza wake Subhanahu kwa alivyo mtia katika nafsi yake matarajio ya rehema yake. Alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Usiniache mpweke bila ya kuwa na mrithi, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi. Kwani Wewe ndiye utakaye baki baada ya kumalizika viumbe vyote.
 

90. Tukamtimizia matumaini yake, na tukamwitikia dua yake, na tukamtunukia juu ya ukongwe mwanawe, Yahya, tukamfanya mkewe tasa aweze kuzaa. Hakika wasafi hao Manabii walikuwa wepesi wa kutenda kheri tunayo waitaka waitende, na wanatuomba kwa kutumai rehema yetu, na kuikhofu adhabu yetu. Na walikuwa hawamtukuzi mtu wala hawamwogopi mtu isipo kuwa Sisi tu.
 

91. Pamoja na hawa simulia kisa cha Maryamu aliye ulinda uke wake, nasi tukamfikishia siri katika siri zetu. Tukamjaalia achukue mimba bila ya mume, na tukamjaalia mwanawe azaliwe bila ya baba. Akawa yeye na mwanawe dalili iliyo wazi ya uweza wetu kugeuza sababu na vinavyo sabibishwa. Na hakika Sisi ni waweza wa kila kitu.
 

92. Hakika mila hii, nayo ndiyo Uislamu, ndiyo mila iliyo sahihi inayo kupasini kuilinda, kwa kuwa ni mila moja iliyo shikamana wala haikukhitalifiana baina ya hukumu zake. Basi nanyi msifarikiene katika mila hii kwa makundi na vyama. Na Mimi ndiye Muumba wenu, na Mwenye kumiliki mambo yenu yote. Basi niabuduni Mimi tu, wala msinishirikishe na mwengine.
 

93. Na juu ya kuwepo uwongozi huu aghlabu ya watu wamegawanyika kwa mujibu wa matamanio yao, wakafanya mambo yao ya Dini mapande mapande, wakawa makundi mbali mbali. Na kila kundi litaturejea Sisi tulihisabie vitendo vyake.
 

94. Basi mwenye kutenda vitendo vyake vyema, naye ni mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Dini yake aliyo iridhia, hatopunguziwa kitu katika juhudi yake. Bali atalipwa malipo kaamili. Na Sisi ni wenye kuiandika hiyo juhudi yake. Basi hakitopotea kitu.
 

95. Na haitakuwa kwa watu wa mji tulio uteketeza kwa sababu ya dhulma yao kwamba hawatarejea kwetu Siku ya Kiyama, bali hapana budi kuwa watarejea na tutawahisabia vitendo vyao viovu.
 

96. Mpaka itapo funguliwa milango ya shari na ufisadi, wakaingia wana wa Juju na Maajuju wakikimbizana kuteremka milimani na majiani kwa kufanya vitendo vya fujo na rabsha.
 

97. Na ikakaribia miadi iliyo haina budi kutimizwa, nayo ni Siku ya Kiyama, wakawa wale walio kufuru wanakutikana wakikodoa macho yao kwa wingi wa kitisho, wakipiga makelele kusema: Kitisho gani hichi cha kutuangamiza! Hakika sisi tulighafilika na Siku hii. Bali tulikuwa ni wenye kujidhulumu nafsi zetu kwa ukafiri na inda.
 

98. Wataambiwa makafiri hawa: Nyinyi na hiyo miungu mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Moto wa Jahannamu. Nyinyi mtaingia humo muadhibiwe!
 

99. Lau kama hawa mlio waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni miungu inayo stahiki kuabudiwa, wasingeli ingia nanyi humo. Na nyote, wenye kuabudu na kuabudiwa, mtabaki Motoni, wala hamtatoka.
 

100. Humo watatoa pumzi zitokazo vifuani kwa sauti kama ya mwenye kukabwa, kwa dhiki watayo pata, na hawatasikia la kuwafurahisha.
 

101. Hakika wale tulio wakubalia kwa kufuata kwao Haki na vitendo vya kheri, na tukawaahidi malipo mema, hao watawekwa mbali kabisa na Jahannamu na adhabu yake.
 

102. Hawatasikia sauti ya Moto wake unavyo vuma. Nao huko watapata kila ambacho nafsi inatamani, daima milele.
 

103. Hawato huzunishwa na Kitisho Kikubwa kinacho wafazaisha makafiri. Na Malaika watawapokea kwa kuwapongeza kwa kusema: Hii ndiyo Siku yenu ya neema aliyo kuahidini Mola wenu Mlezi!
 

104. Siku tutapo zikunja mbingu kama zinavyo kunjwa karatasi katika kitabu. Na tutawarejeza viumbe kwa ajili ya hisabu na malipo. Wala hatushindwi kuwarejeza, kwani tuliwaumba mara ya kwanza. Na kama tulivyo waanza tutawarejeza. Ahadi yetu kwa hayo ni ahadi ya kweli. Daima Sisi tunatenda tunayo yaahidi.
 

105. Na tulikwisha andika katika Zaburi - nacho ni Kitabu cha Daud baada ya Taurati - kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema wapate kuitengeza, na kusahilisha njia za maisha bora humo. ("Bali wenye upole watairithi nchi"..Zaburi 37.11 "Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele".. Zaburi 37.29)
 

106. Hakika katika haya tuliyo yataja, khabari za Manabii pamoja na kaumu zao, na khabari za Pepo na Moto, yanatosha kuwakumbusha na kuwafanya wazingatie watu walio tayari kumuabudu Mwenyezi Mungu pekee na hawasalitiki na mapambo ya dunia.
 

107. Na hatukukutuma, ewe Nabii, ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.
 

108. Ewe Nabii! Sema: Hakika kiini cha Wahyi aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni kwamba hakika nyinyi hamna Mungu isipo kuwa Yeye. Na yote yaliyo bakia niliyo funuliwa yanafuata asili hii. Ikiwa mambo ni hivyo, basi inakuwajibikieni mjisalimishe na mnyenyekee kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
 

109. Wakito ujali wito wako, basi waambie: Nimekufunzeni yote aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi; na kwa hivyo tumekuwa sawa kwa kuyajua hayo. Wala mimi sijui hayo ya kufufuliwa na kuhisabiwa mliyo ahidiwa, yatakuwa karibu au mbali.
 

110. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua yote yasemwayo, mnayo yadhihirisha na mnayo yaficha.
 

111. Na sijui pengine huko kupewa muhula na kuakhirishiwa adhabu nyinyi ndio Mwenyezi Mungu anakufanyieni mtihani tu, na kukustarehesheni kwa ladha za maisha mpaka alipo kadiria Mwenyezi Mungu kukuhisabieni kwa hikima yake.
 

112. Ewe Nabii! Sema: Ewe Mola Mlezi! Tuhukumu baina yangu na hawa nilio wafikishia Wahyi kwa uadilifu ili wasiwe sawa Waumini na makafiri. Na Mola wetu Mlezi Mwenye kuneemesha kwa neema kubwa, Mwenye kustahiki kuhimidiwa na kushukuriwa, ndiye wa kutakiwa msaada kuvunja uzushi mnao zua, enyi makafiri.
 

Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani