1. Hizi ni Aya za Kitabu cha
kusomwa, chenye kubainisha, chenye kuweke wazi.
2. Watapenda, na watatamani sana
makafiri wanao zikanya Aya za Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, watapo ona
adhabu ya Siku ya Kiyama, lau kuwa walisilimu walipo kuwapo duniani, na
wakafuata kwa ikhlasi Dini ya Mwenyezi Mungu.
3. Lakini sasa wamo katika
kughafilika, hawazingatii adhabu itakayo wapata Akhera! Basi ukisha wafikishia
ujumbe wako, na ukawaonya, waachilie mbali. Wao hawana hamu ila kula, na
kustarehe kwa ladha za dunia. Tamaa ya uwongo inawazuga. Na hakika bila ya shaka
yoyote watakuja jua yatakayo wapata pale watapo yaona kwa macho yao Siku ya
Kiyama.
4. Na ikiwa wao wanataka
wateremshiwe adhabu ya duniani, kama Mwenyezi Mungu alivyo wateketeza walio kuwa
kabla yao, basi wajue kuwa Mwenyezi Mungu hauteketezi mji wowote ila kwa wakati
wake maalumu.
5. Hawatangulii wala hawataakhari.
6. Na uovu wa hali yao na wingi wa
kughafilika kwao hata imefika hadi kumuita Nabii wao kwa kejeli wakisema: Ewe
uliye teremshiwa Kitabu cha kukumbusha! Hapana shaka kuwa wewe una wazimu moja
kwa moja! Huko kumuita kuwa ndiye aliye teremshiwa Ukumbusho, yaani Mawaidha,
hakukuwa ila ni kwa kejeli tu, kumfanyia maskhara.
7. Na hadi ya ukafiri wao
walizidisha juu ya matusi hayo na kejeli kwa kusema: Laiti badala ya hicho
Kitabu kilicho teremshwa ungeli tuletea Malaika wakawa ndio hoja yenyewe, kama
wewe ni msema kweli miongoni mwa wenye kusema kweli!
8. Na Mwenyezi Mungu aliye tukuka
neno lake aliwajibu: Sisi hatuwateremshi Malaika ila huwa pamoja nao Haki ya
nguvu yenye kuthibiti ambayo haina njia ya kuikataa. Basi wakiikanya huwa tena
hawapewi muhula wowote, bali huteremshiwa adhabu ya hapa hapa duniani hapo hapo!
9. Na hakika, kwa ajili ya kuwa
Wito wa Nabii huyu kwendea Haki udumu mpaka Siku ya Kiyama, hatuwateremshi
Malaika, bali tumewateremshia hii Qur'ani ambayo kukumbusha kwake kunaendelea
daima dawamu. Na Sisi ndio wenye kuilinda isiingiliwe na mageuzo na mabadiliko
yoyote mpaka kusimama Kiyama.
10. Na ewe Mtume
Muaminifu! Usihuzunike; kwani Sisi tuliwatuma Mitume kabla yako kwa mataifa
ambao wameshikilia upotovu kama hao walivyo shikilia. Na wao wamepita pamoja na
wa kale walio teketezwa kwa ukafiri wao!
11. Wala mtindo wao hao
walio watangulia kwa kushikilia upotovu haukuwa ila kuwafanyia maskhara Mitume
wao, Mtume baada ya Mtume, kama wanavyo kufanyia kejeli wewe! Huo ndio mtindo wa
wapotovu!
12. Kama tulivyo itia
Qur'ani katika nyoyo za Waumini ikaingiza mwangaza, basi kadhaalika tumeingiza
upotovu katika nyoyo za walio pigwa muhuri wa ukosefu; hali ya katika nyoyo zao
ikawa kinyume cha hayo. Upotovu ukatia mizizi katika roho zao.
13. Wakhalifu hao
hawaamini. Na mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwapa muhula mpaka waione adhabu
chungu ya Siku ya Kiyama ndio kama ulivyo kwisha tangulia.
14. Watu hao wanataka
wateremshiwe Malaika. Ewe Nabii! Usidhani kuwa ndio wataamini wakiteremshiwa.
Bali hata tungeli wafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda huko wakaona
maajabu yaliyoko, na wakawaona Malaika,
15. Bado wasingeli amini,
na wangesema: Macho yetu yamefumbwa tusione, na yamefunikwa. Bali hayo si lolote
ila ni uchawi tu, tumerogwa! Basi hapana faida ya ishara yoyote maadamu nyoyo
zao zimeenea ukafiri.
16. Na Sisi tumeweka
mbinguni sayari na nyota, kwa makundi yenye hisabu zake na yenye kukhitalifiana
umbo lake na sura yake. Na kadhaalika tukazipamba kwa wenye kuziangalia kwa
kutuza na kuzingatia, na kuchunguza kwazo dalili za uwezo wa Muumbaji wao.
17. Lakini Sisi
tumezihifadhi na kila shetani anaye stahiki kupigwa vimondo na kufukuzwa kwenye
rehema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
18. Na yeyote katika hao
mashetani wanao jaribu kuibia kusikiliza maneno yanayo jiri baina ya wakaazi wa
hizi nyote, basi Sisi tunampopoa kwa vijinga vya moto vya mbinguni vinavyo
onekana wazi.
19. Na tumekuumbieni
ardhi, na tumekutengenezeeni mpaka ikawa kama busati lilio tandikwa, na tukaweka
ndani yake milima iliyo simama imara. Na tumekuotesheeni ndani namna mbali mbali
za mimea ya kukufaeni kwa uhai wenu, na tumeifanya kwa vipimo na zama maalumu
katika kukua kwake, na faida yake kwa kula, na kwa kadiri ya haja zenu na kwa
vipimo vyake, na sura yake kwa umbo na tabia. Aya hii inaeleza uhakika wa
uumbaji ambao haukujuulikana ila katika zama za hivi karibuni. Nayo ni kuwa kila
kabila ya mimea imefanana kati yao kwa kuonekana na undani wake, hata katika
sehemu zake ndogo ndogo, katika viungo vyake vyote vya hiyo mimea. Na hali
kadhaalika katika "Khalaya" au "Cells" za hiyo mimea ya kabila fulani, kwa ajili
ya kutimiza kazi iliyo kusudiwa kiungo hicho cha mmea. Na pia sehemu za mimea ya
hizo kabila zao na vilivyo undwa katika viungo vyake utaona mnasaba wake
umethibiti kila mwaka, ukilinganisha kwa wakati ule ule katika miaka mingine
20. Na tumekujaalieni
katika ardhi sababu za maisha mema. Kwani ndani yake yamo mawe ya kujengea
majumba, na wanyama mnao nafiika kwa nyama yao, au ngozi zao, au manyoa yao. Na
yapo maadeni yanayo toka chini ya ardhi, na mengineyo. Kama ilivyo kuwa humo
zipo sababu za kukuleteeni nyinyi maisha mema, basi humo pia wanapata maisha
wenginewe ambao wapo chini ya mamlaka yenu, kama watoto na wafwasi, ambao
Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye waruzuku wao na nyinyi.
21. Na hapana chochote cha
kheri ila kiko kwetu kama mahodhi yaliyo jaa, nasi tunakiweka tayari na
tunakitoa kwa wakati wake. Na hatuwateremshii waja wetu ila kwa kiasi maalumu,
kwa mujibu tunavyo pima kwa hikima yetu ya maumbile.
22. Na Sisi tulipeleka
pepo zilizo beba mvua na zilizo beba mbegu za mimea, na tukateremsha maji ya
kukunywesheni. Na hayo ni kwa kufuata vile tutakavyo. Na yeyote yule hawezi
kuyatenda kama hayo ila awe nayo kwake kama mahodhi au mabirika. Aya hii
imeitangulia sayansi kwa kusema kuwa upepo unafanya kazi kubwa katika kubeba
pollen, chembe dume za kupandishia mimea, kupelekea sehemu za uke za mimea
mingine, na kwa hivyo yakazalikana mazao. Na pia haikujuulikana ila mwanzo wa
karne hii tuliyo nayo kwamba upepo unazalisha mawingu yanayo nyesha mvua. Kwani
"Nucleons" ambazo juu yake hujumuika sehemu za mvuke wa maji na zikawa chembe
chembe za maji ndani ya wingu, ndizo chanzo cha mvua inayo chukuliwa na pepo
kupelekwa kwenye majimbo yanayo fikiwa na mawingu. Misingi ya hizo "Nucleons" ni
chumvi ya bahari, na vinavyo chukuliwa na upepo juu ya uso wa ardhi, na "Oxides"
na vumbi vumbi, n.k. Na vyote hivyo ni lazima kwa ajili ya mvua. "Wala si nyinyi
mnayo yaweka". Imethibiti kwa sayansi ya kisasa kuwa mvua inaanza kwa mvuke
kutokana na uso wa ardhi na bahari, kisha inarejea hali ile ile tena kama ilivyo
tajwa. Ikinya mvua hunywesha kila kilicho na uhai katika ardhi, na huinywesha
ardhi yenyewe. Wala haiwezekani kuzuilika, kwa sababu ikichuruzika kutokana na
vyote vyenye uhai na katika ardhi ikaingia baharini, tena kisha huanza kuzunguka
mara ya pili kwa kupanda mvuke kutoka baharini. Basi hali ni hivyo mzunguko.
Hapa ndio inabainika maana ya Aya "Wala si nyinyi mnayo yaweka."
23. Na ni Sisi tu peke
yetu ndio tunavipa vitu vyote uhai, kisha tunavipelekea mauti, kwani uumbaji
wote ni wetu.
24. Na kila mmoja wenu ana
muda wake alio pimiwa. Sisi ndio tunao ujua. Tunawajua walio tangulia kwa kufa
na kuwa hai, na pia wanao taakhari.
25. Na hakika walio
tangulia na walio taakhari watakusanywa wakati mmoja. Na Mwenyezi Mungu
atawahisabia na atawalipa. Na hayo ni kwa mujibu wa hikima yake na ujuzi wake.
Na Yeye ndiye anaye itwa Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. 26. Na Sisi katika
kuumba kwetu walimwengu katika dunia hii, tumeumba namna mbili - Tumemuumba mtu
kwa udongo mkavu wenye kutoa sauti ukigongwa.
26. Na Sisi katika kuumba
kwetu walimwengu katika dunia hii, tumeumba namna mbili - Tumemuumba mtu kwa
udongo mkavu wenye kutoa sauti ukigongwa.
27. Na makhaluku wengine
ni majini, ambao tuliwaumba mbele, alipo umbwa asili yake Iblisi kutokana na
moto mkali mno unao toka katika tundu za mwili wa mtu.
28. Ewe Nabii! Kumbuka
asli ya viumbe. Pale alipo sema Aliye kuumba, Mola Mlezi wa viumbe vyote,
kuwaambia Malaika: Mimi nataka kumuanzisha mtu niliye muumba kutokana na udongo
mkavu, wenye kutoa sauti ukigongwa, nao umebadilika rangi, na una sura.
29. Nikisha kamilisha
kumuumba, na nikampulizia roho ambayo ninaimiliki, basi teremkeni kwa nyuso zenu
mkimsujudia, kwa kumwamkia na kumhishimu.
30. Wakasujudu wote kwa
kuit'ii amri ya Mwenyezi Mungu.
31. Lakini Iblisi
alijivuna na akakataa kuwa pamoja na Malaika waliyo it'ii amri ya Mwenyezi
Mungu.
32. Hapo basi Mwenyezi
Mungu Mtukufu alisema: Ewe Iblisi! Kitu gani kilicho kupelekea hata ukaasi na
usiwe pamoja na wanyenyekevu walio sujudu?
33. Iblisi akasema: Si
shani yangu mimi kumsujudia mtu uliye muumba kwa udongo mkavu, wenye kutoa sauti
ukigongwa, nao umegeuka rangi, wenye kutiwa sura.
34. Mwenyezi Mungu Mtukufu
akasema: Ukiwa wewe umekuwa a'asi, umetokana na ut'iifu wangu, basi tokelea
mbali kwenye Bustani hii! Kwani hakika wewe umefukuzwa kwenye rehema yangu na
pahala pa hishima.
35. Na Mimi nimekwisha
kuhukumia ubaidike na rehema na utukufu mpaka Siku ya Kiyama, Siku ya Hisabu na
Malipo. Na hapo ndipo utapo pata adhabu, wewe na wanao kufuata .
36. Iblisi akasema, hali
naye kesha kuwa ni mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu: Ewe Muumba wangu! Nipe muhula,
nibakishe usinitwae mpaka Siku ya Kiyama, Siku watapo fufuliwa watu wakawa hai
baada ya kufa kwao.
37. Mwenyezi Mungu Mtukufu
akasema: Wewe utabakishwa, umepewa muhula,
38. Mpaka wakati niliyo
ukadiria, ninao ujua Mimi. Na kama utavyo kuwa mrefu una kikomo.
39. Akasema Iblisi,
mkhalifu, a'asi: Ewe Muumba wangu unaye nibakisha! Umenitakia upotofu, nami
nikatumbukia ndani yake. Basi kwa sababu hiyo nahakikisha kuwa nitawapambia
wanaadamu maovu wayaone mazuri, na nitafanya kila juhudi kuwapotoa wote!
40. Wala hawatoepukana na
upotovu wangu ila wale waja wako walio kufanyia ikhlasi Wewe na nisio weza
kuzimiliki nyoyo zao kwa zilivyo kuwa imara kwa kukumbuka Wewe.
41. Hakika usafi wa waja
walio isafia niya Dini yao ndio Njia Iliyo Nyooka, na haki yangu nisiikiuke,
kwani hao siwezi kuwapotoa. (Tafsiri hii yaonyesha maneno hayo ni ya Iblisi.
Lakini Tafsiri nyengine zinasema maneno hayo ni ya Mwenyezi Mungu, kwa mfano ya
Abdulla Saleh, Abdulla Yusuf, Pickthall, Razi, Baidhawi, Qurtubi, Zamakhshari,
Ibn Kathir, Assad.)
42. Mwenyezi Mungu Mtukufu
amesema: Hakika waja wangu walio nisafia Mimi Dini yao wewe huna uwezo wa
kuwapoteza. Lakini wapotovu, walio zama katika upotovu, walio kufuata wewe, basi
hao ndio unayo madaraka juu ya nyoyo zao.
43. Na hakika Moto mkali
mno ndio wameahidiwa hao wote kuwa ndiyo adhabu ya kutia uchungu.
44. Wala huo Moto mkali
hauna mlango mmoja tu, bali una milango saba kwa ajili ya wingi wanao stahiki
kuingia humo. Na kila mlango una kundi lake makhsusi. Na kila kundi una cheo
chake maalumu cha kulingana na uovu wake.
45. Haya ni malipo ya
wanao mfuata Shetani. Ama wale ambao Shetani kashindwa kuwapotoa, kwa kuwa
wameweka kinga baina yake na nyoyo zao, hao watapata Mabustani yaliyo bora, na
chemchem zinazo pita .
46. Mola wao Mlezi
atawaambia: Ingieni katika Bustani hizi kwa utulivu na amani. Kwani hapana khofu
juu yenu, hamhuzunikii nyakati zenu.
47. Na hakika watu wa
Imani wataishi katika kheri hii na nafsi zao zimetua. Kwani tumezitoa chuki
zilizo kuwamo katika nafsi hizo. Wote hao watakuwa ndugu waketi juu ya viti vya
enzi zikitazamana nyuso zao kwa furaha na mahaba, wala hawawi mmoja nyuma ya
mwenzie wakichunguliana visogoni.
48. Hawapatwi na machofu
huko. Na hiyo ni neema ya daima, wala hawatotoka humo milele.
49. Ewe Nabii muaminifu!
Wape khabari waja wangu wote kwamba Mimi ni Mwingi wa kughufiria na kusamehe kwa
mwenye kutubu, akaamini, na akatenda mema. Na kwamba Mimi ni Mwingi wa
kuwarehemu.
50. Na wape khabari kwamba
adhabu ninayo wateremshia wenye kuasi na kukufuru ni adhabu yenye kutia machungu
kweli, na adhabu yoyote nyengineyo haihisabiwi kuwa ina machungu mbele ya hii.
51. Ewe Nabii! Waambie
pia, katika kubainisha rehema yangu makhsusi katika dunia na adhabu yangu kwa
wenye kuasi humo, khabari ya Malaika walio mfikia Ibrahim kama wageni.
52. Ewe Muaminifu! Watajie
pale walipo ingia kwake, naye akawaogopa. Wao wakamwambia: Amani kwako, na
tulia! Yeye akasema: Sisi tunakuogopeni, kwani mmetujia kwa ghafla, sio wakati
wa dasturi wa kufika wageni, na hatujui mna nini!
53. Wakasema: Usiogope, na
tuwa moyo! Kwani tunakubashiria mwana, ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu atampa siku
zijazo za uhai wake ilimu kubwa. Inaonyesha hapa kuwa bishara hii si ya Ismail
a.s. Kwani Ismail alikuwa kesha zaliwa, naye na mama yake Haajir walikuwa wapo
Makka. Bishara hii ni ya Ibrahim na mkewe, basi kwa hivyo ni ya Is-haq mwana wa
Ibrahim na Sara.
54. Akasema: Vipi
mnanibashiria mtoto na hali mimi nimekwisha patikana na udhaifu wa ukongwe. Kwa
njia gani, basi, mnanibashiria jambo hili la ajabu?
55. Wakasema: Sisi
tunakubashiria jambo lilio thibiti, ambalo halina shaka kabisa. Basi usiwe
katika wanao kata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
56. Ibrahim akasema: Mimi
sikati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Kwani hawakati tamaa na rehema ya
Mwenyezi Mungu ila walio potea wasio utambua utukufu wake na uwezo wake.
57. Alivyo kuwa kaanza
kuzoeana nao, alisema: Ikiwa mmenibashiria khabari hii nzuri, je mna jambo gani
jenginelo mlilo nalo baada ya haya, enyi wajumbe mlio tumwa na Mwenyezi Mungu?
58. Wakasema hakika sisi
tumetumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa watu walio fanya ukhalifu katika Haki ya
Mwenyezi Mungu na haki ya Nabii wao, na haki ya nafsi zao wenyewe. Ukhalifu ndio
mtindo wao. Watu wenyewe ni kaumu ya Luut'i. Basi tutawateketeza.
59. Wala hakusalimika na
huo ukhalifu na adhabu yake ila ahli zake yeye Luut'i. Basi hao Mwenyezi Mungu
Mtukufu ametuamrisha tuwaokoe wote.
60. Na hatoangamia katika
ahli zake ila mkewe, kwani yeye hakumfuata mumewe, bali yu pamoja na hao
wakosefu ambao wanao stahiki adhabu.
61. Wale Malaika walio
tumwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuteremsha yaliyo ahidiwa, walipo fika nchi ya
Luut'i na watu wake,
62. Luut'i aliwaambia:
Watu nyinyi sikujuini, na nafsi yangu inatishika nanyi. Naogopa msituletee
balaa.
63. Wakasema: Usituogope,
kwani hatukukujia kwa unalo liogopa, bali tumekujia kwa jambo la kukufurahisha,
nalo ni kuwateremshia adhabu hawa watu wako walio kukadhibisha na wakawa
wanaitilia shaka hiyo adhabu au wanaikanya.
64. Nasi tumekujia kwa
amri iliyo thaabiti isiyo na shaka, nayo ni kuiteremsha adhabu. Na kutimiza
ahadi ni katika sifa yetu, kwa amri ya Mwenyezi Mungu.
65. Ilivyo kuwa adhabu
itawateremkia, basi wewe na ahli zako mlio andikiwa kuokoka, tokeni baada ya
kwisha ingia usiku.
66. Na Mwenyezi Mungu
Subhanahu wa Taa'la alimfunulia Luut'i kwa kumwambia: Sisi tumewahukumia na
kuwakadiria wakosefu kuteketea. Watang'olewa itapoingia asubuhi, wala hatobaki
hata mmoja wao.
67. Asubuhi kulipo
pambazuka waliwaona Malaika kwa sura ya binaadamu wazuri. Wao wale
wakawafurahia, wakaja ili wafanye nao vitendo vyao viovu, vya kuwaingilia
wanaume.
68. Luut'i akaogopa wasije
wakatenda vitendo vyao viovu. Akasema: Hawa ni wageni wangu, basi
msinifedheheshe kwa vitendo vyenu vibaya.
69. Na mwogopeni Mwenyezi
Mungu Mtukufu! Msifanye uchafu wenu, mkanipatisha hizaya na madhila mbele yao!
70. Wale wakhalifu
wakasema: Kwani si tulikukataza wewe usimkaribishe mtu yeyote, na hivi sasa tena
unatuzuia tusifanye nao tunayo yatamani?
71. Ili kuwanabihisha njia
ya maumbile ya kisharia, Nabii wa Mwenyezi Mungu Luut'i akasema: Hawa mabinti wa
mji huu, nao ni binti zangu, waoeni ikiwa mnataka kukidhi matamanio yenu.
72. Ewe Nabii Muaminifu!
Naapa kwa haki ya uhai wako! Hawa wamo katika mghafala, hawajui yatakayo
wateremkia. Wamekuwa kama walio lewa! Hakika wao wamo katika upotovu,
wanatapatapa, hawajui wapite wapi.
73. Na walipo kuwa wao
wamo katika ulevi wao wa mghafala nyoyo zao na akili zao zikachotwa na ukelele
mkali mno wa kutisha, wakati jua lilipo chomoza.
74. Mwenyezi Mungu Aliye
takasika katekeleza hukumu yake, akasema: Miji yao tukaifanya juu chini kwa
kuivuruga, na tukawateremshia udongo ulio fanyika mawe ukiwateremkia kama mvua.
Majumba yao yakaporomoka. Na wakitoka nje hukuta hiyo mvua ya mawe. Kwa hivyo
wakawa wamezungukwa kila jiha.
75. Haya yaliyo washukia
kaumu Luut'i ni alama wazi ya kuonyesha vipi Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo
timiza ahadi yake. Wajuao mambo wanayatambua hayo, na wanayaelewa matokeo yake
kwa alama zake, kwani kila kitendo chenye sifa ya ukosefu kina alama yake isiyo
potea. Matokeo yake ni mfano wa haya, duniani na Akhera.
76. Na mabaki ya mji huu
yapo yamesalia. Nayo yapo njiani katika njia inayo pitiwa na watu. Anaye taka
kuwaidhika kwayo anaweza kuwaidhika.
77. Kwa kuwa mabaki yake
yapo kwenye njia iliyo wazi ni dalili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutimiza onyo
lake, na Waumini wenye kut'ii Haki wanatambua hayo.
78. Kama kaumu ya Luut'i
walivyo kadhibisha, kadhaalika wakaazi wa Kichakani kwenye msitu wenye matunda
walimkanya Mtume wao. Wakawa madhaalimu wenye kudhulumu mno katika imani yao na
maingiliano yao.
79. Tukawateremshia nakama
yetu. Na mabaki yao yapo njiani yanaonekana, na mpita njia akiwa ni mtu wa Imani
basi anaweza kuzingatia kwayo.
80. Na kama walio tangulia
hali kadhaalika wakaazi wa Hijr walimkanusha Mtume wao aliye tumwa kwao, na kwa
hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote. Kwani ujumbe wa Mwenyezi Mungu ni mmoja.
Watu wa Hijr ndio Thamud. Na Hijr ni bonde baina ya Madina na Sham. Tazama
maelezo juu ya Aya 73 ya Surat Al-Aa'raaf.
81. Tuliwabainishia hoja
zenye kuonyesha uwezo wetu, na Utume wa Mtume wetu, nao wakayapuuza, wala
wasiyafikiri.
82. Nao walikuwa watu
wenye nguvu na wajenzi. Walikuwa wakijenga majumba yao katika milima na
wakiichonga hiyo hiyo milima. Na wao walikuwa wakijiamini kuwa wametua na nafsi
zao na mali yao.
83. Walipo kufuru na
wakakanya, zikawajia sauti za kutisha, za kuonya kuteketea kwao, wakahiliki
wakati wa asubuhi.
84. Wala mali waliyo
yachuma na majumba waliyo yajenga hayakuwalinda na hilaki iliyo wateremkia.
85. Hatukuumba mbingu na
ardhi na vilivyo kati yao katika anga, na viliomo ndani yake, watu na wanyama,
na mimea na visio na uhai, na vinginevyo ambavyo mwanaadamu havijui, isipo kuwa
kwa uadilifu, na hikima, na maslaha ambayo hayaambatani na fisadi ya kudumu
isiyo na mwisho. Na kwa hivyo basi ni lazima siku ya kukomesha shari ifike bila
ya shaka yoyote. Basi ewe Nabii Mtukufu! Wasamehe hao washirikina adhabu ya
duniani, na ingiana nao kwa kuwastahamilia maudhi yao. Na kuwaita wito kwa
hikima ni kuingiliana kwa usamehevu na upole.
86. Ewe Nabii! Mwenyezi
Mungu aliye kuumba na akakulea, ni Mwenye viumbe vyote, na anajua hali yako na
yao. Yeye anastahiki umtegemezee mambo yako na yao. Naye anajua maslaha yako na
yao.
87. Ewe Nabii Muaminifu,
tumekupa Aya saba za Qur'ani, nazo ni Sura ya Al- Fatiha unayo ikariri katika
kila Sala, na humo yamo ya kutunyenyekea na maombi ya uwongofu yaliyo kaamili.
Na tumekupa Qur'ani Tukufu yote. Na ndani yake mna hoja, na miujiza. Kwa hivyo
wewe una nguvu ambazo zinakufalia usamehe.
88. Ewe Mtume! Usivitazame
kwa kuvitamani na kuvitaka vitu vya starehe ya dunia tulivyo wapa makafiri wa
kishirikina, na Kiyahudi, na Kikristo, na Kimajusi. Kwani hivyo ni duni kwa
kulinganisha na ulio pewa wewe katika kuwasiliana nasi, na Qur'ani Tukufu. Wala
usiwasikitikie kwa sababu ya kuendelea kwao na madhambi. Nawe tulia, na
unyenyekee, na wachukue Waumini ulio nao kwa upole. Kwani hao ni nguvu za Haki,
na watu wa Mwenyezi Mungu.
89. Ewe Nabii! Waambie
makafiri wote: Mimi nakuonyeni na adhabu kali, na nakubainishieni maonyo yangu
kwa hoja za kukata.
90. Haya ni kama maonyo ya
walio igawanya Qur'ani wakaifanya ati ni mashairi, na ukohani, na hadithi za
kale na mengineyo. Nao wasiiamini juu ya kusimama hoja juu yao.
91. Hao waliifanya Qur'ani
vipande mbali mbali, nayo hali kuwa haikubali kugawika kwa umuujiza wake na
ukweli wake.
92. Ikiwa hiyo hali yao,
basi Wallahi kwa Aliye kuumba akakulinda na akakulea, hapana shaka tutawahisabu
wote Siku ya Kiyama,
93. Kwa vitendo vyao vya
kuudhi, na kufuru, na kejeli.
94. Basi wewe tangaza wito
wa Haki, wala usishughulike na wayatendao washirikina na maneno yao.
95. Na hao washirikina
wanao ukejeli wito wako hawatokushinda, wala hawatoweza kukuingilia kati baina
yako na wito wako.
96. Hao washirikina mawazo
yao yamedhoofika, ndio wakafanya kuwa Mwenyezi Mungu anao miungu mingine ya
masanamu. Na watakuja jua matokeo ya ushirikina wao itapo wateremkia adhabu
chungu.
97. Nasi tunajua dhiki ya
moyo inayo kupata kwa wanayo yasema ya ushirikina na kejeli na dharau.
98. Ikikupata dhiki hiyo
mkimbilie Mwenyezi Mungu Mtukufu umwelekee, na umt'ii na umnyenyekee, na utake
msaada kwa Sala, kwani humo ndio imo poza.
99. Na shikilia ibada ya
Mwenyezi Mungu aliye kuumba, akakulinda, mpaka ifike amri ya yakini, nayo ni
Kiyama na miadi.
Rudi kwenye
sura
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani