1. Alif
Lam Ra - Kwa kuanzia harufi hizi ni kunabihisha muujiza wa Qur'ani, juu ya kuwa
imeundwa kwa harufi hizi hizi zinazo tumiwa kwa kusemea. Na pia kuwazindua watu
waisikilize. Haya yaliyo tajwa katika Sura hii ni Kitabu kilicho teremshwa kwako
wewe, Muhammad, kutokana nasi, ili uwatoe watu wote kwenye kiza cha ukafiri na
ujinga waendee kwenye nuru ya Imani na ilimu, kwa kusahilishiwa na Mola wao
Mlezi. Na nuru hiyo ndiyo Njia ya Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kwa
kuadhibisha, na Mwenye kuhimidiwa kwa kuneemesha.
2. Njia ya
Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Mwenye kuumba na kumiliki kila kiliomo mbinguni na
kwenye ardhi. Ikiwa hii ndiyo hali ya Mungu wa Haki, basi makafiri, wenye
kukanya, watahilikika kwa adhabu iliyo kali.
3. Hao ndio
walio khiari uhai wa duniani kuliko Akhera, na wanawazuia watu wasifuate Sharia
ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotoa Sharia katika macho ya watu ili wapate
kuikataa. Hao ndio wanao elezwa katika yaliyo tajwa kuwa wamepotelea mbali na
Haki.
4. Na Sisi
hatukumtuma Mtume yeyote kabla yako, ewe Nabii, ila kwa lugha ya kaumu yake ile
tuliyo mtumia, ili apate kuwafahamisha aliyo kuja nayo, na wao wayafahamu, na
wayaelewe kwa wepesi. Wala si juu yake yeye kuwa lazima waongoke. Mwenyezi Mungu
Mwenyewe ndiye humwacha apotee anaye mtaka kwa kuwa huyo si tayari kuitaka Haki.
Na humwongoa amtakaye kwa kuwa kajitayarisha vyema kufuata Haki. Naye Mwenyezi
Mungu ndiye Mwenye nguvu ambaye hashindiki kwa atakalo, na ambaye anayapanga
mambo yote kwa mahala pao. Basi haachi kupotea wala haongoi ila kwa hikima yake.
5. Na tulimtuma
Musa na tukamuunga mkono kwa miujiza yetu. Tukamwambia: Watoe watu wako, Wana wa
Israili, kwenye kiza cha ukafiri na ujinga uwapeleke kwenye nuru ya Imani na
ilimu, na uwakumbushe vituko na nakama aliyo wapelekea Mwenyezi Mungu kaumu za
kabla yao. Hakika katika kukumbusha huko zipo dalili kubwa za kuthibitisha
Upweke wa Mwenyezi Mungu, zinamlingania kwenye Imani kila mwenye kuthibiti kuwa
na ukamilifu wa kuweza kuvumilia balaa, na kushukuru neema. Na hii ni sifa ya
Muumini.
6. Ewe Nabii!
Wakumbushe watu wako, huenda wakazingatia, wakati Musa alipo waambia watu wake
kwa kufuata amri ya Mola wako Mlezi: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu,
pale alipo kuvueni kutokana na kaumu ya Firauni, nao wakikupatilizeni kwa adhabu
ovu kabisa. Wakikufanyisheni kazi ngumu, wakiwachinja watoto wenu wa kiume, na
wakiwaacha wa kike na kuwaweka katika unyonge na udhalili bila ya kuwauwa. Na
mateso yote yaliyo tajwa na kuokoka ni mtihani mkubwa unao toka kwa Mwenyezi
Mungu, ili upate kudhihiri uwezo wa kusubiri na kushukuru.
7. Na
kumbukeni, enyi Wana wa Israil, pale Mola wenu Mlezi alipo kufunzeni, na
akasema: Wallahi! Mkishukuru kwa neema niliyo kupeni ya kukuvueni, na mengineyo,
kwa kuthibiti juu ya Imani na ut'iifu, basi hapana shaka nitakuzidishieni neema
yangu. Na mkiikanya neema yangu kwa ukafiri na maasi, basi hakika nitakuadhibuni
kwa adhabu ya kutia uchungu. Kwani adhabu yangu ni kali kwa wanao kanya.
8. Na Musa
aliwaambia watu wake walipo mpinga na kumkanya: Mkizikanya neema za Mwenyezi
Mungu, wala msishukuru kwa Imani na ut'iifu, nyinyi na wote waliomo duniani,
basi hakika hayo hayatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote. Kwani Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kujitosha, hahitajii shukra za wanao shukuru. Yeye ni Mwenye kustahiki
kuhimidiwa kwa dhati yake, bila ya yeyote kumhimidi.
9. Je!
Haijakufikilieni khabari za walio tangulia kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na A'adi,
na Thamud, na kaumu nyenginezo zilizo kuja baada yao, ambao hapana anaye wajua
ila Mwenyezi Mungu kwa wingi wao. Hao walijiwa na Mitume wao kwa hoja zilizo
wazi kuthibitisha ukweli wao. Na hao wakaweka mikono yao kwenye vinywa vyao, kwa
mastaajabu na kukanya. Wakawaambia Mitume: Sisi tunaikataa miujiza na ishara
mlizo kuja nazo. Na hakika sisi tuna shaka na hayo mnayo tuitia, mambo ya Imani
na Tawhidi, ya kuwa Mungu ni mmoja. Sisi hatukuyakinika na chochote, na tuna
shaka nayo!
10. Mitume
wakawaambia watu wao, kwa mastaajabu, kuvunja shaka zao za kuwepo Mwenyezi Mungu
na kuwa Yeye ni Mmoja peke yake: Hivyo katika kuwepo Mwenyezi Mungu Mmoja peke
yake ipo shaka yoyote, na hali Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi bila ya kuwepo
mfano wa kuigiza? Na Yeye anakuiteni apate kukusameheni baadhi ya madhambi mliyo
yatenda kabla hamjaamini, na anakuakhirisheni mpaka umalizike muda wenu! Hao
watu wakawaambia Mitume wao kwa kuudhi: Nyinyi si chochote ila ni watu tu,
wanaadamu, kama sisi. Hamna ubora wowote wa kukufadhilisheni juu yetu hata mpewe
Utume. Mnataka kwa huo wito wenu mtuzuie tusiabudu walio kuwa wakiabudu baba
zetu! Basi tuleteeni hoja iliyo wazi katika tunazo kwambieni.
11. Mitume wao
wakawaambia: Sisi si chochote ila ni watu kama nyinyi, kama mlivyo sema.
Walakini Mwenyezi Mungu huwateua awatakaye miongoni mwa waja wake akawapa Unabii
na Utume. Wala hatuna sisi uwezo wa kukuleteeni hoja mnayo taka ila Mwenyezi
Mungu apendavyo. Na ni juu ya Mwenyezi Mungu tu peke yake ndio wategemee
Waumini, na wamtegemee kwa kustahamilia inda zenu na upinzani wenu.
12. Na sisi
tuna udhuru gani wa kuacha kumtegemea Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye aliye
tuongoza kila mmoja wetu kwenye njia yake na maelekeo yake aliyo mwekea, na
akamlazimisha afuate katika Dini? Na hakika sisi tunatilia mkazo tegemeo letu
kwa Mwenyezi Mungu; na hapana shaka tutayavumilia maudhi yenu ya inadi na kutaka
miujiza. Na juu ya Mwenyezi Mungu peke yake ndio humtegemea wanao tegemea.
13. Wakuu wa
makafiri majabari wenye madaraka wakaazimia watumie nguvu walipo shindwa wote
kupambana kwa hoja na dalili. Wakawaambia Mitume wao: Na liwe moja ya mawili.
Ama tukutoeni katika nchi yetu, au muingie katika dini yetu. Mwenyezi Mungu
akawafunulia Mitume kwa wahyi: Tutawateketeza hao makafiri kwa dhulma yao!
14. Na baada
ya kuwateketeza tutakuwekeni nyinyi katika ardhi yao. Na huko kuwekwa kwa
Waumini ni kweli, hakika, kwa mwenye kukhofu kusimama mbele yangu kwa ajili ya
hisabu, na akakhofu ahadi yangu ya adhabu. Kwani mwenye kuingia na khofu huwa
mt'iifu.
15. Hao Mitume
waliomba nusura wawashinde hao watu wao wanao wapinga, baada ya kukata tamaa
kuwa hawataamini tena. Mwenyezi Mungu aliwanusuru, na wakafuzu, na akakhasiri
kila mwenye kiburi, akakataa kumt'ii Mwenyezi Mungu, akawa shadidi wa upinzani.
(Haya yaliyo wapata Mitume huwapata watu wa Mungu wote wanao wania Haki hata
katika zama zetu. Ushindi wa mwisho daima unakuwa kwa walio wema, hoja kuvumilia
na kuendelea na kazi ya Mungu).
16. Kushindwa
kwa hao madhaalimu kunatangulia hapa duniani, na baada yake Akhera ipo adhabu ya
Jahannamu. Huko watanyweshwa maji yanayo kirihi kama usaha unao toka kwa watu wa
Motoni!
17. Kunywa
kwake ni taklifu, ni kama wanayagugumia, na wala hayeshi kiu, kwani hayumkini
kuyaonea tamu kwa ukarihi wake na uchafu wake! Na mtu anakuwa ni kama
amezungukwa na mauti kila upande kwa shida ziliopo, na wala huko katika
Jahannamu hafi akapumzika na yanayo mfika, bali kila wakati anakuta adhabu
nyengine kali zaidi.
18. Hakika
hali za vitendo vya kheri wavifanyavyo makafiri duniani na pato lake, kwa kuwa
havikujengwa juu ya msingi wa Imani, hali yake ni kama jivu. Ukaja upepo mkali
ukalipeperusha siku ya kimbunga kilipo kaza. Siku ya Kiyama hawapati chochote
kutokana na vitendo vyao vya namna hivyo vya duniani. Hayumkini wao kunafiika na
chochote kutokana navyo, kwani hivyo havina thawabu, kama mtu mwenye vumbi
linalo peperuka katika upepo asilo weza kulikamata. Na watu hawa wapotovu
hujiona wenyewe ati kuwa ndio wanafanya mema, na ilhali vitendo vyao viko mbali
kabisa na Njia ya Haki.
19. Ewe unae
semezwa! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi zisimame juu ya
Haki kwa mujibu wa hikima yake? Na Mwenye kuweza haya basi anaweza
kukuteketezeni, enyi makafiri, na akitaka akaleta viumbe wengine badala yenu
nyinyi, ambao watakubali kuwepo kwake, na kwamba Yeye ni Mmoja wa pekee.
20. Na kuondoa
huko na kuleta si muhali wala si uzito kwa Mwenyezi Mungu.
21. Makafiri
wote watadhihiri kutoka makaburini kwao, waonekane kwa ajili ya kuhisabiwa na
Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kudhihiri huko hakuna shaka, ni kama kwamba yametokea
hivi sasa. Hapo wale wenye maoni ya kinyonge miongoni mwa wafwasi watawaambia
waongozi wenye kiburi: Sisi tulikuwa wafwasi wenu katika kuwakanusha Mitume na
kuwapiga vita, na kuzipuuza nasaha zao. Basi je, hii leo, hamtuondolei kidogo
baadhi ya adhabu? Wakubwa walio takabari watasema: Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu
ametuongoa kwenye njia ya kuokoka, na akatuwafikia, basi nasi tungeli kuongozeni
na tungeli kuitieni muifuate hiyo njia. Walakini sisi tumepotea na kwa hivyo
tukakupotezeni nyinyi, yaani tumekuchagulieni tuliyo jichagulia nafsi zetu. Na
leo hii sisi na nyinyi ni sawa sawa, tukisikitika au tukastahamili. Hapana pa
kuikimbilia adhabu hii!
21. Makafiri
wote watadhihiri kutoka makaburini kwao, waonekane kwa ajili ya kuhisabiwa na
Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kudhihiri huko hakuna shaka, ni kama kwamba yametokea
hivi sasa. Hapo wale wenye maoni ya kinyonge miongoni mwa wafwasi watawaambia
waongozi wenye kiburi: Sisi tulikuwa wafwasi wenu katika kuwakanusha Mitume na
kuwapiga vita, na kuzipuuza nasaha zao. Basi je, hii leo, hamtuondolei kidogo
baadhi ya adhabu? Wakubwa walio takabari watasema: Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu
ametuongoa kwenye njia ya kuokoka, na akatuwafikia, basi nasi tungeli kuongozeni
na tungeli kuitieni muifuate hiyo njia. Walakini sisi tumepotea na kwa hivyo
tukakupotezeni nyinyi, yaani tumekuchagulieni tuliyo jichagulia nafsi zetu. Na
leo hii sisi na nyinyi ni sawa sawa, tukisikitika au tukastahamili. Hapana pa
kuikimbilia adhabu hii!
23. Na Akhera
wataingizwa wenye kuamini, na wakatenda vitendo vyema, katika Mabustani yanayo
pitiwa na mito chini ya majumba yake, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na
amri yake. Maamkio yao humo kutokana na Malaika ni kufahamisha amani na utulivu.
24. Je, ewe
mtu! Hujui vipi Mwenyezi Mungu alivyo fananisha neno la Haki lilio zuri, na neno
la uwongo lilio baya? Amelimathili neno zuri lenye faida kuwa ni kama mti wenye
manufaa. Asili yake ni mizizi iliyo shikilia baraabara kwenye ardhi na matawi
yake yamenyanyuka kuelekea mbinguni.
25. Hutoa
matunda yake kila wakati aliyo uweka Mwenyezi Mungu yazae kwa mapendekezo ya
aliye yaumba. Hivyo hivyo ndio tamshi la Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu, ni
lenye kuthibiti katika moyo wa Muumini. A'mali yake inapanda kwa Mwenyezi Mungu,
na inamfikilia baraka zake na thawabu zake kila wakati. Na Mwenyezi Mungu
anawabainishia watu kwa mifano, anashabihisha maana kwa vitu wavijuavyo ili
Waumini wawaidhike.
26. Neno la
uwongo baya mfano wake ni kama mti mbaya ulio ng'olewa, umetupwa juu ya ardhi.
Haukusimama imara. Hali kadhaalika neno la uwongo lilio kataliwa halina
uthabiti, kwa kuwa halikuungwa mkono na hoja.
27. Mwenyezi
Mungu anawathibitisha imara wanao amini juu ya neno la Haki katika uhai wa
duniani na Siku ya Kiyama pia. Na Mwenyezi Mungu huwabaidisha nalo neno hilo
makafiri kwa kutojitengenezea wenyewe. Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo,
akiwathibitisha baadhi na kuwaacha kupotea wenginewe. Hapana wa kumtoa kombo kwa
hukumu yake, wala mwenye kuurudisha uamuzi wake!
28. Ewe
msikilizaji! Hebu huwaangalii hao washirikina ambao, badala ya kushukuru neema
ya Mwenyezi Mungu ya kumleta Muhammad na Dini yake, wakaingia kumkataa Mwenyezi
Mungu Mtukufu, na wakawasabibisha wafwasi wao kutumbukia katika nyumba ya hilaki
kwa upotovu wao.
29. Na nyumba
hiyo ndiyo Jahannamu wakiteswa kwa uvukuto wake. Na makaazi maovu mno ni
Jahannamu.
30. Na
wakamfanyia Mwenyezi Mungu Mmoja wa pekee mifano ya masanamu wakiyaabudu, kwa
ajili ya kuwa natija ya vitendo vyao iwe kuwapoteza watu wasifuate Njia ya
Mwenyezi Mungu! Ewe Nabii! Waambie hao walio potea: Stareheni na matamanio yenu,
kwani marejeo yenu ni Motoni!
31. Ewe
Muhammad! Waambie waja wangu walio sadiki, wakaamini, na wakatenda mema: Shikeni
Sala, na toeni baadhi ya tuliyo kuruzukuni katika njia za kheri, kwa siri na kwa
dhaahiri, kabla ya kufika siku ambayo haifai kitu kupatana kibiashara wala
hisani ya urafiki.
32. Ni
Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye zianzisha mbingu na viliomo ndani yake, na
ardhi na viliomo ndani yake. Na akateremsha kutoka mawinguni maji ya kumiminika.
Na kwa sababu yake akakutoleeni riziki ya matunda, na mazao mengine na miti. Na
Yeye akakufanyieni vyombo vya baharini vikufaeni vinakwenda na kupakia riziki
zenu, na bidhaa zenu za biashara, kwa idhini yake na kutaka kwake. Na akaifanya
mito ya maji matamu ikunufaisheni kwa kunywa nyinyi na kumwagia katika mashamba
yenu.
33. Na
akalifanya jua na mwezi yakufaeni daima dawamu, kwa mwangaza na maslaha ya mimea
na wanyama. Na akajaalia usiku ukufaeni kwa kupumzika na mchana kwa kufanya
kazi.
34. Na
akakutengenezeeni yote mnayo yahitajia katika maisha yenu ambayo anastahiki
kuombwa, sawa sawa ikiwa mmemuomba au la. Na mkizihisabu neema alizo
kuneemesheni Mwenyezi Mungu, hamwezi kuzidhibiti namna zake, seuze idadi yake!
Hakika huyo mwenye kukanya ambaye akalipa ukafiri kuwa ni malipo ya neema alizo
pewa, basi ni mwingi wa udhalimu na ukafiri!
35. Ewe Nabii!
Ili watu wako wapate kuzingatia na waache ushirikina wao, wakumbushe kauli ya
baba yao Ibrahim baada ya kuijenga Alkaaba. Alisema: Ewe Mola Mlezi! Ujaalie mji
huu wenye Alkaaba uwe wa amani, ulindwe na wenye kudhulumu. Na unibaidishe, niwe
mbali, mimi na wanangu na ibada ya masanamu.
36. Kwani
masanamu yamepelekea kupotea watu wengi kwa kuyaabudu. Basi katika dhuriya
zangu, wenye kunifuata mimi na wakakuabudu Wewe kwa ikhlasi, basi hao ni watu wa
Dini yangu. Na wenye kuniasi kwa kushika ushirikina, basi Wewe ni Muweza wa
kuwaongoa, kwani Wewe ni Mwingi wa maghfira na rehema.
37. Ewe Mola
wetu Mlezi! Hakika mimi nimewafanyia maskani baadhi ya dhuriya zangu katika
bonde la Makka ambalo halioti mimea, kwenye Nyumba yako uliyo kataza isiingiliwe
na kuvunjiwa hishima yake, na ukajaalia sehemu za jirani yake ziwe na amani. Ewe
Mola wetu Mlezi! Wakirimu wapate kushika Sala karibu na Nyumba hii. Na zijaalie
nyoyo za bora ya watu ziwapende kwa kuizuru Nyumba yako. Na uwaruzuku matunda
kwa kuletwa na hao watakao kuja, ili wapate kushukuru neema yako kwa Sala na
Dua.
38. Ewe Mola
wetu Mlezi! Ni sawa sawa kwako tunayo fanya siri na tunayo fanya dhaahiri. Kwani
Wewe unajua maslaha yetu, na unatuonea huruma zaidi kuliko sisi wenyewe. Na
hapana lifichikanalo kwako hata likiwa dogo, katika ardhi na katika mbingu. Basi
hapana haja sisi ya kukuomba. Lakini juu ya hivyo tunaomba kwa kuonyesha kuwa
sisi ni waja wako, twanyenyekea utukufu wako, na tunahitajia uliyo nayo, Wewe!
39.
Alhamdulillahi, Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu, aliye nipa juu ya kuwa ni mzee
wa miaka mingi, na nimekwisha kata tamaa ya kuzaa, Ismail na kisha Is-haq!
Hakika Mwenyezi Mungu anasikia na ananipokelea maombi yangu.
40. Ewe Mola
wangu Mlezi! Niwezeshe nitimize Sala kwa inavyo takikana. Na wawezeshe
watimilize kadhaalika wale walio wa kheri katika dhuriya zangu. Ewe Mola wetu
Mlezi ipokee dua yangu kwa mapokezi ya kukubaliwa.
41. Ewe Mola
wetu Mlezi! Nisamehe madhambi yaliyo niponyoka, na wasamehe wazazi wangu, na
Waumini wote, Siku itapo hakikishwa hisabu, na baadae ikawa malipo.
42. Ewe Mtume!
Wala usidhani kabisa kuwa Mola wako Mlezi ameghafilika na vitendo wafanyavyo
wenye kudhulumu, kuupiga vita Uislamu na Waislamu wenyewe. Bali Yeye anaujua
ukhalifu wao. Na amekadiria kuakhirisha kuwaadhibu mpaka Siku nzito. Macho yao
yatabaki yamekodoka, hawawezi kuyafumba, wala kupepesa kwa kitisho watacho
kiona.
43. Nao wako
mbioni kumwendea anaye wita, vichwa vyao vimeelekea juu mbinguni, macho yao
hayapepesi hata wakitaka, na nyoyo zao tupu hazina wazo lolote kwa wingi wa
khofu.
44. Ewe Nabii!
Waeleze watu khabari za vitisho vya Siku ya Kiyama watapo sema walio zidhulumu
nafsi zao kwa ukafiri na maasi: Mola wetu Mlezi, tuakhirishie adhabu, uturejeshe
duniani, na utupe muhula kwa muda mdogo, walau tudiriki kuitikia wito wako wa
Tawhidi na kuwafuata Mitume. Nao wataambiwa: Leo ndio mwasema haya? Na mmesahau
ya kwamba mliapa nyinyi ya kuwa mkifa neema hizi hazitokuondokeeni mtapo
fufuliwa Siku ya Kiyama.
45. Na mkakaa
duniani katika maskani zile zile za wale walio tangulia kuzidhulumu nafsi zao
kwa ukafiri na maasi miongoni mwa kaumu zilizo kuwa kabla yenu. Na ikadhihiri
kwenu kwa kuona mabaki ya vile tulivyo waadhibu wao, na nyinyi msiwaidhike. Na
tukakuelezeni waliyo yafanya wao, na nini kilicho wafika. Nanyi msizingatie.
46. Na
wakapanga hao washirikina njama zao kutaka kuvunja Daa'wa, yaani Wito. Na
Mwenyezi Mungu anazijua vyema hila zao. Wala vitimbi vyao haviwezi kuiondoa
Sharia iliyo thibiti imara kama milima.
47. Ewe Mtume!
Usidhani kuwa Mwenyezi Mungu atawatupa Mitume wake kwa kwenda kinyume na ahadi
aliyo wapa kuwa atawanusuru. Kwani Yeye daima ni Mwenye kushinda, hapana mmoja
awezaye kumzuia kwa alitakalo, ni Mkali wa kulipiza kwa anaye mkanya na kumuasi.
48. Basi
Mwenyezi Mungu atalipizia Siku ya Kiyama itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine
sio hii ya sasa, na mbingu hali kadhaalika zigeuzwe ziwe nyengine, na viumbe
watolewe makaburini mwao kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu asiye na mshirika, wala wa
kumshinda.
49. Utawaona
makafiri Siku ya Kiyama wamefungwa pingu pamoja na mashetani wao.
50. Ngozi zao
zimepakwa lami inayo chiririka, imekuwa kama ndio nguo juu ya ngozi zao. Na moto
umewapamba na kuwagubika nyuso zao.
51.
Wanafanyiwa hayo ili Mwenyezi Mungu apate kumlipa kila mmoja wao kwa aliyo
yachuma katika dunia. Na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu Siku ya Kiyama,
wala hapana kitu cha kumshughulisha.
52. Hii
Qur'ani ni Tangazo la kuwanasihi na kuwaonya na kuwakhofisha adhabu ya Mwenyezi
Mungu, na ili wajue ya kwamba wakikhofu wakazingatia kuwa hakika hapana mungu
ila Mungu Mmoja, na ili wenye akili wakumbuke utukufu wa Mola wao Mlezi, na kwa
hivyo wajitenge mbali na yale yatayo waletea hilaki.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani