1. "Alif Mym
Ra" hizi ni harufi za kutamkwa zimeanzia baadhi ya Sura za Qur'ani. Nazo
zinaashiria kuwa huu ni muujiza juu ya kuwa ni harufi wanazo zitumia Waarabu
katika maneno yao ya kawaida! Na harufi hizi zilikuwa zikitamkwa huwavutia
Waarabu waisikilize Qur'ani! Kwani wale mapagani (washirikina) waliambizana
wasiisikilize hii Qur'ani. Ikawa Waumini wakianzia harufi hizi huvutia masikio
ya washirikina wakawa wanasikiliza. Hakika hizo Aya au Ishara tukufu ndio hii
Qur'ani, Kitabu chenye shani kubwa, uliyo teremshiwa wewe Nabii kwa haki na
ukweli kutokana na Mwenyezi Mungu, aliye kuumba, na akakuteuwa. Lakini wengi wa
washirikina walio yakanya yaliyo kuja ya Haki si watu wa kuikubali Haki. Bali
wao wanaipinga kwa inda.
2. Hakika aliye
kiteremsha hichi Kitabu ni Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye aliye zinyanyua hizi
mbingu mnazo ziona zenye nyota zipitazo bila ya nguzo mnazo ziona, wala hazijui
mtu ila Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa amezifunganisha hizo na ardhi kwa funganisho
zisio katika ila akipenda Mwenyezi Mungu. Na amedhalilisha jua na mwezi chini ya
Ufalme wake na kwa ajili ya manufaa yenu. Na jua na mwezi yanazunguka kwa mpango
maalumu kwa muda alio ukadiria Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la. Na Yeye
Subhanahu anapanga kila kitu katika mbingu na ardhi, na anakubainishieni Ishara
zake za kuumba kwa kutaraji mpate kuamini kuwa Yeye ni Mmoja wa pekee.
3. Na
Subhanahu, Mwenyezi Mungu Aliye takasika, ndiye aliye kukunjulieni ardhi,
akaidhalilisha ili muweze kutembea juu yake mashariki na magharibi. Na Yeye
akajaalia katika hii ardhi milima iliyo simama imara, na mito ya maji matamu
inayo miminika. Na akajaalia kwa hayo maji matunda ya kabila mbali mbali yanayo
zaliana, na kati ya kabila hizo namna mbali mbali, mengine matamu na mengine
makali, mengine meupe, na mengine meusi. Na Yeye Subhanahu huufunika mchana kwa
usiku. Na hakika katika huu ulimwengu na ajabu zake zimo alama wazi za
kuthibitisha uwezo wa Mwenyezi Mungu na Umoja wake kwa anaye fikiri akazingatia.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia katika kila mimea dume na jike ili ipate
kupandishika sehemu ya uke kwa chembe za uzazi zilioko katika sehemu za ume. Na
kwa hivyo ndio huzalikana namna kwa namna na kwa wingi.
4. Na hakika
hiyo ardhi nafsi yake ina maajabu. Ndani yake vipo vipande vilivyo karibiana,
navyo juu ya hivyo vina udongo mbali mbali. Vingine ardhi yaabisi, na vingine
vya rutba, ijapo kuwa ni udongo ule ule. Ndani yake yapo mabustani yaliyo jaa
miti ya mizabibu, na ndani yake mazao mengine yanavunwa, na mitende yenye kuzaa,
nayo ama iliyo kusanyika au iko mbali mbali. Na yote hayo ijapo kuwa inanyweshwa
maji yale yale yanakhitalifiana kwa utamu wao. Na hakika katika ajabu hizi zipo
dalili wazi za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa mwenye akili ya kufikiria.
Aya hii tukufu inaonyesha ilimu ya ardhi (Geology) na ilimu ya mazingira
(Ecology) na athari yao juu ya sifa za mimea. Inajuulikana katika ilimu kuwa
rutuba ya ardhi inategemea juu ya chembe chembe za maadeni zinazo khitalifiana
kwa namna na ukubwa, na maji yanayo toka kwenye mvua, na hewa, na vitu vyenye
asili ya uhai, kama mimea na vyenginevyo, ambavyo hupatikana juu ya udongo au
ndani yake. Huwapo hivyo kwa mamilioni vidogo vidogo hata havionekani kwa jicho
tu. Kwa jumla ukizingatia haya utaona yanaonyesha uwezo wa Muumba na busara ya
uumbaji, kwani ardhi kama wasemavyo wakulimu inakhitalifiana kila shubiri. Na
inajuulikana kwa wanazuoni wa sayansi kuwa ukipatikana upungufu katika hivyo
vitu vya msingi katika udongo basi hudhihirisha upungufu wake katika mimea, na
kwa hivyo wakulima hujalizia upungufu huo kwa kutia mbolea mbali mbali na
hutengeneza hali ya mazingira. Na hayo yana athari zake juu ya mazao ikiwa kwa
mmea wa namna moja au namna mbali. Ametakasika Mwenyezi Mungu ambaye katika
mikono yake upo ufalme wa kila kitu, naye ni Muweza wa kila kitu.
5. Na hakika
mambo ya washirikina juu ya dalili hizi ni ya ajabu. Ikiwa wewe Muhammad utas-
taajabia jambo, basi la ajabu ni hiyo kauli yao wanapo sema: Ati baada ya kufa,
na baada ya kwisha kuwa mchanga, tutakuwa wahai tena upya? Huu ndio mtindo wa
wanao mkufuru Muumba wao. Akili zao zimefungwa na upotovu. Na marejeo yao ni
Motoni watakapo dumu humo; kwani hao ni wenye kukanya juu ya kuwa mwenye kuweza
kuanzisha anaweza kurejesha.
6. Na huko
kupita mpaka upotovu kunawapelekea kutaka wateremshiwa adhabu haraka haraka
badala ya kuomba hidaya itayo waokoa. Na wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu
hawateremshii adhabu duniani akitaka. Na zimekwisha wapitia adhabu watu mfano
wao kwa hayo, katika alio wateketeza Mwenyezi Mungu kabla yao. Lakini ni shani
ya Mwenyezi Mungu kusamehe dhulma ya mwenye kutubia akarejea kwenye Haki, na
kumteremshia adhabu kali anaye endelea na upotovu.
7. Na husema
hao makafiri wasio amini muujiza mkubwa, yaani Qur'ani: Hebu na amteremshie Mola
wake Mlezi alama ya unabii wake wa kuonekana kama kuiendesha milima akawa
Mwenyezi Mungu anaonyesha wazi uhakika wa Nabii wake katika jambo hili! Na Yeye
Subhanahu anamwambia: Hakika wewe ni Nabii wa kuwaonya kwamba kuna adhabu mbaya
wakiendelea na upotovu wao. Na kila kaumu wanaye Mtume wa kuwaongoza kwenye
Haki, na muujiza wa kubainisha ujumbe wake. Si wao wa kuchagua. Lao ni kujibu
upinzani na kuleta mfano wake!
8. Aliye mpa
Mtume huo muujiza mkubwa kabisa ni Yeye anaye jua kila kitu, na anazijua nafsi
za binaadamu tangu kuumbwa kwao kutokana na mbegu za uzazi katika tumbo la mama
mpaka wakati wa kufa kwao. Basi Yeye anaijua mimba anayo ichukua kila mwanamke
kama ni mume au mke, kinacho punguka tumboni na kilicho zidi wakati, mpaka
utimie muda wa mimba, na mtoto akamilike kukua, azaliwe. Kila kitu kwake Yeye
Subhanahu kina kipimo maalumu, na muda maalumu.
9. Yeye
anayajua ya ghaibu tusiyo yahisi, na tunayo yashuhudia kwa ujuzi zaidi kuliko
tunavyo shuhudia sisi na kuona. Na Yeye Subhanahu ni Mwenye shani kubwa iliyo
tukuka juu ya kila kiumbe.
10. Anazijua
hali zenu zote katika maisha yenu, na maneno yenu na vitendo vyenu vyote. Basi
anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza, vitendo na maneno. Na anajua vile
mnavyo jificha usiku na kujitokeza mchana. Na yote ni sawa katika ujuzi wake.
11. Na
Mwenyezi Mungu Aliye takasika ndiye anaye kuhifadhini. Kila mtu anao Malaika
wanao mlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na wanapeana zamu kumlinda mbele na
nyuma yake. Na hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu habadilishi hali ya watu kutoka
shida kwendea neema, na kutoka nguvu wakawa dhaifu, mpaka wao wenyewe wageuze
waliyo nayo kufuatana na hali wanayo iendea. Na Mwenyezi Mungu akitaka
kuwateremshia watu maovu basi hawana wa kuwanusuru ataye walinda na amri yake,
wala wa kuwatazamia mambo yao kuwakinga na yatayo wateremkia.
12. Na uwezo
wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ulimwengu unaonekana wazi, na athari zake zipo
dhaahiri. Ni Yeye anaye kuonesheni umeme, ukakutisheni kuuona au mkakhofu
isikujieni mvua wakati msio ihitaji ikakuharibieni mazao, au mkatumai kwa umeme
itakuja mvua kubwa mnayo ihitajia kwa maslaha ya ukulima. Ni Yeye anaye yafanya
mawingu yaliyo jaa mvua.
13. Na hakika
radi zinamnyenyekea Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la kwa unyenyekevu ulio
timia, mpaka ikawa sauti yake mnayo isikia ni kama kwamba inamtakasa na
kumsabihi kwa kumhimidi, kumsifu na kumshukuru, kwa kuumba kwake kama ni ishara
ya unyenyekevu wake. Na vile vile Roho safi msizo ziona, yaani Malaika, pia
zinamtakasa Yeye. Na Yeye ndiye anaye peleka moto wa radi unao unguza ukampata
amtakaye. Na juu ya kuwepo ishara hizi zinazo onekana zenye dalili ya uwezo wake
Subhanahu wao bado wanabisha shani ya Mwenyezi Mungu Aliye takasika. Na Yeye ni
Mwenye nguvu kubwa za kuvipinga vitimbi vya maadui.
14. Na hayo
masanamu wanayo yaomba kwa woga na kutafuta amani badala ya Mwenyezi Mungu pekee
hayawajibu wito na maombi yao. Hali yao ni kama mwenye kukunjua kiganja chake
akinge maji ya kunywa na kiganja kisifike mdomoni. Na hali yao ikiwa ni hii,
basi hizo dua zao haziwi ila kupotea na kukhasirika.
15. Na vyote
viliomo mbinguni na duniani, vitu, watu, majini, na Malaika, vinamnyenyekea
Mwenyezi Mungu kwa matakwa yake na utukufu wake, vikitaka visitake. Hata vivuli
vyao kadhaalika, vikirefuka na kufupika kwa mujibu wa nyakati za mchana adhuhuri
na jioni, kwa kufuata anavyo amrisha Mwenyezi Mungu na anavyo kataza.
16. Mwenyezi
Mungu amemuamrisha Nabii wake ajadiliane na washirikina kwa kuwaongoa na
kuwabainishia. Akamwambia: Ewe Nabii! Waambie: Nani aliye ziumba mbingu na
ardhi, naye ndiye Mwenye kuzilinda, na Mwenye kuviendesha viliomo humo? Tena
uwaeleze jawabu iliyo sawa hiyo wanayo ishindania. Waambie: Huyo ni Mwenyezi
Mungu anaye abudiwa kwa haki, hana mwenginewe. Basi ni waajibu wenu mumuabudu
Yeye peke yake. Tena waambie: Mnaziona dalili zilizo thibiti zinazo onyesha
uumbaji wake kila kitu peke yake? Na juu ya hivyo mnawafanya masanamu kuwa ni
miungu, bila ya kukubali kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja! Na haya masanamu
hayajifai wenyewe kheri wala shari! Vipi basi mnayafanya sawa na Muumba Mwenye
kupanga? Nyinyi mnafanya sawa baina ya Muumba wa kila kitu na asiye miliki kitu!
Mmekuwa kama anaye fanya sawa baina ya viwili vinavyo gongana! Basi hebu ni sawa
baina ya mwenye kuona na asiye ona? Je, giza totoro na mwangaza unao ng'aa ni
sawa? Je, usawa huo unaingia akilini mwao? Au upotovu wao umepita hadi hata
wanadai kuwa hayo masanamu yao ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika kuumba na
kupanga, hata yakawadanganyikia wasijue mambo ya uumbaji, kama walivyo potea
katika kuabudu? Waambie ewe Nabii! Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Muumba wa kila
kiliopo. Na Yeye ni peke yake katika kuumba na kuabudiwa, Mwenye kushinda kila
kitu.
17. Na hakika
neema zake Mtukufu mnaziona, na masanamu yenu hayana athari yoyote katika neema
hizo. Yeye ndiye anaye kuteremshieni mvua kutoka kwenye mawingu, na mito na
mabonde yakamiminika maji, kila kitu kwa kadiri yake aliyo ikadiria Mwenyezi
Mungu Mtukufu, kwa ajili ya kuzalisha mimea, na matunda ya miti. Na mito inapo
miminika hubeba juu yake visio kuwa na manufaa, na huwa katika hivyo vyenye
nafuu hubakia, na visio na faida hupita. Mfano wa hayo ni Haki na baat'ili,
kweli na uwongo. Haki hubakia na baat'ili ikapita. Na katika maadeni yanayo
yayushwa kwa moto kwa kufanyia mapambo, kama dhahabu na fedha, na yanayo tumiwa
kwa manufaa mengine kama chuma na shaba, kadhaalika sehemu isiyo na faida huwa
juu kama povu na hutupwa. Na yenye nafuu ndio hubakia. Kadhaalika katika imani.
Potovu hupita, na iliyo ya kweli hubakia. Kwa mfano kama huu Mwenyezi Mungu
Subhanahu anabainisha ukweli wa mambo, na hupiganisha mifano hii kwa hii ili
yote yabainike wazi.
18. Watu kwa
mujibu wa kupokea kwao uwongofu ni mafungu mawili. Fungu moja lilio itikia wito
wa Mwenyezi Mungu Muumba Mwenye kupanga. Hilo litapata malipo mema duniani na
Akhera. Fungu jengine lisilo itikia wito wa Aliye waumba. Hawa watapata malipo
maovu Akhera. Na lau kuwa wanamiliki kila kiliomo duniani na mfano wake mara ya
pili, hawawezi kujikinga na hayo malipo maovu! Lakini watapata kumiliki hayo?
Kwa hivyo yao wao ni hisabu ya kuwaudhi, na wataishia katika Jahannamu, na huko
ni pahali paovu mno pa kuishi.
19. Hakika
walio ongoka na walio potoka hawawi sawa. Basi je, anaye jua ya kuwa uliyo
teremshiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliye kulea akakuumba akakuteuwa kufikisha
ujumbe wake, kuwa ni Haki isiyo na shaka yoyote...je huweza kuwa huyo kama aliye
potea akaitupa Haki, hata akawa kama kipofu? Hakika hawatambui Haki wakazingatia
utukufu wa Mwenyezi Mungu, ila watu wenye akili ya kufikiri.
20. Hao ndio
wanao tambua Haki. Wao ndio wanao timiza ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyo
juu yao kwa muujibu wa maumbile, na kwa muujibu wa maagano yao na ahadi zao
walizo fungamana nazo; wala hawavunji maagano walio fungamana nayo kwa jina la
Mwenyezi Mungu baina yao na waja wenzi wao, na kwa maagano makubwa walio jifunga
nayo kwa maumbile yaliyo wafanya waitambue Haki na waamini, isipo kuwa walipo
jipoteza wenyewe nafsi zao.
21. Hao ni
Waumini; ada yao ni mapenzi na ut'iifu. Hao wanaamini mapendo baina ya watu, na
wanahurumia jamaa zao, na wanawasaidia wenzi wao katika Haki, na wao wanaijua
Haki ya Mwenyezi Mungu, na wanaiogopa hisabu ya kuwachusha Siku ya Kiyama, na
kwa hivyo wanajikinga na madhambi kwa kadri wawezavyo.
22. Na
wanavumilia maudhi wakitafuta radhi za Mwenyezi Mungu iwasaidie katika Njia ya
kuwania Haki. Wanashika Sala kama inavyo pasa kusafisha roho zao, na kumkumbuka
Mola wao Mlezi. Na wanatoa kutokana na mali aliyo wapa Mwenyezi Mungu kisirisiri
na kwa dhahiri bila ya kutaka kuonyesha watu, na kwa maovu wanao tendewa wao
wanalipa mema. Na wao kwa sifa hizi watapata malipo mema kwa kukaa katika ahsani
ya nyumba, nayo ndiyo Pepo.
23. Hayo ndiyo
malipo mema, ya ukaazi wa moja kwa moja katika Bustani za neema. Watakuwa wao
humo pamoja na wazazi wao walio kuwa njema Imani yao na a'mali yao. Pamoja nao
pia watakuwa na wake zao na dhuriya zao (wazao wao). Na Roho Safi zitawasalimu
na kuwaingilia kila upande.
24. Hizo Roho
zitawaambia: Amani ya milele ni yenu kwa sababu ya kuvumilia kwenu maudhi, na
kusubiri kwenu katika kupambana na matamanio yenu. Ni mazuri mno haya malipo
mnayo yapata, nayo ni kupata makaazi katika Nyumba ya Neema ya Peponi.
25. Hakika
sifa za Waumini wema ni kinyume na sifa za washirikina waovu. Kwani washirikina
huvunja ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo chukua kwao kwa mujibu wa maumbile na
ambayo walijifunga nayo. Kwa hivyo wamekhalifu maumbile yao na akili zao kwa
kuabudu mawe yasiyo wafaa wala kuwadhuru. Na wanavunja ahadi zao wanazo
fungamana na waja wenzao, tena wanakata makhusiano yao ya mapenzi na watu, na
makhusiano yao na Mwenyezi Mungu. Hawazifuati amri zake, wala hawamuabudu Yeye
pekee. Na wanafanya uharibifu katika ardhi kwa uvamizi na kufanya uadui na
kuvuka mipaka, na kuacha kuitengeneza dunia wakanafiika nayo! Na Mwenyezi Mungu
Aliye takasika hapendi uchafuzi na ufisadi.
26. Na ikiwa
hao washirikina wanaona kuwa wao wamepewa mali mengi, na Waumini ni mafakiri,
wanyonge, basi wajue kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu humpa riziki kunjufu amtakaye
akizishika sababu na humdhikisha amtakaye. Basi Yeye humpa Muumini na asiye kuwa
Muumini. Kwa hivyo msidhani kuwa wingi wa mali mikononi mwao kuwa ni dalili ya
kuwa wao ndio wamo katika Haki. Lakini wao hufurahi kwa hayo mali walio pewa,
juu ya kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu humpa dunia anaye mpenda na asiye mpenda. Na
maisha ya duniani si chochote ila ni starehe duni yenye kupita!
27. Na hakika
hao washirikina walio banwa na wingi wa pupa na papara husema: Je, huyu Nabii
hakuteremshiwa muujiza mwengine kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Ewe Nabii! Waambie:
Sababu ya kutokuwa na Imani nyinyi si upungufu wa miujiza, bali ni upotovu tu!
Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Aliye tukuka humwacha apotee anaye mtaka
apotee, maadamu anaendelea katika njia ya upotovu. Na humwongoa aendee kwenye
Haki yule ambae daima hurejea kwa Mwenyezi Mungu.
28. Na hakika
hawa wanao rejea kwa Mwenyezi Mungu, na wanaikubali Haki, ndio hao walio amini
ambao nyoyo zao zinatua anapo tajwa na kukumbukwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa
Qur'ani au vyenginevyo. Na hakika nyoyo hazitulii na kutua ila kwa kukumbukwa
utukufu wa Mwenyezi Mungu na uwezo wake na kuombwa radhi yake kwa kumt'ii.
29. Na hakika
wanao inyenyekea Haki, na wakasimama kutenda vitendo vyema, hao watapata malipo
mema, na mwisho mzuri.
30. Kama
tulivyo wapelekea kaumu zilizo kwisha pita Mitume wakawaeleza yaliyo ya Haki, na
wakapotea walio potea, na wakaongoka walio ongoka, na tukawapa miujiza ya
kuonyesha Utume wao, kadhaalika tumekutuma wewe kwa umma wa Kiarabu na
wenginewe, na kabla yao zimekwisha pita kaumu nyengine. Na muujiza wako ni hii
Qur'ani uwasomee, uwawekee wazi maana yake na utukufu wake. Na wao wanaikanya
rehema ya Mwenyezi Mungu walio pewa kwa kuteremshiwa Qur'ani. Basi ewe Nabii!
Waambie: Mwenyezi Mungu ndiye aliye niumba, na anaye nilinda, na anaye nirehemu.
Hapana mungu wa kuabudiwa kwa Haki ila Yeye. Namtegemea Yeye tu, na kwake ndio
marejeo yangu na yenu.
31. Wao
wanataka muujiza mwingine usio kuwa huu wa Qur'ani, juu ya ubora wa athari yake,
lau kuwa kweli wanaitaka Haki na wanaikubali. Lau kuwa kuna Kitabu cha kusomwa
kikaiendesha milima, kikapasua ardhi, au kikawasemeza maiti, basi Kitabu hicho
kinge kuwa hii Qur'ani! Lakini watu hawa wana inda tu. Mwenyezi Mungu peke yake
ndiye mwenye amri yote katika miujiza na malipo ya hao wakanyao. Na katika hayo
ana uwezo kaamili. Ikiwa hao wamo katika hali hii ya inadi, basi je walio it'ii
Haki hawajakata tamaa bado na kuamini kwa hawa makafiri, na wakajua kwamba
kufuru yao ni kuyakataa matakwa ya Mwenyezi Mungu? Na lau kuwa Mwenyezi Mungu
angeli taka waongoke watu wote basi wangeli ongoka! Na hakika uwezo wa Mwenyezi
Mungu uko dhaahiri mbele yao. Basi haziachi balaa kali kali za kuwateketeza
zikiwasibu, au kuwateremkia karibu yao, mpaka itimie ahadi ya Mwenyezi Mungu
aliyo wapa. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu havunji miadi yake.
32. Na ikiwa
hao wanao kanya wamekufanyia kejeli kwa hayo unao waitia na kwa Qur'ani, basi
walifanyiwa maskhara vile vile Mitume walio tumwa kabla yako wewe, ewe Nabii.
Basi usihuzunike, kwani mimi nawapa muhula tu hawa wanao kanya, kisha
nitawatwaa, na hapo itakuwa adhabu kali isiyo wezekana kuelezwa wala kujuulikana
hali yake.
33. Hakika
washirikina wamefanya upumbavu katika kukanya kwao, wakamfanyia Mwenyezi Mungu
washirika wa kuwaabudu. Kwani ati huyo ambaye ndiye Mwenye kuhifadhi na
kuangalia kila nafsi, na kuipimia kwa kuilipa kheri na shari inayo ichuma,
atakuwa wa kufananishwa na haya masanamu? Ewe Nabii! Waambie: Yaelezeni yalivyo
kweli! Je, hayo masanamu ya hai? Yanaweza kujikinga na madhara? Yakiwa mawe
hayanufaishi wala hayadhuru, basi mbona mnajidanganya nafsi zenu kuwa miungu
hiyo ndio imemwambia Mwenyezi Mungu hayo ambayo mnadhani kuwa Yeye hayajui ya
ardhi hii? Au mnaiweka kwenye cheo cha kuiabudu kwa maneno yanayo toka katika
ndimi zenu? Hakika iliyopo ni kuwa watu hawa wamezugwa na mazingatio yao na
mawazo yao ya upotovu. Na kwa sababu hiyo wameiacha Njia ya Haki wakabaki
wakitanga tanga! Na wenye kupotea kama hao, basi hawana wa kuwaongoa yeyote,
kwani wameziachisha nafsi zao Njia ya Uwongofu.
34. Duniani
watapata adhabu kwa kushindwa na kutekwa na kuuliwa, ikiwa Waumini watakwenda
katika njia ya Haki. Na hapana shaka adhabu ya Akhera itayo wateremkia ni kali
zaidi na ya kudumu zaidi. Hapana wa kuwakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu Mwenye
uwezo wa kila kitu.
35. Ikiwa hawa
watapata adhabu hii, Waumini watapata Pepo na neema zake. Na hayo wamekwisha
ahidiwa. Na hali ya Bustani walio ahidiwa wanao simama juu ya Haki na wakaweka
kinga baina ya upotovu na Imani, ni kuwa itapitiwa chini ya miti yake maji
matamu, na matunda yake ni ya daima hayasiti, na kivuli chake vilevile ni cha
daima. Na haya ndiyo malipo ya wale wanao jikinga na shari. Ama makafiri wanao
kanya, malipo yao ni kuingia Motoni.
36. Na wale
ambao walio pewa ujuzi wa Vitabu vilivyo teremshwa ni waajibu wao wakifurahie
Kitabu hichi ulicho teremshiwa wewe. Kwani hichi ni maendeleo ya ule ule ujumbe
wa Mwenyezi Mungu. Na wanayo ifanya dini kuwa ni sababu ya kufanya makundi mbali
mbali wanayakataa baadhi ya uliyo teremshiwa kwa uadui na chuki tu. Basi ewe
Nabii! Waambie: Hakika mimi sikuamrishwa ila nimuabudu Mwenyezi Mungu, na
nisimshirikishe katika ibada yake na kitu chochote. Na kwendea kumuabudu Yeye
peke yake ndio ninalingania, ninaita, na kwake Yeye peke yake ndio marejeo
yangu.
37. Na kama
vilivyo teremka Vitabu vya mbinguni, tumekuteremshia wewe hii Qur'ani ili iwe ni
hakimu baina ya watu kwa yaliyo baina yao, na iwe ni hakimu wa Vitabu vilivyo
tangulia kuwa ni vya kweli. Na hii Qur'ani tumeiteremsha kwa lugha ya Kiarabu.
Wala usitake kuwafurahisha washirikina au Ahli Lkitab (watu wa Biblia), baada ya
ufunuo na ilimu iliyo kufikia. Na ukitaka kuwaridhi basi hutakuwa na wa
kukusaidia au kukulinda mbele ya Mwenyezi Mungu. Hapa anaambiwa Nabii, khasa
wanasemezwa Waumini wote. Na mahadharisho ya Waumini ni kweli kweli hivyo; na
kwa Nabii ni kwa ajili ya kubainisha kuwa juu ya kuwa yeye ni mteuliwa, na
mtukufu wa daraja, bado anafaa kuhadharishwa.
38. Na ikiwa
washirikina wanachochea watu wastaajabu kuwa wewe una wake na dhuriya, yaani
wazao, na wanataka ulete muujiza mwengine usio kuwa Qur'ani, basi tulileta kabla
yako Mitume wenye wake na wana vile vile. Kwani Mtume ni mwanaadamu, na ana sifa
za kibinaadamu. Lakini yeye ni mbora kuliko wote. Wala Nabii hawezi kuleta
muujiza kama apendavyo yeye au wapendavyo watu wake! Bali aletaye muujiza ni
Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye anaye toa idhini. Kila kizazi katika vizazi kina
amri yao aliyo waandikia Mwenyezi Mungu ya kuwasilihi. Na kila kizazi kina
muujiza wake unao wanasibu. (Nabii Isa a.s. anasimuliwa katika Injili ya Yohana
5.30 kuwa alisema: Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe.)
39. Mwenyezi
Mungu hufuta sharia na miujiza, na akaleta badala yake atakayo na
akaithibitisha. Na kwake Yeye ipo asili ya Sharia zilizo thibiti zisio geuka, na
ndio kwenye Umoja na asili ya fadhila zote, na mengineyo.
40. Na
tukikuonyesha baadhi ya malipo au adhabu tulizo waahidi, au tukakujaalia ufe
kabla ya hayo, ungeli ona kitisho kitacho washukia washirikina, na ungeli ona
neema za Waumini! Lakini haya hayakukhusu wewe, juu yako wewe ni kufikisha
Ujumbe tu, na kwetu Sisi peke yetu ndio hisabu.
41. Na hakika
dalili za adhabu na kushindwa zipo! Hawaangalii kwamba Sisi tunazifikia nchi
walizo kuwa wakizitawala zinachukuliwa na Waumini kidogo kidogo? Na kwa hivyo
tunawapunguzia wao ardhi zilio wazunguka. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye wa
kuhukumu kushinda na kushindwa, na thawabu na adhabu. Na wala hapana wa kuipinga
hukumu yake. Na hisabu yake ni ya mbio mbio, haihitajii kupitiwa na wakati
mrefu, kwani Yeye ni Mjuzi wa kila kitu. Basi ishara zipo! Aya hii ina ukweli
ulio fikiliwa na uchunguzi wa kisayansi za hivi sasa, ya kwamba imethibiti kuwa
dunia inazunguka, na kuwa inayo mvuto kama simaku. Hayo yamepelekea kubabataa
katika ncha mbili za kaskazini na kusini, North Pole na South Pole. Na hivyo ni
kupunguka katika ncha mbili za ardhi. Na kadhaalika imejuulikana kuchopoka mbio
za sehemu za gasi zilizo funika huu mpira wa dunia kukipindukia nguvu za mvuto
wa ardhi, basi hutoka nje ya dunia. Na haya yanatokea mfululizo, na kwa hivyo
ardhi, yaani dunia, inakuwa katika hali ya kupunguka moja kwa moja katika ncha
zake. Haya yanakuwa kwa kuifasiri ardhi kuwa ni dunia, si nchi ya maadui wa
Waumini. Yaelekea taf siri hii kwa Aya hii tukufu, ijapo kuwa wafasiri wengi
wamefasiri kuwa muradi wa "ardhi" ni nchi za maadui.
42. Na walio
kuwa kabla yao waliwapangia Mitume wao mipango ya uwovu. Lakini Mwenyezi Mungu
Subhanahu ndiye Mwenye mipango yote kwa makafiri walioko sasa na walio
watangulia. Na watapata malipo kwa wanayo yatenda, na Yeye anayajua ayatendayo
kila kiumbe. Na ikiwa wao hawajui kuwa mwisho mwema ni wa Waumini, basi Siku ya
Kiyama watajua kwa kuona nani atapata mwisho mwema kwa kukaa katika Nyumba ya
neema.
43. Na hadi ya
ushindani wao hao wanao kanya na hawaikubali Haki ni kukwambia: Ewe Nabii! Wewe
si Mtume aliye toka kwa Mwenyezi Mungu! Basi waambie: Yanitosha mimi kuwa
Mwenyezi Mungu ndiye wa kunihukumia mimi nanyi, na anaye ijua hakika ya Qur'ani
na ajabu zake za miujiza ya kushangaza inayo ingia katika akili ziliyo nzima.
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani