1.
Sura inaanza kwa Jina la Mwenyezi Mungu ambaye hapana anayefaa kuabudiwa ila
Yeye aliye sifika kwa kila sifa za ukamilifu, na ametakasika na kila la
upungufu. Yeye ndiye Mwenye rehema ambaye ananeemesha kwa neema kubwa na ndogo,
na za kuwapa wote, na za kuwapa walio khusika. Na Yeye ndiye mwenye kusifika kwa
sifa ya Rehema yenye kudumu. (Kauli ya mwanzo aliyo semezwa Mtume s.a.w. na
kuamrishwa na Mwenyezi Mungu ni "Iqra` bismi Rabbika", yaani: "Soma kwa jina la
Mola wako Mlezi!" Naye Mtume s.a.w. amesema: "Jambo lolote lisilo anziwa kwa
Bismillahi ni pungufu." Kila Sura ya Qur'ani, isipo kuwa Sura Attawba, imeanziwa
kwa Bismillahi Rrahmani Rrahim.)
2. Sifa njema za namna yote na
katika kila hali ni za Mwenyezi Mungu pekee. Na tunamsifu Yeye kwa sifa zote kwa
sababu Yeye ndiye mwenye kuviumba viumbe vyote na mwenye kuviangalia na kuvilea.
(Neno Rabb, kwa Kiarabu, lina maana ya Ubwana na Ulezi na Utengenezaji. Ndiyo
tukatumia Mola Mlezi. Neno Baba lina upungufu.)
3. Na Yeye ndiye Mwenye rehema ya
kudumu, na rehema inatokana naye. Ananeemesha kwa neema zote ndogo na kubwa.
(Arrahman ni jina lake Mwenyezi Mungu tu, na hafai mtu kuitwa hivyo.)
4. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye
kumiliki Siku ya Malipo na Hisabu, yaani Siku ya Kiyama, anafanya atakavyo wala
hapana mwenye kushirikiana naye walau kwa kuonekana tu.
5. Hatumuabudu yeyote ila Wewe tu,
wala hatutaki msaada kwa yeyote ila kwako tu.
6. Tunakuomba utuwafikishe kuendea
Njia ya haki, na kheri na mafanikio.
7. Na njia hiyo ndiyo ya waja wako ulio wawezesha kukuamini Wewe, na
ukawajaalia neema ya uwongofu na radhi, sio njia ya walio stahiki kupata
ghadhabu zako na wakaiwacha njia ya haki na kheri, kwa sababu hao wameitupa
imani kukuamini Wewe na kuelekea kwenye uwongofu wako.
(Hapana katika Vitabu vyote vitakatifu, vya dini
zote, dua inayo lingana na hii kwa uzuri wake, na utimilivu wake. Baada ya
kumsifu Mwenyezi Mungu kwa Rehema yake isio na ukomo wala kipimo, na kumshukuru
Mola Mwenye kuviumba na kuviangalia na kuvilea kwa huruma viumbe vyote, na
kuhakikisha kuwa tunajua kuwa hapana Mungu ila Yeye tu wa kuabudiwa na kuombwa
msaada, na kuwa hapana wa kumuingilia katika Ufalme wake na Uwezo wake wa kulipa
hisabu kwa kila alitendalo mtu, hapo tena ndio tunaomba. Na tunaomba nini? Si
mkate wa kula, wala riziki yoyote, wala jambo lolote la manufaa ya kimwili
duniani, bali tunaomba Uwongofu kwenye Njia Iliyo Nyooka, Njia ya kumwendea Yeye
Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema. Tunaomba tusiendee njia waliyo ifuata wale
walio kasirikiwa na Mwenyezi Mungu, kwa kuwa walifunzwa wakajua, lakini kwa
chuki na jeuri wakakataa kuongoka, wala sio njia ya wale ambao labda kwa ujinga
wamepotea. Hiyo kwa mukhtasari ndiyo Dua ambayo Waislamu, wanafunzwa waiombe, na
wanaiomba mara kadhaa wa kadhaa katika Sala zao, na katika kila fursa inapo
tokea.)
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani