Kwanza yanipasa nimshukuru Mwenyezi Mungu Jalali, asiye kuwa na mithali, kwa neema zake za kila hali na kila mahali, hata nikaweza, mimi mja mpungufu, kutimiza kazi hii tukufu, ya kuutarjimu Msahafu pamoja na Tafsiri inayo itwa, "AL-MUNTAKHAB FI TAFSIRI 'L-QUR'AN" kwa lugha ya Kiswahili. Kwa kazi hii nawashukuru wote walio simama nami kutekeleza waajibu, ambao mimi ungeli nishinda peke yangu. Mtaalamu mmoja wa Kizungu alisema: "Haidhurishi kitu mwaandishi akiwa hana ufundi, maadamu anao masahibu wa dhati ambao anawasiliana nao vizuri." Mimi, Alhamdulillahi, nilipata wenzangu wa dhati wa kunisaidia katika kazi yangu hii tangu mwanzo wake mpaka kuishia kwake kwa kunisahihishia makosa katika muswadda.
Lakini nasikitika katika watatu wa kunisahihishia makosa,
mmoja wao, Dk. Ahmed Murshid, ambaye ni Rais wa Idara ya Lugha katika Chuo Kikuu cha Ummul Quraa
(Makka-T'aif) haikumkinika kutimiza kazi yake kwa umbali wa mawasiliano baina ya nilipo mimi na
alipo yeye. Juu ya hivyo msaada niliyo upata kwake na nasaha
zake si haba. Nuksani ni yangu.
Wa pili aliye nisaidia kusahihisha makosa ni Dk. Jaafar Tijani aliye kuwa
ustaadhi wa lugha katika Vyuo Vikuu vya Dar es salaam na Nairobi na sasa
anasomesha Kiingereza katika Maahad al Islami ya Maskati. Yeye ameupitia Msahafu
mzima, na maoni yake yamenifaa sana.
Mtaalamu wa tatu aliye
nichungulia na kunisahishishia muswadda wangu kwa utulivu mno ni Mwanachuoni
Sheikh Hamoud bin Ali Al Harthy. Yeye si kama amesahihisha lugha tu, bali, kwa
kutumia ilimu ya Tafsiri aliyo jaaliwa kuwa nayo kwa vizuri, ameyapa uzani
mwingine masahihisho yake. Kwa hakika kusahihisha kwake kumekuwa kwangu ni darsa
kaamili, hata mwishoe sikuweza ila kumwambia:
"Lau kuwa si Hamoud angeliteketea Ali", kama alivyo sema Sayyidna
Omar R.A. kwa mnasaba wa Sayyidna Ali R.A.
Sehemu kubwa kabisa ya upungufu wa juhudi zangu imeondolewa na kazi
waliyo ifanya Sheikh Hamoud na Dr. Jaafar. Kama dosari iliyo bakia, na najua
imebakia nyingi, inatokana ama na ujinga wangu, au ukaidi wangu kutojali
mashauri ya watu wanao jua zaidi kuliko mimi.
Wa mwisho kumtaja, wala si
wa mwisho wa kunifadhili, siwachi kumshukuru Sheikh Said Abdalla Seif Al-Hatimy
aliye upitia muswadda mara ya mwisho naye hali ni mgonjwa. Kaweza kunizindua
mwahala kadhaa wa kadhaa.. Namshukuru yeye na namshukuru Mufti wa Oman, Sheikh
Ahmed Al-Khalili, aliye chukua taklifu kumtafuta mchunguzi wa kutosha kwa kazi
hii muhimu.
Ijapo kuwa umuhimu wa kazi
yangu ni kutarjimu yaliyo andikwa katika hii Tafsiri inayo itwa Al-Muntakhab,
ilinipasa kuzipitia Tafsiri kadhaa wa kadhaa nyenginezo ili nipate kufahamu
vilivyo makusudio ya hayo niliyo kuwa ninayatarjimu. Miongoni mwa hizo ni
Tafsiri za Kiarabu ya Jalalein, ya Ibn Kathir, ya Zamakhshari, ya Baidhawi, ya
Shaltout (Juzuu kumi), ya Qurt'uby, "Attafsir Alkabir" ya Imam Arrazi,
"Haymayanu Zzaad" ya Muhammad bin Yusuf, na mwanzo wa "Jawaahiru Ttafsir" ya
Sheikh Ahmed Al-Khalili, Mufti wa Oman, na "Fi Dhilali Al-Qur'an" ya Sayyid
Qut'b. Ama za Kiswahili ni za marehemu Sheikh Al-Amin bin Aly Mazrui
(baadhi ya Juzuu), na Sheikh Abdulla Saleh Al-Farsy. Tena ya Sheikh
Abdulla Yusuf Ali, na ya Muhammad Asad, na ya Muhammad Pickthall (za
Kiingereza).
Sheikh Hamoud bin Ali Al
Harthy ameongezea katika upungufu wangu kwa Tafsiri nyengine ambazo
sinazo. Miongoni mwa hizo ni Tafsiri ya Almaraghy na Tafsiri ya Manara ambazo
yeye amezirejea mara nyingi katika kusahihisha muswadda wa maandishi haya.
Kadhaalika yamenifaa makamusi kadhaa wa kadhaa, na katika hayo ni khasa makamusi
yaliyo khusika na maneno ya Qur'ani kama ya Sheikh Makhluf aliye kuwa Mufti wa
Misri, na "Mu'jamu Alfaadhi Al-Qur'ani Alkarim" ya Majmau' Al lughati Al
A'rabiya.
Mbali ya hao wanazuoni
walio upitia muswadda wangu, wapo wengi walio nisaidia kwa njia mbali mbali.
Wanangu mara kadhaa wa kadhaa nilikuwa nikiwauliza kila ninapo kwama katika
kutarjimu. Na wapo walio nisaidia kwa upande wa kifundi, kama mwanangu
Muhammad Ali, aliye nipatia Computer; na yeye pamoja na wenziwe, Suleiman
Shahbal na Walid Muhammad Badr wakanifundisha kutumia hiyo Computer ambayo ndiyo
iliyo niwezesha kufanya kazi hii kwa wepesi. Na pia namshukuru kijana mwema wa
Kisham, Basim Ist'wany, ambaye alipo jua nini ninalo lifanya, alijitolea
kunisaidia bure juu ya kuwa kutengeneza Computer ndiyo kazi yake ya kumpatia
maisha. Pia siwezi ila nimshukuru Bw. Abdulrahman Salim Basadiq, aliye nitunukia
"Printer" mpya ghali kwa ajili ya kazi zangu. Mwenyezi Mungu awajaze kheri
wote nilio wataja na nisio wataja.
Katika walio nishajiisha
kikweli katika kazi hii ni Dr Ezzeddin Ibrahim, Mshauri wa Mtukufu Rais Sheikh
Zayid bin Sultan Al Nahyan, Rais wa U.A.E. Yeye anastahiki shukrani zangu
za dhati.
Ama hima ya Dr Mustafa Momen, sahibu yangu wa miaka mingi, haiwezi
kusahaulika kabisa kwa kuchukua kwake hima ya kunihimiza mimi kuendelea nayo
kazi hii, na khatimaye yeye akaifikisha kwenye nadhari ya Al Imam Al Akbar
Sheikh Jaad al Haq Ali Jaad Al Haq, Sheikh wa Al Azhar. Mwenyezi Mungu ndiye
Mlipaji. Atawalipa Mashekhe hawa watukufu kwa juhudi yao kulifikisha neno la
Mwenyezi Mungu kwa wasemao Kiswahili kwa kuwaletea Tafsiri ya mwanzo iliyo
kamilika katika lugha ya Kiswahili kwa njia iliyo nyepesi, na isiyo na
mapendeleo ya kimadhehebu, na yenye kuelezwa kwa kuambatana na ilimu za sayansi
za kisasa kila inapo hitajika.
Kwa wazazi wangu, na
mashekhe zangu, na walimu wangu, sina ila shukra za daima, kwani wao ndio walio
nilea na kunifunza, hata nikajua nilicho jua. Wao hao na mwenzangu wa maisha,
marehemu mke wangu, nawaombea maghfira na rehema kwa Mwenyezi Mungu. Ilikuwa
hamu yangu walau mke wangu marehemu awahi kushirikiana nami katika furaha nilipo
maliza kuandika Tarjuma hii, na awahi kuuona Msahafu huu ulio tarjumiwa kwa njia
hii umepigwa chapa. Lakini yote ni ya Mwenyezi Mungu.
Katika Utangulizi wa wenye
kuifasiri hii Qur'ani imefahamika kuwa katika Kiarabu "Tafsiri" ni "maelezo ya
maana ya Qur'ani". Kazi hiyo siyo niliyo ifanya mimi, wala mimi sina uwezo wa
kufanya hayo. Nililo lifanya ni kugeuza lugha ya Kiarabu kwa Kiswahili, kwa
kufuata uwongozi wa wataalamu walio kwisha ifasiri Qur'ani kwa kuieleza kwa
hicho hicho Kiarabu. Kazi yangu ni "Kutarjimu tafsiri", yaani kugeuza maana ya
maneno kutokana na Kiarabu nikayaingiza katika Kiswahili, kama afanyavyo
mkalimani katika mahkama.
Basi hii ni Tarjuma ya
Kiswahili ya Tafsiri ya Qur'ani iliyo fasiriwa na wanazuoni wakubwa wa Misri
walio jikusanya katika kikundi kinacho itwa Halmashauri ya Qur'ani na
Sunna chini ya uangalizi wa Baraza Kuu la Mambo ya Kiislamu. Tafsiri hiyo
inaitwa: AL-MUNTAKHAB FI TAFSIRI 'L-QUR'AN. Maana yake ni "YALIYO PEMBULIWA
KATIKA TAFSIRI YA QUR'ANI". Qur'ani Tukufu imefasiriwa, au imeelezwa, na watu
wengi sana. Tafsiri zake ni kwa mamia na mamia. Lakini zote hizo ni za watu
binafsi. Kila mojapo ni maoni ya mwanachuoni fulani. Hii Al-Muntakhab, kwa mara
ya kwanza ni juhudi ya kikundi cha wanazuoni walio pembua kutoka Tafsiri mbali
mbali, na wakakhiari walio yaona ni muwafaka ndio wakayakubali. Kwa hivyo kama
ilivyo mkinika Tafsiri hii ya AL-MUNTAKHAB imejaribu kuepuka khitilafu za
kimadhehebu katika mambo ya Fiqhi na Itikadi. Kwa sababu hii na kwa kuwa
imejaribu kueleza mambo ambayo yamekwisha hakikishwa na ilimu za sayansi, ndio
nikavutika nayo mimi na nikataka kuiandika kwa lugha ya Kiswahili, ili
Waswahili wenzangu wasio jua Kiarabu wapate nao kuifahamu na iwaongoze kama
ilivyo niongoza mimi. Kwa kuwa urefu wake ni wa wasitani, wa kutosha
kufahamisha, na si wa kuchosha, basi nimeona ni mnasaba sana kwa wasomaji wa
Kiswahili ambao wamekwisha onjeshwa utamu wa Qur'ani kwa tafsiri za Sheikh
Al-amin bin Aly Mazrui na Sheikh Abdulla Saleh Al-Farsy au walio isikia ikisomwa
tafsiri ya Jalaleini misikitini.
Mtaona kuwa mimi humu
sikutumia kuendeleza maandishi yangu kwa mujibu wa mtindo unao juulikana kuwa ni
wa "Standard Swahili". Mimi nimejitahidi kuandika kama ninavyo sema mwenyewe, na
khasa kama nilivyo kuwa nawasikia wazazi wangu wakisema nami. Wao na wenzao wao
nawachukulia kuwa ni mfano mwema kwa kusema Kiswahili kwa kuwa hawakuharibiwa
lugha yao kwa maskuli tuliko pelekwa sisi.
Kiswahili kabla hajaja mkoloni
kutulazimisha tutumie maandishi yake kilikuwa kinaandikwa kwa harufi za Kiarabu,
kama kinavyo andikwa Kiurdu, na Kifursi, na Kimalay, na Kiturki kabla Kamal
Ataturki hajaingiwa na shauku ya kutaka kuiga Uzungu katika kila kitu.
Katika kitabu "The
Swahili: Idiom and Identity" Mabwana Alamin M. Mazrui na Ibrahim Noor Shariff
wametaja vipi katika 1931 marehemu Sheikh Al-Amin bin Aly Mazrui alivyo
hadharisha khatari ya kuacha kutumia maandishi ya Kiarabu katika lugha ya
Kiswahili, na akaonya kuwa haya lazima yatakuja kuathiri vibaya matamshi ya
vizazi vijavyo. Akitumia gazeti lake la Al-Islah, aliwahimu umma wake wakipige
pande hicho alicho kiita "Kiswahili cha skuli".
Kazi tuliyo nayo sisi hii leo ina ncha mbili:
(1) Kufundisha watu kutumia harufi za Kiarabu kuandikia Kiswahili kama walivyo kuwa wakiandika wote hapo zamani kabla ya kuja wakoloni. Hapana jambo jepesi kama hilo. Kwa majaribio yangu nimeweza kuwafundisha vijana kadhaa wa kadhaa wa Kitanzania kusoma na kuandika kwa harufi za Kiarabu kwa muda wa siku chache tu na wakaweza kuisoma Qur'ani popote nilipo wafungulia. Nimetunga kijitabu juu ya hayo nilicho kiita: "Jifunze Kusoma na Kuandika Kiarabu kwa Wiki Tatu", ambacho kimepigwa chapa. Yeyote anaweza kujifunza mwenyewe kwa kufuata uwongozi uliomo katika kijitabu hicho, badala ya mtu kupitisha mwaka au miaka chuoni, na pengine aondokee patupu kwa kufunzwa kwa namna ya kizamani.
(2) Ncha ya pili ni kuzitumia hizi hizi harufi za Kizungu, lakini iwafikiwe baadhi yake zitengenezwe kwa kufuata matamshi fas'ihi ya Kiswahili. Kiswahili si lugha ya pekee inayo tumia hizi harufi za Kizungu, zinazo itwa za Kirumi. Lugha ya Kiingereza ni mfano mzuri kabisa wa lugha inayo tamkwa kwa namna isiyo kuwa ile inavyo andikwa.
Kusema kuwa Kiswahili kilegezwe, na kikamuliwe utamu wake wote, kwa sababu wageni wa lugha wanaona dhiki kutamka baadhi ya maneno yake, ni hadi ya kutudharau. Imekuwa kama lugha hii haina mwenyewe wa kuitetea. Mbona hapana aliye thubutu kukidharau Kiarabu, au Kiingereza, au Kifaransa, au hata Kizulu, Kixhosa au Kitsandawi au Kinyamwezi? Kila lugha ina hishimiwa usemi wake, na mbinu zake, na matamshi yake, wageni wakipenda wasipende.
Mimi, basi, katika maandishi
haya nimejaribu kuipa sura fikra yangu ya kufanya niwezavyo kwa wepesi bila ya
matatizo, sana kwa kutumia ' kuonyesha kuwa harufi fulani itamkwe kama inavyo
stahiki kutamkwa.
Kadhaalika katika uendelezi wa maneno ambayo kwa hicho
Kiswahili cha Skuli hufanywa maneno mbali mbali yakaungwa pamoja, na ilhali ni
maneno mbali, mimi nimeyafanya ni maneno mbali. Kwa mfano "aliyekuja". Sifahamu
kwa nini haya maneno mawili, ambayo ukiyaandika kwa harufi za Kiarabu ni mawili,
na ukiyafasiri kwa Kiarabu au kwa Kiingereza pia ni zaidi ya neno moja,
tuyaandike hivyo, na tusiandike hivi: "aliye kuja"?
Mtaona katika maandishi
haya nimejaribu nisiongeze langu ila katika maelezo nilipo ona inahitaji kwa
ajili ya kuzidi kuwafahamisha wasomaji wa Kiswahili. Na hapo yale yangu
nimeyatia baina ya mipinde miwili, kama hivi: (...).
Nitashukuru sana kupata
maoni ya wasomaji, khasa ya kunionyesha nilipo kosa, ili katika nakla zijazo
baadaye tupate kusahihisha makosa yetu.
Wassalamu Alaykum.
Ali Muhsin Barwani
S.L.P.
10679
Dubai
U.A.E.
26 Mfungo Tano 1413
25 Agosti
1992