1. Alif Lam Mim - Hizi ni harufi za
kutamkwa na zikasikilizana, zilizo letwa ili kubainisha kwamba hii Qur'ani yenye
kuwaemea watu kuiiga imetungwa kwa harufi hizi hizi mnazo ziweza kuzitamka
vizuri. Na pia ni kwa ajili ya kuwazindua wasikilizaji na wapate kuiangalia
Haki.
2. Hivyo watu wanadhani kwamba wataachiliwa tu
hivi hivi kwa sababu ya kutamka kwao shahada mbili basi, bila ya kujaribiwa kwa
mitihani na shida ili utambulikane ukweli wa Imani yao? La, sivyo hivyo! Bali
hapana budi kutiwa mithanini.
3. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu alikwisha
zijaribu kaumu zilizo tangulia kwa kuwapa shida na namna mbali mbali za
neema na mitihani, ili yapate kuonekana yale ambayo Yeye anayajua tangu mwanzo,
na awatengue baina ya walio kuwa wakweli katika Imani yao, na waongo.
4. Wanadhani wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu na
wanamuasi kwamba watatuponyoka katika kukimbia kwao kuikimbia adhabu ya Mwenyezi
Mungu na malipo yake? Kuhukumu kwao huku ni kuovu mno!
5. Mwenye kuamini kufufuliwa, na akawa anataraji
malipo ya Mwenyezi Mungu, na anaikhofu adhabu yake, basi huyo Imani yake ni ya
kweli. Basi na aingie kwenye vitendo vyema. Kwani Siku iIliyo ahidiwa itakuja
tu, hapana hivi wala hivi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maneno ya waja,
ni Mwenye kuvijua vitendo vyao. Na atamlipa kila mmoja kwa anavyo stahiki.
6. Na mwenye kuwania jihadi kwa sababu ya
kutukuza Neno la Mwenyezi Mungu, na akapambana na nafsi yake ivumilie juu ya
ut'iifu, basi malipo ya jihadi yake yatamrudia mwenyewe. Na hakika Mwenyezi
Mungu aliye takasika si mhitaji wa ut'iifu wa walimwengu.
7. Na wale walio sifika kwa Imani na wakatenda
mema hapana shaka tutawaondolea makosa yao, na tutawasamehe, na tutawalipa bora
ya malipo kwa vitendo vyao vyema.
8. Na Mwenyezi Mungu amemuamrisha mwanaadamu
afanye ukomo wa uwezo wake kuwafanyia wema wazazi wake na kuwat'ii. Na
wakikushikilia kumfanyia shirki Mwenyezi Mungu - na hayo hayakubaliki katika
ilimu wala akili - basi usiwat'ii. Na marejeo ya viumbe vyote ni kwa Mwenyezi
Mungu, na Yeye atawaeleza waliyo yatenda duniani, na atawalipa kwayo.
9. Na walio msadiki Mwenyezi Mungu na Ujumbe
wake, na wakatenda mema, basi hao hapana shaka Mwenyezi Mungu atawaingiza pamoja
na walio wema, wapate malipo yao na wayastarehee.
10. Na miongoni mwa watu yupo ambaye husema kwa
ulimi wake: Tumeamini. Na akipata dhiki yoyote kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
hukereka na akafitinika hata katika dini yake. Wala haifikirii adhabu ya
Mwenyezi Mungu ya Siku ya Kiyama. Yeye huyo huwa kama kwamba anafanya mateso ya
wanaadamu kuwa sawa na adhabu ya Mwenyezi Mungu ya Akhera. Mwenyezi Mungu
akiwanusuru Waumini, akawapa ushindi kuwashinda maadui zao na wakapata ngawira,
watu hao wanao dhihirisha imani huja wakawaambia Waislamu: Sisi ni wenzenu
katika Imani. Basi hebu tupeni nasi fungu letu la ngawira. Wasidhani watu hawa
kwamba mambo yao yamefichikana kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu anayajua
yaliomo vifuani mwa watu, ikiwa unaafiki au Imani.
11. Na hapana shaka Mwenyezi Mungu
atawadhihirishia watu yale ambayo Yeye anayajua tangu hapo. Atawatenga mbali
mbali baina ya Waumini na wanaafiki. Na kila mmoja atamlipa kwa alilo litenda.
12. Waongozi wa shirki walikuwa wakiwaambia wale
walio ingia katika Uislamu kwa usafi wa niya: Kueni kama mlivyo kuwa katika dini
yetu. Na fuateni tunayo fuata sisi. Na ikiwa kama huko kutakuwapo kufufuliwa na
kuhisabiwa ambako nyinyi mnakuogopa, basi sisi tutakubebeeni madhambi yenu.
Hapana mtu atakayembebea mwenzie dhambi zake. Hakika hao makafiri ni waongo tu
katika hiyo ahadi yao.
13. Basi makafiri wataibeba wenyewe mizigo yao
mizito, na juu ya hiyo watabeba mfano wa mizigo ya wale walio wapoteza na
wakawazuia wasiifuate Haki. Na hapana shaka yoyote watahisabiwa Siku ya Kiyama
kwa walio kuwa wakiyazua ya uwongo duniani, na watapewa adhabu kwa hayo.
14. Na Mwenyezi Mungu alimtuma Nuhu ende kwa
watu wake awaite wafuate Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Akakaa nao
miaka mia tisa na khamsini akiwalingania. Nao hawakumuitikia. Mwenyezi Mungu
akawazamisha kwa kuwapelekea tufani (kimbunga), nao ni wenye kujidhulumu nafsi
zao kwa ukafiri.
15. Mwenyezi Mungu akamtimilizia Nuhu ahadi
yake, na akamwokoa yeye na Waumini walio panda naye jahazi. Na akakifanya kisa
chao ni funzo kwa walio kuja baadae.
16. Na kumbuka, ewe Mtume, kisa cha Ibrahim,
pale alipo wataka watu wake wamuamini Mwenyezi Mungu Mmoja na wamt'ii Yeye, na
akawanabihisha kwamba kuamini ni bora kwao kuliko kukanusha, ikiwa wao wana
ujuzi na akili.
17. Akawaambia: Nyinyi hamuabudu badala ya
Mwenyezi Mungu ila vinyago na masanamu mnayo yaunda kwa mikono yenu. Na mnazua
uwongo na mnayaita kuwa miungu. Na haya masanamu mnayo yaabudu badala ya
Mwenyezi Mungu hayakufaini wala hayakudhuruni, wala hayawezi kukupatieni riziki.
Basi tafuteni riziki kwa Mwenyezi Mungu peke yake, na muabuduni Yeye tu, na
mshukuruni Yeye tu kwa neema zake. Kwani kwake Yeye ndio marejeo yenu nyote,
naye atakulipeni kwa mujibu wa vitendo vyenu.
18. Na mkishikilia kunikadhibisha mimi basi
hamtanidhuru kitu. Kwani bila ya shaka nimekwisha kwambieni kwamba Mitume wa
kabla yangu walikanushwa na kaumu zao, na hawakuwadhuru kitu, bali
walijidhuru wenyewe nafsi zao, pale Mwenyezi Mungu alipo waangamiza kwa sababu
ya kukadhibisha kwao. Basi Mjumbe hana jukumu lolote ila kufikisha Ujumbe wake
kwa kaumu yake kwa uwazi.
19. Hakika wamekwisha ona na wamejua kwamba
hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye anzisha uumbaji, na akisha akaurudisha tena.
Basi vipi ikawa wanakanusha kufufuliwa Siku ya Akhera kwa ajili ya hisabu na
malipo? Hakika kurejesha tena kwa Mwenyezi Mungu ni jambo jepesi zaidi.
20. Ewe Mtume! Waambie hawa wanao kanusha:
Tembeeni katika ardhi, na zingatieni vilivyo vitu mbali mbali alivyo viumba
Mwenyezi Mungu. Na angalieni mabaki ya waliyo kuwa kabla yenu, baada ya kwisha
kufa kwao na majumba yao waliyo yaacha. Na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu kwa
kudra yake atayarejesha yote hayo mwishoe kwa kufufua, nako ndiko huko kuumba
umbo la baadaye. Hali kadhaalika shani yenu. Hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu ni
Mwenye kutimia uwezo wake juu ya kila kitu.
"Sema: Tembeeni katika ardhi
na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba
umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu." Aya hii
tukufu inawahimiza wachunguzi wende katika dunia wapate kuvumbua vipi ulianza
uumbaji wa vitu, tangu wanyama, na mimea mpaka visio kuwa na uhai. Kwani mabaki
ya uumbaji wa mwanzo yamehifadhiwa baina ya tabaka za ardhi na juu yake. Na kwa
hivyo ardhi ni daftari lilio sajiliwa ndani yake taarikhi yote ya uumbaji, tangu
mwanzo wake mpaka hivi sasa.
21. Mwenyezi Mungu atawaadhibu awatakaye baada
ya uumbaji mwingine, na hao ndio wale wenye kukanusha hayo. Na atawarehemu
awatakaye, nao ndio Waumini wenye kuyakubali hayo. Na kwake Yeye peke yake ndio
marejeo ya viumbe vyote kwa ajili ya hisabu na malipo.
22. Enyi mnao kadhibisha! Nyinyi hamtaweza
kuishinda kudra ya Mwenyezi Mungu; sawa sawa mkiwa katika ardhi au katika
mbingu. Bali hiyo kudra yake imekuzungukeni nyinyi. Wala nyinyi hamna mlinzi wa
kukulindeni na Mwenyezi Mungu, wala msaidizi wa kukuzuilieni adhabu yake.
23. Na wale wanao zikataa dalili za Mwenyezi
Mungu zinazo thibitisha upweke wake, na wakawakadhibisha Mitume wake na Vitabu
vyake, na wakakanusha kufufuliwa na kuhisabiwa - watu hao hawana tamaa ya kupata
rehema ya Mwenyezi Mungu. Na watu hawa watapata adhabu kali yenye kutia uchungu.
24. Na pale Ibrahim alipo waamrisha watu wake
wamuabudu Mwenyezi Mungu na waache ile ibada ya masanamu waliyo kuwa nayo,
hawakuwa na jawabu yoyote ya kumjibu ila kukakamia katika ukafiri, na kuambizana
wenyewe kwa wenyewe: Muuweni, au mchomeni moto! Basi wakamtupa motoni. Lakini
Mwenyezi Mungu akaufanya moto uwe baridi na wenye salama kwake. Na akamwokoa
nao. Hakika kwa kubwatika vitimbi vyao na kuokoka kwake zipo dalili zilizo wazi
kwa watu wanao isadiki Tawhidi (upweke) wa Mwenyezi Mungu na kudra yake.
25. Ibrahim akawaambia watu wake: Kwa nini
mnaabudu miungu ya uwongo, na wala hamkatazani, kwa sababu ya mapenzi ya
madhambi mliyo yakhiari katika maisha yenu ya dunia? Kisha hali itabadilika Siku
ya Kiyama. Huko waongozi watawakataa wafuasi wao. Na wafwasi watawalaani
waongozi wao. Na marejeo ya wote ni Motoni. Wala hamtakuwa na msaidizi wa
kukuzuilieni msiingie humo.
26. Na alikuwa katika wa mwanzo wa kuitikia wito
wa Ibrahim, ni Lut'i. Akasadiki, na kabla yake alikuwa kesha kuwa mwenye kushika
Tawhid. Na Ibrahim akasema kwa kut'ii amri ya Mwenyezi Mungu: Mimi ninahama
kwendea upande aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi nihamie, na nikakae na huko
niwaitie watu wamfuate Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu wa kuweza
kunilinda na maadui zangu, Mwenye hikima ambaye haniamrishi ila lilio la kheri.
27. Na Mwenyezi Mungu akamtunukia Ibrahim kwa
kumpa mwana, naye ni Is-haq, na kumpa mjukuu, naye ni Yaa'qub. Na akamfanyia
ukarimu kwa kumjaalia Unabii katika dhuriya zake, na kuwateremshia Vitabu vya
mbinguni, na kwa kumlipa bora ya malipo katika dunia, naye huko Akhera kuwa ni
miongoni mwa bora ya watu wema.
28. Na ewe Mtume! Kumbuka pale tulipo mtuma
Lut'i kwa kaumu yake, akawataka waishike Tawhidi ya Mwenyezi Mungu na ut'iifu
wake. Na akawakataza kitendo kichafu walicho kuwa wakikitenda, ambacho hajapata
kukitenda yeyote katika viumbe vya Mwenyezi Mungu.
29. Hakika hayo myatendayo ni maovu na
yanahilikisha. Kwani nyinyi mnawafanya mambo machafu wanaume, na mnaikata
njia ya uzazi; na khatima ya hayo ni kutoweka kabisa. Na katika mikutano yenu
mnatenda maovu bila ya kumkhofu Mwenyezi Mungu wala kuoneana haya baina yenu.
Wala watu wake hawakumsikia, wala hawakuwa na jawabu ya kumpa ila kumfanyia
maskhara tu. Na wakamtaka alete upesi hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu aliyo
watishia kwayo, ikiwa yeye ni mkweli kwa hayo ayasemayo.
30. Basi Lut'i akamtaka msaada Mwenyezi Mungu
kupambana nao, na akamwomba amnusuru juu ya watu wake wenye kufanya fisadi
katika nchi.
31. Na walipo kuja Malaika wa Mwenyezi Mungu kwa
Ibrahim, a.s. kwa kumbashiria, walisema kwamba wameamrishwa kuwaangamiza watu wa
mji huo kwa sababu ya kufisidi kwao na kujidhulumu kwao wenyewe kwa ushirikina
na kutenda uchafu.
32. Ibrahim a.s. akawaambia Malaika: Hakika
katika huo mji yumo Lut'i. Basi vipi mtawaangamiza hao naye yumo kati yao.
Malaika wakamjibu kwamba wao wanajua nani waliomo humo, na kwamba wao kwa hakika
watamwokoa Lut'i na ahali zake wasipate adhabu, isipo kuwa mkewe. Yeye huyo
atakuwa miongoni mwa watao angamizwa kwa sababu ya ukafiri wake na uovu wake.
33. Walipo ondoka wale Malaika walio tumwa
kumuendea Lut'i naye akawaona, alihuzunika kwa kuwakhofia uadui wa watu
wake, na akaemewa asiwe na hila ya kuweza kuwalindai. Wao, basi, wakampoza na
wakamwambia: Kabisa usiukhofu uadui wa kaumu yako juu yetu, wala usihuzunike kwa
ajili yetu. Kwani sisi hakika tumekuja kuwaangamiza watu wa mji huu, na
tutakuokoa wewe na ahali zako. Lakini mkeo atakuwa pamoja na wenye kuangamia.
34. Malaika wakasema: Hakika sisi tumetumwa
kutimiliza amri ya Mwenyezi Mungu kwa kuwateremshia watu wa mji huu adhabu
itokayo mbinguni kwa sababu ya uchafu wao na ukafiri wao.
35. Na Mwenyezi Mungu akauteketeza mji huu, na
akaacha humo mabaki yaliyo wazi, ili yawe ni dalili ya kuonyesha aliyo wafanyia
Mwenyezi Mungu, na funzo kwa mwenye kuzingatia.
36. Na Mwenyezi Mungu aliwapelekea watu wa
Madyana Mtume kutokana nao wenyewe, naye ni Shuaibu. Akawaita waishike Tawhidi
ya Mwenyezi Mungu, na wamuabudu Yeye tu, na waiogope Siku ya Mwisho, na watende
vitendo ambavyo kwavyo watumai kupata malipo mema kwa Mwenyezi Mungu, na
akawakataza kukimbilia kutenda ufisadi katika nchi.
37. Wakamkanusha na wakamuasi. Basi Mwenyezi
Mungu akawaangamiza kwa tetemeko kubwa mno lilio wavunjia majumba yao. Wakawa
humo wameanguka maiti.
38. Na ewe Mtume! Watajie hawa walio
danganyikiwa kw mali zao na madaraka yao vifo vya A'di na Thamudi pale
tulipo waangamiza. Na yapo yamebakia mabaki ya majumba yao yenye kuonyesha
utajiri wao. Na sababu ya kuangamizwa huko ni kwa kuwa Shetani aliwazaini,
aliwapambia vitendo vyao viovu, nao wakamfuata. Basi akawaachisha Njia ya Haki
ambayo walikuwa wakiijua kwa kufunzwa na Mitume.
39. Na ewe Mtume! Watajie hawa walio ghurika kwa
mali yao na madaraka yao, kifo cha Qaruni na Firauni na Hamana na yaliyo wapata
katika ada ya Mwenyezi Mungu kuwahiliki wakanushao. Na Mwenyezi Mungu
aliwatumia Musa naye akawa na miujiza iliyo wazi ya kuthibitisha ukweli wake.
Lakini wao walimkadhibisha, na wakakataa kumuitikia kwa kiburi chao tu. Na wala
wao hawakuweza kuishinda kudra ya Mwenyezi Mungu kwa kuikimbia adhabu yake.
40. Kila kaumu katika kaumu zote zilizo
wakadhibisha Mitume wao Mwenyezi Mungu ameziangamiza kwa sababu ya kufuru zao
walizo zifanya na maasi yao. Baadhi ya kaumu hizo Mwenyezi Mungu
alizihiliki kwa upepo wa kimbunga ulio wapopoa kwa mawe. Na baadhi yao
waliangamia kwa ukelele wenye kuvuma wenye kuhiliki. Na baadhi yao Mwenyezi
Mungu aliwadidimiza katika ardhi. Na baadhi yao aliwazamisha majini. Wala
adhabu hizi hazikuwa ni kudhulumiwa na Mwenyezi Mungu, bali sababu yake ni kwa
kufuru yao wenyewe na kutenda maasi kwao.
41. Shani ya hao waongo wenye kumfanya urafiki
asiye kuwa Mwenyezi Mungu na kumtegemea asiye faa kutegemewa, ni kama shani ya
buibui mwenye kuifanya nyumba ya kumlinda, na hali nyumba yake ndiyo nyumba
isiyo faa kabisa kutumika kwa ulinzi. Na lau kuwa hawa waongo ni watu wa
ujuzi na utambuzi wasinge fanya hayo.
"Mfano wa walio wafanya walinzi
badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika
nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.":
Nyumba za buibui anazo jenga kwa ajili ya maskani yake na kwa ajili ya
kukamatia mateka wake zimeundwa kwa wembamba mno, kwani hizo ni nyuzi zilizo
kuwa hadi ya mwisho wa wembamba, zinashinda wembamba wa hariri. Na kwa hivyo
mfumo wake umekuwa ni wa mwisho wa udhaifu kuliko nyumba zote walizo jijengea
wanyama kuwa ni makaazi yao.
42. Hakika Mwenyezi Mungu, Subhanahu, anajua
vyema upotovu wa kuwaabudu hiyo miungu ya uwongo. Na Yeye Subhanahu ndiye Mwenye
kushinda kila kitu, Mwenye hikima katika kuendesha na kuweka sharia.
43. Na mazingatio haya na mifano hii, Mwenyezi
Mungu anawatajia watu ili wawaidhike na wazingatie. Na hawazingatii haya ila
wenye akili ambao wanapima.
44. Mbali na aliyo yataja Mwenyezi Mungu ya visa
na mifano na ishara ipo Ishara moja iliyo wazi kabisa, nayo ni uumbaji wa mbingu
na ardhi kwa uwezo na hikima, na kipimo kilicho kamilika, kwa maslaha ya watu.
Na katika haya zipo dalili za kweli kwa wenye kuiamini Haki.
45. Ewe Nabii! Soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu,
wala usiwashughulikie. Na timiza Sala kwa inavyo stahiki. Kwani Sala pamoja na
ikhlasi, kwa dhati yake humwachisha, mwenye kuishika, madhambi makubwa na kila
maovu yanayo katazwa na Sharia. Na bila ya shaka, kumcha Mwenyezi Mungu, na
kumhudhurisha kwa kumkumbuka katika Sala na kwengineko kuna athari kubwa zaidi
na thawabu nyingi zaidi. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda, yakiwa ya
kheri au shari. Naye atakulipeni kwayo.
46. Wala msijadiliane na wanao kukhalifuni
katika Mayahudi na Wakristo ila kwa njia yenye uwongofu kabisa, na laini kabisa,
na inayo pelekea zaidi kukubalika. Isipo kuwa wale walio pita mpaka katika
ubishi, basi hao hapana ubaya mkiwakabili kwa mkazo. Na waambieni mnao jadiliana
nao: Sisi tumeiamini Qur'ani tulio teremshiwa sisi, na Taurati na Injili mlizo
teremshiwa nyinyi. Na tunaye muabudu sisi, na mnaye muabudu nyinyi, ni mmoja. Na
sisi tunamnyenyekea Yeye peke yake.
47. Na kama tulivyo wateremshia vitabu Mitume wa
kabla yako, tumekuteremshia wewe hii Qur'ani. Basi wale tulio wapa Kitabu
(Biblia) kabla ya Qur'ani, na wakaizingatia na wakaifuata, wanaiamini hii
Qur'ani. Na miongoni mwa hawa Waarabu (washirikina) wapo wanao iamini. Na hapana
wanao zikataa Ishara zetu - baada ya kudhihiri kwake na kuondoka kila shaka juu
yake - ila walio shikilia ukafiri.
48. Wala wewe hukuwa ukisoma kitabu chochote
kabla ya Qur'ani. Wala hukuwa ukiandika kwa mkono wako wa kulia. Na lau kuwa
wewe ni katika ya wanao soma na kuandika wangetilia shaka watu wapotovu kuwa
hiyo Qur'ani haitoki kwa Mwenyezi Mungu.
49. Kitabu hichi si cha kutiliwa shaka, bali
hizi ni Ishara zilizo wazi zilizo hifadhiwa katika vifua vya watu ambao Mwenyezi
Mungu amewapa ilimu. Na hazikatai Ishara zetu, baada ya kuzijua, ila wenye
kuidhulumu Haki na wakazidhulumu nafsi zao.
50. Na makafiri katika majadiliano yao na ukaidi
wao walisema: Mbona hakuteremshiwa miujiza ya kuiona kwa macho kama iliyo
wateremkia Mitume wa kabla yake? Waambie: Miujiza yote iko kwa Mwenyezi
Mungu. Huiteremsha anapo taka. Ama mimi nimetumwa kuonya kwa uwazi, sio
kuleta hayo mtakayo.
51. Wanataka Ishara hizo, nao
haiwatoshi wao kuwa Sisi tumekuteremshia hichi Kitabu wanacho somewa? Na huu
ndio Muujiza wa kudumu milele na zingapita zama. Hakika kwa kuteremka Kitabu
hichi juu yako bila ya shaka ni rehema kwao na kwa vizazi vyote vijavyo baada
yao, na ni kumbusho la daima dawamu lenye manufaa kwa watu ambao shani yao ni
kuamini wanapo onyeshwa wazi Njia ya Uwongofu.
52. Sema: Yanitosha mimi na yakutosheni nyinyi
ya kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Shahidi kuwa mimi nimefikisha niliyo tumwa
kwenu. Na hayo ndiyo chanzo cha mambo yangu na mambo yenu. Wala hakifichiki
kwake chochote cha mbinguni na duniani. Na walio muabudu asiye kuwa Mwenyezi
Mungu, na wakamkataa Mwenyezi Mungu na wasimkhusishe Yeye tu kwa ibada, hao ndio
walio nunua ukafiri kwa Imani, na wakasibiwa na khasara iliyo wazi.
53. Na makafiri wanakufanyia ushindani ya kuwa
kama unaweza basi waletee kwa haraka hiyo adhabu ulio waonya kuwa
itawapata. Na lau kuwa wakati maalumu haukuwekwa kwa mujibu wa hikima
yetu, tungeli waletea kwa haraka hiyo adhabu wanayo ihimiza. Ninaapa itawatokea
kwa ghafla, na hali wao hawana khabari.
54. Wanakutaka waletewe upesi adhabu, nayo
itawajia tu, hapana hivi wala hivi. Na hakika, Jahannamu imewazunguka makafiri
kwa yakini.
55. Siku itapo wafunika adhabu kutoka juu, licha
ya kutoka chini, na Malaika aliye wakilishwa kuwaadhibu atapo sema: Onjeni jazaa
ya hayo maovu mliyo kuwa mkiyatenda!
56. (Mwenyezi Mungu anasema:) Enyi waja wangu
mlio niamini Mimi na Mtume wangu! Hakika ardhi yangu ni kunjufu kwa atakaye
kukimbia kutoka katika nchi za shirki. Kimbieni mje kwangu mpate kunisafia Mimi
ibada.
57. Kila nafsi itaonja uchungu wa mauti bila ya
shaka yoyote. Kisha mtarejea kwetu, na mtakuja lipwa kwa hayo mliyo yatanguliza,
ikiwa ya kheri au ya shari.
58,59. Na walio muamini Mwenyezi
Mungu na Vitabu vyake na Mitume wake, na wakatenda vitendo vyema, tunaapa kwamba
bila ya shaka tutawaweka katika makaazi ya starehe kwenye maghorofa yapitayo
mito chini yake. Neema zake haziwakatikii. Ni nzuri mno jazaa hii kuwa ni ujira
wa wenye kutenda, wenye kusubiri kwa yanayo wapata kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
wanapo acha nchi zao na watu wao na mali yao, nao wakimtegemea Mwenyezi Mungu
peke yake katika hali zao zote.
60. Na wanyama wengi wanao ishi nanyi katika
ardhi ambao, kwa unyonge wao, hawawezi kubeba riziki yao na wakaihamisha kwa
ajili ya kuila au kuiweka akiba. Ni Mwenyezi Mungu ndiye ambaye anawatengezea
sababu za kuwaruzku na kuwaweka hai. Na Yeye anakutengenezeeni nyinyi sababu za
riziki zenu na maisha yenu. Na Yeye ni Mwenye kumiliki kila alicho kiumba kwa
kusikia na kukijua.
61. Na ninaapa ukiwauliza washirikina: Nani
aliye ziumba mbingu na ardhi, na akalit'iisha jua na mwezi, na akayafanya hayo
yawanufaishe watu? Hapana shaka watasema: Kaviumba hivyo Mwenyezi Mungu. Wala
hawamtaji mwenginewe. Basi inakuwaje wanaacha kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja
Mtukufu, baada ya kukiri kwao huku?
62. Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye,
na humdhikishia amtakaye, kwa mujibu wa inavyo wafikiana na ujuzi wake kwa ajili
ya maslaha. Kwani hakika Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.
63. Ninaapa, lau kuwa utawauliza: Nani anaye
teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi kwa mimea baada ya kuwa na
ukame? Hapana shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi,
kuwa wanaikubali Haki. Lakini wengi wao hawafahamu kuwa wenyewe wanajitia
katika migongano ya maneno.
64. Na haya maisha ya duniani si chochote ila ni
starehe ya muda wenye ukomo. Wanapumbazika walio ghafilika kama wanavyo
pumbazika watoto wadogo, na wanacheza kwa muda fulani na kisha wanatawanyika. Na
hakika makaazi ya Akhera ndio makaazi ya maisha ya kweli, yaliyo kamilika, yenye
kudumu. Na kweli hizi ni zenye kuthibiti, wangeli zitambua hawa lau kuwa ni watu
wa kutambua vilivyo.
65. Hao kwa walivyo sifika kwa ushirikina,
wakipanda vyombo vya baharini, na wakapata kidogo katika vitisho vyake,
humuelekea Mwenyezi Mungu kwa kumwomba kwa ikhlasi ili awaondolee madhara. Na
akisha waokoa akawafikisha nchi kavu mara hukimbilia kurejea kwenye ushirikina.
66. Ili wapate kuzikanya neema tulizo wapa, na
wapate kunafiika kwa yale yanayo ridhiana na pumbao lao katika maisha haya. Basi
watakuja yajua matokeo ya ukafiri pale watapo iona adhabu iliyo chungu.
67. Makafiri wa Makka wameingia upofu, hawazioni
neema za Mwenyezi Mungu alizo wamiminia, wala hawaoni kwamba hakika Sisi
tumeufanya mji wao kuwa umehifadhika, haushambuliwi wala hauvamiwi, mtakatifu;
watu wake hawatekwi nyara, wala ndani yake havitokei vita. Na hali kote jirani
zao watu wananyakuliwa! Hawa wamepofuka hawazioni neema hizi, basi wanasadiki
yasiyo na asli yoyote, na wanamkanusha Muhammad na yote aliyo yaleta!
68. Na hapana aliye dhulumu zaidi kuliko yule
anaye msingizia Mwenyezi Mungu jambo ambalo hakulitolea sharia, au
akaikadhibisha Dini ya Haki inapo mfikilia. Hakika katika Jahannam ndiko kwenye
makaazi ya watu hawa madhaalimu, makafiri.
69. Na wale walio fanya
ukomo wa juhudi zao, na wakastahamili mashaka kwa sababu ya kuinusuru Dini yetu,
hapana shaka tutawazidishia kuwaongoa kuendea kheri na Haki. Na hakika Mwenyezi
Mungu bila ya shaka yu pamoja na wale wanao fanya vizuri vitendo vyao;
atawasaidia na atawanusuru. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi kuliko wote.