1. T'a Sin Mim, harufi za kutamkwa
kubainisha kuwa Qur'ani hii ni muujiza wa harufi hizi hizi za mazungumzo yenu,
na ili kuwazindua wenye kusikia.
2. Ewe Mtume! Aya hizi tunazo kufunulia wewe ni
Aya za Qur'ani yenye kubainisha kwa uwazi, yenye kudhihirisha Haki iwe mbali na
uwongo, na halali iwe mbali na haramu, na itoe ahadi ya kulipwa thawabu, na
kuhadharisha na adhabu.
3. Tunakusimulia baadhi ya khabari za Musa na
Firauni kwa ukweli, ili wapate kuzizingatia Waumini.
4. Hakika Firauni alipandwa na kiburi, na akapita
mipaka katika udhalimu wake, na akatakabari mno katika nchi ya Misri. Akawafanya
watu wa nchi hiyo makundi makundi, akiwanyanyua baadhi yao na akiwadhalilisha
wenginewe, na khasa aliwadhoofisha Wana wa Israili. Akawa anawachinja watoto wao
wanaume na akiwabakisha wanawake. Kwa hakika huyo alikuwa ni katika walio pita
hadi katika ujabari na ufisadi.
5. Na Mwenyezi Mungu akataka kuwafadhilisha alio
wafanya wanyonge Firauni katika nchi, na awafanye ndio wa kuongoza katika njia
za kheri, na awarithishe ufalme na madaraka ya nchi.
6. Na tuwathibitishe katika nchi, na wawe na
pahali pao humo. Na tuwathibitishie Firauni na Hamana na majeshi yao yale waliyo
kuwa wakiyakhofu, nayo ni kuondoka ufalme wake kwa mkono wa mwenye kuzaliwa
katika Wana wa Israili.
7. Na Mwenyezi Mungu alimfahamisha mama yake
Musa, alipo kuwa anamkhofia asichinjwe na Firauni kama alivyo kuwa akiwachinja
watoto wanaume wa Bani Israili, kwamba amnyonyeshe kwa kituo na hatauliwa na
Firauni. Ikiwa anaogopa asije kutambulikana amtie katika sanduku, na amtie
katika mto wa Nile bila ya khofu wala huzuni. Kwani bila ya shaka Mwenyezi Mungu
amedhamini kumhifadhi na kumrejeshea mwenyewe, na kumtuma kwa Wana wa Israili.
8. Watu wa Firauni wakamchukua, ili aliyo kadiria
Mwenyezi Mungu yatimie, yaani Musa apate kuwa Mtume mwenye kuwapinga wao, na
mwenye kuwaletea huzuni, kwa kuitoa kombo dini yao na kuishambulia dhulma yao.
Hakika Firauni na Hamana na wasaidizi wao walikuwa ni watu wenye madhambi, walio
pindukia mipaka katika ujeuri na uharibifu.
9. Mke wa Firauni alipo mwona mtoto alimwambia
mumewe: Mtoto huyu atatuletea furaha mimi na wewe. Tumweke, tusimuuwe, kwa
kutaraji kuwa atakuja tufaa kuendesha mambo yetu. Au tumfanye mwenetu wa kumlea.
Na wao kumbe hawatambui aliyo mkadiria Mwenyezi Mungu.
10. Na mama yake Musa akawa hajitambui kwa dhiki
iliyo muingia kwa kuwa mwanawe kaangukia mikononi mwa Firauni. Akawa
anakurubia kujitambulisha kwamba yeye ndiye mama yake. Lau ingeli kuwa Mwenyezi
Mungu hakuutia imara moyo wake kwa kusubiri, basi angeli tangaza kuwa huyo ni
mwanawe, jinsi alivyo kuwa akimhurumia, na pia ili awe miongoni mwa Waumini
wenye kutulia.
11. Yule mama akamwambia dada yake Musa: Mfuatie
upate kujua khabari zake. Basi akawa anamwona kwa mbali na anatahadhari
asitambulikane, na Firauni na watu wake wakawa hawajui kama yule ni dada yake.
12. Mwenyezi Mungu alimjaalia yule mtoto akatae
ziwa la kila mnyonyeshaji kabla hawajamjia mama yake. Watu wa Firauni wakaingiwa
na ghamu, na wakashughulishwa na hayo. Yule dada yake ndio akawaambia:
Nikuongozeni kwenye ukoo utakao muangalia huyu mtoto, na kumnyonyesha, na
kumlea, nao watamtazama vizuri?
13. Wakaukubali uwongozi wake, na Mwenyezi Mungu
akamrudisha kwa mama yake, ili nafsi yake itue, na afurahi kwa kurudi kwake,
wala asihuzunike kwa kuwa mbali naye, na ili azidi kujua ya kwamba ahadi ya
Mwenyezi Mungu aliyo mpa kuwa atamrudishia imetimia wala hayendi kinyume. Lakini
watu wengi walikuwa hawajui kurudi Musa kwa mama yake, kwani hayo yote
yalifichikana kwao.
14. Na Musa alipo kwisha kuwa mtu mzima, na
akakamilika, Mwenyezi Mungu alimpa hikima na ilimu. Na hisani kama hii
tuliyo mpa Musa na mama yake, tunawapa wema wote kwa ajili ya wema wao.
15. Musa akaingia mjini Misri wakati walipo kuwa
watu wake wameghafilika. Akawakuta watu wawili wanapigana. Mmoja ni katika Wana
wa Israili, na mwengine katika kaumu ya Firauni. Yule Muisraili akamtaka msaada
kumpiga khasimu yake. Naye Musa akamsaidia. Akampiga konde yule khasimu,
akamuuwa bila ya kukusudia. Musa akajuta na akasema: Hakika mimi kuja kufanya
kitendo hichi ni kazi ya Shetani. Hakika Shetani ni adui aliye wazi kwa uadui na
kupoteza.
16. Musa akasema kwa kunyenyekea kwa Mwenyezi
Mungu na majuto: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu kwa niliyo
yatenda. Basi nighufirie kitendo changu hichi. Mwenyezi Mungu akamuitikia ombi
lake na akamsamehe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkuu wa kusamehe, Mkunjufu wa
rehema.
17. Musa akasema kwa kunyenyekea: Ewe Mola wangu
Mlezi! Kwa haki ya kunineemesha kwako kwa kunipa hikima, na ilimu, niwezeshe
nitende kheri na yanayo faa. Ukiniwezesha hivyo basi kabisa sitakuwa msaidizi wa
makafiri.
18. Kulipo pambazuka asubuhi Musa alikuwapo
mjini, Misri, naye yumo katika khofu, akitaraji kufikiwa na madhara kutokana na
watu kwa sababu vile alivyo muuwa Mmisri. Akamwona yule Muisraili aliye mtaka
msaada jana, naye akamtaka msaada mara ya pili katika ugomvi na Mmisri mwengine.
Musa akamkemea kwa kumwambia: Hakika wewe mtu matata mno, na dhaahiri wewe ni
mpotovu. Unafanya yale yale uliyo yafanya jana, na unaniita tena nikusaidie!
19. Na Musa alipo taka kumtumilia nguvu Mmisri,
ambaye ni adui wao wote wawili; kwa sababu ya uadui huu, yule mtu alidhani kuwa
Musa atamuuwa, basi akasema: Unataka kuniuwa kama ulivyo muuwa mtu jana?
Wewe hutaki ila kuwa muasi tu katika nchi, wala hutaki kuwa miongoni wanao
lingania maslaha na kheri.
20. Akaja mtu mmoja Muumini katika kaumu ya
Firauni kutoka mwisho wa mji, ilipo enea khabari ya Musa kumuuwa Mmisri. Yule
mtu akamwambia Musa kwamba watu wanapanga kutaka kumuuwa. Akamwambia: Toka mji,
ukimbie usije ukauliwa! Hakika mimi ni katika wanao kupa nasaha.
21. Musa akautoka mji naye amejaa khofu wasije
maadui wakamdhuru, akimnyenyekea Mwenyezi Mungu amwokoe na udhalimu wa
makafiri.
22. Alipo elekea Madyana, kijiji cha Shuaibu -
kwa kuwa huko iko amani - alimwomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu amwongoe njia
ya kheri na ya kuokoka.
23. Alipo yafikia maji ya Madyana wanapo
nyweshea maji alikuta karibu na kisima kundi la watu wengi mbali mbali
wanawanywesha wanyama wao wa mifugo. Na pahali pa chini kuliko hapo pao
akawakuta wanawake wawili wanawazuia kunywa maji kondoo na mbuzi wao. Musa
akawaambia: Mbona mko mbali na maji? Wakajibu: Hatuwezi kusukumana, na wala
hatunyweshi sisi mpaka hawa wachunga wamalize wao kunywesha. Na baba yetu ni
mkongwe, hawezi kuchunga wala kunywesha wanyama.
24. Musa akajitolea kuwakhudumia akawanyweshea.
Kisha akenda kuegemea mti akipumzika baada ya kuhangaika kule, naye akisema kwa
unyenyekevu: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mwenye haja ya kheri yoyote na
riziki yoyote utayo niletea.
25. Mmmoja wa wale mabinti akaja na ujumbe
kutoka kwa baba yake baada ya kwisha jua khabari za Musa na wao wale mabinti.
Naye akaja na huku anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita ili akulipe ujira
kwa ulivyo tunyweshea maji. Basi alipo kwenda kwake na akamsimulia kisa chake
cha kutoka Misri, akasema yule mzazi wa mabinti: Usikhofu; umekwisha okoka kwa
hao watu madhaalimu. Kwani Firauni hana madaraka juu yetu.
26. Mmoja wa wale mabinti alisema: Ewe baba
yangu! Mchukue umpe kazi ya kuchunga kondoo na mbuzi na kuwasimamia kwa haja
zao. Hakika huyu ni mbora wa kumuajiri kwa sababu ya nguvu zake na uaminifu
wake.
27. Shuaibu a.s. akamwambia: Mimi nataka kukuoza
mmoja wa hawa mabinti zangu kwa mahari ya kunifanyia kazi muda wa miaka minane.
Ukitimiza kumi itakuwa ni khiari yako. Wala mimi sitaki kukulazimisha huo muda
mrefu. Na Inshallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mimi ni katika watu wema,
wenye kwenda nawe kwa ihsani na kutimiza ahadi.
28. Musa akasema: Hayo uliyo niahidi ni sawa
sawa baina yangu na wewe. Muda wowote katika huo nitakao kufanyia kazi itakuwa
nimekutimizia ahadi yako. Wala mimi sitaki zaidi kuliko hayo. Na Mwenyezi Mungu
ni shahidi kwa tunayo yasema.
29. Musa alipo timiza muda wake walio patana, na
akawa mume wa binti wa yule aliye mpokea, na akawa anarudi Misri, aliona njiani
mwake katika upande wa Mlima wa T'uri moto unawaka. Akawaambia walio kuwa pamoja
naye: Kaeni hapa. Mimi nimeuona moto, nimefurahi nao katika giza hili.
Nitawendea nikuleteeni khabari ya njia, au nipate kijinga cha moto mpate walau
moto wa kuota kujilinda na baridi.
30. Musa alipo ufikia moto alio uona alisikia
kutoka upande wa kulia kwenye mti wenye kumea katika eneo lilio barikiwa ubavuni
mwa Mlima, wito wa juu ukisema: Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu ambaye
hapana anaye stahiki kuabudiwa isipo kuwa Yeye, Mwenye kuumba viumbe vyote na ni
Mwenye kuvilinda na kuvihifadhi na kuvilea.
31. Na akanadiwa: Tupa chini fimbo yako.
Akaitupa chini. Mwenyezi Mungu akaigeuza ikawa nyoka. Musa alipo iona inakwenda
kama nyoka alikhofu, na akakimbia kwa kufazaika. Akaambiwa: Ewe Musa! Njoo,
unaitwa urejee pahala pako, wala usiogope. Kwani wewe ni katika walio hifadhiwa
na kila cha kuchukiza.
32. Na uingize mkono wako kwenye uwazi wa nguo
yako utatoka mweupe, bila ya ila wala maradhi. Na jiambatishe mkono wako ubavuni
mwako katika nguo ukiwa una khofu. Wala usishituke kwa kuona fimbo imekuwa
nyoka, na kuona mkono wako umekuwa mweupe. Kwani miujiza hii miwili inatokana na
Mwenyezi Mungu ya kumkabili nayo Firauni na kaumu yake watapo ukabili Ujumbe
wako kwa kuukadhibisha na hali wametoka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu.
33. Musa akasema, kwa khofu na kuomba msaada:
Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimemuuwa mtu katika hao, na nina khofu
watakuja niuwa kwa kisasi.
34. Na ndugu yangu, Harun, ni fasihi zaidi ulimi
wake kuliko mimi. Basi mtume awe pamoja nami katika kufikisha Utume, kwani mimi
nina khofu watanikanusha.
35. Mwenyezi Mungu akasema, kuitikia ombi lake:
Tutakutia nguvu kwa kumtuma Harun. Na tutakupeni nyinyi wawili madaraka, na
tutakuungeni mkono kwa miujiza. Kwa hivyo hawatoweza kukuvamieni. Na nyinyi
wawili na walio kufuateni na wakaongoka kwa msaada wenu, mtakuwa wenye
kuwashinda hawa makafiri.
36. Musa alipo wakabili kwa wito wake ulio
tiliwa nguvu na miujiza iliyo wazi, waliyakanusha waliyo yaona, na wakasema:
Haya si chochote ila ni uchawi unao mzulia Mwenyezi Mungu. Na hatukupata kusikia
haya unayo tuitia kwa baba zetu wa zamani walio tangulia.
37. Na Musa alisema kumjibu Firauni na kaumu
yake: Mola wangu Mlezi anajua kwa hakika kuwa mimi nimeleta Ishara hizi zenye
kuonyesha Haki na Uwongofu kutokana naye Yeye. Basi Yeye ndiye shahidi wangu kwa
haya, ikiwa nyinyi mnanikadhibisha. Na Yeye anajua kuwa mwisho mwema ni wetu
sisi watu wa Haki. Hakika makafiri hawapati kheri.
38. Na Firauni alipo shindwa kuhojiana na Musa,
na akaendelea na jeuri zake, alisema: Enyi wahishimiwa! Mimi sijui kama yupo
mungu wenu mwenginewe isipo kuwa mimi. Na akamuamrisha waziri wake Haman
amchomee matufali, na amjengee mnara mrefu apande, ende kumtazama huyo mungu
anaye mlingania Musa.
39. Firauni na majeshi yake wakaendelea
wakifanya kiburi katika nchi ya Misri kwa upotovu. Na wakadhani kuwa kabisa
hawato fufuliwa Akhera kwa ajili ya hisabu na malipo.
40. Tukamng'oa Firauni kwenye utawala wake, na
tukawavutia taratibu yeye na majeshi yake mpaka baharini, na tukawazamisha na
huku tunawatupia sababu ya dhulma yao. Basi zingatia, ewe Muhammad, na
uwahadharishe watu wako watazame vipi unakuwa mwisho wa wenye kudhulumu katika
dunia yao. Na hakika wewe ni mwenye kusaidiwa kupata ushindi juu yao.
41. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Na
tukawafanya hao ni wenye kuitia watu kwenye ukafiri, ambao khatima yake ni Moto.
Na Siku ya Kiyama hawampati wa kuwanusuru na kuwatoa kwenye adhabu.
42. Na tukawafanya katika dunia hii wenye kupata
laana, yaani wenye kutolewa wasiipate rehema yetu; na Siku ya Kiyama watakuwa
miongoni mwa walio angamizwa. Na yaliyo simuliwa katika Aya mbili hizi juu yao
ni dalili ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.
43. Na kwa yakini Mwenyezi Mungu alimteremshia
Musa Taurati, baada ya kuwahiliki wakanushao katika kaumu zilizo tangulia, ili
iwe nuru ya nyoyo. Kwani nyoyo hizo zilikuwa gizani, haziijui Haki wala uwongozi
mwema. Kwani hao walikuwa wakitangatanga tu katika upotovu, na hawaijui njia ya
kupatia rehema kwa mwenye kutenda kwa ajili yake, na wakawaidhika kwa yaliyomo
katika hiyo Taurati, na wakakimbilia kuzifuata amri, na kuyaacha yaliyo katazwa.
44. Wala wewe Muhammad, hukuwa na Musa upande wa
magharibi wa huo mlima, pale Mwenyezi Mungu alipo agana naye kumuamrisha Ujumbe.
Wala hukuishi zama za Musa, wala hukushuhudia alipo fikisha Utume. Basi vipi
hawa watu wako wanakanusha Utume wako na wewe unawasomea khabari za walio
tangulia?
45. Na lakini Sisi tumeziumba kaumu nyingi
katika vizazi vilivyo pitiwa na zama ndefu, hata wakasahau maagano yaliyo
chukuliwa kwao. Na wewe, ewe Mtume, hukuwa mkaazi wa Madyana hata ndio
uwasimulie watu wa Makka khabari zao. Lakini Sisi tumekutuma wewe, na tumekupa
khabari zao kwa njia ya wahyi (Ufunuo).
46. Wala wewe, ewe Mtume, hukuwepo hapo kando ya
mlima pale Mwenyezi Mungu alipo mwita Musa na akamteuwa kumpa Utume wake. Lakini
Mwenyezi Mungu amekujuvya haya kwa njia ya wahyi (ufunuo), kutokana na rehema
yake kwako na kwa umma wako, wapate kufikisha hayo kwa kaumu ambayo haikupata
kufikiwa na Mtume kabla yako wewe, ili wakumbuke.
47. Ingeli kuwa makafiri wanapo patwa na mateso
kwa sababu ya ukafiri wao wakataka udhuru na wakadai wakisema: Ewe Mola wetu
Mlezi! Mbona hukutuletea Mtume tukamuamini na tukaikubali miujiza yake nasi
tukawa miongoni mwa Waumini, basi usinge kuwepo Ujumbe wa Mitume.
48. Na alipo ileta Mtume wa Mwenyezi Mungu
Qur'ani kutokana na Mwenyezi Mungu, makafiri walisema: Laiti yeye angeli pewa
miujiza ya kuonekana na kama aliyo pewa Musa, na Kitabu cha kuteremka mara moja
kama Taurati! Na hali hao walimkataa Musa na Ishara zake, kama hivi leo wanavyo
mkataa Muhammad na Kitabu chake, na wakasema: Sisi tunawakataa wote wawili. Basi
kukataa ndiko kuliko pelekea kuikanya miujiza.
49. Ewe Mtume! Waambie: Ikiwa hamuiamini Taurati
na Qur'ani basi leteni kitabu kingine kinacho toka kwa Mwenyezi Mungu kilicho na
uwongofu bora kuliko hivyo, au kama hivyo, nami nikifuate pamoja nanyi, ikiwa
nyinyi mnasema kweli katika hayo madai yenu kwamba tuliyo kuja nayo ni uchawi.
50. Na ikiwa hawaitikii wito wako kwa kuleta
kitabu kiongofu zaidi, basi jua kuwa wamebanwa na hawakubakiliwa na hoja yoyote,
na kwamba kwa hayo wanafuata pumbao zao tu. Na hapana aliye zidi kwa upotovu
kuliko yule anaye fuata pumbao lake katika dini, bila ya uwongofu kutokana na
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu hamwafiki mwenye kuidhulumu nafsi yake kwa
kufuata upotovu bila ya kuitafuta Haki.
51. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu
amewateremshia Qur'ani kwa utungo, baadhi yake ikifuatia baadhi kwa mujibu wa
inavyo takikana na hikima, na kulingana na ahadi, na maonyo, na hadithi,
na mazingatio, ili wapate kupima na kuyaamini yaliomo ndani yake.
52. Wale ambao tuliwateremshia Taurati na Injili
kabla ya kuteremka Qur'ani, na wakaviamini vitabu hivyo viwili, na wakasadiki
yaliyo tajwa humo juu ya khabari za Muhammad na Kitabu chake, hao wanamuamini
Muhammad na Kitabu chake.
53. Na hao wakisomewa Qur'ani hufanya haraka
kutangaza Imani yao, na husema: Tumeyaamini hayo, kwani hayo ni Haki inayo toka
kwa Mola wetu Mlezi; na sisi tulimjua Muhammad na Kitabu chake hata kabla ya
kuteremka kwake, nasi tukanyenyekea kabla ya kusomwa kwake.
54. Hao ambao waliiamini Qur'ani na yaliyo
teremshwa kabla yake, watapewa malipo yao maradufu - kwa ajili ya kuvumilia kwao
mateso yaliyo wapata kwa ajili ya Imani, na wakakhiari vitendo vyema, na
wakayakabili maovu kwa kusamehe na ihsani, na wakatoa katika njia ya kheri
kutokana na mali aliyo wapa Mwenyezi Mungu.
55. Na wanapo sikia upotovu wa wajinga hujitenga
mbali nao, kwa kujiepusha na kuondoka, na husema: Sisi tuna a'mali yetu na
hatuiachi, na nyinyi mna a'mali yenu ya upotovu na madhambi yake yapo juu yenu.
Na sisi tunakuacheni na mambo yenu, kwani sisi hatupendi kusuhubiana na
majaahili.
56. Ewe Mtume! Hakika wewe una pupa sana kutaka
hawa watu wako waongoke. Lakini wewe huwezi kumuingiza katika Uislamu kila
umpendaye. Lakini Mwenyezi Mungu humwongoa kuendea Imani yule anaye mjua kuwa
ameelekea uwongofu na ameukhiari. Na Yeye ndiye Mwenye kujua, wala hapana ajuaye
zaidi kuliko Yeye, nani atakaye ingia katika safu za wenye kuongoka.
57. Na washirikina wa Makka walimwambia Mtume
s.a.w. kwa kujitolea udhuru kwa kubakia kwao katika dini yao: Tukikufuata wewe
katika dini yako Waarabu watatutoa katika nchi yetu, na watatushinda katika
utawala wetu. Na hakika wao ni waongo katika kutoa udhuru wao huo. Kwani
Mwenyezi Mungu alikuwa kawaweka imara na madhubuti katika nchi yao. Na akaifanya
nchi takatifu yenye amani, hawashambuliwi wala hawauwawi, na hali wao ni
makafiri. Na wanaletewa matunda na kheri nyengine za aina nyingi, ambazo
Mwenyezi Mungu anawaletea kutoka kila upande. Basi huwaje awaondolee amani, na
awaachilie wakinyakuliwa wakiongeza juu ya utakatifu wa Nyumba ya Alkaaba Imani
kumuamini Muhammmad! Lakini wengi wao hawaijui Haki. Lau kuwa wanaijua
wasinge khofu kunyakuliwa.
58. Watu hawa hawazingatii yaliyo wapata kaumu
zilizo kwisha tangulia. Iliangamizwa miji ya walio ghurika na neema za Mwenyezi
Mungu, na kisha wakazikanusha na wakamkanusha Mwenyezi Mungu. Na haya majumba
yao yamekuwa matupu, magofu, hayafai kukaliwa ila nadra tu kwa wapita njia. Na
yamebaki hayana mwenye kuyamiliki baada yao ila Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu na
ukarimu.
59. Na haikuwa katika hikima ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu - naye ndiye Mola wako Mlezi aliye kuumba na kukuteuwa - kuiangamiza
miji mikubwa ila baada ya kuwapelekea watu wake Mtume mwenye miujiza iliyo wazi
awasomee Kitabu kilicho teremshwa, na awabainishie sharia, na kisha wawe
hawaamini. Wala Sisi hatuangamizi miji mikubwa ila wakiwa watu wake wanaendelea
na udhalimu na uadui.
60. Na kila kitu mlicho ruzukiwa katika starehe
za dunia na mapambo yake kina ukomo wake kwa muda mfupi. Hayo yasikuzuieni
kuamini na kutenda vitendo vyema. Kwani hakika yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu huko
Akhera, nayo ni thawabu na neema za milele, yana nafuu zaidi, na yana dawamu
kuliko hayo yote. Basi kwa nini hamtumii akili zenu badala ya pumbao zenu?
61. Hawi sawa mwenye kuamini na akatenda mema na
akastahiki ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya malipo mema na Pepo, na akayapata
kama alivyo muahidi Mwenyezi Mungu; kulingana huyu na yule aliye kanusha na
akatenda vitendo viovu, na yakamzuga maisha ya dunia na mapambo yake, na kisha
Siku ya Kiyama akawa katika walio hudhurishwa kwa ajili ya hisabu, na akawa
katika wenye kuhiliki kwa adhabu.
62. Ewe Mtume! Kumbuka siku watapo simama hawa
mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuhisabiwa, naye Subhanahu akawaita kwa
kuwatahayarisha: Wako wapi hao miungu mlio dai kuwa ni washirika wangu, wapate
kukuteteeni na kukuombeeni?
63. Watasema waongozi wa makafiri katika walio
stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na vitisho vyake: Ewe Mola wetu Mlezi! Hawa
tulio waita kwenye shirki na tukawapambia upotovu tuliwapoteza. Kwa sababu wao
walikhiari ukafiri na wakaupokea, kama sisi tulivyo ukhiari na tukaupokea. Leo
sisi tunajitenga nao kwako na ukafiri walio ukhiari duniani. Hawakuwa wao
wakituabudu sisi; bali wakiabudu pumbao zao, na wakit'ii matamanio yao.
64. Na Mwenyezi Mungu kuwaamrisha makafiri ni
kwa kuwatahayarisha tu, kwa vile kuwataka wawaite wale miungu ya ushirikina
wawaokoe na adhabu yake, kama walivyo dai. Wakaitikia kwa unyonge, na wakawaita
kwa kuwa hawana hila. Wasipate jawabu yoyote. Wakaiona adhabu walio ahidiwa iko
mbele yao, na wakatamani lau kuwa katika dunia yao wangeli kuwa Waumini walio
ongoka, jinsi ya adhabu iliyo wafikia.
65. Na ewe Mtume! Taja vile vile siku
washirikina watapo itwa na Mwenyezi Mungu kwa kutahayarishwa, na
wakaambiwa: Mliwajibu nini Mitume wangu nilio watuma kwenu wakuiteni
kwenye Imani, nao wakafikisha Ujumbe?
66. Khabari hizo zikawapita hawazitambui kama
kwamba ni vipofu. Ikawa hapana amuulizae mwenziwe, kwani wote walikuwa sawa sawa
wameshindwa kujibu.
67. Hii ndiyo hali ya washirikina. Ama mwenye
kutubu kutokana na shirki yake, na akaamini Imani ya kweli, na akatenda mema,
basi huyo hutaraji kuwa kwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa walio fuzu kuipata radhi
ya Mwenyezi Mungu, na neema ya kudumu yenye kuendelea milele.
68. Na Mola wako Mlezi anaumba atakalo kwa uwezo
wake. Na anamkhitari amtakaye kwa hikima yake kumpa Ujumbe na ut'iifu kwa kujua
kwake mwenyewe kufaa kwao. Wala hawawezi viumbe, na wala si haki, kumchagulia
Mwenyezi Mungu walitakalo katika dini potovu, na miungu ya uwongo. Mtukufu
ametakasika shani yake na washirika.
69. Ewe Mtume! Mola wako Mlezi anajua baraabara
yaliomo katika vifua vya washirikina ya uadui wao juu yako, na wanayo tangaza
kwa ndimi zao ya kukushutumu na kukupinga kwa ulivyo teuliwa kupewa Utume.
70. Na Mola wako Mlezi, ewe Mtume, ndiye
Mwenyezi Mungu wa Haki, ndiye pekee Mwenye Ungu, Mwenye kustahiki peke yake
kuhimidiwa na waja wake katika dunia kwa neema zake na uwongofu wake, na katika
Akhera kwa uadilifu wake na kulipa kwake. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye hukumu,
na kuamua baina ya waja wake. Na kwake Yeye ndiyo marejeo ya kwendea.
71. Ewe Mtume! Sema: Enyi watu! Niambieni,
Mwenyezi Mungu akikufanyieni usiku uendelee mfululizo bila ya mchana mpaka
Siku ya Kiyama, je! Mnaye yeyote asiye kuwa Mwenyezi Mungu wa kukuleteeni mchana
wenye mwangaza mkaweza kushughulikia maisha yenu na kuendesha mambo yenu ya
dunia? Hamna hayo nyinyi. Basi kwa nini hamsikii kwa sikio la kuwaza na
kuzingatia?
72. Ewe Mtume! Waambie watu: Mwenyezi Mungu
akikujaalieni mchana mfululizo bila ya usiku mpaka Siku ya Kiyama, yupo asiye
kuwa Mwenyezi Mungu wa kukuleteeni usiku mkapata kupumzika na kazi za mchana?
Hamna hayo nyinyi. Basi kwa nini hamzioni Ishara za Mwenyezi Mungu,
mkaamini na mkaongoka?
73. Na miongoni mwa rehema za Mwenyezi Mungu kwa
viumbe vyake ni kuwa kawaumbia usiku na mchana, inayo fuatana, ili wapate
kupumzika usiku, na washughulikie kutafuta riziki zao na manufaa yao mengine
wakati wa mchana, na watambue fadhila za Mwenyezi Mungu juu yao wapate
kumshukuru.
"Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya usiku
umekukalieni moja kwa moja, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye
kuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii? Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu
angeli ufanya mchana umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani
asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je,
hamwoni? Na ni katika rehema zake amekufanyieni usiku na mchana mpate kupumzika
humo na mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru." Hapana shaka kuwa
kuumbwa kwa dunia kwa namna yake ilivyo sasa na ilivyo wekwa kwa mnasaba wa jua,
na kuzunguka kwake wenyewe kwa wenyewe kila siku, na kulizunguka jua kila mwaka,
hapana shaka kwamba haya yanaonyesha dhaahiri uwezo wa Mwenyezi Mungu na upweke
wake.
Na Aya tukufu inawazindua watu watambue ukweli ambao yawapasa
wauelewe, nao ni kwamba Yeye Mtukufu lau kuwa aliumba dunia iwe na usiku wa
milele, au iwe na mchana wa milele, basi hapanapo mungu mwengine anaye weza
kuwaneemesha watu kwa mchana na usiku wa kufuatana kama hivi.
Na
hivyo ni kuwa lau kuwa dunia inazunguka juu ya msumari-kati wake na pia
kulizunguka jua kwa kiwango kimoja kiasi ya siku 365 takriban, yangeli tokea
mabadiliko makubwa mno. Miongoni mwao ni kudumu giza katika nusu ya dunia, na
kudumu mwangaza katika nusu ya pili takriban. Na kwa hivi joto lingeli panda
katika nusu yenye mwangaza kwa kiasi kisicho weza kuchukulika. Na nusu yenye
giza ingeganda kwa barafu. Na pande zote mbili zisingeweza kuchukua kitu
chochote chenye uhai. Ama huu mpango ulivyo sasa unapelekea kupishana usiku na
mchana, na kwa hivyo kunapatikana mapumziko na utulivu wakati wa usiku, na
kushughulika wakati wa mchana. Na hali ya hewa inasilihi uhai wa binaadamu, na
wanyama, na mimea. Na haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu juu ya waja wake,
ambazo zinapelekea tukubali uwezo wake, na tudumu kumshukuru.
74. Na pia, ewe Mtume, kumbuka siku watapo
itwa washirikina na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa wito wa kuwatahayarisha,
wakaambiwa: Wako wapi washirika ambao mkidai kuwa ni miungu wa kukunusuruni, au
waombezi wa kukuombeeni?
75. Na Siku ya Kiyama tutatoa kutoka kila umma
shahidi, naye ndiye Nabii wao, wa kutoa ushahidi dhidi yao kwa waliyo kuwa
wakiyafanya duniani. Hapo Sisi tutawaambia wakhalifu miongoni mwao: Nini hoja
yenu kwa mliyo kuwa mkiyatenda ya ushirikina na maasi? Watashindwa kujibu, na
watajua hapo kuwa Haki yote iko kwa Mwenyezi Mungu, tangu mwanzo mpaka mwisho.
Na yatapotea, kama vinavyo potea vitu vilio potea, yote waliyo kuwa wakimzulia
Mwenyezi Mungu.
76. Sura hii inasimulia kisa cha Qaruni. Naye
alikuwa katika kaumu ya Musa. Akapanda kiburi juu yao kwa kughurika kwa nafsi
yake na mali yake. Na Mwenyezi Mungu alikuwa kampa khazina za mali mengi. Hata
ikawa funguo zake tu zikiwaemea kundi la wanaume wenye nguvu! Na alipo
ghurika na neema ya Mwenyezi Mungu juu yake, na akakufuru kwa sababu yake, watu
walimpa nasaha, wakamwambia: Usidanganyike kwa mali yako, wala furaha kwa ajili
yake isikusaliti hata ukaacha kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kwani hakika Mwenyezi
Mungu hawapendi watu walio danganyika na wakasalitika. Na funzo la kisa hichi ni
kuwa makafiri walio mkataa Muhammad s.a.w. walighurika na mali yao. Basi Qur'ani
inawaelezea kuwa mali yao si chochote cha kutajika ukilinganisha na mali ya
Qaruni.
77. Na katika utajiri na neema alizo kupa
Mwenyezi Mungu toa fungu kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi Mungu, na tenda a'mali
kwa ajili ya makaazi ya Akhera. Na wala usiinyime nafsi yako fungu lake kwa
matumizi ya halali katika dunia. Na wafanyie wema waja wa Mwenyezi Mungu, kama
vile alivyo kufanyia wema wewe kwa neema zake. Wala usifanye uharibifu katika
ardhi ukapita mipaka ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu
hawafurahii mafisadi kwa vitendo vyao viovu.
78. Basi Qaruni hakusikia nasaha ya watu wake,
na akasahau fadhila ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yake. Na akajifanya hajui kwamba
Mwenyezi Mungu alikwisha waangamiza wengi walio mzidi yeye sana katika uwezo na
mazoezi ya kuchuma mali kwa njia mbali mbali za uchumi. Na wakosefu hawaulizwi
madhambi yao, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anayajua. Basi wataingizwa Motoni
bila ya hisabu. Kuulizwa kwao ni kwa ajili ya kutahayarishwa tu.
79. Na Qaruni hakujali nasaha za watu wake.
Akawatokea naye kajipamba mapambo yake. Wakadanganyika naye wale walio kuwa
wanapenda starehe za maisha ya dunia, na wakatamani nao wangeli kuwa nayo mali
na hadhi kubwa ya maisha kama aliyo pewa Qaruni
80. Ama wale ambao Mwenyezi Mungu amewaruzuku
ilimu yenye manufaa hawakusalitika na hayo. Wakawaelekea walio danganyika kwa
kuwanasihi wakiwaambia: Msiyatamani haya, wala msiiache Dini. Kwani yaliyoko kwa
Mwenyezi Mungu ya thawabu na neema ni safi zaidi kwa mwenye kuamini na akatenda
mema. Na hiyo ni nasiha ya kweli ambayo hawaikubali ila wenye kuzipiga jihadi
nafsi zao, na wakasubiri katika ut'iifu.
81. Mwenyezi Mungu akamdidimiza katika ardhi, na
ardhi ikammeza yeye na nyumba yake na vyote vilio kuwemo ndani yake, mali na
mapambo yake. Hakuwa na wasaidizi wa kumkinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na
wala yeye mwenyewe hakuweza kujinusuru nafsi yake.
82. Na wale walio kuwa karibuni wakikitamani
cheo chake cha duniani, wakawa wanatamka maneno ya masikitiko na majuto baada ya
kuyafikiri yaliyo msibu yeye. Wakawa wanasema: Hakika Mwenyezi Mungu humkunjulia
riziki amtakaye katika waja wake Waumini na wasio kuwa Waumini. Na humdhikisha
amtakaye katika hao. Na wakawa wanasema kwa kushukuru: Lau kuwa Mwenyezi Mungu
hakutufanyia hisani kwa kutupa uwongofu tukafuata Imani, na akatuhifadhi
tusiporonyoke angeli tutia katika mitihani kwa kutukubalia tuliyo kuwa
tunayatamani, na akatufanyia kama alivyo mfanyia Qaruni. Hakika wanao ipinga
neema ya Mwenyezi Mungu hawafanikiwi kwa kuokoka na adhabu yake.
83. Hayo ndio makaazi ambayo umesikia khabari
zake, ewe Mtume, na zikakufikia sifa zake, nayo ni Pepo. Tumeiweka
makhsusi kwa ajili ya Waumini wat'iifu, wasio taka kujipa ubora na utukufu wa
kidunia, na wala hawapotoki kuendea ufisadi na maasi. Na mwisho mwema ni wa wale
ambao nyoyo zao zimejaa khofu ya Mwenyezi Mungu, na wanatenda yanayo mridhisha
Yeye.
84. Mwenye kuja na wema, nao ni Imani na vitendo
vyema, atapata malipo marudufu kwa ajili yake. Na mwenye kuja na uovu, nao ni
ukafiri na maasi, halipwi ila mfano wa vitendo vyake viovu.
85. Hakika Mwenyezi Mungu aliye
kuteremshia Qur'ani na akakulazimisha uifikishe kwa watu na ushikane nayo hapana
shaka atakurudisha kwenye miadi, nako ni Siku ya Kiyama, ili apambanue baina
yako na wale wanao kukadhibisha. Ewe Mtume! Waambie makafiri: Mola wangu Mlezi
ndiye anaye jua kwa ujuzi usio pikuliwa na yeyote, nani aliye mpa uwongofu na
uwongozi, na nani aliye tumbukia katika upotovu unao tambulikana na kila mwenye
akili nzima.
86. Ewe Mtume! Wewe hukuwa wewe ukitaraji na
ukingojea uteremshiwe hii Qur'ani. Lakini Mwenyezi Mungu amekuteremshia kutoka
kwake kwa kukurehemu wewe na umma wako. Basi ikumbuke neema hii, na shikilia
kuifikisha. Wala usiwe wewe na wanao kufuata kuwa wasaidizi wa makafiri kwa
wanayo yataka.
87. Wala makafiri wasikuachishe kuzifikisha Aya
za Mwenyezi Mungu na kuzitenda, baada ya kwisha teremka wahyi (ufunuo) kutoka
kwa Mwenyezi Mungu, na ukawa ndio Ujumbe wako. Na shikilia Wito kuwaitia watu
kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu. Wala usiwe wewe wala wanao kufuata katika
wasaidizi wa washirikina kwa kuwasaidia kwa wayatakayo.
88. Wala usimwabudu mungu yeyote isipo kuwa
Mwenyezi Mungu tu. Kwani hapana kabisa mungu wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa
Yeye. Kila kitu isipo kuwa Mwenyezi Mungu kitaangamia na kwisha. Wa kudumu
milele ni Yeye Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye mwenye hukumu ya kutekeleza duniani
na Akhera. Na kwake Yeye ndiyo yako marejeo ya viumbe vyote, hapana hivi wala
hivi.