1. Harufi hizi na mfano wa hizi ndizo
zikakusanyika kuifanya Qur'ani kuwa ni muujiza ulio washinda watu kuiga mfano
wake, ijapo kuwa hizo harufi ndizo wanazo zitamka. Basi mwenye kuitilia shaka
hii Qur'ani kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu au la, basi na alete mfano wake. Na
hatoweza.
2. Maneno haya niliyo kufunulia ni Aya za Kitabu
chenye kuweka wazi hukumu zote ziliomo ndani yake.
3. Ewe Nabii! Hebu jionee huruma nafsi yako.
Usijikere kwa kuhuzunukia inadi ya watu wako, na kuto amini kwao.
4. Sisi tunaweza kuwaletea muujiza wa
kuwalazimisha Imani, wat'ii kwa unyenyekevu amri yake, na yatimie unayo
yatarajia. Lakini hatuwaletei, kwa sababu mwendo wetu ni kuwaongoza watu waamini
bila ya kuwalazimisha, ili isikosekane hikima ya kujaribiwa kwa mitihani, na
yanayo kuja baada yake ya thawabu na adhabu.
5. Wala Mwenyezi Mungu hawaletei watu wako kwa
ufunuo wake ya kuwakumbusha Dini ya Haki kuwa ni rehema kwao, ila wao huzua upya
upinzani na ukafiri kuukataa. Kwani njia ya uwongofu imekwisha zibwa mbele yao.
6. Hawa hakika wamekadhibisha Haki uliyo ileta,
na wakaifanyia maskhara. Lakini wewe wasubirie. Wataona matokeo ya maskhara yao
ya kuangamiza.
7. Hivyo hao wanatenda watendavyo katika ukafiri
wao na kukadhibisha kwao wala hawaangalii baadhi ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu
katika hii hii ardhi? Lau kuwa wanaangalia kwa kuzingatia wangeli ongoka. Hebu
wazingatie hii mimea ya kila namna yenye manufaa tunayo itoa Sisi kwenye ardhi,
na wala hawezi hayo isipo kuwa Mungu Mmoja Muweza.
8. Hakika katika kutoka kwa hii mimea ni dalili
kubwa ya kuwepo Muumba Muweza. Lakini wengi wa watu si wenye kuamini.
9. Hakika Mwenye kumiliki mambo yako, na Mwenye
kukulinda, ndiye atakaye waadhibu hao wanao kadhibisha, na ndiye Mwenye
kuwafadhili Waumini kwa rehema.
10. Ewe Muhammad! Watajie watu wako kisa cha
Musa pale Mola wako Mlezi alipo mwita: Ewe Musa! Nenda kwa Utume kwa watu walio
dhulumu nafsi zao kwa ukafiri, na wakawadhulumu Wana wa Israili kwa kuwafanya
watumwa na kuwauwa watoto wao wanaume.
11. Nenda kwa kaumu ya Firauni; kwani hao
wamepita mipaka katika dhulma yao. Ama ajabu ya watu hawa! Hawaogopi nini litalo
wafika kwa vitendo vyao hivi, wakatahadhari?
12. Musa akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi
nina khofu wasije kuukataa ujumbe wangu kwa kiburi na inda.
13. Na mimi nimejaa dhiki kwa kuwa wataniambia
mwongo, na ulimi wangu si mkunjufu wa kuweza kuhojiana nao kama ninavyo
penda. Basi mtume Jibril ende kwa ndugu yangu aje kuniunga mkono katika
hii kazi yangu.
14. Na watu hawa wana kisasi juu yangu. Kwani
mimi nilimuuwa mtu katika wao. Basi nina khofu watakuja niuwa kwa kisasi
kabla sijatimiza kazi yangu. Hayo yananizidisha khofu.
15. Mwenyezi Mungu akamwambia: Hawatokuuwa. Na
kwa mintarafu ya Haruni nimekukubalia ombi lako. Basi nendeni nanyi mmejizatiti
na miujiza yetu. Mimi niko pamoja nanyi kwa ulinzi. Nayasikia yanayo jiri baina
yenu na Firauni. Nyinyi mtapata ushindi, na kuungwa mkono.
16. Muelekeeni Firauni na mwambieni: Sisi ni
Watume wawili tumetumwa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
17. Anakwambia Mola Mlezi wa walimwengu wote:
Waachilie huru Wana wa Israili, wende nasi.
18. Firauni akamwambia Musa kwa kumsimbulia,
naye alimtambua walipo ingia na wakakadimisha Ujumbe wao, kwani alilelewa mle
mle katika kasri lake: Hatukukulea sisi ulipo kuwa mtoto? Na ukaishi chini ya
ulezi wetu kwa miaka mingi katika umri wako?
19. Na ukatenda makosa yako ya jinaya maovu
kumuuwa mtu katika kaumu yangu, na ukazikanusha neema zangu nilizo kufanyia,
hukuwahifadhi raia zangu, ukaushambulia ungu wetu kwa kudai kuwa wewe ati ni
Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
20. Musa akasema: Niliyafanya uliyo yataja kwa
kutojua yanayo faa kutambulikana kwa akili nayo ni jambo la kuuwa. Basi hapana
masimbulizi juu yangu.
21. Nikakukimbieni nilipo khofu kuwa mtakuja
niuwa kwa jinaya hii ambayo sikuukusudia. Mola wangu Mlezi akanitunukia fahamu
na ilimu, kwa fadhila zake na neema zake, na akanifanya mmoja katika Mitume.
22. Musa akaashiria sifa katika sifa ovu kabisa
za Firauni, nayo ni kuwa kawafanya watumwa Wana wa Israili, na akiwauwa watoto
wao wanaume. Na akakataa kukuita kule kulelewa kwake katika jumba la Firauni
kuwa ni neema, kwani yaliyo sabibisha hayo ni yale aliyo kwisha yataja, ndio
yeye alitupwa mtoni aokoke asiuliwe. Akaishia kwenye jumba la Firauni. Na lau
kuwa si hivyo basi angeli lelewa na wazazi wake.
23. Firauni akasema: Na nini hizo sifa za Mola
Mlezi wa walimwengu wote ambaye unakithiri kumtaja, na wewe unadai kuwa ni Mtume
wake, na hali sisi hatujui lolote khabari zake?
24. Musa akasema: Yeye huyo ndiye Mwenye
kuzimiliki mbingu na ardhi na kila kilio baina yao. Ikiwa nyinyi mna yakini ya
ukweli wa jawabu hii basi mtanafiika, na mtaongoka, na mtajua kuwa ufalme wa
Firauni wa kujidai haufui dafu mbele ya Ufalme wake Mwenyezi Mungu. Kwani ufalme
wa Firauni haupindukii hata eneo moja katika hii dunia.
25. Firauni kuonyesha mastaajabu kwa wale walio
mzunguka kwa kuwa Musa katika jawabu yake alipo mtaja Mola wake Mlezi na
akadhukuru Ufalme wake hakuugusia hata kidogo ufalme wa Firauni, alisema:
Mwayasikiaje maneno ya Musa?
26. Musa akiendelea na usemi wake bila ya kujali
hasira za Firauni na uchafu wa maneno yake, akasema: Ndiye huyo Mola Mlezi wa
walimwengu wote, aliye kuumbeni nyinyi na baba zenu walio tangulia. Na miongoni
mwa hao walikuwako walio dai ungu kama unavyo dai wewe. Na wao wameteketea. Na
wewe utateketea, na hayo unayo yadai yatapotelea mbali. Kwani Mungu wa kweli
hafi.
27. Firauni akwaambia watu wake yale yanayo
mtibuwa roho na kumghadhibisha, akautaja Utume wa Musa ni kwao wao, wala si
kwake yeye, na akambandikiza wazimu, kwa kuwa ati akiulizwa kitu hujibu kingine,
na anamsifu Mola Mlezi kwa sifa za kiajabu ajabu. Na kwa hivyo Firauni
anawahimiza wamkadhibishe.
28. Musa akasema: Ikiwa nyinyi mna akili, basi
uaminini Ujumbe wangu. Kwani kuchomoza jua na kuchwa kwake kwa mpango madhubuti
ni dalili wazi ya Mwenye kuumba. Kwa hivyo basi ni nyinyi ndio mnastahiki
kuambiwa wendawazimu.
29. Firauni akamwambia Musa: Ukimfuata mungu
yeyote badala yangu mimi, utakuwa mmoja katika wanao ijua hali yao mbaya katika
magereza yangu. Na yeye Firauni kaangukia kitisho hichi baada ya kushindwa
kuondoa athari za kazi za Muumbaji.
30. Musa akasema kwa upole kwa kutumai asaa
akaamini: Utanitia gerezani hata nikikuletea ushahidi mkubwa wa ukweli wa haya
niyasemayo?
31. Firauni akasema: Ulete ushahidi utao onyesha
Unabii wako kama wewe kweli unasema kweli katika wito wako. Kasema hayo kwa
tamaa ya kuwa huenda akapata kipengee cha udhaifu katika hoja zake.
32. Musa akaitupa fimbo yake mbele yao. Ikageuka
nyoka kweli kweli, si kitu cha uwongo cha uchawi kinacho fanana na nyoka.
33. Musa akautoa mkono wake kutoka mfukoni
mwake. Hiyo ni Ishara ya pili. Nao ukawa mweupe, bila ya maradhi, hata
wakashangaa watazamaji kwa kumetuka kwake.
34. Firauni akawaambia watu wake: Hakika Musa ni
mchawi bingwa katika uchawi wake. Kasema hayo kwa kuchelea watu wake wasiifuate
Haki waliyo iona kwa Musa.
35. Tena Firauni akasema: Mchawi huyu anataka
kunifanyia kahari apate kukutoeni katika hii nchi yenu. Na haya ni uchochezi
dhidi ya Musa, kwani katika la dhiki mno katika hayo yaliyo dhiki ni mtu kuiacha
nchi yake, na khasa ikiwa kwa kahari. Naye akataka mawazo ya wale walio kuwa
wanamuabudu. Kasahau ungu wake kwa nguvu za Ishara za Musa.
36. Watu wake wakamwambia: Akhirisha kukata
shauri yao hawa, na uwatume askari wende wawakusanye wachawi katika raia zako.
Kwani uchawi hupingwa kwa uchawi.
37. Watakuletea wengi, na wote wamebobea kwa
uchawi, na wamemshinda Musa kwa ufundi na ustadi. Wamekusudia kwa haya
kumpunguzia dukuduku lake Firauni.
38. Wakakusanywa wachawi kutoka kila upande wa
nchi. Wakawekewa wakati wa mchana siku ya Sikukuu kukutana na Musa.
39. Na watu wakahimizana kuhudhuria siku hiyo
waone ramsa wakiambizana: Mtakusanyika? Yaani ndio: Mkusanyike!
40. Wakatangaza matarajio yao ya kushinda
wachawi, ili wapate kuthibiti katika dini yao, na pia ndio kampeni ya nguvu na
juhudi apate kushindwa Musa.
41. Walipo kuja wachawi kwa Firauni walimwambia:
Je! Tutapata kwako ujira mkubwa pindi tukishinda?
42. Firauni akasema: Naam, mtapata mnacho
kisema. Na juu ya huo ujira mkubwa mtakuwa watu wa karibu kwangu, watu wa cheo
na madaraka.
43. Ulipo fika wakati ulio wekwa katika siku
iliyo pangwa Musa aliwaambia wachawi: Tupeni huo uchawi mnao taka kuutupa.
44. Wakazitupa kamba zao na fimbo zao, na watu
wakazugwa wakaona kama ni nyoka wanakwenda. Wakaapa kwa utukufu wa Firauni na
nguvu zake hapana shaka hawa leo watashinda
45. Musa tena akatupa fimbo yake. Mara ikawa
joka kubwa likaingia kuvimeza vile walivyo vizua kwa uchawi, navyo ni kamba na
fimbo, wakidanganya kuwa ni nyoka wanao kwenda.
46. Wachawi wakaanguka wakasujudu kumsujudia
Mwenyezi Mungu, walipo yakinika kuwa mambo ya Musa si uchawi.
47. Wakasema ili kutia mkazo kule kusujudu kwao
kwa kauli yao: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.
48. Na wakabainisha kuwa hakika Mola Mlezi wa
walimwengu wote walio muamini ndiye: Mola Mlezi wa Musa na Harun.
49. Firauni kwa kukasarika kuwa wale wachawi
wamemuamini Musa bila ya yeye kuwapa ruhusa, aliwatishia ya kwamba yeye ndiye
mwalimu wao aliye wafunza fani za uchawi, na watakuja jua adhabu itakayo
wateremkia. Akawaambia: Nitakata mikono yenu na miguu yenu mbali mbali, nitakata
wa kulia huu kwa wa kushoto huu, na kinyume cha hayo. Na nyote nitakutundikeni
juu ya misalaba.
50. Wachawi wakasema: Hapana la kutudhuru sisi
kwa adhabu unazo tutishia, kwani sisi ni wenye kurejea kwenye malipo ya Mola
wetu Mlezi. Na Yeye ndiye mbora wa kulipa na mbora wa kuadhibu.
51. Hakika sisi tunataraji Mola wetu Mlezi
atatusamehe makosa yetu tuliyo yafanya zamani, kwa kuwa sisi ndio wa mwanzo wa
Waumini katika kaumu yako.
52. Na Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Musa a.s.
atoke usiku usiku pamoja na Waumini miongoni mwa Wana wa Israili, ilipo kuwa
tena haiwi kumsubirisha Musa. Mpango ukawa wa makundi mawili kwamba atangulie
Musa na kaumu yake, na Firauni afuatie na kaumu yake, mpaka waingie katika
maingilio ya njia ya baharini, na Mwenyezi Mungu awateketeze.
53. Firauni akawatuma askari wake katika miji ya
mamlaka yake, wawakusanye wenye maguvu katika kaumu yake, alipo jua kuwa Musa
kesha toka na Wana wa Israili, ili awazuie lile walilo kusudia.
54. Firauni akasema: Hakika hawa Wana wa Israili
walio kimbia na Musa ni taifa dogo kwa nguvu zao. Idadi yao ni chache. Anasema
hayo kutia mori katika nyoyo za askari wake.
55. Na wao juu ya hivyo, wanatutibua roho kwa
kuvunja amri yetu na kutoka bila ya idhini yetu.
56. Na sisi ni wengi. Miongoni mwa ada zetu ni
kuchukua hadhari, na kuwa macho, na kupania.
57. Tukawatoa Firauni na askari wake kwenye nchi
yao iliyo fanana na mabustani yapitiwayo na mito kati yao, wakaangamia kwa
kujitenga kwao na Haki, na kuchochewa kutaka kumfuatia Musa, kama ilivyo kuja
katika Aya tatu zilizo tangulia.
58. Tukawatoa, kadhaalika, kwenye khazina za
dhahabu na fedha, na majumba waliyo kuwa wakiyakalia, wakineemeka kwa uzuri wake
na ubora wa starehe zake.
59. Ni kutoka kama huku kwa ajabu tulivyo
kueleza ndivyo tulivyo watoa, na tukawapa ufalme huo na kila namna ya
neema zilizo kuwamo Wana wa Israili, baada ya kuwa masikini hawana mbele wala
nyuma.
60. Firauni na watu wake wakakaza mwendo ili
wapate kuwawahi Wana wa Israili. Wakawakuta wakati wa kuchomoza jua.
61. Walipo onana makundi mawili, watu wa Musa
walisema: Hakika Firauni na watu wake watatupata. Basi tutaangamia.
62. Musa akasema: Hakika mimi ninao uangalizi wa
Mwenyezi Mungu unao nifuata kwa kunihifadhi. Na Yeye ataniongoza kwenye Njia ya
uwokovu. Amesema hayo ili awatuze kuwa watasalimika, na iwe mbali na mawazo yao
fikra ya kutisha kwamba watakuja patikana.
63. Tukamuamrisha Musa kwa wahyi, ufunuo, aipige
bahari kwa fimbo yake. Ikapasuka bahari njia kumi na mbili kwa mujibu wa idadi
ya mataifa ya Wana wa Israili. Kila njia katika hizo njia ilikuwa na kizuizi cha
maji yaliyo nyanyuka kama mlima ulio simama imara.
64. Tukawajongeza Firauni na kaumu yake mpaka
wakaingia kwenye zile njia nyuma ya Musa na kaumu yake.
65. Tukamwokoa Musa na walio kuwa pamoja naye
kwa hifadhi ya bahari nayo imeshikamana, mpaka wakamalizika kuvuka.
66. Kisha tukamzamisha Firauni pamoja na walio
kuwa pamoja naye kwa kuwafudikiza kwa maji pale walipo wafuata.
67. Hakika katika vituko hivi vya ajabu vya
kiungu pana funzo la kuzingatia kwa atakaye kunafiika. Lakini watu wengi si
wenye kusadiki.
68. Hakika Muumba wako na Mlezi wako ndiye huyo
Mwenye nguvu katika kuwaadhibu wanao kanusha, Mwenye kuwaneemesha kwa rehema
Waumini.
69. Ewe Mtume! Na wasomee makafiri hadithi ya
Ibrahim , Alayhi Ssalaam.
70. Alipo mwambia baba yake: Mnaabudu kitu gani
hichi, ambacho hakifai kuabudiwa? Anakusudia kwa hayo kuyakebehi masanamu.
71. Wakasema kujibu kwa njia ya kujitapa:
Tunaabudu masanamu, nasi tunadumu daima dawamu tukiyaabudu, kwa kuyaadhimisha na
kuyatukuza!
72. Ibrahim akasema: Kwani yanasikia madua yenu?
Au yanakuitikieni mnapo yaomba? Kwa hayo anakusudia kuwanabihisha upotovu wa
mwendo wao.
73. Au yanakuleteeni manufaa mnapo yat'ii? Au
yanakupatilizeni kwa madhara mkiyaasi?
74. Wakasema: Hawafanyi lolote katika hayo.
Lakini sisi tumewakuta baba zetu wakiyaabudu mfano wa ibada yetu. Basi sisi
tukawafwata kwa waliyo kuwa wakiyafanya.
75. Ibrahim akasema kwa kuwasusuika: Je!
Mlifikiri hata mkalijua jambo lolote lilio kupelekeeni kudumu na kuyaabudu hayo
masanamu?
76. Nyinyi na baba zenu wa zamani - ati haya
yanastahiki kuabudiwa au la? Lau mngeli zingatia mngeli jua kuwa hakika nyinyi
mko katika upotovu ulio wazi.
77. Kwani hakika hao mnao waabudu badala ya
Mwenyezi Mungu ni maaadui kwangu mimi na kwenu. Basi mimi siwaabudu hao. Lakini
ninaye muabudu na najijongeza kwake ni Muumba wa walimwengu wote, na Mwenye
kumiliki mambo yao, na Mwenye kuwalinda.
78. Ambae ndiye aliye nizua kabla sijawa
chochote akaniumba kwa bora ya umbo, na akanitunukia uwongofu wa kunifikishia
kwenye mafanikio yangu ya duniani na Akhera.
79. Na Yeye ndiye aliye nineemesha kwa vyakula
na vinywaji, na akaniwezesha kuvipata na kunafiika kwavyo, ili kuhifadhi uhai
wangu.
80. Na yakinishukia maradhi ni Yeye ndiye anaye
niponesha, kwa kunisahilishia sababu za kupona na kuniwezesha kuzipata.
81. Na Yeye ndiye atanifisha ikifika ajali
yangu, na tena atanihuisha mara nyengine kwa ajili ya hisabu na malipo.
82. Na Yeye ndiye ninaye mtumai kunighufiria na
kuyasemehe makosa yangu madogo madogo ya kujikwaa duniani, utapo fika
wakati wa hisabu.
83. Ibrahim a.s. akasema kwa kuomba: Mola wangu
Mlezi! Nitunukie ukamilifu wa ilimu na vitendo, ili nipate kustahili kuubeba
Ujumbe wako na hukummu kwa waja wako, na niwezeshe niungane pamoja na kundi la
watendao wema.
84. Na nijaalie nipate sifa nzuri na kumbusho
jema kwa kaumu zitazo kuja baada yangu, mabaki yake yasalie mpaka Siku ya
Kiyama.
85. Na nijaalie katika waja wako ulio watunukia
neema za Peponi, kuwa ni malipo kwa sababu ya Imani yao kukuamini Wewe, na ibada
yao kukuabudu Wewe.
86. Na mjaalie baba yangu astahili msamaha kwa
kumwezesha kuwa Muislamu. Na yeye alikuwa kamuahidi kusilimu siku alio
achana naye, kwani yeye huyo baba alikuwa ameitupa kando njia ya uwongofu na
uwongozi.
87. Wala usinitie aibu au hizaya mbele ya watu,
Siku watapo tolewa makaburini kwa ajili ya hisabu na malipo.
88. Siku ambayo hapana mtu ataye nafiika kwa
mali ayatoe, au kwa wana wamsaidie.
89. Isipo kuwa aliye kuwa Muumini, na akamkabili
Mwenyezi Mungu na moyo ulio mzima, hauna maradhi ya ukafiri, na unaafiki, na
riya (kujionesha).
90. Na Pepo itajongezwa, na itakaribishwa pahala
pa watu wema. Basi wataiendea wale walio jikinga na ukafiri na maasi, na
wakaikubali Imani na ut'iifu duniani.
91. Na Moto utaletwa mbele ya walio iacha Dini
ya Haki, mpaka ndimi zake zikaribie kuwanyakua, nao watakuwa majutoni.
92. Wakaambiwa kwa kuwatahayarisha: Iko wapi
hiyo miungu yenu mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu?
93. Badala ya Mwenyezi Mungu, na mnadai kuwa ati
ndio itakuombeeni hii leo? Je! Inakufaeni kitu kwa kukunusuruni, au hata
inajifaa wenyewe kujisaidia? Hapana lolote. Kwani wao na miungu yao ni kuni za
Moto.
94. Watatumbukizwa katika Jahannamu kifudifudi,
wakipinduliwa pinduliwa mpaka waishie ndani kabisa shimoni, wao na walio
wapoteza na wakawatia katika madhambi na upotovu.
95. Na pamoja nao watakuwapo wasaidizi wa
Ibilisi walio kuwa wakiwapambia shari na madhambi, au wale watu na majini walio
wakiwafuata katika maasi.
96. Watasema huku wakiungama makosa yao, na huku
wanagombana na miungu yao waliyo kuwa wakiiabudu:
97. Wallahi! Hakika sisi tulikuwa katika dunia
yetu tumepotea kweli, na wajinga wa kutupwa, na tumeiacha Haki ambayo haina
kificho ndani yake.
98. Pale tulipo kufanyeni nyinyi tulio kuabuduni
badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ati ni sawa sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote
katika kustahiki kuabudiwa, juu ya kuwa hamjiwezi wala hamfai kwa lolote.
99. Wala hapana walio tutia katika hilaki hii
ila wakosefu walio tupotoa tukaiwacha Njia Iliyo Nyooka.
100. Basi hapana wa kuombwa akaja kutuvua na
adhabu hii kama tulivyo dhania pale kwanza.
101. Wala hapana rafiki wa kuwaonea uchungu kwa
hali yao, licha ya kuwaokoa.
102. Basi hapo ndio wanajitamania nafsi zao lau
wangeli rejea duniani wapate kuwa Waumini ili waokoke.
103. Na hakika katika khabari za Ibrahim zilizo
tajwa yapo mawaidha na mazingatio kwa mwenye kutaka mawaidha na akazingatia. Na
wala si wengi katika watu wako wanao somewa khabari hizi wenye kuitikia wito
wako.
104. Na hakika hapana shaka Mola wako Mlezi ni
Muweza wa kuwaadhibu wanao kadhibisha, naye ni Mfadhili wa watu wema kwa neema
nyingi.
105. Na Mwenyezi Mungu ametaja khabari za Nuhu
kwa kauli yake: Kaumu ya Nuhu iliukanusha Utume wake, wakamrudishia mwenyewe.
Kwa kitendo hicho ikawa wamewakadhibisha Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa
wito wao ni mmoja katika asli yake na lengo lake.
106. Waliukanusha Utume huu pale alipo waambia
ndugu yao Nuhu - ndugu kwa makhusiano ya nasaba si kwa Dini - akiwahadharisha:
Hamumchi Mwenyezi Mungu, mkaacha kuabudu wenginewe?
107. Hakika mimi ni Mtume, nimetumwa kwenu
nikuongoeni kwenye Njia ya wongofu, na ni muaminifu wa kufikisha huu Ujumbe.
108. Basi mkhofuni Mwenyezi Mungu, na fuateni
amri yangu katika hayo ninayo kuitieni kwayo ya kumuamini Mwenyezi Mungu wa
pekee na kumt'ii.
109. Na wala sitaki kwenu ujira kwa ajili ya
ninayo kupeni ya nasaha na wito. Na sina malipo ila kwa Mwenye kuwaumba viumbe
wote, Aliye miliki mambo yao.
110. Basi tahadharini na adhabu ya Mwenyezi
Mungu, na fuateni ninayo kuamrisheni.
111. Watu wa Nuhu, huku wakiukataa wito wake,
walisema: Hatutokuwa na imani nawe maadamu wanakufuata watu duni kabisa, wasio
kuwa na hadhi wala mali.
112. Nuhu akasema: Kitu gani cha kunijuvya
uchache wa hadhi yao na mali yao? Nikitakacho mimi kwao ni Imani yao bila ya
kutafuta kuzijua kazi zao.
113. Hapana wa kuwalipa kwa vitendo vyao na
kazi zao ila Mola wangu Mlezi; kwani Yeye ndiye anaye yajua vyema ya
undani wao. Kama nyinyi ni watu watambuzi mngeli tambua hayo.
114. Wala mimi siye wa kuwafukuza watu wanao
uamini wito wangu vyovyote itavyo kuwa hali yao ya ufakiri au utajiri, kwa
sababu ati ya kukubalieni nyinyi kwa mtakalo ili ndio mpate kuniamini.
115. Mimi si chochote ila ni Mtume niliye toka
kwa Mwenyezi Mungu kuwaonya walio wajibikiwa kwa onyo lilio wazi, kwa
ushahidi wa kutenganisha baina ya kweli na uwongo, bila ya farka yoyote baina ya
mtukufu na mnyonge. Basi vipi itanifalia mimi kuwafukuza Waumini kwa sababu ya
ufakiri wao?
116. Wakasema: Ewe Nuhu! Ikiwa hutoacha huu
wito wako basi jua yakini tutakupopoa mawe. Yaani wanakusudia kwa haya kumtishia
kumuuwa.
117. Nuhu kuonyesha kushikilia watu wake
kuukadhibisha wito wake, alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu
wamenikanusha! Kuthibitisha kuwa wanastahiki maapizo yake.
118. Basi tuhukumie baina yangu na wao, kwa
hukumu ya kuwaangamiza wanao pinga Upweke wako, na wakamkadhibisha Mtume wako!
Na niokoe mimi na Waumini walio pamoja nami na adhabu ya uasi wao.
119. Ndio hivyo tukamwokoa yeye pamoja na walio
amini katika safina iliyo pakia pomoni wao hao pamoja na mahitaji yao, kwa
kuitikia dua yake.
120. Baada ya kuokoka kwa Nuhu na walio amini,
Mwenyezi Mungu aliwazamisha walio baki katika kaumu ya Nuhu walio kuwa
hawakuamini.
121. Hakika katika yaliyo simuliwa na Qur'ani
juu ya khabari za Nuhu ni hoja ya kuthibitisha ukweli wa Mitume na uwezo
wa Mwenyezi Mungu. Na katika watu walio somewa hadithi hizi si wengi walio
amini.
122. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye
Mwenye nguvu za kumuadhibu kila jabari mwenye inda, Mwenye kuwaneemesha
wachamngu kwa kila namna ya fadhila.
123. Kabila ya A'di ilimkanusha Mtume wao Hud
a.s. Na kwa hivyo wakawa ndio wamewakadhibisha Mitume wote, kwa kuwa wito wao ni
mmoja katika asli yake na lengo lake.
124. Alipo waambia ndugu yao Hud: Hamumwogopi
Mwenyezi Mungu, mkamsafia ibada?
125. Hakika mimi nimetumwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu ili nikuongoeni mfuate uwongozi, na ni mwenye kuulinda ujumbe wa Mwenyezi
Mungu. Naufikisha ujumbe huo kama alivyo niamrisha Mola wangu Mlezi.
126. Basi ifuateni amri ya Mwenyezi
Mungu. Na ikhofuni adhabu yake. Na t'iini ninayo kuamrisheni yanayo toka
kwa Mwenyezi Mungu.
127. Wala kwa hii nasaha yangu na uwongozi
wangu sitaki kwenu ujira. Sina malipo isipo kuwa kwa Muumba wa viumbe vyote.
128. Je! Mnasimamisha juu ya kila pahala palipo
nyanyuka katika nchi jengo refu kwa ajili ya kujifakhirisha, na mnakutana humo
kwa mambo ya upuuzi na fisadi? Mwenyezi Mungu Subhanahu anataka kwa haya
kuwazindua watende yatakayo wanufaisha, na anawatahayarisha kwa kuacha kwao
Imani na vitendo vyema.
129. Na mnajenga majumba ya fakhari na imara,
na mahodhi ya maji, kwa kutaraji kuishi milele katika dunia hii, kama kwamba
hamtakufa.
130. Na mnapo ingia kutesa, mnapita kiasi
katika uasi na uvamizi wa jeuri, mnauwa, na mnapiga kwa chuki bila ya
huruma.
131. Mwogopeni Mwenyezi Mungu katika kutumia
nguvu, Na fuateni amri yangu katika ninayo kuitieni. Kwani hayo hakika ndiyo
yatakayo kukufaeni na ndiyo yatakayo dumu zaidi.
132. Na tahadharini na ghadhabu za Mwenyezi
Mungu aliye kukunjulieni neema zake, kwa mnayo yajua yaliyo mbele yenu ya vipawa
vyake vya namna mbali mbali.
133. Kama alivyo kupeni mifugo kama ngamia, na
ng'ombe, na kondoo, na mbuzi, na wana wenye nguvu, wakukulindieni mifugo yenu,
na kukusaidieni katika shida za maisha.
134. Na mabustani yenye matunda, na chemchem
zenye kutiririka maji mnayo yahitajia.
135. Mimi nina khofu asije Mwenyezi Mungu
akakuteremshieni adhabu kali hapa duniani, na Akhera akakutieni katika Moto wa
Jahannamu kwa sababu ya ujabari wenu na starehe alizo kustarehesheni Mwenyezi
Mungu.
136. Wakasema kwa kumkejeli: Ni sawa kwetu,
ukitupa waadhi na kutuonya au ukawa si katika wenye kutoa waadhi.
137. Haya uliyo tuletea si lolote ila ni uwongo
na upotovu wa watu wa zamani. Wao wamezoea kuzua kama hivyo. Kwa hivyo sisi
hatutaacha tuliyo kuwa nayo.
138. Wala sisi hatutaadhibiwa kwa vitendo
tuvitendavyo.
139. Basi wakaendelea kushikilia kumkanusha.
Mwenyezi Mungu akawafanyia haraka kuwateketeza. Hakika katika hayo aliyo
wateremshia Mwenyezi Mungu kina A'di kwa kuwa ni malipo kwa ukanushi wao, ni
hoja inayo juulisha ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na si wengi katika
wanao somewa khabari za A'adi walio Waumini.
140. Na Mola wako Mlezi ndiye Mtenda nguvu wa
kuwashinda hao majabari, Mwenye kuwarehemu Waumini.
141. Kabila ya Thamud ilimkanusha Saleh katika
Ujumbe wake na wito wake, na kwa hivyo ikawa wamewakanusha Mitume wote, kwa kuwa
asli ya Ujumbe ni moja, na lengo ni moja.
142. Ewe Mtume! Watajie watu wako, wakati ule
kina Thamud walipo ambiwa na ndugu yao kwa uzao na uwananchi, si kwa dini,
Saleh: Hamumwogopi Mwenyezi Mungu, mkamuaabudu Yeye tu?
143. Hakika mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu
kwenu kwa mambo yenye kheri yenu na mafanikio yenu. Na mimi ni mwenye kuuhifadhi
Ujumbe huu kama nilivyo upokea kwa Mwenyezi Mungu.
144. Kwa hivyo tahadharini na adhabu ya
Mwenyezi Mungu, na nifuateni kwa haya ninayo kuitieni kwayo kutokana na amri
zake.
145. Wala sitaki kwenu ujira wowote kwa hii
nasaha yangu na uwongozi wangu. Ujira wangu uko kwa Mwenye kumiliki walimwengu
wote.
146. Lilio wazuia ni kule kuamini kwao kwamba
ati wataselelea katika zile starehe, watasalimika na adhabu, na kutoweka, na
mauti,
147. Katika mabustani ya matunda, na chemchem
zenye kutoa maji matamu,
148. Na konde zilizo wiva, na mitende ambayo
mazao yake yamedhihiri mapevu na laini.
149. Na mnachonga milimani majumba kwa ufundi
na ustadi katika hayo mnayo yaunda.
150. Basi iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu,
kwa kuto mshukuru kwenu kwa neema zake; na pokeeni nasiha yangu na muitende.
151. Wala msiit'ii amri ya walio pindukia
mipaka kwa ushirikina na kufuata pumbao na matamanio.
152. Ambao wanapitisha maisha yao katika ardhi
kwa uharibifu, wala hawafanyi ya maslaha ya kutengeneza nchi.
153. Wakasema: Wewe si chochote isipo kuwa
miongoni mwa walio rogwa kikweli mpaka zikapotea akili zao. Na katika jawabu hii
mna ukali na usafihi.
154. Wewe si chochote ila ni mmoja unaye fanana
na sisi kwa ubinaadamu, basi yawaje uwe bora kuliko sisi kwa Unabii na Utume? Na
ukiwa wewe ni mkweli katika madai yako basi lete muujiza wa kuonyesha
uthibitisho wa Utume wako.
155. Saleh akawaambia - alipo pewa na Mwenyezi
Mungu ngamia jike kuwa ni muujiza wake: Huyu hapa ngamia jike wa Mwenyezi Mungu,
amekutoleeni kuwa ni Ishara. Yeye ana sehemu yake ya maji katika siku moja; siku
hiyo msinywe nyinyi. Na nyinyi mna sehemu yenu siku nyengine. Kunyweni siku
hiyo.
156. Wala msimletee madhara yoyote huyu ngamia,
msije mkahiliki kwa adhabu kubwa.
157. Wakamchinja ngamia, kinyume na walivyo
wafikiana na Saleh. Kwa hivyo wakastahiki kuwashukia adhabu, wakawa ni wenye
kujuta kwa kitendo chao hicho.
158. Basi ikawateketeza adhabu aliyo waahidi
Saleh, wala majuto hayakuwakinga na adhabu ya ukosefu wao. Hakika katika
kusimulia kisa chao pana dalili ya kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu
kuwateketeza makafiri na kuwaokoa Waumini. Na si wengi katika watu wako wenye
kuamini.
159. Na hakika bila ya shaka aliye kuumba ndiye
Yeye Muweza wa kuwateketeza wapinzani, na Mfadhili wa kuwaokoa wachamngu.
160. Alipo waita Lut'i watu wake wamuabudu
Mwenyezi Mungu pekee, na waache ushirikina, waliwakanusha Mitume wote.
161. Ewe Mtume! Watajie watu wako pale Lut'i
alipo waambia watu wake, naye ni ndugu yao na shemeji yao:
162. Hakika mimi nimetumwa kwenu na Mwenyezi
Mungu nikuleteeni Dini ya Haki. Nami ni muaminifu wa kuifikisha Dini hii.
163. Basi tahadharini na adhabu ya Mwenyezi
Mungu, na ifuateni amri yangu kwa ninayo kuitieni.
164. Wala mimi sitaki kwenu ujira kwa uwongofu
na uwongozi ninao kuitieni. Sina ujira ila kwa Mwenye kumiliki viumbe vyote na
Mlezi wao.
165. Lut'i alisema: Nyinyi mnastarehea
kuwaingilia wanaume mkaacha wanawake? Kwa hayo anakusudia kuyakanya yale waliyo
yazoea ya vitendo vichafu.
"Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia
wanaume?" Yaani kazi ya liwat'i, ambayo tangu asli yake ni ukosefu muovu, unao
chusha hata kuusikia, kinyume na maumbile, unao mteremsha mwanaadamu chini
kabisa. Na lau kuwa unaenea basi huharibu sunna ya kuoa, nayo ni sunna ya
maumbile, hata uzazi ukatike na ulimwengu usite kuendelea.
Na
kwa liwat'i huenea maradhi kama yanavyo enea kwa uzinzi kama tego, kisonono,
donda ndugu, maradhi ya ngozi kama ukurutu, na hutokea ishara za kudhoofika
nyama za nyuma hata ikawa mtu hawezi kujizuia kutokwa na choo ovyo. Na nyuma
kwake mtu huchanua kukawa kama mdomo wa tarumbeta. Na huko nyuma hujaa vijidudu
vya maradhi na hivyo humuambukiza mwenye kumuingilia na yeye hivyo vijidudu
vikenda mletea maradhi mengine ya njia za mkojo. Na huenda huyo mwenye kufanywa
mambo hayo akawa mpumbavu hafai kitu, ikiwa kaanza tangu utotoni. Na huenda
akajidai kuonesha ujanadume mwingi kuliko kiasi kwa kutaka kuficha upungufu wake
wa uume. (Karibuni imedhihiri kuwa maradhi ya khatari kabisa ya AIDS [Ukimwi]
yameenea zaidi sana kwa watendao kitendo hichi na watumiao madawa ya ulevi,
ijapo kuwa na wazinzi nao hupata!).
Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa
Taa'la ameukemea ukosefu huu katika Aya kadhaa wa kadhaa, na akabainisha hikima
ya Mwenye kuhukumu kwa kuharimisha huku, kwa kusema: " Je! Katika viumbe vyote
mnawaingilia wanaume? Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika
wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!"
166. Na mnaacha aliyo kuumbieni Mwenyezi Mungu
ya kustarehe na wake zenu walio halali yenu? Ama hakika nyinyi ni watu mlio
pindukia mipaka ya udhalimu katika kufanya maasi.
167. Walikasirika kwa kule kuwakataza na
kuwakemea kwa sababu ya jambo ovu na wakasema: Kama hukuacha kutukebehi
tutakutoa mji kwa izara kubwa.
168. Lut'i akasema: Hakika mimi nakichukia mno
hichi kitendo chenu, wala sitoacha kabisa kukipinga na kukikebehi.
169. Na akamwomba Mola wake Mlezi amwokoe yeye
na ahali zake na wayatendayo wale wajinga, baada ya kwisha kata tamaa kuwa
hawamsikilizi.
170. Mwenyezi Mungu akamuitikia ombi lake,
akamwokoa yeye na wale walio fuata wito wake, kwa kuwatoa wote majumbani mwao
wakati wa kuteremka adhabu kuwashukia wenye kukanusha.
171. Ila mkewe kizee aliye baki, na hakutoka
nao. Yeye akaangamia kwa kufuru zake na ukhaini wake, kwa kuwaunga mkono
wakosefu.
172. Kisha Mwenyezi Mungu akawahiliki makafiri
watendao uovu kwa hilaki kali na mbaya.
173. Na Mwenyezi Mungu aliwateremshia wale watu
wapotovu mawe kutoka mbinguni, yakawateketeza. Na ilikuwa mvua ya kutisha kwa
wingi wake na namna yake. Basi mvua ovu ya walio kwisha onywa ni mvua hiyo,
kwani iliteremka kwa uangamizi mkubwa mno!
174. Hakika adhabu ile iliyo wateremkia watu
wale hapana shaka ni hoja yenye kuonyesha utimilivu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Wala si wengi katika watu wako wenye kusadiki hayo.
175. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka
ndiye Yeye Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kusifika kwa rehema iliyo kamilika.
Huwapa adhabu watendao dhambi, na huwalipa wema Waumini.
176. Hichi kisa cha Shuaibu pamoja na Watu wa
Al Aykat, Machakani, nao ni msitu wenye miti mizuri, karibu na Madian. Kikundi
cha watu waliteremkia hapo na wakakaa. Mwenyezi Mungu akawapelekea Shuaibu kama
alivyo wapelekea watu wa Madian. Wakamkadhibisha katika wito wake. Na kwa hivi
wakawa wamekanusha risala za Mitume wote.
177. Ewe Muhammad! Watajie watu wako pale
Shuaibu alipo waambia watu wa Machakani: Je! Hamumkhofu Mwenyezi Mungu
mkamuamini? Wakaingia kumkadhibisha.
178. Hakika mimi nimetumwa na Mola Mlezi wa
walimwengu wote nikuongoeni na nikuongozeni. Nami ni muaminifu wa kuufikisha
ujumbe wake kwenu.
179. Basi tahadharini na adhabu ya Mwenyezi
Mungu. Na nit'iini kwa kufuata amri za Mwenyezi Mungu, na kuziokoa nafsi zenu na
madhambi.
180. Na mimi kwa hivi kukuongozeni na
kukufunzeni sikutakini ujira wowote. Mimi sina malipo kaamili kwa sababu ya kazi
yangu ila kutokana na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
181. Shuaibu akawaamrisha kutimiza vipimo kwa
ukamilifu wanapo pima, kwani ilikuwa ada yao kupunguza kwa pishi na mizani,
kupunguza haki za watu kwa kuwapunja na kuwapimia kasoro.
182. Na wapimieni watu kwa mizani ya sawa sawa,
ili wachukue haki yao kwa uadilifu ulio nyooka.
183. Wala msiwapunguzie watu haki zao, wala
msipite katika nchi mkifisidi kwa kuuwa, na uharamia, na kufanya madhambi, na
kufuata pumbao.
184. Na tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu
aliye kuumbeni, na akaumba kaumu zenye nguvu na takaburi zilizo tangulia.
185. Wakasema: Wewe si chochote ila ni mtu
aliye sibiwa na uchawi mkali na ikapotea akili yake.
186. Na wewe si chochote ila ni mmoja wetu sawa
na sisi kwa utu. Basi vipi ujipe ubora kuliko sisi kwa Utume? Nasi tunaamini
kuwa wewe ni mwongo wa kubobea.
187. Basi hebu tuangushie vipande vya adhabu
kutoka mbinguni ikiwa ni katika wasemao kweli kwa huu ujumbe wako! Na
chini ya shauri hii kwa hakika pana kila namna ya ubishi.
188. Shuaibu akasema: Mola wangu Mlezi ni
Mjuzi, upeo wa kujua, wa maasi yote myatendayo, na adhabu mnayo stahiki. Yeye
atakuteremshieni hayo kwa wakati wake alio ukadiria. Na huu ndio hadi ya mwisho
wa kumwachilia Mwenyezi Mungu kila kitu, na kuwatisha hao makafiri.
189. Lakini wao waliendelea kumkadhibisha.
Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa adhabu ya joto kuu mno. Wakawa wanatapa tapa
hawana pa kukimbilia. Walipo pata kiwingu cha kuwapa kivuli kukinga mwako wa jua
walijikusanya chini yake. Mwenyezi Mungu akawateremshia moto, ukawateketeza wote
katika siku ya kitisho kikubwa mno.
190. Hakika adhabu iliyo wateremkia watu wa
Machakani kuwa ni malipo ya uasi wao, ni dalili ya ukamilifu wa uwezo wa
Mwenyezi Mungu. Na hawakuwa wengi wa watu wako wenye kusadiki.
191. Na hakika Mola wako Mlezi hapana shaka
ndiye Yeye aliye tengeka kwa Nguvu na Ushindi, Mwenye kuwaneemesha Waumini kwa
rehema nyingi.
192. Na hakika hii Qur'ani iliyo tajwa ndani
yake visa vya kweli imeteremshwa kutoka kwa Mwenye kuumba walimwengu wote,
Mwenye kumiliki mambo yao, na Mlezi wao. Basi khabari zake ni za kweli. Na
hukumu yake inatimizwa mpaka Siku ya Kiyama.
193. Ameiteremsha Roho muaminifu, naye ni
Jibril a.s.,
194. Juu ya moyo wako ulio tulia kuihifadhi na
kuifahamu, na idhibitike katika moyo wako iwe madhubuti isisahaulike, ili upate
kuwaonya wakhalifu kwa adhabu ziliomo ndani yake.
195. Jibril amekuteremshia kwa lugha ya
Kiarabu, yenye maana wazi, yenye hoja zilizo dhaahiri kwa wanayo hitajia ya
kutengeneza mambo yao ya dunia na Dini.
196. Na hakika kuitaja Qur'ani na kueleza kuwa
inatoka kwa Mwenyezi Mungu kumteremshia Muhammad s.a.w. yametajwa katika
Vitabu vya Manabii walio tangulia.
197. Je! Hawa wenye inda wanaikataa Qur'ani na
hali wao wanayo hoja inayo onyesha ukweli wa Muhammad s.a.w., nayo ni
ilimu ya wanazuoni wa Wana wa Issraili juu ya Qur'ani kama ilivyo katika vitabu
vyao?
198. Na lau tungeli mteremshia mtu asiye kuwa
Mwaarabu, anaye weza kusema Kiarabu lakini si kwa ufasihi, wasingeli waza
kumtuhumu kuwa kaizua.
199. Na angeli wasomea baraabara kinyume na ada
bado wangeli mkanusha, na wakapatia kisababu kwa ukafiri wao.
200. Sisi tumekutia huko kukanusha katika nyoyo
za wakosefu; na tumekuthibitisha kama tulivyo kuthibitisha katika nyoyo za
wenye sifa kama zao.
201. Basi hapana njia ya wao kuacha tabia yao
ya ukafiri mpaka wateseke kwa hiyo adhabu kali walio ahidiwa.
202. Itawateremkia adhabu kwa ghafla bila ya
kuitaraji, wala wao hawajui kama inakuja.
203. Watasema itapo teremka hiyo adhabu: Je,
tutapewa muhula? Haya ni kwa majuto kwa kupitiwa na Imani na kutaka
waakhirishiwe adhabu. Lakini hawajibiwi.
204. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Watu wa
Makka wameghurika na kuchelewesha kwangu kuwaadhibu, basi ndio wanaihimiza?
Anakusudia Subhanahu Aliye takasika kuzisafihi akili zao kwa sababu ya
kuhimiza kwao adhabu juu ya kuwaonya na kuwatisha.
205. Je, umefikiri ukajua, kama Sisi
tuliwastarehesha kwa uhai kwa muda wa miaka mingi pamoja na maisha mema?
206. Kisha ikawateremkia adhabu iliyo ahidiwa.
207. Kustarehe kwao kwa umri mrefu na maisha
mema hakutowakinga hata chembe na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwani adhabu ya
Mwenyezi Mungu itakuja tu, kama si leo kesho. Wala hapana kheri katika neema
ambayo khatima yake ni adhabu.
208. Na mwendo wetu kwa kaumu zote ni kuwa
hatuuteketezi umma ila baada ya kuwatumia Mitume wa kuwaonya kwa kufuata hoja,
209. Wakumbuke na wazingatie. Wala si shani
yetu kudhulumu hata tuuadhibu umma kabla ya kuwaletea Mtume.
210. Qur'ani inakataa waliyo yasema makafiri wa
Makka ya kwamba Muhammad anafuata majini, nao ndio wanampa Qur'ani.
Qur'ani inasema: Mashetani hawakuiteremsha hii Qur'ani.
211. Wala haiwafalii wao kuiteremsha, na
hawawezi kufanya hivyo.
212. Kwani hao hakika wanazuiwa wasiisikie
Qur'ani pale inapo funuliwa kwa Muhammad s.a.w.
213. Basi wewe muelekee Mwenyezi Mungu
ukiendelea na usafi wako wa ibada, wala usishughulike na fisadi za madai ya
washirikina na mwendo wao muovu. Na hivi kutakiwa Mtume s.a.w. awe na ikhlasi ya
namna hii ni wito kwa jamii ya watu waliomo katika umma wake.
214. Watie khofu ya adhabu ya shirki na maasi
walio karibu nawe katika jamaa zako.
215. Na kuwa mpole kwa wanao itikia wito wako
wa Imani.
216. Pindi wakikuasi na wasikufuate basi
jitenge nao, na jitenge na vitendo vyao vya ushirikina na maasi yote.
217. Na tegemeza mambo yako kwa Mwenye nguvu,
Mwenye uweza wa kuwatenda nguvu adui zako kwa utukufu wake, na kukunusuru wewe
na kumnusuru kila mwenye kufanya a'mali yake kwa usafi wa niya.
218. Ambaye anakuona pale unapo simama kwa
ibada za usiku na vitendo vyote vya kheri.
219. Na anaona mwendo wako kati ya wanao sali,
kwa kusimama, na kukaa, na kurukuu na kusujudu, pale unapo waongoza katika Sala.
220. Hakika Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kusikia
dua zako na dhikri zako, ndiye Mjuzi wa kujua niya yako na vitendo vyako. Ni
kama kwamba Subhanahu anamwambia: Usichukue taklifu kubwa bila ya kiasi katika
mashaka ya ibada, kwani uyatendayo yote nayaona na nayasikia Mimi.
221. Washirikina walisema: Mashetani ndio
wanamsomea Qur'ani Muhammad. Qur'ani ikawajibu: Nikupeni khabari watu gani
Mashetani ndio wanawateremkia, na wakawashawishi?
222. Wanamteremkia kila mwenye kubeba dhambi za
namna mbaya kabisa za uwongo, na madhambi ya kuchusha kabisa. Nao ni hao
makohani mafisadi ambao tabia zao na tabia za Mashetani ni jinsi moja na
zimewafikiana.
223. Hao hutega masikio yao kwa Mashetani, na
kwao wakapata mambo ya dhana dhana tu. Na wengi wao ni waongo, na huzidisha tena
juu ya kauli walizo zipata kwa Mashetani.
224. Makafiri wanasema: Hii Qur'ani ni
mashairi, na Muhammad ni mtungaji mashairi. Mwenyezi Mungu ameyavunja haya kwa
kuthibitisha kuwa hakika Qur'ani imejaa hikima na hukumu. Mpango wake unapingana
na mpango wa mashairi ambao unategemea juu ya kweli na uwongo. Na amebainisha
kwamba hali ya Muhammad s.a.w. inapingana na hali ya watungaji mashairi. Yeye
anasema kwa hikima, wao wanasema kwa udanganyifu. Na hii ndiyo hali ya wengi
katika watungaji mashairi.
225. Kwani huwaoni vile wanavyo tangatanga
katika mabonde ya maneno wala hawaongoki kwenye Haki?
226. Na kwamba wao husema kwa ndimi zao wasio
yaambatisha na vitendo vyao?
227. Lakini walio hidika kwa hidaya ya Mwenyezi
Mungu, na wakatenda mema mpaka zikatua katika nafsi zao sifa bora, na
wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi mpaka ikathibiti khofu katika nyoyo zao,
hawa basi huyafanya mashairi kama dawa ilio sibu kwa ugonjwa wake. Na hupambana
kwa ajili ya kuiwania Dini yao na kusimamisha Haki, inapo kuwa Haki inafanyiwa
jeuri. Na walio dhulumu nafsi zao kwa shirki na kumkejeli Mtume kwa mashairi,
watatafuta wapi pa kuikimbia shari na hilaki wanayo iendea.