1. Sura hii tumeifunua na tumewajibisha
hukumu zake, na tumeteremsha ndani yake dalili zilizo wazi za kuthibitisha uwezo
wa Mwenyezi Mungu na upweke wake, na kwamba Kitabu hichi kinatoka kwake, ili
mpate kuwaidhika.
2. Na miongoni mwa hukumu hizo ni hukumu ya
mwanamke na mwanamume wenye kuzini. Basi kila mmoja wao mpigeni fimbo mia. Wala
huruma kwao isikuzuieni kutimiza hukumu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu
na Siku ya Mwisho. Kwani yanayo takikana na Imani ni kukhiari kumridhi Mwenyezi
Mungu kuliko kuwaridhi watu. Na wahudhurie baadhi ya jamaa Waumini waone hiyo
adhabu inavyo tekelezwa, ili adhabu hiyo iwatishe wenginewe wasitende hivyo.
3. Mwanamume muovu aliye zoea uzinifu hapendi
kumwoa ila mchafu anaye zini au mshirikina. (1). Na mwanamke mchafu
ambaye kazi yake ni uzinifu hapendelei kuolewa ila na mchafu anaye zini;au
mshirikina. Na ndoa namna hii haiwaelekei Waumini, kwa kuwa imeshabihi fiski na
kupelekea kutuhumiwa.
(1) Haya ikiwa haikupita toba. Na tafsiri ya haya
ni kuwa inabainishwa tabia za washirikina au wazinifu kuwa wao hawapendi ila
mambo ya ufisadi tu. Na kwa mujibu wa maoni ya Hambali na Ahli-Dhaahir (na pia
Ibadhi) haisihi ndoa ya mwanamume mzinifu au mwanamke mzinifu kabla ya toba.
4. Na wanao watuhumu wanawake wenye hishima zao
wasio na makosa kwa tuhuma ya uzinzi bila ya kuleta mashahidi wane wa
kuthibitisha tuhuma yao, waadhibuni kwa kuwapiga fimbo thamanini, na wala
ushahidi wao usikubaliwe tena kwa jambo lolote muda wa uhai wao. Basi hawa ndio
wanao faa kuitwa kwa jina la walio toka vibaya kwenye mipaka ya Dini.
Maoni ya Wataalamu juu ya Aya 2-4
" Mzinifu mwanamke na
mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala
isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi
mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la
Waumini. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke
mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina.
Na hayo yameharimishwa kwa Waumini. Na wanao wasingizia wanawake
mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na
msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu." Makosa katika Sharia ya
Kiislamu ni mambo yaliyo harimishwa na Mwenyezi Mungu akayakemea kwa kuyawekea
adhabu au izara ya kufedhehesha. Na maharimishwa hayo ama ni kutenda kilicho
katazwa kukitenda, au kuacha kutenda kilicho amrishwa na Sharia kutendwa. Na
sababu ya kuharimishwa haya yaliyo katazwa ni kuwa hayo ni kupiga vita moja
katika maslaha yanayo kubaliwa katika Uislamu. Na maslaha hayo yanayo kubaliwa
ni matano, nayo ni:
1. Kuhifadhi nafsi. 2. Kuhifadhi
Dini.
3. Kuhifadhi akili.
4. Kuhifadhi mali 5. Kuhifadhi
hishima.
Kuuwa kwa mfano ni kuipiga vita nafsi. Na kurtadi, kutoka
katika Uislamu, ni kuipiga vita Dini. Na kutumia vinavyo levya ni kuipiga vita
akili. Na wizi ni kuyapiga vita mali. Na uzinzi ni kuipiga vita
hishima.
Na wanazuoni wa ilimu ya Fiqhi (Sharia) wameyagawa makosa
sehemu mbali mbali. Lakini sisi yatutosha kwa sababu ya kueleza Aya hizi kugawa
kwa mujibu wa uzito wa adhabu zake, na namna ya kiasi chake. Nayo yamegawika
mafungu matatu:
1. H'udud, yaani Adhabu. 2. Kisasi au Diya 3.
Izara, au Fedheha.
Ama H'udud, au Adhabu, ni makosa ambayo
yanaonekana kuwa yanaingilia kuvunja Haki ya Mwenyezi Mungu, au kuwa Haki ya
Mwenyezi Mungu ni kubwa zaidi ndani yake kuliko haki ya binaadamu. Na kwa hivyo
ndio Mwenyezi Mungu akaiwekea MIPAKA ndio maana khasa ya H'udud. Kaiwekea mipaka
adhabu yake katika Qur'ani au katika Sunna za Mtume s.a.w. Ama makosa ya Kisasi
na Diya ni makosa ambayo baadhi kubwa yake yamewakhusu wenyewe waja. Mwenyezi
Mungu amewekea adhabu za baadhi yake katika Qur'ani au katika Sunna za Mtume
s.a.w., na amewaachilia mengine wapime wenyewe wenye madaraka. Mfano wa hayo
makosa ya kumwaga damu, kama kuuwa na kukata viungo, na kujuruhu.
Ama
makosa ya Izara, Uislamu umejitosheleza kwa kutaja mwisho wa ukali na mwisho wa
upole katika adhabu zao, na kuachia yaliyo baki wenye kutawala wahukumie kwa
kila kosa kwa mujibu wa hali na zama yanapo tokea makosa.
Makosa ya
H'udud ni saba:
1. Uzinzi. 2. Kuzulia wanawake mahashumu wasio
na makosa.
3. Udhalimu. 4. Wizi. 5. Uharamia.
6.Ulevi.
7. Kurtadi. (Kutoka katika Uislamu).
Mwenyezi
Mungu ameyawekea mipaka yote makosa hayo na ameyaleta kwa hisabu yake katika
Qur'ani, kama alivyo wekea adhabu zake katika Qur'ani vile vile, isipo kuwa
adhabu ya mwenye kuzini naye amewahi kuoa, yaani Zaani Muh's'an, ambaye hupigwa
mawe, na mlevi na adhabu yake ni fimbo thamanini, na adhabu ya mwenye kurtadi
ambaye jaza yake ni kuuwawa. Hayo yamekuja katika Sunna.
Na zimezoea
hizi kanuni za kuundwa na watu katika kupinga makosa ya uzinzi kwa adhabu
khafifu kama vile kifungo, hata ndio uchafu ukaenea kati ya watu, na fiski na
ukahaba ukazagaa, na hishima zikapotea, na maradhi yakakithiri, na nasaba za
ukoo zikachanganyika. Katika jambo la ajabu ni kuwa hizi kanuni za kisasa za
nchi zinazo ambiwa za kistaarabu ndio zinazo yalinda makosa haya. Katika kanuni
za adhabu za Kifaransa, kwa mfano, wazinzi wasio oa wala kuolewa hawapati adhabu
yoyote maadamu wao wakiwa wamekwisha fikilia utu uzima. Kwa kuwa ati uhuru wao
wa binafsi unataka waachiliwe wajifanyie wenyewe watakalo. Ama mzinzi mwanamume
aliye na mke, au mwanamke mwenye mume, basi huyo adhabu yake ni kifungo. Lakini
mwana sharia wa serikali haingii kuchunguza ila akipata mashtaka kutokana na
mume au mke. Na inaonyesha kuwa ni haki ya mume tu kuwa hilo kosa limetokea au
la, kwani ikiwa yeye ndiye aliye fikisha mashtaka, basi yeye anaweza kuyafuta
pia, na uchunguzi utasita. Na yeye anaweza kumsamehe mkewe akatoka gerezani
kabla ya kutimiza muda wa kifungo chake ijapo kuwa hukumu ilikuwa ni juu yake
huyo mwanamke mwishoni.
Na wapo baadhi ambao ati wanaushutumu Uislamu
kwa ukali wake kushadidia kwake kuadhibiwa wazinifu. Yaliyo elekea zaidi ni kuwa
lau wangeli zingatia kuwa kama ilivyo kuwa adhabu ni kali, hali kadhaalika
umeshadidiwa ushahidi kwa jambo hili. Kwani ijapo kuwa katika kosa la mauwaji
yatosha ushahidi wa mashahidi wawili waadilifu, katika uzinzi ni lazima
wapatikane mashahidi wane waadilifu walio ona kitendo hicho kwa macho yao, au
aungame mkosa!
Hayo, na tunaona kuwa Qur'ani Tukufu imelazimisha kuwa
kupigwa hizo fimo kuwe jahara ili mkosa ajuulikane, na iwe ni onyo kuwakhofisha
wenginewe.
5. Lakini mwenye kutubu katika wao akajuta kwa
maasi yake, na akaazimia kuwa mt'iifu na kuonyesha ukweli wa toba yake kwa
kwenda kwake mwendo mwema, basi Mwenyezi Mungu atamsamehe kumuadhibu.
6. Na hao wanao watuhumu wake zao kuwa wamezini
na hawana mashahidi wanao takikana kushuhudia ukweli wa tuhuma yao, basi
anatakikana mmoja wa hao kama anataka isimpate adhabu, ashuhudie kwa Mwenyezi
Mungu mara nne kuwa yeye ni mkweli katika hiyo tuhuma yake.
7. Na mara ya tano aseme kuwa yeye anastahiki
kutengwa na rehema ya Mwenyezi Mungu akiwa ni mwenye kusema uwongo kwa hayo.
8. Baada ya haya mwanamke akinyamaza kimya
itampasa kupata adhabu ya uzinzi. Ili kujikinga na adhabu yampasa ashuhudie kwa
Mwenyezi Mungu mara nne kwamba mumewe ni mwongo kumtuhumu yeye kwa uzinzi.
9. Na ataje katika mara ya tano kuwa yeye
mwanamke anastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu imshukie ikiwa mumewe ni mwenye
kusema kweli katika tuhuma yake.
10. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufanyieni
fadhila na akakurehemuni, na kuwa Yeye ni Mwingi wa kukubali toba za waja wake,
na Mwenye hikima katika vitendo vyake vyote, asingeli kufanyieni sharia za
hukumu hizi, na angeli fanya haraka kukuadhibuni duniani kwa maasia.
11. Hakika hao walio zua uwongo ulio potoka na
kila uwongofu kumzulia Aisha, mke wa Nabii s.a.w. walipo mtangazia uzushi, ni
kikundi wanao ishi pamoja nanyi. Msidhani kituko hichi ni shari kwenu, bali
ndiyo kheri yenu; kwa sababu kimewapambanua baina ya wanaafiki na Waumini wa
kweli. Na ukadhihiri ukarimu wa walio wema na wenye kuingiwa na uchungu. Na kila
mtu katika hawa walio tuhumu watapata malipo yao kwa mujibu wa kadri alivyo
shiriki katika uzushi huu. Na mkuu wa kikundi hichi ndiye ataye pata adhabu
kubwa kwa ukubwa wa makosa yake.
12. Ilikuwa inavyo takikana kwa Imani ni kuwa
wakati wa kusikia huu uzushi, ni Waumini wanaume na wanawake wajidhanie nafsi
zao kheri ya usafi na unadhifu, na waseme kwa kupinga: Huu ni uwongo ulio wazi
umezuliwa, kwa kuwa haya yamemkhusu bora ya Mitume na bora ya wanawake walio wa
kweli.
13. Je! Hao wazushi walileta mashahidi wane wa
kushuhudia hayo waliyo yasema? Hawakufanya hayo...Na ikiwa hawakufanya basi hao
kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu ni waongo.
14. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufanyieni
fadhila kwa kubainisha hukumu, na hakukurehemuni duniani kwa kuacha kuleta
adhabu kwa haraka, na Akhera kwa kukusameheni, angeli kuteremshieni adhabu kubwa
kwa sababu ya kujiingiza kwenu katika uzushi huu.
15. Mmezichukua khabari hizo kwa ndimi zenu na
mkazieneza kati yenu. Wala nyinyi hamkujua kuwa hizo ni khabari za kweli, na
mkaona jambo hili ni dogo si la kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu, au sana adhabu
yake ni ndogo; na ilhali ni jambo kubwa kweli la kuadhibiwa adhabu kali na
Mwenyezi Mungu.
16. Yanayo faa ni kuwa baada ya kusikia maneno
haya ya uwongo ni kuambizana msiyazungumze, kwa sababu si laiki yenu, na
mustaajabie kuzuliwa uwongo muovu wa namna hii wa khatari.
17. Na hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni
msirudie tena kufanya maasi namna hii kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini wa kweli.
Kwani sifa za Imani zinapingana na mwendo huu.
18. Na Mwenyezi Mungu anakuteremshieni Aya zenye
kuonyesha hukumu kwa uwazi dhaahiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa Ujuzi,
hapana asicho kijua katika vitendo vyenu. Naye ni Mwenye hikima kwa kila anacho
kitungia sharia na kukiumba. Kwani kila sharia zake na uumbaji wake ni kwa
mujibu wa hikima.
19. Hakika hao wanao penda kutangaza machafu,
wakayatangaza baina ya Waumini watapata adhabu yenye kutia uchungu duniani
kwa mateso yaliyo kwisha pasishwa, na Akhera watatiwa Motoni ikiwa hawato tubu.
Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zenu zote, za dhaahiri na zilizo
fichikana. Na nyinyi hamjui anayo yajua Yeye.
20. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu
yenu na rehema yake kwenu, na kuwa Yeye ni Mwingi wa upole, Mkunjufu wa rehema,
asingeli kubainishieni hukumu, na angeli kuleteeni mateso kwa haraka hapa
duniani kwa maasi yenu.
21. Enyi mlio amini! Hifadhini nafsi zenu kwa
Imani. Wala msimfuate Shetani anaye kuvutieni kwenda tangaza uchafu na maasi
baina yenu. Na mwenye kumfuata Shetani basi huyo amekwisha a'si, kwani Shetani
anaamrisha madhambi makubwa makubwa na maasi mabaya. Na lau kuwa si fadhila ya
Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake kwenu kwa kubainisha hukumu na kukubali
toba ya wenye kuasi asinget'ahirika hata mmoja wenu na uchafu wa maasi. Lakini
Mwenyezi Mungu anamsafisha mwenye kumuelekea Yeye kwa kumwezesha kuwa mbali na
maasi, au kwa kumsamehe kwa kutubu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia kila
kauli, Mwenye kujua kila kitu, na atakulipeni kwayo.
22. Wala wasiape wema wenu wenye nafasi kuwa
watazuia kuwafanyia hisani jamaa zao na masikini na walio hama makwao katika
Njia ya Mwenyezi Mungu na wengineo kwa sababu za kibinafsi, kama vile kuwa
wamewatendea uovu fulani. Lakini inatakikana wawasamehe na wayaachilie mbali
makosa yao. Na ikiwa mnapenda Mwenyezi Mungu akusameheni maovu yenu basi
wafanyieni wanao kufanyieni mabaya mfano wa anavyo kufanyieni nyinyi Mola wenu
Mlezi. Na fuateni mwendo wake kwani Yeye ni Mkunjufu wa kusamehe na kurehemu.
Aya hii imeteremka pale Abu Bakar r.a. alipo apa kumkatia msaada
jamaa yake Mist'ah bin Uthaathah hapo alipo ingia Mist'ah katika uzushi alio
zuliwa bibi Aisha r.a.
23. Hakika hao wanao wasingizia wanawake wema
walio safi, ambao hawadhaniwi hayo, bali wao kwa kumshughulikia Mwenyezi Mungu
hata wameghafilika na hayo wanayo singiziwa, Mwenyezi Mungu atawatenga mbali na
rehema yake katika dunia na Akhera, na watapata adhabu kubwa ikiwa hawatotubu.
24. Adhabu hiyo itakuwa Siku ya Kiyama ambapo
itakuwa hapana njia ya kuikataa. Bali waliyo yatenda yatathibiti juu yao, kwa
kuwa zitawashuhudia ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao, kwa madhambi yote
waliyo yatenda. Na hayo ni kwa kudhihiri athari ya vitendo vyao juu ya viungo
hivyo, au kwa kutamkishwa na Mwenyezi Mungu ambaye anatamkisha kila kitu.
25. Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu
iliyo kwisha hukumiwa wapewe kwa ukamilifu wake bila ya upungufu. Na hapo
wataujua kwa ujuzi wa yakini Ungu wa Mwenyezi Mungu na hukumu za Sharia yake, na
ukweli wa ahadi yake na kitisho chake. Kwani yote hayo yatakuwa wazi hayana
kificho.
26. Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na
wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na kadhaalika wanawake wema ni wa wanaume
wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Basi yamkini vipi kuwepo uwovu katika
wema ulio hifadhiwa nao ni mke wa mwema muaminifu Mtume Mtukufu s.a.w.? Na wema
hawa wamehifadhika na tuhuma wanazo wasingizia hao waovu. Na wao wana maghfira
ya Mwenyezi Mungu kwa vijidhambi vidogo vidogo ambavyo mwanaadamu hakosekani
kuwa navyo. Na watapata ukarimu mkubwa wa kupata neema za Peponi.
27. Enyi mlio amini! Msiingie katika
nyumba zisio kuwa zenu ila baada ya kutaka idhini kwa wakaazi wake na
mkaruhusiwa kuingia, na baada ya kuwatolea salamu wakaazi wake - na salamu
ni bora kwenu kuliko kuingia tu bila ya kutoa salamu. Na Mwenyezi Mungu
amekuwekeeni sharia hii ili mpate kunasihika na muifuate.
28. Na ikiwa katika hizo nyumba hamkumkuta mtu
wa kukupeni idhini basi msiingie mpaka aje wa kukuruhusuni. Na ikiwa
hakukuruhusuni na akakutakeni mrudi nyuma, basi rudini; wala msishikilie kutaka
ruhusa ya kuingia. Kwani kurejea nyuma ni hishima zaidi na usafi zaidi kwa nafsi
zenu. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zenu zote na atakulipeni, basi
msende kinyume na uwongozi wake.
29. Na mkitaka kuingia nyumba za umma zisio
kaliwa na watu makhsusi na ndani yake zipo haja zenu, kama vile maduka,
mahoteli, nyumba za ibada, hapana ubaya kuingia bila ya kutaka ruhusa. Na
Mwenyezi Mungu anajua kwa ujuzi wa timamu kabisa vitendo vyenu vyote vya
dhaahiri na vilivyo fichikana. Basi tahadharini na kwenda kinyume naye.
30. Ewe Nabii! Waambie Waumini katika yanayo
pelekea zina na kutilisha shaka, wasitazame yanayo harimishwa kutazama, nayo ni
tupu za wanawake na sehemu za uzuri wao, na wanaume wahifadhi tupu zao kwa
kuzisitiri na kuto zitumilia kwa njia isiyo ruhusiwa na Sharia. Adabu hiyo ndio
ina hishima zaidi na safi zaidi kwao wasiingie katika maasi na tuhuma. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua baraabara yote wayatendayo, na atakuja walipa
kwayo.
31. Vile vile ewe Nabii, waambie wanawake
Waumini, wanaamrishwa waache kutazama yaliyo harimishwa, na wazihifadhi tupu zao
kwa kuzisitiri na kutoingiliwa ila kwa njia ya Kisharia. Na wasiwaonyeshe
wanaume ya kuwavutia katika uzuri wa umbo lao na mapambo, kama kifua, mabega,
vidani, isipo kuwa yale tangu hapo yamedhihiri, kama uso na mikono. Na ewe
Nabii! Watake hao wanawake wajisitiri mwahali zilipo funuka nguo, kama shingo na
kifua. Na hayo kwa kuteremshia vitambaa vya kichwani. Na wasiachilie kuonekana
uzuri wao ila kwa waume zao, na jamaa ambao ni haramu kuoana nao milele, kama
baba zao, au baba za waume wao, au watoto wao, au watoto wa waume zao kwa wake
wengine, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao. Na mfano wa
hawa ni wanawake wenzao, sawa sawa wakiwa waungwana au wajakazi, na wanaume
wanao ishi nao na hawana tena haja ya wanawake kwa ukongwe. Na kadhaalika watoto
wadogo ambao hawajafikilia miaka ya kutamani. Na pia watake wanawake wasifanye
vituko vya kutaka kuwavutia wanaume kama kugonga miguu chini ili isikilizane
milio ya mitali na kugesi iliyo fichikana ndani ya nguo. Na tubuni nyote kwa
Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, kwa mlivyo iacha amri ya Mwenyezi Mungu. Na
shikamaneni na adabu za Dini mpate kuongokewa katika dunia na Akhera yenu.
32. Na saidieni katika kujitenga na zina
na yanayo pelekea zina, kwa kuwaoza ambao bado hawajaoana miongoni mwa wanaume
wenu na wanawake wenu, na walio kuwa wanafaa kwa hayo katika watumwa wenu. Na
wala umasikini usiwe sababu ya kuzuilia kuoa. Kwani Mwenyezi Mungu atasahilisha
njia za maisha mazuri kwa mwenye kutaka kuishi maisha safi. Na fadhila za
Mwenyezi Mungu ni kunjufu, na Yeye anajua kabisa niya za watu, na kila lipitalo
katika ulimwengu.
33. Na ambao hawakupata uwezo wa fedha za kuolea
basi wafuate mojapo wa njia nyengine kama saumu na riyadha (1) na kazi za
kutumia akili . Kwa hayo hujikurupusha mpaka Mwenyezi Mungu akawafungulia kwa
fadhila zake zitakazo wawezesha kuoa. Na watumwa ambao wanataka kuandikiana
nanyi ili wapate uhuru wao ni waajibu juu yenu kuwakubalia walitakalo, mkijua
kuwa watatimiza kutekeleza na wanaweza. Na juu yenu kuwasaidia waweze kutimiza
walio andikiana nanyi, na hayo ama ni kwa kuwapunguzia shuruti mlizo andikiana
nao, au kwa kuwapa mali katika mali aliyo kuneemesheni Mwenyezi Mungu, mkawapa
katika Zaka au Sadaka. Na ni haramu juu yenu kuwafanya vijakazi vyenu njia ya
pato la duniani rakhisi kwa kuwafanya makahaba, na mkawalazimisha kwa hayo. Na
vipi mnakwenda kumlazimisha uchafu anaye taka kuwa safi? Na mwenye
kuwalazimisha, basi Mwenyezi Mungu humsamehe mwenye kulazimisha pindi akitubu
kwa dhambi zake za kulazimisha. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa
maghfira na rehema.
(1)Haya yanaelezwa na kauli ya Mtume s.a.w.: "Enyi
vijana! mwenye kuweza kuwoa na aoe kwani hivyo linalindwa jicho, unahifadhiwa
utupu. Asiye weza na afunge, kwani hivyo ni kinga yake."
34. Na Sisi tumekuteremshieni katika Sura hii na
nyenginezo Aya zilizo wazi zenye kubainisha hukumu. Na tumekuteremshieni mifano
ya hali mbali mbali za walio tangulia, na uwongozi, na mawaidha ambayo kwayo
watapata faida wenye kumkhofu Mwenyezi Mungu.
35. Mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha Nuru ya
katika mbingu na ardhi. Yeye ndiye Mwenye kunawirisha vyote hivyo kwa nuru yote
tunayo iona na tukenda ndani yake, na ya maana, kama Nuru ya Haki na uadilifu,
na ilimu, na fadhila, na uwongofu, na Imani, na kwa ushahidi na athari kama
alivyo waahidi viumbe vyake, na kwa vyote vinavyo onyesha kuwepo kwa Mwenyezi
Mungu, na vikalingania Imani kumuamini Yeye Subhanahu. Na mfano wa Nuru yake
Tukufu na dalili zake zilizo zagaa kwa uwazi ni kama mfano wa Nuru ya taa yenye
kung'aa kwa ukali kabisa, iliyo wekwa kwenye shubaka la ukutani ili kuukusanya
mwangaza wake na kuzidi kuupa nguvu. Na taa hiyo imevikwa tungi la kigae safi
linameremeta kama inavyo meremeta nyota. Na taa ile inawaka kwa mafuta ya mti
wenye baraka nyingi, ulio pandwa kwenye udongo mzuri na pahali pazuri. Mti
huu ni mzaituni unao mea pahala pa kati na kati. Basi huo si wa mashariki
ukakosa joto la jua wakati wa alasiri, wala si wa magharibi ukakosa joto la jua
wakati wa asubuhi. Bali huo uko juu ya kilele cha mlima, au katika uwazi wa
ardhi unao patisha jua mchana kutwa. Mafuta ya mti huu yanakaribia kutoa mwanga
kwa ubora wa usafi wake hata ikiwa hayajaguswa na moto wa taa. Mambo haya yote
yanazidisha mwangaza wa hiyo taa juu ya mwangaza wake, na Nuru juu ya Nuru.
Na namna hii ndio zinakuwa dalili zilizo enea katika ulimwengu, za kuonekana
na kupimika kwa akili; ni Ishara zilizo wazi hazitaki kutiliwa shaka yoyote kwa
kuwepo Mwenyezi Mungu, na kuwajibikia Imani kumuamini Yeye, na Risala za Mitume
aliyo waleta. Na Mwenyezi Mungu humwezesha kufikia Imani amtakaye kwa njia ya
dalili hizi ikiwa huyo mtu atajaribu kunafiika na nuru ya akili yake. Na
Mwenyezi Mungu ameleta mifano ya kuweza kuhisiwa na kuonekana ili iwe wepesi
kuelewa mambo ya kiakili. Na Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, anawajua wenye
kuangalia Ishara zake na wenye kuzipuuza na wakapanda kiburi. Naye atawalipa kwa
hayo.
36. Hakika wapo watu wanao mtakasa Mwenyezi
Mungu na wanamuabudu misikitini ambayo Mwenyezi Mungu ameamrisha ijengwe na
iamirishwe kwa kudhukuriwa Mwenyezi Mungu, nao wameshughulikia hayo asubuhi na
jioni.
37. Dunia na yaliomo duniani ya kuuza na kununua
hayawashughulishi wakaacha kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kumzingatia. Wao
wanashika Sala, na wanatoa Zaka, na huku wakiikhofu Siku ya Kiyama ambapo nyoyo
zitakuwa hazina utulivu kwa sababu ya wasiwasi na hamu, na kungojea matokeo, na
macho yatadahadari kwa mhangaiko na kushtuka kwa vituko vigeni wanavyo viona, na
wingi wa vitisho.
38. Na malipo ya vitendo vyao ni kulipwa sawa
sawa kwa ubora wa malipo kwa vitendo vyao vyema, na watapata fadhila kwa kupewa
zaidi kuliko wanavyo stahiki. Kwani Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa fadhila, humpa
amtakaye katika waja wake wema kipao kikubwa, asichoweza mtu kukihisabu wala
wenye kuhisabu hawawezi kukisia.
39. Na hao walio pinga na wakakanya wanadhani
wenyewe kuwa wamefanya vizuri, na kwamba vitendo vyao vizuri vitawaletea faida
Siku ya Kiyama. Lakini hao wamekosea katika dhana yao hiyo. Kwani mfano wa
vitendo vyao katika upotovu wake na kukosa maana ni kama mmetuko unao tokea
unapo angukia mwako wa jua wakati wa adhuhuri juu ya ardhi tambarare jangwani.
Mwenye kiu hudhania kuwa ni maji. Hata akiyafikia asikute chochote chenye
manufaa kama alivyo dhania. Hali kadhaalika vitendo vya makafiri siku ya malipo
vitakuwa vumbi lilio tawanyika. Na kafiri ataikuta adhabu ya Mwenyezi Mungu
inamngojea kwa utimilivu wake bila ya nuksani. Hakika hisabu ya Mwenyezi Mungu
hapana shaka inakuja. Na Yeye, Aliye takasika, ni Mwepesi katika kuhisabu kwake,
hachelewi wala hakosei.
40. Na huu mfano mwengine wa vitendo vya
makafiri. Mfano wake ni mfano wa giza la bahari kubwa iliyo tanda yenye kina
kirefu. Mawimbi yake yanapigana na kusukumana wenyewe kwa wenyewe. Nayo
yamefunikwa na mawingu mazito meusi hayapitishi mwangaza. Katika giza hili
lililo rundikana msafiri wa baharini hawezi kuuona mkono wake hata akiukurubisha
machoni. Basi anabaki ameduwaa amebabaika hajijui. Na vipi ataona kitu
atokane na butaa hili bila ya kupata Nuru ya kumwongoa katika mwendo wake, na
kumwokoa na kugongana na kuhiliki. Na basi kama hali hiyo hiyo makafiri
hawapati faida katika vitendo vyao, wala hawatoki katika upofu wao na upotovu
wao, wala hawajiokoi nafsi zao, ila kwa Nuru ya Imani. Kwani hana Nuru ya
kumwongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. Basi atakuwa katika walio teketea.
"Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani.
Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta
Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwepesi wa kuhisabu." Sarabi si chochote ila mandhari ya mwangaza yanayo
sabibishwa na marejeo (reflection) ya miale inayo toka kwenye vitu vyenye kutoa
mwanga. Na hiyo hurejeshwa tena kutokana na ardhi pana tupu, yaani uwanda, na
kupanda kidogo kidogo mkabala na uso wa ardhi, na joto linapo panda wakati wa
mchana, basi miale hiyo inayo rejea ikifika kwa jicho la mwenye kuangalia huona
vile vitu vimegeuka juu chini kama kwamba kwenye kiyoo kikubwa kilicho tanda. Na
kadhaalika mbingu safi ya rangi ya kibuluu huonekana kama kwamba ni ziwa la maji
juu ya uso wa ardhi. Na vile vitu vingine kama miti miti na mitende iliyo
onekana juu chini inazidi kuonyesha kama kwamba ni vivuli kwenye maji. Na hii
Sarabi huzidi kudhihiri kwa uwazi kabisa inapo kuwa khitilafu ni kubwa baina ya
joto la uso wa ardhi na angani katika hewa. Na hayo huonekana zaidi majangwani
na nyandani na kwenye barabara za jangwani za lami zilio nyooka. Kwa maelezo
hayo inaonekana kuwa Sarabi ni kiini macho tu.
Maoni ya wataalamu juu
ya Aya 40:
" Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na
mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu
mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru
hawi na nuru." Aya hii tukufu imekusanya yaliyo muhimu kabisa katika midharuba
ya baharini. Ni maarufu kuwa midharuba ya bahari kuu huwa na mawimbi yanayo
khitalifiana urefu wao na ukubwa wao au mnyanyuko wao, hata inaonekana kama
kwamba hayo mawimbi yanapandana moja juu ya mwenzie, na kwa hivyo yakaziba
mwangaza wa jua kwa vile hiyo midharuba inasabibisha kurundika kwa mawingu
mazito ambayo nayo huuziba mwangaza wa jua, na kwa hivyo husabibisha giza mtu
asiweze kuona kitu juu ya kuwa macho yake mazima. Na ilivyo kuwa Mtume s.a.w.
kazaliwa na kakulia jangwani, kuja maelezo kama haya ya undani ya ki-ilimu kwa
ulimi wake kuwa ni ufunuo ulio tokana na Mwenyezi Mungu, ni ushahidi kuwa
Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu, na kuwa ni muujiza wa Mtume huyu
mtukufu.
41. Ewe Nabii! Hujui kwa yakini kwamba kwa
Mwenyezi Mungu hunyenyekea kila kiliomo mbinguni na duniani? Na wanamnyenyekea
ndege vile vile, nao wamekunjua mbawa zao? Basi viumbe vyote hivi vinanyenyekea
amri ya Mwenyezi Mungu na mipango yake. Vinamtakasa na washirika na kila lisio
na laiki naye. Na kila kimojawapo kinajua kwa kujaaliwa na Mwenyezi Mungu yaliyo
kiwajibikia katika unyenyekevu na kutakasa na kutimiza wadhifa wa maisha. Na
Mwenyezi Mungu nyuma yao anajua kwa utimilivu wa kujua Sala ya kila mwenye
kusali, na kusabihi kwa mwenye kusabihi, na yote wayafanyayo waja. Basi huwaje
makafiri wakawa hawaamini?
42. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye
kumiliki mbingu na ardhi na viliomo ndani yao, na ndiye Mwenye madaraka juu yao,
na wote watarejea kwake Siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na malipo.
43. Ewe Nabii! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu
huyavuta mawingu, kisha huyakusanya na kuyarindika moja juu ya moja. Utaona mvua
inatoka kwenye mawingu. Na Mwenyezi Mungu huteremsha kutokana na mawingu yaliyo
rindikana yanayo shabihi milima (1) kwa ukubwa wake, vipande vya barafu kama
changarawe, vikawaangukia watu vikawaletea manufaa au madhara, kufuatana na
kanuni zake na matakwa yake, wala asiwateremshie wenginewe kwa mujibu apendavyo
Yeye Subhanahu, Mtendaji, Mwenye kukhitari. Mwangaza wa umeme unao tokea kwa
kugongana mawingu hukaribia kutia upofu kwa ukali wake. Na mambo kama haya ya
kuonekana ni dalili za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu ambao unao wajibisha
kuleta Imani ya kumuamini Yeye. (2)
(1) Hajui kushabihiana baina ya
mawingu na milima ila mwenye kupanda ndege (eropleni) inayo ruka juu ya
mawingu, akayaona kutoka huko juu kama ni milima na vilima. Ilivyo kuwa ndege
hizo hazijawa bado zama za Mtume s.a.w. basi hii inakuwa ni dalili kuwa maneno
haya yanatokana na Mwenyezi Mungu anaye jua ya juu na chini.
(2) "Je!
Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha,
kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na huteremsha
kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na
akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua macho." Aya
hii tukufu imeutangulia msafara wa sayansi. Kwani hii yaeleza daraja za kuundika
mawingu yanayo rindikana, na sifa zake, na yaliyo juulikana hivi karibuni
ki-sayansi ya kwamba mawingu ya mvua huanzia kwa sura ya moja moja kisha
yakajumuika yakawa kikundi, ndiyo hayo mawingu yaliyo rindikana, yaani
mawingu yanayo endelea kukua kwa kuelekea utosini. Hayo hukua kimo chake hata
kufikia urefu wa kilomita 15 au 20, na hapo huonekana kama ni milima mikubwa
iliyo nyanyuka.
Na yajuulikanayo ki-sayansi ni kuwa mawingu yaliyo
rindika yanapitia daraja tatu, nazo:
Daraja ya kukusanyika na
kukua.
Daraja ya kunyesha.
Na mwisho daraja ya
kumalizikia.
Kama ilivyo kuwa mawingu hayo - nayo ni peke yao - yenye
mvua ya mawe na inabeba nguvu za umeme (electricity, Kahrabaa) , huweza
kuwa yakashika mfululizo wa umeme na radi, hata huweza ikawa ni miripuko karibu
40 kwa dakika moja, hata mtu anaye tazama akawa hawezi tena kuona kwa ukali wa
mwanga wake. Na haya ndiyo khasa yanayo wapata marubani wa meli na ndege wakati
wa midharuba ya radi.
44. Mwenyezi Mungu huzigeuza hali za usiku na
mchana kwa urefu na ufupi, na kwa kuanzia na kumalizikia, kwa mizunguko ya
falaki. Hakika katika hayo pana mazingatio kwa wenye akili zilio nzima zenye
busara, na kwa njia hiyo wakamuamini Mwenyezi Mungu.
45. Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na
ndiye aliye anzisha kila kitu kwa kupenda kwake. Na akaumba kila kilicho hai
kutokana na asili moja ya shirika, nayo ni maji. Na kwa hivyo kila kihai
hakiachi kuwa na maji. Kisha zinawakhitalifisha khitilafu nyengine kwa namna, na
uwezo, na sura, na kadhaalika. Katika wanyama wapo wanao tambaa kwa matumbo yao,
kama samaki, na nyoka. Na wapo wanao kwenda kwa miguu miwili kama wanaadamu na
ndege. Na wapo wanao kwenda kwa miguu mine kama mahayawani wengi wa kufugwa na
wa mwituni. Mwenyezi Mungu huumba apendavyo kwa njia mbali mbali, kuonyesha
uwezo wake na ujuzi wake. Kwani ni
Mwenye kutaka atakacho, na Mwenye
kukhitari apendacho. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
"Na Mwenyezi Mungu
ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo
yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine.
Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu."
Maji katika Aya hii tukufu ni maji ya uzazi, yaani vinyama vinavyo toa manii. Na
Aya hii si kama imetangulia msafara wa sayansi katika kubainisha kuzalikana mtu
kutokana na tone la manii, kama ilivyo kuja katika kauli yake Aliye tukuka:
"Hebu naajitazame mtu, ameummbwa kwa kitu gani? Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa
kuchupa." (Sura Att'alaq 5,6), bali imetangulia pia katika kubainisha kwamba
kila kinyama kinacho kwenda kwenye ardhi kimeumbwa kwa njia ya kuzalikana na
vinyama vya manii, na vinga khitalifiana hivyo vinyama vya manii na sifa zao
katika kila namna mnamo hizo namna za vinyama. Katika maana za kisayansi ambazo
zaweza kuwa nazo hii Aya ni kuwa maji ni msingi wa kila kiumbe kilicho hai. Kwa
mfano mwili wa mtu umekusanya 70% ya uzito wake kuwa ni maji. Yaani mtu mwenye
uzito wa kilo 70, kiasi kilo 50 ni maji. Na kabla ya kuteremka Qur'ani
haya hayakuwa yakijuulikana kabisa ya kuwa mtu ana sehemu hii kubwa ya
mwili wake kuwa ni maji.
Na maji ndio chakula cha dharura kabisa kwa
mwanaadamu. Kwani hali mtu yamkini aishi siku 60 bila ya kula chakula chochote,
hawezi kuishi bila ya maji kwa zaidi kuliko siku 3 mpaka 10 mwisho wake.
Na maji ndio msingi wa kufanyika damu, na maji ya limfo, na ya katika
ubongo wa mifupa, vimwagavyo na mwili, kama mkojo, na jasho, na machozi, na
mate, na nyongo, na maziwa, na maji yanayo patikana katika viungo, na ambayo
ndiyo sababu ya ulaini wa mwili. Na yakikosekana 20% ya maji yake basi
mwanaadamu hukabiliwa na mauti.
Na maji huyayusha vyakula
vikasahilika kufyonzeka. Na kadhaalika huyayusha makombo yenye asili ya vilivyo
hai au maadini katika mkojo na jasho. Na kwa namna hii maji yana sehemu kubwa
zaidi na muhimu kabisa katika kuumbwa kwa mwili. Na kwa hivyo yamkini kusema
kwamba kila kiumbe kilicho hai kimeumbwa kutokana na maji.
46. Na hakika Sisi tumeteremsha kwa wahyi Aya
zilizo wazi za kubainisha hukumu na mawaidha, na zinazo piga mifano. Na Mwenyezi
Mungu humwezesha kwenye kheri ampendaye katika waja wake ambao wapo tayari
kuziangalia na kufaidika nazo.
47. Na wanaafiki husema kwa ndimi zao:
Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na tunazifuata amri zao. Na wanapo tiwa
mtihanini kikundi kati yao hukataa kushirikiana na Waislamu katika kazi ya
kheri, kama Jihadi na nyenginezo, baada ya kauli yao hii. Na watu hawa si
Waumini wa kweli, wala hawastahiki kutumiliwa jina la Waumini kwao.
48. Na katika hali zao ni kuwa wakitakiwa
kuhukumiwa mbele ya Mtume kwa jambo alilo literemsha Mwenyezi Mungu, unaafiki wa
baadhi yao hudhihiri, na wao hukataa kuhukumiwa wakijua kuwa haki ni ya wale
makhasimu zao.
49. Ama wakijua kuwa haki iko upande wao basi
humjia Mtume mbio mbio ili awahukumu baina yao na makhasimu zao.
50. Na kwa nini wanasimama msimamo huu katika
kushitakiana mbele ya Mtume? Ni kwa sababu nafsi zao zimesibiwa na maradhi ya
upofu, na kwa hivyo haziridhiki na hukumu yako ya haki? Au ni kwa kuwa wao
wanatilia shaka uadilifu wa Muhammad s.a.w. katika kuhukumu? Si lolote katika
hayo kabisa. Lakini hao ni madhaalimu walio dhulumu nafsi zao na wengineo kwa
sababu ya ukafiri wao na unaafiki wao na kuiacha kwao haki.
51. Hakika kauli ya haki ifaayo kwa Waumini wa
kweli wanapo itwa wahukumiwe kwa mujibu wa yaliyo kuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, ni kuwa waseme kwa kukubali na kunyenyekea: Tumesikia wito wako,
ewe Muhammad! Na tumeridhia hukumu yako. Na hao ndio watao kuwa watu wa
kufanikiwa katika dunia yao na Akhera yao.
52. Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na kuridhia
anayo yaamrisha Mtume s.a.w. na wakaiogopa dhati ya Mwenyezi Mungu Tukufu, na
wakaukumbuka Utukufu wake, na wakaikhofu ghadhabu yake, hao ndio watakao
pata radhi ya Mwenyezi Mungu na mapenzi yake, na neema za Pepo, na ndio wenye
kupata kheri tupu.
53. Na wanaafiki wanaapa kwa ukomo wa nguvu za
viapo vyao, kwamba wewe, Muhammad, ukiwaamrisha watoke nawe kwenda vitani
watakut'ii. Waambie: Msiape! Kwani mambo yatakikanayo kwenu mnayajua, hapana
hata mmoja wenu asiye yajua. Wala yamini zenu za uwongo haziondoi ujuzi huo. Na
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua baraabara kila linalo tokana nanyi, na
Yeye atakulipeni kwayo.
54. Waambie: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini
Mtume kwa ut'iifu wa kweli wenye kuonyesha vitendo vyenu. Wanaafiki wakipuuza
wasifuate, basi juu ya Muhammad ni waajibu wa aliyo twishwa tu na Mwenyezi
Mungu, nayo ni amri ya kufikilisha Ujumbe, wala hakukalifishwa uwongofu wao. Na
nyinyi juu yenu ni hayo aliyo kutwikeni Mwenyezi Mungu nayo ni kufuata na
kut'ii. Na mtapata adhabu ikiwa mtaendelea na uasi. Na mkimt'ii Mtume
mtaongoka kwenye kheri. Na yeye haimpasi ila kufikisha kwa uwazi - mkit'ii
au mkiasi - na yeye kesha fikisha.
55. Mwenyezi Mungu amewaahidi katika nyinyi
walio isadiki Haki na wakaifuata, na wakatenda vitendo vyema, kwa ahadi ya kutia
mkazo, ya kwamba atawafanya makhalifa (wafwatizi, warithi) wa wale walio
watangulia wawarithi katika kuhukumu na utawala katika nchi, kama ilivyo kuwa
hali ya walio watangulia. Na atawasimamishia Uislamu kuwa ndio Dini yao aliyo
wapendekezea. Basi watakuwa na heba na madaraka. Na ataibadilisha hali yao
ya khofu iwe ya amani, wawe wananiabudu Mimi nao wametua. Hawanishirikishi Mimi
na chochote kile katika ibada. Na wenye kukhiari ukafiri baada ya ahadi hii ya
kweli, au wakartadi wakaacha Uislamu, basi hao ndio walio toka nje, walio asi,
wapinzani.
56. Na shikeni Sala kwa ukamilifu wa nguzo
katika utulivu na unyenyekevu, ili ipate kuwa inazuia uchafu na mambo mabaya. Na
wapeni Zaka wanao stahiki. Na mt'iini Mtume kwa yote anayo kuamrisheni, ili
mpate kutaraji rehema ya Mwenyezi Mungu na radhi yake.
57. Ewe Nabii! Usidhani kuwa makafiri wataweza
kumkwepa Mwenyezi Mungu asiwashike kwa madhambi yao, au watu wa Haki wasiwaone
pahala popote pale katika ardhi. Bali Yeye ni Muweza, na marejeo yao Siku
ya Kiyama ni Motoni. Na marejeo maovu kabisa ni marejeo yao.
58. Enyi mlio amini! Yakupaseni muamrishe
watumishi wenu na vijana wenu ambao bado hawajabalighi wasikuingilieni vyumbani
mwenu ila baada ya kutaka idhini katika nyakati tatu, nazo ni kabla ya Sala ya
alfajiri (1) , na pale mnapo punguza nguo zenu wakati wa kupumzika mchana, na
baada ya Sala ya Isha mnapo jitayarisha kulala. Kwani nyakati hizi mtu
hubadilisha mavazi ya kulalia badala ya mavazi ya kutokea, na huonekana sehemu
za mwili ambazo hazifai kuonekana. Wala hapana ubaya kwenu wala kwao kuingia
bila ya ruhusa nyakati nyenginezo, kwa sababu ni jamba la ada watu wa nyumbani
kupitiana kwa maslaha yao. Na kwa uwazi wa namna hii Mwenyezi
Mungu anakubainishieni Aya za Qur'ani ili akuwekeeni
wazi hukumu. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, Mkubwa wa
hikima, anajua yanayo silihi kwa waja wake, na anawatungia Sharia zinazo
wanasibu, na kwa kadri ya haja yao.
(1)"Enyi mlio amini! Nawakutakeni
idhini iliyo wamikiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni
mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu
adhuhuri, na baada ya Sala ya isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu.
Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi.
Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi Mwenye hikima." Aya hii tukufu ni moja katika Aya zinazo elekeza nadhari
ya watu wazingatie yaliyo laiki katika jamii za watu khasa ndani ya ukoo.
Nayo kuwa kuchanganyika kwa watumishi na watoto katika aila yao huenda
kukapindukia mipaka ya hishima za maingiano, wakawa wanawaingilia wenginewe bila
ya kutaka idhini katika nyakati maalumu zilizo tajwa katika Aya. Na kwa kuwa
nyakati hizo ni nyakati za faragha na uhuru wa binafsi, na kuvua nguo nzito
nzito, Aya hii imekusudia kuweka Sharia ya kutaka idhini katika nyakati hizo
kutokana na watumishi na vijana ili wasione ambayo yanahisabiwa kuwa ni siri,
ambayo ni kama utupu ambao wapasa kusitiriwa. Na kwa hivyo wanaelekezwa
watu wa ukoo wavae mavazi yanayo kuwa laiki ya kukabiliana hata wao kwa
wao, ili hishima yao ibaki imehifadhika, na uhuru wao umedhaminika, na adabu zao
zimechungika. Na Qur'ani ndio inaayo faa khasa kutuongoza tufuate mwendo ulio
bora na wa juu. (Ikiwa watoto wa nyumbani haiwafalii kuwaingilia watu katika
nyakati hizo za faragha zilizo tajwa, seuze watu mbali!)
59. Na vijana vyenu wakifikilia umri wa
kubalighi inawapasa watake ruhusa ya kuingia kila nyumba, na kila wakati, kama
ilivyo wapasa wenzao wa kabla yao. Na kwa mfano wa uwazi kama huu Mwenyezi Mungu
anakuwekeeni wazi Aya zake alizo ziteremsha. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu
ni Mkunjufu wa ujuzi, Mkubwa wa hikima. Anajua linalo wasilihi waja wake, na
anawaatungia Sharia zinazo wanasibu, na kwa kadri ya haja yao.
60. Na wanawake wakongwe ambao hawatumai
kuolewa, hawalaumiwi wakipunguza baadhi ya nguo zao, kwa sharti wasiwe
wanajishauwa kwa kuonyesha uzuri wa mwili wao ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha
usitiriwe. Lakini kujihishimu kwa kujisitiri kwa ukamilifu ni bora kwao kuliko
kujifunua. Na Mwenyezi Mungu anawasikia wayasemayo, na anayajua makusudio yao,
na atawalipa kwa hayo.
61. Wenye udhuru kama vile vipofu, viguru,
wagonjwa hawana lawama, bali hata nyinyi wazima hamna lawama kula katika
nyumba za watoto wenu, kwani hizo ni nyumba zenu. Wala kula katika nyumba za
baba zenu, na mama zenu, na ndugu zenu wanaume na ndugu zenu wanawake, au nyumba
za ami zenu, au mashangazi zenu, au wajomba zenu, au mama wadogo, dada wa mama
zenu, au nyumba ambazo mmewakilishwa kuzitazama, au nyumba za rafiki zenu mnao
changanyika nao, ikiwa hamna yaliyo harimishwa humo. Na hayo ikijuulikana kuwa
mwenye nyumba ameruhusu yeye au mkewe. Wala hapana ubaya kula humo pamoja au
mbali mbali. Na muingiapo katika nyumba toeni salamu kwa waliomo ambao hao ni
baadhi yenu kwa umoja wa Dini na ujamaa. Kwani hao ni kama nyinyi. Na maamkio
haya ni maamkio yaliyo wekewa Sharia, yenye baraka na thawabu, na pia ndani yake
nyoyo hupoa. Na kwa mfano kama huu Mwenyezi Mungu anazifafanua Aya kwa ajili
yenu mpate kuelewa waadhi na hukumu ziliomo ndani yake, na mpate kuzifahamu na
mzitende.
62. Hakika Waumini wenye kusadiki ni wale ambao
wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wala hawamwachi Mtume peke yake
katika jambo muhimu linalo hitajia wajumuike pamoja kwa ajili yake, kama mfano
wa Jihadi. Ila baada ya kumtaka ruhusa ya kuondoka na wakakubaliwa, hakika wanao
kukadiri wewe, ewe Nabii, kama unavyo stahiki, na wanatambua umuhimu wa huo
mkusanyiko hawaondoki ila baada ya wewe kukubali. Hao ndio wenye kusadiki katika
Imani yao kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi wakikutaka ruhusa hawa
kwenda kufanya baadhi ya maslaha yao mpe ruhusa umtakaye katika wao, pindi
ukimwona kuwa ana haja kweli ya kuondoka, na si dharura kwa mkutano kuwapo yeye.
Juu ya hivyo waombee maghfira kwa Mwenyezi Mungu kwa kuondoka kwao, ambako kwa
hakika hakuelekei kabisa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na
rehema.
63. Fanyeni hima kuhishimu wito wa Mtume
kukuiteni kukusanyika kwa mambo muhimu. Na muitikieni huo wito wake, wala
msifanye wito huo kama mnavyo itana nyinyi kwa nyinyi, kuwa inafaa kupuuza na
kuondoka mpendavyo. Wala msiondoke ila baada ya kutaka ruhusa na mkakubaliwa, na
tena iwe katika mipaka ya ufinyo kabisa, na dharura za shida. Na Mwenyezi Mungu
Subhanahu anawajua wanao ondoka bila ya idhini wakijificha ficha kati ya
watu ili ati Mtume asiwaone. Na watahadhari wanao kwenda kinyume na amri ya
Mwenyezi Mungu asije Subhanahu akawapatiliza kwa uasi wao wakapata mateso makali
duniani kama ukame na mitetemeko, au akawapa adhabu yenye wingi wa uchungu aliyo
waandalia Akhera, nayo ni ya Motoni.
64. Zindukaneni enyi
watu! Mjue kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kumiliki mbingu na ardhi,
na viliomo ndani yao. Anayajua mlio nayo, ukafiri wenu na Uislamu wenu, na
uasi wenu, na ut'iifu wenu. Basi msiende kinyume na amri yake. Na Yeye atawapa
khabari watu, watapo rejea kwake Siku ya Kiyama, kwa yote waliyo yatenda
duniani, na atawalipa kwayo. Kwani Yeye amekizunguka kila kitu kwa ujuzi wake.