1. Kumethibiti kufanikiwa kwa Waumini wanao
muamini Mwenyezi Mungu na waliyo kuja nayo Mitume; na wamefuzu kwa wayatakayo.
2. Hao ambao wameambatisha juu ya Imani yao
vitendo vyema. Basi hao katika Sala zao humuelekea Mwenyezi Mungu kwa nyoyo
zenye kumkhofu na kumnyenyekea, wanahisi unyenyekevu wa mwisho kwake Yeye .
3. Hao wanashughulikia mambo ya maana, wanapuuza
vitendo na maneno yasiyo na kheri ndani yake.
4. Nao wanashikilia kutoa Zaka kuwapa wanao
stahiki. Kwa hivyo wanakusanya ibada ya mwili na ibada ya mali, na baina ya
kujisafisha nafsi na kuyasafisha mali.
"Na ambao wanatoa Zaka,": Huu
waajibu wa kutoa Zaka unapelekea kujenga mashikamano ya umoja baina ya Waislamu,
na kutia katika moyo wa kila mtu kuwa ana jukumu kwa nduguye, anahisi kama
anavyo hisi yeye, na anaungulika kama anavyo ungulika yeye. Kwa hivyo ni waajibu
wake kufanya awezavyo kumkinga na balaa za kilimwengu, na machungu ya ukosefu.
Kwa hivyo fakiri au masikini hatomchukia tajiri, bali wote watahisi kama
ni ukoo mmoja unao saidiana na wenye kushikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu.
Wala mwenye deni hakati tamaa kuweza kulipa deni lake lilio bakia ikiwa hana cha
kumalizia hilo deni. Wala haianguki chini azma ya mujaahidi anaye pigana katika
Njia ya Mwenyezi Mungu kuinusuru Dini yake na kukomboa nchi yake kwa sababu ya
kukosa mali ya kutimizia makusudio yake. Wala msafiri au mgeni mhitaji aliye
mbali na mali yake hakosi wa kumkidhia haja zake kwa kumsaidia mpaka afike
kwake. Na juu ya haya Zaka ilikuwa ni njia moja katika njia kubwa ulio
chukua Uislamu kukombolea mateka na wafungwa na kuondoa utumwa. Na Uislamu
umeongeza kutimiza malengo yake ya kijamii kwa ulimwengu mzima ikatupilia mbali
chuki zinazo chusha za kidini, na ikatoa ruhusa Zaka wapewe makafiri ikihitajia
haja kuwakopesha. Hali kadhaalika hupewa wale wanao itumikia Zaka, kama
kuikusanya na kuigawa. Pia waandishi, na wasafiri, na wanao khasiri kwa ajili ya
kupatanisha wenye kugombana, na wanao wasaidia Waislamu katika vita. Ama
makusudio ya kiuchumi ya Zaka ni kuondoa ufakiri popote ulipo, na
kumsaidia kila mwenye haja kama ilivyo kwisha tangulia.
5. Nao wanajihifadhi nafsi zao wasiingiane na
wanawake.
"Na ambao wanazilinda tupu zao, isipo kuwa kwa wake zao au kwa
iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. Lakini anaye
taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka." Aya hizi zinaambatana na
Aya nyengine ziliomo katika Suratun Nur zilio anzia: "Mzinifu mwanamke na
mzinifu mwanamume, mpigeni kila mmoja wao bakora mia." Hakika Aya hizi tukufu
zilizo tajwa zinaashiria maovu ya katika umma yanayo tokea kwa uzinzi. Ama
katika umma ni kuvurugika nasaba ya watoto isijuulikane, ama katika siha ni
sehemu mbili. KWANZA ni katika mwili, mfano wa kisonono, tego, AIDS n.k.
Kisonono huweza kuzalisha maradhi ya urithi kwa watoto hata huweza kuleta upofu.
Ama tego (Syphilis) huenea katika mishipa ya damu na ya hisiya na huweza kuishia
wazimu, na pia huenea mpaka kwa vizazi, na huenda mtoto akafa tumboni au akatoka
na kilema. Ama maradhi ya AIDS (Ukimwi) hayo ni maafa yasiyo semeka, Mwenyezi
Mungu atulinde nayo. PILI ni kuathirika mishipa ya hisiya na akili, kwani
uzinzi huweza kuathiri dhamiri ya mtu, na kuadhibika nayo, na hata mwishoe
huweza kuingia wazimu.
6. Isipo kuwa kwa njia ya ndoa ya kisharia, au
wenye kumiliki masuria. (1) Hao hawalaumiwi.
(1) Zamani utumwa ulikuwa ni
jambo la kawaida, na ilikuwa mtu akiweza kuchukua katika wajakazi wake
akawafanya kuwa ni wakeze. Na Uislamu ulihalalisha utumwa wa mateka katika vita
vilivyo fuata sharia ikiwa maadui nao wanakamata watumwa, basi ilikuwa ni halali
kuwatendea wao hali kadhaalika. Ikiwa maadui hawawafanyi mateka kuwa ni watumwa
basi ilikuwa haiwafalii Waislamu kuwafanya mateka kuwa ni watumwa.
7. Mwenye kutaka kuingiliana na mwanamke bila ya
kupitia njia hizi mbili, basi huyo amevuka mipaka ya sharia hadi ya kuvuka.
8. Na (hao Waumini) wawe ni wenye kuhifadhi kila
walicho pewa kuwa ni amana, ikiwa mali au neno au kitendo au chenginecho, na
watimize kila ahadi iliyo baina yao na Mwenyezi Mungu au na watu.
Wasikhuni amana, wala wasivunje ahadi.
9. Na wawe wenye kudumisha kutimiza Sala kwa
nyakati zake, na kuzitekeleza kwa nguzo zake na unyenyekevu wake, mpaka
yapatikane makusudio yake. Nayo ni kuachisha uchafu na maovu.
10. Hawa wenye kusifiwa hivi ndio watakao rithi
kheri yote na wataipata Siku ya Kiyama.
11. Hawa ndio Mwenyezi Mungu atawafadhili kwa
kuwapa Firdausi, ndio pahala pa juu kabisa huko Peponi, wastarehe humo peke yao.
12. Yawapasa watu waangalie asli ya kuumbwa
kwao; kwani hiyo ni dalili za kuonyesha uwezo wetu zenye kupelekea kumuamini
Mwenyezi Mungu, na kuamini kufufuliwa. Kwani Sisi tumemuumba mtu kutokana na
asli ya udongo.
13. Kisha tukaumba vizazi vyake, navyo ni kuwa
tulimfanya mtu kwanza tone ya mbegu ya uzazi - yaani maji yenye kila sifa ya
uhai wa mwanzo. Tukaiweka kwenye tumbo la uzazi, napo ni pahala pa utulivu
palipo lindwa.
14. Kisha tukaifanya hii mbegu ya manii baada ya
kuipandisha na yai la mwanamke kuwa damu. Kisha damu tukaigeuza kuwa kipande cha
nyama, kisha tukafanya mafupa, na mafupa tukayavika nyama. Kisha tukatimiza
uumbaji wake mwishoe baada ya kuipulizia roho kuwa kiumbe kingine mbali ili
kuanza kumjenga. Shani ya Mwenyezi Mungu imetukuka kwa utukufu wake na uwezo
wake. Yeye hana mshabaha wake na yeyote katika kuumba kwake na kutengeza kwake
na kuanzisha kwake.
15. Kisha hakika nyinyi wanaadamu baada ya haya
mambo yenu tuliyo yataja ni wenye kuyaendea mauti bila ya shaka yoyote.
16. Na kisha nyinyi mtafufuliwa Siku ya Kiyama
kwa ajili ya kuhisabiwa na kulipwa jaza yenu.
17. Na hakika Sisi tumeziumba mbingu saba zilizo
nyanyuka juu yenu. Ndani yake vipo viumbe ambavyo hatukughafilika navyo.
Tunavihifadhi na tunaviendesha. Na Sisi kabisa hatughafiliki na viumbe vyetu
vyote. Bali tunavilinda visipotee na kuharibika, na tunavipangia mambo yao yote
kwa hikima.
"Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa
wenye kughafilika na viumbe." Hizo njia saba zilizo tajwa katika hiyo Aya
maana yake ni mbingu saba, na kwamba hizo si mbingu moja, na Mwenyezi Mungu
haghafiliki na mbingu hizo na viumbe viliomo ndani yake.
18. Na Sisi tumeteremsha kutoka mbinguni mvua
kwa hikima na kipimo katika umbo lake na kuteremka kwake. Na kusahilisha kwa
ajili ya manufaa tumeijaalia ikae juu ya uso wa ardhi na ndani yake chini. Na
Sisi hakika ni wenye kuweza kuiondoa wasipate kunafiika nayo. Lakini hatukufanya
hayo kwa kukuoneeni huruma. Basi muaminini Mwenye kuiumba na mumshukuru.
"Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza katika
ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa." Aya hii tukufu inaashiria maana ya
kisayansi yenye kukhusu mzunguko wa maji katika ardhi. Yajuulikana kuwa mvuke
unao paa kutoka baharini hupelekea kufanyika mawingu ambayo ndiyo huteremsha
mvua. Na hivyo ndio chanzo cha maji matamu juu ya uso wa ardhi, na ndio chombo
cha msingi cha uhai wa ardhini. Kutokana na mvua ndio huzuka mito inayo zua uhai
katika sehemu kamwe zisio pitikiwa na mvua. Kisha hiyo mito inamiminika
baharini, na khulka inarejea tena kutoka baharini kwenda angani na kwendea
nchi kavu, na kisha kuingia baharini mara ya pili. Isipo kuwa baadhi ya hayo
maji ya mvua yanatulia na yanazama kuhifadhika katika mahodhi ya chini ya ardhi,
yakawekeka kwa muda mrefu. Mfano wa hayo ni hayo maji yanayo patikana chini ya
Jangwa la Magharibi katika Libya, ambayo yamegunduliwa na watafiti hivi karibuni
kutokana na asli yake ya kale. Na huenda maji kama haya yalio hifadhika chini
yakapatwa na mabadiliko ya joto wanayo yaita wataalamu wa ilimu ya t'abaka za
ardhi (Geology) kuwa ni Mikondo ya Jiolojia, ikenda hiyo na maji mpaka pahala
pengine pakavu, ikaleta uhai baada ya kuwa ni maiti.
Na Aya hii
inaonyesha hikima kubwa ya uenezaji wa maji kwa kipimo, yaani kipimo cha haki na
hikima, kwa ajili ya kuleta manufaa na kupinga madhara. Na tena maana nyengine
ya Aya tukufu ni kufahamisha apendavyo Mwenye Kuumba, Aliye tukuka, navyo ni
kujaalia yawepo maji ya kiasi maalumu katika bahari za ulimwengu kutosha kuwepo
mizani ya joto la kufaa katika sayari hii, na ili isiwepo khitilafu kubwa mno
baina ya joto la siku za joto, na baridi ya siku za baridi, hata ikawa ni muhali
kubakia uhai, kama ilivyo katika sayari nyengine na katika mwezi. Kadhaalika
maji ya ardhi yanateremka kwa kiasi maalumu, hayazidi yakafunika ardhi yote,
wala hayatindikii sana hata yasipatikane hata kidogo kunyweshea baadhi ya nchi
kavu.
19. Kwa haya maji tukakuumbieni mabustani ya
mitende na mizabibu yenye matunda mengi kwa ajili yenu, na katika hayo nyinyi
mnakula.
20. Na tumekuumbieni mti wa zaituni unao ota
katika jimbo la Mlima wa Sinai. Katika matunda yake yanapatikana mafuta yanayo
kufaeni. Na hizo zaituni ni kitoweo cha chakula kwa wanao kula.
"Na mti
utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na kuwa kitoweo kwa walao." Aya hii
tukufu inathibitisha kuwa mti wa zaituni ni miongoni mwa neema alizo mneemesha
Mwenyezi Mungu binaadamu na ambazo baadhi yake zimetajwa katika Aya zilizo
tangulia. Na la kuongeza kwenye Aya hii ni kuwa mzaituni ni miongoni mwa miti ya
mbao inayo ishi muda mrefu sana, zaidi ya mamia ya miaka. Kwa hivyo hauhitajii
juhudi kubwa kwa mtu, bali huendelea kuzaa wenyewe mfululizo. Kadhaalika una
sifa ya kuwa daima kijani, unapendeza kuutazama.
Uchunguzi wa
kisayansi unaonyesha kwamba zaituni ni katika chakula kizuri. Kwani ndani yake
imo Protein nyingi. Vile vile zimo chumvi za Calcium, chuma na Phospohorous. Na
hivi ni muhimu na vya kutegemewa katika chakula cha binaadamu. Na juu ya hivyo
zaituni inayo Vitamin A na Vitamin B. Na kutokana na tunda lake hutolewa mafuta
ya zaituni, ambayo ni mafuta bora ya mafuta mepesi. Mafuta haya hutumiwa
katika chakula. Uchunguzi wa kitabibu unaongeza kusema kuwa zipo faida
nyengine katika mafuta ya zaituni, nazo ni kuwa zinasaidia kwa jumla katika
viungo vya usagaji wa chakula, na khasa maini. Nayo yanashinda ubora mafuta yote
yanayo tokana na mimea na wanyama, kwa kuwa hayasabibishi maradhi ya mishipa ya
damu kama mafuta mengineyo, na kadhaalika yanalainisha ngozi. Na mafuta ya
zaituni yana matumizi mengine mengi katika sanaa (ufundi), kwani yanatumiwa
katika kufanya sabuni nzuri kabisa, na vitu vinginevyo katika ufanyaji wa
vyakula na vitu vya sanaa.
21. Na nyinyi mnapata kutokana na nyama hoa,
nyama wa kufuga, nao ni ngamia, ng'ombe, kondoo na mbuzi, mambo yanayo onyesha
uwezo wetu na fadhila zetu juu yenu kwa kukuneemesheni. Tunakunywesheni kutoka
matumboni mwao maziwa safi, matamu, mepesi kwa wenye kuyanywa. Na mbali ya
maziwa mnapata manufaa mengine kama nyama, na sufi, na manyoya. Na kutokana na
hao nyinyi mnaishi na mnaruzukiwa.
22. Na juu ya hawa wanyama wa kufuga na marikebu
nyinyi mnapanda, na mnapakia mizigo. Basi Sisi tumekuumbieni njia za
usafirishaji na upakizi nchi kavu na baharini. Na kwa hizo mnapata kuwasiliana
nyinyi kwa nyinyi.
23. Na katika visa vya watu wa kale pana
mazingatio kwa ajili yenu mpate kuamini. Basi Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake,
naye akawaambia: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu pekee. Kwani nyinyi
hamna anaye stahiki kuabudiwa asiye kuwa Yeye. Hamwogopi adhabu yake, na
kuondoka neema zake mkimuasi?
24. Wakubwa wa kaumu yake walio kufuru
wakiukanya wito wake na wakizuia watu wasimfuate, walisema: Hapana khitilafu
yoyote baina ya Nuhu na nyinyi. Kwani yeye ni mtu kama nyinyi, lakini anataka
kujipa ubora juu yenu kwa huu wito wake. Na lau kuwa wapo Mitume wanao toka kwa
Mwenyezi Mungu kama anavyo dai yeye, basi ange waletea Malaika. Sisi hatukupata
kusikia wito huu katika taarikhi za baba zetu walio tangulia, wala kutumwa
binaadamu kuwa ni Mtume.
25. Huyu si chochote ila ni mtu mwenye wazimu.
Na kwa hivyo wakasema: Ngojeni, na mstahamilieni mpaka ukashifike wazimu wake,
au kufike kuangamia kwake.
26. Nuhu akamwomba Mola wake Mlezi baada ya
kukata tamaa kuamini kwao, akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru nao, na watie
adabu kwa sababu ya kuukadhibisha kwao wito wangu!
27. Tukamwambia kwa njia ya ufunuo (wahyi): Unda
jahazi, nawe utalindwa na uangalizi wetu. Shari yao haitokupata, nasi
tutakuongoza katika kazi yako. Na ikifikilia miadi ya kuwaadhibu, na ukaona
tanuri inafoka maji kwa amri yetu, basi waingize katika jahazi katika kila namna
ya viumbe vilivyo hai dume na jike. Na waingize ahali zako, isipo kuwa walio
kwisha thibitika adhabu yao kwa kukosa kwao Imani. Wala usiniombe kuwaokoa wale
walio dhulumu nafsi zao na wakawadhulumu na wengineo kwa ukafiri na uasi. Kwani
Mimi nimewahukumia kuwazamisha kwa sababu ya dhulma yao ya ushirikina na uasi.
"Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu!
Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila
namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake
imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya
shaka watazamishwa." Hakika haya maelezo ya Tofani lilio tokea ijapo kuwa ni kwa
mukhtasari tu katika hizi Aya tukufu, kwa mwenye akili ya kuzingatia yana maana
na mambo ya hakika mengi ya ki-ilimu ambayo yanawapitia watu wengi. Na "tanuri"
kwa lugha ni jiko la kuchomea mikate, au pia ni uso wa ardhi na kila chenye
kutimbuka maji, na kila penye mkusanyiko wa maji.
Na si wepesi kusema
kwa yakini taarikhi ya hiyo Tofani, kwani zilitokea tofani nyingi zama za kale,
kama katika Babilonia, Bara Hindi na Amerika.
Na zipo baadhi ya
hadithi za kienyeji mbali mbali zinazo taja khabari ya Tofani. Lakini
haielekei kuwa hadithi hizo ndio zimekhusu hii Tofani kubwa au Tofani ya Nuhu.
Uchunguzi umethibitisha na pia zimeonekana tofani nyingi ulimwenguni. Na tofani
ya mwisho ya ulimwengu mzima ilikuwa sababu yake ni kumalizika kipindi cha
barafu cha mwisho, na kuyayuka barafu nyingi ya kaskazini kabisa na kusini
kabisa kwa dunia. Na sisi hatujui kwa yakini lini mizani iligeuka na tanuri
ikafurika - yaani uso wa ardhi - kwa kupanda kwa ghafla kwa hivyo kuyayuka
barafu, hata yakapanda juu maji ya bahari na ya kamwagika maji.
Yafaa
kutaja kuwa kuyayuka barafu ya zama za barafu za mwisho kulileta hali ya hewa
yenye mvua nyingi sana katika sehemu za dunia zilio mbali na huko kaskazini na
kusini kabisa kwa ulimwengu, kama vile katika Bahari ya Kati (Mediterenian).
Vyo vyote vile ilivyo inakubalika kuwa hatuna ushahidi wa kuweza kusema
lini khasa zilikuwa hizo zama za Nuhu na kaumu yake. Yaliyo dhaahiri kuwa yote
hayo ni muujiza wa Mwenyezi Mungu. Na katika miujiza ni kuwa Nuhu aliwanasihi
watu wake na akawaonya na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu akafunua
kuwa atawazamisha ikiwa hawakutengenea. Na tena akamfunulia aunde marikebu.
Kisha ikaja amri ya Mwenyezi Mungu, na mizani ikapinduka, na tanuri ikafurika,
ikamiminika mvua kuthibitisha aliyo yasema Mwenyezi Mungu kumwambia Nuhu ya
kwamba Mwenyezi Mungu anajua kuwa hatoamini mtu katika kaumu yake baada ya wale
walio kwisha amini.
28. Na ukisha panda na ukatua wewe na walio
pamoja nawe katika jahazi hiyo basi sema kwa kumshukuru Mola wako Mlezi:
Alhamdulillahi! Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliye tuokoa
na shari ya watu makafiri walio asi.
29. Na useme: Ewe Mola Mlezi! Nijaalie nishuke
mashukio yenye baraka, pahala pazuri pa kukaa wakati wa kuteremka nchi kavu. Na
unitunukie amani hapo. Kwani ni Wewe tu peke yako unaye weza kututeremsha pahala
pa kheri na amani na salama.
30. Hakika katika kisa hichi yapo mazingatio na
mawaidha mengi. Na hakika Sisi tunawajaribu (tunawapa mitihani) waja wetu kwa
kheri na shari. Na ndani ya nafsi zao wana utayarisho wa yote hayo.
31. Tena baada ya kaumu ya Nuhu tukaumba namna
ya watu wengine, na wao ni A'adi.
32. Tukawapelekea Huud. Naye ni katika wao.
Tukawaambia kwa ulimi wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake. Kwani nyinyi
hamna Mungu anaye stahiki kuabudiwa asiye kuwa Yeye. Ni Yeye peke yake anaye faa
mumwogope. Basi, jee mmeikhofu adhabu yake mkimuasi?
33. Na wakubwa katika kaumu yake walio
kufuru na kukadhibisha kukutana na Mwenyezi Mungu na mambo ya Akheria ya hisabu
na malipo, na tukawapa sehemu kubwa ya starehe na neema, wakasema kwa kukanusha
wito wake, na kuwazuia watu wasimfuate: Hapana khitilafu yo yote baina ya Huud
na nyinyi. Anakula chakula hicho hicho mnacho kila nyinyi. Na anakunywa vinywaji
hivyo hivyo mnavyo vinywa nyinyi. Mfano wa huyu hawezi kuwa Mtume, kwa sababu
hana sifa msizo kuwa nazo nyinyi.
34. Na wakawahadharisha kwa nguvu na mkazo,
wakiwaambia: Mkimt'ii mtu aliye kama nyinyi kwa utu wake, basi nyinyi hakika
mtakuwa mmekhasiri kwa kuwa hamtapata manufaa yo yote mkimfuata.
35. Wakawaambia pia katika kukanya kufufuliwa:
Hivyo Huud anakuahidini kuwa mtafufuliwa kutoka makaburini kwenu baada ya kwisha
kufa kwenu, na mkawa udongo na mafupa yasiyo kuwa na nyama na mishipa?
36. Hayo anayo kuahidini ni ya mbali mno,
wala hayatakuwa abadan.
37. Hapana uhai ila mmoja tu. Nao ndio huu uhai
wa duniani, ambao tunauona una mauti na uhai unao tupitia. Kinacho zaliwa
kinazaliwa, na kilicho hai kinakufa. Wala hatutofufuliwa baada ya kwisha kufa
kabisa.
38. Huyu si chochote ila ni mtu aliye mzulia
Mwenyezi Mungu, na akadai kwamba Mwenyezi Mungu kamtuma yeye. Na amesema uwongo
katika hayo anayo tuitia. Wala hatutomsadiki abadan.
39. Huud akasema baada ya kwisha kata tamaa
kuamini kwao: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na uwatie adabu, kwa sababu ya
kuukadhibisha wito wangu.
40. Mwenyezi Mungu akamwambia Huud kuzidi
kutilia nguvu ahadi yake: Baada ya muda mchache watakuja juta, kwa waliyo
yafanya, itapo wateremkia adhabu.
41. Ukawachukua ukelele mkali ulio wahilikisha
kama walivyo stahiki. Tukawafanya kwa udhalili na udhaifu kama vijiti na majani
ya miti yanayo chukuliwa na maji ya mvua. Na huko ni kuteketea na kupotelea
mbali na rehema kwa madhaalimu kwa ukafiri wao na uasi wao.
42. Kisha baada yao tukawaumba kaumu nyengine
wasio kuwa wao, kama kaumu ya Saleh na ya Luut'i na ya Shuaib.
43. Kila umma una zama zake maalumu,
hazitangulii wala hazikawii.
44. Kisha tukawatuma Mitume wetu wakifuatana,
kila mmoja kwa kaumu yake. Kila akija Mtume kwa kaumu yake waliukadhibisha wito
wake. Nasi tukawateketeza mfululizo, na tukazifanya khabari zao ni hadithi za
watu kusimuliana na kuzistaajabia. Basi hao kaumu wasio isadiki Haki wala
hawaifuati wametengeka mbali na rehema, na wamehiliki.
45. Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni,
tukawapa dalili za kukata kuthibitisha ukweli wa ujumbe wao, na hoja wazi yenye
kudhihirisha kuwa wao ni kweli wametumwa kutoka kwangu.
46. Tuliwatuma wawili hao kwa Firauni na kaumu
yake. Wakakataa kuamini kwa ajili ya takaburi, na wao ni watu walio kuwa
wakisifika kwa kiburi, na majivuno, na ujeuri.
47. Wakasema kwa mastaajabu na kukanya: Je,
tuuamini wito wa watu wawili walio ni wanaadamu kama sisi, na tena watu wao hawa
Wana wa Israili ni wenye kutunyenyekea sisi na kutut'ii kama ni watumwa?
48. Basi waliwafanya waongo katika huo wito wao,
na wakawa wenye kuhiliki kwa kuzamishwa.
49. Na hakika tulimfunulia Musa Taurati apate
kuwaongoa watu wake kwa yaliyomo ndani yake ya uwongozi kwendea hukumu na njia
za mafanikio.
50. Na tumemjaalia Isa bin Maryamu na mama yake,
kwa vile kuchukua mimba bila ya kuingiliwa na mtu, na kuzaliwa yeye Isa bila ya
baba, kuwa dalili ya kukata ya uwezo wetu wenye kushinda. Na tukamweka
Maryamu pahala pa kukaa penye ardhi iliyo nyanyuka na kukunjuka panapo faa
kukaa, na pana maji mengi. Na hayo ndiyo yanayo wezesha maisha ya starehe.
51. Tumewaambia Mitume wawafikishie watu wao:
Kuleni vyakula vya kila namna vya halali na vizuri, na stareheni na ishukuruni
neema yangu kwa vitendo vyema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa myatendayo na
nitakulipeni kwayo.
52. Na tukawaambia wawafikishie watu wao:
Hakika hii Dini niliyo kutumeni muifikishe ni Dini moja kwa mintarafu ya Imani
na misingi ya sharia. Na hakika nyinyi ni umma mmoja katika vizazi vyote.
Miongoni mwao wapo walio ongoka, na wapo walio potoka. Na Mimi ndiye Mola wenu
Mlezi niliye kuamrisheni muifuate, basi iogopeni adhabu yangu pindi mkiasi.
53. Lakini watu walilikata kata hili jambo la
Dini yao. Wapo kati yao walio ongoka, na wapo walio potoka ambao wakafuata
matamanio yao, wakafarikiana kwa sababu hiyo wakawa makundi mbali mbali yenye
kufanyiana uadui. Kila kikundi kinafurahi kwa walio nayo, kwa kudhania kuwa wao
tu ndio walio sibu.
54. Basi, ewe Muhammad, waachilie mbali makafiri
na ujinga wao na kughafilika kwao, maadamu wewe umekwisha wanasihi, mpaka
Mwenyezi Mungu awahukumie adhabu baadae.
55. Hivyo hawa maasi wanadhani ya kwamba pale
Sisi tunapo wawacha wakistarehe na mali na watoto tulio wapa
56. Ndio basi Sisi tumekuwa radhi nao, na kheri
zikawamiminikia mbio mbio na kwa wingi? Hao ni kama wanyama, hawatambui, kwa
kuwa hawazitumii akili zao. Mimi si radhi nao. Na hizi neema ni kuwapururia tu,
kuwapa muda.
57. Hakika wale ambao humkhofu Mwenyezi Mungu na
humwogopa, na zimejaa ndani yao khofu ya Mwenyewe Subhanahu,
58. Na wale ambao wanaziamini Ishara za Mola wao
Mlezi ziliomo ulimwenguni na zinazo somwa katika Kitabu kilicho teremshwa,
59. Na wale ambao hawamshirikishi Mwenyezi Mungu
na yeyote,
60. Na wale ambao wanatoa katika vile anavyo
waruzuku Mwenyezi Mungu, na wanafanya a'mali yao na hali wao wana khofu
wasifanye taksiri, kwa sababu bila ya shaka wao ni wenye kurejea kwa Mwenyezi
Mungu kwa kufufuliwa na watahisabiwa,
61. Hao wote hukimbilia na a'mali zao kuendea
kupata kheri, na wao ni wenye kuwatangulia wengineo katika kupata huko.
62. Na Sisi hatumlazimishi mtu yeyote ila kwa
analo liweza kulifanya, kwa sababu limo ndani ya makdara yake. Na kila a'mali
katika a'mali za waja zimesajiliwa kwetu katika kitabu, na tutawapa khabari zake
kama zilivyo. Na wao hawatadhulumiwa kwa kuongezewa adhabu wala kupunguziwa
thawabu.
63. Lakini makafiri kwa sababu ya inadi yao na
chuki zao ni wenye kughafilika na kufanya kheri, na kujikalifu kufanya
liwezekanalo, na kwamba kuna hisabu ya kuchungua kila kitu. Na mbali na hayo
bado wanavyo vitendo vingine viovu wanavyo dumu navyo.
64. Na Sisi tunapo wapatiliza adhabu matajiri
wenye kudeka katika starehe zao hupiga makelele na wakayayatika kuomba msaada.
65. Basi tunawaambia: Msiyayatike, wala msiombe
msaada hivi sasa. Hamtatoka ndani ya adhabu yangu, wala kuyayatika kwenu hakufai
kitu.
66. Hamna udhuru. Kwani Aya zangu zenye
kuteremshwa kwa wahyi zilikuwa mkisomewa, nanyi mkizipuuza kwa mapuuza yenye
kugeuza hali zenu, na wala hamkuzisadiki, wala hamkuzifuata kwa vitendo.
67. Na nyinyi katika mapuuza yenu mlikuwa
mnatakabari na mnafanyia maskhara, mkiutaja huu Wahyi kwa sifa mbaya mnapo
kutana katika taanusi zenu za usiku.
68. Je! Hawa wenye kupuuza wamekuwa wajinga hata
hawakuizingatia Qur'ani wakaijua kwamba hii hakika ni Haki? Au huu wito wa
Muhammad kwao umekuwa ni namna mbali kuliko walio kuja nayo Mitume wengine kwa
kaumu zilizo kwisha tangulia walio ambao baba zao waliwawahi?
69. Au hawamjui Mtume wao Muhammad aliye kulia
kati yao katika tabia zake tukufu ambazo hazijapata kuwa na uwongo, na wao
hivi sasa wanaukataa wito wake kwa dhulma na husda.
70. Au wanasema kuwa huyu ni mwendawazimu?
Hasha! Huyu hakika kawaletea Dini ya Haki, na wengi wao wanaichukia haki, kwani
hiyo ni kinyume na matamanio yao na mapenzi yao, basi kwa hivyo hawamuamini.
71. Ingeli kuwa Haki inafuata matamanio yao
ufisadi ungeli enea ulimwenguni, na hawa za nafsi zingeli pambana wenyewe kwa
wenyewe. Lakini Sisi tumewapelekea Qur'ani ambayo inawakumbusha haki ambayo
inapasa wote wajumuike juu yake. Na juu ya hivyo wao wanayapuuza hayo.
"Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika
mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao
wanajitenga mbali na ukumbusho wao." Hilo neno "Haki" ni tamko lenye maana
kadhaa. Huweza kuwa maana yake ni "Mwenyezi Mungu" Subhanahu wa Taa'la , mfano
wa kauli yake Mtukufu: "Ametukuka Mwenyezi Mungu wa Haki". Pengine huwa maana
yake ni "Qur'ani" , kwa mfano :"Hakika Sisi tumekutuma kwa Haki". Na huenda
kukusudiwa "Dini yote", yaani miongoni mwake ni Qur'ani na Sunna (Hadithi)
Sahihi, mfano wa kauli yake: "Na sema: Imekuja Haki na uwongo umetoweka".
Na iliyo dhaahiri katika tamko la Haki hapa ni kuwa makusudio yake ni ile maana
ya kwanza, yaani "Mwenyezi Mungu" Aliye takasika na kutukuka. Na kwa
hivyo maana iliyo kusudiwa na Aya ni: Lau kuwa mwenendo wa Mwenyezi Mungu
unafuatana na watakayo na wanayo yapendekeza makafiri mpango usingeli
bakia katika hali iliyo simamia shani ya mpango wa mbingu na ardhi na wa viumbe
viliomo ndani yake. Lakini Mwenyezi Mungu Mwenye hikima kuu na uwezo wa kutenda
na ujuzi wake ulio enea kwa viumbe vyake na hikima yake ikadhamini kwa
mpango madhubuti, na Qur'ani kusema kwa uwazi ya kwamba mbingu zina
viumbe, anatuelekeza tufahamu:
* Kwanza kuwa Kuamini hayo kwa jumla
ni yakini, tuache tafsili yake mpaka apendavyo Mwenyezi Mungu Subhanahu
kuidhihirisha kwa kuambatana na kauli yake: "Tutawaonyesha Ishara zetu
angani na katika nafsi zao."
* Pili: Anatuelekeza kwenye utafiti wa
kisayansi kama tunaweza "kwani kufikilia hakika hii inatutilia nguvu Imani yetu.
Na Imani ndiyo lengo muhimu katika kuelekea kwetu kwenye Ishara hizo."
72. Kwani, ewe Nabii! Unawataka ujira kwa
huku kufikisha kwako ujumbe? Hayakuwa hayo! Kwa kuwa ujira hakika ujira wa Mola
wako Mlezi ni bora zaidi kuliko walio nao wao; na Yeye ndiye Mbora wa kutoa.
73. Na hakika wewe, ewe Muhammad, hapana shaka
yoyote unawaitia Dini ambayo ndiyo Njia Iliyo Nyooka yenye kupelekea Uwokovu.
74. Na hakika hao wasio iamini Akhera na yalioko
huko ya Pepo au Moto wanaiacha Njia Iliyo Nyooka inayo mhifadhi mpitaji
wakaishika njia ya ubabaishi na misukosuko na ufisadi.
75. Na lau tungeli warehemu, na tukawaondolea
madhara yalio wateremkia katika miili yao, na ukame katika mali yao, na mfano wa
hayo, basi hapana shaka yoyote wangeli zidi ukafiri, na wakaendelea katika maasi
na jeuri.
76. Na Sisi kwa hakika tuliwapa adhabu kama kwa
kuwauwa au kuwaletea njaa. Na wala hawakumnyenyekea Mola wao Mlezi, bali
waliendelea na jeuri zao na kiburi chao kiasi ya kuondoka tu hiyo adhabu.
77. Wanashikilia kupuuza kwao mpaka pale tunapo
wapatiliza kwa adhabu kali ya njaa au mauwaji hapa duniani huwa tena
wanababaika na kukata tamaa, hawaioni njia ya kuvuka.
78. Na yawaje mkamkufuri Mwenyezi Mungu na hali
ni Yeye ndiye aliye kuumbieni usikizi mkaisikia Haki, aliye kupena uwezo wa
kuona mkauona ulimwengu na viliomo ndani yake, na akakupeni akili mzingatie
kwayo utukufu wake mpate kuamini? Hakika nyinyi hamumshukuru Mwenye kuumba vyote
hivyo kwa Imani na ut'iifu ila kwa uchache tu, nao ni uchache mno!
79. Na Yeye ndiye aliye kuumbeni duniani, na
kwake Yeye peke yake ndio mtarejeshwa Siku ya Kiyama kwa ajili ya malipo.
80. Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na
kwa amri yake na sharia zake ndio usiku na mchana zinapitishana. Na
kukhitalifiana kwazo kwa urefu na ufupi, hamzingatii hiyo kuwa ni dalili
ya uwezo wake na kupasa kumuamini Yeye na kuamini kufufuliwa?
"Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye
mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu?" Aya zenye kutaja usiku na
mchana zimekuja mwahala mwingi katika Qur'ani tukufu, na haya yanaonyesha kuwa
Mwenyezi Mungu wa Haki, Aliye takasika na kutukuka, anawakumbusha waja wake kwa
Ishara hii ya uumbaji; na kwa kuwa yamo maana ya ndani inawapelekea wenye
kufikiri wazidi kuzingatia na kuchungua. Na kukhitalifiana usiku na mchana
kunatokana na pande mbili kubwa:
Kwanza: Kukhitalifiana kwa wakati,
urefu na ufupi. Na Pili: Kukhitalifiana kwa dhaahiri ya tabia na isiyo
onekana.
* Kwanza - Khitilafu kwa nyakati:
Mchana ni
kipindi cha wakati baina ya kudhihiri ncha ya jua na inapo potea upeo wa macho,
pale linapoonekana kwa jicho kama linagusa uso wa ardhi. Na ilivyo kuwa kwa
hakika pale pahali pake pa kuzama jua sipo hapo upeo wa macho, bali tunaona tu
hivyo kwa kuwa miale inayo tokana na jua inapinda inapo pita katika matabaka ya
anga mpaka inapo fikilia kwenye jicho la mtazamaji, na yeye akaliona jua kama
lipo huko upeo wa macho. Lilio kweli ni kuwa kuzama huku kuko chini kuliko
upeo wa macho kwa kadri ya dakika 35 kwa kipimo cha mduara.
Na Usiku
ni kipindi cha kutimiliza wakati wa mchana mpaka kitimilie kipindi cha mzunguko
wa ardhi juu ya nafsi yake kutoka magharibi kwendea mashariki. Na baina ya Usiku
na Mchana vipo vipindi viwili, navyo vya magharibi na mapambazuko. Na kipindi
cha mchana kinakhitalifiana kwa mujibu wa hali ya uwazi wa pahala na musimu wa
mwaka. Hali kadhaalika kipindi cha usiku kinakhitalifiana hivyo hivyo kwa
kufuatana haya. Na nyakati za Sala na Saumu zinawekwa kufuatana na matulio
ya jua huko upeo wa macho.
* Pili - Khitilafu katika yanayo dhihiri
katika tabia:
Na madhaahiri haya ni ya namna nyingi, na yanazalikana
kutokana na michanganyiko ya miale ya jua, inayo onekana na isiyo onekana, na
vitu vilio beba nguvu za umeme pamoja na vifuniko vya anga na nyuso za bahari na
majangwa n.k. Kadhaalika yapo mambo ya kuonekana kama kupatwa kwa jua na mwezi,
na nyota zenye kufanya mikia, nyota za dasturi na nyota ziendazo na mawingu
meupe, na nyota zinazo anguka, na ambazo hufumbwa na ukali wa anga la jua
kuonekana mchana, ilhali usiku huonekana wazi. Na muhimu kabisa katika
yanayo onekana kuwa ni khitilafu baina ya usiku na mchana ni huu mwangaza wa
mchana. Na sababu yake ni kuwa miale inayo toka kwenye jua inapo piga juu ya
funiko la anga, ambalo kwa hakika ni sehemu ndogo ndogo zenye chembe chembe
ndogo mno za vumbi, hizo hurejesha mwangaza na kuutawanya pande mbali mbali.
Ikiwa hali ya anga ni safi, na vile vichembe chembe vya vumbi ni vidogo sana, na
jua liko upeo wa macho, basi rangi inayo enea zaidi na inayo onekana kwa macho
zaidi, inakuwa ya kibuluu. Ama wakati wa kuchomoza jua au
kuchwa basi mbingu huonekana na rangi ya machungwa yenye kupiga wekundu,
na mwangu wa kibuluu unatawanyika. Nz kwa hivyo mbingu utosini huelekea kuwa
kibuluu khafifu.
Na wakati wa kuchwa jua tunaona rangi ya kijani
kiasi ya nukta moja hivi au akali pembezoni mwake. Huu huitwa mmetuko wa kijani,
na aghlabu yake huonekana unapo kuwa baharini, au nyuma ya kilele cha mlima, au
hata kwenye kuta za majumba. Na asli ya kuonekana hivi ni kwa ajili ya kugeuka
na kutawanyika miale ya jua hata ikatoa rangi mbali mbali katika hizo
kijani.
Mukhtasari wa haya ni kuwa miale ya jua ina rangi zinazo
onekana na zisizo onekana. Na zinakhitalifiana kwa urefu wa mawimbi yake na
kufuata kwake sifa hiyo. Kwa hivyo ndio tunaona kwa migongano hiyo mwangaza wa
mchana, mazigazi (sarabi), upinde wa mvua, na rangi za aina mbali mbali zinazo
zunguka jua, na mengineyo katika Ishara za mbinguni za ulimwengu tuuonao. Na
linapo potea jua jioni mbingu inaonekana kwa rangi mbali mbali kwa sababu ya
kuparaganyika mwangaza katika matabaka ya anga la juu. Na kila jua likiteremka
unapungua mwangaza wa jioni, na zinapungua zile rangi zake za tabia, mpaka
likifikilia daraja ya duara 18.5 mbingu inakuwa kiza. Na wataalamu wa nyakati
wameweka kuwa huu ndio wakati wa kuambiwa kuwa usiku umekuwa giza na kwa hivyo
ndio wakati wa kuadhinia Sala ya Isha. Na wakati huo khasa ndio huanza mwangaza
wa nyota kama sura ya mnara wa sukari na tako lake liko upeo wa magharibi. Na
hivyo huendelea katika masiku safi ya siku za baridi mpaka kilele cha ile "cone"
au "makhruut'" yaani sura ya mnara wa sukari kifikie utosini. Na kati kati
ya usiku hudhihiri rangi za kuchomoza jua kidogo kidogo wakati wa mapambazuko
kwanza kama kilele cha ile "cone" au "makhruut'" . Kilele chake hicho huzidi
kupanda , na tako lake hutanuka kwenye upeo wa mashariki mpaka inapo dhihiri
alfajiri, yaani linapo kuwa jua liko chini ya upeo wa macho wa mashariki kwa
kadri ya daraja 18.5 za duara. Na hapo ndio wakati wa kuadhiniwa Sala ya
Alfajiri. Na rangi za mapambazuko huanza kudhihiri kwa taratibu kinyume na zile
za kuchwea jua magharibi. Na imedhihiri karibuni kuwa jua lina kifuniko
chembamba kimetanda angani takriban kimekaribia kufunika anga lote la
ardhi. Kifuniko hichi chembemba ndicho kinacho sabibisha kuleta rangi mbali
mbali za katika anga.
Mambo haya mbali mbali ambayo tumeyataja kama
ni mifano isiyo na ukomo imetuonyesha vipi mbingu inavyo kuwa pindi ikiwa hapana
mawingu wala hapana pepo za mchanga. Kwani hapo tena huwa ni kiza. Na
ikiwa mawingu yamebeba matone ya maji ya mvua basi hayo hupambana na miale ya
jua, na hufanyika kama huo upinde wa mvua katika hali maalumu.
Na ikiwa mawingu yenyewe ni ya namna fulani ambayo yanabeba maji yaliyo
ganda (crystals) "kristali" zenye pande sita, basi maji hayo huingiana na miale
ya jua na hiyo miale huvunjika ndani ya hayo maji (kama mwaangaza upitavyo
katika kigae cha thuraya, "prism") kisha mwangaza huo ukatoka nje kwa rangi
mbali mbali. Na katika hali fulani fulani ndio hutokea rangi nzuri nzuri
kulizunguka jua. Na wakati wa weusi wa usiku utaziona nyota kama kwamba zipo
karibu nasi na kwa hakika hizo ziko mbali kwa masafa makubwa sana ya kukisiwa
kwa miaka na miaka ya mwendo wa mwanga. Vile vile tunaona katika anga hili nyota
na sayari na nyota mkia na vimondo kama kwamba zipo karibu, utadhani kuwa
khitilafu ya masafa imeondoka kabisa. Na haya ndiyo yanayo tupelekea tutambue
maana iliyo fichikana ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na tumeifanya mbingu
kama dari iliyo hifadhiwa; nao wamezipuuza Ishara zetu." Kama tulivyo kwisha
eleza kuwa juu ya miale inayo tokana na jua kuna miale inayo tokana na vitu
vingine vya eneo la jua vyenye nishat'i ya nguvu, na vyenye kubeba nguvu za
umeme. Kadhaalika inatokana na hizo miale iliyo juu ya zambarau Ultra Violet
Rays. Vitu hivi na miale hii inapambana na matabaka ya anga la juu, na
huathirika kwa mvuto wa smaku kuizunguka dunia. Kwa hivyo hulitibua anga la
kaskazini na kusini, na huleta kiza katika mbingu ya kaskaazini kama kwamba ni
pazia kuzuia mianga yenye rangi nzuri nzuri za kijani zenye kumili kwenye
wekundu na kibuluu. Sura hizi hubaki pengine muda wa saa kadhaa katika
mbingu ya kaskazini, na zaidi waweza kuziona masiku kadhaa wa kadhaa linapo kuwa
jua linashitadi. Mapazia haya si kama unayaona kaskazini tu, bali hata pia
katika kati kati ya dunia.
Na katika mbingu vipo vibebaji nguvu za
umeme katika mawingu na anga ambavyo huzalikana kutokana navyo radi na mimetuko
katika anga la juu. Mambo yote haya yanayo onekana ambayo tunayashuhudia
yanatupelekea tufahama maana ya ndani ya kauli yake Subhanahu wa Taa'la: "Hakika
katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi na kukhitalifana usiku na mchana pana Ishara
kwa wenye akili."
Kutokana na yaliyo pita kwa mambo ya dhaahiri ya
maumbile inabainikana kwamba haya yanakuwa kwa sababu ambazo
hayumkini mwanaadamu kuingilia ndani yake. Na hakika ni Mwenyezi
Mungu, Aliye tukuka shani yake, ndiye mwenye kuleta hizo khitilafu za usiku na
mchana, wala hawezi binaadamu kabisa siku yoyote kuweza kugeuza usiku wala
mchana. Na Yeye Mwenyezi Mungu Aliye tukuka shani yake ndiye anaye zifuatanisha
usiku na mchana kwa mizani madhubuti na vipimo baraabara, na anaendesha
siku zote mwaka ingia mwaka toka.
81. Hawakuzingatia hayo, bali waliwafuata
wakanushaji walio kwisha tangulia, wakasema kama walivyo sema hao.
82. Katika kukanusha kwao kufufuliwa, walisema:
Hivyo sisi tutafufuliwa baada ya kwisha geuka mchanga na mifupa?
83. Sisi tuliahidiwa haya, na pia baba zetu
waliahidiwa hayo hayo hapo zamani. Haya si chochote ila ni ahadi za uwongo
walizo buni watu wa zamani.
84.. Ewe Muhammad! Waambie: Ni nani aliye
imiliki ardhi na viliomo ndani yake, tangu watu mpaka viumbe vyote? Kama nyinyi
mna ujuzi nijibuni.
85. Watakiri kuwa ardhi ni ya Mwenyezi Mungu.
Basi hapo tena waambie: Hamkumbuki kuwa Mwenye kumiliki hayo ndiye anaye faa
kuabudiwa peke yake?
86. Waambie tena: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu
saba na Mola Mlezi wa A'rshi Kuu? (Kiti Kikuu cha Enzi)
87. Watakiri kuwa huyo ni Mwenyezi Mungu. Basi
waambie: Je! Hamwogopi matokeo ya ushirikina wenu na ukafiri wenu na
kumuasi kwenu Mwenye uumbaji huu wote mkubwa?
88. Waambie vile vile: Nani mwenye ufalme wa
kila kitu mkononi mwake, na mwenye madaraka yasio na ukomo katika kila kitu, na
ambaye ndiye kwa uwezo wake analinda kila kitu, wala hayamkiniki yeyote
kumlinda yeyote na adhabu yake? Kama nyinyi mnaijua jawabu, basi nijibuni.
89. Watakiri kuwa hakika huyo ni Mwenyezi Mungu.
Waambie: Basi huwaje mkadanganyika kwa pumbao na kuchochewa na
mashetani, na mkaacha ut'iifu wa Mwenyezi Mungu?
90. Hakika Sisi tumewabainishia Haki kwa ndimi
za Mitume, na wao ni waongo katika kila jambo linalo khitalifu na Haki
hii.
91. Mwenyezi Mungu hakumchukua yeyote kuwa ni
mwanawe. Yeye ametakasikia na hayo. Wala hana mshirika. Angeli kuwa na mshirika
basi kila mmoja wao angejipa madaraka ya pekee kwa alivyo viumba, na vikawa ndio
milki yake, na wangeli gombana wenyewe kwa wenyewe kama wanavyo onekana wafalme
wanavyo fanya. Na ulimwengu ungeli fisidika kwa mizozano hiyo. Basi Mwenyezi
Mungu ametakasika na hayo wayasemayo washirikina yanayo kwenda kinyume na Haki.
92. Na Yeye amevizunguka vitu vyote kwa
kuvijua. Anajua tusiyo yaona na tunayo yaona. Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo
wanayo mnasibisha nayo makafiri kuwa ati ana washirika.
93. Ewe Nabii! Sema: Ukiwateremshia adhabu ulio
waahidi hapa duniani nami nipo pamoja nao,
94. Basi nakuomba usinifanye mwenye
kuadhibiwa pamoja na makafiri waasi.
95. Na Sisi tunaweza kwa utimilivu kukuonyesha
adhabu tulio waahidi ikiwateremkia. Basi wewe tuwa ujue kuwa tutashinda.
96. Wewe endelea na wito wako, na ukabili uovu
wao kwa vitendo vilivyo vizuri kama kusamehe au vyenginevyo. Na Sisi tunajua
vyema wanakutaja vipi wewe, na wanavyo usema kwa ubaya huo wito wako kwa uwovu
na uzushi. Na Sisi tutawalipa kwa hayo.
97. Nawe sema: Ewe Mola Mlezi! Najilinda kwako
na wasiwasi wa mashetani wasiniingilie katika nafsi yangu kwa vitendo visio
kupendeza.
98. Na ewe Mola Mlezi! Najilinda kwako wasiwe
nami katika kitendo chochote ili kitendo hicho kiwe
kimetakasika, safi, kwa ajili ya ridhaa yako tukufu.
99. Wanaendelea kuwakanusha mpaka utapo fika
wakati wa kufa mmoja wao hujuta na akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nirudishe
duniani.
100. Ili nipate kufanya a'mali njema katika
mali au wakati nilio acha. Wala ombi lake halitokubaliwa. Kwani haya ni maneno
anayasema bila ya faida, hayakubaliwi. Na pindi akikubaliwa hatotenda kitu. Na
juu ya yote hatorudi kabisa! Kwani mauti ni kizuizi baina yao na hayo wanayo
yatamani mpaka Mwenyezi Mungu atapo wafufua.
101. Ukifika wakati wa kufufuliwa
tutawafufua kutoka makaburini kwao. Na hayo ni kwa mfano wa kupulizwa tarumbeta
watafufuka nao wamefarikiana. Hapana mtu utaomfaa ujamaa wake na fulani. (Ujamaa
Kiswahili maana yake makhusiano ya nasaba, sio usoshalisti.) Wala hapana mtu
atae muomba mtu kitu cha kumfaa. Kwani kila mmoja wao siku hiyo atakuwa
kashughulika na lake.
102. A'mali (Vitendo) ndio mizani ya kupimia.
Mwenye Imani nzuri na vitendo vyema atakuwa na uzito katika mizani ya Mwenyezi
Mungu. Hao ndio walio fuzu.
103. Na asiye kuwa na thawabu au vitendo vyenye
uzito mbele ya Mwenyezi Mungu, hao ndio walio zikhasiri nafsi zao kwa kuziuza
kwa Shetani. Nao wataadhibiwa Motoni, wadumu humo.
104. Moto utawababua nyuso zao, nazo zitakuwa
zimekunjana kwa uwovu wa mwisho wao.
105. Mwenyezi Mungu anawakemea na anawaambia:
Aya zangu zilizo kuwa zinateremshwa zilikuwa mkisomewa duniani, nanyi
mkizikadhibisha.
106. Watasema nao wanakiri makosa yao :
Ewe Mola wetu Mlezi! Maasi yetu yalikuwa mengi, ndio yakatupatia mashaka, na
tukawa wenye kupotea tukaiacha njia ya sawa.
107. Na watasema: Mola wetu Mlezi! Tutoe Motoni
na uturejeshe duniani. Basi tukirudi tena kwenye ukafiri na uasi basi tutakuwa
kweli ni twenye kujidhulumu nafsi zetu.
108. Na Mwenyezi Mungu atawaambia kwa
kuwadharau na kuwabeza: Kaeni humo kwa madhila na unyonge, wala msiseme nami
kabisa!
109. Mimi sikukudhulumuni, bali nyinyi
mmejidhulumu wenyewe. Kwani Waumini wema katika waja wangu walikuwa wakisema
duniani: Ewe Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tughufirie na uturehemu. Na Wewe
ndiwe Mbora wa wanao rehemu.
110. Na nyinyi daima mlikuwa mkiwafanyia
maskhara, mpaka maskhara yenu yakakusahaulisheni kunikumbuka Mimi na kuniabudu
Mimi. Basi hamkuamini wala hamkut'ii. Nanyi mlikuwa mkiwacheka kwa kejeli.
111. Hakika Mimi hii leo nimewalipa wao kwa
mafanikio, kwa kuwa waliyavumilia maskhara yenu na maudhi yenu.
112. Mwenyezi Mungu atawaambia makafiri:
Mliishi miaka mingapi huko duniani?
113. Watasema kwa kuyaona mafupi maisha yao kwa
adhabu wanayo ikuta: Tuliishi muda wa siku moja au baadhi ya siku hivi. Basi
waulize wanao weza kuhisabu, sisi tumeshughulishwa na hii adhabu.
114. Basi Mwenyezi Mungu atawaambia: Hamkuishi
duniani ila muda mchache tu. Na lau ingeli kuwa mnajua malipo ya ukafiri na uasi
na kwamba starehe ya duniani ni chache mngeli amini na mkat'ii.
115. Je! Mlidhani kuwa tulikuumbeni bila ya
hikima ndio mkafanya ufisadi katika ardhi, na mkadhani kuwa hamtafufuliwa mpate
kulipwa?
116. Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Na
Yeye ndiye Mwenye kumiliki ufalme wote. Hapana Mwenye kuabudiwa kwa Haki isipo
kuwa Yeye. Na Yeye ndiye Mwenye A'rshi Tukufu.
117. Na mwenye kumuabudu mungu mwengine pamoja
na Mwenyezi Mungu hana ushahidi wa kumfanya huyo astahiki kuabudiwa. Hakika
Mwenyezi Mungu atampa adhabu kwa ushirikina wake bila ya shaka yoyote. Hakika
makafiri hawaongokewi. Bali watao ongokewa ni Waumini.
118. Na sema, ewe Nabii, ukimlingania Mwenyezi
Mungu na kumnyenyekea: Ewe Mola wangu Mlezi! Nisamehe dhambi zangu, na nirehemu.
Kwani Wewe ni Mbora wa wanao rehemu, kwa sababu rehema yako imeenea na ipo
karibu kwa watendao mema.