1. Enyi watu! Tahadharini na adhabu ya Mola
wenu Mlezi, na wekeni katika nyoyo zenu makumbusho ya Siku ya Kiyama. Kwani
mtingishiko utao tokea hapo ni mkubwa, wenye kuhangaisha na kutikisa viumbe.
2. Siku mtapo kiona Kiyama mtaona kitisho chake
kinafikilia ukubwa wake hata kama yupo mwanamke anaye nyonyesha na ziwa lake
limo katika mdomo wa mwanawe, basi hapana shaka atamsahau na amwachilie mbali.
Na kama yupo mwanamke ana mimba basi ataiharibu mimba kabla ya kufika wakati
wake wa kuzaa kwa ajili ya fazaa na kitisho. Na ewe mwenye kuangalia! Ukiona
hali ya watu Siku hiyo namna wanavyo onekana hawanazo, na wanapo kwenda
wanayumba, utadhani wamelewa, na ilhali hawakulewa. Lakini kitisho walicho
kishuhudia, na khofu ya adhabu kuu ya Mwenyezi Mungu ndiyo iliyo waondoshea
utulivu wao.
3. Na juu ya onyo hili kali na la kweli bado wapo
baadhi ya watu inadi yao au kufuata kwao kijinga huwapelekea katika mambo ya
kubishana juu ya Mwenyezi Mungu na sifa zake, wakamsingizia kuwa ati ana
washirika, au wakaukataa uweza wake wa kufufua na kuwalipa watu kwa vitendo
vyao. Na kwa huo ubishi wao na kukataa kwao hawategemei ilimu sahihi, au hoja ya
kweli; lakini wao hufuata tu nyayo za kila shetani aliye muasi Mola wake Mlezi,
aliye baidika na uwongofu.
4. Mwenyezi Mungu amehukumu kuwa anaye mfuata
Shetani na akamfanya kuwa ni rafiki yake na mlinzi wake, na mwongozi wake, basi
humpotoa na njia ya Haki, na akamuelekeza kwenye upotovu unao pelekea kwenye
Moto unao waka na kuripuka.
5. Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya
kukufufueni baada ya kufa, basi katika kuumbwa kwenu ipo dalili ya kuweza kwetu
kufufua. Tulikuumbeni asili yenu kutokana na udongo, kisha tukaufanya tone ya
manii, kisha baada ya muda tukaigeuza ikawa kipande cha damu iliyo
gandana.(1) Kisha tukaifanya kipande cha nyama yenye sura ya kibinaadamu,
au isiyo kuwa na sura, ili tukubainishieni uweza wetu wa kuanza uumbaji na
kuendeleza kukuza kwa viwango na madaraja, na kugeuza kutoka hali hii na kuingia
nyengine. Na katika viliomo katika matumbo ya mzazi vipo tunavyo viharibu
tuvitakavyo na tunaviweka imara na madhubuti tuvitakavyo, mpaka utimie
muda wa kuzaliwa. Kisha tunakutoeni kwenye matumbo ya mama zenu muwe
watoto wachanga. Kisha tunakuleeni mpaka mkamilike akili na nguvu. Na baada ya
hayo wapo katika nyinyi ambao Mwenyezi Mungu huwafisha, na wapo ambao umri wao
hurefushwa mpaka wakafikia ukongwe wa kupiswa, ujuzi wao na kufahamu kwao mambo
kukasita. Na aliye kuumbeni kwa sura hii tangu mwanzo hashindwi kukurudisheni
tena. Na jambo jengine la kukuonyesha kudra ya Mwenezi Mungu kufufua ni kuwa
wewe unaiona ardhi kavu yabisi; tukiiteremshia maji uhai unaitambalia, na hiyo
ardhi hugutuka, na huzidi na hututumka kwa maji na hewa iliyo ingia ndani yake,
na hapo tena hutokeza namna mbali mbali za mimea inayo furahisha kuiona, na
uzuri wake ukazagaa, na mwenye kuiona roho yake ikakunjuka.
(1)(Maurice Bucaille, mtaalamu wa Kifaransa maarufu aliye silimu,
amelifasiri neno A'laqa kwa maana ya "kitu kilicho tundikwa". Na hivyo ndivyo
inavyo thibitisha Sayansi ya hivi sasa, kuwa mbegu ya uzazi ikisha pandikizwa
huja ikaning'inia kama iliyo tundikwa kwenye tumbo la uzazi. Tazama
pia 23.14, 40.67, 75.37-38 na kadhaalika Sura ya 5 ya Annisaa Aya 129,
inayo eleza kuwa msimwache mke "kama aliye tundikwa")
6, 7. Hayo yaliyo tangulia ya kuumbwa
binaadamu, na mimea ya kupanda, ni ushahidi ya kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu
ndiye Mungu wa Haki. Na kwamba hakika Yeye ndiye anaye huisha maiti wakati wa
kufufuliwa kama vile alivyo anza kuwaumba. Na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa
kila kitu, na kwamba hakika Kiyama kinakuja tu bila ya shaka kuhakikisha ahadi
yake. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawahuisha waliomo makaburini kwa
kuwafufua kwa ajili ya hisabu na malipo.
8. Na juu ya yaliyo tangulia bado wapo baadhi ya
watu wanao jadili juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu, na wanakanya kufufuka bila ya
msingi wowote wa ki-ilimu, wala uwongozi wa kweli, au Kitabu kilicho toka kwa
Mwenyezi Mungu cha kumwonyesha. Basi ubishi wake ni wa pumbao na inda tu.
9. Na pamoja na hayo hugeuka upande kwa kiburi na
kukataa kuikubali Haki. Na watu wa namna hii itakuja wapata hizaya na udhalili
duniani kwa ushindi wa Neno la Haki, na Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu
atawaadhibu kwa Moto wa kuunguza.
10. Na ataambiwa: Hayo unayo yapata ya hizaya na
adhabu ni kwa sababu ya uzushi wako na kiburi chako; kwani hakika Mwenyezi Mungu
ni Muadilifu, hadhulumu. Wala hawaweki sawa Muumini na kafiri, na mwema na
muovu; bali kila mmoja wao atamlipa kwa mujibu wa vitendo vyake.
11. Na miongoni mwa watu wapo wa namna ya
tatu, ambao Imani bado haijatulia katika nyoyo zao, bali itikadi yao inayumba
yumba. Maslaha ya nafsi zao ndiyo yanatawala katika Imani yao. Wakipata kheri
hufurahi na hutulizana. Na wakipata shida yoyote katika nafsi zao, au mali zao,
au wana wao, hurejea ukafirini. Hao huwa wamekosa duniani raha ya utulivu kwa
hukumu ya Mwenyezi Mungu na nusura yake, kama Akhera walivyo kosa neema ambayo
Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini walio thibiti na wakasubiri. Hiyo khasara ya
mara mbili ndiyo khasara ya kweli kweli iliyo wazi.
12. Mwenye kukhasiri hivi humuacha Mwenyezi
Mungu na akayaabudu masanamu yasiyo weza kumdhuru pindi akito yaabudu, wala
hayamfai kitu pindi akiyaabudu. Kitendo chake huyo ndio kupotelea mbali na haki
na uwongofu.
13. Badala ya Mwenyezi Mungu anamwomba ambaye
madhara yake kwa kuharibu akili na kutawala mawazo ovyo ni karibu zaidi kwa
nafsi kuliko kuitakidi msaada wake. Muabudiwa huyo ni muovu mno wa kumtaraji
msaada, na muovu mno kumfanya rafiki.
14. Hakika wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na
Mitume wake kwa Imani yenye kuambatana na vitendo vyema, Mola wao Mlezi atawatia
Siku ya Kiyama katika Bustani zipitwazo chini ya miti yake na mito. Hakika
Mwenyezi Mungu hutenda apendavyo kumuadhibu mharibifu na kumlipa mema mtenda
mema.
15. Ikiwa miongoni mwa makafiri yupo anaye dhani
kwamba Mwenyezi Mungu hatamsaidia Nabii wake, basi na anyooshe kamba mpaka
kwenye dari ya nyumba yake. Kisha ajinyonge, na akadirie katika nafsi yake na
atazame, je, kitendo chake hicho kitaondoa hayo yanayo muudhi ya kuwa Mwenyezi
Mungu anamnusuru Mtume wake?
16. Mfano wa tulivyo bainisha hoja zetu zi wazi
katika tuliyo kwisha wateremshia Mitume. Tumemteremshia Muhammad Qur'ani yote,
nayo ni Aya zilizo wazi ili ziwe ni hoja juu ya watu. Na hakika Mwenyezi Mungu
humuongoa amtakaye kuwaongoa ili isalimike tabia yake na abaidike mbali na inadi
na yanayo sabibisha hayo.
17. Hakika wanao muamini Mwenyezi Mungu na
Mitume wake wote, na Mayahudi wanao nasibika na Musa, na waabuduo nyota na
Malaika, na Wakristo wanao nasibika na Isa, na Majusi wanao abudu moto, na
washirikina wanao abudu masanamu..hakika wote hawa Mwenyezi Mungu atakuja
wapambanua mbali mbali Siku ya Kiyama kwa kumdhihirisha mwenye haki na aliye
potea kati yao. Kwani Yeye anajua vyema vitendo vyote vya viumbe vyake. Na
atawalipa kwa vitendo vyao.
18. Ewe mwenye akili! Hujui kwamba hakika
Mwenyezi Mungu vinamnyenyekea na kumt'ii vyote viliomo mbinguni na katika ardhi,
na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi katika watu
wanamuamini Mwenyezi Mungu na wanafuata maamrisho yake, na kwa hivyo wanastahiki
Pepo? Na wapo wengi miongoni mwao wanao puuza na wala hawamuamini, wala
hawayatendi maamrisho yake, na kwa hivyo wanastahiki adhabu na hizaya. Na anaye
fukuzwa na Mwenyezi Mungu kutokana na rehema yake basi hawezi yeyote kumhishimu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. Kwani Yeye hutenda ayapendayo.
19. Haya ni makundi mawili walio zozana kwa
mambo yaliyo mkhusu Mola wao Mlezi, na yanayo mstahiki na yasio mstahiki.
Kikundi kimoja kikamuamini na kikundi kingine kikakataa. Basi wale walio kataa
na kukufuru Mwenyezi Mungu amewaandalia Siku ya Kiyama moto utao wazunguka na
kuwapamba kila upande, kama nguo inavyo upamba mwili. Na kuzidi kuwaadhibu
Malaika watawamiminia maji ya moto mno juu ya vichwa vyao!
20. Yatawapenya mpaka kwenye matumbo yao,
viliomo ndani viyayuke kama zitavyo yayuka ngozi zao!
21. Na pia wataandaliwa marungu ya chuma.
22. Kila wakijaribu kutoka Motoni kwa wingi wa
machungu na dhiki Malaika watawapiga nayo hayo marungu, na watarudishwa huko
huko waliko kuwako. Na watawaambia: Onjeni adhabu ya Moto unao unguza kuwa ni
malipo ya ukafiri wenu.
23. Ama walio amini na wakatenda vitendo vyema,
hao bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaingiza kwenye Mabustani yanayo pita mito
kati ya majumba yake na miti yake. Humo watastarehe kwa kila namna ya starehe,
na Malaika watawapamba vikuku vya mikono vya dhahabu na watawapamba kwa lulu.
Ama nguo zao za kawaida zitakuwa za hariri.
24. Na ziada ya starehe yao humo Peponi ni kuwa
Mwenyezi Mungu atawajaalia wawe na kauli njema, na vitendo vizuri vya kusifika.
Basi watakuwa wakimtakasa Mwenyezi Mungu na kumtukuza, na watakuwa wenyewe kwa
wenyewe wakiamiliana kwa mapenzi na amani.
25. Hakika wale walio kufuru, yaani walio mkataa
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na pamoja na hayo wakawa mtindo wao kuwazuia watu
wasiingie katika Uislamu, na kuwafanyia pingamizi Waumini kuingia kwenye Msikiti
Mtakatifu wa Makka - na ilhali Mwenyezi Mungu ameufanya huo ni pahala pa amani
kwa watu wote, mkaazi na mpita njia - atawapa watu hao adhabu kali. Na hali
kadhaalika kila atakaye kengeuka na Haki, na akatenda udhalimu wowote katika
pahala patakatifu, Mwenyezi Mungu atamuadhibu adhabu ya kutia uchungu.
26. Ewe Nabii! Watajie hawa washirikina wanao
dai kuwa ati wanamfuata Ibrahim a.s. na wakaifanya Nyumba Takatifu kuwa ni
pahala pa kuwekea masanamu yao; watajie kisa cha Ibrahim na Nyumba Takatifu
tulipo mwongoza mpaka pahala pake, na tukamuamrisha aijenge, na
tukamwambia: Usinishirikishe Mimi na kitu chochote katika ibada. Na isafishe
Nyumba yangu na masanamu na uchafu, ili iwe ni pahala pa makusudi ya mwenye
kuizunguka kwa kut'ufu, na mwenye kukaa hapo na akafanya ibada.
27. Ewe Nabii! Wajuvye watu kwamba hakika
Mwenyezi Mungu amewalazimisha wawezao miongoni mwao waijie hii Nyumba. Basi
waitikie wito wako, watakujia kwa miguu na kwa kupanda ngamia aliye konda kwa
ajili ya safari ya kutoka mbali.
28. Ili wapate manufaa yao ya Kidini kwa
kutekeleza Hija na manufaa ya kiduniani kwa kujuana na ndugu zao Waislamu na
kushauriana nao katika mambo ya Dini yao na dunia yao. Nao wataje jina la
Mwenyezi Mungu katika Siku ya Idi Kubwa na siku tatu zifwatazo, pale wanapo
chinja walio jaaliwa, ikiwa ngamia, au ng'ombe au kondoo na mbuzi. Kuleni
mpendacho katika hao, na muwalishe walio patwa na shida na ufakiri.
29. Tena baada ya hao yawapasa waondoe takataka
na uchafu ulio wapata wakati ule wa Ih'ram (yaani kuharimia Hija), nao ni
majasho na safari ndefu. Pia waondoe nadhiri walizo mwekea Mwenyezi Mungu, ikiwa
wameweka nadhiri yoyote. Na waizunguke kwa kwenda kwa miguu ile Nyumba iliyo
jengwa kwa ajili ya ibada ya Mwenyezi Mungu duniani.
30. Na mwenye kuzishika amri za Mwenyezi Mungu
na makatazo yake katika Hija yake kwa kuzitukuza katika nafsi yake, hayo
yatakuwa ni kheri yake katika dunia yake na Akhera yake. Na Mwenyezi Mungu
amekuhalalishieni kula nyama hoa, (mifugo) yaani ngamia, ng'ombe, kondoo na
mbuzi, ila katika hali mnazo zijua kwa mlivyo kwisha somewa katika Qur'ani, kama
vile nyamafu na nyenginezo. Basi epukaneni na kuabudu masanamu, kwani ibada hiyo
ni uchafu wa kiakili na kiroho, na haimwelekei mwanaadamu kufanya hivyo. Na
epukaneni na kusema uwongo, kumzulia Mwenyezi Mungu au mwanaadamu.
31. Na kuweni wenye kumsafia niya Mwenyezi
Mungu, wenye pupa kutaka kuifuata Haki, bila ya kumfuata mshirika wowote na
Mwenyezi Mungu katika ibada. Kwani mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu ameanguka
huyo kutoka kwenye ngome ya Imani, na amesalitiwa na upotovu, na ameitia nafsi
yake katika hilaki ya kutisha kabisa. Ikawa hali yake kama hali ya mtu aliye
poromoka kutoka mbinguni na midege ikamrarua akakatika mapande mapande, asibakie
hata alama. Au kama aliye peperushwa na upepo mkali, na mwili ukatawanyika
mwahala mbali mbali.
32. Hakika mwenye kuitukuza Dini ya Mwenyezi
Mungu na faridha ya Hija na a'mali zake na mihanga inayo pelekwa kwa ajili
mafakiri wa Al-Haram, na wakachagua walio nona wazima, hawana ila, basi huyo
ndio amemcha Mwenyezi Mungu. Kwani kutukuza kwake hayo ni matokeo ya unyenyekevu
wa nyoyo zilizo amini, na alama katika alama za usafi wa niya.
33. Katika kutoa mihanga hii yapo manufaa ya
kidunia. Mnawapanda na mnakunywa maziwa yake mpaka wakati wa kuwachinja. Kisha
mnapata manufaa ya Kidini vile vile pale mnapo wachinja kwenye Nyumba Takatifu
kwa kutafuta kujikaribisha kwa Mwenyezi Mungu.
34. Hizi faridha za Hija hazikukhusuni nyinyi
peke yenu. Kwani tumewajaalia jamaa wote walio amini mambo ya kuwakaribisha kwa
Mwenyezi Mungu, na wanataja jina lake, na wanamtukuza wakati wanapo chinja kwa
kumshukuru kwa neema aliyo waneemesha, na kuwasahilishia wanyama wa mifugo, nao
ni ngamia, ng'ombe, mbuzi na kondoo. Na Mwenyezi Mungu aliye kuwekeeni sharia
nyinyi na wao ni Mungu Mmoja. Basi yasalimisheni mambo yenu yote kwake Yeye peke
yake. Na vitendo vyenu visafisheni kwake, wala msimshirikishe na yeyote. Na ewe
Nabii! Wape bishara ya Pepo na thawabu nyingi wale walio safisha niya zao kwa
Mwenyezi Mungu na wakawa wanamnyenyekea Yeye miongoni mwa waja wake,
35. Wale ambao akitajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao
hupapatika kwa kumkhofu, na hunyenyekea kwa kutajwa kwake, na ambao wanasubiri
kwa masaibu ya karaha na shida yanayo wapata kwa kujisalimisha mbele ya amri
yake na hukumu yake, na wakashika Sala kwa ukamilifu wake, na wakatoa baadhi ya
mali aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu katika njia za kheri.
36. Nasi tumefanya uchinjaji ngamia na ng'ombe
n.k. katika Hija kuwa ni katika matukuzo ya Dini yalio dhaahiri. Na nyinyi kwa
hayo mnajileta karibu na watu. Nanyi katika hao mnapata kheri nyingi katika
dunia kwa kuwapanda, na kunywa maziwa yake. Na Akhera mnapata malipo na thawabu
kwa kuwachinja na kuwalisha mafakiri. Basi tajeni jina la Mwenyezi Mungu wakati
mnapo wapanga kwa safu kwa ajili ya kuwachinja. Mkisha wachinja kuleni sehemu
mkitaka, na walisheni mafakiri walio kinai hawaombi, na ambao wanalazimika
kuomba kwa haja. Na kama tulivyo fanya kila kitu kiwe kit'iifu kwa tuyatakayo
kwa ajili ya manufaa yenu, na tumedhalilisha hivyo vikut'iini nyinyi ili mpate
kuishukuru neema yetu kubwa iliyo juu yenu.
37. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu haangalii
sura zenu wala vitendo vyenu, lakini anaangalia nyoyo zenu. Wala hataki kwenu
mambo ya kujionyesha tu kwa kuchinja na kumwaga damu. Lakini anataka kwenu moyo
wenye kunyenyekea. Basi hapati radhi yake mwenye kugawa hizo nyama wala damu.
Lakini linalo pata radhi yake ni uchamngu wenu na usafi wa niya zenu.
Kuwadhalilisha hao wanyama tulivyo wadhalilisha ni kwa ajili ya kukunafiisheni,
mpate kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa vile alivyo kuongoeni hata mkatimiza ibada za
Hija. Na ewe Nabii! Wape khabari njema watu wema walio tengeneza a'mali zao na
niya zao kuwa watapata malipo makuu.
38. Hakika Mwenyezi Mungu huwalinda Waumini na
huwahami na huwanusuru kwa Imani yao. Kwani Yeye hawapendi wenye kukhuni dhamana
zao, wenye kupita mipaka katika ukafiri wao kumkataa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi
Mungu hamsaidii yule asiye mpenda.
39. Mwenyezi Mungu amewaruhusu Waumini wanao
pigwa vita na washirikina wawarejezee uadui wao, kwa sababu ya dhulma iliyo
wapata nao wakasubiri kwa muda mrefu. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuweza
kuwanusuru vipenzi vyake Waumini.
" Wameruhusiwa kupigana wale
wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni
Muweza wa kuwasaidia" Yaliyo tajwa na Qur'ani Tukufu kukhusu hukumu iliomo
katika Aya 39 yamezitangulia kanuni zilizo kuja kuwekwa na madola baada yake,
nayo ni kuwa mtu kujitetea nafsi yake ni sharia vyovyote vile itavyo kuwa
matokeo yake. Na kwamba mwenye kuitetea nafsi yake, na mali yake, na nchi yake,
hawi ni mkosa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya uadilifu, ijapo kuwa ameuwa
mtu au ameteketeza roho nyingi. Aya hii imepasisha kuwa Waislamu wanayo ruhusa
kujitetea pindi wakivamiwa. Na kwa hivyo tunafahamu kuwa vita vya Waislamu
vilikuwa vita vya utetezi na kujilinda si vita vya kushambulia na kuvamia. Na
kwamba Waislamu waliusimamisha Uislamu na wakaupa nguvu kwa hoja zilizo wazi, na
dalili zilizo dhaahiri.
40. Hao ambao makafiri wamewadhulumu na
wakawalazimisha waache mji wao wa Makka wauhame. Na wao hawakuwa na kosa lolote
ila ni kuwa walimjua Mwenyezi Mungu na wakamuabudu Yeye pekee. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu hakuwatumilia kwa ajili ya Haki wasaidizi wa kumnusuru Yeye na
wakamtetea kupinga jeuri za madhaalimu, basi hapana shaka upotovu ungeli enea,
na majeuri wangeli endelea katika jeuri zao, na sauti ya haki wangeli
inyamazisha. Wala wasingeli achiliwa Wakristo makanisa yao, wala mamonaki
(wat'awa wa Kikristo) wasinge baki na monastari zao (nyumba zao za ibada), wala
Mayahudi wansinge kuwa na masinagogi yao, wala Waislamu wasinge kuwa na misikiti
yao, ambamo mote humo hutajwa kwa wingi jina la Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu amechukua juu ya nafsi yake ahadi ya nguvu ya kwamba atamsaidia
na kumnusuru kila anaye isaidia Dini yake, na atamtukuza kila mwenye kulitukuza
Neno la Haki katika ulimwengu. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu haiendi kinyume. Kwani
Yeye ni Mwenye nguvu wa kutimiza alitakalo, Mtukufu hashindwi na yeyote.
41. Hao Waumini tulio waahidi kuwanusuru ndio
hao ambao tukiwapa madaraka katika nchi wanalinda makhusiano yao na Mwenyezi
Mungu na pia na wanaadamu wenzao. Kwa hivyo hushika Sala kwa utimilifu wake, na
huwapa Zaka wanao stahiki kupewa, na huamrisha kila lenye kheri, na hukataza
kila lenye shari. Na mambo yote hurejea kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Basi Yeye
humtukuza amtakaye, na humdhalilisha amtakaye.
42. Ewe Nabii! Ukiwa unapata makanusho, kuambiwa
mwongo, na maudhi kutokana na watu wako, basi usisikitike. Zingatia taarikh kwa
yaliyo wapata Mitume wa kabla yako, utaona kwamba wewe si Mtume wa kwanza aliye
kanushwa na kuudhiwa na watu wake. Kwani kabla ya hawa walio kukanusha wewe,
kaumu Nuhu walimkadhibisha Mtume wao Nuhu, na kaumu ya A'ad walimkadhibisha
Mtume wao Huud, na kina Thamud walimkanusha Mtume wao Saleh.
43. Na kaumu ya Ibrahim walimkanusha Mtume wao
Ibrahim, na kaumu Lut'i walimfanyia hayo hayo Mtume wao Lut'i.
44. Na watu wa Madiana walimkanusha Mtume wao
Shua'ib. Na Firauni na watu wake walimkanusha Mtume wa Mwenyezi Mungu Musa.
Mitume hao wote yaliwapata yanayo kupata wewe. Na Mimi niliwapa muhula hao
wakanushao ili wapate kutubia waongoke, na waitikie Wito wa Haki. Lakini wakazua
na wakaendelea na kuwakadhibisha Mitume wao na kuwaudhi. Wakazidisha madhambi
juu ya madhambi yao. Basi nikawaadhibu ukomo wa kuwaadhibu. Angalia taarikhi yao
utaona kuwa adhabu yangu ilikuwa kali mno, pale nilipo ibadilisha neema ikawa
nakama, na uzima ukawa ni maangamizo, na badala ya ujenzi ukawa uharibifu.
45. Basi tuliwatekeza watu wengi wa miji ambayo
waliiamirisha, kwa sababu ya udhalimu wao na kukanusha kwao Mitume wao. Zikawa
paa za nyumba zao zimeangukia kuta zake, hazina wakaazi. Kama kwamba jana
hazikuwapo. Visima vingapi vilivyo bomoka na maji yake yakapotea, na majumba
mangapi madhubuti yaliyo jengwa kwa mawe na saruji na chokaa, yamekuwa magofu
hayana wakaazi!
46. Hivyo wao wanasema wayasemayo na wanahimiza
waletewe adhabu, nao hawatembei ulimwenguni wakaona kwa macho yao walivyo
teketea hao madhaalimu wakanushao? Huenda hapo nyoyo zao zikagutuka kutokana na
ghafla iliyo wapamba, na wakatia akilini yanao wapasa wakafuata hayo ya wito wa
Haki unao waitia. Na masikio yao yakisikia vifo vya hao makafiri huenda wao
wakazingatia. Lakini wapi! Ya mbali hayo kuwa watu hawa waweze kuzingatia kwa
wanayo yaona au kuyasikia maadamu nyoyo zao zimekuwa kama mawe. Kwani kipofu wa
kweli siye yule aliye pofuka macho, lakini ni yule aliye pofuka moyo na hatambui
kitu.
47. Na makafiri wa Makka wameshikwa na
udanganyifu, na hawana wanalo litambua juu ya kuwepo dalili zote hizi. Kwa hivyo
ndio wanakuhimiza, wewe Nabii, uwaletee adhabu ulio waahidi. Wanasema hayo kwa
upinzani na kejeli. Na hayo hapana shaka yoyote yatawapata, lakini kwa wakati
alio uweka Mwenyezi Mungu, ama duniani au Akhera. Naye hendi kinyume na ahadi
yake, hata ikipita miaka. Kwani siku moja kwake ni kama miaka elfu mnayo
ikadiria na kuihisabu.
"Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini
Mwenyezi Mungu hatakwenda kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku
moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi." Qur'ani kwa
Aya hii tukufu imeutangulia msafara wa wana sayansi kwa kueleza kuwa zama ni
kipimo cha mnasaba, na kwamba fikra ya kuwa zama kwa ulimwengu ni moja kama watu
wa zamani walivyo kuwa wakifikiri ni makosa.
48. Na wengi katika watu wa mijini walikuwa
madhaalimu kama wao. Nami nikawapa muhula wala sikuwafanyia haraka kuwaadhibu.
Na kisha nikawateremshia hiyo adhabu. Na ni kwangu Mimi tu ndio marejeo ya wote
Siku ya Kiyama; na hapo nitawalipa kwa wanayo stahiki. Basi enyi makafiri!
Msighurike kwa kuchelewa adhabu kukufikieni.
49. Ewe Nabii! Waambie hao wanao kanusha, wanao
kuhimiza waletewe adhabu: Sio kazi yangu mimi kukulipeni kwa vitendo vyenu. Bali
hakika mimi ni mwenye kukuhadharisheni kwa hadhari iliyo wazi kwamba kuna
adhabu. Na Mwenyezi Mungu ndiye wa kukuhisabuni na kukulipeni.
50. Na wale walio muamini Mwenyezi Mungu na
Mtume wake, na wakatenda vitendo vyema, watapata kutokana na Mwenyezi Mungu
kusamehewa dhambi zao walizo ziingia, kama kadhaalika watavyo pata riziki ya
ukarimu huko Peponi.
51. Na wale walio jikukusa nafsi zao katika
kuipiga vita Qur'ani kushindana na Waumini na kuwapinga, wakitamani na kudai kwa
uwongo, kwamba wao watapata wayatakayo - watu hao watabaki milele katika adhabu
ya Motoni.
52. Ewe Nabii! Usihuzunike kwa hizi hila za
makafiri. Yalimpata kama haya kila Mtume katika Mitume wetu, na kila Nabii
katika Manabii wetu. Nayo ni kuwa kila wakiwasomea kitu kwa kuwaita waifuate
Haki Mashetani wa kibinaadamu walio asi wakiyapinga ili waubat'ilishe Wito, na
wawatie shaka watu kwa yale wanayo somewa. Makusudio yao ni kujiingiza kati
baina ya Nabii na matamanio yake ya kutaka Wito wake uitikiwe. Lakini Mwenyezi
Mungu huyaondoa wayatakayo. Na mwishoe Haki ndiyo inayo shinda anapo isimamisha
Mwenyezi Mungu sharia yake, na akamnusuru Mtume wake. Na Yeye ndiye Mwenye
kuzijua hali za watu na vitimbi vyao, Mwenye hikima katika vitendo vyake.
Anaweka kila kitu pahala pake.
53. Na hakika Mwenyezi Mungu amewawezesha waasi
wanao kataa Haki waweze kutumbukiza shakashaka na vikwazo katika Njia ya Wito
ili uwe ni mtihani na majaribio kwa watu. Makafiri ambao nyoyo zao zimegeuka
mawe, na wanaafiki ambao nyoyo zao zina maradhi, huzidi upotovu kwa kueneza
shakashaka hizi na kuziunga mkono. Na si ajabu madhaalimu hawa kusimama msimamo
huu, kwani wao wamezama katika upotovu na wamevuka mpaka katika inadi na
mfarakano.
54. Na ili walio pewa ilimu ya sharia na Imani
wazidi Imani na kujua kwamba wayasemayo Mitume na Manabii hakika ni kweli iliyo
teremka kutokana na Mwenyezi Mungu. Na kwamba Mwenyezi Mungu hakika anawalinda
Waumini kwa hima yake kutokana na matatizo yote yanayo wapitikia. Na huwaongoa
kwenye maarifa ya Njia Iliyo Nyooka nao wakaifuata.
55. Na walio kufuru hawatengenei. Bali
wanaendelea kuitilia shaka Qur'ani mpaka wafikiwe na mauti, iwafikie adhabu ya
Siku isiyo kuwa na kheri kwao wala rehema; nayo ni Siku ya Kiyama.
56. Siku ambayo madaraka ya nguvu, na uendeshaji
mambo usio na ukomo wote, ni wa Mwenyezi Mungu pekee. Siku hiyo ndipo atapo
hukumu baina ya waja wake. Walio amini na wakatenda mema watadumu katika Bustani
zilizo jaa kila namna ya neema.
57. Na walio kufuru na wakazikanusha Aya za
Qur'ani tulizo mteremshia Muhammad, hao watakuta adhabu ya madhila na fedheha.
58. Na wenye kuacha nchi zao kwa ajili ya
kutukuza shani ya Dini yao wakitafuta radhi za Mwenyezi Mungu, kisha wakauliwa
katika uwanja wa Jihadi, au wakafa vitandani mwao, Mwenyezi Mungu atawalipa
malipo mazuri kabisa. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kutoa thawabu za
ukarimu.
59. Na hakika atawatia katika Pepo kwenye vyeo
watavyo ridhika navyo na vitawafurahisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuzijua vyema hali zao, basi atawalipa malipo bora, naye ni Mpole huyasamehe
makosa yao madogo madogo ya kuteleza.
60. Huo ndio mwendo wetu katika kuwalipa watu.
Hatuwadhulumu. Na Muumini mwenye kulipiza kisasi kwa aliye mfanyia uovu, na
akalipiza kwa kadri ya alivyo tendewa bila ya kuzidisha, kisha yule mkosa akaja
kumfanyia uadui tena baada yake, basi hakika Mwenyezi Mungu anatoa ahadi ya
nguvu kuwa atamnusuru na kumsaidia yule aliye dhulumiwa. Na hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwingi wa kumsamehe mwenye kulipiza kama alivyo dhulumiwa. Hamtii
makosani kwa hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, basi huyasitiri
makosa ya kuteleza ya mja wake mt'iifu, wala hamfedhehi Siku ya Kiyama.
61. Msaada huo ni mwepesi kwa Mwenyezi Mungu,
kwani Yeye ni Muweza wa kila kitu. Na katika Ishara za uwezo wake zilio wazi
mbele yenu ni utawala wake juu ya ulimwengu wote. Huzungusha usiku na mchana,
pengine huzidi huu au huzidi huu. Inakuwa baadhi ya kiza cha usiku pahala pa
mwanga wa mchana. Na pengine huwa kinyume cha hivyo. Naye Subhanahu juu ya uwezo
wake husikiliza kauli ya aliye dhulumiwa, na anaviona vitendo vya mwenye
kudhulumu. Basi humtia adhabuni.
62. Huo ndio msaada wa wenye kudhulumiwa unao
tokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kutenda kwake katika ulimwengu kama
atakavyo bila ya kiwango ni kama muonavyo matokeo yake; na kwa hakika Yeye ndiye
Mungu wa Haki ambaye hapana mungu mwenginewe pamoja naye. Na kwamba masanamu
wanayo yaabudu washirikina ni uwongo, hayana ukweli, na Mwenyezi Mungu peke yake
ndiye aliye tukuka juu ya vyote isipo kuwa Yeye Mwenyewe kwa shani yake, na ni
Mkuu wa madaraka.
63. Ewe mwenye akili! Huzingatii haya yalio
kuzunguka uyaonayo kwa macho yenye kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu, ukamuabudu
Yeye peke yake? Yeye ndiye anaye iteremsha mvua kutoka mawinguni, na ardhi
ikageuka rangi ya kijani kibichi kwa mimea inayo chipuka, baada ya kuwa na
ukame. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole mno kwa waja wake, na anajua vyema
yanayo wanufaisha na kwa hivyo akawatengenezea kwa kudra yake.
64. Kila kiliomo mbinguni na katika ardhi ni
chake Yeye, na kinamtumikia Yeye peke yake, na anakiendesha kama apendavyo. Na
Yeye hawahitajii waja wake, bali wao ndio wanao mhitajia Yeye. Na Yeye ndiye
anaye stahiki peke yake kuhimidiwa na kusifiwa na viumbe vyote.
65. Ewe mwenye akili! Huyaangalii yaonekanayo
kwa macho ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, ukaona anavyo wasahilishia watu wote
kunafiika na ardhi na viliomo ndani yake? Na akawatengenezea bahari za kwendea
ndani yake marikebu kwa mujibu apendavyo Yeye? Na akazishika sayari zote ziliomo
angani kwa kudra yake hata zisikosee mpango wake, au zikaangukia kwenye ardhi,
isipo kuwa akitaka kwa mapenzi yake. Hakika Mwenyezi Mungu Aliye takasika
ni Mwingi wa huruma na rehema kwa waja wake. Kwa hivyo amewatengenezea kila njia
za maisha mema. Huwaje basi baada ya haya yote hamumsafii niya Yeye kwa
kumshukuru na kumuabudu?
"Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu
amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa
amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu." Aya hii
tukufu inakusanya maana za kisayansi za ndani. Mbingu, nayo ni kila kilicho juu
yetu, inaanza kwa kuifunika ardhi kwa hewa, tena kwa anga, tena kwa vyombo vya
mbinguni vinavyo toa mwanga kama nyota n.k. na visio toa mwanga wake mwenyewe
kama mwezi, na sayari nyengine, na nyota mkia, na vumbi la ulimwengu, n.k. Vyote
hivi vinakuwa vilivyo na vinashikana kwa athari ya nguvu mbali mbali. Muhimu wa
hizo ni mvuto na nguvu inayo tokana na kule kuzunguka kwao.
Yamedhihiri mapenzi ya Mwenyezi Mungu na huruma zake kwa waja wake kuwa
katengeneza kifuniko cha angani kina namna za gasi mbali mbali ambazo ni dharura
kwa uhai. Kama pia anawalinda wakaazi wa duniani na mianga na vimondo n.k.
vinavyo zunguka angani na ambavyo vinapo karibia kwenye ardhi huungua kabla
havijafika chini.
Na katika mapenzi yake na rehema yake Mwenyezi
Mungu ni kuwa hivyo vimondo vinavyo anguka kwenye ardhi ni nadra sana kutokea,
na hutokea mwahala wasipo kaa watu. Jambo hili la dhaahiri laonyesha huruma na
rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Na haya yanatilia nguvu na kusadikisha
kauli yake Mwenyezi Mungu: " na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila
kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye
kurehemu."
66. Na Yeye ndiye aliye kupeni uhai. Kisha
anakufisheni unapo malizika muda wenu. Kisha tena atakufufueni Siku ya Kiyama
kwa ajili ya hisabu na malipo. Hakika mwanaadamu baada ya neema zote hizi na
ushahidi wote huu ni mwingi wa kumkataa Mwenyezi Mungu na kuzikataa neema zake
alizo mpa.
67. Tumewajaalia katika kila umma walio kwisha
tangulia wawe na sharia zao makhsusi zinazo ambatana na zama zao, za kumuabudia
Mwenyezi Mungu, mpaka zinapo kuja futwa na zijazo baadae. Na kwa hivyo
tumewajaalia watu wako, ewe Nabii, wawe na Sharia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu
mpaka Siku ya Kiyama. Ilivyo kuwa hivi ndio amri yetu na mpango wetu, basi hao
wanao jiabudia kwa dini zao zilizo pita, haiwafalii wao kutia mkazo katika
kukupinga wewe. Kwani hakika sharia yako wewe imefuta sharia zao. Basi
usijishughulishe na kujadiliana nao. Nawe endelea kuwaita watu wende kwa Mola
wako Mlezi kwa mujibu wa unavyo pewa wahyi (ufunuo). Hakika wewe unafuata
Uwongofu Ulio Nyooka wa Mola wako Mlezi.
68. Na wakishikilia kuendea kukujadili basi
waachilie mbali, na waambie: Mwenyezi Mungu anajua zaidi vitendo vyenu, na
malipo mnayo yastahiki.
69. Mwenyezi Mungu atahukumu baina yangu na
nyinyi Siku ya Kiyama katika hayo mnayo khitalifiana nami. Atamlipa thawabu
aliye ongoka na atamuadhibu aliye potoka.
70. Ewe mwenye akili! Jua kuwa ujuzi wa Mwenyezi
Mungu umekusanya kila kiliomo mbinguni na duniani. Hapana kitendo cha hawa
washindani kinacho fichika kwake. Vyote hivyo vimekwisha andikwa katika Ubao
ulio hifadhiwa (Lauhun Mahfuudh). Kwani kujua kwake Mwenyezi Mungu na
kuvithibiti kwake ni kazi nyepesi kabisa kwake.
71. Na washirikina huabudu badala ya Mwenyezi
Mungu masanamu na watu ambao haikuteremka hoja yoyote ya kuwaabudu hao katika
Kitabu cha mbinguni chochote. Wala wao hawana ushahidi wowote wa kuingia
akilini. Lakini wanafanya yote hayo kufuata pumbao na mila tu. Wala hao
washirikina walio zidhulumu nafsi zao na wakazidharaulisha akili zao hawato pata
msaidizi wa kuwanusuru, na kuwakinga na adhabu ya Moto Siku ya Kiyama, kama
wanavyo jidai.
72. Ewe Nabii! Hawa washirikina mtu akiwasomea
Aya zetu zilizo wazi, na ambazo ndani yake mna ushahidi wa ukweli wa hayo unao
waitia, na ubaya wa ibada zao, utaona katika nyuso zao ghadhabu na chuki inayo
wajaa, hata inakaribia kuwapelekea kutaka kumuuwa huyo anaye wasomea. Ewe Nabii!
Waambie kwa kuwazindua na kuwaonya: Je! Mtanisikiliza nikwambieni yaliyo kuwa
mabaya zaidi kuliko hiyo chuki inayo kuunguzeni roho? Ni Moto ambao Mwenyezi
Mungu amewaahidi walio kufuru kama nyinyi Siku ya Kiyama. Na hapana mwisho mbaya
na makaazi maovu kuliko hayo.
73. Enyi watu! Sisi tunakufahamisheni ukweli wa
ajabu, basi hebu usikilizeni na muuzingatie. Haya masanamu hayataweza kabisa
kuumba chochote hata kikiwa kitu duni kabisa kama nzi; hata ikiwa yote
yakisaidiana katika kuumba huko. Bali huyu makhluku duni kabisa akiwanyang'anya
chochote katika hizo sadaka wanazo pewa masanamu hawawezi kumzuia au kumfukuza.
Unyonge gani basi huo wa kushindwa na nzi kutoweza kurejesha alicho pokonya. Na
nzi ni kitu dhaifu mno! Wote wawili ni wanyonge. Bali hayo masanamu ambayo kama
mnavyo ona ni dhaifu zaidi, basi huwaje mwanaadamu mwenye akili akenda kuyaabudu
na kutaka yamnafiishe.
74. Hawa washirikina hawamjui Mwenyezi
Mungu kama anavyo faa kujuulikana, wala hawamtukuzi kama anavyo stahiki
kutukuzwa, walipo kwenda kumshirikisha katika ibada na vitu visio kuwa na maana
kabisa. Na hali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muweza wa kila kitu, Asiye shindika na
yeyote.
75. Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na hikima yake
yamempelekea kuteuwa Wajumbe kutokana na Malaika, na kutokana na wanaadamu, ili
wafikishe sharia yake kwa viumbe vyake. Basi huwaje mkampinga aliye mchagua
Mwenyewe kuwa ni Mjumbe wake kwenu? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia
wayanenayo waja wake, Mwenye kuviona vitendo wavitendavyo. Naye atawalipa
kwavyo.
76. Na Yeye Subhanahu anajua hali zao zilizo
dhaahiri na za ndani. Hapana kinacho fichika kwake. Na kwake Yeye pekee ndiyo
yanarejea mambo yote.
77. Enyi mlio amini! Msishughulikie upotovu wa
makafiri. Nyinyi endeleeni na kutimiza Sala zenu kwa ukamilifu kwa kurukuu na
kusujudu. Na muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni na akakuruzukuni. Wala
msimshirikishe naye na yeyote. Na tendeni kila lenye kheri na manufaa, ili mpate
kuwa watu wema, walio bahatika katika Akhera yenu na dunia yenu.
78. Na wanieni katika Jihadi ya kunyanyua Neno
la Mwenyezi Mungu na kutafuta radhi zake mpaka mwashinde maadui zenu na
myashinde matamanio yenu. Kwani Yeye Subhanahu amekukaribisheni kwake, na
amekuteueni muinusuru Dini yake, na amekujaalieni muwe Umma wa katikati. Wala
hakukulazimisheni katika aliyo kuwekeeni Sharia lolote lenye mashaka juu yenu
msilo weza kulichukua. Na amekufanyieni mepesi katika yanayo kuleteeni
mashaka, na katika msiyo yaweza amekufanyieni ruhusa namna mbali mbali. Basi
ishikeni Dini hii, kwani hii ndiyo Dini ya baba yenu Ibrahim katika misingi
yake. Na Yeye Subhanahu ndiye aliye kuiteni Waislamu, (yaani Wanyenyekevu)
katika Vitabu vya mbinguni vilivyo tangulia, na pia katika hii Qur'ani kwa
ut'iifu wenu kwa yale aliyo kutungieni sharia. Basi kueni kama alivyo kuiteni
Mwenyezi Mungu ili muwe mwisho wenu mnamshuhudia Mtume kama amekufikishieni
ujumbe nanyi mkatenda aliyo kufikishieni, mpate kufanikiwa, na muwe mashahidi
kwa kaumu zilizo tangulia kwa yaliyo kuja katika Qur'ani kwamba Mitume wao nao
walifikisha ujumbe. Na ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu amekuchagueni nyinyi khasa
kuwa ni wat'iifu kwake, mkashika Sala kwa ukomo wa ukamilifu wake, basi ni
waajibu wenu kulipa hayo kwa kumshukuru na kumt'ii, mshike Sala kwa utimilifu
wake, na mwape Zaka wanao stahiki, na mumtegemee Mwenyezi Mungu katika mambo
yenu yote, na mchukue kwake msaada, kwani Yeye ndiye Msaidizi wenu na ndiye wa
kuwanusuru.
Yeye ndiye Mbora wa ulinzi na Mbora wa kunusuru.