1. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameanza Sura hii
kwa harufi, nazo ni T'a na Ha, ili kupingana na makafiri wanao kanya, na kuwa
kama ishara ya kwamba hii Qur'ani imeundwa kwa hizi hizi harufi mnazo zitumia
katika kusema kwenu. Na juu ya hivyo nyinyi mmeajizika (yaani mmeshindwa, ndio
likatokea hilo neno "Muujiza") kuleta Sura walau ndogo, au baadhi ya Aya zilizo
mfano wa Qur'ani.
2. Ewe Mtume! Sisi hatukukufunulia wewe Qur'ani
hii iwe ni sababu ya kukupa dhiki ya nafsi yako kwa kuwasikitikia hao wapuuzi
kukupuuza wewe.
3. Lakini tumekuteremshia iwe ni kumbusho kwa
mwenye kumkhofu Mwenyezi Mungu apate kumt'ii.
4. Hii Qur'ani umeteremshiwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, Mwenye uwezo, Muumba ardhi na mbingu zilio nyanyuka juu.
5. Mtukufu wa rehema, ametawala sawa sawa juu ya
Ufalme wake.
6. Ni wake Yeye tu, Subhanahu, ufalme wa mbinguni
na viliomo humo, na wa ardhi na viliomo juu yake, na ufalme wa vilio baina ya
hivyo, na maadeni na kheri nyenginezo zilizo fichikana chini ya ardhi.
7. Na kama uwezo wa Mwenyezi Mungu ulivyo kusanya
kila kitu, kadhaalika ujuzi wake pia umekusanya kila kitu. Na ewe mtu,
ukinyanyua sauti kwa kusema, basi Mwenyezi Mungu anajua. Kwani Yeye anajua
unapo sema na mtu, na anajua unapo zungumza na nafsi yako.
8. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mungu wa Pekee,
Mwenye kustahiki kuabudiwa peke yake. Kwani Yeye amesifika kwa sifa za
ukamilifu, naye ndiye Mwenye bora ya sifa.
9. Ewe Nabii! Unajua khabari za Musa na Firauni?
10. Pale Musa alipo uona moto katika safari yake
ya usiku kutoka Madyana kwendea Misri, akamwambia mkewe na walio kuwa naye:
Ngojeni hapa! Mimi nimeuona moto ule; natumai nitakupatieni kijinga cha
moto kutoka kule mpate kuashia moto, au huko nitapata mtu wa kuniongoza njia.
11. Alipo fika huko, akasikia sauti yenye kutoka
juu inamwita: Ewe Musa!
12. Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mola wako
Mlezi! Basi vua viatu vyako kwa hishima ya pahala hapa; kwani wewe upo
katika bonde safi lenye baraka, nalo ni T'uwa.
13. Na Mimi Mwenyezi Mungu nimekuteuwa wewe kwa
kukupa Utume. Basi sikiliza haya ninayo kufunulia uyajue na ukawafikishie watu
wako.
14. Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa
Pekee, hapana wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Mimi. Basi niamini Mimi, na
niabudu Mimi, na dumu daima katika kuishika Sala ili uwe daima unanikumbuka.
15. Hakika Saa ndiyo miadi ya kukutana nami;
nami miadi hiyo nimeificha kwa waja wangu, na nimewaonyesha ishara zake. Hiyo
Saa itakuja bila ya shaka yoyote, na kila nafsi itahisabiwa kwa iliyo tenda.
16. Ewe Musa! Asikuachishe kuiamini Saa na
kujitayarisha kwa ajili yake yule ambaye haisaidiki, na akafuata pumbao lake
akahiliki.
17. Na nini hicho ulicho kamata kwa mkono wako
wa kulia?
18. Musa akajibu: Hii ni fimbo yangu,
najikongojea ninapo kwenda, na ninachungia kondoo na mbuzi wangu, na inanifaa
kwa manufaa mengine, kama kuwatetea hayawani wangu.
19. Mwenyezi Mungu Subhanahu akamwambia
Musa: Itupe hiyo fimbo chini kwenye ardhi.
20. Musa akaitupa; akashtuka kuiona imegeuka
nyoka anakwenda!
21. Akamwogopa. Mwenyezi Mungu akamtuza kwa
kumwambia: Mwokote wala usikhofu, kwani tutamrejesha hali yake kama ya kwanza.
22. Na ingiza mkono wako ndani ya mfuko wa nguo
ukiambatisha na ubavu wako, utatoka mweupe safi bila ya maradhi. Na huo
tumekufanyia ni muujiza wa pili wa Utume wako...
23. Ili tukuonyeshe baadhi ya miujiza yetu
mikubwa iwe ni dalili ya ukweli wa Utume.
24. Nenda kwa Firauni umtake amuamini Mwenyezi
Mungu Mmoja wa Pekee. Kwani yeye Firauni amepindukia mipaka kwa ukafiri wake na
ujeuri wake.
25. Musa akamnyenyekea Mola wake Mlezi kwa
kumwomba: Nikunjulie kifua changu, iniondoke ghadhabu, nitimize ujumbe wa Mola
wangu Mlezi.
26. Na unisahilishie kazi yangu ili nipate
kutimiza waajibu wangu.
27. Na likate fundo la ulimi wangu, nibainishe
maneno,
28. Ili watu wafahamu vyema niyasemayo.
29. Na nijaalie mtu wa kuniunga mkono katika
watu wangu,
30. Naye ni ndugu yangu Harun.
31. Anizidishe nguvu zangu.
32. Na umshirikishe nami katika kubeba mizigo ya
ujumbe na kuifikisha.
33. Ili tukithirishe kukutakasa na yasiyo kuwa
laiki yako,
34. Na tuyakariri majina yako mazuri kwa wingi.
35. Ewe Mola wetu
Mlezi! Hakika Wewe daima unatuangalia sisi, na
unayashughulikia mambo yetu...
36. Mwenyezi Mungu akamwita Mtume wake, Musa,
kwa kusema: Nimekwisha kukubalia uliyo yaomba, na hii ni zawadi tulio kutunukia
wewe kwa hisani.
37. Na Sisi tumewahi zamani kukufadhili wewe kwa
hisani bila ya kuomba.
38. Tulipo mwongoza mama yako kwa uwongozi wenye
nafuu katika maisha yako.
39. Tulimuamrisha akuweke, na hali wewe ni mtoto
mchanga wa kunyonya, katika kisanduku, na kisha hicho kisanduku akitie katika
mto, ili usije kuuliwa na Firauni, pale alipo kuwa anawauwa watoto wote wanaume
wa Banu Israili. Tukayafanya maji ya mto yachukue kisanduku kile mpaka
ufukweni. Kwa mujibu wa mipango yetu Firauni, adui yangu na wako, akakichukua
kile kisanduku. Nami nikakupa mapenzi ya rehema na ulinzi, ukapendwa na kila
aliye kuona. Ukapata malezi mazuri yaliyo bora chini ya ulinzi wangu.
40. Ewe Musa! Jua ya kwamba zamani Sisi
tulikwisha kukufanyia hisani pale dada yako alipo kuwa anakwenda akiangalia hali
yako ulipo kuwa katika jumba la Firauni, na akawaona wanakutafutia mtu wa
kukunyonyesha. Ni yeye aliye waongoza kwa mama yako, nasi tukakurejesha kwake
apate kufurahi kukuona uhai na umerejea kwake, na asite huzuni na kilio. Na
ulipo kua, na ukamuuwa mtu katika kaumu ya Firauni bila ya kukusudia, tukakuvua
kutokana na dhiki iliyo kupata, na tukakusalimisha na shari yao. Ukenda mpaka
Madyana na huko ukakaa miaka kadhaa wa kadhaa, kisha ukatoka Madyana ukarejea
kwa muda tulio kukadiria kwa ujumbe wako..
41. Na nikakuteua kukupa Wahyi (Ufunuo) na
kubeba Utume wangu.
42. Nenda, wewe na nduguyo, nanyi mkisaidiwa na
miujiza yangu yenye kuashiria Unabii na Utume, wala msidhoofike katika kutimiza
Ujumbe wangu, wala msighafilike kunikumbuka na kuniomba msaada.
43. Nenda pamoja na duguyo Harun kwa Firauni.
Hakika huyo amepindukia mipaka katika ukafiri wake na jeuri zake.
44. Mtakeni kwa upole na ulaini aniamini
Mimi kwa kutaraji asaa akakumbuka Imani aliyo isahau, na akaogopa matokeo
ya ukafiri wake na ujeuri wake.
45. Musa na Harun wakanyenyekea kwa Mwenyezi
Mungu, wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tunaogopa huyu Firauni
asituvamie kwa madhara, na akapindukia mpaka katika uovu.
46. Mwenyezi Mungu akawapoza kwa kusema:
Msimkhofu Firauni; kwani Mimi ni pamoja nanyi kukuangalieni na kukulindeni,
nayasikia ayasemayo, na nayaona ayatendayo. Sitomwachia kukudhuruni.
47. Nendeni kwa Firauni, na mwambieni: Hakika
sisi ni Mitume tulio tumwa kwako na Mola wako Mlezi. Tumekuja kukutaka umuamini
Yeye, na uwaache Wana wa Israili watoke utumwani na adhabuni. Na sisi
tumekuletea muujiza kutokana na Mwenyezi Mungu kuwa ni ushahidi wa ukweli wa
haya tunayo kuitia, na mwenye kuufuata uwongofu atasalimika na adhabu ya
Mwenyezi Mungu na kughadhibika kwake.
48. Na hakika Mwenyezi Mungu ametufunulia sisi
kuwa adhabu yake kali itamshukia anaye tukadhibisha, na akapuuza wito wetu.
49. Firauni kwa ujeuri wake na ujabari wake
akasema: Ewe Musa! Ni nani huyo Mola wenu Mlezi?
50. Musa akamjibu: Mola wetu Mlezi ni yule aliye
kipa neema ya umbo kila kilicho umbwa, akakiumba kwa sura aliyo ipenda Yeye
Subhanahu, na akakielekeza kwa alivyo kiumbia.
"Akasema: Mola wetu
Mlezi ni yule aliye kipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoa." Mwenyezi Mungu
Subhanahu amekijaalia kila kiumbe kina sifa zake makhsusi za kutekeleza kazi
yake kilicho umbiwa nacho katika maisha, kama alivyo pewa hidaya mwanaadamu.
51. Firauni akasema: Je, nini hali ya karne za
zamani, na yaliyo pitikana huko?
52. Musa akasema: Ujuzi wa karne hizo uko kwa
Mola wangu Mlezi peke yake. Hayo yamedhibitiwa katika madaftari ya vitendo vyao.
Hapana kitendo kinacho mpotea asikijue, wala Yeye hasahau.
53. Yeye huyo ndiye Mungu Mwenye kuwafadhili
waja wake kwa kuwaumba na kuwalinda. Amekutengenezeeni ardhi, akaikunjua kwa
uwezo wake, na akakupasulieni njia mnazo pitia, na akakuteremshieni mvua zinazo
leta mito, na Yeye Subhanahu akatoa namna mbali mbali za mimea, inayo
khitalifiana kwa rangi, na utamu, na manufaa. Mingine myeupe, mingine myeusi,
myengine mitamu na mingine michungu..
54. Naye Subhanahu amewaelekeza waja wake
wanufaike kwa mimea aliyo watolea, kwa kula na kulishia mifugo yao na kama hayo.
Na akataja kuwa katika kuumba huku, na kuanzisha huku, na kutumia huku, ni
dalili zilizo wazi za kumwongoa mwenye akili afikie Imani ya kumuamini Mwenyezi
Mungu na kuamini Mitume wake.
55. Na kutokana na udongo wa ardhi hii ndio
Mwenyezi Mungu amemuumba Adam na dhuriya zake. Na humo ndio anawarudisha baada
ya kufa kwa ajili ya kusitiri miili yao. Na kutoka humo atawatoa tena
kuwafufua na kuwalipa kwa waliyo yatenda.
56. Na hakika Sisi kwa kupitia kwa Musa
tulimwonyesha Firauni miujiza ya dhahiri ya kuunga mkono Ujumbe wa Musa na
ukweli wake kwa yote aliyo simulia kutokana na Mwenyezi Mungu na athari ya uwezo
wake. Juu ya hayo Firauni alishikilia ukafiri wake, akayakadhibisha yote hayo,
na akakataa kuyaamini.
57. Firauni akamwambia Musa: Je, umetujia upate
kututoa katika nchi yetu ipate kuwa mikononi mwa watu wako kwa uchawi wako ulio
ulia watu?
58. Basi sisi tutauvunja huo uchawi wako. Weka
miadi baina yetu na wewe, tukutane, wala tusikhitalifiane.
59. Musa akawajibu: Miadi yetu ni siku ya Idi
yenu mnapo jipamba, na watu wakusanyike kabla ya adhuhuri siku hiyo, waone
yatayo kuwa baina yetu na nyinyi.
60. Firauni akaondoka na akayashughulikia mambo
mwenyewe. Akakusanya mipango yake, na wakuu wa wachawi, na zana za uchawi. Kisha
akahudhuria na yote hayo kwa mujibu wa miadi.
61. Musa akawaambia kuwahadharisha maangamizo ya
Mwenyezi Mungu na adhabu yake, na akawakataza wasizue uwongo, kwa kumdaia ungu
Firauni, na kuwakadhibisha Mitume wa Mwenyezi Mungu, na kuikataa miujiza. Na
akawatisha kwamba Mwenyezi Mungu atawapatiliza kwa adhabu wakiendelea na hayo,
na akatilia mkazo sana khasara ya mwenye kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu.
62. Wakatishika na maonyo ya Musa, wakaingia
kusemezana wao kwa kwao wakivutana, na kila mmoja akitoa maoni yake juu ya aliyo
yasema Musa.
63. Wakawafikiana kwamba Musa na Harun ni
wachawi ambao wanafanya hila kutaka kuwatoa katika nchi yao, kwa kuwapokonya
madaraka, yatoke mikononi mwao. Na hayo ni kwa uchawi, ili Wana wa Israili
wapate ushindi. Na wawaharibie watu wa Firauni imani yao wanayo iona kuwa ni
nzuri!
64. Basi fanyeni njama zenu muwafikiane kitu
kimoja cha kumfanyia Musa, kisha mkusanye wateuliwa, ili watazamaji waingiwe na
kitisho kwa heba yao. Atakaye fuzu leo basi ndio kashinda kweli.
65. Wachawi walimkabili Musa kwa rai moja, na
wakamkhiarisha kwa majivuno na kiburi, waanze wao au aanze yeye kuonyesha
ubingwa wake.
66. Musa akasema: Bali anzeni nyinyi! Basi
wakazitupa kamba zao na fimbo zao. Zikamdhihirikia Musa, kwa uchawi, kuwa
zimegeuka nyoka zinakwenda.
67. Musa akaingiwa na khofu kwa aliyo yaona kwa
kuzugwa na uchawi, na kuona huenda watu wakadanganyika kwa uchawi wakadhani ni
muujiza.
68. Mwenyezi Mungu akamdiriki kwa upole,
akamwambia: Usiogope kitu. Wewe utaushinda tu leo huu upotovu wao.
69. Itupe hiyo fimbo uliyo nayo mkononi mwako wa
kulia ivimeze hivyo walivyo vizua kwa uchawi. Kwani hayo waliyo yaunda ni
mazonge tu ya uchawi, na hakika mchawi popote alipo hawezi kufuzu.
70. Musa akaitupa fimbo yake, na hapo hakika
ikageuka kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu ikawa joka kubwa la kutisha. Likavimeza
vyote walivyo unda wao. Wachawi walipo uona muujiza huu mbio mbio wakasujudu kwa
kuyakinika na ukweli wa Musa, huku wakisema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu Mmoja wa
Pekee, Mola Mlezi wa Harun na Musa, Mola Mlezi wa kila kitu.
71. Firauni akasema: Vipi mnamuamini huyu bila
ya ruhusa yangu? Hakika huyu ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi, wala
kitendo chake hichi si muujiza kama mnavyo dhani! Akawatishia kwa kusema: Kwa
yakini nitaikata mikono yenu na miguu yenu mbali mbali, mkono wa kulia kwa mguu
wa kushoto n.k. Na hakika nitakubandikeni misalabani kwenye vigogo vya mitende.
Na hapo mtajua ni mungu gani kati yetu aliye mkali zaidi na kudumu zaidi katika
mateso - mimi au mungu wa Musa?
72. Wachawi wakasimama imara juu ya Imani yao,
na wakajibu vitisho vya Firauni kwa kauli yao: Sisi hatuendelei na kubakia nawe
katika ukafiri baada ya kwisha tubainikia yaliyo ya kweli katika muujiza wa
Musa. Wala sisi hatutakukhiari wewe kuliko Mungu wa Musa ambaye ndiye aliye
tuumba. Basi wewe tenda utakayo yatenda! Madaraka yako hayapindukii maisha haya
mafupi.
73. Kwani hakika sisi ni wenye kusimama juu ya
Imani kumuamini Mola wetu Mlezi wa Haki, ili atufutie madhambi yetu yaliyo pita,
na atusamehe huku kushughulikia uchawi ulio tulazimisha tujifunze na tuufanye!
Na Mola wetu Mlezi ni Mbora wa malipo kuliko wewe, akit'iiwa; na ufalme wake na
uwezo wake kulipa unadumu zaidi kuliko wako.
74. Hakika anaye kufa katika ukafiri akakutana
na Mwenyezi Mungu hali naye ni mkhalifu basi malipo yake ni Jahannamu. Humo
hafi, akapumzika na adhabu; wala hawi hai wa maisha ya kustarehe na neema.
75. Na mwenye kukutana na Mola wake Mlezi naye
yumo katika Imani na a'mali njema, basi huyo atakuwa na vyeo vya juu.
76. Vyeo hivyo ni Bustani za Peponi za kudumu
katika neema. Baina ya miti yake inapita mito, na humo watadumu milele. Hayo ni
malipo ya mwenye kuitakasa nafsi yake na ukafiri kwa kuijaza Imani, na ut'iifu
baada ya ukafiri na maasi.
77. Tena vikapishana vituko baina ya Firauni na
Musa. Mwenyezi Mungu akampa Wahyi (ufunuo) Mtume wake, Musa, atoke Misri na Wana
wa Israil, wakati wa usiku. Na aipige bahari kwa fimbo yake, utatokea muujiza
mwingine, nao ni kufunguka njia kavu baharini. Naye akamtuliza asiingiwe na
khofu kuwa atakamatwa na Firauni, au kuwa atazama katika maji!
78. Musa akafanya kama alivyo muamrisha Mwenyezi
Mungu. Akatoka Firauni na askari wake nyuma yake, akawakuta kwenye bahari.
Akenda nyuma yao kwenye njia iliyo funguka baharini kwa ajili ya Musa na kaumu
yake. Na hapo ukatokea muujiza; nao ni maji kumfudikiza Firauni na kaumu yake,
wakazama wote!
79. Hivi ndivyo Firauni alivyo potea yeye na
watu wake wakaacha Haki, wakateketea wote!
80. Enyi Wana wa Israili! Sisi tulikuokoeni na
adui yenu, Firauni, na tukakuahidini kuokoka kwa ulimi wa Musa kuwa mtafika
salama mpaka kwenye kando ya mlima. Na tulikuteremshieni Manna na Salwa, chakula
kizuri, cha tam-tam na nyama ya ndege nono.
81. Kuleni vitu hivi vizuri tulivyo kuruzukuni
bila ya taabu yoyote kwenu. Wala msidhulumu, wala msiingie kumuasi Mwenyezi
Mungu katika maisha haya ya starehe, isije kukuteremkieni ghadhabu yangu. Kwani
anaye teremkiwa na ghadhabu yangu huporomoka katika matabaka ya chini kabisa ya
mateso ya Mwenyezi Mungu.
82. Na hakika Mimi ni Mtukufu wa Kusamehe kwa
anaye acha ukafiri wake, na akatengeneza Imani, na akatenda yaliyo mema, na
akadumu juu ya hayo mpaka akakutana na Mwenyezi Mungu.
83. Musa aliwatangulia watu wake kwenda mlimani,
apate kuzungumza na Mola wake Mlezi. Mwenyezi Mungu akamuuliza sababu ya kufanya
kwake haraka kufika mbele kabla ya kaumu yake.
84. Musa akasema: Hakika watu wangu wapo karibu
nami, watanikuta. Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi nimewatangulia ili kutaka
kukuridhisha Wewe.
85. Mwenyezi Mungu akamwambia: Sisi tumewafanyia
mtihani watu wako baada ya wewe kuwawacha. Wakaingia katika fitna; Msamaria
amewapotoa!
86. Musa akawarejea watu wake naye kaghadhibika
sana, na huzuni ya uchungu. Akawasemeza watu wake kwa hamaki: Mola wenu Mlezi
alikuahidini kuwa atakuokoeni na atakuongoeni, kwa kuiteremsha Taurati na kupata
ushindi kwa kuingia nchi takatifu. Haujapita muda mrefu wa ahadi ila nyinyi
mmekwisha sahau ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Kwa kitendo chenu kiovu
hichi mnataka ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ikuteremkieni kwa maasi yenu aliyo
kuhadharisheni nayo? Mmesahau ahadi yenu mliyo nipa kuwa mtafuata mwendo wangu,
na mtafuata nyayo zangu?
87. Watu wa Musa wakasema kwa kutafuta udhuru:
Hatukwenda kinyume na ahadi yako kwa khiari yetu. Lakini tulipo toka Misri
tulibebeshwa mizigo ya mapambo ya watu. Kisha tukaona - kwa uzito wake kwetu -
tuepukane nayo. Msamaria akawasha moto katika shimo, tukaitupa hiyo mizigo. Na
kadhaalika Msamaria naye katupa vyombo alivyo kuwa navyo.
88. Basi Msamaria akawaundia ndama aliye na
mwili wa dhahabu, ukipita upepo ndani yake, hutoa sauti, husikilizana kama mlio
wa ng'ombe, ili udanganyifu utimie. Akawaita wamuabudu na wao wakamwitikia.
Akasema yeye na wafwasi wake: Huyu ndiye mungu wenu, na ndiye mungu wa Musa.
Akasahau Msamaria kuwa ni wepesi mtu, akizingatia na kutafuta dalili, kufahamu
kuwa ndama hawezi kuwa mungu.
89. Macho yaliingia upofu yalipo zingatia kuwa
huyu ndama ni mungu! Hawaoni kwani hawarejezei kauli yao? Wala hawezi
kuwaondolea madhara yoyote? Wala kuwaletea manufaa yoyote?
90. Na Harun alikuwa pamoja nao ilipo tokea
fitna hii. Naye kabla ya kurejea Musa a.s. alikwisha waambia: Enyi watu wangu!
Nyinyi mmeingia katika fitna ya Msamaria kwa upotovu huu! Hakika Mungu wenu wa
Haki ni Mwenyezi Mungu, Arrahman, Mwingi wa Rehema, wala hana mwenginewe.
Nifuateni mimi kwa haya ninayo kunasihini, na ishikeni rai yangu kwa kuachilia
mbali upotovu huu.
91. Wakasema: Sisi tutaendelea kumuabudu huyu
ndama mpaka atakapo rejea Musa kwetu!
92. Musa kwa kuathirika na aliyo yajua na
kuyaona ya watu wake, alisema: Ewe Harun! Sababu gani iliyo kukataza hata
usiwazuie na upotovu ulipo kwisha waona wameuingia?
93. Na usisimame msimamo wangu kwa kuwanasihi
kama nilivyo chukua ahadi kwako? Hukunifuata katika ahadi niliyo ahidiana nawe,
au umevunja amri yangu?
94. Harun akamwambia Musa: Ewe mwana wa mama
yangu! Usinichukulie papara kwa hasira zako, wala usizishike ndevu zangu na
kichwa changu. Hakika mimi nilikhofu lau ningeli wafanyia ukali, wakafarikiana
makundi na mapande usije ukaniambia: Umewagawanya Wana wa Israil, wala
hukuyafuata niliyo chukua ahadi kwako.
95. Musa a.s. akamwambia Msamaria: Jambo hili
jambo gani la khatari ambalo laonekana ni balaa ulilo lizua?
96. Msamaria akamwambia Musa: Nimejua ustadi wa
ufundi na mbinu zake wasizo zijua Wana wa Israil; nikawaundia sanamu la ndama
lenye kutoa sauti, na nikachukua sehemu ya Taurati nikaitia ndani ya ndama,
kuwazuga watu. Basi ndio hivyo, nafsi yangu imenizaini nifanye hayo niliyo
yafanya.
97. Musa akamwambia Msamaria: Tokana nasi, na
uwe mbali nasi. Na jaza yako duniani uwe unatanga tanga ovyo, na watu
wakikukimbia, mpaka usiwe na makhusiano na yeyote, na asiwepo ndudu ya mtu
kukukaribia, wala wewe usimkaribie mtu. Na hakika adhabu yako kesho Akhera
umewekewa kwa ahadi huwezi kuikimbia! Musa tena akimbeua
huyo mungu wake kwa kusema: Tazama sasa nini tunalo mfanyia huyu mungu wako ulio
kaa wewe ukimuabudu, na kwa sababu yake ukawafitini watu! Tutamuunguza, na kisha
tutamtawanya baharini apotelee mbali!
98. Musa akaingia kutimiza aliyo yasema, na
kisha baada ya mazingatio hayo aliwaelekea Wana wa Israili kuwaambia: Hakika
Mungu wenu ni Mmoja. Yeye ndiye ambaye hapana anaye abudiwa kwa haki isipo kuwa
Yeye. Na ujuzi wake umeenea kila kitu kilicho kuwa na kitakacho kuwa.
99. Ewe Mtume! Kama tulivyo kusimulia khabari za
Musa, tunakupa khabari za kweli za kaumu zilizo tangulia. Na Sisi
tumekuteremshia wewe Kitabu kutoka kwetu, ndani yake yamo mawaidha kwako na kwa
umma wako, ya kukufaeni katika Dini yenu na dunia yenu.
100. Mwenye kuacha kukiamini Kitabu hicho na
kufuata uwongofu wake, basi amepotea katika maisha yake, na Siku ya Kiyama
atakuja naye amebeba madhambi ya aliyo yatenda, na atalipwa kwa adhabu kali.
101. Na atadumu katika adhabu hii, na ni mzigo
muovu kweli huo Siku ya Kiyama.
102. Ewe Mtume! Watajie umma wako Siku ambayo
tutawaamrisha Malaika walipulize baragumu la kuwafufua watu kutoka makaburini,
na kuwaita hapo pa mkutano, na tutapo wachunga wakhalifu kwendea ufundoni na
nyuso zao rangi ya buluu kwa khofu na kitisho.
103. Wakinong'onezana wao kwa wao katika
udhalili na kubabaika jinsi walivyo ona maisha ya dunia ni mafupi, hata waone
kama kwamba hawajapata kustarehe nayo, na wala hawakukaa humo duniani ila siku
kumi tu!
104. Wala si kama hiyo minong'ono yao ndiyo
haisikilizani, kwani Sisi tunajua vyema wao wananong'onezana nini, na tunayajua
vyema wanayo yasema wale walio kuwa mahodari zaidi kulinganisha hisiya zao kwa
dunia, kuwa hayo maisha ya duniani ni kama kwamba hayakutimia hata siku moja.
105. Ewe Mtume! Wanakuuliza hao wanao kanya
kufufuliwa, nini hali ya milima Siku ya Kiyama hiyo unayo itaja? Wajibu:
Mwenyezi Mungu ataivuruga kama mchanga, kisha ataipeperusha kwa upepo kama
vumbi!
106. Na pahala pao baada ya kwisha vurugika
milima patakuwa sawa sawa laini.
107. Hutoona kwenye ardhi kudidimia wala
kunyanyuka, kama kwamba haikupata kukaliwa kabla yake.
108. Siku ya Kiyama watu wakisha toka
makaburini, watamfuata mwenye kuwaita mpaka pahala pa mkutano nao wamesalimu
amri. Hawezi yeyote kati yao kuelekea kulia wala kushoto. Sauti zote
zimenyenyekea kwa utulivu na kitisho kwa utukufu wake Arrahmani, Mwingi wa
Rehema. Basi husikii ila sauti ya chini kabisa ya mnong'ono.
109. Siku hiyo hapana uombezi unao faa kitu,
ila wa aliye pata hishima ya Mwenyezi Mungu kwa kuruhusiwa naye na kuridhiwa
aseme. Na hapana uombezi wa yeyote utao faa ila wa aliye pata ruhusa ya Mwenyezi
Mungu kuombea, na akawa ni Muumini, na Mwenyezi Mungu akaridhia kauli yake kwa
Tawhidi na Imani.
110. Na Mwenyezi Mungu, aliye tukuka shani
yake, anayajua mambo yao waliyo yakadimisha katika dunia yao na waliyo
yaakhirisha. Yeye Subhanahu anawapangia mambo yao kwa mujibu wa ujuzi wake. Na
wao hawaijui mipango yake na hikima zake.
111. Nyuso zitadhalilika Siku hii, na
zitamnyenyekea Mwenyezi Mungu Aliye Hai asiye kufa, Mwenye kusimamia kupanga
mambo yote ya viumbe vyake. Na amepoteza uwokofu na thawabu Siku ya Akhera
mwenye kuidhulumu nafsi yake duniani, na akamshirikisha Mola wake Mlezi.
112. Na mwenye kutenda mambo ya ut'iifu, naye
akawa anayasaidiki aliyo yaleta Muhammad, s.a.w. huyo hana khofu ya kuzidishiwa
makosa yake au kupunguziwa mema yake.
113. Na mfano wa maelezo haya ya haki yaliyo
kwisha tangulia katika Sura hii, ya kumtukuza Mwenyezi Mungu, na hadithi ya Musa
na khabari za Kiyama, Mwenyezi Mungu ameyateremsha katika Kitabu hichi cha
Qur'ani kwa lugha ya Kiarabu, na ameeleza mara kwa mara kwa njia za kuonya
ili watu waweze kutanabahi waache maasi, na Qur'ani iwazindue upya kwa kuwapa
mawaidha na mazingatio.
114. Basi ametukuka na dhana dhana, na
amejitenga na kushabihiana na viumbe, huyo Mfalme ambaye anahitajiwa na watawala
na wanao tawaliwa, Mwenye haki katika Uungu wake na Utukufu wake. Na wewe, ewe
Muhammad, usiifanyie haraka Qur'ani kabla Malaika hajakusomea. Na sema: Ewe Mola
wangu Mlezi, nizidishe ilimu kwa Qur'ani na maana zake.
115. Ewe Mtume! Sisi tulimuusia Adam tangu
mwanzo, asende kinyume na amri yetu, akasahau ahadi yetu akenda kinyume. Na
hatukumwona tangu mwanzo wake kuwa ana azma baraabara, na ukakamavu wa kutosha
asiingiliwe na Shetani akamtia wasiwasi katika nafsi yake.
116. Ewe Mtume! Na kumbuka pale Mwenyezi Mungu
alipo waamrisha Malaika wamtukuze Adam kwa njia aliyo itaka Yeye Subhanahu, na
wakafuata. Lakini Iblisi, naye alikuwa pamoja nao, alikuwa jini, akenda kinyume
akakataa, akatolewa akafukuzwa!
117. Mwenyezi Mungu akamsemeza Adam kwa
kumwambia: Hakika huyu Shetani aliye kwenda kinyume na amri yetu ya
kukuadhimisha wewe ni adui yako wewe na Hawa, mkeo. Basi tahadhari na uchochezi
wake kukuingizeni katika maasi, isije kuwa ndio sababu ya kutoka kwenu kwenye
Bustani hii, ukaja pata taabu, ewe Adam, katika maisha baada ya kutoka kwenye
Bustani.
118. Sisi tunakudhaminia mahitaji ya maisha
yako katika Bustani. Humo hutopata njaa wala hutakuwa uchi.
119. Na wala hutopata kiu, wala hutopata joto
la jua, kama wanavyo pata wanao sumbuka nje ya Bustani.
120. Shetani akamfanyia hila akimnong'oneza
katika roho yake, kumraghibisha yeye na mkewe, waule ule mti walio katazwa,
akiwaambia: Ewe Adam! Mimi nitakuonyesha mti huo, ataye kula basi ataishi
milele, na atapata ufalme usio na mwisho.
121. Akamwonyesha mti ulio katazwa. Adam na
mkewe wakakhadaika kwa kudanganywa na Iblisi, na wakasahau makatazo ya Mwenyezi
Mungu, na wakaula. Utupu wao ukadhihiri, kuwa ni malipo ya tamaa yao, mpaka
wakasahau wakaingia katika ukhalifu. Wakawa wakikata majani ya miti ya Bustani
ile ili wajisitiri utupu wao. Ikawa Adam kamkhaalifu Mola wake
Mlezi. Hayo yalikuwa kabla hajapewa Unabii. Akayakosa maisha ya milele aliyo
kuwa anayatamani, na yakaharibika maisha yake.
122. Kisha Mwenyezi Mungu alimteuwa ampe Utume,
na akaipokea toba yake, na akamwongoa atake udhuru na aombe msamaha.
123. Mwenyezi Mungu aliwaamrisha Adam na mkewe
watoke kwenye Bustani, wateremke kwenye ardhi, naye Subhanahu akawaambia kwamba
utakuwapo uadui baina ya vizazi vyao, na kwamba Yeye Subhanahu atawaongoa kwa
uwongofu na uwongozi. Mwenye kufuata uwongofu wa Mwenyezi Mungu hatoingia katika
maasi duniani, wala hatoteseka kwa adhabu.
124. Na mwenye kujiepusha na uwongofu wa
Mwenyezi Mungu na ut'iifu wake, basi ataishi maisha yasiyo na starehe, hatokinai
na chochote anacho pewa na Mwenyezi Mungu, wala hatokuwa radhi na hukumu ya
Mwenyezi Mungu na kudra yake. Mpaka ikija Siku ya Kiyama atakuja kwenye mkutano
wa hisabu atashikwa kwa madhambi yake, naye hana hoja ya kutoa, kama alivyo kuwa
duniani ni kipofu hazioni ishara zote za Mwenyezi Mungu.
125. Na kwenye mkutano huo atamuuliza Mola wake
Mlezi kwa fazaa: Ewe Mola wangu Mlezi! Vipi umenisahaulisha hoja, hata nisiweze
kujitolea udhuru, na umenisimamisha kama kipofu, na hali mimi duniani nilikuwa
naona kila kitu, nikishindana na kutetea?
126. (Naye atajibiwa:) Mambo kwako ndivyo kama
yalivyo. Zimekujilia dalili zetu, na Mitume wetu duniani; yote hayo
ukayasahau, na ukajitia upofu, na hukuamini. Na leo basi kadhaalika unaachwa
umesahauliwa umo katika adhabu na fedheha.
127. Na mfano wa malipo haya mabaya tunamlipa
duniani mwenye kutenda maasi, na akamkadhibisha Mwenyezi Mungu na ishara zake.
Na hakika adhabu za Akhera zina uchungu mkali zaidi, na zinadumu zaidi kuliko za
dunia.
128. Vipi wanajitia upofu na ishara za Mwenyezi
Mungu, na wanajua kuwa tumezihiliki kaumu nyingi zilizo tangulia kwa sababu ya
ukafiri wao, nao hawakuwaidhika kwao juu ya kuwa wao wanapita wanatembea
kwenye majumba yao na maskani zao, na wanayaona magofu yao na athari ya adhabu
zilizo wapata? Hakika mambo kama hayo peke yake ni mawaidha kwa watu wenye akili
za kufahamu.
129. Na lau kuwa haikutangulia hukumu ya Mola
wako Mlezi ya kuwaakhirishia adhabu mpaka siku ya miadi maalumu, nayo ni Siku ya
Kiyama, basi adhabu lazima ingeli wapata hapa hapa duniani kama ilivyo kwisha
wapata makafiri wa karne zilizo pita.
130. Ewe Mtume! Vumilia hayo wayasemayo ya
kukukadhibisha na kuukejeli Utume wako, na mtakase Mola wako Mlezi na yote
yasiyo mfalia kwa kumsifu, na kumuabudu Yeye pekee daima, na khasa kabla ya jua
kuchomoza, na kabla halijachwa. Na mtakase, umuabudu katika saa za usiku, na
katika ncha za mchana kwa kusali, ili yadumu mawasiliano yako na Mwenyezi Mungu,
upate kutua kwa hayo uliyo nayo, na uridhike kwa uliyo kadiriwa.
131. Wala usivuke mipaka kwa kuangalia yale
mambo ya starehe ya namna mbali mbali tuliyo waonjesha makafiri. Kwani starehe
hizi ni uzuri na pambo la duniani tu analo wafanyia mtihani kwayo Mwenyezi Mungu
waja wake. Na Mwenyezi Mungu anakuwekea wewe Akhera yaliyo bora zaidi na yenye
kudumu zaidi kuliko starehe hizi.
132. Na waelekeze ahli zako washike Sala kwa
nyakati zake. Kwani Sala ni kiungo chenye nguvu kabisa cha kuwaunganisha na
Mwenyezi Mungu, na kudumu kuishika Sala kwa nyakati zake ndio ukamilifu. Sisi
hatukulazimishi ujiruzuku nafsi yako, bali ni Sisi ndio kazi yetu kukuruzuku. Na
hakika mwisho wa kusifiwa duniani na Akhera ni wa watu wema na wenye kumcha
Mungu.
133. Na makafiri katika inadi yao wanasema: Kwa
nini Muhammad hatuletei dalili inayo toka kwa Mola wake Mlezi inayo tulazimisha
sisi kumuamini? Na vipi wao wanaipinga Qur'ani, nayo imewajia hali imekusanya
yaliyomo katika Vitabu vilivyo tangulia katika khabari za watu walio pita, na
maangamizo yao kwa sababu ya kuwakadhibisha Mitume? Na Muhammad si wa kwanza
katika hayo!
134. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu ange wafanyia
haraka kuwahiliki makafiri hawa, kabla ya kumtuma Muhammad kwao, wange toa
udhuru Siku ya Kiyama kwa kusema: Ewe Mola wetu Mlezi! Kwa nini hukutuletea
Mtume duniani mwenye ishara tumfuate, kabla hujatuteremshia adhabu na hizaya
Akhera? Lakini sasa hawana udhuru wowote baada ya kutumiwa Mtume.
135. Ewe Mtume! Waambie hawa wenye inda: Hakika
sisi sote tunangojea yatavyo kwenda mambo yetu na yenu. Na mtajua kwa hakika
nani katika makundi mawili walio watu wa Dini ya Haki, na wenye kuongoka kwa
uwongofu wa Mwenyezi Mungu.