1. Hizi harufi moja moja za kutamkwa zinaonyesha kuwa Qur'ani ni muujiza ulio undwa kwa harufi, na pia ni kuwazindua watu waisikilize.
 

2. Ewe Mtume! Hizi ni hadithi za Mola wako Mlezi kwa rehema yake kueleza kisa cha mja wake na Nabii wake, Zakariya.
 

3. Pale alipo muelekea Mwenyezi Mungu na akamwomba kwa siri wasijue watu.
 

4. Akasema: Mola wangu Mlezi! Mimi nimekwisha dhoofika, na kichwa changu kimejaa mvi. Na mimi sikuwa na bahati mbaya pale ninapo kuomba, bali bahati yangu siku zote ni nzuri, unaniitikia ninapo kuomba.
 

5. Na mimi ninaogopa kuwa jamaa zangu hawatashika vyema amri za Dini baada ya kufa kwangu. Na mke wangu bado ni tasa, hazai. Basi niruzuku mwana, kwa fadhila yako, atakaye shika pahala pangu kwa watu wangu baada yangu.
 

6. Anirithi ilimu na Dini. Na awarithi Ukoo wa Yaaqub ufalme. Ewe Mola wangu Mlezi! Na mjaalie awe maridhia kwako na kwa watu.
 

7. Akaitwa: Ewe Zakariya! Sisi tunakubashiria khabari nzuri kuwa utapata mwana, na jina tumemwita: Yahya. Hatujapata kumwita mtu yeyote kwa jina hilo kabla yake.
 

8. Zakariya akasema kwa mastaajabu: Ewe Mola wangu Mlezi! Vipi nipate mwana, na hali mke wangu ni tasa, na mimi nimo katika miaka ya ukongwe?
 

9. Mwenyezi Mungu akamfunulia mja wake, Zakariya: Mambo ni kama ulivyo bashiriwa, na kwamba kupewa wewe mtoto juu ya ukongwe wako na utasa wa mkeo ni jambo jepesi kwangu Mimi. Wala usiyaone hayo kuwa ni ya mbali hayawezi kuwa. Kwani Mimi nilikuumba wewe kabla yake, na hali hukuwa kitu chochote.
 

10. Zakariya akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nijaalie alama ya kuonyesha kuwa nitapata hayo uliyo nibashiria.  Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Alama yako ni kuwa hutaweza kusema muda wa masiku matatu, nawe ni mzima wa hisiya na ulimi.
 

11. Zakariya akawatokea watu wake kutoka kwenye msala, na akawaashiria wamtakase Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni.
 

12. Yahya akazaliwa, akakua, na kisha akapata wito, na akaamrishwa ayatende yaliomo katika Taurati kwa juhudi na kuazimia. Na Mwenyezi Mungu alimpa utotoni mwake ilimu ya Dini na kufahamu hukumu za sharia.
 

13. Mwenyezi Mungu akampa tabia ya huruma, na utukufu wa nafsi, na akamjenga katika uchamungu.
 

14. Na Mwenyezi Mungu alimjaalia mwema mno kwa wazazi wake wote wawili, na akiwafanyia hisani. Wala hakumfanya awe jeuri kwa watu, wala awe mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu.
 

15. Na salama na amani iwe kwake, asipatikane na madhara wala maudhi siku ya kuzaliwa kwake, na siku ya kufa kwake, na siku atapo fufuliwa kuwa hai tena.
 

16. Ewe Mtume! Taja katika Qur'ani hadithi ya Maryamu, pale alipo jitenga na jamaa zake na watu wote, akenda upande wa mashariki ya pale alipo kuwepo.
 

17. Akafunga pazia baina yake na hao watu. Mwenyezi Mungu akamtuma Jibril amwendee kwa sura ya mwanaadamu kaamili, ili asishituke kumwona kwa sura yake ya Malaika ambayo hakuizoea.
 

18. Maryamu akasema: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, anikinge nawe, ikiwa unatarajiwa umche Mwenyezi Mungu, na umwogope.
 

19. Malaika akasema: Mimi si lolote ila nimetumwa na Mola wako Mlezi niwe ni sababu ya kuwa wewe upate mwana aliye safi wa kheri.
 

20. Maryamu akasema: Vipi nipate mwana na hajanikaribia mwanamume yeyote, na mimi si kahaba?
 

21. Malaika akasema: Mambo ni kama unavyo sema: Hakukugusa mwanamume. Mola wako Mlezi amesema: Kukupa mwana bila ya baba ni jambo jepesi kwangu, na hilo liwe ni Ishara kwa watu ya kuonyesha ubora wa uwezo wetu, kama ilivyo kuwa ni rehema kwa mwenye kufuata uwongofu wake. Na huku kuumbwa kwa Isa ni amri iliyo kwisha kadiriwa, ni lazima iwe.
 

22. Matakwa ya Mwenyezi Mungu yakatimia. Maryamu akachukua mimba ya Isa kwa namna alivyo itaka Mwenyezi Mungu. Akatoka na mimba yake akenda pahala mbali na watu.
 

23. Machungu ya uzazi yakamchukua mpaka kwenye shina la mtende   alitegemee, na apate kujisitiri. Akawaza vipi watavyo udhika watu wake naye kwa haya; akatamani afilie mbali, asahaulike kabisa, wala asitajike.
 

24. Malaika akamtangazia kutoka pahala kwa chini yake: Usihuzunike kwa upweke wako, na kukosa chakula na cha kukinywa, na maneno ya watu. Mwenyezi Mungu kesha jaalia karibu nawe kijito kidogo.
 

25. Na hebu tikisa huo mtende, zitakuangukia tende mbivu nzuri.
 "Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia tende nzuri zilizo mbivu." Imethibiti kuwa tende, khasa zile rat'ab, yaani "fresh" zina faida kubwa sana katika mwili, na nyepesi katika tumbo.
 

26. Basi kula hizo tende na kunywa maji hayo, na tua roho yako. Na ukikutana na mtu yeyote ambaye hakupendezewa na hali yako hii, basi muashirie kuwa wewe umo katika saumu, na husemi na mtu.
 

27. Maryamu akenda kwa watu wake naye kambeba Isa. Wakamwambia kwa mastaajabu na kuudhika: Umefanya kitendo kiovu!
 

28. Ewe wa kizazi cha Harun, aliye kuwa Nabii Mchamngu Mahashumu! Vipi umefanya uliyo yafanya na baba yako hakuwa na tabia mbovu, wala mama yako hakuwa kahaba!
"Ewe dada wa Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba." Imeandikwa katika Encyclopaedia Britannica kuwa Qur'ani imekosea kosa la kihistoria ilipo mwita Maryamu "Dada wa Harun," ilihali baina ya Maryamu huyu na Harun nduguye Musa ni karne nyingi. Wamesahau hawa kuwa Udugu kwa Kiarabu upo kwa kushabihiana. Makusudio ya hapa ni kushabihiana kwa wema na kuchamngu, yaani ewe uliye mshabihi Harun kwa wema na uchamngu, nini kilicho kugeuza hali yako njema ukawa hivyo? Wala baba yako hakuwa mtu muovu wa kutenda mabaya, wala mama yako kufanya uchafu. (Kadhaalika Maryamu ni ukoo wa Harun, na pengine huitwa "Binti wa Imran", na Imran ni baba yake Harun.)
 

29. Akawaashiria yule mtoto waseme naye. Wakasema: Vipi tuzungumze na mtoto mchanga ambaye bado yumo katika ubeleko?
 

30. Isa alipo sikia maneno yao Mwenyezi Mungu alimtamkisha akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Atanipa Injili, na ataniteuwa niwe Nabii.
 

31. Atanijaalia na baraka, nikifunza kheri, na nikiwafaa watu, na ananiamrisha nishike Sala, na nitoe Zaka muda wa uhai wangu.
 

32. Kama alivyo niamrisha niwe mwema kwa mama yangu, wala hakunifanya niwe jabari kwa watu, wala mwenye kumuasi Yeye.
 

33. Na amani iwe juu yangu kutokana na Mwenyezi Mungu siku ya kuzaliwa kwangu, na siku ya kufa kwangu, na siku ya kufufuliwa kwangu nikawa hai tena.
 

34. Huyo mwenye kusifiwa kwa sifa hizo ndiye Isa bin Maryamu. Na hii ndiyo kauli ya kweli iliyo mkhusu yeye wanayo ipinga wapotovu  na wakamtilia shaka unabii wake hao wenye kutia shaka.
 

35. Wala haifai wala haingii akilini kuwa Mwenyezi Mungu awe na mwana. Yeye ametakasika na hayo! Shani yake Subhanahu ni akipitisha hukumu ya jambo lolote basi alitakalo huwa bila ya muhali, kwa tamko tu la kusema: Kuwa! Na hilo jambo huwa.
 

36. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wangu, na ndiye Bwana wenu. Basi muabuduni Yeye. Wala msimshirikishe na yeyote. Hii ninayo kuitieni ndiyo Njia itakayo kufikishieni kwenye mafanikio.
 

37. Na juu ya iliyo kwisha tangulia katika kauli ya haki iliyo mkhusu Isa, watu wa Biblia wamekhitalifiana wao kwa wao, na wakazua madhehebu mbali mbali. Na makafiri watapata adhabu kali watapo hudhurishwa Siku ya Hisabu, na wakashuhudia msimamo wa Kiyama, na wakakuta malipo maovu kabisa.
 

38. Watakuwa na masikio makali, na macho yenye nguvu siku watakayo kutana na Mwenyezi Mungu! Lakini wao hii leo duniani kwa kujidhulumu nafsi zao, na kuacha kwao kunafiika kwa kusikia na kuona, wamo katika upotovu wa kuiacha haki, na hayo ni dhaahiri isiyo na uficho.
 

39. Ewe Mtume! Wahadharishe hawa wenye kudhulumu na siku watakayo juta kwa kupindukia kwao mipaka katika haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya nafsi zao wenyewe! Na hapo hisabu yao itakuwa imekwisha, na malipo wamekwisha yapata! Na hali huko duniani walikuwa wameghafilika na Siku hiyo, hawakusadiki kuwa kutakuwako kufufuliwa na kulipwa.
 

40. Hebu jamani! Nawajue watu kuwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye mrithi wa kuurithi ulimwengu wote na kila kiliomo ndani yake. Na hisabu yao wote ni juu ya Mwenyezi Mungu.
 

41. Ewe Mtume! Watajie watu katika Qur'ani hadithi ya Ibrahim. Hakika yeye alikuwa mtu mkweli kabisa, katika kauli yake na vitendo vyake, na mwenye kueleza vilivyo khabari za Mwenyezi Mungu.
 

42. Na taja pale Ibrahim alipo msemeza baba yake kwa upole akimwambia: Ewe baba yangu! Vipi unayaabudu masanamu yasiyo sikia wala hayaoni, wala hayawezi kukuletea kheri wala kukukinga na shari?
 

43. Ewe baba yangu! Mimi yamenijia kwa njia ya ufunuo (wahyi) wa Mwenyezi Mungu ambayo wewe hukuyapata, ya kumjua Mwenyezi Mungu, na kujua yanayo mlazimu mwanaadamu kwa Mola wake Mlezi. Basi nifuate mimi kwa hayo ninayo kuitia ya Imani, nitakuonyesha Njia Iliyo Nyooka itakayo kufikisha kwenye haki na mafanikio.
 

44. Ewe baba yangu! Usimt'ii Shetani anaye kuzaini uabudu masanamu. Ni mtindo wa Shetani kumuasi Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema na kuikhalifu amri yake.
 

45. Ewe baba yangu! Mimi nakuogopea ukiendelea na ukafiri utapatilizwa kwa adhabu kali kutokana na Mwingi wa Rehema, ukawa mwenzio ni Shetani Motoni, wewe unamkaribia, na yeye anakukaribia.
 

46. Baba akasema  kumwambia Ibrahim naye kakasirika naye, akimtolea ndaro: Yawaje unawawacha miungu yangu, ewe Ibrahim, na unanitaka nimuabudu Mungu wako? Kama hukusita kuwatukana masanamu basi hapana shaka nitakupiga kwa mawe. Tahadhari nami! Niondokelee kwa muda mrefu, mpaka nipoe hamaki zangu.
 

47. Ibrahim bado akamtwaa pole baba yake akamwaga kwa kusema: Salamun A'laika!  Amani iwe juu yako! Nitamwomba Mola wangu Mlezi akuongoe na akusamehe. Na Mola wangu Mlezi amenizoeza kuwa na huruma nami, na kuwa karibu nami.
 

48. Na hivyo mimi basi nakuondokeeni, na najitenga na hiyo miungu mnayo iabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Nami namuabudu Mola wangu Mlezi tu peke yake, kwa kutaraji kuwa apokee ut'iifu wangu, wala yasipotee matarajio yangu.
 

49. Ibrahim alipo jitenga na baba yake na kaumu yake na miungu yao, Mwenyezi Mungu alimkirimu kwa kumpa dhuriya wema, juu ya kuwa alikuwa kesha kata tamaa ya kupata watoto. Kwani yeye na mkewe walikwisha kuwa ni wakongwe, si wa kuzaa tena. Mwenyezi Mungu akawatunukia Is-haq, na kutokana na Is-haq akazaliwa Yaaqub, na akawateuwa wote wawili wawe Manabii.
 

50. Na tukawapa, juu ya cheo cha Unabii, kheri nyingi za Dini na dunia kwa rehema zetu. Na tukawarithisha duniani makumbusho mema ya daima kwa ulimi wa kweli mtukufu wa kutaja sifa zao.
 

51. Ewe Mtume! Wasomee watu katika Qur'ani hadithi ya Musa. Yeye alikuwa ni mwenye niya safi kwa nafsi yake, na moyo wake, na mwili wake, kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu alimteuwa  kwa kumpa Unabii na Utume.
 

52. Nasi tulimtukuza, na tukamwita kwenye Mlima wa T'ur. Musa akasikia huo wito wa Mwenyezi Mungu kwa upande wa kulia. Nasi tukamkaribisha kwa kumtukuza, na tukamteuwa ili tunong'one naye.
 

53. Tukampa rehema yetu na neema yetu, na tukamchagua pamoja naye nduguye Harun awe Nabii vile vile, ili amsaidie kufikisha ujumbe.
 

54. Ewe Mtume! Wasomee watu yaliyomo katika Qur'ani katika kisa cha Ismail. Hakika yeye alikuwa ni mkweli wa kutimiza ahadi yake.  Na alimuahidi baba yake kuwa atasubiri pindi akimchinja kama alivyo amrishwa na Mwenyezi Mungu. Na akatimiza ahadi yake, na Mwenyezi Mungu akamtolea fidia kondoo badala yake na akamtukuza kwa kumpa Utume na Unabii.
 

55. Na alikuwa akiwaamrisha watu wake kushika Sala na kutoa Zaka, na akawa katika makamo matukufu katika kumridhi Mola wake Mlezi.
 

56. Ewe Mtume! Wasomee watu yaliyomo katika Qur'ani hadithi ya Idris. Dasturi yake ilikuwa ni ukweli wa kauli, na vitendo, na a'mali. Na Mwenyezi Mungu alimpa utukufu wa Unabii.
 

57. Na kwa hayo Mwenyezi Mungu alimnyanyua cheo cha juu.
 

58. Hao walio kwisha tajwa, ni miongoni alio waneemesha Mwenyezi Mungu katika Manabii, katika dhuriya wa Adam na dhuriya wa tulio waokoa pamoja na Nuhu na dhuriya wa Ibrahim kama Ismail; na katika dhuriya wa Yaaqub, kama Manabii wa Wana wa Israil; na miongoni tulio waongoa kwenye Haki na tukawachagua walinyanyue Neno la Mwenyezi Mungu.. Hawa pindi wakisikia Aya za Mwenyezi Mungu wanasomewa huingia khofu, na huanguka mpaka chini wakimsujudia Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu.
 

59. Tena baada ya wateuliwa hawa wakatokea wa vizazi vingine wasio kuwa waongofu kama hao. Wakaacha Sala, wakapuuza kunafiika na uwongofu wake, na wakashughulikia maasi. Hawa, basi, watakuja kuta malipo ya maasi yao na upotovu wao duniani na akhera.
 

60. Lakini watao zidiriki nafsi zao kwa kutubia, na kwa Imani ya kweli, na vitendo vyema, basi Mwenyezi Mungu ataipokea toba yao na atawaingiza Peponi, na atawalipa sawa ujira wao.
 

61. Bustani hizo za Peponi ni makaazi ya milele kwa mujibu wa ahadi ya Arrahmani, Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, kuwaahidi waja wake walio tubia, na wakamuamini kwa ghaibu, bila ya kumwona. Basi wao wataingia humo bila ya shaka yoyote, kwani ahadi ya Mwenyezi Mungu haina kinyume.
 

62. Na hao katika Bustani hizo za Peponi hawatakuwa na mazungumzo ya upuuzi, wala hawatasikia ila kheri na amani. Na riziki yao ni tele na imedhaminiwa haina ukomo.
 

63. Na hakika Mwenyezi Mungu huwapa Pepo hiyo iwe yao wale ambao duniani walikuwa ni wachamngu, wakaacha maasi na wakatenda mema yanayo stahiki.
 

64. Na wakati wanapo ingia wakatulia humo husema kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu: Hatukuingia Peponi, wala hatuondoki  kutoka hapa kwenda penginepo, ila kwa amri ya Mwenyezi Mungu na fadhila yake. Kwani Yeye, Subhanahu, ndiye Mwenye kumiliki, Mwenye kudabiri, na Mwenye kujua ya mbele yetu na ya nyuma yetu. Wala Yeye Mwenyezi Mungu hasahau kutimiza ahadi yake aliyo waahidi waja wake wachamngu.
 

65. Kwani Yeye, Subhanahu, ndiye Muumba, na Mwenye kumiliki mbingu na ardhi na viliomo baina yake; na ndiye Mwenye kuyaendesha mambo yao yote; na ndiye peke yake Mwenye kustahiki kuabudiwa. Basi muabudu Yeye tu; na ushikilie kumuabudu, nawe hali umesubiri na umetua. Kwani Yeye, Subhanahu, ndiye Mwenye kustahiki peke yake kuabudiwa, wala hana mwenzie anaye stahiki kuabudiwa, au kuitwa kwa jina lake.
 

66. Na mwanaadamu kwa mastaajabu kuwa atafufuliwa husema: Vipi nitafufuliwa niwe hai tena, baada ya kwisha kufa na kuteketea?
 

67. Vipi huyu binaadamu anamstaajabia Mwenyezi Mungu kuweza kumfufua Akhera, na hakumbuki kwamba Yeye Mtukufu alimuumba duniani naye hakuwa chochote, na hali kurejesha kuumba ni jambo jepesi kuliko kuanza kuumba hapo mwanzo, ukipima kwa akili.
 

68. Ikiwa hili jambo la kufufuliwa linaonekana ni geni, wanalikataa makafiri, basi naapa kwa Aliye kuumba na akakulea, na akakukuza, Siku ya Kiyama tutawakusanya makafiri pamoja na mashetani wao, walio wazaini hata wakauona ukafiri mzuri, tutawakusanya wote kuizunguka Jahannamu, nao wamepiga magoti kwa udhalili na wingi wa kitisho na kufazaika.
 

69. Kisha kwa yakini kutoka kila kikundi tutawatoa wale walio shadidi ya ukafiri kumkufuru Mwenyezi Mungu na kumuasi, tutawapeleka wao mbele kwenye adhabu iliyo kali kabisa.
 

70. Na Sisi tunawajua vyema zaidi kati yao wanao stahiki kuingia Motoni na kuungua humo.
 

71. Na enyi viumbe! Hapana yeyote kati yenu ila atahudhuria hapo. Muumini atauona Moto na atapita, na kafiri atatumbukia. Amri hii lazima itimizwe, hukumu ya Mwenyezi Mungu imekwisha pita.
 

72. Tena kwa rehema yetu, tutawakusanya wachamngu na tutawaokoa na Jahannamu. Na tutawaacha humo wale walio dhulumu nafsi zao, wakipiga magoti, kwa kuwaadhibu.
 

73. Na walikuwa makafiri duniani pindi wakisomewa Aya za Mwenyezi Mungu zenye kueleza wazi, wakizipuuza, na wakiwaambia Waumini kwa majivuno ya mali yao na watu wao: Nyinyi si kama sisi katika dunia. Sisi tuna cheo bora zaidi kuliko nyinyi, na hadhi zetu mabarazani ni kubwa zaidi. Hali kadhaalika itakuwa hali yetu Akhera mnayo iamini nyinyi.
 

74. Ingeli wafalia hawa makafiri wange waidhika kwa yaliyo wapata watu wengi walio watangulia. Wao walimkufuru Mwenyezi Mungu, na wakawa na cheo bora zaidi katika dunia, na starehe nyingi zaidi, na wakipendeza kuwaangalia. Na Mwenyezi Mungu akawateketeza kwa ukafiri wao - nao ni wengi. Na katika mabaki yao pana mafunzo kwa mwenye kuzingatia.
 

75. Ewe Mtume! Waambie hawa: Aliomo katika upotovu na ukafiri Arrahmani, Mwingi wa Rehema, humpa muhula, akamkunjulia umri, azidi ujabari wake na upotovu wake. Na makafiri huwakariria Waumini kauli kwa kusema: Kundi gani, baina yetu na nyinyi, lenye hadhi zaidi na bora katika mabaraza na majlisi? Mpaka watakapo ona yale walio ahidiwa, nayo ama kuadhibiwa na Waislamu duniani kwa kuuwawa na kutekwa, au kupata hizaya ya Siku ya Kiyama. Hapo tena watajijua kuwa hadhi yao ni duni, na msaada wao ni dhaifu.
 

76. Ama wenye kuamini Ishara za Mwenyezi Mungu, pindi wakizisikia tu wanazikubali. Na Mwenyezi Mungu huwazidishia tawfiki kwa vitendo vyao vizuri. Na vitendo vyema ni bora na vinadumu zaidi kwa Mwenyezi Mungu kwa malipo, na kuwa mwisho wake ni mwema.
 

77. Yafaa ustaajabu, ewe Mtume, huu mtindo wa anaye kanya Ishara za Mwenyezi Mungu. Mtu huyu amefitinika na dunia yake, akakanya kufufuliwa, akasema, kwa maskhara: Hakika Mwenyezi Mungu atanipa Akhera hiyo mnayo dai mali na wana nitafakhari nayo huko. Naye anadhani kuwa Akhera ni kama dunia, hukisiwa ya huko kama yalivyo huku. Amesahau kuwa huko ni malipo ya mema na mabaya, na kwamba kuzidiana huko ni kwa vitendo vyema.
 

78. Kwani huyo kafiri ameijua siri ya ghaibu, hata aieleze kwa ukweli? Na kwani amechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwa hayo hata awe na tamaa?
 

79. Basi na ayaache hayo anayo yazua. Kwani Sisi tunamhisabia uzushi wake, na atakuta adhabu yake imekunjuliwa muda mrefu kuliko anavyo fikiri.
 

80. Mwenyezi Mungu atampokonya yote anayo tafakhari nayo duniani, mali na wana; na atamteketeza. Na atakuja Akhera, peke yake, mtupu, hana mali wala mwana wala msaidizi.
 

81. Hao makafiri wamewafanya miungu mingine mbali mbali badala ya Mwenyezi Mungu wakaiabudu, ili wawe ndio waombezi wao Akhera.
 

82. Yawapasa waachilie mbali hayo wanayo yadhani. Hiyo miungu itakuja wapinga ibada yao na wataikanya. Na hiyo miungu itakuwa ndio makhasimu wa washirikina, na itaomba waadhibiwe.
 

83. Ewe Mtume! Hujui kama Sisi tumewapa madaraka mashetani juu ya makafiri - nao wamewazuga hawa makafiri - wanawaghuri na huwapelekea kwenye maasi waiache haki na wawafuate wao.
 

84. Basi ewe Mtume! Usiingie dhiki moyo wako kwa ukafiri wao, wala usiwatakie adhabu ya haraka. Kwani Sisi tunawawacha hivi duniani kwa muda wenye kiwango maalumu, na tunawadhibitia  a'mali zao na madhambi yao, ili Akhera tuwahisabie.
 

85. Ewe Mtume! Itaje Siku tutapo wakusanya wachamngu kuwapeleka Peponi makundi kwa makundi yaliyo tukuzwa.
 

86. Na tutawachunga wakosefu kuwasukumia Jahannamu nao wamebanwa na kiu, kama wanavyo chungwa wanyama kwenda kwenye maji.
 

87. Na hapana ataye kuwa na mamlaka ya uombezi Siku hiyo yeyote isipo kuwa aliye pata ruhusa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ahadi aliyo mpa.
 

88. Washirikina, na Mayahudi, na Wakristo wamesema: Mwenyezi Mungu amejifanyia mwana kutokana na Malaika au kutokana na watu.
 

89. Enyi mlio sema hivyo, mmeleta jambo linalo chusha mno! Linalo chusha katika akili iliyo kaa sawa.
 

90. Mbingu zakaribia kupasuka kwa hayo, na ardhi kudidimia, na milima kuanguka mapande mapande!
 

91. Vituko hivyo vya mbingu, na ardhi, na milima, vyakaribia kutokea kwa sababu ya kumbandikiza Mwenyezi Mungu mwana!
 

92. Wala hayaingii akilini kuwa Mwenyezi Mungu awe na mwana; kwani kuthibiti kuwa na mwana Yeye inahitajia awe Yeye ni mwenye kuzuka, mwenye mwanzo na mwisho, na kuwa Yeye awe na haja ya mwana.
 

93. Hapana yeyote aliomo mbinguni na kwenye ardhi  ila atamjia Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Siku ya Kiyama hali naye ni mtumwa wake mwenye kuunyenyekea Ungu wake.
 

94. Ujuzi wake umewaenea wao wote na wanayo yatenda. Hapana aliye fichikana kwake, wala chochote katika vitendo vyao.
 

95. Na wote hao watamjia Siku ya Kiyama hali ni wapweke, hawana wasaidizi wa kuwasaidia, wala wana, wala mali.
 

96. Hakika Waumini wenye kutenda mema Mwenyezi Mungu anawapenda, na anawapendezesha kwa watu.
 

97. Na hakika Sisi tumeifanya hii Qur'ani kuwa ni nyepesi, kwa lugha yako, ili kwa radhi ya Mwenyezi Mungu na neema zake uwape bishara nzuri wanao fuata amri zake, na wakaepuka makatazo yake. Na pia upate kuwaonya kwa hii Qur'ani wale wanao ipinga na wakakazana  kuifanyia khasama, kuwa watapata ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu zake.
 

98. Ewe Mtume! Isikuhuzunishe inadi yao  kwako. Kwani Mwenyezi Mungu amekwisha wahiliki kabla yao kaumu kadhaa wa kadhaa katika vizazi vilivyo tangulia. Wote wamemalizika. Huwaoni hata mmoja wao, wala huwasikii sauti yao.