1. Kuhimidiwa, yaani kusifiwa na
kushukuriwa kwa wema, anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye
amemteremshia mja wake, Muhammad, hii Qur'ani. Na wala hakujaalia kuwa ndani
yake kipo chochote cha dosari, kilicho kwenda kombo na kuacha usawa. Bali ndani
yake mna Haki tupu, isiyo na shaka yoyote.
2. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia Qur'ani
imesimama, imenyooka sawa sawa katika mafunzo yake ili kuwaonya wanao kufuru na
kukataa, kuwa watapata adhabu kali itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na iwape bishara
njema wanao isadiki, ambao wanatenda vitendo vyema, ya kwamba watapata malipo
mazuri.
3. Malipo hayo ni Pepo watakayo kaa humo milele.
4. Na kiwaonye kwa njia makhsusi wale walio
msingizia Mwenyezi Mungu kuwa ana mwana, na hali Yeye ametakasika kuwa kama
viumbe, akawa mwenye kuzaa au akazaliwa mtoto wake.
5. Wala wao hawana ujuzi wowote wa hayo wala baba
zao hawakuwa nao huo. Ni uzushi mkubwa mno huu wa kutoa neno hili vinywani mwao!
Wayasemayo ni uzushi, na wala hapana uzushi mkubwa kushinda huu.
6. Ewe Nabii! Usijihiliki nafsi yako bure kwa
kuhuzunika na kusikitika kwa kuacha kwao kuitikia Wito wako, na kuisadiki hii
Qur'ani.
7. Sisi tumewaumba kwa kheri na shari, na
tumevifanya vilio juu ya ardhi ni pambo lake kwa ajili ya manufaa ya watu wake.
Hivyo tunawatendea vitendo kama ni mtihani wapate kudhihiri kati yao wenye
a'mali njema. Basi aliye pumbazwa na ulimwengu, na asiishughulikie Akhera, huwa
amepotea. Na aliye iamini Akhera, huyo huwa ameongoka.
8. Baada ya kumalizika dunia Sisi tutavifanya
vyote vilio juu ya dunia kama ardhi tambarare isio na mimea baada ya kuwa
imeamirika kwa mazao ya kijani yenye uhai.
*
9. Walio pumbazwa na starehe za dunia wanakanya
kufufuliwa, ilihali hakika ya mambo inathibitisha pana uhai baada ya usingizi
mrefu. Na hichi kisa cha Watu wa Pangoni kwenye mlima na bao lilio andikwa
majina yao baada ya kufa kwao hakikuwa ni ajabu ya pekee, tukaziacha ishara zote
nyenginezo. Ijapo kuwa kisa hicho si cha kawaida, lakini hakikuwa ndio cha ajabu
kushinda ishara zetu nyengine zenya kuonyesha uweza wetu.
10. Taja pale walipo kwenda hao vijana kwenye
pango, wakafanya hapo ndipo pahali pa kujificha baada ya kukimbia ushirikina na
washirikina kuhifadhi Dini yao. Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Tupe maghfira
kutoka kwako, na utulinde na adui yetu, na tusahilishie hidaya na tawfiki katika
mambo yetu!
11. Tukaipokea dua yao hiyo, tukawalaza kwa
salama katika hilo pango kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa.
12. Kisha Mwenyezi Mungu aliwaamsha baada ya
kulala kwa muda mrefu, ili matokeo yake yawe ni kudhihirisha ujuzi wetu ni nani
katika makundi mawili aliye sibu kukisia muda wa kulala kwao.
13. Ewe Mtume! Sisi tunakusimulia khabari zao
kweli kweli: Hakika hao walikuwa vijana katika zama zilizo pita ambao walikuwa
wameshika Dini ya Haki. Walimuamini Mola wao Mlezi kuwa ni Mmoja tu, na ilihali
wamezungukwa na washirikina. Na Sisi tukawazidisha wawe na yakini.
14. Na tulizithibitisha nyoyo zao juu ya Imani
na subira ya kuvumilia shida, pale walipo simama mbele ya watu wao wakasema kwa
kujifunga kwa ahadi: Ewe Mola wetu Mlezi! Wewe ndiye wa Haki, Mola Mlezi wa
mbingu na ardhi! Sisi hatumuabudu mungu mwenginewe. Wala hatutoiwacha itikadi
hii. Wallahi! Tukisema jenginelo basi itakuwa tunasema lilio mbali kabisa na
kweli!
15. Kisha wakaambiana wenyewe kwa wenyewe: Hawa
watu wetu wamemshirikisha Mwenyezi Mungu. Lau kuwa wameleta hoja iliyo wazi ya
kuthibitisha ungu wa hivyo wanavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Hakika watu
hawa ni wenye kudhulumu kwa vitendo vyao hivyo. Wala hapana aliye zidi udhaalimu
kuliko mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo kwa kumsingizia washirika.
16. Na wakaambiana wao kwa wao: Maadamu sisi
tumejitenga nao hao katika ukafiri wao na ushirikina wao, basi kimbilieni
pangoni mlinde Dini yenu. Mola wenu Mlezi atakukunjulieni maghfira yake, na
atakusahilishieni mambo yenu kwa njia za kukufaeni katika maisha yenu.
Haijuulikani kwa hakika ni nani hao Ahlil Kahf, wala zama zao, wala
hilo pango lipo wapi walilo kimbilia hao vijana. Pamoja na hayo hapana ubaya
kuchunguza, huenda pakapatikana mwangaza japo kidogo juu yake. Ilivyo kuwa
Qur'ani Tukufu imetaja kuwa hao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi
basi hapana budi kuwa wao na watu wao waliteswa kwa sababu ya Dini, hata wakaona
hao vijana wakimbilie pangoni kujificha. Na Taarikhi ya zamani inataja kuwa
yalikuwako mateso ya dini katika nchi za Mashariki ya kale yaliyo tokea nyakati
mbali mbali. Tutataja katika yafuatayo mateso mawili huenda moja wapo likaelekea
na kisa hichi:-
Ya kwanza yalitokea zama za mfalme wa Kisaluki,
Antiokhus IV, aliye itwa kwa jina la kupanga Nabivanis (kiasi ya 176-84 K.K.).
Huyo alipo shika ufalme wa Shamu, na akawa amemili mno kwenye ustaarabu wa
Kigiriki na ilimu zake, aliwalazimisha Mayahudi wa Palistina, nayo ilikuwa chini
ya Shamu tangu mwaka 194 K.K. washike dini ya Kigiriki, na akavunja sharia zao,
na akanajisi Hekalu lao kwa kuweka humo sanamu la Zeus, mungu mkuu wa Magiriki,
juu ya madhibahu (kibulani), na kumtolea mihanga ya nguruwe humo. Tena huyo
mfalme aliteketeza kwa moto nakla za Taurati zote alizo zipata. Kwa mwangaza huu
yaonekana kuwa hawa vijana walikuwa ni Mayahudi, na kwao ni popote katika
Palastina, au khasa ni katika Yerusalemu. Na ikawa wakaamka mnamo mwaka 126 B.K.
zama za utawala wa Warumi wa Mashariki. Yaani kabla ya kuzaliwa Mtume Muhammad
s.a.w. (nako kulikuwa kiasi mwaka 571 B.K.) kwa kiasi ya miaka mia nne na
arubaini na tano takriban.
Ama mateso ya pili yalitokea zama za
Mfalme wa Ufalme wa Kirumi, Hadriatus (117-138). Mfalme huyu aliwatenda Mayahudi
kama alivyo watendea Antiokhus tuliye kwisha mtaja sawa sawa. Matokeo ya hayo ni
kuwa Mayahudi walitangaza uasi dhidi ya utawala wa Kirumi mwaka 132.
Wakawafukuza askari wa ulinzi wa Kirumi, wakaiteka Yerusalemu, na wakatoa sarafu
yao ya makumbusho ya ugombozi wa Mji Mtakatifu. Wakashika khatamu za utawala kwa
muda wa miaka mitatu. Mwishoni Hadriatus na jeshi lake wakagutuka,
wakaushinda uasi, na wakairudisha Palastina chini ya ut'iifu, na wakairudisha
Yerusalemu, na wakauvunjilia mbali uwananchi wa Kiyahudi kabisa. Viongozi wa
Mayahudi wakauwawa na Mayahudi wakauzwa sokoni kuwa watumwa. Matokeo ya hayo ni
kuwa mambo yote ya Kiyahudi aliyapiga marfuku Hadriatus na akapiga marfuku
mafunzo ya Kiyahudi na sharia zao.
Kwa mujibu wa mwangaza huu wa
taarikhi yaonekana kuwa vijana hawa walikuwa ni Mayahudi, na pahala pao ni
popote katika Mashariki ya kale, au katika Yerusalemu yenyewe. Yaonekana kuwa
waliamshwa mnamo mwaka 435 B.K., yaani kabla ya kuzaliwa Mtume wetu s.a.w. kwa
miaka mia na thalathini. Yaonekana kuwa yale mateso ya mwanzo yameelekeana zaidi
na kisa hichi cha Watu wa Pangoni, kwa sababu yalikuwa ni ya shida zaidi. Ama
mateso ya Kikristo hayaelekeani na kuzaliwa kwa Mtume s.a.w.
17. Na lile pango lilikuwa kwenye mlima, lina
nafasi ndani. Lilielekea kaskazini, linapigwa na upepo mzuri. Jua likichomoza
muanga wake huwa kuliani mwao, na miale yake huwa mbali nao; na likichwa
huwa kushotoni mwao. Kwa hivyo lile jua halipigi ndani ya pango, na kwa hivyo
walisalimika na joto la jua, na upepo wa kaskazi unawaingilia. Na yote hayo ni
katika ishara za kudra ya Mwenyezi Mungu. Na anaye pata tawfiki ya Mwenyezi
Mungu kuokoka basi huokoka, na aliye kosa tawfiki hatopata wa kumwongoa baada
yake.
18. Na wewe ukiwaona utadhani wamacho, nao kwa
hakika wamelala. Na katika usingizi wao tulikuwa tunawageuza kulia na kushoto
mara kwa mara ili kuwahifadhi miili yao isidhurike na ardhi wakafanya madonda.
Na mbwa aliye wafuata alinyoosha miguu yake ya mbele mlangoni, naye kalala pia
kama kwamba yu macho. Ungeli watokea nao wamo katika hali ile ungeli toka mbio
na moyo umejaa khofu kwa walivyo kuwa wanatisha katika kulala kwao. Hapana
anaye waona ila atatishika nao. Hayo ili wasikaribiwe na mtu, wala wasiguswe na
mtu mpaka wishe muda wao.
19. Kama tulivyo walaza tuliwaamsha wapate
kuulizana wenyewe kwa wenyewe wamelala muda gani? Mmoja wao akasema:
Umekupitieni muda gani katika usingizi? Wakasema: Tumelala muda wa siku au
baadhi ya siku. Walivyo kuwa hawana yakini nayo hayo wakasema: Mwachieni mambo
haya Mwenyezi Mungu; kwani Yeye ni Mjuzi zaidi wa haya. Na ende mmoja wenu
mjini, na achukue hizi sarafu za fedha achague chakula kizuri kabisa akuleteeni
mle. Na awe na mafahamiano mema. Wala mambo yenu yasijuulikane na mtu yeyote.
20. Kwani hao watu wakikuoneni watakuuweni kwa
kukupopoeni mawe, au watakurejesheeni katika ukafiri kwa nguvu. Nanyi mkirejea
ukafirini basi hamtaongokewa kabisa duniani wala Akhera.
21. Na kama tulivyo walaza na tukawaamsha
tulikuja watambulisha kwa watu wa ule mji wapate kujua kuwa ahadi ya Mwenyezi
Mungu ya kufufua wafu ni ya kweli. Na Kiyama hapana shaka kitakuja. Watu
wa ule mji wakamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Kisha Mwenyezi Mungu
akawafisha wale vijana. Watu sasa wakazozana kwa mintarafu yao. Baadhi yao
wakasema: Jengeni jengo kwenye mlango wa pango, na tuwaache wao na shani yao.
Kwani Mola wao Mlezi anaijua vyema hali yao. Na wakasema wenye kusikilizwa
miongoni mwao: Hapa pahala pao tutafanya msikiti kwa sababu ya ibada.
22. Watasema kikundi fulani katika Watu wa
Kitabu (Biblia) wanao jiingiza katika mzozano wa kisa cha Ahlil Kahf (Watu wa
Pangoni) kwamba hao walikuwa watatu na wa nne wao ni mbwa wao. Na wengine
wanasema: Walikuwa watano, na wa sita wao ni mbwa wao. Tena wengine
wanasema: Wao ni saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Waambie hawa wanao
khitalifiana: Mola wangu Mlezi ni Mjuzi ambaye hapana wa kumshinda ujuzi wake
kuijua idadi yao. Wala hapana wajuao ila watu wachache tu ambao Mwenyezi Mungu
amewajuvya hisabu yao. Basi wewe usijadiliane na hao wanao khitalifiana juu ya
mas-ala ya hao vijana, ila majadiliano ya juu juu ya upole, bila ya kujaribu
kuwakinaisha. Kwani wao hawakinaiki. Wala msimuulize yeyote kati yao juu ya
khabari zao. Wewe hakika imekwisha kujia iliyo kweli isiyo na shaka.
23. Wala usiseme kabisa kwa jambo unalo azimia
kulendea na kujihimu kulitenda: Mimi nitalifanya hilo baadae!
24. Ila kusema huko kuambatane na kupenda kwa
Mwenyezi Mungu kwa kusema: Inshallah, yaani Mwenyezi Mungu akipenda. Na ukisahau
jambo, basi kimbilia kumtaja Mwenyezi Mungu; na useme unapo azimia kufanya jambo
na kuliambatanisha na kupenda kwa Mwenyezi Mungu: Huenda Mola wangu Mlezi
akaniwafikisha kwenye bora kuliko nililo azimia kufanya, na lenye kuongoka
zaidi.
25. Na hakika hao vijana walikaa katika pango
lao nao wamelala kwa miaka mia tatu, na ikazidi tisa.
Aya hii
inaonyesha ukweli wa ilimu ya Falaki (Astronomy), nayo ni kuwa ni miaka 300 kwa
mwendo wa jua, na miaka 309 kwa hisabu ya mwezi unao fuatwa na Waislamu. Aya hii
imeitangulia ilimu ya Falaki.
26. Ewe Mtume! Waambie watu: Mwenyezi Mungu peke
yake ndiye Mwenye kujua zama zao zote. Kwani Yeye Subhanahu ndiye aliye khusika
kujua siri za mbingu na ardhi. Jinsi gani kulivyo tukuka kuona kwake kwa viumbe
vyote! Na jinsi gani kulivyo tukuka kusikia kwake kwa kila cha kusikilizana! Na
hapana katika wa mbinguni na wa katika ardhi wa kuendesha mambo yao isipo kuwa
Yeye. Na wala hapana wa kumshiriki katika hukumu yake kiumbe chochote.
27. Ewe Mtume! Soma uliyo funuliwa kwa wahyi
katika Qur'ani. Na katika hayo yamo uliyo funuliwa ya khabari za hao vijana.
Wala usisikilize hayo maskhara yao ya kutaka ubadilishe muujiza wa Qur'ani kwa
muujiza mwingine. Kwani hakika hapana wa kuyageuza anayo simulia Mwenyezi Mungu
maneno ya haki katika miujiza yake. Hakika hapana awezae kubadilisha hayo. Wala
usende kinyume na amri ya Mola wako Mlezi, kwani hapo tena hutapata wa
kumkimbilia kukuhifadhi naye.
28. Ewe Mtume! Shikamana na usuhuba wa masahaba
wako Waumini, wanao muabudu Mwenyezi Mungu peke yake asubuhi na jioni daima,
huku wanataka radhi zake. Wala jicho lako lisiwawache hao kuwaangalia wapinzani
wa kikafiri kwa kutaka kustarehe nao katika mapambo ya maisha ya dunia. Wala
usikubali kuwafukuza Waumini mafakiri katika baraza yako kwa kumridhisha huyo
tuliye mghafilisha moyo wake na kutukumbuka Sisi, kwa kuwa yeye mwenyewe hakuwa
tayari kwa hayo, na akawa ni mtumwa wa pumbao lake, na mambo yake katika vitendo
vyake vyote hayakufuata njia iliyo sawa. Na anapo katazwa Nabii, basi ndio
wanakatazwa wengineo (yaani sote sisi). Na hakika Nabii s.a.w. hataki maisha ya
dunia na pumbao lake. Lakini makatazo hayo anaelekezewa Nabii ili wenginewe
watahadhari na kutaka pumbao la dunia. Kwani ikiwa yaweza kuwa kwake kutaka
pumbao la kimwili, basi kila mwanaadamu yaweza kuwa katika nafsi yake. Kwa hivyo
ajilinde.
29. Sema ewe Mtume!: Hakika haya niliyo kuja
nayo ni kweli tupu iliyo toka kwa Mola wenu Mlezi. Basi anaye taka kuyaamini na
ayaamini. Kwani hiyo ni kheri yake mwenyewe. Na anaye taka kuyakataa na akatae.
Kwani huyo haidhulumu ila nafsi yake mwenyewe. Hakika Sisi tumekwisha muwekea
tayari anaye jidhulumu nafsi yake kwa ukafiri Moto utao mzunguka kama khema. Na
hao walio dhulumu wakiomba wasaidiwe kwa maji huko katika Jahannamu, wataletewa
maji kama mafuta yaliyo tibuka yamoto mno, hubabua nyuso kwa uvukuto wake!
Kinywaji hicho ni kibaya mno, na Jahannamu ni pahali paovu pa mapumziko yao!!
30. Ama wale walio muamini Mwenyezi Mungu na
Dini ya Haki uliyo funuliwa wewe, na wakatenda aliyo waamrisha Mola wao Mlezi,
nayo ni vitendo vyema, basi Sisi hatuto wapotezea ujira wao wa vitendo vyema
walivyo vitenda.
31. Watu hao watakuwa na Mabustani ambayo
watastarehe ndani yake daima dawamu. Kati baina ya miti na majumba yake inapita
mito, na watapambiwa yanayo onekana ni ya starehe katika dunia, kama mapambo ya
dhahabu, na mavazi yao ni nguo za kijani za hariri za kila namna, wakiegemea juu
ya makochi na matakia na mapazia. Watapata malipo bora, na Bustani nzuri ya
kudumu na kustarehe. Humo watapata kila wakitakacho.
32. Ewe Mtume! Bainisha baina ya hali ya
makafiri matajiri na Waumini mafakiri kwa kuwapigia mfano ulio tokea hapo zamani
baina ya watu wawili: kafiri na Muumini. Huyo kafiri alikuwa na vitalu viwili
vya mizabibu, na tukavizungushia mitende kwa ajili ya pambo na faida pia. Na
baina ya hivyo vitalu tukaweka makulima mengine yaliyo stawi na kutoa mazao.
33. Na kila kitalu kikawa kinatoa mazao yake kwa
wingi na kubaariki. Wala hapana kilicho tindikia. Na tukapasua mto unamiminika
kati yao.
34. Na huyo mwenye vitalu alikuwa na mali
mengine yenye kutoa mazao yake pia. Basi ikamuingia ghururi kwa neema ile.
Katika ile ghururi yake akamwambia mwenzie yule Muumini nao walikuwa
wakijadiliana: Mimi nina mali mengi kuliko wewe, na ninakushinda kwa nguvu za
jamaa zangu na wasaidizi.
35. Kisha akaingia katika kitalu chake kimojapo
pamoja na yule mwenzie Muumini, naye huku amejaa ghururi, akamwambia: Sidhani
kabisa kuwa kitalu hichi kitapotea!
36. Wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na pindi
ikawa nikirejea kwa Mola wangu Mlezi kwa kufufuliwa kama unavyo dai wewe, basi
Wallahi! Hapana shaka nitapata bustani bora kuliko kitalu hiki huko Akhera.
Kwani mimi ni mtu wa neema kwa kila hali. Yeye huyu anakisia hayo ya ghaibu kwa
haya yaliyoko sasa. Wala hajui kuwa Akhera malipo yake ni kwa Imani na vitendo
vya kheri.
37. Mwenzie Muumini akamjibu: Unajiachilia
kumkufuru Mola wako Mlezi aliye kuumba tangu asli yako ya Adam kutokana na
udongo, kisha kutokana na tone ya maji-maji ya mbegu ya uzazi, kisha akakufanya
mtu aliye kamilika? Ikiwa unajiona bora kwa mali yako na jamaa zako, basi
mkumbuke Mola wako Mlezi na asli yako ya udongo.
38. Lakini mimi ninasema: Hakika aliye niumba
mimi na akaumba ulimwengu wote huu ni Mwenyezi Mungu Mola wangu Mlezi. Na mimi
namuabudu Yeye peke yake, wala simshirikishi na yeyote.
39. Na lau kuwa ungeli sema unapo ingia katika
hii bustani yako ya duniani na ukaangalia viliomo ndani yake: Haya Mashaallah!
Ndio aliyo yataka Mwenyezi Mungu. Wala mimi sina nguvu ya kuyapata haya bila ya
msaada wa Mwenyezi Mungu. Hayo inge kuwa ni shukrani za kupelekea kudumu neema
yako. Tena akazidi kumwambia: Ikiwa umeniona mimi ni duni kuliko wewe kwa mali
na watoto na wasaidizi...
40....basi huenda Mola wangu Mlezi akanipa bora
kuliko hiyo bustani yako, hapa duniani au kesho Akhera, na akaipelekea bustani
yako kudra yake aliyo ikadiria, kama radi mathalan kutoka mbinguni. Na ikawa
ardhi kavu inayo teleza haimei kitu, wala unyayo hautulii juu yake.
41. Au maji yake yakazama katika ardhi,
yasipatikane, wala usiweze kuyachota kwa kumwagia katika shamba.
42. Mwenyezi Mungu kampatiliza yule kafiri,
akayateketeza mavuno yote ya kitalu chake, na hicho kitalu chenyewe
akakiangamiza, na akang'oa hata mizizi yake. Yule kafiri akabakia akipindua
pindua viganja vyake kwa kusikitikia gharama alizo zitoa katika kukiamirisha
kitalu chake, na baadae kuja kikapatilizwa na uharibifu. Akatamani lau kuwa
hakumshirikisha Mola wake Mlezi na yeyote.
43. Katika balaa hii hakuwa na jamaa wa kuja
mnusuru badala ya Mwenyezi Mungu kama alivyo kuwa akijitapa. Wala hakuwa anaweza
kujisaidia nafsi yake.
44. Kwani katika kila hali nusura iko kwa
Mwenyezi Mungu wa Haki peke yake. Na Yeye Subhanahu ni Mwema kwa mja wake
Muumini, humkirimu kwa malipo, na humfanyia mema matokeo yake.
45. Ewe Mtume! Watajie watu mfano wa maisha ya
duniani, vipi uzuri wake na kupendeza kwake, na mara hupotelea mbali. Ni kama
mfano wa maji yanayo teremka kutoka mbinguni yakamwagiwa mimea ikanawiri,
ikastawi. Kisha punde si punde ikakauka, ikawa vibua vikavu vilivyo katika
katika vikipeperushwa na upepo. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuleta na
kuondoa akitakacho.
46. Mali na wana ni pambo na starehe kwenu
katika uhai wa duniani, na pia ndio nguvu zenu. Lakini vyote hivyo havina
dawamu. Hivyo vina mwisho wake, havibakii. Na vitendo vyema vyenye kubaki ni
bora kwenu mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye hukumimieni kwa ukarimu thawabu zake,
na hivyo ndio bora ya matumaini ya binaadamu.
47. Na ewe Mtume! Waonye watu kwa Siku ambayo
vyote viliopo vitaondoka. Milima itaondoka, na mtaiona ardhi tupu wazi imetanda,
hapana chochote kilicho kuwapo cha kuisitiri. Na tutawafufua watu kwa ajili ya
hisabu, na hatutamwacha hata mmoja kati yao.
48. Na Siku hii watu watahudhurishwa kwa makundi
wakipangwa kwa masafu kwa ajili ya hisabu. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu atasema:
Tumekufufueni kutokana na mauti, kama tulivyo kuumbeni pale mara ya mwanzo. Na
mmetujia peke yenu, mmoja, mmoja, bila ya mali, na bila ya wana. Na duniani
mlikuwa mkikanusha kufufuliwa na kuhisabiwa.
49. Na katika mkono wa kila mmojapo kitawekwa
kitabu cha vitendo vyake. Waumini watakiona na watafurahi kwa yaliyomo humo. Na
wakanushaji wataona nao wamejaa khofu kwa vitendo viovu viliomo humo. Watasema
wakisha ona hayo: Hilaki gani hii! Tunastaajabia kitabu hichi hakikuacha hata
dogo katika vitendo vyetu, wala kubwa, ila kimetuandikia! Na wataona malipo ya
waliyo yatenda ni ya haki. Wala Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote katika waja
wake.
50. Ewe Mtume! Watajie mwanzo wa kuumbwa kwao,
ili wajue kuwa wao wametokana na udongo, basi wasikae wakidanganyika na hayo
waliyo nayo, wakamnyenyekea Iblisi, adui wa baba yao. Kwani yeye alikuwa katika
majini, akajivuna, na akamuasi Mwenyezi Mungu. Basi yawaje baada ya kwisha jua
khabari zake mkamfanya yeye na kizazi chake kuwa ndio wasaidizi wenu badala ya
Mwenyezi Mungu. Na hao ndio adui zenu! Badala hii ni ovu kwa mwenye kuidhulumu
nafsi yake na akamt'ii Shetani.
*
51. Mimi sikumwonyesha Iblisi wala dhuriya zake
nilipo umba mbingu wala ardhi, wala sikuwashuhudisha baadhi yao nilipo waumba
wenzao ili wanisaidie. Wala sikuwa nina haja ya msaidizi wowote, licha kuwa
nikatafute wapotovu ndio wawe wasaidizi wangu. Basi yawaje mnakwenda mt'ii
Shetani na mkaniasi Mimi?
*
52. Watajie siku atayo waambia Mwenyezi Mungu
washirikina: Waiteni hao mlio kuwa mkidai duniani kuwa ni washirika wangu katika
ibada ili wakuombeeni kwa mujibu wa madai yenu. Nao watawaita, na hao hawato
waitikia. Nasi tumejaalia sasa hapana baina yao ila ni maangamio tu kwa
makafiri, baada ya kuwa duniani walikuwa na mawasiliano ya ibada na mapenzi.
*
53. Na wakosefu watauona Moto na watayakinika
kuwa hapana shaka watauingia tu. Wala hawatakuwa na pahala pengine badala yake.
*
54. Na Mwenyezi Mungu amewatajia watu katika
Qur'ani hii, wanayo ikanusha na wakataka waletewe muujiza mwenginewe, mifano
namna kwa namna, ili wapate kuwaidhika kwayo. Lakini mwanaadamu tabia yake ni
kupenda kubishana. Akiwa kafiri basi atabisha hata kwa uwongo.
*
55. Na hapana lililo wazuia washirikina kuamini
zilipo wafikia sababu za kuongoka, nazo ni huyu Mtume na Qur'ani, isipo kuwa
ukaidi wao na kumtaka Mtume awaletee aliyo waletea Mwenyezi Mungu wale watu wa
zamani, nayo ni kuangamizwa moja kwa moja kama kulio wapata hao wa kale, au
awaletee adhabu ya dhaahiri hivi.
*
56. Lakini Mwenyezi Mungu hawatumi Mitume wake
ila kwa ajili ya kutoa bishara njema na kuonya. Wala hawatumi kwa ajili ya hao
wenye inda wawatake walete muujiza makhsusi. Lakini walio kufuru wanaacha hoja,
na wanabishana na Mitume kwa upotovu ili waipotoe Haki. Na msimamo wao kwa
Qur'ani na maonyo ni msimamo wa mwenye kejeli na maskhara ambaye hana makusudio
ya kutafuta hakika ya mambo.
57. Na hapana yeyote aliye dhaalimu mkubwa zaidi
kuliko huyo anaye waidhiwa kwa Ishara za Mola wake Mlezi naye asizingatie, na
akasahau nini matokeo ya maasi yake anayo yatenda! Hakika Sisi kwa sababu ya
kuelekea kwao kwenye ukafiri tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao, basi nyoyo zao
hazitambui wala haziingii mwangaza. Na masikioni mwao tumetia uziwi basi
hawasikii la kuwafahamisha! Nawe, ewe Mtume! Ukiwaita kwenye Dini ya Haki hawato
ongoka maadamu tabia yao ni hii.
58. Na Mola wako Mlezi Mtukufu Mwingi wa
kusamehe makosa ya waja wake, Mwenye rehema kunjufu kwa mwenye kumuelekea, lau
angeli penda kuwatwaa kwa maovu wayatendayo basi angeli wapatiliza upesi upesi
kama alivyo kwisha watangulizia wenginewe. Lakini hii ni hikima yake aliyo
ikadiria. Anawaakhirisha mpaka ufike wakati atapo waonjesha adhabu kali kabisa.
Na hapo hawatopata pa kukimbilia na kuwalinda.
59. Na hii basi ndio miji ya kale tuliyo
iteketeza pale watu wao walipo dhulumu kwa kuwakanusha Mitume wao. Na Sisi
tukawawekea miadi ya kuwaangamiza isiyo na khitilafu. Hali kadhaalika itakuwa ya
hao katika kaumu yako wanao kanusha, ikiwa hawaamini.
60. Na hakika hapana mtu anaye jua ya Mwenyezi
Mungu ila Yeye Mwenyewe anapo mpa kipawa hicho Nabii au mtu mwema. Ewe
Mtume! Simulia kuwa Musa bin Amran alimwambia kijana wake, mtumishi wake,
mwanafunzi wake: Sitoacha kwenda mpaka nifike zinapo kutana bahari mbili, au
basi nitaendelea kwenda tu muda mrefu.
61. Basi Musa na kijana wake walipo fikilia
pahala panapo kusanyika bahari mbili wakamsahau samaki wao walio kuwa
wamemchukua kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Akatumbukia baharini, akashika njia yake
katika maji!
62. Musa na kijana wake walipo fika mbali na
pahala pale, na wakaona njaa na machofu Musa akamwambia kijana wake: Tupe cha
kukila. Hakika tumepata taabu na mashaka katika safari yetu hii.
63. Kijana wake akasema: Unakumbuka? Pale tulipo
pumzika kwenye lile jabali, basi mimi nilimsahau yule samaki. Na hapana aliye
nisahaulisha ila Shetani. Na hapana shaka samaki yule katumbukia baharini.
Na mimi hakika najistaajabia kusahau kwangu huku.
64. Musa akamwambia: Haya yaliyo tokea ndiyo
tuliyo kuwa tunayataka kwa mujibu wa hikima anayo itaka Mwenyezi Mungu. Basi
wakarejea nyuma kwa njia yao ile ile waliyo jia, wakizifuata nyayo zao.
65. Mpaka wakafika kwenye lile jabali. Hapo
wakamkuta mja miongoni mwa waja wangu walio wema, tuliye mpa hikima, na tukampa
ujuzi mwingi kutokana kwetu.
66. Musa akamwambia yule mja mwema: Je nende
nawe upate kunifunza nami aliyo kufunza Mwenyezi Mungu?
67. Akamwambia hutaweza kustahamili kufuatana
nami.
68. Na utawezaje kustahamilia jambo lisilo pata
kukufika mfano wake?
69. Musa akasema: Inshallah, Mwenyezi Mungu
akipenda, utaniona mimi ni mwenye kusubiri, na mt'iifu kwako kwa yote utayo
niamrisha.
70. Yule mja mwema akasema: Basi ukinifuata na
ukayaona usiyo yafahamu, usiingie kuniuliza mpaka nianze mimi kukusimulia.
71. Wakatoka wakitambaa na mfukwe wa bahari
mpaka wakakuta jahazi wakaipanda. Yule mja mwema akaitoboa jahazi ile nayo
imo safarini. Musa akapinga kwa kusema: Umeitoboa makusudi upate kuwazamisha
watu wake? Ama hakika umefanya jambo ovu!
72. Yule mja mwema akasema: Mimi nilikwisha
kwambia kuwa hakika wewe hutoweza kusubiri kuwa nami.
73. Musa akamwambia: Usinichukulie kwa kusahau
wasia wako, wala usinikutishe mashaka katika kutafuta ilimu kwako, na ukaifanya
hiyo kazi nzito.
74. Na baada ya kutoka kwenye jahazi ile
wakaingia kuendelea na safari yao. Njiani wakamkuta kijana. Yule mja mwema
akamuuwa yule kijana! Musa akasema kwa kuchukia: Unakwenda muuwa mtu asiye na
kosa lolote, na wala hakumuuwa mtu yeyote? Hakika umefanya jambo ovu kweli
kweli!
75. Mja mwema akamwambia Musa: Mimi nalikwambia
kwamba wewe hutaweza kustahamili ukanyamaza kimya usiniulize.
76. Musa akasema: Nikikuuliza lolote baada ya
mara hii basi usifuatane nami, kwani umekwisha fikilia kiwango cha kupata udhuru
wa kutokuwa nami.
77. Wakenda hata wakafika kwenye mji. Wakawataka
watu wake wawape chakula, wakakataa kuwakirimu. Wakakuta ukuta umeinama
wakaribia kuanguka. Yule mja mwema akaudiriki. Akaujenga mpaka akausimamisha
sawa. Musa akasema: Ungeli taka ungeli weza kudai ujira kwa kazi uliyo ifanya.
78. Mja mwema akasema: Huku kutaaradhi kwako
mara kwa mara kwa niyatendayo mimi ndio sababu ya kufarikiana mimi nawe. Sasa
basi nitakueleza hikima ya yote haya ambayo wewe huyajui undani wake, wala
hukuweza kuyasubiria yaliyo fichikana ukangojea kujua hakika yake na siri yake.
79. Ama ile jahazi niliyo itoboa ilikuwa ni ya
watu wanyonge wenye haja, ambao kazi yao ni ya baharini wakitafuta riziki yao.
Basi mimi nikataka kukitia ila chombo chao kisitakikane. Kwani nyuma yao
yuko mfalme mtindo wake ni kupokonya kila jahazi nzima. (Kughusubu,
kupokonya, hata kukiitwa "kutaifisha" ni dhambi kubwa kabisa kwa Mwenyezi
Mungu, kwani ni dhulma.)
80. Ama yule kijana niliye muuwa, baba yake na
mama yake walikuwa ni Waumini. Tulikuwa tunajua kuwa angeli ishi angeli kuwa
ndio sababu ya ukafiri wao.
81. Basi tukataka kwa kumuuwa huyo mtoto
Mwenyezi Mungu awape badala yake aliye bora zaidi kwa dini, na mwema zaidi, na
mwenye huruma.
82. Ama ule ukuta nilio usimamisha, bila ya
ujira, ulikuwa wa vijana wawili mayatima katika watu wa ule mji. Na chini yake
ilikuwako khazina walio achiwa na baba yao. Naye alikuwa ni mtu mwema. Basi
Mwenyezi Mungu alitaka kuwahifadhia khazina yao ile mpaka wakue wawe na akili
zao, na wajitolee wenyewe khazina yao kuwa ni rehema kwao, na kumtukuza baba yao
kwa kupitia dhuriya zake. Nami sikufanya niliyo yafanya kwa jitahada ya nafsi
yangu. Bali nimefanya hayo kwa kuongozwa na Mwenyezi Mungu. Hii ni tafsiri ya
hayo yaliyo fichikana kwako wewe Musa, nawe usiweze kuyavumilia.
83. Ewe Mtume! Baadhi ya makafiri wanakuuliza
khabari za Dhul-Qarnaini. Waambie nitakusimulieni baadhi ya khabari zake.
84. Tumemtilia nguvu amri yake katika ardhi,
akiendesha humo mambo kwa mazingatio yake na utawala wake. Na tukampa ujuzi
mwingi kwa njia ambazo kwazo akiweza kuongoza mambo.
85. Kwa kutumia njia hizo aliweza kueneza
madaraka yake katika ardhi, na akafuata njia mpaka akafika huko magharibi kunako
kuchwa jua.
86. Akenda mpaka akafika pahala mbali huko
upande wa magharibi, akalikuta jua kwa linavyo onekana kwa macho kama kwamba
linazama pahala penye chemchem ya maji ya moto na matope meusi. Na karibu ya
chemchem hii Dhul- Qarnaini aliwakuta watu makafiri. Mwenyezi Mungu akamtia
moyoni mwake afanye mojapo ya mambo mawili: Ama awaite kwenye Imani, na hili kwa
hakika ni jambo zuri; au awapige vita ikiwa hawakuitikia wito wa Imani.
87. Dhul-Qarnaini akawatangazia: Katika wao
aliye jidhulumu nafsi yake kwa kubakia katika ushirikina, basi amestahiki adhabu
ya duniani kutokana naye, na kisha atarejea kwa Mola wake Mlezi. Naye
atamuadhibu adhabu kali wasio ijua.
88. Na ama mwenye kumuitikia, na akamuamini Mola
wake Mlezi, na akatenda mema, basi atapata malipo mazuri Akhera, na hapa duniani
tunamchukulia kwa upole na wepesi.
89. Kisha Dhul-Qarnaini akaendelea vile vile
huku akiomba tawfiki ya Mwenyezi Mungu, na akafuata njia ya kufikilia matokea
jua upande wa mashariki.
90. Hata akafika linapo chomoza jua, kwa
ionekanavyo kwa macho, mwisho wa majenzi. Akawaona watu wanaishi katika ushenzi
kabisa. Hawana hata cha kuwasitiri na joto.
91. Na kama Dhul-Qarnaini alivyo waita watu wa
magharibi waje kuamini basi kadhaalika aliwaita hawa, na akenda nao mwendo ule
ule wake wa mwanzo.
92. Kisha akaendelea vile vile akitumia mbinu
alizo msahilishia Mwenyezi Mungu za kumpa tawfiki, akishika njia baina ya
mashariki na magharibi.
93. Mpaka akafika - katika safari yake ya tatu -
pahala mbali baina ya milima miwili mirefu...Na huko akakuta watu ambao
hawafahamu wanalo ambiwa ila kwa uzito na mashaka.
Hiyo ngome au
boma baina ya milima miwili iliyo tajwa katika maelezo ya juu ni milima ya
Azarbajan na Arminia, na kauli nyingine ni kaskazini ya mwisho katika jimbo la
Turkistan.
94. Walipo ziona nguvu zake na uwezo wake
wakamtaka awasimamishie ngome ya kuwalinda na Juju-wa-maajuju. Nao hao ni watu
wanao waonea maya, na wanawafisidia na kuwaharibia nchi yao. Na wao walikuwa
watayari wamlipe ujira kwa kazi hiyo.
95. Akawajibu kwa kuwaambia: Mali na madaraka
aliyo nijaalia Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko hayo mnayo taka kunipa.
Akaanza kusimamisha hiyo ngome, na akawataka wamsaidie kama wawezavyo kwa watu
na zana ili awatimizie wayatakayo.
96. Akawataka wamkusanyie vipande vya chuma.
Wakakusanya kama alivyo taka. Akajenga kwa hivyo ngome ndefu iliyo lingana na
kingo za milima hiyo miwili. Kisha akawaamrisha wawashe moto, wakauwasha, mpaka
chuma kikayayuka. Tena akamimina juu yake shaba iliyo kwisha yayushwa; ikawa
ngome madhubuti, haipitiki.
97. Basi wale mahasidi hawakuweza kulikwea lile
boma, jinsi lilivyo kwenda juu, wala kulitoboa kwa ugumu wake.
98. Dhul-Qarnaini alipo kwisha jenga ile ngome
alisema kumshukuru Mwenyezi Mungu: Ngome hii ni rehema iliyo toka kwa Mola wangu
Mlezi kwa ajili ya waja wake. Na itabaki hivi hivi imesimama mpaka ije amri ya
Mwenyezi Mungu kuiteketeza. Hapo tena itakuwa sawa sawa na ardhi. Na amri ya
Mwenyezi Mungu ni lazima itimie bila ya muhali.
99. Na tangu kujengwa boma hilo Juju-wa-maajuju
wakabaki nyuma yake wakipambana wenyewe kwa wenyewe, na wengine wakasalimika na
shari yao. Ikifika Siku ya Kiyama likapulizwa baragumu Mwenyezi Mungu
atawakusanya viumbe wote kwa ajili ya hisabu na malipo.
100. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaonyesha wazi
makafiri Jahannamu iwatie kitisho na awatumbukize humo.
101. Na hayo ni kwa kuwa macho yao walipo kuwa
duniani yalikuwa yameghafilika hayaoni Ishara za Mwenyezi Mungu kama kwamba
yamezibwa na pazia; na walikuwa kwa upotovu wao hawawezi kusikia Wito wa Haki,
kama mtu aliye kuwa kiziwi.
"Wale ambao kwamba macho yao yalikuwa
paziani hayanikumbuki, na wakawa hawawezi kusikia": Ni wale ambao macho yao
yameghafilika na kunizingatia Mimi katika mbingu na ardhi. Na kwa hivyo hii Aya
tukufu inazindua watu wazingatie yote yalio wazunguka yanayo onyesha Ishara za
kuwepo Mwenyezi Mungu.
102. Je, macho ya makafiri yamepofuka hata
wakadhani kwamba kuwafanya watumwa wangu, Malaika na Isa, kuwa ni miungu,
wakiwaabudu badala yangu Mimi, kutawapa manufaa na kuwakinga na adhabu? Hakika
Sisi tumewaandalia Jahannamu ndio pahali pao pa kukaa wapate huko malipo wanayo
yastahiki.
103. Ewe Mtume! Waambie hawa makafiri: Je,
nikutajieni watu watao pata khasara mno kwa vitendo vyao na watao kosa thawabu?
104. Ni hao vilio haribika vitendo vyao katika
maisha ya duniani kwa kuharibika itikadi yao, na hali wao wanaitakidi kuwa ndio
wanafanya vitendo vyema!
105. Hao ndio walio zikataa dalili za uwezo wa
Mwenyezi Mungu, na wakaikanusha Siku ya kufufuliwa na kuhisabiwa. Basi vitendo
vyao vimepotea bure, na Siku ya Kiyama watastahiki kudharauliwa na kupuuzwa,
kwani hawana a'mali ya kutiwa maanani!
106. Hayo ndiyo tuliyo yabainisha na
tukayapambanua, hali ya hawa; na malipo yao kwa hayo ni Jahannamu kwa sababu ya
kufuru zao na kuzifanyia maskhara Ishara za Mwenyezi Mungu alizo ziteremsha, na
Mitume alio watuma.
107. Hakika walio thibiti katika Imani na
wakatenda mema, malipo yao ni Bustani za Firdausi watazo ziingia.
108. Wataneemeka milele, wala hawatataka badala
yake chochote.
109. Ewe Mtume! Waambie watu: Hakika ujuzi wa
Mwenyezi Mungu umekusanya kila kitu. Na lau kuwa maji ya baharini ni wino wa
kuandikia maneno ya Mwenyezi Mungu yanayo onyesha ujuzi wake na hikima yake,
basi wino huo ungeli malizika, na hata ungeli ongezwa wino mwingine kama huo,
kabla ya kumalizika maneno ya Mwenyezi Mungu!
110. Ewe Mtume! Waambie watu: Hakika mimi ni
mtu tu kama nyinyi, nimetumwa kwenu, nikufunzeni aliyo nifunza Mwenyezi Mungu.
Nimefunuliwa (yaani nimepewa Wahyi) ya kwamba Mungu wenu ni Mmoja, hana mshirika
wake. Anaye tumai kukutana na Mwenyezi Mungu na kupata malipwa yake, basi
naatende vitendo vyema kwa usafi wa niya, na ajitenge mbali na kumshirikisha
Mwenyezi Mungu na chochote katika ibada.