1. Mwenyezi Mungu aliye takasika na kila ambalo lisio laiki naye. Yeye ndiye aliye mchukua mja wake Muhammad wakati wa usiku kutoka Msikiti Mtakatifu wa Makka kwendea Msikiti wa Mbali wa Baitul Muqaddas, ambao tuliwabarikia wakaazi majirani wa Msikiti huo katika mahitaji yao, ili tumwonyeshe baadhi ya Ishara zetu zenye ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kuwa Mimi ni Mungu Mmoja peke yangu, na ukubwa wa uwezo wangu! Hakika Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
 

2. Na hakika hiyo Baitul Muqadda ilikuwa inakaliwa na Wana wa Israili baada ya Musa, mpaka walipo fanya fisadi yao humo, wakafukuzwa hapo zamani.  Haya ijapo kuwa Sisi tulimpa Musa Taurati, na tukatia ndani yake uwongofu, na tukawaambia: Msimfanye yeyote wa kumtegemezea mambo yenu isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
 

3. Nyinyi Wana wa Israili mmezalikana kutokana na wale watu safi wema walio kuwa na Nuhu katika safina baada ya kuwa wameamini. Nasi tukawaokoa wasizame. Basi mfanyeni Nuhu kuwa ndiye mwongozi wenu wa kumfuata, kama walivyo mfanya wazee wenu walio tangulia. Kwani hakika yeye alikuwa mja wa wingi wa shukrani kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake.
 

4. Na tukatekeleza hukumu yetu kwa Wana wa Israili katika tuliyo yaandika katika Lauhun Mahfuudh, Ubao Ulio Hifadhiwa, ya kwamba watafanya ufisadi katika Nyumba Takatifu (Baitul Muqaddas) bila ya shaka yoyote mara mbili.  Kila mara katika hizo itakuwa ni udhaalimu na uasi, na kuacha hukumu za Taurati, na kuwauwa Manabii, na mtasaidiana katika madhambi, na kwamba utawala wenu utaenea, na kutukuka na kupanda kichwa na kiburi kwa dhulma zenu.
 

5. Na ulipo fika wakati wa kukuleteeni adhabu mara ya kwanza, tulikupatilizeni, kwa sababu ya fisadi yenu, kwa kukusalitishieni watu wa kali kupigana. Wakakuingilieni mpaka ndani ya majumba, hapana walicho kiacha, ili wakuuweni. Na ahadi ya kukuadhibuni ilikuwa ni ahadi haina budi kutimizwa.
 

6. Kisha mambo yenu yalipo kaa sawa, na mkaongoka, na mkatengeneza umoja wenu, na mkaacha ufisadi, tukakurejezeeni ushindi juu ya wale makhasimu zenu. Nasi tukakuruzukuni mali na wana, na mkazidi kuwa wingi kwa idadi.
 

7. Na tukawambia: Mkifanya wema na mkamt'ii Mwenyezi Mungu, wema wenu utakufaeni nafsi zenu duniani na Akhera. Na mkifanya uovu kwa maasi, basi mnajiharibia nafsi zenu vile vile. Na utapo kuja wakati wa adhabu pale mara ya mwisho katika zile mara mbili za ufisadi wenu katika nchi, tutakupelekeeni maadui zenu, wafanye athari za uovu na madhila na huzuni zidhihiri nyusoni mwenu. Na matokeo yake ni kuingia katika Msikiti wa Baitul Muqaddas, wakauharibu kama walivyo ingia na wakauharibu mara ya kwanza, wakateketeza watacho kipata kwa uteketezi mkubwa.
 

8. Asaa Mola wenu Mlezi akakurehemuni baada ya hiyo mara ya pili pindi mkitubu. Na mkirejea kwenye ufisadi Nasi tutarejea kukuadhibuni. Na tumeifanya Jahannam kuwa ndiyo gereza la kuwafungia makafiri!
 

9. Hakika hii Qur'ani inawaongoza watu kwenye njia ambayo ndiyo njia iliyo kaa sawa kabisa kuliko njia zote, na ndiyo njia ya salama kabisa ya kufikilia kwenye furaha ya kweli katika dunia. Na wabashirie wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wenye kuit'ii Haki na wanatenda vitendo vyema, kuwa watapata ujira mkubwa Siku ya Kiyama.
 

10. Na hakika wale ambao hawaiamini Akhera tumewatengenezea adhabu ya machungu makali.
 

11. Ni katika tabia ya mwanaadamu kufanya haraka katika kuwahukumia watu kwa yanayo wapata, na katika kauli zake na vitendo vyake. Naye hukimbilia kulingania shari kama anavyo lingania kheri. Naye hufanya haraka kumuapiza kwa Mwenyezi Mungu amteremshia shari yule aliye mkasirisha, kama anavyo fanya haraka kuomba kheri.
 

12. Na Sisi tumejaalia usiku na mchana, kwa namna yao na kupishana kwao, kuwa ni alama zenye kuonyesha Upweke wetu na Uwezo wetu. Tukauondoa mwangaza kwenye usiku, na kisionekane kitu. Na alama yake ni giza liso kuwa na jua. Hiyo ni ishara kubwa. Na mchana tukaufanya wa kuangaza. Hapo laonekana jua, ile ishara kuu, ili mpate kwenda mtakako wakati huo katika kutafuta maisha yenu. Na katika kuja usiku na mchana mpate kujua idadi ya miaka na hisabu za miezi na siku. Na Sisi tumekubainishieni kila kitu kwa uwazi kwa sababu ya maslaha yenu, ili isimame hoja juu yenu baada kutimia neema.
 

13. Na kila mtu tumemfungamanisha na a'mali yake, vitendo vyake, kama koja lilioko shingoni. Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu kilicho andikwa vitendo vyake vyote. Atakiona kitabu hicho kiwazi iwe wepesi kwake kukisoma.
 

14. Ataambiwa: Soma kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa duniani alikuwa hajui kusoma. Soma kitabu cha a'mali zako. Hicho leo kinatosha kukuhisabia na kukudhibitia vitendo vyako.
 

15. Mwenye kufuata njia ya Haki basi anajifaa mwenyewe, na mwenye kuiacha basi anajipoteza mwenyewe. Wala hapana mwenye kubeba dhambi zake akambebea dhambi za mwenginewe. Wala haitufalii kumuadhibu yeyote kwa kutenda kitu kabla hatujampelekea Mtume kutoka kwetu amwonyeshe njia ya Haki na kumkataza maovu.
 

16. Na pindi tukikadiria tangu azali katika Lauhun-mahfuudh kuwateketeza watu wa mji fulani kwa mujibu wa hikima yetu, basi Sisi huwasalitisha wale walio jidekeza kwa taanusi katika huo mji, wakafanya fisadi zao, wakaacha njia ya Haki, na wakawafuata wenginewe bila ya kutambua, na kwa hivyo huo mji wote tena hapo hustahiki kuangamizwa. Nasi huuangamiza vikubwa mno!
 

17. Na kaumu nyingi zilizo kuja baada ya Nuhu tuliziangamiza kwa kuwaasi Manabii wao. Na yakutosha kuwa ni ishara ya Mola wako Mlezi kwamba Yeye ni Mjuzi wa kila kitu kama kilivyo, kwa ujuzi wa Mwenye kuona. Naye anazo khabari za dhambi za waja wake, na Mwenye kuziona. Hapana chochote katika vitendo vya waja wake asicho kijua, na Yeye atawalipa kama wanavyo stahiki.
 

18. Mwenye kutaka starehe za dunia hii ipitayo na akazitumikia kwa kutafutia kisingizio, wala asiwe na yakini na miadi, na wala asingojee malipo ya Akhera, tutamletea haraka haraka tuyatakayo ya duniani kwa ukunjufu na wasaa. Haya ni kwa tumtakaye kumletea haraka. Kisha tutamuandalia kwa Akhera Jahannamu ahilikike kwa joto lake, naye hali awe ni mwenye kushutumiwa kwa aliyo yatenda, mwenye kutengwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu.
 

19. Na mwenye kuitaka Akhera kwa vitendo vyake, naye akawa navyo hivyo vitendo, na akawa anamuamini Mwenyezi Mungu na malipo yake, basi watu kama hao vitendo vyao vitakubaliwa na Mwenyezi Mungu na watapata malipo kwa ajili yake.
 

20. Na Sisi tutawakunjulia neema za Mola wako Mlezi hapa duniani makundi yote mawili, pindi wakichukua khatua ya kufikia hayo. Wala neema za Mola wako Mlezi hatonyimwa yeyote, akiwa Muumini au akiwa kafiri, maadamu wakishika njia za kuzitafuta.
 

21. Hebu angalia kwa kuzingatia vipi tulivyo wafadhilisha baadhi ya waja wetu kuliko wengine, kwa kuwapa mali na vyeo na nafasi, pindi wakishika njia za kuyapata hayo katika dunia. Na hayo ni kwa hikima tunayo ijua Sisi. Na tafauti zao katika Akhera ni kubwa zaidi kuliko tafauti zao za duniani. Kwa hivyo yatakikana waishughulikie Akhera, kwani huko ndiko kwenye kutukuka kwa kweli na kuzidiana kwa hakika.
 

22. Ewe mwenye jukumu! Usimfanyie Mwenyezi Mungu kuwa na mshirika, utakuja fedheheka kwa kudharauliwa, na utajaaliwa uwe mwenye kutupika.
 

23. Na Mola wako Mlezi amehukumu kuwa msimuabudu yeyote isipo kuwa Yeye. Na pia muwafanyie wema kwa ukamilifu wazazi wenu wawili. Na hao, au mmoja wao, wakifikilia kwako hali ya unyonge na mwisho wa umri wao, basi lisikutoke tamko la kuchoka nao au kuudhika kwa yanayo kupata kutokana nao. Wala usiwahamakie. Na nena nao maneno mazuri, laini, yenye kuwaonyesha ihsani na kuwahishimu.
 

24. Na wafanyie upole, na wanyenyekee kwa kuwaonea huruma, na uwaombee: Ewe Mola Mlezi! Warehemu wote wawili, kama walivyo nifanyia huruma walipo nilea utotoni.
 

25. Enyi watu! Mola wenu Mlezi anajua kuliko nyinyi yaliyomo katika dhamiri zenu, na atakuhasibuni kwayo kwa thawabu na i'kabu. Na mkiwa mnakusudia wema na mkautenda, tena mkatokea baadhi yenu mkateleza, na kisha mkarejea kwa Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Subhanahu atakusameheni. Kwani Yeye ni Mwenye kusamehe daima kwa wale wanao rejea kwake.
 

26. Na wape jamaa zako haki yao kwa kuwafanyia wema na kuwaunga; na kadhaalika masikini mwenye haja, na msafiri aliye katikana na mali yake. Wape hao haki yao katika Zaka na sadaka, wala usiyavuruge mali yako kwa utumiaji ovyo usio na maslaha.
 

27. Kwani wabadhirifu (watumiaji ovyo) wenzao ni Mashetani, wanapokea minong'ono yao wanapo wachochea wafanye ufisadi na watumie kwa uharibifu. Na ni mtindo wa Shetani daima kukufuru neema ya Mola wake Mlezi. Na sahibu yake ni hali kadhaalika.
 

28. Ukilazimika kujikurupusha na hao walio tajwa wenye haja, kwa sababu ya shida uliyo nayo, na ukawa hukuwapa kwa kuto kuwa nacho cha kuwapa sasa, na ilhali unataraji Mwenyezi Mungu atakufungulia baadae, basi nena nao kwa maneno mema ya kuwapa imani nawe.
 

29. Wala usiuzuilie mkono wako kutoa katika mambo ya kheri, ukaufanya kama ulio fungwa pingu za chuma shingoni mwako ukawa huwezi kuukunjua. Wala usiukunjue wote kabisa kwa kutumia ovyo. Utakuja tukanika kwa ubakhili na majuto, au utabaki huna kitu umefilisika kwa sababu ya ubadhirifu na israfu.
 

30. Hakika Mola wako Mlezi humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na humdhikisha katika wao amtakaye. Kwani Yeye anawajua vyema tabia zao, na anaziona hali zao. Basi Yeye humpa kila mmoja wao, pindi akishika njia zake, kwa inavyo wafikiana na hikima yake Mwenyezi Mungu.
 

31. Ikiwa yaliyo khusiana na riziki yamo mikononi mwa Mwenyezi Mungu, basi haikufaliini kuwauwa watoto wenu kwa kukhofu ufakiri utao weza kutokea. Kwani Sisi ni Wenye kudhamini riziki zao na riziki zenu. Hakika kuwauwa hao ni dhambi kubwa.
 

32. Wala msiukaribie uzinzi, kwa kuziingilia sababu zinazo pelekea uzinzi. Jambo hilo ni jambo la aibu na uovu usio fichikana, na hapana njia mbovu kama hiyo.
 

33. Wala msiuwe nafsi yoyote ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa ila kuuwa huko kukiwa kwa haki, kwa kuwa nafsi hiyo inastahiki kuuwawa kwa ajili ya kisasi au kuwa ni adhabu ya sharia. Na mwenye kuuliwa kwa kudhulumiwa Sisi tumempa jamaa yake wa karibu haki juu ya yule muuwaji, kwa kutaka kwa Qadhi auliwe kwa kisasi. Lakini naye asipite mpaka katika kuuwa, akataka kumuuwa mtu mwengine asiye kuwa muuwaji, au kwa kuwauwa wawili badala ya mmoja. Kwani Mwenyezi Mungu amemsaidia huyo kwa kumpa haki ya kisasi au kulipwa fidiya. Basi haimfalii kukiuka mipaka iliyo wekwa.
 

34. Wala msiyatumie mali ya yatima ila kwa njia iliyo bora kabisa, ya kuiamirisha na kuikuza. Na endeleeni hivyo mpaka huyo mtoto afike umri wa utambuzi kuweza kuendesha mambo yake. Na akisha fika hivyo basi mkabidhini mali yake, na timizeni ahadi zote mlizo chukua. Kwani Mwenyezi Mungu atamsaili aliye vunja ahadi kwa kuvunja kwake, na atamhisabia kwa hayo.
 

35. Na mnapo mpimia mushtiri mpimieni vilivyo, na pimeni mizani kwa uadilifu. Kwani kuweka sawa vipimo na mizani ni bora kwenu kwa hapa duniani, kwa sababu huwaraghibisha watu kufanya nanyi biashara. Na malipo mazuri zaidi ni ya Akhera.
 

36. Ewe mtu! Usifuate maneno wala vitendo usivyo vijua. Basi usiseme: Nimesikia...na hali hukusikia. Au: Najua...na hali hujui. Kwani masikio, macho na moyo, vyote hivyo Siku ya Kiyama vitamuuliza mtu kwa alivyo tenda kwavyo.
 

37. Wala usitembee katika ardhi kwa kiburi na majivuno. Kwani vyovyote utavyo fanya huwezi kuipasua ardhi kwa nguvu za mkanyago wako, na kama utavyo kuwa mrefu huwezi kuipita urefu milima.
 

38. Yote hayo yaliyo tajwa katika mausio ni mambo mabaya yaliyo katazwa na yanayo chusha na kuchukiza kwa Mola wako Mlezi.
 

39. Na hayo ni katika aliyo kufunulia Mola wako Mlezi, katika kuijua haki kwa dhati yake, na kheri ipate kutendwa. Wala usimfanyie Mwenyezi Mungu kuwa na mungu mwengine, usije kutupwa katika Jahannamu ukijilaumu na ukilaumiwa, umeangamia na umefurushwa mbali na rehema za Mola wako Mlezi.
 

40. Subhanahu anayachukia wayasemayo makafiri kwamba Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu. Anasema: Mola wenu Mlezi amekufadhilisheni kuliko Mwenyewe kwa kukupeni nyinyi watoto wanaume wenye nguvu, na Yeye akawafanya Malaika ni banati  zake kwa mnavyo dai? Kwa maneno yenu haya mnazua matusi makubwa.
 

41. Sisi tumebainisha katika Qur'ani hii kwa uwazi mzuri, tukipiga mifano na kutoa mawaidha na hukumu, ili wapate kwaidhika hawa washirikina. Lakini nyoyo zao zimekuwa kama mawe. Kubainisha huku hakukuwazidishia ila kuzidi kuwakimbiza na Haki.
 

42. Ewe Nabii! Ili kudhihirisha upotovu wa madai yao wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu, sema: Lau kuwa wapo miungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu kama wasemavyo, hao miungu wangeli tafuta njia kumfikilia huyo Mwenye Ufalme wa mwisho ili wapate kushindana naye.
 

43. Mwenyezi Mungu ametakasika kabisa kama anavyo stahiki, na ametukuka aliye mkuu shani yake  na yote wanayo dai kuwa wapo pamoja na Yeye miungu wengine.
 

44. Hakika mbingu saba na ardhi, na viumbe vyote viliomo humo, vinamtakasa na kumtukuza, na vinaonyesha uzuri wa kuumba kwake, na kutakasika kwake Subhanahu na kila upungufu, na kukamilika ufalme wake, na kwamba Yeye hana mshirika na yeyote katika viumbe wa Ufalme wake uliyo enea. Vyote hivyo vinamtakasa na kumsifu. Lakini makafiri hawafahamu hoja hizi kwa kutawaliwa nyoyo zao na mghafala. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwao, na Mwenye kuwasamehe wanao tubu. Kwa hivyo hawafanyii haraka kuwapa adhabu.
 

45. Ewe Nabii! Unapo soma Qur'ani inayo taja dalili za Haki, Sisi huweka pazia, lenye kukuficha baina yako na wale wasio amini kufufuliwa na malipo, pale wanapo taka kukushambulia. Kwa hivyo hawakuoni.
 

46. Na kwa mujibu wa hikima yetu ya kupotoa na kuongoa huweka vifuniko juu ya nyoyo zao, wasipate kuifahamu Qur'ani ilivyo. Na katika masikio yao hutia uziwi basi hawasikii lenye manufaa kwao. Hayo ni kwa sababu ya kupindukia katika inda yao na majivuno yao. Na pale unapo mtaja Mola wako Mlezi katika Qur'ani peke yake bila ya kuwataja miungu yao, wao basi hurejea nyuma wakaacha kukusikiliza.
 

47. Sisi tunajua vyema vile wanavyo isikiliza Qur'ani nao ilhali wanaikejeli na kuifanyia maskhara na huku wanakusikiliza. Nao wanayaficha yaliyo semwa. Na hiyo ndiyo kauli ya wenye kudhulumu katika siri zao, wakisema: Ikiwa mtamfuata huyu basi hamumfuati ila mtu aliye geuzwa akili yake.
 

48. Hebu angalia vipi walivyo kushabihisha; wamekushabihisha na mtu aliye rogwa, na wakakuita kohani, mtunga mashairi, wakaipotea njia ya hoja. Kwa hivyo wasiweze kupata njia ya kuzua tusi linalo kubalika, au kwa hivyo wakaukosa uwongofu, na wasiipate njia ya kuufikilia.
 

49. Wanao kataa kuwa watafufuliwa  wanasema: Hivyo tutafuliwa baada ya kwisha kuwa mafupa yaliyo bunguliwa, na mapande mbali mbali, tukawa hai na umbo jipya? Haya hayaingii akilini.
 

50. Ewe Nabii!  Waambie: Hata mkiwa mawe yasiyo na uhai, au chuma, ambacho ni kigumu kuliko jiwe,
 

51. Au umbo jingenelo lolote ambalo mnaona kwa mawazo yenu haliwezi kuwa hai, basi hapana shaka yoyote mtafufuliwa! Watasema kwa kuona ni muhali: Nani atakaye turejesha hivyo? Waambie: Atakurjesheeni Mwenyezi Mungu, yule yule aliye kuumbeni mara ya kwanza. Watakutikisia vichwa vyao kwa mastaajabu, nao wakisema kwa kejeli: Huko kufufuliwa unako tuahidi kutakuwa lini? Waambie: Nataraji kutakuwa karibu!
 

52. Na siku atapo kufufueni Mwenyezi Mungu kutoka makaburini kwenu, mtafufuliwa nanyi mkimshukuru na kumsifu  Mola wenu Mlezi kwa ukamilifu wa uwezo wake. Na mtadhani kuwa hamkukaa makaburni kwenu ila muda mchache tu. Mtaona muda ni mfupi kwa mnasaba ya hayo mnayo yaendea.
 

53. Ewe Nabii! Waambie waja wangu Waumini wanapo pambana na washirikina waseme maneno yaliyo bora ya kukinaisha, na waachilie mbali kutumia maneno makali makali yanayo sabibisha shari na uharibifu. Kwani Shetani huleta fisadi baina ya Waumini na makafiri, kwa kuwa yeye ni adui aliye wazi wa binaadamu.
 

54. Mola wenu Mlezi ndiye anaye jua vyema mwisho wa mambo yenu. Akipenda atakurehemuni kwa kukupeni tawfiki ya Imani, (uwezo wa kuamini) au akipenda atakupeni adhabu kwa kuikosa hiyo Imani. Wala Sisi hatukukupeleka wewe uwe ni mwakilishi wao kwa mambo yao, hata uwalazimishe kuamini. Bali tumekutuma uwe ni mbashiri kuwapa khabari njema wenye kusadiki, na mwonyaji kuwaonya wanao kanusha. Waachilie mbali, na waamrishe  sahaba zako wawastahamilie.
 

55. Na Mola wako Mlezi anajua vilivyo vyote viliomo mbinguni na ardhini, na anajua hali zao. Basi anawakhiari miongoni mwao kwa kuwapa Unabii awatakao. Naye amekukhiari wewe kwa kukupa Utume wake. Basi haiwafalii wao kuudhika na Unabii wako. Na hao Manabii si wote sawa sawa kwa daraja mbele yake Aliye tukuka shani yake. Bali baadhi yao ni bora kuliko wenginewe. Naye amewatukuza baadhi ya Manabii juu ya wengine kwa miujiza, na wingi wa wafwasi, si kwa ufalme. Basi alitukuzwa Daudi kwa kuwa kapewa Zaburi, si kwa kuwa kapewa ufalme. Basi hapana ajabu kuwa wewe, Muhammad, ukapata fadhila kubwa kabisa kwa kuwa umepewa Qur'ani.
 

56. Waambie hawa wanao abudu viumbe na wanadai kuwa hao ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu: Waombeni hao mnao waabudu inapo kuteremkieni shida, au mkakhofu kuwa itakushukieni. Hamtopata kwao chochote cha kukuondoleeni madhara yenu, wala kuyahamisha akapewa mwinginewe.
 

57. Na hakika hawa viumbe wanao waomba wale wanao waabudu, wao wenyewe wanamuabudu Mwenyezi Mungu, na wanaomba wapate daraja na cheo kwake kwa ut'iifu, na wana pupa ya kutaka wawe karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, na wanatumaini kupata kwake rehema, na wanaikhofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mwenyezi Mungu inatakikana kutahadhari nayo na kuiogopa!
 

58. Na ni mazoea yetu kuuteketeza kila mji na watu wake unapo dhulumu mji huo. Au huwapa adhabu kali watu wake kwa mauwaji au vyenginevyo. Basi watu wako watahadhari, kwani hukumu yetu imekwisha hukumiwa, na imekwisha andikwa katika Kitabu chetu.
 

59. Watu wako wamekutaka uwaletee Ishara na miujiza. Nao hawakukinaika kwa yaliyo wajia ambayo huwakinaisha wenye akili. Na mwendo  wetu umekwisha wapitia hao wanao taka miujiza, na wanapo kubaliwa wasiamini, nao ni kuwang'olea mbali kwa adhabu kama tulivyo wafanyia wa kale.  Miongoni mwa hao ni watu wa Thamud. Walitaka miujiza, akawa ngamia mke ni muujiza wazi kwao wa kuondoa shaka zote. Wakamkanusha, yakatokea kwao yaliyo tokea! Na imekuwa hikima ya Mwenyezi Mungu kuwa asiwakubalie hayo waliyo yataka, kwa kuchelea wasiikatae miujiza, kwa kutarajia watakuja amini miongoni mwao, au watakuja zaa watakao amini. Na miujiza hakika Sisi huwapelekea watu kwa kuwatia khofu na kitisho.
 

60. Ewe Nabii! Kumbuka tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amewazunguka hao watu. Wao wamo wamedhibitiwa na kudra yake. Basi wewe wafikishie Ujumbe wala usimwogope yeyote katika wao. Mwenyezi Mungu atakulinda nao. Na mambo ya ajabu uliyo yaona katika Usiku wa Israi (Safari ya Usiku), hatukuyafanya Sisi ila yawe ni mtihani na majaribio kwa wanaadamu. Kwa hayo ipate kuzidi Imani ya Muumini, na ukafiri wa kafiri. Na wala hatukuufanya ule mti ulio subiwa katika Qur'ani, nao ni Mti wa Zaquum, unao mea huko Motoni, isipo kuwa ni kuwafanyia  wao pia mtihani pale walipo sema: Moto unaunguza mti, basi vipi mti umee katika moto? Pia ni kuzidi kuwahadharisha kwa hayo. Lakini kuwahadharisha kwetu hakuwazidishii isipo kuwa kupindukia kiwango kikubwa kabisa.
 

61. Na Mwenyezi Mungu anakumbusha asli ya kuumba na uadui baina ya mwanaadamu na Iblisi, pale alipo waambia Malaika: Msujudieni Adam kwa kumuamkia na kumhishimu kwa kumuinamia. Hapo hapo wakasujudu. Isipo kuwa Iblisi akakataa, na akasema kwa chuki: Vipi nimsujudie uliye muumba kwa udongo, na hali mimi umeniumba kwa moto. Mimi ni bora kuliko yeye.
 

62. Iblisi akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hebu nambie khabari za huyu uliye mtukuza juu yangu, ukaniamrisha nimsujudie. Kwa nini ukamtukuza kuliko mimi, na mimi ni bora kuliko yeye? Naapa kwa Utukufu wako! Ukinibakisha nihai mpaka Siku ya Kiyama, basi nitawahiliki dhuriya zao watao wazaa kwa kuwaghuri, isipo kuwa wachache tu kati yao utakao walinda na kuwahifadhi.
 

63. Mola akamwambia kwa kumtisha na kumlegezea kamba: Endelea na shani yako uliyo jichagulia kuifuata. Atakaye kut'ii wewe katika wana wa Adam, basi Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yako na yao, malipo ya kutosha yaliyo kamilika.
 

64. Na wazuge na wavute kwa kuwaita wamuasi Mwenyezi Mungu hao unao waweza miongoni mwao. Na fanya kila juhudi yako ya namna zote za udanganyifu. Na shirikiana nao katika kuchuma mali ya haramu, na kuyatumia kwa haramu, na kuwakufurisha watoto na kuwaghuri wafanye fisadi. Na wape ahadi za uwongo, kama kuwa miungu yao itawaombea, na kuwa watapata utukufu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya nasaba zao. Na Shetani hawaahidi wafwasi wake ila kwa udanganyifu na uficho.
 

65. Ama waja wangu walio nisafia niya Mimi wewe huna uwezo wa kuwapotoa, kwa kuwa wao wanamtegemea Mola wao Mlezi. Na Yeye anatosha kabisa kuwa ni wa kuwanusuru wakimtaka msaada wa kusalimika nawe.
 

66. Mola wenu Mlezi ni Yeye peke yake ndiye anaye ziendesha marikebu baharini ambazo kwazo nyinyi mnatafutia manufaa kwa biashara na mengineyo. Yeye daima ni Mwenye rehema kwenu.
 

67. Mkisibiwa na madhara na mkakabiliwa na  khatari katika bahari, hukukimbieni wote hao muwaombao kwa haja zenu isipo kuwa Mwenyezi Mungu peke yake. Kwani nyinyi hapo hamumkumbuki mwenginewe. Lakini akisha kuvueni na kuzama na akakufikisheni nchi kavu, mnaacha Tawhid, kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja, na mnakufuru neema. Ndio mtindo wa binaadamu daima kukataa neema.
 

68. Na hapo tukisha kuvueni mkafika nchi kavu, kwani ndio mmeaminisha kuwa basi haikupateni adhabu ya Mwenyezi Mungu? Hasha! Akitaka anaweza akaipindua ardhi ikakuteketezeni chini yake. Na akitaka atakupelekeeni upepo mkali ukutupieni kokoto na mawe, na wala msipate wa kukulindeni na yanayo kupateni.
 

69. Au nyinyi mmeaminisha kuwa Mola wenu Mlezi hatakurejesheni tena baharini, na akuleteeni tufani la upepo livunjilie mbali hicho chombo chenu? Akakuzamisheni kwa sababu ya kuto thamini neema yake pale alipo kuokoeni mara ya kwanza? Tena hapo hamtapata wa kukuteteeni kwetu kwa tuliyo kufanyieni ili mpate kusalimika.
 

70. Na hakika Sisi tumewatukuza wana wa Adam kwa kuwapa umbo zuri lilio nyooka, na matamshi, na uwezo wa kukhiari mambo. Na tukawapa hishima na utukufu pindi wakit'ii. Na tukawapakia nchi kavu juu ya wanyama, na baharini katika marikebu, na tukawaruzuku vitu vitamu, na tukawafadhilisha fadhila kubwa kuliko viumbe vingi kwa kuwapa akili na kuweza kufikiri.
 

71. Ewe Nabii! Waambie watu wako: Siku tutapo waita kila kikundi kwa alama zao wanazo zijua, au mwongozi wao wanaye mfuata, au Nabii, au Kitabu wakaambiwa: Enyi watu wa Musa! Au Enyi watu wa Qur'ani! Na kadhaalika, ili wapokee vitabu vya a'mali zao. Basi atakaye pokea kitabu cha a'mali zake kwa mkono wake wa kulia, na hao ndio wenye bahati njema, hao watasoma kitabu chao kwa furaha.  Na wala hawatapunguziwa katika ujira wao duni ya kitu.
 

72. Ama yule wa kikundi kingine yatamhuzunisha atayo yaona. Na atazibiwa njia za kuokoka. Na atakuwa kipofu asione pa kuepuka adhabu yake, kama alivyo kuwa duniani kipofu haioni Njia ya Haki na Uwongofu! Na anaye kuwa duniani kipofu (wa moyo) basi Akhera ni kipofu zaidi, na yu mbali zaidi na Njia ya Kheri.
 

73. Hakika washirikina wanatafuta kila njia wakuachishe Qur'ani utafute miujiza myengineyo, ili uwe kama uliye tuzulia Sisi uwongo. Na hapo ndio watakufanya uwe rafiki yao! Na hila hizi zimekaririwa na zimekuwa nyingi. Na kwa hivyo ungeli karibia kuyafuata wayatakayo, ila kwa kuwa wewe ni Mtume wetu uliye muaminifu, hayakuwa hayo.
 

74. Upole wetu umekugubika wewe, tukakulinda usiwakubalie matakwa yao, na tukakupa nguvu usimame juu ya Haki. Na lau kuwa si hayo ungeli karibia kuwakubalia kwa tamaa ya kuwa huenda ikafika siku imani yao ikakamilika baadae wakisha anza kuingia katika Uislamu.
 

75. Na lau ungeli karibia kuwaelekea hao, basi tungeli kukusanyia adhabu za duniani tukazifanya mardufu, na adhabu za Akhera nazo tukaziongeza mara mbili vile vile. Na wala usingeli pata yeyote wa kukunusuru na adhabu. Lakini hayo hayawi kabisa, hayawezi kumfikilia Mtume wetu Muaminifu.
 

76. Na makafiri wa Makka wamejaribu, na walikaribia kukuudhi mpaka wakutoe kwenye ardhi ya Makka kwa uadui wao na chuki zao. Na lau yangeli kuwa hayo, basi wao nao wasingeli baki humo ila muda mchache tu, kisha washindwe katika hayo mambo yao, na hukumu iwe ya Mwenyezi Mungu.
 

77. Na huo ndio mwendo wetu kwa Mitume wa kabla yako - huwahiliki wale wanao wafukuza Manabii wao. Na wala hapana mabadiliko katika mwendo wetu.
 

78. Shika Sala zilizo faridhiwa, tangu kupinduka jua kati ya mbingu kuelekea upande wa machwea jua, mpaka kiza cha usiku. Na hizi ndizo Sala za Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha. Na pia shika Sala ya Alfajiri ambayo wanaishuhudia Malaika.
 

79. Na katika wakati wa usiku amka, kwa kusali Sala ya Tahajjud. Hiyo ni ibada ya zaidi juu ya zile Sala Tano. Hii imekukhusu wewe tu, kwa kutaraji kuwa Mola wako Mlezi atakuweka Siku ya Kiyama makamo watakao kusifia viumbe.
 

80. Na sema: Ewe Mola Mlezi! Niingize maingizo ya kuridhisha matukufu katika kila unapo niingiza katika jambo au pahala. Na unitoe kwa kutoka kunako ridhisha kutukufu. Na kwa fadhila yako nijaalie nguvu za kunisaidia niwashinde maadui zangu.
 

81. Na sema ukiwaonya watu wako washirikina: Haki ya Tawhid, Imani ya Mungu Mmoja, na Dini ya Kweli na Uadilifu, imekwisha fika. Na uwongo, na ushirikina, na dini ya ufisadi na dhulma, yote hayo yameondoka. Kwani uwongo daima hauna dawamu.
 

82. Na vipi Haki isiwe na nguvu na hali Sisi tunateremsha katika Qur'ani dawa ya kuponyesha maradhi ya shaka katika vifua vya watu, na sababu za kuwapatia rehema wanao iamini! Na madhaalimu hawana linao wazidia ila khasara tu kwa kuikataa kwao.
 

83. Na hakika katika maumbile ya mwanaadamu ni kujidanganya na kukata tamaa. Tukimneemesha kwa kumpa uzima na ukunjufu wa mali, hupuuza kutukumbuka na kutuomba, na hujitenga nasi kwa kiburi na majivuno! Na akiguswa na shari, kama ugonjwa na ufakiri, huwa mwingi wa kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
 

84. Ewe Nabii! Waambie makafiri wa Kikureshi kwa kuepuka kuchochea ugomvi na makindano: Kila mmoja wetu na mmoja wenu anatenda na anakwenda kwa kufuata njia yake. Na Mola wenu Mlezi ni Mjuzi mno, wala hana ajuaye kuliko Yeye kumjua nani aliye shika njia sawa na kufuata Haki. Na huyo humlipa ujira wake kaamili. Na kumjua aliye potea njia, na huyo humpa adhabu kama anayo stahiki.
 

85. Ewe Muhammad! Watu wako wanakuuliza kwa kutomezwa na Mayahudi: Nini hakika ya Roho? Waambie: Roho ni katika ilimu yake Mwenyewe Mola wangu Mlezi aliyo jikhusisha nayo Yeye. Na nyinyi hamkupewa ilimu ila chache tu ukilinganisha na ilimu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
 

86. Na lau tungeli taka kuifuta kabisa kifuani mwako hiyo Qur'ani tuliyo kufunulia tungeli fanya hivyo, na kisha usingeli mpata yeyote wa kukunusuru katika watu wako.
 

87. Lakini tumeiacha Qur'ani ibaki vile vile kifuani mwako kwa rehema kutoka kwa Mola wako Mlezi, kwani fadhila zake kwako wewe ni kubwa mno katika muujiza huu.
 

88. Waambie, kwa kushindana nao, kama wanaweza walete mfano wake. Nao hawawezi! Hata wakikusanyika watu na majini wakasaidiana kuleta mfano wa hii Qur'ani kwa mpango wake na maana yake, hawawezi; na wanga saidiana wao kwa wao.
 

89. Na katika Qur'ani hii tumewaeleza watu kwa namna mbali mbali kila maana kama ni mifano katika maajabu yake. Lakini watu wengi walikataa ila kupinga na kuchukia.
 

90. Ilipo dhihiri kushindwa kwao na Qur'ani, na wakabanwa kwa hoja, wakataka waletewe ishara nyingine na miujiza mingine. Hicho ni kitendo cha mwenye kushindwa hoja, aliye emewa na kutahayari. Ndio wakasema: Hatutokuamini mpaka ututimbulie katika ardhi ya Makka chemchem ambayo maji yake hayakatiki.
 

91. Au uwe nacho kitalu Makka cha mitende na mizabibu chenye kupita mito kati yake! (Kwa kujua kuwa ardhi ya Makka ni kavu haioti kitu.)
 

92. Au mbingu ituangukie vichwani mwetu kwa mapande kama ulivyo dai kuwa Mwenyezi Mungu anatuahidi hayo. Au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika tukabiliane nao macho kwa macho!
 

93. Au uwe na nyumba iliyo pambwa kwa dhahabu, au upae mbinguni. Na hata hivyo hatukusadiki mpaka ukituletea kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kinacho thibitisha ukweli wako tukisome!  Waambie: Mola wangu Mlezi ametakasika kabisa na kuhukumiwa na yeyote, au yeyote kushirikiana naye katika kudra yake! Mimi si chochote ila ni mwanaadamu kama Mitume wote wengineo. Na wala wao hawakuwaletea watu wao muujiza ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
 

94. Na nini  kilicho wazuilia washirikina wa Makka kuifuata Haki ulipo wajia wahyi (ufunuo) pamoja na miujiza isipo kuwa madai yao kwa ujinga wao ya kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hatumi Mitume wanaadamu, ila huwa ni Malaika!
 

95. Sema kwa kuwarudi: Lau kuwa duniani badala ya wanaadamu wapo Malaika wanatembea kama wanaadamu na wamekaa humo, basi tungeli wateremshia kutoka mbinguni Malaika kuwa ni Mitume wao katika jinsi yao. Lakini Malaika si kama binaadamu; na wangeli kuja basi wange kuja kwa sura za watu.
*
 

96. Sema: Kama mnaukataa Utume wangu, basi Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutuhukumu baina yangu na nyinyi, akathibitisha ukweli wa Ujumbe wangu kwenu. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kujua hali zenu, na Mwenye kuviona vitendo vyenu. Naye ni Mwenye kukulipeni kwa hivyo.
 

97. Waambie: Yule ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa kwa kuwa yu tayari kufuata uwongofu, basi huyo ni mwongofu. Na anaye mpotoa kwa kufisidika khulka yake, hutopata wa kuwanusuru asiye kuwa Yeye wa kuwaongoa duniani. Na Akhera tutawakusanya wakikokotwa juu ya nyuso zao, hawaoni, wala hawasemi, wala hawasikii. Na mahali pao wanapo pelekwa kukaa ni Jahannamu. Kula moto ukipungua ukali wake Mwenyezi Mungu anazidi kuuchochea uwake kwa nguvu zaidi.
 

98. Adhabu hiyo ndiyo malipo yao kwa sababu ya kuzikataa dalili tulizo waletea za kuthibitisha Haki, na kwa ile kauli yao kusema: Hivyo sisi tutafufuliwa kwa umbo jipya baada ya kwisha kuwa mifupa na vumbi?
 

99. Jee wameghafilika na hawakujua kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi, juu ya ukubwa wao, ni Mwenye kuweza kuumba watu na majini kama wao? Na Mwenye kuweza hayo, vipi awe hawezi kuwarejesha wao upya, na hilo ni jepesi zaidi kwake! Na Yeye Subhanahu ameweka muda maalumu wa kuwarejesha tena baada ya kwisha kufa, na huo hauna shaka kuwa. Na muda huo ndio Siku ya Kiyama. Na juu ya hivyo walio zidhulumu nafsi zao kwa ukafiri wanakataa baada ya kuletewa hoja hizi. Na hayo si kwa lolote ila kwa ukafiri tu.
 

100. Waambie hawa washirikina: Lau kuwa mnazimiliki riziki za Mola wangu Mlezi, mngeli zifanyia ubakhili kwa kuogopa ufakiri. Kwani ni tabia ya watu kuwa na pupa na ubakhili. Na Mwenyezi Mungu, Mkwasi na Karimu, humpa anacho taka amtakaye, na huteremsha miujiza aitakayo Yeye, sio waitakayo watu. Na Yeye katika yote hayo ni Mwenye hikima na Mjuzi.
 

101. Na lau hawa watu wangeli letewa hizo ishara wazitakazo, wange zigeuzia uso, wala wasinge ziamini! Na Sisi tulimpa Musa Ishara tisa wazi (1). Na juu ya hivyo wakakufuru. Na Firauni akasema: Hakika mimi nakuona wewe, Musa,  ni mtu uliye rogwa!
(1) Hizo ishara tisa ni: 1. Fimbo, 2. Mkono Mweupe, 3. Tufani, 4. Nzige na vyura na chawa na damu, 5. Ukame na upungufu wa mazao, 6. Kupasuka bahari, 7. Kutimbuka maji baharini, 8. Kuning'inia mlima kama kivuli, 9. Kusemezwa na Mola wake Mlezi.
 

102. Musa akasema: Ewe Firauni! Unajua vyema kuwa aliye ziteremsha Ishara hizi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Kwani ni Yeye ndiye Mwenye kuweza hayo. Nazo Ishara hizo zi wazi, zinakuonyesha ukweli wangu. Lakini wewe unafanya kiburi na inadi tu. Na hakika mimi nakuona wewe, Firauni, kuwa ni mwenye kuangamia ikiwa hutoacha inadi yako.
 

103. Firauni akashikilia uasi wake, akataka kumtoa Musa na Wana wa Israili katika nchi ya Misri. Tukamzamisha yeye na askari wake wote.
 

104. Tukamvua Musa na kaumu yake, na baada ya kumzamisha Firauni tukasema kuwaambia
Wana wa Israili: Kaeni katika nchi takatifu ilioko Sham. Ukija wakati wa uhai wa pili tutakutoeni makaburini kwenu kwa mchanganyiko. Kisha tutakuhukumuni kwa uadilifu.
 

105. Na hatukuiteremsha Qur'ani ila kwa kuunga mkono hikima ya Mwenyezi Muungu, iliyo pelekea kuteremshwa kwake. Nayo hiyo Qur'ani kwa dhati yake haikuteremka ila kuwa imekusanya Ukweli wote. Kwani itikadi zake ndizo zilizo sawa, na hukumu zake ndizo zilizo nyooka. Na wewe, ewe Nabii, hatukukutuma ila uwe mbashiri wa kuwabashiria Pepo wenye kuamini, na mwonyaji kuwaonya wanao ukanya Moto. Basi wewe huna jukumu lolote ikiwa wao hawaamini.
 

106. Na hii Qur'ani tumeigawa na tumeiteremsha kipande kipande kwa muda mrefu, ili uwasomee watu kwa taratibu wapate kuifahamu. Tumeiteremsha kidogo kidogo kwa utulivu bila ya matatanisho.
 

107. Waambie makafiri wa Makka kwa kuwatisha: Jichagulieni nafsi zenu mlitakalo - kuiamini Qur'ani au la! Kwani hakika walio pewa ilimu sawa na fahamu baraabara kabla ya kuteremka kwake, wakisomewa Qur'ani huangukia kwenye nyuso zao kwa kusujudu na kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu.
 

108. Na wao husema: Mola wetu Mlezi ametakasika na ila ya kwenda kinyume na ahadi yake ya kuneemesha na kuadhibu alio ahidi. Kwani ahadi yake lazima itimie bila ya shaka yoyote.
 

109. Na huangukia tena kwenye nyuso zao mara ya pili wakilia kwa kumkhofu Mwenyezi Mungu, na Qur'ani inawazidisha unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu.
 

110. Waambie hawa washirikina: Mwiteni Mwenyezi Mungu kwa jina la Allah, au jina la Rahman; kwani jina lolote mtalo mwitia ni zuri. Yeye Mtukufu ana majina mengi mazuri mazuri. Wala hamdanganyikiwi kwa kutumia majina mengi kuwa kwa hivyo mwenye kuitwa ni zaidi ya Mmoja. Na unapo soma Qur'ani katika Sala zako, basi usipaze sauti yako wakasikia washirikina wakakusibabi na wakakuudhi. Wala usifanye kwa siri hata Waumini wakawa hawasikii. Kuwa kati kati katika kusoma kwako.
 

111. Nasema Alhamdulillah, Himdi zote, yaani sifa na shukrani, ni za Mwenyezi Mungu ambaye hakuzaa mwana, kwani hamhitajii; wala hana mshirika katika ufalme, kwani Yeye peke yake ndiye aliye uanzisha; wala hana msaidizi wa kumtia nguvu kwa udhaifu fulani unao mpata. Na mtukuze Mola wako Mlezi kwa utukufu mkubwa ulio laiki naye.