1. Enyi washirikina! Kuweni na yakini
kwamba aliyo kuahidini Mwenyezi Mungu kuwa yatakuwa Siku ya Kiyama yapo
karibu kutokea bila ya shaka. Basi msifanye maskhara kwa kuyahimiza yatokee.
Mwenyezi Mungu ametakasika na kuwa na mshirika wa kuabudiwa badala yake. Na hiyo
miungu mnayo mshirikisha naye haiwezi jambo lolote.
2. Mwenyezi Mungu huteremsha Malaika kwa yanayo
huisha nyoyo katika Wahyi wake (ndio hiyo Roho) juu ya anaye mkhiari kumpa Utume
katika waja wake, ili watu wajue kwamba hapana mungu wa kuabudiwa kwa Haki ila
Mimi. Basi jitengeni na yanayo nikasirisha na yatayo kuleteeni adhabu. Na
shikamaneni na ut'iifu ili ukukingeni na adhabu.
3. Yeye ameumba mbingu na ardhi kwa mujibu wa
hikima. Ametakasika kuwa na mshirika wa kufanya lolote katika utawala wake, au
wa kuabudiwa kama Yeye.
4. Amemuumba kila mmoja katika wanaadamu kutokana
na maji maji yasiyo shikamana, nayo ni manii. Kutokana na hayo ndio anakuwa mtu
mwenye nguvu za kujitetea nafsi yake, mshindani na makhasimu zake, mwenye kuweka
wazi hoja zake.
5. Enyi waja! Mwenyezi Mungu amekufadhilini -
amekuumbieni nyama hoa, wanyama wa kufuga, kama ngamia, na ng'ombe, na
kondoo, na mbuzi, ili mpate kutokana na sufi zao na manyoa yao vifaa vya
kukupatieni joto kujihifadhi na baridi, na mle nyama yao mhifadhi uhai wenu.
6. Na mnapata kwao raha na furaha mnapo waona
wanarejea kutoka machungani na matumbo yao na viwele vimejaa, na mnapo toka nao
kwenda makondeni na machungani wakikimbilia malisha yao.
7. Na wanakubebeeni mizigo yenu mizito mpaka
kwenye miji ambayo hamwezi kuifikilia bila yao isipo kuwa mzitie nafsi zenu
katika juhudi na mashaka makubwa. Hakika Mola wenu Mlezi aliye kutengenezeeni
hayo yote kwa ajili ya raha yenu bila ya shaka ni Mwingi wa upole, na Mkunjufu
wa rehema kwenu.
8. Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni farasi, na
nyumbu, na punda mpate kuwapanda. Na mnawafanya ni pambo la kuingiza furaha
katika nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu atakuja umba msivyo vijua sasa, katika
vyombo vya kupanda na vya kukata masafa miongoni mwa alivyo msahilishia Mwenyezi
Mungu binaadamu pindi akitumia akili yake na akafikiri kwayo, na akaongoka kwa
kutumia kila uwezo.
9. Na juu ya Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa
fadhila yake na rehema yake, kukuonesheni Njia Iliyo Nyooka ya kukufikisheni
kwenye kheri. Na zipo njia zilizo potoka zisio fika kwenye Haki. Na lau angeli
taka kukuongoeni nyote angeli kuongoeni kwenye Njia Iliyo Nyooka, lakini
amekuumbieni akili ya kutambua, na matakwa ya kuelekea, na akakuacheni na khiari
yenu.
10. Yeye ndiye anaye teremsha maji kutoka jiha
ya mbinguni. Katika hayo mnapata kunywa, na mengine ndio inapelekea miti kumea.
Nanyi hupeleka wanyama wenu wakale kwenye miti hiyo, nao wakupeni maziwa, na
nyama, na sufi, na manyoa, na nywele.
11. Kwa maji yateremkayo mbinguni humea makulima
ambayo tunakutoleeni nafaka na mizaituni, na mitende, na mizabibu na mengineyo,
katika kila namna ya matunda mlayo mbali yaliyo tajwa. Hakika kuwepo vitu hivi
ni alama ya kuwaongoa watu wanao nufaika kwa akili zao, wakazingatia uwezo uliyo
patisha hayo.
12. Na Mwenyezi Mungu ameufanya usiku
ukutumikieni kwa kuufanya uwe ndio wakati wenu wa kupumzika na mchana ni
muwafaka kuhangaika kwenu na kwenda kwa kazi zenu, na jua kukuleteeni joto na
mwangaza, na mwezi mpate kujua idadi ya miaka na hisabu, na nyota zinazo
kutumikieni kwa amri ya Mwenyezi Mungu ili mpate kujua njia katika kiza. Hakika
katika hayo zipo alama na dalili kwa watu ambao wananufaika kwa akili aliyo wapa
Mwenyezi Mungu.
13. Na pamoja na aliyo kuumbieni Mwenyezi Mungu
katika mbingu na akakutengenezeeni kwa faida yenu, amekuumbieni pia juu ya ardhi
wanyama namna nyingi, na mimea, na vitu visio na uhai. Na ndani ya ardhi yamo
maadeni ya rangi na sura mbali mbali na faida mbali mbali. Na yote hayo kwa
manufaa yenu. Hakika katika hayo zipo dalili wazi na nyingi kwa watu wanao
zingatia, na wakawaidhika, na wakajua kwa hayo uwezo wa Aliye waumba, na rehema
yake.
14. Ni Yeye aliye idhalilisha bahari, na
akaifanya ikutumikieni, mpate kuvua na mle nyama za samaki, laini na mpya mpya.
Na mtoe humo baharini mapambo kama lulu na marijani. Na ewe mwenye kuangalia
ukazingatia, unaona marikebu zinavyo pita baharini zikikata maji nazo
zimesheheni bidhaa na vyakula. Mwenyezi Mungu ameyadhalilisha hayo ili mnafuike
nyinyi, na mtafute riziki kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu kwa njia ya biashara na
nyenginezo, na mpate kumshukuru kwa aliyo kutengenezeeni, na hayo ni kwa
kukutumikieni nyinyi.
15. Na Mwenyezi Mungu amefanya katika ardhi
milima iliyo simama imara, ili kuizuia isiyumbe yumbe.(Mwaka 1956 wataalamu wa
geology, ilimu ya tabaka za ardhi, wamegundua kuwa kweli milima inasaidia
kuizuia ardhi isitaharaki na kuachana. Wamevumbua kuwa mabara, continents, yamo
katika kutaharaki. Kwa mfano kusini ya Amerika iliambatana na Afrika ya
Magharibi, na ilisota mpaka ikafanyikana milima ya Andes. Hali kadhaalika
Milima ya Himalaya ikazuia kusota kwa Bara Hindi. Pia wamegundua kuwa maki ya
gamba la ardhi kwa kawaida halizidi kilomita 6, lakini chini ya milima hufika
hata kilomita 35. Basi ni kweli kuwa milima ni kama vigingi vya kuzuia ardhi
isiyumbe, kama ilivyo sema Qur'ani miaka 1400 iliyo pita.)
Na Mwenyezi
Mungu amefanya katika ardhi mito inayo pita na maji yanayo faa kunywa na
kunyweshea makulima, na njia zilizo tengenezwa ili mpate kuzipitia kwendea
mtakako.
16. Na Mwenyezi Mungu ameweka alama za
kuwaongoza watu katika safari zao kwenye ardhi, na hivyo wanapata uwongozi
katika safari zao kwa nyota ambazo ameziweka mbinguni ziwaongoze wanapo kuwa
gizani hawazioni alama za ardhini.
17. Hebu ni sawa kwa mwenye akili nzima baina ya
Muweza na asiye weza, hata akamfanya Mwenye kuumba yote haya sawa na asiye weza
kuumba kitu? Enyi washirikina! Hivyo hamzioni athari za uwezo wa Mwenyezi Mungu
mkazingatia na mkamshukuru kwazo Mwenyezi Mungu?
18. Na mkitaka kuzihisabu neema za Mwenyezi
Mungu juu yenu, hamwezi kuzidhibiti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
kusamehe, Mkunjufu wa rehema. Basi tubuni kwake, na mumsafie ibada, ili apate
kukusameheni na kukurehemuni.
19. Na Mwenyezi Mungu kwa ujuzi wake ulio
kusanya kila kitu, anajua mnayo yaficha na mnayo yadhihirisha. Na hapana
chochote kinacho fichikana kwake cha siri yenu na jahari yenu.
20. Huyu Muumba, na Mjuzi wa kila kitu, ndiye
Yeye peke yake anaye stahiki kuabudiwa. Ama hayo masanamu mnayo yaabudu, hayo
hayawezi kuumba chochote, hata nzi. Bali hayo yenyewe yameumbwa, na pengine
mmeyaunda nyinyi wenyewe kwa mikono yenu.
21. Na hayo ni vitu visivyo na roho kama maiti,
hayana hisiya yoyote, wala hayataharaki, wala hayajui Kiyama kitakuja lini, wala
lini watafufuliwa hao wanao yaabudu. Wala si laiki yenu, enyi wenye akili, baada
ya haya mkadhani kuwa yatakufaeni kitu hata mkayashirikisha na Mwenyezi Mungu
katika kuyaabudu.
22. Na imekwisha wekwa wazi kwa kila dalili
kwamba hakika Mungu wenu anaye pasa mumuabudu peke yake ni Mungu Mmoja ambaye
hana mshirika wake. Na juu ya hayo wale wasio amini kufufuliwa na kuhisabiwa,
nyoyo zao zinaukataa Upweke wake. Kiburi chao kinawazuia kufuata Haki na
kuit'ii.
23. Hapana shaka kwamba Mwenyezi Mungu anayajua
wanayo yaficha na wanayo yatangaza, ikiwa ni itikadi au maneno au vitendo. Naye
atawahisabu kwa yote hayo, na atawaadhibu kwa kiburi chao. Kwani hakika Yeye
Subhanahu hawapendi wanao jivuna hata hawataki kusikia Haki na kuifuata.
24. Na wakiulizwa hao makafiri wanao jivuna:
Mola wenu Mlezi kamteremshia nini Muhammad? Wao hujibu kwa inda: Hayo anayo dai
kuwa Mwenyezi Mungu kamteremshia si chochote ila uzushi na upuuzi walio tunga
watu wa zamani naye akayanukulu na akawa anayakariri tu.
25. Wanasema hayo ili wawazuie watu wasimfuate
Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na mwisho wa kuishia mambo yao ni kuwa wataadhibiwa
Siku ya Kiyama kwa adhabu ya upotovu wao kwa ukamilifu, na adhabu ya baadhi ya
watu walio kuwa wakiwakhadaa na kuwadanganya mpaka wakapotea bila ya ilimu wala
kuchungua! Zingatia, ewe mwenye kusikia, kwa huu uovu wa madhambi wanayo
yafanya, vipi ukali wa adhabu watayo pata!
26. Na hawa makafiri wenye kiburi walitanguliwa
na wengine mfano wao. Walipanga njama zao kuwapangia Manabii wao, na wakafanya
hila kuwapoteza watu. Na Mwenyezi Mungu alizibomoa njama zao, akaiharibu miji
yao. Akawateremshia adhabu katika dunia ambayo hawakuitaraji.
27. Na kisha huko Akhera watapo fufuliwa watu na
wakahisabiwa kwa vitendo vyao, Mwenyezi Mungu atawasimamisha msimamo wa hizaya
na fedheha, atapo wafedhehi na afichue waliyo kuwa wakiyaficha vifuani mwao.
Atawaambia: Wako wapi hao miungu mliyo ifanya kuwa ni washirika wangu kwa
kuwaabudu? Nanyi kwa ajili yao mlikuwa mkinipiga vita Mimi na Mitume
wangu! Wako wapi wapate kukuungeni mkono, kama mlivyo kuwa mkidai?
Hawatoweza kujibu! Na hapo tena wale wanao ijua Haki, miongoni mwa Manabii, na
Waumini, na Malaika, watasema: Leo ndiyo hizaya na adhabu mbaya kabisa
zitawashukia makafiri!
28. Hizaya itawashukia makafiri walio endelea na
ukafiri wao mpaka Malaika walipo watoa roho, nao wamejidhulumu nafsi zao kwa
ushirikina na kutenda maovu, na wakasalimu amri tena baada ya inadi ndefu walipo
jua hakika ya makosa yao. Wakasema uwongo kwa jinsi walivyo shituka: Hatukuwa
duniani tukifanya maasi yoyote! Malaika na Manabii watawaambia: Hasha! Hakika
nyinyi ni waongo, bali mmetenda maasi maovu kabisa! Na Mwenyezi Mungu,
Subhanahu, anajua vyema kila dogo na kubwa mlilo kuwa mkilitenda katika dunia
yenu. Hakukuleteeni faida yoyote huko kukataa kwenu!
29. Na baada ya hayo wataambiwa: Mwisho wenu ni
kuingia Motoni, na adhabu ya huko ni ya milele, haikatiki! Na mbaya mno nyumba
ya Jahannamu kuwa ni makaazi ya kila mwenye kutakabari akakataa kufuata Haki na
Imani ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake.
30. Na walio muamini Mwenyezi Mungu na
wakajikinga na kila linalo mghadhibisha Yeye ikiwa neno, au kitendo, au itikadi,
wataambiwa: Mola wenu Mlezi kamteremshia nini Mtume wake? Wao watasema:
Amemteremshia Qur'ani...ndani yake mna kheri ya duniani na Akhera kwa watu wote,
na kwa hivyo wakawa miongoni mwa watu wema. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu huwalipa
wema kwa maisha mazuri katika uhai huu wa duniani. Na pahala pao Akhera ni bora
na pazuri zaidi kuliko waliyo yapata duniani. Na nyumba watayo ikaa wachamngu
Akhera ni hadi ya raha yake!
31. Nazo ni Bustani madhubuti za kudumu, zenye
kupitiwa na mito chini ya majumba na miti yake. Na hao watapata kila neema
waipendayo. Na mfano kama huu ndio malipo ya mema anayo walipa Mwenyezi Mungu
wachamngu wote wanao muamini, na wakajikinga na yanayo mkasirisha, na
wakavifanya vyema vitendo vyao.
32. Na ndio hao Malaika huzichukua roho zao na
hali wamesafika na uchafu wa ushirikina na maasi. Na Malaika watawaambia kwa
kuwatuza: Amani kwenu itokayo kwa Mwenyezi Mungu! Baada ya hii leo hamtopata la
karaha. Na ifurahieni Pepo mtakayo ingia kwa sababu ya vitendo vyema mlivyo
vitanguliza katika dunia yenu.
33. Hao ndio wachamngu walio jitengenezea Akhera
yao. Na hayo ndiyo malipo yao. Ama washirikina kwa sababu ya inadi yao na
kubakia kwao kwenye ushirikina wao, hawataraji ila Malaika waje kunyakua roho
zao nao wamezidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na vitendo vya shari. Na itawajia
adhabu ya Mola wako Mlezi iwateketeze wote. Na kama walivyo fanya makafiri hawa,
basi walikwisha wafanyia Manabii wao wale walio watangulia, na Mwenyezi Mungu
akawaadhibu kwa vitendo vyao. Wala Yeye hakuwadhulumu pale alipo waadhibu,
lakini wao wenyewe walizidhulumu nafsi zao walipo zitia katika adhabu kwa
ukafiri wao.
34. Yakawasibu malipo ya maovu waliyo yatenda,
na adhabu waliyo kuwa wakiikanya na kuikejeli ikawazunguka.
35. Na washirikina wakasema kwa inda na ukosefu:
Lau kama Mwenyezi Mungu angeli penda tumuabudu Yeye tu peke yake na tumt'ii kwa
anayo tuamuru, basi tusingeli muabudu mwenginewe, wala tusingeli harimisha sisi
wenyewe kitu asicho harimisha Yeye kama Bahira na Saiba. Na hii ni hoja potovu
wanayo itafutia njia katika ukafiri wao. Na makafiri walio kwisha tangulia
walitoa hoja kama hizo, baada ya kuwapelekea Mitume wetu, wakaamrisha Tawhidi
(kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja), na kumt'ii Yeye, na wakawakataza ushirikina na
kuharimisha asivyo harimisha Mwenyezi Mungu. Hoja ikasimama dhidi yao. Na Mitume
wetu wakatimiza tuliyo waamrisha wayafikishe. Na juu yetu kuwahisabu wao. Na
Mitume hawana jukumu zaidi ya hayo.
36. Na kila umma tuliwapelekea Mtume awaambie:
Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake. Na jitengeni na kila jabari mharibifu.
Na wafikishie ujumbe, na uwaongoze. Basi kikundi kikasikiliza uwongozi na
kikafuata, na Mwenyezi Mungu akakiongoa kwa kuwa kilijitayarisha vizuri kufuata
Njia Iliyo Nyooka. Na kikundi kingine kikapuuza kusikia Haki, kikastahiki kwenda
njia potovu, na Mwenyezi Mungu akakipelekea adhabu. Na ikiwa nyinyi, washirikina
wa Makka, mna shaka na haya, basi tembeeni katika nchi za karibu nanyi,
muangalie, mzingatie nini kilicho washukia wanao kanusha, kina A'ad na Thamud na
Kaumu Luut'i. Na vipi ilikuwa khasara yao na hilaki yao katika mwisho wao!
37. Ewe Nabii! Ikiwa una hamu mno ya kuwaongoa
washirikina katika watu wako, kwa kutumia ukomo wa juhudi yako, basi usiihiliki
nafsi yako kwa huzuni ikiwa hayo uyatakayo hayawi. Kwani hao wamekwisha milikiwa
na matamanio. Na Mwenyezi Mungu hawalazimishi kuongoka walio khiari upotovu na
wakaushikilia, kwani Yeye huwaacha wajichagulie wenyewe, nao watapata malipo
yao, nayo ni adhabu kubwa. Na wala hawatapata Siku ya Kiyama wa kuwanusuru na
kuwalinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
38. Na washirikina juu ya kumshirikisha Mwenyezi
Mungu wameongezea kuikanusha Siku ya Kiyama. Wameapa, ukomo wa nguvu zao za
kuapa, na wakakazania kwamba Mwenyezi Mungu hamfufui aliye kufa! Nao ni waongo
katika viapo vyao, na Mwenyezi Mungu atawafufua wote! Kwani Yeye amejichukulia
ahadi mwenyewe, na Mwenyezi Mungu kabisa hatokwenda kinyume na ahadi yake.
Lakini watu wengi miongoni mwa makafiri hawaijui hikima ya Mwenyezi Mungu katika
kuumba huu ulimwengu, na kwamba Yeye hakuumba kwa mchezo tu, wala wao hawajui
hisabu yake na malipo yake.
39. Hakika katika uadilifu wa Mwenyezi Mungu ni
kuwa atawafufua wote baada ya kufa kwao ili ipate wadhihirikia hakika ya mambo
waliyo khitalifiana. Waumini wapate kujua kuwa wao wako katika Haki, na makafiri
wajue kwamba wao walikuwa makosani kwa kumfanyia Mwenyezi Mungu washirika katika
Ungu, na pia ni waongo kwa kuapa kwao kwamba Mwenyezi Mungu hamfufui aliye kufa,
na ili yote makundi mawili yapate malipo yao kwa kujua na kwa sababu zake.
40. Na kuwafufua watu Siku ya Kiyama si jambo
zito kwetu, hata hao makafiri wakayaona hayawi. Kwani Sisi tutakapo kitu kiwe
hatuna haja ya lolote ila ni kusema tu: Kuwa! Na kinakuwa kama tutakavyo.
41. Na Waumini walio yaacha majumba yao kwa
ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na usafi wa imani yao, baada ya kudhulumiwa na
washirikina, tutawalipa duniani, kwa ikhlasi yao na kustahamili kwao adhabu,
maisha mema yasiyo patikana ila kwa jihadi. Na Siku ya Kiyama ujira wao utakuwa
mkubwa zaidi, na neema zao za Peponi ni kubwa zaidi. Lau kuwa wapinzani wao
wangeli jua hayo wasingeli wadhulumu na wakazidhulumu nafsi zao.
42. Na hao Wahajiri (Walio hama) ndio walio
vumilia adhabu walio ipata kwa sababu ya Itikadi yao, na wakamwachia hali yao
Mwenyezi Mungu peke yake, bila ya kumbali mwenginewe. Kwa ajili ya hayo
tumewapa bora ya malipo.
43. Na kabla ya kukutuma wewe, ewe Nabii, kwa
umma wako, hatukuwatuma kwa kaumu zilizo tangulia ila watu wanaume tulio
wafunulia kwa Wahyi yale tunayo yataka wawafikishie. Wala hatukuwatuma Malaika
kama watakavyo makafiri wa kaumu yako. Basi, enyi makafiri, waulizeni wenye
kuvijua Vitabu vya mbinguni, kama nyinyi hamyajui hayo. Watajua kuwa Mitume wote
wa Mwenyezi Mungu hawakuwa ila wanaadamu, wala si Malaika.
44. Na hao Mitume tuliwaunga mkono kwa miujiza
na dalili zilizo wazi za kuthibitisha ukweli wao. Na tuliwateremshia Vitabu vya
kuwabainishia sharia zao zenye maslaha yao. Na wewe, ewe Nabii, tumekuteremshia
Qur'ani uwabainishie watu Itikadi na Hikima ziliomo ndani yake, na uwatake
waizingatie, kwa kutaraji kuwa watazingatia, na watawaidhika, na mambo yao
yanyooke.
45. Yafaa vipi basi baada ya yote haya kuwa hao
washirikina wakaendelea katika inda yao, na wakampangia vitimbi Mtume? Je, kwani
wamedanganyika na upole wa Mwenyezi Mungu kwao, hata wakaitakidi kuwa
wameaminika na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na ardhi haitowameza kama ilivyo
mfanyia Qaaruun? Au kuwa adhabu haitowajia kwa ghafla katika kimbunga kama
ilivyo wapata kina Thamud nao hawajui inatoka wapi?
46. Au ikawahiliki kati ya nyendo zao katika
nchi kwa ajili ya biashara nao wapo mbali na makwao, hata wasiweze kuikwepa
adhabu ya Mwenyezi Mungu? Kwani Yeye haemewi na chochote akitakacho!
47. Au akawateremshia adhabu katika nafsi zao na
mali yao kidogo kidogo, na hali wao kila wakati wa hiyo adhabu wamo katika khofu
na kuingoja iwateremkie. Basi, enyi washirikina! Msiendelee, mkajidanganya kwa
kuchelewa adhabu yenu! Upole wake Mwenyezi Mungu ulio enea, na rehema yake iliyo
kunjuka, ndio iliyo hukumu asikuleteeni kwa haraka adhabu ya hapa duniani, ili
mpate kufikiri na kuzingatia. Kwani Yeye Subhanahu ni Mpole na Mwenye kurehemu.
*
48. Hao makafiri wameghafilika na Ishara za
Mwenyezi Mungu zilizo wazunguka. Wala hawatazami wakazingatia vitu alivyo viumba
Mwenyezi Mungu vilivyo tulia, na hali vivuli vyake vinakwenda. Mara vinanyookea
kulia na mara kushoto, vikifuata mwendo wa jua mchana, na mwendo wa mwezi usiku.
Na vyote hivyo vinat'ii amri ya Mwenyezi Mungu, vinafuata hikima ya mipango
yake. Na lau washirikina wangeli zingatia haya, wangeli jua kuwa Muumba wake, na
Mwenye kuyapanga ni Yeye peke yake anaye stahiki kuabudiwa na kunyenyekewa,
Muweza wa kuwahiliki akitaka.
49. Ni kwa Mwenyezi Mungu pekee - wala si kwa
mwenginewe - hunyenyekea na kut'ii vyote alivyo viumba mbinguni na viumbe
viliomo na vyendavyo katika ardhi. Na mbele yao ni Malaika wanao nyenyekea wala
hawatakabari na kumt'ii.
Aya hii imeitangulia sayansi kwa kusema kuwa
katika baadhi ya sayari upo uhai katika mfumo huu wetu wa jua, au nje yake.
Sayansi sasa inajaribu kutaka kuvumbua hayo.
50. Na hali yao ni kuwa daima wamo katika
kumkhofu Mola wao Mlezi, Mwenye uwezo na nguvu, na wanafanya anayo waamrisha.
51. Mwenyezi Mungu amesema: Msiabudu wawili,
wala msifanye miungu wawili. Kwani kushiriki katika ibada kunapingana na
Umoja wa kuumba. Wa kuabudiwa kwa Haki ni Mungu Mmoja tu. Basi niogopeni Mimi
wala msimkhofu mwengine.
52. Yeye pekee ndiye mwenye vyote viliomo
mbinguni na katika ardhi, kwa kuviumba na kuvimiliki na kumuabudu. Basi ni haki
yake Yeye tu pekee kuabudiwa na kuhimidiwa na kunyenyekewa, na kutarajiwa rehema
yake, na kuogopwa adhabu yake.
53. Na neema yoyote ikikujieni, basi inatoka kwa
Mwenyezi Mungu peke yake. Kisha kikikupateni chochote cha kukudhuruni
msiyayatike kwa ukomo wa kelele zenu kwa mwenginewe yeyote isipo kuwa Yeye.
54. Kisha akiitikia maombi yenu na
akakuondoleeni madhara baadhi yenu huisahau Haki ya Mwenyezi Mungu ya Umoja wake
na kumsafia ibada Yeye tu, wakamshirikisha Muumba wao na Mlezi wao, na
wakawaabudu naye wenginewe.
55. Hayo hutokea ili mwisho wao huwa kuikanya
fadhila yetu kwa yale tuliyo wapa. Basi enyi makafiri! Stareheni na hayo msiyo
yatolea Haki ya shukrani. Mtakuja kuujua mwisho wa ukafiri!
56. Na washirikina huyapa masanamu yao, ambayo
wanayaita kwa ujinga wao kuwa ni miungu, sehemu ya kujikaribisha kwayo kutokana
na zile riziki tulizo wapa Sisi, katika makulima na mifugo na vyenginevyo.
Nakuulizeni, kwa Utukufu wangu, enyi washirikina, hayo mliyo khitalifiana kwayo
katika uwongo wenu na upotovu mlio uzua. Na Mimi nitakulipeni kwayo.
57. Na hujaalia kumpa Mwenyezi Mungu yale
wayachukiayo wao, kwa kudai kuwa Malaika ni watoto wake wa kike, na wao
wanawaabudu. Mwenyezi Mungu apishe mbali na hayo! Na wao ati wanajipa
wayapendayo nayo ni watoto wanaume.
58. Na akiambiwa mmoja wao kwamba amepata mtoto
wa kike, uso wake unasawijika kwa huzuni, naye amejaa hasira na amekasirika.
59. Anajaribu kujificha watu wasiione huzuni ya
machungu yaliyo mpata kwa kupewa khabari ya binti aliye zaliwa. Anatapatapa:
amwache hai juu ya fedheha anayo iona, kama anavyo jigamba? Au amzike katika
udongo naye yuhai mpaka afe? Ewe msikilizaji! Zingatia uwovu wa vitendo vya watu
hawa! Na uovu gani wa kumhukumia Mwenyezi Mungu mabinti ambao wao wanawachukia!
60. Ni hali mbaya ya wasio amini Akhera na yote
yaliyoko huko ya thawabu na adhabu, nayo ni ile haja ya kutaka watoto wa kiume
na kuchukia watoto wa kike. Na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu. Yeye ni Mkwasi,
hahitajii kitu, wala hana haja ya mtoto. Naye ni Mwenye kushinda, Mwenye nguvu,
wala hana haja ya msaidizi.
61. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli fanya
haraka kuwaadhibu watu kwa dhulma zao wanazo zifanya, basi asingeli mwacha hata
mnyama mmoja juu ya ardhi. Lakini Yeye kwa upole wake na hikima yake
anawaakhirisha madhaalimu mpaka wakati aliyo uweka, nao ndio wakati utapo kwisha
muda wao. Ukija wakati huo hawato taakhari hata kidogo, wala hawato tangulia.
62. Na washirikina wanamnasibisha Mwenyezi Mungu
mabinti na ushirika mambo ambayo wao wanayachukia. Na ndimi zao zinatamka uwongo
wanapo dai ya kwamba, kama walivyo kuwa na utajiri na utawala duniani, basi
kadhaalika Akhera nao watapata malipo mema kwa Mwenyezi Mungu watapo fufuliwa;
nayo ni Pepo! Hapana shaka hao watatiwa Motoni, nao watasukumwa huko kabla ya
wengineo.
63. Ewe Nabii! Jua kwa yakini kwamba Sisi
tuliwatuma Mitume kabla yako kwa kaumu nyingi kama tulivyo kutuma wewe kwa watu
wote. Lakini Shetani aliwapambia ukafiri, na ushirikina, na maasi. Basi
wakawakanya Mitume wao, na wakawaasi, na wakamsadiki Shetani na wakamt'ii yeye.
Basi yeye amekuwa ndiye mwenye kuyatawala mambo yao katika dunia, akiwapambia
mambo ya kuwadhuru. Na Akhera watapata adhabu yenye machungu makali.
64. Na hatukukuteremshia wewe hii Qur'ani isipo
kuwa upate kuwabainishia watu haki katika yale waliokhitalifiana kwayo katika
dini, na ili ipate kuwa ni uwongofu ulio timia na rehema ilio enea kwa kaumu
yenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Kitabu alicho kiteremsha.
65. Na Mwenyezi Mungu ameteremsha kutoka
mbinguni maji yanayo bebwa na mawingu, akaifanya ardhi ikamea na ikawa na uhai,
baada ya kuwa kabla yake kavu haina uhai. Hakika katika hayo pana dalili wazi ya
kuwepo Mwenye kudabiri Mwenye hikima.
Maji huteremka kutoka mbinguni
kuangukia ardhini, na huko huyayusha chumvi chumvi zake za namna mbali
mbali ambazo hunyonywa na mimea kugeuka kwenye uhai.
66. Na enyi watu! Hakika katika nyama hoa, yaani
mifugo, ngamia, ng'ombe, na kondoo na mbuzi, mna mawaidha yanayo faa kuzingatiwa
na kufuatwa uwongofu wake wa kumtoa mtu ujingani akaingia kumjua Mwenye kuumba,
Aliye anzisha kila kitu, Mwenye hikima. Na Sisi tunakunywesheni kutokana na
baadhi ya viliomo matumboni mwa hao wanyama vilio zidi katika chakula na damu
maziwa safi, matamu, mepesi kuyapata kwa wanao kunywa.
Katika viwele vya
wanyama wa mifugo imo namna ya mitoki (glands) ambayo inachuja maziwa. Mitoki
hiyo inanyweshwa na mishipa inayo leta madda maalumu kutokana na damu, na
(chyle); hicho ni chakula kilicho tayarishwa. Viwili hivyo huwa vimekwisha
lainishwa kwa kumezwa kama ni chakula. Kisha hapo hizo glands za maziwa huteuwa
sehemu yenye kuhitajiwa kwa kufanya maziwa kutokana na vitu viwili hivyo, damu
na chyle, na humiminiwa maji maalumu kugeuza hivyo vikawa maziwa yenye
kukhitalifiana na asili yake kwa rangi na utamu kabisa.
67. Na kutokana na matunda ya mitende na
mizabibu tuliyo kuneemesheni kwayo na tukakuwezesheni kuitumia, mnakamua maji
yake yakatoka ulevi usio kuwa mzuri, na chakula kilicho kuwa kizuri. Hakika
katika haya pana alama yenye kuonyesha uwezo na rehema kwa watu wanao nafiika
kwa akili zao. (Kitu kile kile kina faida kikitumiwa kwa sharia za Mwenyezi
Mungu za maumbile, na kile kile kikawa na madhara kikitumiwa kinyume na hizo
sharia.)
68. Ewe Nabii! Zingatia jinsi Mwenyezi Mungu
alivyo mfahamisha nyuki, kama kwamba amemfunulia kwa Wahyi, akamwonyesha sababu
za uhai wake, na njia za maisha yake. Akamfunza ajenge masega yake katika
mapango, na katika uwazi wa miti, na kwenye maburuji ya majumba na mizabibu.
69. Kisha Subhanahu akamhidi Nyuki ale matunda
ya miti na mimea mbali mbali, na akamsahilishia afuate njia alizo mtengezea Mola
wake Mlezi, na akatoa kutokana na matumbo yake kinywaji, nacho ni asali, chenye
rangi mbali mbali. Na hiyo asali imekuwa ni dawa ya kuwaponyesha watu. Hakika
katika hayo pana ufundi wa ajabu wa kuonyesha nguvu, na kuwepo Mwenye kuumba, na
Mwenye kuweza, Mwenye hikima. Wenye kutumia akili zao wananufaika kwa mazingatio
hayo, na watapata furaha ya daima.
Asali ya nyuki ni mchanganyiko
wa glucose na livulose, nayo ni namna ya sukari ambayo ni nyepesi kabisa
kutumika mwilini, na madaktari wamevumbua karibu kuwa glucose ina faida kutibu
maradhi mengi, kwa kupiga sindano, na kwa mdomo na kwa nyuma, kwa kuwa inatia
nguvu, na inapinga sumu ya maadeni kadhaa wa kadhaa, na sumu inayo patikana kwa
maradhi ya viungo, kama kuingia sumu kwa mkojo na maradhi ya kuwa manjano
jaundice na mengineyo. Vile vile imethibiti kuwa Vitamin nyingi hupatikana humo,
na khasa Vitamin B complex.
70. Mwenyezi Mungu amekuumbeni, na amekujaalieni
kila mtu na ajali yake. Kati yenu wapo wanao kufa mapema, na wengine wanao fikia
ukongwe wakarejea katika hali ya udhaifu. Wakawa wanadhoofika kidogo kidogo,
zikipungua nguvu zao za mwili, na mifupa na viungo na mishipa. Mwisho wao wakawa
hawajiwezi kujifanyia lolote liwapasalo! Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa
siri za kuumba kwake, ni Muweza wa kutimiza alitakalo.
71. Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi
yenu kwa riziki kuliko wengineo. Amemruzuku bwana mwenye kumiliki kuliko mtumwa
mamluki. Wala walio ruzukiwa kingi hawawapi watumwa wao hata nusu ya riziki yao,
ili wapate kuwa wote na riziki sawa! Basi ikiwa hawa makafiri hawakubali watumwa
wao washirikiane nao katika riziki iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu, nao wote ni
wanaadamu kama wao, basi vipi wao wanataka kumshirikisha Mwenyezi Mungu na
viumbe vyake katika mambo yasio kuwa laiki naye Subhanahu wa Taa'la, nako ni
kustahiki kuabudiwa? Basi je, macho ya hao washirikina yataendelea kufumbika
baada ya yote haya, wakabaki wakipinga neema za Mwenyezi Mungu juu yao kwa
kumshirikisha Yeye na wengineo?
72. Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake wa jinsi
yenu mtulie nao. Tena amekupeni, kutoka kwa wake zenu, wana na wajukuu, na
akakuruzukuni vitu vya kufurahisha nafsi zenu alivyo kuhalalishieni. Je, baada
ya haya ndio baadhi ya watu humshirikisha Mwenyezi Mungu, na wakaamini upotovu,
na wakazipinga neema za Mwenyezi Mungu zinazo onekana, ambazo zinastahiki
shukrani kutoka kwao, na kumsafia ibada Mwenyezi Mungu?
Ndoa ni
mfungamano mtakatifu ambao ndio asili ya ukoo na kiini cha umma na jamii. Na
ndoa ni mpango wa kuidhibiti ile khulka waliyo nayo wanaadamu na wanyama, nayo
ni kutamani kuingiliana. Lau ingeli kuwa hapana ndoa iliyo kadiriwa kudhibiti
ile khulka ya kutamaniana basi binaadamu wangeli kuwa sawa na wanyama kwa
kufuata fujo na uchafu wa kuingiliana. Na hapo mwanaadamu asingeli kuwa yule
kiumbe aliye mjaalia Mwenyezi Mungu kuwa na akili na fikra na akamtukuza kuliko
viumbe vyengine, na akamrithisha mamlaka ya ardhi. Ilivyo kuwa mpango wa
Mwenyezi Mungu katika uhai huu ni kutengeneza khulka kwa ndoa ili binaadamu awe
juu kuliko wanyama wengine, hali kadhaalika binaadamu kwa upande mwengine
ameumbiwa kupenda kubakia. Na ilivyo kuwa hapana njia ya kubakia yeye mwenyewe,
naye anayajua hayo kutokana na baba zake na babu zake na vitu vyote vilio hai,
basi njia pekee ni yeye kuzaa dhuriya wapate kuishi na kuendelea daima.
Na labda lenye kuweka wazi kabisa ile khulka yake ni kauli ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu: "Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na
akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizri
vizuri."
73. Na wakawa badala ya Mwenyezi Mungu wakaabudu
masanamu ambayo hayawezi kuwapa riziki yoyote hata chembe, sawa sawa ikiwa
riziki hiyo inatoka mbinguni kama maji, au kutokana na ardhi kama matunda ya
miti na mimea. Na miungu hiyo haiwezi kufanya lolote kama hayo, wala duni ya
hayo!
74. Na ilivyo kuthibitikieni kuwa asiye kuwa
Mwenyezi Mungu hakufaeni kitu, basi msiseme kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu
ana yeyote wa kumshabihi, ikawa kisingizio cha kuwaabudu hao kwa vipimo
vipotovu, na kushabihisha kusio kweli kwa ajili ya kuwaabudu hao pamoja naye!
Hakika Mwenyezi Mungu anajua upotovu wa mnayo yatenda, naye atakulipeni kwayo na
hali nyinyi mmo katika mghafala hamjui ubaya wa mwisho wenu!
75. Mwenyezi Mungu amepiga mfano kufahamisha
ufisadi walio nao washirikina. Mtumwa aliye milikiwa kama mtumwa mamluki,
hanalo aliwezalo kulitenda; na muungwana anaye ruzukiwa na Mwenyezi Mungu
riziki ya halali, naye anatoa katika hiyo riziki kwa siri na dhaahiri! Je, ni
sawa watumwa wasio weza kitu, na waungwana wenye nacho na wanatumia walicho
nacho? Hakika Mwenyezi Mungu anamiliki kila kitu, na anafanya katika ufalme wake
kama apendavyo. Na asiye kuwa Yeye hamiliki chochote. Basi huyo hastahiki
kuabudiwa na kuhimidiwa. Sifa zote ni haki ya Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye
ndiye Mwenye Utukufu peke yake, kwani kila kheri inatoka kwake, na kila zuri
linarejea kwake. Wala hawatendi hao wanayo yatenda kwa kujua, bali wanatenda kwa
kuwafuata wakubwa zao. Bali wengi wao hawajui, na wanaziambatisha neema za
Mwenyezi Mungu kwa wengineo, na wanawaabudu hao badala yake!
76. Mwenyezi Mungu amekupigieni mfano mwengine,
wa watu wawili. Mmoja wao kiziwi-bubu; hafahamu wala hafahamiki, mzigo kwa aliye
mlazimu kumtazama. Bwana wake akimuelekeza kokote harejei na faida yoyote. Basi,
je, mtu huyu atakuwa sawa na mtu mwenginewe aliye fasihi wa kusema, anasikia
vyema, anaamrisha haki na uadilifu, naye mwenyewe ameshika Njia iliyo kaa sawa,
isiyo kwenda upogo? Huyo kiziwi asiye sikia wala kusema wala hafahamu wala
hafahamiki, ndio mfano wa masanamu wanayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu.
Kwani hayo hayasikii wala hayasemi wala hayafai kitu. Hayawezi hayo kulingana na
Mwenye kusikia, Mwenye kujua, Mwenye kuwaita watu wende kwenye kheri na haki, na
kwenye Njia Iliyo Nyooka.
77. Na ni ya Mwenyezi Mungu tu peke yake yote
wasiyo yajua waja katika mbingu na katika ardhi. Wala jambo la kuja Siku ya
Kiyama, na kufufuliwa watu, haraka yake na upesi wake kwa Mwenyezi Mungu,
si chochote ila ni kama kufumba na kufumbua jicho! Bali ni duni kuliko hivyo,
jinsi ya upesi wake. Hakika uwezo wa Mwenyezi Mungu ni mkubwa mno, Yeye haemewi
na kitu.
78. Na Mwenyezi Mungu amekutoeni kutokana na
matumbo ya mama zenu hali hamjui chochote katika yaliyo kuzungukeni. Na
akakupeni kusikia na kuona na nyoyo, kuwa ndio silaha za kujifunzia na kufahamu,
ili mpate kumuamini kwa njia ya ilimu, na mumshukuru kwa alivyo kufadhilini.
Utabibu wa kisasa umethibitisha kuwa kuweza kusikia kunaanza mapema
sana katika maisha ya mtoto mchanga, mnamo wiki chache za mwanzo. Ama kuona
huanza mwezi wa tatu. Wala kuona hakuwi baraabara mpaka katika mwezi wa sita.
Ama "moyo " wa kufahamu na kutambua huwa baada ya hayo. Mpango ulio letwa na
Qur'ani ni mpango unao lingana na hisiya hizo.
79. Je! Hao washirikina hawawaangalii ndege
walio jaaliwa waweze kuruka hewani juu, kwa kupewa na Mwenyezi Mungu mbawa kubwa
kuliko miili yao, wakiikunjua na kuikunja. Na Mwenyezi Mungu akaidhalilisha hewa
kuwabeba hao ndege. Hapana anaye washika huko angani ila Mwenyezi Mungu kwa
nidhamu aliyo itengeneza Yeye Mwenyewe! Hakika katika kuwatazama hao ndege, na
kuzingatia hikima ya Mwenyezi Mungu katika kuwaumba, ni ishara kubwa ya
kuwanafiisha walio kuwa tayari kuamini.
Ndege wanaruka kwa sababu
kadhaa wa kadhaa katika kuumbwa kwao. Muhimu kuliko yote ni lile umbo lao la
kuchongoka, na kuwa mbawa zao zilivyo tanda zenye manyoya, na mafupa yenye uwazi
na myepesi na vifuko vya hewa kati ya matumbo yao, navyo vimeambatishwa na
mayavuyavu (mapafu). Hivyo vifuko hujaa hewa wakati wa kuruka, basi huzidi hao
ndege kuwa wepesi.
*
80. Na Mwenyezi Mungu
Subhanahu wa Taa'la ndiye aliye kujaalieni mkaweza kusimamisha nyumba zenu ili ziwe maskani yenu. Na
akakujaalieni kutokana na ngozi za ngamia, na ng'ombe, na kondoo na wanyama
wengineo mkafanya mahema ambayo ni kama nyumba za kukalia, na mkihama nayo mnapo
safiri na mnapo tua. Na kutokana na sufi zao, na nywele zao, na manyoya yao,
mkafanya matandiko ya kutumia hapa duniani mpaka itakapo fika ajali yenu ya
kuondoka.
81. Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni miti na vitu
vyenginevyo vya kukupeni vivuli kukulindeni na taabu ya joto, na amekufanyieni
mapango milimani, nanyi mkafanya humo maskani kama nyumba. Pia amekuumbieni nguo
za sufi na pamba na kitani na vyenginevyo, ili kukuhifadhini na joto la jua, na
nguo za chuma za kukulindeni katika vita na adui zenu. Kama alivyo kujaalieni
hayo, basi kadhaalika amekutimizieni neema zake kwa kukupeni Dini iliyo simama
sawa, ili mpate kuifuata amri yake, na mumsafie ibada Yeye tu si na mwenginewe.
82. Wakikupuuza, ewe Nabii, hao unao waita
wafuate Uislamu, basi wewe huna jukumu kwa mapuuza yao. Haikulazimu wewe ila
kufikisha ujumbe kwa uwazi, na hayo umekwisha fanya.
83. Kupuuza kwao hao makafiri si kwa kuwa
hawajui kwamba Mwenyezi Mungu Subhanahu ndiye chanzo cha kila neema zote wanazo
zipata, lakini wao hutenda vitendo vya wanao kanya neema, kwa vile hawamshukuru
Mola Mlezi kwazo. Na wengi wao wamekazania kuwafuata baba zao katika kumkataa
Mwenyezi Mungu, mpaka wakawa wengi wao ndio wapinzani.
84. Ewe Nabii! Mhadharishe kila anaye mkataa
Mola wake Mlezi kwa yatakayo tokea Siku tutakapo muinua kutokana na kila umma
shahidi wa kuwashuhudia kwa walivyo mpokea Mtume wa Mola wao Mlezi. Na pindi
akitaka kafiri kutoa udhuru, hatapewa ruhusa ya kutaka kutoa udhuru. Wala
hatapatikana mwombezi wa kumtengenezea maombezi, kwa kutakiwa warejee waache
sababu za Mwenyezi Mungu kuwakasirikia. Kwani Akhera sio pahala pa kutubia.
85. Na wale walio jidhullumu nafsi zao kwa
kukufuru watakapo iona Jahannamu, na wakataka wapunguziwe adhabu, hawato jibiwa,
wala hawato akhirishwa kuingia Jahannamu hata dakika moja.
86. Na walio wafanya miungu yao washirika wa
Mwenyezi Mungu na wakawaabudu watapo sema: Ewe Mola Mlezi wetu! Hawa ndio
washirikishwa wetu tulio tukiwaabudu kwa makosa. Basi tupunguzie adhabu
kwa kuwapa wao baadhi ya adhabu! Washirikishwa wao watajibu: Ama hakika nyinyi
washirikina waongo kwa kudai kwenu kuwa sisi ni washirika wa Mwenyezi Mungu, na
kwamba nyinyi mkituabudu! La kweli ni kuwa mkiabudu matamanio yenu tu, wala sisi
hatukuwa washirika kama mlivyo dai. (Nabii Isa a.s. amesema: "Ndipo nitawaambia
dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe, ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu." - Injili
ya Mathayo 7.21-27)
87. Hapo tena wale washirikina walio mshirikisha
Mwenyezi Mungu watasalimu amri, waikubali hukumu yake, na yawaondokee yale
mawazo yao kwamba walio kuwa wakiwaabudu yatakuja waombea na kuwakinga na
adhabu!
88. Walio kufuru na wakawazuia wengine kufuata
Njia ya Mwenyezi Mungu, nayo ndiyo Njia ya kheri na haki, tutawazidishia adhabu
juu ya adhabu wanayo stahiki kwa ukafiri wao, kwa walivyo kusudia kuwafisidi na
kuwapotosha waja wa Mwenyezi Mungu!
89. Ewe Nabii! Wahadharishe makafiri katika
kaumu yako kwa yatakayo wapata Siku tutapo watolea kila umma shahidi wa
kuwashuhudia, naye ndiye Nabii wao, ambaye atakuwa ni mmoja wao, ili wawe hawana
kisingizio. Na wewe, ewe Nabii, tutakuleta uwashuhudie hao walio kukadhibisha.
Na tangu hivi sasa yawapasa wazingatie! Sisi tumekuteremshia wewe Qur'ani,
ambayo ndani yake kila kitu kimebainishwa kwa haki. Na ndani yake umo uwongofu,
na rehema, na bishara ya Pepo kwa wenye kuifuata na kuiamini.
90. Mwenyezi Mungu anawaamrisha waja wake
uadilifu wa maneno na vitendo, na katika kila jambo wakusudie lilio bora, na
walifadhilishe kuliko jenginelo. Kama anavyo amrisha kuwapa jamaa zenu wanacho
hitajia, ili kuzidi kutia nguvu makhusiano ya mapenzi kati ya ukoo. Na Mwenyezi
Mungu anakataza kutenda kila la makosa, na khasa madhambi yaliyo pita mpaka kwa
ubaya, na kila kisicho pendeza katika sharia na akili nzuri. Hali kadhaalika
anakataza kumfanyia uadui mtu. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika anakukumbusheni
haya, na anakuelekezeni kwenye mambo mema, mpate kukumbuka fadhila zake kwa
maelekezo yake mema,basi ndio mfanye anavyo kwambieni.
91. Na timizeni ahadi mlizo jitolea nafsi zenu
kwa kumshuhudisha Mwenyezi kuwa mtazitekeleza, maadamu ahadi hizo ni kwa mujibu
wa sharia ya Mwenyezi Mungu. Wala msivunje viapo vyenu kwa kutotimiza baada ya
kuvitilia nguvu kwa kumtaja Mwenyezi Mungu, na kuazimia kikweli kutimiza. Nanyi
mlipo toa ahadi mlitia maanani kuwa Mwenyezi Mungu ndiye dhamini wenu kwamba
mtatekeleza, na kwamba Mwenyezi Mungu anakuangalieni na kukuoneni. Basi
shikamaneni na ahadi zenu na viapo vyenu, kwani Mwenyezi Mungu Subhanahu
anakujueni yupi katika nyinyi anaye timiza na anaye kwenda kinyume, yupi anaye
tekeleza na yupi anaye vunja. Basi atakulipeni kwa mnayo yafanya.
92. Wala msiwe katika kwenda kinyume na viapo
vyenu baada ya kuvithibitisha mfano wa mwanamke mwendawazimu anaye sokoto sufi,
ikisha kuwa nyuzi akazifumua tena. Mkafanya viapo vyenu kuwa ni njia ya
kudanganya na kukhadaa watu, na huku mkijitafutia udhuru kwa kuwa ama nyinyi ni
wengi zaidi au mna nguvu zaidi kuliko wao, au mnakusudia kuwaunga mkono maadui
wenye nguvu zaidi kuliko wao, au kwa kuwa mnataraji kuzidi nguvu kwa khiana! Na
hakika Mwenyezi Mungu anakufanyieni mtihani. Mkikhiari kutimiza ahadi mtapata
mavuno ya duniani na Akhera. Mkielekea khiana, basi ni khasara yenu. Na hakika
Siku ya Kiyama atakubainishieni ukweli wa khitilafu zenu za duniani, na
atakulipeni kwa mujibu wa vitendo vyenu.
Aya mbili hizi zinaonyesha
kuwa msingi wa makhusiano baina ya Waislamu na wengineo pamoja na uadilifu ni
kutimiza ahadi, na kwamba makhusiano baina ya mataifa hayasimami sawa ila kwa
kutimiza ahadi, na kwamba dola za Kiislamu zikijifunga kwa mapatano basi
zijifunge kwa jina la Mwenyezi Mungu. Maana ya hayo ni kuwa inakuwapo yamini ya
Mwenyezi Mungu na kuwa Yeye ndiye dhamini. Na Aya inafahamisha mambo matatu,
ambayo lau kuwa mataifa yangeli yatimiza basi amani ingeli enea:
* Kwanza: Haifai mapatano kuwa ndio njia ya kufanya khadaa. Ikiwa hivyo
inakuwa ni udanganyifu. Na udanganyifu haufai katika makhusiano baina ya
wanaadamu, sawa sawa ikiwa baina ya mtu na mtu, au kikundi na kikundi, au baina
ya madola.
* Pili: Kutimiza ahadi peke yake ni nguvu. Na mwenye
kuvunja ahadi ni kama mwenye kuvunja alicho kijenga kwa sababu za nguvu. Basi
anakuwa kama mpumbavu anaye tatua uzi wake kila akisha usokota.
*
Tatu: Haimfalii mtu kuvunja ahadi kwa sababu ya kutafuta nguvu au kutaka
kuzidisha kipande cha ardhi.
93. Mwenyezi Mungu ange taka angeli kufanyeni
nyote umma wa namna moja kwa jinsi, na rangi, na imani, bila ya khitilafu. Na
hayo ni kwa kukupeni umbo jengine, mkawa kama Malaika wasio na uwezo wa kukhiari
watakalo. Lakini ametaka muwe jinsi na rangi mbali mbali, na akakupeni uwezo wa
kukhiari wenyewe. Mwenye kukhiari matamanio ya dunia kuliko kumridhi Mwenyezi
Mungu, anaachwa kwa ayatakayo. Na mwenye kutaka kumridhi Mwenyezi Mungu kwa
vitendo vyema, anasahilishiwa kwa anayo yataka. Na kuweni na yakini kuwa nyote
nyinyi mtakuja ulizwa Siku ya Kiyama juu ya mliyo yatenda duniani, na mtalipwa
kwa vitendo vyenu.
94. Wala msishike njia ya khiana, mkafanya viapo
ndio njia ya udanganyifu na khadaa. Kwa hivyo nyayo zenu zitateleza mlikosee
lengo lilio sawa, na kwa hivyo ikapelekea mkaiwacha Njia ya Mwenyezi Mungu ya
kutimiza ahadi, na mkawa ni mfano muovu wa khiana, na watu wakaja waona kuwa
Waislamu ni watu wabaya, na wakautupilia mbali Uislamu wenyewe. Na uovu
ukateremka duniani kwa sababu yenu kwa kuto kuaminini kwa vile mnavyo kwenda
kinyume na njia ya haki, nanyi ikakuteremkieni adhabu kali yenye kutia machungu.
95. Wala msibadilishe ahadi ya kweli kweli kwa
kutaka pato la dunia, na hilo ni duni na lingali onekana kubwa. Maana yaliopo
kwa Mwenyezi Mungu, malipo ya wanao hifadhi ahadi zao duniani, na malipo ya
Akhera ya milele, ni bora kwenu kuliko yote yanayo kudanganyeni kwa kuvunja
ahadi. Basi zingatieni na mfahamu, ikiwa nyinyi ni watu wa ilimu na utambuzi
baina ya jema na lisio kuwa jema. Wala msitende ila lilio na maslaha kwenu
duniani na Akhera.
96. Kwani neema mlizo nazo zina mwisho hata
zingeli kaa muda mrefu. Na neema zilioko kwa Mwenyezi Mungu Akhera ni za milele
wala hazishi. Na Sisi tutawalipa wenye kuvumilia mashaka ya taabu kwa ajili ya
tuliyo waahidi, nayo ni kupata bora ya malipo marudufu kwa vitendo vyao,
waneemeke kwayo daima milele Akhera.
97. Hakika mwenye kutenda mema duniani, sawa
sawa akiwa mwanamume au mwanamke, akajiingiza katika huo wema kwa nguvu za
imani, kwa kila linalo wajibika kwa kuliamini, basi Sisi hatuna budi kumfanya
aishi maisha mazuri yasiyo kuwa na machungu, yenye ndani yake ukinaifu na
kuridhika na kuvumilia masaibu ya dunia, na shukrani kwa neema anazo zipata kwa
Mwenyezi Mungu. Na Akhera hapana budi ya kuwa tutawalipa watu wa namna hii bora
ya malipo kwa kuzidi marudufu kwa vitendo vyao vya duniani.
98. Kinacho linda nafsi isighurike na pumbao ni
Qur'ani. Ewe Muumini! Ukitaka kuishi maisha ya mbali na kuchezewa na Shetani, na
upate wema wa kote kuwili, duniani na Akhera, basi Mimi nakuongoza kwenye
jambo litakalo kusaidia kwa hayo. Jambo lenyewe ni kuisoma Qur'ani. Na
unapo taka kusoma Qur'ani, anzia kwa kumuomba Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi
akuepushe na wasiwasi wa Shetani, aliye fukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu,
na anaona uzuri kuwaghuri watu awaingize katika kumuasi Mwenyezi Mungu.
99. Ukifanya haya kwa kumsafia niya Mwenyezi
Mungu, basi atakulinda na Shetani, na atakuondolea wasiwasi. Kwani Shetani hana
athari kwa walio jaa Imani ya Mwenyezi Mungu, na wakamtaka msaada na kumtegemea
Yeye peke yake.
100. Bali taathira yake Shetani na khatari yake
ni juu ya wale ambao nyoyo zao hazina mfungamano wala mapenzi na Mwenyezi Mungu.
Basi hao hawana la kuwalinda na athari za Shetani. Watamfuata huyo kama rafiki
anavyo mfuata rafiki yake, mpaka watumbukie katika kumshirikisha Mwenyezi Mungu
katika kumuabudu pamoja na miungu mingine isiyo weza kuleta madhara wala
manufaa.
101. Na tukikuletea muujiza badala ya muujiza
ulio sawa na tulio waletea Manabii walio tangulia, na tukakuletea wewe hii
Qur'ani kuwa ni muujiza wenyewe, wanakusingizia kuwa umeizua tu hii, na kwamba
unamzulia Mwenyezi Mungu uwongo! Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mjuzi kwa
ujuzi usio pikuliwa kuijua miujiza anayo wateremshia Manabii wake. Lakini wengi
wao watu hawa si watu wa ilimu wa kujua lilio kweli.
102. Ewe Nabii! Waambie kuwabainishia muujiza
wako: Hakika hii Qur'ani kaniteremshia mimi Jibril, Roho safi, kutokana kwa Mola
wangu Mlezi, kwa kufuatana na kukusanya Haki, ili kwayo azitie imara nyoyo za
Waumini, na ili iwe ni Uwongofu kwa watu wote waongokewe, na iwape bishara njema
ya neema Waislamu wote.
103. Hakika Sisi tunajua wayasemayo makafiri wa
Makka, nayo: Hamfundishi Muhammad hii Qur'ani ila mtu tunaye mjua, naye ni
kijana wa Kirumi. Wala hamteremshii Malaika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama
asemavyo! Na kauli yao hii ni ya uwongo. Kwani huyo kijana wanaye sema kuwa
anakufundisha wewe ni mgeni, hajui Kiarabu vizuri. Na Qur'ani ni lugha ya
Kiarabu kilicho wazi cha ufasihi, hata imekuwa nyinyi wabishi mmeshindwa kuleta
mfano wake. Basi hizo tuhuma zenu zina maana gani?
104. Hakika hao wasio zikubali Ishara za
Mwenyezi Mungu ambazo wameshindwa kuleta mfano wake, na wakashikilia kuzikataa
juu ya kuemewa kwao, Mwenyezi Mungu hawaongoi. Nao Akhera watapata adhabu kali
kwa sababu ya ukafiri wao na inadi yao!
105. Hakika wanao jasirisha kumzulia Mwenyezi
Mungu uwongo ni wale wasio ziamini Ishara za Mwenyezi Mungu, na hao peke yao
ndio walio fikilia ukomo wa uwongo. Na wewe, Nabii, si katika watu hao hata wa
kutuhumie hivyo.
106. Hao wanao tamka ukafiri baada ya kuamini
watapata ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Isipo kuwa aliye lazimishwa kutamka maneno
ya ukafiri na hali moyo wake umesimama imara katika Imani. Huyo atavuka,
haitompata ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Ama ambao nyoyo zao zinafurahia ukafiri,
na ndimi zao zinakubaliana na yaliyo nyoyoni mwao, hao watapata ghadhabu
kali kwa Mwenyezi Mungu ambaye amewaandalia adhabu kubwa katika Akhera.
107. Na hiyo ghadhabu na adhabu waliyo stahiki
kuipata, ni kwa sababu ya kupenda kwao mno neema za duniani na starehe zake za
kupita njia, hata zikawaweka mbali na Haki, na zikawatia upofu wasiione kheri.
Basi Mwenyezi Mungu akawaachilia mbali na huo ukafiri wanao upenda. Huo ndio
mwendo wake anavyo watendea viumbe vyake, huwaacha kama hawa, na huwaacha
asiwahidi kwa sababu ya ufisadi wao wenyewe, na kukakamia katika upotovu.
108. Hao ndio Mwenyezi Mungu amewapiga
muhuri wa mghafala katika nyoyo zao, hata zikawa haziikubali Haki, na katika
masikio yao wakawa hawasikii kwa sikio la fahamu na mazingatio wakawa kama
viziwi, na katika macho yao hata wakawa hawaoni ishara na dalili zilio mbele
yao. Hao ndio walio zama katika kughafilika na Haki. Hao hawana kheri mpaka
uondoke mghafala katika akili zao.
109. Hao hapana shaka yoyote ndio peke yao
watakao khasiri kila kheri katika Akhera!
110. Tena, ewe Nabii! Jua kuwa Mola wako Mlezi
ni Mwenye kuwasaidia na kuwanusuru walio hama Makka kukimbiza Dini yao
isikandamizwe, na nafsi zao zisiadhibiwe na washirikina. Kisha wakapigana Jihadi
kwa kadiri ya uwezo wao, kwa maneno na vitendo, wakavumilia mashaka na taabu, na
yaliyo wakuta kwa ajili ya Dini yao. Hakika Mola wako Mlezi baada ya hayo waliyo
yastahamilia ni Mwenye kuwasamehe wakitubu, Mwenye kuwarehemu, basi hato
wachukulia kwa walio lazimishwa kuyafanya.
111. Ewe Nabii! Watajie watu wako, kwa
kuwahadharisha, Siku ambayo kila mtu atakuwa hana linalo mshughulisha ila
kujitetea nafsi yake. Hayamshughulishi ya mzazi wala mwana. Siku hiyo ndiyo Siku
ya Kiyama! Na Mwenyezi Mungu siku hiyo atailipa kila nafsi malipo ya vitendo
iliyo tenda, ikiwa kheri au shari. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu hata mtu mmoja.
112. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu amewapigia
mfano watu wa Makka kisa cha mji mmojapo. Watu wake walikuwa wamekaa kwa amani,
hawana adui anaye waingilia. Wametua, hawana dhiki ya maisha, riziki inawajia
kwa wasaa kutoka kila pahali. Wakazibeua neema za Mwenyezi Mungu, wasimshukuru
kwa kumt'ii na kutekeleza amri zake. Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa masaibu
yaliyo wazunguka kila upande. Wakaonja uchungu wa njaa na vitisho, baada ya
utajiri na amani walio kuwa nayo. Na hayo kwa sababu ya kukakamia kwao katika
ukafiri na maasi.
113. Nao alikwisha wajia Mtume kutokana nao
wenyewe. Ilikuwa ni waajibu wao wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hayo, lakini
walimwambia mwongo, kwa inda na husda tu. Adhabu ikawatwaa nao hali wamo katika
udhalimu, na kwa sababu ya hiyo dhulma.
114. Ikiwa washirikina wanazikufuru neema za
Mwenyezi Mungu na wanazigeuza kuwa ni nakama, basi nyinyi Waumini elekeeni
kwenye shukra. Na kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu na
akakufanyieni kuwa ni vizuri kwenu, wala msijiharimishie nafsi zenu. Na
ishukuruni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu kwa kumt'ii Yeye tu peke yake,
ikiwa kweli mnamkusudia Yeye tu kwa ibada.
115. Kwani hakika Mwenyezi Mungu
hakukuharimishieni isipo kuwa nyamafu, na damu inayo tiririka kutokana na mnyama
wakati wa kumchinja, na nyama ya nguruwe, na kilicho chinjwa kwa asiye kuwa
Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kulazimishwa na shida ya njaa kula kitu
alicho kuharimishieni Mwenyezi Mungu, bila ya kutaka, na wala bila ya kupita
hadi ya kiasi cha kuondoa ile dharura, basi hakika Mwenyezi Mungu hayachukulii
hayo. Kwani Yeye Subhanahu ni Mwenye kuwasamehe waja wake. Huwasamehe wanapo
tumbukia katika makosa wasio endelea nayo. Naye ni Mwenye kuwarehemu kwa vile
anawazuia vitu vinavyo wadhuru, na anawaruhusu kwa kuhifadhi uhai wao.
116. Na ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu amekwisha
kubainishieni kilicho halali na kilicho haramu, basi shikamaneni na hayo aliyo
kubainishieni, wala msithubutu kuhalalisha na kuharimisha ovyo kufuata ndimi
zenu. Mkawa mnasema: Hichi halali, na hichi haramu. Matokeo ya hizo kauli zenu
ni kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na kumkhusisha na asiyo yasema! Hakika wanao
mzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawapati kheri wala mafanikio.
117. Wakiendelea kufuata matamanio yao ya
kidunia, basi hakika starehe yao hiyo ni chache na haina dawamu, na Akhera
watapata adhabu kali.
118. Wala hawakuharimishiwa ila Mayahudi tu
vile vitu tulivyo kusimulia, ewe Nabii, kabla ya kuteremka Aya hizi. Na vitu
hivyo ni kuwa kila mnyama mwenye makucha, na shahamu za ng'ombe na kondoo, ila
ilio beba migongo yao au matumbo, au iliyo changanyika na mifupa. Na Sisi
hatukuwadhulumu kwa kuwaharimishia hayo, lakini wamejidhulumu wenyewe
kuyasabibisha hayo kwa kupita mipaka na ushari wao, na kuacha kusimama kwenye
yalio halali...
119. Kisha wanao tenda maovu kwa kupitikiwa, au
kwa kuacha kuzingatia vilivyo matokeo yatayo tokea, na baadae wakatubia,
wakajitengeneza nafsi zao na vitendo vyao, basi hakika Mola wako Mlezi, ewe
Nabii, atawasamehe hao madhambi yao. Kwani hakika Yeye Subhanahu baada ya toba
hiyo ni Mwingi wa kusamehe madhambi, na ni Mkunjufu wa rehema kwa waja wake.
120. Hakika Ibrahim, mnaye tafakhari naye
nyinyi washirikina na Mayahudi, alikuwa amekusanya kila fadhila njema, na yu
mbali na upotovu wenu, ni mt'iifu wa amri ya Mola wake Mlezi, na wala hakuwa
mshirikina kama nyinyi.
121. Alikuwa mwenye kushukuru kwa neema za Mola
wake Mlezi. Na kwa haya yote ndio Mwenyezi Mungu alimteua ili abebe Ujumbe wake,
na akamwezesha kufuata Njia ya Haki Iliyo Nyooka yenye kufikilia kwenye neema ya
kudumu.
122. Na tumemjaalia duniani atajike vyema, na
hakika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema wanao neemeshwa kwa Pepo za Allah
na radhi zake.
123. Ewe Nabii! Baada ya Ibrahim kwa karne
nyingi, tulikupa Wahyi wewe, na tukakuamrisha umfuate Ibrahim katika wito wake
wa kulingania Tawhid, na fadhila njema, na kujiepusha na dini za uwongo. Kwani
yeye hakuwa katika wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu, kama wanavyo msingizia hawa
washirikina.
124. Wala sio kuitukuza siku ya Ijumaa na
kuiacha Jumaamosi kama ilivyo katika Uislamu kuwa ni kukhitalifiana na alivyo
kuwa akifanya Ibrahim, kama wanavyo dai Mayahudi. Kwani kuharimishwa kuvua (na
kufanya kazi nyengine) siku ya Jumaamosi, ndio Siku ya Sabato, kwa sababu ya
kuitukuza haikuwamo katika sharia ya Ibrahim. Hayo walilazimishwa Mayahudi tu
(ambao hata hawakuwapo zama za Ibrahim). Na juu ya hivyo hawakuitukuza, bali
baadhi yao waliacha kutukuza huko, na wakenda kinyume na amri ya Mola wao Mlezi.
Basi yawaje hata wanawatia makosani wengine kwa kutolazimishwa kutukuza jambo
ambalo wao walio lazimishwa wameliasi? Ewe Nabii! Kuwa na yakini kuwa Mola wako
Mlezi atawahukumu hao Siku ya Kiyama katika hayo mambo wanayo khitalifiana
kwayo, na atamlipa kila mmoja wao kwa vitendo vyake.
125. Ewe Nabii! Lingania, uwite watu kwenye
Njia ya Haki ambayo Mola wako Mlezi amewataka watu wako waifuate. Na katika huo
Wito wako pita njia ambayo inamnasibu kila mmoja wao. Waite wenye vyeo vya juu
katika wao kwa maneno ya hikima kwa mujibu wa akili zao. Na watu wa kawaida
walio baki kati yao walinganie kwa kuwapa mawaidha yanao waelekea, na kuwapigia
mifano ya mambo wanayo pambana nayo ya kuwapeleka kwenye Haki, na uwaongoze
kwenye njia fupi inayo wanasibu. Na jadiliana na watu wa dini zilizo tangulia
katika watu wa Biblia, yaani Mayahudi na Wakristo, kwa kutumia hoja za kiakili,
Mant'iqi, na maneno laini, na majadiliano mazuri, si maneno ya ukali na matusi,
ili uwakinaishe na uwavutie. Hii ndiyo njia ya Daa'wa (Wito), kuwaita watu
kumwendea Mwenyezi Mungu -watu wa mila zote. Basi ifuate njia hii unapo waita,
na baada ya hayo yaliyo baki mwachilie Mola wako Mlezi, ambaye anamjua aliye
zama katika upotovu kati yao na akawa mbali na njia ya uwokovu, na nani ambaye
aliye salimika, akaongoka, na akayaamini hayo uliyo waletea.
126. Enyi Waislamu! Mkitaka kuwaadhibu wale
wanao kufanyieni uadui wakakuvamieni, basi waadhibuni kwa kadiri walivyo
kutendeeni, wala msizidishe kuliko hivyo. Na kuweni na yakini kwamba
mkistahamili, msijilipizie kisasi, itakuwa ni kheri zaidi kwenu hapa duniani na
Akhera. Basi toeni adhabu kwa ajili ya Haki, wala msiadhibu kwa ajili ya nafsi
zenu.
127. Na ewe Nabii! Subiri! Kwani hivyo ndio
yatakusahilikia mengi katika mashaka ya maisha, na yataondoka matatizo yake.
Wala usisikitike kwa kuwa watu wako hawaitikii Wito wako, na hawakuamini. Wala
usione dhiki kifuani mwako kwa hila zao na vitimbi vyao vya kuukaba roho Wito
wako. Kwani vitendo vyao havitakudhuru kitu. Na wewe umekwisha tekeleza waajibu
wako, na umemcha Mola wako Mlezi.
128. Kwani hakika Mola wako Mlezi yu pamoja na
wale wanao jikinga na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kuyaepuka anayo yakataza,
na wakazifanya a'mali zao ziwe nzuri kwa sababu ya Mwenyezi Mungu kwa kukubali
kumt'ii. Yeye atawanusuru duniani, na Akhera atawalipa bora ya malipo.