1. Alif, Lam, Raa. Hizi harufi na mfano wake, zinazo fanya
maneno yenu, enyi Waarabu, ndizo hizo hizo zinazo fanya Aya za hichi Kitabu,
ambacho ni muujiza unao waemea watu kuuiga. Muujiza ulio wazi unao fafanua kwa
kila mwenye kutafuta uwongozi ndani yake, na uwongofu. Na kwa hizi harufi za
kutamkika zikasikilizana sauti yake wanazinduliwa watu watanabahi. Basi
wasikilize, ijapo kuwa waliwafikiana kuwa wasisikilize.
2. Hakika Sisi tumemteremshia Mtume wetu haya
maneno kwa lugha yenu ya Kiarabu yasomwe na yahifadhiwe, ili muyafahamu, na
muwafikishie watu wote.
3. Sisi tunakusimulia, ewe Nabii, visa vizuri
kabisa kwa kukufunulia Kitabu hichi. Na kabla ya haya ulikuwa umeghafilika nayo,
huyajui, haya, wala mawaidha yaliomo ndani yake, na Aya zake zilizo wazi.
4. Katika visa hivi, ewe Nabii, kipo hichi kisa
cha Yusuf, (1) pale alipo mwambia baba yake: Ewe babaangu! Hakika mimi nimeona
usingizini nyota hidaa'shara, na jua, na mwezi. Nimeona vyote hivyo
vikininyenyekea, vikisujudu mbele yangu.
(1) Yusuf, Alayhi Ssalam,
alikuwa mwana wa Yaaqub, Muabrani, Mkanaani. Akauzwa Misri katika enzi ya
utawala wa wavamizi wa kigeni waitwao Wahiksos. Na kwa ionekanavyo hao Wahiksos
ni katika kabila za Kisami walio ingia Misri kutoka Sham wakaiteka Delta ya
Misri mnamo mwaka 1730 k.k. ( kabla ya Nabii Isa a.s.) na kabla ya kumalizika
enzi ya ukoo wa kumi na tatu wa Mafirauni. Wakaihukumu Misri kwa muda wa karne
unusu. Wakafukuzwa mnamo mwaka 1580 k.k. na Ahmas wa Mwanzo aliye anzisha ukoo
wa 18. Wakatolewa nje ya mipaka ya Misri.
5. Baba yake akamwambia: Ewe mwanangu!
Usiwasimulie nduguzo ndoto yako hii. Itakuja watia husda katika nyoyo zao, na
Shetani atawachochea wazue njama kukupinga. Watakuja kufanyia hila na vitimbi!
Hakika Shetani ni adui wazi wa binaadamu!
6. Kama ulivyo jiona katika ndoto kuwa ni bwana
wa kut'iiwa, mwenye cheo na madaraka, basi Mola wako Mlezi atakuteuwa na
atakukhitari, akufunze kufasiri ndoto, kwa kukupa Unabii na Utume, kama hapo
zamani, kabla ya baba yako, Yaa'qub, alivyo wafanyia baba zako, Ibrahim na
Is-haq. Hakika Mola wako Mlezi ni mwingi wa hikima, basi hakosei. Ni mwingi wa
ujuzi, basi humteuwa katika waja wake anaye mjua kuwa anastahili kuteuliwa.
7. Hakika katika kisa cha Yusuf na nduguze zipo
dalili na mazingatio kwa waulizao, wenye kutaka kujua.
8. Walipo semezana nduguze Yusuf kwa baba: Bila
ya shaka Yusuf na nduguye kwa baba na mama wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko
sisi. Na sisi ni kikundi chenye nguvu, chenye kumfaa yeye zaidi kuliko wao!
Hakika baba yetu kwa kumfadhilisha Yusuf na nduguye kuliko sisi yumo makosani,
na yuko mbali na haki. Yalio sawa yapo wazi yanaonekana.
9. Muuweni Yusuf, au mtupeni nchi iliyo mbali na
baba yenu, asiyo weza kuifikia. Yatakuwafikieni nyinyi tu mapenzi ya baba yenu,
na atakuelekeeni nyinyi tu. Na baada ya kumtenga Yusuf naye kwa kumuuwa au
kumhamisha mtakuwa watu wema. Kwani Mwenyezi Mungu atakubali toba yenu, na baba
yenu atapokea udhuru wenu.
10. Mmoja wao katika wasemaji alisema: Msimuuwe
Yusuf. Hayo ni makosa makubwa. Lakini mtupeni asipo onekana ndani ya kisima,
baadhi ya wapita njia watakuja mwokota, watapo tumbukiza ndoo yao kisimani. Hao
watakwenda naye pahala pambali nanyi na baba yenu vile vile. Haya ikiwa nyinyi
mna lazima mumpeleke mbali na mtimize kwa kitendo hayo mtakayo.
11. Baada ya kuwafikiana kumbaidisha Yusuf
(kumpeleka mbali) walisema: Ewe baba yetu! Nini kinacho kutia shaka nasi hata
unamtenga Yusuf nasi, wala huoni pana usalama anapo kuwa nasi? Sisi
tunakuhakikishia kuwa sisi tunampenda, na tunamwonea huruma, na tunamtakia
kheri, na tunamwongoza kwenye kheri. Hapati kwetu isipo kuwa mahaba, na nasiha
safi kabisa.
12. Mwache ende nasi kesho machungani.
Atastarehe kwa kula vyakula vizuri, atacheza na atafurahi. Na sisi kwa yakini
tuna hima ya kumhifadhi kumkinga na madhara yoyote.
13. Mzee akasema: Hakika mimi naona huzuni
mkiondoka naye, akawa mbali nami. Na nina khofu nikikuaminini asije akaliwa na
mbwa mwitu na nyinyi mmeghafilika naye.
14. Wakasema: Tunakuapia, akiliwa na mbwa, na
hali sisi ni kundi lenye nguvu, basi itakuwa ni fedheha na khasara kwetu!
Likitokea hilo unalo liogopa basi sisi tutakuwa tumekhasiri kila linalo pasa
kulishughulikia, na kuwa lisitokee. Basi tuwa kwa hayo! Hatutadharau kumlinda,
ikiwa hivyo itakuwa tunajipelekea wenyewe kupotea na kupuuza.
15. Walipo kwenda naye mbali na baba yake,
na wakakubaliana rai yao ya kumtumbukiza ndani ya kisima, walifanya hayo waliyo
yaazimia. Sisi tukamtia moyoni mwake Yusuf atulie, na awe na imani ya Mwenyezi
Mungu, kuwa bila ya shaka atakuja waeleza haya mambo yao waliyo yapanga na
wakayatenda, na wala wao wenyewe hawajui hapo utapo waambia kwamba wewe ndiye
Yusuf waliye mfanyia vitimbi, na wakadhani wamekwisha mmaliza na wameepukana
naye!
16. Walirejea kwa baba yao usiku, wakijitia
huzuni, na kupiga makelele kwa kilio!
17. Wakasema: Ewe baba yetu! Sisi tulikwenda
kushindana kupiga mishale na kwenda mbio, na tukamwacha Yusuf kwenye vitu vyetu
avilinde. Mbwa mwitu akamla, na sisi tuko mbali tumeshughulika na mashindano! Na
wewe hutusadiki tunayo yasema, ijapokuwa tunasema haki na kweli!
18. Wakaileta kanzu yake nayo ina damu, ati kuwa
ni ushahidi wa yale madai yao ya kuwa ile ni damu ya Yusuf, apate kusadiki baba
yao! Walakini yeye alisema: Hakika huyo mbwa mwitu hakumla kama mnavyo singizia,
bali nafsi zenu zimekupelekeeni kufanya jambo kubwa, na mkalitimiza! Langu mimi
ni kusubiri subira njema isiyo legalega kwa mliyo nikutisha. Na Mwenyezi Mungu
pekee ndiye anaye takiwa msaada kwa huo upotovu mlio uzua na mnao udai.
19. Wakaja watu upande ule wa kisima katika
msafara wao wa kwendea Misri. Wakamtuma mtu kati yao wa kuchota maji kisimani
awaletee. Akatumbukiza ndoo yake, akiivuta na Yusuf kang'ang'anilia!
Yule mchota maji akapiga kelele za furaha: Kheri! Kheri gani hii na furaha! Huyu
ni kijana! Wakamficha katika vitu vyao, wakamfanya ni bidhaa ya biashara! Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyazunguka yote wayatendayo kwa ujuzi wake.
20. Wakamuuza Misri kwa bei ya chini kabisa, si
kiasi chake! Thamani yake ilikuwa ni pesa chache tu! Wala hawakuwa wakimtakia
Yusuf thamani kubwa, kwa kukhofia wasije watu wake wakamkuta wakamtambua, na
wakawapokonya Yusuf.
21. Yule aliye mnunua kule Misri
alimwambia mkewe: Mfanyie wema huyu, na umhishimu, ili makao yake hapa nasi yawe
mazuri. Huenda akatufaa, au tukamfanya kuwa ni mwenetu. Kama yalivyo kuwa
makaazi yake ni mazuri na ya hishima, basi kadhaalika tulimjaalia Yusuf katika
nchi ya Misri cheo kingine kikubwa, ili atekeleze uadilifu na mipango mizuri, na
ili tumfunze kufasiri mambo na ndoto, ajue yatakayo kuwa kabla hayajwa, ili awe
tayari kuyakabili! Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kutimiza kila jambo alitakalo.
Kabisa haemewi na kitu. Lakini watu wengi hawajui siri ya hikima yake, na undani
wa mipango yake.
22. Na Yusuf alipo timia ukomo wa nguvu zake
tukampa hukumu yenye kusibu, na ilimu yenye kufaa. Na kama malipo haya tuliyo
mpa yeye kwa wema wake, ndio tunavyo wapa wote walio wema kwa vitendo vyao
vyema.
23. Na yule bibi aliye kuwa Yusuf anakaa
nyumbani kwake, naye anamjua madaraka yake, alitaka kumghuri aache mwendo wake
ulio safi. Akawa anajipitisha pitisha mbele yake kuonyesha uzuri wake, na
kujitamanisha kwake. Hata mwishoe akamfungia milango, na akamwambia: Njoo
kwangu, nimejitoa kwako! Yusuf akasema: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu,
aniepusha na hiyo shari! Na vipi nifanye uchafu huo nawe, na mumeo mheshimiwa ni
bwana wangu aliye niweka bora ya makamo? Hakika hawafuzu wanao wadhulumu watu
kwa udanganyifu na khiana, wakajitia wenyewe katika maasi ya uzinzi!
24. Na yule bibi aliazimia aingiane naye, na
nafsi ya Yusuf ilimvutia kwake, lau kuwa hakuiona nuru ya Mwenyezi Mungu ya haki
imezagaa mbele ya macho yake. Basi hakuufuata mvutio wa nafsi, na akayashinda
matamanio, na akajizuilia maasi na khiana. Akathibiti juu ya usafi na kutakasika
kwake. Ndio hivi tulivyo mthibitisha Yusuf kwenye usafi na kutakasika, ili
tumuepushe na uovu wa khiana na maasi ya uzinzi. Hakika yeye ni miongoni mwa
waja wa Mwenyezi Mungu walio itakasa dini yao kwa Mwenyezi Mungu.
25. Yusuf akakimbilia mlangoni kutaka kutoka, na
yule bibi naye akapiga mbio amtangulie ili amzuie kutoka. Akaivuta kanzu yake
kwa nyuma ili kumzuia, akaichana. Hapo wakapambana na mume wa yule bibi
mlangoni! Yule bibi akasema kumchongea Yusuf: Hapana malipo ya mwenye kutaka
kumfanya mkeo mambo mabaya ila atiwe gerezani, au akutishwe adhabu chungu!
26. Yusuf akasema kujitetea: Ni yeye ndiye
aliyenitaka, na akajaribu kunikhadaa! Ikawa ni kusutana. Alikata hukumu mmojapo
katika jamaa zake mwenyewe yule mwanamke kwa kusema: Ikiwa kanzu yake imechanwa
mbele, basi huyu bibi kasema kweli katika madai yake, na huyu kijana ni mwongo
kwa aliyo yasema.
27. Na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma, basi
huyu mwanamke kasema uwongo, na kijana ni mkweli kwa aliyo yasema.
28. Mume alipoona kuwa kanzu ya Yusuf imechanwa
mgongoni alimwambia mkewe: Huku kumtuhumu kwako kijana kwa yaliyo tokea na hali
yeye hana makosa, ni katika vitimbi vyenu, enyi wanawake. Hakika vitimbi vyenu
ni vikuu mno!
29. Ewe Yusuf wachilia mbali mambo haya, na wewe
yafiche wala usiyaseme. Na wewe, mwanamke, omba maghfira kwa dhambi yako. Hapana
shaka kuwa wewe ni katika wenye dhambi, wenye kuyakusudia makosa, na kutenda
maasi, na kuwasingizia wengine uasi wasio ufanya!
30. Khabari zikawafikia baadhi ya wanawake wa
mjini, wakazungumza wakisema: Mke wa Mheshimiwa anamzaini mtumishi wake na
anamkhadaa amkubalie anayo yataka kwake! Ama kweli amesalitika kwa mahaba hata
hajitambui! Hakika sisi tunaamini kuwa kwa mwendo wake huu ameingia kwenye
upotovu na makosa yaliyo wazi.
31. Yule bibi alipo yasikia masengenyo yao wale
wanawake na kuwa wanamsema kwa vibaya, aliwaalika nyumbani kwake na akawapangia
matakia na mito ya kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu, baada ya kwisha
hudhuria na wakakaa wakiegemea. Akawaletea chakula na visu vya kulia. Akamwambia
Yusuf: Hebu watokee! Alipotokeza wakamwona walistaajabu. Uzuri wake ulio pita
mpaka uliwatwaa wasijitambue, wakawa wanajikata mikono yao jinsi ya kushtuka
kwao, na huku wanadhani wanakata chakula! Wakasema kwa mastaajabu na kushituka:
Hasha Lillahi! Mungu apishe mbali! Huyu tunaye mwona si binaadamu! Hapana
binaadamu mwenye uzuri namna hii, na mwenye jamali kama hivi, na usafi kama huu,
na kunyooka kama huku! Huyu ni Malaika tu, mwenye uzuri huu, na sifa hizi zilio
timia!
32. Tena mke wa Mheshimiwa alisema kufuatiliza
maneno yao: Huyu kijana ambaye uzuri wake umekuzugeni na ukakuemeeni hata
yakatokea yaliyo tokea ndiye ambaye nyinyi mliye nilaumu kwa ajili yake! Na mimi
kweli nilimtaka, na nikafanya juhudi kumghuri anikubalie, naye akajizuia na
akakataa. Kama kwamba vile anavyo kataa ndio anazidi kumtia hamu yule mwanamke!
Akasema mwanamke: Na mimi naapa! Kama hafanyi ninayo muamrisha atapata
adhabu ya kifungo, na atakuwa katika madhalili wenye kudharauliwa!
33. Yusuf akasema naye alisikia vile vitishio,
na akasikia kwa wale wanawake nasiha ya kuwa amkubalie, akasema: Ewe Mola wangu
Mlezi! Nakhiari kifungo kuliko hayo anayo nitakia huyu mwanamke. Kwani hayo ni
kukuasi Wewe. Na kama Wewe hunikingi na shari ya vitimbi vyao na hila zao
nitakuja wakubalia, na nitakuwa miongoni mwa wajinga walio potea.
34. Mwenyezi Mungu akamuitikia, na akamuepusha
na shari ya vitimbi vyao. Hakika Yeye peke yake ndiye Mwenye kusikia maombi ya
wenye kukimbilia kwake, na Mwenye kujua yanao wafaa.
35. Kisha ikadhihiri rai ya Mheshimiwa na watu
wake, baada ya kwisha ona dalili zilizo wazi kuwa Yusuf hana makosa.
Wakakubaliana rai hii, na wakaapa kuitimiza. Nayo ni kumtia yeye gerezani kwa
muda mfupi au mrefu, ili kumkinga mkewe na maneno mabaya, na kumuepusha na
masengenyo ya watu!
36. Wakaingia pamoja na Yusuf vijana wawili
katika watumishi wa Mfalme. Mmoja wao akasema: Mimi nimeota usingizini kuwa
ninakamua zabibu kutengeneza mvinyo. Mwingine akasema: Mimi nimeota nimebeba
kichwani mwangu mikate, na ndege wanaila! Hebu tuambie, ewe Yusuf, tafsiri ya
haya tuliyo ota, na mambo yetu yataishia vipi. Sisi tunaamini kuwa wewe ni
katika watu wanao sifika kwa wema na kujua tafsiri za ndoto.
37. Yusuf akawaambia kutilia mkazo yale waliyo
yajua kwake Yusuf: Hakitowahi kukufikieni chakula kuwa ni riziki mliyo kadiriwa
ila nami nitakwambieni kitavyo kujieni kabla ya kukufikieni. Na nitakutajieni
mapishi yake na vipi kilivyo. Namna hivyo ndivyo tafsiri ya ndoto na khabari
zilizo fichikana katika alivyo nifunza Mola wangu Mlezi na akanifunulia, kwani
nilimtakasia Yeye tu ibada yangu. Na nikakataa kumshirikisha na kitu chochote.
Na nikajitenga mbali na dini ya watu wasio msadiki Mwenyezi Mungu, na wala
hawamuamini Yeye kwa njia iliyo sawa, nao wanaikanya Akhera na hisabu zake.
38. Mimi nimeacha mila ya hawa makafiri, na
nikafuata Dini ya baba zangu Ibrahim, na Is-haaq, na Yaa'qub. Nikamuabudu
Mwenyezi Mungu pekee. Haitufalii sisi kumfanyia Mwenyezi Mungu mshirika yeyote
yule, akiwa Malaika, au jini, au mwanaadamu, licha ya masanamu ambayo hayaleti
manufaa wala madhara, wala hayasikii, wala hayaoni! Hiyo ndiyo Tawhidi aliyo
tutunukia Mwenyezi Mungu sisi na watu wote, kwa vile alivyo tuamrisha
tuwafikilishie ujumbe. Lakini wengi wa watu hawaipokei fadhila hii kwa shukrani,
bali wanaikataa!
39. Enyi wenzangu wawili wa gerezani! Je mabwana
wengi mbali mbali ni bora mtu kuwanyenyekea kuliko Mwenyezi Mungu Mmoja asiye
shindika?
40. Hamuabudu badala ya Mwenyezi Mungu ila
majina tu mliyo yazua nyinyi na baba zenu kwa mawazo bila ya kuwepo kweli.
Mwenyezi Mungu hakuwateremshia hao hoja wala ushahidi wowote! Hapana wa kuhukumu
nini kinacho faa kuabudiwa na kipi hakifai ila Mwenyezi Mungu tu. Yeye
ameamrisha msimnyenyekee yeyote mwenginewe, na mumuabudu Yeye peke yake. Hiyo
ndiyo Dini iliyo nzima iliyo nyooka, ambayo dalili zote na ushahidi unaelekea
kwake. Lakini aghlabu ya watu hawataki uwongozi wa dalili hizi, wala hawajijui
kuwa wamo katika ujinga na upotovu.
41. Enyi wenzangu wawili wa gerezani! Hii basi
ndiyo tafsiri ya ndoto zenu: Ama mmoja wenu aliye kamua zabibu katika ndoto
yake, atatoka jela, na atakuwa akimnywesha mvinyo Mfalme. Na ama huyu wa pili
atatundikwa msalabani, na ataachwa msalabani ndege wakimla kichwa chake.
Yamekwisha timia hayo mambo kama nilivyo eleza kwa mujibu mlivyo nitaka nieleze
tafsiri ya hizo ndoto!
42. Akamwambia yule aliye kuwa atavuka: Nitaje
kwa Mfalme kwa sifa zangu, na kisa changu. Asaa huenda akanifanyia insafu
akanivua na haya mateso! Shetani alimshughulisha akamsahaulisha kutaja kisa cha
Yusuf kwa Mfalme. Basi Yusuf akabaki gerezani kwa miaka isiyo pungua mitatu.
43. Mfalme akasema: Nimeota usingizini kuna
ng'ombe saba wanene wanaliwa na wengine saba walio konda madhaifu. Na nimeota
mashuke saba mabichi, na mengine saba makavu. Enyi wakuu wanazuoni na wenye
maarifa! Nitoleeni fatwa ya hizi ndoto zangu, ikiwa ni kweli nyinyi mnajua
tafsiri za ndoto na mnaweza kuzitolea fatwa.
44. Wakasema: Hizi ni ndoto zilizo korogeka
ovyo, na wasiwasi wa kuzuka tu katika nafsi ya mtu! Na sisi si wenye kujua
tafsiri ya ndoto za ovyo ovyo.
45. Akasema yule mtu aliye okoka katika wawili
alio kuwa nao Yusuf gerezani, na akakumbuka wasia wa Yusuf, baada ya kupita muda
mrefu: Mimi nitakwambieni tafsiri ya ndoto aliyo itaja mfalme. Nipelekeni kwa
huyo mwenye ilimu ya kuifasiri.
46. Yule mtumishi wa kumletea mfalme ulevi
akenda kwa Yusuf, akamwita: Yusuf! Ewe uipendaye kweli! Tueleze nini maana ya
ndoto ya ng'ombe saba wanene kuliwa na ng'ombe saba walio konda. Na ndoto
ya mashuke saba mabichi na mengine makavu? Nataraji kurejea kwa watu nami nina
fatwa yako, ili nao wapate kujua maana yake, na waujue ujuzi wako na fadhila
yako.
47. Yusuf akasema: Tafsiri ya ndoto hizo ni kuwa
mtalima katika ardhi ngano, na shairi kwa muda wa miaka saba mfululizo kwa
ukulima wa juhudi. Mtacho vuna kihifadhini, mkiache katika mashuke yake,
isipokuwa kidogo mtacho kila katika miaka hiyo, kwa uangalizi mzuri.
Aya
hii inawafikiana na ilimu za kisasa kuwa kuweka punje katika mashuke yake
inakuwa ni hifadhi zisiharibike kwa hali ya hewa na mengineyo, na juu ya hivyo
faida yake ya chakula inabaki kwa ukamilifu zaidi.
48. Kisha baada ya miaka hii ya neema itakuja
saba ya ukame. Mtakula kile mlicho weka akiba, isipo kuwa kidogo mtacho kificha
na kukihifadhi, ili kiwe mbegu ya kupandia baadae
49. Kisha baada ya miaka hiyo ya ukame utakuja
mwaka watu watasaidiwa kwa mvua, na watakamua zabibu na zaituni, na kila cha
kukamuliwa.
50. Mfalme akamwona Yusuf atakuwa na faida naye
kwa ule uwezo wake kuifasiri ndoto yake, na akaazimia amwite. Akawaamrisha
wasaidizi wake wamlete. Alipo mfikia mjumbe akamwabia kuwa mfalme
anamtaka, khabari hiyo haikumpapatisha, juu ya kuwa ina bishara ya
kufunguliwa kwake. Wala kule kutamani kutoka kwa mfungwa kwenye dhiki za jela na
taabu zake hakukuitikisa subira yake. Akakhiari angoje mpaka idhihirike kuwa
hana makosa kuliko kufanya haraka kutoka na huku yale aliyo tuhumiwa bado
yamemganda. Akamwambia mjumbe: Rejea kwa bwana wako umtake ayaangalie tena yale
mashtaka niliyo shitakiwa, awaulize wale wanawake walio kusanywa na mke wa
Mheshimiwa kwa kunifanyia hila mimi, wakababaika na wakajikata mikono yao: Je!
Walipo toka kwenye yale majaribio walikuwa wanaamini kuwa mimi sina makosa na
safi, au waliniona ni mchafu na mzinifu? Mimi nataka haya ipate kuonekana hakika
katika macho ya watu. Ama Mola wangu Mlezi anavijua vyema vitimbi vyao!
51. Mfalme akawakusanya wale wanawake, na
akawauliza: Ilikuwa vipi hali yenu pale mlipo jaribu kumkhadaa Yusuf aghafilike
na wema wake na usafi wa nafsi yake? Je, mlimwona amemili kwenu? Wakamjibu:
Mwenyezi Mungu ametakasika! Hakumsahau mja wake hata uchafuke usafi wake. Sisi
hatukuona kwake lolote la kumtia dosari. Hapo basi wema ukapata nguvu katika
moyo wa Zuleikha (mke wa Mheshimiwa) akaingia kusema: Sasa kweli
imedhihiri! Ni mimi ndiye niliye mkhadaa, na nikajaribu kumzaini kinyume na
nafsi yake kwa kumghuri. Lakini yeye alishikilia usafi wake! Na sasa nahakikisha
kuwa yeye ni katika watu wa kweli. Na ni haki tupu alipo nirudishia tuhuma mimi
na kunitia makosani!
52. Haya mimi naungama kwa kweli ninayo itoa,
apate kuwa na yakini Yusuf kuwa mimi sikuchukua fursa ya kuto kuwepo alipo kuwa
gerezani nikaendelea na khiyana, na nikamdhulumu kwa kumtuhumu. Na kwa kuwa
hakika Mwenyezi Mungu haijaalii kufanikiwa mipango ya makhaini.
53. Wala sidai kuwa nafsi yangu haitelezi; kwani
ni tabia ya nafsi kumili kwenye matamanio, na kupendelea maovu na shari. Isipo
kuwa nafsi aliyo ilinda Mwenyezi Mungu na akaiweka mbali na maovu. Na hakika
mimi ninatumai rehema ya Mwenyezi Mungu na msamaha wake, kwani Yeye ni Mkunjufu
wa kusamehe dhambi za wenye kutubu, na yu karibu wa kuwarehemu waja wake walio
kosa.
54. Usafi wa Yusuf ulipo dhihiri kwa mfalme,
aliazimu amwite. Akawatuma watu wake wamlete awe wake yeye mwenyewe wa kumsafia
niya. Basi alipo hudhuria na yakapita baina yao mazungumzo, mfalme akaathirika
na utukufu wa Yusuf kwa usafi wa nafsi yake, na ubora wa rai zake! Akamwambia:
Sasa wewe kwangu utakuwa na cheo cha hishima kilicho thibiti. Na wewe ni
muaminifu kwangu ninaye kuamini.
55. Mfalme akajua kwake Yusuf kuwa yeye ni
muangalizi mwema na mweza wa kazi yake. Na Yusuf akahisi hayo. Hapo akataka
amfanye waziri akamwambia: Nitawalishe juu ya khazina zote za mamlaka yako, na
ghala za nchi yako. Kwani mimi kama ulivyo yakinika mwenyewe naweza kuendesha
mambo ya serikali, nami ni mlinzi, na najua kupanga na kuendesha mambo.
56. Mfalme alilikubali ombi lake, akamfanya
waziri wake. Hivyo basi Mwenyezi Mungu alimneemesha Yusuf kwa neema nzuri,
akampa madaraka na uwezo katika nchi ya Misri, akienda humo atakapo. Na hii
ndiyo shani yake Mwenyezi Mungu kwa waja wake, humpa neema yake amtakaye katika
wao, wala hawanyimi thawabu zao, bali huwapa ujira wao wa wema wautendao kwa
kuwalipa mema hapa hapa duniani.
57. Na malipo yao ya Akhera ni bora zaidi na
yanalingana zaidi na hao wanao msadiki Yeye na Mitume wake, na ikawa
wanaingojea Siku ya Hisabu na wanaikhofu.
58. Ukame ukazidi kushtadi katika nchi jirani na
Misri. Ikawapata watu wa Yaa'qub shida vile vile kama ilivyo wapata
wengineo. Watu walikwenda Misri kutoka kila pande baada ya kujua
matengenezo ya Yusuf ya kuweka akiba chakula, na kujitayarisha kwake kwa
miaka ya ukame. Yaa'qub aliwatuma wanawe wende kutafuta chakula, lakini akabaki
naye nduguye Yusuf kwa mama kwa kumkhofia. Wale watoto wake walipo fika Misri
wakenda moja kwa moja kwa Yusuf, naye akawatambua, lakini wao hawakumjua.
59. Yusuf akaamrisha wakaribishwe ugeni, na
wapewe mahitaji wanayo yataka. Wakapewa hayo. Akaingia kuzungumza nao na
kuwauliza hali zao kama mtu asiye wajua! Naye anawajua vyema. Nao wakamwambia
kuwa wamemwacha ndugu yao mmoja kwa baba yao, kwani hapendi kuachana naye. Naye
huyo ni Bin-yamini nduguye Yusuf kwa baba na mama. Basi yeye akasema: Mwacheni
ndugu yenu aje nanyi, wala msiogope chochote. Nyinyi mmekwisha ona vipi ninavyo
kutimizieni vipimo vyenu, na ninavyo kukirimuni.
60. Mkitomleta ndugu yenu huyu, basi hampati
chakula kwangu, wala msijaribu kunijia tena.
61. Nduguze wakasema: Tutajaribu kusema na baba
yake ageuze rai yake, iondoke khofu yake juu ya mwanawe. Na sisi
tunakuhakikishia kuwa hatutokasiri wala kulegalega katika hayo.
62. Walipo taka kuondoka aliwaambia wafwasi
wake: Watilieni thamani ya bidhaa yao waliyo kuja nayo humo humo pamoja na
mizigo yao, ili waione watakapo rudi kwa watu wao, wapate kurejea tena kwa
kutumai kupewa chakula kwa kuamini kuwa tunatimiza ahadi, na wawe na imani ya
usalama wa ndugu yao, na baba yao azidi kutua nafsi yake.
63. Walipo rejea kwa baba yao walimsimulia kisa
chao na Mheshimiwa wa Misri, na upole wake kwao, na kwamba amewaonya kuwa
atawanyima kuwapimia chakula baadae ikiwa hatokuwa nao Bin-yamini; na kwamba
amewaahidi kuwatimizia kipimo na atawatukuza pindi wakirudi na ndugu yao.
Wakamwambia baba yao: Mwache ende nasi ndugu yetu, kwani ukimpeleka yeye
tutapimiwa chakula cha kutosha tunacho kihitajia. Nasi tunakuahidi ahadi ya
nguvu ya kwamba tutafanya juhudi kumlinda.
64. Yaa'qub yalimtibuka moyoni mwake yale ya
zamani, akayaunganisha na haya mapya. Akawaambia wanawe: Nikikukubalieni itakuwa
hali yangu ni ya ajabu; kwani nikikuaminini kwa huyu ndugu yenu haitakuwa ila
mfano wa pale nilipo kuaminini kwa Yusuf. Mkamchukua kisha mkarudi mkisema:
Kaliwa na mbwa mwitu! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye anaye nitosheleza katika
kumlinda mwanangu. Wala mimi simtegemei mtu ila Yeye, kwani Yeye ndiye Mlinzi
aliye na nguvu kuliko wote, na rehema yake ni kunjufu mno, hatonipa tena
machungu ya ndugu yake baada ya yale ya Yusuf.
65. Na wale nduguze Yusuf hawakujua kuwa Yusuf
aliwatilia bidhaa zao katika mizigo yao. Walipo ifungua wakakuta mali yao, na
wakaona hisani aliyo wafanyia Yusuf, wakaitumia hiyo kuzidi kumpoza moyo
Yaa'qub, na kumkinaisha awakubalie kwa aliyo yataka Mheshimiwa. Wakazidi
kumshikilia akubali, wakamkumbusha makhusiano yao yalio wafunga kwa baba mmoja.
Wakasema: Ewe baba yetu! Unataka wema gani zaidi kuliko haya, na hayo yatayo
kuwa? Haya mali yetu tumerudishiwa bila ya kuchukuliwa chochote. Basi natusafiri
na ndugu yetu, na tuwaletee watu wetu mahitaji, nasi tutamchunga ndugu yetu, na
tutaongeza mahitaji shehena ya ngamia kuwa ni haki ya ndugu yetu! Kwani yule
Mheshimiwa kapanga kuwa kila mtu humpa shehena ya ngamia.
66. Waliweza wana wa Yaa'qub kumkinaisha baba
yao, na maneno yao yakampata palipo. Akaacha kushikilia kumzuia mwanawe asende
Misri na nduguze. Lakini moyo wake haukuwacha kuwa na haja ya kuzidi kutuzwa.
Kwa hivyo aliwaambia: Sitomwacha ende nanyi ila baada ya kunipa dhamana ya
nguvu. Niahidini kwa Mwenyezi Mungu kwamba mtanirudishia mtapo rudi. Na wala
msiache kumrudisha ila mkiangamia nyinyi au ikawa adui amekuzungukeni
akakushindeni. Wakamkubalia na wakampa ahadi aliyo itaka. Na hapo tena
akamshuhudisha Mwenyezi Mungu ahadi yao na viapo vyao kwa kusema: Mwenyezi Mungu
anayashuhudia na kuyaona yote haya yanayo pita baina yetu.
67. Yaa'qub alitua kwa ahadi ya watoto wake.
Kisha huruma ilimpelekea kuwausia kuwa watapo ingia Misri waingie kupita milango
mbali mbali, ili watu wasiwapige kijicho, huenda wakadhurika. Akasema: Wala mimi
sina uwezo wa kukulindeni na madhara. Kwani mwenye kuzuia madhara ni Mwenyezi
Mungu tu, na hukumu ni yake Yeye pekee. Mimi nimemtegemea Yeye, na mambo yangu
na yenu yote nimemwachia Yeye. Na juu yake Yeye peke yake wategemee wote wanao
tegemeza mambo yao, kwa kumuamini Yeye.
68. Wale vijana wakapokea wasia wa baba yao,
wakapitia milango mbali mbali. Wala hayo si kama ndiyo ya kuwazuilia madhara
walio kwisha andikiwa na Mwenyezi Mungu! Na Yaa'qub akijua hayo, kwani yeye
alikuwa na ilimu tuliyo mfundisha. Lakini wasia wake ulikuwa ni kwa haja aliyo
kuwa nayo nafsini mwake tu, nayo ni huruma ya baba kwa wanawe ambayo
ameidhihirisha katika huu wasia. Na hakika watu wengi hawana ujuzi kama alio
kuwa nao Yaa'qub wakamwachia mambo yao Mwenyezi Mungu awalinde.
69. Walipo ingia kwa Yusuf aliwapokea kwa
hishima, na khasa yule nduguye kwa baba na mama ndio akamchukua na akampa siri
kwa kumwambia: Usitie shaka mimi ni nduguyo Yusuf. Basi usihuzunike kwa waliyo
kufanyia wewe na waliyo nifanyia mimi.
70. Basi baada ya kuwakirimu kwa kuja kwao, na
kuwapimia chakula, na kuwazidishia shehena ya nduguye, aliwafungia mizigo yao
kwa ajili ya safari. Tena akawaamrisha wasaidizi wake watumbukize chombo cha
kunywea katika mzigo wa Bin-yamini. Kisha mmoja wa wasaidizi wa Yusuf alinadi:
Enyi wasafiri! Ngojeni! Nyinyi ni wezi!
71. Wakashituka nduguze Yusuf kwa kutangaziwa
yale, wakawaelekea wale wenye kunadi wakawauliza: Mmepoteza nini, na mnatafuta
nini?
72. Wale wasaidizi wakajibu: Tunatafuta kikopo,
nacho ni chombo anacho nywea mwenyewe mfalme. Na malipo yake kwa mwenye kukileta
ni shehena nzima ya chakula anayo ibeba ngamia. Yule mkubwa wao alitilia mkazo
hayo kwa kusema: Na mimi ninadhamini kutimiza ahadi hii.
73. Nduguze Yusuf wakasema: Hakika kututuhumu
sisi kwa wizi ni jambo la ajabu mno! Na tunahakikisha kwa kiapo ya kwamba nyinyi
wenyewe mmeona katika mwendo wetu na tunavyo ishika dini yetu katika mara mbili
tulipo kuja hapa kuwa mmejua yakini kuwa sisi hatutaki kuleta uharibifu
katika nchi yenu. Wala si katika tabia yetu kuwa ni wezi.
74. Na Yusuf alikwisha waamrisha wafwasi wake
wawaache nduguze waamue nini malipo anayo stahiki kupata yule atakaye
onekana nacho kile kikopo, ili apate kumchukua nduguye kwa hukumu yao wenyewe,
na iwe hukumu yao ndiyo ya kukata shauri, isiwepo njia ya kumwombea. Basi watu
wa Yusuf wakawaambia wale nduguze: Nini malipo ya wevi kwenu wanapo gundulikana
ni katika nyinyi?
75. Na kwa kuwa wana wa Yaa'qub walikuwa na
yakini kuwa wao hawakukiba kile kikopo walisema bila ya kusitasita: Malipo ya
mwenye kuchukua hicho kikopo ni kushikwa huyo na afanywe mtumwa. Ndio hivi sisi
tunavyo walipa wenye kudhulumu wakachukua mali ya watu.
76. Shauri ikaishia ipekuliwe mizigo, na ikawa
lazima kufanya mambo baraabara ili isionekane kuwa kuna mpango ulio pangwa.
Yusuf mwenyewe ndiye aliye fanya uchunguzi, baada ya kwisha tengeza mambo.
Akaanza kupekua mizigo ya wale ndugu kumi, kisha ndio akaingia kuupekua
mzigo wa nduguye. Humo akakitoa kile kikopo, na kwa hivyo hila yake ikafuzu.
Akawa na haki kwa hukumu ya nduguze kumshika Bin-yamini. Hivi ndivyo Mwenyezi
Mungu alivyo mpangia mambo Yusuf. Hakuwa anaweza yeye kumshika nduguye kwa
mujibu wa sharia ya mfalme wa Misri tu ila kwa kutaka Mwenyezi Mungu. Naye
alitaka. Basi tulimpangia mambo Yusuf, na tukamwezesha kuzirekibisha sababu na
mipango baraabara na hila nzuri. Na haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu,
ambaye humtukuza katika vyeo vya ujuzi amtakaye. Na juu ya kila mwenye ilimu
yupo mwenye kumzidia katika ujuzi!
77. Kule kugunduliwa kikopo katika mzigo wa
ndugu yake kwa ghafla kuliwashangaza nduguze na kukawababaisha. Kwa hivyo
wakataka kujivua kuwa wao wote hawana makosa ila huyo na Yusuf, na kusema kuwa
tabia ya wizi wameirithi kwa mama yao. Wakasema: Si ajabu kuwa huyo kaiba, kwani
nduguye khalisa aliwahi kwiba vile vile! Na Yusuf akatambua kijembe chao wanacho
mpigia, na yakamuudhi hayo. Lakini aliyaficha, na akawawekea jawabu moyoni mwake
lau kuwa amesema wazi jawabu yenyewe inge kuwa hivi: Nyinyi mko katika hali ovu
zaidi, na nyinyi ni duni zaidi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, na
kutambua ukweli wa maneno yenu ya kumsingizia nduguye fedheha ya wizi.
78. Wakawa hawana budi kujaribu kumvua ndugu yao
au kumtolea fidia kwa kutaka kutimiza ile ahadi yao waliyo mpa Yaa'qub.
Wakaingia kutaka kumlainisha moyo Yusuf kwa kumtajia uzee wa baba yao,
wakamwambia: Ewe Mheshimiwa! Huyu ndugu yetu ana baba mtu mzima sana. Basi
mfanyie huruma umchukue mmoja wetu mwenginewe awe badala ya mwanawe huyu ambaye
ndiye anaye mpenda moyoni mwake. Matarajio yetu ni kuwa utatukubalia mambo yetu.
Kwenu tumekwisha ona tabia yako ya ukarimu, na tumehakikisha mwendo wako wa
kupenda kufanya hisani na kutenda mema.
79. Wala haikufalia kwa Yusuf kuvunja mpango
alio mkubalia Mwenyezi Mungu, na kumwachia nduguye atoke mkononi mwake. Kwa
hivyo maombi yao hayakumlainisha kitu. Akawajibu jawabu mkato, kwa kuwaambia:
Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu isije nafsi yangu ikadhulumu kwa kumzuia
yeyote yule isipo kuwa yule yule tuliye mkuta nayo mali yetu. Tukimchukua
mwenginewe kwa kumuadhibu tutakuwa katika hao walio vuka mipaka kwa kumshika
asiye na makosa kwa madhambi ya mwovu.
80. Ilipo katika tamaa yao, wakavunjika moyo
kukubaliwa maombi yao, wakenda pembeni peke yao wakishauriana juu ya msimamo wao
na baba yao. Ilipo ishia shauri kwa mkubwa wao mwenye kupanga mambo yao,
aliwaambia: Haikufalieni kuisahau ahadi ya kiapo mliyo mpa baba yenu ya
kuwa mtamhifadhi ndugu yenu mpaka mrudi naye, wala mlivyo fungana naye kabla
yake kuwa mtamlinda Yusuf, na hayo mkayavunja! Kwa hivyo mimi nitabaki Misri
wala sitotoka ila afahamu baba yetu ukweli wa hali hii, na akaniachilia nirejee
kwake, au Mwenyezi Mungu anihukumie kurejea kwa hishima, na akanisahilishia njia
kwa sababu yoyote ile. Na Yeye ndiye Mbora wa uadilifu kuliko mahakimu wote.
81. Rejeeni nyinyi kwa baba yenu, na msimulieni
kisa chote hichi. Na mwambieni: Mkono wa mwanao ulikunjuka akakiiba kikopo cha
mfalme, na kimekutikana katika bahasha yake. Kwa huo wizi wake ndio ameshikwa.
Nasi hatukwambii ila tuliyo yaona, na wala sisi hatukuwa tunajua yaliyo
fichikana katika hukumu ya Mwenyezi Mungu pale tulipo kutaka nawe ukatupa
tumhifadhi na turejee naye kwako kama tulivyo ahidiana na tukafungana. Na
Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa uadilifu kuliko mahakimu wote.
82. Na ikiwa wewe una shaka na haya tunayo
kwambia mtume mtu akuletee ushahidi wa watu wa Misri. Na pia wewe mwenyewe
waulize wasafiri wenzetu tulio rudi nao, ipate kudhihiri kuwa sisi hatuna
lawama. Nasi tunakuhakikishia kuwa sisi ni wakweli katika haya tuyasemayo.
83. Wakarejea wana walio baki kwa Yaa'qub.
Wakamueleza kama alivyo wausia kaka yao mkubwa. Khabari ile ikamtibua huzuni
zake, zikazidi kwa kumpoteza mwanawe wa pili. Wala hakutua nafsi yake kwa kuwa
wao hawana makosa ya kusabibisha kupotea kwake, naye angali na machungu kwa
waliyo mfanyia Yusuf. Akapiga ukelele kwa kuwatuhumu akiwaambia: Niya yenu
haikusalimika katika kumhifadhi mwanangu, lakini nafsi zenu zimekuchocheeni
mumpoteze kama mlivyo mpoteza nduguye. Lau kuwa nyinyi hamkutoa fatwa ya kuwa
mwizi ashikwe afanywe mtumwa kuwa ndiyo adabu ya mwizi huyo Mheshimiwa
asingeli mshika mwanangu, wala asingeli baki kaka yenu huko Misri. Lakini mimi
sina hila ila kustahamili katika msiba wangu kwa maliwaza mema, huku nikitaraji
kwa Mwenyezi Mungu anirudishie wanangu wote. Kwani Yeye ndiye Mwenye ujuzi ulio
zunguka hali yangu na hali zao. Na Yeye ndiye Mwenye hikima yenye kushinda, na
kwa hiyo ndio hunitendea na hunipangia.
84. Akadhikika kwa waliyo yasema, akajitenga
nao, kashughulika na msiba wake na huzuni kumkosa Yusuf. Macho yake yakafanya
kiza kwa wingi wa huzuni, naye akiificha sana.
Huzuni kubwa huleta
ugonjwa wa macho unao itwa Glocoma, na weupe huzidi mpaka mtu mwisho
anakuwa kipofu.
85. Siku zikapita na Yaa'qub kazama katika
majonzi yake. Wanawe wakaogopa isije kuwa khatari. Wakamkabili kumtaka apunguze
huzuni yake, nao wako baina ya kumwonea huruma na kuchukia kuwa bado yu ngali
akimkumbuka Yusuf wakamwambia: Kama hukujipunguzia nafsi yako hapana shaka
kumkumbuka Yusuf kutakuzidishia machungu yako yakukondeshe mpaka ukaribie kufa,
au ufe khasa!
86. Maneno yao hayakumuathiri hata chembe.
Akawajibu kwa kusema: Mimi sikukushitakieni, wala sikukutakeni mnipunguzie
machungu yangu! Mimi sina ila Mwenyezi Mungu tu wa kumnyenyekea na kumshitakia
dhiki zangu nzito na nyepesi. Wala siwezi kumficha hayo wala lolote nisilo
liweza, kwani mimi natambua wema wake wa kutenda na ukunjufu wa rehema yake,
jambo ambalo nyinyi hamlijui!
87. Na kuwa na imani na Mwenyezi Mungu ndio
huhuisha matumaini. Kwa hivyo zile dhiki za moyo hazikuondoka kwa matarajio ya
Yaa'qub kumrudia wanawe, na yakamtia katika moyo wake kuwa wangali wahai, na
kwamba wakati wa kukutana nao ndio umefika. Akawaamrisha wanawe wende
wakawatafute, akawaambia: Enyi wanangu! Rejeeni Misri muwe na kaka yenu, na
mumtafute Yusuf na nduguye, muulize khabari zao kwa upole bila ya watu kujua.
Wala msikate tamaa kwa Mwenyezi Mungu kuturehemu kwa kuwarudisha. Kwani hawakati
tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa wale wanao kanya.
88. Nduguze Yusuf walimwitikia baba yao kwa
matakwa yake. Wakatoka kwenda Misri, na wakajaribu kukutana na mtawala wake
ambaye baadae ikadhihiri kuwa ndiye Yusuf! Walipo ingia kwake walisema: Ewe
Mheshimiwa! Sisi na watu wetu tumepata shida ya njaa na madhara ya mwili na
nafsi. Na tumekuletea mali chache ndio bidhaa yetu. Nayo ni ya kukataliwa kwa
kuwa ni kidogo na mbaya, wala haitoshi kwa hayo tunayo taraji kwako. Lakini sisi
tunataraji kwako utupimie kwa ukamilifu na utacho tuzidishia kiwe ni sadaka
unayo tupa. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu huwalipa wenye kutoa sadaka
thawabu njema kabisa.
89. Yusuf akaingiwa na huruma ya udugu ambayo
inasamehe maovu. Akaanza kuwafunulia khabari zake kwa kuwaambia kwa lawama: Je!
Mmejua ule uovu mlio mfanyia Yusuf kwa kumtumbukiza kisimani, na maudhi mlio
mfanyia nduguye, mkafanya hayo kwa ujinga ulio kusahaulisheni huruma na udugu?
90. Kuzinduliwa huku kwa furaha kuliwatambulisha
kwamba huyu ndiye Yusuf. Wakamtazama kisha wakasema kwa yakini: Hakika wewe
ndiye kweli Yusuf! Na Yusuf mwenye ukarimu aliwaambia kwa kuwakubalia: Mimi
ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufadhili kwa kutuvua kwa
salama tusihiliki, na kwa kutupa hadhi na madaraka! Na hayo yamekuwa ni malipo
ya Mwenyezi Mungu kwa usafi wangu na wema wangu. Na hakika Mwenyezi Mungu haachi
ukapotea ujira wa mtendaji mema na akaendelea nao.
91. Wakasema: Uliyo sema ni kweli, na
tunakuhakikishia kwa kiapo kwamba hapana shaka Mwenyezi Mungu amekutukuza kwa
uchamngu, na subira, na sera njema. Na amekupa pia utawala na cheo cha
juu. Na sisi hakika tulikuwa wenye kutenda dhambi kwa tuliyo kutendea wewe
na nduguyo. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu ametudhalilisha kwako, na ametulipa malipo
ya wenye kutenda dhambi.
92. Yule Nabii mtukufu akawajibu kwa kusema:
Hapana lawama kwenu leo, wala kusutana. Lenu kutoka kwangu ni msamaha ulio mwema
kwa fadhila ya nasaba na haki ya udugu. Na namuomba Mwenyezi Mungu akusameheni
na akughufirieni. Na Yeye ndiye Mwenye rehema kuu.
93. Kisha Yusuf akawauliza khabari za baba yao.
Walipo mwambia kuwa hali yake ni mbaya na hawezi kuona kwa wingi wa hamu na
majonzi, aliwapa kanzu yake, na akawaambia: Rejeeni kwa baba yangu, na hii kanzu
mwekeeni usoni pake. Kwa hivyo atakuwa na yakini kuwa mimi nimo katika salama,
na moyo wake utajaa furaha, na Mwenyezi Mungu atamjaalia iwe ni sababa ya
kurejea kuona kwake. Hapo tena njooni naye kwangu, na ahali zenu wote pamoja.
94. Wakaondoka na ile kanzu. Na moyo wa Yaa'qub
ulikuwa umezama kungojea nini litalo leta safari ya wanawe. Na Mwenyezi Mungu
alikuwa yu pamoja naye katika kungojea huko, ikawa roho yake imeshikamana na
roho zao. Basi ule msafara wao ulipo toka nchi ya Misri katika njia yake
kumwendea yeye, aliwaambia ahali zake hayo kwa kusema: Mimi naihisi harufu
ninayo ipenda ya Yusuf inanijaa. Na lau kuwa sikhofu kwamba mtanituhumu kwa
niyasemayo ningeli kwambieni mengi ya Yusuf kuliko hizi hisiya na mawazo.
95. Wale ahali zake wakamjibu jawabu kali
wakiapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa yeye yu ngali kuropokwa kwake na kupiswa kwake
kwa uzee! Basi akajitayarisha alivyo jitayarisha kwa mapenzi yake yaliyo pita
kiasi ya kumpenda Yusuf, na kuendelea kwake kumkumbuka na kutaraji kukutana
naye.
96. Akashikilia tamaa yake akingojea rehema ya
Mwenyezi Mungu, na ahali zake wakashikilia kumdhania dhana mbovu mpaka alipo
fika mtu aliye chukua kanzu na kumbashiria kwamba Yusuf yupo salama salmina.
Ilipo wekwa kanzu usoni kwa Yaa'qub akainusa harufu yake, moyo wake ulijaa
furaha, macho yake yakarejea kuona. Yule mjumbe alipo msimulia hali ya Yusuf, na
kwamba anamtaka yeye asafiri ende pamoja na ahali zake, aliwageukia walio kuwa
naye akiwakumbusha ule utabiri wake, na akiwakaripia kwa vile walivyo
mkadhibisha. Akawataka wakumbuke yale aliyo wahakikishia pale punde kwamba yeye
anaijua rehema ya Mwenyezi Mungu na fadhila yake wasio ijua wao.
97. Hapo wakamkabili kwa kumtaka msamaha,
wakimtaraji awasamehe, na awatakie kwa Mwenyezi Mungu maghfira kwa madhambi yao.
Kwani wao walimhakikishia katika kule kutubu kwao kwamba wao walikuwa ni wenye
kutenda madhambi.
98. Akasema Yaa'qub nitaendelea kutaka msamaha
kwa Mwenyezi Mungu kufutiwa dhambi zenu. Na hakika Yeye peke yake ndiye mwenye
maghfira ya milele na rehema ya daima.
99. Yaa'qub akasafiri kwenda Misri pamoja na
ahali zake mpaka akafika huko. Walipo ingia kwa Yusuf, naye alikuwa kawapokea
kwenye milango ya Misr, huruma na shauku ilimpeleka kwa haraka kwa baba na mama
yake! Akawakaribisha na akawataka wao na ahali zake wakae Misri kwa amani na
salama kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
100. Msafara ukenda ndani ya nchi ya Misri
mpaka ukafika kwenye nyumba ya Yusuf. Wakaingia, na Yusuf akawatanguliza wazazi
wake akawaweka kwenye kochi. Yaa'qub na ahali zake wakajaa furaha kwa uzuri wa
mapokezi aliyo watengezea Mwenyezi Mungu katika mikono ya Yusuf. Kwani kwa hayo
ukoo wote umekusanyika hapo baada ya mfarakano, na umetukuka makamu makubwa ya
utukufu na hishima. Wakamuamkia maamkio yaliyo zowewa na watu tangu zamani ya
kuwaamkia maraisi na watawala. Wakaonyesha unyenyekevu kwa utawala wake. Yale
yalimkumbusha Yusuf ile ndoto yake ya utotoni. Akamwambia baba yake: Hii ndio
tafsiri ya ndoto niliyo iota na nikakusimulia ya kwamba nimeota usingizini kuwa
nyota kumi na moja na jua na mwezi zinanisujudia; ni hivi basi Mola wangu Mlezi
ameitimiza, na amenitukuza na amenifanyia hisani. Amedhihirisha kuwa sina
makosa, na akanitoa kifungoni, na akakuleteni kutoka jangwani tukutane, baada ya
Shetani kutufisidi baina yangu na ndugu zangu, akawachochea dhidi yangu. Na haya
yote yasinge kuwa bila ya Mwenyezi Mungu kuyafanya. Yeye ndiye wa kupanga na
kuyafanya mambo yatimie kama atakavyo. Na Yeye ndiye Mwenye kuzunguka kila kitu
kwa ujuzi wake, ambaye hukumu yake ni yenye kushinda katika kila jambo na
kadhiya.
101. Yusuf akamwelekea Mwenyezi Mungu
akimshukuru kwa kuzihisabu neema zake juu yake, na akimwomba amzidishie fadhila
zake, kwa kusema: Ewe Mola wangu Mlezi! Neema zako kwangu ni nyingi mno, na bora
mno! Umenipa utawala, na nakuhimidi kwa hayo. Ukanitunukia ilimu ya kufasiri
ndoto kama ulivyo nitunukia! Ewe Muumba mbingu na ardhi! Wewe ndiye uliye miliki
mambo yangu yote, na Mtawala wa neema za uhai wangu na baada ya kufa kwangu!
Nifungamanishe nawe kwa ulivyo waridhia Manabii wako katika Dini ya Kiislamu, na
uniingize katika kundi la ulio waongoa kwenye wema miongoni mwa baba zangu, na
waja wako walio wema, walio safika.
102. Ewe Nabii! Haya tuliyo kusimulia ni katika
khabari zilizo pita za kale. Hazikukufikia ila kwa wahyi ulio toka kwetu. Wala
wewe hukuwapo pale nduguze Yusuf walipo kuwa wakipanga njama. Wala wewe hukuwa
unavijua vitimbi vyao ila kwa kusimuliwa nasi.
103. Na wapo wengi ambao tabia zao zina maradhi
zinazo wazuia wasisadiki haya unayo funuliwa, hata moyo wako ukiwa una shauku
namna gani waamini, au nafsi yako ikafanya juhudi gani waongoke.
104. Wala hatukusudii kwa hadithi za uwongofu
unazo waeleza kuwa ndio upate malipo au manufaa. Ikiwa hawaongoki hawa
usiwahuzunikie. Mwenyezi Mungu atawaongoa watu wengineo. Kwani Sisi
hatukuwateremshia wao tu peke yao. Na haya si chochote ila ni mawaidha, na
mazingatio kwa kila aliye umbwa na Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi.
105. Na dalili ni nyingi mno za kuonyesha
kuwepo Muumba, na Upweke wake, na Ukamilifu wake, ziliomo katika mbingu na
ardhi, ambazo wanaziona watu wako, na wanazipuuza kwa inda, hawataki
kuzizingatia.
106. Na kati yao wapo wenye kumsadiki Mwenyezi
Mungu, wanamkubali kuwa ni Mola Mlezi, na kwamba Yeye ni Muumba wa kila kitu.
Lakini imani ya wengi wao haikusimama juu ya msingi madhubuti wa Tawhid! Basi
hawaukubali Upweke wa Mwenyezi Mungu kwa njia ya usafi. Lakini katika nafsi zao
umo mchanganyiko wa imani unao wapelekea katika njia za washirikina, mapagani.
107. Kwani wamechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu
asiwaadhibu, wakadhaminika isiwapate adhabu ya kuwagubika kwa nakama yake, kama
ilivyo wafanyia walio watangulia kabla yao? Au Kiyama kisiwajie kwa ghafla,
kikawatesa nao wameshikamana na ushirikina na ukafiri na kisha mwisho wao uwe
Motoni?
108. Ewe Muhammad! Wazindue mwisho wa uwezo
wako, na waonyeshe hadi ya juhudi yako, uwaambie: Huu ndio Mwendo wangu na Njia
yangu. Nawaita watu wafuate Njia ya Mwenyezi Mungu. Na mimi nimethibiti
katika hili jambo langu, na kadhalika anayaitia hayo kila mwenye kunifuata na
akaiamini sharia yangu. Na namtakasa Mwenyezi Mungu Subhanahu na kila kisicho
kuwa laiki yake. Wala mimi simshirikishi Yeye na kitu chochote.
109. Wala Sisi hatukuacha mtindo wetu katika
kuwateuwa Mitume tulipo kuteuwa wewe, ewe Nabii! Wala hali ya kaumu yako haikuwa
mbali na hali ya kaumu nyengine zilizo tangulia. Kwani hatukuwateuwa Malaika
kabla yako, bali tuliwateuwa wanaume wanaadamu katika watu wa mijini,
ukawateremkia Ufunuo, yaani Wahyi. Tukawatuma kuwa ni wabashiri na waonyaji.
Wenye kuongoka wakawaitikia, na wapotovu wakawafanyia inda! Je, watu wako
wameghafilika na kweli hii? Je, wamekalishwa kitako wasiweze kutembea wakaona
hao wa kale tulivyo wateketeza duniani? Na mwisho wao ni Motoni; wakaamini wenye
kuamini tukawaokoa na tukawanusuru duniani. Na malipo ya Akhera ni bora kwa
wenye kumkhofu Mwenyezi Mungu, wasimshirikishe wala wasimuasi. Zimeharibika
akili zenu, enyi wakaidi, hata hamwezi kufikiri wala kuzingatia!
110. Ewe Muhammad! Wala usione nusura yangu
inakawia, kwani nusura yangu ipo karibu na hakika inakuja. Na Sisi tuliwatuma
kabla yako Mitume, na kwa mujibu wa hikima yetu msaada wetu ulikawilia. Na wao
wakawa wanaendelea kukanywa na watu wao, mpaka nafsi zilipo tikisika, wakahisi
kukata tamaa, nusura yetu ikawadiriki; tukawaneemesha kwa kuwaokoa na kuwaletea
amani wale walio stahili kutaka uwokofu kwetu, nao ni Waumini. Tukawageuzia
maovu wale walio tenda dhambi kwa inadi na wakashikilia ushirikina. Wala hapana
awezae kuizuia adhabu yetu isiwafikie watu wakosefu.
111. Na Sisi
tumekufunulia tuliyo kufunulia katika visa vya Manabii ili kuuthibitisha moyo
wako, na iwe ni hidaya kwa watu wako. Na tumetengeneza mazingatio na waadhi wa
kuwanawirisha wenye akili na busara, na wanao tambua kuwa Qur'ani ni haki na
kweli. Hizi hazikuwa ni hadithi za kutunga, wala nganu za kuzua. Bali hakika ni
kweli na ufunuo, wahyi, wenye kuhakikisha ukweli wa yaliyo pita katika Vitabu
vya mbinguni, na walio kuja nayo Mitume wengine! Na zinabainisha yanayo hitaji
kufafanuliwa katika mambo ya Dini, na zinaongoa kwendea katika Haki na Njia
Iliyo Nyooka, na zinafungua milango ya rehema ya Mwenyezi Mungu ili aongoke
mwenye kufuata uwongofu wake, na akawa miongoni mwa Waumini wa kweli.