1. Harufi hizi - Alif Lam Raa - ni sawa na
A.L.R. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameanzia Sura hii. Na Yeye ndiye anajua muradi
wake. Na juu ya hivyo zinaashiria kuwa Qur'ani imeundwa kwa harufi hizi hizi za
Alifbete, na nyinyi mmeshindwa kuleta mfano wake! Na kwa harufi hizi za kutamkwa
zinawazindua washirikina, wakawa wanasikiliza, ijapo kuwa wanawafikiana kuwa
wasizisikilize Aya Tukufu hizi na mfano wake ambazo ni Aya za Qur'ani yenye
hikima katika mpango wake na maana zake, na ambayo imekusanya hikima na kila
linalo wanafuisha watu katika Dini yao na dunia yao.
2. Haiwafalii watu kustaajabu wakakanusha
wahyi wetu tunao mfunulia mtu mmoja wao, naye ni Nabii Muhammad s.a.w., ili
awahadharishe watu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na awape bishara njema wale
miongoni mwao walio amini, ya kwamba hapana shaka yoyote wana cheo kitukufu cha
juu kwa Mola wao Mlezi. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu haigeuki. Wala haiwafalii hao
watu wakanushi kumsema Muhammad, Mtume wetu, kuwa yeye ni mchawi maarufu.
3. Enyi watu! Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi
Mungu aliye umba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake katika siku sita (1)
ambazo kipimo chake hakijui ila Mwenyezi Mungu. Akatandaza utukufu wa utawala
wake, peke yake, na akayapanga mambo yote ya viumbe vyake. Basi hapana yeyote
mwenye chochote pamoja na utawala wa Mwenyezi Mungu. Wala hawezi yeyote katika
viumbe vyake hata kumwombea mtu isipo kuwa kwa ruhusa yake. Huyo, basi, ndiye
Mwenyezi Mungu Muumba, huyo ndiye Mola wenu Mlezi, na ndiye Mlinzi wa neema
zenu. Basi muabuduni Yeye peke yake, na msadikini Mtume wake, na kiaminini
Kitabu chake. Juu yenu kukumbuka neema za Mwenyezi Mungu, na zingatieni Ishara
zake zinazo thibitisha Upweke wake.
(1) Mwenyezi Mungu ameumba viumbe
vyote kwa vipindi sita, na vipindi hivi ni viwango vya mamilioni ya makarne na
makarne. Na hivyo ndivyo vinavyo itwa Siku Sita. Na katika kila nguzo za
ulimwengu zipo Ishara wazi zilizo zagaa za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu
Mtukufu. Miongoni mwa hizi, ni hivi kufanywa jua na mwezi na nyota kunyenyekea
kwa faida ya binaadamu. Na kadhaalika kupishana zamu usiku na mchana, na kuwa
mchana unaingilia kiza cha mbingu. Na umetajwa usiku mbele kwa kuwa kiza ndio
asli. Ama mchana umezuka kwa kuathirika kwa mwangaza wa jua katika anga la
ardhi, ambayo hiyo ardhi inazunguka wenyewe kwa wenyewe kama pia ili ipate
mwangaza wa jua, mara upande huu na mara upande huu.
4. Kama Mwenyezi Mungu alivyo anzisha uumbaji wa
viumbe peke yake, basi marejeo yenu, na marejeo ya viumbe vyote ni kwake Yeye.
Na Mwenyezi Mungu ameahidi hivyo kwa ahadi ya kweli isiyo na khitilafu. Na
hakika Yeye Subhanahu ameanzisha kuumba viumbe kwa kudra yake, na vitapo teketea
atavirejesha kwa kudra yake, ili awalipe Waumini wenye kumt'ii thawabu kwa
uadilifu ulio timia. Ama makafiri, wao huko katika Jahannamu
watapewa vinywaji vinavyo tokota kweli kweli, na watapata adhabu yenye
kutia machungu kuwa ni malipo ya ukafiri wao.
5. Na Mola wenu Mlezi ndiye aliye ziumba mbingu
na ardhi, na akalifanya jua litoe mwanga, na mwezi utoe nuru. Na akajaalia mwezi
uwe na vituo ili vikusaidieni kuweza kupima nyakati zenu, na mjue idadi ya miaka
na hisabu (1). Na wala Mwenyezi Mungu hakuumba hayo ila kwa hikima. Na Yeye
Subhanahu katika Kitabu chake anazikunjua Ishara zenye kuonyesha Ungu wake
na ukamilifu wa uwezo wake, ili mpate kuzingatia kwa akili zenu, na mkubali kwa
yanayo hitajia ujuzi.
(1) Aya hii ya 5 inahakikisha ukweli wa kisayansi
ambao haukujuulikana na hiyo sayansi ila hivi mwishoni. Hapo kwanza
haukujuulikana, nao ni kuwa jua ni umbo lenye kuwaka moto, na ndio chanzo cha
nguvu za kufanyia kazi zote, kwa Kiarabu huitwa T'aaqa, na kwa Kiingereza
Energy, na kwa Kiswahili cha sasa Nishati. Katika nguvu hizo ni huo Mwangaza na
Joto. Ama mwezi hauwaki moto, bali unarudisha mwangaza wa jua, kama kioo, kwa
hivyo huonekana una nuru. Kwa hivyo Subhanahu ameeleza kuwa jua lina mwangaza wa
asli, na mwezi unatoa nuru tu. Na Aya hii imeashiria hakika ya nyendo za falaki,
nayo ni kuwa mwezi unaizunguka ardhi, na kila siku unakuwa katika mahala fulani
kwa mintarafu ya dunia. Ukimaliza mzunguko wake ndio unatimia mwezi, huu wa siku
30 au 29. Kwa hivyo tunaweza kujua kiasi cha mwaka, na kwa hivyo twaweza kujua
hisabu za miaka, miezi na siku.
6. Hakika katika kufuatana usiku na mchana na
kukhitalifiana kwao, kwa kuzidi na kupungua, na katika uumbaji wa mbingu na
ardhi na vitu vyote viliomo humo, zipo dalili zilizo wazi na hoja zilizo
dhaahiri zenye kuhakikisha Ungu wa Mwenye kuumba, na uwezo wake. Hayo ni kwa
wenye kutaka kuiepuka ghadhabu yake na wakaiogopa adhabu yake.
Aya hii ya
6 inaashiria hakika inayo onekana, nayo kukhitalifiana urefu wa usiku na mchana
kwa mwaka mzima katika pahala popote duniani. Na kadhaalika kufuatana mchana na
usiku, na kuwa mchana ni wa kuangaza na kuonana, na usiku ni giza. Na maana ya
hayo ni kuwa msingi wake ni kuwa dunia inazunguka wenyewe kwa wenyewe kama pia
juu ya msumari wake, na vile vile inalizunguka jua. Na yote hayo ni dalili ya
uwezo wa Mwenye kuumba katika kuanzisha uumbaji. Ujuzi wa mambo hayo wakati wa
Mtume s.a.w. haukuwepo. Na hii ni dalili nyengine ya kwamba haya hayakuwa ila ni
wahyi, ufunuo, ulio toka kwa Mwenyezi Mungu kumpa Mtume s.a.w.
7. Hakika wale wasio amini kufufuliwa na kukutana
na Mwenyezi Mungu Siku ya Mwisho, na wakaamini - kwa kudhani tu - kuwa uhai wa
duniani ndio mwisho wao na hapana baada yake uhai mwingine, na wakatulia nyoyo
zao kwa hayo, na wala wasijue nini kitakuwa baada yake, na wakaghafilika
na Ishara za Mwenyezi Mungu juu ya kufufuliwa na kuhisabiwa,
8. Watu hao, makaazi
yao watakapo dumu ni Motoni. Hayo ni malipo kwa waliyo yachuma ya
ukafiri na vitendo viovu.
9. Hakika walio amini Imani ya kweli kweli, na
wakatenda mema katika dunia yao, Mola wao Mlezi atawathibitisha kwenye Uwongofu
kwa sababu ya Imani yao, na Siku ya Kiyama atawatia katika Bustani
zipitazo mito kati yake, na wataneemeka kwa neema za milele.
10. Dua za Waumini katika Bustani hizo ni
kumsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu na kila waliyo kuwa wakiyasema makafiri
duniani, na kusalimiwa na Mwenyezi Mungu, na kusalimiana wao kwa wao ili
kuthibitisha amani na utulivu. Na kukhitimishia dua yao ni kumhimidi Mwenyezi
Mungu kwa tawfiqi yake, kuwawezesha, kufikia Imani na kufuzu kwao kuipata radhi
yake.
11. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli waitikia
watu wanapo jiapizia shari kama vile wanavyo jihimizia kuitaka kheri, angeli
waangamiza akawateketeza wote. Lakini Yeye anawachukulia kwa upole basi
anaakhirisha kuwateketeza, ili kungojea wadhihirishe walio nayo kwa mujibu
wa anavyo wajuulia, upate kuonekana wazi uadilifu wake kwa atavyo walipa.
Wanaachwa na ushahidi wa kutosha umesimama dhidi yao, nao makusudi wanakengeuka
na kuelekea njia ya upotovu na udhalimu.
12. Na mtu akisibiwa na madhara katika nafsi
yake au mali yake au mfano wa hayo, huhisi unyonge wake, na humwomba Mola
wake Mlezi kwa hali yoyote - akiwa kajinyoosha, au kakaa kitako, au kasimama -
amwondolee dhiki zake! Mwenyezi Mungu akisha mwitikia, na akamwondolea hizo
shida zake, humuacha kando Mwenyezi Mungu na akaendelea na maasi yake, na
akasahau fadhila za Mwenyezi Mungu juu yake, kama kwamba hakupatikana na madhara
yoyote, wala hajapata kumwomba amwondolee! Na mfano wa mtindo huu Shetani
ndio huwazaini Makafiri, akawapambia vitendo vyao viovu, na uzushi wao mpotovu,
wakaona yote hayo ni mazuri.
13. Na Sisi tulikwisha ziangamiza kaumu zilizo
kutangulieni kwa sababu ya kufuru zao walipo wajia Mitume na Ishara zilizo wazi
za kusadikisha wito wao wa kuitia Imani. Na Mwenyezi Mungu akijua, kwa ajili ya
kung'ang'ania kwao ukafiri na uasi, kuwa haitopatikana Imani kwao! Basi enyi
makafiri wa Kikureshi! Zingatieni! Kama tulivyo waangamiza walio kuwa kabla
yenu, kadhaalika tutawalipa wakosefu kwa maangamizo.
14. Enyi Umma wa Muhammad! Tumekujaalieni muwe
makhalifa wa ardhi, mshike pahala pa walio kutangulieni, ili tukujaribuni
tudhihirishe mtacho kikhiari, ut'iifu au uasi, baada ya mlivyo kwisha jua yaliyo
wapata walio kutangulieni.
15. Zilipo dhihiri Aya (Ishara) za Qur'ani
kutokana na Mtume wetu Muhammad juu ya washirikina, walisema makafiri wasio
ikhofu adhabu ya Mwenyezi Mungu wala hawataraji thawabu zake: Tuletee kitabu
kinginecho kisicho kuwa hii Qur'ani. Au badilisha yaliyomo humu, yale yasiyo
tupendeza. Waambie ewe Mtume: Hayumkini wala haijuzu mimi kugeuza au
kubadilisha kwa nafsi yangu. Mimi si chochote ila ni mwenye kufuata na mwenye
kufikisha kile kinacho funuliwa kwangu kutokana na Mola wangu Mlezi. Mimi
naogopa, nikienda kinyume na Wahyi, Ufunuo, wa Mola wangu Mlezi, adhabu ya Siku
ambayo khatari yake ni kuu, na kitisho chake ni kikubwa!
16. Waambie ewe Mtume! Lau kuwa Mwenyezi Mungu
angeli taka kuwa asiniteremshie Qur'ani kutoka kwake, wala mimi
nisikufikishieni, asingeli teremsha, wala mimi nisingeli kusomeeni, na wala
Mwenyezi Mungu asingeli kufundisheni. Lakini Yeye kateremsha, na kanituma mimi
kwayo, na mimi nimekusomeeni kama alivyo niamrisha. Na mimi nilikwisha kaa nanyi
wakati mrefu kabla ya kupewa Utume, na mimi sikudai Utume wakati huo, wala
sikukusomeeni kitu chochote. Na nyinyi mmeshuhudia kuwa mimi ni mkweli na
muaminifu. Lakini umekuja Ufunuo na nimeamrishwa niusome. Basi hebu yatieni
akilini haya mambo, na myazingatie, na yakutanisheni yaliyo pita ya zamani na ya
yaliopo sasa.
17. Hapana mtu aliye jidhulumu nafsi zaidi
kuliko anaye kufuru na akamzulia uwongo Mwenyezi Mungu, au akazikanusha Ishara
za Mwenyezi Mungu alizo kuja nazo Mtume wake. Hakika hafuzu kafiri katika
vitendo vyake. Naye amekhasiri khasara iliyo wazi kwa ukafiri wake na
amemghadhibisha Mwenyezi Mungu.
18. Na hawa washirikina wanao mzulia Mwenyezi
Mungu kuwa ana washirika, wanaabudu masanamu ya upotovu. Hayawadhuru wala
hayawanufaishi. Na wanasema: Masanamu haya yatatuombea kwa Mwenyezi Mungu Siku
ya Akhera! Ewe Mtume! Waambie: Hivyo nyinyi mnamwambia Mwenyezi Mungu kuwa ana
washirika ambao hawajui, la katika mbingu wala katika ardhi? Mwenyezi Mungu
ametakasika na kuwa na washirika, na yote mnayo zua kwa kuwaabudu hao washirika.
19. Watu kwa maumbile yao hawakuwa ila ni Umma
mmoja tu. Kisha tukawapelekea Mitume wawaongoze na wawaongoe kwa mujibu wa
Ufunuo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ikawa tabia ya kibinaadamu iliyo pelekea kheri
na shari ndiyo sababu ya kuwa na nguvu zaidi shari katika baadhi yao. Juu yao
hao matamanio na nyendo za Shetani zikatawala, na kwa hivyo wakakhitalifiana. Na
lau kuwa hukumu ya Mola wako Mlezi haikutangulia ya kuwapa muhula makafiri kwa
ajili yako, Ewe Nabii, na kuakhirisha maangamizo yao mpaka siku maalumu iliyo
ahidiwa, Mwenyezi Mungu angeli wapelekea upesi maangamizo na adhabu, kwa sababu
ya mfarakano waliyo uingia, kama zilivyo ingia kaumu zilizo kwisha pita.
20. Na hawa washirikina wanasema: Hivyo Muhammad
hateremshiwi muujiza usio kuwa hii Qur'ani, wa kutuyakinisha Utume wake? Waambie
Ewe Mtume! Kuteremshwa Ishara ni jambo la ghaibu, hapana alijuaye ila Mwenyezi
Mungu. Kama Qur'ani haikufaini basi ngojeni hukumu ya Mwenyezi Mungu baina yangu
na nyinyi katika hayo mnayo yabisha. Na mimi ni pamoja nanyi katika wanao
ngojea.
21. Katika mitindo ya watu ni kuwa pale tunapo
waneemesha baada ya kwisha patwa na shida katika nafsi zao, au ahli zao (watu
wao), au mali zao, hawamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema anazo waneemesha na
kuwaondolea madhara. Bali huyakaabili hayo kwa kukakamia katika kuzikadhibisha
na kuzikataa Ishara za Mwenyezi Mungu! Ewe Mtume! Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ni
Muweza wa kukuhilikini na kukuadhibuni upesi upesi, lau kuwa si hukumu yake
tangu hapo kukupeni muhula mpaka siku ya miadi aliyo iweka mwenyewe kwa ilimu
yake peke yake. Hakika Wajumbe wetu, Malaika waliyo wakilishwa juu yenu
wanaviandika vitimbi mnavyo vipanga, na Yeye Mwenyezi Mungu atakuhisabieni na
atakulipeni.
22. Mwenyezi Mungu mnaye ikufuru neema yake, na
mnakanusha Ishara zake, ndiye Yeye anaye kuezesheni kwenda na kutembea nchi kavu
kwa miguu au kwa vipando, na baharini kwa vyombo alivyo fanya vikutumikieni,
vinavyo kwenda juu ya maji, kama anavyo visahilishia Mwenyezi Mungu kwa upepo
mzuri unao puliza kwa amani mpaka kufikilia huko vyendako. Hata mkisha tumaini
na mkafurahia huvuma tena upepo mkali ukatibua mawimbi kutoka kila upande, na
mkayakinika kuwa hapana ila kuhiliki tu! Katika shida kama hii hamna tegemeo ila
Mwenyezi Mungu. Hapo basi mnamwomba madua kwa usafi wa niya, kwa kuyakinika kuwa
hapana mwokozi isipo kuwa Yeye, na mnampa ahadi kuwa pindi akikuvueni na balaa
hiyo mtamuamini, na mtakuwa wenye kushukuru.
23. Na akisha waokoa kutokana na khatari ya
kuteketea, wanavunja ahadi yao, na mara wanarejea kwenye fisadi walizo kuwa nazo
kabla! Enyi watu mvunjao ahadi! Hakika matokeo ya kupindukia mipaka ya starehe
na kudhulumu kwenu yatarejea juu yenu peke yenu. Na hakika hizo starehe mnazo
zistarehea katika dunia yenu ni starehe za kidunia zenye mwisho.
Kisha marejeo yenu ya mwisho ni kwa Mwenyezi Mungu, na Yeye atakulipeni kwa
vitendo vyenu mlivyo vitanguliza duniani.
24. Hakika hali ya uhai wa dunia kwa uzuri wake
na starehe zake, na kisha baada ya hayo kutoweka, si chochote ila ni kama hali
ya maji yanayo teremka mbinguni, yakachanganyika na mimea ya ardhi inayo liwa na
watu na wanyama. Mimea hiyo ikastawi na ikatoa matunda, na ardhi ikapambika kwa
kunawiri. Uzuri huo ukisha fika ukomo wake, na wenyewe wakayakinika kuwa kweli
ni mali yao, na kuwa watanafiika kwa matunda yake na neema zake, amri yetu ya
kuondoa yote hayo ikaja. Tukaifanya kama kwamba iliyo fyekwa, na kama kwamba
haijapata kukaliwa wala haikupata kuwa na uzuri kabla yake! Na hali zote mbili
za kustawi na kunawiri ya kufurahia watu na kinyume cha hayo, ni mambo ya
kuondoka na kutoweka! Na kama alivyo bainisha Mwenyezi Mungu kwa mifano
iliyo wazi, anabainisha Aya zake na anafafanua hukumu zake na Ishara kwa watu
wanao fikiri na wanapima kwa akili.
Aya hii inaashiria ukweli ulio anza
kuchomoza, nao ni kuwa mwanaadamu kwa kuifanya ilimu imtumikie ameweza
kuyamiliki anayo yataka. Hata inapo kuwa karibu ya kufikilia ukweli huu
kukamilika, na akaona huyo mwanaadamu amekwisha fikilia kilele cha ujuzi, hapo
basi amri ya Mwenyezi Mungu hutokea.
25. Na Mwenyezi Mungu anawaitia waja wake kwa
Imani na vitendo vyema wendee Peponi, makao ya amani na utulivu. Na Yeye
Subhanahu humwongoa amtakaye - kwa kuwa kesha jitayarisha vyema na kaelekea
kheri - kwenye Njia ya Haki, nayo ni ya Salama.
26. Wanao tenda mema kwa kuitikia Wito wa
Mwenyezi Mungu, wakaamini na wakafanya kheri kwa Dini yao na dunia yao, hao
watapata wema katika Akhera, na wema huo ni Pepo. Na tena watapata yaliyo zidi
hayo kwa fadhila na ukarimu wa Mwenyezi Mungu. Wala nyuso zao hazitafunikwa na
huzuni na hamu na fedheha. Hawa ndio watu wa Peponi watakao neemeka humo daima
milele.
27. Na wale ambao hawakuitikia Wito wa Mwenyezi
Mungu, wakakufuru, wakatenda maasi, watalipwa kwa mujibu ya uovu walio utenda.
Na hawana mlinzi wa kuwakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na nyuso zao
zitasawajika kwa ghamu na huzuni kama kwamba zimefunikwa na weusi wa kiza cha
usiku! Na hao ndio watu wa Motoni, watasononeka humo milele.
28. Ewe Mtume! Kumbuka kitisho cha siku watapo
kusanywa viumbe vyote, kisha tuwaambie walio mshirikisha Mwenyezi Mungu katika
ibada zao: Simameni pahala penu nyinyi na hao mlio wafanya washirika wa Mwenyezi
Mungu, muangalie mtafanywa nini? Patatokea mfarakano baina ya washirikina na hao
miungu yao ya uwongo walio washirikisha na Mwenyezi Mungu. Hao miungu
watajitenga na wale wafwasi wao, kwa kusema: Sisi hatukukutakeni mtuabudu. Wala
nyinyi hamkuwa mkituabudu sisi! Hakika mlikuwa mkiyaabudu matamanio yenu tu!
29. Mwenyezi Mungu anatutosheleza kwa ilimu yake
na hukumu yake kuwa ni Shahidi wa kutupambanua baina yetu na nyinyi. Sisi
tulikuwa mbali nanyi, wala hatukuwa tunafaidika vyovyote kwa huko kutuabudu
kwenu.
30. Katika msimamo huo kila mtu atajua kheri
gani au shari gani aliyo ifanya, na atalipwa malipo yake. Na hapo hao
washirikina watayakinika kuwa kweli Mwenyezi Mungu ni Mmoja na wa pekee, Mwenye
Haki. Na yote waliyo kuwa wakimzulia Mwenyezi Mungu yatavunjika.
31. Ewe Mtume! Lingania kwenye Tawhidi safi, na
useme: Nani anaye kuleteeni riziki kutoka mbinguni inapo teremka mvua, na katika
ardhi inapo mea mimea na kuzaa? Na nani aliye kupeni kusikia na kuona? Na nani
anaye toa vilio hai kutokana na vilio maiti, kama mimea, nayo ni hai kutokana na
ardhi maiti? Nani anaye mtoa maiti kutokana na hai, kama mtu anavyo kufa? Na
nani anaye panga na kuendesha mambo yote ya ulimwengu kwa kudra yake na hikima
yake? Wataungama: Hapana pa kukimbilia! Kwa hakika ni Mwenyezi Mungu peke
yake ndiye mtenda yote. Ewe Mtume! Waambie watapo ungama: Si waajibu mkubwa
kuit'ii Haki, na kumkhofu Mwenyezi Mungu, Mmiliki Ufalme wote?
32. Huyo basi ndiye Mwenyezi Mungu mliye mkiri,
na Yeye tu peke yake ndiye Mola wenu Mlezi aliye thibiti kuwa ni Mola na Mlezi,
na akapasa kuabudiwa pekee, wala hapana mwenginewe. Na hapana baada ya Haki ya
Umoja wa Mwenyezi Mungu na kumuabudu Yeye tu, ila kutumbukia katika upotovu, nao
ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kumuabudu mwenginewe. Basi vipi mnaiacha Haki
mkauendea upotovu?
33. Kama ulivyo thibiti Ungu wa Mwenyezi Mungu
na kumuabudu Yeye, vile vile imethibiti hukumu juu ya walio tokana na amri ya
Mwenyezi Mungu wakimuasi kwa kuwa hawaifuati Haki. Kwani hakika Mwenyezi Mungu
Mtukufu hawaongoi kwenye Haki ila wanao ishika njia yake, sio wanao mfanyia
uasi.
34. Ewe Mtume! Waambie hao washirikina: Yupo
yeyote katika hao mlio wafanya washirika wa Mwenyezi Mungu mkawaabudu, awezaye
kuanzisha kuumba tangu mwanzo, na tena akarejea tena baada ya kwisha toweka?
Hapana shaka watashindwa kujibu! Basi hapo tena waambie: Allah, Mwenyezi Mungu,
tu peke yake, ndiye anaye anzisha kuumba kutokana na kuto kuwepo, na tena viumbe
vikitoweka huvirejesha. Vipi basi nyinyi mnaiacha Imani?
35. Ewe Mtume! Waambie hao washirikina: Yupo
yeyote katika hao mlio wafanya washirika wa Mwenyezi Mungu mkawaabudu, awezaye
kupambanua baina ya uwongofu na upotovu, akawaongoza watu kwenye Njia ya Haki?
Wataemewa! Basi, je! Yupi bora kufuatwa - Mwenye kuweza kuongoa kwendea Haki au
asiye weza hata kujiongoa nafsi yake? Naye huyo hawezi kumwongoa mtu, ila yeye
anahitaji mtu wa kumwongoa. Hao ndio kama wakuu wa makafiri, mapadri na mamonaki
ambao ndio mmewafanya ni waola mkamuacha Mwenyezi Mungu!! Nini basi kilicho
kupelekeeni kukengeuka hata mkawashirikisha hawa na Mwenyezi Mungu? Na nini hali
ya ajabu iliyo kusukumeni kwenye hizo hukumu na sharia za kigeni?
36. Wengi wa washirikina hawafuati katika
itikadi zao ila dhana potovu zisio kuwa na dalili zozote! Na kwa jumla, dhana
haifidi kitu, wala haiwezi kuwa ni badala ya kuijua Haki, na khasa ikiwa dhana
yenyewe ni ya kuzua tu, kama hizi dhana za washirikina. Na hakika Mwenyezi Mungu
anayajua vyema wayafanyayo wakuu wa ukafiri na wafuasi wao, naye atawalipa kwa
hayo.
37. Haiwezi kutokea kuwa hii Qur'ani aizue mtu
yeyote, kwani katika kuwa haiwezi kuigwa, na katika uwongofu wake, na hukumu
zake, hayumkini kuwa itoke kwa yeyote isipo kuwa kwa Mwenyezi Mungu tu. Nayo
inasadikisha Vitabu vya mbinguni vilivyo tangulia katika mambo ya Haki yaliyo
tajwa humo, na inaweka wazi yaliyo kwisha andikwa na kuthibitishwa katika mambo
ya hakika na sharia. Hapana shaka kuwa Qur'ani hii ina cheo maalumu kwa Mwenyezi
Mungu, nayo ni muujiza ambao hapana mtu anaye weza kuleta mfano wake.
38. Bali hawa washirikina wanasema: Muhammad
kaizua hii Qur'ani mwenyewe! Ewe Mtume! Waambie: Ikiwa hii Qur'ani ni kazi ya
mwanaadamu, basi nyinyi leteni Sura moja tu mfano wake, na muwatake
muwatakao, isipo kuwa Mwenyezi Mungu, waje kukusaidieni; ikiwa nyinyi ni wasema
kweli katika madai yenu kuwa hii Qur'ani nimeitunga mimi.
39. Bali hawa washirikina wamekimbilia
kuikadhibisha Qur'ani bila ya kuzingatia, wakajua yaliomo ndani yake! Wao
wenyewe hawakutazama mna nini, wala hawakusita kuitafuta tafsiri yake, na kutaka
kuelewa hukumu zake kwa kuwauliza wenginewe! Na kukadhibisha namna hii bila ya
ujuzi, ndivyo walivyo wakanusha makafiri wa kaumu za zamani Mitume wao na Vitabu
vyao! Basi, ewe mwanaadamu! Angalia yaliishiaje mambo ya walio kadhibisha walio
tangulia. Waliachiliwa mbali na wakateketezwa kwa adhabu! Na huu ndio mwendo wa
Mwenyezi Mungu kwa mfano wa hao.
40. Na miongoni mwa hawa wakanushao wapo ambao
watakuja iamini Qur'ani baada ya kuyafahamu yaliyomo ndani yake, na wakayaelewa
maana yake. Na kipo miongoni mwao kikundi ambacho hakiamini wala hakiachi
upotovu wake! Na Allah Subhanahu wa Taa'la anawajua vyema wakanushao mafisadi,
na atawalipa kwa vitendo vyao.
41. Na ewe Mtume! Wakishikilia kuendelea na
kukukadhibisha baada ya kuwadhihirikia wazi dalili za Unabii wako, basi wewe
waambie: Hakika mimi nitalipwa kwa a'mali yangu,(vitendo vyangu); na nyinyi
mtalipwa kwa a'mali yenu kama itakavyo kuwa. Na mimi naendelea na Wito wangu, na
nyinyi hamtahisabiwa kwa a'mali yangu, wala mimi sitahisabiwa kwa a'mali yenu.
Basi nyinyi fanyeni mpendavyo. Na Mwenyezi Mungu atamlipa kila mtu kwa aliyo
yachuma.
42. Na katika hawa makafiri wapo wanao
kusikiliza wewe, Mtume, pale unapo waita wafuate Dini ya Mwenyezi Mungu, na hali
nyoyo zao zimefungwa hazikubali Wito wako. Basi wewe huwezi kuwafanya hawa
viziwi wakusikie na waongoke. Na khasa ilivyo kuwa juu ya uziwi wao, hawafahamu
uyasemayo.
43. Na wengine wapo wanao kutazama na
wanalifikiria jambo lako, na wanaona dalili zilizo wazi za Unabii wako. Lakini
bado hawaongoki wakafuata. Mfano wa hayo ni mfano wa kipofu, nawe huwezi
kuwaongoa hao vipofu. Upofu wa macho ni kama upofu wa moyo. Wote hawana
uwongofu! Kipofu haioni njia kwa kuhisi, na mpotovu haongoki kwa maana.
44. Hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu atawalipa
watu kwa vitendo vyao kwa uadilifu na haki, wala hatamdhulumu hata mmoja wapo
kwa kitu chochote. Lakini watu wanajidhulumu nafsi zao kwa kukhiari kwao ukafiri
kuliko Imani.
45. Ewe Mtume! Wahadharishe na Siku tutayo
wakusanya kwa ajili ya Hisabu, wawe na hakika kuwa Siku ya Akhera itakuja, baada
ya kuwa walikuwa wakiikanusha na wakikumbuka maisha yao ya duniani tu. Waone ni
kama saa moja tu ya mchana, hapana wasaa wa kufanya kitendo chochote cha kheri,
na wajuane wao kwa wao wakilaumiana kwa kufuru na upotovu walio kuwa nao!
Wamekhasiri wakanushao Siku ya Akhera na wasitangulize vitendo vyema katika
dunia yao, na wakakosa neema za Akhera kwa kufuru zao.
46. Ewe Mtume! Tukikuonyesha baadhi ya tunayo
waahidi, nayo kuwa utawashinda na wao watapata adhabu, au tukakufisha kabla ya
kuyaona yote hayo, vyovyote vile hawawezi kuepuka kurejea kwetu tuwahisabie na
kuwalipa. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mwenye kuwachungua na Mwenye kujua kila
walitendalo, naye atawalipa.
47. Na kila umma ulijiwa na Mtume akafikisha
wito wa Mwenyezi Mungu, akaamini aliye amini, na akakanusha aliye kanusha.
Ikifika Siku ya kufufuliwa, Mtume wao atakuja na kuwatolea ushahidi wale walio
mkadhibisha kuwa hao ni makafiri, na walio amini kuwa ni Waumini. Basi Mwenyezi
Mungu atawahukumu kwa uadilifu ulio timia. Hatomdhulumu yeyote katika malipo
anayo stahiki.
48. Na makafiri wanakusudia kuikanusha Siku ya
Akhera, basi wanaihimiza kwa kejeli na kusema: Itakuwa lini hiyo adhabu unayo
tuahidi, kama wewe, ewe Mtume, na hao walio pamoja nawe, ni wakweli katika hayo
mnayo yaamini na mnatuitia sisi tuyakubali?
49. Ewe Mtume! Waambie: Mimi sina uwezo wa
kujitendea mwenyewe kheri wala shari, ila kwa aliyo niwezesha Mwenyezi Mungu.
Basi vipi niweze kuihimiza ije upesi hiyo adhabu? Hakika kila umma una ukomo
wake aliyo uwekea Mwenyezi Mungu tangu na tangu. Ukiwadia ukomo huo basi
hawatoweza kuuchelewesha hata kidogo, kama wasivyo weza kuutanguliza!
50. Waambie wanao himiza ifike adhabu: Hebu
niambieni, ikikufikieni adhabu ya Mwenyezi Mungu usiku au mchana, pana faida
gani watayo ipata wakosefu wenye madhambi kutaka ije kwa haraka? Na hali adhabu
yote ni mbaya!
51. Sasa mnaikanusha adhabu? Tena itapo
kufikieni mtaambiwa kwa kubeuliwa: Je! Sasa mnaamini kwa kuwa mnaiona, na nyinyi
huko duniani mlikuwa mkiihimiza kwa dharau na kukanusha!
52. Tena Siku ya Kiama wataambiwa walio
jidhulumu nafsi zao kwa kukufuru na kukanusha: Onjeni adhabu ya milele..sasa
hamlipwi ila kwa a'mali zenu mlizo zitenda duniani.
53. Na makafiri, kwa njia ya kejeli na kukataa,
wanakutaka wewe, Mtume, uwaambie hivyo ni kweli hayo uliyo yaleta katika Qur'ani
na khabari za kufufuliwa, na adhabu? Waambie: Naam! Kwa haki ya Muumba wangu
aliye niumba, hakika hayo yatakuwa bila ya shaka yoyote. Wala nyinyi hamtoshinda
wala hamwezi kuzuia adhabu aitakayo Mwenyezi Mungu kukuleteeni.
54. Na lau kuwa vitu vyote viliomo duniani ni
mali ya kila nafsi iliyo dhulumu kwa ushirikina na kukanusha, ingeli vitoa fidia
kwa adhabu itayo wakabili Siku ya Kiyama, na ambayo wataviona vitisho vyake. Na
hapo basi majuto na masikitiko yatawajaa nyoyoni mwao kwa kutoweza kuyatamka, na
kwa fazaa itayo wapata kwa kuiona adhabu! Na hukumu ya Mwenyezi Mungu itapita
juu yao kwa uadilifu, na wala hawatodhulumiwa katika malipo hayo, kwani hayo ni
matokeo ya waliyo yatenda duniani!
55. Watu nawajue kuwa hakika Mwenyezi Mungu
ndiye Mwenye kumiliki na Mwenye madaraka makuu juu ya vyote viliomo mbinguni na
duniani. Na pia wajue kuwa ahadi yake ni ya kweli. Basi Yeye hashindwi na kitu,
na hapana yeyote ataye epuka malipwa yake. Lakini wao wamedanganyika na maisha
ya dunia, hawajui hayo kwa ujuzi wa yakini!
56. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu anavihuisha vitu
baada ya kuwa havipo, na anaviondoa baada ya kuwapo. Na kwake Yeye tu ndio
marejeo katika Akhera. Na mwenye kuwa hivyo hapana kuu la kumshinda.
57. Enyi watu! Kimekujieni kwa ulimi wa Mtume
Muhammad Kitabu kilicho toka kwa Mwenyezi Mungu. Ndani yake mna makumbusho ya
Imani, na ut'iifu, na mawaidha ya kuhimiza kheri, na kukataza vitendo viovu, na
kueleza mzingatie khabari za walio kutangulieni, na kukutakeni muangalie utukufu
wa uumbaji ili mpate kuuelewa utukufu wa Muumba. Na ndani ya Kitabu hicho mna
dawa ya maradhi ya nyoyo zenu, maradhi ya shirki na unaafiki; na mna uwongofu wa
kuendea Njia Iliyo Nyooka. Na yote hayo ni rehema kwa Waumini wanao itikia wito.
58. Ewe Mtume! Waambie: Furahieni fadhila ya
Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu kwa kuiteremsha Qur'ani, na kubainisha
Sharia ya Islamu. Na hii ni bora kuliko starehe zote anazo zikusanya mtu
duniani, kwa sababu hichi ni chakula cha nyoyo na dawa ya maradhi yake.
59. Ewe Mtume! Waambie makafiri walio pewa
baadhi ya starehe za duniani: Niambieni khabari ya vyakula vizuri vya halali
alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, mkajifanya wenyewe ni watungaji sharia,
mkahalalisha vingine na mkaharimisha vingine, bila ya kufuata Sharia ya Mwenyezi
Mungu! Hakika Mwenyezi Mungu hakukupeni ruhusa mfanye hayo, bali nyinyi
mnamzulia uwongo Mwenyezi Mungu.
60. Na watadhani nini Siku ya Kiyama hao walio
mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, wakajipa kuhalalisha na kuharimisha bila ya kuwa
nayo dalili yoyote? Hakika Mwenyezi Mungu amewaneemesha neema nyingi na
amezihalalisha kwao kwa fadhila yake, na amewawekea Sharia yenye kheri kwao.
Lakini hawamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hayo, bali wanamzulia Mwenyezi Mungu
uwongo!
61. Ewe Mtume! Hakika wewe umefikisha ujumbe
wako, na hayo Mwenyezi Mungu anayajua. Na hapana jambo lolote katika mambo yako,
na huwasomei Qur'ani, na wewe na umma wako hamtendi kitu, ila Sisi
tunayashuhudia na tunayaangalia mnapo yaingia kwa juhudi. Na Mola wako Mlezi
haachi kujua chochote hata kikiwa kina uzito wa chembe hichi, ikiwa katika
mbingu au katika ardhi, kidogo na kikubwa. Vyote hivyo vinadhibitiwa katika
Kitabu kilichoko kwa Mwenyezi Mungu, nacho ni chenye kubainisha wazi.
62. Enyi watu! Tanabahini na mjue ya kuwa wenye
kumuelekea Mwenyezi Mungu kwa Imani na ut'iifu Yeye anawapenda, na wao
wanampenda. Hawana khofu ya kuhizika duniani, wala kupata adhabu ya Akhera. Wala
wao hawahuzuniki kwa kukosa starehe za duniani, kwa kuwa watapata kwa Mwenyezi
Mungu yaliyo makubwa na mengi kuliko hayo.
63. Na hao ndio walio yasadiki yote yaliyo toka
kwa Mwenyezi Mungu, na wakaifuata Haki, na wakayaepuka maasi, na wakamkhofu
Mwenyezi Mungu katika kila walitendalo.
64. Kwa wapenzi hawa wa Mwenyezi Mungu pana
bishara ya kheri hapa duniani, kwa vile Mwenyezi Mungu amewaahidi kuwapa ushindi
na utukufu, na Akhera itatimia ahadi ya Mwenyezi Mungu. Na ahadi ya Mwenyezi
Mungu haigeuki. Na haya ndiyo waliyo bashiriwa kwayo duniani, na watayapata
Akhera. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
65. Ewe Mtume! Usihuzunuke kwa wayasemayo
washirikina ya kejeli, na matusi, na kukadhibisha. Wala usidhani kuwa hali yao
hii itadumu. Bali ushindi ni wako, na Uislamu utatukuka, kwani utukufu wote ni
wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ushindi upo mkononi mwake, na Yeye atakunusuru
uwashinde hao makafiri. Na Yeye Subhanahu ni Mwenye kuyasikia wanayo kuzulia, na
Mwenye kuyajua wanayo dhamiria. Na Yeye atawalipa kwa hayo.
66. Enyi watu! Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu
peke yake vyote viliomo mbinguni na duniani, kwa kuviumba, na kuvimiliki, na
kuviendesha. Na hao wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu kwa hakika hawawafuati hao
miungu ya ushirikina. Hao si chochote ila wanafuata mawazo tu, wanadhani kuwa
uwezo umo katika vitu ambavyo havijifai wenyewe, la kwa manufaa wala madhara.
67. Hakika huyo Mwenye kumiliki viliomo katika
mbingu na ardhi, ndiye aliye kuumbieni usiku mpate kupumzika na mahangaiko ya
mchana. Na amekuumbieni mchana wenye kuangaza mpate kufanya kazi na mshughulikie
maslaha yenu. Hakika katika kuumbwa usiku na mchana zipo dalili zilizo wazi kwa
wenye kusikia na wakapima.
68. Na ikiwa wanao abudu masanamu wamefanya
ushirikina wa kuabudu mawe, na hawakumtakasa Mwenyezi Mungu kwa haki ya
kumtakasa, na wakasema kuwa Allah, Mwenyezi Mungu, ana mwana, basi Mwenyezi
Mungu ametakasika na hayo. Yeye hana haja ya kuwa na mwana; kwani kuwa na mwana
kunaonyesha wazi kutaka kubakia ukoo wako baada ya kufa kwako. Na Mwenyezi Mungu
hafi. Yeye ni Mwenye kubakia milele. Na vyote viliomo katika mbingu na viliomo
katika ardhi ni vyake, vimeumbwa na vinaendeshwa na Yeye. Na nyinyi wazushi,
hamna hoja yoyote wala dalili ya hayo mnayo zua! Basi msikhitalifiane juu ya
Mwenyezi Mungu kwa mambo yasiyo na msingi wa hakika.
69. Ewe Mtume! Waambie:
Hao wanao mtungia Mwenyezi Mungu uwongo, na wanadai kuwa ana
mwana, hawatafanikiwa milele.
70. Wao wana starehe hapa duniani ya
kudanganyika nayo. Nayo ni chache, ikiwa itachukua muda mrefu au mfupi,
ukilinganisha na hayo yanayo wangojea! Kisha marejeo yao ni kwetu, Sisi.
Tutawahisabia na tutawaonjesha adhabu ya kutia uchungu kwa sababu ya ukafiri
wao.
71. Yanayo kupata kutoka kwa watu wako,
yaliwapata Manabii walio kutangulia. Basi wasomee hawa watu, Ewe Mtume, aliyo
kuteremshia Mola wako Mlezi katika Qur'ani kisa cha Nuhu, Mtume wa Mwenyezi
Mungu. Alipo iona chuki na uadui wa watu wake kwa ujumbe wake, aliwaambia: Enyi
watu wangu! Ikiwa kuwa pamoja nanyi kwa ajili ya kufikisha ujumbe kumekuwa ni
shida juu yenu, basi mimi ni mwenye kuendelea na wito wangu, na ni mwenye
kushikilia hapo hapo, na ni mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu katika hili jambo
langu. Basi nyinyi na washirika wenu jifungeni madhubuti katika shauri yenu,
wala msiufiche uadui wenu kwangu kabisa, wala msinipe muhula wowote kwa maovu
mnayo nipangia kunitendea, kama kweli mnaweza kuniletea madhara. Kwani Mola
wangu Mlezi ananilinda.
72. Na ikiwa mtabaki kukataa wito wangu, basi
hayo hayatanidhuru mimi kitu. Kwani mimi sikufanya hivyo kwa kutaraji kupokea
ujira kwenu ambao naogopa nitaukosa, kwa sababu ya kukataa kwenu! Ujira wangu
mimi nautaka kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na Yeye ameniamrisha niwe Muislamu,
nimsalimishie Yeye mambo yangu yote.
73. Na juu ya juhudi hizo, na kukakamia huko
aliko kakamia Nuhu kwa ajili ya kutaka kuwaongoa hao watu wake, bado
walishikilia kuendelea na kumkanusha na kumfanyia uadui. Basi Mwenyezi Mungu
alimwokoa yeye pamoja na wenye kumuamini, wakapanda marikebu. Na akawajaalia hao
ndio walio iamirisha nchi baada ya kuteketea makafiri, walio gharikishwa na
tofani. Hebu angalia, ewe Muhammad! Vipi walio puuza onyo ulivyo malizikia
mwisho wao mbaya.
74. Baada ya Nuhu tuliwatuma Mitume wengine
wakilingania Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu, wakibashiria kheri na wakionya,
na wakiungwa mkono na miujiza yenye kuonyesha ukweli wao. Watu wao wakawakanya
kama walivyo kanya kaumu ya Nuhu. Haukuwa mwendo wa wapinzani kuwa wat'iifu, kwa
sababu kule kukadhbisha kwao kulikuwa ni mbele kuliko kuzingatia na
kupima. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu alipiga muhuri wa upotovu juu ya nyoyo za wale
ambao mtindo wao ni kuzifanyia uadui hakika na Ishara zilizo wazi!
75. Kisha baada yao tulimtuma Musa na ndugu yake
Haruni wende kwa Firauni, mfalme wa Misri na watu wake wakuu makhsusi, kuwaita
wamuabudu Mwenyezi Mungu peke yake. Nao waliungwa mkono na hoja zenye nguvu.
Firauni na kaumu yake walitakabari wakakataa kuitikia wito wa Musa na Haruni.
Kwa kukataa kwao huko wakawa wamefanya makosa makubwa na dhambi.
76. Ilipo dhihiri Haki yetu kwa mkono wa Musa,
ule muujiza wa Musa - nao ni fimbo kugeuka nyoka mbele ya macho yao - wao
walisema: Hakika huu ni uchawi ulio dhaahiri!
77. Musa akawaambia kukanya uzushi wao: Nyinyi
mnaita Haki iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu kuwa ni uchawi? Hivyo hii kweli mliyo
iona kwa macho yenu ni uchawi? Basi hivi hapa mimi nakutakeni mthibitishe kwamba
huu ni uchawi. Waleteni wachawi wathibitishe hayo mnayo yadai. Na wachawi
hawafanikiwi abadan!
78. Firauni na watu wake walimwambia Musa:
Hapana shaka wewe umekuja kwa makusudi ya kutuachisha dini ya baba zetu, na mila
za kaumu yetu, ili nyinyi wawili mpate kuwa na wafuasi; wewe na nduguyo mpate
ufalme na utukufu na urais wa kutawala na kuhukumu! Kwa hivyo basi sisi
hatutakuaminini nyinyi wala huo utume wenu!
79. Firauni na kaumu yake wakadai kuwa Musa na
nduguye ni wachawi, wala si Mitume! Akawataka watu wake wamhudhurishe kila aliye
hodari katika fani za uchawi katika mamlaka yake.
80. Walipo hudhuria wachawi, na wakasimama mbele
ya Musa kupambana naye kwa uchawi wao mbele ya watu, Musa aliwaambia: Leteni huo
uchawi mlio nao!
81. Walipo tupa kamba zao na fimbo zao, Musa
aliwaambia: Huo mlio fanya ni uchawi kweli, na Mwenyezi Mungu Subhanahu
atauvunja kwa mkono wangu! Hakika Mwenyezi Mungu hawasahilishii mafisadi vitendo
vyao vikawa vizuri na vyenye nafuu.
82. Ama Haki hapana shaka
Mwenyezi Mungu atainusuru na ataiunga mkono kwa uwezo wake na hikima yake hata
makafiri wakisaidiana katika kuichukia na kuipiga vita.
83. Na juu ya kudhihiri Ishara zote za
kusadikisha Ujumbe, wale walio muamini Musa hawakuwa ila ni kikundi cha watu
wachache tu katika kaumu ya Firauni. Waliamini juu ya kuwa wakiogopa asije
Firauni na walio pamoja naye wakawaachisha waliyo yaamini. Jeuri za Firauni
zilikuwa kubwa mno katika Misri! Hakika yeye ni katika walio pita upeo katika
kutakabari na kujivuna.
84. Ama Musa aliwaambia Waumini kwa kuwawasa na
kuwashajiisha: Enyi watu wangu! Ikiwa Imani imekwisha ingia nyoyoni mwenu kwa
kumsafishia niya Mwenyezi Mungu, basi msimwogope yeyote mwenginewe. Nanyi
msalimishie Yeye mambo yenu yote, na mtegemeeni Yeye, na muwe na yakini mwishoe
atakunusuruni, ikiwa nyinyi mmethibiti katika Uislamu.
85. Waumini wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi
Mungu peke yake. Kisha wakamwomba Mola wao Mlezi asiwatie katika mitihani na
mateso ya makafiri.
86. Wakamwomba Mola wao Mlezi wakisema: Kwa vile
ulivyo tumiminia neema na rehema, na kwa wingi wa rehema yako unayo sifika nayo,
tuokoe na hawa watu wanao kataa, wenye kudhulumu.
87. Tukawafunulia Musa na nduguye Haruni kuwapa
amri wafanye nyumba za kukaa watu wao katika nchi ya Misri, na watu wa Imani
wenye kufuata wito wa Mwenyezi Mungu wazielekee nyumba hizo, na wawe wanashika
Sala kwa sura ya ukamilifu. Na Waumini wanabashiriwa kheri!
88. Walivyo shikilia makafiri katika kumfanyia
inda Musa, alimwomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: Ewe Mola Mlezi wangu! Hakika
Wewe umempa Firauni na watukufu wake starehe za duniani, na mali, na wana, na
utawala. Na matokeo ya neema hizi ni kupita kwao mipaka katika kupotea na
kupoteza watu waache Njia ya Haki! Ewe Mwenyezi Mungu! Yafutilie mbali mali yao,
na uwaache katika kiza cha nyoyo zao, wasijaaliwe kuipata Imani mpaka waione kwa
macho adhabu iliyo chungu, ambayo ndiyo mwisho unao wangojea, ili wawe ni onyo
kwa wengineo.
89. Mwenyezi Mungu akasema: Dua zenu
zimeitikiwa. Basi endeleeni katika Njia Iliyo Nyooka, na iwacheni njia ya wale
wasio jua mambo yalivyo, wala hawaifuati Haki iliyo wazi.
90. Tulipo wavusha bahari Wana wa Israili,
Firauni na askari wake waliwafuatia nyuma yao, tukawafunika kwa bahari! Alipo
kuwa anazama, Firauni alisema: Nimemsadiki Allah, Mwenyezi Mungu, walio msadiki
Wana wa Israili, na wakamfuata. Na mimi ni katika wenye kut'ii walio
wanyenyekevu!
91. Mwenyezi Mungu hakukupokea kuamini huko kwa
Firauni ambako alikuwa hana budi nako. Toba hiyo ilikuwa pale mauti yamekwisha
mkabili, naye aliishi maisha yake yote katika kumuasi Mwenyezi Mungu, akifisidi
nchi, naye akafa kafiri wa kutupwa!
92. Na leo siku ulipo angamia tutautoa mwili
wako baharini, na tutauweka uwe ni onyo na funzo kwa hao walio kuwa wakikuabudu,
na hawakuwa wakikutarajia utapata mwisho huu wa hizaya wa machungu.(1) Lakini
watu wengi wanaghafilika na Ishara zilizo wazi na zilizo zagaa katika ulimwengu,
na ambazo zinathibitisha uwezo wetu.
(1) Inaonyesha Aya hii tukufu kuwa
mwili wa Firauni utabaki umehifadhiwa ili watu wauone, na wapime kwa macho yao
hali ya ule mzoga wa yule aliye kuwa akijiona ni mungu, na akiwaambia watu wake
wanao mnyenyekea: Hamna mungu ila mimi!
Kadhaalika tujue kuwa kutoka
Wana wa Israili katika nchi ya Misri kulikuwa mwishoni mwa karne ya kumi na tatu
kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s., katika enzi ya mmoja wa Mafirauni wa Ukoo wa
kumi na tisa, naye ni Minfitah mwana wa Ramsis wa Pili, ambaye ndiye aliye
wakandamiza Wana wa Israili akawalazimisha wamjengee Jiji la ufalme wake.
Uvumbuzi wa machimbo ya vitu vya kale wa hivi karibuni
umedhihirisha kuwa jina la mji huo ulio funikika chini ya ardhi, ni "Bur'amsis".
Kulikuwa kutoka kwa Wana wa Israili pamoja na Musa ni kwa ajili ya wito wa
Tawhidi, Umoja wa Mwenyezi Mungu, na kuikata shemere ya Firauni iliyo
wadhalilisha, na ikawakutisha adhabu ya mwisho.
Na ilikuwa
haijuulikani na Waarabu ambao hawajui kusoma na kuandika, wala kwa wengineo,
kwamba mwili wa Firauni huyu ungalipo mpaka hii leo. Lakini Qur'ani imeyataja
hayo, na ukweli wake umethibiti mwaka 1900 B.K., yaani karne kumi na tatu baada
ya kuteremka Qur'ani. Je, hii si dalili ya kuwa imetoka kwa Mungu?
93. Na tuliwaweka vyema Wana wa Israili wakaishi
katika nchi nzuri na huku wakiihifadhi Dini yao, nao wako mbali na dhulma iliyo
kuwa ikiwapata; riziki na neema zimewajalia. Lakini mara baada ya kuonja
neema ya utukufu baada ya unyonge, yaliwasibu maradhi ya kufarikiana.
Wakakhitalifiana juu ya kuwa imekwisha bainika kweli na uwongo! Mwenyezi
Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama, na atamlipa kila mmoja kwa alilo
tenda.
94. Ikikuingia shaka wewe au mwengineo katika
huu wahyi tuliyo kuteremshia, basi waulize watu wa Vitabu vilivyo tangulia
walivyo teremshiwa Manabii wao. Kwao utapata jawabu ya kukata, yenye kuwafikiana
na haya tuliyo kuteremshia wewe. Na hayo ni kutilia mkazo ukweli wa uwazi wa
dalili pindi ikitokea shaka yoyote. Basi hapana njia ya kutia shaka. Sisi
tumekuteremshia Haki isiyo na shaka yoyote. Basi usishindane na yeyote
mwenginewe katika kutia shaka na kutaradadi.
95. Wala usiwe wewe, wala yeyote katika wanao
kufuata, miongoni mwa wanao kadhibisha hoja na Ishara zilio wazi, msije mkaingia
khasarani na ghadhabuni, kama hali ya makafiri wasio amini. Na akisemezwa Nabii
basi ndio wanasemezwa wote wanao mfuata.
96. Hakika wale iliyo kwisha pita juu yao hukumu
ya kuwa wao ni makafiri, kwa kujuulikana inadi yao na chuki zao, hawatoamini
hata ukijihangaisha vipi nafsi yako kuwakinaisha.
97. Na ukiwajia na kila hoja, na iwe wazi vipi,
hawakinaiki. Wataendelea tu na upotovu wao mpaka wamalizikie kupata adhabu
chungu.
98. Lau kila mji ungeli amini ingeli wafaa Imani
yao. Lakini hawaamini, na kwa hivyo hayapatikani manufaa. Ila kaumu ya Yunus.
Kwani wao waliamini, na wakapata manufaa yao. Tuliwaondolea hizaya na machungu,
na tukawapa starehe ya dunia inayo pita, mpaka ifike Siku ya Kiyama.
99. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka watu
wote katika ardhi waamini, wangeli amini. Basi wewe usihuzunike kwa ukafiri wa
washirikina. Wala haiwi Imani ila kwa khiari. Basi wewe huwezi kuwalazimisha
watu kwa nguvu ili wafuate Haki na waitikie. Haikupasii kutaka kuwalazimisha
waamini, wala hutoweza, hata ukijitahidi vipi.
100. Hawezi mtu kuamini ila akiielekeza nafsi
yake kwa hayo, na Mwenyezi Mungu akamsahilishia sababu na njia za hayo. Ama yule
asiye ielekea Imani huyo basi amestahiki kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu,
na kupata adhabu yake. Na mwendo wa Mwenyezi Mungu ni kuwapa adhabu na ghadhabu
wale wanao zipuuza na kuzikataa hoja zilio wazi, na wala hawazizingatii.
101. Ewe Nabii! Waambie hawa wenye inda:
Tazameni Ishara zilizo wazi zinazo onyesha Ungu na Upweke wa Mwenyezi Mungu
zilio enea katika mbingu na ardhi. Lakini Ishara, juu ya wingi wake, na maonyo
na yangawa na nguvu, hayawafai kitu watu wanao kataa na wala hawatumii akili
zao. Hawa wanao kanya kama hawaamini, basi hawatoangalia.
Aya hii na Aya
nyingi nyenginezo zinaita watu wajifunze kwa kuangalia na kuzingatia
(Observation). Na inaita watu wajifunze ilimu ya ulimwengu na viliomo ndani
yake, kwani huo ulimwengu umedhalilishwa kwa ajili ya mwanaadamu. Kisha hizo Aya
zinataka watu waingie katika ilimu za kujaribu (Experimental Science). Kwani
hiyo ni njia ya kujua kwa kuona vinavyo onekana.
102. Basi hao wakanyao wanangojea lolote ila
kufikiwa na siku za shida kama zilizo wapata kaumu ya Nuhu, na kaumu ya Musa, na
wengineo? Ewe Nabii! Waambie: Ikiwa mnangojea mfano wa hayo, basi ngojeni! Nami
pia nangojea pamoja nanyi. Na karibu hivi mtasibiwa na kushindwa, na Siku ya
Kiyama mtapata adhabu.
103. Kisha Sisi huwaokoa Mitume wetu na Waumini
kutokana na adhabu hiyo. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewaahidi kuwaokoa, na ahadi
yake ni ya kweli, wala hayendi kinyume.
104. Ewe Mtume! Waambie: Ikiwa mna shaka na
ukweli wa Dini niliyo tumwa kuileta kwenu, basi jueni kuwa kama mtavyo tia shaka
mimi kabisa sitoabudu hayo masanamu mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu!
Lakini mimi namuabudu Mwenyezi Mungu ambaye mambo yenu yote yapo mikononi mwake.
Yeye ndiye anaye kutoeni roho. Na Yeye ameniamrisha niwe katika wanao muamini
Yeye.
105. Ewe Nabii! Simama sawasawa, umuelekee
Mwenyezi Mungu vilivyo. Wala usijitie katika miongoni mwa walio mshirikisha
Mwenyezi Mungu. Epukana nao, na uwe mbali nao, wewe na Waumini wanao kufuata.
106. Wala usimkimbilie kwa kumwomba na
kumuabudu yeyote asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Hao hawakuletei manufaa wala
madhara. Ukifanya hayo inakuwa umekwisha ingia miongoni mwa washirikina walio
dhulumu. Na anayo katazwa Nabii, ndio wanakatazwa umma wake wote. Na hivyo ndio
ukomo wa kukanya. Kwani kumkanya ambaye hayumkiniki kutenda anacho kanywa, ndio
hadi ya kukanya.
107. Ewe Nabii! Yakikusibu madhara kutoka kwa
Mwenyezi Mungu, hapana wa kuyaondoa ila Yeye. Na akikujaalia kheri hapana anaye
weza kukunyima yeyote. Kwani yeye anagawa kheri kuwapa waja wake kwa fadhila
yake. Na Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa maghfira, Mkuu wa rehema.
108. Ewe Mtume! Fikisha wito wa Mwenyezi Mungu
kwa watu wote! Na waambie: Enyi watu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteremshieni
Sharia ya Haki kutokana naye. Anaye taka kuongoka basi afanye haraka. Kwani
faida ya uwongofu wake utamrejea mwenyewe. Na mwenye kushikilia upotovu
utamuangukia mwenyewe. Na mimi sikuwakilishwa nikulazimisheni muamini, wala
kukutawalini.
109. Ewe Mtume! Thibiti
juu ya Dini ya Haki. Na fuata wahyi ulio teremshiwa, nawe uwe na subira kwa
maudhi yanayo kufika kwa ajili ya Njia ya Da'wa (Wito), mpaka Mwenyezi Mungu
ahukumu baina yako na wao, kwa vile alivyo kuahidi kuwa atawapa ushindi Waumini,
na watahizika makafiri. Na Yeye ndiye mbora wa mahakimu. >