1. Nabii Muhammad (s.a.w.)
katolewa Makka na kalazimishwa kuihama kwa sababu ya vitimbi vya mapagani,
washirikina, na kwa kuazimia kwao kumuuwa, ili Waislamu wapate kuwa na dola yao.
Naye akenda kukaa Madina kwenye amani na manusura. Huko ikawa hapana budi ila
kuwania kujilinda na uvamizi wa maadui, wasije wenye Imani wakapata mateso.
Vikatokea hivyo Vita vya Badri. Waumini wakapata ushindi ulio wazi na ngawira
nyingi waliziteka. Ikatokea khitilafu kidogo na suala katika shauri la ugawaji
wa hizo ngawira. Ndio hivyo Mwenyezi Mungu anasema: Wanakuuliza khabari ya
ngawira, zende wapi? Apewe nani? Ni za nani? Zigawanywe vipi? Ewe Nabii!
Waambie: Hizo ngawira ni za Mwenyezi Mungu kwanza. Na Mtume, kwa amri ya Mola
wake Mlezi, ndiye mwenye madaraka ya kuzigawa. Basi wacheni kukhitalifiana kwa
ajili ya hayo. Na uwe mtindo wenu ni kumkhofu Mwenyezi Mungu na kumt'ii. Na
tengenezeni yaliyo baina yenu, na mfanye mapenzi na uadilifu ndio makhusiano
baina yenu. Kwani hakika hizi ndizo sifa za watu wa Imani.
2. Ama hakika Waumini wa haki na
kweli daima wanakuwa na khofu na ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu. Akitajwa Allah
Subhanahu, Mwenyezi Mungu Aliye takasika, nyoyo zao hufazaika, na zikajaa khofu.
Kwa hivyo kila wakisomewa Aya za Qur'ani Imani yao inazidi kuwa imara, na wao
huzidi unyenyekevu na ujuzi, na wala hawamtegemei yeyote ila Mwenyezi Mungu
aliye waumba, na ndiye anaye walinda na kuwaendeleza.
3. Na hao Waumini walio wa kweli
katika Imani, wanashika Sala kwa kutimiza nguzo zake, na kukamilisha unyenyekevu
na ut'iifu, ili wawe daima katika kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na wanatoa katika
mali aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, kwa ajili ya Jihadi, na
mambo yote ya kheri, na kuwasaidia wanyonge.
4. Hakika hawa wanao sifika kwa
sifa hizi ndio khasa wanao sifika kwa Imani kwa haki na kweli. Na malipo yao ni
kupata vyeo vya ngazi ya juu kwa Mwenyezi Mungu. Yeye Allah Subhanahu ndiye
ataye wapa radhi zake, na maghafira wanapo teleza, na duniani atawapa riziki
njema, na Akhera neema ya daima.
5. Ushindi, bila ya shaka, upo
mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Na funguo za mambo yote ziko kwake. Na hali ya
Waumini katika kukhitalifiana kwao katika mambo ya ngawira ni kama hali yao pale
alipo kuamrisha Mwenyezi Mungu utoke ukapigane na washirikina katika Badri, nayo
ni Haki iliyo thibiti. Kwani miongoni mwa Waumini kulikuwapo na kikundi kilicho
chukia vita kweli kweli.
6. Wanajadiliana nawe hao wa
kikundi hicho, na wanajaribu kutilia nguvu kauli yao katika jambo la haki, nalo
ni kutoka kwa ajili ya Jihadi. Na kumbe wao walikuwa na wenzao walio toka kwenda
kupokonya mali ya Makureshi yaliyo kuwa yanakwenda Sham, na wasiyapate. Kikundi
hichi kikakhiari kurejea baada ya kuona wamenusurika, kwa kujuvywa na
Mtume, na kwamba makafiri wanawaogopa, na kwa kuwa hadi wakivichukia vita, na
kuwa hawajui litalo wapata. Na walipo kuwa wakiviendea vita walikuwa kama wanao
sukumwa kwenda kufa, na wao wanaona kitacho wauwa, na yanawapata mateso yake.
7. Enyi Waumini! Kumbukeni ahadi ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu kwenu kwamba atakupeni ushindi juu ya moja katika makundi mawili,
hilo lenye silaha na nguvu. Na hali nyinyi mnapendelea kupambana na hilo kundi
jengine lenye mali na watu tu. Na hilo ni msafara wa Abu Sufyan. Nanyi mkakhiari
mali yasiyo kuwa na wapiganaji. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka
kuithibitisha Haki kwa mapendo yake na uwezo wake na kwa maneno yake yaliyo
kwisha tangazwa, na ili aung'oe kabisa ukafiri katika Bara Arabu kwa ushindi wa
Waumini.
Aya hizi tukufu zinatoa sura ya yanayo pita katika nafsi wakati
wa vita, nako ni kutamani kukutana na maadui wachache na kuchukia kukutana na
wengi, na kupenda kuteka mali na ngawira; na ilhali Mwenyezi Mungu Mtukufu
anataka kuitukuza Dini na ishinde Haki na wang'oke makafiri.
8. Ili athibitishe Haki, na
auondoe upotovu, hata wakichukia makafiri ambao wamedhulumu Haki ya Mwenyezi
Mungu na Haki ya Waumini na Haki ya nafsi zao wenyewe.
9. Na enyi Waumini! Kumbukeni nanyi mnagawana
ngawira na mnakhitalifiana, mlipo omba uwokovu na msaada, na mkaandikiwa kuwa
hapana la kukuepusheni na vita. Mwenyezi Mungu alikuitikieni maombi yenu,
akakuungeni mkono kwa kukuleteeni (Malaika) Roho zilizo safi nyingi zinazo fika
elfu zinazo fuatana, zikija moja baada ya moja.
Walipo jua wapiganaji
Waumini kuwa hapana njia ya kuepukana na vita wakaomba msaada kwa Mwenyezi
Mungu, naye Mwenyezi Mungu Mtukufu akawaitikia, na akawaunga mkono kwa Malaika
elfu walio fuatana. Yaani alianza kwa kupeleka msaada kwa vikosi vilivyo fuatana
ili iwe wepesi kwa kila kikosi kuelekea pahala pake katika vita pasiwepo kukaa
bure au kupigana makumbo. Na ifikapo misaada ya majeshi ya vita roho hufurahi na
moyo huingia nguvu. Na hayo ndiyo aliyo yakusudia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa
kauli yake: "Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo
zenu zituwe." Na ushindi daima unatokana na Mwenyezi Mungu.
10. Wala Mwenyezi Mungu
Mtukufu hakujaalia huko kukuungeni mkono kwa (Malaika) hizo Roho safi ila ni
kuwa ni kukupeni khabari njema, kama bishara kwenu kuwa mtashinda, mpate kutua
nyoyo na msonge mbele. Na Mwenyezi Mungu anakusaidieni, na wala ushindi hauji
ila kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye kushinda, ambaye anaye
panga mambo kwa pahala pake kwa mujibu wa ujuzi wake usio pitikiwa na chochote.
11. Enyi Waumini! Kumbukeni wakati mlipo ingiwa
khofu kwa upungufu wa maji, na kuwaogopa maadui. Mwenyezi Mungu alikupeni
utulivu, kwa kukuleteeni usingizi, mkalala mkatua. Akakuteremshieni maji kutoka
mbinguni mkajisafishia, na mkauondoa wasiwasi wa Shetani, na nyoyo zenu zikawa
imara kwa msaada wa Rahmani na pia ardhi ikashikamana kwa hayo maji, na miguu
yenu ikaweza kukanyaga bila ya kudidimia katika mchanga.
Aya hii
inaashiria fadhila ya Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya wapiganaji Waumini kwa
kupatikana hali ya amani kwa kupumzika kwa usingizi, na kuteremka mvua kwa
kujitahirisha na kukoga, na kushikamana mchanga kwa kuwepo maji, basi nyayo
zikasimama imara. Inajuulikana kuwa mchanga laini unawaletea taabu wapiganaji na
unakuwa pingamizi katika kwenda huku na huko ambako ni katika dharura za vita
muhimu. Na aya ya pili inaeleza maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaambia
Malaika wawathibitishe Waumini na watie khofu katika nyoyo za makafiri. Na ni
maarufu kuwa khofu ikiwatawala askari katika midani huwaletea kuemewa. Na katika
Aya hii tukufu panaashiriwa pahali pa kupiga napo ni juu ya shingo na kuvikata
vidole vinavyo kamata silaha mkononi.
12. Enyi Waumini!
Kumbukeni pale Mwenyezi Mungu alipo wafunulia wale wenye Roho zilio t'ahirika,
yaani Malaika, watie ndani ya nyoyo zenu kuwa Mimi ni pamoja nanyi, nakuungeni
mkono, na ninakusaidieni, kwa kuwaambia: Zitieni nguvu nyoyo za walio amini,
wait'ii Haki na wapigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mimi nitaifanya
khofu izitawale nyoyo za washirikina, nao watakuogopeni. Nanyi enyi Waumini!
Wapigeni vichwani mwao vilio juu ya shingo zao, na kateni vidole vyao vinavyo
kamata panga.
13. Ukawa ushindi na
kuungwa mkono nyinyi, na kwao ni kitisho na fazaa, kwani wao walikuwa upande
mmoja, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake walikuwa upande mwengine, kwa kuwa
wao walimpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi ndio Mwenyezi Mungu
anawateremshia adhabu chungu. Na adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.
14. Enyi Waumini! Hivyo
ndio vita, basi vionjeni, na muwe na yakini kuwa mtapata nusura na kuungwa
mkono. Na wanao pinga Ishara za Mwenyezi Mungu watapata adhabu nyengine Siku ya
Kiyama, nayo ni adhabu ya Moto.
15. Enyi mlio isadiki Haki
na mkait'ii! Mkikutana na wale walio kufuru katika uwanja wa vita nao
wanakujieni kwa wingi wao, msiwakimbie mkazipa mgongo panga zao.
16. Na asiye wakaabili uso
kwa uso, basi Mwenyezi Mungu amekasirika naye, na marejeo yake ni Motoni. Na huo
ndio mwisho muovu kweli. Na mwenye kuacha kuwakaabili kwa kuwa ni hila na mbinu
za vita, au kaacha kikosi kwenda jiunga na kikosi kingine cha Waumini apate kuwa
na nguvu zaidi za mpambano, huyo hana dhambi.
17. Na nyinyi Waumini,
pale mnapo washinda, na mkawauwa mlio wauwa katika wao, basi hakika si nyinyi
mlio wauwa kwa nguvu zenu, lakini ni Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliye kupeni
ushindi na kuweza kuwauwa, kwa msaada wake kwenu na kutia khofu katika nyoyo
zao. Na wewe Mtume, pale ulipo warushia mchanga na kokoto nyusoni mwao
kuwafazaisha, si wewe ulio rusha, lakini ni Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliye
rusha, na wao wakafazaika. Na hayo Mwenyezi Mungu ameyafanya kuwaneemesha
Waumini kwa neema njema. Katika hayo pana majaribio ya nguvu kwao, ili ionekane
ikhlasi yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mambo yao, Mwenye kusikia
maneno yao, na Mwenye kujua mambo ya maadui zao na kauli zao pia.
18. Huo ndio ushindi
mkubwa, na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kudhoofisha kila hila za makafiri.
19. Ikiwa nyinyi
washirikina mlikuwa mkining'inia mapazia ya Al Kaaba na huku mnaomba
yapambanuliwe baina yenu na Waumini ijuulikane haki ipo wapi, basi sasa
imekwisha kujieni hukumu ya kupambanua, na ushindi si wenu, bali ni wa Waumini.
Na nyinyi mkirejea tena kufanya uadui Nasi tutakushindeni tena. Wala kukusanyika
kwenu kwa ajili ya madhambi hakutakufaeni kitu! Hata ikiwa idadi yenu kubwa
vipi! Kwani hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao isaidiki Haki na
wanaikubali.
20. Enyi mlio isadiki
Haki, na mkaifuata! Hakika mmejua ushindi umepatikana kwa msaada wa Mwenyezi
Mungu na kumt'ii Mtume wake. Basi endeleeni kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume.
Wala msiupuuze wito wa Mtume anao itia Haki, nanyi mnamsikia na mnafahamu
ayasemayo.
21. Wala msiwe kama
wanaafiki wanao sema: Tumeisikia Haki na tumefahamu. Lakini hawaifuati wala
hawaiamini. Basi wamekuwa kama wasio sikia.
22. Hao washirikina na
wanaafiki ni kama wanyama waovu kabisa walio sibiwa na uziwi, kwa hivyo
hawasikii; na wakasibiwa na ububu, kwa hivyo hawasemi. Basi wao ni viziwi
kwa Haki, na hivyo hawasikii, wala hawaitamki na hawaielewi!!
23. Na Mwenyezi Mungu kwa
ilimu yake ya tangu na tangu lau angeli ona ndani yao kuwa, katika hali
yao hivi sasa, itakuja patikana kheri yoyote kwao hao kwa nafsi zao, na kwa
watu, na kwa Haki, basi angeli wafanya wasikie kusikia kwa kuongoka hata Haki
ikaingia akilini mwao. Na hata wangeli isikia na wakaifahamu Haki basi bado
wasingeli ifuata. Na mapuuza hayawaachi kwa kuzidiwa na pumbao.
24. Enyi mlio isadiki
Haki na mkaifuata! Muitikieni Mwenyezi Mungu kwa kufikisha anayo kuamrisheni. Na
muitikieni Mtume katika vile anavyo fikisha anayo yaamrisha Mwenyezi Mungu, pale
anapo kuiteni Mtume kufuata amri za Mwenyezi Mungu ambazo zitakuleteeni uzima wa
miili yenu, na roho zenu, na akili zenu, na nyoyo zenu. Na mjue kwa yakini kuwa
Mwenyezi Mungu ni Mwenya kuangalia nyoyo zenu. Huzielekeza atakavyo. Basi Yeye
huingilia baina yenu na nyoyo zenu zinapo ingiliwa na matamanio, Yeye basi
hukuokoeni nayo ikiwa nyinyi wenyewe mnajielekeza kwenye Njia iliyo nyooka. Na
nyinyi nyote mtakusanywa kwake Siku ya Kiyama, na huko ndiko malipo yatakuwa.
25. Na jikingeni na
Dhambi kubwa ya kufisidi jamii yenu, kama vile kuacha kwenda kwenye Jihadi, na
kufarikiana mkagawana mapande mapande, na kama kuacha kuamrisha mema na kukataza
maovu. Kwani Fitna hiyo, Dhambi hiyo, haiwapati wale walio dhulumu peke yao,
bali inawapata wote. Na mjue kuwa bila ya shaka kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu ni
kali hapa duniani na Akhera pia.
26. Na hebu kumbukeni,
enyi Waumini, katika hali ya kuwa mna nguvu, pale mlipo kuwa wachache na
wanyonge. Maadui walikudhilini kwa unyonge wenu, nanyi mlishikwa na khofu wasije
maadui zenu kukunyakueni. Basi tena mkahama kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na
makaazi yenu yakawa Yathrib (Madina). Na mkapata manusura kwa msaada wa Mwenyezi
Mungu na tawfiki yake, na akakuruzukuni ngawira njema kutaraji mtashukuru kwa
neema hii, na muendelee katika Njia ya Jihadi kulinyanyua Neno la Haki.
27. Enyi mlio isadiki
Haki mkaifuata! Haikufaliini kumkhini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kufanya
urafiki na maadui wa Haki, na kukhuni katika ngawira, au kwa kuacha kwenda
kwenye Jihadi. Wala msikhuni amana mnazo pewa nanyi mnajua amri na makatazo
yake.
28. Enyi Waumini, wenye
kusadiki! Jueni kuwa fitna ya nafsi zenu inatokana na kupita mpaka katika
mapenzi yenu kwa watoto wenu na mali yenu. Basi isiwe kupenda kwenu kuyapenda
mali na wenenu yakazidi kuliko mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hayo
yatakuharibieni mambo yenu. Na jueni kuwa malipo ya Mwenyezi Mungu yanakutosheni
kuliko mali na watoto.
29. Enyi mlio isadiki
Haki na mkaifuata! Mkizinyenyekea amri za Mwenyezi Mungu kwa siri na
dhaahiri, Mwenyezi Mungu atakujaalieni katika nafsi zenu uwezo wa kupambanua
baina ya Haki na upotovu, na atakutunukieni ushindi wa kutenga baina yenu na
maadui zenu, na atakusitirieni maovu yenu yaondoke, naye akusameheni. Na Yeye
Subhanahu daima ni Mwenye fadhila kubwa.
30. Na kumbuka ewe Nabii,
neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yako, pale washirikina walipo panga njama
kukutia nguvuni - ama wakufunge, au wakuuwe, au wakutoe mji! Hakika walikupangia
mipango miovu! Na Mwenyezi Mungu Mtukufu alikupangia utokane na shari yao. Na
mpango wa Mwenyezi Mungu ndio wa kheri, na una nguvu zaidi, na ndio wenye
kushinda.
31. Na ewe Nabii! Kumbuka
inda ya washirikina ulipo kuwa ukiwasomea Aya za Qur'ani Tukufu, nazo ni Ishara
zetu. Ujahili wao na ghururi yao iliyo pita kiasi iliwapelekea kusema: Tungeli
taka kusema kama isemavyo hii Qur'ani tungeli sema; kwani humu hamna chochote
ila visa walivyo viandika watu wa kale!
32. Na kumbuka, ewe
Nabii, vipi walivyo kuwa wanakupinga na kumpinga Mwenyezi Mungu hata kwa inda
yao wakasema kumwambia Mwenyezi Mungu, Mola wao Mlezi: Ikiwa haya unayo kuja
nayo ni mambo madhbuti, basi zijaalie mbingu zitunyeshee mawe, au tuletee adhabu
yoyote iliyo kali yenye uchungu!
33. Si katika hikima ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaadhibu katika dunia kwa adhabu kali na hali wewe upo
miongoni mwao unaitia Haki, nawe unataraji asaa wataitikia. Wala si mtindo wa
Mwenyezi Mungu kuwaadhibu wenye kuasi nao wangali wanamuomba maghfira na wamo
kuyavua yale waliyo nayo.
34. Hakika hali yao iliyo
sasa inaruhusu kuwaadhibu, kwani wanawazuia watu wasiutumie Msikiti ambao
Mwenyezi Mungu ameutukuza kwa kuharimisha vita karibu yake. Lakini Mwenyezi
Mungu anawaakhirisha kwa alivyo wakadiria katika ujuzi wake kuwa wengi wao
watakuja amini. Wao wakati huu wa sasa sio walinzi wa kuunusuru huo Msikiti
Mtukufu, bali wao wameunajisi kwa kutia ibada ya masanamu ndani yake. Ama wa
kuunusuru hakika ni Waumini, wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu. Lakini wengi katika
washirikina hawaijui Dini, wala hawajui cheo cha Nyumba hiyo Tukufu.
35. Na maombi yao kwenye
Nyumba hii Tukufu (Al Kaaba) si chochote ila ni kupiga myunzi na makofi. Ilivyo
kuwa hiyo ndiyo hali yenu, basi wacha mauti yakupateni, na yaonjeni katika
uwanja wa vita, upate kubaidika ushirikina kutokana na Al Kaaba. Na kuuliwa huko
kwenu ni kwa sababu ya ukafiri wenu.
36. Hakika hao wanao
zipinga Ishara za Mwenyezi Mungu na wanamshirikisha na miungu mingine, hutoa
mali yao ili wawazuie watu wasiifuate Imani ya Haki! Nao wataendelea kutoa hayo
mali, kisha hayo mali, kwa kuwapotea bure bila ya pato walitakalo, yatawaletea
majuto na machungu. Na katika uwanja wa mpambano watashindwa hapa duniani, na
kisha watakusanywa wote katika Jahannam, wakibaki na ukafiri wao.
37. Kwa kushindwa
makafiri duniani na kuadhibiwa Motoni Akhera Mwenyezi Mungu anapambanua aliye
khabithi wa roho na vitendo na maneno, awe mbali na aliye mwema wa roho yake na
moyo wake. Na awafanye wale waovu makhabithi wapandane wenyewe kwa wenyewe, huyu
juu ya huyu, na awatie Motoni Siku ya Kiyama. Na hao washirikina mafisadi ndio
wenye kukhasiri peke yao, duniani na Akhera.
38. Hakika juu ya vitisho
hivi, mlango wa matarajio ungali wazi. Basi ewe Nabii wa rehema! Waambie hawa
wapinzani kuwa wakikoma, wakaacha inadi yao na ushirikina wao, basi hapana shaka
Mwenyezi Mungu atawasamehe vile vitendo vyao vilivyo kwisha pita. Na wakiendelea
na upotovu wao, na wakarudia tena kukupigeni vita, basi mwendo wa Haki kwa walio
tangulia umethibiti utakuwa ule ule, nao ni kuwa Haki lazima iushinde upotovu,
pindi ikiwa wale watu wa Haki wakishika ut'iifu na njia za ushindi.
39. Na endeleeni kuwapiga
vita washirikina mpaka waache kuharibu itikadi za Waumini kwa kuwatesa na
kuwaudhi. Wakiacha ukafiri na kuwaudhi Waumini, na wakamsafia Dini Mwenyezi
Mungu, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvijua vitendo vyao, na atawalipa kwavyo.
40. Na wakiendelea na
kupuuza kwao na kuwaudhi Waumini, basi enyi Waumini, jueni ya kuwa nyinyi mko
katika ulinzi wa Mwenyezi Mungu, na huo ndio ulinzi wenye kupendeza na wenye
nguvu kabisa. Na Yeye ndiye Mwenye kukunusuruni, na nusura yake ndio yenye nguvu
zaidi na bora zaidi.
41. Na enyi Waislamu!
Jueni kuwa katika mali ya makafiri mliyo yateka, hukumu yake ni kugawiwa mafungu
matano. Fungu moja ni la Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa zake Mtume, na
mayatima, nao ni watoto wadogo wa Waislamu waliofiwa na baba zao nao ni
mafakiri; na masikini, nao ni wale Waislamu wenye haja; na msafiri, naye ni
mwenye kukatikiwa safari yake ya halali. Na yaliyo khusishwa katika hiyo sehemu
moja katika tano kuwa ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume hukhusishwa kwa maslaha ya
umma kama anavyo pasisha Mtume katika uhai wake, au, baada ya kufa kwake, Imam.
Na yaliyo baki katika ile Khumsi watapewa walio kwisha tajwa. Ama sehemu nne
nyengine katika ghanima (ngawira), na Aya ikanyamaza kimya juu yake, ni za wale
walio pigana. Basi jueni hayo, na myajue ikiwa mmemuamini Mwenyezi Mungu kweli,
na mmeziamini Ishara tulizo mteremshia mja wetu, Muhammad, za kumthibitisha na
kumsaidia, siku ya Mpambanuo, tulipo pambanua baina ya ukafiri na Imani, nayo
ndiyo siku lilipo kutana kundi lenu na kundi la makafiri katika Badri. Na
Mwenyezi Mungu Mwenye kudra kubwa juu ya kila kitu aliwapa ushindi Waumini juu
ya uchache wao, kuwashinda makafiri juu ya wingi wao.
42. Na kumbukeni mlipo
kuwa bondeni ng'ambo hii ya karibu na Madina, na wao makafiri wako ng'ambo ile
ya mbali, na msafara wenye bidhaa mlio kuwa mnautaka uko karibu zaidi nanyi
upande wa baharini. Na lau kuwa mmepeana miadi ya kukutana kwa kupigana
basi msinge wafikiana hivyo. Lakini Mwenyezi Mungu kapanga mkutane bila ya
miadi, na bila ya kutaka wao, ili apate kutekeleza jambo ambalo katika ujuzi
wake limekwisha thibiti litokee tu, wala hapana jenginelo. Jambo lenyewe ni kuwa
vitokee vita vitavyo pelekea nyinyi mshinde na wao washindwe. Ipate kuondoka
shaka - wateketee wa kuteketea kwa hoja wazi ya kuonekana, nako ni kushindwa
makafiri juu ya wingi wao; na wahuike Waumini kwa hoja iliyo wazi, nako ni
kushinda kulio toka kwa Mwenyezi Mungu kuwapa Waumini wachache. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusikia na kujua. Haimfichikii kauli wala niya yoyote ya pande
zote mbili.
43. Na kumbuka, ewe
Mtume! Pale Mwenyezi Mungu alipo kufadhili kwa kukuonyesha usingizini ndoto ya
kuwa hilo jeshi la maadui ni dogo, ili akutulizeni nyoyo muamini kuwa
mtawashinda, kwa hivyo muwe imara kuwakaabili. Na lau angeli kuacheni muwaone
wengi, bila ya kukuthibitisheni kwa ndoto hiyo, mngeli waogopa, na mkasita sita
kupigana nao, na mngeli emewa, na mkazozana msonge mbele au mrudi. Lakini
Mwenyezi Mungu amekuvueni na hayo, na akakuokoeni na matokeo yake, kwani hakika
Yeye ni Mwenye kuyajua vyema yaliyomo ndani ya vifua vya watu.
44. Na kumbuka, ewe
Mtume! Alipo kuonyeshemi Mwenyezi Mungu kuwa maadui zenu mnapo kutatana
nao ni wachache katika macho yenu, kama alivyo waonyesha wao kuwa nyinyi ni
wachache, na kwa kuwa tangu hapo wao wana ghururi ndani ya nafsi zao kuwa ni
wengi, ili kila mmoja wenu awanie kupigana na mwenzie, na kwa hivyo yatimie
aliyo kwisha yaamrisha Mwenyezi Mungu. Na ilikuwa hapana budi hayo yatimie. Na
kwa Mwenyezi Mungu ndio hurejea mambo yote ya ulimwengu. Halitendeki jambo
ila alilo kwisha lihukumia na kuzitengeneza sababu zake.
45. Enyi mlio amini!
Mkikutana na kikosi cha wapiganaji katika adui zenu, basi kuweni imara, wala
msiwakimbie. Na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa kufuata uwezo wake, na ahadi yake
ya kuwasaidia Waumini, mkikithirisha kumkumbuka na kumtaja pamoja na kuwa imara
na kusubiri. Mkifanya hivyo ndio matarajio yenu ya kupata mafanikio yatapo
timia.
46. Na mt'iini Mwenyezi
Mungu na Mtume wake katika mambo mlio amrishwa na mlio katazwa. Na wacheni
kuzozana na kukhitalifiana. Hayo ndiyo yanayo pelekea kupoteza nguvu na
kushindwa. Na vumilieni mkipata shida za vita. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja
na wanao vumilia wakasubiri kwa kuwapa msaada na kuwaunga mkono, na kuwalipa
malipo mema.
47. Wala msiwe kama wale
walio toka kwenye majumba yao, nao wana ghururi (udanganyifu) kwa nguvu na neema
walizo nazo, wakijifakhari na kujionyesha mbele za watu, wakitaka wasifiwe kwa
ushujaa na ushindi, na wao huku wanapinga watu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na
wanaupinga Uislamu. Na Mwenyezi Mungu amevizunguka vitendo vyao kwa ujuzi na
uwezo. Na Yeye atakuja walipa duniani na Akhera.
48. Na kumbukeni, enyi
Waislamu! Pale Shetani alipo kuja kuwazaini hawa washirikina kwa kuwaonyesha
kuwa wayatendayo ni mazuri kwa uchochezi wake, akiwaambia: Hapana mtu ye yote
anaye weza kuwashinda. Na akawahakikishia kuwa yeye atawalinda, na kuwanusuru!
Yalipo kutana makundi mawili katika vita, vitimbi vyake na uchochezi wake
ukavunjika. Akarejea nyuma, na akajitoa nao, akaogopa Mwenyezi Mungu
asimuangamize. Na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
49. Na kumbuka ewe Mtume!
Walipo sema wanaafiki miongoni mwa makafiri na wale wenye Imani dhaifu walipo
kuoneni mmesimama imara: Hawa Waislamu wameghurika kweli na dini yao! Na hakika
mwenye kumwakilisha Mwenyezi Mungu jambo lake, na akamuamini Yeye, na
akamtegemea Yeye, basi hapana shaka kuwa Mwenyezi Mungu atamkifia amwondolee
hamu yake, na atamnusuru na maadui zake. Kwani hakika Mwenyezi Mungu madaraka
yake yana nguvu, naye ni Mwenye hikima katika mipango yake.
50. Na lau kuwa
unaona, ewe Mtume, kile kitisho kikubwa, kinacho wateremkia hawa makafiri,
wakati ule Malaika wanapo wafisha na kuwang'oa roho zao, nao wakiwapiga mbele na
nyuma, na wakiwaambia: Onjeni adhabu ya Moto kwa sababu ya vitendo vyenu viovu!!
51. Na hakika Mwenyezi
Mungu si mwenye kuwadhulumu waja wake kwa kuwaadhibu kwa madhambi waliyo
yatenda. Bali huo ni uadilifu, kwa sababu hawawi sawa muovu na mwema. Basi
kuadhibiwa kwake ni kwa vitendo viovu alivyo vitenda mwenyewe.
52. Hakika ada ya hawa
washirikina, na shani yao katika ukafiri, ni kama shani ya Mafirauni na majabari
wote walio baki walio kuwa kabla yao. Walizipinga Ishara za Mwenyezi Mungu, basi
Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa madhambi yao. Wala Yeye si mwenye kuwadhulumu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu katika kutekeleza hukumu yake, na Mkali wa
kumlipa anaye stahiki adhabu.
53. Na huu ni uadilifu
katika kulipa, kwa sababu Mwenyezi Mungu hakika haibadilishi neema anayo
waneemesha watu, kama vile neema ya amani, kutononoka, na afya, mpaka wao
wenyewe waigeuze hali yao na sababu zake! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia
wayasemayo, na Mwenye kuyajua wayatendayo.
54. Kama ilivyo kuwa ada
yao na mtindo wao hawa katika kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na neema zake
ni kama mtindo wa watu wa Firauni na walio watangulia, hali kadhaalika ada yao
na shani yao katika kuendelea kuwakadhibisha Mitume wake, na dalili za Unabii
wao, ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla yao. Basi wamefanana hao
katika kukanusha Ishara, na kuupinga Utume wa Mitume, na kuwakadhibisha, na
kuendelea juu ya mwendo huo vile vile. Na kila mmoja Mwenyezi Mungu amemtia
mkononi kwa dhambi zake -wale kwa midharuba, na vimbunga, na kadhaalika; na watu
wa Firauni kwa kuwazamisha. Na wote walikuwa ni madhaalimu wa nafsi zao. Kwa
hivyo walistahiki adhabu iliyo wafika.
55. Hakika katika vyote
vilio enea juu ya uso wa ardhi walio waovu mno mbele ya Mwenyezi Mungu
katika hukumu yake na uadilifu wake, ni makafiri walio kakamia juu ya ukafiri
wao,
56. Nao ni wale
ulio fungamana nao kwa mikataba, nao wakawa hawaachi kuivunja kila mara; na watu
hao ni Mayahudi ambao hawachelei utukufu wa Mwenyezi Mungu, wala hawakhofu
kupatilizwa naye, wala adhabu yake.
57. Basi ewe Mtume! Ukiwakuta hawa wavunjao
mapatano, na ukasadifiana nao katika vita nawe umeshinda, basi watishe
baraabara kwa kuwapa adhabu ya kuwatia uchungu na kuwaogopesha wale walio nyuma
yao, upate kuwafarikisha walio baki. Mateso haya ndiyo ya kuwakumbusha
uovu wa kuvunja mapatano, na kuwazuia wenginewe wasitende kama hayo.
Katika Aya tukufu hizi tunahadharishwa na wale wanao toa ahadi na kisha
wakazivunja. Hawa yafaa wapewe adhabu ya kutia mfano kwao na kwa walio nyuma
yao. Na katika Aya hii unabainishwa umuhimu wa kuvuruga askari wa adui walio
nyuma. Hizi ni mbinu za vita za kisasa, kwani kuzua vurugo katika askari wa
nyuma hutosha kuleta fujo na kupelekea jeshi kutawanya askari wake kulinda
mgongo wake, na kwa hivyo zinavunjika nguvu zake.
Juu ya hivyo katika
sehemu za nyuma katika midani ndio huwapo mambo yaliyo khusu idara ya jeshi
ambayo juu yake ndio jeshi linategemea kwa msaada. Ukileta vurugu hapa hupelekea
kukosekana nidhamu yote ya jeshi, na kwa hivyo ndio huleta kuemewa na
kushindwa.
58. Na ukiona alama za
hao watu kutaka kuleta khiana kuvunja maagano yaliyo baina yako na wao, ikate
njia yao wasiweze kukukhuni, kwa kuwatangazia wewe kuvunja hayo mapatano, mpaka
walijue jambo lako, na wasiweze kukukhuni. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi
makhaini, wala haridhii kuwa nyinyi msifike kwa sifa yao.
59. Wala wasidhani walio
kufuru kuwa wamekwisha tangulia na wameiepuka adhabu ya kukhuni kwao na kwenda
kinyume! Wao kabisa hawatamshinda Mwenyezi Mungu asiwazunguke na kuwatia
nguvuni, bali Yeye peke yake ni Muweza, na atawalipa kwa nguvu zake na uadilifu
wake.
60. Enyi Umma wa Kiislamu! Tayarisheni kila
muwezavyo nguvu za vita za namna zote kwa ajili ya kujizatiti kwa ajili ya
kupigana, na wekeni askari walinzi na farasi wao mipakani na kando kando
ya nchi, ili kwa hivi mjitayarishe na ulinzi mwatie kiwewe adui za
Mwenyezi Mungu na adui zenu miongoni mwa hao makafiri ambao wamo kungojea
likupateni jambo. Na pia mpate kuwatishia wenginewe ambao nyinyi
hamwajui hivi sasa, lakini Mwenyezi Mungu anawajua, kwani
hapana jambo linalo jificha kwake. Na kila mnacho kitoa kwa kuzitayarisha nguvu
zenu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi Yeye atakulipeni malipo ya kutosha, bila
ya kupunguka hata chembe katika mnayo stahiki katika fadhila ya Mola wenu Mlezi
Katika Aya hii tukufu pana kuhimizwa na kuamrishwa kujitayarisha kwa
ajili ya kupambana na adui. Kwani vita, zamani na sasa, ni jambo la khatari na
muhimu kabisa. Juu yake inategemea kheri na shari, kufa kupona kwa umati na
umati. Basi yapasa kujitayarisha, kujizatiti, na kujitengeneza kwa jiha mbali
mbali za vifaa na silaha na zana. Kuingia vitani bila ya kujipatia zana
zote na kujitayarisha ni kutafuta kushindwa. Na tunaona hivi sasa madola yanavyo
jiandaa wakati wa amani na vita, na yanavyo jenga siasa zao na mipango yao na
wanavyo kusanya uwezekano wao wote ili wapate ushindi katika vita. Na vita sasa
havimsazi mtu. Wanashiriki katika vita wanajeshi na raia. Kwa hivyo ndio inapasa
zaidi kujitengeneza kila mmoja wao kwa matengenezo ya kuwakusanya na
kuwaweka tayari wote ili upatikane ushindi.
61. Maadui wakielekea kutaka amani na kuacha
uadui wao, basi nawe ewe Mtume, elekea kwenye amani. Kwani vita sio lengo, bali
wewe unakusudia kujilinda tu na uadui wao na upinzani wao kupinga wito wako.
Basi kubali amani, na umtegemee Mwenyezi Mungu, wala usikhofu vitimbi vyao na
njama zao! Yeye Subhanahu ni Mwenye kuzisikia njama zao, ni Mwenye kuijua
mipango yao. Hapana kinacho fichikana kwake.
Huu ni msingi mkuu katika
misingi ya Uislamu, Dini ya Salama. Na leo tunasikia kila dola duniani ina nadi
Usalama, na kwa hivyo ukaundwa Umoja wa Mataifa.
62. Ikiwa hao maadui wanataka kukukhadaa na
kukufanyia ujanja kwa hivyo kuonyesha kuwa wanataka amani, basi Mwenyezi Mungu
anakutosheleza kukulinda na vitimbi vyao kwa kila upande. Kwani Yeye alikwisha
tangulia kukuunga mkono kwa kukupa ushindi pale alipo kutengenezea sababu zilizo
onekana na za siri za kutia imara nyoyo za Waumini katika Wahajiri, wahamiaji
walio toka Makka, na Ansari, wasaidizi wa Madina.
*
63. Na Mwenyezi Mungu
akawaweka pamoja kwa mapenzi baada ya mtafaruku na uadui, hata wakawa marafiki
mbele yako, wakizisabilia roho zao na mali yao kwa ajili ya wito wako. Na wewe
hata ungeli toa mali yote na vitu vyote vya nafuu viliomo duniani kwa ajili ya
kuwaunga pamoja huku, usinge weza kuyapata hayo. Kwa sababu nyoyo zimo katika
mkono wa Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye aliye waunganisha, kwa kuwaongoa kwenye
Imani na mapenzi na udugu. Hakika Yeye Mtukufu ni Mwenye nguvu na Mwenye
kushinda. Anawapangia waja wake kwa mujibu wa manufaa yao.
64. Ewe Nabii! Hakika
Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kukudhamini wewe na wenye kukufuata miongoni
mwa Waumini katika kila jambo lenye maana kwenu.
65. Ewe Nabii! Wahimize
Waumini wende vitani kwa ajili ya kulinyanyua Neno la Mwenyezi Mungu, na
wapendezeshe kwa yatayo wafwatia katika kheri ya dunia na Akhera watayo ipata,
ili nafsi zao ziingie nguvu. Nayo ikiwa wapo kati yenu watu ishirini walio
shikamana na Imani na subira na ut'iifu, basi watawashinda makafiri mia mbili.
Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio fahamu ukweli wa mambo, kwani hawana Imani,
wala subira, wala tamaa ya kupata thawabu.
66. Ilivyo kuwa ni
waajibu wenu enyi Waumini, kusubiri mnapo kutana na maadui zenu katika hali ya
kuwa mna nguvu, ijapo kuwa wamekuzidini mara kumi, sasa Mwenyezi Mungu
amekuruhusini katika hali isiyo kuwa ya nguvu, kuwa mvumilie ikiwa adui
kakuzidini mara mbili basi. Hayo ni kwa kukujua kwake kuwa hamna nguvu nyingi,
kwa hivyo mmefanyiwa wepesi na mmesahilishiwa, baada ya kuwa heba ya
Uislamu imeingia katika nafsi za makafiri. Kwa hivyo mkiwa nyinyi ni wapiganaji
mia wenye kusubiri mnaweza kuwashinda makafiri mia mbili. Na mkiwa elfu moja
mtawashinda elfu mbili, kwa Mwenyezi Mungu kupenda na kusaidia. Na Mwenyezi
Mungu yu pamoja na wenye kusubiri kwa nusura yake na kuunga mkono kwake.
67. Haimfalii Nabii
yeyote kukamata mateka, au kuchukua fidia, au kutoa bure msamaha, mpaka ashinde,
na maadui waone wameshindwa, na wawe wamepata pigo kubwa hata kuwa hawawezi tena
kupigana katika nchi. Lakini, nyinyi jamaa wa Kiislamu, mmefanya haraka
katika Vita vya Badri kukamata mateka kabla hamjatamakani mkawa imara katika
nchi. Mnatafuta manufaa ya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera, kwa
kutukuzwa Neno la Haki, na lisikushughulisheni la dunia. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye nguvu, Mwenye kushinda. Hukupangieni mambo yenu kwa mujibu wa faida yenu.
68. Ingeli kuwa hapana
hukumu iliyo kwisha tangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kumsamehe mwenye
kujitahidi japo kuwa amekosa, basi ingeli kupateni adhabu kubwa kwa papara mliyo
ifanya.
69. Basi sasa tumieni
mlicho kipata katika fidia kwa kuwa ni halali kwenu, wala si uchumi muovu. Na
mcheni Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote. Hakika Mwenyezi Mungu ni mkubwa wa
kusamehe na kumrehemu amtakaye katika waja wake pindi akirejea.
70. Ewe Nabii! Waambie
hao mateka walio angukia mikononi mwenu: Ikiwa katika nyoyo zenu ipo kheri anayo
ijua Mwenyezi Mungu, Yeye atakulipeni yaliyo bora zaidi kuliko hicho walicho
kichukua Waumini, na atakusameheni ushirikina wenu na madhambi mliyo kuwa nayo.
Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghfira na rehema kwa mwenye kutubia madhambi
yake.
71. Na pindi wakitaka
kukukhuni, kwa vile baadhi yao walivyo onyesha kumili kwenye Uislamu, pamoja na
nyoyo zao kupenda kukufanyia khiana makusudi, wewe usivunjike moyo. Mwenyezi
Mungu atakupa uwezo juu yao. Kama hapo kwanza walipo mkhini Mwenyezi Mungu kwa
kumfanyia wenzi na washirika wa kuwaabudu, na wakaikufuru neema yake, na Yeye
aliwaweza kwa kukupa ushindi juu yao katika Badri, juu ya kuwa jeshi lako ni
dogo na lao ni kubwa. Na Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye ushindi,
Muendeshaji kwa hikima yake, aliwathibitisha wakawa na nguvu waja wake Waumini
kwa nusura yake.
72. Hakika walio isadiki
Haki na wakaikubali hukumu yake, wakahama Makka, wakapigana Jihadi kwa mali yao
na roho zao, na wale walio wapa makaazi wakimbizi ugenini, wakamsaidia Mtume wa
Mwenyezi Mungu, wanapigana vita na wale wanao wapiga vita. Wanamfanyia uadui
anao wafanyia uadui. Wao kwa wao wanasaidia kuunga mkono Haki, na kutukuza Neno
la Mwenyezi Mungu. Na wale wasio hama, haijathibiti kupata ulinzi na msaada wa
Waumini, mpaka wahajiri. Lakini wakikutakeni muwanusuru na wanao wakandamiza
katika Dini, basi wanusuruni. Wakikutakeni muwasaidie dhidi ya watu ambao mna
mapatano nao, na wala hawakuvunja mapatano hayo, basi msiwakubalie. Na Mwenyezi
Mungu anayaona myatendayo, hana kinacho fichika kwake. Basi simameni kwenye
mipaka yake msije mkatumbukia katika adhabu yake.
73. Na walio kufuru wao
ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Na wao husaidiana kwa mambo ya upotovu, na
wanaungana mkono kukufanyieni nyinyi uadui. Basi nyinyi msifanye nao urafiki.
Mkikhaalifu, yaani mkenda kinyume na haya mkawafanya ni wenzenu itaingia fitna
katika safu zenu, na utakuwa uharibifu mkubwa katika nchi.
74. Na walio amini, na
wakahajiri, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio wapa
makaazi, na wakaisaidia Haki na Neno la Mwenyezi Mungu - hao ndio walio na Imani
ya kweli. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu atawasamehe, na watapata riziki kubwa
duniani na Akhera.
75. Na walio amini baada
ya wale wa mwanzo, na mwishoe wakahama nao, na wakapigana Jihadi pamoja na walio
tangulia, basi hao ni katika nyinyi, kwa mkusanyo wa Muhaajirina (Walio hama
Makka) na Ansari (walio msaidia Mtume, watu wa Madina). Hao wanastahiki ulinzi
na haki kama ziliopo baina ya nyinyi kwa nyinyi. Na walio kuwa wame
nasibiana katika Waumini - juu ya urafiki wa Imani -wana urafiki zaidi wa kuwa
ni jamaa. Basi hao wanazidiana katika mapenzi, na mali, na kusaidiana, na
kuungana mkono. Na Mwenyezi Mungu ameyabainisha hayo katika Kitabu chake.
Naye ni Mwenye kujua kila kitu.