1. Kuhimidiwa, yaani kusifiwa na kutajwa kwa wema, ni kwa Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi, na akaumba, kwa kudra yake,  giza na mwangaza, kwa manufaa ya waja wake (1), na kuambatana na hikima yake. Tena pamoja na neema zote hizi nzuri hawa makafiri wanakwenda mshirikisha Mwenyezi Mungu, na wakawafanya wengineo ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada!!
(1) Aya hii tukufu ni ishara ya ubora wa kuumba, na ubora wa kuumba unaonyesha Umoja na Upweke wa Mwenye kuumba na utukufu wake. Kwani mbingu na nyota zake, na sayari zake, na jua, na mwezi - vyote hivyo ni ushahidi wa Umoja wake. Na ardhi na viliomo ndani yake, navyo ni wanyama, mimea na visio na uhai, na milima na mabonde, na rutuba na ukame, na viliomo chini ya ardhi maadeni magumu na yanayo tiririka, na bahari na viliomo ndani yake kama lulu na vilio hai - vyote hivyo vinaonyesha Umoja wa Mwenye kuumba. Na giza la kila namna, kama giza la jabali, na bahari, na mapango, na ukungu ulio funga moja kwa moja hata mtu akiutoa mkono wake anakaribia kuwa asiouone - pia vyote hivyo vinaonyesha ujuzi usio kuwa na mfano, wa kuanzisha kuumba, wa Mwenyezi Mungu Aliye viumba. Hali kadhaalika nuru, na sababu zake mbali mbali, kama nuru ya jua, na mwangaza wa mwezi, na mwangaza wa nyota ... vyote hivyo vinaonyesha uanzishaji wa Mwenyezi Mungu wa kuumba bila ya kiigizo.
 

 2. Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuanzeni kwa kukuumbeni kutokana na udongo. Kisha akamkadiria kila mmoja wenu ana zama maalumu za uhai, kisha uhai huo unakwisha kwa kufa. Na muda maalumu ulio wekwa wa kufufuliwa kutoka kaburini uko kwake Yeye pekee. Kisha tena enyi makafiri! Mnabisha uwezo wa Mwenyezi Mungu kufufua, na kustahiki kwake peke yake kuabudiwa?

 

 3. Na ni Yeye peke yake anaye stahiki kuabudiwa katika mbingu na katika ardhi. Anajua kila mnacho kificha na mnacho kionyesha. Na anajua yote mnayo yatenda, Naye atakulipeni kwa hayo.

 

 4. Wala washirikina hawaletewi ishara yoyote katika ishara za Muumbaji wao zinazo shuhudia Umoja wake na ukweli wa Mitume wake, ila wao huikataa na kuibeza ishara hiyo, wala hawaizingatii, wala hawaitii maanani!

 

 5. Wao wameikanusha Qur'ani ilipo wajia, na ilhali hiyo ni Haki isiyo changanyika na upotovu! Basi yatawapata mateso ya duniani, na adhabu ya Akhera, kama ilivyo eleza Qur'ani. Na hapo utawabainikia ukweli wa onyo lake walilo kuwa wakilifanyia maskhara.

 

 6. Hivyo wao hawajui kuwa kabla yao tuliwaangamiza umati kwa umati?  Tuliwapa sababu za nguvu na kuselelea katika nchi tusizo pata kukupeni nyinyi, enyi makafiri. Na tuliwakunjulia riziki na starehe. Tukawateremshia mvua nyingi iliyo wanufaisha katika maisha yao, na tukaifanya mito inapita chini ya majumba yao ya fakhari. Nao basi wasishukuru kwa neema hizo. Kwa hivyo tukawaangamiza kwa sababu ya ushirikina wao na kukithiri dhambi zao.  Baada yao tukawaleta watu wengine walio bora kuliko wao.

 

 7. Ewe Nabii! Hata tungeli kuteremshia dalili ya ujumbe wako iliyo andikwa katika karatasi, na wao wakaiona kwa macho yao, na wakahakikisha kwa kuiwekea mikono yao juu yake, basi pia wangeli sema kwa chuki tu: Hichi tunacho kigusa si chochote ila ni uchawi tu.

 

 8. Tena wanasema: Tunataka Mwenyezi Mungu amteremshia Malaika huyu anaye dai Utume amsadikishe! Na lau kuwa Sisi tungeli waitikia hilo ombi lao, tukampeleka Malaika kama walivyo toa shauri, kisha wakafanya inda yao wasimuamini, basi amri ya kuwaangamiza ingesha pitishwa, tena hao wasinge pewa muhula hata chembe.

 

 9. Na lau kuwa tunge jaalia huyo wa kumuunga mkono Mtume ni Malaika kama watakavyo hao, basi tungeli mfanya katika sura ya mwanaadamu, ili wapate kumwona na kufahamiana naye. Kwani wao hawawezi kumwona Malaika katika sura yake ya asili.(1) Tena mambo yangeli watatiza na kuwadanganyikia kwa kupelekwa kwa sura ya mwanaadamu, na tungeli watia katika makosa yale yale yalio wazonga.
(1) Kauli hii inaashiria maana ambayo wenye ilimu za kisasa wanaitaja. Wenye ilimu za mambo ya kiroho wanasema kuwa roho zina mwili khafifu, mwembamba na mwepesi, mfano wa ng'amba. Nazo hazidhihiri wala hazionekani. Na hayumkiniki kuonekana roho ila zikivaa huo mwili.  Na Malaika hawana kiwiliwili. Katika viumbe vyote vya kiroho Malaika ndio khafifu kabisa kushinda vyote. Na hayumkini kuonekana ila kwa sura ya mwili. Na huu mwili ndio unakuwa kama mwanaadamu.

 

 10. Ewe Nabii! Makafiri waliwafanyia maskhara mengi Mitume wa kabla yako. Adhabu waliyo waonya nayo Mitume wao iliwazunguka hao wafanyao maskhara. Na kwanza hayo ndio waliyo kuwa wakiyakejeli.

 

 11. Ewe Nabii! Waambie hawa makafiri: Nendeni pande zote duniani, mzingatie vipi maangamio yalivyo kuwa  mwisho wa wanao wakanusha Mitume wao. Uzingatieni vyema mwisho huu na khatima hiyo.

 

 12. Ewe Nabii! Waambie hawa wapinzani: Nani Mmiliki mbingu na ardhi, na viliomo ndani yao? Wakiemewa, wape jawabu ambayo hakuna nyengineyo, nayo ni: Hakika Mwenye kuvimiliki vyote hivyo ni Mwenyezi Mungu peke yake, wala hana mshirika. Na Yeye amejiwajibishia Mwenyewe rehema kuwarehemu waja wake. Kwa hivyo hawafanyii haraka kuwaadhibu, na anakubali toba yao. Hakika, atakukusanyeni Siku ya Kiyama ambayo haina shaka. Walio zipoteza nafsi zao, na wakazipelekea kwenye adhabu katika Siku hii, ni wale ambao hawamsadiki Mwenyezi Mungu, wala Siku ya Hisabu.

 

 13. Ni vya Mwenyezi Mungu vya kila zama, kama ilivyo kuwa vyake vya kila pahala. Naye ndiye Mwenye kusikia kila la kusikiwa, na Mwenye kujua kila la kujuulikana.

 

 14. Sema ewe Nabii! Mimi simfanyi yeyote kuwa ni mungu na msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu, Allah,  tu. Yeye peke yake ndiye aliye ziumba tangu mwanzo mbingu na ardhi kwa nidhamu isiyo kuwa na kiigizo kilicho tangulia. Naye ndiye Mwenye kuwaruzuku chakula waja wake, wala Yeye hahitaji kwao chakula. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ameniamrisha niwe wa mwanzo wa kusilimu, na amenikataza kumshirikisha Yeye na yeyote mwenginewe katika kumuabudu.

 

 15. Sema: Mimi naogopa, nikenda kinyume na amri ya Mola Mlezi wangu na nikamuasi nisije nikapata adhabu ya hiyo Siku ya shida.

 

 16. Mwenye kuepushwa adhabu hii Siku ya Kiyama, basi Mwenyezi Mungu amemrehemu. Na huko ndiko kufuzu kulio thibiti, kulio wazi.

 

 17. Mwenyezi Mungu akikupatiliza kwa ovu, basi hapana wa kuliondoa hilo ila Yeye Mwenyewe. Na akikupa kheri basi hapana awezae kuirudisha fadhila yake, kwani Yeye ni Muweza wa kila kitu.

 

 18. Yeye ndiye Mwenye kushinda kwa uwezo wake, Aliye juu, juu ya waja wake, Aliye  sifika kwa hikima katika kila alifanyalo, Mwenye kuvizunguka kwa ujuzi wake vinavyo onekana na vinavyo fichikana.

 

 19. Ewe Nabii! Waambie hao wanao kukanusha na wanao taka ushahidi wa Utume wako: Kitu gani chenye ushahidi mkubwa, na chenye kustahiki kusadikiwa kuliko vyote? Kisha uwambie: Hakika Mwenyezi Mungu ndiye shahidi mkubwa kushinda wote wa kushuhudia baina yangu na nyinyi katika ukweli wa haya ninayo kuleteeni. Na Yeye ndiye aliye iteremsha hii Qur'ani ili iwe ni hoja ya ukweli wangu, nipate kukuhadharisheni nyinyi na kila itakayo mfikia khabari yake. Nayo ni hoja ya kukata, inayo shuhudia ukweli wangu. Kwani nyinyi hamwezi kuleta mfano wake! Waulize: Hivyo nyinyi mnaitakidi kuwa Mwenyezi Mungu ana miungu wenziwe? Kisha uwambie: Mimi sishuhudii hayo, wala sisemi hivyo, wala sikukubalieni kwa hayo. Hapana shaka wa kuabudiwa kwa haki ni Mungu Mmoja. Na mimi ni mbali kabisa na hayo masanamu mnayo mshirikisha Naye.

 

 20.  Tulio  wapa  Vitabu  vya  mbinguni, Mayahudi na Wakristo, wanamjua vyema Muhammad na ukweli wa Utume wake kutokana na hivyo Vitabu vyao vya Biblia, kama wanavyo wajua watoto wao. Walio zipoteza nafsi zao hawayakubali yale wanayo yajua. Kwa hivyo hao hawaamini.

 

 21. Na hapana mtu aliye zidi kuidhulumu nafsi yake na Haki, kuliko anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, na akadai kuwa Yeye Subhanahu ana mwana au mshirika, au akamwambatisha lolote lisilo laiki yake, au akazikanya dalili zenye kuonyesha Umoja wake Mwenyezi Mungu na ukweli wa Mitume wake. Hakika madhaalimu hawatopata kheri duniani wala Akhera.

 

 22. Na watajie yatakayo tokea Siku tutapo kusanya viumbe vyote kwa ajili ya hisabu. Kisha tutawaambia kwa kuwahizi walio kuwa wakiwaabudu wenginewe pamoja na Mwenyezi Mungu: Wako wapi mlio wafanya ni washirika wa Mwenyezi Mungu, wapate kukufaeni?

 

 23. Kisha hayatakuwa matokeo ya hayo matatizo yao magumu pahala hapo ila kujitoa kimaso-maso kutokana na ushirikina wao kwa kusema uwongo. Waseme: Wallahi Mola Mlezi wetu! Hatukumshirikisha nawe yeyote katika ibada.

 

 24. Angalia vipi wanavyo jitia makosani wenyewe kwa uwongo huu. Na vile walivyo kuwa wameviunda wenyewe kwa kuviabudu, navyo ni mawe tu, na wakadai kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu, sasa vimewapotea

 

 25. Na miongoni mwao wapo wanao kusikiliza unapo soma Qur'ani, si kwa sababu waifahamu na ipate kuwaongoa, lakini ni kwa ajili wapate njia ya kuitoa kombo na kuikejeli.
    Na Sisi kwa sababu hiyo tumewazuilia wasiweze kunafiika kwa akili zao na masikio yao. Imekuwa kama kwamba akili zao zimefunikwa haziwezi kuelewa baraabara; na kama kwamba masikio yao yana uziwi unao wazuia wasizisikie Aya za Qur'ani. Na hawa hata wakiona kila dalili hawaamini. Hata wakikujia wakujadili kwa upotovu wanasema walio kufuru, huku wakisukumiza na ukafiri wao: Haya si chochote ila hadithi za uwongo zilizo tungwa na watu wa zamani wa kabla yako!

 

 26. Wao huwazuia watu wasiiamini Qur'ani, na wao wenyewe hujitenga nayo. Inakuwa wao hawanafiiki, wala hawawachii wenginewe wakanafiika! Na kwa kitendo hicho hawadhuru ila nafsi zao, na wao hawatambui ubaya wa wayatendayo.

 

 27.Ewe Nabii! Lau ungeli waona hawa makafiri, watavyo simama mbele ya Moto wakisononeka na vitisho vyake, ungeli ona jambo la ajabu lenye kutisha, nao wanatamani warejeshwe tena duniani, wakisema: Laiti tungeli rudishwa duniani tukatengeneza tuliyo yaharibu! Wala hatutakanusha Ishara za Mola wetu Mlezi. Na tutakuwa miongoni wa Waumini.

 

 28. Na kauli yao hii haikuwa ila kwa kuwa haimkiniki tena kuficha wala kufanya ukaidi katika yale anayo waambia Mtume. Na lau kama wakirudishwa duniani wataurejea tena ukafiri alio wakataza Mwenyezi Mungu. Haya ni kwa ghururi zao kughurika na mapambo ya dunia, na kwa kufuata kwao matamanio yao. Na hakika hao wanasema uwongo kwa kudai kuwa wataamini pindi wakirejeshwa duniani.

 

 29. Na lau wakirejeshwa duniani watairudia ile ile sera yao ya mwanzo, na watasema:  Hatuna  sisi  uhai  mwingine ila huu huu uhai wa kidunia. Wala sisi hatutafufuliwa baadae.

 

 30. Lau ungeli waona watavyo simama mbele ya Mola wao Mlezi kwa ajili ya kuhisabiwa, na wao wanaujua ukweli wa aliyo wateremshia Mwenyezi Mungu Mitume wake, ungeli ona uovu wa hali yao pale Mwenyezi Mungu atapo waambia:  Je, haya mnayo yashuhudia sasa sio kweli mliyo kuwa mkiikataa huko duniani kwenu? Nao watajibu hali ni wanyonge: Kwani! Tunaapa kwa Mola Mlezi wetu, ni kweli! Tena baada ya hayo Mwenyezi Mungu atawaambia: Ingieni Motoni kwa sababu ya mlivyo kuwa mmeshikilia ukafiri.

 

 31. Hakika wamekhasiri walio kanya kukutana na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu na malipo ya Siku ya Kiyama, na wakaendelea na kukanusha kwao mpaka yalipo wafuma mambo ya Siku ya Kiyama wakajuta na wakasema: Ole wetu (yaani msiba wetu) kwa kupuuza kwetu kuifuata Haki huko duniani! Nao siku hiyo watakuwa wanaanguka kwa kuemewa na uzito wa dhambi zao! Ni mabaya mno  hayo madhambi wanayo yabeba!

 

 32. Na huo uhai wa duniani walio uona makafiri kuwa ndio uhai wa pekee, na ambao hawaukusudii kwa kufanya vitendo vya kumridhi Mwenyezi Mungu, uhai huo si chochote ila ni mchezo usio kuwa na manufaa, na pumbao la kujipumbazia tu!! Na hakika nyumba ya Akhera ndio khasa uhai wa kweli. Huo unawanufaisha zaidi wale wanao mwogopa Mwenyezi Mungu na wanazifuata amri zake. Basi hamtii akilini jambo hili lilio wazi? Hivyo hamfahamu linalo kudhuruni na linalo kufaeni?

 

 33. Ewe Nabii! Sisi tunajua kuwa yanakuhuzunisha haya wayasemayo makafiri ili kukukadhibisha. Basi wewe usihuzunike kwa hayo. Kwani hakika wao hawakutuhumu wewe kuwa ni mwongo, walakini wao kwa kujidhulumu nafsi zao na kuidhulumu haki, wanashindana kwa inda, na wanazikanya kwa ndimi zao dalili za ukweli wako, na alama za Unabii wako.

 

 34. Na hakika Mitume wa kabla yako walikabiliwa na ukanushi na maudhi kutokana na kaumu zao, kama walivyo kufanyia wewe kaumu yako. Nao wakasubiri juu ya kukanushwa na kuudhiwa, mpaka tulipo wanusuru. Basi nawe subiri kama walivyo subiri wao, mpaka ikujie nusura yetu. Wala hapana la kugeuza ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwa atawanusuru wenye kusubiri. Lazima hayo yatimie. Na Sisi tumekusimulia kutokana na khabari za hao Mitume, na tulivyo waunga mkono. Ndani ya hayo mna maliwaza yako, na maelezo  kuwa yeyote mwenye kuchukua Ujumbe lazima ahimili kila namna ya shida.

 

 35. Ikiwa unaona dhiki kwa kukataa kwao kuitikia wito wako, basi kama unaweza kutafuta njia ya kupita chini ya ardhi, au ngazi ya kupandia mbinguni ukawaletea dalili ya kuthibitisha ukweli wako, fanya hivyo! Lakini huna uwezo huo. Basi poa roho yako, na usubiri kungojea hukumu ya Mola Mlezi wako. Lau kuwa Mwenyezi Mungu ange penda basi angeli walazimisha wote hao wayaamini ulio kuja nayo, wakitaka wasitake. Lakini Yeye amewaacha kwa ajili ya kuwafanyia mtihani, kuwajaribu. Basi usiwe miongoni mwa wasio ijua hukumu ya Mwenyezi Mungu na mwendo wake kwa viumbe.

 

 36. Hakika wanao itikia wito wa Haki ni wale wanao ukubali - wale ambao wanao sikia kwa msikio wa kufahamu na kuzingatia. Ama hao walio potoka kabisa hawanafiiki kwa wito wako, kwani wao wamo katika hukumu ya maiti. Na Mwenyezi Mungu atawafufua kutoka makaburini Siku ya Kiyama, na atawarejeza kwake awahisabu kwa waliyo yafanya.

 

 37. Na makafiri washupavu wamesema: Tunataka ateremshiwe Muhammad dalili ya kuonekana kutoka kwa Mola wake Mlezi, itayo shuhudia ukweli wa huu wito wake! Waambie, ewe Nabii: Hakika Mwenyezi Mungu anaweza kuteremsha hiyo dalili muitakayo.  Lakini wengi wao hawajui nini hikima ya Mwenyezi Mungu katika kuziteremsha Ishara. Na hayo hayafuati matamanio yao. Na lau kuwa Yeye akiwakubalia hilo walitakalo, na kisha wakakanusha baada yake, basi atawateketeza tu. Lakini wengi wao hawajui nini matokeo ya vitendo vyao!!

 

 38. Na dalili yenye nguvu kabisa ya uwezo wa Mwenyezi Mungu na hikima yake, na rehema yake, ni kuwa Yeye kaumba kila kitu, na wala hapana juu ya ardhi mnyama anaye tambaa juu yake au chini yake, wala ndege arukaye kwa mbawa zake katika anga, ila Mwenyezi Mungu amewaumba kuwa ni jamii za umati kama mlivyo nyinyi. Na amewajaalia wawe na sifa zao, na vitambulisho vyao, na mipango yao ya maisha yao. Hatukukiacha kitu katika Kitabu kilicho andikwa kilioko kwetu ila tumekithibitisha. Na ikiwa wanakanusha, basi watafufuliwa pamoja na kaumu zote kwa ajili ya hisabu Siku ya Kiyama.

 

 39. Na ambao hawakuzisadiki dalili zetu zinazo onyesha uwezo wetu na ukweli wa Utume wako, basi hao hawakunafiika na hisiya zao kuwawezesha kuitambua Haki. Kwa hivyo wakawa wanababaika katika upotovu wa ushirikina na inda, kama anavyo babaika kiziwi-bubu katika giza la usiku, hawezi kuepuka kuangamia. Lau kuwa watu hawa wameelekea kheri Mwenyezi Mungu angeli wawezesha wamfikie, kwani Yeye Subhanahu akitaka kumpoteza mtu kwa ufisadi wake alio ukusudia, basi humwachilia mbali na shani yake; na akitaka kumwongoa mtu kwa kuwa makusudio yake ni sawa, basi humsahilishia njia ya Imani iliyo wazi na iliyo nyooka.

 

 40. Ewe Nabii! Waambie hawa makafiri: Nambieni, ikikujieni adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu hapa duniani, au ikikujieni Kiyama kwa vitisho vyake, mtamuelekea yeyote asiye kuwa Mwenyezi Mungu mkimnyenyekea wakati huo akufaeni kwa lolote, kama nyinyi mnasema kweli katika kumuabudu kwenu asiye kuwa Mwenyezi Mungu?

 

 41.  Bali  nyinyi mnamuelekea Yeye mnapo muomba akakuondoleeni mnacho taka kiondolewe, pindi akipenda. Na mnapo kuwa katika hali hii ya shida mnawasahau hao mnao wafanya ni washirika wake Mwenyezi Mungu!!

 

 42. Yasikudhiki, ewe Nabii, yanao kupata kwa watu wako. Kwani Sisi tuliwapeleka Mitume kabla yako kwa kaumu nyingi kabla ya umma wako huu, nao wakawaambia ni waongo. Nasi tukawapatiliza kwa adhabu zilizo wateremkia, na yaliyo wadhuru miili yao, ili walau wanyenyekee na warejee kwa Mwenyezi Mungu.

 

 43.   Na  lililo  takikana  ni  kuwa  warejee  kwa  Mola wao Mlezi. Lakini hawakufanya  hayo.  Bali  zikaendelea  nyoyo  zao  katika ugumu  wao,   na  Shetani  akawapambia  vile   vitendo   vyao vibaya, (wakaviona vizuri).

 

 44. Walipo acha kuwaidhika kwa ufakiri na maradhi tulio wapa kuwa ni mtihani, tukawajaribu baada yake kwa kuwapa riziki zenye wasaa. Tukawafungulia milango ya kila sababu za riziki, mpaka walipo furahia neema zetu, na wao wasimshukuru Mwenyezi Mungu kwa hayo, ikawajia adhabu ghafla. Wakawa wanadahadari, wamekata tamaa, hawaipati njia ya kuokoka.

 

 45. Ikateketezwa kabisa kaumu hii, yenye kudhulumu,  asibakie hata mmoja. Alhamdulillahi, wa kuhimidiwa kwa sifa zote njema ni Mwenyezi Mungu, mwenye kuwalea viumbe kwa neema na nakama, na mwenye kuisafisha ardhi na ufisadi wa wenye kudhulumu.

 

 46. Waambie, ewe Nabii: Hebu nambieni--Mwenyezi Mungu akinyakua kusikia kwenu, na akazifunika  nyoyo zenu zisiweze kutambua kitu, akakufanyeni viziwi, vipofu hamfahamu kitu - mtamuabudu mungu gani isipo kuwa Mwenyezi Mungu atakae weza kukurejesheeni aliyo kunyang'anyeni Mwenyezi Mungu? Ewe Nabii! Tazama vipi tunavyo ziweka wazi hoja na kuzipanga mbali mbali. Kisha pamoja na haya wao wanakataa kuzizingatia na kunafiika kwazo.

 

 47. Sema: Hebu nambieni--Ikikufikieni adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghafla bila ya kuitarajia, au ikakujieni kwa dhaahiri nanyi mnaitaraji, kwa kuwa mmeonywa kuwa itakuja - hivyo adhabu hiyo itamsibu yeyote ila wale watu walio jidhulumu nafsi zao kwa kushikilia ukafiri na upotovu? Hakika haitamsibu mwenginewe.

 

 48. Na Sisi hatuwatumi Manabii ila ni kwa ajili ya kuwabashiria wenye kuamini mambo ya kheri na thawabu, na kuwahadharisha na adhabu wale wanao kufuru. Basi wenye kuuamini wito wao, na wakatenda mema, hawatakuwa na khofu ya kuwapata shari, wala hawatahuzunika kwa kuikosa kheri.

 

 49. Na wale wanao zikanusha dalili zilio wazi za ukweli wa waliyo kuja nayo Mitume, watapata adhabu kwa kutoka kwao kwenye ut'iifu na Imani.

 

 50.  Ewe  Mtume!  Waambie hawa makafiri: Mimi sikwambiini kuwa mimi nina madaraka aliyo nayo Mwenyezi Mungu hata nikuitikieni kwa mnayo yataka. Wala sidai kuwa mimi nina ilimu ya mambo ya ghaibu, ambayo Mwenyezi Mungu hakunijuvya. Wala sisemi kuwa mimi ni Malaika ninaweza kupanda mbinguni! Mimi si chochote ila ni mwanaadamu tu. Sifuati ila Mwenyezi Mungu anacho nifunulia. Sema ewe Nabii: Je, wanakuwa sawa, aliye potoka na aliye ongoka katika kuzijua kweli hizi? Hivyo, inakuelekeeni nyinyi mkautupa uwongofu ninao kuleteeni, msiuzingatie kwa akili zenu hata ikakubainikieni Haki?

 

 51. Na wahadharishe kwa yaliyomo katika hii Qur'ani wale wanayo khofu vitisho vya Siku watapo wachunga Malaika kwa ajili ya hisabu na malipo, Siku ambayo itayo kuwa haina wa kunusuru wala kuombea ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, wahadharishe wajitenge mbali na vinavyo mkasirisha Mwenyezi Mungu.

 

 52. Na ewe Nabii! Usiitikie wito wa makafiri walio panda vichwa, ukawatenga Waumini wanyonge, wanao muabudu Mwenyezi Mungu daima, wala hawatafuti ila radhi zake. Wala usivishughulikie vitimbi vya washirikina juu ya hawa Waumini. Kwani wewe mbele ya Mwenyezi Mungu huna jukumu juu ya vitendo vyao, kama wao wasivyo kuwa na jukumu juu ya chochote katika vitendo vyako. Na ukiwakubalia hawa makafiri wenye kani, na ukawatenga Waumini, utakuwa miongoni mwa walio dhulumu.

 

 53. Na kwa majaribio kama haya ambayo ndio ada yetu kuyatenda, tukawafanyia mtihani walio takabari kwa kuwatanguliza wanyonge wawe mbele kusilimu; wapate kusema wenye kiburi, wanao pinga, wakifanya kejeli: Hivyo ni hawa mafakiri ndio alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwetu  sote kwa kuwapa hiyo kheri aliyo waahidi Muhammad? Hakika hawa mafakiri wanaijua neema ya Mwenyezi Mungu juu yao kwa kuwapa tawfiki ya kuifikia Imani, na kwa hivyo wanamshukuru.  Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua zaidi nani anashukuru fadhila yake na neema yake.

 

 54. Na wakikujia wanao isadiki Qur'ani waambie kwa kuwahishimu: Assalamu Alaikum, Amani juu yenu. Nakubashirieni rehema kunjufu ya Mwenyezi Mungu, ambayo amejilazimisha Yeye Mwenyewe, kwa fadhila yake, na ambayo inahukumu kuwa yeyote katika nyinyi akitenda ubaya bila ya kuzingatia matokeo yake, kisha akarejea kwa Mwenyezi Mungu naye amejuta, ametubu, na akatengeneza a'mali zake, basi Mwenyezi Mungu atamghufiria, kwani Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghfira, na mkunjufu wa rehema.

 

 55. Na kwa mfano wa bayana hiyo iliyo wazi, tunaweka wazi dalili mbali mbali, ipate kudhihiri njia ya Haki wanayo ipitia Waumini, na ibainishe njia ya upotovu wanayo ipitia makafiri.

 

 56. Ewe Nabii! Waambie hawa makafiri: Hakika Mwenyezi Mungu amenikataza kuwaabudu hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Basi mimi sifuati matamanio yenu. Kwani nikikufuateni nitakuwa nimekengeuka kuiacha Haki, na sitokuwa katika waongofu!

 

 57. Waambie: Mimi nipo juu ya Sharia iliyo wazi, iliyo teremshwa kutoka kwa Mola wangu Mlezi. Na nyinyi mmeikanusha Qur'ani iliyo ileta Sharia hii. Na mimi sina uwezo kuileta hiyo adhabu mnayo ihimiza ije. Bali hayo yamo katika uwezo wa Mwenyezi Mungu, na yamelazimika na kupenda kwake na hikima yake. Na hakuna amri wala madaraka ila ya Mwenyezi Mungu tu. Akipenda Yeye atakuleteeni adhabu kwa haraka, na akipenda ataichelewesha. Yeye Subhanahu, Aliye takasika, anafuata katika hayo hikima yake, naye ni mbora wa kuhukumu baina yangu na nyinyi.

 

 58. Sema: Lau ingeli kuwa kumo katika makadara yangu kukuteremshieni hiyo adhabu mnayo ihimiza ije, ningeli kuteremshieni kwa kukasirika kwa ajili ya Mola Mlezi wangu. Na hapo mambo yangeli kwisha baina yangu na nyinyi. Walakini amri ni ya Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mwenye kujua kuliko wote wanayo stahiki makafiri katika adhabu ya haraka, au ya kuakhirika.

 

 59. Ni Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ujuzi wa milango yote ya vilio ghaibu, visio juulikana na wengine. Hapana Mwenye kukusanya ujuzi wa hivyo ila Yeye (1), na anao wataka kuwapa baadhi yake. Naye ujuzi wake umekusanya vitu vyote vilioko nchi kavu na vilioko baharini. Wala halidondoki jani, jani lolote lile, ila Yeye analijua, wala haianguki mbegu chini ya ardhi, wala chochote kilicho kinyevu au kikavu, ila Yeye Subhanahu anakijua kwa utimilifu.
(1) Kauli hii inafahamisha kuwa kujua mambo ya ghaibu kuko kwa Mwenyezi Mungu, na funguo za hayo ziko kwake tu. Na mambo ya ghaibu ni mafungu mawili: Ghaibu Mut'laq ambayo hayumkini kutambulikana na akili, kama mambo yatakayo mfikia mtu katika mustakbali. Na Ghaib Nisbiy hizi ni siri za ulimwengu na viliomo ndani yake, na kuweza kuvitumia kwa maslaha ya watu. Ujuzi wa hayo huweza kughibu kwa vizazi kadhaa, kisha ukadhihiri.. Na funguo ya hizi pia ziko kwa Mwenyezi Mungu, humwezesha amtakaye katika waja wake wale wanao zama kuusoma ulimwengu. Na katika hayo ni haya ya uvumbuzi ambao tunauona anao ufikilia mwanaadamu kwa kuwezeshwa  na Mwenyezi Mungu Mtukufu.

 

 60. Na Yeye ndiye anakulazeni usiku, na anakuamsheni mchana. Na anajua mnayo yachuma, mpaka utimie muda wa kumfikia kila mmoja wenu ajali yake duniani ya kufa. Kisha Siku ya Kiyama mtarejeshwa nyote nyinyi kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Tena atakwambieni a'mali zenu mlizo tenda duniani, njema au mbaya, na akulipeni kwazo.

 

 61. Naye ndiye Mwenye kushinda kwa uwezo wake, aliye tukuka kwa ufalme wake juu ya waja wake, na anaye kupelekeeni Malaika wa kudhibiti kila vitendo vyenu, mpaka ufike mwisho wa kila mmoja wenu, ishikwe roho yake na Malaika wetu tunao wapeleka kwa kazi hiyo. Na wao hao Malaika hawafanyi taksiri katika kazi walio wakilishwa kuitenda.

 

 62. Tena hawa maiti watafufuliwa Siku ya Kiyama, na watasimamishwa mbele ya Mola Mlezi wao ambaye ndiye anayatawala mambo yao peke yake. Jueni kuwa Yeye tu ndiye wa kuamua baina ya viumbe na kuwahisabu katika Siku hiyo, naye ni Mwepesi wa kuhisabu na kulipa.

 

 63. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Nani anaye kuvueni na vitisho vya bara na baharini vinapo kutokeeni, mkamuaungukia na mkamwomba kwa unyenyekevu wa dhaahiri na wa ndani, mkisema: Tunaapa! Kama ukituvua na vitisho hivi tutakuwa katika wanao kiri fadhila yako, na wanao dumu kukushukuru?

 

 64. Sema: Ni Allah, Mwenyezi Mungu wa pekee, ndiye aliye kuokoeni na vitisho hivi, na kila shida nyengineyo. Na kisha nyinyi pamoja na hayo mnamshirikisha na wengine katika ibada, ambao hawawezi kuondoa shari wala kuleta kheri!

 

 65. Sema: Hakika ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye awezaye kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu au chini yenu, au kukufanyeni nyinyi kwa nyinyi mkawa maadui, mkawa mataifa yenye kuwa mbali mbali matamanio yao, yenye kuchukiana, mkitesana nyinyi kwa nyinyi kwa mateso machungu na makali! Angalia vipi hoja zinavyo onyesha uwezo wetu na kustahiki kwetu peke yetu kuabudiwa, ili wapate kuzingatia na kuifahamu Haki.

 

 66. Na kaumu yako wameikanusha Qur'ani, nayo ni Haki ambayo haina cha kukanushwa ndani yake. Ewe Nabii! Waambie: Mimi sikuwekwa kuwa ni muwakilishi wa kukulindeni, na kupima vitendo vyenu na kukulipeni kwavyo. Bali mambo yenu katika hayo yako kwa Mwenyezi Mungu.

 

 67. Kila khabari iliyo letwa na Qur'ani ina wakati wake wa kutimia. Nanyi mtakuja jua ukweli wa khabari hizi zitapo tokea.

 

 68. Na ukihudhuria katika baraza za makafiri, ukawakuta wanazikosoa Aya za Qur'ani, au wanazifanyia maskhara, basi wewe waepuke mpaka watapo ingia katika mazungumzo mengine. Na ukisahau na ukakaa nao wakati wa mazungumzo yao hayo mapotovu, kisha ukaikumbuka amri ya Mwenyezi Mungu ya kujitenga nao, basi usikae tena na watu madhaalimu baada ya kukumbuka.

 

 69. Na wenye kumcha Mwenyezi Mungu hawana dhambi katika dhambi za hawa madhaalimu, ikiwa wataendelea na upotovu wao. Lakini yapasa kuwasemeza na kuwakumbusha, asaa huenda wakaiogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu, na wakaacha upotovu.

 

 70. Na ewe Nabii, waachilie mbali wale walio fanya sharia yao, mwendo wao, pumbao na mchezo, na wakakhadaika na maisha ya dunia wakaacha ya Akhera. Na daima kumbusha kwa Qur'ani, na wahadharishe vitisho vya Siku ambayo nafsi itafungika na a'mali yake, itapo kuwa hapana wa kunusuru wala wa kusaidia isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Na kila fidia ya kujiokoa haitokubaliwa. Hao makafiri watafungwa katika adhabu kwa sababu ya shari waliyo itenda. Katika Jahannamu watapewa kinywaji kimoto mwisho wa umoto, na adhabu chungu mno kwa sababu ya kufuru zao.

 

 71. Waambie hawa makafiri kwa kuwasibabi: Je, inasihi kuwa tumuabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, asiye weza kutuletea nafuu wala dhara? Na turejee kwenye shirki baada ya kuwa Mwenyezi Mungu kesha tupa tawfiqi ya kufikia Imani? Na tuwe kama aliye zugwa na mashetani na wakampoteza katika ardhi, akawa yuko katika pweleo lisilo weza kumwongoa kufuata Njia iliyo nyooka, na hali anao marafiki walio ongoka nao wanajaribu kumwokoa atoke kwenye upotofu, huku wakisema: Rejea kwenye njia yetu iliyo sawa; naye akawa hawaitikii!! Sema ewe Nabii: Hakika Uislamu ndio uwongofu na ndio uwongozi, na vyenginevyo ni upotofu tu. Na Mwenyezi Mungu ametuamrisha tuufuate Uislamu. Naye ndiye Muumba wa viumbe vyote, na ndiye Mwenye kuviruzuku, na Mwenye kupanga mambo yao.

 

 72. Waachilieni mbali hao washirikina baada ya kuwa mmewaita kwenye uwongofu, na nendeni kwenye ibada ya Mola wenu Mlezi. Na timizeni Sala kwa njia ya unyenyekevu ulio kamilika kabisa. Na mkhofuni Mwenyezi Mungu, na timizeni amri zake. Kwani kwake Yeye ndio mtakusanywa nyote nyinyi.

 

 73. Na ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akasimamia uumbaji wake kwa Haki na hikima. Na wakati wowote Mwenyezi Mungu akitaka kiwe kitu kinakuwa papo hapo. Vitu huwa kwa neno: "Kuwa". Na kila neno lake ni la kweli na la haki. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye uweza wa kutenda usio na ukomo Siku ya Kiyama, siku litapo pulizwa barugumu la kutangazwa ufufuo. Naye, Subhanahu, ndiye Mwenye kutulia juu ya ujuzi wake wa mambo yaliyo fichikana na yanayo onekana. Na ndiye anaye endesha mambo yake yote kwa hikima, na ndiye Mwenye kukusanya katika ujuzi wake mambo yaliyo fichikana na mambo yaliyo dhihiri.

 

 74. Na ewe Nabii! Kumbuka yaliyo kuwa pale Ibrahim alipo mwambia baba yake, Azar, naye ameudhika naye kwa kuwaabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu: Haikufalii wewe kuyafanya masanamu kuwa ni miungu. Hakika mimi nakuona wewe na kaumu yako walio nawe katika ibada hii, ni dhaahiri kuwa mko mbali na Njia ya Haki.

 

 75. Kama alivyo ona Ibrahim - kwa tawfiqi yetu - upotovu wa watu wake katika kuyafanya masanamu ndio miungu, kadhaalika tumemwonyesha ufalme wetu mkubwa wa mbinguni na duniani na viliomo humo, ili aweze kusimamisha hoja kwa watu wake, na ili azidi kuamini.

 

 76. Ibrahim alimwomba Mola wake Mlezi, naye Mwenyezi Mungu akamhidi. Usiku ulipo kuja ukauziba mchana kwa kiza chake, akaona nyota inameremeta. Akasema: Huyu ndiye Mola wangu Mlezi. Ilipo potea, akasema kwa kuukataa ungu wa nyota: Sikubali kuabudu miungu inayo ondoka na kugeuka!

 

 77. Alipo uona mwezi umechomoza baada ya hayo, akasema akijiambia mwenyewe: Huyu ndiye Mola wangu Mlezi. Ulipo ondoka mwezi, na kukadhihiri kuvunjika ungu wake, akasema ili kuzielekeza nafsi zao ziombe hidaya: Ninaapa, kama Mola Mlezi wangu hakunihidi kwenye Haki, basi hapana shaka nitakuwa katika watu wanao babaika, (wasio jua mojapo la kulishika).

 

 78. Tena baada ya hayo, akaliona jua linachomoza. Akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu, kwani huyu ni mkubwa kuliko nyota zinavyo onekana. Lilipo kuchwa, likapotea, akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika kumshirikisha kwenu Mwenyezi Mungu na masanamu kwa kuyaabudu.

 

 79. Alipo kwisha ona udhaifu wa viumbe alimuelekea aliye viumba, akisema: Mimi nimeyaelekeza makusudio yangu kwa kumuabudu Mwenyezi Mungu pekee, ambaye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi. Nimejitenga na kila njia isipo kuwa Njia yake Yeye tu. Wala mimi, baada ya nilivyo kwisha ona dalili za Tawhidi (Umoja wa Allah), si katika wanao ridhia kuwa miongoni mwa washirikina kama wao.

 

 80. Na juu ya hivyo, watu wake walijadiliana naye katika Umoja wa Mwenyezi Mungu, na wakamtisha kuwa atapata ghadhabu ya miungu yao. Basi yeye akawaambia: Haikufaliini nyinyi kuzozana nami katika Umoja wa Mwenyezi Mungu, naye amekwisha nihidi kufikia Haki. Wala siogopi ghadhabu ya miungu yenu mnayo ifanya ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Lakini Mola wangu Mlezi akipenda madhara yatatokea, kwa kuwa Yeye pekee ndiye Muweza. Naye Mola wangu Mlezi amekusanya ilimu ya vitu vyote, na hao miungu yenu haina chochote inacho jua!  Je, mmeghafilika na yote hayo, na hamtambui kuwa mjinga aliye emewa hastahiki kuabudiwa?

 

 81. Na katika ajabu ni kuwa mimi niiogope hiyo miungu yenu ya uwongo, na nyinyi hamna khofu kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu iliyo simama ushahidi wa Umoja wake, nyinyi mna shiriki kuabudu vitu ambavyo havina ushahidi kuwa vinastahiki kuabudiwa. Basi katika hali hii kikundi gani baina ya sisi chenye haki ya utulivu na amani, ikiwa kweli nyinyi mnaijua Haki na mnaitambua?

 

 82. Wanao muamini Allah, (Mwenyezi Mungu), na wasiichanganyishe imani yao hii na ibada ya yeyote asiye kuwa Yeye - hao tu ndio wenye haki ya kupata utulivu, na ni wao tu ndio walio ongoka kuishika Njia ya Haki na Kheri.

 

 83. Na hiyo hoja kubwa ya Ungu wetu, na Umoja wetu, tulimpa Ibrahim aisimamishe kupambana na watu wake, naye kwa hiyo akatukuka juu yao. Na mtindo wetu kwa waja wetu ni kuwa tunamnyanyua madaraja kwa ujuzi na hikima tumpendaye katika wao. Hakika Mola Mlezi wako, ewe Nabii, ni Mwenye hikima. Huweka kila kitu pahala pake. Ni Mwenye kuwajua wepi wanastahiki kutukuzwa, na wepi hawastahiki.

 

 84. Na Sisi tulimpa Ibrahim, Is-haq na Yaaqub bin Is-haq. Na tukamwezesha kila mmoja wao kufikia Haki na Kheri, kama baba yao. Na kabla yake tulimwezesha Nuhu hivyo hivyo, na tukawaongoa katika wazao wa Nuhu, Daud, na Suleiman, na Ayyub, na Yusuf, na Musa, na Harun. Kama tulivyo walipa hawa, tunawalipa wafanyao wema kwa wanavyo stahiki.

 

 85. Na tuliwaongoa Zakariya, na Yahya, na Isa, na Ilyas - kila mmoja wao katika hawa ni miongoni mwa waja wetu walio wema.

 

 86.   Na  tuliwaahidi Ismail,  na Alyasaa, na Yunus, na Lut'; na tukawafadhilisha  kila  mmoja  wa  hawa wote kushinda walimwengu wote wa zama zao, kwa kuwapa uwongofu na Unabii.

 

 87. Na tuliwateuwa baadhi ya mababa wa hao, na dhuriya zao, na ndugu zao, na tukawakhitari wao, na tukawawezesha waifuate Njia isiyo kwenda upogo.

 

 88. Hiyo ndiyo tawfiqi kubwa waliyo ipata watu hawa, nayo ni tawfiqi (uwezesho) iliyo tokana na Mwenyezi Mungu, ambayo humwafiqia (humwezesha) amtakaye katika waja wake. Na lau wangeli shiriki watu hawa walio khitariwa zingeli potea a'mali zao za kheri zote walizo zifanya, na wasingeli pata thawabu.

 

 89. Hao ndio tulio wapa Vitabu vilivyo teremshwa, na ilimu zenye manufaa, na utukufu wa Unabii. Na washirikina wa Makka wakiyapinga mambo haya matatu, basi wamekwisha ahidiwa watu wengine wasiyo yakataa hayo wayachunge na wanafiike kwayo.

 

 90. Hao ndio Mwenyezi Mungu amewawezesha kuishika Njia ya Haki na kheri. Basi nyinyi wafuateni hao katika mambo waliyo wafikiana kwayo, nayo ni mambo ya misingi ya Dini, na misingi ya mwendo mwema, wala msifuate njia nyengine isiyo kuwa yao... Ewe Nabii! Waambie watu wako kama wao hawa walivyo waambia watu wao: Sitaki kwenu ujira kwa ajili ya kulifikisha Neno la Mwenyezi Mungu! Hii Qur'ani si chochote ila ni Ukumbusho kwa walimwengu wote, wala sina lengo mimi ila kuwa nyinyi mnafiike na hii Qur'ani.

 

 91. Na hawa makafiri hawakumkadiria Mwenyezi Mungu na rehema yake na hikima yake kwa anavyo stahiki, walipo kanya kuteremshwa ujumbe wake kwa binaadamu yeyote!  Ewe Nabii! Waambie washirikina na wanao waunga mkono katika hayo miongoni mwa Mayahudi: Nani aliye kiteremsha Kitabu alicho kuja nacho Musa, ambacho kina nuru iliyo zagaa, na uwongofu wa kuongozea? Nyinyi Mayahudi mnakifanya hicho kuwa ni maandiko yaliyo gawiwa mafungu mbali mbali. Yanayo kubaliana na mapendo yenu mnayaonyesha, na mengi mnayaficha yale yanayo kupelekeeni kuiamini na kuisadiki Qur'ani. Na kutokana na Kitabu hicho mmejifunza mambo ambayo nyinyi na baba zenu hamkuwa mkiyajua!! Na ewe Nabii! Jawabu wape wewe kwa kuwaambia: Mwenyezi Mungu ndiye aliye iteremsha Taurati. Kisha waache wakiendelea katika upotovu, wakicheza kama watoto wadogo.

 

 92. Na hii Qur'ani tumeiteremsha - kama tulivyo iteremsha Taurati - ina kheri nyingi, na itabaki mpaka Siku ya Kiyama. Inasadikisha Vitabu vilivyo teremshwa mbele yake, inaeleza khabari ya kuteremkwa kwao, ili iwape bishara Waumini, na iwakhofishe makafiri wa Makka na pembezoni mwake pande zote za dunia juu ya ghababu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa hawakuifuata. Na wale wanao isadiki Siku ya malipo, kule kutaraji kwao thawabu na kukhofu adhabu, kunawapelekea kuiamini hii Qur'ani. Na kwa hivyo wao wanahifadhi kutekeleza Sala kwa ukamilifu na utimilivu.

 

 93.  Nabii  huyu  hakusema  uwongo alipo  tangaza kuwa Qur'ani imetoka kwaMwenyezi   Mungu.   Na  hapana  mwenye  kumshinda kwa udhaalimu huyo aliye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, au akasema: Nimepata wahyi (ufunuo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila ya kuwa kapata wahyi wowote ule. Vile vile hapana dhaalimu mkubwa zaidi kuliko anaye sema: Mimi nitaleta maneno sawa na hayo aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa unaijua hali ya hao madhaalimu nao wamo katika shida za mauti, na Malaika wanazing'oa roho zao kutokana na miili yao, kwa ukali na nguvu, ungeli ona vitisho vya kushitua vinawashukia! Wakati huo hao huambiwa: Sasa malipo yenu ya adhabu ya kudhalilisha na kufedhehesha yanaanza.  Malipo haya ni kwa vile mlivyo kuwa mkimzulia Mwenyezi Mungu bila ya haki, na ni malipo kwa kuwa kiburi chenu kilikuzuieni msiangalie na kuzipima Aya, Ishara, za uumbaji za Mwenyezi Mungu ziliomo katika Qur'ani.

 

 94. Na Mwenyezi Mungu atawaambia Siku ya Kiyama: Sasa bila ya shaka mmekwisha yakinisha kwa nafsi zenu kuwa kweli mmefufuliwa kutoka makaburini kwenu, kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza. Na mmetujia hali ni wapweke, hamna mali, wala watoto, wala marafiki. Na mmeviacha nyuma yenu vyote tulivyo kupeni na mkaghurika navyo. Na wala Sisi hatuwaoni pamoja nanyi hao waombezi ambao mlidai kuwa watakunusuruni kwa Mwenyezi Mungu, na kuwa wao ati ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada! Makhusiano yote baina yenu na wao yamekwisha katika, na yamekupoteeni mliyo kuwa mkidai kuwa yatakufaeni.

 

 95. Hakika dalili za uwezo wa Mwenyezi Mungu kufufua, na kuwa ni Yeye pekee anaye stahiki kuabudiwa, na kufufua kwake watu kutoka makaburini, zimeenea na zimo za namna mbali mbali. Kwani ni Yeye peke yake ndiye anaye ipasua mbegu ukachipua mmea, na ni Yeye ndiye anaye ipasua kokwa ukatokeza mti. Na hivyo humfufua aliye hai kutokana na kisicho kuwa hai, kama mtu kutokana na udongo. Na akatoa kisicho kuwa hai kutokana na kilicho hai, kama maziwa kutokana na mnyama. Huyo Muweza Mtukufu ndiye Mungu wa Haki. Basi kisiwepo kitu cha kukugeuzeni mkaacha kumuabudu Yeye mkaviabudu vyenginevyo.
Imeunganishwa Aya hii ya kupasua mbegu na kokwa, na Aya ya kupambazua asubuhi ambayo inaashiria kuwepo mwangaza, na kiza, na ya kwamba mwangaza umeshikamana kwa nguvu na kukua kwa mimea na miti. Hayo ni kwa kuwa mbegu na kokwa baada ya kuchipua zinahitajia chakula. Na chakula hichi kinatokana na mbolea maalumu kutokana na ardhi, na pia kutokana na mwangaza wa jua. Kwa hivyo mizizi yao inakwenda chini kutafuta chakula cha ardhi, na vigogo vyake na matawi inapata chakula kutokana na mwako wa jua ambalo ndilo linachomoza asubuhi.

 

 96. Ni Yeye ndiye anaye toa mwangaza wa mchana kutokana na giza- giza la asubuhi, ili vilivyo hai viende kupata njia za maisha yao. Na akaufanya usiku uwe ni wa mapumziko ya mwili na roho, na akaufanya mwendo wa jua na mwezi wende kwa mpango mzuri kabisa ili watu wajue nyakati za ibada zao na maisha yao. Huo ndio mpango ulio fanywa kwa hikima, ndio tadbiri ya Mwenye uwezo Mwenye kuumiliki ulimwengu, Mwenye kukusanya kila kitu katika ujuzi wake.

 

 97.  Yeye  ndiye  aliye  kufanyieni  nyota zikuongozeni kwa zilivyo pangwa mfike mwendako, nanyi mnakwenda kizani usiku, bara au baharini. Hakika Sisi tumezibainisha dalili za rehema yetu, na uwezo wetu, kwa ajili ya watu ambao wanao nufaika kwa ilimu.

 

 98. Yeye ndiye aliye kutoeni kwenye asli moja, nayo ni baba wa watu wote, Adam. Na Adam ametoka kwenye ardhi. Basi ardhi ndio kituo chenu muda wa uhai wenu, na ndipo pahala pa kupaaga baada ya kufa kwenu, na mkapotea chini yake. Na tumezibainisha dalili za uwezo wetu kwa watu wanao zingatia na kufahamu mambo yalivyo.

 

 99. Naye ndiye anaye teremsha kutoka mawinguni maji, ambayo kwayo akatoa kila namna ya mimea. Kuna mimea inayo toa majani laini kuwa ni mboga, na tunatoa pia mimea ya kuzaa punje nyingi zimepandana wenyewe kwa wenyewe. Na kutokana na makole ya mitende mna mashada yamebeba tende, wepesi kuzipata. Na pia tumetoa kutokana na maji mizabibu, na zaituni, na makomamanga. Katika hiyo yapo matunda yalio fanana kwa sura, na yasiyo fanana kwa utamu, na harufu, na namna ya faida yake. Hebu yaangalieni kwa kupima na kuzingatia matunda yake inapo zaa hiyo miti, na matunda yanapo wiva, vipi yanapo komaa baada ya kupitia hali mbali mbali! Hakika katika haya zipo ishara kwa wanao itafuta Haki na wanaamini na kunyenyekea.
Aya hii inafahamisha maana kwa ilimu ya sayansi, nayo ni kuwa maji husaidia mimea kuchipua. Mbegu iliyo kaa tu haitaharaki husisimka kwa kupata maji ikaanza kumea, ikafanya kazi yake ya uhai. Mimea tena hukua na kutoa majani yenye rangi ya kijani, nayo ni madda inayo itwa "Chlorophyl". Hiyo Klorofil ni lazima kuwepo kwa ajili ya kujenga chakula kwa msaada wa mwangaza wa jua, na kuweza kuukuza mmea na kutoa matunda na mbegu nyengine.

 

 100. Juu ya dalili hizi makafiri wamewafanya Malaika na mashetani ni washirika wa Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ndiye aliye waumba hao. Haiwafalii kujua hayo wakamuabudu asiye kuwa Yeye, naye ndiye aliye waumba Malaika na mashetani. Haitakikani wawaabudu hao nao wameumbwa kama wao!! Na hawa makafiri wakambunia Mwenyezi Mungu wana. Wakristo wakadai kuwa Masihi ni mwana wa Mungu, na baadhi ya washirikina wa Kiarabu wakadai kuwa Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu. Na huo ni ujinga, kutokuwa na ilimu! Mwenyezi Mungu Mtukufu ameepukana na hayo wanayo muambatisha naye Subhana!

 

 101. Mwenyezi Mungu, ambaye ameziumba mbingu na ardhi bila ya kuwa na kiigizo kilicho tangulia, vipi awe na mwana, kama wanavyo dai hawa, na hali Yeye hana mke, naye ndiye aliye umba vitu vyote?  Miongoni mwa vitu hivyo ni hao wanao wafanya washirika wake. Naye ni Mjuzi wa kila kitu, na anawahisabia wasemayo na watendayo, na ni Mwenye kuwalipa kwa kauli yao na vitendo vyao.

 

 102. Huyo aliye sifika kwa sifa za ukamilifu ndiye Allah, Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu, ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye, Muumba wa kila kitu vilivyo kuweko, na vitavyo kuwa. Basi ni Yeye tu Mwenye kustahiki kuabudiwa. Basi muabuduni Yeye, na Yeye peke yake ndiye Mwenye kutawala kila kitu na kila jambo. Marejeo yote ni kwake tu.

 

 103. Macho hayamuoni dhati yake, na Yeye anajua undani wa macho na vyenginevyo. Naye ni Mjuzi hakimpotei kitu, ni Mwenye khabari za kila kitu.

 

 104. Ewe Nabii! Waambie watu: Zimekwisha kujieni kutoka kwa Muumba wenu na Mwenye kumiliki mambo yenu yote, hoja na maelezo wazi katika hii Qur'ani. Hizo zinakuangazieni Njia ya Haki. Basi mwenye kunafiika kwazo, manufaa ni yake mwenyewe. Na mwenye kujitenga nazo, basi amejidhuru mwenyewe! Wala mimi si mlinzi wenu, bali mimi ni Mjumbe ninakufikishieni niliyo tumwa kwenu.

 

 105. Na mfano wa uchambuzi kama huu wa pekee katika kueleza dalili za maumbile, ndivyo tunavyo eleza Ishara zetu katika Qur'ani kwa njia namna kwa namna na kwa mbali mbali, ili kusimamisha hoja za kuwashinda hao wapingao. Kwa hivyo wao hawapati ila kuzua uwongo, wakakutuhumu kuwa haya umejifunza kwa watu, wala hayakutoka kwa Mwenyezi Mungu. Nasi tunabainisha haya uliyo teremshiwa, nayo ni Haki isiyo athirika na kipendacho moyo, kwa ajili ya watu ambao wanayo ielewa Haki na wanainyenyekea.

 

 106. Ewe Nabii! Fuata wahyi ulio kujia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye kumiliki na kuendesha mambo yako. Hakika Yeye peke yake ndiye Mungu anaye stahiki kut'iiwa na kunyenyekewa. Basi shikamana na ut'iifu wake, wala usibali inadi za washirikina.

 

 107. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka wamuabudu Yeye peke yake angeli walazimisha kwa nguvu na kwa uweza wake. Lakini Yeye amewaachilia watumie khiari yao. Na Sisi hatukukufanya wewe kuwa ni muangalizi wao, ukiwahisabia vitendo vyao. Wala wewe hukulazimishwa kuwa usimamie kuwapangia na kuwatengenezea mambo yao.

 

 108. Enyi Waumini! Msiyatukane masanamu ya washirikina wanayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, isije chuki yao kwa hayo ikawapelekea hasira ya kumtukana Mwenyezi Mungu kwa uadui na ujinga. Kama tulivyo wapambia hawa kupenda masanamu yao, kila umma una a'mali yake kwa mujibu wa makdara yao. Na marejeo ya wote ni kwa Mwenyezi Mungu peke yake Siku ya Kiyama. Naye atawaeleza khabari ya vitendo vyao, na atawalipa kwavyo.

 

 109. Na washirikina waliapa ukomo wa viapo vyao, kuwa ikiwajia Ishara ya kuiona katika Ishara walizo zitaka, basi yakini hiyo itakuwa ni sababu ya kuamini kwao. Sema ewe Nabii: Ishara hizi ziko kwa Mwenyezi Mungu. Yeye peke yake ndiye Mwenye madaraka juu yake hizo ishara. Mimi sina uweza wa hayo. Nyinyi Waumini, hamjui ninayo yajua Mimi.  Hata zikiwajia Ishara hizi hawataamini.

 

 110. Na nyinyi pia hamjui kuwa Sisi tumezigeuza nyoyo zao zinapo kuja Ishara huzitafutia visababu na tafsiri, na tunayageuza macho yao kwa mambo ya dhana na mawazo tu. Kwa hivyo baada ya kuja Ishara hali yao inakuwa kama mwanzo. Nasi tunawawacha wakipotea katika dhulma yao na inadi yao.

 

 111.  Hakika  hao  walio  apa kuwa ikiwajia Ishara wataiamini, ni  waongo. Mwenyezi Mungu anaijua vilivyo imani yao. Lau kuwa sisi tungeli teremsha Malaika wakawaona kwa macho, na maiti wakawasemeza baada ya kufufuliwa makaburini mwao, na kuwakusanyia kila kitu mbele yao kikiwakabili na kuwabainishia haki, bado wasingeli amini ila akipenda Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa waamini. Na wengi hawaitambui Haki wala hawaifuati, kwa sababu nyoyo zao zimesibiwa na upofu wa kijahiliya.

 

 112. Kama ilivyo kuwa hao wamekufanyia uadui na inadi, na hali wewe unataka kuwaongoa, basi kadhaalika tumemfanyia kila Nabii anaye peleka ujumbe wetu, maadui katika wanaadamu majeuri na majini majeuri, ambao wanajificha kwako na huwaoni, wakitiliana wasiwasi kwa maneno ya kupamba-pamba na udanganyifu, yasiyo na ukweli. Basi kwa hayo huingiza ghururi kwa uwongo! Na hayo yote ni kwa kudra ya Mwenyezi Mungu na kutaka kwake. Na lau angeli taka wasingeli fanya hayo. Lakini hayo ni kwa ajili ya kuzisafisha nyoyo za Waumini. Basi waachilie mbali hao walio potea na kufuru zao za maneno yao wanayo yazua.

 

 113. Wao huyapindua maneno ya upotovu wazidanganye nafsi zao na ziridhie, na zielekee huko huko vile vile nyoyo za walio kama wao majeuri wasio iogopa Akhera, wanao itakidi kuwa uhai ni dunia tu, na waingie katika madhambi na maasi kwa sababu ya kuto iamini kwao Siku ya Akhera.

 

 114. Ewe Nabii! Waambie: Hii ni hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa Haki, iliyo bainishwa na Aya zilio zagaa. Basi haijuzu nitafute hukumu isiyo kuwa yake Yeye ya kutupambanua baina yangu na nyinyi. Mwenyewe Subhana kesha hukumu, na ameteremsha Kitabu kitukufu kiwe ni hoja juu yenu. Nanyi mmeshindwa kuleta mfano wake. Nacho kinabainisha Haki na uadilifu. Na wale walio pewa Kitabu wanajua kuwa hii Qur'ani imetoka kwa Mwenyezi Mungu, na imekusanya Haki, kama vilivyo bashiri vitabu vyao, ijapo kuwa wanajaribu kuyaficha hayo. Basi wewe Nabii, pamoja na walio kufuata, msiwe katika wenye kutilia shaka Haki baada ya kubainishwa kwake.

 

 115. Na hakika hukumu ya Mwenyezi Mungu imekwisha toka. Basi maneno ya Mola wako Mlezi ya kweli na ya uadilifu yametimia kwa kuteremshwa Kitabu hichi Kitukufu, chenye kukusanya ukweli. Na ndani imo mizani ya kweli ya kupimia Haki na upotovu. Wala hapana wa kuyageuza maneno ya Mwenyezi Mungu na Kitabu chake. Naye Subhana ni Mwenye kusikia kila lisemwalo, Mwenye kukijua kila kinacho toka kwao.

 

 116. Na ikiwa Subhanahu ndiye mwenye hukumu ya uadilifu inayo  rejewa kwenye Vitabu vyake katika kutafuta Haki na kuijua, basi ewe Nabii, usiwe wewe na walio pamoja nawe, mkamfuata yeyote anaye achana na kauli ya Haki, hata ikiwa hao ni wengi wa idadi. Kwani ukiwafuata aghlabu ya watu ambao hawategemei Sharia iliyo teremshwa na Mwenyezi Mungu, watakuweka mbali na Njia ya Haki iliyo nyooka. Na hiyo ndiyo Njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na watu hao hawendi ila nyuma ya dhana na mawazo tu, na wala hawasemi ila kwa kukisia tu;  hawategemei hoja na ushahidi.

 

 117. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye kujua kwa ujuzi ambao hapana mfano wake, kuwajua hao ambao wamekuwa mbali na Njia ya Haki, na hao ambao wameongoka na uwongofu ukawa ndio sifa yao.

 

 118. Ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye anaye wajua walio hidika na walio potea, basi msielekee kwenye upotovu wa washirikina wa kuharimisha baadhi ya nyama hoa (nyama wa kufuga). Basi kuleni katika hao, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu amekuruzukuni hao, na amewafanya ni halali na wazuri, na hapana madhara kuwala. Na mnapo wachinja litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao, maadamu nyinyi mnamuamini Yeye na mnamnyenyekea.

 

 119. Na hakika hapana sababu yoyote au dalili ya kukuzuieni kula nyama aliye tajiwa jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu juu yake wakati wa kuchinja miongoni mwa nyama hoa. (yaani nyama wa kufuga.) Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Aliye tukuka amekwisha kubainishieni vilio harimishwa, katika hali isiyo kuwa ya dharura, kama mzoga na damu (na nguruwe). Watu wengi wanaacha Haki, si kwa lolote, ila kufuata pumbao la nafsi zao tu, bila ya kuwa wamepewa ilimu, au hoja iliyo thibiti kwao. Kama hao Waarabu walio jiharimishia wenyewe baadhi ya wanyama wa kufuga. Wala nyinyi hamna makosa kwa kula kilicho zaliwa, bali wao ndio wamepita mipaka kwa kuharimisha kilicho halali. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mjuzi wa hao walio pindukia mipaka kwa ujuzi usio na mfano wake kwa hakika.

 

 120. Sio uchamngu kuharimisha alicho halalisha Mwenyezi Mungu. Hakika uchamngu ni kuacha madhambi ya nje na ndani. Basi wacheni madhambi katika vitendo vyenu, vinavyo onekana na vilivyo fichika. Na bila ya shaka wanao chuma madhambi watalipwa kwa kadri ya madhambi wayatendayo.

 

 121. Ilivyo kuwa hao wanyama ni halali kwenu kwa kuwachinja, basi msile yule ambaye hakutajiwa jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu wakati wa kumchinja, ikiwa limeachwa kutajwa makusudi, au limetajwa jina jingine lisilo kuwa la Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwani hivyo ni upotovu, na kutokana na hukumu ya Mwenyezi Mungu! Na hakika majeuri, Iblisi na wasaidizi wake, huwatia tia katika vifua vya wale walio kwisha watawala, ili wajadiliane nanyi kwa upotovu, na wakupelekeeni kuharimisha alivyo halalisha Mwenyezi Mungu. Nanyi mkiwafuata mtakuwa mfano wao katika kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

 

 122. Na nyinyi kwa Imani yenu si mfano wa washirikina hata kidogo. Basi haiwezi kuwa hali ya aliye kama maiti katika kupotea kwake, na Mwenyezi Mungu akampa nuru ya kuhidika, ambayo ni kama uhai, na akampa nuru ya Imani na hoja zilizo wazi, na kwa mwangaza wa nuru hiyo akaongoka na akawa anatembea nayo, haiwezi kuwa hali hiyo mfano wa hali ya ambaye kwamba anaishi katika giza lilio gubika. Na kama Mwenyezi Mungu alivyo ipamba Imani katika nyoyo za watu wa Imani, vile vile Shetani ameipamba shirki katika nafsi za madhaalimu wapinzani.

 

 123. Ewe Nabii! Usistaajabu ukiwaona wakuu wa wakosefu katika Makka wanapanga njama za shari za kila namna! Kwani  huo ndio mtindo wao  katika kila mji mkubwa. Wakuu wa wakosefu wake huwa kazi yao kuzua vitimbi vya shari. Na malipo ya uovu wake utakuja waangukia wenyewe, lakini wao hawatambui wala hawahisi.

 

 124. Hakika hawa wakuu wa wakosefu huwahusudu watu walio pewa na Mwenyezi Mungu ilimu, na Unabii, na uwongofu. Basi ikiwajia hoja ya kukata hawaikubali, lakini husema: Hatuikubali Haki mpaka tuteremshiwe wahyi kama wanavyo teremshiwa Mitume. Na hali ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye ujuzi ambao haulingani na ujuzi wa mtu yoyote, kujua nani anaye stahiki kupata Utume wake. Ni Yeye ndiye anaye teuwa nani katika viumbe vyake ampe Utume wake. Hawa wenye inda, ikiwa wanataka ukubwa kwa inadi ya namna hii, basi watakuja pata unyonge na udhalili hapa duniani kwa sababu hiyo, na kesho Akhera watakuja pata adhabu kali kwa sababu ya huko kupanga kwao uwovu.

 

 125. Ikiwa hao wamepotea, na nyinyi mkaongoka, basi ni kwa kutaka Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwa hukumu yake. Aliye muandikia hidaya humkunjulia kifua chake kwa nuru ya Uislamu. Na aliye muandikia kupotea kifua chake huwa na dhiki ya kweli kweli, kama kinavyo mbana kifua mwenye kupanda pahala pa juu, kama vile mbinguni. Pumzi humpaa, asiweze kitu! Na kwa hivi Mwenyezi Mungu huwaandikia ufisadi na kukatika tamaa hao ambao hawakujaaliwa kuwa na Imani katika shani yao.
Masomo ya ilimu za sayansi yamethibitisha kuwa mwanaadamu kila akipanda juu kunadhoofika kuvuta pumzi kwake kwa pua. Mpaka akifika mnyanyuka wa futi 12,000 huwa hawezi kuvuta kwa pua, na huvuta pumzi kwa mdomo. Na hivyo huvuta kwa shida, na akifanya juhudi yoyote ya nguvu huzidi taabu ya kuvuta pumzi. Na hata kusema humletea shida katika pumzi. 

 

 126. Na hii tuliyo ibainisha ndio Njia ya Haki Iliyo Nyooka. Nasi tumeipambanua na tumeiweka wazi kwa watu wote, na wala hawanufaiki kwayo ila wale ambao shani yao ni kukumbuka na kutaka hidaya.

 

 127. Na hawa wanao kumbuka na wanao amini watapata Nyumba ya Amani, nayo ndiyo Pepo. Nao watakuwa chini ya ulinzi na urafiki wa Mwenyezi Mungu na mapenzi yake na nusra yake, kwa sababu ya mambo ya kheri waliyo yatenda duniani.

 

 128.  Na  ilivyo kuwa wale walio ifuata Njia ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka watapata amani na ulinzi wa Mwenyezi Mungu, basi wale walio ifuata njia ya Shetani watapata malipo ya maasi waliyo yafanya hapo watapo kusanywa wote Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu Aliye tukuka kwa Utukufu wake atawaambia hao majini na watu walio tenda dhambi: Enyi mlio kusanyika, katika majini hadi mmekithiri kuwapoteza watu, hata wamekufuateni wengi! Tena watasema wale watu walio wafuata: Ewe Muumba wetu na Mwenye kutusimamia! Hakika sisi kwa sisi tulipeana manufaa, na tukapeana starehe kwa matamanio; na sasa ajali yetu uliyo tuwekea imekwisha fika. Hapo Mwenyezi Mungu Aliye tukuka kwa utukufu wake atasema: Makaazi yenu ya kukaa ni Motoni. Mtadumu humo milele, isipo kuwa Mwenyezi Mungu atakao penda kuwavua katika wale wasio kanya Ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Na hakika vitendo vya Mwenyezi Mungu daima vinakuwa kwa mujibu wa hikima na ujuzi.

 

 129. Kama tulivyo wawacha waasi wa kibinaadamu na wa kijini wakistareheshana wao kwa wao, basi amewajaalia madhaalimu wawe ni marafiki wao kwa wao, kwa sababu ya madhambi makubwa wanayo yachuma.

 

 130. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaambia Siku ya Kiyama: Enyi watu na majini! Mitume wamekujieni wakikutajieni hoja na dalili zilizo wazi, na wakikusomeeni Aya, na wakikuonyeni na mkutano wa Mwenyezi Mungu katika Siku yenu hii. Basi vipi mnakanusha? Nao watajibu: Tunakubali wenyewe madhambi tuliyo yatenda. Na maisha ya kidunia yaliwakhadaa kwa starehe zake, na wakajikiria nafsi zao kuwa hakika wao walikuwa wapinzani.

 

 131. Na huku kutuma Mitume, wenye kuonya na kubainisha ni kwa kuwa Mola wako Mlezi, ewe Nabii, haiangamizi miji kwa dhulma yao na watu wake wameghafilika na Haki tu.  Bali hapana budi ila awabainishie kwa uwazi na awaonye.

 

 132. Na kila mtenda kheri au mtenda shari ana daraja yake ya malipo kwa anayo yatenda. Ikiwa kheri atapata kheri, na ikiwa shari basi atapata shari. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika ndiye Muumba, si Mwenye kughafilika na wanayo yatenda. Bali hakika vitendo vyao vimo katika Kitabu kisicho acha dogo wala kubwa ila hulitia hisabuni.

 

 133. Na Mwenyezi Mungu  Mtukufu, Mola wako Mlezi, ni Mkwasi, hahitajii waja wala ibada zao. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye rehema iliyo kusanya kila kitu. Na kwa mujibu wa hayo ndio akakuamrisheni mtende mema, na akakukatazeni maovu. Naye ndiye Muweza. Akitaka atakuondoeni na alete duniani wenginewe wa kufuatia baada yenu kwa mujibu wa atakavyo. Wala hilo si gumu kwake Subhanahu, Aliye takasika. Kwani Yeye alikuumbeni kutokana na uzao wa wengine walio kutangulieni. Nanyi mkawa ndio warithi wa ardhi baada yao.

 

 134. Na hayo anayo kuonyeni kwayo, nayo ni adhabu, na anayo kubashirieni kwayo, nayo ni thawabu baada ya kufufuliwa, na kukusanywa, na kuhisabiwa, yatakuja tu hapana hivi wala hivi. Wala nyinyi hamwezi kumshinda huyo anaye kutakeni Siku hiyo. Basi hamna uwezo wa kukataa kukusanyika wala kuhisabiwa.

 

 135. Ewe Nabii! Waambie kwa kuwatisha: Fanyeni kama mpendavyo kwa ukomo wa uwezo wenu. Na mimi nitafanya kwa mujibu wa Haki. Na mwishoe bila ya shaka mtajua nani atakuwa na khatima njema katika makaazi ya Akhera. Na hayo watayapata watu wa Haki, hapana hivi wala hivi. Kwa sababu nyinyi ni madhaalimu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuwaandikia kufuzu walio dhulumu.

 

 136. Na washirikina, ambao wanayaabudu masanamu, wamo katika udanganyifu wa daima. Wao hufanya katika aliyo yaumba Mwenyezi Mungu Mtukufu, katika mazao ya mimea, na ngamia, na ng'ombe, na kondoo, fungu la Mwenyezi Mungu Mtukufu wakiwatumilia wageni na wenye haja, na fungu jingine hulitumia katika kuwakhudumia masanamu ambayo wameyafanya ni washirika wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa mujibu wa madai yao! Ama walicho wawekea masanamu huwafikia masanamu yao, na hukitumia kwa ajili yao. Na walicho muwekea Mwenyezi Mungu Mtukufu hakifiki chochote kwa hao wageni na mafakiri! Uovu ulioje huu wa hukumu yao ya dhulma! Kwani wao wameyafanya masanamu ndio wenziwe Mwenye kuumba hiyo mimea na wanyama, na hawatumii inavyo stahiki hicho walicho mwekea Mwenyezi Mungu.

 

 137. Kama ilivyo kuwa hayo mawazo yao yalivyo wapambia huo mgawanyo wa dhulma katika mazao ya mimea, na ngamia, na ng'ombe, na kondoo, alio umba Mwenyezi Mungu, basi kadhaalika mawazo yao yamewapambia, kutokana na hayo masanamu ambayo wanadai kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu, kuwauwa watoto wao pale wanapo zaliwa, na kuwa ati waliweka nadhiri kwa miungu yao kuwachinja watoto wao! Na hakika hayo mawazo yao yanawaangamiza na yanawavurugia mambo ya dini, kwa hivyo hawaielewi vilivyo! Na ilivyo kuwa mawazo yao yamezisaliti akili zao hadi hiyo, basi wewe waachilie mbali wao na hayo wanayo mzulia Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kukuzulia wewe. Nao watakuja pata malipo ya huo uzushi wao. Na hayo ndio matakwa ya Mwenyezi Mungu, kwani angeli taka wasingeli fanya hayo.

 

 138. Na katika mawazo yao ni kusema kwao: Ngamia hawa, na ng'ombe hawa, na mbuzi na kondoo hawa, na mazao haya ya mimea, ni marfuku. Hayali mtu ila wamtakaye katika utumishi wa masanamu. Hayo ni kwa madai yao ya uwongo, wala hayatokani na Mwenyezi Mungu. Na pia husema: Ngamia hawa wameharimishwa migongo yao, basi hapana ruhusa mtu kuwapanda. Nao juu ya hao hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu wanapo wachinja hao ngamia, na ng'ombe, na mbuzi na kondoo. Na hayo ni kwa kule kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ushirikina wao. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu atawalipa adhabu huko Akhera kwa sababu ya uzushi wao, na kuharimisha kwao vitu ambavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuharimisha.

 

 139.  Na  katika mawazo yao ya uwongo hawa washirikina ni kuwa wanasema: Viliomo matumboni mwa wanyama walio watenga, walio zuwiwa wasichinjwe wala wasipandwe - viliomo matumboni mwao, yaani watoto, wanafaa kuliwa na wanaume, na haramu kwa wanawake. Na juu ya hivyo akizaliwa naye kesha kufa wote wanashirikiana wanakula! Mwenyezi Mungu Mtukufu atawalipa kwa uwongo wao walio mzulia kwa kitendo chao. Kwani wanadai kuwa kuharimishwa huku kunatokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu, na ni Mwenye hikima. Vitendo vyake vyote ni kwa mujibu wa hikima. Naye atawalipa wenye dhambi kwa dhambi zao.

 

 140. Hakika wamekhasiri hao walio wauwa watoto wao kwa ujinga na kwa mawazo ya uwongo, bila ya kujua nini matokeo ya kitendo chao, wala sababu yake; na wakajiharimishia nafsi zao riziki alizo waruzuku Mwenyezi Mungu katika mimea, na wanyama, huku wakimzulia Mwenyezi Mungu kwa kudai kuwa ni Yeye ndiye aliye harimisha. Na hakika wamejitenga mbali na Haki kwa sababu hiyo. Na kwa sababu ya uzushi huu hawakuwa katika wanao sifika kwa uwongofu.

 

 141. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye umba bustani za matunda. Ipo miti inayo pandwa na kuegemezwa juu ya chanja, na ipo isiyo hitajia chanja. Na ameumba mitende, na mimea mingine inayo toa matunda yanayo khitalifiana kwa rangi, na utamu, na sura, na harufu na mengineyo. Na ameumba mizaituni, na makomamanga (makudhumani), yenye kushabihiana katika baadhi ya sifa zake, na isiyo shabihiana, ijapo kuwa udongo huenda ukawa ule ule, na yote ikawa inanyweshwa na maji yale yale. Basi kuleni matunda yake mkipenda, na toeni sadaka yake yanapo wiva na kuyachuma. Wala msifanye fujo katika kula, mkajidhuru wenyewe, na mkawadhuru mafakiri katika kuwanyima haki yao. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi watumiao kwa fujo, katika mwendo wao na vitendo vyao.

 

 142. Na Mwenyezi Mungu ameumba katika nyama hoa, nao ni ngamia, na ng'ombe, na kondoo, na mbuzi, wale wanao beba mizigo yenu, na wale ambao katika sufi yao na manyoya yao na nyewele zao mnatoa matandiko. Na hiyo ni riziki aliyo kujaalieni Mwenyezi Mungu. Basi kuleni alicho kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, wala msimfuate Shetani na marafiki zake katika kuzua vya halali na haramu, kama walivyo kuwa wakifanya watu wa Jahiliya! Hakika Shetani hakutakiini kheri, kwa sababu yeye ni adui yenu, mwenye uadui dhaahiri.

 

 143. Mwenyezi Mungu ameumba katika kila namna ya nyama hoa dume na jike. Hizo basi ni namna nane. Kondoo namna mbili, mbuzi namna mbili. (ngamia na ng'ombe wametajwa katika Aya inayo fuata.)  Ewe Muhammad! Waambie washirikina kukanya hayo waliyo yaharimisha: Nini sababu ya kuharimisha katika hawa kama mnavyo dai? Ni kwa kuwa madume? Au kwa kuwa ni kuwa matumboni ya mama zao? Hayo hayawezi kuwa hivyo, kwa sababu nyinyi hamkuharimisha watoto waliomo tumboni kabisa!! Nambieni kwa mategemeo baraabara, ikiwa nyinyi mnasema kweli katika kuhalalisha na kuharimisha.

 

 144. Na Mwenyezi Mungu ameumba ngamia namna mbili, dume na jike, na ng'ombe namna mbili mbili vile vile. Ewe Muhammad! Waambie kwa kuwakanya: Nini sababu ya kuwaharimisha hao mlio harimisha kama mnavyo dai? Ni kwa kuwa wao ni madume? Sivyo hivyo; kwa sababu pengine mnahalalisha madume! Au ni kwa kuwa majike? Pia sio hivyo, kwa sababu mnahalalisha majike wakati mwingine! Au kwa kuwa wana watoto matumboni mwao? Pia sio hivyo, kwa sababu hamkuharimisha watoto walio matumboni daima. Nanyi mnadai kuwa kuharimisha huku kunatokana na Mwenyezi Mungu! Nyinyi mlikuwapo Mwenyezi Mungu alipo kuharimisheni haya na mkamsikia makatazo yake? Kabisa hayo hayakuwa. Wacheni mlio nayo; kwani hiyo ni dhulma. Na hapana mwenye kudhulumu zaidi kuliko mwenye kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu, akamnasibisha nayo mambo yasiyo toka kwake, wala hayana tegemeo lolote la ki-ilimu la kutegemea, bali huyo anataka kuwapotosha watu tu! Mwenyezi Mungu hawawafikishi wenye kudhulumu wakikhiari njia ya upotovu.

 

 145. Ewe Nabii! Sema: Hivi sasa sipati katika panapo toka mambo ya kuhalalisha na kuharimisha katika niliyo funuliwa mimi wahyi juu ya chakula kilicho harimishwa kula mlaji, isipo kuwa kitu hicho kiwe ni nyamafu, kimekufa na hakikuchinjwa kwa njia za sharia; au damu inayo tiririka, au nyama ya nguruwe - kwani hivyo vilivyo tajwa vinadhuru, na vichafu, havijuzu kula. Na pia katika vitu vilivyo harimishwa kula vinavyo toka katika itikadi sahihi, kwa kuwa wakati wa kuchinjwa lilitajwa jina lisilo kuwa la Mwenyezi Mungu, kama sanamu au muabudiwa mwenginewe! Juu ya hivyo mwenye kulazimika kwa dharura kula kitu katika hivi vilivyo harimishwa, bila ya kuwa anatafuta utamu tu wa kula, na bila ya kupita mpaka wa ile dharura, basi huyo hana dhambi. Kwa sababu Mola wako Mlezi ni Mwenye kughufiria, na Mwenye kurehemu.

 

 146. Basi hivi ndivyo tulivyo kuharimishieni nyinyi. Na Mayahudi tuliwaharimishia nyama na shahamu na kila kitu cha wenye makucha katika wanyama, kama ngamia na wanyama wawindao. Na katika ng'ombe na mbuzi na kondoo tuliwaharimishia shahamu yake tu, ila shahamu ya mgongoni, au iliyoko matumboni, au iliyo changanyika na mafupa. Na kuharimishwa huku kulikuwa kwa ajili ya kuwatesa tu kwa ajili ya dhulma zao, na kuziachisha nafsi zao waweze kujilinda na matamanio.  Na hakika Sisi tunasema kweli katika maneno yetu yote, na miongoni ya hayo ni khabari hii.

 

 147. Wakanushi wakikukanusha katika haya tuliyo kuletea wahyi, waambie kwa kuwahadharisha: Hakika Mola Mlezi wenu, ambaye anapasa mumuamini Yeye peke yake, na mfuate hukumu zake, ana rehema iliyo enea na kumfikia kila anaye mt'ii, na pia anaye muasi kwa kuwa hafanyi haraka kuwaadhibu. Na lakini haitakikani mghurike na hivyo kuwa rehema yake imeenea kote, kwa sababu adhabu yake haina budi kuwafikia hao wakhalifu.

 

 148. Kwa kutaka kujitolea udhuru kwa ushiriki wao, na kule kuharimisha vyakula alivyo halalisha Mwenyezi Mungu, na kukanusha yaliyo wafikia kuwa Mwenyezi Mungu kaudhika nao kwa vitendo vyao, washirikina watasema: Ushirikina wetu na kuharimisha alicho halalisha Mwenyezi Mungu, ni kwa mujibu wa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kuridhi kwake! Na lau angeli penda Yeye kinyume cha hayo, na angeli chukia tuyatendayo, basi tusingeli mshirikisha sisi wala walio tutangulia, na wala tusingeli harimisha kitu chochote alicho tuhalalishia. Na walio kabla yao waliwakadhibisha Mitume wao, kama hawa wanavyo kukadhibisha wewe. Na waliendelea katika kukanusha kwao mpaka ikawafikia adhabu yetu! Waambie hawa wanao kanusha: Jee mnao ushahidi wa kutegemea ulio sahihi ya kwamba Mwenyezi Mungu amekuridhieni nyinyi mumshirikishe na mhalalishe, mkatutolea? Katika maneno yenu hamfuati ila kudhania tu. Na hiyo haitoshelezi chochote katika Haki. Na nyinyi si chochote, si lolote, ila ni waongo tu katika hayo mnayo dai.

 

 149. Ewe Nabii! Sema: Mwenyezi Mungu ana hoja iliyo wazi kuwa nyinyi ni waongo katika madai yenu kuwa Mwenyezi Mungu ameridhia vitendo vyenu! Wala hamna hoja katika ushirikina wenu, na kuhalalisha kwenu, na kuharimisha kwenu, na mengineyo. Na Mwenyezi Mungu angeli taka mhidike angeli kuhidini nyote mkafuata Njia ya Haki. Lakini hakutaka hayo kwa kuwa nyinyi mmekhiari njia ya upotovu.

 

 150. Ewe Nabii! Waambie: Leteni wasaidizi wenu watakao kushuhudieni kwamba kweli Mwenyezi Mungu ameharimisha hivi mnavyo dai kuwa ni haramu. Wakihudhuria na wakashuhudia, basi wewe usiawasadiki, kwa sababu hao ni waongo. Wala usifuate matamanio ya hawa walio kanusha hoja za uumbaji na Qur'ani inayo somwa, na ambao hawaiamini Akhera nao wanamshirikisha Mwenyezi Mungu, wanamfanya Yeye sawa na hao miungu inayo abudiwa kwa uwongo.

 

 151. Ewe Nabii! Waambie: Njooni nikubainishieni yaliyo haramu ambayo inatakikana mshughulike nayo, na mjitenge nayo. Msimfanye yeyote kuwa ni mshirika na Mwenyezi Mungu, kwa shirki ya namna yoyote. Wala msiwafanye uovu wazazi wenu, bali wafanyieni wema mwisho wa wema. Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya kukufikieni ufakiri, au mnao ogopa usikufikieni siku za usoni. Kwani nyinyi sio mnao toa riziki. Bali Sisi ndio tunakuruzukuni nyinyi na tunawaruzuku wao. Wala msikaribie uchafu wa uzinzi, kwani huo ni katika mambo mabaya yanayo katazwa, sawa sawa ikiwa jahara au kwa siri asiyo iona ila Mwenyezi Mungu. Wala msiuwe nafsi yoyote aliyo kataza Mwenyezi Mungu kuiuwa kwa kutokuwapo kupasa kwake, ila ikiwa kuuwa huko ni kwa haki ya kutekeleza hukumu ya mahkama. Mwenyezi Mungu amekuamrisheni kwa amri ya nguvu muepuke haya yaliyo katazwa ambayo akili ya maumbile inakwambieni muepukane nayo, ili nanyi myatie akilini hayo.

 

 152.  Wala  msiyatumie  mali ya yatima ila kwa njia iliyo bora kabisa ya kuyahifadhi na kuyakuza. Na endeleeni hivyo mpaka huyo yatima afike umri wa uwongofu, atapo weza  mwenyewe kuendesha mambo yake baraabara. Hapo tena ndio mpeni mali yake. Wala msipunje vipimo na mizani kwa kupunguza mnapo toa, au kuongeza mnapo chukua. Bali pimeni kwa uadilifu kama muwezavyo. Na Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi ila kwa kadiri iwezavyo bila ya karaha. Na mkisema neno katika kuhukumu, au ushahidi, au khabari, au mfano wa hayo, basi msikengeuke mkaacha uadilifu na ukweli. Bali hakikisheni kusema sawa, bila ya kuzingatia makhusiano ya jinsi, yaani uke na ume, au rangi, au ujamaa au ushemeji. Wala msitengue ahadi za Mwenyezi Mungu alizo chukua kwenu kwa taklifu, wala ahadi zilio baina yenu wenyewe kwa wenyewe, katika mambo yaliyo fungamana na maslaha yaliyo ruhusiwa kisharia. Bali timizeni ahadi hizi zote. Mwenyezi Mungu amekuamrisheni kwa kutilia mkazo mjitenge na yaliyo katazwa, na mkumbuke kuwa Sharia ni kwa ajili ya maslaha yenu.

 

 153. Wala msiiache Njia niliyo kuwekeeni, kwani hiyo ndiyo Njia Iliyo Nyooka itayo kufikisheni kwenye mafanikio ya duniani na Akhera. Bali ifuateni Njia hii, wala msifuate njia nyingine za upotovu alizo kukatazeni Mwenyezi Mungu, ili msije kufarikiana mkawa makundi makundi na mapande mapande, ya madhehebu na vyama, na mkawa mbali na Njia ya Mwenyezi Mungu iliyo kaa sawa. Mwenyezi Mungu amekuamrisheni kwa amri ya nguvu ili msije mkamkhalifu Yeye.

 

 154. Na tulimteremshia Musa Taurati kwa kumtimizia neema mtu aliye simama msimamo mwema katika mambo ya Dini. Na tuliiteremsha kwa kueleza wazi kila jambo katika mafunzo yalio nasibiana na watu wake, na ni uwongofu kwendea Njia iliyo sawa, na rehema kwao kwa kuifuata. Na hayo ni hivyo ili Wana wa Israili waiamini Siku ya kukutana na Mola wao Mlezi, Siku ya Kiyama na kuhisabiwa kwa mambo walio amrishwa kuyafanya.

 

 155. Na hii Qur'ani ni Kitabu, kilicho barikiwa, tulicho kiteremsha, chenye kukusanya kheri za Mwenyezi Mungu,  na manufaa ya Dini na dunia. Basi kifuateni, na ogopeni msende kinyume chake, ili Mola wenu Mlezi apate kukurehemuni.

 

 156. Tumeiteremsha hii Qur'ani ili msipate kutoa udhuru kwa uasi wenu mkasema: Wahyi haukuteremka ila kwa mataifa mawili tu ya kabla yetu, nao ni watu wa Taurati na watu wa Injili. Na sisi hatuna ilimu kabisa ya kusoma vitabu vyao na kufahamu uwongozi uliomo humo.

 

 157.  Na Sisi tumeiteremsha Qur'ani ili wasiseme pia: Lau kuwa sisi tumeteremshiwa ufunuo kama walivyo teremshiwa wao, tungeli washinda kwa uwongofu, na hali yetu ingeli kuwa bora zaidi, kwa sababu ya akili zetu ni pana zaidi na sisi tumetengenea vizuri! Baada ya hii leo hamna hoja ya kuasi kwenu. Wala hapana udhuru wa kauli yenu hii. Kwani Qur'ani imekujieni kutoka kwa Mola Mlezi wenu, nayo ni alama iliyo wazi ya ukweli wa Muhammad. Inabainisha yote mnayo yahitajia katika Dini yenu na dunia yenu. Inakuongoeni kwenye Njia iliyo sawa, na rehema kwenu kuifuata. Na hapana mwenye kudhulumu zaidi kuliko huyo anaye zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu alizo ziteremsha katika Vitabu vyake, na Ishara zake alizo ziumba katika ulimwengu, naye akazipuuza na asiziamini, na wala asizitende! Na Sisi tutawaadhibu hao wanao zikataa Ishara zetu, wala hawazingatii adhabu yenye mwisho wa uchungu, kwa sababu ya kukataa kwao na kuacha kuzingatia kwao.

 

 158. Hoja imekwisha simama ya kuwa kuamini ni waajibu. Na watu hawa hawakuamini. Basi wanangojea nini ndio waamini? Je, wanangojea wawajie Malaika wawe ni Mitume badala ya kuwa wanaadamu, au wawe ni mashahidi kushuhudia ukweli wako? Au aje Mwenyewe Mola wako Mlezi, wamwone, au ashuhudie ukweli wako? Au zije baadhi ya alama za Mola wako Mlezi zishuhudie ukweli wako? Na pindi zikija hizo alama za Mola wako Mlezi za kuwapelekea kuamini, basi Imani yao haitowafaa kitu. Kwani hiyo itakuwa ni Imani ya kahari, hawana hila. Na sasa tena haimfalii mwenye kuasi toba yake na ut'iifu wake. Kiwango cha kufanya waajibu kimekwisha pita! Waambie hawa wanao kataa na kukanusha: Ngojeni moja ya mambo hayo matatu, nanyi endeleeni katika kukanusha kwenu. Nasi pia tunangoja hukumu ya Mwenyezi Mungu juu yenu.

 

 159. Hakika walio igawanya Dini moja ya Haki kwa itikadi za uwongo, na sharia za upotovu, na wakawa kwa sababu hiyo makundi  mbali mbali; unawadhania ni wamoja, kumbe nyoyo zao zimekhitalifiana, wewe huna jukumu kwa kufarikiana kwao na uasi wao, wala wewe huwezi kuwahidi. Wewe hulazimiki ila kufikisha Ujumbe. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kumiliki mambo yao kwa kuwaongoa na kuwalipa, kisha awatajie  Siku ya Kiyama yale waliyo kuwa wakiyafanya duniani na awalipe kwayo.

 

 160. Mwenye kutenda mema atalipwa thawabu zake mpaka mara kumi kwa kufadhiliwa na kukirimiwa. Na mwenye kutenda ovu hatoadhibiwa ila kwa kadri ya maasi yake tu, kwa uadilifu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hapo hapana dhulma kwa kumpunguzia mtu thawabu, wala kumzidishia adhabu.

 

 161. Sema ewe Nabii kwa kubainisha Dini ya Haki unayo ifuata: Hakika Mola wangu ameniongoza, na ameniwafikisha kuishika Njia Iliyo Nyooka, yenye kufika ukomo wa kukamilika na kunyooka. Na Dini hii ndiyo aliyo ifuata Ibrahim akaacha itikadi zote potovu. Na Ibrahim hakuwa akimuabudu mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, kama wanavyo dai washirikina.

 

 162.  Sema:  Hakika  Sala yangu na ibada zangu, na niyafanyayo katika hali ya uhai wangu, nayo ni ut'iifu, na Imani na vitendo vyema ninavyo kufa navyo, vyote hivyo nimevisafia kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu Aliye umba vitu vyote, na kwa hivyo akastahiki kuabudiwa Yeye peke yake, na kut'iiwa Yeye peke yake.

 

 163. Hana mshirika katika kuumba, wala katika kustahiki kuabudiwa. Naye Yeye Mola Mlezi wangu ameniamrisha kwa hayo nimfanyie ikhlasi (usafi wa niya) katika Tawhidi (kutakasisha upweke wake) na vitendo. Na mimi ni wa kwanza wa kumnyenyekea, kumfuata, na mkamilifu wao wa ut'iifu na kusilimu.

 

 164. Sema ewe Muhammad, kuwakatalia washirikina wito wao kwako, uwakubalie ushirikina wao: Nimtafute wa kumuabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ndiye Muumba wa kila kitu? Na waambie kuwakatalia kuwa wao hawawezi kukubebea makosa yako ikiwa utawakubalia:  Hapana nafsi inayo tenda kitu ila itapata malipo yake wenyewe peke yake. Hachukui mtu dhambi za mwenziwe. Kisha mtafufuliwa kwa Mola Mlezi wenu baada ya mauti, naye atakupeni khabari ya hayo mliyo khitalifiana kwayo duniani, katika mambo ya itikadi, na atakulipeni kwayo.  Basi vipi nimuasi Mwenyezi Mungu kwa kutegemea ahadi yenu ya uwongo.

 

 165. Na Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye kufanyeni makhalifa (walio chukua pahala pa) kaumu zilizo tangulia katika kuamirisha ulimwengu. Naye amewanyanyua baadhi yenu kuliko wengine kwa daraja nyingi katika mambo yanayo onekana na yasiyo onekana kwa vile kukupeni njia za kuyafikilia, ili apate kukujaribuni, kukufanyieni mtihani, katika hizo neema alizo kupeni, vipi mtazishukuru, na katika sharia alizo kupeni mtazitumia vipi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwepesi wa kuwaadhibu wakhalifu, kwani hakika adhabu yake itakuja tu bila ya shaka, na kila lijalo lipo karibu. Na Yeye ni mwenye maghfira makubwa kwa makosa ya wenye kutubu na wakatengenea, na Mkunjufu wa rehema kwao.