1. Enyi Waumini! Jilazimisheni kutimiza ahadi zote baina yenu na Mwenyezi  Mungu,  na  ahadi za kisharia zilio baina yenu na watu wengineo.  Na  Mwenyezi  Mungu amekuhalalishieni kula nyama howa, yaani nyama wa kufuga, kama ngamia, ng'ombe, kondoo, mbuzi n.k. ila wale mlio tajiwa kuwa ni haramu. Wala haikujuzieni kuwinda barani pale mnapo kuwa mmeharimia Hija, au mpo katika eneo la ardhi takatifu. Hakika Mwenyezi Mungu huhukumu apendavyo kwa hikima yake. Yeye ndiye Muumbaji, na ndiye Mwenye kujua jema na baya la viumbe vyake. Na haya ni miongoni mwa ahadi za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu.
 

 2.  Enyi Waumini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Mwenyezi Mungu, yaani ibada alizo amrisha Mwenyezi Mungu, kama ibada za Hija wakati wa Ihram (1), na sharia na hukumu nyenginezo. Wala msivunje hishima ya miezi mitakatifu kwa kuzua vita katika miezi hiyo. Wala msipinge wanyama wanao pelekwa Makka, kwa kupokonya au kuzuia wasifike huko, wala msiwavue vigwe walivyo fungwa shingoni mwao kuwa ni alama kuwa wamekusudiwa kupelekwa Nyumba Takatifu, na kuwa watakuwa dhabihu wa Hija. Wala msiwapinge wanao kusudia kwenda Hija nao wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Na mkisha vua Ihram na mkatoka kwenye eneo la Alharam, basi mnaweza kuwinda mtakavyo. Wala msipelekewe na chuki yenu kubwa kwa wale walio kuzuieni kufika kwenye Msikiti wa Makka mkawafanyia uadui. Enyi Waumini! Saidianeni katika kutenda kheri na mambo yote ya ut'iifu, wala msisaidiane katika  maasi, na kupindukia mipaka aliyo iweka Mwenyezi Mungu. Na ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na nguvu zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuwaadhibu wale wanao mkosa.
(1) Mwenye kuhiji akisha "harimiya" (yaani kunuia kuhiji) huwa haramu kwake baadhi ya mambo, kama kuvaa nguo iliyo shonwa, kukata nywele, kuwinda, n.k.  mpaka amalize "Ihram" nako ndio kwisha ibada ya Hija.

 

 3.  Enyi Waumini! Mwenyezi Mungu amekuharimisheni kula nyamafu, yaani aliye kufa bila ya kuchinjwa kisharia.(1) Na damu inayo tiririka, na nyama ya nguruwe, na yule ambaye wakati wa kuchinjwa ametajiwa jina lisilo kuwa la Mwenyezi Mungu, na aliye kufa kwa kunyongwa, au aliye pigwa mpaka akafa, au aliye kufa kwa kuanguka, au kwa kupigwa pembe, au kwa kuliwa na mnyama mwingine. Ama yule mnaye mdiriki angali yu hai naye ni mnyama wa halali kuliwa, mkamchinja, basi huyo ni halali kwenu. Mwenyezi Mungu ameharimisha kula wanyama walio tolewa sadaka au mhanga kwa masanamu. Na pia ameharimisha kuagua yaliyo ghaibu kwa uganga wa kupiga ramli, na mfano wa hayo. Kula chochote katika vilivyo tajwa kuwa ni haramu ni dhambi kubwa, na ni kutoka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Tangu sasa tamaa ya makafiri kuiviza Dini yenu imekwisha potea. Basi msiwaogope kuwa watakushindeni, bali ogopeni kutofuata amri zangu. Leo nimekukamilishieni hukumu za Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu kwa kukupeni nguvu na kukuimarisheni, na nimekukhitarieni UISLAMU uwe ndiyo Dini. Lakini mwenye kulazimika kwa njaa akala kidogo katika hivyo vilivyo harimishwa, akala ili asife, bila ya kukusudia uasi, basi Mwenyezi Mungu humsamehe mtu huyo kwa kulazimika kula cha haramu asije akafa. Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma na rehema kwa alivyo halalisha.
(1) Hafi mnyama wenyewe ila kwa maradhi, na hayo maradhi humdhuru mwanaadamu akila nyama yake, na huenda maradhi mengine yakawa ya kuambukiza. Katika damu vimo vijidudu vya maradhi. Ama katika nyama ya nguruwe mna vitu kadhaa wa kadhaa vya kumdhuru mtu. Na vilivyo chinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na walio chinjiwa masanamu au mashetani, hayo ni mambo ya ibada potovu. Na vilivyo nyongeka, na vilivyo anguka, na kupigwa pembe ni sawa na mfu, au mzoga, kwa kuwa vimekufa kwa vifo vibaya, na khasa kwa kuwa damu yake haikutoka imevilia humo humo.

 

 4. Ewe Mtume! Waumini wanakuuliza nini walicho halalishiwa katika vyakula na vyenginevyo? Waambie: Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni kila chema kipendacho nafsi njema. Na pia amekuhalalishieni kula kinacho windwa na wanyama wenu mlio wafunza kuwinda, kwa kutokana na alivyo kufunzeni Mwenyezi Mungu. Basi kuleni wanacho winda wanyama hao mlio watuma, na mtaje jina la Mwenyezi Mungu pale mnapo watomeza. Na mcheni Mwenyezi Mungu kwa kuzishika sharia zake, wala msikiuke mipaka yake. Tahadharini kumkhalifu Mwenyezi Mungu katika hayo, kwani Yeye ni Mwepesi wa kuhisabu.

 

5. Leo, yaani tangu kuteremka Aya hii, mmehalalishiwa kila kilicho chema kipendacho nafsi njema; na pia mmehalalishiwa chakula cha Watu wa Kitabu (Mayahudi na Wakristo), na walio chinja wao, katika vitu ambavyo havikutajwa kuwa ni haramu, kama ilivyo kuwa wao ni halali kwao kula chakula chenu. Na mmehalalishiwa nyinyi kuwaoa wanawake wema wa Kiislamu na wa Ahlil Kitaab (Mayahudi na Wakristo). Hayo kwa sharti mkiwapa mahari yao kwa kusudi ya kuwaoa, sio kwa kuingiana nao kinyume na sharia kwa jahara au kwa kuwaweka mahawara kinyumba. Na mwenye kuipinga Dini, basi amepoteza malipo ya a'mali yake aliyo dhani kuwa ndiyo itamkaribisha, naye huko Akhera ni katika walio hiliki.

 6. Enyi Waumini! Mkitaka kusali nanyi hamna udhu, tawadhini kwa kukosha nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake maji kichwa kizima au baadhi yake. Na mkoshe miguu yenu mpaka vifundoni. Mnapo taka kusali nanyi mna janaba kwa kuingiliana na wake zenu, basi kogeni mwili mzima. Ikiwa mna maradhi ambayo hayakufaliini kutumia maji, au mpo safarini na ipo taabu ya maji, au mmetoka chooni kukidhi haja, au mmeingiliana (kwa lugha ya Qur'ani "kugusana") na wanawake na msipate maji, basi inakupaseni kutayamamu, yaani kujipaka vumbi lilio safi. Na hayo ni kwa kupangusa kwa hilo vumbi nyuso zenu na mikono yenu. Na Mwenyezi Mungu hataki kukudhikini katika hayo anayo kuamrisheni, bali anakupeni sharia za kukusafisheni ndani na nje, ili atimize neema zake juu yenu kwa uwongofu, na kubainisha na kusahilisha, mpate kumshukuru kwa uwongofu wake na kutimilia neema yake kwa kudumisha ut'iifu kwake.
T'ahara (Usafi)   wa  Kiislamu  una maana mbili: Moja ni kumwelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu moyoni kwa kujiweka tayari kwa hayo,  na  kufunga azimio kusimama mbele yake na hali ni mwenye  nafsi iliyo  t'aahiri, na moyo ulio safi kabisa kwake Yeye tu.    Pili ni unadhifu wa dhaahiri kwa udhu. Na katika hayo ni  kuvikosha  viungo  vyote vinavyo weza kuchafuka. Na udhu ni jambo  la  kufanywa mara kwa mara, na huweza kufika hata kutwa mara tano. Pia kuna kukoga unapo ingiliana na mke, na wakati wa damu ya mwezi na uzazi. Udhu na kukoga ni kuondoa takataka zenye vijidudu vya maradhi, na pia huleta uchangamfu kwa kusisimua damu ya kwenye ngozi, na kupoza mishipa. Na kwa hivyo Mtume s.a.w. aliusia: "Ukihamaki tawadha".

 

 7. Kumbukeni, enyi Waumini, neema za Mwenyezi Mungu alizo kuneemesheni kwa kukuongoeni kwenye Uislamu. Jitahidini kutimiza ahadi yake aliyo itaka kwenu wakati mlipo muunga mkono Mtume wake, Muhammad, kuwa mtamsikia na mtamt'ii. Na mcheni Mwenyezi Mungu kwa kuzihifadhi ahadi hizi. Yeye, Subhanahu, ni Mjuzi sana   wa yote yaliyo fichikana nyoyoni mwenu, naye atakulipeni kwayo.

 

 8. Enyi Waumini! Jitahidini kutimiza haki za Mwenyezi Mungu, na shuhudieni kwa haki baina ya watu. Chuki zenu kubwa kwa watu fulani zisikupelekeeni mkaacha kuwafanyia uadilifu. Bali jilazimisheni uadilifu, kwani hiyo ndiyo njia ya kupelekea kumcha Mwenyezi Mungu, na kuepukana (1) na ghadhabu yake. Na mcheni Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote; kwani Yeye, Sub hanahu, anayajua vilivyo yote mnayo yafanya, naye atakulipeni kwayo.
(1)  Uislamu unalingania uadilifu moja kwa moja, sawa kwa  rafiki na adui.Haifai chuki ikakupelekea kudhulumu. Na hayo unapo  amiliana na watu, na kuamiliana baina ya dola ya Kiislamu na  dola nyenginezo. Na kumfanyia uadilifu adui kunaambiwa na Qur'ani kuwa ni karibu zaidi na uchamngu na usafi wa kidini.  Lau  kuwa wasia huu ungeli tumiwa katika sharia za baina ya madola basi pasingeli kuwapo vita. Kama kila dini ina kitambulisho chake na alama, basi kitambulisho cha Uislamu ni Dini ya Mungu Mmoja na Uadilifu.

 

 9. Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake amewaahidi walio isadiki Dini yake na wakatenda mema kuwa atawasamehe dhambi zao, na  atawalipa badala yake thawabu.

 

 10. Na wale wanayo ipinga Dini ya Mwenyezi Mungu, na wakakanusha Ishara zinazo onyesha Umoja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ukweli wa Ujumbe wake, hao ni watu wa kudumu katika Jahannamu.

 

 11. Enyi Waumini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu katika wakati wa shida, pale baadhi ya Washirikina walipo kusudia kukuuweni nyinyi na Mtume wenu, Mwenyezi Mungu akazuia balaa yao isikufikieni, na akakuokoeni. Shikamaneni na kumcha Mwenyezi Mungu, na mumtegemee Yeye peke yake, katika mambo yenu. Kwani Yeye anakutosheni. Inavyo muelekea Muumini ni kumtegemea Mwenyezi Mungu peke yake daima milele.

 

 12. Mwenyezi Mungu alichukua ahadi kutokana na Wana wa Israili kuwa watamsikia na watamt'ii. Akawateulia marais thinaashara kutokana miongoni mwao ili itimie hiyo ahadi. Na Yeye Mwenyezi Mungu akawaahidi ahadi ya nguvu kuwa atakuwa pamoja nao, atawasaidia na atawanusuru ikiwa watashika Sala kama ipasavyo, na watatoa Zaka walizo faridhiwa, na watawasadiki Mitume wake wote, na watawanusuru, na watatoa mali kwa ajili ya mambo ya kheri.  Na kwamba pindi wakifanya hayo basi Mwenyezi Mungu atawafutia dhambi zao, na atawatia katika Bustani zake zipitazo mito kati yake. Na mwenye kukufuru, na akavunja ahadi baada ya hayo, basi huyo amepotoka na hakufuata njia iliyo kaa sawa iliyo nyooka.

 

 13. Basi kwa sababu ya Wana wa Israili kuvunja agano lao ndio wakastahiki kufukuzwa kutokana na rehema ya Mwenyezi Mungu. Nyoyo zao zikawa ngumu, si laini za kupokea Haki; na wakaingia kupotoa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyomo katika Taurati kutokana na maana yake ya asli, na yafuate yanayo wafikiana na wapendavyo wao.  Wakaachilia mbali pande kubwa ya mambo waliyo amrishwa katika Taurati !! Na wewe, Mtume, huachi kuona kila namna ya khadaa na uvunjaji wa ahadi kwa hawa Wana wa Israili, isipo kuwa kwa wachache tu miongoni mwao ambao wanakuamini wewe. Hao hawakhuni wala hawadanganyi. Basi, ewe Mtume! Yasamehe yaliyo pita kutokana na watu hawa, na wachilia mbali, bali wafanyie wema. Kwani Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.

 

 14. Hali kadhaalika Mwenyezi Mungu alichukua ahadi kwa Wakristo, ambao wamesema: Sisi ni Manasara, kwa kuwa wataiamini Injili, na watamuamini Mwenyezi Mungu Mmoja. Nao wakaacha mengi walio amrishwa katika Injili. Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa hayo, kwa kutia uadui na khasama baina ya wao kwa wao, wakawa makundi mbali mbali yenye uadui mpaka Siku ya Kiyama. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaambia waliyo kuwa wakiyafanya, na atawalipa kwayo.

 

 15. Enyi Watu wa Kitabu! Amekujilieni Mtume wetu, Muhammad, akiita watu wafuate Haki. Anakufichulieni mengi mliyo kuwa mkiyaficha katika Taurati na Injili. Na anayaacha mengi katika mliyo yaficha ambayo hayana haja kuyadhihirisha. Amekuleteeni kutoka kwa Mwenyezi Mungu Sharia kaamili, ambayo Sharia hiyo peke yake ni nuru, na inabainishwa na Kitabu kilicho wazi.

 

 16. Mwenyezi Mungu kwa Kitabu hichi anawaongoa kwenye njia ya uwokofu wanao elekea kutaka radhi zake, na anawatoa kwenye giza la ukafiri kuendea mwangaza wa Imani kwa tawfiki yake, na anawaongoza kwenye njia ya Haki.

 

 17. Hakika wamekufuru wale wanao dai ati Mwenyezi Mungu ndiye Masihi mwana wa Maryamu!! Ewe Mtume! Waambie hao wanao thubutu kuchezea cheo cha Ungu: Hapana ye yote anaye weza kuzuia matakwa ya Mwenyezi Mungu akitaka kumteketeza Isa na mama yake, na kuwahiliki wote waliomo katika ardhi. Kwani ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yao ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye huumba mfano autakao. Na Mwenyezi Mungu ana uweza mkubwa kabisa. Hashindwi na kitu.

 

 18. Na Mayahudi na Wakristo husema: Sisi ndio tulio fadhiliwa, kwani sisi ndio wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake atupendao. Waambie ewe Mtume! Basi kwa nini anakuadhibuni kwa dhambi zenu, na anakutieni katika moto wa Jahannamu? Waongo nyinyi! Nyinyi, kama wanaadamu wengineo, ni viumbe, na mtahisabiwa kwa vitendo vyenu. Na maghfira yamo mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake, humsamehe amtakaye. Na adhabu yake ni kwa amtakaye kumuadhibu. Kwani ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo baina yao  ni wa Mwenyezi  Mungu  tu,  na  kwake  Yeye  ndio marejeo ya mwisho.

 

 19. Enyi Watu wa Kitabu! Umekujieni ujumbe wa Mtume wetu ambaye anakudhihirishieni Haki, baada ya kusita ujumbe kwa muda wa zama, ili msitafute udhuru wa ukafiri wenu, kwa kudai ati kuwa Mwenyezi Mungu hakukuleteeni mbashiri wa kukupeni khabari njema, wala mwonyaji wa kukuhadharisheni. Sasa, basi, huyo amekujilieni mbashiri na mwonyaji. Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila jambo - na katika hayo mambo ni kutuma Mitume, na kukuhisabuni kwa mliyo nayo.

 

 20. Na taja, ewe Mtume! pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu kwa kushukuru na kut'ii, kwa kuwa amewateua Manabii wengi miongoni mwenu, na akakufanyeni watukufu kama wafalme baada ya kuwa mlikuwa wanyonge chini ya utawala wa Firauni, na akakupeni neema nyingi nyenginezo ambazo hawajapewa wowote wengineo.

 

 21.  Enyi watu wangu! T'iini amri ya Mwenyezi Mungu. Ingieni ardhi takatifu aliyo kujaalieni Mwenyezi Mungu muingie, wala msirejee nyuma kuwaogopa hao watu wake majabari, mkaja  kukosa nusura ya Mwenyezi Mungu na radhi zake.

 

 22. Wana wa Israili wakaikhalifu amri ya Mwenyezi Mungu na wakasema: Ewe Musa! Katika nchi hii wamo watu majabari. Sisi hatuna nguvu za kupambana nao. Basi hatutoingia humo maadamu wao wamo. Wakitoka basi tena hapo sisi tutaingia.

 

 23. Wawili kati ya wakubwa wao walio kuwa wanamwogopa Mwenyezi Mungu, na ambao Mwenyezi Mungu amewapa neema ya imani na ut'iifu, walisema:  Enyi watu! Waingilieni hao majabari wa mjini kwa kupitia mlangoni kwa ghafla. Mkifanya hivyo nyinyi mtawashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu peke yake katika mambo yenu yote, ikiwa nyiny ni wenye Imani ya kweli.

 

 24. Lakini wakakakamia katika ukhalifu wao. Wakasema: Ewe Musa! Sisi bila ya shaka yoyote tumekwisha azimia kuwa hatutaingia nchi hii kabisa, maadamu wamo hao majabari. Basi tuache na yetu; kwani wewe huna madaraka yoyote juu yetu. Nenda wewe na Mola wako Mlezi mkapigane nao hao majabari. Sisi tutakaa hapa hapa hatubanduki.

 

 25. Hapo tena Musa akamrejea Mola wake Mlezi akisema: Mola wangu Mlezi! Sina madaraka ila juu ya nafsi yangu na ndugu yangu. Basi tuhukumie baina yetu na hawa watu wakaidi.

 

 26. Mwenyezi Mungu akamuitikia Musa, akawapigia marfuku hao wakhalifu wasiingie nchi hiyo kwa muda wa miaka arubaini, wakipotea ovyo majangwani hawajui wendako wala watokako. Mwenyezi Mungu akamwambia Musa kama kumuasa: Usisikitike kwa masaibu yaliyo wasibu, kwani hawa ni wapotovu, wameiasi amri ya Mwenyezi Mungu.

 

 27. Hakika kupenda kutenda uadui ni tabia ya baadhi ya watu. Basi ewe Nabii! Wasomee Mayahudi - na wewe ni msema kweli - khabari za Haabila na Qaabila, wana wawili wa Adam. Kila mmoja alichinja dhabihu kama ni mhanga kwa kutaka kuruba kwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu alimkubalia mmoja kwa ajili ya usafi wa niya yake, na akamkatalia wa pili kwa kuwa niya yake haikuwa safi. Basi yule aliye kataliwa akamhusudu mwenzie na akamuahidi kuwa atamuuwa. Yule nduguye akamrudi kwa kumbainishia kuwa Mwenyezi Mungu hapokei a'mali ila kwa wachamngu walio safisha niya zao katika kule kutafuta kuruba.

 

 28. Akamwambia: Shetani akikuzuga hata ukaninyooshea mkono ili kuniuwa, mimi sitofanya kama hivyo, wala sitanyoosha  mkono wangu kwa ajili ya kukuuwa. Hakika mimi naogopa adhabu ya Mola wangu Mlezi, naye ndiye Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.

 

 29. Mimi sitakuzuia utapo taka kuniuwa ili upate kubeba dhambi za kuniuwa mimi pamoja na dhambi zako za tangu hapo za kutomsafia niya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo wewe unastahiki huko Akhera kuwa katika watu wa Motoni. Na hayo ni malipo ya haki ya Mwenyezi Mungu kumlipa kila mwenye kudhulumu.

 

 30. Basi nafsi yake ilimsahilishia kukhalifiana na maumbile, kumuuwa nduguye, akamuuwa. Kwa hivyo akawa kwa mujibu wa hukumu ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa walio khasiri, kwa kuwa ameipoteza imani yake na amempoteza nduguye.

 

 31. Baada ya kumuuwa yakamjia majuto na kubabaika. Akawa hajui amfanyeje maiti! Mwenyezi Mungu akampeleka kunguru akafukua udongo amzike kunguru mwengine aliye kufa, ili amfunze muuwaji vipi kumsitiri mwenzake aliye kwisha kufa. Alipo hisi uovu wa aliyo yatenda, alijuta kwa ukhalifu wake, akasema: Nimeshindwa hata kuwa kama kunguru huyu nikamsitiri ndugu yangu? Akawa basi miongoni wa walio juta kwa makosa yake, na kwenda kinyume na yanavyo takikana na maumbile.

 

 32. Kwa sababu ya uasi huo na kupenda kwa baadhi ya watu kuwafanyia uadui wenginewe, ndio tukawajibisha kumuuwa muuwaji, kwani mwenye kumuuwa mtu bila ya sababu zinazo pasa kisasi (1), au bila ya kufanya uharibifu katika nchi, ni kama amewauwa watu wote. Yeye huyo amemwaga damu za watu, na amewashajiisha wengine wafanye kama hayo. Kwa hivyo kumuuwa mmoja ni kama kuwauwa watu wote kwa kujiletea maudhiko  ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Na mwenye kumhuisha mtu kwa kumlipia kisasi, basi ni kama amewahuisha watu wote kwa kuhifadhi damu ya wanaadamu isimwagwe ovyo. Huyo anastahiki thawabu nyingi kutokana na Mola wake Mlezi. Sisi tumewatumia Mitume wetu kutilia mkazo hukumu yetu kwa dalili na hoja.  Kisha baadaye wengi miongoni mwa Wana wa Israili walipindukia mipaka katika uharibifu wao katika nchi.
(1) Maneno haya yanaonyesha kuwa kumfanyia uadui mtu mmoja ni kuwafanyia jamii ya watu, na kulipa kisasi ndio kuhuisha jamii. Katika Sharia ya Kiislamu kisasi ni haki ya waliy-amri, yaani aliye mkhusu maiti. Akipenda atasamehe achukue fidiya, na akipenda atataka kisasi na akitimize. Naye anapo samehe anayo haki ya kumfedhehesha mkosefu akiwa amekithiri uwovu wake na uharibifu.

 

 33. Hakika adhabu ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kuacha hukumu za Sharia, na wakafanya uharibifu katika nchi kwa uharamia na kunyan'ganya mali, ni kuuliwa pindi wakiuwa, na kutundikwa msalabani, pindi wakiuwa na wakapokonya mali ya watu, na kukatwa mikono yao na miguu kwa mabadilisho (yaani mkono wa kulia na mguu wa kushoto, au kinyume cha hayo), pindi ikiwa watavamia watu njiani na kuwapokonya mali bila ya kuwauwa. Na ikiwa watawatisha watu tu, basi adabu yao ni kuhamishwa nchi au wafungwe. Adhabu hizo ni hizaya ya hapa duniani tu, na Akhera watapata adhabu kuu, nayo ni adhabu ya Motoni.

 

 34. Ila wale walio tubu, miongoni mwa hawa wanao piga vita nidhamu na wakavamia watu majiani, kabla hamjawatia mkononi mkawakamata. Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu itaondoka, itabaki juu yao haki za waja wa Mwenyezi Mungu wazirejeshe. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na rehema.
Katika hukumu hii inabainishwa kuwa Sharia inaangalia ukhalifu unao athiri jamii, na kwa hivyo adhabu yake ni kali kwa kuwafikiana na kitisho chake kwa wapendao amani. Mazingatio hapa si kwa mujibu wa kile kitendo cha ukhalifu, bali kwa mujibu wa kiasi ya kitisho na fazaa inayo letwa na hicho kitendo.

 

 35. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kwa kujitenga na anayo yakataza , na kut'ii amri zake. Na takeni kuyafanya yatakayo kukurubisheni kupata thawabu zake, nayo ni kutenda mambo ya ut'iifu na mambo ya kheri. Na wanieni kwa jihadi katika Njia yake kwa kuitukuza Dini yake na kuwapiga vita maadui zake. Huenda kwa hivyo mkafuzu mkapata karama zake na thawabu zake.

 

 36. Hakika walio kufuru hata lau kuwa wana kila namna ya mali yote yaliyomo duniani na mambo mengine yanayo onekana yenye maana katika uhai, na wakawa nayo mfano wa yaliyomo duniani juu ya hayo yaliomo humo, na wakataka yawe ni fidiya wajiokoe na adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama kwa ukafiri wao, basi fidiya hiyo yote haitofaa kitu. Wala Mwenyezi Mungu hawakubalii hayo. Hapana njia yo yote ya wao kuepukana na malipo ya ukafiri wao;  nao watapata adhabu kali.

 

 37. Hawa makafiri wanatamani kutoka Motoni, na wala hawatatoka humo. Watapata adhabu ya daima dawamu.

 

 38. Na mwanamume aliye iba, na mwanamke aliye iba, ikateni mikono yao kuwa ni malipo ya madhambi waliyo yatenda, na njia ya kuwaonya wenginewe wasitende jambo hilo. Hiyo ni hukumu ya Mwenyezi Mungu, na amri ya Mwenyezi Mungu ndiyo yenye kushinda, naye ndiye Mwenye hikima katika kutunga Sharia. Kila ukhalifu ameuwekea malipo yake, yenye kumzuia mtu asitende tena na wengine watahadhari wasifanye kama hayo. (Ajabu iliopo ni kuwepo wajinga wakashtushwa na amri hii ya Mwenyezi Mungu aliye tuumba, na wasiseme lolote kuwa katika China wakati wa vita na Taiwan ilikuwapo sharia ya kuwa mwizi auwawe, na katika baadhi ya wilaya za Amerika mpaka hii leo ipo sharia ya kuwa mwizi wa farasi auwawe, na katika Kenya adabu ya wizi wa kutumia nguvu ni kunyongwa, na katika sharia za Kiingereza na nchi zote za magharibi mtu ana haki ya kuuwa kwa ajili ya kulinda mali na roho. Ikiwa ni haki ya mtu kumuuwa atakaye kuja kwiba, jee ni kuu hilo kwa serikali kumkata mkono aliye kwisha iba?) Kwa kuwepo sharia kama hii ndiyo ikawa wizi umetoweka katika nchi kama Saudi Arabia, na ukawa vururu kwengineko.

 

 39. Lakini mwenye kutubu baada ya kutenda kosa lake hilo, na akatengeneza vitendo vyake, na akanyoosha mwendo wake, basi Mwenyezi Mungu hakika humkubalia toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi mno wa kusamehe na kurehemu.

 

 40. Jua, ewe mwenye fahamu, kwa ujuzi wa yakini, ya kwamba ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kumiliki kila kitu kiliomo katika mbingu na ardhi. Yeye humpa adhabu yake amtakaye, kwa hikima yake na uwezo wake. Na humsamehe amtakaye, kwa hikima yake na rehema yake. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

 

 41. Ewe Mtume! Visikuhuzunishe vitendo vya makafiri wanao wania ukafiri wa kila aina, hawa wadanganyifu wenye khadaa wasemao kwa ndimi zao: Tumeamini, ilhali nyoyo zao hazifuati haki. Na miongoni mwa Mayahudi wapo wanao kithiri kusikiliza uzushi wa makohani wao na wanayakubali, na wanakisikiliza na kukikubali kikundi maalumu miongoni mwao, na hawaji barazani kwako  kwa sababu ya kiburi na chuki! Na hawa huyageuza maneno ya Taurati kutokana pahala pake, baada ya Mwenyezi Mungu kwisha yasimamisha na kuyahukumia! Nao huwaambia wafwasi wao: Mkipewa maneno haya yaliyo potoshwa na kubadilishwa yakubalini na muyafuate. Na kama mkipewa mengine tahadharini nayo msiyakubali. Basi, ewe Mtume! Usihuzunike Mwenyezi Mungu akimhukumia mtu kupotea  kwa  kumziba moyo wake,  wewe hutoweza kumwongoa, au  kumnafiisha  kwa chochote asicho mtakia Mwenyezi Mungu. Na hao ndio walio pita mipaka katika upotovu na inda. Mwenyezi Mungu Mwenyewe hakutaka kuzisafisha nyoyo zao na uchafu wa chuki, na inadi, na ukafiri. Duniani watapata madhila, kwa kufedheheka na kushindwa, na Akhera watapata adhabu kuu.

 

 42. Hao hukithiri kusikiliza ili wapate kuzua, na hukithiri kula mali ya haramu ambayo hayana baraka yoyote, kama  vile  rushwa na riba na mengineyo. Basi wakikujia kukutaka uwahukumu, wewe wahukumu pindi ukiona hayo yana maslaha, au jipuuze nao. Na ukijipuuza nao hawatokudhuru kwa lolote, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye wa kukulinda na watu. Na ukihukumu baina yao basi hukumu kwa uadilifu alio kuamrisha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda waadilifu, naye huwahifadhi na huwalipa thawabu.

 

 43. Ama ajabu ya watu hawa Mayahudi! Vipi wanataka hukumu yako na hali wao wanayo hukumu ya Mwenyezi Mungu imeandikwa katika Taurati? Na kinacho staajabisha ni kuwa wao huikataa hukumu yako inapo kuwa haikubaliani na mapendeleo yao, ijapo kuwa imewafikiana na ilivyo katika kitabu chao! Watu hawa sio miongoni mwa Waumini wanaoit'ii Haki.

 

 44. Hakika Sisi tumemteremshia Musa Taurati. Ndani yake mna uwongofu unao endea Haki, na mna bayana yenye kutoa mwangaza unao nawirisha hukumu wanazo zihukumia Manabii, na wale walio safisha nafsi zao kwa ajili ya Mola wao Mlezi, na wanazuoni wenye kufwata njia ya Manabii, na wale walio chukua ahadi kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu kisibadilishwe, kwa kukilinda na kushuhudia kuwa hicho ndiyo Haki. Basi msiwakhofu watu mnapo hukumu, na nikhofuni Mimi tu, Mimi Mola wenu Mlezi, Mola Mlezi wa walimwengu wote. Wala msizibadilishe Aya zangu nilizo ziteremsha kwa thamani duni ya kutaka starehe ya dunia, kama vile mrungura au kutaka cheo! Na wote wasio hukumu kwa mujibu alivyo teremsha Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa makafiri.

 

 45. Tumewalizimisha Mayahudi katika Taurati wafuate sharia ya kisasi kwa ajili ya kuhifadhi maisha ya watu. Basi tukahukumu mwenye kuuwa auwawe. Mwenye kutofoa jicho la mtu atofolewe. Kadhaalika pua kwa pua, sikio kwa sikio, jino kwa jino, na jaraha hivyo hivyo lilipiziwe kisasi ikimkinika. (Hiyo ni hukumu ya Mayahudi kama ilivyo katika Kutoka 21.23-25; Mambo ya Walawi 24.18-21; Kumbukumbu la Torati 19.21. Katika Uislamu ipo fursa ya msamaha.)
Mwenye kusamehe akatolea sadaka ile haki ya kulipiza kisasi kwa mkhalifu, basi hiyo sadaka huwa ni kafara kwake. Mwenyezi Mungu naye atamfutia sehemu ya madhambi yake. Na watu wasio hukumu kwa mujibu wa alivyo teremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio wenye kudhulumu.

 

 46. Na baada ya hawa Manabii tulimtuma Isa mwana wa Maryamu, naye ni mwenye kufuata njia yao, na kuithibitisha Taurati iliyo mtangulia. Naye tulimteremshia Injili  yenye uwongofu kuelekea Haki, na yenye kubainisha hukumu, na tuliiteremsha ili isadikishe Taurati iliyo tangulia, na ndani yake pana uwongofu wa kupelekea Haki, na ni mawaidha kwa wachamngu. (Tazama Injili ya Mathayo 5.17 maneno ya Nabii Isa: "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.")

 

 47. Na Sisi tuliwaamrisha wafuasi wa Isa, yaani Watu wa Injili, Wakristo, wahukumu kwa hukumu alizo teremsha Mwenyezi Mungu. Na wasio hukumu kwa mujibu wa alivyo teremsha Mwenyezi Mungu basi hao wameiacha  Sharia ya Mwenyezi Mungu, ni waasi.

 

 48. Na wewe, ewe Nabii, tumekuteremshia Kitabu kikamilifu, nacho ni Qur'ani, chenye kushikamana na haki katika hukumu zake zote na khabari zake, chenye kuwafikiana na kuthibitisha Vitabu vyetu vilivyo tangulia, na kinavishuhudia kuwa ni Vitabu vya Mwenyezi Mungu, na kinalinda yaliyo sahihi, kwa sababu hii Qur'ani haibadiliki. Basi hukumu baina ya Watu wa Kitabu, Mayahudi na Wakristo, wakikutaka uwahukumu kwa mujibu alivyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Wala katika hukumu yako usifuate matamanio yao na matakwa yao, usije ukapotoka ukaacha Haki iliyo kujia.  Kila umma katika nyinyi watu, tumeujaalia kuwa na njia yake ya kuitambua Haki, na njia iliyo wazi ya Dini ya kuifuata. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka angeli kufanyeni nyote kundi moja lililo wafikiana, lenye mwendo mmoja, hazikhitalifiani njia zake za kupita kwa zama zote. Lakini Yeye amekujaalieni hivi ili iwe kama mtihani kwenu katika hizo Sharia alizo kupeni, atambulikane mwenye kut'ii na mwenye kuasi. Basi tumieni fursa hii, na mfanye haraka kuwania kutenda vitendo vya kheri. Kwani marejeo yenu nyote yatakuwa kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Hapo atakwambieni hakika ya hayo mliyo kuwa mkikhitalifiana, na kila mmoja wenu atalipwa kwa a'mali yake.

 

 49. Na wewe ewe Mtume! Tumekuamrisha uhukumu baina ya watu kwa alivyo teremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matakwa yao katika kuhukumu. Na wahadharishe wasije kukugeuza ukaacha baadhi ya aliyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Pindi wakiipuuza hukumu ya Mwenyezi Mungu na wakataka nyengineyo, basi jua kuwa Mwenyezi Mungu anataka kuwapatiliza kwa kuwafisidia mambo yao, kwa vile zilivyo kwisha fisidika nafsi zao kwa sababu ya madhambi yao waliyo yatenda kwa kukhalifu hukumu zake na Sharia yake. Kisha  atawalipa vitendo vyao vyote huko Akhera (1). Na hakika watu wengi ni wenye kuziasi hukumu za Sharia.
(1) Maneno haya yanatukuza Sharia ya Kiislamu katika kuwahukumu watu. Kwanza  inatukuka kwa kuwa ni hukumu ya uadilifu na haifuati mipango ya watu ijapo kuwa ni mipotovu, bali inahukumu juu ya hiyo mipango ya watu kwa kheri na shari. Pili Kanuni huwa katika dola ni moja tu kwa watu wote na mat'abaka yote.

 

 50. Je, hao wanao kataa amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu wanataka wahukumiwe kwa hukumu ya Kijahiliya, ya kijinga,  ya kabla ya kufika Uislamu, kulipo kuwa hapana uadilifu, bali matamanio  ya nafsi tu ndiyo yliyo kuwa yakihukumu, na mapendeleo na udanganyifu ndio msingi wa hukumu?  Huo ndio mwendo wa watu wa zama za Kijahiliya! Yuko aliye bora kuliko Mwenyezi Mungu kuhukumu watu wenye kuyakinika na Sharia na wenye kunyenyekea Haki? Kwa hakika hao ndio wanao tambua ubora wa hukumu za Mwenyezi Mungu.

 

 51. Enyi mlio amini! Si halali kwenu kuwachukua Mayahudi na Wakristo mkawafanya ndio marafiki zenu. Wao hao ni sawa sawa katika kukufanyieni uadui. Na mwenye kufanya urafiki nao, basi ni kundi moja nao. Na hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi wanao jidhulumu nafsi zao kwa kufanya urafiki na makafiri.

 

 52. Ilivyo kuwa kuwafanya hao marafiki hawafanyi ila walio dhulumu, basi utaona kuwa wanao wafanya makafiri ndio rafiki zao wana maradhi katika nyoyo zao, maradhi ya udhoofu na unaafiki. Wao husema: Tunaogopa usije kutupata msiba kwa kugeuka mambo na wao wasitusaidie!  A'saa, huenda, Mwenyezi Mungu akamletea Mtume wake kufunguka mambo, na Waislamu wakawashinda maadui zao, au ukadhihiri unaafiki wa hao wanaafiki, wakaamkia majuto, wakijuta kwa zile kufuru na shaka shaka walizo kuwa wakizificha katika nafsi zao.

 

 53. Na hapo tena Waumini wa kweli watasema kuwastaajabia wanaafiki: Ndio hawa walio kula yamini kwa viapo vya kupita kiasi kwa jina la Mwenyezi Mungu, ya kwamba wao ni wenzenu katika Dini, wenye kuamini kama nyinyi? Wamesema uwongo! Na vitendo vyao vimefisidika, wakawa wamekosa Imani na nusura kutokana na Waumini.

 

 54. Enyi mlio amini! Mwenye kurejea ukafirini katika nyinyi, baada ya kuamini, hamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Yeye ametukuka na hayo. Badala yao ataleta kaumu iliyo bora kuliko hao, na wao hao Mwenyezi Mungu atawapenda, na atawafikisha kwenye uwongofu, na ut'iifu. Na wao watampenda Mwenyezi Mungu, kwa hivyo watamt'ii. Nao watakuwa na unyenyekevu na huruma kwa ndugu zao Waumini, na watakuwa wakali na wenye nguvu mbele ya maadui zao makafiri. Watapigana jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama yoyote ya mwenye kulaumu! Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu humpa amtakaye anaye muwafikia kheri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa fadhila kwa anaye stahiki.

 

 55. Enyi Waumini!  Urafiki wenu nyinyi uwe na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na nyinyi kwa nyinyi katika wanao shika Sala, na wanatoa Zaka, nao wananyenyekea.

 

 56. Na mwenye kufanya urafiki na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Waumini na wakawa hao ndio wa kuwategemea kwa msaada na nusura, basi huyo atakuwa katika Hizbu (yaani kundi) ya Mwenyezi Mungu, na Hizbu ya Mwenyezi Mungu ndio yenye kushinda na kufuzu.

 

 57. Enyi mlio amini! Msiwafanye maadui wa Uislamu walio ifanyia maskhara Dini yenu wakaichezea - nao ni Mayahudi na Wakristo na washirikina, kuwa ndio wasaidizi, wala msifanye urafiki nao. Na mkhofuni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni wakweli katika Imani yenu.

 

 58. Na katika kejeli zao kukufanyieni ni vile pale mnapo ita kwenda kusali katika adhana, wao huifanyia maskhara Sala yenu, na hukuchekeni, wakafanya ni mchezo. Na hayo ni kwa sababu kuwa wao ni kaumu wasio na akili, wala hawatambui farka iliopo baina ya upotofu na uwongofu.

 

 59. Sema ewe Mtume! Enyi Watu wa Kitbu! Hivyo mnatuchukia kwa kuwa tunamuamini Mwenyezi Mungu na tunaamini tuliyo teremshiwa sisi, nayo ni Qur'ani, na Vitabu vilio sahihi vilio teremshiwa Manabii wa zamani, na kwa kuwa tunaamini kuwa wengi wenu mmeitupa Sharia ya Mwenyezi Mungu?

 

 60. Waambie: Nikwambieni malipo maovu kabisa kutokana na Mwenyezi Mungu? Ni hivyo vitendo vyenu nyinyi mlio tengwa mbali na Mwenyezi Mungu na rehema yake, na mkakasirikiwa kwa sababu ya ukafiri wenu na uasi wenu, na mkazibwa nyoyo zenu, mkawa kama manyani na nguruwe, na mkamuabudu Shetani, na mkafuata upotovu. Nyinyi ndio mko katika daraja ya mwisho katika shari, kwa sababu nyinyi ni watu walio potea kabisa, mkaiwacha Njia ya Haki.

 

 61. Wanaafiki wakikujia husema uwongo, na hukwambia: Tumeamini. Nao wamekuingilia na hali ni makafiri, na wametoka kwenu nao ni makafiri vile vile!  Na Mwenyezi Mungu anaujua vyema unaafiki wanao uficha. Na Yeye ndiye atakaye waadhibu.

 

 62. Na utawaona wengi wao hawa wanakimbilia kufanya maasi na kuwatendea uadui wengineo, na pia katika kula mali ya haramu kama rushwa (mrungura) na riba! Uwovu gani huu wautendao!

 

 63. Si ingelikuwa vyema lau kuwa wanazuoni wao na makohani wangeli wakataza kusema uwongo, na kula haramu? Uwovu mkubwa huo wanao ufanya kwa kuacha kusemezana na kukatazana maasi.

 

 64. Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba, haukukunjuka ukatoa! Mwenyezi Mungu ameifumba mikono yao wao, na amewatenga mbali na rehema yake! Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, anajitosha. Yeye hutoa apendavyo. Na hakika wengi wa watu kwa kupita kiasi katika upotovu wao, haya yalio teremka kwako huwazidisha udhalimu na ukafiri, kwa sababu ya chuki na husda yao. Na Sisi tumetia baina yao kwa wao uadui na bughdha mpaka Siku ya Kiyama. Kila wanapo washa moto kumpiga vita Mtume na Waumini, Mwenyezi Mungu huuzima kwa kumpa ushindi Nabii wake na wafuasi wake. Na wao wanajitahidi kueneza fisadi katika nchi, na kufanya vitimbi, na kutia fitina, na kuchochea vita. Na Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.

 

 65. Na lau kuwa Watu wa Kitabu, yaani Mayahudi na Wakristo, wangeli uamini Uislamu na Nabii wake, na wakaacha madhambi tuliyo yataja, tungeli wafutia makosa yao, na tungeli watia katika Bustani (Pepo) za neema, wakastarehe humo.

 

 66. Na lau kuwa wao wamezihifadhi Taurati na Injili kama zilivyo teremshwa, na wakazitenda, na wakaamini yote waliyo teremshiwa kutokana na Mola wao Mlezi, nayo ni Qur'ani, Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia riziki ikiwajia kutoka kila upande. Na wao si wote sawa katika upotovu. Miongoni mwao, wapo jamaa walio waadilifu, wana akili zao timamu. Hao ndio wale walio muamini Muhammad na wakaiamini Qur'ani. Lakini wengi wao wanatenda vitendo viovu, na wanasema mabaya, na wanajitenga na haki.

 

 67. Ewe uliye tumwa na Mwenyezi Mungu! Waeleze watu yote uliyo funuliwa na Mola wako Mlezi, na waite wafuate huo ujumbe, wala usiogope maudhi ya yeyote. Na ukitofanya hivyo basi imekuwa hukufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Kwani wewe umekalifishwa ufikishe ujumbe kwa watu wote. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na maudhi ya makafiri. Ni mtindo wake Mwenyezi Mungu kuwa hamnusuru aliye potea akaiacha Haki.  Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi makafiri kwenye Njia iliyo kaa sawa.

 

 68. Ewe Mtume! Waambie Watu wa Kitabu (yaani Biblia): Hakika nyinyi hamtakuwa mnafuata Dini sahihi ila mtapo zitangaza hukumu zote za Taurati na Injili na mkazitenda. Na mkaiamini Qur'ani iliyo teremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kwa ajili ya kuwaongoa watu.  Na yakinika, ewe Mtume, kwamba wengi wa Watu wa Kitabu watazidi udhalimu, na ukafiri, na inadi, juu ya Qur'ani kwa uhasidi wao na chuki. Basi usiwahuzunikie watu ambao wametiwa muhuri wa upinzani.

 

 69. Hakika walio muamini Mwenyezi Mungu (yaani Waislamu), na wafwasi wa Musa katika Mayahudi, na walio toka kwenye dini nyenginezo, na wafwasi wa Isa katika Manasara - wote hao wakisafisha imani yao kwa Mwenyezi Mungu, na wakaamini kufufuliwa na malipo na wakatenda mema kama ilivyo funzwa na Uislamu, hao wote watasalimika na adhabu na watakuwa katika furaha ya Peponi Siku ya Kiyama.

 

 70. Sisi tuliagana na Mayahudi, Wana wa Israili, kwa agano madhubuti katika Taurati kuwa wafuate hukumu zake. Na tukawapelekea Manabii wengi wawabainishie, na wawatilie mkazo ahadi yetu. Lakini walivunja ahadi.Wakawa kila akiwajia Mtume ambaye hakuwafikiana na matamanio yao, ama walimkanusha au walimuuwa.

 

 71. Na hao Wana wa Israili walidhani hawatapata majaribio, yaani shida za kuwafafanua baina ya walio simama imara na wasio simama imara. Kwa hivyo hawakuweza kustahamili, bali wengi wao walipotea wakawa kama vipofu na viziwi. Wakaiacha Haki, na Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa madhila. Baadae walipo rejea kwa Mwenyezi Mungu na wakatubu, alikubali toba zao, na akawarejeshea utukufu wao. Lakini baadae tena wakaingia katika upotofu, na wakawa kama vipofu na viziwi! Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema, na atashuhudia vitendo vyao, na atawalipa kwavyo.

 

 72. Wenye kudai kuwa Mwenyezi Mungu yu katika Isa bin Maryam hata akawa yeye Mungu, kama wasemavyo Wakristo hii leo, hakika wamekufuru! Yeye Isa hana dhambi ya haya, kwani hakupata kudai hivyo hata mara moja. Bali yeye aliwaamrisha Wana wa Israili wamsafie imani Mwenyezi Mungu peke yake kwa kusema: Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye niumba mimi na nyinyi, na ndiye anaye niendeshea mambo yangu yote, na kwamba kila mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu malipo yake ni kuwa hatoingia Peponi kabisa, bali ataingia Motoni, kwa kuwa amekiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuvunja mipaka yake hataepuka na adhabu.(Yesu kasema: "Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja." Marko 12.28. "Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe".Yohana 5.30 "Ninapaa kwenda kwa...Mungu wangu naye ni Mungu wenu." Yohana 20.17 )

 

 73. Haiwi mwenye kudai kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja katika Utatu, kama wadaivyo Wakristo sasa, awe anamuamini Mwenyezi Mungu.!! Na hakika iliyo thibiti ni kuwa hapana mungu ila Mwenyezi Mungu mmoja pekee. Na ikiwa hawa walio potoka hawatoacha itikadi zao potovu, wakarejea kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu, hapana budi ila itawasibu adhabu kali. (Biblia inasema kuwa ya kwanza katika Amri Kumi alizo pewa Musa ni: "Usiwe na miungu mingine ila mimi." - Kutoka 20.3. "Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa Bwana ndiye Mungu, hapana ila yeye." - Kumbukumbu la Torati 4.35. Katika Injili ya Yohana 17.3 Yesu anamsemeza Mwenyezi Mungu: "Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma.")

 

 74. Je! Watu hawa hawaziachilii mbali hizo itikadi za uzushi na uwongo, wakarejea kwenye Imani ya Mwenyezi Mungu, na wakaomba wafutiwe dhambi zao walizo zitenda? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira, Mwingi wa rehema.

 

 75. Isa bin Maryamu si chochote ila ni mwanaadamu aliye pata neema ya Mwenyezi Mungu kwa kuteuliwa kuwa ni Mtume kama walivyo mtangulia wengi kabla yake. Na Mama yake Isa ni mmoja katika wanawake, aliye jaaliwa kuwa ni mkweli katika kauli yake na mwenye kumuamini Mola wake Mlezi. Na yeye na mwanawe, Isa, walikuwa wana mahitajio yanayo hitajiwa na kila mwanaadamu, kama kula na kunywa, na kwenda haja. Na hizo ni dalili za ubinaadamu wao. Basi hebu zingatia, ewe mwenye kusikia, hali ya hao walio ingia upofu hata hawaoni dalili za Ishara zilizo wazi ambazo amewabainishia Mwenyezi Mungu. Tena zingatia vipi wanaiacha Haki juu ya kuwa ni iwazi kabisa.

 

 76. Ewe Mtume! Waambie hawa wapotovu: Vipi mnamuabudu mungu asiye weza kukudhuruni kwa lolote mkiacha kumuabudu, wala hawezi kukufaeni kwa lolote mkimuabudu!! Vipi mnaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu ambaye Yeye ndiye Mungu Mwenye uweza wa kila kitu, naye ni Mwenye kusikia, na Mwenye ujuzi.

 

 77. Ewe Mtume! Waambie Watu wa Kitabu, yaani Mayahudi na Wakristo: Mwenyezi Mungu anakukatazeni msivuke mipaka katika itikadi zenu hata mkaingia katika upotovu, mkawafanya baadhi ya viumbe vyake kuwa ni miungu; au mkakanusha ujumbe wa baadhi ya Mitume. Na anakukatazeni kufuata matamanio ya watu walio kutangulieni, walio acha njia ya uwongofu, na wakawazuia watu wengi kuifuata njia hiyo, na wakaendelea katika kuiepuka Njia ya Haki.

 

 78. Mwenyezi Mungu amewatenga mbali na rehema yake wale makafiri miongoni mwa Wana wa Israili, na haya yameteremka katika Zaburi juu ya Nabii wake Daud, na katika Injili juu ya Nabii wake Isa mwana wa Maryam. Na hayo ni kwa sababu ya uasi wao, kutokana na ut'iifu wa Mwenyezi Mungu na kuzama kwao katika udhalimu na ufisadi.(Katika Zaburi Daud anawaapiza Mayahudi:"Wewe, Mungu, uwapatilize. Na waanguke kwa mashauri yao, Uwatoe nje kwa ajili ya wingi wa makosa yao, kwa maana wamekuasi Wewe." - Zaburi 5.10. Katika Injili Yesu anawalaani: "Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehannum?" - Mathayo 23.33.)

 

 79. Mtindo wao ulikuwa kutoambizana. Hapana amkatazaye mwenzie kufanya uovu. Kufanya kwao uovu na kuacha kukatazana ni katika vitendo vinavyo chusha mno!

 

 80. Utawaona wengi miongoni mwa Wana wa Israili hufanya urafiki na washirikina, mapagani, na wanawafanya hao ndio wenzi wao wakishirikiana katika kuupiga vita Uislamu! Kitendo hichi kiovu wanajirimbikizia wenyewe nafsi zao, waje kupata malipo yake kwa kupata ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na wapate kudumu milele katika adhabu ya Jahannamu.(Hayo yalikuwa zama za Mtume s.a.w. na mpaka hii leo. Mayahudi wanatafuta kila rafiki ambaye atauvunja Uislamu, ilhali yafaa wawaone Waislamu ndio wa karibu mno nao, kwa kuwa wanaamini Mungu Mmoja na wanaamini Manabii wao wote.)

 

 81. Na lau kuwa itikadi yao ni sawa kama inavyo faa iwe kwa kumuamini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake Muhammad s.a.w., na Qur'ani aliyo teremshiwa, basi wasingeli wafanya makafiri kuwa ni wenzao kuwapinga Waumini. Lakini wengi miongoni mwa Wana wa Israili ni maasi, wameacha dini.

 

 82. Ewe Nabii! Tunakuhakikishia ya kwamba utaona hapana watu wanao kuchukia na kukubughudhi wewe na wanao kuamini kama Mayahudi na hawa wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu katika ibada. Na utawakuta walio karibu mno nawe kwa mapenzi ni wafwasi wa Isa, walio jiita wenyewe "Manasara". Kwa sababu wamo miongoni mwao makasisi wanao ijua dini yao, na marahibu (mamonaki) wat'awa, wanao mcha Mola Mlezi, na kuwa wao hawana kiburi cha kuwazuia wasisikie Haki. (Na haya yameonakana kuwa Waislamu wengi duniani asili yao walikuwa Manasara, Wakristo. Wao wakisha pata fursa ya kuufahamu Uislamu huufuata, lakini ni wachache miongoni mwa Mayahudi walio silimu. Kinacho wazuia ni kiburi. Lakini walio silimu basi wamekuwa Waislamu wakubwa.)

 

 83. Na pia miongoni mwa Manasara wakiisikia Qur'ani aliyo teremshiwa Mtume huathirika nayo, macho huwatiririka machozi, kwa kuwa wanajua kuwa wanayo yasikia ni kweli tupu, basi nyoyo zao humili kwayo, na ndimi zao huomba dua kumwomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: Mola wetu Mlezi! Tumekuamini Wewe na Mitume wako, na Haki ulio wateremshia. Basi ipokee Imani yetu, na utufanye miongoni mwa Umma wa Muhammad ulio wafanya mashahidi na hoja kwa watu wote Siku ya Kiyama.

 

 84.   Na  nini cha kutuzuia tusimsadiki Mwenyezi Mungu peke yake, na Haki iliyo teremka kwa Muhammad? Na hali sisi tunamtaraji Mwenyezi Mungu atuingize Peponi pamoja na watu wenye Imani njema na vitendo vyema.

 

 85. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu amewaandikia malipo kwa vile kuungama kwao, nayo ni Bustani yenye kupita mito chini ya miti yake, na majumba ya fakhari ya kukaa humo daima, pamoja na watu ambao ni njema itikadi zao na vitendo vyao.

 

 86.   Na  walio  mpinga  Mwenyezi  Mungu  na  Mitume  wake, na wakazikanya  dalili   alizo   wateremshia   kuwa   ni uwongofu  wa kufikia Haki, ni wao peke yao wanao stahiki adhabu kali katika Jahannamu.

 

 87. Enyi mlio amini! Msijiharimishie nafsi zenu vitu vizuri alivyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, wala msipite mipaka aliyo kuwekeeni Mwenyezi Mungu ya kufuata mambo ya wastani. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi watu wanao pindukia mipaka.

 

 88. Na kuleni vitu alivyo kupeni Mwenyezi Mungu na akavifanya vyepesi kwenu, na akavifanya ni halali na ni vizuri kwa nafsi zenu. Na daima mwogopeni Mwenyezi Mungu, na mt'iini Yeye maadamu nyinyi mnamuamini Yeye.

 

 89. Mwenyezi Mungu hakutiini adabu kwa sababu ya kuapa kiapo msicho kusudia. Bali hakika Yeye hukutieni adabu kwa sababu ya kuvunja viapo mlivyo vikusudia na yamini mliyo jifunga nayo. Basi ikiwa mmevunja kiapo itakupaseni mfanye jambo la kukughufirieni dhambi zake. Na  mambo yenyewe ni: kuwalisha mafakiri kumi kwa siku moja, kwa chakula cha kawaida mnacho kila nyinyi na jamaa zenu mnao waangalia, yaani watu wenu wa nyumbani bila ya israfu wala ubakhili. Au kuwavika mafakiri kumi kwa kivazi kilicho zowewa. Au kumkomboa mtu kutoka utumwani. (Na mfano wa mtumwa ni mtu alioko kifungoni kwa dhulma, au chini ya utawala wa dhulma.)  Ikiwa mwenye kuapa hawezi kutenda lolote katika hayo, basi itampasa afunge siku tatu. Na kila moja katika mambo haya hufuta dhambi za mwenye kuapa kiapo cha kutilia niya na akakivunja. Nanyi zilindeni yamini zenu, msiape katika mambo yasiyo kuwa laiki yake, na wala msiache kutenda kitendo cha kughufiria dhambi pindi mkivunja kiapo. Kwa mpango huu Mwenyezi Mungu anakufafanulieni hukumu zake ili mpate kushukuru neema zake kwa kuzijua na kuzifuata vilivyo.
Katika hukumu ya yamini pana mawili yafaa tuyazingatie.  Kwanza: Uislamu umeraghibisha sana kukomboa watumwa. Sababu nyingi zinazo wajibisha hayo. Kafara nyingi za dhambi zinahitaji kukomboa. Kafara ya kula mchana Ramadhani yahitaji ukombozi, n.k. Na katika hayo yanaonyesha Uislamu unachukia utumwa. Uislamu uliukiri utumwa kwa kuwa maadui wao walikuwa wakiwatia utumwani Waislamu, basi na Uislamu ukaruhusu kuwatendea wao vivyo hivyo.   Pili: Uislamu unakazania kulisha masikini kila ikipatikana fursa.

 

 90. Enyi wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu na Vitabu vyake na Mitume wake, wenye kuifuata Haki! Kunywa au kuvuta chochote kinacho lewesha, kucheza kamari, na kusimamisha mawe ya kutolea mihanga kwa ajili ya masanamu mnayo yaabudu, na kuagua kwa mishale (1), na mawe, na karatasi za kuagulia kudra iliyo ghaibu...yote hayo si chochote ila ni uchafu wa kiroho, na upotovu. Na hayo ni kupambiwa na Shetani tu. Basi yaachilieni mbali ili mpate kufuzu duniani kwa maisha bora, na Akhera mpate Janna yenye neema.
(1) Kuagua kwa mishale: ilikuwa ikiandikwa juu ya vijiti, kimoja kiliandikwa: "Mola wangu Mlezi kaniamuru", na kingine:"Mola wangu Mlezi kanikataza", na kingine hakikuandikwa kitu. Hutiwa vijiti hivyo katika mfuko kisha huchanganywa, na kohani hutia mkono wake akachomoa kimojapo, na akamjuvya mwenye kuuliza lilio aguliwa.

 

 91. Bila ya shaka Shetani hana atakalo kwa kukushawishini kunywa ulevi na kucheza kamari ila kuleta khitilafu na ugomvi na kuchukiana baina yenu ili mdhoofike kwa kuondoka masikizano, na uvunjike umoja wenu, kwa sababu anavyo kukupendeleeni mnywe ulevi na mcheze kamari. Na hayo ili mpate kuacha kumuabudu Mwenyezi Mungu, na muache Sala, ili Akhera yenu iwe ovu kama ilivyo dunia yenu. Basi jee! Baada ya nyinyi kujua maovu haya hamyatupilii mbali ninayo kukutazeni, mkamkosesha Iblisi makusudio yake?
Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliye takasika ametaja mambo mane yaliyo pelekea kuharimishwa ulevi na kamari:
* La Kwanza - Kuwa nafsi yake ni uchafu na uovu, kwani hayumkiniki kusifika kuwa ni mambo mazuri, kwa kuwa madhara yake yanaonekana wazi. Katika ulevi kuna uharibifu wa akili, na katika kamari ni kupoteza mali, na kwa yote mawili hayo upo uharibifu wa moyo. Na Shetani ndiye mwenye kuyapamba hayo.
* La pili - Hayo hueneza uadui na chuki. Kamari humalizikia ugomvi, na kama haifikii hayo basi huleta chuki na bughdha.  Na ulevi ndio Mama wa Maasi. Utamwona mtu mwenye adabu zake mpole, akisha kunywa hugeuka nyama mwitu, akatenda mambo ya ukhalifu, kwani ulevi huidhoofisha sauti ya utu inayo mkataza mwanaadamu kutenda maovu. Utamwona mtu anajizuia kufanya kitendo kiovu, lakini akisha kunywa ulevi, au akavuta bangi, japo kidogo, huiendea shari bila ya kujali. Basi si kama ulevi unaharibu akili tu, bali unalaza dhamiri ya mtu. Anakuwa hana junaha.
* La tatu: Ni kuwa kamari na ulevi huuwa moyo. Mtu huwa hamkumbuki Mwenyezi Mungu, na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndiko kunako huisha nyoyo.
* Lane: Maasi hayo yanamzuilia mtu na Sala. Kamari na ulevi humsahaulisha Muumini na Sala zake, na akiwa anasali hatimizi nguzo zake kama zitakikanavyo. Basi inakuwa Sala zake ni kuinama na kuinuka bila ya kufuatana na moyo.  Kwa hivyo basi imethibiti kuwa kuharimishwa mvinyo, pombe, tembo, bangi n.k. si kwa sababu ya kulevya kwake tu, bali ni kwa kumziba mtu fahamu zake, kumgubika asitambue atendalo. Na kwa hivyo ndio imepokewa kuwa kinacho levya kwa wingi wake, basi hata kidogo chake ni haramu, kwani hicho kidogo nacho kinapumbaza akili. Na juu ya haya pana madhara ya mwili kama madaktari walivyo thibitisha.
Kwa hivyo ulevi hata kidogo ni haramu. Mwenyezi Mungu Subhanahu ametaja sababu mbili za kuharimisha ulevi, na udaktari  umezidisha kuwa ulevi kidogo haupotezi akili, lakini huzidisha uchangamfu au husabibisha hali ya huzuni na kuona dhiki ya moyo. Na katika hali zote mbili anakuwa mtu amepungukiwa na ukamilifu wa akili yake kubeba jukumu, na kwa hivyo hutenda vitendo ambavyo kwa dhahiri ni sawa kumbe ni madhara. Ama kuuzoea ulevi hudhuru maini, matumbo, na mishipa ya akili na hisiya, na hurithisha madhara mpaka kwa vizazi.

 

 92. Na fuateni amri ya Mwenyezi Mungu na amri ya Mtume wake kwa yale anayo kuleteeni kutoka kwa Mola wake Mlezi. Na yaepukeni mbali yatakayo kuleteeni adhabu mnapo kwenda kinyume. Mkitofuata anayo kuamrisheni Mwenyezi Mungu kuweni na yakini kuwa Yeye atakupeni adabu. Wala nyinyi hamna udhuru wowote baada ya kuwa Mtume amekwisha wabainishieni adabu ya kupewa wakhalifu. Na hakika haimpasi Mtume wetu ila kukujuvyeni hukumu zetu tu, na kukubainishieni kwa ukamilifu wa uwazi.

 

 93. Walio mkubali Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakatenda mema, hawana dhambi kwa vyakula vya halali na vizuri wanavyo kula, wala vya haramu walivyo wahi kula zamani kabla hawajajua kuwa ni haramu, ikiwa wanamkhofu Mwenyezi Mungu na wakajitenga navyo vyakula hivyo baada ya kujua kuwa vinakatazwa. Kisha ikawa wao wakaendelea kumkhofu Mwenyezi Mungu na kuzikubali sharia zake, na kisha wakadumu katika khofu yao ya kumwogopa Mwenyezi Mungu katika kila hali, na wakawa wanafanya a'mali zao kwa usafi wa niya, na kwa njia ya ukamilifu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wenye ikhlasi katika vitendo vyao kwa kadri ya ikhlasi yao na a'mali yao.

 

 94. Enyi mlio amini! Hakika Mwenyezi Mungu anakufanyieni mtihani wakati wa Hija kwa kukuharimishieni baadhi ya wanyama na ndege ambao mnaweza kuwawinda kwa wepesi kwa mikono yenu na mikuki yenu. Makusudio ni kutaka wajuulikane ambao wanamt'ii Mwenyezi Mungu ijapo kuwa hawaonekani na watu. Na wanao pindukia mipaka aliyo iweka Mwenyezi Mungu baada ya kuibainisha watakuja pata adhabu kali.

 

 95. Enyi ambao mmeamini! Msiuwe nyama wa kuwinda nanyi mmenuia Hija na Umra na mmo kuzitimiliza.  Na mwenye kumuuwa mnyama kama huyo kwa kukusudia basi itampasa atoe fidiya mfano wa mnyama aliye muuwa, ikiwa katika ngamia, ng'ombe au kondoo. Na hujuulikana huyo mfano wake kwa kukadiriwa na watu wawili waadilifu kati yenu, wahukumu na wawape mafakiri kwenye Al Kaaba, au atoe badala yake awape, au atoe chakula kadiri ya yule mnyama kuwapa mafakiri. Kila fakiri apewe chakula cha kumtosha kutwa yake. Hayo ndio kuondoa dhambi za kuwinda kuliko katazwa. Au badala ya hayo yote, afunge idadi ya siku za kadri ya wale masikini iliyo mbidi kuwalisha lau angewalisha. Na Mwenyezi Mungu amelazimisha hayo ili huyo mwenye kufanya lile kosa apate kuhisi matokeo ya kosa lake na uwovu wa malipo yake. Mwenyezi Mungu, lakini, amesamehe ukhalifu ulio tendekea kabla ya jambo hilo halijaharimishwa. Na mwenye kurejea tena kufanya uovu baada ya kujua kuwa ni haramu, basi hakika Mwenyezi Mungu atampa adabu kwa kitendo chake, naye Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda hashindiki, Mkali wa kumuadhibu anaye kakamia kutenda dhambi. (Tunaona kuwa Uislamu ulianzisha kulinda mazingara, na utajiri wa asili tangu hapo kale. Kutokana na kuhifadhiwa wanyama na ndege wa porini huko Makka, ndio hii leo tunaona zipo nyanda na mapori yanayo hifadhiwa wanyama wake, kwa mujibu wa utaalamu wa kisasa.)

 

 96. Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni kuvua wanyama wa baharini, na muwale, na wanufaike kwao wakaazi wenyeji na wasafiri. Na amekuharimishieni kuwinda wanyama wa bara wasio fugwa kwa kawaida majumbani, katika muda ule unapo kuwa katika Hija au Umra, kwenye eneo takatifu linalo itwa Alharam. Na mzingatieni Mwenyezi Mungu, na iogopeni adhabu yake. Basi msende kinyume naye, kwani nyinyi mtarejea kwake Siku ya Kiyama, na hapo atakulipeni kwa yote mliyo yatenda. (Huu ni mfano katika mifano mingi ya Uislamu tangu hapo kale unavyo pendelea kulinda tabia ya mazingara kwa kuhifadhi wanyama wasiuliwe ovyo, na miti isikatwe ovyo, na hata maji ya mito na maziwa yasitumiwe kwa fujo, kwani Mwenyezi Mungu hawapendi wafujaji!)

 

 97. Mwenyezi Mungu ameijaalia Al Kaaba, nayo ni hiyo nyumba aliyo itukuza na akaharimisha watu na wanyama kufanyiwa uadui ndani yake na karibu yake, ameijaalia kuwa yenye kusimama na yenye kutukuzwa, na yenye kuwapa amani watu, na iwe ndiyo Kibla cha kuelekea watu katika Sala zao, na watu waiendee kwa Hija wawe ni wageni wa Mwenyezi Mungu, na ili watende yale ya kuupa nguvu umoja wao. Hali kadhaalika ameufanya mwezi wa Hija na wanyama wanao tolewa dhabihu, na khasa wale wanao vishwa vigwe ili watambuliwe na wanao waona kuwa hao wametolewa hidaya kwenye hiyo Nyumba. Na natija ya kuweka yote hayo ni kuwa mpate kuyakinika kuwa ujuzi wake Mwenyezi Mungu umeenea kila kitu kilioko mbinguni kunakotoka wahyi (ufunuo) wa sharia, na umeenea duniani, anako weka sharia ya kuwaletea watu maslaha yao. Na hakika ujuzi wa Mwenyezi Mungu umeenea juu ya kila kitu.

 

 98. Enyi watu! Jueni kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali, humteremkia anaye halalisha vya haramu, naye pia ni Mwingi wa kusamehe dhambi za mwenye kutubu na akaingia kumt'ii. Naye ni Mwenye rehema sana, na kwa hivyo hamchukulii mtu papo kwa papo kwa kila alitendalo.

 

 99. Haimlazimikii Mtume ila kuwafikishia watu anayo funuliwa yeye, ili isimame hoja juu yao na wasiwe na kisingizio chochote cha kuwa ati hawakuonywa wala hawakufunzwa. Basi yajueni anayo kuleteeni Mtume, kwani Mwenyezi Mungu anayajua mnayo dhihirisha na mnayo yaficha.

 

 100. Ewe Nabii! Waambie watu: Si sawa sawa vile vizuri anavyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu na vibaya anavyo kuharimishieni. Kwani farka iliyo baina ya viwili hivyo kwa Mwenyezi Mungu ni kubwa, na hata hivyo vibaya vingawa ni vingi na vinawapendeza watu wengi. Basi enyi wenye akili! Ufanyeni ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu uwe ni kinga yenu isikupateni adhabu yake kwa kukhiari vilivyo vyema, na kujiepusha na viovu, ili mpate kuwa miongoni walio fuzu duniani na Akhera.

 

 101. Enyi mlio amini! Msimuulize Nabii mambo ambayo Mwenyezi Mungu amekuficheni mkataka yafichuliwe, na mkamuuliza Nabii katika uhai wake, kwani Qur'ani inamteremkia bado. Na Mwenyezi Mungu atakubainishieni itapo hitajika. Mwenyezi Mungu amekusameheni kwa yasiyo tajwa, hatokuadhibuni kwayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, na Mwenye wasaa katika upole. Basi hana papara katika kuadhibu.

 

 102. Katika jamaa walio kutangulieni walikuwapo walio uliza mfano wa haya, mambo mazito mazito;  na Manabii wao walipo wakalifisha ya kufanya wakaona mazito kuyatenda, wakayaacha, na wakawa ni wenye kuyakanya. Kwani Mwenyezi Mungu hupendelea wepesi, wala hapendelei uzito; na huwakalifisha watu kwa wanayo yaweza.

 

 103. Mwenyezi Mungu  hakukupeni ruhusa kuharimisha kitu alicho kuhalalishieni,  na kwa hivyo mkenda mkawapasua ngamia masikio yao,   na mkajizuia kuwatumia mkawaita "Bahira" mkawawacha kwa kuwekea nadhiri, na mkawaita "Saiba"; na mkaharimisha kula kondoo dume, na mkawatoa kuwa tunza kwa masanamu; na hata kondoo akizaa dume na jike mkamwita "Wasila", na mkakataa kumchinja dume lake. Wala Mwenyezi Mungu hakukufanyieni sharia ya kukuharimishieni msimtumie ngamia dume baada wakisha zalikana kutokana naye matumbo kumi, naye mkamwita "Hami"! Mwenyezi Mungu hakukutungieni sharia yoyote ya namna hiyo. Lakini walio kufuru wanazua uwongo na wanamsingizia Mwenyezi Mungu. Na wengi wao hawatumii akili.
Wakati wa Jahiliya, kabla ya Uislamu, Waarabu wakijiharimshia wenyewe asiyo yaharimisha Mwenyezi Mungu. Katika hizo ni kuwa:-
1. Ngamia akizaa mara tano na mtoto wa mwisho akawa dume, basi wakimpasua sikio lake na wakaharimisha kumpanda, na akawa haijuzu kumfukuza kwenye kunywa maji au kula machunga. Na wakimwita: "Bahira", yaani aliyepasuliwa sikio.
2. Ilikuwa mtu husema:  Nikirejea safarini, au nikipona maradhi yangu, basi ngamia wangu ni "Saiba",  yaani aliye achwa, na anakuwa kama "Bahira".
3. Na walikuwa kondoo akizaa jike humfanya huyo mtoto ni wao, na akizaa dume humfanya ni wa miungu yao; na akizaa dume na jike basi hawamtoi mhanga huyo dume tena kwa miungu yao, na humwita huyo kondoo jike: "Wa'sila", yaani amemuwasilia nduguye dume.
4. Na pia walikuwa akitokana na fahali mizao kumi basi husema mgongo wake umehamika,yaani umehifadhika, na wakamwita "Hami". Huwa basi hapandwi, wala hatwikiwi mizigo.

 

 104. Na hawa makafiri wakiambiwa: Njooni kwenye yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu katika Qur'ani, na aliyo yaeleza Mtume, ili mpate kuongoka kwa kuyafuata, wao husema: Yanatutosha tuliyo wakuta nayo baba zetu. Yawafalia hawa kusema hayo? Ijapo kuwa hao baba zao ni kama nyama hoa, hawajui lolote la haki, wala hawaijui njia ya kuendea yaliyo sahihi.

 

 105. Enyi mlio amini! Fanyeni pupa ya kwendea kwenye matengenezo ya nafsi zenu kwa kumt'ii Mwenyezi Mungu. Upotovu wa mwengineo hautakudhuruni ikiwa nyinyi mmo kwenye uwongofu na mnalingania Haki. Na nyote nyinyi marejeo yenu ni Mwenyezi Mungu peke yake Siku ya Kiyama. Hapo atakupeni khabari ya vitendo vyenu, na kila mmoja wenu atamlipa kwa aliyo yatanguliza, na wala hapana hata mmoja atae shikwa kwa dhambi za mwenginewe.

 

 106. Enyi mlio amini! Mmoja wenu anapoona alama za kukaribia mauti na akataka kuusia lolote basi kushuhudia wasia huo iwe: kushuhudia  watu  wawili  waadilifu  katika  jamaa zenu,  au watu wawili wengineo ikiwa mmo safarini na ishara za mauti zikatokea. Wazuieni wawili hao baada ya Sala wanapo kusanyika watu, na waape kwa jina la Mwenyezi Mungu wakisema: Hatubadilishi kwa kiapo chake kwa chochote, hata ikiwa ni kutufaa sisi au yeyote katika jamaa zetu. Wala hatutaficha ushahidi alio tuamrisha Mwenyezi Mungu kuutimiza baraabara. Kwani tukificha ushahidi au tukasema lisio la kweli, tutakuwa miongoni mwa wenye kudhulumu na kustahiki adhabu ya Mwenyezi Mungu.

 

 107. Na ikionekana kuwa mashahidi wawili hao wamesema uwongo katika ushahidi wao, au wameficha kitu, basi walio na haki zaidi kushika mahala pao ni wawili wengine walio karibu zaidi kukhusika na warithi wa maiti. Hao washike pahala pao baada ya Sala, wadhihirishe uwongo wa walio tangulia, na waape kwa Mwenyezi Mungu kuwa wale mashahidi wa mwanzo walisema uwongo, na: Yamini yetu inafaa zaidi kuliko yamini ya wale, na wala hatuitupi haki katika yamini zetu, wala hatuwatuhumu mashahidi wale kwa uzushi. Kwani tukifanya hivyo tutakuwa katika walio dhulumu, wenye kustahiki adhabu ya mwenye kumdhulumu mwenginewe.

 

 108. Hukumu hii ndiyo njia ya karibu mno ya kuwezesha mashahidi watoe ushahidi ulio sawa kwa kuhifadhi kiapo chao kwa Mwenyezi Mungu, au kwa kuogopa kufedheheka kwa kudhihiri uwongo wao, pindi ikiwa warithi watakula yamini kupinga kiapo chao. Nanyi mumuangalie sana Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu na amana zenu, na zit'iini hukumu zake, na muwe radhi nazo. Kwani katika hayo ndiyo yanapatikana maslaha yenu. Na msikhalifu hukumu za Mwenyezi Mungu, msije kutoka kwenye ut'iifu wake,  kwani Yeye hamnafiishi kwa uwongzi wake mwenye kutoka katika ut'iifu wake.

 

 109. Nanyi ikumbukeni Siku ya Kiyama pale Mwenyezi Mungu atapo wakusanya mbele yake Mitume wote akawauliza:  Hao kaumu zenu niliyo kutumeni kwao wamekujibuni nini?  Waliamini au walikanya? Na hao kaumu wakati huo watakuwa wamehudhuria ili hoja iwe juu yao kwa ushahidi wa Mitume wao wakisema:  Hakika sisi hatujui yaliyo tokea baada yetu kwa hao ulio tupeleka kwao. Ni Wewe peke yako ndiye unaye jua hayo, kwa kuwa Wewe ndiye uliye kusanya ujuzi wa vilivyo fichikana kama unavyo jua viliyo dhaahiri.

 

 110. Na wakati huo, Mwenyezi Mungu atamwambia Isa mwana wa Maryamu miongoni mwa Mitume:  Kumbuka neema niliyo kuneemesha wewe na mama yako katika dunia, nilipo kutia nguvu kwa Wahyi,(Ufunuo), na nikakutamkisha nawe ni mtoto mchanga ili kumuondolea tuhuma aliyo tuhumiwa mama yako, kama nilivyo kutamkisha nawe ni mtu mzima kwa ufunuo niliyo kufunulia; na nilipo kuneemesha kwa kukufunza kuandika, na nikakuwezesha kusema na kutenda yaliyo sawa, na nikakufunza Kitabu cha Musa na Injili niliyo kuteremshia wewe, na nikakuwezesha kutenda miujiza asiyo weza mtu mwingine kuitenda, ulipo tengeneza ndege kwa udongo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, ukapuliza akawa ndege aliye hai kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, si kwa uweza wako, na ukamponesha mtoto kipofu, na ukamponesha mkoma kwa idhini na uweza wa Mwenyezi Mungu, na yakawa kwa kupitia mikononi mwako makadara ya kufufuka maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na kudra yake, na pale nilipo wazuia Mayahudi wasikuuwe na kukusalibu nilipo waletea miujiza wapate kuamini, nao baadhi yao walikanya na wakadai kuwa hiyo miujiza si lolote ila ni dhaahiri uchawi tu. (Katika Injili ya Luka inasemwa "Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu." Luka 22.43. Na katika Injili ya Yohana 5.30 Yesu anakiri: "Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe.")

 

 111. Ewe Mtume! Watajie umma wako yaliyo tokea tulipo watia hima kikundi cha alio wataka Isa wamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake Isa, na wakamuitikia wakawa ndio Wanafunzi wake makhsusi, na wakasema: Tumeamini. Na shuhudia ewe Mola wetu Mlezi, kuwa sisi tumesafi niya zetu, na tunafuata amri zako, yaani Waislamu.

 

 112. Ewe Nabii! Taja pia yaliyo tokea pale wafuasi wa Isa wenye ikhlasi walipo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Hivyo Mola wako Mlezi atakuitikia ukimtaka akuteremshie chakula kutoka mbinguni? Isa akawaambia kuwajibu: Kama nyinyi ni kweli mnamuamini Mwenyezi Mungu, basi mkhofuni Yeye, na fuateni amri zake na makatazo yake. Wala msitafute hoja ila nilizo kuleteeni.

 

 113. Wakasema: Hakika sisi tunataka kula katika chakula hicho, ili nyoyo zetu zitue kwa kudra ya Mwenyezi Mungu tunayo iamini, na tujue kwa kuona kwa macho ya kuwa hakika ni kweli hayo unayo twambia yanatoka kwake Subhanahu, Aliye takasika, na tupate kutoa ushahidi kwa muujiza huu kwa hao ambao hawakuuona.

 

 114. Isa akawaitikia, na akasema: Ewe Mola wetu Mlezi, uliye miliki mambo yetu yote! Tuteremshie chakula kutoka mbinguni, kiwe ni siku-kuu kwetu kitapo teremka kwa walio amini miongoni mwetu, kwa walio tangulia na walio taakhari, na kiwe ni muujiza wa kutilia nguvu wito wako, na uturuzuku riziki njema, na Wewe ndiye Mbora wa kuruzuku.

 

 115. Mwenyezi Mungu akamwambia: Mimi nitakuteremshieni chakula kutoka mbinguni. Lakini mtu yeyote atakaye pinga neema hii baada ya kuteremka, basi Mimi nitampa adabu ambayo sijapata kumpa mtu yeyote. Kwani huyo atakuwa anakanya baada ya kwisha shuhudia dalili ya Imani aliyo itaka mwenyewe.

 

 116. Ewe Nabii! Taja yatakayo tokea Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu atapo mwambia Isa bin Maryamu kauli ya kutangaza haki: Ati wewe ndiye uliye waambia: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu, na muache kumuabudu Mwenyezi Mungu wa pekee? Isa atasema: Mimi ninakutakasa mtakaso wa ukamilifu ya kuwa Wewe huna mshirika. Wala hainifalii mimi nitake jambo ambalo sina haki nalo hata chembe.  Lau  kuwa  nimesema  hayo,  basi  Wewe  ungeli jua. Kwani Wewe unayajua yaliyo fichikana ndani ya nafsi yangu, licha yanayo dhihiri kwa kuyasema. Wala mimi siyajui unayo nificha. Hakika Wewe ndiye Mwenye ujuzi ulio enea kila kilicho fichikana na kilicho ghibu. (Wakristo wote wanamuabudu Yesu, na Wakatoliki wanamwomba Maryamu pia, na wanamwita: "Mama wa Mungu")

 

 117. Mimi sikuwaambia ila uliyo niamrisha niwafikishie. Nimewaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake. Kwani Yeye ndiye Mwenye kumiliki mambo yangu na yenu. Na mimi nilikuwa naijua hali yao nilipo kuwa nao. Na ulipo malizika muda uliyo nikadiria nikae nao ulikuwa Wewe peke yako ndiye unaye wajua. Na Wewe ni Mwenye kujua kila kitu.

 

 118. Ukiwaadhibu kwa waliyo yatenda basi hao ni waja wako, unawafanya upendavyo. Na ukiwasamehe, basi hakika Wewe peke yako ndiye Mtenda nguvu usiye shindwa, Mwenye hikima yenye kufikilia kila linalo toka kwako.

 

 119. Mwenyezi Mungu atasema:  Hii ndiyo siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Watapata mabustani yanayo pitiwa na mito chini ya miti yake. Na humo watakaa, wala hawatatoka milele, wakistarehe humo kwa radhi ya Mwenyezi Mungu anavyo waridhia wao, na wao watavyo kuwa radhi kwa malipo alio walipa. Na Neema hiyo ndio kufuzu kukubwa.

 

 120. Ufalme wa mbinguni na katika ardhi na vyote viliomo humo ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye peke yake ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa, na Yeye tu ndiye Mwenye uweza ulio timia kutekeleza kila alitakalo.