1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni
kutokana na nafsi moja, na kutokana na nafsi hiyo akamuumba mkewe, na kutokana
na hao wawili, wakaenea wanaume na wanawake wengi. Basi nyote mnatokana na nafsi
moja. Mcheni Mwenyezi Mungu mnaye mtaka msaada kwa kila mnacho kihitajia, na kwa
jina lake ndio mnaombana nyinyi kwa nyinyi katika mambo yenu. Pia
tahadharini na kuacha kuwasaidia jamaa zenu, wa karibu na wa mbali. Kwani
Mwenyezi Mungu daima anakuangalieni. Hapana chochote katika mambo yenu kinacho
fichikana kwake. Na Yeye ndiye Mwenye kukulipeni.
2. Na wapeni mayatima mali yao wanayo stahiki, na
yalindeni mali yao vizuri, wala msiwape kilio duni mkawanyima kizuri. Wala
msichukue mali yao mkaongezea kwenye mali yenu. Hakika kitendo hicho ni dhambi
kubwa.
3. Ilivyo kuwa mnakhofu kuwadhulumu mayatima kwa kuwa
hiyo ni dhambi kubwa, basi kadhaalika khofuni machungu ya wake zenu kwa kuacha
kuwafanyia uadilifu baina yao, na kuzidisha juu ya wane. Basi mnaweza kuoa
wawili, au watatu, au wane, ikiwa mna imani kuwa mtaweza kufanya uadilifu.
Mkiogopa kuwa hamtaweza kufanya uadilifu basi oeni mmoja tu, au jitoshelezeni na
wajakazi walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hayo ni afadhali kuliko kwenda
kuingia katika dhulma na ujeuri (1). Na ni afadhali msije mkawa na watoto wengi
bila ya kiasi hata mshindwe kuwatazama.(Wafasiri wengi wamependelea kufasiri
"Alla Tau'luu" kuwa "Kutofanya jeuri au dhulma." Lakini hii AL MUNTAKHAB
imekhiari tafsiri hii ya "msikithirishe wana", ambayo ndiyo aliyo ifuata Imam
Shaafii r.a., naye alitanguliwa na Maimamu wanazuoni wa Kiislamu, Zayd bin Aslam
r.a.na Jabir bin Zayd r.a. kama alivyo simulia Daar Qut'ni, na imetajwa katika
Tafsir ya Qurt'uby juzuu ya 5 sahifa 22.)
(1) Sharia ya Kiislamu si peke
yake inayo ruhusu kuoa wake wengi, miongoni mwa sharia za dini za mbinguni.
Sharia ya Taurati inamruhusu mwanamume kuoa idadi ya wanawake atakao. Na imetaja
kuwa Manabii walikuwa wakioa wake kwa makumi na makumi. Na Taurati ni katika
Agano la Kale la Biblia ambalo linafuatwa pia na Wakristo katika mambo ambayo
hayakukatazwa katika Injili au Barua za Mitume. Na hakika iliopo ni kuwa hapana
popote katika Agano Jipya panapo pinga sharia hiyo ya kuruhusu kuoa wake zaidi
ya mmoja.
Kanisa katika Karne za Kati liliruhusu
hayo, na wafalme wa Ulaya wa Kikristo walio kuwa na wake wengi ni
maarufu katika taarikh (historia).
Khitilafu iliyopo ni kuwa Uislamu
ndiyo dini ya kwanza kuweka idadi maalumu, isipindukiwe. Imeweka kiwango kwa
mambo matatu.
* (Kwanza) wasipindukie hao wake kuliko wane.
* (Pili) asidhulumike mmoja katika hao wake,
* (Tatu) awe mtu
anaweza kuwakimu hao wake.
Shuruti mbili za mwisho zimelazimu kila
ndoa, ijapokuwa ni ya kwanza. Wanazuoni wa
Kiislamu wa sharia na wanga khitalifiana wanakubaliana pamoja kuwa mume
ambaye anajua kuwa hawezi kuwafanyia uadilifu wakeze ni haramu kwake kidini
kuongeza wake. Ila uharamu huu ni wa kidini, watawala na mahakimu hawawezi
kumuingilia. Kwani uadilifu ni jambo la nafsi yake mtu, na dhamiri yake, na
uwezo wa kutazama ni jambo la mnasaba halifungamani na mizani mojapo. Ni yeye
mwenyewe atakaye pata adhabu Siku ya Kiyama akikhalifu amri hiyo. Dhulma au
kutokuweza kukimu kunategemea hali ya siku zijazo, na mikataba haifungamani na
mambo ambayo huenda yakawa au yasiwe, bali ni juu ya yaliyoko, na ilivyo kuwa
dhaalimu huenda akawa muadilifu, na asiye weza sasa hueza akaweza baadae, kwani
mali huja na kuondoka, juu ya hivyo Uislamu unasema mwanamume akimdhulumu mkewe
au akashindwa kumkimu, basi mwanamke anaweza kutaka kufarikishwa na mume
huyo, lakini hazuiliki na kuandikiana mkataba akifanya hayo kwa radhi yake na
khiari yake.
Na Uislamu kwa kufungua mlango wa kuoa wake zaidi ya
mmoja lakini kwa mikazo kama hivyo ilivyo elezwa imekuwa umepiga vita magonjwa
ya kijamii:
* Kwanza - Huenda ikawa idadi ya wanaume wanao faa kuoa
ikawa chini kuliko wanawake wanao faa kuoelewa. Khasa huwa hayo baada ya vita.
Imeonakana katika baadhi ya nchi za Ulaya imewahi kufika idadi ya wanawake
kuwazidi wanaume baada ya vita kwa mara saba! Kwa hivyo ni hishima ya mwanamke
katika hali kama hizo kuwa mke-mwenza kuliko kuwa akibahashika kama malaya, bila
ya mume.
* Pili - Huenda kutokea baina ya mwanamume na mwanamke hali
inayo walazimisha ama waingiane kiharamu au waoane kisharia. Ni maslaha
kwa umma yawe hayo kwa mujibu wa sharia. Na ni bora kwa mwanamke kuwa mke
kuliko kuwa hawara wa mwanamume huyu baada ya huyu. Ikiwa hii ni sura mbaya ya
kuoa wake wengi, basi juu ya hivyo ni afadhali kuliko kuwa na mke mmoja.
Kwani kuoa wake zaidi ya mmoja kama itavyo kuwa vibaya kunakinga shari kubwa
zaidi kwa umma, nayo ni umalaya na maovu yanayo pandana nayo.
* Tatu
- Mwanamke hakubali kuolewa na mume mwenye mke ila ikiwa ni kwa dharura iliyo
kweli. Ikiwa mke wa kwanza atapata madhara kwa uke-wenza, basi huyu mwenzie
atapata madhara makubwa zaidi kwa kuharimishwa mume kabisa, kwa kuwa ama ufe uke
wake au apotee kwa wanaume majiani. Madhara makubwa hukingwa kwa madhara yaliyo
akali.
* Nne - Imeonakana kuwa vijana wengi hawapendi kuoa, hata
inakisiwa kuwa vijana wanao oa kwa kulinganisha na wafaao kuoa hawazidi kuliko
60%. Na haya yanazidi kila mwaka. Kupinga khatari hii hapana ila kuruhusu kuoa
wake wengi.
* Tano - Huenda mke akapata maradhi ambayo hayamruhusu
kulala na mumewe, au huenda akawa tasa. Ni maslaha ya umma na maslaha ya binafsi
kuoa mke mwengine. (Wakati huo huo ikawa kumpa talaka huyo mke ni madhara
makubwa zaidi kwa mke na ukatili kwa mume kufanya.)
Kwa sababu kama
hizi na nyenginezo Uislamu umeufungua mlango kwa shida na dhiki, na haukuufunga
kabisa. Hivi sasa tunamwona Askofu Mkuu katika Uingereza anaona kuwa dawa ya
pekee ya kuondoa uharibifu ulio uingilia ukoo wa Kiingereza ni kufungua mlango
wa kuoa wake zaidi ya mmoja. Hakika Uislamu ni Sharia ya Mwenyezi Mungu ambaye
anajua kila kitu. Kwani Yeye ndiye Mjuzi Mwenye hikima. (Haya tukijua kuwa dini
ya Kikristo haikatazi kuoa wake wengi. Ni sharia zilizo tungwa na makanisa ya
Kizungu tu kwa kufuata mila zao ndizo zinazo lazimisha kuoa mke mmoja. Basi hiyo
ni mila ya Wazungu, wala si sharia ya dini yoyote duniani. Bali Uislamu ndiyo
Dini pekee katika dini zote iliyo wekea kiwango, na kudhibiti idadi ya wanawake
kuoa, kwa maslaha ya Umma.)
4. Wapeni wanawake mahari yao kuwa ni kipawa, tunza iliyo
safi. Na nyinyi hamna haki yoyote katika hayo mahari. Ikiwa hao wanawake kwa
radhi ya nafsi zao wenyewe wakakubali kusamehe sehemu yoyote ya mahari mliyo
kwisha ahadiana, basi hapo mnayo ruhusa kuchukua na mkatumia kwa kheri na
salama.
5.Wala msiwape wasio na akili ya kutosha kuendesha mambo
yao mali yao, nayo ni mali yenu vile vile. Kwani mali ya yatima na ya mchache wa
akili yamekulazimuni myatazame yasiharibike. Mwenyezi Mungu ameyajaalia mali
hayo ya kukimu maisha. Wapeni kutokana na pato lake sehemu kama
wanavyo hitajia kwa kula, na wavisheni na muwatendee vyema, na mseme nao maneno
ya kuwaridhisha sio ya kuwaudhi au kuwadhili.
6. Na kabla ya hao mayatima kufika umri wa kubaalighi
wajaribuni, mpate kujua akili zao na hali zao na maarifa yao katika kuendesha
mambo. Hata wakifika wakati wa kusilihi kuoa na mkauona uwekevu wao, na
matayarisho kuchukua jukumu, basi hapo wapeni mali yao wenyewe. Wala nyinyi
msiyale mali yao kwa fujo, mkifanya haraka mpatilize kabla hawajabaalighi wakawa
watu wazima ikabidi haki yao kurudi. Na akiwa katika mawasii anajitosha kwa
utajiri, basi ajizuie asichukue chochote kuwa ni ujira kutazama mali ya
mayatima. Na akiwa fakiri muhitaji basi ajitosheleze kuchukua ujira wa uangalizi
kwa kadri ya ada ilivyo. Na mnapo wakabidhi mayatima mali yao wekeni mashahidi
wa kushuhudia. Na mjue kuwa Mwenyezi Mungu daima yupo nyuma yenu, na Yeye ndiye
Mhasibu, na Yeye ndiye Muangalizi. Na Yeye anatosha kuwa Mhasibu na Muangalizi.
7. Wanaume wanalo fungu lao katika mali waliyo yaacha
kurithiwa wazazi wawili na jamaa walio karibia. Na wanawake, aidha, wana
fungu lao, bila ya kunyimwa au kupunjwa. Na mafungu hayo yamethibiti, na
yamefaridhiwa, na yamekadiriwa, yakiwa mali yenyewe kidogo au mengi.
8. Na pindi ikiwa wamehudhuria wakati ule wa kugawanya
urithi baadhi ya jamaa ambao hawarithi, na ni mayatima na masikini, basi
wakirimuni kwa kuwapa chochote katika huo urithi ili kuzipoza nafsi zao, na
kuondoa uhasidi katika nyoyo zao. Na ni vizuri pia katika kuwapa kuleta maneno
laini na udhuru mwema.
9. Watu watahadhari na kuwadhulumu mayatima, na
wawaogopee watoto wao wanyonge wasije na wao wakadhulumiwa kwa watendavyo wazee
kwa mayatima wa watu wengine. Na wamwogope Mwenyezi Mungu katika kuwatendea
mayatima. Na waseme maneno yaliyo kaa sawa yanayo fuata haki, wala wasimdhulumu
yeyote.
10. Hakika wanao wadhulumu mayatima kwa kuchukua mali
yao bila ya haki, hakika wanakula yatakayo wapelekea Motoni. Na Mwenyezi Mungu
atawaadhibu Siku ya Kiyama kwa moto mkali wenye kutia machungu.(Je, huwaje basi
adhabu ya mwenye kudhulumu mali ya Mwenyezi Mungu? Wakfu za misikiti, madrasa
n.k.? Na huwaje mwenye kuuwa ili apate kudhulumu mali ya mayatima wa hao alio
wauwa?)
11. Mwenyezi Mungu anakuamrisheni katika mambo ya
kuwarithisha watoto wenu na wazazi wenu, pindi mtakapo kufa, kwa njia
inayo leta uadilifu na maslaha. Nayo ni kuwa sehemu ya mwanamume ni sawa
na sehemu ya wanawake wawili, ikiwa watoto wanao rithi ni wanaume na wanawake.
Ikiwa watoto wote ni wanawake watupu, na idadi yao imezidi wawili, basi sehemu
yao ni thuluthi mbili za tirka, yaani mali yaliyo achwa na maiti. Inafahamika
katika madhumuni ya Aya kuwa fungu la binti wawili ni kama fungu la walio zidi
hapo. Na akiwa mtu amemuacha binti mmoja tu, basi fungu lake ni nusu ya alicho
kiacha. Na akiwa mtu amemuacha baba na mama, basi kila mmojapo kati ya hao
atapata sudusi, yaani sehemu moja katika sita, ikiwa huyo maiti alikuwa na mtoto
mmoja - mwanamume au mwanamke - pamoja na hao wazazi wake. Akiwa hana mtoto na
wakamrithi wazazi wake tu, basi mama sehemu yake ni thuluthi, na kilicho baki ni
cha baba. Na ikiwa huyo maiti alikuwa na ndugu, basi mama yake atapata sudusi na
kilicho baki ni cha baba, na wale ndugu hawapati chochote. Mafungu hayo hupewa
wanao stahiki baada ya kwisha lipwa deni lilio kuwa juu ya maiti, na kutimiza
yale aliyo yausia katika mipaka aliyo ruhusu Mwenyezi Mungu. Hii ni hukumu ya
Mwenyezi Mungu. Na huu ndio uadilifu na ndio hikima. Na nyinyi hamjui ni nani
kwenu mwenye manufaa zaidi kwenu, baina ya wazazi na wana. Na kheri khasa ni
aliyo yaamrisha Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ndiye Mwenye kuyajua maslaha yenu, na
ndiye Mwenye hikima katika yale aliyo kulazimisheni.
12. Fungu la mume ni nusu ya alicho acha mke ikiwa huyo
mke hakuacha mtoto kutokana na mume huyo au mwenginewe. Akiwa huyo mke ana
mtoto, basi mumewe atapata robo baada ya kutolewa wasia aliye uusia huyo
mwanamke au kulipwa deni lake. Na fungu la mke au wake ni robo ya alicho acha
mume ikiwa hakuacha mtoto kwa wake hao au wenginewe. Akiwa anaye mwana kutokana
na hao au wake wenginewe basi mke huyu au wake hawa watapata thumni ya tirka
baada ya wasia alio usia au deni. Na mwana wa mwana, yaani mjukuu, ni kama mwana
katika haya yaliyo tangulia. Na akiwa maiti ni mwanamume au mwanamke, naye hana
mwana wala mzazi, na kamwacha ndugu mume kwa mama, au ndugu wawili wa kike kwa
mama, basi kila mmoja wao atapata sudusi, yaani sehemu moja katika sita. Na
wakiwa wengi kuliko hivyo watashirikiana katika thuluthi, watagawana sawa sawa
wanaume na wanawake kwa mujibu wa ushirika, baada ya kulipa madeni yaliyo kuwa
juu yake, na kutimiza wasia ambao haudhuru urithi, nao ni wasia usio pindukia
thuluthi iliyo baki baada ya kulipa madeni. Basi, enyi Waumini! Jilazimisheni
kufuata aliyo kuusieni Mwenyezi Mungu; kwani Yeye hakika ni Mwenye kujua vyema
nani miongoni mwenu anaye dhulumu na nani anaye fanya uadilifu, Yeye ni Mpole
hafanyi haraka kutoa adhabu.
13. Hizo ni hukumu zilizo tajwa kueleza khabari ya
mirathi na mengine yaliyo tangulia ni Sharia za Mwenyezi Mungu aliye zipanga kwa
ajili ya waja wake wazijue wala wasizikiuke. Na Mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na
Mtume wake katika alivyo hukumu Yeye malipwa yake yatakuwa ni Pepo ipitayo mito
kati yake, na atakaa humo daima dawamu. Na huko ndiko kushinda kukubwa.
Mpango wa mirathi uliyo bainishwa na Qur'ani Tukufu ni mpango wa uadilifu
na haki kuliko kanuni zote za mirathi nyenginezo duniani. Na haya wameyakiri
wataalamu wa sharia wote wa Ulaya. Na huu ni mmoja katika ushahidi wa kuwa
Qur'ani inatokana na Mwenyezi Mungu, kwani haya au yaliyo karibia haya hayakuwa
yakijuulikana kwa Waajemi wala kwa Warumi wala katika sharia zozote za kabla ya
Uislamu. Na sharia hii ya Kiislamu imefuata mipango hii ya uadilifu:
* Kwanza - Umefanywa urithi kwa mujibu apendavyo Mwenyezi Mungu, sivyo
apendavyo mwenye mali, bila ya kupuuza kabisa mapenzi yake huyo. Amepewa huyo
ruhusa ya kufanya wasia kwa thuluthi ya mali kwa ajili ya mambo mema, kama
kutimiza kasoro katika waajibu wake wa dini, kama Zaka ambazo alikuwa hakuzitoa,
au kuwajaalia kitu wahitaji alio khusiana nao kwa ujamaa au mapenzi nao
hawastahiki urithi. Na amezuiliwa kufanya wasia ikiwa hayo yatapelekea maasi au
yatachochea kuendelea maasia. Na thuluthi mbili zilizo baki baada ya wasia, au
mali yote ikiwa hapana wasia, Mwenyezi Mungu Mtunga sharia, amejipa Yeye
kuzigawa kwa haki.
* Pili - Katika kuchukua madaraka ya ugawaji
tirka, Mwenyezi Mungu Aliye takasika, amempa aliye karibu zaidi kuliko
mwenginewe, bila ya kuzingatia ukubwa au udogo. Kwa hivyo ndio ikawa watoto wana
sehemu kubwa zaidi katika mirathi, kwani wao ndio kiendelezo cha yule maiti, na
pia kuwa wao aghlabu ni wanyonge. Juu ya hivyo hawakukoseshwa, bali
wameshirikiana nao, mama na bibi, baba na babu, ijapokuwa wanachukua akalli
kuliko watoto.
* Tatu - Yaonekana kuwa mirathi ni kwa kadri ya haja.
Kwa hivyo sehemu ya watoto ni kubwa kwa sababu haja yao ni kubwa zaidi, na wao
ndio wanayakabili maisha, na kina baba na mama wanayapa mgongo maisha. Ama
zingatio la haja ndilo lililo pelekea kuwa fungu la mwanamke liwe nusu ya fungu
la mwanamume katika aghlabu ya hali za mirathi. Haya ni kwa kuwa mwanamume
inambdi zaidi kukabili matumizi, kwa kuwa yeye anatakikana awalishe watoto na
awatazame, amtumilie mwanamke. Maumbile ya kibinaadamu yamemfanya mwanamke ndiye
asimamie kazi za nyumbani na kulea watoto, kuangalia raha zao, na mwanmume awe
ni wa kuhangaika nje kiuchumi alete fedha za kutumia nyumba nzima. Kumpa kila
mmoja kwa kadri ya haja ndio uadilifu. Kuweka sawa kwa wenye haja mbali mbali ni
udhalimu.
* Nne - Sharia ya Kiislamu katika kugawa kwake tirka ya
maiti inakusudia kugawa sio kurundika. Kwa hivyo haikufanya
urithi wende kwa mtoto mkubwa peke yake, wala haikuwapa wanaume tu na
kuwachilia mbali wanawake, wala watoto wakaachwa wazazi. Wala hawakukoseshwa
wasio kuwa katika uti wa nasaba, kama ndugu, na maami, na banu-ami n.k. Urithi
unaendelea mpaka kwa wanao karibia ukoo, lakini aliye karibu hufadhilika zaidi.
Na shida kutokea kuwa mrithi ni mmoja tu.
* Tano - Mwanamke
hakoseshwi kurithi, kama ilivyo kuwa ada ya Waarabu. Hivi ni kumhishimu mwanamke
na kumpa haki yake. Na juu ya haya Uislamu hauzuii kurithi ujamaa wa mwanamke,
bali hurithi jamaa walio kuwa upande wake, kama wanavyo rithi jamaa upande wa
baba. Makaka na madada kwa upande wa mama wanachukua pale wanapo chukua ndugu wa
baba na mama, bali katika hali nyengine wanachukua watoto wa kwa mama na
kuchukua ndugu wanaume na wanawake. Na haya bila ya shaka ni kuutukuza umama, na
kuutambua ukaribu wake. Haya hayakuwa yakijuulikana kabla yake, walakini hii ni
Sharia ya Mwenyezi Mungu aliye Mjuzi na Mwenye hikima.
14. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na
Mtume wake na akaikiuka mipaka aliyo iweka Mwenyezi Mungu, na huku
akihalalisha kukiuka huko basi mtu huyo atalipwa Moto, na humo atakaa milele,
akiadhibiwa mwili wake juu ya kuadhibiwa roho yake.
15. Na wale wanawake wanao zini wakishuhudiwa na
mashahidi wanaume wane walio waadilifu, basi wazuieni wasitoke nyumbani kwa
ajili ya kuwalinda na kuzuia usiendelee ufisadi na shari mpaka wafe, au Mwenyezi
Mungu awafungulie njia ya maisha yaliyo sawa kwa kuolewa na kutubu. (Wafasiri
wengine wanasema hukumu hii ni kwa wanawake wanao fanya mambo machafu wenyewe
kwa wenyewe, sio ya zina baina ya mwanamke na mwanamume. Kwa kuhifadhi heshima
ya wanawake inalazimu wapatikane mashahidi wane, badala ya wawili, walio ona
kitendo khasa, sio kuwatuhumu watu kwa jambo ovu kama hilo bila ya mashahidi
wane walio shuhudia kwa macho yao.)
16. Mwanamume na mwanamke walio zini, nao hawajaoa (au
kuolewa), wapewe adhabu maalumu, pindi ikithibiti hiyo zina kwa mashahidi wane
waadilifu. Wakitubu baada ya kupewa adhabu, basi msiwatajie hayo maasi waliyo
yatenda, wala msiwaaziri. Hakika Mwenyezi Mungu kwa rehema yake anakubali toba
ya wenye kutubu.
17. Hakika toba imedhaminiwa na Mwenyezi Mungu kwa
watendao maovu katika hali ya ujinga, na kupitikiwa na kutoangalia vyema, kisha
wakafanya haraka ya kutubu kabla ya kufikiwa na mauti. Hawa basi
MwenyeziMungu anaikubali toba yao, naye ni Mjuzi, haumfichikii ukweli wa toba,
ni Mwenye hikima, hakosei katika kupima.
18. Toba isiyo kubaliwa ni ya wanao fanya maasi kisha
hawafanyi haraka kuyajutia mpaka mmoja afikwapo na mauti. Tena hapo husema: Sasa
mimi natangaza majuto na toba. Kadhaalika toba haikubaliwi kutokana na wanao
kufa katika ukafiri. Mwenyezi Mungu ameyaandalia makundi mawili hayo adhabu ya
kutia uchungu huko kwenye nyumba ya malipo, Akhera.
19. Enyi mlio amini! Haikujuziini kuwafanya wanawake
kama bidhaa, mkiwarithi wake zenu bila ya mahari na bila ya ridhaa yao. Wala
msiwadhulumu kwa kuwadhikisha ili wapate kusamehe baadhi ya mahari mlio wapa.
Wala msiwadhiki ili wapate kukurejesheeni mali mlio wapa, ila ikiwa wakifanya
kosa wazi la kuwacha ut'iifu, au la tabia mbovu, au la ukahaba. Hapo mnaweza
kuwadhikisha au kuchukua baadhi ya mlicho wapa wakati wa kufarikiana nao. Na ni
waajibu wenu, enyi Waumini, kukaa na wake zenu kwa vizuri, kwa maneno mema na
vitendo vyema. Ikiwa mtawachukia kwa aibu fulani katika tabia au katika umbo au
mengineyo, basi juu ya hivyo subirini. Msifanye haraka kuwaacha, kwani asaa
Mwenyezi Mungu akajaalia kheri nyingi katika hicho hicho mkichukiacho. Na ujuzi
wa mambo yote uko kwa Mwenyezi Mungu tu.
20. Na pindi ikiwa mnataka kubadili mke pahala pa mke
mwengine, na ikawa mmempa mmoja wao mali mengi basi si halali kwenu kuchukua
chochote katika hayo. Jee mtachukua hayo kwa njia ya upotovu na kwa dhambi iliyo
wazi?
21. Na vipi ikufalieni nyinyi kutaka kurudishiwa mahari
mliyo kwisha yatoa, na hali mlikwisha changanyika nyinyi kwa nyinyi, na wao
wanawake wakafungamana nanyi kwa agano lenye nguvu ambalo kwalo Mwenyezi Mungu
amewajibisha muingiane nao kwa ndoa.
22. Wala nyinyi, watoto,
msiwaoe wanawake walio wahi kuolewa na baba zenu. Jambo hilo ni uchafu na
linachusha, na linakirihiwa na Mwenyezi Mungu na watu. Na hiyo ni njia ovu
kabisa. Lakini Mwenyezi Mungu anasamehe yaliyo kwisha tendeka katika zama za
ujahili.
Waarabu katika zama za
ujahili walikuwa na ada zisio mpa heshima mwanamke, bali zikimdhulumu sana, na
zikikata makhusiano mema katika ukoo. Ilikuwa mtu akifa baba yake na akawa na
wake wasio kuwa mama yake mzazi, akilazimishwa kuwaoa, au akiwarithi wake za
baba yake bila ya ndoa mpya. Na ilikuwa mtu akimwacha mke basi humpokonya kwa
dhulma na uadui mahari yote aliyo mpa. Na walikuwapo walio kuwa wakimzuia huyo
mt'laka asiolewe na mtu mwengine, kwa jeuri na inda. Ukaja Uislamu, ukamlinda
mwanamke na dhulma hii iliyo wazi, ukakataza kurithiwa mke, na kumpokonya mahari
yake hata chembe, ijapo kuwa ni mali mengi, na ukakataza kumzuia mt'alaka
asiolewe, au kumkera ili apate kutaka yeye mke t'alaka kwa kutoa mali. Na katika
mtindo wao Waarabu wa jahiliya ilikuwa yafaa mtu kumwoa aliye kuwa mke wa baba
yake na akafarikiana naye kwa t'alaka au mfano wake. Uislamu ukakataza hayo, na
ukauwita mtindo huo ni uchafu, kwa sababu ni jambo baya analo lichukia
Mwenyezi Mungu na kila mwenye akili sawa. Huo ndio uadilifu wa Mwenyezi
Mungu.
23. Mwenyezi
Mungu amekuharimishieni kuwaoa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu (ndugu
wanawake) na shangazi zenu, na khaalati zenu (mama wadogo) na binti wa ndugu, na
binti wa dada, na mama walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama
wakwe. Na walio harimishwa bila ya kunasibiana kwa damu ni: mama wa kunyonyesha,
dada wa kunyonya (1), mama mkwe, binti za wake kwa waume wengine ikiwa hao wake
wameingiliwa, na wake wa watoto mlio wazaa, na kuwaoa pamoja ndugu wawili.
Yaliyo pita katika siku za ujahili yamesamehewa. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe kwa yaliyo pita kabla ya mpango huu, na Mwenye kuwarehemu katika
aliyo kuwekeeni sharia.
(1) Ni
Sharia ya Kiislamu pekee iliyo harimisha kwa sababu ya kunyonyesha. Anaye nyonya
anakula kutokana na mwili wa mnyonyeshaji kama anavyo kula kutokana na mama yake
ndani ya tumbo lake. Wote hao wawili wanakuwa ni sehemu yake huyo mtoto. Hapana
khitilafu baina ya kukua ndani ya chumba na ndani ya tumbo. Na katika
kuharimisha kwa kunyonyesha ni kumtukuza mnyonyeshaji, kwani anakuwa kama mama.
Na haya ni kuzidi kushajiisha kunyonyesha kimaumbile, sio kwa chupa, kwa watoto
wachanga.
24. Haramu kwenu kuoa wake za
watu wote, waungwana na wasio waungwana, ila mateka mlio wateka katika vita
baina yenu na makafiri. Kwani ndoa zao zilizo pita zinafutika kwa kutekwa.
Wanakuwa halali kwenu baada ya kuhakikisha hawana mimba. Basi shikeni aliyo
kuandikieni Mwenyezi Mungu kuhishimu mlicho katazwa. Isipo kuwa hao wanawake
Waumini walio maharimu yenu, mwaweza kutafuta wanawake mkawaoa kwa mali yenu,
bila ya kuzini au kuweka kinyumba. Kila mwanamke mliye starehe naye baada ya
kumwoa mpeni mahari yake kama mlivyo patana. Hapana ubaya kwenu ikiwa
watakuridhieni kupunguza au kuongeza. Mwenyezi Mungu daima anayaangalia mambo ya
waja wake, na ni mwenye kuwapangia hukumu zinazo wasilihi kwa maisha yao.
25. Asiye weza kati yenu
kuwaoa wanawake Waumini wa kiungwana basi na aowe anaye muweza katika wanawake
Waumini walio milikiwa. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema ukweli wa Imani yenu na
ikhlasi yenu. Wala msione uvunjifu kuwaowa hao vijakazi, kwani nyinyi na wao ni
sawa katika Dini. Basi waoweni kwa idhini ya watu wao, na muwape mahari
yao mliyo wakadiria kwa mujibu ya ilivyo zowewa kati yenu kwa ajili ya
kutendeana mema na kutimiza haki. Na chagueni wanawake walio safi, msichague
wazinifu kwa dhaahiri wala mahawara wa kinyumba. Na hao wakija zini baada ya
kuolewa basi adabu yao ni nusu ya muungwana. Na huku kuhalalishiwa kuowa
wajakazi mnapo kuwa hamuwezi kunajuzu kwa anaye ogopa taabu zinazo pelekea zina.
Na mkisubiri kuto owa wajakazi na mkakaa safi ni bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwingi wa maghfira, na Mkubwa wa kurehemu.
26. Mwenyezi Mungu anataka
kukuwekeeni wazi njia yenye maslaha kabisa, na akuongoeni kwenye nyendo njema za
walio kuwa kabla yenu, na akurejesheni kwenye njia ya ut'iifu wake. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuyajua vyema mambo yenu, ni Mwenye kupanga baraabara katika
hukumu zake kwa yanayo silihi mambo yenu.
27. Na Mwenyezi Mungu anataka
mrejee katika ut'iifu wake, na wale wanao fuata ladha zao, na matamanio yao
machafu, miongoni mwa makafiri na waasi, wanataka muwe mbali kabisa na njia ya
haki.
28. Mwenyezi Mungu anataka
kukufanyieni wepesi katika kutunga sharia ambazo ndani yake zina sahala na
takhfifu kwenu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu amemuumba mwanaadamu
kiumbe dhaifu katika kupambana na matamanio na maelekeo ya nafsi. Kwa hivyo
yanayo mlazimu katika sharia yana wepesi na wasaa. Na hayo kwa fadhila yake na
taisiri yake Mwenyezi Mungu ndiyo anayo walazimisha waja wake.
29. Enyi mlio amini!
Msinyang'anyane mali nyinyi kwa nyinyi. Lakini ipo ruhusa kufanya biashara kwa
kuridhiana. Wala msijiteketeze kwa kuacha amri za Mola wenu Mlezi. Wala
mmoja wenu asimtende uwovu mwenziwe, kwani nyote ni nafsi moja. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye rehema daima kwenu.
30. Na mwenye kuyatenda aliyo
yaharimisha Mwenyezi Mungu kwa uvamizi na kupindukia haki yake, basi tutamtia
Motoni ateketee huko. Na hayo ni madogo na mepesi kabisa kwa Mwenyezi Mungu.
31. Mkiyaachilia mbali
madhambi makubwa makubwa anayo kukatazeni Mwenyezi Mungu, tutakusameheni makosa
yaliyo duni ya hayo, maadamu mnafanya ukomo wa juhudi yenu kwenda sawa; na
tutakuwekeni duniani na Akhera mwahali penye ihsani na hishima kwenu.
32. Wala haifai wanaume
kutamani yale waliyo khusishwa nayo wanawake, wala haiwafalii wanawake kutamani
waliyo khusishwa nayo wanaume. Kwani kila kikundi kina sehemu yake kwa
mujibu wa tabia ya maumbile ya kazi zinazo wawajibikia, na haki wanazo ongezewa.
Basi kila mmoja ajielekeze kutaraji ziada ya fadhila za Mwenyezi Mungu kwa
kukuza vipawa alivyo pewa yeye na kutafuta msaada juu ya waajibu ulio juu yake.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi timamu wa kila kitu, na mtu amepewa namna ya kila
kitu kinacho msilihi.
33. Na wote, wanaume na
wanawake, tumewajaalia kuwa wanastahiki urithi wao wa kuwarithi wazazi wawili,
na jamaa, na wale ambao mfiliwa amefungamana nao kwa agano ambalo matokeo yake
ni kuwa amrithi ijapokuwa si jamaa, na amsaidie pindi anahitajia msaada kuwa ni
badala yake. Basi mpeni haki yake kila mwenye haki, wala msipunguze kitu. Hakika
Mwenyezi Mungu anakuangalieni kwa kila kitu, na yuko pamoja nanyi, anashuhudia
yote myafanyayo.
34. Wanaume wana haki ya
kuwaangalia na kuwachunga wanawake, na kuwasimamia katika mambo yao kwa vile
Mwenyezi Mungu amewapa wao wanaume sifa za kuweza kuisimamia haki hii, na kwa
kuwa wao ndio wanao hangaika na kufanya juhudi ya kutafuta mali ya kuutumilia
ukoo mzima. Basi wanawake wema wanakuwa ni wat'iifu kwa Mwenyezi Mungu na
waume zao. Ni wenye kuhifadhi vyote ambavyo waume zao hawavioni kwa sababu
Mwenyezi Mungu ameamrisha vihifadhiwe, na kwa kuwapa wao tawfiki. Na wanawake
wanao onyesha kuanza uasi wanasihini kwa maneno yenye kuathiri. Kama hawakusikia
tenganeni nao kitandani. Hawakusikia, watieni adabu kwa pigo dogo, si la
kuwajuruhi wala kuwadhalilisha. Wakirejea kwenye ut'iifu wenu kwa njia mojapo
katika hizi tatu basi msiwatafutie kisababu cha kuwatesa zaidi kuliko haya.
Hakika Mwenyezi Mungu yuko juu yenu, naye atakupatilizeni pindi mkiwaudhi wake
zenu au mkawafanyia jeuri.
35. Pindi pakitokea
kukhitalifiana baina ya mke na mume, na mkakhofia kutokea kufarikiana kutako
leta t'alaka, chagueni waamuzi wawili. Mmoja kutokana na upande wa mume na
mwengine upande wa mke. Wakitaka kusuluhiana Mwenyezi Mungu atawawafikisha
wafikilie lilio kheri kwa wote wawili, nako ama kukaa kwa wema au kuachana kwa
ihsani. Hakika Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu cha waja wake, kilicho
dhihiri na kilicho fichikana.
36. Nanyi muabuduni Mwenyezi
Mungu peke yake, wala msimfanyie washirika katika Ungu na kuabudiwa. Na
watendeeni wema wazazi wenu bila ya taksiri yoyote, na pia jamaa zenu, na
mayatima, na walio fakirika kwa sababu ya kuemewa au kupata masaibu katika mali
yao, na jirani mliye karibiana naye kwa nasaba, na jirani mtu mbali, na mwenzio
katika kazi au njia au majlisi, na msafiri mhitaji asiye kuwa na kituo katika
nchi maalumu, na watumwa wenu wanaume na wanawake mlio wamiliki. Hakika
Mwenyezi Mungu hampendi anaye jipa ubora juu ya watu wengine, na hawachukulii
watu kwa huruma, na anakithirisha kujisifu mwenyewe kwa kujifakhiri.
37. Hao ndio wanao ongeza juu
ya takaburi na tafakhuri yao ila ya kuwafanyia watu ubakhili kwa mali yao na
juhudi yao. Tena ikawa wanawataka watu wafanye ubakhili kama wao. Kazi yao
ni kukhofia neema na fadhila ya Mwenyezi Mungu isiwatoke. Kwa hivyo, basi,
hawajifai wenyewe wala hawawafai watu. Wapinzani kama hao tumekwisha waandalia
adhabu ya kutia machungu na ya kudhalilisha.
38. Na
Mwenyezi Mungu hawapendi wanao toa mali kwa ajili ya kuonekana na watu,
wapate kuwasifu na kuwatukuza, na ilhali wao si wenye kumuamini Mwenyezi Mungu
wala Siku ya Malipo. Kwani hao wamemfuata Shetani naye amewapoteza. Na
mwenye kuwa rafiki yake ni Shetani basi ana rafiki mbaya kweli.
39. Ama wamelaanika watu hawa! Kingewadhuru nini wao lau
kuwa wamemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Akhera, na wakatoa katika alicho wapa
Mwenyezi Mungu kwa kufuatana na Imani hii, na usafi wa niya, na kutaraji thawabu
kama ilivyo wajibikia? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kwa ujuzi kaamili mambo
yote yaliyo wazi na yaliyo fichikana ndani.
40. Hakika Mwenyezi Mungu hamdhulumu mtu hata kidogo. Basi
hampunguzii ujira wake mtu, wala adhabu yake hamzidishii kabisa. Bali
humzidishia mtenda mema thawabu zake mardufu hata zikiwa kidogo vipi. Na humpa
kwa fadhila yake malipo makubwa yasiyo lingana na hayo mema yake ambayo
yamekwisha zidishwa mardufu.
41. Vipi basi itakuwa hali ya hao mabakhili wanao pingana na
aliyo yaamrisha Mwenyezi Mungu, tutapo mleta Siku ya Kiyama kila Nabii awe ni
shahidi juu ya kaumu yake, na tukakuleta wewe, ewe Nabii Muhammad, kuwa ni
shahidi juu ya kaumu yako, na hali miongoni mwao wapo hao wanao zuia mali yao na
wanao pinga?
42. Yatapo tokea haya watatamani hao wapinzani wanao pinga
lau kuwa wangeli potea chini ya ardhi kama wanavyo potea maiti makaburini! Na
wao hawawezi kumficha Mwenyezi Mungu kitu chochote katika mambo yao, na hali zao
na vitendo vyao vitadhihiri.
43. Enyi mlioamini! Msende kusali misikitini nanyi mmo
katika hali ya ulevi mpaka muwe mnafahamu myasemayo. Wala msiingie misikitini
nanyi mna janaba, ila ikiwa ni kupita njia tu bila ya kusita, mpaka mtahirike
kwa kukoga. Na mkiwa ni wagonjwa hamuwezi kutumia maji kwa kuogopa maradhi
yasikuzidini au kuchelewa kupona, au mkiwa mmo safarini na ipo shida ya kupata
maji, basi tumieni mchanga ulio safi. Kadhaalika mmoja wenu akitoka chooni, au
mkawaingilia wanawake na mkawa hamkupata maji ya kujitahirishia kwa kukosekana
kwake, basi vile vile chukueni mchanga safi upigeni kwa mikono yenu, na
mpangusie nyuso zenu na mikono yenu. Hakika ni shani ya Mwenyezi Mungu kuwa ni
Mwenye kusamehe sana na Mwenye kufuta dhambi.
44. Hebu huyastaajabii mambo ya hawa walio pewa sehemu ya
Vitabu vilivyo tangulia wanavyo acha uwongofu na wakatafuta upotovu katika mambo
yaliyo wakhusu nafsi zao! Na wao tena wanakutakeni nyinyi mjitenge na Haki
ambayo ndiyo Njia ya Mwenyezi Mungu Iliyo Nyooka!
45. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi kuliko nyinyi kuwajua
maadui zenu wa kweli, na anatambua zaidi yaliyo ndani ya nafsi zao. Ulinzi wa
Mwenyezi Mungu unakulindeni, na unakuangalieni, na unakutosheni. Basi
msitafute ulinzi wa mwenginewe usio kuwa wake. Msaada na nusura yake
inakutoshelezeni; basi msiwe kutaka msaada wa mwenginewe.
46. Miongoni mwa Mayahudi kipo
kikundi kazi yao kugeuza geuza maana ya maneno. Wao husema
kimoyomoyo kumwambia Mtume s.a.w.: Tumesikia hayo maneno, na hatuifati hiyo
amri. Na pia husema: Sikia maneno yetu - hukusikia wito. Wakikusudia kwa hayo
kumuapiza Mtume. Na husema: Sikia bila ya kusikilizwa. Tamko hilo
wanalipindua maana. Muradi wao ni kumuapiza, na wanajidai kuwa muradi wao ni
kumwombea dua. Na husema: "Raai'na", wakipindua ndimi zao wakijitia kuwa
wanakusudia "Undhurna" yaani "Tuangalie". Wanaonyesha kuwa wanataka uangalizi
wake, na kumbe wanakusudia neno la Kiyahudi lenye maana ya "Mpumbavu" ili
kuibeza Dini ya Kiislamu.
Na lau kuwa wangeli
nyooka sawa wakasema: "Tumesikia na tumet'ii" badala ya hiyo kauli yao ya
"Tumesikia na tumeasi", na wakasema: "Sikia" na wasiseme "Bila ya kusikilizwa",
na wakasema :"Undhurna" yaani "Tuangalie", badala ya "Raa'ina", ingeli kuwa
bora kwao kuliko hayo wayasemayo, na ingeli kuwa ndiyo njia ya uadilifu
zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu amewatoa katika rehema yake kwa ule upinzani wao.
Kwa hivyo huwaoni miongoni mwao wanao mwitikia mwenye kuwaitia Imani ila
wachache tu.
47. Enyi mlio pewa Kitabu alicho teremsha Mwenyezi Mungu!
Iaminini Qur'ani tuliyo mteremshia Muhammad, inayo sadikisha mliyo nayo, kabla
hatujawateremshia adhabu ya kufutwa nyuso zenu zikawa kama visogo, hazina pua,
wala macho, wala nyusi. Au tukakutoeni katika rehema yetu kama tulivyo watoa
wale walio ikhalifu amri yetu wakatenda waliyo katazwa ya kuvua samaki siku ya
mapumziko,(Sabt au Sabato) siku ya Jumaamosi. Na hukumu ya Mwenyezi Mungu ni
yenye kutimizwa tu, wala hapana cha kuipinga.
48. Hakika Mwenyezi Mungu hafuti dhambi za ushirikina,
kumfanya Yeye ana mshirika yeyote. Na husamehe dhambi zilio chini ya huo
ushirikina kwa amtakaye miongoni mwa waja wake. Na mwenye kumshirikisha
Mwenyezi Mungu basi amemzulia Mwenyezi Mungu na ametenda dhambi kubwa mno isiyo
stahiki kusamehewa.
49. Hustaajabii hali ya hao makafiri wanao zua kwa vitendo
vyao? Vitendo vyao viovu wao wanaviona kuwa ni vizuri. Wanajisifu kuwa kwa
vitendo hivyo wao wametakasika. Na ni Mwenyezi Mungu tu peke yake ndiye anaye
jua jema na baya. Yeye ndiye wa kumtakasa amtakaye, na wala hamdhulumu mtu
yeyote kadiri yake hata chembe.
50. Vipi watu hawa wanavyo mzulia Mwenyezi Mungu uwongo kwa
haya na mengineyo mfano wa haya! Yatosha uwovu ulio wazi kwa huu uwongo wao
kuyakashifu maovu yao.
51. Hebu huwastaajabii hawa walio pewa sehemu ya ujuzi wa
Kitabu wanavyo ridhia ibada ya masanamu na Shetani, na wanavyo sema kuwa hao
waabuduo masanamu ni afadhali wameongoka kwenye Njia kuliko Waislamu wenye
kuamini?
52. Hao ndio alio watupa Mwenyezi Mungu na akawafukuzilia
mbali kutoka kwenye rehema yake. Na mwenye kutupwa na Mwenyezi Mungu na
akatolewa kwenye rehema yake basi kabisa huyo hana wa kumnusuru na kumlinda na
ghadhabu ya Mola wake Mlezi.
53. Hao wamekoseshwa neema ya kuifuata haki, kama walivyo
koseshwa na utawala. Na lau wakipewa utawala hawanufaishi watu hata chembe.
54. Na vipi watu hawa wanavyo waonea maya Waarabu? Na
wakaona ni jambo kuu kuwa Mwenyezi Mungu alivyo wapa fadhila yake kwa kuwatolea
Nabii kutokana nao, na ilhali Mwenyezi Mungu alimpa Ibrahim na ukoo wake - naye
ni baba yenu (Mayahudi na Wakristo), na baba yao (Waislamu pia) - Kitabu kilicho
teremshwa kwa ufunuo, na Unabii na Utawala ulio mkubwa!
55. Miongoni mwa walio pelekewa Nabii Ibrahim na ukoo wake
wapo wenye kukiamini Kitabu kilicho teremshiwa kwao, na wapo walio kipa nyongo
wakajitenga nacho. Na jaza ya hawa wenye kujitenga na wito wa Haki ni Jahannamu
yenye moto wa kuteketeza.
56. Hakika wanao pinga hoja zetu zenye kubainisha wazi wazi,
na wakawakanusha Manabii, tutakuja watia kwenye Moto utakao babua ngozi zao. Na
kila zikisita kuhisi adhabu Mwenyezi Mungu atawabadilishia ngozi nyengine mpya
ili machungu ya adhabu yabaki yakiendelea. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
ushindi katika mambo yake, na Mwenye hikima katika vitendo vyake. Humuadhibu
mwenye kumpinga na akabaki na upinzani mpaka kufa kwake.
Qur'an Tukufu imeitangulia sayansi ya
kisasa, ikathibitisha kuwa katika ngozi mishipa ya kuhisi, Navo, imetanda
kama wavu, na hiyo hupokea mishipa yote ya kuhisi machungu, joto na baridi na
mengineyo. Na hayo hayakujuulikana ila hivi karibuni.
57. Na ambao walio yasadiki yaliyo wajia kutoka kwa Mola wao
Mlezi, na wakatenda vitendo vyema, tutawalipa kwa Imani yao na vitendo vyao na
tutawaingiza katika Mabustani ya Peponi yapitayo mito chini ya miti yake. Uhai
wao hauna kikomo kabisa. Nao humo watakuwa na wake walio t'ahirika na kila la
aibu na uchafu. Tutawapa uhai wa starehe chini ya vivuli vizuri vya kudumu,
waishi maisha mema yenye neema isiyo kwisha.
58. Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni nyinyi Waumini
mrejeshe vyote mlio pewa amana, kutokana na Mwenyezi Mungu au kutokana na watu,
kwa wenyewe kwa uadilifu. Basi msifanye jeuri katika kuhukumu. Haya ni
mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu Mlezi. Basi yafanyieni pupa kuyafuata. Bora
ya mawaidha ni yanayo tokana naye Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu daima ni Mwenye
kusikia yasemwayo, ni Mwenye kuyaona yatendwayo. Basi anamjua anaye rejesha
amana, na anaye fanya khiana, na anaye hukumu kwa uadilifu, na anaye fanya
jeuri. Na kila mmoja atamlipa kwa atendalo.
59. Enyi mlio sadiki aliyo kuja nayo Muhammad! Mt'iini
Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume, na wale wanao tawala mambo yenu miongoni mwa
Waislamu wanao simama juu ya haki na uadilifu, na wanatekeleza Sharia ya
Mwenyezi Mungu. Na mkizozana katika jambo baina yenu basi rejeeni kwenye Kitabu
cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake ili mpate kujua hukumu yake. Kwani
Yeye Mwenyezi Mungu amekuteremshieni Kitabu chake na Mtume wake amebainisha
hicho Kitabu. Na katika hayo ipo hukumu ya hayo mnayo khitalifiana kwayo. Haya
ni kwa mujibu wa Imani yenu kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na haya
ndio bora kwenu ili mpate kuongoka kwendea uadilifu katika mnayo khitalifiana
kwayo, na mwisho wake ndio mzuri zaidi. Kwani hivyo ndio kuzuia zisitokee
khilafu zinazo pelekea ugomvi na upotovu.
60. Ewe Nabii! Huwastaajabii hao wanao dai kuwa wanasadiki
Kitabu ulicho teremshiwa wewe na vilivyo teremshwa kabla yako wewe, wanataka
wahukumiwe katika ugomvi wao kwenye upotovu na uharibifu na hukumu isiyo kuwa ya
Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu amekwisha waamrisha wayapinge hayo, wala
wasitake kuhukumiwa kwa hayo. Na Shetani anataka awaachishe Njia ya Haki na
Uwongofu, awapotezelee mbali.
61. Na wakiambiwa: Njooni kwenye Qur'ani na Sharia aliyo
iteremsha Mwenyezi Mungu, na njooni kwa Mtume wake akubainishieni, utaona hao
wanaafiki wanajitenga nawe kabisa wanakukataa.
62. Itakuwaje hali basi yakiwateremkia masaibu kwa sababu ya
uovu wao na upotovu wa vitendo vyao, na wasipate pa kukimbilia ila kwako! Hapo
basi watakuapia Mungu mbele yako kuwa wao hawakukusudia kwa maneno yao na
vitendo vyao ila wema tu na kutaka mapatano.
63. Hao ndio wanao kula yamini kuwa hawakutaka ila wema na
vitendo vya muwafaka. Mwenyezi Mungu anayajua vyema yaliyomo katika nyoyo zao,
na anaujua uwongo wa hiyo kauli yao. Basi wewe usishughulike na maneno yao.
Waite kwenye haki kwa mawaidha yaliyo mema, na sema nao maneno yenye hikima
yenye kuathiri yanayo fika ndani ya nyoyo zao.
64. Na Sisi hatukumtuma Mtume yeyote ila jambo lake kuu ni
kuwa at'iiwe, na ut'iifu huo ni kwa ruhusa iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu.
Na hakika mwenye kwenda kinyume, au kukanusha, au kukhaalifu, anakuwa ni mwenye
kujidhulumu mwenyewe. Na lau kuwa hawa walio jidhulumu wakirejea kwenye
uwongofu, wakakujia wakiomba msamaha kutokana na Mwenyezi Mungu kwa yale waliyo
yatenda, na wewe ukawaombea msamaha kwa mujibu wa ujumbe wako na kwa
ulivyo ona ilivyo geuka hali yao, basi hapana shaka watamkuta Mwenyezi Mungu,
Aliye takasika na kutukuka, ni Mwingi wa kukubali toba, na Mwenye kuwarehemu
waja wake.
65. Naapa kwa jina la Mola wako Mlezi! Hawahisabiwi kuwa ni
Waumini wa Haki na wenye kuinyenyekea, mpaka watakapo kufanya wewe hakimu
muamuzi wa mizozo inayo tokea baina yao. Kisha nafsi zao zisione dhiki kwa
utavyo hukumu, na wakunyenyekee kama wanavyo nyenyekea Waumini wa kweli.
66. Na lau kuwa Sisi tumewalazimisha mashaka ya mwisho, kwa
kuwaamrisha wapigane Jihadi moja kwa moja, na wajitolee nafsi zao kutilifu, au
watoke nje waache majumba yao kwenda pigana Jihadi daima, wasinge kubali kut'ii
ila wachache tu. Lakini Mwenyezi Mungu, Aliye takasika na kutukuka, hakalifishi
ila linalo wezekana. Na lau kuwa wange fanya hayo na wakafuata haki yake ingeli
kuwa ni kheri yao ya duniani na Akhera. Na hivyo ndiyo inavyo pelekea kuthibiti
Imani, na kuingia imara, na kuleta utulivu.
67. Na lau kuwa wamesimama juu ya Haki aliyo ilazimisha
Mwenyezi Mungu kwa kadri ya uweza wao, Mwenyezi Mungu angeli wapa malipo makubwa
kwa fadhila yake.
68. Na kwa sababu ya kut'ii kwao kwa uweza wao inakuwa
hakika Mwenyezi Mungu amewaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka isio pindukia kiasi
kwa kuzidi au kupungua.
69. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume kwa kuzifuata
kwa unyenyekevu amri zao na kuridhia hukumu yao, basi huyo yu pamoja na alio
waneemesha Mwenyezi Mungu kwa uwongofu na kuwawezesha duniani na Akhera. Na watu
hao ni Manabii wake, na wafuasi wao walio wasadiki na kuwakubali na wakafuata
nyendo zao, na Mashahidi walio kufa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na watu wema
watendao mema kwa siri na dhaahiri. Na hapana la kushinda uzuri kuliko
kuwa pamoja na watu hawa - haingii mashakani mwenye kukaa nao, wala hayachoshi
mazungumzo yao.
70. Hayo ni makao matukufu kwa mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu
na Mtume wake. Hiyo ni fadhila kubwa inayo tokana na Mwenyezi Mungu. Naye
anavijua sana vitendo vyenu, naye atakulipeni kwavyo. Yamtosha Muumini kuwa
Mwenyezi Mungu anamjua, naye lake ni kumt'ii Mola wake Mlezi na kutafuta radhi
zake.
71. Enyi Mlio amini! Daima kuweni na hadhari na maadui wenu.
Jizatitini kupambana na vitimbi vyao. Na mkitoka kwenda vitani tokeni kwa vikosi
vikosi, au tokeni nyote pamoja.
72. Na wahadharisheni wanao kaa
nyuma wasende nanyi vitani. Miongoni mwa hao hao mnao ishi nao wakajizuia
wasifuatane nanyi kwenda kupigana, mkipatwa na shida na masaibu katika Jihadi,
wao wa kikundi hicho, kwa kufurahia yaliyo kusibuni, husema: Mwenyezi Mungu
katufanyia kheri kwa kuwa hatukwenda nao vitani.
73. Na mnapo pata fadhila ya ushindi kutokana na Mwenyezi
Mungu, mkapata ngawira za vita, kikundi hicho hicho, kwa kuona maya na kutamani,
husema: Laiti tungeli kuwa nao katika vita hivi, nasi tukapata mafanikio ya
ngawira nzuri. Na husema haya na hayo kama kwamba hapakuwepo mapenzi yoyote
yaliyo wafunga wao na nyinyi.
74. Ikiwa yupo kati yenu anaye bakia nyuma asende kupigana
kutokana na udhaifu wa Imani yake, au ulegevu wa azma yake, basi na wapigane,
kuinua Neno la Mwenyezi Mungu na kuwania Haki, wale walio uza uhai wao wa dunia
kutafuta uhai wa Akhera. Na mwenye kupigana vita kwa ajili ya kunyanyua Neno la
Mwenyezi Mungu na kuwania Haki, atapata moja ya mema mawili. Ama atauliwa apate
fadhila ya kufa shahidi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, au atashinda, apate
fadhila ya kufuzu katika dunia. Naye katika hali zote mbili atapewa na Mwenyezi
Mungu ujira mkubwa katika Akhera.
75. Vipi inakufalieni kuwa msipigane katika Njia ya Mwenyezi
Mungu na hali wanyonge, wanaume na wanawake na watoto wao, wanayayatika kuomba
msaada wa kuwanusuru, huku wakimwomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu wakisema:
Ewe Mola Mlezi wetu! Tutoe kwenye utawala wa hawa madhaalimu, na kwa nguvu
zako na rehema yako tuwezeshe tuwe chini ya utawala wa Waumini; na
tujaalie kutoka kwako mgombozi wa kutunusuru!
76. Walio isadiki Haki na wakaifuata, hupigana kwa ajili ya
kulitukuza Neno la Mwenyezi Mungu, na uadilifu, na Haki. Na wale wanao pinga
wakafanya inadi hupigana kwa ajili ya dhulma na uharibifu. Kwa hivyo hawa
wamekuwa ni vipenzi vya Shetani. Basi enyi Waumini! Wapigeni vita hao, kwani wao
ni wenzake Shetani na wasaidizi wake. Na jueni kuwa nyinyi mtawashinda tu kwa
kuungwa mkono na Mwenyezi Mungu, kwani mpango wa Shetani, na ingawa mkubwa vipi
ufisadi wake, ni dhaifu, hauna nguvu. Na Haki ndiyo yenye ushindi.
77. Ewe Muhammad! Hebu huwaangalii ukawastaajabia wale walio
taka kupigana kabla ya kuja ruhusa, wakaambiwa: Bado haujafika wakati wa vita.
Basi izuieni mikono yenu msipigane. Bali shughulikieni kushika Sala, na kutoa
Zaka. Na Mwenyezi Mungu alipo waamrisha wapigane kikawa kikundi kimoja
kati yao kikawa kinawaogopa watu kama kumkhofu Mwenyezi Mungu, au zaidi.
Wakasema kwa kuona ni mageni hayo: Kwa nini ukatuamrisha kupigana? Wao
walidhani kuwa kuamrishwa vita kunahimiza ajali yao, na kwa hivyo wakasema: Hebu
lau ungeli tungojea muda kidogo tupate kustarehe na ulimwengu! Waambie:
Songeni mbele mkapigane hata ikiwa mtakufa mashahidi, kwani starehe ya dunia,
ingawa ni kubwa vipi, ni chache ukilinganisha na starehe ya Akhera. Na Akhera ni
bora na kubwa zaidi kwa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, na huko mtakuja lipwa kwa
vitendo vyenu vya duniani, wala hampunguziwi hata chembe katika ujira wenu.
78. Hakika hayo mauti mnayo yakimbia yatakukuteni popote
pale mlipo, na hata mkikaa ndani ya ngome zilizo jengwa madhubuti imara. Na hao
wenye imani legevu na dhaifu husema pindi wapatapo ushindi na ngawira:
Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na pindi wapatapo lawama au
kushindwa wao hukwambia wewe: Ewe Muhammad! Haya yanatokana na wewe.
Haya si lolote ila kukufanya kuwa wewe ni mkorofi, na kukutupia lawama wewe
badala ya nafsi zao. Basi waambie: Kila linalo kupateni, mnalo lipenda na
mnalo lichukia, linatokana na kudra ya Mwenyezi Mungu, na linatokana na
majaribio yake na mitihani yake. Wana nini watu hawa madhaifu hata hawajakaribia
kujua usawa wa maneno wanayo ambiwa?
79. Ewe Nabii! Kufanikiwa, na neema, na afya, na salama
unayo ipata inatokana na fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako. Yeye anafanya haya
kukufadhili kukufanyia hisani. Na inapo kusibu shida, na mashaka, na udhiya, na
ya karaha, basi yanatokana na nafsi yako mwenyewe kwa sababu ya upungufu fulani
au makosa uliyo yatenda. Haya anaambiwa Mtume s.a.w. ni kama mfano wa wanaadamu
wote ijapo kuwa halikutokea kwake la uovu. Kwani Mtume anaambiwa: Tumekutuma
kuwa Mtume kutoka kwetu kwa watu wote. Na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kufikisha
kwako huo ujumbe na juu ya kuitikia kwao hao watu. Na Yeye ni Mjuzi wa kutosha.
80. Mwenye kumt'ii Mtume basi ndio amemt'ii Mwenyezi Mungu,
kwani yeye haamrishi ila alicho amrisha Mwenyezi Mungu. Wala hakatazi ila alicho
kataza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo kumt'ii yeye (Mtume s.a.w.) ndio kutenda na
kuacha kwa ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kukataa kukut'ii wewe basi,
kwani Sisi hatukukupeleka wewe ila uwe ni mbashiri na mwonyaji tu, sio uwe ni
mlinzi wao na muangalizi wao, uwalindie vitendo vyao. Hayo ni yetu Sisi
sio yako.
81. Na kikundi hichi kinacho tapatapa husema: Amri
yako tunait'ii. Hatuna kwako ila kut'ii unayo amrisha na kukataza. Lakini
wakisha toka kwako wakawa mbali nawe, baadhi yao hupanga vijambo vyao usiku
usiku, kinyume na unavyo waambia ya kuwaamrisha na kuwakataza. Na Mwenyezi
Mungu, Subhanahu wa Taa'la, Aliye takasika na Kutukuka, anayadhibiti yote wanayo
yapanga kwa siri. Basi usiwashughulikie, na wapuuze, na mwachie mambo yao
Mwenyezi Mungu, na wewe mtegemee Yeye. Na Mwenyezi Mungu ni wa kutosha kuwa ni
Mtegemewa wako, na Mlinzi wako wa kumwachilia mambo yako yote.
82. Basi hao wanaafiki hawakizingatii Kitabu cha Mwenyezi
Mungu wakajua hoja za Mwenyezi Mungu zilio juu yao kuwa ni waajibu kut'ii na
kufuata amri yako? Na kwamba Kitabu hichi kinatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa
yalivyo shikamana maana yake na hukumu zake, na kinavyo fungamana wenyewe kwa
wenyewe? Hii ni dalili kuwa ni kweli kinatoka kwa Mwenyezi Mungu; kwani
lau kuwa kinatokana na mwenginewe basi maana yake yangeli gongana, na hukumu
zake zingeli khitalifiana sana.
83. Na hichi kikundi cha wanaafiki kikipata khabari zozote
zilio khusu nguvu au udhaifu wa Waislamu huzitangaza na kuzieneza nje, ili
kuwababaisha Waislamu au kuwatia khofu katika nyoyo zao, au ili zifike khabari
zao kwa maadui wao. Na lau kuwa hawa wanaafiki watangazao wamerudisha
jambo lilio khusu usalama au kitisho kwa Mtume na kwa wakuu wa mambo miongoni
mwa waongozi na Masahaba wakubwa, wakataka kwao kujua hakika, wangeli jua hao
wanao jitahidi kuchungua mambo na kuyatangaza, kuwa yaliyo kweli yanatokana na
Mtume na waongozi wengine. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu
juu yenu kwa alivyo zithibitisha nyoyo zenu juu ya Imani, na kuzuia fitina, na
rehema yake kwa kukupeni sababu na njia za ushindi, wengi wenu wangeli fuata
upotovu wa Shetani, na wasingeli okoka kutokana na upotovu wake ila wachache tu.
84. Na kama wapo kati yenu mfano wa hawa wanaafiki basi
wapuuzilie mbali. Na wewe pigana kwa ajili ya Neno la Mwenyezi Mungu na kwa
ajili ya Haki. Wewe huna jukumu ila la nafsi yako tu. Kisha waite Waumini wende
vitani, na wahimize. Huenda Mwenyezi Mungu kwa kupitia kwako na kwao akazuia
hayo mashambulio ya makafiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukuungeni mkono, na
ni Mwenye kukunusuruni. Na Yeye ana nguvu kuliko wote, na mkali kuliko wote
katika kuwaadhibu makafiri.
85. Na hawa wanaafiki husaidia ufisadi, na watu wa Imani
husaidia Haki. Na mwenye kusaidia jambo jema ana fungu lake la thawabu. Na
mwenye kuwasaidia watu waovu naye ana mzigo wake wa dhambi katika malipo yake.
Na Mwenyezi Mungu ana uweza juu ya kila kitu, na Mwenye kujua kila kitu.
86. Akikuamkieni mtu yeyote kwa maamkio ya salamu, au dua,
au ya namna yoyote ya hishima, au namna nyengine yoyote ile, basi mjibuni kwa
maamkio yaliyo mazuri zaidi, au kwa uchache mjibuni kama alivyo kuamkieni yeye.
Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kutia hisabuni kila kitu, kikubwa na
kidogo.
87. Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu ila Yeye, wala hapana
mwenye uweza ila Yeye, hapana shaka atakufufueni baada ya kufa kwenu, na
atakukusanyeni kwenye kituo cha kuhisabiwa kwa ajili ya malipo. Hayo hayana
shaka. Yeye anasema hayo, basi msiyatilie shaka maneno yake. Na kauli gani iliyo
ya kweli zaidi kuliko kauli ya Mwenyezi Mungu?
88. Haikufaliini, enyi Waumini, kukhitalifiana katika
mas-ala yaliyo khusu wanaafiki, ambao wanadhihirisha Uislamu na wanaficha
ukafiri. Haikufaliini kukhitalifiana kwa mas-ala yao, kuwa ati wao ni Waumini au
makafiri? Wauwawe au waachiliwe? Je, wameelekea kuongoka au hawatarajiwi
uwongofu? Fahamu zao zimegeuzwa kwa yaliyo chumwa na vitendo vyao. Shari imekuwa
ndio inayo wahukumu, basi usimtarajie kuongoka yule ambaye Mwenyezi Mungu kwa
ujuzi wake wa tangu na tangu kesha mkadiria asiongoke. Kwani aliye andikwa
katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu wa tangu azali kuwa ni mwenye kupotea basi huna
njia ya kumwongoa.
89. Hakika nyinyi mnapenda kuwaongoa hawa wanaafiki, na wao
wanapenda nyinyi mkufuru kama wao, ili muwe nyote sawa kwa ukafiri. Ilivyo
kuwa hivyo basi msitake wa kukuungeni mkono miongoni mwao. Wala msiwafanye
wenzenu, mpaka wakubali kutoka huko kwao kuwania Jihadi kwa ajili ya Uislamu.
Hivyo tu ndio itawatoka sifa ya unaafiki. Lakini wakiyakataa hayo, wakaungana na
maadui zenu, basi wauweni popote mtapo wapata, wala msiwaone kuwa ni
wenzenu, wala msiwachukulie kuwa ndio wasaidizi wenu.
90. Katika wanaafiki, wanao stahiki kuuliwa kwa fisadi yao
kuwafisidi umma wa Waumini, watoe wale ambao wamefungamana na kaumu ambao baina
yao na Waumini yapo mapatano ya kuzuia kuuliwa aliye fungamana na upande mmoja
wapo. Au vile vile ambao wametatizwa hawajui wapigane pamoja na watu wao, ambao
ni maadui wa Waislamu wasio na mkataba nao, au wapigane pamoja na Waumini? Kwani
hakika wale wa kwanza inakatazwa kuwauwa kwa ajili ya mkataba, na wengine
inakatazwa kuwauwa kwa kuwa hawajui moja wapo la kutenda. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu Mtukufu amependa angeli wajaalia hao wakupigeni vita. Ilivyo kuwa
wamekhiari kukaa tu wasikupigeni na wakaingiana nanyi kwa salama na amani, basi
haikufaliini nyinyi kuwauwa. Hapana ruhusa kufanya hayo.
91. Mkiwashinda washirikina, hao wanaafiki huwa pamoja
nanyi; na washirikina wakiwashinda Waislamu, wao huwa pamoja na washirikina. Wao
hutaka wapate amani kwa Waislamu na wapate amani kwa jamaa zao washirikina. Hawa
wamo katika upotovu na unaafiki wa moja kwa moja. Ikiwa hawatoacha kukupigeni
vita na wakakutangazieni amani na salama, basi wauweni popote muwapatapo. Kwani
kwa kuto kujitenga na kukupigeni vita, basi inakuwa Waumini wana haki kuwauwa.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa Waumini hoja iliyo wazi kuwapiga vita.
92. Kuwagawa wanaafiki namna hii ni kwa ajili ya kutoka
shakani, ili Muumini asimuuwe Muumini mwenziwe kwa kumdhania kuwa ni mnaafiki.
Na haijuzu kumuuwa Muumini ila kwa kukosea, bila ya kukusudia. Na katika
hali ya kumuuwa Muumini kwa kukosea akiwa anaishi chini ya utawala wa dola ya
Kiislamu, basi atatoa muuwaji diya kuwapa walio fiwa kuwa ni fidia kwa mtu
waliye mkosa, na tena amkomboe mtumwa aliye Muumini iwe ni kuwafidia umma wa
Kiislamu kwa walicho kosa. Kwani kumkomboa Muumini ni kama kumhuisha mtu kwa
kumpatia uhuru. Inakuwa kwa kukomboa shingo ya Muumini ni kuulipa umma wa
Kiislamu kwa walicho kosa.(1)
Ikiwa aliye uliwa
yumo katika watu ambao wana mapatano ya amani na Waislamu, basi yapasa kumpa
uhuru mtumwa na kuwalipa watu wa maiti diya, kwani inakuwa hawaichukui hiyo diya
kwa kuwaudhi Waislamu kwa sababu ya mapatano yao. Na ikiwa mwenye kuuwa bila ya
kukusudia hakupata mtumwa Muumini wa kumkomboa, basi afunge miezi miwili
mfululizo, asile mchana hata siku moja. Hayo yawe ni kuitengeza nafsi na
kujizoesha kuwa na hadhari zaidi. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Aliye
tukuka anazijua sana nafsi za watu na niya zao. Naye ni Mwenye hikima, anajua
kuzipanga adhabu zake.
(1)"Kuulipa" kwa kuwa utumwa ni amana ya mtu, na kumkomboa
mtumwa ni kumhuisha mtu. Akiuliwa Muumini kwa kukosea, na mwenye kuuwa akakomboa
shingo ya Muumini basi huyo amehuisha na kuulipa umma.
93. Hakika mwenye kumuuwa Muumini kwa mauwaji ya kukusudia
na kuona ndio ndivyo mauwaji hayo, jaza yake inayo lingana na ukhalifu huo ni
kuingizwa Motoni milele, na kughadhibikiwa na Mwenyezi Mungu na afukuzwe
kutokana na rehema yake. Na Mwenyezi Mungu amemtengezea Akhera adhabu kubwa,
kwani kitendo hichi ndio ukhalifu mkubwa kabisa katika dunia.
94. Kutahadhari msije mkamuuwa Muumini ni waajibu katika
wakati wa kwenda vitani. Mkisafiri kwa ajili ya Jihadi ya Njia ya Mwenyezi Mungu
jijuvyeni hakika ya hao mnao pigana nao kabla ya kupambana. Je, hao wamesilimu
au bado ni washirikina. Wala msimwambie anaye kutoleeni salamu kuwa ni
ishara ya amani: Wewe si Muumini, kwa kuwa mnataka kumnyang'anya
mali yake na kondoo wake. Bali ipokeeni salamu yake, kwani kwa Mwenyezi Mungu
amekuahidini kupata ngawira nyingi nyenginezo. Na nyinyi, enyi Waumini! Mlikuwa
hivyo hivyo katika ukafiri kabla ya hayo, na Mwenyezi Mungu amekuhidini. Basi
hakikisheni mambo ya hao mnao wakuta. Na Mwenyezi Mungu anajua baraabara, na
hapana chochote kinacho fichikana kwake. Na Yeye hakika ni Mwenye kuhisabu kwa
mujibu wa ujuzi wake.
95. Na hakika Jihadi pamoja na kuchukua hadhari inayo
takikana ina fadhila kubwa sana. Basi hawawi sawa wanao kaa majumbani mwao
wasende kupigana Jihadi na wale Mujaahidiina, wanao pigana kwa mali yao na nafsi
zao. Kwani Mwenyezi Mungu amewanyanyua wale Mujaahidiina daraja, cheo cha juu
kuwashinda wale wanao kaa nyuma; ila ikiwa wale wanao kaa nyuma wana udhuru unao
wazuia kutoka kwenda vitani. Hapo inakuwa udhuru wao unawatoa lawamani, juu ya
kuwa wanao pigana wana fadhila na cheo makhsusi. Mwenyezi Mungu amewaahidi
makundi yote mawili mashukio mema, na matokeo mazuri.
96. Na cheo hichi walicho khusishwa nacho hao wanao pigana
Jihadi ni cheo kikubwa, cha juu, hata imekuwa ni kama cheo cha
kutafautisha sana baina yao na wengineo. Na kwa ajili ya cheo hichi watapata
maghfira makubwa na rehema kunjufu.
97. Na hakika ni waajibu wa Muislamu kuhamia kwenye dola ya
Kiislamu asiishi katika udhalili. Malaika watawauliza wakisha kufa: Mlikuwaje
hata mkaridhia maisha ya unyonge na kudharauliwa? Na wao watajibu: Tulikuwa
wanyonge katika nchi hiyo tukionewa. Malaika watawaambia: Kwani ardhi ya
Mwenyezi Mungu haikuwa kunjufu ina wasaa, mkaweza kuhama badala ya kuishi katika
uonevu? Watu hao wanao kubali uonevu, na wao wanaweza kuondoka, makao yao
yatakuwa ni Jahannamu. Na hayo ni mashukio maovu kabisa. Basi Muislamu
haimfalii kuishi katika udhalili, bali aishi na utukufu wake na hishima yake.
98. Juu ya hivyo wanasameheka na adhabu hii wale wasio weza
kusafiri miongoni mwa wanaume, na wanawake, na watoto, wasio na nguvu, na hawana
hila, wala hawakupata njia ya kutoka.
99. Na hao wanatarajiwa kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu. Na
ni shani yake Mwenyezi Mungu kusamehe na kughufiria.
100. Anaye hama kutafuta njia za kuiwania Haki na kuiunga
mkono, atakuta duniani kwingi endako ambako maadui wa Haki wanahizika. Na
atapata wasaa wa uhuru, na makao ya hishima,na thawabu, na ujira mkubwa. Aliye
toka kwake kuhamia dola ya hishima, ambayo ndiyo dola ya Mwenyezi Mungu na
Mtumewe, kisha yakamdiriki mauti kabla hajafika endako, basi ujira wake
umethibiti. Mwenyezi Mungu amemkirimu kwa kujiwajibishia kumlipa ujira wake, na
kumghufiria na kumrehemu. Ni shani yake kughufiria na kurehemu.
101. Sala ni faridha isiyo epukika. Haiachiki Sala kwa ajili
ya safari, lakini hana dhambi anaye fupisha Sala safarini. Watokao kwenda safari
wakikhofia kuwa makafiri watawaletea ya kuwaudhi, wanaweza kufupisha Sala. Sala
za rakaa nne zisaliwe rakaa mbili. Kutahadhari na kuingiliwa na makafiri ni
waajibu, kwani wao ni maadui, na uadui wao uwazi.
102. Ewe Nabii Muaminifu, ukiwa nao na Sala ya Jamaa
inasaliwa, msisahau kutahadhari na maadui. Na hayo ni kuwagawa Waislamu makundi
mawili. Moja lianze kusali kwa kukufuata wewe, na wakati huo la pili lisimame
kwa hadhari na silaha likilinda vifaa. Ukisha nusu ya Sala, kundi lilio sali
nawe lende nyuma yako, na lije jengine lisali nawe Sala iliyo bakia. Kisha
litimize sehemu waliyo ikosa. Na lile la kwanza lisali baki ya Sala. Na hii
huitwa "Laahiqah", yaani iliyo kutwa (1) na nyengine inaitwa "Masbuuqah", yaani
iliyo tanguliwa ,kwa kuwa inasaliwa mwanzo wa Sala ya Jamaa; na "Laahiqah"
inasaliwa mwisho wa Sala ya Jamaa. Mpango huu ni kwa sababu isikosekane Sala, na
kutahadhari na makafiri ambao wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu
wapate kukuvamieni kwa ghafla, na wakumalizeni nanyi mmo katika Sala. Vita na
washirikina ni waajibu, na havina ukomo. Lakini hapana dhambi juu yenu kusita
kwa ajili ya udhuru kama mvua au maradhi, juu ya kuwa lazima muwe na hadhari ya
kudumu. Na hii ni adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa makafiri hapa duniani, na Akhera
amewaandalia adhabu ya fedheha na udhalili.
(1) "Laahiq" ni anaye sali na Imam mwanzo wa Sala na
akalazimika kusali iliyo baki peke yake, na "Masbuuq" anaye iwahi sehemu ya
mwisho ya Sala ya Jamaa, kisha akatimiza sehemu aliyo ikosa peke yake.
103. Na mkisha Sala ya vita, inayo itwa Sala ya Khofu,
msisahau kumkumbuka Mwenyezi Mungu daima. Mkumbukeni nanyi mmesimama, mnapigana,
mmekaa, na mmelala. Kwani kumkumbuka Mwenyezi Mungu Mtukufu kunatia nguvu nyoyo,
na kuzituliza. Khofu ikiondoka pakawa na utulivu basi timizeni Sala kwa
ukamilifu, kwani Sala imefaridhiwa juu ya Waumini isaliwe kwa nyakati zake.
104. Msilegee kuwafukuzia makafiri walio kwisha
kukutangazieni vita na wanajaribu kukushambulieni kila pahala. Hakika vita
havikosi maumivu. Ikiwa nyinyi Waumini mmepata majaraha na mengineyo, na wao
makafiri pia wameyapata machungu. Khitilafu yenu ni kuwa wao hawapiganii Haki,
wala hawataraji kitu kwa Mwenyezi Mungu; na nyinyi mnataka Haki na mnataraji
radhi za Mwenyezi Mungu na neema za kudumu. Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo
vyenu na vyao, naye ni Mwenye hikima, anamlipa kila mtu kwa alitendalo.
105. Tumekuteremshia hii Qur'ani kwa haki na kwa kweli.
Imekusanya kila lilio la haki. Inabainisha haki mpaka Siku ya Kiyama, ili iwe ni
taa yako ya kukupa mwangaza kuwahukumu watu. Basi hukumu baina yao, wala
usiwepiganie walio makhaaini.
106. Na unapo hukumu baina ya watu muelekee Mwenyezi Mungu,
na ukumbuke utukufu wake, na uombe maghfira yake na rehema yake. Kwani
kughufiria na kurehemu ndio shani yake Subhanahu wa Taa'la.
107. Wala usiwatetee wale wanao fanya khiana, na wakaendelea
mno katika kuificha hiyo khiana katika nafsi zao. Kwani Mwenyezi Mungu hampendi
ambaye mtindo wake ni khiana na kufanya madhambi.
108. Wanajificha, na wanataka kujisitiri kwa watu wasiione
khiana yao. Wala hayumkini kuzificha khiana zao kwa Mwenyezi Mungu, na ilhali
Yeye daima yu pamoja nao. Na wao usiku usiku hukubaliana kwa maneno yasiyo
mridhi Mwenyezi Mungu ya kuwasingizia tuhuma watu wasio na makosa. Na Mwenyezi
Mungu Mtukufu anajua vyema, na hapana kitu kinacho weza kujificha na ujuzi wake.
109. Ikiwa nyinyi mnawatetea hao wakosa wasipate adhabu ya
duniani, basi hatopatikana wa kuwatetea Siku ya Kiyama mbele ya Mwenyezi Mungu
na kukubali kuwa ni mlinzi wao wa kuwasaidia.
110. Mlango wa toba, hakika, uwazi. Anaye tenda kitendo
kiovu cho chote, au akajidhulumu nafsi yake kwa kufanya maasi, kisha akamtaka
msamaha Mwenyezi Mungu Mtukufu, atamkuta Mwenyezi Mungu yu tayari kukubali toba
yake, na kumghufiria madhambi yake. Kwani ndio mwendo wake Mwenyezi Mungu
kughufiria na kurehemu.
111. Hakika madhara ya madhambi ni juu ya yule yule
ayatendayo. Mwenye kuchuma madhambi basi anajidhuru mwenyewe. Na alitendalo
linamuangukia mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu Aliye takasika na kutukuka anajua
aliyo yatenda, na atamchukulia kwa mujibu wa hikima yake. Atamuadhibu au
atamsamehe kwa mujibu wa hikima yake.
112. Na mwenye kutenda makosa na madhambi kisha akamsingizia
mwenginewe asiye na kosa alilo litenda - kama vile mwizi kaiba kitu kisha
akamsingizia wizi mtu mwengine - mtu huyo ana dhambi mbili. Moja ni uwongo na
uzushi, na la pili lile kosa lilio wazi la kwiba.
113. Lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufadhili kwa kukuteremshia
Wahyi, Ufunuo, na akakupa rehema ya kutambua na kufahamu hakika, kikundi cha
wapotovu kingependa kukupoteza. Lakini hawapotezi ila nafsi zao. Kwani Mwenyezi
Mungu ni muangalizi wako, na ndiye mwenye kukuonyesha haki. Hayakufikilii
madhara ya mipango yao na upotezi wao. Yeye Mwenyezi Mungu amekuteremshia
Qur'ani Tukufu ambayo hiyo ndiyo mizani ya haki, na ameutuza moyo wako kwa
hikima, na amekufundisha Sharia na hukumu ambazo ulikuwa hukuzijua ila kwa
kufunuliwa na Yeye. Hakika fadhila za Mwenyezi Mungu juu yako daima ni kubwa.
114. Hakika wale wanao kaa wakipanga mambo yao kisirisiri,
mambo hayo hayana kheri, kwa sababu shari ndio huchipuka katika ufichoni.
Lakini ikiwa mazungumzo hayo ni kwa jambo la sadaka ya kuwapa watu, au kufanya
jambo lolote lisio baya, au kupanga mipango ya kusuluhisha baina ya watu, hayo
si mabaya. Kwani hayo ni mambo ya kheri. Na mwenye kufanya hivyo kwa kutafuta
radhi za Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataa'la, basi Mwenyezi Mungu atampa malipo
makubwa duniani na Akhera.
115. Na anaye mpinga Mtume s.a.w. baada ya kwisha itambua
Njia ya Haki na Uwongofu, na akaifuata njia isiyo kuwa ya Waumini, na akaingia
kwenye urafiki na maadui wa Waumini, basi huyo atakuwa na hao. Kwani amekhiari
kuwa hao ndio wawe marafiki zake na walinzi wake. Mwenyezi Mungu atakuja mtia
Motoni Siku ya Kiyama.
116. Hakika mwisho huu wa kuumiza ni wao hao vile vile,
kwani hao ni maadui wa Uislamu. Mfano wake ni mfano wa mwenye kumshirikisha
Mwenyezi Mungu. Hakika kila dhambi yaweza kughufiriwa, ila kumshirikisha
Mwenyezi Mungu, na kumuabudu mwenginewe asiye kuwa Yeye, na kumpinga Mtume
katika Haki. Ni shani ya Mwenyezi Mungu kusamehe madhambi, ila
dhambi ya kumshirikisha Yeye katika ibada. Kwa jenginelo lisilo kuwa hili Yeye
humsamehe amtakaye. Anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu katika ibada na kumtegemea,
basi huyo ameipotea Haki, na amekuwa mbali nayo mno; kwani mtu huyo ameifisidi
akili yake na nafsi yake pia.
117. Katika upotovu ulio wazi kabisa ambao uko mbali
na Haki ni ule wa mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Huyo anaabudu kitu
ambacho hakisikii wala hakioni, hakidhuru wala hakinafiishi. Na huita hiyo
miungu yake kwa majina ya kike, kama Laata na Uzza na Manaata na mengineyo ya
majina ya kike. Yeye hakika kwa hivyo anamuabudu Shetani.
118. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amekwisha mfukuza
huyu Shetani kutokana na kivuli cha rehema yake, na amemjaalia awe katika
njia ya upotovu. Na Shetani ameapa, na amejichukulia ahadi mwenyewe, kuwa
atachota miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu idadi maalumu awapumbaze
kwa upotovu wake na awatie wasiwasi kwa shari yake.
119. Hakika kiapo chake Shetani ni kuwa atawapoteza wale
anao wapumbaza kwa kuwatenga mbali na Haki, na kuchochea pumbao lao na matamanio
yao, mpaka wakawa wamepotea wanatanga tanga katika mawazo na tamaa za uwongo.
Wakisha kuwa katika kuzainiwa huku na tamaa hizo chini ya utawala wake Shetani,
tena huwatokomeza kwenye mambo yasiyo ingia akilini, na huwapelekea hao wafikiri
kufanya hayo ni ibada. Na ilhali haya yote ni mawazo ya uwongo tu. Basi
huwatia wasiwasi wakatenda mambo, kama kwa mfano kuwakata masikio baadhi ya
ngamia wao, wageuze khulka aliyo iumba Mwenyezi Mungu. Wakafanya kuwa ngamia
aliye katwa masikio yake hachinjwi, wala hafanyishwi kazi, wala hazuiliwi kwenda
machungani atakavyo. Yote haya ni kwa amri yake Shetani kuwazaini. Tena huwatia
wasiwasi mpaka wakaona kuwa hayo ni katika dini. Na hakika wao inakuwa
wanamfuata yeye Shetani, na wanamfanya yeye ndiye wa kuwanusuru, na ndiye wa
kumfuata badala ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shetani ndiye
msaidizi wake wa kumfuata, basi amekhasiri khasara kubwa iliyo wazi. Kwani hapo
anakuwa amepotea njia ya Haki, na ameipumbaza akili yake, na utampata ufisadi
duniani, na adhabu Akhera.
120. Shetani huwapambia shari, wakaiona nzuri, na huwaahidi
manufaa watayo pata pindi wakitenda kitendo fulani, na huwatia katika nafsi zao
matumaini ya kuyatumai. Na hapana lolote analo waahidi na analo wapambia ila ni
udanganyifu mtupu.
121. Hakika hao walio zipoteza akili zao na wakafuata
wasiwasi wa Shetani anao watia katika nafsi zao, mwisho wao ni kuendea
Jahannamu, wala hawatapata njia ya kutoka huko.
122. Huu ndio mwisho wa wafuasi wa Shetani. Ama mwisho wa
wafuasi wa Mwenyezi Mungu ni mzuri. Wao ndio walio muamini Mwenyezi Mungu na
Mtume wake, na wakatenda mema, wala hawazugwi na mawazo ya uwongo. Hakika Siku
ya Kiyama Mwenyezi Mungu Mtukufu atawatia katika mabustani yapitayo mito kati
yake, chini ya vivuli. Na hayo ni makubwa mno kuliko bustani hizi za duniani. Na
hayo ni yakini, kwani ahadi hizo ni ahadi za Mwenyezi Mungu, na ahadi zake
haziwi ila ni hakika isiyo geuka, wala haina udanganyifu. Yeye ni mmiliki wa
kila kitu. Wala haiwezi kufikirika kuwa yupo yeyote yule aliye mkweli kwa neno
lake na ahadi yake kuliko Mwenyezi Mungu.
123. Malipo siyo ayatamaniyo mtu na kuyaota bila ya vitendo
vyema vizaavyo matunda. Malipo siyo myatamaniyo nyinyi, Waislamu.
Wala siyo wayatamaniayo na kuyaota Ahlu-l-Kitabi, Watu wa Biblia, Mayahudi na
Wakristo. Bali malipo na kuepukana na adhabu ni kwa Imani na Vitendo Vyema.
Atendaye maovu atalipwa kwa vitendo vyake. Wala hampati mlinzi wala wa kumnusuru
ila Mwenyezi Mungu.
124. Watendao mema, kwa kadiri ya uwezo wao nao wanamuamini
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wataingia kwenye Pepo ya neema, wala
hawatapunguziwa hata chembe. Na hapana khitilafu baina ya malipo ya mwanamume na
ya mwanamke, kwani mwanamke naye ana waajibu wake, malipo ya vitendo vyema, na
adhabu kwa vitendo vibaya.
125. Msingi wa vitendo vyema ni itikadi iliyo sawa. Na
bora ya dini ni kumtakasikia niya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ukawa uso wako, na
akili yako, na nafsi yako, yote haitaki kitu isipo kuwa kumridhi Mwenyezi Mungu
Subhanahu. Kwa hivyo basi ndio fahamu zako zitanyooka sawa kuufahamu ujumbe wa
Mitume, na ndio utaweza kushika daima vitendo vilivyo bora, na ukamfuata Baba wa
Manabii, Ibrahim a.s. Kwani dini yake Ibrahim ndiyo Dini ya Mwenyezi Mungu, na
ndiyo Dini inayo elekeza kutaka Haki daima. Na kwa Ibrahim ndiyo umekutana umoja
wa Dini, kwa Waislamu, na Mayahudi na Wakristo. Basi ifuateni njia yake.
Mwenyezi Mungu hakika amemkirimu Ibrahim, akamwita "Rafiki Mwendani".
126. Hakika wa kumtakasia niya ni Mwenyezi Mungu, na ndio
kwake Yeye inapasa uusilimishe uso wako, yaani umuelekee na umnyenyekee. Huko
ndiko kumsafia niya Mwenyezi Mungu aliye umba ulimwengu wote, na ndiye mwenye
kuumiliki. Vitu vyote viliomo mbinguni na duniani - nyota, sayari, jua, mwezi,
milima, mabonde, majangwa, mashamba n.k. ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye
Mwenye kubainikiwa na kila kitu, Mwenye kujua kwa ujuzi mkamilifu wa kuvizunguka
vitu vyote avitendavyo mwanaadamu. Na Yeye atamlipa kheri akitenda kheri,
na shari akitenda shari.
127. Watu walimtaka Mtume s.a.w. awambie nini hukumu ya
sharia juu ya wanawake. Na wanawake walikuwa, na wangali bado kuwa, ni watu
wanyonge. Basi Mwenyezi Mungu amembainishia Nabii wake ili naye abainishe hali
ya wanawake, na hali ya wanyonge wengine katika ukoo miongoni mwa watoto na
mayatima. Na akataja kuwa mayatima wanawake ambao wanaolewa wala hawachukui
mahari yao, na watoto, na mayatima, wote hao watendewe kwa uadilifu na huruma na
kuraiwa. Na kwamba kila kheri itendwayo basi hakika Mwenyezi Mungu anaijua, na
Yeye ndiye atakaye ilipa.
128. Na mwanamke akikhofia kuwa mumewe anapuuza mambo ya
nyumbani au anayatupa, hayajali, wala hayashughulikii, basi hapana dhambi kwa
wote hao wawili kutafuta njia za kusuluhiana kwa mapatano mema na kukurubiana.
Na mwenye akili kati yao ni yule anaye anza kutaka masikizano. Na suluhu daima
ina kheri, haina shari ndani yake. Linalo zuia masikizano ni kule kuwa kila
mmoja kung'ang'ania haki yake kwa ukamilifu, na ugumu na uchoyo wa nafsi unapo
wamiliki watu. Wala hapana njia ya kurejeza mapenzi ila mmojapo kati ya wawili
kulegeza kamba. Na huyo ndiye mwema, mchamngu, mwenye kujihifadhi na dhulma. Na
mwenye kutenda vitendo vyema na akamcha Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu
anayo khabari ya vitendo vyake, na atamlipa kwavyo.
129. Kuwafanyia uadilifu wake kwa mapenzi ya daima yasiyo
chafuliwa na udanganyifu, na kutendeana usawa katika mapenzi ikawa nipe
nikupe, ni jambo lisilo wezekana kuwa. Kadhaalika haiwezi
kuwepo usawa katika kuwapenda wake, ikiwa kuna zaidi kuliko mke mmoja. Walakini
mkijitahidi, basi msimfanyie ujeuri mmoja wapo, mkamili upande mmoja, na
mkamwacha mwengine si mke si mt'alaka. Yapasa mjitengeneze, na muendeshe nyumba
zenu kwa wema si kwa ufisadi. Na mcheni Mwenyezi Mungu apate kughufirieni na
akurehemuni. Ni shani yake kughufiria na kurehemu.
130. Ikiwa suluhu haikumkinika na ikawa chuki (au
karaha) imeshika nguvu zaidi, basi inalazimika kufarikiana. Na
wakifarikiana Mwenyezi Mungu atawatosheleza kila mmoja wao kutokana
na ukunjufu wa rehema yake na fadhila yake. Na riziki ziko katika mikono
ya Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye Mwenye hikima, na hupanga mambo yote kwa
mipango yake.
131. Kiini cha Dini ni kumnyenyekea Mwenye
kuumba ulimwengu, Mwenye utukufu na ukarimu, na kuukubali
ufalme wake usio na ukomo. Kwani ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo
mbinguni na katika ardhi. Na kwa
huu Ufalme usio na ukomo amesema: Tumewausia watu wa dini zilizo
toka mbinguni, katika Watu wa Kitabu na nyinyi Waislamu,
mumkhofu Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na msiwe mnakufuru
katika ibada yake, maana Yeye ndiye Mwenye utawala mkubwa kushinda wote. Hapana
kitu kilicho toka nje ya utawala wake. Yeye ni Mkwasi, yaani mwenye kujitosha
wala hakuhitajiini nyinyi. Juu ya hivyo Yeye anakuhimidini kwa imani yenu, kwani
kwa kuwa Yeye ni Mwenye kujitosheleza mwenyewe, juu ya hivyo anasifu na
kushukuru vitendo vyema vya waja wake.
132. Kupanga kila kitu cha mbinguni na duniani ni kazi ya
Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Aliye tukuka. Yeye ndiye Mwenye madaraka,
Mwenye kuendesha, Mwenye kupanga. Yatosha kuwa Yeye ndiye Mtawala aliye amrisha
ulimwengu ukajipanga ulivyo jipanga, na akawaamrisha watu wamuabudu, na
wamtegemezee Yeye mambo yao, na wamche Yeye.
133. Hakika nyinyi enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Mko chini ya
ufalme wa Mwenyezi Mungu Mwenye uweza na Mwenye nguvu. Akipenda
atakufisheni na alete wengine kabisa. Na Yeye Mwingi wa Utukufu ni
Muweza wa hayo, na Muweza wa kila kitu.
134. Na watu, pindi wakitafuta neema za dunia zilizo halali
kwa njia ya haki iliyo nyooka sawa, basi hakika Mwenyezi Mungu atawapa neema za
duniani na Akhera; kwani Yeye ndiye aliye miliki neema zote mbili.
135. Uadilifu ndio nidhamu ya maumbile. Na hiyo ndiyo sharia
ambayo haiwezi kuwapo ndani yake maoni ya kukhitalifiana. Basi enyi mlio mt'ii
Mwenyezi Mungu wa Haki, na wito wa Mitume wake, kuweni macho nafsi zenu katika
kuut'ii uadilifu, na kuweni macho kwa ajili ya watu. Mfanyieni insafu aliye
dhulumiwa, na msimame imara, si kwa ajili ya kumpendelea tajiri, au kumwonea
huruma masikini. Kwani Mwenyezi Mungu aliye waumba matajiri na masikini
anastahiki zaidi kuangalia hali ya tajiri au fakiri. Matamanio ndiyo yanayo
mpelekea mtu kumili nafsi yake, basi msiyafuate matamanio mkaacha uadilifu. Na
mkikengeuka mkaacha uadilifu, au mkapuuza kusimamisha uadilifu, basi mjue
Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo, tena anayajua kwa ujuzi wa ndani. Naye
atakulipeni kwa mujibu wa a'mali yenu; ikiwa njema mtalipwa wema, ikiwa ovu
mtalipwa shari.
136. Kwa hakika Ujumbe wa mbinguni ni mmoja, kwa kuwa yule
Mwenye kutuma ni Mmoja, naye ni Mwenyezi Mungu. Basi enyi mlio amini! Mt'iini
Mwenyezi Mungu na mumsafie niya. Na msadikini Mtume wake Muhammad, na msadiki
yaliyo kuja katika Kitabu chake alicho mteremshia, na mtende yaliyo amrishwa
humo. Na sadikini Vitabu vilivyo teremshwa kabla yake kama alivyo teremsha
Mwenyezi Mungu bila ya mageuzo wala kusahau. Aminini yote hayo. Kwani mwenye
kumkanusha Mwenyezi Mungu, Muumba wa viumbe vyote, na Malaika, na Mwenye kuyajua
yaliyo fichikana, na Vitabu vya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na akaikanusha
Siku ya Mwisho, basi huyo ameipotea Njia Iliyo Nyooka, na ametokomea mbali
katika njia ya upotovu.
137. Hakika Imani ni kuit'ii Haki kusio kuwa na ukomo, na
kunako endelea daima. Basi wanao taradadi wakababaika si Waumini. Hao ambao
wanaamini, kisha wakakufuru, kisha wakaamini, kisha wakakufuru, na kwa hivyo
wakazidi ukafiri wao - Mwenyezi Mungu hatakuwa wa kuwaghufiria watu hao hivyo
vitendo vyao viovu, wala hatawaongoa kwenye Haki. Kwani kusamehe kwa Mwenyezi
Mungu kunahitajia toba, na kujing'oa na shari, na uwongofu wake ni kwa wale
wanao ielekea Haki na wanaitaka.
138. Ewe Mtume Mtukufu! Waonye wanaafiki kwamba Siku ya
Kiyama watapata adhabu chungu yenye kuumiza.
139. Hao wanaafiki huufanya utawala wa makafiri uwe juu yao,
na wanawawacha Waumini. Basi hebu hivyo wanataka wapate utukufu kwa hawa
makafiri? Hakika utukufu uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye huwapa waja wake
wenye kuamini. Na mwenye kutaka utukufu kwa Mwenyezi Mungu atatukuka, na mwenye
kutaka utukufu kwa mwenginewe atadhalilika.
140. Mwenyezi Mungu amekwisha kuteremshieni katika Qur'ani
Tukufu kwamba kila mkisikia Aya za Kitabu nyinyi mnaamini, na makafiri wanapinga
na wanakejeli. Na ikiwa hivyo ndiyo hali ya makafiri na wanaafiki, na mkasikia
kejeli zao, basi msikae nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine waache
dhihaki zao. Na nyinyi ikiwa hamtofanya hivyo, mkawa mnasikiliza kejeli zao,
basi mtakuwa nanyi kama wao katika kuifanyia maskhara Qur'ani. Mwisho wa
makafiri na wanaafiki ni muovu mno, kwani Mwenyezi Mungu atawakusanya wote hao
katika Moto wa Siku ya Kiyama.
141. Mtindo wa wanaafiki ni kukungojeeni kama
anavyo ngojea mwenye husda na maya anaye tamani mpate masaibu mnapo kuwa katika
vita na maadui. Mkishinda kwa nusra ya Mwenyezi Mungu, na mkafungukiwa njia ya
Haki, wao huwaambia Waumini - na hali wao ule ushindi walio pewa wenye Imani na
Mwenyezi Mungu umewashtusha : Sisi hatukuwa nanyi? Kwa maana sisi ni jamaa
zenu! Na ikiwa ni zamu ya makafiri kupata ushindi, basi wao huwaendea na
kuwaambia: Sisi hatukuyashughulikia mambo yenu hata yakawa ni yetu? Na
hatukukupeni mapenzi yetu, na tukakulindeni na hawa Waumini? (yaani sisi ni
wenzenu). Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la atakuhukumuni baina yenu na hawa
wanaafiki Siku ya Kiyama. Wala Mwenyezi Mungu hatowapa makafiri njia kuwashinda
Waumini maadamu Waumini watashikamana na sifa ya Imani ya kweli na vitendo
vyema.
142. Hakika wanaafiki, kwa ule
unaafiki wao, wanadhani kuwa wanamkhadaa Mwenyezi Mungu Mtukufu na
wanamficha hakika ya nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Yeye ndiye
anaye wakhadaa wao. Basi Yeye huwapururia kuwapa muhula, na anawawacha mpaka
wabobee katika maovu yao, kisha ndio awahisabu kwa waliyo yatenda. Na hawa
wanaafiki wana dhaahiri ya kuonekana, na ya ndani ya nafsi zao. Yale ya
kuonekana ni vile kuwa wakiinuka kwenda kusali huinuka kwa uvivu, kwa
unyong'onyo. Na sala yao ni riya tu, kuonyesha, si ya kweli. Na ya ndani ni kuwa
hawakumbuki kumtaja Mwenyezi Mungu ila kwa nadra, kwa tukizi. Na lau kuwa
wanamkumbuka vilivyo wangeli uacha unaafiki
143. Na hawa wanaafiki ni watu wanao taradadi, wanababaika.
Kwenu hawapo, na kwao makafiri hawapo katika kila hali. Na hayo ni kwa
sababu ya udhaifu wa imani, na udhaifu wa nafsi, na kwa sababu ya kupotoka na
Haki. Na mwenye kuandikiwa kupotoka na Mwenyezi Mungu tangu hapo azali, basi
huna njia wewe ya kumwongoa sawa.
144. Hakika katika sababu za unaafiki ni kuwa wanaafiki
wamewafanya watu wasio kuwa Waumini kuwa ndio walinzi wao, marafiki zao,
watawala wao, na ndio wa kuwanusuru. Enyi Waumini! Yaacheni haya, muepukane
nayo. Wala msiwafanye makafiri ndio wa kukunusuruni, wakukutawalini,
mkawanyenyekea. Na hapana shaka yoyote mkifanya hivyo mnampa Mwenyezi Mungu hoja
iliyo wazi ya kukuhojini. Mtakuja ingia pamoja na wanaafiki, na mtadhalilika.
Kwani inakuwa hamfanyi utukufu wenu utoke kwa Mwenyezi Mungu, na kwa haki, na
vitendo vyema.
145. Hakika wanaafiki kwa sababu ya unaafiki wao watakuwa
katika vina vya Jahannamu. Wao wako chini kabisa huko, na daraja ya mwisho
kabisa. Wala hutompata wa kuwanusuru, wa kuwatetea na adhabu hiyo.
146. Isipo kuwa wale katika wao walio tubia, na wakarejea
kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na wakaungana naye Yeye peke yake, na wakajitakasa,
na wakaelekeza nyuso zao kwake, na wakatenda mema. Wakifanya haya basi ndio
wanakuwa miongoni mwa Waumini. Watapata malipo ya Waumini. Na Mwenyezi Mungu
Mtukufu amekwisha waahidi Waumini malipo makubwa duniani na Akhera.
147. Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hana alitakalo kwenu ila
mumuamini Yeye, na muishukuru neema yake. Mkiwa hivyo basi hampati adhabu, bali
mtapata malipo ya kheri na shukrani. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni
Mwenye kushukuria waja wake kwa vitendo vyema, na ni Mjuzi, anajua hali zao zote
njema na mbaya.
148. Mwenyezi Mungu anawakataza waja wake wasiseme maneno
maovu, ila yule aliye patwa na dhulma. Ni halali kwake kumshitaki aliye
mdhulumu, na autaje uovu aliyo tendewa. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mwenye
kusikia vyema maneno ya aliye dhulumiwa. Na ni Mjuzi wa dhulma ya mwenye
kudhulumu. Na atamlipa kwa kitendo chake hicho.
149. Mkiyadhihirisha mema myatendayo, au mkayaficha, au
mkamsamehe anaye kufanyieni uovu, Mwenyezi Mungu atakulipeni kwa kufuata khulka
yake Mtukufu, ya kusamehe na hali ana uwezo kaamili. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu
ni mwingi mno wa kusamehe, Mwenye kukamilika uwezo wake.
150. Hakika wasio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na
wanao taka kufanya ubaguzi katika imani ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na
wanasema: Tunawaamini baadhi ya Mitume, sio wote, hao wanawaamini wawapendao na
wanawakataa wasio wapenda. Na lilio waajibu ni kuwaamini wote, kwani Imani
haikubali kukatwa mapande mapande.
151. Hawa wote ndio walio ungama ukafiri wao ulio wazi. Na
Mwenyezi Mungu amekwisha waahidi wao na mifano ya hao adhabu kali yenye
kudhalilisha.
152. Na ama wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake,
wala hawakumkanusha hata mmoja wapo kati yao, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu
atawalipa malipo makubwa kwa ajili ya Imani yao iliyo kamilika. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwingi wa maghfira kwa wenye kutubu, na ni Mwenye kuwarehemu waja wake.
153. Ewe Mtume! Watu wa Kitabu, yaani Mayahudi
wapendao kuudhi, wanakutaka ulete dalili ya ukweli wa unabii wako. Uwaletee
kitabu makhsusi kiwateremkie kutoka mbinguni kithibitishe ukweli wa utume wako,
na kiwatake wakuamini na kukut'ii! Ukiyaona makuu hayo wayatakayo, wewe usifanye
haraka. Kwani wenzao walio tangulia walifanya kero vile vile, wakamtaka Musa
makubwa kuliko hayo. Walimwambia: Tuonyeshe Mwenyezi Mungu tumwone kwa macho.
Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa lile kero lao na dhulma yao kwa kuwapiga radi
iliyo wateketeza!! Kisha watajie hawa watu kosa kubwa zaidi na ovu zaidi,
nalo ni pale walipo mfanya ndama kuwa ni mungu wao, wakamwacha Mwenyezi Mungu
aliye waumba. Haya baada ya kwisha ona dalili zote alizo zionyesha Musa kwa
Firauni na kaumu yake!! Kisha juu ya hayo Mwenyezi Mungu akawakunjulia usamehevu
wake kwao, na Mwenyezi Mungu akampa nguvu Musa kwa hoja zilio wazi, na neno
madhubuti.
154. Mwenyezi Mungu akaunyanyua mlima juu ya Wana wa Israili
ili kuwatisha kwa kule kuikataa kwao sharia ya Taurati, mpaka wakaikubali.
Akachukua kwao agano, na akawaamrisha waingie mjini hali wakimnyenyekea Mwenyezi
Mungu. Wala wasiyakiuke aliyo waamrisha kushika ibada katika siku ya Sabato,
yaani Jumaamosi.(Imeitwa "Sabt" Kiarabu, "Shabbath" Kiyahudi, "Sabbath"
Kiingereza, na "Sabato" Kiswahili, maana yake "Mapumziko" kwa kuwa ni siku ya
mapumziko kwa Mayahudi.) Na Mwenyezi Mungu alichukua kwao ahadi ya nguvu.
155. Mwenyezi Mungu akawakasirikia kwa sababu ya kuvunja
agano hili, na kuzikataa ishara za Mwenyezi Mungu, na kwa kuwauwa Manabii kwa
dhulma, na kuendelea katika upotovu wao kwa kusema: Nyoyo zetu zimefungwa
hazikubali hayo unayo tuitia! Nao hawasemi kweli katika kauli yao hiyo, bali
Mwenyezi Mungu amezifuta nyoyo zao kwa ukafiri wao, basi ni wachache tu kati yao
wanao amini.
156. Na Mwenyezi Mungu
amewaghadhibikia Mayahudi kwa sababu ya kufru yao na
kumzulia Maryam uzushi mkubwa.
157. Na Mwenyezi Mungu pia amewaghadhibikia kwa
kusema kwao uwongo: Hakika sisi tumemuuwa Masihi Isa bin Maryamu, Mtume wa
Mwenyezi Mungu. Na kweli ya yakini ni kuwa hawakumuuwa kama wanavyo zua.
Wala hawakumsalibu kama wanavyo dai. Lakini walifananishiwa, nao wakadhani kuwa
wamemuuwa na wamemsalibu. Na hakika walimuuwa na kumsalibu aliye shabihiana
naye. Nao wakaja kukhitalifiana baada ya hayo, kuwa aliyeuwawa ni Isa au mtu
mwengine? Na wote hao, kwa hakika, wamo katika shaka tu juu ya jambo hilo. Kweli
iliyopo ni kuwa hawana ujuzi nayo mambo haya, ila ni dhana dhana tu. Kabisa
hawakumuuwa Isa. (Wataalamu wa Biblia mpaka hii leo wamo kuzozana katika jambo
hili. Mwenye kuzichungua Injili zinazo kubaliwa na Wakristo ataona kuwa hazina
uthibitisho kuwa aliye salibiwa ndiye Yesu, au hata huyo naye alikufa msalabani
au la.)
158. Bali Mwenyezi Mungu alimtukuza kwake, akamwokoa na
maadui zake, wasimsalibu na wasimuuwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda,
hashindiki, ni Mwenye hikima katika vitendo vyake. (Taaurati inayo kubaliwa na
Mayahudi na Wakristo imesema kuwa anaye kufa kwa kutundikwa msalabani
amelaaniwa. Ndio maana Mayahudi wakawa na hamu wamtundike Nabii Isa ili
wathibitishe kuwa huyo si chochote ila ni mlaanifu. Je, Mwenyezi Mungu Mtukufu
vipi aachilie jambo hilo liwe kwa Mtume wake?)
159. Na hapana mmojapo katika Watu wa Kitabu (Mayahudi na
Wakristo) ila atakuja tambua uhakika wa Isa (kuwa ni Nabii wa kweli wa Mwenyezi
Mungu, si mwana haramu, wala si mwana wa Mungu) kabla ya kufa kwake, na kuwa
yeye Isa ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na atakuja amini imani
ambayo haitomfaa kitu, kwa kuwa wakati wake umekwisha pita. Na Siku ya Kiyama
Isa atatoa ushahidi juu yao kuwa yeye alifikisha ujumbe, na kuwa yeye ni mtumwa
wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
160. Kwa sababu ya udhalimu wao Mayahudi Mwenyezi Mungu
amewapa adabu - amewakataza vyakula mbali mbali vilivyo vizuri, vimekuwa kwao
haramu, na ilhali kwanza vilikuwa halali kwao. Na kwa udhalimu wao wamewazuia
watu wengi wasiingie katika Dini ya Mwenyezi Mungu.
161. Na kwa sababu ya kupenda kula riba - na Mwenyezi Mungu
alikwisha wakataza hayo - na kuchukua mali ya watu kwa njia isiyo ya haki, ndio
ikawa adabu ya dini ni kuwazuilia na kula vyakula vilivyo vizuri. Na Mwenyezi
Mungu amewawekea hao walio kufuru adhabu yenye kutia machungu.
162. Lakini walio bobea katika ilimu, yaani wataalamu kweli
kweli, miongoni mwa Mayahudi, na Waumini katika umma wako, ewe Nabii, wanasadiki
wahyi ulio funuliwa wewe, na walio letewa Mitume wa kabla yako. Na wanao shika
Sala baraabara, na wanatoa Zaka, na wanamuamini Mwenyezi Mungu na kufufuliwa na
hisabu, hao Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mema kabisa kwa imani yao na ut'iifu
wao.
163. Hakika Sisi tumekufunulia wewe, ewe Nabii!
(tumekuteremshia Wahyi), Qur'ani na Sharia, kama tulivyo wafunulia kabla yako
Nuhu na Manabii wa baada yake, na kama tulivyo wapa Wahyi Ibrahim, na Ismail, na
Is-haq, na Yaakub, na wajukuu zake, nao wale walio kuwa Manabii wa Mwenyezi
Mungu miongoni mwa dhuriya (wazao) wa Yaakub, na Isa, na Ayubu, na Yunus, na
Haarun, na Suleiman, na kama tulivyo mfunulia Daud tukamteremshia Kitabu cha
Zabur.
164. Kadhaalika tumewatuma Mitume wengi ambao tumekwisha
taja khabari zao kabla yake. Na Mitume wengine hatukukusimulia hadithi zao. Na
njia ya kumpa Wahyi Musa ilikuwa Mwenyezi Mungu akisema naye moja kwa moja nyuma
ya pazia, lakini bila ya kuwepo mwengine kati.
165. Tuliwapeleka Mitume hao kuwapa bishara njema ya thawabu
wenye kuamini, na kuwaonya adhabu wale walio kufuru, ili watu wasiwe na hoja ya
kumtafutia kisababu Mwenyezi Mungu baada ya kwisha wapeleka Mitume. Na Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu, ni Mshindi, wala hana yeyote madaraka pamoja naye,
na ni Mwenye hikima kwa atendayo.
166. Lakini ikiwa hao watu hawashuhudii kukusadikisha, basi
Mwenyezi Mungu Mwenyewe anashuhudia kuwa aliyo kuteremshia ni sahihi. Hakika
Yeye amekuteremshia hayo kwa hikima, na kwa mujibu wa ujuzi wake. Na Malaika nao
wanashuhudia hayo kadhaalika. Na ewe Mtume! Yakutosha wewe ushahidi wa Mwenyezi
Mungu, kuliko ushahidi wowote mwenginewe.
167. Hakika wale ambao wamekufuru wasikusadiki wewe, na
wakawazuia watu wasiingie katika Dini ya Mwenyezi Mungu, bila ya shaka wamekuwa
mbali mno na Haki.
168. Wale walio kufuru, na wakajidhulumu nafsi zao, na
wakamdhulumu Mtume kwa kuupinga ujumbe wake, na wakawadhulumu watu walipo
wafichia Haki, Mwenyezi Mungu hatowasamehe kamwe maadamu watabaki katika ukafiri
wao. Wala hatawapa uwongofu wa kuijua njia ya kuvuka. Sio mtindo wake Subhanahu
kuwasamehe watu kama hao nao wangali kubaki katika upotovu wao.
169. Lakini atawapeleka kwenye njia ya Motoni, na humo
wabakie daima dawamu. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jambo jepesi.
170. Enyi watu! Amekwisha kukujieni Mtume huyu, Muhammad, na
Dini ya Haki kutokana na Mola Mlezi wenu. Basi yaaminini aliyo kuja nayo; ndiyo
itakuwa kheri yenu. Na pindi mkikataa ila kukufuru tu, basi mjue kwamba Mwenyezi
Mungu ni Mkwasi na imani yenu, hana haja nayo. Yeye ndiye Mwenye kukumilikini
nyinyi. Kwani vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi ni vyake Yeye, kwa
kuvimiliki, kuviumba na kuviendesha atakavyo. Naye ni Mwenye kuvijua vyema
viumbe vyake, ni Mwenye hikima katika uendeshaji wake. Haupotezi ujira wa mwema,
wala hapuuzi kumlipa mwovu.
171. Enyi Watu wa Kitabu!
Msipindukie haki, mkazidisha kupita kiasi katika dini yenu, wala msimzulie
uwongo Mwenyezi Mungu, mkaukanya utume wa Isa, au mkamfanya kuwa ni Mungu pamoja
na Mwenyezi Mungu. Kwani Masihi ni Mtume kama walivyo Mitume wengine. Mwenyezi
Mungu amemuumba kwa uwezo wake na neno lake alilo mbashiria kwalo,
na Jibrili akampulizia Maryamu roho ya Mwenyezi Mungu. Hii ni siri katika siri
za uwezo wake Mwenyezi Mungu. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake wote
imani ya kweli. Wala msidai kuwa katika Ungu kuna Utatu!! Tokeni katika
upotovu huu, itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu, wala
hana mshirika wake. Naye ametakasika na kuwa na mwana! Na kila kilioko katika
mbingu na ardhi ni chake. Na Yeye Mwenyewe anajitosha peke yake kuwa ni
Mwendeshaji wa Ufalme wake. (Kuitwa Nabii Isa Neno au Roho iliyo toka kwa Mungu,
hakumpi Ungu. Yeye ni neno kwa kuumbwa kwa amri ya "Kun", "Kuwa" akawa. Haya ni
kuwapinga Mayahudi walio dai kuwa yeye ni mwanaharamu. Basi wanaambiwa kuwa
ameumbwa kama vilivyo umbwa vitu vyote, kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Naye ni Roho
iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu kama walivyo pewa Waumini wote (58.22) na alivyo
puliziwa Adam (15.29) na kwa hivyo wanaadamu wote (32.7-9). Hapana hata pahala
pamoja katika Injili ziliomo katika Biblia ambapo Yesu (Nabii Isa a.s.) alijiita
mwenyewe Mwana wa Mungu. Kila mara akijiita Mwana wa Adamu. Na alipo mwita Mungu
Baba, alikusudia ni Baba wa watu wote, kama alipo sema: "Ninapaa kwenda kwa Baba
yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu." Injili ya Yohana
10.33-36.)
172. Masihi hakujiona bora hata akatae kuwa ni mtumwa wa
Mwenyezi Mungu, wala hawakujiona bora Malaika walio karibishwa. Na mwenye
kutakabari na kujiona mtu wa juu hataweza kuikimbia adhabu ya Mwenyezi
Mungu Siku atakayo wakusanya watu kwa ajili ya hisabu.
173. Ama walio amini wakatenda mema atawalipa thawabu za
vitendo vyao, na atawazidishia kwa fadhila yake, kwa kuwakirimu na kuwaneemesha.
Na ama wale walio kataa kumuabudu, na wakajiona bora wasimshukuru, hao
amewaandalia adhabu yenye machungu makali. Hapana msaidizi wa kuwakinga nayo
wala wa kuwanusuru.
174. Enyi watu wote! Zimekwisha kujieni dalili zilizo wazi
za ukweli wa Mtume Muhammad. Na tumekuteremshieni kwa ulimi wake Qur'ani iliyo
wazi kama mwangaza, unao angaza Njia, na inayo kuongozeni kwendea mafanikio.
175. Ama walio msadiki Mwenyezi Mungu na ujumbe wake alio
leta, na wakaifuata Dini yake, atawatia katika Bustani zake Akhera, na
atawamiminia rehema yake, na atawakusanya katika ukunjufu wa fadhila yake, na
atawawezesha hapa duniani kuthibiti katika Njia yake Iliyo Nyooka.
176. Ewe Nabii! Wanakuuliza vipi atarithiwa aliye kufa naye
akawa hana mwana, wala mzazi. Sema: Hakika hukumu ya Mwenyezi Mungu katika
urithi wa hawa ni kuwa, akiwa maiti ana ndugu wa kike basi atapata nusu ya
tirka. Na akiwa maiti ni mwanamke naye ana ndugu wa kiume basi atarithi mali
yote. Na ikiwa ameacha ndugu wawili wa kike, basi watapata hao thuluthi mbili
(1) ya urithi. Na ikiwa hao ndugu ni mchanganyiko wanaume na wanawake, basi
fungu la mwanamume ni sawa na mafungu mawili ya wanawake. Mwenyezi Mungu
anakubainishieni haya msije mkapotea katika kugawa mafungu ya urithi. Na
Mwenyezi Mungu ni Mkamilifu wa ujuzi wa a'mali zenu na vitendo vyenu vyote. Na
atakulipeni kwavyo. (Angalia: Urithi wa ndugu katika Aya hii ni wa ndugu
khalisa, yaani ndugu kwa baba na mama, au ndugu kwa baba. Ama urithi wa ndugu
kwa mama tu umekwisha tajwa katika Aya 12 ya Sura hii ya Annisaa.)
(1) Na Sunna (Mafunzo ya Mtume)
imebainisha kuwa wakizidi kuliko ndugu wa kike wawili, pamoja na Aya ya mirathi
iliyo tajwa, kuwa wakizidi kuliko binti wawili, watachukua thuluthi mbili. Ni
bora kuwa zaidi kuliko ndugu wawili wa kike, kwa sababu mabinti ni karibu zaidi
kwa maiti.
Tuzingatie kuwa
kwa mujibu wa kanuni za Kizungu za kurithi, ambazo zimetokana na kanuni ya
Kirumi, ndugu wanaume wala wa kike wala watoto wao hawarithi. Na juu ya hivyo
mwenye mali anayo ruhusa kumkata yeyote asipate urithi wake. Uislamu umekataza
haya. Warithi lazima wapate urithi wao, ila mtu anayo haki ya kuandika wasia
kujihukumia kisicho zidi thuluthi moja ya mali yake.(W.H. Ingrams katika kitabu
chake Zanzibar Its History and Its People ameandika: "Hakika Sharia Takatifu
yaonekana kuwa ni ya haki zaidi sana kuliko hata mpango wa Kiingereza wa
kugawanya mali. Katika Zanzibar [na bila ya shaka katika Waislamu wote] hapana
mwendo wa kuwa mtu "kukatwa urithi akabakishwa na shilingi moja tu"; vyo vyote
vile, ni sehemu ndogo tu ndiyo inaweza kuandikiwa wasia, na yaliyo baki lazima
yagawiwe kwa warithi kwa mujibu wa kiwango maalumu.")