Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

0. KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE
KUREHEMU; 0

1. Alif Lam Ra. (A.L.R.) Hichi ni Kitabu tulicho
kiteremsha kwako ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye muwangaza, kwa
idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa, 1

2. Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye vyote
viliomo katika mbingu na ardhi. Na ole wao makafiri kwa adhabu kali! 2

3. Wale wanao fadhilisha maisha ya dunia kuliko Akhera,
na wanawazuilia watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotosha.
Hao wamepotelea mbali. 3

4. Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa kaumu yake ili
apate kuwabainishia. Basi Mwenyezi Mungu humuacha akapotea amtakaye, na
akamwongoa amtakaye. Naye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima. 4

5. Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu,
tukamwambia: Watoe watu wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na
uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila
mwenye kusubiri akashukuru. 5

6. Na Musa alipo waambia watu wake: Kumbukeni neema ya
Mwenyezi Mungu aliyo kujaalieni, pale alipo kuokoeni kutokana na watu wa Firauni
walio kupeni adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja wenenu wanaume, na wakiwawacha
hai wanawake. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unao toka kwa Mola wenu
Mlezi. 6

7. Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru
nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali. 7

8. Na Musa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote waliomo
duniani, hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Anajitosha, Msifiwa. 8

9. Je! Hazikukufikieni khabari za walio kabla yenu?
Kaumu ya Nuhu, na A'adi, na Thamud, na walio baada yao, ambao hapana awajuaye
ila Mwenyezi Mungu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao
wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakataa
hayo mliyo tumwa, na hakika sisi tuna shaka kubwa na mnayo tuitia. 9

10. Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi
Mungu, Muumba mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu,
na akupeni muhula mpaka muda ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni
wanaadamu kama sisi. Mnataka kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu. Basi
tuleteeni hoja ilio wazi. 10

11. Mitume wao wakawaambia: Sisi kweli si chochote ila
ni wanaadamu kama nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu humfanyia hisani amtakaye katika
waja wake. Wala sisi hatuwezi kuleta uthibitisho ila kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu ndio wategemee Waumini. 11

12. Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na
hali Yeye ametuongoa kwenye Njia zetu. Na hapana shaka sisi tutayavumilia hayo
maudhi mnayo tuudhi. Na juu ya Mwenyezi Mungu wategemee wanao tegemea. 12

13. Na walio kufuru wakawaambia Mitume wao: Tutakutoeni
katika nchi yetu, au mrudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea
wahyi: Hakika tutawaangamiza walio dhulumu. 13

14. Na tutakuwekeni katika ardhi baada yao. Haya ni kwa
anaye ogopa kusimamishwa mbele yangu, na akaogopa maonyo yangu. 14

15. Na wakaomba ushindi, na akashindwa kila jabari
mkaidi. 15

16. Ambaye nyuma yake ipo Jahannamu, na atanywishwa maji
ya usaha. 16

17. Awe anayagugumia, wala hawezi kuyameza. Na mauti
yawe yanamjia kutoka kila upande, naye wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu
nyengine kali vile vile. 17

18. Mfano wa walio mkufuru Mola wao Mlezi - vitendo vyao
ni kama jivu linalo peperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya mdharba.
Hawawezi kupata chochote katika waliyo yafanya. Huko ndiko kupotelea mbali. 18

19. Huoni kuwa Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi
kwa Haki? Akitaka atakuondoeni na alete viumbe wapya! 19

20. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu si jambo gumu. 20

21. Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu.
Wanyonge watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu
hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi
Mungu angeli tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu
tukipapatika au tukisubiri; hatuna pa kukimbilia. 21

22. Na Shet'ani atasema itapo katwa hukumu: Hakika
Mwenyezi Mungu alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini
sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi
mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa
mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa
tangu zamani kunishirikisha na Mwenyezi Mungu. Hakika madhaalimu watakuwa na
adhabu chungu. 22

23. Na walio amini na wakatenda mema wataingizwa katika
Mabustani yapitayo mito kati yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi.
Maamkio yao humo yatakuwa: Salaam. 23

24. Hebu hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyo piga mfano
wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako
mbinguni. 24

25. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola
wake Mlezi. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka. 25

26. Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, ulio
ng'olewa juu ya ardhi. Hauna imara. 26

27. Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli
ya imara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha
kupotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo. 27

28. Hebu hukuwaona wale walio badilisha neema ya
Mwenyezi Mungu kwa kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya
maangamizo? 28

29. Nayo ni Jahannamu! Maovu yaliyoje makaazi hayo! 29

30. Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze
watu kwenye Njia yake. Sema: Stareheni! Kwani marejeo yenu ni Motoni! 30

31. Waambie waja wangu walio amini, washike Sala, na
watoe katika tulivyo waruzuku, kwa siri na dhaahiri, kabla haijafika Siku isiyo
kuwa na biashara wala urafiki. 31

32. Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi,
na akateremsha maji kutoka mbinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki
yenu. Na akafanya yakutumikieni majahazi yanayo pita baharini kwa amri yake, na
akaifanya mito ikutumikieni. 32

33. Na akalifanya jua na mwezi kwa manufaa yenu daima
dawamu, na akaufanya usiku na mchana kwa manufaa yenu. 33

34. Na akakupeni kila mlicho muomba. Na mkihisabu neema
za Mwenyezi Mungu hamwezi kuzidhibiti. Hakika mwanaadamu ni dhaalimu mkubwa,
mwenye kuzikufuru neema. 34

35. Na Ibrahim alipo sema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ujaalie
mji huu uwe wa amani, na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu. 35

36. Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hayo yamewapoteza watu
wengi. Basi aliye nifuata mimi huyo ni wangu, na aliye niasi, hakika Wewe ni
Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. 36

37. Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya
dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu,
ewe Mola wetu Mlezi, ili washike Sala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee
kwao, na waruzuku matunda, ili wapata kushukuru. 37

38. Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe unajua tunayo
yaficha na tunayo yatangaza. Na hapana kitu kinacho fichikana kwa Mwenyezi Mungu
katika ardhi wala katika mbingu. 38

39.
Alhamdulillahi! Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu
aliye nipa juu ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye
kusikia maombi. 39

40. Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala,
na katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu. 40

41. Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote
wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu. 41

42. Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayo
yafanya madhaalimu. Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku yatapo kodoka macho
yao. 42

43. Nao wako mbioni, vichwa juu, na macho hayapepesi, na
nyoyo zao tupu. 43

44. Na waonye watu siku itapo wajia adhabu, na walio
dhulumu waseme: Ewe Mola wetu Mlezi! Tuakhirishe muda kidogo tuitikie wito wako
na tuwafuate Mitume. Kwani nyinyi si mliapa zamani kwamba hamtaondokewa? 44

45. Na mkakaa katika maskani zile zile za walio
zidhulumu nafsi zao. Na ikakudhihirikieni jinsi tulivyo watendea. Nasi
tukakupigieni mifano mingi. 45

46. Na kwa hakika walifanya vitimbi vyao, na vitimbi
vyao anavijua Mwenyezi Mungu. Wala vitimbi vyao si vya kuondosha milima. 46

47. Basi usimdhanie Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye
kuwavunjia ahadi yake Mitume wake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda, na
ni Mwenye kulipiza. 47

48. Siku itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine, na
mbingu pia. Nao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwenye nguvu. 48

49. Na utaona wakhalifu siku hiyo wamefungwa katika
minyororo; 49

50. Nguo zao zitakuwa za lami, na Moto utazigubika nyuso
zao. 50

51. Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyo
yachuma. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu. 51

52. Hili ni Tangazo liwafikie watu, liwaonye, na wapate
kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili. 52
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani