Tarjuma ya Quran Tukufu kwa
kiswahili

KWA JINA
LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake
zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilicho toka kwa Mwenye Hikima na Mwenye
Khabari, 1

2. Ili msimuabudu isipo kuwa Allah, Mwenyezi Mungu.
Hakika mimi kwenu ni mwonyaji na mbashiri nitokae kwake. 2

3. Na ili mumwombe msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie
kwake. Atakustarehesheni starehe nzuri mpaka muda maalumu. Na atampa kila mwenye
fadhila, fadhila yake. Na ikiwa mtakengeuka basi mimi nakukhofieni adhabu ya
hiyo Siku Kubwa. 3

4. Marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu tu. Naye ni Muweza
wa kila kitu. 4

5. Hebu angalia! Ati wanafunika vilivyomo vifuani mwao
ili wamfiche Mwenyezi Mungu! Jueni kuwa wanapo jigubika nguo zao Yeye anajua
wanayo yaficha na wanayo yatangaza. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo
vifuani. 5

6. NA HAKUNA mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake
iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika
Kitabu chenye kubainisha. 6

7. Na Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika
siku sita. Na Kiti chake cha Enzi kilikuwa juu ya maji, ili akufanyieni mtihani
ajuulikane ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo. Na wewe ukisema:
Nyinyi hakika mtafufuliwa baada ya kufa; wale walio kufuru husema: Hayakuwa haya
ila ni uchawi uliyo wazi. 7

8. Na tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda ulio kwisha
hisabiwa wao husema: Nini kinacho izuia hiyo adhabu? Jueni! Siku itakapo wajia
basi haitoondolewa hiyo kwao. Na yatawazunguka yale waliyo kuwa wakiyafanyia
mzaha. 8

9. Na tukimwonjesha mtu rehema inayo toka kwetu, kisha
tukamwondolea, hukata tamaa akakufuru. 9

10. Na tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyo mpata
husema: Taabu zimekwisha niondokea. Hakika yeye hujitapa na kutafakhari.
10

11. Ila wale walio subiri wakatenda mema. Hao watapata
msamaha na ujira mkubwa. 11

12. Basi labda utaacha baadhi ya yale yaliyo funuliwa
kwako, na kifua kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema: Mbona
hakuteremshiwa khazina, au wakaja naye Malaika? Wewe ni mwonyaji tu, na Mwenyezi
Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu. 12

13. Au wanasema: Ameizua? Sema: Basi leteni Sura kumi
zilizo zuliwa mfano wa hii, na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa
mnasema kweli. 13

14. Na wasipo kuitikieni, basi jueni ya kwamba (hii
Qur'ani) imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana mungu ila
Yeye. Basi je! Nyinyi ni Waislamu? 14

15. Wanao taka maisha ya dunia na pumbao lake tutawalipa
humo vitendo vyao kaamili. Na wao humo hawatopunjwa. 15

16. Hao ndio ambao hawatakuwa na kitu Akhera ila Moto,
na yataharibika waliyo yafanya, na yatapotea bure waliyo kuwa wakiyatenda.
16

17. Basi je, mtu aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola
wake Mlezi, inayo fuatwa na shahidi anaye toka kwake, na kabla yake kilikuwa
Kitabu cha Musa kilicho kuwa mwongozi na rehema - hao wanamuamini, na anaye
mkataa katika makundi, basi Moto ndio pahala pa miadi yao. Basi usiwe na shaka
juu ya hayo. Hii ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi; lakini watu wengi
hawaamini. 17

18. Na nani aliye dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye
mzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao Mlezi, na
mashahidi watasema: Hawa ndio walio mtungia uwongo Mola wao Mlezi. Laana ya
Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu, 18

19. Ambao wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na
wanaitakia ipotoke, na wanaikataa Akhera. 19

20. Hao hawawezi kushinda katika ardhi, wala hawana
walinzi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa adhabu. Hawakuwa wakiweza
kusikia wala hawakuwa wakiona. 20

21. Hao ndio walio zikhasiri nafsi zao, na yakawapotea
waliyo kuwa wakiyazua. 21

22. Bila ya shaka hakika wao ndio wenye kukhasiri huko
Akhera. 22

23. Hakika wale walio amini,na wakatenda mema, na
wakanyenyekea kwa Mola wao Mlezi, hao ndio watu wa Peponi, na humo watadumu.
23

24. Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu kiziwi, na
mwenye kuona na anasikia. Je, wawili hawa wanakuwa sawa kwa kufananishwa? Basi,
je, hamfikiri? 24

25. Na Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akawaambia:
Hakika mimi ni mwonyaji kwenu ninaye bainisha, 25

26. Ya kwamba msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu tu.
Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Chungu. 26

27. Na wakasema wakuu walio kufuru katika kaumu yake:
Hatukuoni wewe ila ni mtu tu kama sisi, wala hatukuoni wamekufuata ila wale
walio kuwa kwetu watu duni, wasio kuwa na akili. Wala hatukuoneni kuwa mna ubora
wowote kutushinda sisi. Bali tuna hakika nyinyi ni waongo. 27

28. Akasema: Enyi watu wangu! Hebu fikirini! Ikiwa mimi
ninayo hoja wazi iliyo toka kwa Mola wangu Mlezi, na amenipa rehema kutoka
kwake, nayo ikakufichikieni; je, tukulazimisheni kuikubali hali nyinyi
mnaichukia? 28

29. Na enyi watu wangu! Mimi sikuombeni mali kwa ajili
ya haya. Mimi sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu; na mimi sitawafukuza walio
amini. Hakika wao watakutana na Mola wao Mlezi, lakini mimi nakuoneni mnafanya
ujinga. 29

30. Na
enyi watu wangu! Ni nani atakaye nisaidia kwa Mwenyezi Mungu nikiwafukuza hawa?
Basi je, hamfikiri? 30

31. Wala
sikwambiini kuwa nina khazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi najua mambo ya
ghaibu; wala sisemi: Mimi ni Malaika. Wala siwasemi wale ambao yanawadharau
macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri - Mwenyezi Mungu anajua yaliomo
katika nafsi zao - hapo bila ya shaka ninge kuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.
31

32. Wakasema: Ewe Nuhu! Umejadiliana, na umekithirisha kutujadili. Basi tuletee
hayo unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli. 32

33. Wakasema: Ewe Nuhu! Umejadiliana, na umekithirisha kutujadili. Basi tuletee
hayo unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli. 33

34. Wala
nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka kukunasihini, ikiwa Mwenyezi Mungu anataka
kukuachieni mpotee. Yeye ndiye Mola wenu Mlezi; na kwake mtarejeshwa. 34

35. Au
ndio wanasema: Ameizua? Sema: Ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na
mimi sikhusiki na makosa myatendayo. 35

36. Na
akafunuliwa Nuhu akaambiwa: Hataamini yeyote katika watu wako ila wale walio
kwisha amini. Basi usisikitike kwa waliyo kuwa wakiyatenda. 36

37. Na
unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu. Wala usinisemeze
kuwatetea walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa. 37

38. Na
akawa anaunda jahazi, na kila wakipita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Yeye
akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli na sisi tunakukejelini kama mnavyo tukejeli.
38

39. Nanyi
mtakuja jua ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye mteremkia
adhabu ya kudumu. 39

40. Hata
ilipo kuja amri yetu, na tanuri ikafoka maji, tulisema: Pakia humo wawili
wawili, dume na jike, kutoka kila aina, na ahali zako, isipo kuwa wale ambao
imekwisha wapitia hukumu; na watu walio amini. Na hawakuamini pamoja naye ila
wachache tu. 40

41 Na
akasema: Pandeni humo kwa Bismillahi, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, kwenda kwake
na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
41

42. Ikawa
inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuhu akamwita mwanawe naye alikuwa
mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi, wala usiwe pamoja na makafiri. 42

43. Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. (Nuhu) akasema: Leo hapana
wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu ila aliye mrehemu mwenyewe. Na wimbi
likawatenganisha, akawa katika walio zama. 43

44. Na
ikasemwa: Ewe ardhi! Meza maji yako. Na Ewe mbingu! Jizuie. Basi maji
yakadidimia chini, na amri ikapitishwa, na (jahazi) likasimama juu ya (mlima) wa
Al Juudiy. Na ikasemwa: Wapotelee mbali watu walio dhulumu! 44

45. Na
Nuhu alimwomba Mola wake Mlezi: Ee Mola Mlezi wangu! Hakika mwanangu ni katika
ahali zangu, na hakika ahadi yako ni haki. Na Wewe ni Mwenye haki kuliko
mahakimu wote. 45

46. Akasema: Ewe Nuhu! Huyu si katika ahali zako. Mwendo wake si mwema. Basi
usiniombe jambo usio na ujuzi nalo. Mimi nakuwaidhi usije ukawa miongoni mwa
wajinga. 46

47. Nuhu
akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi najikinga kwako nisikuombe nisio na ujuzi
nalo. Na kama hunisamehe na ukanirehemu, nitakuwa katika walio khasiri.
47

48. Ikasemwa: Ewe Nuhu! Shuka kwa salama itokayo kwetu, na baraka nyingi juu
yako na juu ya watu walio pamoja nawe. Na zitakuwapo kaumu tutakazo
zistarehesha, na kisha zitashikwa na adhabu chungu itokayo kwetu. 48

49 Hizi
ni katika khabari za ghaibu tunazo kufunulia. Hukuwa ukizijua wewe, wala watu
wako, kabla ya hii. Basi subiri! Hakika Mwisho ni wa wachamngu. 49

50. Na
kwa kina A'adi tulimtuma ndugu yao Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu! Nyinyi hamna mungu isipo kuwa Yeye. Nyinyi si chochote ila ni
wazushi tu. 50

51. Enyi
watu wangu! Sikuombeni ujira kwa ajili ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa Yule
aliye niumba. Basi hamtumii akili? 51

52. Na
enyi watu wangu! Muombeni msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake.
Atakuleteeni mbingu zenye kunyesha mvua ya kumiminika, na atakuzidishieni nguvu
juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke mkawa wakosefu. 52

53. Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi. Wala sisi hatuiachi miungu yetu
kwa kufuata kauli yako. Na wala sisi hatukuamini wewe. 53

54. Sisi
tunasema: Baadhi katika miungu yetu imekusibu kwa baa. Akasema: Hakika mimi
namshuhudisha Mwenyezi Mungu, na nyinyi shuhudieni, ya kwamba mimi najitenga
mbali na hao mnao wafanya washirika, 54

55. Mkamwacha Yeye. Basi nyote nyinyi nipangieni vitimbi, na kisha msinipe
muhula! 55

56. Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wangu na Mola Mlezi
wenu. Hapana kiumbe yeyote ila Yeye anamwendesha atakavyo. Hakika Mola wangu
Mlezi yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka. 56

57. Na
ikiwa watarudi nyuma, basi mimi nimekwisha kufikishieni niliyo tumwa kwenu. Na
Mola wangu Mlezi atawaleta watu wengine badala yenu, wala nyinyi hamumdhuru kitu
Yeye. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu. 57

58. Ilipo
fika amri yetu, tulimwokoa Hud na walio amini pamoja naye, kwa rehema itokayo
kwetu. Na tukawaokoa na adhabu ngumu. 58

59. Na
hao ndio kina A'adi. Walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, na wakawaasi Mitume
wake, na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inda. 59

60. Na
wakafuatishiwa laana katika dunia hii na Siku ya Kiyama. Basi tambueni
mtanabahi! Hakika kina A'adi walimkufuru Mola wao Mlezi. Na tambueni mtanabahi
kuwa hakika waliangamizwa kina A'adi, kaumu ya Hud. 60

61. Na
kina Thamud tuliwapelekea ndugu yao Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Yeye ndiye aliye kuumbeni katika
ardhi, na akakuwekeni humo. Basi mwombeni msamaha, kisha mtubu kwake. Hakika
Mola wangu Mlezi yupo karibu, anaitikia maombi. 61

62. Wakasema: Ewe Saleh! Hakika kabla ya haya ulikuwa unatarajiwa kheri kwetu.
Je, unatukataza tusiwaabudu waliyo kuwa wakiwaabudu baba zetu? Na hakika sisi
tuna shaka na wasiwasi kwa hayo unayo tuitia. 62

63. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninazo dalili zilizo wazi kutokana
na Mola wangu Mlezi, naye akawa kanipa rehema kutoka kwake - je, ni nani atakaye
ninusuru kwa Mwenyezi Mungu nikimuasi? Basi nyinyi hamtanizidishia ila khasara
tu. 63

64. Enyi
watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu ni Ishara kwenu. Basi mwacheni ale
katika ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya, isije ikakuangamizeni
adhabu iliyo karibu. 64

65. Wakamchinja. Basi (Saleh) akasema: Stareheni katika mji wenu muda wa siku
tatu. Hiyo ni ahadi isiyo kuwa ya uwongo. 65

66. Basi
ilipo kuja amri yetu tulimwokoa Saleh na wale walio amini pamoja naye kwa rehema
yetu kutokana na hizaya ya siku ile. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu
Mwenye kushinda. 66

67. Na
ukelele uliwaangamiza wale walio dhulumu, wakapambazukiwa nao ni maiti majumbani
mwao. 67

68. Kama
kwamba hawakuwako huko. Hebu zingatieni! Hakika kina Thamud walimkufuru Mola wao
Mlezi. Hebu zingatieni! Thamud wamepotelea mbali! 68

69. Na
wajumbe wetu walimjia Ibrahim kwa bishara njema, wakasema: Salama! Naye akasema:
Salama! Hakukaa ila mara akaleta ndama wa kuchoma. 69

70. Basi
alipoona mikono yao haimfikilii aliwatilia shaka, na akawaogopa. Wakasema:
Usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut'. 70

71. Na
mkewe alikuwa kasimama wima, akacheka. Basi tukambashiria (kuzaliwa) Is-haq, na
baada ya Is-haq Yaaqub. 71

72. Akasema: Je, hivyo mimi nizae, na hali yangu ni kikongwe na huyu mume wangu
ni kizee? Hakika haya ni mambo ya ajabu! 72

73. Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu
na baraka zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika Yeye ndiye Msifiwa
wa kutukuzwa. 73

74. Basi
khofu ilipo mwondoka Ibrahim, na ikawa ile bishara imemfikia, alianza
kujadiliana nasi juu ya kaumu ya Lut'. 74

75. Hakika Ibrahim alikuwa mpole, ana huruma, na mwepesi wa kurejea kwa Mwenyezi
Mungu. 75

76. (Akaambiwa): Ewe Ibrahim! Wachilia mbali haya! Kwa hakika amri ya Mola wako
Mlezi imekwisha kuja, na hakika hao itawafikia adhabu isiyo rudi nyuma.
76

77. Na
wajumbe wetu walipo kuja kwa Lut' aliwahuzunukia na akawaonea dhiki. Akasema:
Hii leo ni siku ngumu! 77

78. Wakamjia kaumu yake mbio mbio. Na kabla ya haya walikuwa wakitenda maovu.
Yeye akasema: Enyi watu wangu! Hawa binti zangu, ndio wametakasika zaidi kwenu.
Basi mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi mbele ya wageni wangu. Hivyo, hamna
hata mtu mmoja miongoni mwenu aliye ongoka? 78

79. Wakasema: Bila shaka umekwisha jua hatuna haki juu ya binti zako, na
unayajua tunayo yataka. 79

80. Akasema: Laiti ningeli kuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo yenye
nguvu! 80

81. (Wajumbe) wakasema: Ewe Lut'! Sisi ni wajumbe wa Mola wako Mlezi. Hawa
hawatakufikia. Na wewe ondoka pamoja na ahali zako usiku ungalipo. Wala yeyote
miongoni mwenu asitazame nyuma, isipo kuwa mkeo, kwani yeye utamfika msiba
utakao wafika hao. Hakika miadi yao ni asubuhi. Je, asubuhi si karibu? 81

82. Basi
ilipo fika amri yetu tuliigeuza nchi juu chini, na tukawateremshia mvua ya
changarawe za udongo mgumu ulio kamatana wa Motoni, 82

83. Zilizo tiwa alama kwa Mola wako Mlezi. Na haya hayako mbali na wenye
kudhulumu wengineo. 83

84. Na
kwa watu wa Madyana tuliwatumia ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu!
Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye, wala msipunguze vipimo na
mizani. Mimi nakuoneni mmo katika hali njema, nami nakukhofieni adhabu ya Siku
kubwa hiyo itakayo kuzungukeni. 84

85. Na
enyi watu wangu! Timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwakhini watu
vitu vyao; wala msieneze uovu katika nchi mkafanya uharibifu. 85

86. Alivyo kubakishieni Mwenyezi Mungu ndiyo bora kwa ajili yenu, ikiwa nyinyi
ni Waumini. Wala mimi siye mlinzi wenu. 86

87. Wakasema: Ewe Shua'ibu! Ni sala zako ndizo zinazo kuamrisha tuyaache waliyo
kuwa wakiyaabudu baba zetu, au tuache kufanya tupendavyo katika mali zetu? Ama
hakika wewe ni mstahamilivu kweli na mwongofu! 87

88. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili wazi inayo tokana na
Mola wangu Mlezi, na ikawa Yeye ameniruzuku riziki njema kutoka kwake? Wala mimi
sipendi kukukhalifuni nikafanya yale ninayo kukatazeni. Sitaki ila kutengeneza
kiasi ninavyo weza. Na sipati kuwezeshwa haya ila na Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye
ninategemea, na kwake Yeye naelekea. 88

89. Na
enyi watu wangu! Kukhalifiana nami kusikupelekeeni hata mkasibiwa kama walivyo
sibiwa watu wa Nuhu, au watu wa Hud, au watu wa Saleh. Na watu wa Lut' si mbali
nanyi. 89

90. Na
ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi, tena tubuni kwake. Hakika Mola wangu Mlezi
ni Mwenye kurehemu na Mwenye upendo. 90

91. Wakasema: Ewe Shua'ibu! Mengi katika hayo unayo yasema hatuyafahamu. Na sisi
tunakuona huna nguvu kwetu. Lau kuwa si jamaa zako tunge kupiga mawe, wala wewe
si mtukufu kwetu. 91

92. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani jamaa zangu ni watukufu zaidi kwenu kuliko
Mwenyezi Mungu? Na Yeye mmemueka nyuma ya migongo yenu! Hakika Mola wangu Mlezi
ni Mwenye kuyazunguka yote mnayo yatenda. 92

93. Na
enyi watu wangu! Fanyeni mwezayo, na mimi pia ninafanya. Karibuni mtajua ni nani
itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na nani aliye mwongo. Na ngojeni, mimi pia
ninangoja pamoja nanyi. 93

94. Na
ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Shua'ibu na wale walio amini pamoja naye kwa
rehema yetu. Na ukelele uliwanyakua walio dhulumu, na wakapambaukiwa majumbani
mwao wamekufa kifudifudi! 94

95. Kama
kwamba hawakuwamo humo. Zingatia walivyo angamia watu wa Madyana, kama walivyo
angamia watu wa Thamud! 95

96. Na
hakika tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na uthibitisho ulio wazi 96

97. Kwa
Firauni na waheshimiwa wake. Lakini wao walifuata amri ya Firauni, na amri ya
Firauni haikuwa yenye uwongofu. 97

98. Siku
ya Kiyama atawatangulia watu wake na atawaingiza Motoni. Na muingio muovu ulioje
huo! 98

99. Nao
wamefuatishiwa laana hapa duniani na Siku ya Kiyama. Ni mabaya yalioje watakayo
pewa! 99

100. Hizi
ni katika khabari za miji, tunakusimulia. Mingine ipo bado na mingine imefyekwa.
100

101. Na
Sisi hatukuwadhulumu, lakini wao wenyewe wamejidhulumu. Na miungu yao waliyo
kuwa wakiiomba badala ya Mwenyezi Mungu haikuwafaa kitu ilipo kuja amri ya Mola
wako Mlezi. Na hiyo miungu haikuwazidishia ila maangamizo tu. 101

102. Na
ndio kama hivyo ndivyo inavyo kuwa Mola wako Mlezi anapo ikamata miji inapo kuwa
imedhulumu. Hakika mkamato wake ni mchungu na mkali. 102

103. Hakika katika haya ipo ishara kwa yule anaye ogopa adhabu ya Akhera. Hiyo
ndiyo Siku itakayo kusanyiwa watu, na hiyo ndiyo Siku itakayo shuhudiwa.
103

104. Na
Sisi hatuiakhirishi ila kwa muda unao hisabiwa. 104

105. Siku
hiyo itakapo fika, hatosema hata mtu mmoja ila kwa idhini yake Mwenyezi Mungu.
Kati yao watakuwamo waliomo mashakani na wenye furaha. 105

106. Ama
wale wa mashakani hao watakuwamo Motoni wakiyayayatika na kukoroma. 106

107. Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako
Mlezi. Hakika Mola wako Mlezi hutenda apendavyo. 107

108. Na
ama wale walio bahatika, wao watakuwamo Peponi wakidumu humo muda wa kudumu
mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hicho ni kipawa kisio na
ukomo. 108

109. Basi
usiwe na shaka juu ya wanayo yaabudu hao. Hawaabudu ila kama walivyo abudu baba
zao zamani. Na hakika Sisi tutawatimilizia fungu lao bila ya kupunguzwa.
109

110. Na
kwa yakini tulimpa Musa Kitabu; zikazuka khitilafu ndani yake. Na lau kuwa si
neno lilio kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka ingeli
hukumiwa baina yao. Na hakika wao wamo katika shaka juu yake inayo wahangaisha.
110

111. Na
hakika Mola wako Mlezi atawatimilizia malipo ya vitendo vyao. Hakika Yeye anayo
khabari ya wayatendayo. 111

112. Basi, simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wewe na wale wanao elekea kwa
Mwenyezi Mungu pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote
myatendayo. 112

113. Wala
msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi
badala ya Mwenyezi Mungu, wala tena hamtasaidiwa. 113

114. Na
shika Sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na
mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka. 114

115. Na
subiri, kwani Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanao fanya wema. 115

116. Basi
mbona hawakuwamo katika watu wa kabla yenu wenye vyeo na wasaa wanao kataza
uharibifu katika nchi, isipo kuwa wachache tu, ambao ndio tulio waokoa? Na walio
dhulumu walifuata starehe zao, na wakawa ni wakosefu. 116

117. Wala
hakuwa Mola wako Mlezi wa kuihiliki miji kwa dhulma tu na hali watu wake ni
watenda mema. 117

118. Na
Mola wako Mlezi angeli penda ange wafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini
hawaachi kukhitalifiana, 118

119. Isipo kuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu; na kwa hiyo ndio Mwenyezi
Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako Mlezi: Kweli kweli nitaijaza
Jahannam kwa majini na watu pamoja. 119

120. Na
yote tunayo kusimulia katika khabari za Mitume ni ya kukupa nguvu moyo wako. Na
katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini. 120

121. Na
waambie wale wasio amini: Fanyeni muwezavyo, nasi pia tunafanya. 121

122. Na
ngojeni, na sisi tunangoja. 122

123. Na
ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyo fichikana katika ardhi na mbingu, na
mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu Yeye na umtegemee Yeye. Na Mola wako
Mlezi haghafiliki na yale mnayo yatenda. 123
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una
ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani