Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. H'a, Mim. 1

2. Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye
nguvu, Mwenye kujua. 2

3. Anaye samehe dhambi na anaye pokea toba, Mkali wa
kuadhibu, Mwenye ukarimu, hakuna mungu ila Yeye; marejeo ni kwake. 3

4. Hawazibishi Ishara za Mwenyezi Mungu ila walio
kufuru; basi kusikughuri wewe kutanga tanga kwao katika nchi. 4

5. Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na makundi
mengine baada yao. Na kila taifa lilikuwa na hamu juu ya Mtume wao wamkamate. Na
walibishana kwa upotovu ili kuipindua haki. Kwa hivyo niliwakamata. Basi
ilikuwaje adhabu yangu! 5

6. Namna hivi limewathibitikia makafiri neno la Mola
wako Mlezi ya kwamba wao ni watu wa Motoni. 6

7. Wale wanao beba A'rshi, na wanao izunguka,
wanamsabihi na kumhimidi Mola wao Mlezi, na wanamuamini, na wanawaombea msamaha
walio amini kwa kusema: Mola wetu Mlezi! Umekienea kila kitu kwa rehema na
ujuzi. Basi wasamehe walio tubu na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu
ya Jahannamu. 7

8. Mola wetu Mlezi! Na waingize katika Bustani za Milele
ulizo waahidi. Na uwape haya pia wale walio fanya mema miongoni mwa wazee wao na
wake zao na dhuriya zao. Hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 8

9. Na waepushe na maovu; kwani umwepushaye maovu siku
hiyo, hakika umemrehemu; na huko ndiko kufuzu kukubwa. 9

10. Kwa hakika wale walio kufuru watanadiwa: Bila ya
shaka kukuchukieni Mwenyezi Mungu ni kukubwa kuliko kujichukia nyinyi nafsi
zenu, mlipo kuwa mnaitwa kwenye Imani nanyi mkakataa. 10

11.
Watasema: Mola wetu Mlezi! Umetufisha mara mbili, na
umetuhuisha mara mbili! Basi tunakiri madhambi yetu. Basi je, ipo njia ya
kutoka? 11

12. Hayo ni hivyo kwa sababu mlikuwa akiombwa Mwenyezi
Mungu peke yake mnakataa. Na akishirikishwa mnaamini. Basi hukumu ni ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu Mkuu. 12

13. Yeye ndiye anaye kuonyesheni Ishara zake, na
anakuteremshieni kutoka mbinguni riziki. Na hapana anaye kumbuka ila anaye
rejea. 13

14. Basi mwombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu,
na wangachukia makafiri. 14

15. Yeye ndiye Mwenye vyeo vya juu, Mwenye A'rshi.
Hupeleka Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake, ili kuonya kwa
Siku ya Mkutano. 15

16. Siku watakayo dhihiri wao. Hapana kitacho fichikana
chochote chao kwa Mwenyezi Mungu. Ufalme ni wa nani leo? Ni wa Mwenyezi Mungu
Mmoja Mtenda nguvu. 16

17. Leo kila nafsi italipwa kwa iliyo chuma. Hapana
dhulma leo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu. 17

18. Na waonye siku inayo kurubia, wakati nyoyo zitakapo
fika kooni, nao wamejaa huzuni. Madhaalimu hawatakuwa na rafiki, wala mwombezi
wa kuitikiwa. 18

19.
(Mwenyezi Mungu) anajua khiyana ya macho na yanayo
ficha vifua. 19

20. Na Mwenyezi Mungu huhukumu kwa haki; lakini hao
wanao waomba badala yake hawahukumu chochote. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye
kusikia Mwenye kuona. 20

21. Kwani hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyo
kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Hao walikuwa wamewazidi hawa kwa nguvu na
athari katika nchi. Na Mwenyezi Mungu aliwatia mkononi kwa sababu ya madhambi
yao. Na wala hapakuwa wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu. 21

22. Hayo ni kwa sababu walikuwa wanawajia Mitume wao kwa
hoja zilizo wazi, lakini wakawakataa, ndipo Mwenyezi Mungu akawakamata. Bila ya
shaka Yeye ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu. 22

23. Na kwa yakini tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu
na uthibitisho ulio wazi, 23

24.
Kumwendea Firauni na Hamana na Qaruni, wakasema:
Huyu ni mchawi, mwongo mkubwa. 24

25. Basi alipo waletea Haki inayo toka kwetu, walisema:
Waueni watoto wanaume wa wale walio muamini na wawacheni hai wanawake wao. Na
haviwi vitimbi vya makafiri ila katika upotovu. 25

26. Na Firauni akasema: Niachieni nimuuwe Musa, naye
amwite Mola wake Mlezi! Mimi nachelea asije kubadilishieni dini yenu, au
akatangaza uharibifu katika nchi. 26

27. Na Musa akasema: Mimi najikinga kwa Mola wangu Mlezi
na Mola wenu Mlezi anilinde na kila mwenye jeuri asiye iamini Siku ya Hisabu. 27

28. Na akasema mtu mmoja Muumini, aliye kuwa mmoja
katika watu wa Firauni aliye ficha Imani yake: Mtamuuwa mtu kwa sababu anasema
Mola wangu Mlezi ni Mwenyezi Mungu? Na hali naye amekujieni na hoja zilizo wazi?
Na akiwa yeye mwongo basi uwongo wake ni juu yake mwenyewe, na akiwa mkweli
yatakufikieni baadhi ya hayo anayo kuahidini. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi
apindukiaye mipaka, mwongo mkubwa. 28

29. Enyi watu wangu! Leo mna ufalme, mmeshinda katika
nchi; basi ni nani atakaye nisaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama
ikitufikia? Firauni akasema: Sikupeni shauri ila ile niliyo iona, wala
sikuongozeni ila kwenye njia ya uwongofu. 29

30. Na akasema yule aliye amini: Enyi watu wangu! Hakika
mimi nakukhofieni mfano wa siku za makundi, 30

31. Mfano wa hali ya watu wa Nuhu na A'di na Thamudi na
wale wa baada yao. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja. 31

32. Na enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni Siku ya
mayowe. 32

33. Siku mtakapo geuka kurudi nyuma. Hamtakuwa na wa
kukulindeni kwa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuhukumiwa na Mwenyezi Mungu kupotea,
basi huyo hana wa kumwongoa. 33

34. Na alikwisha wajieni Yusuf zamani kwa dalili zilizo
wazi, lakini nyinyi mliendelea katika shaka kwa yale aliyo kuleteeni; mpaka
alipo kufa mkasema: Mwenyezi Mungu hataleta kabisa Mtume baada yake. Kama hivyo
Mwenyezi Mungu humwacha kupotea anaye pindukia mipaka katika maasi anaye jitia
shaka. 34

35. Hao ambao wanajadiliana katika Ishara za Mwenyezi
Mungu pasipo ushahidi wowote ulio wafikia, ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi
Mungu na mbele ya walio amini. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu apigavyo muhuri juu ya
kila moyo wa jeuri anaye jivuna. 35

36. Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili
nipate kuzifikia njia, 36

37. Njia za mbinguni ili nikamwone Mungu wa Musa. Na kwa
hakika mimi bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu. Na hivi ndivyo Firauni
alivyo pambiwa ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa Njia. Na vitimbi vya
Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu. 37

38. Na yule aliye amini alisema: Enyi watu wangu!
Nifuateni mimi, nitakuongozeni njia ya uwongozi mwema. 38

39. Enyi watu wangu! Hakika haya maisha ya dunia ni
starehe ipitayo tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima. 39

40. Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo uwovu
wake, na anaye tenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi
hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu. 40

41. Na enyi watu wangu! Kwa nini mimi nakuiteni kwenye
uwokofu, nanyi mnaniita kwenye Moto? 41

42. Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu na nimshirikishe
na yule ambaye simjui, nami nakuiteni kwa Mwenye nguvu Mwenye kusamehe? 42

43. Bila ya shaka mnaye niitia kumuabudu hastahiki wito
duniani wala Akhera. Na hakika marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu. Na wanao
pindukia mipaka ndio watu wa Motoni! 43

44. Basi mtayakumbuka ninayo kuambieni. Nami namkabidhi
Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu anawaona waja wake. 44

45. Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa hila
walizo zifanya. Na adhabu mbaya itawazunguka watu wa Firauni. 45

46.
Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itapo fika
Saa ya Kiyama patasemwa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa! 46

47. Na watapo hojiana huko Motoni, wanyonge watawaambia
walio jitukuza: Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi je, hamtuondolei sehemu
ya huu Moto? 47

48. Watasema walio jitukuza: Hakika sote sisi tumo humo
humo! Kwani Mwenyezi Mungu kesha hukumu baina ya waja! 48

49. Na walio Motoni watawaambia walinzi wa Jahannamu:
Mwombeni Mola wenu Mlezi atupunguzie walau siku moja ya adhabu. 49

50. Nao watasema: Je! Hawakuwa wakikufikieni Mitume wenu
kwa hoja zilio wazi? Watasema: Kwani? Watasema: Basi ombeni! Na maombi ya
makafiri hayawi ila ni kupotea bure. 50

51. Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu
na walio amini katika uhai wa duniani na siku watapo simama Mashahidi, 51

52. Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru wao, nao
watapata laana, na watapata makaazi mabaya kabisa. 52

53. Na kwa hakika tulimpa Musa uwongofu, na
tukawarithisha Wana wa Israili Kitabu, 53

54. Ambacho ni Uwongofu na Ukumbusho kwa wenye akili. 54

55. Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni
kweli. Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa
kumhimidi jioni na asubuhi. 55

56. Hakika hao wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi
Mungu bila ya uthibitisho wowote uliyo wajia, hawana vifuani mwao ila kutaka
ukubwa tu, na wala huo hawaufikilii. Basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika
Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona. 56

57. Bila ya shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa
zaidi kuliko kuwaumba watu. Lakini watu wengi hawajui. 57

58. Na kipofu na mwenye kuona hawalingani; na walio
amini na watendao mema hawalingani na muovu. Ni machache mnayo yakumbuka. 58

59. Hakika Saa (ya Kiyama) itafika, nayo haina shaka.
Lakini watu wengi hawaamini. 59

60. Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni.
Kwa hakika wale ambao wanajivuna na kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu
wadhalilike. 60

61. Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni usiku ili mpate
kutulia humo, na mchana wa kuonea. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye
fadhila juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru. 61

62. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi, Muumba wa
kila kitu. Hapana mungu ila Yeye; basi mnageuzwa wapi? 62

63. Namna hivi ndivyo walivyo geuzwa walio kuwa
wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu. 63

64. Ni Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni ardhi kuwa ni
pahala pa kukaa, na mbingu kuwa dari. Na akakutieni sura, na akazifanya nzuri
sura zenu, na akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu
Mlezi. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. 64

65. Yeye ndiye aliye Hai - hapana mungu isipo kuwa Yeye.
Basi muabuduni Yeye mkimsafishia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi
Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. 65

66. Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba
badala ya Mwenyezi Mungu, zilipo nijia hoja zilizo dhaahiri kutokana na Mola
wangu Mlezi. Na nimeamrishwa nisilimu kwa Mola wa walimwengu wote. 66

67. Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone
la manii, kisha kwa pande la damu, kisha akakutoeni katika hali ya mtoto
mchanga, kisha mpate kufikilia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu
wapo wanao kufa kabla, na ili mfikie muda ulio kwisha wekwa, na ili mpate
kufahamu. 67

68. Yeye ndiye anaye huisha na anaye fisha. Akihukumu
jambo liwe, basi huliambia: Kuwa! Likawa. 68

69. Je! Huwaoni wale wanao bishana katika Ishara za
Mwenyezi Mungu? Wanageuziwa wapi? 69

70. Ambao wamekanusha Kitabu na yale tuliyo watuma
Mitume wetu. Basi watakuja jua. 70

71. Zitakapo kuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku
wanabururwa 71

72. Katika maji ya moto, kisha wanaunguzwa Motoni, 72

73. Tena wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa
mkiwashirikisha. 73

74. Badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea,
bali tangu zamani hatukuwa tukiomba kitu! Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anawaachia
makafiri wapotelee mbali. 74

75. Haya ni kwa sababu mlikuwa mkijitapa katika ardhi
pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa mkijishaua. 75

76. Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo
milele. Basi ni maovu yaliyoje makaazi ya wanao takabari! 76

77. Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya
kweli. Na ama tukikuonyesha baadhi ya yale tuliyo waahidi au tukikufisha, lakini
wao watarudishwa kwetu tu. 77

78. Na bila ya shaka tuliwatuma Mitume kabla yako.
Wengine katika hao tumekusimulia khabari zao, na wengine hatukukusimulia. Na
haiwi Mtume alete Ishara yoyote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Basi ikija
amri ya Mwenyezi Mungu huhukumiwa kwa Haki, na hapo wapotofu watakhasiri. 78

79. Mwenyezi Mungu aliye kujaalieni nyama hoa, mifugo,
ili muwapande baadhi yao, na muwale baadhi yao. 79

80. Na katika hao mnayo manufaa kadhaa wa kadhaa, na
mnapata kwao haja ziliomo vifuani mwenu; na mnachukuliwa juu yao, na juu ya
marikebu. 80

81. Naye anakuonyesheni Ishara zake. Basi Ishara gani za
Mwenyezi Mungu mnazo zikataa? 81

82. Kwani hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje
mwisho wa walio kuwa kabla yao? Wao walikuwa wengi kuliko hawa, na wamewashinda
kwa nguvu na athari katika nchi. Wala hayakuwafaa hayo waliyo kuwa wakiyachuma. 82

83. Walipo wajia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi
walijitapa kwa ilimu waliyo kuwa nayo. Basi yakawazunguka waliyo kuwa
wakiyafanyia maskhara. 83

84. Walipo iona adhabu yetu walisema: Tumemuamini
Mwenyezi Mungu kuwa ni wa pekee, na tunaikataa miungu tuliyo kuwa
tukiishirikisha naye. 84

85. Lakini imani yao haikuwa yenye kuwafaa kitu wakati
ambao wamekwisha iona adhabu yetu. Huu ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kuwa
kwa waja wake. Na hapo walio kufuru walikhasiri. 85
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani