Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. H'a Mim 1

2. Uteremsho huu umetoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye
kurehemu. 2

3. Hichi ni Kitabu kilicho pambanuliwa Aya zake, cha
kusomwa kwa Kiarabu kwa watu wanao jua. 3

4. Kitoacho khabari njema, na chenye kuonya. Lakini
wengi katika wao wamepuuza; kwa hivyo hawasikii. 4

5. Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa
hayo unayo tuitia, na masikio yetu yana uziwi, na baina yetu na wewe lipo pazia.
Basi wewe tenda, nasi tunatenda. 5

6. Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa
kwangu ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea
Yeye, na mumtake msamaha, na ole wao wanao mshirikisha, 6

7. Ambao hawatoi Zaka na wanaikataa Akhera. 7

8. Hakika wanao amini na wakatenda mema watakuwa na
ujira usio na ukomo. 8

9. Sema: Hivyo nyinyi mnamkataa aliye umba ardhi katika
siku mbili, na mnamfanyia washirika? Huyu ndiye Mola Mlezi wa walimwengu wote.
9

10. Na akaweka humo milima juu yake, na akabarikia humo
na akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Haya ni sawa kabisa kwa wanao
uliza. 10

11. Kisha akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi,
akaziambia hizo na ardhi: Njooni, kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili
vikasema: Tumekuja nasi ni wat'iifu. 11

12. Basi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili, na
akazipangia kila mbingu mambo yake. Na tukaipamba mbingu ya chini kwa mataa na
kwa ulinzi. Hichi ndicho kipimo cha Mwenyezi Mungu Mwenye Kujua. 12

13. Basi wakipuuza wewe sema: Nakuhadharisheni adhabu
mfano wa adhabu ya A'di na Thamudi, 13

14. Walipo wajia Mitume mbele yao na nyuma yao
wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu! Wakasema: Angeli taka Mola wetu
Mlezi bila ya shaka angeli wateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo
mliyo tumwa. 14

15. Ama kina A'di walijivuna katika nchi bila ya haki,
na wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba
Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa
wanazikataa Ishara zetu! 15

16. Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za
ukorofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya
shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa. 16

17. Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walipenda upofu
kuliko uwongofu. Basi uliwachukua moto wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya
yale waliyo kuwa wakiyachuma. 17

18. Na tukawaokoa walio amini na wakawa wanamcha-mngu.
18

19. Na siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu
kwenye Moto, nao wakikgawanywa kwa makundi. 19

20. Hata watakapo ufikia Moto yatawashuhudia masikio
yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyo kuwa wakiyatenda. 20

21. Na wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini
mmetushuhudilia? Nazo zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha
kila kitu! Na Yeye ndiye aliye kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu
mtarejeshwa. 21

22. Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na
macho yenu, na ngozi zenu, zisikushuhudilieni. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi
Mungu hayajui mengi katika mliyo kuwa mkiyatenda. 22

23. Basi hiyo dhana yenu mliyo kuwa mkimdhania Mola
wenu Mlezi. Imekuangamizeni; na mmekuwa miongoni mwa walio khasiri. 23

24. Basi wakisubiri Moto ndio maskani yao. Na wakiomba
radhi hawakubaliwi. 24

25. Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo
mbele yao na nyuma yao. Basi ikawathibitikia kauli wawe pamoja na mataifa yaliyo
pita kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye
kukhasirika. 25

26. Na walio kufuru walisema: Msiisikilize Qur'ani hii,
na timueni zogo, huenda mkashinda. 26

27. Basi hapana shaka tutawaonjesha hao walio kufuru
adhabu kali, na hapana shaka tutawalipa malipo mabaya ya yale waliyo kuwa
wakiyafanya. 27

28. Hayo ndiyo malipo ya Maadui wa Mwenyezi Mungu -
Moto! Humo watakuwa na maskani ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa
wakizikataa Ishara zetu. 28

29. Na walio kufuru watasema: Mola wetu Mlezi!
Tuonyeshe walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu
yetu, wapate kuwa miongoni wa walio chini kabisa. 29

30. Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi
Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope,
wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa. 30

31. Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na
katika Akhera, na humo mtapata kinacho tamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata
mtakavyo vitaka. 31

32. Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye
kurehemu. 32

33. Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa
Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?
33

34. Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio
jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki
jamaa wa kukuonea uchungu. 34

35. Lakini hawapewi wema huu ila wanao subiri, wala
hawapewi ila wenye bahati kubwa. 35

36. Na Shet'ani akikuchochea kwa uchochezi wewe jikinge
kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. 36

37. Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na
mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye
viumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu. 37

38. Na ikiwa watajivuna, basi hao walioko kwa Mola wako
Mlezi wanamtakasa Yeye usiku na mchana, na wao hawachoki. 38

39. Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi
nyonge, lakini tunapo iteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila
ya shaka aliye ihuisha ardhi ndiye atakaye huisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa
kila kitu. 39

40. Hakika wale wanao upotoa ukweli uliomo katika
Ishara zetu hawatufichikii Sisi. Je! Atakaye tupwa Motoni ni bora au atakaye
kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayo
yatenda. 40

41. Kwa hakika wanayo yakataa mawaidha haya yanapo
wajia (wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu.
41

42.
Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake.
Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa. 42

43.
Huambiwi ila yale yale waliyo ambiwa Mitume wa
kabla yako. Hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ni Mwenye maghfira, na ni
Mwenye adhabu chungu. 43

44. Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni
wangeli sema: Kwanini Aya zake haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na
Mtume Mwaarabu? Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na poza kwa wenye kuamini. Na
wasio amini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao
wanaitwa nao wako pahala mbali. 44

45. Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea
khitilafu kati yake. Na lau kuwa halikwisha tangulia neno la Mola wako Mlezi
wangeli hukumiwa. Na hakika wao wamo katika shaka yenye kuwatia wasiwasi.
45

46. Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi
yake, na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako
Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja. 46

47. UJUZI wa kuijua Saa ya Kiyama unarudishwa kwake tu
Mwenyezi Mungu. Na matunda hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui
mimba, wala hazai, ila kwa kujua kwake. Na siku atakayo waita, akawaambia: Wako
wapi washirika wangu? Hapo watasema: Tunakiri kwako ya kwamba hapana miongoni
mwetu anaye shuhudia hayo. 47

48. Na wakawapotea wale walio kuwa wakiwaomba hapo
kwanza, na wakawa na yakini kuwa hawana pa kukimbilia. 48

49.
Mwanaadamu hachoki kuomba dua za kheri, na inapo
mpata shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa. 49

50. Na pindi tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada
ya kumgusa dhara, bila ya shaka husema: Haya nayastahiki mimi, wala sidhani kuwa
Kiyama kitakuja. Na hata nikirudishwa kwa Mola wangu Mlezi bila ya shaka nina
mema yangu kwake! Basi kwa yakini tutawaelezea walio kufuru hayo waliyo yatenda,
na kwa yakini tutawaonjesha adhabu ngumu. 50

51. Na tukimneemesha mwanaadamu hugeuka na kujitenga
upande, na inapo mgusa shari, huwa na madua marefu marefu. 51

52. Sema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi
Mungu, nanyi ikawa ndio mmeyakataa, ni nani aliye potea zaidi kuliko aliye
katika upinzani wa mbali? 52

53.
Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na
katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi
kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu? 53

54. Ama wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao
Mlezi! Ama hakika Yeye amekizunguka kila kitu. 54
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una
ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani