Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1. Sifa zote
njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi, aliye wafanya Malaika
kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili-mbili, na tatu- tatu, na nne-nne. Huzidisha
katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu. 1

2. Rehema ambayo
Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hapana wa kuizuia. Na anayo izuia hapana wa
kuipeleka isipo kuwa Yeye. Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 1

3. Enyi watu!
Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo muumba mwengine asiye kuwa
Mwenyezi Mungu anaye kupeni riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana mungu
ila Yeye tu. Basi wapi mnako geuzwa? 3

4. Na
wakikukanusha, basi walikwisha kanushwa Mitume kabla yako. Na mambo yote
yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu. 4

5. Enyi watu!
Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya
dunia, wala mdanganyifu asikudanganyeni juu ya Mwenyezi Mungu. 5

6. Hakika
Shet'ani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi
lake liwe katika watu wa Motoni. 6

7. Walio kufuru
watakuwa na adhabu kali; na walio amini na wakatenda mema watapata msamaha na
ujira mkubwa. 7

8. 8. Je! Yule aliye pambiwa a'mali zake mbaya na akaziona ni
njema - basi hakika Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye, na humwongoa
amtakaye. Basi nafsi yako isijihiliki kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu
anajua wanayo yafanya. 8

9. Na Mwenyezi
Mungu ndiye anaye zituma Pepo ziyatimue mawingu, nasi tukayafikisha kwenye nchi
iliyo kufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa kwake. Ndivyo kama hivyo kutakavyo
kuwa kufufuliwa. 9

10. Mwenye
kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye hupanda neno
zuri, na a'mali njema Yeye huitukuza. Na wanao panga vitimbi vya maovu watapata
adhabu kali. Na vitimbi vya hao vitaondokea patupu. 10

11. Na Mwenyezi
Mungu amekuumbeni kutokana na udongo. Kisha kwa tone la manii. Kisha
akakufanyeni mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote hachukui mimba, wala
hazai, ila kwa ilimu yake. Na wala hapewi umri mwenye umri mrefu, wala
hapunguziwi katika umri wake, ila yamo hayo katika Kitabu. Hakika hayo ni mepesi
kwa Mwenyezi Mungu. 11

12. Na bahari
mbili haziwi sawa; haya ni matamu yenye ladha, mazuri kunywa. Na haya ni ya
chumvi, machungu. Na kutokana na bahari zote mnakula nyama mpya (isiyo chacha).
Na mnatoa mapambo mnayo yavaa. Na unaona ndani yake marikebu zinakata maji ili
mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru. 12

13. Anauingiza
usiku katika mchana, na anauingiza mchana katika usiku. Na amelifanya jua na
mwezi kutumikia. Kila kimojapo kinakwenda kwa muda maalumu. Huyo ndiye Mwenyezi
Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Na hao mnao waomba badala yake hawamiliki
hata ugozi wa kokwa ya tende. 13

14. Mkiwaomba
hawasikii maombi yenu; na hata wakisikia hawakujibuni. Na Siku ya Kiyama
watakataa ushirikina wenu. Na hapana atakaye kupa khabari vilivyo kama Yeye
Mwenye khabari. 14

15. Enyi watu!
Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye
kujitosha, Msifiwa. 15

16. Akitaka
atakuondoeni na alete viumbe vipya. 16

17. Na hilo si
gumu kwa Mwenyezi Mungu. 17

18. Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Na aliye topewa na
mzigo wake akiomba uchukuliwe hautachukuliwa hata kidogo, na angamwomba jamaa
yake. Hakika wewe unawaonya wale wanao mcha Mola wao Mlezi kwa ghaibu, na
wanashika Sala. Na anaye jitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na
marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu. 18

19. Na kipofu na
mwenye kuona hawalingani. 19

20. Wala giza na
mwangaza. 20

21. Wala kivuli
na joto. 21

22. Wala
hawalingani walio hai na maiti. Hakika Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye.
Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini.22

23. Hukuwa wewe
ila ni mwonyaji. 23

24. Hakika Sisi
tumekutuma wewe kwa Haki, kuwa ni mbashiri na mwonyaji. Na hapana umma wowote
ila ulipata mwonyaji kati yao. 24

25. Na
wakikukanusha basi walikwisha wakanusha walio kuwa kabla yao. Mitume wao
waliwajia kwa dalili wazi wazi na kwa maandiko na Kitabu chenye nuru. 25

26. Kisha
nikawakamata walio kufuru. Basi kuchukia kwangu kulikuwaje? 26

27. Je! Huoni
kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo tumeyatoa
matunda yenye rangi mbali mbali. Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu
yenye rangi mbali mbali, na myeusi sana. 27

28. Na katika
watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao zinakhitalifiana. Kwa hakika wanao
mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe. 28

29. Hakika wale
wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakashika Sala, na wakatoa kwa siri na
kwa dhaahiri katika tulivyo waruzuku, hao hutaraji biashara isiyo bwaga. 29

30. Ili Yeye
awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika
Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye shukrani. 30

31. Na hayo
tuliyo kufunulia kutoka Kitabuni ni Kweli yenye kusadikisha yaliyo kuwa kabla
yake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni Mwenye khabari na Mwenye kuona. 31

32. Kisha
tumewarithisha Kitabu hao ambao tuliwateuwa miongoni mwa waja wetu. Kati yao
yupo aliye jidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliye tangulia
katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu. 32

33. Mabustani ya
milele watayaingia. Huko watavikwa vikuku vya dhahabu, na lulu, na nguo zao humo
ni za hariri. 33

34. Na watasema:
Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye tuondolea huzuni
zote. Hakika Mola wetu Mlezi bila ya shaka ni Mwenye kusamehe, Mwenye shukrani. 34

35. Ambaye kwa
fadhila yake ametuweka makao ya kukaa daima; humu haitugusi taabu wala humu
hakutugusi kuchoka. 35

36. Na walio
kufuru watakuwa na Moto wa Jahannamu, hawahukumiwi wakafa, wala hawatapunguziwa
adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila mwenye kuzidi ukafiri. 36

37. Na humo
watapiga makelele: Mola wetu Mlezi! Tutoe tufanye mema sio yale tuliyo kuwa
tukiyafanya. Kwani hatukukupeni umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka? Na
akakujieni Mwonyaji? Basi onjeni! Kwani walio dhulumu hawana wa kuwanusuru. 37

38. Kwa hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa siri za mbinguni na ardhi. Hakika Yeye ni Mjuzi wa
yaliomo vifuani. 38

39. Yeye ndiye
aliye kufanyeni manaibu katika ardhi. Na anaye kufuru, basi kufuru yake ni juu
yake; na kufuru za makafiri haziwazidishii kwa Mola wao Mlezi ila kuchukiwa.
Wala kufuru za makafiri haziwazidishii ila khasara. 39

40. Sema:
Mnawaona hawa miungu wenu wa kishirikina mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu!
Nionyesheni wameumba sehemu gani katika ardhi? Au wana ushirika wowote katika
mbingu? Au tumewapa Kitabu nao kwa hicho wakawa na hoja zilizo wazi? Lakini
madhaalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu tu. 40

41. Hakika
Mwenyezi Mungu ndiye anaye zuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka
hapana yeyote wa kuzizuia isipo kuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole Mwenye kusamehe.
41

42. Na waliapa
kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwajia mwonyaji bila ya shaka
watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote. Lakini alipo wajia mwonyaji
hakuwazidishia ila kuikimbia hiyo Haki, 42

43. Kwa
kutakabari kwao katika nchi, na kufanya vitimbi vya uovu. Na vitimbi viovu
havimsibu ila mwenyewe aliye vifanya. Hebu hawangojei yalio wasibu watu wa kale?
Basi hutapata mabadiliko katika mtindo wa Mwenyezi Mungu. Wala hutapata mageuko
katika mwendo wa Mwenyezi Mungu. 43

44. Je!
Hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao?
Na hao walikuwa wana nguvu zaidi kuliko wao. Na hapana kitu kinacho weza
kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni wala katika ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye
kujua, Mwenye uweza. 44

45. . Na lau
kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa waliyo yachuma, basi asingeli
muacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja. Lakini Yeye anawachukulia mpaka ufike
muda maalumu. Basi ukifika muda wao basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona
waja wake baraabara. 45
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani